49 Bible Verses About Eating Meat

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Eating Meat
  1. 1 Ndipo Mungu akambariki Noa na wanawe, akiwaambia, “Zaeni mkaongezeke kwa idadi na mkaijaze tena dunia. 2 Wanyama wote wa duniani, ndege wote wa angani, kila kiumbe kitambaacho juu ya ardhi, na samaki wote wa baharini wamekabidhiwa mikononi mwenu, nao watawaogopa na kuwahofu. 3 Kila kitu chenye uhai kiendacho kitakuwa chakula chenu. Kama vile nilivyowapa mimea mbalimbali, sasa nawapa kila kitu.

    4 “Lakini kamwe msile nyama ambayo bado ina damu ya uhai wake, kwa maana damu ni uhai. 5 Hakika damu ya uhai wenu nitaidai. Nitaidai kutoka kwa kila mnyama. Kutoka kwa kila mwanadamu pia nitaidai kwa ajili ya uhai wa mtu mwenzake.

    6 “Yeyote amwagaye damu ya mwanadamu,

    damu yake itamwagwa na mwanadamu,

    kwa kuwa katika mfano wa Mungu,

    Mungu alimuumba mwanadamu.

  2. 24 Mungu akasema, “Ardhi na itoe viumbe hai kulingana na aina zake: wanyama wa kufugwa, viumbe vitambaavyo ardhini na wanyama pori, kila mnyama kulingana na aina yake.” Ikawa hivyo. 25 Mungu akafanya wanyama pori kulingana na aina zake, wanyama wa kufugwa kulingana na aina zake, na viumbe vyote vitambaavyo juu ya ardhi kulingana na aina zake. Mungu akaona kuwa hili ni jema.

    26 Ndipo Mungu akasema, “Tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu, wakatawale juu ya samaki wa baharini na ndege wa angani, juu ya mifugo, juu ya dunia yote, na juu ya viumbe wote watambaao juu ya nchi.”

    27 Kwa hiyo Mungu akamuumba mtu kwa mfano wake mwenyewe,

    kwa mfano wa Mungu alimuumba;

    mwanaume na mwanamke aliwaumba.

    28 Mungu akawabariki na akawaambia, “Zaeni na mkaongezeke, mkaijaze tena dunia na kuitiisha. Mkatawale samaki wa baharini, ndege wa angani, na kila kiumbe hai kiendacho juu ya ardhi.”

    29 Kisha Mungu akasema, “Nimewapa kila mche utoao mbegu juu ya uso wa dunia yote, na kila mti wenye matunda yenye mbegu ndani yake. Vitakuwa chakula chenu. 30 Nao wanyama wote wa dunia, ndege wote wa angani, na viumbe vyote viendavyo juu ya ardhi: yaani kila kiumbe chenye pumzi ya uhai, ninawapa kila mche wa kijani kuwa chakula.” Ikawa hivyo.

    31 Mungu akaona vyote alivyoumba, na tazama, ilikuwa vizuri sana. Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya sita.

  3. 14 Ninajua tena nimehakikishiwa sana katika Bwana Yesu kwamba hakuna kitu chochote ambacho ni najisi kwa asili yake. Lakini kama mtu anakiona kitu kuwa ni najisi, basi kwake huyo kitu hicho ni najisi. 15 Kama ndugu yako anahuzunishwa kwa sababu ya kile unachokula, basi huenendi tena katika upendo. Usiruhusu kile unachokula kiwe sababu ya kumwangamiza ndugu yako ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake. 16 Usiruhusu kile ambacho unakiona kuwa chema kisemwe kuwa ni kiovu. 17 Kwa maana Ufalme wa Mungu si kula na kunywa, bali ni haki, amani na furaha katika Roho Mtakatifu. 18 Kwa sababu mtu yeyote anayemtumikia Kristo kwa jinsi hii, anampendeza Mungu na kukubaliwa na wanadamu.

    19 Kwa hiyo na tufanye bidii kutafuta yale yaletayo amani na kujengana sisi kwa sisi. 20 Usiiharibu kazi ya Mungu kwa ajili ya chakula. Hakika vyakula vyote ni safi, lakini ni kosa kula kitu chochote kinachomsababisha ndugu yako ajikwae. 21 Ni afadhali kutokula nyama wala kunywa divai au kufanya jambo lingine lolote litakalomsababisha ndugu yako ajikwae.

    22 Je, wewe unayo imani? Ile imani uliyo nayo, uwe nayo nafsini mwako mbele za Mungu. Heri mtu yule asiye na sababu ya kujihukumu nafsi yake kwa ajili ya kile anachokifanya. 23 Lakini kama mtu ana shaka kuhusu kile anachokula, amehukumiwa, kwa sababu hakula kwa imani. Kwa kuwa chochote kinachofanywa pasipo imani ni dhambi.

  4. 1 Roho asema waziwazi kwamba katika siku za mwisho baadhi ya watu wataiacha imani na kufuata roho zidanganyazo na mafundisho ya mashetani. 2 Mafundisho kama hayo huja kupitia kwa waongo ambao ni wanafiki, hali dhamiri zao zikiungua kwa kuchomwa moto. 3 Wao huwakataza watu wasioe na kuwaagiza wajiepushe na vyakula fulani, ambavyo Mungu aliviumba ili vipokewe kwa shukrani na wale wanaoamini na kuijua kweli. 4 Kwa maana kila kitu alichokiumba Mungu ni chema, wala hakuna kitu chochote cha kukataliwa kama kikipokewa kwa shukrani, 5 kwa sababu kimetakaswa kwa neno la Mungu na kwa kuomba.

  5. 1 Bwana akawaambia Mose na Aroni, 2 “Waambieni Waisraeli: ‘Kati ya wanyama wote waishio juu ya nchi, hawa ndio mtakaowala: 3 Mwaweza kula mnyama yeyote mwenye kwato zilizogawanyika sehemu mbili na ambaye hucheua.

    4 “ ‘Kuna wanyama wengine ambao hucheua tu au wenye kwato zilizogawanyika tu, lakini hao kamwe msiwale. Ngamia ingawa hucheua hana kwato zilizogawanyika; kwa kawaida ya ibada hiyo ni najisi kwenu. 5 Pelele ingawa hucheua hana kwato zilizogawanyika; huyo ni najisi kwenu. 6 Sungura ingawa hucheua hana kwato zilizogawanyika; huyo ni najisi kwenu. 7 Naye nguruwe ingawa anazo kwato zilizogawanyika sehemu mbili, hacheui; huyo ni najisi kwenu. 8 Kamwe msile nyama yao wala kugusa mizoga yao; wao ni najisi kwenu.

    9 “ ‘Kuhusu viumbe wote wanaoishi ndani ya maji ya bahari na vijito, mtakula wale wote wenye mapezi na magamba. 10 Lakini viumbe wote ndani ya bahari au vijito wasio na mapezi na magamba, wakiwa miongoni mwa makundi au viumbe wote ndani ya maji, hao ni machukizo kwenu. 11 Nao watakuwa machukizo kwenu. Msile nyama yao, nayo mizoga yao itakuwa machukizo. 12 Chochote kinachoishi ndani ya maji ambacho hakina mapezi na magamba kitakuwa chukizo kwenu.

    13 “ ‘Wafuatao ndio ndege watakaokuwa machukizo kwenu, hivyo msiwale kwa sababu ni chukizo: tai, furukombe, kipungu, 14 mwewe mwekundu, aina zote za mwewe mweusi, 15 aina zote za kunguru, 16 mbuni, kiruka-njia, dudumizi, kipanga, shakwe, aina zote za kipanga, 17 bundi, mnandi, bundi mkubwa, 18 mumbi, mwari, nderi, 19 korongo, koikoi wa aina yoyote, hudihudi na popo.

    20 “ ‘Wadudu wote warukao ambao hutembea kwa miguu minne watakuwa chukizo kwenu. 21 Lakini wako viumbe wenye mabawa ambao hutembea kwa miguu minne mtakaowala: wale wenye vifundo katika miguu yao ya kurukaruka juu ya ardhi. 22 Miongoni mwa hawa, mtakula nzige wa aina zote, senene, parare au panzi. 23 Lakini viumbe wengine wote wenye mabawa na wenye miguu minne ni machukizo kwenu.

  6. 1 Sasa kuhusu chakula kilichotolewa sadaka kwa sanamu, tunajua kwamba “sisi sote tuna ujuzi.” Lakini ujuzi hujivuna, bali upendo hujenga. 2 Mtu yeyote anayedhani kwamba anajua kitu, bado hajui kama impasavyo kujua. 3 Lakini mtu ampendaye Mungu, hujulikana naye Mungu.

    4 Hivyo basi, kuhusu kula chakula kilichotolewa sadaka kwa sanamu: Tunajua kwamba “Sanamu si kitu chochote kabisa duniani,” na kwamba “Kuna Mungu mmoja tu.” 5 Kwa kuwa hata kama wapo hao wanaoitwa miungu, kama wakiwa mbinguni au duniani (kama ilivyo kweli wapo “miungu” wengi na “mabwana” wengi), 6 kwetu sisi yuko Mungu mmoja, aliye Baba, ambaye vitu vyote vyatoka kwake na kwa ajili yake sisi twaishi; na kuna Bwana mmoja tu, Yesu Kristo, ambaye kwa yeye vitu vyote vimekuwepo na kwa yeye tunaishi.

    7 Lakini si wote wanaojua jambo hili. Baadhi ya watu bado wamezoea sanamu kuwa halisi hivi kwamba wanapokula chakula kama hicho wanadhani kimetolewa sadaka kwa sanamu na kwa kuwa dhamiri zao ni dhaifu, dhamiri yao inanajisika. 8 Lakini chakula hakituleti karibu na Mungu, wala hatupotezi chochote tusipokula, wala hatuongezi chochote kama tukila.

    9 Lakini angalieni jinsi mnavyotumia uhuru wenu usije ukawa kikwazo kwao walio dhaifu. 10 Kwa maana kama mtu yeyote mwenye dhamiri dhaifu akiwaona ninyi wenye ujuzi huu mkila katika hekalu la sanamu, je, si atatiwa moyo kula chakula kilichotolewa sadaka kwa sanamu? 11 Kwa njia hiyo, huyo ndugu mwenye dhamiri dhaifu, ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake, ataangamia kwa sababu ya ujuzi wenu. 12 Mnapotenda dhambi dhidi ya ndugu zenu kwa njia hii na kujeruhi dhamiri zao zilizo dhaifu, mnamkosea Kristo. 13 Kwa hiyo, kama kile ninachokula kitamfanya ndugu yangu aanguke katika dhambi, sitakula nyama kamwe, nisije nikamfanya ndugu yangu aanguke.

  7. 1 Mkaribisheni yeye ambaye imani yake ni dhaifu, lakini si kwa kugombana na kubishana juu ya mawazo yake. 2 Mtu mmoja imani yake inamruhusu kula kila kitu, lakini mwingine ambaye imani yake ni dhaifu, hula mboga tu. 3 Yeye alaye kila kitu asimdharau yeye asiyekula. Wala yeye asiyekula kila kitu asimhukumu yule alaye kila kitu, kwa maana Mungu amemkubali. 4 Wewe ni nani hata umhukumu mtumishi wa mtu mwingine? Kwa bwana wake tu anasimama au kuanguka. Naye atasimama kwa sababu Bwana anaweza kumsimamisha.

  8. 14 Yesu akaita tena ule umati wa watu, akawaambia, “Nisikilizeni, kila mmoja wenu na mwelewe jambo hili. 15 Hakuna kitu kinachomwingia mtu kimtiacho unajisi, lakini kile kimtokacho ndicho kimtiacho unajisi. [ 16 Kama mtu yeyote ana masikio ya kusikia na asikie.]”

    17 Akiisha kuuacha ule umati wa watu na kuingia ndani, wanafunzi wake wakamuuliza maana ya mfano ule. 18 Akawajibu, “Je, hata nanyi hamwelewi? Je, hamfahamu kwamba kitu kimwingiacho mtu hakimtii unajisi? 19 Mtu akila kitu hakiingii moyoni mwake bali tumboni, na baadaye hutolewa nje ya mwili wake.” (Kwa kusema hivi, Yesu alivihalalisha vyakula vyote kuwa ni “safi.”)

    20 Akaendelea kusema, “Kile kimtokacho mtu ndicho kimtiacho unajisi. 21 Kwa maana kutoka ndani ya moyo wa mtu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wizi, uuaji, uzinzi, 22 tamaa mbaya, uovu, udanganyifu, ufisadi, wivu, matukano, kiburi na upumbavu. 23 Maovu haya yote hutoka ndani ya mtu, nayo ndiyo yamtiayo mtu unajisi.”

  9. 28 Kwa maana imempendeza Roho Mtakatifu na sisi tusiwatwike mzigo wowote mkubwa zaidi ya mambo haya yafuatayo ambayo ni ya lazima: 29 Kwamba mjiepushe na vyakula vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, au kula nyama ya mnyama aliyenyongwa, na mjiepushe na uasherati. Mkiyaepuka mambo haya, mtakuwa mmefanya vyema.

    Kwaherini.

  10. 23 “Vitu vyote ni halali,” lakini si vitu vyote vilivyo na faida. “Vitu vyote ni halali,” lakini si vyote vinavyojenga. 24 Mtu yeyote asitafute yaliyo yake mwenyewe, bali kila mtu atafute yale yanayowafaa wengine.

    25 Kuleni chochote kinachouzwa sokoni, bila kuuliza swali lolote kwa ajili ya dhamiri. 26 Kwa maana, “Dunia na vyote vilivyomo ni mali ya Bwana.”

    27 Kama ukikaribishwa chakula na mtu asiyeamini nawe ukikubali kwenda, kula kila kitu kitakachowekwa mbele yako bila kuuliza maswali kwa ajili ya dhamiri. 28 Lakini kama mtu yeyote akikuambia, “Hiki kimetolewa kafara kwa sanamu,” basi usikile kwa ajili ya huyo aliyekuambia na kwa ajili ya dhamiri. 29 Nina maana dhamiri ya huyo aliyekuambia, wala si kwa ajili ya dhamiri yako. Lakini kwa nini uhuru wangu uhukumiwe na dhamiri ya mtu mwingine? 30 Kama nikila kwa shukrani, kwa nini nashutumiwa kwa kile ambacho kwa hicho ninamshukuru Mungu?

    31 Basi, lolote mfanyalo, kama ni kula au kunywa, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu. 32 Msiwe kikwazo kwa mtu yeyote, wawe Wayahudi au Wayunani, au kwa kanisa la Mungu, 33 kama hata mimi ninavyojaribu kumpendeza kila mtu kwa kila namna. Kwa maana sitafuti mema kwa ajili yangu mwenyewe bali kwa ajili ya wengi, ili waweze kuokolewa.

  11. 16 Kwa hiyo mtu asiwahukumu ninyi kuhusu vyakula au vinywaji, au kuhusu kuadhimisha sikukuu za dini, au Sikukuu za Mwezi Mwandamo au siku ya Sabato. 17 Hizi zilikuwa kivuli cha mambo ambayo yangekuja, lakini ile iliyo halisi imo ndani ya Kristo. 18 Mtu yeyote asiwaondolee thawabu yenu kwa kusisitiza kunyenyekea kwake na kuabudu malaika. Mtu kama huyo hudumu katika maono yake, akijivuna bila sababu katika mawazo ya kibinadamu. 19 Yeye amepoteza ushirikiano na Kichwa, ambaye kutoka kwake mwili wote unalishwa na kushikamanishwa pamoja kwa viungo na mishipa, nao hukua kwa ukuaji utokao kwa Mungu.

    20 Kwa kuwa mlikufa pamoja na Kristo, mkayaacha yale mafundisho ya msingi ya ulimwengu huu, kwa nini bado mnaishi kama ninyi ni wa ulimwengu? Kwa nini mnajitia chini ya amri: 21 “Msishike! Msionje! Msiguse!”? 22 Haya yote mwisho wake ni kuharibika yanapotumiwa, kwa sababu msingi wake ni katika maagizo na mafundisho ya wanadamu. 23 Kwa kweli amri kama hizo huonekana kama zina hekima, katika namna za ibada walizojitungia wenyewe, na unyenyekevu wa uongo na kuutawala mwili kwa ukali, lakini hayafai kitu katika kuzuia tamaa za mwili.

  12. 36 Walipokuwa bado wanazungumza hayo, Yesu mwenyewe akasimama katikati yao, akasema, “Amani iwe nanyi!”

    37 Wakashtuka na kuogopa wakidhani kwamba wameona mzuka. 38 Lakini Yesu akawauliza, “Kwa nini mnaogopa? Kwa nini mna shaka mioyoni mwenu? 39 Tazameni mikono yangu na miguu yangu, mwone kuwa ni mimi hasa. Niguseni mwone; kwa maana mzuka hauna nyama na mifupa, kama mnionavyo kuwa navyo.”

    40 Aliposema haya, akawaonyesha mikono na miguu yake. 41 Wakashindwa kuamini kwa ajili ya furaha na mshangao waliokuwa nao. Akawauliza, “Mna chakula chochote hapa?”

    42 Wakampa kipande cha samaki aliyeokwa, 43 naye akakichukua na kukila mbele yao.

  13. 10 “ ‘Mwisraeli yeyote au mgeni anayeishi miongoni mwao ambaye atakunywa damu yoyote, nitakuwa kinyume cha mtu huyo atakayekunywa damu na kumkatilia mbali na watu wake. 11 Kwa kuwa uhai wa kiumbe uko ndani ya damu, nami nimewapa hiyo damu ili mfanyie upatanisho kwa ajili yenu wenyewe juu ya madhabahu; damu ndiyo ifanyayo upatanisho kwa ajili ya maisha ya mtu. 12 Kwa hiyo, ninawaambia Waisraeli, “Hakuna hata mmoja wenu anayeruhusiwa kunywa damu, wala mgeni anayeishi miongoni mwenu haruhusiwi kunywa damu.”

    13 “ ‘Mwisraeli yeyote au mgeni anayeishi miongoni mwenu ambaye atamwinda mnyama au ndege anayeruhusiwa kuliwa ni lazima aimwage damu na kuifunika kwa udongo, 14 kwa sababu uhai wa kila kiumbe ni katika damu yake. Ndiyo sababu nimewaambia Waisraeli, “Kamwe msinywe damu ya kiumbe chochote, kwa sababu uhai wa kila kiumbe ni katika damu yake; yeyote atakayekunywa damu ni lazima akatiliwe mbali.”

    15 “ ‘Mtu yeyote, awe mzawa au mgeni, ambaye atakula mzoga wa kitu chochote ama kilichouawa na wanyama mwitu ni lazima afue nguo zake na aoge kwa maji, naye atakuwa najisi kwa kawaida ya ibada mpaka jioni, kisha atakuwa safi.

  14. 19 “Kwa hivyo uamuzi wangu ni kwamba, tusiwataabishe watu wa Mataifa wanaomgeukia Mungu. 20 Badala yake, tuwaandikie kwamba wajiepushe na vyakula vilivyonajisiwa kwa kutolewa sanamu, wajiepushe na uasherati, au kula mnyama aliyenyongwa, na damu.

  15. 3 Kila mwaka mtu huyu alikwea kutoka mji wake ili kuabudu na kutoa dhabihu kwa Bwana Mwenye Nguvu Zote huko Shilo, ambapo Hofni na Finehasi, wana wawili wa Eli, walikuwa makuhani wa Bwana. 4 Kila mara ilipofika siku ya Elikana kutoa dhabihu, aliwapa mafungu Penina mkewe na wanawe wote pamoja na binti zake. 5 Lakini alimpa Hana fungu maradufu kwa sababu alimpenda, ingawa Bwana alikuwa amemfunga tumbo. 6 Kwa sababu Bwana alikuwa amemfunga tumbo, mke mwenzake alikuwa anamchokoza ili kumuudhi. 7 Hili liliendelea mwaka baada ya mwaka. Kila mara Hana alipokwenda katika nyumba ya Bwana, mke mwenzake alikuwa akimkasirisha mpaka analia na kushindwa kula. 8 Elikana mumewe akawa anamwambia, “Hana, kwa nini unalia? Kwa nini huli? Kwa nini kuvunjika moyo? Je, mimi si bora zaidi kwako kuliko watoto kumi?”

  16. 9 Siku ya pili yake, walipokuwa wameukaribia mji, wakati wa adhuhuri, Petro alipanda juu ya nyumba kuomba. 10 Alipokuwa akiomba akahisi njaa, akatamani kupata chakula. Lakini wakati walikuwa wakiandaa chakula, akalala usingizi mzito sana. 11 Akaona mbingu zimefunguka na kitu kama nguo kubwa kikishushwa duniani kwa ncha zake nne. 12 Ndani yake walikuwepo aina zote za wanyama wenye miguu minne, nao watambaao nchini, na ndege wa angani. 13 Ndipo sauti ikamwambia “Petro, ondoka, uchinje na ule.”

    14 Petro akajibu, “La hasha Bwana! Sijawahi kamwe kula kitu chochote kilicho najisi.”

    15 Ile sauti ikasema naye mara ya pili, “Usikiite najisi kitu chochote Mungu alichokitakasa.”

    16 Jambo hili lilitokea mara tatu na ghafula ile nguo ikarudishwa mbinguni.

  17. 20 Usiwe miongoni mwa wanywao mvinyo,

    au wale walao nyama kwa pupa,

    21 kwa maana walevi na walafi huwa maskini,

    nako kusinzia huwavika matambara.

  18. 6 Mbwa mwitu ataishi pamoja na mwana-kondoo,

    naye chui atalala pamoja na mbuzi,

    ndama, mwana simba na ngʼombe wa mwaka mmoja watakaa pamoja,

    naye mtoto mdogo atawaongoza.

    7 Ngʼombe na dubu watalisha pamoja,

    watoto wao watalala pamoja,

    na simba atakula majani makavu kama maksai.

    8 Mtoto mchanga atacheza karibu na shimo la nyoka,

    naye mtoto mdogo ataweka mkono wake

    kwenye kiota cha fira.

    9 Hawatadhuru wala kuharibu

    juu ya mlima wangu mtakatifu wote,

    kwa kuwa dunia itajawa na kumjua Bwana

    kama maji yajazavyo bahari.

  19. 3 Msile kitu chochote ambacho ni machukizo. 4 Hawa ndio wanyama mtakaokula: ngʼombe, kondoo, mbuzi, 5 kulungu, paa, kongoni, paa mweupe, mbuzi-mwitu, pofu na kondoo wa mlimani. 6 Mnaweza kumla mnyama yeyote mwenye kwato zilizogawanyika mara mbili, pia yule anayecheua. 7 Hata hivyo, miongoni mwa wale wanaocheua au wale walio na kwato zilizogawanyika kamwe msile ngamia, sungura na pelele. Iwapo wanacheua, lakini hawana kwato zilizogawanyika; ni najisi kwenu kwa taratibu za kiibada. 8 Nguruwe pia ni najisi; ingawa ana kwato zilizogawanyika, hacheui. Msile nyama yake wala kugusa mzoga wake.

    9 Katika viumbe hai vyote viishivyo kwenye maji, mnaweza kula yeyote aliye na mapezi na magamba. 10 Lakini chochote kisicho na mapezi na magamba msile; kwenu ni najisi.

    11 Mnaweza kula ndege yeyote aliye safi. 12 Lakini wafuatao msiwale: tai, furukombe, kipungu, 13 kengewa mwekundu, kengewa mweusi, mwewe wa aina yoyote, 14 kunguru wa aina yoyote, 15 mbuni, kiruka-njia, dudumizi, kipanga wa aina yoyote, 16 bundi, mumbi, bundi mkubwa, 17 mwari, nderi, mnandi, 18 korongo, koikoi wa aina yoyote, hudihudi na popo.

    19 Wadudu wote warukao kwa makundi ni najisi kwenu, msiwale. 20 Lakini viumbe vyote vyenye mabawa vilivyo safi mwaweza kula.

    21 Msile kitu chochote mtakachokuta kimekufa. Mnaweza kumpa mgeni yeyote anayeishi katika mojawapo ya miji yenu, naye anaweza kula au mnaweza kumuuzia mtu wa nchi nyingine. Lakini ninyi ni watu watakatifu kwa Bwana Mungu wenu.

    Msitokose mwana-mbuzi katika maziwa ya mama yake.

  20. 8 Lakini Danieli alikusudia kuwa hatajitia unajisi kwa chakula cha mfalme na divai, naye akamwomba mkuu wa maafisa ruhusa ili asijinajisi kwa njia hii. 9 Basi Mungu alikuwa amemfanya huyo mkuu wa maafisa kuonyesha upendeleo na huruma kwa Danieli, 10 lakini huyo mkuu wa maafisa akamwambia Danieli, “Ninamwogopa bwana wangu mfalme, aliyeagizia chakula na kinywaji chenu. Kwa nini aone nyuso zenu zikiwa mbaya kuliko za vijana wengine wa rika lenu? Mfalme atakata kichwa changu kwa sababu yenu.”

    11 Ndipo Danieli akamwambia mlinzi aliyeteuliwa na huyo mkuu wa maafisa kuwasimamia Danieli, Hanania, Mishaeli na Azaria, 12 “Tafadhali wajaribu watumishi wako kwa siku kumi. Usitupe chochote ila nafaka na mboga za majani tule, na maji ya kunywa. 13 Baadaye ulinganishe sura zetu na vijana wanaokula chakula cha mfalme, ukawatendee watumishi wako kulingana na unachoona.” 14 Basi akakubali jambo hili, akawajaribu kwa siku kumi.

    15 Mwisho wa zile siku kumi, walionekana kuwa na afya na kunawiri zaidi kuliko yeyote kati ya wale vijana waliokula chakula cha mfalme. 16 Hivyo mlinzi wao akaondoa chakula chao na divai yao waliopangiwa kula na kunywa, akawapa nafaka na mboga za majani badala yake.

    17 Mungu akawapa hawa vijana wanne maarifa na ufahamu wa kila aina ya maandiko na elimu. Naye Danieli aliweza kufahamu maono na aina zote za ndoto.

    18 Mwisho wa muda uliowekwa na mfalme kuwaingiza kwake, mkuu wa maafisa akawaleta mbele ya Mfalme Nebukadneza. 19 Mfalme akazungumza nao, akaona hakuna aliyelingana na Danieli, Hanania, Mishaeli na Azaria. Hivyo wakaingia katika utumishi wa mfalme. 20 Katika kila jambo la hekima na ufahamu kuhusu kile mfalme alichowauliza, aliwaona bora mara kumi zaidi kuliko waganga na wasihiri wote katika ufalme wake wote.

    21 Naye Danieli akabaki huko mpaka mwaka wa kwanza wa utawala wa Mfalme Koreshi.

  21. 42 Msile kiumbe chochote kitambaacho juu ya ardhi, kiwe kitambaacho kwa tumbo lake, au kitambaacho kwa miguu minne au kwa miguu mingi; ni chukizo. 43 Msijitie unajisi kwa chochote katika viumbe hivi. Msijitie unajisi kwa viumbe hivyo au kutiwa unajisi navyo. 44 Mimi ndimi Bwana Mungu wenu; jitakaseni mwe watakatifu, kwa sababu mimi ni mtakatifu. Msijitie unajisi wenyewe kwa kiumbe chochote kile kiendacho juu ya ardhi. 45 Mimi ndimi Bwana niliyewapandisha mtoke Misri ili niwe Mungu wenu. Kwa hiyo kuweni watakatifu kwa sababu Mimi ni mtakatifu.

    46 “ ‘Haya ndiyo masharti kuhusu wanyama, ndege, kila kiumbe hai kiendacho ndani ya maji, na kila kiumbe kiendacho juu ya ardhi. 47 Ni lazima mpambanue kati ya kilicho najisi na kilicho safi, kati ya viumbe hai vinavyoweza kuliwa na vile visivyoweza kuliwa.’ ”

  22. 2 Mchana kutwa nimeinyoosha mikono yangu

    kwa watu wakaidi,

    wanaokwenda katika njia ambazo si nzuri,

    wafuatao mawazo yao wenyewe:

    3 taifa ambalo daima hunikasirisha

    machoni pangu,

    wakitoa dhabihu katika bustani

    na kufukiza uvumba juu ya madhabahu za matofali;

    4 watu waketio katikati ya makaburi

    na kukesha mahali pa siri,

    walao nyama za nguruwe,

    nazo sufuria zao zina mchuzi wa nyama zilizo najisi,

    5 wasemao, ‘Kaa mbali; usinikaribie,

    kwa maana mimi ni mtakatifu mno kwako!’

    Watu wa aina hiyo ni moshi katika pua zangu,

    ni moto uwakao mchana kutwa.

    6 “Tazama, jambo hili hubakia limeandikwa mbele zangu:

    sitanyamaza, bali nitalipiza kwa ukamilifu;

    nitalipiza mapajani mwao:

  23. 1 Basi watu wakalalamika kwa habari ya taabu zao masikioni mwa Bwana, naye alipowasikia, hasira yake ikawaka. Ndipo moto kutoka kwa Bwana ukawaka miongoni mwao na kuteketeza baadhi ya viunga vya kambi. 2 Watu walipomlilia Mose, akamwomba Bwana, nao moto ukazimika. 3 Hivyo mahali pale pakaitwa Tabera, kwa sababu moto kutoka kwa Bwana uliwaka miongoni mwao.

    4 Umati wa watu wenye zogo waliokuwa miongoni mwao walitamani sana chakula kingine, Waisraeli wakaanza kulia tena na kusema, “Laiti tungekuwa na nyama tule! 5 Tunakumbuka wale samaki tuliokula huko Misri bila gharama, pia yale matango, matikitimaji, mboga, vitunguu, na vitunguu saumu. 6 Lakini sasa tumepoteza hamu ya chakula; hatuoni kitu kingine chochote isipokuwa hii mana!”

    7 Mana ilifanana kama mbegu za giligilani, nayo ilikuwa na rangi ya manjano iliyopauka. 8 Hao watu walikwenda kukusanya, kisha waliisaga kwa mawe ya kusagia ya mkono au kuitwanga kwenye vinu. Waliipika vyunguni au kutengeneza maandazi. Ladha yake ilikuwa kama kitu kilichotengenezwa kwa mafuta ya zeituni. 9 Umande ulipoanguka kambini wakati wa usiku, pia mana ilianguka pamoja nao.

    10 Mose akasikia watu wa kila jamaa wakilia, kila mmoja kwenye mlango wa hema lake. Bwana akakasirika mno, naye Mose akafadhaika. 11 Akamuuliza Bwana, “Kwa nini umeleta taabu hii juu ya mtumishi wako? Nimekufanyia nini cha kukuchukiza hata ukaweka mzigo huu wa watu hawa wote juu yangu? 12 Je, watu hawa wote mimi ndiye niliyewatungisha mimba? Je, ni mimi niliyewazaa? Kwa nini unaniambia niwachukue mikononi mwangu, kama vile mlezi abebavyo mtoto mchanga, hadi kwenye nchi uliyowaahidi baba zao? 13 Nitapata wapi nyama kwa ajili ya watu wote hawa? Wanaendelea kunililia wakisema, ‘Tupe nyama tule!’ 14 Mimi siwezi kuwabeba watu hawa wote peke yangu, mzigo ni mzito sana kwangu. 15 Kama hivi ndivyo unavyonitendea, uniue sasa hivi, yaani kama nimepata kibali machoni pako, wala usiniache nione maangamizi yangu mwenyewe.”

    16 Bwana akamwambia Mose: “Niletee wazee sabini wa Israeli, unaowafahamu kama viongozi na maafisa miongoni mwa watu. Walete katika Hema la Kukutania, ili waweze kusimama huko pamoja nawe. 17 Nami nitashuka na kusema nawe huko. Nami nitachukua sehemu ya Roho iliyo juu yako na kuiweka juu yao. Watakusaidia kubeba mzigo wa watu hao ili usije ukaubeba peke yako.

    18 “Waambie hao watu: ‘Jiwekeni wakfu wenyewe kwa ajili ya kesho, wakati mtakapokula nyama. Bwana aliwasikia mlipolia, mkisema, “Laiti tungekuwa na nyama tule! Tulikuwa na hali nzuri zaidi katika nchi ya Misri!” Sasa Bwana atawapa nyama, nanyi mtaila. 19 Hamtaila kwa siku moja tu, au siku mbili, au tano, kumi au siku ishirini, 20 bali kwa mwezi mzima mpaka iwatokee puani, nanyi mtaichukia kabisa, kwa kuwa mmemkataa Bwana, ambaye yupo miongoni mwenu, nanyi mmelia mbele zake, mkisema, “Hivi kwa nini tulitoka Misri?” ’ ”

    21 Lakini Mose alisema, “Mimi niko hapa miongoni mwa watu 600,000 wanaotembea kwa miguu, nawe umesema, ‘Nitawapa nyama ya kula kwa mwezi mzima!’ 22 Je, wangeweza kupata nyama ya kuwatosha hata kama makundi ya kondoo na ya ngʼombe yangechinjwa kwa ajili yao? Je, wangetosheka hata kama samaki wote wa baharini wangevuliwa kwa ajili yao?”

    23 Bwana akamjibu Mose, “Je, mkono wa Bwana ni mfupi sana? Sasa utaona kama jambo nililolisema litatimizwa kwa ajili yako au la.”

    24 Kwa hiyo Mose akatoka na kuwaambia watu lile ambalo Bwana alikuwa amesema. Akawakusanya wazee wao sabini, akawasimamisha kuzunguka Hema. 25 Kisha Bwana akashuka katika wingu na kunena na Mose, naye akachukua sehemu ya Roho iliyokuwa juu ya Mose na kuiweka juu ya wale wazee sabini. Roho aliposhuka juu yao, wakatoa unabii, lakini hawakufanya hivyo tena.

    26 Lakini, watu wawili, ambao majina yao ni Eldadi na Medadi, walibaki kambini. Walikuwa wameorodheshwa miongoni mwa wale wazee sabini, lakini hawakutoka kwenda kwenye Hema. Lakini Roho pia alishuka juu yao, nao wakatabiri huko kambini. 27 Mwanaume mmoja kijana alikimbia na kumwambia Mose, “Eldadi na Medadi wanatoa unabii kambini.”

    28 Yoshua mwana wa Nuni, ambaye alikuwa msaidizi wa Mose tangu ujana wake, akajibu akasema, “Mose bwana wangu, wanyamazishe!”

    29 Lakini Mose akajibu, “Je, unaona wivu kwa ajili yangu? Ningetamani watu wote wa Bwana wangekuwa manabii na kwamba Bwana angeweka Roho yake juu yao!” 30 Ndipo Mose na wale wazee wa Israeli wakarudi kambini.

    31 Kisha ukatokea upepo kutoka kwa Bwana, nao ukawaletea kware kutoka baharini. Ukawaangusha kwenye eneo lote linalozunguka kambi na kujaa ardhini kimo cha mita moja hivi kutoka ardhini kwenye eneo la umbali wa mwendo wa siku moja kila upande. 32 Mchana kutwa na usiku kucha pamoja na siku nzima iliyofuata watu walitoka kwenda kuokota kware. Hakuna mtu yeyote aliyekusanya chini ya homeri kumi. Kisha wakazianika kuzunguka kambi yote. 33 Lakini walipokuwa wakila nyama, ilipokuwa ingali kati ya meno yao na kabla hawajamaliza kula, hasira ya Bwana ikawaka dhidi ya watu, naye akawapiga kwa tauni. 34 Kwa hiyo mahali hapo pakaitwa Kibroth-Hataava, kwa sababu huko ndiko walipowazika watu ambao walitamani sana chakula kingine.

    35 Kutoka Kibroth-Hataava watu wakasafiri mpaka Haserothi na kukaa huko.

  24. 20 Bwana Mungu wenu atakapokuwa ameongeza nchi yenu kama alivyowaahidi, nanyi mkitamani nyama na mkisema, “Ningependa nyama,” hapo unaweza kula nyingi upendavyo. 21 Kama mahali ambapo Bwana Mungu wenu atapachagua kuweka Jina lake ni mbali sana kutoka kwenu, unaweza kuchinja wanyama kutoka makundi yenu ya ngʼombe, ya mbuzi na ya kondoo ambayo Bwana amewapa, kama nilivyokuamuru, na mkiwa katika miji yenu wenyewe mnaweza kula nyingi mtakavyo. 22 Mle kama vile mngekula paa na kulungu. Wote walio najisi kiibada na walio safi mwaweza kula. 23 Lakini hakikisheni kwamba hamkunywa damu, kwa sababu damu ni uhai, kamwe msile uhai pamoja na nyama. 24 Hamruhusiwi kamwe kunywa damu; imwageni juu ya ardhi kama maji. 25 Msinywe damu, ili mweze kufanikiwa ninyi pamoja na watoto wenu baada yenu, kwa sababu mtakuwa mkifanya lililo haki machoni pa Bwana.

  25. 1 Uketipo kula chakula na mtawala,

    angalia vyema kile kilicho mbele yako,

    2 na utie kisu kooni mwako

    kama ukiwa mlafi.

    3 Usitamani vyakula vyake vitamu

    kwa kuwa chakula hicho ni cha hila.

  26. 10 Yesu akaita ule umati wa watu, akawaambia, “Sikilizeni na mwelewe: 11 kinachomfanya mtu kuwa najisi mbele za Mungu si kile kiingiacho kinywani mwake, bali ni kile kitokacho kinywani mwake.”

    12 Kisha wanafunzi wake wakamjia na kumuuliza, “Je, unajua kwamba Mafarisayo walichukizwa sana waliposikia yale uliyosema?”

    13 Akawajibu, “Kila pando ambalo Baba yangu wa mbinguni hakulipanda, litangʼolewa. 14 Waacheni; wao ni viongozi vipofu, wanaoongoza vipofu. Kama kipofu akimwongoza kipofu mwenzake, wote wawili watatumbukia shimoni.”

    15 Petro akasema, “Tueleze maana ya huu mfano.”

    16 Yesu akawauliza, “Je, bado ninyi hamfahamu? 17 Je, hamwelewi kwamba chochote kiingiacho kinywani huenda tumboni, na hatimaye hutolewa nje kikiwa uchafu? 18 Lakini kitokacho kinywani hutoka moyoni, na hiki ndicho kimtiacho mtu unajisi. 19 Kwa maana ndani ya moyo hutoka mawazo mabaya, uuaji, uzinzi, uasherati, wizi, ushahidi wa uongo na masingizio. 20 Haya ndiyo yamtiayo mtu unajisi; lakini kula bila kunawa mikono hakumtii mtu unajisi.”

  27. 17 “ ‘Hii ni kanuni ya kudumu kwa vizazi vijavyo, popote muishipo: Msile mafuta yoyote ya mnyama wala damu.’ ”

  28. 22 Bwana akamwambia Mose, 23 “Waambie Waisraeli: ‘Msile mafuta yoyote ya ngʼombe, kondoo wala mbuzi. 24 Mafuta ya mnyama aliyekutwa amekufa au ameraruliwa na mnyama pori yanaweza kutumika kwa kazi nyingine yoyote, lakini kamwe msiyale. 25 Mtu yeyote alaye mafuta ya mnyama ambaye ametolewa sadaka kwa Bwana kwa moto ni lazima akatiliwe mbali na watu wake. 26 Popote mtakapoishi, kamwe msinywe damu ya ndege yeyote wala ya mnyama. 27 Ikiwa mtu yeyote atakunywa damu, mtu huyo lazima akatiliwe mbali na watu wake.’ ”

  29. 1 Kwa hiyo, ndugu zangu, nawasihi kwa rehema zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu na inayompendeza Mungu, hii ndiyo ibada yenu yenye maana. 2 Msifuatishe tena mfano wa ulimwengu huu, bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu. Ndipo mtaweza kuonja na kuhakikisha ni nini mapenzi ya Mungu yaliyo mema, yanayopendeza machoni pake na ukamilifu.

  30. 1 Bwana akamwambia Mose na Aroni katika nchi ya Misri, 2 “Mwezi huu utakuwa mwanzo wa miezi kwenu, yaani mwezi wa kwanza wa mwaka wenu. 3 Iambie jumuiya yote ya Israeli kwamba katika siku ya kumi ya mwezi huu, kila mtu atatwaa mwana-kondoo mmoja kwa ajili ya familia yake, mmoja kwa kila nyumba. 4 Ikiwa nyumba yoyote ina watu wachache wasioweza kumaliza huyo mwana-kondoo mzima, nyumba hiyo itabidi ishirikiane na nyumba ya jirani wa karibu, baada ya kuzingatia idadi ya watu waliomo. Mtaangalia ni kiasi gani cha nyama kitahitajika kulingana na mahitaji ya kila mtu. 5 Wanyama mtakaowachagua, lazima wawe wa kiume wa umri wa mwaka mmoja wasiokuwa na dosari, mwaweza kuwachukua kati ya kondoo au mbuzi. 6 Tunzeni wanyama hao mpaka siku ya kumi na nne ya mwezi, ambapo lazima watu wa jumuiya yote ya Israeli wachinje wanyama hao wakati wa jioni. 7 Ndipo watakapochukua baadhi ya hiyo damu na kuipaka kwenye vizingiti vya juu na miimo ya milango ya nyumba ambamo watakula wana-kondoo hao. 8 Usiku huo huo watakula nyama iliyookwa kwenye moto, pamoja na mboga chungu za majani na mikate isiyotiwa chachu. 9 Msile nyama mbichi wala iliyochemshwa, lakini iwe imeokwa kwenye moto, kichwa, miguu na nyama zake za ndani. 10 Msibakize nyama yoyote mpaka asubuhi; nazo kama zitabakia mpaka asubuhi, lazima mziteketeze kwa moto. 11 Hivi ndivyo mtakavyokula: Mtajifunga mikanda viunoni, mtakuwa mmevaa viatu vyenu miguuni na kushika fimbo zenu mkononi mwenu. Mle kwa haraka; hii ni Pasaka ya Bwana.

    12 “Usiku huo huo nitapita katika nchi yote ya Misri na kumuua kila mzaliwa wa kwanza, wa wanadamu na wa wanyama, nami nitaihukumu miungu yote ya Misri. Mimi ndimi Bwana. 13 Damu itakuwa ishara kwa ajili yenu ya kuonyesha nyumba ambazo mtakuwamo; nami nitakapoiona damu, nitapita juu yenu. Hakuna pigo la uharibifu litakalowagusa ninyi nitakapoipiga Misri.

  31. 11 Bwana akamwambia Mose, 12 “Nimesikia manungʼuniko ya Waisraeli. Waambie, ‘Jioni mtakula nyama, na asubuhi mtashiba mikate. Ndipo mtajua ya kwamba Mimi ndimi Bwana Mungu wenu.’ ”

    13 Jioni ile kware wakaja wakaifunika kambi na asubuhi kulikuwa na tabaka la umande kuzunguka kambi.

  32. 26 “ ‘Msile nyama yoyote yenye damu ndani yake.

    “ ‘Msifanye uaguzi wala uchawi.

  33. 31 “Ninyi mtakuwa watu wangu watakatifu. Kwa hiyo msile nyama ya mnyama aliyeraruliwa na wanyama pori; mtupieni mbwa.

  34. 15 Hata hivyo, mnaweza kuwachinja wanyama wenu katika miji yenu yoyote ile na kula nyama nyingi mpendavyo kama vile mmemchinja paa au kulungu, kulingana na baraka mtakazojaliwa na Bwana Mungu wenu. Watu walio najisi au walio safi wanaweza kula.

  35. 2 Wakati huo, mimi Danieli nikaomboleza kwa majuma matatu. 3 Sikula chakula kizuri; nyama wala divai havikugusa midomo yangu; nami sikujipaka mafuta kamwe mpaka majuma matatu yalipotimia.

  36. 20 Basi akaondoka, akaenda kwa baba yake.

    “Lakini alipokuwa bado yuko mbali, baba yake akamwona, moyo wake ukajawa na huruma. Akamkimbilia mwanawe, akamkumbatia na kumbusu.

    21 “Yule mwana akamwambia baba yake, ‘Baba, nimekosa mbele za Mungu na mbele yako. Sistahili kuitwa mwanao tena.’

    22 “Lakini baba yake akawaambia watumishi, ‘Leteni upesi joho lililo bora sana, tieni pete kidoleni mwake na viatu miguuni mwake. 23 Leteni ndama aliyenona, mkamchinje ili tuwe na karamu, tule na kufurahi. 24 Kwa maana huyu mwanangu alikuwa amekufa na sasa yu hai tena; alikuwa amepotea na sasa amepatikana!’ Nao wakaanza kufanya tafrija.

  37. 26 Yesu akawajibu, “Amin, amin nawaambia, ninyi hamnitafuti kwa kuwa mliona ishara na miujiza, bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba. 27 Msishughulikie chakula kiharibikacho, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele, ambacho Mwana wa Adamu atawapa. Yeye ndiye ambaye Mungu Baba amemtia muhuri.”

    28 Ndipo wakamuuliza, “Tufanye nini ili tupate kuitenda kazi ya Mungu?”

    29 Yesu akawajibu, “Kazi ya Mungu ndiyo hii: Mwaminini yeye aliyetumwa naye.”

    30 Hivyo wakamuuliza, “Utafanya ishara gani ya muujiza, ili tuione tukuamini? Utafanya jambo gani? 31 Baba zetu walikula mana jangwani, kama ilivyoandikwa, ‘Aliwapa mikate kutoka mbinguni ili wale.’ ”

    32 Yesu akawaambia, “Amin, amin nawaambia, si Mose aliyewapa mikate kutoka mbinguni, bali Baba yangu ndiye anawapa mkate wa kweli kutoka mbinguni. 33 Kwa maana mkate wa Mungu ni yule ashukaye kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima.”

    34 Wakamwambia, “Bwana, kuanzia sasa tupatie huo mkate siku zote.”

    35 Yesu akawaambia, “Mimi ndimi mkate wa uzima. Yeye ajaye kwangu, hataona njaa kamwe na yeye aniaminiye, hataona kiu kamwe. 36 Lakini kama nilivyowaambia, mmeniona lakini bado hamwamini. 37 Wale wote anipao Baba watakuja kwangu na yeyote ajaye kwangu, sitamfukuzia nje kamwe. 38 Kwa kuwa nimeshuka kutoka mbinguni si ili kufanya mapenzi yangu, bali mapenzi yake yeye aliyenituma. 39 Haya ndiyo mapenzi yake yeye aliyenituma, kwamba, nisimpoteze hata mmoja wa wale alionipa, bali niwafufue siku ya mwisho. 40 Kwa maana mapenzi ya Baba yangu ni kwamba kila mmoja amtazamaye, Mwana na kumwamini awe na uzima wa milele, nami nitawafufua siku ya mwisho.”

  38. 25 “Kwa hiyo nawaambia, msisumbukie maisha yenu kwamba mtakula nini au mtakunywa nini; au msumbukie miili yenu kwamba mtavaa nini. Je, maisha si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi?

  39. 4 Mara baada ya kupambazuka, Yesu akasimama ufuoni, lakini wanafunzi hawakumtambua kwamba alikuwa Yesu.

    5 Yesu akawaambia, “Wanangu, je, mna samaki wowote?”

    Wakamjibu, “La.”

    6 Akawaambia, “Shusheni nyavu upande wa kuume wa mashua yenu nanyi mtapata samaki.” Wakashusha nyavu na tazama wakapata samaki wengi mno hata wakashindwa kuvutia zile nyavu zilizojaa samaki ndani ya mashua.

    7 Yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu akamwambia Petro, “Huyu ni Bwana!” Simoni Petro aliposikia haya, akajifunga nguo yake kwa kuwa alikuwa uchi, naye akajitosa baharini. 8 Wale wanafunzi wengine wakaja kwa ile mashua huku wakikokota ule wavu uliyojaa samaki, maana hawakuwa mbali na nchi kavu, ilikuwa yapata dhiraa 200 9 Walipofika ufuoni, wakaona moto wa makaa na samaki wakiokwa juu yake na mikate.

    10 Yesu akawaambia, “Leteni baadhi ya hao samaki mliovua sasa hivi.”

    11 Simoni Petro akapanda kwenye mashua na kuukokota ule wavu pwani. Ulikuwa umejaa samaki wakubwa 153. Ingawa samaki walikuwa wengi kiasi hicho, ule wavu haukuchanika. 12 Yesu akawaambia, “Njooni mpate kifungua kinywa.” Hakuna hata mmoja wa wanafunzi aliyethubutu kumuuliza, “Wewe ni nani?” Kwa sababu walijua ya kuwa ni Bwana. 13 Yesu akaja, akachukua ule mkate, akawapa na vivyo hivyo akawagawia pia wale samaki. 14 Hii ilikuwa mara ya tatu Yesu kuwatokea wanafunzi wake baada yake kufufuliwa kutoka kwa wafu.

  40. 25 Lakini kuhusu wale watu wa Mataifa walioamini, tumewaandikia uamuzi wetu: kwamba wajitenge na vyakula vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, au kula nyama ya mnyama aliyenyongwa, na wajiepushe na uasherati.”

  41. 6 Hivyo Abrahamu akaharakisha akaingia hemani kwa Sara, akamwambia, “Chukua vipimo vitatu vya unga laini haraka, ukande na uoke mikate.”

    7 Kisha Abrahamu akakimbia kwenda kwenye kundi, akachagua ndama mzuri, laini na akampa mtumishi, ambaye aliharakisha kumtayarisha. 8 Kisha akaleta jibini, maziwa na nyama ya yule ndama iliyoandaliwa, akaviweka mbele ya wageni. Walipokuwa wakila, alisimama karibu nao chini ya mti.

    9 Wakamuuliza, “Yuko wapi Sara mkeo?”

    Akasema, “Yuko huko, ndani ya hema.”

  42. 1 Jumuiya yote ya Kiisraeli ikaondoka Elimu, wakafika Jangwa la Sini, lililokuwa kati ya Elimu na Sinai, siku ya kumi na tano ya mwezi wa pili baada ya kutoka Misri. 2 Huko jangwani hiyo jumuiya yote wakawanungʼunikia Mose na Aroni. 3 Waisraeli wakawaambia, “Laiti tungelikufa kwa mkono wa Bwana huko Misri! Huko tuliketi tukizunguka masufuria ya nyama na tukala vyakula tulivyovitaka, lakini ninyi mmetuleta huku jangwani ili mpate kuua mkutano huu wote kwa njaa.”

  43. 29 “ ‘Kuhusu wanyama watambaao juu ya ardhi, hawa ni najisi kwenu: kicheche, panya, aina yoyote ya mijusi mikubwa, 30 guruguru, kenge, mijusi ya ukutani, goromoe na kinyonga. 31 Hao wote watambaao juu ya ardhi ni najisi kwenu. Yeyote agusaye mizoga yao atakuwa najisi mpaka jioni.

  44. 27 Leteni sadaka zenu za kuteketezwa juu ya madhabahu ya Bwana Mungu wenu, vyote nyama na damu. Damu ya dhabihu zenu lazima imiminwe kando ya madhabahu ya Bwana Mungu wenu, lakini nyama mnaweza kula.

  45. 33 Kisha mtu mmoja akamwambia Sauli, “Tazama, watu wanatenda dhambi dhidi ya Bwana kwa kula nyama yenye damu.”

    Akasema, “Mmevunja uaminifu. Livingirisheni jiwe kubwa hapa mara moja.” 34 Kisha Sauli akasema, “Nendeni miongoni mwa watu, mwaambie, ‘Kila mmoja wenu aniletee ngʼombe wake na kondoo, mwachinjie hapa na mle. Msitende dhambi dhidi ya Bwana kwa kula nyama ikiwa na damu ndani yake.’ ”

    Hivyo kila mmoja akaleta ngʼombe wake jioni ile na kumchinja hapo.

  46. 1 Hekima amejenga nyumba yake;

    amechonga nguzo zake saba.

    2 Ameandaa nyama na kuchanganya divai yake;

    pia ameandaa meza yake.

    3 Amewatuma watumishi wake wa kike, naye huita

    kutoka mahali pa juu sana pa mji.

    4 Anawaambia wale wasio na akili,

    “Wote ambao ni wajinga na waje hapa!

    5 Njooni, mle chakula changu

    na mnywe divai niliyoichanganya.

    6 Acheni njia zenu za ujinga nanyi mtaishi;

    tembeeni katika njia ya ufahamu.

  47. 6 Juu ya mlima huu Bwana Mwenye Nguvu Zote ataandaa

    karamu ya vinono kwa mataifa yote,

    karamu ya mvinyo wa zamani,

    nyama nzuri sana na divai zilizo bora sana.

  48. 21 “ ‘Hivi ndivyo asemavyo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli: Endeleeni, ongezeni sadaka zenu za kuteketezwa juu ya dhabihu zenu nyingine, mle nyama hiyo wenyewe!

  49. 14 Ndipo nikasema, “Sivyo Bwana Mwenyezi! Kamwe mimi sijajitia unajisi. Tangu ujana wangu hadi sasa sijala kamwe kitu chochote kilichokufa au kilichoraruliwa na wanyama wa mwituni. Hakuna nyama yeyote najisi iliyoingia kinywani mwangu.”