38 Bible Verses About Immigration
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
-
33 “ ‘Wakati mgeni anaishi pamoja nawe katika nchi yako, usimnyanyase. 34 Mgeni anayeishi pamoja nawe ni lazima umtendee kama mmoja wa wazawa wa nchi yako. Mpende kama unavyojipenda mwenyewe, kwa maana ulikuwa mgeni katika nchi ya Misri. Mimi ndimi Bwana Mungu wako.
-
17 Kwa kuwa Bwana Mungu wenu ni Mungu wa miungu na Bwana wa mabwana, Mungu mkuu, mwenye uweza na wa kutisha, ambaye hana upendeleo na hapokei rushwa. 18 Huwapigania yatima na wajane, humpenda mgeni, akimpa chakula na mavazi. 19 Nanyi wapendeni wageni, kwa kuwa ninyi wenyewe mlikuwa wageni huko Misri.
-
22 Wakati huo Abimeleki na Fikoli mkuu wa majeshi yake wakamwambia Abrahamu, “Mungu yu pamoja nawe katika kila kitu unachofanya. 23 Sasa niapie hapa mbele za Mungu kwamba hutanitenda hila mimi, watoto wangu wala wazao wangu. Nitendee mimi na nchi ambayo unaishi kama mgeni wema ule ule ambao nimekutendea.”
24 Abrahamu akasema, “Ninaapa hivyo.”
25 Ndipo Abrahamu akalalamika kwa Abimeleki kuhusu kisima cha maji ambacho watumishi wa Abimeleki walikuwa wamekinyangʼanya. 26 Lakini Abimeleki akasema, “Sijui ni nani ambaye amefanya hili. Hukuniambia, leo tu ndipo ninasikia habari zake.”
27 Hivyo Abrahamu akaleta kondoo na ngʼombe, akampa Abimeleki, nao watu hawa wawili wakafanya mapatano. 28 Abrahamu akatenga kondoo wa kike saba kutoka kwenye kundi, 29 Abimeleki akamuuliza Abrahamu, “Ni nini maana ya hawa kondoo wa kike saba uliowatenga peke yao?”
30 Abrahamu akamjibu, “Upokee hawa kondoo wa kike saba kutoka mkononi mwangu kama ushahidi kuwa nilichimba kisima hiki.”
31 Hivyo mahali pale pakaitwa Beer-Sheba, kwa sababu watu wawili waliapiana hapo.
32 Baada ya mapatano kufanyika huko Beer-Sheba, Abimeleki na Fikoli mkuu wa majeshi yake wakarudi katika nchi ya Wafilisti. 33 Abrahamu akapanda mti wa mkwaju huko Beer-Sheba, na hapo akaliitia jina la Bwana, Mungu wa milele. 34 Naye Abrahamu akakaa katika nchi ya Wafilisti kwa muda mrefu.
-
17 Usipotoshe hukumu ya mgeni au yatima, au kuchukua vazi la mjane kama rehani. 18 Kumbukeni kwamba mlikuwa watumwa huko Misri, naye Bwana Mungu wenu akawakomboa kutoka huko. Hii ndiyo sababu ninawaamuru kutenda hili.
19 Unapovuna shamba lako na ukasahau mganda, usirudi kuuchukua. Acha kwa ajili ya mgeni, yatima na mjane, ili Bwana Mungu wako aweze kukubariki wewe katika kazi zote za mikono yako. 20 Unapovuna zeituni kutoka miti yako, usirudie matawi mara ya pili. Acha kilichobaki kwa ajili ya mgeni, yatima na mjane. 21 Unapochuma zabibu katika shamba lako la mizabibu usirudie tena. Acha zinazobaki kwa ajili ya mgeni, yatima na mjane. 22 Kumbuka kwamba mlikuwa watumwa katika nchi ya Misri. Ndiyo sababu ninawaamuru kufanya hili.
-
5 Kama kweli mkibadili njia zenu na matendo yenu, mkatendeana haki kila mmoja na mwenzake, 6 kama msipomwonea mgeni, yatima wala mjane, na kumwaga damu isiyo na hatia mahali hapa, nanyi kama msipofuata miungu mingine kwa madhara yenu wenyewe, 7 ndipo nitawaacha mkae mahali hapa, katika nchi niliyowapa baba zenu milele na milele.
-
31 “Mwana wa Adamu atakapokuja katika utukufu wake na malaika wote watakatifu pamoja naye, ndipo atakapoketi juu ya kiti cha enzi cha utukufu wake. 32 Mataifa yote watakusanyika mbele zake, naye atawatenga kama mchungaji anavyotenga kondoo na mbuzi. 33 Atawaweka kondoo upande wake wa kuume, na mbuzi upande wake wa kushoto.
34 “Ndipo Mfalme atawaambia wale walioko upande wake wa kuume, ‘Njooni, ninyi mliobarikiwa na Baba yangu; urithini Ufalme ulioandaliwa kwa ajili yenu tangu kuumbwa kwa ulimwengu. 35 Kwa maana nilikuwa na njaa mkanipa chakula, nilikuwa na kiu mkaninywesha, nilikuwa mgeni mkanikaribisha, 36 nilikuwa uchi mkanivika, nilikuwa mgonjwa mkanitunza, nami nilikuwa kifungoni mkaja kunitembelea.’
37 “Ndipo wale wenye haki watakapomjibu, ‘Bwana, ni lini tulikuona ukiwa na njaa tukakulisha, au ukiwa na kiu tukakunywesha? 38 Lini tulikuona ukiwa mgeni tukakukaribisha, au ukiwa uchi tukakuvika? 39 Tena ni lini tulikuona ukiwa mgonjwa tukakutunza, au ukiwa kifungoni tukakutembelea?’
40 “Naye Mfalme atawajibu, ‘Amin nawaambia, kwa jinsi mlivyomtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.’
41 “Kisha atawaambia wale walio upande wake wa kushoto, ‘Ondokeni kwangu, ninyi mliolaaniwa, nendeni kwenye moto wa milele ulioandaliwa kwa ajili ya ibilisi na malaika zake. 42 Kwa maana nilikuwa na njaa hamkunipa chakula, nilikuwa na kiu hamkuninywesha, 43 nilikuwa mgeni nanyi hamkunikaribisha, nilikuwa uchi hamkunivika, nilikuwa mgonjwa hamkunitunza, na nilikuwa gerezani nanyi hamkuja kunitembelea.’
44 “Ndipo wao pia watajibu, ‘Bwana ni lini tulikuona ukiwa na njaa au kiu, au ukiwa mgeni au uchi, au ukiwa mgonjwa na kifungoni na hatukukuhudumia?’
45 “Naye atawajibu, ‘Amin nawaambia, kwa jinsi ambavyo hamkumtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu walio wadogo, hamkunitendea mimi.’
46 “Ndipo hawa watakapoingia kwenye adhabu ya milele, lakini wale wenye haki wataingia katika uzima wa milele.”
-
1 Endeleeni kupendana kama ndugu. 2 Msisahau kuwakaribisha wageni, kwa kuwa kwa kufanya hivyo, watu wengine waliwakaribisha malaika pasipo kujua. 3 Wakumbukeni wale waliofungwa gerezani kana kwamba ninyi mmefungwa pamoja nao. Pia wakumbukeni wale wanaotendewa vibaya, kana kwamba ni ninyi wenyewe mnateswa.
-
21 “Usimtendee mgeni vibaya au kumwonea, kwa kuwa nanyi mlikuwa wageni huko Misri.
22 “Usimdhulumu mjane wala yatima. 23 Kama ukifanya hivyo nao wakinililia, hakika nitasikia kilio chao. 24 Hasira yangu itawaka, nami nitawaua kwa upanga, wake zenu watakuwa wajane na watoto wenu watakuwa yatima.
-
9 “Hivi ndivyo asemavyo Bwana Mwenye Nguvu Zote: ‘Fanyeni hukumu za haki, onyesheni rehema na huruma ninyi kwa ninyi. 10 Msimwonee mjane wala yatima, mgeni wala maskini. Msiwaziane mabaya mioyoni mwenu ninyi kwa ninyi.’
-
5 “Basi nitakuja karibu nanyi ili kuhukumu. Nami nitakuwa mwepesi kushuhudia dhidi ya wachawi, wazinzi, waapao kwa uongo, wanaopunja vibarua malipo yao, wanaowaonea wajane na yatima, na wanaowanyima wageni haki, lakini hawaniogopi mimi,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.
-
9 Lakini ninyi ni taifa teule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu walio milki ya Mungu, mlioitwa ili kutangaza sifa zake yeye aliyewaita kutoka gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu. 10 Mwanzo ninyi mlikuwa si taifa, lakini sasa ninyi ni taifa la Mungu. Mwanzo mlikuwa hamjapata rehema, lakini sasa mmepata rehema.
11 Wapenzi, ninawasihi, mkiwa kama wageni na wapitaji hapa ulimwenguni, epukeni tamaa mbaya za mwili ambazo hupigana vita na roho zenu. 12 Kuweni na mwenendo mzuri mbele ya watu wasiomjua Mungu, ili kama wanawasingizia kuwa watenda mabaya, wayaone matendo yenu mema nao wamtukuze Mungu siku atakapokuja kwetu.
13 Kwa ajili ya Bwana, tiini kila mamlaka iliyowekwa na wanadamu: Kwa mfalme kwani ndiye aliye na mamlaka ya juu zaidi, 14 au kwa maafisa aliowaweka, kwa kuwa mfalme amewatuma ili kuwaadhibu wale wanaokosa, na kuwapongeza wale watendao mema. 15 Kwa maana ni mapenzi ya Mungu kwamba kwa kutenda mema mnyamazishe maneno ya kijinga ya watu wapumbavu. 16 Ishini kama watu huru, lakini msitumie uhuru wenu kama kisingizio cha kutenda uovu, bali ishini kama watumishi wa Mungu. 17 Mheshimuni kila mtu ipasavyo: Wapendeni jamaa ya ndugu waumini, mcheni Mungu, mpeni heshima mfalme.
-
19 “Alaaniwe mtu apotoshaye haki ya mgeni, yatima au mjane.”
Kisha watu wote watasema, “Amen!”
-
9 “Usimwonee mgeni; ninyi wenyewe mnajua jinsi mgeni anavyojisikia, kwa sababu mlikuwa wageni Misri.
-
9 Bwana huwalinda wageni
na kuwategemeza yatima na wajane,
lakini hupinga njia za waovu.
-
48 “Mgeni aishiye miongoni mwenu ambaye anataka kuadhimisha Pasaka ya Bwana ni lazima wanaume wote waliomo nyumbani mwake wawe wametahiriwa, ndipo aweze kushiriki kama mzawa. Mwanaume yeyote asiyetahiriwa haruhusiwi kuila. 49 Sheria iyo hiyo itamuhusu mzawa na mgeni anayeishi miongoni mwenu.”
-
14 Usimwonee mtu maskini na mhitaji ambaye umemwajiri, akiwa ni nduguyo Mwisraeli au mgeni anayeishi katika mojawapo ya miji yenu. 15 Mlipe ujira wake kila siku kabla ya jua kutua, kwa sababu yeye ni maskini na anautegemea ujira huo. La sivyo, anaweza kumlilia Bwana dhidi yako, nawe ukapata hatia ya dhambi.
-
9 “ ‘Wakati uvunapo mavuno ya nchi yako, usivune hadi kwenye mipaka ya shamba lako, wala usikusanye mabaki ya mavuno yako. 10 Usirudi mara ya pili katika shamba lako la mizabibu, wala usiokote zabibu zilizoanguka chini. Ziache kwa ajili ya maskini na mgeni. Mimi ndimi Bwana Mungu wako.
-
22 “ ‘Mnapovuna mavuno ya ardhi yenu, msivune hadi mpakani mwa shamba lenu, au kukusanya masazo ya mavuno yenu. Hayo utayaacha kwa ajili ya maskini na mgeni. Mimi ndimi Bwana Mungu wenu.’ ”
-
1 Bwana akawa amemwambia Abramu, “Ondoka kutoka nchi yako, uache jamii yako na nyumba ya baba yako, uende hadi nchi nitakayokuonyesha.
2 “Mimi nitakufanya taifa kubwa
na nitakubariki,
Nitalikuza jina lako,
nawe utakuwa baraka.
3 Nitawabariki wale wanaokubariki,
na yeyote akulaaniye nitamlaani;
na kupitia kwako mataifa yote duniani
yatabarikiwa.”
4 Hivyo Abramu akaondoka kama Bwana alivyokuwa amemwambia; naye Loti akaondoka pamoja naye. Wakati Abramu alipoitwa aondoke Harani, alikuwa na miaka sabini na mitano.
-
2 ‘Sikia neno la Bwana, ee mfalme wa Yuda, wewe uketiye kwenye kiti cha enzi cha Daudi: wewe, maafisa wako na watu wako mnaopitia malango haya. 3 Hili ndilo Bwana asemalo: Tenda haki na adili. Mwokoe mkononi mwa mdhalimu yeye aliyetekwa nyara. Usimtendee mabaya wala ukatili mgeni, yatima au mjane, wala usimwage damu isiyo na hatia mahali hapa. 4 Kwa kuwa ukiwa mwangalifu kushika maagizo haya, ndipo wafalme watakaokalia kiti cha enzi cha Daudi watakapoingia kupitia malango ya jumba hili la kifalme, wakiwa wamepanda magari na farasi, huku wakifuatana na maafisa wao na watu wao. 5 Lakini kama hutayatii maagizo haya, asema Bwana, ninaapa kwa nafsi yangu kwamba jumba hili litakuwa gofu.’ ”
-
21 “Mtagawanya nchi hii miongoni mwenu kufuatana na makabila ya Israeli. 22 Mtaigawanya kuwa urithi kwa ajili yenu na kwa ajili ya wageni wanaoishi miongoni mwenu na ambao wana watoto. Wao watakuwa kwenu kama wenyeji wazawa wa Israeli, pamoja na ninyi watagawiwa urithi miongoni mwa makabila ya Israeli. 23 Katika kabila lolote mgeni atakapoishi hapo ndipo mtakapompatia urithi wake,” asema Bwana Mwenyezi.
-
10 Basi kulikuwako na njaa katika nchi, naye Abramu akashuka kwenda Misri kukaa huko kwa muda, kwa maana njaa ilikuwa kali.
-
22 Mtakuwa na sheria iyo hiyo kwa mgeni na kwa mzawa. Mimi ndimi Bwana Mungu wenu.’ ”
-
35 “ ‘Ikiwa mmoja wa wazawa wa nchi yako amekuwa maskini, naye akashindwa kujitegemeza mwenyewe katikati yako, msaidie kama vile ambavyo ungelimsaidia mgeni au kama mkazi wa muda, ili aweze kuendelea kuishi katikati yako. 36 Usichukue riba wala faida yoyote kutoka kwake, bali utamwogopa Mungu wako, ili mzawa wa nchi yako aweze kuendelea kuishi katikati yako. 37 Usimkopeshe fedha ili alipe na riba, wala usimuuzie chakula kwa faida.
-
17 Ndugu zangu, kwa pamoja fuateni mfano wangu na kuwatazama wale wanaofuata kielelezo tulichowawekea. 18 Kwa maana, kama nilivyokwisha kuwaambia mara nyingi kabla, nami sasa nasema tena hata kwa machozi, watu wengi wanaishi kama adui wa msalaba wa Kristo. 19 Mwisho wa watu hao ni maangamizi, Mungu wao ni tumbo, na utukufu wao ni aibu, na mawazo yao yamo katika mambo ya dunia. 20 Lakini uenyeji wetu uko mbinguni. Nasi tunamngoja kwa shauku Mwokozi kutoka huko, yaani, Bwana Yesu Kristo, 21 atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, ili upate kufanana na mwili wake wa utukufu, kwa uweza ule ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote chini yake.
-
26 Kutoka kwa mtu mmoja, yeye aliumba mataifa yote ya wanadamu ili waikalie dunia yote, naye akaweka nyakati za kuishi. 27 Mungu alifanya hivyo ili wanadamu wamtafute na huenda wakamfikia ingawa kwa kupapasapapasa ijapokuwa kwa kweli hakai mbali na kila mmoja wetu. 28 ‘Kwa kuwa katika yeye tunaishi, tunatembea na kuwa na uzima wetu.’ Kama baadhi ya watunga mashairi wenu walivyosema, ‘Sisi ni watoto wake.’
-
27 Kwa maana wote mliobatizwa ndani ya Kristo, mmemvaa Kristo. 28 Wala hakuna tena Myahudi au Myunani, mtumwa au mtu huru, mwanaume wala mwanamke, maana nyote mmekuwa wamoja ndani ya Kristo Yesu. 29 Nanyi mkiwa ni mali ya Kristo, basi ninyi ni wa uzao wa Abrahamu na warithi sawasawa na ile ahadi.
-
28 Mwishoni mwa kila mwaka wa tatu, leteni zaka zote za mazao ya miaka ile na uyahifadhi kwenye miji yenu, 29 ili Walawi (ambao hawana mashamba wala urithi wao wenyewe) na wageni, yatima na wajane wanaoishi kwenye miji yenu wapate kuja kula na kushiba, ili Bwana Mungu wenu apate kuwabariki ninyi katika kazi zote za mikono yenu.
-
15 Jumuiya itakuwa na sheria hizo hizo kwenu na kwa mgeni aishiye miongoni mwenu; hii ni amri ya kudumu kwa vizazi vijavyo. Ninyi na mgeni mtakuwa sawa mbele za Bwana: 16 Sheria hizo hizo na masharti hayo hayo hayo, yatawahusu ninyi na mgeni aishiye miongoni mwenu.’ ”
-
27 Wakiisha kuwaleta mitume wakawaamuru kusimama mbele ya baraza ili kuhani mkuu awahoji. 28 “Tuliwaonya kwa nguvu msifundishe kwa jina hili, lakini ninyi mmeijaza Yerusalemu yote mafundisho yenu na tena mmekusudia kuleta damu ya mtu huyu juu yetu.”
29 Petro na wale mitume wengine wakajibu, “Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu. 30 Mungu wa baba zetu alimfufua Yesu kutoka kwa wafu, ambaye ninyi mlimuua kwa kumtundika kwenye msalaba. 31 Mungu alimtukuza, akamweka mkono wake wa kuume kuwa Kiongozi na Mwokozi ili awape Israeli toba na msamaha wa dhambi. 32 Nasi tu mashahidi wa mambo haya, vivyo hivyo na Roho Mtakatifu ambaye Mungu amewapa wale wanaomtii.”
-
1 Yosefu akaenda na kumwambia Farao, “Baba yangu na ndugu zangu wamekuja kutoka nchi ya Kanaani wakiwa na makundi yao ya kondoo, mbuzi na ngʼombe, pamoja na kila kitu walicho nacho, nao sasa wapo huko Gosheni.” 2 Akachagua ndugu zake watano na kuwaonyesha kwa Farao.
3 Farao akawauliza hao ndugu zake, “Kazi yenu ni nini?”
Wakamjibu, “Watumishi wako ni wachunga mifugo, kama vile baba zetu walivyokuwa.” 4 Pia wakamwambia Farao, “Tumekuja kukaa huku kwa muda mfupi, kwa sababu njaa ni kali huko Kanaani, na mifugo ya watumishi wako haina malisho. Kwa hiyo sasa, tafadhali uruhusu watumishi wako wakae huko Gosheni.”
5 Farao akamwambia Yosefu, “Baba yako na ndugu zako wamekuja kwako, 6 nayo nchi ya Misri ipo mbele yako, uwakalishe baba yako na ndugu zako katika sehemu iliyo bora kupita zote katika nchi. Na waishi Gosheni. Kama unamfahamu yeyote miongoni mwao mwenye uwezo maalum, waweke wawe wasimamizi wa mifugo yangu.”
-
14 “ ‘Mgeni anayeishi miongoni mwenu ambaye anataka kuadhimisha Pasaka ya Bwana, lazima afanye hivyo kwa kufuata desturi na masharti. Lazima masharti yawe sawasawa kwa mgeni na mzawa.’ ”
-
15 Miji hii sita itakuwa mahali pa makimbilio kwa ajili ya Waisraeli, wageni na watu wengine wanaoishi katikati yenu, ili kwamba mtu yeyote ambaye ameua mtu mwingine pasipo kukusudia aweze kukimbilia humo.
-
21 Msile kitu chochote mtakachokuta kimekufa. Mnaweza kumpa mgeni yeyote anayeishi katika mojawapo ya miji yenu, naye anaweza kula au mnaweza kumuuzia mtu wa nchi nyingine. Lakini ninyi ni watu watakatifu kwa Bwana Mungu wenu.
Msitokose mwana-mbuzi katika maziwa ya mama yake.
-
3 Usimwache mgeni aambatanaye na Bwana aseme,
“Hakika Bwana atanitenga na watu wake.”
Usimwache towashi yeyote alalamike akisema,
“Mimi ni mti mkavu tu.”
4 Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana:
“Kwa matowashi washikao Sabato zangu,
ambao huchagua kile kinachonipendeza
na kulishika sana agano langu:
5 hao nitawapa ndani ya Hekalu langu na kuta zake
kumbukumbu na jina bora
kuliko kuwa na watoto wa kiume na wa kike:
nitawapa jina lidumulo milele,
ambalo halitakatiliwa mbali.
6 Wageni wanaoambatana na Bwana
ili kumtumikia,
kulipenda jina la Bwana,
na kumwabudu yeye,
wote washikao Sabato bila kuinajisi
na ambao hushika sana agano langu:
7 hawa nitawaleta kwenye mlima wangu mtakatifu
na kuwapa furaha ndani ya nyumba yangu ya sala.
Sadaka zao za kuteketeza na dhabihu zao
zitakubalika juu ya madhabahu yangu;
kwa maana nyumba yangu itaitwa
nyumba ya sala kwa mataifa yote.”
-
6 Nimjie Bwana na kitu gani na kusujudu
mbele za Mungu aliyetukuka?
Je, nije mbele zake na sadaka za kuteketezwa,
nije na ndama za mwaka mmoja?
7 Je, Bwana atafurahishwa na kondoo dume elfu,
au mito elfu kumi ya mafuta?
Je, nimtoe mzaliwa wangu wa kwanza kwa ajili ya kosa langu,
mtoto wangu mwenyewe
kwa ajili ya dhambi ya nafsi yangu?
8 Amekuonyesha yaliyo mema, ee mwanadamu.
Bwana anataka nini kwako?
Ila kutenda kwa haki na kupenda rehema,
na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako.
-
34 Ndipo Petro akafungua kinywa chake akasema, “Mungu hana upendeleo, 35 Lakini katika kila taifa, kila mtu amchaye na kutenda yaliyo haki hukubaliwa naye.
-
13 Watu hawa wote wakafa katika imani bila kuzipokea zile ahadi, lakini waliziona kwa mbali na kuzishangilia. Nao walikubali kwamba walikuwa wageni na wasiokuwa na maskani hapa duniani. 14 Watu wasemao mambo kama haya, wanaonyesha wazi kwamba wanatafuta nchi yao wenyewe. 15 Kwa kweli kama wangekuwa wanafikiri kuhusu nchi waliyoiacha, wangalipata nafasi ya kurudi huko. 16 Lakini badala yake walitamani nchi iliyo bora zaidi, yaani nchi ya mbinguni. Kwa hiyo Mungu haoni aibu kuitwa Mungu wao, kwa kuwa amekwisha kuandaa mji kwa ajili yao.
Shows Read in context, Share and Copy.