49 Bible Verses About Trusting God

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Trusting God
  1. 5 Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote

    wala usizitegemee akili zako mwenyewe;

    6 katika njia zako zote mkiri yeye,

    naye atayanyoosha mapito yako.

    7 Usiwe mwenye hekima machoni pako mwenyewe;

    mche Bwana ukajiepushe na uovu.

    8 Hii itakuletea afya mwilini mwako,

    na mafuta kwenye mifupa yako.

  2. 1 Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, na udhahiri wa mambo yasiyoonekana. 2 Maana baba zetu wa kale walipongezwa kwa haya.

    3 Kwa imani tunafahamu kwamba ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu, vitu vyote vinavyoonekana havikuumbwa kutoka kwa vitu vinavyoonekana.

  3. 18 Lakini macho ya Bwana yako kwa wale wamchao,

    kwa wale tumaini lao liko katika upendo wake usio na kikomo,

    19 ili awaokoe na mauti,

    na kuwahifadhi wakati wa njaa.

    20 Sisi tunamngojea Bwana kwa matumaini,

    yeye ni msaada wetu na ngao yetu.

    21 Mioyo yetu humshangilia,

    kwa maana tunalitumainia jina lake takatifu.

    22 Upendo wako usio na mwisho ukae juu yetu, Ee Bwana,

    tunapoliweka tumaini letu kwako.

  4. 4 Lakini sanamu zao ni za fedha na dhahabu,

    zilizotengenezwa kwa mikono ya wanadamu.

    5 Zina vinywa, lakini haziwezi kusema,

    zina macho, lakini haziwezi kuona;

    6 zina masikio, lakini haziwezi kusikia,

    zina pua, lakini haziwezi kunusa;

    7 zina mikono, lakini haziwezi kupapasa,

    zina miguu, lakini haziwezi kutembea;

    wala koo zao haziwezi kutoa sauti.

    8 Wale wanaozitengeneza watafanana nazo,

    vivyo hivyo wale wote wanaozitumainia.

    9 Ee nyumba ya Israeli, mtumainini Bwana,

    yeye ni msaada na ngao yao.

    10 Ee nyumba ya Aroni, mtumainini Bwana,

    yeye ni msaada na ngao yao.

    11 Ninyi mnaomcha, mtumainini Bwana,

    yeye ni msaada na ngao yao.

    12 Bwana anatukumbuka na atatubariki:

    ataibariki nyumba ya Israeli,

    ataibariki nyumba ya Aroni,

    13 atawabariki wale wanaomcha Bwana,

    wadogo kwa wakubwa.

    14 Bwana na awawezeshe kuongezeka,

    ninyi na watoto wenu.

  5. 23 Amin, nawaambia, mtu yeyote atakayeuambia mlima huu, ‘Ngʼoka ukatupwe baharini,’ wala asione shaka moyoni mwake, bali aamini kwamba hayo asemayo yametukia, atatimiziwa. 24 Kwa sababu hiyo nawaambia, yoyote mtakayoyaomba mkisali, aminini ya kwamba mmeyapokea, nayo yatakuwa yenu.

  6. 16 sijaacha kumshukuru Mungu kwa ajili yenu, nikiwakumbuka katika maombi yangu. 17 Nazidi kumwomba Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awajalieni ninyi roho ya hekima na ya ufunuo, ili mpate kumjua zaidi. 18 Ninaomba pia kwamba macho ya mioyo yenu yatiwe nuru ili mpate kujua tumaini mliloitiwa, utajiri wa urithi wa utukufu wake kwa watakatifu 19 na uweza wake mkuu usiolinganishwa kwa ajili yetu sisi tuaminio. Uweza huo unaofanya kazi ndani yetu, ni sawa na ile nguvu kuu mno 20 aliyoitumia katika Kristo alipomfufua kutoka kwa wafu, na akamketisha mkono wake wa kuume huko mbinguni, 21 juu sana kuliko falme zote na mamlaka, enzi na milki, na juu ya kila jina litajwalo, si katika ulimwengu huu tu, bali katika ule ujao pia.

  7. 5 Toeni dhabihu zilizo haki;

    mtegemeeni Bwana.

  8. Zaburi ya Daudi.

    1 Kwako wewe, Ee Bwana,

    nainua nafsi yangu,

    2 ni wewe ninayekutumainia,

    Ee Mungu wangu.

    Usiniache niaibike,

    wala usiache adui zangu wakanishinda.

  9. 6 Bwana yuko pamoja nami, sitaogopa.

    Mwanadamu anaweza kunitenda nini?

    7 Bwana yuko pamoja nami,

    yeye ni msaidizi wangu.

    Nitawatazama adui zangu

    wakiwa wameshindwa.

    8 Ni bora kumkimbilia Bwana

    kuliko kumtumainia mwanadamu.

    9 Ni bora kumkimbilia Bwana

    kuliko kuwatumainia wakuu.

  10. 5 Hili ndilo asemalo Bwana:

    “Amelaaniwa yeye amtegemeaye mwanadamu,

    ategemeaye mwenye mwili

    kwa ajili ya nguvu zake,

    ambaye moyo wake

    umemwacha Bwana.

    6 Atakuwa kama kichaka cha jangwani;

    hataona mafanikio yatakapokuja.

    Ataishi katika sehemu zisizo na maji,

    katika nchi ya chumvi ambapo

    hakuna yeyote aishiye humo.

    7 “Lakini amebarikiwa mtu ambaye tumaini lake ni katika Bwana,

    ambaye matumaini yake ni katika Bwana.

    8 Atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji

    uenezao mizizi yake karibu na kijito cha maji.

    Hauogopi wakati wa joto ujapo;

    majani yake ni mabichi daima.

    Hauna hofu katika mwaka wa ukame

    na hautaacha kuzaa matunda.”

  11. 1 Kwa hiyo, kwa kuwa tumekwisha kuhesabiwa haki kwa imani, tuna amani na Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, 2 ambaye kwa kupitia kwake tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo ndani yake sasa tunasimama, nasi twafurahia katika tumaini letu la kushiriki utukufu wa Mungu.

  12. 13 Lakini ndugu, hatutaki mkose kujua kuhusu wale waliolala mauti, ili msihuzunike kama watu wengine wasiokuwa na tumaini. 14 Kwa kuwa tunaamini kwamba Yesu alikufa na kufufuka, na kwa hivyo, Mungu kwa njia ya Yesu atawafufua pamoja naye wale waliolala mautini ndani yake. 15 Kulingana na neno la Bwana mwenyewe, tunawaambia kwamba sisi ambao bado tuko hai, tuliobaki hadi kuja kwake Bwana, hakika hatutawatangulia waliolala mauti. 16 Kwa maana Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni, akitoa amri kwa sauti kuu, pamoja na sauti ya malaika mkuu, na sauti ya tarumbeta ya Mungu. Nao waliokufa wakiwa katika Kristo watafufuka kwanza. 17 Baada ya hilo sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu ili kumlaki Bwana hewani, hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele. 18 Kwa hiyo farijianeni kwa maneno haya.

  13. 17 Waagize wale ambao ni matajiri wa ulimwengu huu waache kujivuna, wala wasiweke tumaini lao katika mali ambayo si ya hakika, bali waweke tumaini lao katika Mungu ambaye hutupatia vitu vyote kwa wingi ili tuvifurahie.

  14. 30 Kuhusu Mungu, njia yake ni kamilifu,

    neno la Bwana halina dosari.

    Yeye ni ngao kwa wote

    wanaokimbilia kwake.

  15. 15 Macho yangu humwelekea Bwana daima,

    kwa kuwa yeye peke yake ndiye ataitoa

    miguu yangu kutoka mtego.

    16 Nigeukie na unihurumie,

    kwa maana mimi ni mpweke na mwenye kuteseka.

    17 Shida za moyo wangu zimeongezeka,

    niokoe katika dhiki yangu.

    18 Uangalie mateso na shida zangu

    na uniondolee dhambi zangu zote.

    19 Tazama adui zangu walivyo wengi,

    pia uone jinsi wanavyonichukia vikali!

    20 Uyalinde maisha yangu na uniokoe,

    usiniache niaibike,

    kwa maana nimekukimbilia wewe.

  16. 3 Akaweka wimbo mpya kinywani mwangu,

    wimbo wa sifa kwa Mungu wetu.

    Wengi wataona na kuogopa

    na kuweka tumaini lao kwa Bwana.

    4 Heri mtu yule amfanyaye Bwana kuwa tumaini lake,

    asiyewategemea wenye kiburi,

    wale wenye kugeukia miungu ya uongo.

  17. 48 Watu wa Mataifa waliposikia haya wakafurahi na kulitukuza neno la Bwana; nao wote waliokuwa wamekusudiwa uzima wa milele wakaamini.

  18. 6 Lakini ile haki itokanayo na imani husema hivi: “Usiseme moyoni mwako, ‘Ni nani atakayepanda mbinguni?’ ” (yaani ili kumleta Kristo chini) 7 “au ‘Ni nani atashuka kwenda kuzimu?’ ” (yaani ili kumleta Kristo kutoka kwa wafu.) 8 Lakini andiko lasemaje? “Lile neno liko karibu nawe, liko kinywani mwako na moyoni mwako,” yaani, lile neno la imani tunalolihubiri. 9 Kwa sababu kama ukikiri kwa kinywa chako kwamba “Yesu ni Bwana,” na kuamini moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, utaokoka. 10 Kwa maana kwa moyo mtu huamini na hivyo kuhesabiwa haki, tena kwa kinywa mtu hukiri na hivyo kupata wokovu.

  19. 8 Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani, wala si kwa matendo yenu mema. Hii ni zawadi kutoka kwa Mungu, 9 si kwa matendo, ili mtu yeyote asije akajisifu.

  20. 15 Hivyo basi, ndugu wapendwa, simameni imara na myashike sana yale mafundisho tuliyowapa ikiwa ni kwa maneno ya kinywa au kwa barua.

    16 Bwana wetu Yesu Kristo mwenyewe na Mungu Baba yetu, aliyetupenda na kwa neema yake akatupatia faraja ya milele na tumaini jema, 17 awafariji mioyo yenu na kuwaimarisha katika kila neno na tendo jema.

  21. 17 Mungu alipotaka kuonyesha kwa udhahiri zaidi ile asili ya kutokubadilika kwa ahadi yake kwa warithi wa ahadi, aliithitibisha kwa kiapo. 18 Mungu alifanya hivyo ili kwa vitu viwili visivyobadilika, yaani ahadi yake na kiapo chake, ambavyo kwavyo Mungu hawezi kusema uongo, sisi ambao tumemkimbilia ili tulishike lile tumaini lililowekwa mbele yetu tuwe na faraja thabiti. 19 Tunalo tumaini hili kama nanga ya roho iliyo imara na thabiti. Tumaini hili huingia katika sehemu takatifu iliyopo nyuma ya pazia, 20 mahali ambapo Yesu mtangulizi wetu aliingia kwa niaba yetu. Yeye amekuwa Kuhani Mkuu milele, kwa mfano wa Melkizedeki.

  22. 23 Tushike kwa uthabiti lile tumaini la ukiri wetu bila kuyumbayumba, kwa maana yeye aliyeahidi ni mwaminifu.

  23. 2 Akasema:

    “Bwana ni mwamba wangu,

    ngome yangu na mwokozi wangu,

    3 Mungu wangu ni mwamba wangu,

    ambaye kwake ninakimbilia,

    ngao yangu na pembe ya wokovu wangu.

    Yeye ni ngome yangu, kimbilio langu

    na mwokozi wangu,

    huniokoa kutoka kwa watu wenye jeuri.

    4 Ninamwita Bwana, anayestahili kusifiwa,

    nami ninaokolewa kutoka kwa adui zangu.

    5 “Mawimbi ya mauti yalinizunguka,

    mafuriko ya maangamizi yalinilemea.

  24. 9 Bwana ni kimbilio la watu wanaoonewa,

    ni ngome imara wakati wa shida.

    10 Wote wanaolijua jina lako watakutumaini wewe,

    kwa maana wewe Bwana,

    hujawaacha kamwe wakutafutao.

  25. 5 Lakini ninategemea upendo wako usiokoma;

    moyo wangu unashangilia katika wokovu wako.

    6 Nitamwimbia Bwana,

    kwa kuwa amekuwa mwema kwangu.

  26. 5 Tutashangilia kwa furaha utakaposhinda,

    tutainua bendera zetu kwa jina la Mungu wetu.

    Bwana na akupe haja zako zote.

    6 Sasa nafahamu kuwa Bwana

    humwokoa mpakwa mafuta wake,

    humjibu kutoka mbingu yake takatifu

    kwa nguvu za wokovu wa mkono wake wa kuume.

    7 Wengine wanatumaini magari ya vita, na wengine farasi,

    bali sisi tutalitumainia jina la Bwana, Mungu wetu.

  27. 3 Mtumaini Bwana na utende yaliyo mema;

    Kaa katika nchi ukafurahie malisho salama.

  28. Kwa mwimbishaji. Kwa ala za nyuzi za uimbaji. Zaburi ya Daudi.

    1 Ee Mungu, sikia kilio changu,

    usikilize maombi yangu.

    2 Kutoka miisho ya dunia ninakuita,

    ninaita huku moyo wangu unadhoofika;

    uniongoze kwenye mwamba

    ule ulio juu kuliko mimi.

    3 Kwa kuwa umekuwa kimbilio langu,

    ngome imara dhidi ya adui.

    4 Natamani kukaa hemani mwako milele,

    na kukimbilia chini ya uvuli wa mbawa zako.

  29. 5 Ee nafsi yangu, upumzike, kwa Mungu peke yake,

    tumaini langu latoka kwake.

    6 Yeye peke yake ndiye mwamba wangu na wokovu wangu;

    ndiye ngome yangu, sitatikisika.

    7 Wokovu wangu na heshima yangu viko kwa Mungu,

    ndiye mwamba wangu wenye nguvu

    na kimbilio langu.

    8 Enyi watu, mtumainini yeye wakati wote,

    miminieni mioyo yenu kwake,

    kwa kuwa Mungu ni kimbilio letu.

  30. 41 Ee Bwana, upendo wako usiokoma unijie,

    wokovu wako sawasawa na ahadi yako,

    42 ndipo nitakapomjibu anayenidhihaki,

    kwa kuwa ninalitumainia neno lako.

    43 Usilinyakue neno la kweli kutoka kinywani mwangu,

    kwa kuwa nimeweka tumaini langu katika amri zako.

    44 Nitaitii amri yako daima,

    naam, milele na milele.

    45 Nitatembea nikiwa huru,

    kwa kuwa nimejifunza mausia yako.

  31. 3 Usiweke tumaini lako kwa wakuu,

    kwa wanadamu ambao hufa,

    ambao hawawezi kuokoa.

    4 Roho yao itokapo hurudi mavumbini,

    siku hiyo hiyo mipango yao yote hukoma.

    5 Heri yeye ambaye Mungu wa Yakobo ni msaada wake,

    ambaye tumaini lake ni katika Bwana, Mungu wake,

    6 Muumba wa mbingu na nchi,

    na bahari na vyote vilivyomo ndani yake:

    Bwana anayedumu kuwa mwaminifu

    milele na milele.

    7 Naye huwapatia haki walioonewa

    na kuwapa wenye njaa chakula.

    Bwana huwaweka wafungwa huru,

  32. 22 Moyo wenye furaha ni dawa nzuri,

    bali roho iliyopondeka hukausha mifupa.

  33. 4 Mtumaini Bwana milele,

    kwa kuwa Bwana, Bwana, ni Mwamba wa milele.

  34. 10 Ni nani miongoni mwenu amchaye Bwana,

    na kulitii neno la mtumishi wake?

    Yeye atembeaye gizani,

    yeye asiye na nuru,

    na alitumainie jina la Bwana,

    na amtegemee Mungu wake.

  35. 36 Aliposikia hayo waliyosema, Yesu akamwambia huyo kiongozi wa sinagogi, “Usiogope. Amini tu.”

  36. 22 Yesu akawajibu, “Mwaminini Mungu.

  37. 43 Manabii wote walishuhudia juu yake kwamba kila mtu amwaminiye hupokea msamaha wa dhambi katika Jina lake.”

  38. 31 Wakamjibu, “Mwamini Bwana Yesu Kristo, nawe utaokoka, pamoja na watu wa nyumbani mwako.”

  39. 8 Kiongozi wa hilo sinagogi, aliyeitwa Krispo, akamwamini Bwana, yeye pamoja na watu wote wa nyumbani mwake. Nao Wakorintho wengi waliomsikia Paulo pia wakaamini na kubatizwa.

  40. 16 Mimi siionei haya Injili ya Kristo kwa maana ni uweza wa Mungu uletao wokovu kwa kila aaminiye, kwanza kwa Myahudi na kwa Myunani pia. 17 Kwa maana katika Injili haki itokayo kwa Mungu imedhihirishwa, haki ile iliyo kwa njia ya imani hadi imani. Kama ilivyoandikwa: “Mwenye haki ataishi kwa imani.”

  41. 20 Kwa kuwa viumbe vyote viliwekwa chini ya ubatili, si kwa chaguo lao, bali kwa mapenzi yake yeye aliyevitiisha katika tumaini, 21 ili kwamba viumbe vyote vipate kuwekwa huru kutoka kwa utumwa wa kuharibika na kupewa uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu.

    22 Kwa maana twajua ya kuwa hata sasa viumbe vyote vimekuwa vikilia kwa maumivu kama utungu wa mwanamke wakati wa kuzaa. 23 Wala si hivyo viumbe peke yao, bali hata sisi ambao ndio matunda ya kwanza ya Roho, kwa ndani tunalia kwa uchungu tukisubiri kwa shauku kufanywa wana wa Mungu, yaani, ukombozi wa miili yetu. 24 Kwa kuwa tuliokolewa kwa tumaini hili. Lakini kama kinachotumainiwa kikionekana hakiwi tumaini tena. Je, kuna mtu anayetumaini kupata kitu alicho nacho tayari?

  42. 14 Lakini watamwitaje yeye ambaye hawajamwamini? Nao watawezaje kumwamini yeye ambaye hawajamsikia? Tena watamsikiaje bila mtu kuwahubiria? 15 Nao watahubirije wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, “Tazama jinsi ilivyo mizuri miguu yao wale wanaohubiri habari njema!”

    16 Lakini si wote waliotii Habari Njema. Kwa maana Isaya asema, “Bwana, ni nani aliyeamini ujumbe wetu?” 17 Basi, imani chanzo chake ni kusikia, na kusikia huja kwa neno la Kristo.

  43. 9 Kwa kweli, mioyoni mwetu tulihisi tumekabiliwa na hukumu ya kifo, ili tusijitegemee sisi wenyewe bali tumtegemee Mungu afufuaye wafu. 10 Yeye aliyetuokoa kwenye hatari kubwa ya kifo na atatuokoa tena. Kwake yeye tumeweka tumaini letu kwamba ataendelea kutuokoa.

  44. 7 Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, sasa nayahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo. 8 Zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara tupu nikiyalinganisha na faida kubwa ipitayo kiasi cha kumjua Kristo Yesu Bwana wangu, ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote, nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nimpate Kristo. 9 Nami nionekane mbele zake bila kuwa na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa imani katika Kristo, haki ile itokayo kwa Mungu kwa njia ya imani. 10 Nataka nimjue Kristo na uweza wa kufufuka kwake na ushirika wa mateso yake, ili nifanane naye katika mauti yake, 11 ili kwa njia yoyote niweze kufikia ufufuo wa wafu.

  45. 6 Kwa hiyo basi, tusilale kama watu wengine walalavyo, bali tukeshe na kuwa na kiasi. 7 Kwa kuwa wote walalao hulala usiku na wale walewao hulewa usiku. 8 Lakini kwa kuwa sisi ni wana wa mchana, basi tuwe na kiasi, tukijivika imani na upendo kama dirii kifuani na tumaini letu la wokovu kama chapeo. 9 Kwa maana Mungu hakutuita ili tupate ghadhabu bali tupate wokovu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. 10 Yeye alikufa kwa ajili yetu ili hata kama tuko macho au tumelala, tupate kuishi pamoja naye. 11 Kwa hiyo farijianeni na kujengana, kama vile mnavyofanya sasa.

  46. 10 (nasi kwa ajili ya hili tunajitaabisha na kujitahidi), kwamba tumeweka tumaini letu kwa Mungu aliye hai, ambaye ni Mwokozi wa watu wote, hasa wale waaminio.

  47. 7 Nimevipiga vita vizuri, mashindano nimeyamaliza, imani nimeilinda. 8 Sasa nimewekewa taji ya haki ambayo Bwana, mwamuzi wa haki, atanitunukia siku ile: wala si mimi tu, bali pia wote ambao wamengoja kwa shauku kudhihirishwa kwake.

  48. 6 Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza Mungu, kwa maana yeyote anayemjia Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko na ya kuwa huwapa thawabu wale wamtafutao kwa bidii.

  49. 10 Usiogope mateso yatakayokupata. Nakuambia ibilisi atawatia baadhi yenu gerezani ili kuwajaribu, nanyi mtapata dhiki kwa muda wa siku kumi. Uwe mwaminifu hata kufa, nami nitakupa taji ya uzima.