58 Bible Verses About Power

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Power
  1. 11 Kisha nikaona mbingu imefunguka na hapo mbele yangu akiwepo farasi mweupe, ambaye yeye aliyempanda aliitwa Mwaminifu na Kweli. Yeye huhukumu kwa haki na kufanya vita. 12 Macho yake ni kama miali ya moto na juu ya kichwa chake kuna taji nyingi. Ana jina lililoandikwa ambalo hakuna mtu yeyote anayelijua isipokuwa yeye mwenyewe. 13 Amevaa joho lililochoviwa katika damu, na Jina lake ni “Neno la Mungu.” 14 Majeshi ya mbinguni walikuwa wakimfuata, wakiwa wamepanda farasi weupe, hali wamevaa mavazi ya kitani safi, nyeupe na nzuri. 15 Kinywani mwake hutoka upanga mkali ambao kwa huo atayaangusha mataifa. “Atayatawala kwa fimbo yake ya utawala ya chuma.” Hulikanyaga shinikizo la mvinyo wa ghadhabu ya Mungu Mwenyezi. 16 Kwenye joho lake na paja lake pameandikwa jina hili:

    Mfalme wa wafalme, na Bwana wa mabwana.

  2. 17 Kwa maana Kristo hakunituma ili kubatiza bali kuhubiri Injili; sio kwa maneno ya hekima ya kibinadamu, ili msalaba wa Kristo usije ukakosa nguvu yake.

    18 Kwa maana ujumbe wa msalaba kwa wale wanaopotea ni upuzi, lakini kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu. 19 Kwa maana imeandikwa:

    “Nitaiharibu hekima ya wenye hekima,

    na kubatilisha akili ya wenye akili.”

    20 Yuko wapi mwenye hekima? Yuko wapi msomi? Yuko wapi mwanafalsafa wa nyakati hizi? Je, Mungu hakufanya hekima ya ulimwengu huu kuwa upumbavu? 21 Kwa kuwa katika hekima ya Mungu, ulimwengu kwa hekima yake haukumjua yeye, ilimpendeza Mungu kuwaokoa wale walioamini kwa upuzi wa lile neno lililohubiriwa. 22 Wayahudi wanadai ishara za miujiza na Wayunani wanatafuta hekima. 23 Lakini sisi tunamhubiri Kristo aliyesulubiwa: yeye kwa Wayahudi ni kikwazo na kwa Wayunani ni upuzi. 24 Lakini kwa wale ambao Mungu amewaita, Wayahudi na pia Wayunani, Kristo ndiye nguvu ya Mungu na pia hekima ya Mungu. 25 Kwa maana upumbavu wa Mungu una hekima zaidi kuliko hekima ya wanadamu, nao udhaifu wa Mungu una nguvu kuliko nguvu ya wanadamu.

    26 Ndugu zangu, kumbukeni mlivyokuwa mlipoitwa. Kwa kipimo cha kibinadamu, si wengi wenu mliokuwa na hekima. Si wengi mliokuwa na ushawishi, si wengi mliozaliwa katika jamaa zenye vyeo. 27 Lakini Mungu alivichagua vitu vipumbavu vya ulimwengu ili awaaibishe wenye hekima, Mungu alivichagua vitu dhaifu vya ulimwengu ili awaaibishe wenye nguvu. 28 Alivichagua vitu vya chini na vinavyodharauliwa vya dunia hii, vitu ambavyo haviko, ili avibatilishe vile vilivyoko, 29 ili mtu yeyote asijisifu mbele zake.

  3. 28 Je wewe, hufahamu?

    Je wewe, hujasikia?

    Bwana ni Mungu wa milele,

    Muumba wa miisho ya dunia.

    Hatachoka wala kulegea,

    wala hakuna hata mmoja

    awezaye kuupima ufahamu wake.

    29 Huwapa nguvu waliolegea

    na huongeza nguvu za wadhaifu.

    30 Hata vijana huchoka na kulegea,

    nao vijana wanaume hujikwaa na kuanguka,

    31 bali wale wamtumainio Bwana

    atafanya upya nguvu zao.

    Watapaa juu kwa mbawa kama tai;

    watapiga mbio wala hawatachoka,

    watatembea kwa miguu wala hawatazimia.

  4. 16 sijaacha kumshukuru Mungu kwa ajili yenu, nikiwakumbuka katika maombi yangu. 17 Nazidi kumwomba Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awajalieni ninyi roho ya hekima na ya ufunuo, ili mpate kumjua zaidi. 18 Ninaomba pia kwamba macho ya mioyo yenu yatiwe nuru ili mpate kujua tumaini mliloitiwa, utajiri wa urithi wa utukufu wake kwa watakatifu 19 na uweza wake mkuu usiolinganishwa kwa ajili yetu sisi tuaminio. Uweza huo unaofanya kazi ndani yetu, ni sawa na ile nguvu kuu mno 20 aliyoitumia katika Kristo alipomfufua kutoka kwa wafu, na akamketisha mkono wake wa kuume huko mbinguni, 21 juu sana kuliko falme zote na mamlaka, enzi na milki, na juu ya kila jina litajwalo, si katika ulimwengu huu tu, bali katika ule ujao pia. 22 Naye Mungu ameweka vitu vyote viwe chini ya miguu yake na amemfanya yeye awe kichwa cha vitu vyote kwa ajili ya Kanisa, 23 ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake yeye aliye yote katika yote.

  5. 5 Sauti ya Mungu hunguruma kwa namna za ajabu;

    yeye hutenda mambo makuu kupita ufahamu wetu.

    6 Huiambia theluji, ‘Anguka juu ya dunia,’

    nayo manyunyu ya mvua, ‘Uwe mvua ya nguvu.’

  6. 15 Yeye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. 16 Kwake yeye vitu vyote vilivyoko mbinguni na juu ya nchi viliumbwa: vitu vinavyoonekana na visivyoonekana, viwe ni viti vya enzi au falme, au wenye mamlaka au watawala; vitu vyote viliumbwa na yeye na kwa ajili yake. 17 Yeye alikuwepo kabla ya vitu vyote, na katika yeye vitu vyote vinashikamana pamoja. 18 Yeye ndiye kichwa cha mwili, yaani kanisa, naye ndiye mwanzo na mzaliwa wa kwanza kutoka kwa wafu, ili yeye awe mkuu katika vitu vyote. 19 Kwa kuwa ilimpendeza Mungu kwamba utimilifu wake wote ukae ndani yake,

  7. 7 Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali roho ya nguvu, ya upendo na ya moyo wa kiasi.

    8 Kwa hiyo usione haya kushuhudia kuhusu Bwana wetu, wala usinionee haya mimi niliye mfungwa kwa ajili yake. Bali uishiriki pamoja nami taabu ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu,

  8. 37 Unijibu mimi, Ee Bwana, nijibu mimi, ili watu hawa wajue kwamba wewe, Ee Bwana, ndiwe Mungu, na kwamba unaigeuza mioyo yao ikurudie tena.”

    38 Kisha moto wa Bwana ukashuka na kuiteketeza ile dhabihu, zile kuni, yale mawe, ule udongo, na pia kuramba yale maji yaliyokuwa ndani ya handaki.

    39 Wakati watu wote walipoona hili, wakaanguka kifudifudi na kulia, “Bwana: yeye ndiye Mungu! Bwana: yeye ndiye Mungu!”

    40 Kisha Eliya akawaamuru, “Wakamateni hao manabii wa Baali. Msimwache hata mmoja atoroke!” Wakawakamata, naye Eliya akawaleta mpaka Bonde la Kishoni na kuwachinja huko.

  9. 6 Mitume walipokuwa wamekusanyika pamoja, wakamuuliza Yesu, “Bwana, je, huu ndio wakati wa kuwarudishia Israeli ufalme?”

    7 Yesu akawaambia, “Si juu yenu kujua nyakati na majira ambayo Baba ameyaweka katika mamlaka yake mwenyewe. 8 Lakini mtapokea nguvu akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu, nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, Uyahudi kote na Samaria, hadi miisho ya dunia.”

    9 Baada ya kusema mambo haya, walipokuwa wanatazama, akachukuliwa juu mbinguni mbele ya macho yao na wingu likampokea wasimwone tena.

  10. 16 Mimi siionei haya Injili ya Kristo kwa maana ni uweza wa Mungu uletao wokovu kwa kila aaminiye, kwanza kwa Myahudi na kwa Myunani pia. 17 Kwa maana katika Injili haki itokayo kwa Mungu imedhihirishwa, haki ile iliyo kwa njia ya imani hadi imani. Kama ilivyoandikwa: “Mwenye haki ataishi kwa imani.”

  11. 14 Kwa sababu hii nampigia Baba magoti, 15 ambaye ubaba wote wa kila jamaa za mbinguni na za duniani unatokana naye. 16 Namwomba Mungu awaimarishe kwa kuwatia nguvu mioyo yenu kwa njia ya Roho wake kwa kadiri ya utajiri wa utukufu wake, 17 ili kwamba, Kristo apate kukaa mioyoni mwenu kwa njia ya imani. Nami ninaomba kwamba ninyi mkiwa wenye mizizi tena imara katika msingi wa upendo, 18 mwe na uwezo wa kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, urefu, kimo na kina upendo wa Kristo, 19 na kujua upendo huu unaopita fahamu, ili mpate kujazwa na kufikia kipimo cha ukamilifu wote wa Mungu.

  12. 7 Ili kunizuia nisijivune kwa sababu ya ufunuo huu mkuu, nilipewa mwiba katika mwili wangu, mjumbe wa Shetani, ili anitese. 8 Kwa habari ya jambo hili nilimsihi Bwana mara tatu aniondolee mwiba huu. 9 Lakini aliniambia, “Neema yangu inakutosha, kwa kuwa uweza wangu hukamilika katika udhaifu.” Kwa hiyo nitajisifu kwa furaha zaidi kuhusu udhaifu wangu, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. 10 Hii ndiyo sababu, kwa ajili ya Kristo, nafurahia udhaifu, katika kutukanwa, katika taabu, katika mateso na katika shida, kwa maana ninapokuwa dhaifu, ndipo nina nguvu.

  13. 2 Kwa kuwa niliamua kutokujua kitu chochote wakati nikiwa nanyi isipokuwa Yesu Kristo aliyesulubiwa. 3 Mimi nilikuja kwenu nikiwa dhaifu na mwenye hofu na kwa kutetemeka sana. 4 Kuhubiri kwangu na ujumbe wangu haukuwa kwa hekima na maneno ya ushawishi bali kwa madhihirisho ya nguvu za Roho 5 ili imani yenu isiwe imejengwa katika hekima ya wanadamu bali katika nguvu za Mungu.

  14. 10 Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. 11 Vaeni silaha zote za Mungu ili kwamba mweze kuzipinga hila za ibilisi.

  15. 6 Hakuna aliye kama wewe, Ee Bwana;

    wewe ni mkuu,

    jina lako ni lenye nguvu katika uweza.

    7 Ni nani ambaye haimpasi kukuheshimu wewe,

    Ee Mfalme wa mataifa?

    Hii ni stahili yako.

    Miongoni mwa watu wote wenye hekima

    katika mataifa na katika falme zao zote,

    hakuna aliye kama wewe.

    8 Wote hawana akili, tena ni wapumbavu,

    wanafundishwa na sanamu za miti zisizofaa lolote.

    9 Huleta fedha iliyofuliwa kutoka Tarshishi

    na dhahabu kutoka Ufazi.

    Kile ambacho fundi na sonara wametengeneza

    huvikwa mavazi ya rangi ya samawi na urujuani:

    vyote vikiwa vimetengenezwa

    na mafundi stadi.

    10 Lakini Bwana ni Mungu wa kweli,

    yeye ndiye Mungu aliye hai, Mfalme wa milele.

    Anapokasirika, dunia hutetemeka,

    mataifa hayawezi kustahimili hasira yake.

    11 “Waambie hivi: ‘Miungu hii, ambayo haikuumba mbingu na dunia, itaangamia kutoka dunia na kutoka chini ya mbingu.’ ”

    12 Lakini Mungu aliiumba dunia kwa uweza wake,

    akaweka misingi ya ulimwengu kwa hekima yake,

    na akazitandaza mbingu kwa ufahamu wake.

    13 Atoapo sauti yake, maji yaliyo katika mbingu hunguruma;

    huyafanya mawingu yainuke kutoka miisho ya dunia.

    Hupeleka umeme wa radi pamoja na mvua,

    naye huuleta upepo kutoka ghala zake.

  16. 34 Maria akamuuliza huyo malaika, “Maadamu mimi ni bikira, jambo hili litawezekanaje?”

    35 Malaika akamjibu, “Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, nazo nguvu zake Yeye Aliye Juu Sana zitakufunika kama kivuli. Kwa hiyo mtoto atakayezaliwa atakuwa mtakatifu, naye ataitwa Mwana wa Mungu. 36 Tazama, jamaa yako Elizabeti amechukua mimba katika uzee wake, na huu ni mwezi wake wa sita, yeye aliyeitwa tasa. 37 Kwa maana kwa Mungu hakuna lisilowezekana.”

  17. 4 Kwa kuwa alisulubiwa katika udhaifu, lakini anaishi kwa nguvu za Mungu. Vivyo hivyo, sisi tu dhaifu kupitia kwake, lakini katika kuwashughulikia ninyi tutaishi pamoja naye kwa nguvu za Mungu.

  18. 10 Hivyo usiogope, kwa maana niko pamoja nawe;

    usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako.

    Nitakutia nguvu na kukusaidia;

    nitakutegemeza kwa mkono wa kuume wa haki yangu.

    11 “Wote walioona hasira dhidi yako

    hakika wataaibika na kutahayarika,

    wale wakupingao

    watakuwa kama vile si kitu, na kuangamia.

  19. 11 Jambo moja Mungu amelisema,

    mambo mawili nimeyasikia:

    kwamba, Ee Mungu,

    wewe una nguvu,

  20. 19 Lakini kama Bwana akipenda, nitafika kwenu mapema, nami nitapenda kujua, si tu kile wanachosema hawa watu jeuri, bali pia kujua nguvu yao. 20 Kwa kuwa Ufalme wa Mungu si maneno matupu tu bali ni nguvu.

  21. 11 Ukuu na uweza, ni vyako, Ee Bwana,

    na utukufu na enzi na uzuri,

    kwa kuwa kila kilichoko mbinguni na duniani

    ni chako wewe.

    Ee Bwana, ufalme ni wako;

    umetukuzwa kuwa mkuu juu ya yote.

  22. 31 Kisha Yesu akashuka kwenda Kapernaumu, mji wa Galilaya, na katika siku ya Sabato akawa anafundisha. 32 Wakashangazwa sana na mafundisho yake, maana maneno yake yalikuwa na mamlaka.

    33 Ndani ya sinagogi palikuwa na mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu. Naye akapiga kelele kwa nguvu akisema, 34 “Tuache! Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Ninakujua wewe ni nani. Wewe ndiwe Aliye Mtakatifu wa Mungu!”

    35 Basi Yesu akamkemea yule pepo mchafu, akisema, “Nyamaza kimya! Nawe umtoke!” Yule pepo mchafu akamwangusha yule mtu chini mbele yao wote, akatoka pasipo kumdhuru. 36 Watu wote wakashangaa, wakaambiana, “Mafundisho haya ni ya namna gani? Anawaamuru pepo wachafu kwa mamlaka na nguvu, nao wanatoka!”

  23. 13 Mlipokuwa wafu katika dhambi zenu na kutokutahiriwa katika asili yenu ya dhambi, Mungu aliwafanya mwe hai pamoja na Kristo. Alitusamehe dhambi zetu zote, 14 akiisha kuifuta ile hati yenye mashtaka yaliyokuwa yanatukabili, pamoja na maagizo yake. Aliiondoa isiwepo tena, akiigongomea kwenye msalaba wake. 15 Mungu akiisha kuzivua enzi na mamlaka, alizifanya kuwa kitu cha fedheha hadharani kwa kuziburura kwa ujasiri, akizishinda katika msalaba wa Kristo.

  24. 14 Haya ni mambo madogo tu katika matendo yake;

    tazama jinsi ulivyo mdogo mnongʼono tunaousikia kumhusu!

    Ni nani basi awezaye kuelewa

    ngurumo za nguvu zake?”

  25. 1 Siku ya Pentekoste ilipowadia, waamini wote walikuwa mahali pamoja. 2 Ghafula sauti kama mvumo mkubwa wa upepo mkali uliotoka mbinguni ukaijaza nyumba yote walimokuwa wameketi. 3 Zikatokea ndimi kama za moto zilizogawanyika na kukaa juu ya kila mmoja wao. 4 Wote wakajazwa na Roho Mtakatifu, wakaanza kunena kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia.

  26. 24 Tena nawaambia, ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita kwenye tundu la sindano kuliko mtu tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu.”

    25 Wanafunzi wake waliposikia haya, walishangaa sana na kuuliza, “Ni nani basi awezaye kuokoka?”

    26 Lakini Yesu akawatazama, akawaambia, “Kwa mwanadamu jambo hili haliwezekani, lakini mambo yote yanawezekana kwa Mungu.”

  27. 17 Wale sabini na wawili wakarudi kwa furaha, na kusema, “Bwana, hata pepo wachafu wanatutii kwa jina lako.”

    18 Yesu akawaambia, “Nilimwona Shetani akianguka kutoka mbinguni kama umeme wa radi. 19 Tazama nimewapa mamlaka ya kukanyaga nyoka na nge na juu ya nguvu zote za adui; wala hakuna kitu chochote kitakachowadhuru. 20 Basi, msifurahi kwa kuwa pepo wachafu wanawatii, bali furahini kwa kuwa majina yenu yameandikwa mbinguni.”

  28. 18 Akitarajia yasiyoweza kutarajiwa, Abrahamu akaamini, akawa baba wa mataifa mengi, kama alivyoahidiwa kwamba, “Uzao wako utakuwa mwingi mno.” 19 Abrahamu hakuwa dhaifu katika imani hata alipofikiri juu ya mwili wake, ambao ulikuwa kama uliokufa, kwani umri wake ulikuwa unakaribia miaka mia moja, au alipofikiri juu ya ufu wa tumbo la Sara. 20 Lakini Abrahamu hakusitasita kwa kutokuamini ahadi ya Mungu, bali alitiwa nguvu katika imani yake na kumpa Mungu utukufu, 21 akiwa na hakika kabisa kwamba Mungu alikuwa na uwezo wa kutimiza lile aliloahidi.

  29. 13 Kisha Bwana akamwambia Mose, “Amka mapema asubuhi, usimame mbele ya Farao, umwambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana, Mungu wa Waebrania: Waachie watu wangu waende, ili kwamba waweze kuniabudu, 14 au wakati huu nitaleta mapigo yangu yenye nguvu dhidi yako, maafisa wako na watu wako, ili upate kujua kuwa hakuna mwingine kama Mimi katika dunia yote. 15 Kwa kuwa mpaka sasa ningelikuwa nimenyoosha mkono wangu na kukupiga wewe na watu wako kwa pigo ambalo lingekufutilia mbali juu ya nchi. 16 Lakini nimekuinua wewe kwa kusudi hili hasa, ili nipate kukuonyesha uwezo wangu, na ili Jina langu lipate kutangazwa duniani yote. 17 Bado unaendelea kujiinua juu ya watu wangu, wala hutaki kuwaachia waende. 18 Kwa hiyo, kesho wakati kama huu nitaleta mvua mbaya sana ya mawe ambayo haijapata kunyesha katika nchi ya Misri, tangu siku ilipoumbwa mpaka leo.

  30. 35 Ee Mungu, wewe unatisha katika mahali patakatifu pako,

    Mungu wa Israeli huwapa watu wake uwezo na nguvu.

    Mungu Asifiwe!

  31. 26 Naye Yesu akawaambia, “Kwa nini mnaogopa, enyi wa imani haba?” Kisha akaamka na kukemea dhoruba na mawimbi, nako kukawa shwari kabisa.

    27 Wale watu wakashangaa, wakisema, “Ni mtu wa namna gani huyu? Hata upepo na mawimbi vinamtii!”

  32. 13 Naweza kuyafanya mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.

  33. 12 Kwa maana Neno la Mungu li hai tena lina nguvu. Lina makali kuliko upanga wowote wenye makali kuwili, hivyo linachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, viungo na mafuta yaliyo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.

  34. 4 Mtumaini Bwana milele,

    kwa kuwa Bwana, Bwana, ni Mwamba wa milele.

  35. 17 “Ee Bwana Mwenyezi, umeumba mbingu na nchi kwa uwezo wako mkuu na kwa mkono ulionyooshwa. Hakuna jambo lililo gumu usiloliweza. 18 Wewe huonyesha upendo kwa maelfu, lakini huleta adhabu kwa ajili ya dhambi za baba mapajani mwa watoto wao baada yao. Ee Mungu mkuu na mwenye uweza, ambaye jina lako ni Bwana Mwenye Nguvu Zote,

  36. 1 Kila mtu na atii mamlaka inayotawala, kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu, nazo mamlaka zilizopo zimewekwa na Mungu. 2 Kwa hiyo yeye anayeasi dhidi ya mamlaka inayotawala anaasi dhidi ya kile kilichowekwa na Mungu, nao wale wafanyao hivyo watajiletea hukumu juu yao wenyewe.

  37. 7 Lakini tunayo hazina hii katika vyombo vya udongo, ili ijulikane wazi kwamba uwezo huu wa ajabu unatoka kwa Mungu wala si kwetu.

  38. 12 Utajiri na heshima vyatoka kwako;

    wewe ndiwe utawalaye vitu vyote.

    Mikononi mwako kuna nguvu na uweza

    ili kuinua na kuwapa wote nguvu,

  39. 3 Mwambieni Mungu, “Jinsi gani yalivyo ya kutisha matendo yako!

    Uwezo wako ni mkuu mno kiasi kwamba

    adui wananyenyekea mbele zako.

    4 Dunia yote yakusujudia,

    wanakuimbia wewe sifa,

    wanaliimbia sifa jina lako.”

    5 Njooni mwone yale Mungu aliyoyatenda,

    mambo ya kutisha aliyoyatenda

    miongoni mwa wanadamu!

    6 Alifanya bahari kuwa nchi kavu,

    wakapita kati ya maji kwa miguu,

    njooni, tumshangilie.

    7 Yeye hutawala kwa uwezo wake milele,

    macho yake huangalia mataifa yote:

    waasi wasithubutu kujiinua dhidi yake.

  40. 14 naye Nebukadneza akawauliza, “Je, ni kweli kwamba ninyi Shadraki, Meshaki na Abednego hamuitumikii miungu yangu wala kuiabudu sanamu ya dhahabu niliyoisimamisha? 15 Basi wakati mtakaposikia sauti ya baragumu, filimbi, marimba, zeze, kinubi, zumari na aina zote za ala za uimbaji, kama mtakuwa tayari kusujudu na kuiabudu hiyo sanamu niliyoitengeneza, vyema sana. Lakini kama hamtaiabudu, mtatupwa saa iyo hiyo ndani ya tanuru iwakayo moto. Naye ni mungu yupi atakayeweza kuwaokoa ninyi, kutoka mkono wangu?”

    16 Shadraki, Meshaki na Abednego wakamjibu mfalme, “Ee Nebukadneza, hatuhitaji kujitetea mbele zako kuhusu jambo hili. 17 Ikiwa tutatupwa ndani ya tanuru iwakayo moto, Mungu tunayemtumikia anaweza kutuokoa na moto, naye atatuokoa kutoka mkononi mwako, ee mfalme. 18 Lakini hata ikiwa hatatuokoa, ee mfalme, tunataka ufahamu kwamba, hatutaitumikia miungu yako wala kuiabudu sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.”

  41. 37 Lakini katika mambo haya yote tunashinda, naam na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. 38 Kwa maana nimekwisha kujua kwa hakika ya kuwa sio mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuja, wala wenye uwezo, 39 wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kingine chochote zitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu, Bwana wetu.

  42. 54 Kwa hiyo, mwili huu wa kuharibika utakapovaa kutokuharibika, nao huu mwili wa kufa utakapovaa kutokufa, ndipo lile neno lililoandikwa litakapotimia: “Mauti imemezwa kwa kushinda.”

    55 “Kuko wapi, ee mauti, kushinda kwako?

    Uko wapi, ee mauti, uchungu wako?”

    56 Uchungu wa mauti ni dhambi na nguvu ya dhambi ni sheria. 57 Lakini ashukuriwe Mungu, yeye atupaye ushindi kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo.

  43. 5 Samsoni akateremkia Timna pamoja na baba yake na mama yake. Walipofika kwenye mashamba ya mizabibu huko Timna, ghafula mwana simba akamjia akimngurumia. 6 Roho wa Bwana akaja juu yake kwa nguvu, naye akampasua yule simba kwa mikono yake bila silaha yoyote kama vile mtu ampasuavyo mwana-mbuzi, wala hakumwambia baba yake wala mama yake aliyoyafanya.

  44. 2 Wakati huo huo wakamletea mtu aliyepooza, akiwa amelazwa kwenye mkeka. Yesu alipoiona imani yao, alimwambia yule mtu aliyepooza, “Mwanangu, jipe moyo mkuu. Dhambi zako zimesamehewa.”

    3 Kwa ajili ya jambo hili, baadhi ya walimu wa sheria wakasema mioyoni mwao, “Huyu mtu anakufuru!”

    4 Lakini Yesu akiyafahamu mawazo yao, akawaambia, “Kwa nini mnawaza maovu mioyoni mwenu? 5 Je, ni lipi lililo rahisi zaidi: kusema, ‘Umesamehewa dhambi zako,’ au kusema, ‘Inuka, uende’? 6 Lakini, ili mpate kujua kwamba Mwana wa Adamu anayo mamlaka duniani kusamehe dhambi…” Ndipo akamwambia yule aliyepooza, “Inuka, chukua mkeka wako, uende nyumbani kwako.” 7 Yule mtu akasimama, akaenda nyumbani kwake. 8 Makutano walipoyaona haya, wakajawa na hofu ya Mungu, wakamtukuza Mungu ambaye alikuwa ametoa mamlaka kama haya kwa wanadamu.

  45. 14 “Mimi ndimi mchungaji mwema. Ninawajua kondoo wangu nao kondoo wangu wananijua. 15 Kama vile Baba anavyonijua mimi, nami ninavyomjua Baba, nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo. 16 Ninao kondoo wengine ambao si wa zizi hili, inanipasa kuwaleta, nao wataisikia sauti yangu, hivyo patakuwa na kundi moja na mchungaji mmoja. 17 Baba yangu ananipenda kwa kuwa ninautoa uhai wangu ili niupate tena. 18 Hakuna mtu aniondoleaye uhai wangu, bali ninautoa kwa hiari yangu mwenyewe. Ninao uwezo wa kuutoa uhai wangu na pia ninao uwezo wa kuutwaa tena. Amri hii nimepewa na Baba yangu.”

  46. 19 Basi mtaniambia, “Kama ni hivyo, kwa nini basi bado Mungu anatulaumu? Kwa maana ni nani awezaye kupinga mapenzi yake?” 20 Lakini, ewe mwanadamu, u nani wewe ushindane na Mungu? “Je, kilichoumbwa chaweza kumwambia yeye aliyekiumba, ‘Kwa nini umeniumba hivi?’ ” 21 Je, mfinyanzi hana haki ya kufinyanga kutoka bonge moja vyombo vya udongo, vingine kwa matumizi ya heshima na vingine kwa matumizi ya kawaida?

    22 Iweje basi, kama Mungu kwa kutaka kuonyesha ghadhabu yake na kufanya uweza wake ujulikane, amevumilia kwa uvumilivu mwingi vile vyombo vya ghadhabu vilivyoandaliwa kwa uharibifu? 23 Iweje basi, kama yeye alitenda hivi ili kufanya wingi wa utukufu wake ujulikane kwa vile vyombo vya rehema yake, alivyotangulia kuvitengeneza kwa ajili ya utukufu wake, 24 yaani pamoja na sisi, ambao pia alituita, si kutoka kwa Wayahudi peke yao, bali pia kutoka kwa watu wa Mataifa?

  47. 9 Maana ukamilifu wote wa Uungu umo ndani ya Kristo katika umbile la mwili wa kibinadamu, 10 nanyi mmepewa ukamilifu ndani ya Kristo, ambaye ndiye mkuu juu ya kila enzi na kila mamlaka.

  48. 6 uliyeumba milima kwa uwezo wako,

    ukiwa umejivika nguvu,

  49. 4 Huzihesabu nyota

    na huipa kila moja jina lake.

    5 Bwana wetu ni mkuu na mwenye uwezo mwingi,

    ufahamu wake hauna kikomo.

  50. 19 Nitakupa funguo za Ufalme wa mbinguni, na lolote utakalolifunga duniani litakuwa limefungwa Mbinguni, nalo lolote utakalofungua duniani litakuwa limefunguliwa mbinguni.”

  51. 10 Pilato akamwambia, “Wewe unakataa kuongea na mimi? Hujui ya kuwa nina mamlaka ya kukuachia huru au kukusulubisha?”

    11 Ndipo Yesu akamwambia, “Wewe hungekuwa na mamlaka yoyote juu yangu kama hungepewa kutoka juu. Kwa hiyo yeye aliyenitia mikononi mwako ana hatia ya dhambi iliyo kubwa zaidi.”

  52. 1 Kwa hiyo, kwa kuwa tuna huduma hii kwa rehema za Mungu, hatukati tamaa. 2 Tumekataa mambo ya siri na ya aibu, wala hatufuati njia za udanganyifu, tukichanganya Neno la Mungu na uongo. Kinyume cha hayo, tunadhihirisha kweli waziwazi na kujitambulisha wenyewe kwenye dhamiri ya kila mtu mbele za Mungu. 3 Hata nayo Injili yetu kama imetiwa utaji, ni kwa wale tu wanaopotea. 4 Kwa habari yao, mungu wa dunia hii amepofusha akili za wasioamini, ili wasione nuru ya Injili ya utukufu wa Kristo, aliye sura ya Mungu. 5 Kwa maana hatujihubiri sisi wenyewe ila tunamhubiri Yesu Kristo kuwa ni Bwana na sisi ni watumishi wenu kwa ajili ya Yesu. 6 Kwa kuwa Mungu, yeye aliyesema, “Nuru na ingʼae gizani,” ameifanya nuru yake ingʼae mioyoni mwetu ili kutupatia nuru ya maarifa ya utukufu wa Mungu katika uso wa Kristo.

  53. 3 Ingawa tunaishi duniani, hatupigani vita kama ulimwengu ufanyavyo. 4 Silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome, 5 tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu, na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo,

  54. 32 Basi niseme nini zaidi? Sina wakati wa kusema habari za Gideoni, Baraka, Samsoni, Yeftha, Daudi, Samweli na manabii, 33 ambao kwa imani walishinda milki za wafalme, walitekeleza haki, na wakapokea ahadi za Mungu; walifunga vinywa vya simba, 34 wakazima makali ya miali ya moto, na wakaepuka kuuawa kwa upanga; udhaifu wao uligeuka kuwa nguvu; pia walikuwa hodari vitani na kuyafukuza majeshi ya wageni.

  55. 3 Mungu wetu yuko mbinguni,

    naye hufanya lolote limpendezalo.

  56. 26 “Natoa amri hii, kwamba katika kila sehemu ya ufalme wangu, lazima watu wamwogope na kumheshimu Mungu wa Danieli.

    “Kwa maana yeye ni Mungu aliye hai,

    naye hudumu milele,

    ufalme wake hautaangamizwa,

    nao utawala wake hauna mwisho.

    27 Huponya na kuokoa;

    hufanya ishara na maajabu

    mbinguni na duniani.

    Amemwokoa Danieli

    kutoka nguvu za simba.”

  57. 30 Ghafula Yesu akatambua kuwa nguvu zimemtoka. Akaugeukia ule umati wa watu na kuuliza, “Ni nani aliyegusa mavazi yangu?”

  58. 25 Kwa maana lazima Kristo atawale mpaka awe amewaweka adui zake wote chini ya miguu yake. 26 Adui wa mwisho atakayeangamizwa ni mauti. 27 Kwa maana Mungu “ameweka vitu vyote chini ya miguu yake.” Lakini isemapo kwamba “vitu vyote” vimewekwa chini yake, ni wazi kwamba Mungu aliyetiisha vitu vyote chini ya Kristo hayumo miongoni mwa hivyo vilivyotiishwa. 28 Atakapokuwa amekwisha kuyafanya haya, ndipo Mwana mwenyewe atatiishwa chini yake yeye aliyetiisha vitu vyote, ili Mungu awe yote katika yote.