35 Bible Verses About Overwhelming Times

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Overwhelming Times
  1. Kwa mwimbishaji. Kwa ala za nyuzi za uimbaji. Zaburi ya Daudi.

    1 Ee Mungu, sikia kilio changu,

    usikilize maombi yangu.

    2 Kutoka miisho ya dunia ninakuita,

    ninaita huku moyo wangu unadhoofika;

    uniongoze kwenye mwamba

    ule ulio juu kuliko mimi.

    3 Kwa kuwa umekuwa kimbilio langu,

    ngome imara dhidi ya adui.

    4 Natamani kukaa hemani mwako milele,

    na kukimbilia chini ya uvuli wa mbawa zako.

  2. 6 Basi, nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake. 7 Mtwikeni yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana na mambo yenu.

    8 Mwe na kiasi na kukesha, maana adui yenu ibilisi huzungukazunguka kama simba angurumaye akitafuta mtu ili apate kummeza. 9 Mpingeni, mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kwamba mateso kama hayo yanawapata ndugu zenu pote duniani.

  3. 28 “Njooni kwangu, ninyi nyote mnaotaabika na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. 29 Jifungeni nira yangu, mjifunze kutoka kwangu, kwa maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtapata raha nafsini mwenu. 30 Kwa maana nira yangu ni laini na mzigo wangu ni mwepesi.”

  4. 6 Msijisumbue kwa jambo lolote, bali katika kila jambo kwa kuomba na kusihi pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. 7 Nayo amani ya Mungu, inayopita fahamu zote, itailinda mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.

  5. 10 Hivyo usiogope, kwa maana niko pamoja nawe;

    usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako.

    Nitakutia nguvu na kukusaidia;

    nitakutegemeza kwa mkono wa kuume wa haki yangu.

  6. 18 Niliposema, “Mguu wangu unateleza,”

    Ee Bwana, upendo wako ulinishikilia.

    19 Wakati wasiwasi ulipokuwa mwingi ndani yangu,

    faraja yako ilinipa furaha nafsini mwangu.

  7. 4 Kwa hiyo roho yangu inazimia ndani yangu,

    moyo wangu ndani yangu unakata tamaa.

  8. 4 Ndipo utapata kibali na jina zuri

    mbele za Mungu na mwanadamu.

    5 Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote

    wala usizitegemee akili zako mwenyewe;

    6 katika njia zako zote mkiri yeye,

    naye atayanyoosha mapito yako.

  9. 28 Je wewe, hufahamu?

    Je wewe, hujasikia?

    Bwana ni Mungu wa milele,

    Muumba wa miisho ya dunia.

    Hatachoka wala kulegea,

    wala hakuna hata mmoja

    awezaye kuupima ufahamu wake.

    29 Huwapa nguvu waliolegea

    na huongeza nguvu za wadhaifu.

    30 Hata vijana huchoka na kulegea,

    nao vijana wanaume hujikwaa na kuanguka,

    31 bali wale wamtumainio Bwana

    atafanya upya nguvu zao.

    Watapaa juu kwa mbawa kama tai;

    watapiga mbio wala hawatachoka,

    watatembea kwa miguu wala hawatazimia.

  10. 34 Kwa hiyo msiwe na wasiwasi kuhusu kesho, kwa sababu kesho itajitaabikia yenyewe. Yatosha kwa siku masumbufu yake.

  11. 33 Nimewaambia mambo haya, ili mpate kuwa na amani mkiwa ndani yangu. Ulimwenguni mtapata dhiki. Lakini jipeni moyo, kwa maana mimi nimeushinda ulimwengu.”

  12. 7 Ili kunizuia nisijivune kwa sababu ya ufunuo huu mkuu, nilipewa mwiba katika mwili wangu, mjumbe wa Shetani, ili anitese. 8 Kwa habari ya jambo hili nilimsihi Bwana mara tatu aniondolee mwiba huu. 9 Lakini aliniambia, “Neema yangu inakutosha, kwa kuwa uweza wangu hukamilika katika udhaifu.” Kwa hiyo nitajisifu kwa furaha zaidi kuhusu udhaifu wangu, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. 10 Hii ndiyo sababu, kwa ajili ya Kristo, nafurahia udhaifu, katika kutukanwa, katika taabu, katika mateso na katika shida, kwa maana ninapokuwa dhaifu, ndipo nina nguvu.

  13. 13 Naweza kuyafanya mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.

  14. Kwa mwimbishaji. Zaburi ya wana wa Kora. Mtindo wa alamothi.

    1 Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu,

    msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso.

    2 Kwa hiyo hatutaogopa, hata kama dunia ikiondolewa

    nayo milima ikiangukia moyoni mwa bahari.

    3 Hata kama maji yake yatanguruma na kuumuka,

    milima nayo ikitetemeka kwa mawimbi yake.

  15. 5 Woga na kutetemeka vimenizunguka,

    hofu kuu imenigharikisha.

  16. 3 Wakati roho yangu inapozimia ndani yangu,

    wewe ndiwe unajua njia zangu.

    Katika njia ninayopita

    watu wameniwekea mtego.

  17. 3 Utamlinda katika amani kamilifu

    yeye ambaye moyo wake ni thabiti

    kwa sababu anakutumaini wewe.

    4 Mtumaini Bwana milele,

    kwa kuwa Bwana, Bwana, ni Mwamba wa milele.

  18. 10 Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. 11 Vaeni silaha zote za Mungu ili kwamba mweze kuzipinga hila za ibilisi. 12 Kwa maana kushindana kwetu si juu ya nyama na damu, bali dhidi ya falme, mamlaka, dhidi ya wakuu wa giza na majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.

  19. 3 Ee Mungu, nilikukumbuka wewe, nikalia kwa huzuni;

    nikatafakari, roho yangu ikadhoofika.

  20. 1 Lakini sasa hili ndilo asemalo Bwana,

    yeye aliyekuumba, ee Yakobo,

    yeye aliyekuhuluku, ee Israeli:

    “Usiogope kwa maana nimekukomboa,

    nimekuita wewe kwa jina lako, wewe u wangu.

    2 Unapopita kwenye maji makuu,

    nitakuwa pamoja nawe,

    unapopita katika mito ya maji,

    hayatakugharikisha.

    Utakapopita katika moto,

    hutaungua,

    miali ya moto haitakuunguza.

    3 Kwa kuwa Mimi ndimi Bwana, Mungu wako,

    yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, Mwokozi wako.

    Ninaitoa Misri kuwa fidia yako,

    Kushi na Seba badala yako.

  21. 36 Kisha Yesu akaenda pamoja na wanafunzi wake mpaka kwenye bustani iitwayo Gethsemane, akawaambia, “Kaeni hapa, nami niende kule nikaombe.” 37 Akamchukua Petro pamoja na wale wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuhuzunika na kufadhaika. 38 Kisha Yesu akawaambia, “Moyo wangu umejawa na huzuni kiasi cha kufa. Kaeni hapa na mkeshe pamoja nami.”

    39 Akaenda mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akaomba akisema, “Baba yangu, kama inawezekana, kikombe hiki na kiniondokee. Lakini si kama nipendavyo mimi, bali kama upendavyo wewe.”

  22. 8 Ndugu wapendwa, hatutaki mkose kujua kuhusu zile taabu tulizopata huko Asia. Kwa maana tulilemewa na mizigo sana, kiasi cha kushindwa kuvumilia, hata tulikata tamaa ya kuishi. 9 Kwa kweli, mioyoni mwetu tulihisi tumekabiliwa na hukumu ya kifo, ili tusijitegemee sisi wenyewe bali tumtegemee Mungu afufuaye wafu. 10 Yeye aliyetuokoa kwenye hatari kubwa ya kifo na atatuokoa tena. Kwake yeye tumeweka tumaini letu kwamba ataendelea kutuokoa. 11 Kama vile mlivyoungana kusaidiana nasi katika maombi, hivyo wengi watatoa shukrani kwa niaba yetu kwa ajili ya baraka za neema tulizopata kwa majibu ya maombi ya wengi.

  23. 9 Je, si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na shujaa. Usihofu wala usivunjike moyo, kwa kuwa Bwana Mungu wako atakuwa pamoja nawe kokote uendako.”

  24. Zaburi ya Daudi.

    1 Bwana ndiye mchungaji wangu,

    sitapungukiwa na kitu.

    2 Hunilaza katika malisho

    ya majani mabichi,

    kando ya maji matulivu huniongoza,

    3 hunihuisha nafsi yangu.

    Huniongoza katika njia za haki

    kwa ajili ya jina lake.

    4 Hata kama nikipita katikati

    ya bonde la uvuli wa mauti,

    sitaogopa mabaya,

    kwa maana wewe upo pamoja nami;

    fimbo yako na mkongojo wako

    vyanifariji.

  25. Zaburi ya Daudi.

    1 Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu,

    nimwogope nani?

    Bwana ni ngome ya uzima wangu,

    nimhofu nani?

  26. 4 Maovu yangu yamenifunika

    kama mzigo usiochukulika.

  27. 1 Yeye akaaye mahali pa salama pake Yeye Aliye Juu Sana,

    atadumu katika uvuli wake Mwenyezi.

    2 Nitasema kumhusu Bwana, “Yeye ndiye kimbilio langu na ngome yangu,

    Mungu wangu, ambaye ninamtumaini.”

  28. Maombi ya mtu aliyechoka. Anapoteseka na kumimina malalamiko yake kwa Bwana.

    1 Ee Bwana, usikie maombi yangu,

    kilio changu cha kuomba msaada kikufikie.

  29. Wimbo wa kwenda juu.

    1 Nayainua macho yangu nitazame vilima,

    msaada wangu utatoka wapi?

    2 Msaada wangu hutoka kwa Bwana,

    Muumba wa mbingu na dunia.

  30. 26 Lakini Yesu akawatazama, akawaambia, “Kwa mwanadamu jambo hili haliwezekani, lakini mambo yote yanawezekana kwa Mungu.”

  31. 32 Wakaenda mahali paitwapo Gethsemane. Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kaeni hapa, nami niende nikaombe.” 33 Kisha akawachukua pamoja naye Petro, Yakobo na Yohana. Akaanza kuhuzunika sana na kutaabika. 34 Akawaambia, “Moyo wangu umejawa na huzuni kiasi cha kufa. Kaeni hapa na mkeshe.”

    35 Akaenda mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akaomba kwamba kama ingewezekana saa hiyo ya mateso imwondokee. 36 Akasema, “Abba, Baba, mambo yote yawezekana kwako. Niondolee kikombe hiki. Lakini si kama nipendavyo mimi, bali vile upendavyo wewe.”

  32. 1 Yesu akawaambia, “Msifadhaike mioyoni mwenu, mnamwamini Mungu, niaminini na mimi pia.

  33. 27 Amani nawaachia, amani yangu nawapa, amani hii niwapayo si kama ile ulimwengu utoayo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiogope.

  34. 37 Lakini katika mambo haya yote tunashinda, naam na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. 38 Kwa maana nimekwisha kujua kwa hakika ya kuwa sio mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuja, wala wenye uwezo, 39 wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kingine chochote zitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu, Bwana wetu.

  35. 1 Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, na udhahiri wa mambo yasiyoonekana.