76 Bible Verses About God's Mercy

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About God's Mercy
  1. 3 Sisi sote pia tuliishi katikati yao hapo zamani, tukitimiza tamaa za asili yetu ya dhambi na kufuata tamaa zake na mawazo yake. Nasi kwa asili tulikuwa wana wa ghadhabu, kama mtu mwingine yeyote. 4 Lakini Mungu kwa upendo wake mwingi kwetu sisi, ambaye ni mwingi wa rehema, 5 hata tulipokuwa wafu kwa ajili ya makosa yetu, alitufanya tuwe hai pamoja na Kristo Yesu, yaani, mmeokolewa kwa neema. 6 Mungu alitufufua pamoja na Kristo na kutuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho katika Kristo Yesu, 7 ili katika ule ulimwengu ujao apate kuonyesha wingi wa neema yake isiyopimika, iliyodhihirishwa kwetu kwa wema wake ndani ya Kristo Yesu. 8 Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani, wala si kwa matendo yenu mema. Hii ni zawadi kutoka kwa Mungu, 9 si kwa matendo, ili mtu yeyote asije akajisifu.

  2. 14 Tuseme nini basi? Je, Mungu ni dhalimu? La, hasha! 15 Kwa maana Mungu alimwambia Mose,

    “Nitamrehemu yeye nimrehemuye,

    na pia nitamhurumia yeye nimhurumiaye.”

    16 Kwa hiyo haitegemei kutaka kwa mwanadamu au jitihada, bali hutegemea huruma ya Mungu. 17 Kwa maana Maandiko yamwambia Farao, “Nilikuinua kwa kusudi hili hasa, ili nipate kuonyesha uweza wangu juu yako, na ili Jina langu lipate kutangazwa duniani yote.”

    18 Kwa hiyo basi, Mungu humhurumia yeye atakaye kumhurumia na humfanya mgumu yeye atakaye kumfanya mgumu.

    19 Basi mtaniambia, “Kama ni hivyo, kwa nini basi bado Mungu anatulaumu? Kwa maana ni nani awezaye kupinga mapenzi yake?” 20 Lakini, ewe mwanadamu, u nani wewe ushindane na Mungu? “Je, kilichoumbwa chaweza kumwambia yeye aliyekiumba, ‘Kwa nini umeniumba hivi?’ ” 21 Je, mfinyanzi hana haki ya kufinyanga kutoka bonge moja vyombo vya udongo, vingine kwa matumizi ya heshima na vingine kwa matumizi ya kawaida?

    22 Iweje basi, kama Mungu kwa kutaka kuonyesha ghadhabu yake na kufanya uweza wake ujulikane, amevumilia kwa uvumilivu mwingi vile vyombo vya ghadhabu vilivyoandaliwa kwa uharibifu? 23 Iweje basi, kama yeye alitenda hivi ili kufanya wingi wa utukufu wake ujulikane kwa vile vyombo vya rehema yake, alivyotangulia kuvitengeneza kwa ajili ya utukufu wake, 24 yaani pamoja na sisi, ambao pia alituita, si kutoka kwa Wayahudi peke yao, bali pia kutoka kwa watu wa Mataifa?

  3. 19 Nayakumbuka mateso yangu na kutangatanga kwangu,

    uchungu na nyongo.

    20 Ninayakumbuka vyema,

    nayo nafsi yangu imezimia ndani yangu.

    21 Hata hivyo najikumbusha neno hili

    na kwa hiyo ninalo tumaini.

    22 Kwa sababu ya upendo mkuu wa Bwana, hatuangamii,

    kwa kuwa huruma zake hazikomi kamwe.

    23 Ni mpya kila asubuhi,

    uaminifu wako ni mkuu.

    24 Nimeiambia nafsi yangu, “Bwana ni fungu langu,

    kwa hiyo nitamngojea.”

  4. 14 Kwa kuwa tunaye Kuhani Mkuu kuliko wote ambaye ameingia mbinguni, Yesu Mwana wa Mungu, basi na tushikamane sana kwa uthabiti na ule ukiri wa imani yetu. 15 Kwa kuwa hatuna Kuhani Mkuu asiyeweza kuchukuliana na sisi katika udhaifu wetu, lakini tunaye mmoja ambaye alijaribiwa kwa kila namna, kama vile sisi tujaribiwavyo: lakini yeye hakutenda dhambi. 16 Basi na tukikaribie kiti cha rehema kwa ujasiri, ili tupewe rehema na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.

  5. 12 Namshukuru Kristo Yesu Bwana wetu, aliyenitia nguvu, kwa sababu aliniona mwaminifu, akaniteua kwa kazi yake. 13 Ingawa wakati fulani nilikuwa mwenye kukufuru, mtesaji na mwenye jeuri, lakini nilipata rehema kwa sababu nilitenda hivyo kwa kutojua na kutoamini kwangu. 14 Neema ya Bwana wetu ilimiminwa juu yangu kwa wingi, ikiambatana na imani na upendo ulio katika Kristo Yesu.

    15 Msemo huu ni wa kweli na unaostahili kukubalika, usemao kwamba: Kristo Yesu alikuja ulimwenguni kuokoa wenye dhambi, ambao mimi ndiye niliye mbaya kuliko wote. 16 Lakini kwa sababu hiyo nilipata rehema, ili katika mimi, niliyekuwa mwenye dhambi kuliko wote, Kristo Yesu apate kuonyesha uvumilivu wake usio na kikomo, ili niwe kielelezo kwa wale watakaomwamini na wapate uzima wa milele. 17 Basi Mfalme wa milele, asiye na mwisho, asiyeonekana, aliye Mungu pekee, apewe heshima na utukufu milele na milele. Amen.

  6. 7 Heri wenye huruma,

    maana hao watapata rehema.

  7. 35 Lakini wapendeni adui zenu, watendeeni mema, wakopesheni bila kutegemea kurudishiwa mlichokopesha. Ndipo thawabu yenu itakapokuwa kubwa, nanyi mtakuwa wana wa Aliye Juu Sana, kwa sababu yeye ni mwema kwa watu wasio na shukrani na kwa wale waovu. 36 Kuweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma.

    37 “Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa. Msilaumu, nanyi hamtalaumiwa. Sameheni, nanyi mtasamehewa.

  8. 4 Nionyeshe njia zako, Ee Bwana,

    nifundishe mapito yako,

    5 niongoze katika kweli yako na kunifundisha,

    kwa maana wewe ni Mungu Mwokozi wangu,

    nalo tumaini langu liko kwako wakati wote.

    6 Kumbuka, Ee Bwana, rehema zako kuu na upendo,

    kwa maana zimekuwepo tangu zamani.

    7 Usizikumbuke dhambi za ujana wangu

    wala njia zangu za uasi,

    sawasawa na upendo wako unikumbuke,

    kwa maana wewe ni mwema, Ee Bwana.

  9. 18 Ni nani Mungu kama wewe,

    ambaye anaachilia dhambi

    na kusamehe makosa

    ya mabaki ya urithi wake?

    Wewe huwi na hasira milele,

    bali unafurahia kuonyesha rehema.

    19 Utatuhurumia tena,

    utazikanyaga dhambi zetu

    chini ya nyayo zako,

    na kutupa maovu yetu yote

    katika vilindi vya bahari.

    20 Utakuwa wa kweli kwa Yakobo,

    nawe utamwonyesha Abrahamu rehema,

    kama ulivyowaahidi kwa kiapo baba zetu

    siku za kale.

  10. 67 Zekaria, baba yake, akajazwa na Roho Mtakatifu, naye akatoa unabii, akisema:

    68 “Ahimidiwe Bwana, Mungu wa Israeli,

    kwa kuwa amewajilia watu wake na kuwakomboa.

    69 Naye ametusimamishia pembe ya wokovu

    katika nyumba ya Daudi mtumishi wake,

    70 kama alivyonena kwa vinywa vya manabii

    wake watakatifu tangu zamani,

    71 kwamba atatuokoa kutoka kwa adui zetu,

    na kutoka mikononi mwao wote watuchukiao:

    72 ili kuonyesha rehema kwa baba zetu

    na kukumbuka Agano lake takatifu,

    73 kiapo alichomwapia baba yetu Abrahamu:

    74 kutuokoa kutoka mikononi mwa adui zetu,

    tupate kumtumikia yeye pasipo hofu

    75 katika utakatifu na haki mbele zake,

    siku zetu zote.

    76 “Nawe mtoto wangu, utaitwa nabii wa Aliye Juu Sana;

    kwa kuwa utamtangulia Bwana

    na kuandaa njia kwa ajili yake,

    77 kuwajulisha watu wake juu ya wokovu

    utakaopatikana kwa kusamehewa dhambi zao,

    78 kwa ajili ya wingi wa rehema za Mungu wetu,

    nuru itokayo juu itatuzukia

    79 ili kuwaangazia wale waishio gizani

    na katika uvuli wa mauti,

    kuiongoza miguu yetu katika njia ya amani.”

  11. 6 Bwana atakuita urudi

    kana kwamba ulikuwa mke aliyeachwa na kuhuzunishwa rohoni;

    kama mke aliyeolewa bado angali kijana

    na kukataliwa,” asema Mungu wako.

    7 “Kwa kitambo kidogo nilikuacha,

    lakini kwa huruma nyingi nitakurudisha.

    8 Katika ukali wa hasira

    nilikuficha uso wangu kwa kitambo,

    lakini kwa fadhili za milele

    nitakuwa na huruma juu yako,”

    asema Bwana Mkombozi wako.

  12. 12 Hivyo semeni na kutenda kama watu watakaohukumiwa kwa sheria ile iletayo uhuru. 13 Kwa kuwa hukumu bila huruma itatolewa kwa mtu yeyote asiyekuwa na huruma. Huruma huishinda hukumu.

  13. 1 Wakumbushe watu kuwanyenyekea watawala na kuwatii wenye mamlaka, wawe tayari kutenda kila lililo jema. 2 Wasimnenee mtu yeyote mabaya, wasiwe wagomvi, bali wawe wapole, wakionyesha unyenyekevu kwa watu wote.

    3 Maana sisi wenyewe wakati fulani tulikuwa wajinga, wasiotii, tukiwa watumwa wa tamaa mbaya na anasa za kila aina. Tuliishi katika uovu na wivu, tukichukiwa na kuchukiana sisi kwa sisi. 4 Lakini wema na upendo wa Mungu Mwokozi wetu ulipofunuliwa, 5 alituokoa, si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyotenda, bali kwa sababu ya rehema zake. Alituokoa kwa kutuosha kwa kuzaliwa mara ya pili na kwa kufanywa wapya kwa njia ya Roho Mtakatifu, 6 ambaye Mungu alitumiminia kwa wingi kwa njia ya Yesu Kristo Mwokozi wetu, 7 ili kwamba, tukiisha kuhesabiwa haki kwa neema yake, tupate kuwa warithi tukiwa na tumaini la uzima wa milele. 8 Hili ni neno la kuaminiwa. Nami nataka uyasisitize mambo haya, ili wale ambao wamemwamini Mungu wapate kuwa waangalifu kujitoa kwa ajili ya kutenda mema wakati wote. Mambo haya ni mazuri tena ya manufaa kwa kila mtu.

    9 Lakini jiepushe na maswali ya kipuzi, mambo ya koo, mabishano na ugomvi kuhusu sheria, kwa sababu hayana faida, tena ni ubatili. 10 Mtu anayesababisha mafarakano, mwonye mara ya kwanza, kisha mwonye mara ya pili. Baada ya hapo, usihusike naye tena. 11 Kwa kuwa unajua kwamba mtu kama huyo amepotoka na tena ni mwenye dhambi. Yeye amejihukumu mwenyewe.

  14. 3 Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo! Kwa rehema zake kuu ametuzaa sisi mara ya pili katika tumaini lenye uzima kupitia kwa kufufuka kwa Yesu Kristo kutoka kwa wafu, 4 ili tuupate urithi usioharibika, usio na uchafu, ule usionyauka: uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu, 5 ninyi ambao mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani, hadi uje ule wokovu ulio tayari kufunuliwa nyakati za mwisho.

  15. 17 “Tengeneza kifuniko cha upatanisho cha dhahabu safi, chenye urefu wa dhiraa mbili na nusu, na upana wa dhiraa moja na nusu. 18 Tengeneza makerubi wawili wa dhahabu iliyofuliwa katika miisho ya hicho kifuniko. 19 Tengeneza kerubi mmoja kwenye mwisho mmoja, na kerubi mwingine kwenye mwisho mwingine; watengeneze makerubi hao wawe kitu kimoja na hicho kifuniko katika miisho hiyo miwili. 20 Makerubi hao watakuwa wametandaza mabawa kuelekea juu, yakitia kivuli hicho kifuniko. Makerubi hao wataelekeana, wakitazama hicho kifuniko. 21 Weka huo Ushuhuda nitakaokupa ndani ya hilo Sanduku la Agano, na uweke hicho kifuniko juu ya hilo Sanduku. 22 Hapo juu ya hicho kifuniko, kati ya hao makerubi wawili walioko juu ya hilo Sanduku la Ushuhuda, hapo ndipo nitakapokutana nawe na kukupa maagizo yangu kwa ajili ya Waisraeli.

  16. Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Baada ya kukemewa na nabii Nathani kwa kuzini na Bathsheba.

    1 Ee Mungu, unihurumie,

    kwa kadiri ya upendo wako usiokoma,

    kwa kadiri ya huruma yako kuu,

    uyafute makosa yangu.

    2 Unioshe na uovu wangu wote

    na unitakase dhambi yangu.

    3 Kwa maana ninajua makosa yangu,

    na dhambi yangu iko mbele yangu daima.

    4 Dhidi yako, wewe peke yako, nimetenda dhambi

    na kufanya yaliyo mabaya machoni pako,

    ili uthibitike kuwa wa kweli unenapo,

    na kuwa na haki utoapo hukumu.

  17. 5 Kisha Bwana akashuka katika wingu akasimama pamoja naye huko, akalitangaza jina lake, Bwana. 6 Bwana akapita mbele ya Mose, akitangaza, “Bwana, Bwana, Mungu mwenye huruma na neema, asiye mwepesi wa hasira, mwingi wa upendo na uaminifu, 7 akidumisha upendo kwa maelfu, pia akisamehe uovu, uasi na dhambi. Lakini haachi kuadhibu mwenye hatia; huwaadhibu watoto na watoto wao kwa ajili ya dhambi ya baba zao hata katika kizazi cha tatu na cha nne.”

  18. 1 Kwa hiyo, ndugu zangu, nawasihi kwa rehema zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu na inayompendeza Mungu, hii ndiyo ibada yenu yenye maana. 2 Msifuatishe tena mfano wa ulimwengu huu, bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu. Ndipo mtaweza kuonja na kuhakikisha ni nini mapenzi ya Mungu yaliyo mema, yanayopendeza machoni pake na ukamilifu.

  19. 8 Bwana ni mwenye neema na mwingi wa huruma,

    si mwepesi wa hasira, bali ni mwingi wa upendo.

    9 Bwana ni mwema kwa wote,

    ana huruma kwa vyote alivyovifanya.

  20. 17 “Basi sasa nguvu za Bwana na zionekane, sawasawa na vile ulivyosema: 18 ‘Bwana si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa upendo na mwenye kusamehe dhambi na uasi. Lakini haachi kumwadhibu mwenye hatia, huadhibu watoto kwa ajili ya dhambi ya baba zao hata kizazi cha tatu na cha nne.’ 19 Kwa kadiri ya upendo wako mkuu, usamehe dhambi ya watu hawa, kama vile ulivyowasamehe tangu wakati walitoka Misri mpaka sasa.”

  21. 10 yeye hatutendei kulingana na dhambi zetu

    wala hatupatilizi kwa kadiri ya maovu yetu.

    11 Kama vile mbingu zilivyo juu ya dunia sana,

    ndivyo wema wake ulivyo mwingi kwa wanaomcha;

    12 kama mashariki ilivyo mbali na magharibi,

    ndivyo Mungu alivyoziweka dhambi zetu mbali nasi.

    13 Kama baba alivyo na huruma kwa watoto wake,

    ndivyo Bwana anavyowahurumia wale wanaomcha;

    14 kwa kuwa anajua tulivyoumbwa,

    anakumbuka kwamba sisi tu mavumbi.

  22. 6 Mtafuteni Bwana maadamu anapatikana;

    mwiteni maadamu yu karibu.

    7 Mtu mwovu na aiache njia yake,

    na mtu mbaya na ayaache mawazo yake.

    Yeye na amrudie Bwana, naye atamrehemu,

    arudi kwa Mungu wetu, kwa kuwa atamsamehe bure kabisa.

    8 “Kwa kuwa mawazo yangu si mawazo yenu,

    wala njia zenu si njia zangu,”

    asema Bwana.

    9 “Kama vile mbingu zilivyo juu kuliko dunia,

    ndivyo njia zangu zilivyo juu kuliko njia zenu

    na mawazo yangu kuliko mawazo yenu.

    10 Kama vile mvua na theluji

    ishukavyo kutoka mbinguni,

    nayo hairudi tena huko

    bila kunywesha dunia

    na kuichipusha na kuistawisha,

    hivyo hutoa mbegu kwa mpanzi

    na mkate kwa mlaji,

    11 ndivyo lilivyo neno langu lile litokalo kinywani mwangu:

    Halitanirudia tupu,

    bali litatimiliza lile nililokusudia

    na litafanikiwa katika kusudi lile nililolituma.

  23. 8 Amekuonyesha yaliyo mema, ee mwanadamu.

    Bwana anataka nini kwako?

    Ila kutenda kwa haki na kupenda rehema,

    na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako.

  24. 15 Lakini wewe, Ee Bwana, ni Mungu wa huruma na neema,

    si mwepesi wa hasira, bali ni mwingi wa upendo na uaminifu.

    16 Nigeukie na unihurumie;

    mpe mtumishi wako nguvu zako,

    mwokoe mwana wa mtumishi wako wa kike.

  25. 12 “Hata sasa,” asema Bwana,

    “nirudieni kwa mioyo yenu yote,

    kwa kufunga, kwa kulia na kuomboleza.”

    13 Rarueni mioyo yenu

    na siyo mavazi yenu.

    Mrudieni Bwana, Mungu wenu,

    kwa maana yeye ndiye mwenye neema

    na mwingi wa huruma,

    si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa upendo,

    huona huruma, hujizuia kuleta maafa.

    14 Ni nani ajuaye? Yeye aweza kugeuka na kuwa na huruma

    na kuacha baraka nyuma yake:

    sadaka za nafaka na sadaka za vinywaji

    kwa ajili ya Bwana Mungu wenu.

  26. 50 Rehema zake huwaendea wale wamchao,

    kutoka kizazi hadi kizazi.

  27. 5 Ee Bwana, wewe ni mwema na mwenye kusamehe,

    umejaa upendo kwa wote wakuitao.

  28. 12 Nenda, ukatangaze ujumbe huu kuelekea kaskazini:

    “ ‘Rudi, Israeli usiye mwaminifu,’ asema Bwana,

    ‘sitakutazama tena kwa uso uliokunjamana,

    kwa kuwa mimi ni mwenye huruma,’ asema Bwana,

    ‘Sitashika hasira yangu milele.

  29. 1 Msifuni Bwana.

    Mshukuruni Bwana, kwa kuwa ni mwema;

    upendo wake wadumu milele.

  30. 9 Bwana Mungu wetu ni mwenye rehema na anayesamehe, hata ingawa tumefanya uasi dhidi yake.

  31. 8 Bwana ni mwingi wa huruma na mwenye neema;

    si mwepesi wa hasira, bali amejaa upendo.

  32. 13 Yeye afichaye dhambi zake hatafanikiwa,

    bali yeyote aziungamaye na kuziacha hupata rehema.

    14 Amebarikiwa mtu ambaye siku zote humcha Bwana,

    bali yeye afanyaye moyo wake kuwa mgumu

    huangukia kwenye taabu.

  33. 13 Nendeni mkajifunze maana ya maneno haya: ‘Nataka rehema, wala si dhabihu.’ Kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.”

  34. 21 Ndipo Petro akamjia Yesu na kumuuliza, “Bwana, ndugu yangu anikosee mara ngapi nami nimsamehe? Je, hata mara saba?”

    22 Yesu akamjibu, “Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini.

    23 “Kwa hiyo Ufalme wa Mbinguni unaweza kufananishwa na mfalme aliyetaka kufanya hesabu zake za fedha na watumishi wake. 24 Alipoanza kufanya hesabu zake, mtu mmoja aliyekuwa anadaiwa talanta 10,000, aliletwa kwake. 25 Kwa kuwa alikuwa hawezi kulipa deni hilo, bwana wake akaamuru kwamba auzwe, yeye, mkewe, watoto wake na vyote alivyokuwa navyo, ili lile deni lipate kulipwa.

    26 “Yule mtumishi akampigia magoti, akamsihi yule bwana akisema, ‘Naomba univumilie, nami nitakulipa deni lako lote.’ 27 Yule bwana wa huyo mtumishi akamwonea huruma, akafuta deni lake lote, akamwacha aende zake.

    28 “Lakini yule mtumishi alipokuwa anatoka nje, akakutana na mtumishi mwenzake aliyekuwa amemkopesha dinari mia moja. Akamkamata, akamkaba koo akimwambia, ‘Nilipe kile ninachokudai!’

    29 “Yule mtumishi mwenzake akapiga magoti akamsihi akisema, ‘Naomba univumilie, nami nitakulipa deni lako lote.’

    30 “Lakini akakataa. Badala yake, alienda akamtupa gerezani hata atakapolipa hilo deni. 31 Watumishi wenzake walipoona haya yaliyotukia wakaudhika sana, nao wakaenda na kumwambia bwana wao kila kitu kilichokuwa kimetukia.

    32 “Yule bwana akamwita yule mtumishi akamwambia, ‘Wewe mtumishi mwovu! Mimi nilikusamehe deni lako lote uliponisihi. 33 Je, haikukupasa kumhurumia mtumishi mwenzako kama mimi nilivyokuhurumia wewe?’ 34 Kwa hasira, yule bwana wake akamtia yule mtumishi mikononi mwa askari wa gereza ili ateswe mpaka atakapolipa yote aliyokuwa anadaiwa.

    35 “Hivi ndivyo Baba yangu wa mbinguni atakavyomfanyia kila mmoja wenu ikiwa hatamsamehe ndugu yake kutoka moyoni mwake.”

  35. 29 Yesu na wanafunzi wake walipokuwa wakiondoka Yeriko, umati mkubwa wa watu ulimfuata. 30 Vipofu wawili walikuwa wameketi kando ya barabara. Waliposikia kwamba Yesu alikuwa anapita, wakapiga kelele wakisema, “Bwana, Mwana wa Daudi, tuhurumie!”

    31 Ule umati wa watu ukawakemea na kuwaambia wanyamaze, lakini wao wakazidi kupaza sauti, wakisema, “Bwana, Mwana wa Daudi, tuhurumie.”

    32 Yesu akasimama na kuwaita, akawauliza, “Mnataka niwafanyie nini?”

    33 Wakamjibu, “Bwana, tunataka kuona.”

    34 Yesu akawahurumia na kuwagusa macho yao. Mara macho yao yakapata kuona, nao wakamfuata.

  36. 21 Lakini sasa, haki itokayo kwa Mungu imedhihirishwa pasipo sheria, ambayo Sheria na Manabii wanaishuhudia. 22 Haki hii itokayo kwa Mungu hupatikana kwa Yesu Kristo kwa wote wamwaminio. Kwa maana hapo hakuna tofauti, 23 kwa kuwa wote wametenda dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu, 24 wanahesabiwa haki bure kwa neema yake kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu. 25 Yeye ambaye Mungu alimtoa awe dhabihu ya upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake. Alifanya hivi ili kuonyesha haki yake, kwa sababu kwa ustahimili wake aliziachilia zile dhambi zilizotangulia kufanywa. 26 Alifanya hivyo ili kuonyesha haki yake wakati huu, ili yeye awe mwenye haki na mwenye kumhesabia haki yule anayemwamini Yesu.

    27 Basi, kujivuna kuko wapi? Kumewekwa mbali. Kwa sheria gani? Je, ni kwa ile ya matendo? La hasha, bali kwa ile sheria ya imani.

  37. 31 Kwa maana Bwana Mungu wenu ni Mungu mwenye huruma, hatawaacha au kuwaangamiza wala kusahau Agano alilofanya na baba zenu, alilowathibitishia kwa kiapo.

  38. 14 Walipofika penye umati wa watu, mtu mmoja akamjia Yesu na kupiga magoti mbele yake, akasema, 15 “Bwana, mhurumie mwanangu. Yeye ana kifafa na anateseka sana. Mara kwa mara huanguka kwenye moto au kwenye maji. 16 Nilimleta kwa wanafunzi wako, lakini hawakuweza kumponya.”

    17 Yesu akajibu, “Enyi kizazi kisichoamini na kilichopotoka! Nitakaa nanyi mpaka lini? Nitawavumilia mpaka lini? Mleteni mvulana hapa kwangu.” 18 Yesu akamkemea yule pepo mchafu, akamtoka yule kijana, naye akapona saa ile ile.

  39. 3 Ahimidiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa huruma na Mungu wa faraja yote. 4 Yeye hutufariji katika taabu zetu, ili tuweze kuwafariji walio katika taabu yoyote kwa faraja ambayo sisi wenyewe tumepokea kutoka kwa Mungu.

  40. 13 Pigeni kelele kwa furaha, enyi mbingu;

    furahi, ee dunia;

    pazeni sauti kwa kuimba, enyi milima!

    Kwa maana Bwana anawafariji watu wake,

    naye atakuwa na huruma kwa watu wake walioumizwa.

  41. 21 Yesu aliondoka mahali pale, akaenda sehemu za Tiro na Sidoni. 22 Mwanamke mmoja Mkanaani aliyeishi sehemu jirani na hizo akaja kwake akilia, akasema, “Nihurumie, Ee Bwana, Mwana wa Daudi! Binti yangu amepagawa na pepo mchafu, na anateseka sana.”

    23 Lakini Yesu hakumjibu neno. Hivyo wanafunzi wake wakamwendea na kumsihi sana, wakisema, “Mwambie aende zake, kwa maana anaendelea kutupigia kelele.”

    24 Yesu akajibu, “Nimetumwa tu kwa ajili ya kondoo wa Israeli waliopotea.”

    25 Lakini yule mwanamke akaja, akapiga magoti mbele ya Yesu, akasema, “Bwana, nisaidie!”

    26 Yesu akajibu, “Si haki kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.”

    27 Yule mwanamke akajibu, “Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yanayoanguka kutoka kwenye meza za bwana zao.”

    28 Ndipo Yesu akamwambia, “Mwanamke, imani yako ni kubwa! Iwe kwako kama unavyotaka.” Naye binti yake akapona tangu saa ile.

  42. 19 Ndipo Bwana akasema, “Nitapitisha wema wangu wote mbele yako, nami nitalitangaza Jina langu, Bwana, mbele ya uso wako. Nitamrehemu yeye nimrehemuye, na pia nitamhurumia yeye nimhurumiaye.”

  43. 14 Daudi akamjibu Gadi, “Nitataabika sana. Afadhali tuangukie mikononi mwa Bwana, kwa maana rehema zake ni kuu, lakini usiniache nianguke mikononi mwa wanadamu.”

  44. 27 Hivyo ukawatia mikononi mwa adui zao, ambao waliwatesa. Lakini walipoteswa, wakakulilia wewe. Kutoka mbinguni uliwasikia, nawe kwa huruma zako kuu ukawapa waokozi, waliowaokoa kutoka mikononi mwa adui zao.

  45. 17 Lakini ninyi wapenzi, kumbukeni yale mitume wa Bwana Yesu Kristo waliyonena zamani. 18 Kwa kuwa waliwaambia, “Siku za mwisho kutakuwa na watu wenye kudhihaki, watakaofuata tamaa zao wenyewe za upotovu.” 19 Hawa ndio watu wanaowagawa ninyi, wafuatao tamaa zao za asili, wala hawana Roho.

    20 Lakini ninyi wapendwa, jijengeni katika imani yenu iliyo takatifu sana tena ombeni katika Roho Mtakatifu. 21 Jilindeni katika upendo wa Mungu mkitazamia kwa furaha rehema ya Bwana wetu Yesu Kristo ili awalete katika uzima wa milele.

    22 Wahurumieni walio na mashaka; 23 wengine waokoeni kwa kuwanyakua kutoka kwenye moto; nao wengine wahurumieni mkiwa na hofu, mkichukia hata vazi lenye mawaa na kutiwa unajisi na mwili.

  46. 15 Kunako mapambazuko, malaika wakamhimiza Loti, wakamwambia, “Fanya haraka! Mchukue mke wako na binti zako wawili walioko hapa, la sivyo utaangamizwa wakati mji utakapoadhibiwa.”

    16 Alipositasita, wale watu wakamshika mkono wake na mikono ya mke wake na binti zake wawili na kuwaongoza salama nje ya mji, kwa kuwa Bwana alikuwa na huruma kwao. 17 Mara walipokwisha kuwatoa nje, mmoja wao akawaambia, “Mkimbie kwa usalama wenu! Msitazame nyuma, wala msisimame popote katika nchi tambarare! Kimbilieni milimani, ama sivyo mtaangamizwa!”

    18 Lakini Loti akawajibu, “La hasha, bwana zangu, tafadhalini! 19 Mtumishi wenu amepata kibali mbele ya macho yenu, nanyi mmeonyesha wema mkubwa kwangu kwa kuokoa maisha yangu. Lakini siwezi kukimbilia milimani, janga hili litanikumba, nami nitakufa. 20 Tazama, hapa kuna mji karibu wa kukimbilia, nao ni mdogo. Niruhusuni nikimbilie humo, ni mdogo sana, ama sivyo? Ndipo maisha yangu yatasalimika.”

    21 Akamwambia, “Vema sana, nitalikubali hili ombi pia, sitauangamiza mji ulioutaja. 22 Lakini ukimbilie huko haraka, kwa sababu sitaweza kufanya lolote mpaka ufike huko.” (Ndiyo maana mji huo ukaitwa Soari.)

  47. 30 Kwa miaka mingi ulikuwa mvumilivu kwao. Kwa njia ya Roho wako ukawaonya kupitia manabii wako. Hata hivyo hawakujali, basi ukawatia mikononi mwa mataifa jirani. 31 Lakini kwa rehema zako kuu hukuwakomesha wala kuwaacha, kwa kuwa wewe ni Mungu mwenye neema na rehema.

  48. 18 Nitaondoka na kurudi kwa baba yangu na kumwambia: Baba, nimetenda dhambi mbele za Mungu na mbele yako. 19 Sistahili tena kuitwa mwanao; nifanye kama mmoja wa watumishi wako.’ 20 Basi akaondoka, akaenda kwa baba yake.

    “Lakini alipokuwa bado yuko mbali, baba yake akamwona, moyo wake ukajawa na huruma. Akamkimbilia mwanawe, akamkumbatia na kumbusu.

    21 “Yule mwana akamwambia baba yake, ‘Baba, nimekosa mbele za Mungu na mbele yako. Sistahili kuitwa mwanao tena.’

    22 “Lakini baba yake akawaambia watumishi, ‘Leteni upesi joho lililo bora sana, tieni pete kidoleni mwake na viatu miguuni mwake. 23 Leteni ndama aliyenona, mkamchinje ili tuwe na karamu, tule na kufurahi. 24 Kwa maana huyu mwanangu alikuwa amekufa na sasa yu hai tena; alikuwa amepotea na sasa amepatikana!’ Nao wakaanza kufanya tafrija.

  49. 8 Kama tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe wala kweli haimo ndani yetu. 9 Kama tukiziungama dhambi zetu, yeye ni mwaminifu na wa haki, atatusamehe dhambi zetu na kutusafisha kutoka kwenye udhalimu wote. 10 Kama tukisema hatukutenda dhambi, twamfanya yeye kuwa mwongo na neno lake halimo ndani yetu.

  50. 18 Hata hivyo Bwana anatamani kutupatia neema,

    anainuka ili kuwaonyesha huruma.

    Kwa kuwa Bwana ni Mungu wa haki.

    Wamebarikiwa wote wanaomngojea yeye!

  51. 14 Kwa kuwa kama mkiwasamehe watu wengine wanapowakosea, Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi pia. 15 Lakini msipowasamehe watu wengine makosa yao, naye Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.

  52. 16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. 17 Kwa maana Mungu hakumtuma Mwanawe kuuhukumu ulimwengu, bali kupitia kwake ulimwengu upate kuokolewa.

  53. 28 Kwa habari ya Injili, wao ni adui wa Mungu kwa ajili yenu, lakini kuhusu kule kuteuliwa kwao ni wapendwa, kwa ajili ya mababa zao wa zamani, 29 kwa maana akishawapa watu karama, Mungu haziondoi, wala wito wake. 30 Kama vile ninyi wakati fulani mlivyokuwa waasi kwa Mungu lakini sasa mmepata rehema kwa sababu ya kutokutii kwao, 31 hivyo nao Waisraeli wamekuwa waasi ili kwamba wao nao sasa waweze kupata rehema kwa ajili ya rehema za Mungu kwenu. 32 Kwa maana Mungu amewafunga wanadamu wote kwenye kuasi ili apate kuwarehemu wote.

  54. 25 Lakini nadhani ni muhimu kumtuma tena kwenu Epafrodito, ndugu yangu na mtendakazi pamoja nami, aliye askari mwenzangu, ambaye pia ni mjumbe wenu mliyemtuma ili ashughulike na mahitaji yangu. 26 Kwa maana amekuwa akiwaonea sana shauku ninyi nyote, akiwa na wasiwasi kwa kuwa mlisikia kwamba alikuwa mgonjwa. 27 Kweli alikuwa mgonjwa, tena karibu ya kufa. Lakini Mungu alimhurumia, wala si yeye tu, bali hata na mimi alinihurumia, nisipatwe na huzuni juu ya huzuni. 28 Kwa hiyo mimi ninafanya bidii kumtuma kwenu ili mtakapomwona kwa mara nyingine, mpate kufurahi, nami wasiwasi wangu upungue. 29 Kwa hiyo mpokeeni katika Bwana kwa furaha kubwa, nanyi wapeni heshima watu kama hawa, 30 kwa sababu alikaribia kufa kwa ajili ya kazi ya Kristo, akihatarisha maisha yake ili aweze kunihudumia vile ninyi hamkuweza.

  55. 2 Unirehemu Bwana,

    kwa maana nimedhoofika;

    Ee Bwana, uniponye,

    kwa maana mifupa yangu

    ina maumivu makali.

  56. 31 Kwa kuwa watu hawakatiliwi mbali

    na Bwana milele.

    32 Ingawa huleta huzuni, ataonyesha huruma,

    kwa kuwa upendo wake usiokoma ni mkuu.

    33 Kwa maana hapendi kuwaletea mateso

    au huzuni watoto wa wanadamu.

  57. 23 Nitampanda katika nchi kwa ajili yangu mwenyewe;

    nami nitaonyesha pendo langu kwake

    yule ambaye nilimwita, ‘Si mpenzi wangu.’

    Nitawaambia wale walioitwa, ‘Sio watu wangu,’

    ‘Ninyi ni watu wangu’;

    nao watasema, ‘Wewe ndiwe Mungu wangu.’ ”

  58. 13 Ni nani aliye na hekima na ufahamu miongoni mwenu? Basi na aionyeshe hiyo kwa maisha yake mema na kwa matendo yake yaliyotendwa kwa unyenyekevu utokanao na hekima. 14 Lakini ikiwa mna wivu na ni wenye chuki na ugomvi mioyoni mwenu, msijisifu kwa ajili ya hayo wala msiikatae kweli. 15 Hekima ya namna hiyo haishuki kutoka mbinguni, bali ni ya kidunia, isiyo ya kiroho, na ya kishetani. 16 Kwa maana panapokuwa na wivu na ubinafsi, ndipo penye machafuko na uovu wa kila namna.

    17 Lakini hekima itokayo mbinguni kwanza ni safi, kisha inapenda amani, tena ni ya upole, iliyo tayari kusikiliza wengine kwa unyenyekevu, iliyojaa huruma na matunda mema, isiyopendelea mtu, tena isiyokuwa na unafiki.

  59. 10 Mwanzo ninyi mlikuwa si taifa, lakini sasa ninyi ni taifa la Mungu. Mwanzo mlikuwa hamjapata rehema, lakini sasa mmepata rehema.

  60. 10 Sikuficha haki yako moyoni mwangu;

    ninasema juu ya uaminifu wako na wokovu wako.

    Sikuficha upendo wako na kweli yako

    mbele ya kusanyiko kubwa.

    11 Ee Bwana, usizuilie huruma zako,

    upendo wako na kweli yako daima vinilinde.

    12 Kwa maana taabu zisizo na hesabu zimenizunguka,

    dhambi zangu zimenikamata, hata nisiweze kuona.

    Zimekuwa nyingi kuliko nywele za kichwa changu,

    nao moyo unazimia ndani yangu.

  61. 27 Yesu alipokuwa akiondoka mahali pale, vipofu wawili wakamfuata wakipiga kelele kwa nguvu na kusema, “Mwana wa Daudi, tuhurumie!”

    28 Alipoingia mle nyumbani wale vipofu wakamjia. Naye Yesu akawauliza, “Mnaamini kwamba ninaweza kufanya jambo hili?”

    Wakamjibu, “Ndiyo, Bwana.”

    29 Ndipo Yesu akagusa macho yao na kusema, “Iwe kwenu sawasawa na imani yenu.” 30 Macho yao yakafunguka. Yesu akawaonya vikali, akisema, “Angalieni mtu yeyote asijue kuhusu jambo hili.” 31 Lakini wao wakaenda na kueneza habari zake katika eneo lile lote.

  62. 8 Kwa habari ya jambo hili nilimsihi Bwana mara tatu aniondolee mwiba huu. 9 Lakini aliniambia, “Neema yangu inakutosha, kwa kuwa uweza wangu hukamilika katika udhaifu.” Kwa hiyo nitajisifu kwa furaha zaidi kuhusu udhaifu wangu, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. 10 Hii ndiyo sababu, kwa ajili ya Kristo, nafurahia udhaifu, katika kutukanwa, katika taabu, katika mateso na katika shida, kwa maana ninapokuwa dhaifu, ndipo nina nguvu.

  63. 11 Kama mnavyojua, tunawahesabu kuwa wabarikiwa wale waliovumilia. Mmesikia habari za uvumilivu wake Ayubu na mmeona kile ambacho hatimaye Bwana alimtendea. Bwana ni mwingi wa huruma, na amejaa rehema.

  64. 10 Upendo na uaminifu hukutana pamoja,

    haki na amani hubusiana.

  65. 4 Ndipo nikaliitia jina la Bwana:

    “Ee Bwana, niokoe!”

    5 Bwana ni mwenye neema na haki,

    Mungu wetu ni mwingi wa huruma.

    6 Bwana huwalinda wanyenyekevu,

    nilipokuwa katika shida kubwa, aliniokoa.

  66. 7 Nitasimulia juu ya wema wa Bwana,

    kwa matendo ambayo apaswa kusifiwa,

    sawasawa na yote ambayo Bwana

    ametenda kwa ajili yetu:

    naam, mambo mengi mema aliyoyatenda

    kwa ajili ya nyumba ya Israeli,

    sawasawa na huruma zake

    na wema wake mwingi.

    8 Alisema, “Hakika wao ni watu wangu,

    wana ambao hawatanidanganya”;

    hivyo akawa Mwokozi wao.

  67. 6 Kwa maana nataka rehema, wala si dhabihu,

    kumkubali Mungu zaidi

    kuliko sadaka za kuteketezwa.

  68. 2 Bwana, nimezisikia sifa zako;

    nami naogopa kwa matendo yako, Ee Bwana.

    Fufua kazi yako katikati ya miaka,

    katikati ya miaka tangaza habari yako;

    katika ghadhabu kumbuka rehema.

  69. 17 “Nao watakuwa watu wangu,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote, “katika siku ile nitakapowafanya watu kuwa hazina yangu. Nitawahurumia, kama vile kwa huruma mtu amhurumiavyo mwanawe anayemtumikia.

  70. 25 Wakati huo mtaalamu mmoja wa sheria alisimama ili kumjaribu Yesu, akamuuliza, “Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?”

    26 Yesu akamjibu, “Imeandikwaje katika Sheria? Kwani unasoma nini humo?”

    27 Akajibu, “ ‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote’; tena, ‘Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.’ ”

    28 Yesu akamwambia, “Umejibu vyema. Fanya hivyo nawe utaishi.”

    29 Lakini yule mtaalamu wa sheria, akitaka kujionyesha kuwa mwenye haki, akamuuliza Yesu, “Jirani yangu ni nani?”

    30 Yesu akamjibu akasema, “Mtu mmoja alikuwa akiteremka kutoka Yerusalemu kwenda Yeriko, naye akaangukia mikononi mwa wanyangʼanyi. Wakampiga, wakaondoka, wakamwacha akiwa karibu kufa. 31 Kuhani mmoja alikuwa akipitia njia ile, alipomwona huyo mtu, akapita upande mwingine, akamwacha hapo barabarani. 32 Vivyo hivyo, Mlawi mmoja naye alipofika mahali pale, alimwona, akapita upande mwingine, akamwacha hapo barabarani 33 Lakini Msamaria mmoja aliyekuwa akisafiri alipomwona, alimhurumia. 34 Akaenda alipokuwa na akasafisha majeraha yake kwa divai na mafuta, kisha akayafunga. Ndipo akampandisha kwenye punda wake, akampeleka mpaka kwenye nyumba ya wageni na kumtunza. 35 Kesho yake, yule Msamaria akachukua dinari mbili akampa yule mwenye nyumba ya wageni na kusema, ‘Mtunze, nami nirudipo nitakulipa gharama yoyote ya ziada uliyotumia kwa ajili yake.’

    36 “Ni yupi basi miongoni mwa hawa watatu wewe unadhani ni jirani yake yule mtu aliyeangukia mikononi mwa wanyangʼanyi?”

    37 Yule mtaalamu wa sheria akajibu, “Ni yule aliyemhurumia.”

    Ndipo Yesu akamwambia, “Nenda, ukafanye vivyo hivyo.”

  71. 9 Yesu akatoa mfano huu kwa wale waliojiamini kuwa wao ni wenye haki na kuwadharau wengine: 10 “Watu wawili walikwenda Hekaluni kusali, mmoja wao alikuwa Farisayo na mwingine alikuwa mtoza ushuru. 11 Yule Farisayo, akasimama, akasali hivi na kuomba kwake mwenyewe: ‘Mungu, nakushukuru kwa sababu mimi si kama watu wengine ambao ni wanyangʼanyi, wadhalimu, na wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. 12 Mimi nafunga mara mbili kwa juma, na natoa sehemu ya kumi ya mapato yangu.’

    13 “Lakini yule mtoza ushuru akasimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua uso wake kutazama mbinguni, bali alijipigapiga kifuani na kusema: ‘Mungu, nihurumie, mimi mwenye dhambi.’

    14 “Nawaambia, huyu mtoza ushuru alirudi nyumbani akiwa amehesabiwa haki mbele za Mungu zaidi ya yule Farisayo. Kwa maana yeyote ajikwezaye atashushwa, na yeyote ajishushaye atakwezwa.”

  72. 8 Kwa maana nawaambia kwamba, Kristo amekuwa mtumishi kwa wale waliotahiriwa ili kuonyesha kweli ya Mungu na kuthibitisha zile ahadi walizopewa baba zetu wa zamani, 9 pia ili watu wa Mataifa wamtukuze Mungu kwa rehema zake. Kama ilivyoandikwa:

    “Kwa hiyo nitakutukuza katikati ya watu wa Mataifa;

    nitaliimbia sifa jina lako.”

    10 Tena yasema,

    “Enyi watu wa Mataifa, furahini

    pamoja na watu wa Mungu.”

    11 Tena,

    “Msifuni Bwana, ninyi watu wa Mataifa wote,

    na kumwimbia sifa, enyi watu wote.”

    12 Tena Isaya anasema,

    “Shina la Yese litachipuka,

    yeye atakayeinuka ili kutawala juu ya mataifa.

    Watu wa Mataifa watamtumaini.”

    13 Mungu wa tumaini awajaze ninyi furaha yote na amani katika kumwamini, ili mpate kujawa na tumaini tele kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.

  73. 31 Ondoeni kabisa uchungu, ghadhabu, hasira, makelele na masingizio pamoja na kila aina ya uovu. 32 Kuweni wafadhili na wenye kuhurumiana ninyi kwa ninyi, mkisameheana, kama vile naye Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.

  74. 9 Kama mkimrudia Bwana ndipo wale ndugu zenu waliotekwa pamoja na watoto wenu watakapoonewa huruma na wale waliowateka na kuwaachia warudi katika nchi hii, kwa kuwa Bwana Mungu wenu ni mwenye neema na huruma, hatageuzia uso wake mbali nanyi kama ninyi mkimrudia yeye.”

  75. 5 Kisha nilikujulisha dhambi yangu

    wala sikuficha uovu wangu.

    Nilisema, “Nitaungama

    makosa yangu kwa Bwana.”

    Ndipo uliponisamehe

    hatia ya dhambi yangu.

  76. Wimbo wa kwenda juu.

    1 Kutoka vilindini ninakulilia, Ee Bwana.

    2 Ee Bwana, sikia sauti yangu.

    Masikio yako na yawe masikivu

    kwa kilio changu unihurumie.

    3 Kama wewe, Ee Bwana, ungeweka kumbukumbu ya dhambi,

    Ee Bwana, ni nani angeliweza kusimama?

    4 Lakini kwako kuna msamaha,

    kwa hiyo wewe unaogopwa.