30 Bible Verses About Envy

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Envy
  1. 19 Basi matendo ya mwili ni dhahiri nayo ni haya: Uasherati, uchafu, ufisadi, 20 kuabudu sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, 21 husuda, ulevi, ulafi na mambo mengine yanayofanana na hayo. Nawaonya, kama nilivyokwisha kuwaonya kabla, kwamba watu watendao mambo kama hayo, hawataurithi Ufalme wa Mungu.

    22 Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, 23 upole na kiasi. Katika mambo kama haya hakuna sheria. 24 Wote walio wa Kristo Yesu wameusulubisha mwili na shauku zake pamoja na tamaa zake. 25 Kwa kuwa tunaishi kwa Roho, basi, tuenende kwa Roho. 26 Tusijisifu bure, tukichokozana na kuoneana wivu.

  2. 13 Ni nani aliye na hekima na ufahamu miongoni mwenu? Basi na aionyeshe hiyo kwa maisha yake mema na kwa matendo yake yaliyotendwa kwa unyenyekevu utokanao na hekima. 14 Lakini ikiwa mna wivu na ni wenye chuki na ugomvi mioyoni mwenu, msijisifu kwa ajili ya hayo wala msiikatae kweli. 15 Hekima ya namna hiyo haishuki kutoka mbinguni, bali ni ya kidunia, isiyo ya kiroho, na ya kishetani. 16 Kwa maana panapokuwa na wivu na ubinafsi, ndipo penye machafuko na uovu wa kila namna.

    17 Lakini hekima itokayo mbinguni kwanza ni safi, kisha inapenda amani, tena ni ya upole, iliyo tayari kusikiliza wengine kwa unyenyekevu, iliyojaa huruma na matunda mema, isiyopendelea mtu, tena isiyokuwa na unafiki.

  3. 4 Upendo huvumilia, upendo hufadhili, upendo hauoni wivu, hauna majivuno, hauna kiburi. 5 Haukosi kuwa na adabu, hautafuti mambo yake, haukasiriki upesi, hauweki kumbukumbu ya mabaya. 6 Upendo haufurahii mabaya bali hufurahi pamoja na kweli.

  4. 30 Moyo wenye amani huupa mwili uzima,

    bali wivu huozesha mifupa.

  5. 1 Kwa hiyo, wekeni mbali nanyi uovu wote na udanganyifu wote, unafiki, wivu na masingizio ya kila namna. 2 Kama watoto wachanga, waliozaliwa sasa, yatamanini maziwa ya kiroho yasiyochanganywa na kitu kingine chochote, ili kwa hayo mpate kukua katika wokovu, 3 ikiwa kweli mmeonja ya kwamba Bwana ni mwema.

  6. 1 Ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama watu wa kiroho, bali kama watu wa mwilini, kama watoto wachanga katika Kristo. 2 Naliwanywesha maziwa, wala si chakula kigumu, kwa kuwa hamkuwa tayari kwa hicho chakula. Naam, hata sasa hamko tayari. 3 Ninyi bado ni watu wa mwilini. Kwa kuwa bado kuna wivu na magombano miongoni mwenu, je, ninyi si watu wa mwilini? Je, si mwaendelea kama watu wa kawaida? 4 Kwa maana mmoja anaposema, “Mimi ni wa Paulo,” na mwingine, “Mimi ni wa Apolo,” je, ninyi si wanadamu wa kawaida?

  7. 4 Tena nikaona kuwa kazi zote na mafanikio yote huchipuka kutokana na wivu wa mtu kwa jirani yake. Hili nalo ni ubatili, ni kukimbiza upepo.

    5 Mpumbavu hukunja mikono yake

    na kujiangamiza mwenyewe.

    6 Afadhali konzi moja pamoja

    na utulivu kuliko konzi mbili pamoja na taabu

    na kukimbiza upepo.

    7 Tena nikaona kitu kingine kilicho ubatili chini ya jua:

    8 Kulikuwepo mwanadamu aliye peke yake,

    hakuwa na mwana wala ndugu.

    Hapakuwa na mwisho wa kazi yake,

    hata hivyo macho yake

    hayakutosheka na utajiri wake.

    Aliuliza, “Ninajitaabisha hivi kwa ajili ya nani,

    nami kwa nini ninajinyima kufurahia?”

    Hili pia ni ubatili,

    ni shughuli yenye taabu!

  8. 28 Nao kwa kuwa hawakuona umuhimu wa kudumisha ufahamu wa Mungu, yeye akawaachilia wafuate akili za upotovu, watende mambo yale yasiyostahili kutendwa. 29 Wakiwa wamejawa na udhalimu wa kila namna, uasherati, uovu, tamaa mbaya na hila. Wamejawa na husuda, uuaji, ugomvi, udanganyifu, hadaa na nia mbaya. Wao pia ni wasengenyaji, 30 wasingiziaji, wanaomchukia Mungu, wajeuri, wenye kiburi na majivuno, wenye hila, wasiotii wazazi wao, 31 wajinga, wasioamini, wasio na huruma na wakatili. 32 Ingawa wanafahamu sheria ya haki ya Mungu kwamba watu wanaofanya mambo kama hayo wanastahili mauti, si kwamba wanaendelea kutenda hayo tu, bali pia wanakubaliana na wale wanaoyatenda.

  9. 3 Ikiwa mtu yeyote atafundisha mafundisho mapotovu wala hakubaliani na mafundisho manyofu ya Bwana wetu Yesu Kristo na yale ya utauwa, 4 huyo amejivuna wala hajui kitu chochote. Yeye amejaa tamaa ya mabishano na ugomvi kuhusu maneno ambavyo matokeo yake ni wivu na mapigano, maneno ya ukorofi, shuku mbaya, 5 na kuzozana kusikokoma kati ya watu walioharibika akili zao, walioikosa kweli, na ambao hudhani kwamba utauwa ni njia ya kupata faida.

    6 Lakini utauwa na kuridhika ni faida kubwa. 7 Kwa kuwa hatukuja humu duniani na kitu chochote, wala hatuwezi kutoka humu na kitu. 8 Lakini kama tuna chakula na mavazi, tutaridhika navyo. 9 Lakini wale watu wanaotamani kuwa na mali kwa haraka huanguka kwenye majaribu, na wamenaswa na tamaa nyingi za kipumbavu zenye kudhuru, zinazowazamisha watu katika uharibifu na maangamizi. 10 Kwa maana kupenda fedha ndiyo shina moja la maovu ya kila namna. Baadhi ya watu wakitamani fedha, wameiacha imani na kujichoma wenyewe kwa maumivu mengi.

  10. 1 “Ita kama unataka, lakini ni nani atakayekujibu?

    Ni yupi kati ya hao watakatifu utakayemgeukia?

    2 Kuweka uchungu moyoni humuua mpumbavu,

    nao wivu humchinja mjinga.

    3 Mimi mwenyewe nimemwona mpumbavu akistawi,

    lakini ghafula nyumba yake ikawa imelaaniwa.

  11. 1 Ni kitu gani kinachosababisha mapigano na ugomvi miongoni mwenu? Je, haya hayatokani na tamaa zenu zinazoshindana ndani yenu? 2 Mnatamani lakini hampati, kwa hiyo mwaua. Mwatamani kupata lakini hampati vile mnavyotaka, kwa hiyo mnajitia katika magomvi na mapigano. Mmepungukiwa kwa sababu hammwombi Mungu. 3 Mnapoomba hampati kwa sababu mnaomba kwa nia mbaya, ili mpate kuvitumia hivyo mtakavyopata kwa tamaa zenu.

    4 Ninyi wanaume na wanawake wazinzi, hamjui ya kwamba urafiki na dunia ni uadui na Mungu? Kwa hiyo mtu yeyote anayetaka kuwa rafiki wa dunia hufanyika adui wa Mungu. 5 Au mwadhani kwamba Andiko lasema bure kuwa huyo Roho ambaye Mungu amemweka ndani yetu hututamani kiasi cha kuona wivu? 6 Lakini yeye hutupatia neema zaidi. Hii ndiyo sababu Andiko husema:

    “Mungu huwapinga wenye kiburi,

    lakini huwapa wanyenyekevu neema.”

    7 Basi mtiini Mungu. Mpingeni ibilisi, naye atawakimbia. 8 Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu ninyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu ninyi wenye nia mbili.

  12. 17 Usiuruhusu moyo wako kuwaonea wivu wenye dhambi,

    bali kila mara uwe na bidii katika kumcha Bwana.

    18 Hakika kuna tumaini la baadaye kwa ajili yako,

    nalo tarajio lako halitakatiliwa mbali.

  13. 15 Basi ilikuwa ni desturi ya mtawala kumfungua mfungwa mmoja aliyechaguliwa na umati wa watu wakati wa sikukuu. 16 Wakati huo alikuwepo mfungwa mmoja mwenye sifa mbaya, aliyeitwa Baraba. 17 Hivyo umati wa watu walipokusanyika, Pilato akawauliza, “Mnataka niwafungulie nani, Baraba au Yesu yeye aitwaye Kristo?” 18 Kwa kuwa alitambua Yesu alikuwa amekabidhiwa kwake kwa ajili ya wivu.

  14. Zaburi ya Daudi.

    1 Usisumbuke kwa ajili ya watendao maovu,

    wala usiwaonee wivu watendao mabaya,

    2 kwa maana kama majani watanyauka mara,

    kama mimea ya kijani watakufa mara.

    3 Mtumaini Bwana na utende yaliyo mema;

    Kaa katika nchi ukafurahie malisho salama.

    4 Jifurahishe katika Bwana

    naye atakupa haja za moyo wako.

  15. 11 Nanyi fanyeni hivi, mkiutambua wakati tulio nao. Saa ya kuamka kutoka usingizini imewadia, kwa maana sasa wokovu wetu umekaribia zaidi kuliko hapo kwanza tulipoamini. 12 Usiku umeendelea sana, mapambazuko yamekaribia. Kwa hiyo tuyaweke kando matendo ya giza na tuvae silaha za nuru. 13 Basi na tuenende kwa adabu kama inavyopasa wakati wa mchana, si kwa kufanya karamu za ulafi na ulevi, si kwa ufisadi na uasherati, si kwa ugomvi na wivu. 14 Bali jivikeni Bwana Yesu Kristo, wala msifikiri jinsi mtakavyotimiza tamaa za miili yenu yenye asili ya dhambi.

  16. 6 Watu walipokuwa wanarudi nyumbani baada ya Daudi kumuua yule Mfilisti, wanawake wakaja kutoka pande zote za miji ya Israeli kumlaki Mfalme Sauli kwa kuimba na kucheza, kwa nyimbo za furaha na kwa matari na zeze.

    7 Walipokuwa wanacheza, wakaimba:

    “Sauli amewaua elfu zake,

    naye Daudi makumi elfu yake.”

    8 Sauli akakasirika sana; sehemu hii ya kurudia rudia ya wimbo huu ilimkasirisha sana. Akafikiri kuwa, “Wamempa Daudi makumi elfu, lakini mimi wamenipa elfu tu. Apate nini zaidi isipokuwa ufalme?” 9 Kuanzia wakati ule na kuendelea Sauli akawa na jicho la wivu juu ya Daudi.

  17. 44 Sabato iliyofuata, karibu watu wote wa mji walikuja kusikiliza neno la Bwana. 45 Lakini Wayahudi walipoona ule umati mkubwa wa watu walijawa na wivu, wakayakanusha maneno Paulo aliyokuwa akisema.

  18. 3 Baada ya muda Kaini akaleta baadhi ya mazao ya shamba kama sadaka kwa Bwana. 4 Lakini Abeli akaleta fungu nono kutoka baadhi ya wazaliwa wa kwanza wa mifugo yake. Bwana akamkubali Abeli pamoja na sadaka yake, 5 lakini Mungu hakumkubali Kaini pamoja na sadaka yake. Kwa hiyo Kaini akakasirika sana, uso wake ukawa na huzuni.

    6 Kisha Bwana akamwambia Kaini, “Kwa nini umekasirika? Kwa nini uso wako una huzuni? 7 Ukifanya lililo sawa, je, hutakubalika? Lakini usipofanya lililo sawa, dhambi inakuvizia mlangoni mwako, inakutamani wewe, lakini inakupasa uishinde.”

    8 Basi Kaini akamwambia ndugu yake Abeli, “Twende shambani.” Walipokuwa shambani, Kaini akamshambulia Abeli ndugu yake, akamuua.

  19. 31 Usimwonee wivu mtu mwenye jeuri

    wala kuchagua njia yake iwayo yote,

    32 kwa kuwa Bwana humchukia mtu mpotovu,

    lakini siri yake iko kwa mwenye haki.

  20. 20 Akaendelea kusema, “Kile kimtokacho mtu ndicho kimtiacho unajisi. 21 Kwa maana kutoka ndani ya moyo wa mtu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wizi, uuaji, uzinzi, 22 tamaa mbaya, uovu, udanganyifu, ufisadi, wivu, matukano, kiburi na upumbavu. 23 Maovu haya yote hutoka ndani ya mtu, nayo ndiyo yamtiayo mtu unajisi.”

  21. 3 Kwa maana niliwaonea wivu wenye kujivuna

    nilipoona kufanikiwa kwa waovu.

  22. 1 Usiwaonee wivu watu waovu,

    usitamani ushirika nao;

    2 kwa maana mioyo yao hupanga mambo ya jeuri,

    nayo midomo yao husema juu ya kuleta madhara.

  23. 15 Ni kweli kwamba wengine wanamhubiri Kristo kutokana na wivu na kwa kutaka kushindana, lakini wengine wanamhubiri Kristo kwa nia njema.

  24. 12 Isaki akapanda mazao katika nchi hiyo, kwa mwaka huo huo, akavuna mara mia, kwa sababu Bwana alimbariki. 13 Isaki akawa tajiri, mali zake zikaendelea kuongezeka mpaka akawa tajiri sana. 14 Akawa na mifugo ya kondoo na ngʼombe, na watumishi wengi sana, kiasi kwamba Wafilisti wakamwonea wivu.

  25. 1 Raheli alipoona hamzalii Yakobo watoto, akamwonea ndugu yake wivu. Hivyo akamwambia Yakobo, “Nipe watoto, la sivyo nitakufa!”

    2 Yakobo akamkasirikia, akamwambia, “Je, mimi ni badala ya Mungu, ambaye amekuzuia usizae watoto?”

  26. 3 Basi, Israeli akampenda Yosefu kuliko yeyote miongoni mwa kaka zake, kwani ni mwanawe wa uzeeni, akamshonea joho lililorembwa vizuri sana. 4 Ndugu zake walipoona kwamba baba yao anampenda Yosefu kuliko yeyote mwingine miongoni mwao, walimchukia na hawakusema naye neno lolote jema.

  27. 17 Usiitamani nyumba ya jirani yako. Usimtamani mke wa jirani yako, wala mtumishi wake wa kiume au wa kike, wala ngʼombe wake au punda wake, wala chochote kile alicho nacho jirani yako.”

  28. 16 Kambini walimwonea wivu Mose,

    na pia Aroni aliyekuwa amewekwa wakfu kwa Bwana.

    17 Ardhi ilifunguka ikawameza Dathani,

    ikawazika Abiramu na kundi lake.

    18 Moto uliwaka katikati ya wafuasi wao,

    mwali wa moto uliwateketeza waovu.

  29. 20 Kwa kuwa nina hofu ya kwamba nitakapokuja naweza kuwakuta nisivyotaka, nanyi mkanikuta msivyotaka. Nina hofu kwamba panaweza kuwa na ugomvi, wivu, ghadhabu, fitina, masingizio, masengenyo, majivuno na machafuko.

  30. 3 Msitende jambo lolote kwa nia ya kujitukuza wala kujivuna, bali kwa unyenyekevu kila mtu amhesabu mwingine bora kuliko nafsi yake. 4 Kila mmoja wenu asiangalie faida yake mwenyewe tu, bali pia ajishughulishe kwa faida ya wengine.

    5 Kuweni na nia ile ile aliyokuwa nayo Kristo Yesu: