78 Bible Verses About Helping the Poor and Needy

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Helping the Poor and Needy
  1. 31 Yeye amwoneaye maskini huonyesha dharau kwa Muumba wao,

    bali yeyote anayemhurumia mhitaji humheshimu Mungu.

  2. 17 Yeye amhurumiaye maskini humkopesha Bwana,

    naye atamtuza kwa aliyotenda.

  3. 34 “Ndipo Mfalme atawaambia wale walioko upande wake wa kuume, ‘Njooni, ninyi mliobarikiwa na Baba yangu; urithini Ufalme ulioandaliwa kwa ajili yenu tangu kuumbwa kwa ulimwengu. 35 Kwa maana nilikuwa na njaa mkanipa chakula, nilikuwa na kiu mkaninywesha, nilikuwa mgeni mkanikaribisha, 36 nilikuwa uchi mkanivika, nilikuwa mgonjwa mkanitunza, nami nilikuwa kifungoni mkaja kunitembelea.’

    37 “Ndipo wale wenye haki watakapomjibu, ‘Bwana, ni lini tulikuona ukiwa na njaa tukakulisha, au ukiwa na kiu tukakunywesha? 38 Lini tulikuona ukiwa mgeni tukakukaribisha, au ukiwa uchi tukakuvika? 39 Tena ni lini tulikuona ukiwa mgonjwa tukakutunza, au ukiwa kifungoni tukakutembelea?’

    40 “Naye Mfalme atawajibu, ‘Amin nawaambia, kwa jinsi mlivyomtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.’

    41 “Kisha atawaambia wale walio upande wake wa kushoto, ‘Ondokeni kwangu, ninyi mliolaaniwa, nendeni kwenye moto wa milele ulioandaliwa kwa ajili ya ibilisi na malaika zake. 42 Kwa maana nilikuwa na njaa hamkunipa chakula, nilikuwa na kiu hamkuninywesha, 43 nilikuwa mgeni nanyi hamkunikaribisha, nilikuwa uchi hamkunivika, nilikuwa mgonjwa hamkunitunza, na nilikuwa gerezani nanyi hamkuja kunitembelea.’

    44 “Ndipo wao pia watajibu, ‘Bwana ni lini tulikuona ukiwa na njaa au kiu, au ukiwa mgeni au uchi, au ukiwa mgonjwa na kifungoni na hatukukuhudumia?’

    45 “Naye atawajibu, ‘Amin nawaambia, kwa jinsi ambavyo hamkumtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu walio wadogo, hamkunitendea mimi.’

    46 “Ndipo hawa watakapoingia kwenye adhabu ya milele, lakini wale wenye haki wataingia katika uzima wa milele.”

  4. 12 Kisha Yesu akamwambia yule aliyewaalika, “Uandaapo karamu ya chakula cha mchana au cha jioni, usialike rafiki zako au ndugu zako au jamaa zako au majirani zako walio matajiri tu. Ukifanya hivyo, wao nao wanaweza kukualika kwao, nawe ukawa umelipwa kile ulichofanya na kupata thawabu yako. 13 Bali ufanyapo karamu, waalike maskini, vilema na vipofu, 14 nawe utabarikiwa kwa sababu hawa hawana uwezo wa kukulipa. Mungu atakulipa wakati wa ufufuo wa wenye haki.”

  5. 9 “ ‘Wakati uvunapo mavuno ya nchi yako, usivune hadi kwenye mipaka ya shamba lako, wala usikusanye mabaki ya mavuno yako. 10 Usirudi mara ya pili katika shamba lako la mizabibu, wala usiokote zabibu zilizoanguka chini. Ziache kwa ajili ya maskini na mgeni. Mimi ndimi Bwana Mungu wako.

  6. 9 Mtu mkarimu yeye mwenyewe atabarikiwa

    kwa kuwa hushiriki chakula chake na maskini.

  7. 16 Kwa namna hii twaweza kulijua pendo la Mungu: Kwa sababu Yesu Kristo aliutoa uhai wake kwa ajili yetu. Nasi imetupasa kuutoa uhai kwa ajili ya hao ndugu. 17 Ikiwa mtu anavyo vitu vya ulimwengu huu na akamwona ndugu yake ni mhitaji lakini asimhurumie, upendo wa Mungu wakaaje ndani ya mtu huyo? 18 Watoto wapendwa, tusipende kwa maneno au kwa ulimi bali kwa tendo na kweli. 19 Basi hivi ndivyo tutakavyoweza kujua ya kuwa sisi tu wa kweli na hivyo twaithibitisha mioyo yetu mbele za Mungu

  8. 9 Basi, Yakobo, Kefa na Yohana, walioonekana kama nguzo za kanisa, walitupa mkono wa shirika, mimi na Barnaba walipotambua ile neema niliyopewa. Wakakubali kwamba sisi twende kwa watu wa Mataifa na wao waende kwa Wayahudi. 10 Walichotuomba ni kwamba tuendelee kuwakumbuka maskini, jambo ambalo ndilo nililokuwa na shauku ya kulifanya.

  9. 13 Mtu akiziba masikio asisikie kilio cha maskini,

    yeye pia atalia, wala hatajibiwa.

  10. 27 Yeye ampaye maskini

    hatapungukiwa na kitu chochote,

    bali yeye awafumbiaye maskini macho

    hupata laana nyingi.

  11. 35 “ ‘Ikiwa mmoja wa wazawa wa nchi yako amekuwa maskini, naye akashindwa kujitegemeza mwenyewe katikati yako, msaidie kama vile ambavyo ungelimsaidia mgeni au kama mkazi wa muda, ili aweze kuendelea kuishi katikati yako. 36 Usichukue riba wala faida yoyote kutoka kwake, bali utamwogopa Mungu wako, ili mzawa wa nchi yako aweze kuendelea kuishi katikati yako. 37 Usimkopeshe fedha ili alipe na riba, wala usimuuzie chakula kwa faida. 38 Mimi ndimi Bwana Mungu wako, niliyekuleta kutoka nchi ya Misri nikupe nchi ya Kanaani, nami niwe Mungu wako.

    39 “ ‘Ikiwa mmoja wa wazawa wa nchi yako amekuwa maskini katikati yako, naye akajiuza kwako, usimfanye atumike kama mtumwa. 40 Atatendewa kama mfanyakazi aliyeajiriwa, au kama mkazi wa muda katikati yako, naye atatumika mpaka Mwaka wa Yubile. 41 Ndipo yeye na watoto wake wataachiwa, naye atarudi kwa watu wa ukoo wake, na kwenye mali ya baba zake. 42 Kwa sababu Waisraeli ni watumishi wangu niliowaleta kutoka nchi ya Misri, kamwe wasiuzwe kama watumwa.

  12. 21 Yeye anayemdharau jirani yake hutenda dhambi,

    bali amebarikiwa yeye aliye na huruma kwa mhitaji.

  13. 8 “Sema kwa ajili ya wale wasioweza kujisemea,

    kwa ajili ya haki za wote walioachwa ukiwa.

    9 Sema na uamue kwa haki,

    tetea haki za maskini na wahitaji.”

  14. 7 Yohana akauambia ule umati wa watu uliokuwa unakuja ili kubatizwa naye, “Ninyi watoto wa nyoka! Ni nani aliyewaonya kuikimbia ghadhabu inayokuja? 8 Basi zaeni matunda yastahiliyo toba. Wala msianze kusema mioyoni mwenu kuwa, ‘Sisi tunaye Abrahamu, baba yetu.’ Kwa maana nawaambia kuwa Mungu anaweza kumwinulia Abrahamu watoto kutoka mawe haya. 9 Hata sasa shoka limeshawekwa tayari kwenye shina la kila mti. Basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni.”

    10 Ule umati wa watu ukamuuliza, “Inatupasa tufanyeje basi?”

    11 Yohana akawaambia, “Aliye na kanzu mbili amgawie asiye nayo, naye aliye na chakula na afanye vivyo hivyo.”

  15. 32 “Msiogope enyi kundi dogo, kwa maana Baba yenu ameona vyema kuwapa ninyi Ufalme. 33 Uzeni mali zenu mkawape maskini. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, mkajiwekee hazina mbinguni isiyokwisha, mahali ambapo mwizi hakaribii wala nondo haharibu. 34 Kwa sababu mahali hazina yako ilipo, hapo ndipo moyo wako utakapokuwa pia.

  16. 16 Mtu mmoja akamjia Yesu na kumuuliza, “Mwalimu mwema, nifanye jambo gani jema ili nipate uzima wa milele?”

    17 Yesu akamjibu, “Mbona unaniuliza habari ya mema? Aliye mwema ni Mmoja tu. Lakini ukitaka kuingia uzimani, zitii amri.”

    18 Yule mtu akamuuliza, “Amri zipi?”

    Yesu akamjibu, “Usiue, usizini, usiibe, usishuhudie uongo, 19 waheshimu baba yako na mama yako, na umpende jirani yako kama nafsi yako.”

    20 Yule kijana akasema, “Hizi zote nimezishika. Je, bado nimepungukiwa na nini?”

    21 Yesu akamwambia, “Kama ukitaka kuwa mkamilifu, nenda, ukauze vitu vyote ulivyo navyo, na hizo fedha uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.”

    22 Yule kijana aliposikia hayo, akaenda zake kwa huzuni, kwa sababu alikuwa na mali nyingi.

    23 Ndipo Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Amin, nawaambia, itakuwa vigumu kwa mtu tajiri kuingia katika Ufalme wa Mbinguni. 24 Tena nawaambia, ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita kwenye tundu la sindano kuliko mtu tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu.”

    25 Wanafunzi wake waliposikia haya, walishangaa sana na kuuliza, “Ni nani basi awezaye kuokoka?”

    26 Lakini Yesu akawatazama, akawaambia, “Kwa mwanadamu jambo hili haliwezekani, lakini mambo yote yanawezekana kwa Mungu.”

    27 Ndipo Petro akamjibu, “Tazama, sisi tumeacha kila kitu na kukufuata! Tutapata nini basi?”

    28 Yesu akawaambia, “Amin, nawaambia, wakati wa kufanywa upya vitu vyote, Mwana wa Adamu atakapoketi kwenye kiti chake kitukufu cha enzi, ninyi mlionifuata pia mtaketi katika viti vya enzi kumi na viwili, mkiyahukumu makabila kumi na mawili ya Israeli. 29 Kila mtu aliyeacha nyumba, au ndugu zake wa kiume au wa kike, baba au mama, watoto au mashamba kwa ajili yangu, atapokea mara mia zaidi ya hayo, na ataurithi uzima wa milele. 30 Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, na walio wa mwisho watakuwa wa kwanza.

  17. 1 Ndugu zangu, kama waaminio katika imani ya Bwana wetu Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, msiwe na upendeleo kwa watu. 2 Kwa maana kama akija mtu katika kusanyiko lenu akiwa amevaa pete ya dhahabu na mavazi mazuri, pia akaingia mtu maskini mwenye mavazi yaliyochakaa, 3 nanyi mkampa heshima yule aliyevaa mavazi mazuri na kumwambia, “Keti hapa mahali pazuri,” lakini yule maskini mkamwambia, “Wewe simama pale,” au “Keti hapa sakafuni karibu na miguu yangu,” 4 je, hamjawabagua na kuwa mahakimu mioyoni mwenu mkihukumu kwa mawazo yenu maovu?

    5 Ndugu zangu, sikilizeni: Je, Mungu hakuwachagua wale walio maskini machoni pa ulimwengu kuwa matajiri katika imani na kuurithi Ufalme aliowaahidi wale wampendao? 6 Lakini ninyi mmemdharau yule aliye maskini. Je, hao matajiri si ndio wanaowadhulumu na kuwaburuta mahakamani? 7 Je, si wao wanaolikufuru Jina lile lililo bora sana mliloitiwa?

    8 Kama kweli mnaitimiza ile sheria ya kifalme inayopatikana katika Maandiko isemayo, “Mpende jirani yako kama unavyoipenda nafsi yako,” mnafanya vyema. 9 Lakini kama mnakuwa na upendeleo kwa watu, mnatenda dhambi, na sheria inawahukumu kuwa ninyi ni wakosaji.

  18. 1 “Angalieni msitende wema wenu mbele ya watu ili wawaone. Kwa maana mkifanya hivyo, hamna thawabu kutoka kwa Baba yenu aliye mbinguni.

    2 “Hivyo mnapowapa wahitaji, msipige panda mbele yenu kama wafanyavyo wanafiki katika masinagogi na mitaani, ili wasifiwe na watu. Amin nawaambia wao wamekwisha kupokea thawabu yao. 3 Lakini ninyi mtoapo sadaka, fanyeni kwa siri, hata mkono wako wa kushoto usijue mkono wako wa kuume unachofanya, 4 ili sadaka yako iwe ni siri. Ndipo Baba yako wa mbinguni, yeye aonaye sirini atakupa thawabu kwa wazi.

  19. 26 Kama mtu akidhani ya kuwa anayo dini lakini hauzuii ulimi wake kwa hatamu, hujidanganya moyoni mwake, wala dini yake mtu huyo haifai kitu. 27 Dini iliyo safi, isiyo na uchafu, inayokubalika mbele za Mungu Baba yetu, ndiyo hii: Kuwasaidia yatima na wajane katika dhiki zao na kujilinda usitiwe madoa na dunia.

  20. 7 Ikiwa kuna mtu maskini miongoni mwa ndugu zenu, katika mji wowote wa hiyo nchi ambayo Bwana Mungu wenu anawapa, msiwe na moyo mgumu wala usimfumbie mkono ndugu yako aliye maskini. 8 Afadhali fungua mikono yako na umkopeshe kwa hiari chochote anachohitaji. 9 Jihadhari usijiwekee wazo hili ovu: “Mwaka wa saba, mwaka wa kufuta madeni umekaribia,” usije ukaonyesha nia mbaya kwa ndugu yako mhitaji na ukaacha kumpa chochote. Anaweza kumlalamikia Bwana dhidi yako nawe utakuwa umepatikana na hatia ya dhambi. 10 Mpe kwa ukarimu na ufanye hivyo bila kinyongo moyoni, ndipo kwa sababu ya hili Bwana Mungu wenu atakubariki katika kazi zako zote na kwa kila kitu utakachokiwekea mkono wako. 11 Siku zote watakuwepo watu maskini katika nchi. Kwa hiyo ninawaamuru mwe na mikono iliyokunjuliwa kuwaelekea ndugu zenu, kuwaelekea maskini na wahitaji katika nchi yenu.

    12 Kama Mwebrania mwenzako, mwanaume au mwanamke, akijiuza kwako na kukutumikia miaka sita, katika mwaka wa saba ni lazima umwache aende zake akiwa huru. 13 Nawe wakati utakapomwachia usimwache aende mikono mitupu. 14 Mpe kwa uhuru kutoka zizi lako la kondoo na mbuzi, kutoka sakafu yako ya kupuria nafaka na kutoka mashinikizo yako ya kukamulia divai. Mpe kama vile ambavyo Bwana Mungu wako alivyokubariki. 15 Kumbukeni kuwa ninyi mlikuwa watumwa huko Misri naye Bwana Mungu wenu aliwakomboa. Ndiyo sababu nimewapa agizo hili leo.

  21. 4 Kufunga kwenu huishia kwenye magomvi na mapigano,

    na kupigana ninyi kwa ninyi kwa ngumi za uovu.

    Hamwezi kufunga kama mnavyofanya leo

    na kutazamia sauti zenu kusikiwa huko juu.

    5 Je, hii ndiyo aina ya mfungo niliouchagua,

    siku moja tu ya mtu kujinyenyekeza?

    Je, ni kwa kuinamisha kichwa chini kama tete,

    na kwa kujilaza juu ya nguo ya gunia na majivu?

    Je, huo ndio mnaouita mfungo,

    siku iliyokubalika kwa Bwana?

    6 “Je, hii si ndiyo aina ya mfungo niliyoichagua:

    kufungua minyororo ya udhalimu,

    na kufungua kamba za nira,

    kuwaweka huru walioonewa,

    na kuvunja kila nira?

    7 Je, sio kushirikiana chakula chako na wenye njaa

    na kuwapatia maskini wasiokuwa na makao hifadhi,

    unapomwona aliye uchi, umvike,

    wala si kumkimbia mtu wa nyama na damu yako mwenyewe?

    8 Ndipo nuru yako itajitokeza kama mapambazuko

    na uponyaji wako utatokea upesi;

    ndipo haki yako itakapokutangulia mbele yako,

    na utukufu wa Bwana utakuwa mlinzi nyuma yako.

    9 Ndipo utaita, naye Bwana atajibu,

    utalia kuomba msaada,

    naye atasema: Mimi hapa.

    “Kama ukiiondoa nira ya udhalimu,

    na kunyoosha kidole na kuzungumza maovu,

    10 nanyi kama mkimkunjulia mtu mwenye njaa nafsi zenu

    na kutosheleza mahitaji ya walioonewa,

    ndipo nuru yenu itakapongʼaa gizani,

    nao usiku wenu utakuwa kama adhuhuri.

    11 Bwana atakuongoza siku zote,

    atayatosheleza mahitaji yako katika nchi kame,

    naye ataitia nguvu mifupa yako.

    Utakuwa kama bustani iliyonyweshwa vizuri,

    kama chemchemi ambayo maji yake hayakauki kamwe.

  22. 42 Mpe yeye akuombaye, wala usimgeuzie kisogo yeye atakaye kukukopa.

  23. 35 Katika kila jambo nimewaonyesha kwamba kwa njia hii ya kufanya kazi kwa bidii imetupasa kuwasaidia wadhaifu, mkikumbuka maneno ya Bwana Yesu mwenyewe jinsi alivyosema, ‘Ni heri kutoa kuliko kupokea.’ ”

  24. 9 Kwa maana mnajua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba ingawa alikuwa tajiri, kwa ajili yenu alikubali kuwa maskini, ili kwa umaskini wake ninyi mpate kuwa matajiri.

  25. 14 Ndugu zangu, yafaa nini ikiwa mtu atadai kuwa anayo imani lakini hana matendo? Je, imani kama hiyo yaweza kumwokoa? 15 Ikiwa ndugu yako au dada hana mavazi wala chakula, 16 mmoja wenu akamwambia, “Enenda zako kwa amani, ukaote moto na kushiba,” pasipo kumpatia yale mahitaji ya mwili aliyopungukiwa, yafaa nini? 17 Vivyo hivyo, imani peke yake kama haikuambatana na matendo, imekufa.

  26. 7 Mwenye haki hujali haki kwa ajili ya maskini,

    bali mwovu hajishughulishi na hilo.

  27. 1 Kila mwisho wa miaka saba ni lazima mfute madeni. 2 Hivi ndivyo itakavyofanyika: Kila mkopeshaji atafuta mkopo aliomkopesha Mwisraeli mwenzake. Hatamtaka Mwisraeli mwenzake au ndugu yake amlipe hilo deni, kwa sababu wakati wa Bwana wa kufuta madeni umetangazwa. 3 Unaweza kudai malipo kwa mgeni, lakini lazima ufute kila deni ambalo unamdai ndugu yako. 4 Hata hivyo, hapatakuwepo maskini miongoni mwenu, kwa kuwa katika nchi Bwana Mungu wenu anayowapa kuimiliki kama urithi wenu, atawabariki sana, 5 ikiwa tutamtii Bwana Mungu wenu kikamilifu na kuwa waangalifu kuyafuata maagizo haya yote ninayowapa leo.

  28. 28 Mwishoni mwa kila mwaka wa tatu, leteni zaka zote za mazao ya miaka ile na uyahifadhi kwenye miji yenu, 29 ili Walawi (ambao hawana mashamba wala urithi wao wenyewe) na wageni, yatima na wajane wanaoishi kwenye miji yenu wapate kuja kula na kushiba, ili Bwana Mungu wenu apate kuwabariki ninyi katika kazi zote za mikono yenu.

  29. 3 Kwa ajili ya neema niliyopewa nawaambia kila mmoja miongoni mwenu, asijidhanie kuwa bora kuliko impasavyo, bali afikiri kwa busara kwa kulingana na kipimo cha imani Mungu aliyompa. 4 Kama vile katika mwili mmoja tulivyo na viungo vingi, navyo viungo vyote havina kazi moja, 5 vivyo hivyo na sisi tulio wengi, tu mwili mmoja katika Kristo, nasi kila mmoja ni kiungo cha mwenzake. 6 Tuna karama zilizotofautiana kila mmoja kutokana na neema tuliyopewa. Kama ni unabii na tutoe unabii kwa kadiri ya imani. 7 Kama ni kuhudumu na tuhudumu, mwenye kufundisha na afundishe, 8 kama ni kutia moyo na atie moyo, kama ni kuchangia kwa ajili ya mahitaji ya wengine na atoe kwa ukarimu, kama ni uongozi na aongoze kwa bidii, kama ni kuhurumia wengine na afanye hivyo kwa furaha.

    9 Upendo lazima usiwe na unafiki. Chukieni lililo ovu, shikamaneni na lililo jema. 10 Pendaneni ninyi kwa ninyi kwa upendo wa ndugu. Waheshimuni na kuwatanguliza wengine. 11 Msiwe wavivu, bali mwe na bidii katika roho mkimtumikia Bwana. 12 Kuweni na furaha katika tumaini, katika dhiki kuweni na saburi, dumuni katika maombi. 13 Changieni katika mahitaji ya watakatifu, wakaribisheni wageni.

  30. 21 “Usimtendee mgeni vibaya au kumwonea, kwa kuwa nanyi mlikuwa wageni huko Misri.

    22 “Usimdhulumu mjane wala yatima. 23 Kama ukifanya hivyo nao wakinililia, hakika nitasikia kilio chao. 24 Hasira yangu itawaka, nami nitawaua kwa upanga, wake zenu watakuwa wajane na watoto wenu watakuwa yatima.

    25 “Kama ukimkopesha mmojawapo wa watu wangu fedha ambaye ni mhitaji, usiwe kama mtu mkopesha fedha; usimtoze riba. 26 Kama ukichukua vazi la jirani kama rehani, ulirudishe kwake kabla jua kuzama, 27 kwa kuwa vazi lake ndilo pekee alilo nalo la kumfunika mwili wake. Ni nini kingine atajifunika nacho? Atakaponililia, nitasikia, kwa kuwa nina huruma.

  31. Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.

    1 Heri mtu yule anayemjali mnyonge,

    Bwana atamwokoa wakati wa shida.

    2 Bwana atamlinda na kuyahifadhi maisha yake,

    atambariki katika nchi

    na hatamwacha katika tamaa ya adui zake.

    3 Bwana atamtegemeza awapo mgonjwa kitandani,

    atamwinua kutoka kitandani mwake.

  32. 12 Najua kwamba Bwana huwapatia maskini haki,

    na kuitegemeza njia ya mhitaji.

  33. 38 Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa. Kipimo cha kujaa na kushindiliwa na kusukwasukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile mpimacho, ndicho mtakachopimiwa.”

  34. 6 Kumbukeni kwamba: Yeyote apandaye kwa uchache pia atavuna kwa uchache, naye apandaye kwa ukarimu pia atavuna kwa ukarimu. 7 Kila mtu atoe kama anavyokusudia moyoni mwake, si kwa uchoyo au kwa kulazimishwa, kwa maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo mkunjufu. 8 Naye Mungu aweza kuwapa kila baraka kwa wingi, ili katika mambo yote kila wakati, mwe na kila kitu mnachohitaji, ili mweze kushiriki kwa wingi katika kila kazi njema. 9 Kama ilivyoandikwa:

    “Ametawanya vipawa vyake kwa ukarimu

    akawapa maskini;

    haki yake hudumu milele.”

    10 Yeye ampaye mpanzi mbegu kwa ajili ya kupanda na mkate kuwa chakula, atawapa na kuzizidisha mbegu zenu za kupanda na kuongeza mavuno ya haki yenu. 11 Mtatajirishwa kwa kila namna ili mpate kuwa wakarimu kila wakati, na kupitia kwetu, ukarimu wenu utamletea Mungu shukrani.

  35. 22 Usiwadhulumu maskini kwa sababu ni maskini,

    wala kumdhulumu mhitaji mahakamani,

    23 kwa sababu Bwana atalichukua shauri lao

    naye atawateka wao waliowateka.

  36. 48 Hakika kama niishivyo, asema Bwana Mwenyezi, dada yako Sodoma pamoja na binti zake, kamwe hawakufanya yale ambayo wewe na binti zako mmefanya.

    49 “ ‘Sasa hii ilikuwa ndiyo dhambi ya dada yako Sodoma: yeye na binti zake walikuwa na majivuno, walafi na wazembe, hawakuwasaidia maskini na wahitaji. 50 Walijivuna na kufanya mambo ya machukizo sana mbele zangu. Kwa hiyo niliwakatilia mbali nami kama mlivyoona.

  37. 16 Yesu akaenda Nazareti, alipolelewa, na siku ya Sabato alikwenda katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake. Akasimama ili asome, 17 naye akapewa kitabu cha nabii Isaya, akakifungua na kukuta mahali palipoandikwa:

    18 “Roho wa Bwana yu juu yangu,

    kwa sababu amenitia mafuta

    kuwahubiria maskini habari njema.

    Amenituma kuwatangazia wafungwa

    kufunguliwa kwao,

    na vipofu kupata kuona tena,

    kuwaweka huru wanaoonewa,

    19 na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubalika.”

    20 Kisha akakifunga kitabu, akamrudishia mtumishi na akaketi. Watu wote waliokuwamo katika sinagogi wakamkazia macho. 21 Ndipo akaanza kwa kuwaambia, “Leo Andiko hili limetimia mkiwa mnasikia.”

  38. 20 Akawatazama wanafunzi wake, akasema:

    “Mmebarikiwa ninyi mlio maskini,

    kwa sababu Ufalme wa Mungu ni wenu.

    21 Mmebarikiwa ninyi mlio na njaa sasa,

    kwa sababu mtashibishwa.

    Mmebarikiwa ninyi mnaolia sasa,

    kwa sababu mtacheka.

  39. 17 Waagize wale ambao ni matajiri wa ulimwengu huu waache kujivuna, wala wasiweke tumaini lao katika mali ambayo si ya hakika, bali waweke tumaini lao katika Mungu ambaye hutupatia vitu vyote kwa wingi ili tuvifurahie. 18 Waagize watende mema, wawe matajiri katika matendo mema, pia wawe wakarimu na walio tayari kushiriki mali zao na wengine. 19 Kwa njia hii watajiwekea hazina kama msingi kwa ajili ya wakati ujao na hivyo watajipatia uzima, yaani, ule uzima ambao ni wa kweli.

  40. 10 Unapomkopesha jirani yako chochote, usiingie nyumbani kwake kutwaa kile anachokitoa kama rehani. 11 Ukae nje na umwache huyo mtu uliyemkopesha akuletee hiyo rehani. 12 Ikiwa mtu huyo ni maskini, usiende kulala ukiwa na hiyo rehani yake katika milki yako. 13 Rudisha vazi lake kabla ya machweo ya jua ili apate kulilalia. Kisha atakushukuru na kitaonekana kama kitendo cha haki mbele za Bwana Mungu wako.

    14 Usimwonee mtu maskini na mhitaji ambaye umemwajiri, akiwa ni nduguyo Mwisraeli au mgeni anayeishi katika mojawapo ya miji yenu. 15 Mlipe ujira wake kila siku kabla ya jua kutua, kwa sababu yeye ni maskini na anautegemea ujira huo. La sivyo, anaweza kumlilia Bwana dhidi yako, nawe ukapata hatia ya dhambi.

  41. 19 Unapovuna shamba lako na ukasahau mganda, usirudi kuuchukua. Acha kwa ajili ya mgeni, yatima na mjane, ili Bwana Mungu wako aweze kukubariki wewe katika kazi zote za mikono yako. 20 Unapovuna zeituni kutoka miti yako, usirudie matawi mara ya pili. Acha kilichobaki kwa ajili ya mgeni, yatima na mjane. 21 Unapochuma zabibu katika shamba lako la mizabibu usirudie tena. Acha zinazobaki kwa ajili ya mgeni, yatima na mjane. 22 Kumbuka kwamba mlikuwa watumwa katika nchi ya Misri. Ndiyo sababu ninawaamuru kufanya hili.

  42. 8 Humwinua maskini kutoka mavumbini

    na humwinua mhitaji kutoka lundo la majivu;

    huwaketisha pamoja na wakuu

    na kuwafanya warithi kiti cha enzi cha heshima.

    “Kwa kuwa misingi ya dunia ni ya Bwana;

    juu yake ameuweka ulimwengu.

  43. 10 Nitapaza sauti yangu nikisema,

    “Ni nani aliye kama wewe, Ee Bwana?

    Wewe huwaokoa maskini kutokana na wale walio na nguvu kuliko wao,

    maskini na mhitaji kutokana na wanaowanyangʼanya!”

  44. 12 Kwa maana atamwokoa mhitaji anayemlilia,

    aliyeonewa asiye na wa kumsaidia.

    13 Atawahurumia wanyonge na wahitaji

    na kuwaokoa wahitaji kutoka mauti.

    14 Atawaokoa kutoka uonevu na ukatili,

    kwani damu yao ni ya thamani machoni pake.

    15 Aishi maisha marefu!

    Na apewe dhahabu ya Sheba.

    Watu wamwombee daima

    na kumbariki mchana kutwa.

  45. 3 Teteeni wanyonge na yatima,

    tunzeni haki za maskini na walioonewa.

    4 Mwokoeni mnyonge na mhitaji,

    wakomboeni kutoka mkononi mwa mwovu.

  46. 24 Kuna mtu atoaye kwa ukarimu, hata hivyo hupata zaidi,

    mwingine huzuia, lakini huwa maskini.

    25 Mtu mkarimu atastawi;

    yeye awaburudishaye wengine

    ataburudishwa mwenyewe.

    26 Watu humlaani mtu awanyimae watu nafaka,

    bali baraka itamkalia kichwani kama taji

    yeye aliye radhi kuiuza.

    27 Yeye atafutaye mema hupata ukarimu,

    bali ubaya huja kwake yeye autafutaye.

  47. 17 jifunzeni kutenda mema!

    Tafuteni haki,

    watieni moyo walioonewa.

    Teteeni shauri la yatima,

    wateteeni wajane.

  48. Mahubiri Ya Yesu Kwenye Mlima

    1 Basi Yesu alipoona makutano, alipanda mlimani akaketi chini, nao wanafunzi wake wakamjia. 2 Ndipo akaanza kuwafundisha, akisema:

    3 “Heri walio maskini wa roho,

    maana Ufalme wa Mbinguni ni wao.

  49. 2 Chukulianeni mizigo ninyi kwa ninyi, nanyi kwa njia hii mtatimiza sheria ya Kristo.

  50. 25 Kwa hiyo kila mmoja wenu avue uongo na kuambiana kweli mtu na jirani yake, kwa maana sisi sote tu viungo vya mwili mmoja. 26 Mkikasirika, msitende dhambi, wala jua lisichwe mkiwa bado mmekasirika, 27 wala msimpe ibilisi nafasi. 28 Yeye ambaye amekuwa akiiba, asiibe tena, lakini lazima ajishughulishe, afanye kitu kifaacho kwa mikono yake mwenyewe, ili awe na kitu cha kuwagawia wahitaji.

    29 Maneno mabaya yasitoke vinywani mwenu, bali yale yafaayo kwa ajili ya kuwajenga wengine kulingana na mahitaji yao, ili yawafae wale wasikiao. 30 Wala msimhuzunishe Roho Mtakatifu wa Mungu, ambaye kwake mlitiwa muhuri kwa ajili ya siku ya ukombozi. 31 Ondoeni kabisa uchungu, ghadhabu, hasira, makelele na masingizio pamoja na kila aina ya uovu. 32 Kuweni wafadhili na wenye kuhurumiana ninyi kwa ninyi, mkisameheana, kama vile naye Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.

  51. 10 “Kwa muda wa miaka sita mtapanda mashamba yenu na kuvuna mazao, 11 lakini katika mwaka wa saba usiilime ardhi wala kuitumia, ili watu walio maskini miongoni mwenu waweze kupata chakula kutoka kwenye hayo mashamba, nao wanyama pori wapate chakula kwa yale mabaki watakayobakiza. Utafanya hivyo katika shamba lako la mizabibu na la mizeituni.

  52. 5 Yeye anaye mdhihaki maskini huonyesha dharau kwa Muumba wake;

    yeyote afurahiaye maafa hataepuka kuadhibiwa.

  53. 20 Huwanyooshea maskini mikono yake

    na kuwakunjulia wahitaji vitanga vyake.

  54. 16 Aliwatetea maskini na wahitaji,

    hivyo yeye akafanikiwa katika yote.

    Je, hiyo si ndiyo maana ya kunijua mimi?”

    asema Bwana.

  55. 13 Naweza kuyafanya mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.

  56. 16 Na msiache kutenda mema na kushirikiana vile vitu mlivyo navyo, kwa kuwa dhabihu kama hizo ndizo zinazompendeza Mungu.

  57. 15 “ ‘Usipotoshe haki; usionyeshe kumpendelea maskini, wala upendeleo kwa mwenye cheo, bali mwamulie jirani yako kwa haki.

  58. 17 Waovu wataishia kuzimu,

    naam, mataifa yote wanaomsahau Mungu.

    18 Lakini mhitaji hatasahaulika siku zote,

    wala matumaini ya walioonewa hayatapotea.

  59. 5 “Kwa sababu ya uonevu wa wanyonge

    na kulia kwa uchungu kwa wahitaji,

    nitainuka sasa,” asema Bwana.

    “Nitawalinda kutokana na wale

    wenye nia mbaya juu yao.”

  60. 5 Heri yeye ambaye Mungu wa Yakobo ni msaada wake,

    ambaye tumaini lake ni katika Bwana, Mungu wake,

    6 Muumba wa mbingu na nchi,

    na bahari na vyote vilivyomo ndani yake:

    Bwana anayedumu kuwa mwaminifu

    milele na milele.

    7 Naye huwapatia haki walioonewa

    na kuwapa wenye njaa chakula.

    Bwana huwaweka wafungwa huru,

    8 Bwana huwafumbua vipofu macho,

    Bwana huwainua waliolemewa na mizigo yao,

    Bwana huwapenda wenye haki.

    9 Bwana huwalinda wageni

    na kuwategemeza yatima na wajane,

    lakini hupinga njia za waovu.

  61. 27 Usizuie wema kwa wale wanaostahili

    ikiwa katika uwezo wako kutenda.

    28 Usimwambie jirani yako,

    “Njoo baadaye, nitakupa kesho”:

    wakati wewe unacho kitu kile karibu nawe.

  62. 2 Tajiri na maskini wanafanana kwa hili:

    Bwana ni Muumba wao wote.

  63. 4 Umekuwa kimbilio la watu maskini,

    kimbilio la mhitaji katika taabu yake,

    hifadhi wakati wa dhoruba

    na kivuli wakati wa hari.

    Kwa maana pumzi ya wakatili

    ni kama dhoruba ipigayo ukuta

  64. 17 “Maskini na wahitaji wanatafuta maji,

    lakini hayapo,

    ndimi zao zimekauka kwa kiu.

    Lakini Mimi Bwana nitawajibu,

    Mimi, Mungu wa Israeli, sitawaacha.

  65. 8 Neno la Bwana likamjia tena Zekaria: 9 “Hivi ndivyo asemavyo Bwana Mwenye Nguvu Zote: ‘Fanyeni hukumu za haki, onyesheni rehema na huruma ninyi kwa ninyi. 10 Msimwonee mjane wala yatima, mgeni wala maskini. Msiwaziane mabaya mioyoni mwenu ninyi kwa ninyi.’

  66. 1 Kama kukiwa na jambo lolote la kutia moyo katika kuunganishwa na Kristo, kukiwa faraja yoyote katika upendo wake, kukiwa na ushirika wowote na Roho, kukiwa na wema wowote na huruma, 2 basi ikamilisheni furaha yangu kwa kuwa na nia moja, mkiwa na upendo huo moja, mkiwa wa roho na kusudi moja. 3 Msitende jambo lolote kwa nia ya kujitukuza wala kujivuna, bali kwa unyenyekevu kila mtu amhesabu mwingine bora kuliko nafsi yake. 4 Kila mmoja wenu asiangalie faida yake mwenyewe tu, bali pia ajishughulishe kwa faida ya wengine.

    5 Kuweni na nia ile ile aliyokuwa nayo Kristo Yesu:

    6 Yeye, ingawa alikuwa na asili ya Mungu hasa,

    hakuona kule kuwa sawa na Mungu

    kuwa kitu cha kushikilia,

    7 bali alijifanya si kitu,

    akachukua hali hasa na mtumwa,

    naye akazaliwa katika umbo la mwanadamu.

    8 Naye akiwa na umbo la mwanadamu,

    alijinyenyekeza, akatii hata mauti:

    naam, mauti ya msalaba!

    9 Kwa hiyo, Mungu alimtukuza juu sana,

    na kumpa Jina lililo kuu kuliko kila jina,

    10 ili kwa Jina la Yesu, kila goti lipigwe,

    la vitu vya mbinguni, na vya duniani,

    na vya chini ya nchi,

    11 na kila ulimi ukiri ya kwamba

    Yesu Kristo ni Bwana,

    kwa utukufu wa Mungu Baba.

  67. 17 Lakini bado mimi ni maskini na mhitaji;

    Bwana na anifikirie.

    Wewe ndiwe msaada wangu na Mwokozi wangu;

    Ee Mungu wangu, usikawie.

  68. 1 Yesu alipoinua macho yake, aliwaona matajiri wakiweka sadaka zao kwenye sanduku la hazina ya Hekalu. 2 Akamwona pia mjane mmoja maskini akiweka humo sarafu mbili ndogo za shaba. 3 Yesu akasema, “Amin, nawaambia, huyu mjane maskini ameweka humo zaidi ya watu wengine wote. 4 Hawa watu wengine wote wametoa sadaka kutokana na wingi wa mali zao. Lakini huyu mjane ametoa kutokana na umaskini wake vyote alivyokuwa navyo, hata kile alichohitaji ili kuishi.”

  69. 32 Wale walioamini wote walikuwa na moyo mmoja na nia moja. Wala hakuna hata mmoja aliyesema chochote alichokuwa nacho ni mali yake mwenyewe, lakini walishirikiana kila kitu walichokuwa nacho. 33 Mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwa Bwana Yesu kwa nguvu nyingi na neema ya Mungu ilikuwa juu yao wote. 34 Wala hapakuwepo mtu yeyote miongoni mwao aliyekuwa mhitaji, kwa sababu mara kwa mara wale waliokuwa na mashamba na nyumba waliviuza, wakaleta thamani ya vitu vilivyouzwa, 35 wakaiweka miguuni pa mitume, kila mtu akagawiwa kadiri ya mahitaji yake.

    36 Yosefu, Mlawi kutoka Kipro, ambaye mitume walimwita Barnaba (maana yake Mwana wa Faraja), 37 aliuza shamba alilokuwa nalo, akaleta hizo fedha alizopata na kuziweka miguuni pa mitume.

  70. 36 Huko Yafa palikuwa na mwanafunzi jina lake Tabitha (ambalo kwa Kiyunani ni Dorkasi). Huyu alikuwa mkarimu sana, akitenda mema na kuwasaidia maskini.

  71. 22 “ ‘Mnapovuna mavuno ya ardhi yenu, msivune hadi mpakani mwa shamba lenu, au kukusanya masazo ya mavuno yenu. Hayo utayaacha kwa ajili ya maskini na mgeni. Mimi ndimi Bwana Mungu wenu.’ ”

  72. 6 Ninyi watenda mabaya mnakwamisha mipango ya maskini,

    bali Bwana ndiye kimbilio lao.

  73. 16 Yeye amwoneaye maskini ili kujiongezea mali,

    naye ampaye tajiri zawadi, wote huwa maskini.

  74. 2 Yohana aliposikia akiwa gerezani mambo ambayo Kristo alikuwa akiyafanya, aliwatuma wanafunzi wake 3 ili wakamuulize, “Wewe ndiye yule aliyekuwa aje, au tumngojee mwingine?”

    4 Yesu akajibu, “Rudini mkamwambie Yohana yale mnayosikia na kuyaona: 5 Vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa habari njema. 6 Amebarikiwa mtu yule asiyechukizwa na mimi.”

  75. 38 Alipokuwa akifundisha, Yesu alisema, “Jihadharini na walimu wa sheria. Wao hupenda kutembea wakiwa wamevaa mavazi marefu, na kusalimiwa kwa heshima masokoni. 39 Pia wao hupenda kukaa kwenye viti vya mbele katika masinagogi, na kupewa nafasi za heshima katika karamu. 40 Wao hula nyumba za wajane, na ili waonekane kuwa wema wanasali sala ndefu. Watu kama hawa watapata hukumu iliyo kuu sana.”

    41 Kisha Yesu akaketi mkabala na sehemu ambapo sadaka zilikuwa zinawekwa na kuangalia umati wa watu wakiweka fedha zao kwenye sanduku la hazina ya Hekalu. Matajiri wengi wakaweka kiasi kikubwa cha fedha. 42 Lakini mjane mmoja maskini akaja na kuweka sarafu mbili ndogo za shaba zenye thamani ya senti mbili.

    43 Yesu akawaita wanafunzi wake, akawaambia, “Amin, nawaambia, huyu mjane maskini ameweka katika sanduku la hazina zaidi ya watu wengine wote. 44 Wengine wote wametoa kutokana na ziada ya mali zao. Lakini huyu mjane ametoa kutokana na umaskini wake, akaweka kila kitu alichokuwa nacho, hata kile alichohitaji ili kuishi.”

  76. 42 Nao wakawa wanadumu katika mafundisho ya mitume, katika ushirika, katika kumega mkate na katika kusali. 43 Kila mtu akaingiwa na hofu ya Mungu, nayo miujiza mingi na ishara zikafanywa na mitume. 44 Walioamini wote walikuwa mahali pamoja, nao walikuwa na kila kitu shirika. 45 Waliuza mali zao na vitu walivyokuwa navyo, kila mtu akagawiwa kadiri ya mahitaji yake. 46 Siku zote kwa moyo mmoja walikutana ndani ya ukumbi wa Hekalu, wakimega mkate nyumba kwa nyumba, wakila chakula chao kwa furaha na moyo mweupe, 47 wakimsifu Mungu na kuwapendeza watu wote. Kila siku Bwana akaliongeza kanisa wale waliokuwa wakiokolewa.

  77. 20 Badala yake:

    “Kama adui yako ana njaa, mlishe;

    kama ana kiu, mpe kinywaji.

    Kwa kufanya hivyo,

    unaweka makaa ya moto yanayowaka kichwani pake.”

    21 Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema.

  78. 8 Kama mtu hawatunzi wale wa jamaa yake, hasa wale wa nyumbani mwake mwenyewe, ameikana imani, tena ni mbaya kuliko yeye asiyeamini.