44 Bible Verses About God's Wrath

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About God's Wrath
  1. 18 Ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni dhidi ya uasi wote na uovu wa wanadamu ambao huipinga kweli kwa uovu wao, 19 kwa maana yote yanayoweza kujulikana kumhusu Mungu ni dhahiri kwao, kwa sababu Mungu mwenyewe ameyadhihirisha kwao. 20 Kwa maana tangu kuumbwa kwa ulimwengu, asili ya Mungu asiyeonekana kwa macho, yaani, uweza wake wa milele na asili yake ya Uungu, imeonekana waziwazi, ikitambuliwa kutokana na yale aliyoyafanya ili wanadamu wasiwe na udhuru.

    21 Kwa maana ingawa walimjua Mungu, hawakumtukuza yeye kama ndiye Mungu wala hawakumshukuru, bali fikira zao zimekuwa batili na mioyo yao ya ujinga ikatiwa giza. 22 Ingawa walijidai kuwa wenye hekima, wakawa wajinga 23 na kubadili utukufu wa Mungu aishiye milele kwa sanamu zilizofanywa zifanane na mwanadamu ambaye hufa, na mfano wa ndege, wanyama na viumbe vitambaavyo.

  2. 35 Baba anampenda Mwana, naye ametia vitu vyote mikononi mwake. 36 Yeyote anayemwamini Mwana ana uzima wa milele, lakini yeye asiyemwamini Mwana hatauona uzima, bali ghadhabu ya Mungu itakuwa juu yake.”

  3. 1 Ni nani huyu anayekuja kutoka Edomu,

    kutoka Bosra, mwenye mavazi yaliyotiwa madoa mekundu?

    Ni nani huyu, aliyevikwa joho la kifahari,

    anayetembea kwa ukuu wa nguvu zake?

    “Mimi ndimi, nisemaye katika haki,

    mwenye nguvu wa kuokoa.”

    2 Kwa nini mavazi yako ni mekundu,

    kama ya yule akanyagaye shinikizo la zabibu?

    3 “Nimekanyaga shinikizo la zabibu peke yangu;

    kutoka mataifa hakuna mtu aliyekuwa pamoja nami.

    Nimewaponda kwa miguu katika hasira yangu

    na kuwakanyaga chini katika ghadhabu yangu;

    damu yao ilitia matone kwenye mavazi yangu,

    na kutia madoa nguo zangu zote.

    4 Kwa kuwa siku ya kisasi ilikuwa moyoni mwangu,

    mwaka wa ukombozi wangu umefika.

    5 Nilitazama, lakini hakuwepo yeyote wa kunisaidia,

    nilishangaa kwa kuwa hakuwepo yeyote aliyetoa msaada;

    hivyo mkono wangu wenyewe ndio ulionifanyia wokovu,

    na ghadhabu yangu mwenyewe ndiyo iliyonitegemeza.

    6 Nilikanyaga mataifa kwa miguu katika hasira yangu,

    katika ghadhabu yangu niliwalewesha,

    na kumwaga damu yao juu ya ardhi.”

  4. 4 Au waudharau wingi wa wema, ustahimili na uvumilivu wake, bila kujua kuwa wema wa Mungu wakuelekeza kwenye toba?

    5 Lakini kwa sababu ya ukaidi wenu na mioyo yenu isiyotaka kutubu, mnajiwekea akiba ya ghadhabu dhidi yenu wenyewe kwa siku ile ya ghadhabu ya Mungu, wakati hukumu yake ya haki itakapodhihirishwa. 6 Kwa maana Mungu atamlipa kila mtu sawasawa na matendo yake. 7 Wale ambao kwa kuvumilia katika kutenda mema hutafuta utukufu, heshima na maisha yasiyoharibika, Mungu atawapa uzima wa milele. 8 Lakini kwa wale watafutao mambo yao wenyewe na wale wanaokataa kweli na kuzifuata njia mbaya, kutakuwa na ghadhabu na hasira ya Mungu. 9 Kutakuwa na taabu na dhiki kwa kila mmoja atendaye maovu, Myahudi kwanza na mtu wa Mataifa pia, 10 bali utukufu, heshima na amani kwa ajili ya kila mmoja atendaye mema, kwa Myahudi kwanza, kisha kwa mtu wa Mataifa. 11 Kwa maana Mungu hana upendeleo.

  5. 17 Msimlipe mtu yeyote ovu kwa ovu. Jitahidini ili mtende yaliyo mema machoni pa watu wote. 18 Kama ikiwezekana, kwa upande wenu kaeni kwa amani na watu wote. 19 Wapendwa, msilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu, maana imeandikwa: “Ni juu yangu kulipiza kisasi, nitalipiza,” asema Bwana. 20 Badala yake:

    “Kama adui yako ana njaa, mlishe;

    kama ana kiu, mpe kinywaji.

    Kwa kufanya hivyo,

    unaweka makaa ya moto yanayowaka kichwani pake.”

    21 Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema.

  6. 21 Lakini sasa, haki itokayo kwa Mungu imedhihirishwa pasipo sheria, ambayo Sheria na Manabii wanaishuhudia. 22 Haki hii itokayo kwa Mungu hupatikana kwa Yesu Kristo kwa wote wamwaminio. Kwa maana hapo hakuna tofauti, 23 kwa kuwa wote wametenda dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu, 24 wanahesabiwa haki bure kwa neema yake kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu. 25 Yeye ambaye Mungu alimtoa awe dhabihu ya upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake. Alifanya hivi ili kuonyesha haki yake, kwa sababu kwa ustahimili wake aliziachilia zile dhambi zilizotangulia kufanywa. 26 Alifanya hivyo ili kuonyesha haki yake wakati huu, ili yeye awe mwenye haki na mwenye kumhesabia haki yule anayemwamini Yesu.

    27 Basi, kujivuna kuko wapi? Kumewekwa mbali. Kwa sheria gani? Je, ni kwa ile ya matendo? La hasha, bali kwa ile sheria ya imani. 28 Kwa maana twaona kwamba mwanadamu huhesabiwa haki kwa njia ya imani wala si kwa matendo ya sheria. 29 Je, Mungu ni Mungu wa Wayahudi peke yao? Je, yeye si Mungu wa watu wa Mataifa pia? Naam, yeye ni Mungu wa watu wa Mataifa pia. 30 Basi kwa kuwa tuna Mungu mmoja tu, atawahesabia haki wale waliotahiriwa kwa imani na wale wasiotahiriwa kwa imani iyo hiyo. 31 Je, basi ni kwamba tunaibatilisha sheria kwa imani hii? La, hasha! Badala yake tunaithibitisha sheria.

  7. 8 Lakini Mungu anaudhihirisha upendo wake kwetu kwamba: Tulipokuwa tungali wenye dhambi, Kristo alikufa kwa ajili yetu.

    9 Basi, kwa kuwa sasa tumehesabiwa haki kwa damu yake, si zaidi sana tutaokolewa kutoka ghadhabu ya Mungu kupitia kwake!

  8. 2 Bwana ni mwenye wivu na Mungu mlipiza kisasi;

    Bwana hulipiza kisasi na amejaa ghadhabu.

    Bwana hulipiza kisasi juu ya watesi wake,

    naye anadumisha ghadhabu yake dhidi ya adui zake.

    3 Bwana si mwepesi wa hasira naye ni mwenye nguvu,

    Bwana hataacha kuadhibu wenye hatia.

    Njia yake ipo katika kisulisuli na tufani,

    na mawingu ni vumbi la miguu yake.

    4 Anakemea bahari na kuikausha,

    anafanya mito yote kukauka.

    Bashani na Karmeli zinanyauka

    na maua ya Lebanoni hukauka.

    5 Milima hutikisika mbele yake

    na vilima huyeyuka.

    Nchi hutetemeka mbele yake,

    dunia na wote waishio ndani yake.

    6 Ni nani awezaye kuzuia hasira yake yenye uchungu?

    Nani awezaye kuvumilia hasira yake kali?

    Ghadhabu yake imemiminwa kama moto,

    na miamba inapasuka mbele zake.

  9. 5 Watu walikuwa wakimwendea kutoka Yerusalemu, Uyahudi yote na nchi zote za kandokando ya Mto Yordani. 6 Nao wakaziungama dhambi zao, akawabatiza katika Mto Yordani.

    7 Lakini alipowaona Mafarisayo na Masadukayo wengi wakija ili kubatizwa, aliwaambia: “Ninyi watoto wa nyoka! Ni nani aliyewaonya kuikimbia ghadhabu inayokuja? 8 Basi zaeni matunda yastahiliyo toba. 9 Wala msidhani mnaweza kusema mioyoni mwenu kuwa, ‘Sisi tunaye Abrahamu, baba yetu.’ Nawaambia kuwa Mungu anaweza kumwinulia Abrahamu watoto kutoka kwa mawe haya. 10 Hata sasa shoka limeshawekwa tayari kwenye shina la kila mti, basi kila mti usiozaa matunda mazuri, hukatwa na kutupwa motoni.

    11 “Mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba. Lakini nyuma yangu anakuja yeye aliye na uwezo kuliko mimi, ambaye sistahili hata kuvichukua viatu vyake. Yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto. 12 Pepeto lake liko mkononi mwake, naye atasafisha sakafu yake ya kupuria, na kuikusanya ngano ghalani na kuyateketeza makapi kwa moto usiozimika.”

  10. 3 Lakini uasherati, usitajwe miongoni mwenu, wala uchafu wa aina yoyote, wala tamaa, kwa sababu mambo haya hayastahili miongoni mwa watakatifu. 4 Wala pasiwepo mazungumzo machafu ya aibu, au maneno ya upuzi au mzaha, ambayo hayafai, badala yake mshukuruni Mungu. 5 Kwa habari ya mambo haya mjue hakika kwamba: Msherati, wala mtu mwovu, wala mwenye tamaa mbaya, mtu kama huyo ni mwabudu sanamu, kamwe hataurithi Ufalme wa Kristo na wa Mungu. 6 Mtu yeyote na asiwadanganye kwa maneno matupu, kwa kuwa hasira ya Mungu huwaka kwa sababu ya mambo kama haya juu ya wale wasiomtii. 7 Kwa hiyo, msishirikiane nao.

  11. 12 Nikatazama akiivunja ile lakiri ya sita. Pakatokea tetemeko kuu la nchi, na jua likawa jeusi kama nguo ya gunia iliyotengenezwa kwa singa za mbuzi, na mwezi wote ukawa mwekundu kama damu. 13 Nyota zilizo angani zikaanguka ardhini kama vile matunda ya mtini yasiyokomaa yaangukavyo wakati mti wake unapotikiswa na upepo mkali. 14 Anga ikatoweka kama vile karatasi isokotwavyo, na kila mlima na kila kisiwa kikaondolewa mahali pake.

    15 Ndipo wafalme wa dunia, wakuu wote, majemadari, matajiri, wenye nguvu na kila mtu, mtumwa na mtu huru, wakajificha katika mapango na kwenye miamba ya milima. 16 Wakaiita milima na miamba wakisema, “Tuangukieni, mkatufiche na uso wake yeye aketiye kwenye kiti cha enzi, na mkatuepushe na ghadhabu ya Mwana-Kondoo! 17 Kwa maana siku ile kuu ya ghadhabu yao imewadia. Je, ni nani awezaye kustahimili?”

  12. 6 Bwana akapita mbele ya Mose, akitangaza, “Bwana, Bwana, Mungu mwenye huruma na neema, asiye mwepesi wa hasira, mwingi wa upendo na uaminifu, 7 akidumisha upendo kwa maelfu, pia akisamehe uovu, uasi na dhambi. Lakini haachi kuadhibu mwenye hatia; huwaadhibu watoto na watoto wao kwa ajili ya dhambi ya baba zao hata katika kizazi cha tatu na cha nne.”

  13. 11 Mungu ni mwamuzi mwenye haki,

    Mungu aghadhibikaye kila siku.

    12 Kama hakutuhurumia,

    atanoa upanga wake,

    ataupinda na kuufunga uzi upinde wake.

    13 Ameandaa silaha zake kali,

    ameweka tayari mishale yake ya moto.

  14. 26 Kama tukiendelea kutenda dhambi kwa makusudi baada ya kupokea ufahamu wa ile kweli, haibaki tena dhabihu kwa ajili ya dhambi. 27 Lakini kinachobaki ni kungoja kwa hofu hukumu ya moto uwakao, utakaowaangamiza adui za Mungu. 28 Yeyote aliyeikataa sheria ya Mose alikufa pasipo huruma kwa ushahidi wa watu wawili au watatu. 29 Je, mnadhani ni adhabu kali kiasi gani anayostahili kupewa mtu aliyemkanyaga Mwana wa Mungu chini ya nyayo zake, yeye aliyeifanya damu ya Agano iliyomtakasa kuwa kitu najisi na kumtendea maovu Roho wa neema? 30 Kwa kuwa tunamjua yeye aliyesema, “Ni juu yangu kulipiza kisasi; nitalipiza.” Tena asema, “Bwana atawahukumu watu wake.” 31 Ni jambo la kutisha kuanguka mikononi mwa Mungu aliye hai.

  15. 11 Kisha nikaona mbingu imefunguka na hapo mbele yangu akiwepo farasi mweupe, ambaye yeye aliyempanda aliitwa Mwaminifu na Kweli. Yeye huhukumu kwa haki na kufanya vita. 12 Macho yake ni kama miali ya moto na juu ya kichwa chake kuna taji nyingi. Ana jina lililoandikwa ambalo hakuna mtu yeyote anayelijua isipokuwa yeye mwenyewe. 13 Amevaa joho lililochoviwa katika damu, na Jina lake ni “Neno la Mungu.” 14 Majeshi ya mbinguni walikuwa wakimfuata, wakiwa wamepanda farasi weupe, hali wamevaa mavazi ya kitani safi, nyeupe na nzuri. 15 Kinywani mwake hutoka upanga mkali ambao kwa huo atayaangusha mataifa. “Atayatawala kwa fimbo yake ya utawala ya chuma.” Hulikanyaga shinikizo la mvinyo wa ghadhabu ya Mungu Mwenyezi. 16 Kwenye joho lake na paja lake pameandikwa jina hili:

    Mfalme wa wafalme, na Bwana wa mabwana.

  16. 9 Kwa maana watu wa maeneo hayo wenyewe wanaeleza jinsi mlivyotupokea na jinsi mlivyomgeukia Mungu mkaacha sanamu, ili kumtumikia Mungu aliye hai na wa kweli 10 na ili kumngojea Mwanawe kutoka mbinguni, ambaye Mungu alimfufua kutoka kwa wafu: yaani, Yesu, yeye aliyetuokoa kutoka ghadhabu inayokuja.

  17. 2 kwa kuwa mnajua vyema kwamba siku ya Bwana itakuja kama mwizi ajapo usiku. 3 Wakati watu wanaposema, “Kuna amani na salama,” maangamizi huwajia ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwanamke mwenye mimba; nao hakika hawatatoroka.

    4 Bali ninyi, ndugu, hampo gizani hata siku ile iwakute ghafula kama mwizi. 5 Ninyi nyote ni wana wa nuru na wana wa mchana. Sisi si wana wa giza wala wa usiku. 6 Kwa hiyo basi, tusilale kama watu wengine walalavyo, bali tukeshe na kuwa na kiasi. 7 Kwa kuwa wote walalao hulala usiku na wale walewao hulewa usiku. 8 Lakini kwa kuwa sisi ni wana wa mchana, basi tuwe na kiasi, tukijivika imani na upendo kama dirii kifuani na tumaini letu la wokovu kama chapeo. 9 Kwa maana Mungu hakutuita ili tupate ghadhabu bali tupate wokovu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. 10 Yeye alikufa kwa ajili yetu ili hata kama tuko macho au tumelala, tupate kuishi pamoja naye.

  18. 19 Basi matendo ya mwili ni dhahiri nayo ni haya: Uasherati, uchafu, ufisadi, 20 kuabudu sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, 21 husuda, ulevi, ulafi na mambo mengine yanayofanana na hayo. Nawaonya, kama nilivyokwisha kuwaonya kabla, kwamba watu watendao mambo kama hayo, hawataurithi Ufalme wa Mungu.

    22 Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, 23 upole na kiasi. Katika mambo kama haya hakuna sheria.

  19. 5 Kwa hiyo, ueni kabisa chochote kilicho ndani yenu cha asili ya kidunia: yaani uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya na ulafi, ambayo ndiyo ibada ya sanamu. 6 Kwa sababu ya mambo haya, ghadhabu ya Mungu inakuja.

  20. 14 “Siku kubwa ya Bwana iko karibu:

    iko karibu na inakuja haraka.

    Sikilizeni! Kilio katika siku ya Bwana

    kitakuwa kichungu,

    hata shujaa atapiga kelele.

    15 Siku ile ni siku ya ghadhabu,

    siku ya fadhaa na dhiki,

    siku ya uharibifu na ukiwa,

    siku ya giza na utusitusi,

    siku ya mawingu na giza nene,

    16 siku ya tarumbeta na mlio wa vita

    dhidi ya miji yenye ngome

    na dhidi ya minara mirefu.

    17 Nitawaletea watu dhiki,

    nao watatembea kama vipofu,

    kwa sababu wametenda dhambi

    dhidi ya Bwana.

    Damu yao itamwagwa kama vumbi

    na matumbo yao kama taka.

    18 Fedha yao wala dhahabu yao

    hazitaweza kuwaokoa

    katika siku hiyo ya ghadhabu ya Bwana.

    Katika moto wa wivu wake

    dunia yote itateketezwa,

    kwa maana ataleta mwisho

    wa wote wanaoishi katika dunia ghafula.”

  21. 6 Kisha nikamwona malaika mwingine akiruka juu angani, naye alikuwa na Injili ya milele ya kuwatangazia wale waishio duniani, yaani, kwa kila taifa, kabila, lugha na jamaa. 7 Akasema kwa sauti kubwa, “Mcheni Mungu na kumpa utukufu, kwa maana saa ya hukumu yake imewadia. Mwabuduni yeye aliyeziumba mbingu, dunia, bahari na chemchemi za maji.”

    8 Malaika wa pili akafuata akisema, “Umeanguka! Umeanguka Babeli Mkuu, ule uliyafanya mataifa yote kulewa kwa mvinyo wa ghadhabu ya uasherati wake.”

    9 Malaika wa tatu akawafuata hao wawili akisema kwa sauti kubwa, “Kama mtu yeyote anamwabudu huyo mnyama na sanamu yake na kutiwa chapa yake kwenye kipaji chake cha uso au kwenye mkono wake, 10 yeye pia atakunywa mvinyo wa hasira kali ya Mungu ambayo imemiminwa katika kikombe cha ghadhabu yake pasipo kuchanganywa na maji. Naye atateswa kwa moto uwakao na kiberiti mbele ya malaika watakatifu na mbele za Mwana-Kondoo. 11 Nao moshi wa mateso yao hupanda juu milele na milele. Hakuna mapumziko, mchana wala usiku, kwa wale wamwabuduo huyo mnyama na sanamu yake, au kwa yeyote anayepokea chapa ya jina lake.” 12 Hapa ndipo penye wito wa subira na uvumilivu wa watakatifu; wale wanaozishika amri za Mungu na kudumu katika uaminifu kwa Yesu.

  22. 9 Bwana akamwambia Mose, “Nimeona watu hawa, nao ni watu wenye shingo ngumu. 10 Sasa niache ili hasira yangu ipate kuwaka dhidi yao, nami nipate kuwaangamiza. Kisha nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa.”

  23. 7 Kumbukeni hili, kamwe msisahau jinsi mlivyomkasirisha Bwana Mungu wenu kwa hasira huko jangwani. Tangu siku mlipotoka Misri mpaka mlipofika hapa, mmekuwa waasi dhidi ya Bwana. 8 Kule Horebu mliamsha ghadhabu ya Bwana, kwa hiyo alikasirika vya kutosha hata akataka kuwaangamiza.

  24. 30 Zamani wakati wa ujinga, Mungu alijifanya kama haoni, lakini sasa anawaamuru watu wote kila mahali watubu. 31 Kwa kuwa ameweka siku ambayo atauhukumu ulimwengu kwa haki akimtumia mtu aliyemchagua. Amewahakikishia watu wote mambo haya kwa kumfufua Kristo kutoka kwa wafu.”

  25. 23 Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti, bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.

  26. 5 Haya yote ni uthibitisho kwamba hukumu ya Mungu ni ya haki, na kwa sababu hiyo ninyi mtahesabiwa kwamba mnastahili kuwa wa Ufalme wa Mungu, mnaoteswa kwa ajili wake. 6 Mungu ni mwenye haki: yeye atawalipa mateso wale wawatesao ninyi 7 na kuwapa ninyi mnaoteseka raha pamoja na sisi, wakati Bwana Yesu atakapodhihirishwa kutoka mbinguni katika mwali wa moto pamoja na malaika wake wenye nguvu. 8 Atawaadhibu wale wasiomjua Mungu na ambao hawakuitii Injili ya Bwana wetu Yesu. 9 Wataadhibiwa kwa uangamivu wa milele na kutengwa na uso wa Bwana na utukufu wa uweza wake, 10 siku hiyo atakapokuja kutukuzwa katika watakatifu wake na kustaajabiwa miongoni mwa wote walioamini. Ninyi pia mtakuwa miongoni mwa hawa kwa sababu mliamini ushuhuda wetu kwenu.

  27. 28 Kwa hiyo, kwa kuwa tunapokea ufalme ambao hauwezi kutetemeshwa, basi na tuwe na shukrani, na hivyo tumwabudu Mungu kwa namna inayompendeza, kwa unyenyekevu na uchaji, 29 kwa kuwa “Mungu wetu ni moto ulao.”

  28. 17 Malaika mwingine akatoka katika hekalu lililoko mbinguni, naye pia alikuwa na mundu mkali. 18 Kisha malaika mwingine, aliyekuwa na mamlaka juu ya moto, akatoka kwenye madhabahu, naye akamwita yule malaika mwenye mundu mkali kwa sauti kubwa, akisema, “Chukua mundu wako mkali ukakusanye vichala vya mizabibu ya dunia, maana zabibu zake zimeiva.” 19 Hivyo yule malaika akauzungusha mundu wake duniani na kukusanya zabibu za dunia na kuzitupa kwenye shinikizo kubwa la ghadhabu ya Mungu. 20 Lile shinikizo likakanyagwa nje ya mji, nayo damu ikatiririka kama mafuriko kutoka hilo shinikizo kufikia kimo cha hatamu za farasi, kwa umbali wa maili 200.

  29. 25 Kabla wala baada ya Mfalme Yosia hapakuwepo na mfalme mwingine yeyote ambaye alimpenda Bwana kwa moyo wake wote, kwa roho yake yote, na kwa nguvu zake zote, sawasawa na Sheria yote ya Mose.

    26 Hata hivyo, Bwana hakuacha ghadhabu yake iliyowaka dhidi ya Yuda kwa sababu ya yale yote ambayo Manase alikuwa amefanya kumghadhibisha. 27 Hivyo Bwana akasema, “Nitamwondoa Yuda mbele zangu kama nilivyomwondoa Israeli, nami nitaukataa Yerusalemu, mji niliouchagua, na Hekalu hili, ambalo nilisema, ‘Jina langu litakaa humo.’ ”

  30. 8 Bwana ni mwingi wa huruma na mwenye neema;

    si mwepesi wa hasira, bali amejaa upendo.

  31. 6 Ameharibu maskani yake kama bustani,

    ameharibu mahali pake pa mkutano.

    Bwana amemfanya Sayuni kusahau

    sikukuu zake zilizoamriwa na Sabato zake;

    katika hasira yake kali amewadharau

    mfalme na kuhani.

    7 Bwana amekataa madhabahu yake

    na kuacha mahali patakatifu pake.

    Amemkabidhi adui kuta

    za majumba yake ya kifalme;

    wamepiga kelele katika nyumba ya Bwana

    kama katika siku ya sikukuu iliyoamriwa.

  32. 13 “Ingieni kupitia mlango mwembamba, kwa maana lango ni pana na njia ni pana ielekeayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa kupitia lango hilo. 14 Lakini mlango ni mwembamba na njia ni finyu ielekeayo kwenye uzima, nao ni wachache tu waionao.

  33. 22 Iweje basi, kama Mungu kwa kutaka kuonyesha ghadhabu yake na kufanya uweza wake ujulikane, amevumilia kwa uvumilivu mwingi vile vyombo vya ghadhabu vilivyoandaliwa kwa uharibifu? 23 Iweje basi, kama yeye alitenda hivi ili kufanya wingi wa utukufu wake ujulikane kwa vile vyombo vya rehema yake, alivyotangulia kuvitengeneza kwa ajili ya utukufu wake, 24 yaani pamoja na sisi, ambao pia alituita, si kutoka kwa Wayahudi peke yao, bali pia kutoka kwa watu wa Mataifa?

  34. 9 Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama watu wengine wanavyokudhani kukawia. Badala yake, yeye anawavumilia ninyi, maana hataki mtu yeyote aangamie, bali kila mtu afikilie toba.

  35. 18 Kukawa na mianga ya umeme wa radi, ngurumo, radi na tetemeko kubwa la ardhi. Hapajawa kamwe na tetemeko la ardhi kama hilo tangu mwanadamu awepo duniani, hivyo lilikuwa tetemeko kubwa ajabu. 19 Ule mji mkubwa ukagawanyika katika sehemu tatu, nayo miji ya mataifa ikaanguka. Mungu akaukumbuka Babeli Mkuu na kumpa kikombe kilichojaa mvinyo wa ghadhabu ya hasira yake.

  36. 12 Mbusu Mwana, asije akakasirika

    nawe ukaangamizwa katika njia yako,

    kwa maana hasira yake inaweza kuwaka ghafula.

    Heri wote wanaomkimbilia.

  37. 4 Wewe si Mungu unayefurahia uovu,

    kwako mtu mwovu hataishi.

    5 Wenye kiburi hawawezi kusimama mbele yako,

    unawachukia wote watendao mabaya.

    6 Unawaangamiza wasemao uongo.

    Bwana huwachukia

    wamwagao damu na wadanganyifu.

  38. 4 Bwana yuko ndani ya Hekalu lake takatifu;

    Bwana yuko kwenye kiti chake cha enzi mbinguni.

    Huwaangalia wana wa watu,

    macho yake yanawajaribu.

    5 Bwana huwajaribu wenye haki,

    lakini waovu na wanaopenda jeuri,

    nafsi yake huwachukia.

    6 Atawanyeshea waovu makaa ya moto mkali

    na kiberiti kinachowaka,

    upepo wenye joto kali ndio fungu lao.

    7 Kwa kuwa Bwana ni mwenye haki,

    yeye hupenda haki.

    Wanyofu watauona uso wake.

  39. 6 Ombolezeni, kwa maana siku ya Bwana i karibu,

    itakuja kama uharibifu kutoka kwa Mwenyezi.

    7 Kwa sababu ya hili, mikono yote italegea,

    moyo wa kila mtu utayeyuka.

    8 Hofu itawakamata,

    uchungu na maumivu makali yatawashika,

    watagaagaa kama mwanamke aliye na utungu wa kuzaa.

    Watatazamana kwa hofu kila mtu na mwenzake,

    nyuso zao zikiwaka kama moto.

    9 Tazameni, siku ya Bwana inakuja,

    siku katili, yenye ghadhabu na hasira kali,

    kuifanya nchi kuwa ukiwa

    na kuwaangamiza wenye dhambi waliomo ndani yake.

    10 Nyota za mbinguni na makundi ya nyota

    havitatoa mwanga wake.

    Jua linalochomoza litatiwa giza

    na mwezi hautatoa nuru yake.

    11 Nitauadhibu ulimwengu kwa ajili ya uovu wake,

    waovu kwa ajili ya dhambi zao.

    Nitakomesha majivuno ya wenye kiburi,

    na nitakishusha kiburi cha watu wakatili.

  40. 11 Waambie, ‘Hakika kama mimi niishivyo, asema Bwana Mwenyezi, sifurahii kifo cha watu waovu, bali kwamba wageuke kutoka njia zao mbaya wapate kuishi. Geukeni! Geukeni kutoka njia zenu mbaya! Kwa nini mkafe, ee nyumba ya Israeli?’

  41. 13 Rarueni mioyo yenu

    na siyo mavazi yenu.

    Mrudieni Bwana, Mungu wenu,

    kwa maana yeye ndiye mwenye neema

    na mwingi wa huruma,

    si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa upendo,

    huona huruma, hujizuia kuleta maafa.

    14 Ni nani ajuaye? Yeye aweza kugeuka na kuwa na huruma

    na kuacha baraka nyuma yake:

    sadaka za nafaka na sadaka za vinywaji

    kwa ajili ya Bwana Mungu wenu.

  42. 5 Lakini nitawaambia nani wa kumwogopa: Mwogopeni yule ambaye baada ya kuua mwili, ana mamlaka ya kuwatupa motoni. Naam, nawaambia, mwogopeni huyo!

  43. 10 Kwa kuwa kama tulipokuwa adui wa Mungu tulipatanishwa naye kwa njia ya kifo cha Mwanawe, si zaidi sana tukiisha kupatanishwa, tutaokolewa kwa uzima wake.

  44. 11 Basi, kwa kuwa tunajua kumcha Bwana, tunajitahidi kuwavuta wengine. Lakini Mungu anatufahamu dhahiri, nami natumaini kwamba tu dhahiri katika dhamiri zenu pia.