73 Bible Verses About Abuse
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
-
19 Ninyi waume, wapendeni wake zenu, wala msiwe na uchungu dhidi yao.
-
4 Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, bali waleeni kwa nidhamu na mafundisho ya Bwana.
-
1 Tuseme nini basi? Je, tuendelee kutenda dhambi ili neema ipate kuongezeka? 2 La hasha! Sisi tulioifia dhambi, tutawezaje kuendelea kuishi tena katika dhambi?
-
17 Msimlipe mtu yeyote ovu kwa ovu. Jitahidini ili mtende yaliyo mema machoni pa watu wote. 18 Kama ikiwezekana, kwa upande wenu kaeni kwa amani na watu wote. 19 Wapendwa, msilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu, maana imeandikwa: “Ni juu yangu kulipiza kisasi, nitalipiza,” asema Bwana. 20 Badala yake:
“Kama adui yako ana njaa, mlishe;
kama ana kiu, mpe kinywaji.
Kwa kufanya hivyo,
unaweka makaa ya moto yanayowaka kichwani pake.”
21 Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema.
-
1 Kwa sababu hii, kwa kuwa tumezungukwa na wingu kubwa namna hii la mashahidi, basi na tuweke kando kila kitu kinachotuzuia na ile dhambi inayotuzinga kwa urahisi, nasi tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa kwa ajili yetu. 2 Basi na tumtazame sana Yesu mwanzilishi na mkamilishaji wa imani yetu, yeye ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake alistahimili msalaba, bila kujali aibu ya huo msalaba, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu.
-
7 Vivyo hivyo ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili, nanyi wapeni heshima mkitambua ya kuwa wao ni wenzi walio dhaifu, na kama warithi pamoja nanyi wa kipawa cha neema cha uzima, ili kusiwepo na chochote cha kuzuia maombi yenu.
8 Hatimaye, ninyi nyote kuweni na nia moja, wenye kuhurumiana, mkipendana kama ndugu, na mwe wasikitivu na wanyenyekevu. 9 Msilipe ovu kwa ovu, au jeuri kwa jeuri, bali barikini, kwa maana hili ndilo mliloitiwa ili mpate kurithi baraka. 10 Kwa maana,
“Yeyote apendaye uzima
na kuona siku njema,
basi auzuie ulimi wake usinene mabaya,
na midomo yake isiseme hila.
11 Mtu huyo lazima aache uovu, akatende mema;
lazima aitafute amani na kuifuatilia sana.
12 Kwa maana macho ya Bwana
huwaelekea wenye haki,
na masikio yake yako makini
kusikiliza maombi yao.
Bali uso wa Bwana uko kinyume
na watendao maovu.”
-
29 Maneno mabaya yasitoke vinywani mwenu, bali yale yafaayo kwa ajili ya kuwajenga wengine kulingana na mahitaji yao, ili yawafae wale wasikiao. 30 Wala msimhuzunishe Roho Mtakatifu wa Mungu, ambaye kwake mlitiwa muhuri kwa ajili ya siku ya ukombozi. 31 Ondoeni kabisa uchungu, ghadhabu, hasira, makelele na masingizio pamoja na kila aina ya uovu. 32 Kuweni wafadhili na wenye kuhurumiana ninyi kwa ninyi, mkisameheana, kama vile naye Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.
-
22 Ninyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana. 23 Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe kama vile Kristo alivyo kichwa cha Kanisa, ambalo ni mwili wake, naye Kristo ni Mwokozi wake. 24 Basi, kama vile Kanisa linavyomtii Kristo, vivyo hivyo na wake nao imewapasa kuwatii waume zao kwa kila jambo.
25 Ninyi waume, wapendeni wake zenu, kama vile Kristo alivyolipenda Kanisa akajitoa kwa ajili yake 26 kusudi alifanye takatifu, akilitakasa kwa kuliosha kwa maji katika Neno lake, 27 apate kujiletea Kanisa tukufu lisilo na doa wala kunyanzi au waa lolote, bali takatifu na lisilo na hatia. 28 Vivyo hivyo imewapasa waume kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe. 29 Hakuna mtu anayeuchukia mwili wake mwenyewe, bali huulisha na kuutunza vizuri, kama Kristo anavyolitunza Kanisa lake. 30 Sisi tu viungo vya mwili wake.
-
21 “Usimtendee mgeni vibaya au kumwonea, kwa kuwa nanyi mlikuwa wageni huko Misri.
22 “Usimdhulumu mjane wala yatima. 23 Kama ukifanya hivyo nao wakinililia, hakika nitasikia kilio chao. 24 Hasira yangu itawaka, nami nitawaua kwa upanga, wake zenu watakuwa wajane na watoto wenu watakuwa yatima.
-
13 Kitu kingine mnachokifanya: Mnaifurikisha madhabahu ya Bwana kwa machozi. Mnalia na kuugua kwa sababu yeye haziangalii tena sadaka zenu wala hazikubali kwa furaha kutoka mikononi mwenu. 14 Mnauliza, “Kwa nini?” Ni kwa sababu Bwana ni shahidi kati yako na mke wa ujana wako, kwa sababu umevunja uaminifu naye, ingawa yeye ni mwenzako, mke wa agano lako la ndoa.
15 Je, Bwana hakuwafanya wao kuwa mmoja? Katika mwili na katika roho wao ni wa Mungu. Kwa nini wawe mmoja? Kwa sababu Mungu alikuwa akitafuta mzao mwenye kumcha Mungu. Kwa hiyo jihadharini wenyewe katika roho zenu, mtu asivunje uaminifu kwa mke wa ujana wake.
16 “Ninachukia kuachana,” asema Bwana, Mungu wa Israeli, “pia nachukia mtu anayejivika jeuri kama vazi,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.
Kwa hiyo jihadharini wenyewe katika roho zenu, wala msije mkavunja uaminifu.
17 Mmemchosha Bwana kwa maneno yenu.
Nanyi mnauliza, “Tumemchosha kwa namna gani?”
Mmemchosha kwa kusema, “Wote watendao mabaya ni wema machoni pa Bwana, naye anapendezwa nao” au “Mungu wa haki yuko wapi?”
-
19 Basi matendo ya mwili ni dhahiri nayo ni haya: Uasherati, uchafu, ufisadi, 20 kuabudu sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, 21 husuda, ulevi, ulafi na mambo mengine yanayofanana na hayo. Nawaonya, kama nilivyokwisha kuwaonya kabla, kwamba watu watendao mambo kama hayo, hawataurithi Ufalme wa Mungu.
22 Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, 23 upole na kiasi. Katika mambo kama haya hakuna sheria.
-
18 Basi je, thawabu yangu ni nini? Thawabu yangu ni hii: Ya kwamba katika kuhubiri Injili niitoe bila gharama, bila kutumia kwa utimilifu uwezo wangu nilio nao katika Injili.
-
20 “Hata hivyo, nina neno dhidi yako: Unamvumilia yule mwanamke Yezebeli ambaye anajiita nabii, lakini anawafundisha na kuwapotosha watumishi wangu ili wafanye uasherati na kula vyakula vilivyotolewa kafara kwa sanamu. 21 Nimempa muda ili atubu kwa ajili ya uasherati wake, lakini hataki. 22 Kwa hiyo nitamtupa kwenye kitanda cha mateso, na nitawafanya hao wanaozini naye kupata mateso makali wasipotubia njia zake.
-
8 “Akaniuliza, ‘Wewe ni nani?’
“Nikamjibu, ‘Mimi ni Mwamaleki.’
9 “Kisha akaniambia, ‘Nikaribie mimi na uniue! Niko katika maumivu makali ya kifo, lakini bado ningali hai.’
10 “Kwa hiyo nikamkaribia nikamuua, kwa sababu nilijua kwamba baada ya kuanguka hangeweza kupona. Nami nikachukua lile taji lililokuwa kichwani mwake na utepe uliokuwa mkononi mwake nami nimevileta hapa kwa bwana wangu.”
-
5 Bwana huwajaribu wenye haki,
lakini waovu na wanaopenda jeuri,
nafsi yake huwachukia.
-
9 Je, hamjui kwamba wasio haki hawataurithi Ufalme wa Mungu? Msidanganyike: Waasherati, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wahanithi, wala walawiti, 10 wala wezi, wala wenye tamaa mbaya, wala walevi, wala wanaodhihaki, wala wanyangʼanyi hawataurithi Ufalme wa Mungu. 11 Baadhi yenu mlikuwa kama hao. Lakini mlioshwa, mlitakaswa, mlihesabiwa haki kwa jina la Bwana Yesu Kristo na katika Roho wa Mungu wetu.
-
1 Basi, kwa kuwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu, Kristo alikoketi mkono wa kuume wa Mungu. 2 Yafikirini mambo yaliyo juu, wala si ya duniani. 3 Kwa maana ninyi mlikufa, nao uhai wenu sasa umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu. 4 Wakati Kristo, aliye uzima wenu, atakapotokea, ndipo nanyi mtakapotokea pamoja naye katika utukufu.
5 Kwa hiyo, ueni kabisa chochote kilicho ndani yenu cha asili ya kidunia: yaani uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya na ulafi, ambayo ndiyo ibada ya sanamu. 6 Kwa sababu ya mambo haya, ghadhabu ya Mungu inakuja. 7 Ninyi pia zamani mlienenda katika mambo haya mlipoishi maisha hayo. 8 Lakini sasa yawekeni mbali nanyi mambo kama haya yote: yaani hasira, ghadhabu, uovu, masingizio na lugha chafu kutoka midomoni mwenu. 9 Msiambiane uongo, kwa maana mmevua kabisa utu wenu wa kale pamoja na matendo yake, 10 nanyi mmevaa utu mpya, unaofanywa upya katika ufahamu sawasawa na mfano wa Muumba wake. 11 Hapa hakuna Myunani wala Myahudi, aliyetahiriwa wala asiyetahiriwa, asiyestaarabika wala aliyestaarabika, mtumwa wala mtu huru, bali Kristo ni yote, na ndani ya wote.
12 Kwa hiyo, kwa kuwa ninyi mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao sana, jivikeni moyo wa huruma, utu wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu. 13 Vumilianeni na kusameheana mtu akiwa na lalamiko lolote dhidi ya mwenzake. Sameheaneni kama vile Bwana alivyowasamehe ninyi.
-
9 Lakini angalieni jinsi mnavyotumia uhuru wenu usije ukawa kikwazo kwao walio dhaifu. 10 Kwa maana kama mtu yeyote mwenye dhamiri dhaifu akiwaona ninyi wenye ujuzi huu mkila katika hekalu la sanamu, je, si atatiwa moyo kula chakula kilichotolewa sadaka kwa sanamu? 11 Kwa njia hiyo, huyo ndugu mwenye dhamiri dhaifu, ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake, ataangamia kwa sababu ya ujuzi wenu. 12 Mnapotenda dhambi dhidi ya ndugu zenu kwa njia hii na kujeruhi dhamiri zao zilizo dhaifu, mnamkosea Kristo.
-
34 Yesu akajibu, “Amin, amin nawaambia, kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi. 35 Mtumwa hakai nyumbani anakotumika siku zote, lakini mwana hukaa nyumbani daima. 36 Hivyo Mwana akiwaweka huru mtakuwa huru kweli kweli.
-
13 Lakini wengine wakawadhihaki wakasema, “Hawa wamelewa divai!”
-
12 Kwa hiyo, msiruhusu dhambi itawale ndani ya miili yenu, ipatikanayo na kufa, ili kuwafanya mzitii tamaa mbaya.
-
15 Ni nini basi? Je, tutende dhambi kwa kuwa hatuko chini ya sheria bali chini ya neema? La, hasha!
-
19 Je, hamjui ya kwamba miili yenu ni hekalu la Roho Mtakatifu akaaye ndani yenu, ambaye mmepewa na Mungu? Ninyi si mali yenu wenyewe, 20 kwa maana mmenunuliwa kwa gharama. Kwa hiyo mtukuzeni Mungu katika miili yenu.
-
15 “Sisi wenyewe ni Wayahudi kwa kuzaliwa na si watu wenye dhambi kama watu wa Mataifa, 16 bado tunajua ya kwamba mtu hahesabiwi haki kwa matendo ya sheria bali kwa njia ya imani katika Yesu Kristo. Hivyo sisi pia, tumemwamini Kristo Yesu ili tupate kuhesabiwa haki kwa njia ya imani katika Kristo, wala si kwa matendo ya sheria, kwa sababu kwa kushika sheria hakuna hata mtu mmoja atakayehesabiwa haki.
17 “Lakini tukitafuta kuhesabiwa haki katika Kristo, inakuwa dhahiri kwamba sisi ni wenye dhambi. Je, ina maana kwamba Kristo amekuwa mtumishi wa dhambi? La hasha! 18 Lakini ikiwa mimi ninajenga tena kile ambacho nimekwisha kukibomoa, basi ninaonyesha kwamba mimi ni mkosaji. 19 Kwa maana mimi kwa njia ya sheria, nimeifia sheria ili nipate kuishi kwa ajili ya Mungu. 20 Nimesulubiwa pamoja na Kristo, wala si mimi tena ninayeishi, bali Kristo ndiye aishiye ndani yangu. Uhai nilio nao sasa katika mwili, ninaishi kwa imani ya Mwana wa Mungu, aliyenipenda na kujitoa kwa ajili yangu. 21 Siibatilishi neema ya Mungu, kwa maana kama haki ingeweza kupatikana kwa njia ya sheria, basi Kristo alikufa bure!”
-
13 Ndugu zangu, ninyi mliitwa ili mwe huru, hivyo msitumie uhuru wenu kama fursa ya kufuata tamaa za mwili, bali tumikianeni ninyi kwa ninyi kwa upendo.
-
9 Nanyi mabwana, watendeeni watumwa wenu kwa jinsi iyo hiyo. Msiwatishe, kwa kuwa mnajua ya kwamba yeye aliye Bwana wenu na Bwana wao yuko mbinguni, naye hana upendeleo.
-
16 Ishini kama watu huru, lakini msitumie uhuru wenu kama kisingizio cha kutenda uovu, bali ishini kama watumishi wa Mungu.
-
6 Abramu akamwambia, “Mtumishi wako yuko mikononi mwako. Mtendee lolote unalofikiri ni bora zaidi.” Ndipo Sarai akamtesa Hagari, hivyo akamtoroka.
-
25 Lakini Yesu akawaita wote pamoja na kuwaambia, “Mnafahamu kuwa watawala wa watu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, nao wenye vyeo huonyesha mamlaka yao. 26 Isiwe hivyo kwenu. Badala yake, yeyote anayetaka kuwa mkuu miongoni mwenu hana budi kuwa mtumishi wenu, 27 naye anayetaka kuwa wa kwanza miongoni mwenu hana budi kuwa mtumwa wenu: 28 kama vile ambavyo Mwana wa Adamu hakuja ili kutumikiwa, bali kutumika na kuutoa uhai wake uwe fidia kwa ajili ya wengi.”
-
41 Wale wanafunzi wengine kumi waliposikia hayo, wakaanza kuwakasirikia Yakobo na Yohana. 42 Lakini Yesu akawaita wote pamoja na kuwaambia, “Mnafahamu kuwa wale wanaodhaniwa kuwa watawala wa watu wa Mataifa huwatawala watu kwa nguvu, nao wenye vyeo huonyesha mamlaka yao. 43 Lakini isiwe hivyo kwenu. Badala yake, yeyote anayetaka kuwa mkuu miongoni mwenu hana budi kuwa mtumishi wenu, 44 na yeyote anayetaka kuwa wa kwanza, hana budi kuwa mtumwa wa wote. 45 Kwa kuwa hata Mwana wa Adamu hakuja ili kutumikiwa, bali kutumika na kuutoa uhai wake uwe fidia kwa ajili ya wengi.”
-
27 “Lakini nawaambia ninyi mnaonisikia: Wapendeni adui zenu. Watendeeni mema wanaowachukia. 28 Wabarikini wale wanaowalaani, waombeeni wale wanaowatendea mabaya. 29 Kama mtu akikupiga shavu moja, mgeuzie na la pili pia. Mtu akikunyangʼanya koti lako, usimzuie kuchukua joho pia. 30 Mpe kila akuombaye, na kama mtu akichukua mali yako usitake akurudishie.
-
6 Mtu yeyote na asiwadanganye kwa maneno matupu, kwa kuwa hasira ya Mungu huwaka kwa sababu ya mambo kama haya juu ya wale wasiomtii.
-
4 Kila mtu atendaye dhambi afanya uasi, kwa kuwa dhambi ni uasi.
-
2 Kutoka tunda la midomo yake mtu hufurahia mambo mema,
bali wasio waaminifu wanatamani sana jeuri.
-
1 Ndugu zangu, msiwe walimu wengi, kwa maana mnafahamu kwamba sisi tufundishao tutahukumiwa vikali zaidi. 2 Sisi sote tunajikwaa katika mambo mengi. Ikiwa mtu yeyote hakosei kamwe katika yale anayosema, yeye ni mkamilifu, naye anaweza kuuzuia pia na mwili wake wote.
3 Tunapotia lijamu kwenye vinywa vya farasi ili kuwafanya watutii, tunaweza kuigeuza miili yao yote. 4 Au angalia pia meli, ingawa ni kubwa sana, nazo huchukuliwa na upepo mkali, lakini hugeuzwa kwa usukani mdogo sana, kokote anakotaka nahodha. 5 Vivyo hivyo ulimi ni kiungo kidogo sana katika mwili, lakini hujivuna majivuno makuu. Fikirini jinsi moto mdogo unavyoweza kuteketeza msitu mkubwa! 6 Ulimi pia ni moto, ndio ulimwengu wa uovu kati ya viungo vya mwili. Ulimi huutia mwili wote wa mtu unajisi na kuuwasha moto mfumo mzima wa maisha yake, nao wenyewe huchomwa moto wa jehanamu.
7 Kwa maana kila aina ya wanyama, ndege, wanyama watambaao na viumbe vya baharini vinafugika na vimefugwa na binadamu, 8 lakini hakuna mtu awezaye kuufuga ulimi. Ni uovu usiotulia, umejaa sumu iletayo mauti.
9 Kwa ulimi tunamhimidi Bwana, yaani Baba yetu, na kwa huo twawalaani watu walioumbwa kwa mfano wa Mungu. 10 Katika kinywa kile kile hutoka baraka na laana. Ndugu zangu, haistahili kuwa hivyo. 11 Je, chemchemi yaweza kutoa katika tundu moja maji matamu na maji ya chumvi? 12 Je, ndugu zangu, mtini waweza kuzaa zeituni, au mzabibu kuzaa tini? Wala chemchemi ya maji ya chumvi haiwezi kutoa maji matamu.
-
2 Bwana hujenga Yerusalemu,
huwakusanya Israeli walio uhamishoni.
3 Anawaponya waliovunjika mioyo
na kuvifunga vidonda vyao.
4 Huzihesabu nyota
na huipa kila moja jina lake.
5 Bwana wetu ni mkuu na mwenye uwezo mwingi,
ufahamu wake hauna kikomo.
6 Bwana huwahifadhi wanyenyekevu
lakini huwashusha waovu mpaka mavumbini.
-
31 Usimwonee wivu mtu mwenye jeuri
wala kuchagua njia yake iwayo yote,
-
22 Usiwadhulumu maskini kwa sababu ni maskini,
wala kumdhulumu mhitaji mahakamani,
23 kwa sababu Bwana atalichukua shauri lao
naye atawateka wao waliowateka.
-
17 “Lakini macho yako na moyo wako vimeelekezwa tu
katika mapato ya udhalimu,
kwa kumwaga damu isiyo na hatia,
kwa uonevu na ukatili.”
-
2 “Mwanadamu, tabiri juu ya wachungaji wa Israeli, tabiri na uwaambie: ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Ole wa wachungaji wa Israeli ambao hujitunza wenyewe tu! Je, haiwapasi wachungaji kutunza kundi la kondoo? 3 Mnakula mafuta ya wanyama, mnavaa mavazi ya sufu na kuchinja kondoo walionona, lakini hamlitunzi kundi. 4 Hamkuwatia nguvu walio dhaifu wala hamkuwaganga wenye maradhi wala kuwafunga waliojeruhiwa. Hamkuwarudisha waliotangatanga wala kuwatafuta wale waliopotea. Badala yake mmewatawala kwa ukali na kwa ukatili. 5 Hivyo walitawanyika kwa sababu hapakuwepo mchungaji, nao walipotawanyika, wakawa chakula cha wanyama wa mwitu wote. 6 Kondoo wangu walitawanyika, wakatangatanga kwenye milima yote na kwenye kila kilima kirefu. Kondoo wangu walitawanyika juu ya uso wa dunia yote bila kuwa na yeyote wa kuwaulizia wala wa kuwatafuta.
-
4 Upendo huvumilia, upendo hufadhili, upendo hauoni wivu, hauna majivuno, hauna kiburi. 5 Haukosi kuwa na adabu, hautafuti mambo yake, haukasiriki upesi, hauweki kumbukumbu ya mabaya. 6 Upendo haufurahii mabaya bali hufurahi pamoja na kweli. 7 Upendo huvumilia yote, huamini yote, hutumaini yote, hustahimili yote.
-
1 Ndugu zangu, ikiwa mtu ameghafilika akatenda dhambi, basi ninyi mlio wa rohoni, mrejesheni upya mtu huyo kwa roho ya upole. Lakini jihadharini, ili ninyi wenyewe msije mkajaribiwa.
-
4 Wao hushangaa kwamba ninyi hamjiingizi pamoja nao katika huo wingi wa maisha ya ufisadi, nao huwatukana ninyi.
-
7 Wapendwa, tupendane, kwa kuwa pendo latoka kwa Mungu. Kila apendaye amezaliwa na Mungu, naye anamjua Mungu. 8 Yeye asiyependa hamjui Mungu, kwa sababu Mungu ni pendo.
-
26 “Ikiwa mtu atampiga mtumwa mwanaume au mwanamke kwenye jicho na kuliharibu, ni lazima amwache huru yule mtumwa kama fidia ya hilo jicho. 27 Kama akimvunja jino mtumwa wa kiume au wa kike, ni lazima amwache huru huyo mtumwa kwa kufidia hilo jino.
-
43 Usiwatawale kwa ukatili, lakini utamcha Mungu wako.
-
14 Usimwonee mtu maskini na mhitaji ambaye umemwajiri, akiwa ni nduguyo Mwisraeli au mgeni anayeishi katika mojawapo ya miji yenu.
-
9 Bwana ni kimbilio la watu wanaoonewa,
ni ngome imara wakati wa shida.
-
12 Kwa maana atamwokoa mhitaji anayemlilia,
aliyeonewa asiye na wa kumsaidia.
13 Atawahurumia wanyonge na wahitaji
na kuwaokoa wahitaji kutoka mauti.
14 Atawaokoa kutoka uonevu na ukatili,
kwani damu yao ni ya thamani machoni pake.
-
8 Hudhihaki na kusema kwa ukorofi,
katika majivuno yao wanatishia kutesa.
-
6 Bwana hutenda haki,
naye huwapa hukumu ya haki wote wanaoonewa.
-
134 Niokoe na uonevu wa wanadamu,
ili niweze kutii mausia yako.
-
24 Usifanye urafiki na mtu mwenye hasira ya haraka,
usishirikiane na yule aliye mwepesi kukasirika,
25 la sivyo utajifunza njia zake
na kujiingiza mwenyewe kwenye mtego.
-
29 Watu wa nchi wanatoza kwa nguvu na kufanya unyangʼanyi, wanawatenda jeuri maskini na wahitaji na kuwaonea wageni, wakiwanyima haki.
-
10 Msimwonee mjane wala yatima, mgeni wala maskini. Msiwaziane mabaya mioyoni mwenu ninyi kwa ninyi.’
-
11 “Heri ninyi watu watakapowashutumu, na kuwatesa na kunena dhidi yenu mabaya ya aina zote kwa uongo kwa ajili yangu.
-
16 Je, hamjui kwamba mnapojitoa kwa mtu yeyote kama watumwa watiifu, ninyi ni watumwa wa yule mnayemtii, aidha watumwa wa dhambi, ambayo matokeo yake ni mauti, au watumwa wa utii ambao matokeo yake ni haki? 17 Lakini Mungu ashukuriwe kwa kuwa ninyi ambao kwanza mlikuwa watumwa wa dhambi, mmekuwa watii kutoka moyoni kwa mafundisho mliyopewa. 18 Nanyi, mkiisha kuwekwa huru mbali na dhambi, mmekuwa watumwa wa haki.
-
1 Kwa hiyo, sasa hakuna hukumu ya adhabu kwa wale walio ndani ya Kristo Yesu, wale ambao hawaenendi kwa kuufuata mwili bali kwa kufuata Roho.
-
1 Kristo alitupa uhuru, akataka tubaki huru. Hivyo simameni imara wala msikubali tena kulemewa na kongwa la utumwa.
-
26 Mkikasirika, msitende dhambi, wala jua lisichwe mkiwa bado mmekasirika,
-
19 Ndugu zangu wapendwa, fahamuni jambo hili: Kila mtu awe mwepesi wa kusikiliza, lakini asiwe mwepesi wa kusema wala wa kukasirika. 20 Kwa maana hasira ya mwanadamu haitendi haki ya Mungu. 21 Kwa hiyo, ondoleeni mbali uchafu wote na uovu ambao umezidi kuwa mwingi, mkalipokee kwa unyenyekevu lile Neno lililopandwa ndani yenu ambalo laweza kuokoa nafsi zenu.
-
23 Yeye alipotukanwa, hakurudisha matukano; alipoteswa, hakutishia, bali alijikabidhi kwa yeye ahukumuye kwa haki.
-
28 Wewe huwaokoa wanyenyekevu,
lakini macho yako ni juu ya wenye kiburi
ili uwashushe.
-
18 Bwana yu karibu na waliovunjika moyo,
na huwaokoa waliopondeka roho.
-
7 Kwa maana nimestahimili dharau kwa ajili yako,
aibu imefunika uso wangu.
8 Nimekuwa mgeni kwa ndugu zangu,
mgeni kwa wana wa mama yangu mwenyewe.
9 Kwa kuwa wivu wa nyumba yako unanila,
matukano ya wale wanaokutukana yameniangukia.
10 Ninapolia na kufunga,
lazima nivumilie matusi.
11 Ninapovaa nguo ya gunia,
watu hunidharau.
12 Wale wanaoketi mlangoni wananisimanga,
nimekuwa wimbo wa walevi.
-
12 Najua kwamba Bwana huwapatia maskini haki,
na kuitegemeza njia ya mhitaji.
-
11 Kinywa cha mwenye haki ni chemchemi ya uzima,
lakini jeuri hufunika kinywa cha mwovu.
-
19 Mtu mwenye kukasirika haraka ni lazima atapata adhabu yake,
kama utamwokoa, itakubidi kufanya hivyo tena.
-
34 “Amri mpya nawapa: Mpendane kama mimi nilivyowapenda ninyi, vivyo hivyo nanyi mpendane. 35 Kama mkipendana ninyi kwa ninyi, kwa njia hii, watu wote watajua kuwa ninyi ni wanafunzi wangu.”
-
33 Ni nani atakayewashtaki wale ambao Mungu amewateua? Ni Mungu mwenyewe ndiye mwenye kuwahesabia haki. 34 Ni nani basi atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu aliyekufa, naam, zaidi ya hayo, aliyefufuliwa kutoka kwa wafu, yuko mkono wa kuume wa Mungu, naye pia anatuombea. 35 Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je, ni shida au taabu au mateso au njaa au uchi au hatari au upanga? 36 Kama ilivyoandikwa:
“Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa;
tumehesabiwa kama kondoo wa kuchinjwa.”
37 Lakini katika mambo haya yote tunashinda, naam na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. 38 Kwa maana nimekwisha kujua kwa hakika ya kuwa sio mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuja, wala wenye uwezo, 39 wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kingine chochote zitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu, Bwana wetu.
-
1 Sisi tulio na nguvu, hatuna budi kuchukuliana na kushindwa kwa wale walio dhaifu wala si kujipendeza nafsi zetu wenyewe. 2 Kila mmoja wetu inampasa kumpendeza jirani yake kwa mambo mema, ili kumjenga katika imani. 3 Kwa maana hata Kristo hakujipendeza mwenyewe, bali kama ilivyoandikwa: “Matukano yao wale wanaokutukana wewe yalinipata mimi.”
-
26 Kama mtu akidhani ya kuwa anayo dini lakini hauzuii ulimi wake kwa hatamu, hujidanganya moyoni mwake, wala dini yake mtu huyo haifai kitu.
-
3 Basi katika hili twajua ya kuwa tumemjua, tukizishika amri zake. 4 Mtu yeyote asemaye kuwa, “Ninamjua,” lakini hazishiki amri zake, ni mwongo, wala ndani ya mtu huyo hamna kweli.
Shows Read in context, Share and Copy.