63 Bible Verses About Prayer

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Prayer
  1. 7 Nanyi mnaposali msiseme maneno kama wafanyavyo watu wasiomjua Mungu. Kwa maana wao hudhani kwamba watasikiwa kwa sababu ya wingi wa maneno yao. 8 Msiwe kama wao, kwa sababu Baba yenu anajua kile mnachohitaji kabla hamjamwomba.

    9 “Hivi basi, ndivyo iwapasavyo kuomba:

    “ ‘Baba yetu uliye mbinguni,

    Jina lako litukuzwe.

    10 Ufalme wako uje.

    Mapenzi yako yafanyike

    hapa duniani kama huko mbinguni.

    11 Utupatie riziki yetu

    ya kila siku.

    12 Utusamehe deni zetu,

    kama sisi nasi tulivyokwisha

    kuwasamehe wadeni wetu.

    13 Usitutie majaribuni,

    bali utuokoe kutoka kwa yule mwovu

    [kwa kuwa Ufalme ni wako, na nguvu,

    na utukufu, hata milele. Amen].’

    14 Kwa kuwa kama mkiwasamehe watu wengine wanapowakosea, Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi pia. 15 Lakini msipowasamehe watu wengine makosa yao, naye Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.

  2. 13 Je, mtu yeyote miongoni mwenu amepatwa na taabu? Basi inampasa aombe. Je, kuna yeyote mwenye furaha? Basi na aimbe nyimbo za kusifu. 14 Je, kuna yeyote miongoni mwenu aliye mgonjwa? Basi inampasa awaite wazee wa kanisa wamwombee na kumpaka mafuta kwa Jina la Bwana. 15 Kule kuomba kwa imani kutamwokoa huyo mgonjwa, naye Bwana atamwinua na kama ametenda dhambi, atasamehewa. 16 Kwa hiyo ungamianeni dhambi zenu ninyi kwa ninyi na kuombeana ili mpate kuponywa. Maombi ya mwenye haki yana nguvu tena yanafaa sana.

    17 Eliya alikuwa mwanadamu kama sisi. Akaomba kwa bidii kwamba mvua isinyeshe, nayo haikunyesha juu ya nchi kwa muda wa miaka mitatu na miezi sita. 18 Kisha akaomba tena, nazo mbingu zikatoa mvua nayo ardhi ikatoa mazao yake.

  3. 9 “Kwa hiyo nawaambia: Ombeni nanyi mtapewa; tafuteni nanyi mtapata; bisheni nanyi mtafunguliwa mlango. 10 Kwa kuwa kila aombaye hupewa; naye kila atafutaye hupata; na kila abishaye hufunguliwa mlango.

    11 “Je, kuna yeyote miongoni mwenu ambaye mtoto wake akimwomba samaki, atampa nyoka badala yake? 12 Au mtoto akimwomba yai atampa nge? 13 Basi ikiwa ninyi mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri, si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa Roho Mtakatifu wale wamwombao!”

  4. 22 Yesu akawajibu, “Mwaminini Mungu. 23 Amin, nawaambia, mtu yeyote atakayeuambia mlima huu, ‘Ngʼoka ukatupwe baharini,’ wala asione shaka moyoni mwake, bali aamini kwamba hayo asemayo yametukia, atatimiziwa. 24 Kwa sababu hiyo nawaambia, yoyote mtakayoyaomba mkisali, aminini ya kwamba mmeyapokea, nayo yatakuwa yenu. 25 Nanyi kila msimamapo kusali, sameheni mkiwa na neno na mtu, ili naye Baba yenu aliye mbinguni awasamehe ninyi makosa yenu. [ 26 Lakini kama ninyi msiposamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu.]”

  5. 12 Amin, amin nawaambia, yeyote aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo yeye atazifanya, naam na kubwa kuliko hizi atazifanya, kwa sababu mimi ninakwenda kwa Baba. 13 Nanyi mkiomba lolote kwa Jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba apate kutukuzwa katika Mwana. 14 Kama mkiniomba lolote kwa Jina langu nitalifanya.

    15 “Kama mnanipenda, mtazishika amri zangu. 16 Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine akae nanyi milele. 17 Huyo ndiye Roho wa kweli ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa sababu haumwoni wala haumjui. Ninyi mnamjua kwa kuwa yuko pamoja nanyi naye anakaa ndani yenu.

  6. 7 “Ombeni nanyi mtapewa; tafuteni nanyi mtapata; bisheni nanyi mtafunguliwa mlango. 8 Kwa kuwa kila aombaye hupewa; naye kila atafutaye hupata; na kila abishaye hufunguliwa mlango.

    9 “Au ni nani miongoni mwenu ambaye mwanawe akimwomba mkate atampa jiwe? 10 Au mwanawe akimwomba samaki atampa nyoka? 11 Ikiwa ninyi basi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri, si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa vitu vizuri wale wamwombao? 12 Kwa hiyo chochote mnachotaka mtendewe na watu, ninyi nanyi watendeeni vivyo hivyo. Kwa kuwa hii ndiyo Sheria na Manabii.

  7. 6 Bwana akasema, “Sikilizeni asemavyo huyu hakimu dhalimu. 7 Je, Mungu hatawatendea haki wateule wake wanaomlilia usiku na mchana? Je, atakawia kuwasaidia? 8 Ninawaambia, atawapatia haki upesi. Lakini je, Mwana wa Adamu atakapokuja ataikuta imani duniani?”

    9 Yesu akatoa mfano huu kwa wale waliojiamini kuwa wao ni wenye haki na kuwadharau wengine: 10 “Watu wawili walikwenda Hekaluni kusali, mmoja wao alikuwa Farisayo na mwingine alikuwa mtoza ushuru. 11 Yule Farisayo, akasimama, akasali hivi na kuomba kwake mwenyewe: ‘Mungu, nakushukuru kwa sababu mimi si kama watu wengine ambao ni wanyangʼanyi, wadhalimu, na wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. 12 Mimi nafunga mara mbili kwa juma, na natoa sehemu ya kumi ya mapato yangu.’

    13 “Lakini yule mtoza ushuru akasimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua uso wake kutazama mbinguni, bali alijipigapiga kifuani na kusema: ‘Mungu, nihurumie, mimi mwenye dhambi.’

    14 “Nawaambia, huyu mtoza ushuru alirudi nyumbani akiwa amehesabiwa haki mbele za Mungu zaidi ya yule Farisayo. Kwa maana yeyote ajikwezaye atashushwa, na yeyote ajishushaye atakwezwa.”

  8. 14 Huu ndio ujasiri tulio nao tunapomkaribia Mungu, kwamba kama tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia. 15 Nasi kama tunajua atusikia, lolote tuombalo, tunajua ya kwamba tumekwisha kupata zile haja tulizomwomba.

    16 Kama mtu akimwona ndugu yake akitenda dhambi isiyo ya mauti, inampasa aombe, naye Mungu atampa uzima mtu huyo. Ninamaanisha wale ambao dhambi yao si ya mauti. Iko dhambi ya mauti, sisemi kwamba utaomba kwa ajili ya hiyo. 17 Jambo lolote lisilo la haki ni dhambi, lakini iko dhambi isiyo ya mauti.

  9. 16 Furahini siku zote; 17 ombeni bila kukoma; 18 shukuruni kwa kila jambo, kwa maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu kwa ajili yenu katika Kristo Yesu.

  10. 10 Basi Danieli alipofahamu kuwa amri ile imetangazwa, alikwenda nyumbani kwenye chumba chake cha ghorofani ambako madirisha yalifunguka kuelekea Yerusalemu. Akapiga magoti na kuomba mara tatu kwa siku, akimshukuru Mungu wake kama alivyokuwa akifanya mwanzoni. 11 Ndipo watu hawa wakaenda kama kikundi na kumkuta Danieli akiomba na kumsihi Mungu kwa ajili ya msaada.

  11. 5 Kama mtu yeyote miongoni mwenu amepungukiwa na hekima na amwombe Mungu, yeye awapaye watu wote kwa ukarimu wala hana kinyongo, naye atapewa. 6 Lakini anapoomba, lazima aamini wala asiwe na shaka, kwa sababu mtu aliye na shaka ni kama wimbi la bahari, lililochukuliwa na upepo na kutupwa huku na huku. 7 Mtu kama huyo asidhani ya kuwa atapata kitu chochote kutoka kwa Bwana. 8 Yeye ni mtu mwenye nia mbili, mwenye kusitasita katika njia zake zote.

  12. 18 Mkiomba kwa Roho siku zote katika sala zote na maombi, mkikesha kila wakati mkiwaombea watakatifu wote.

    19 Niombeeni na mimi pia, ili kila nifunguapo kinywa changu, nipewe maneno ya kusema, niweze kutangaza siri ya Injili kwa ujasiri, 20 ambayo mimi ni balozi wake katika vifungo. Ombeni ili nipate kuhubiri kwa ujasiri kama inipasavyo.

  13. 4 Furahini katika Bwana siku zote, tena nasema furahini! 5 Upole wenu na ujulikane na watu wote. Bwana yu karibu. 6 Msijisumbue kwa jambo lolote, bali katika kila jambo kwa kuomba na kusihi pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. 7 Nayo amani ya Mungu, inayopita fahamu zote, itailinda mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.

  14. 41 Akajitenga nao kama umbali wa kutupa jiwe, akapiga magoti, akaomba 42 akisema, “Baba, kama ni mapenzi yako, niondolee kikombe hiki. Lakini si kama nipendavyo, bali mapenzi yako yatendeke.” 43 Malaika kutoka mbinguni akamtokea, akamtia nguvu. 44 Naye akiwa katika maumivu makuu, akaomba kwa bidii, nalo jasho lake likawa kama matone ya damu yakidondoka ardhini.

  15. 26 Vivyo hivyo, Roho hutusaidia katika udhaifu wetu, kwa sababu hatujui kuomba ipasavyo. Lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa uchungu usioweza kutamkwa. 27 Naye Mungu aichunguzaye mioyo, anaijua nia ya Roho, kwa sababu Roho huwaombea watakatifu sawasawa na mapenzi ya Mungu.

  16. 4 Kaeni ndani yangu, nami nikae ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa matunda lisipokaa ndani ya mzabibu, vivyo hivyo ninyi msipokaa ndani yangu hamwezi kuzaa matunda.

    5 “Mimi ni mzabibu, ninyi ni matawi. Akaaye ndani yangu, nami ndani yake, huyo huzaa sana, maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya jambo lolote. 6 Mtu yeyote asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka. Matawi kama hayo hukusanywa na kutupwa motoni, yakateketea. 7 Ninyi mkikaa ndani yangu na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni lolote mtakalo, nanyi mtatendewa. 8 Kwa hiyo Baba yangu hutukuzwa, kwa vile mzaavyo matunda mengi, nanyi mtakuwa wanafunzi wangu.

  17. 14 Kwa sababu hii nampigia Baba magoti, 15 ambaye ubaba wote wa kila jamaa za mbinguni na za duniani unatokana naye. 16 Namwomba Mungu awaimarishe kwa kuwatia nguvu mioyo yenu kwa njia ya Roho wake kwa kadiri ya utajiri wa utukufu wake, 17 ili kwamba, Kristo apate kukaa mioyoni mwenu kwa njia ya imani. Nami ninaomba kwamba ninyi mkiwa wenye mizizi tena imara katika msingi wa upendo, 18 mwe na uwezo wa kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, urefu, kimo na kina upendo wa Kristo, 19 na kujua upendo huu unaopita fahamu, ili mpate kujazwa na kufikia kipimo cha ukamilifu wote wa Mungu.

  18. 1 Ni kitu gani kinachosababisha mapigano na ugomvi miongoni mwenu? Je, haya hayatokani na tamaa zenu zinazoshindana ndani yenu? 2 Mnatamani lakini hampati, kwa hiyo mwaua. Mwatamani kupata lakini hampati vile mnavyotaka, kwa hiyo mnajitia katika magomvi na mapigano. Mmepungukiwa kwa sababu hammwombi Mungu. 3 Mnapoomba hampati kwa sababu mnaomba kwa nia mbaya, ili mpate kuvitumia hivyo mtakavyopata kwa tamaa zenu.

    4 Ninyi wanaume na wanawake wazinzi, hamjui ya kwamba urafiki na dunia ni uadui na Mungu? Kwa hiyo mtu yeyote anayetaka kuwa rafiki wa dunia hufanyika adui wa Mungu.

  19. 13 “Wakati nitakapofunga mbingu ili isiwepo mvua, au nikiamuru nzige kula mazao ya nchi au nikituma tauni miongoni mwa watu wangu, 14 kama watu wangu, wanaoitwa kwa Jina langu, watajinyenyekesha na kuomba na kuutafuta uso wangu na kuacha njia zao mbaya, basi nitasikia toka mbinguni na kuwasamehe dhambi yao na nitaiponya nchi yao. 15 Sasa macho yangu yatafumbuka na masikio yangu yatasikiliza kwa makini maombi yaombwayo mahali hapa.

  20. 14 Kwa kuwa tunaye Kuhani Mkuu kuliko wote ambaye ameingia mbinguni, Yesu Mwana wa Mungu, basi na tushikamane sana kwa uthabiti na ule ukiri wa imani yetu. 15 Kwa kuwa hatuna Kuhani Mkuu asiyeweza kuchukuliana na sisi katika udhaifu wetu, lakini tunaye mmoja ambaye alijaribiwa kwa kila namna, kama vile sisi tujaribiwavyo: lakini yeye hakutenda dhambi. 16 Basi na tukikaribie kiti cha rehema kwa ujasiri, ili tupewe rehema na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.

  21. 1 Njooni, tumwimbie Bwana kwa furaha;

    tumfanyie kelele za shangwe

    Mwamba wa wokovu wetu.

    2 Tuje mbele zake kwa shukrani,

    tumtukuze kwa vinanda na nyimbo.

    3 Kwa kuwa Bwana ni Mungu mkuu,

    mfalme mkuu juu ya miungu yote.

    4 Mkononi mwake mna vilindi vya dunia,

    na vilele vya milima ni mali yake.

    5 Bahari ni yake, kwani ndiye aliifanya,

    na mikono yake iliumba nchi kavu.

    6 Njooni, tusujudu, tumwabudu,

    tupige magoti mbele za Bwana Muumba wetu,

    7 kwa maana yeye ndiye Mungu wetu,

    na sisi ni watu wa malisho yake,

    kondoo chini ya utunzaji wake.

    Kama mkiisikia sauti yake leo,

  22. 38 Kisha Yesu akawaambia, “Moyo wangu umejawa na huzuni kiasi cha kufa. Kaeni hapa na mkeshe pamoja nami.”

    39 Akaenda mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akaomba akisema, “Baba yangu, kama inawezekana, kikombe hiki na kiniondokee. Lakini si kama nipendavyo mimi, bali kama upendavyo wewe.”

  23. 19 Kwa hiyo, ndugu zangu, kwa kuwa tunao ujasiri wa kupaingia Patakatifu pa Patakatifu kwa damu ya Yesu, 20 kwa njia mpya iliyo hai tuliyofunguliwa kwa ajili yetu kupitia kwenye lile pazia, yaani, mwili wake, 21 basi kwa kuwa tunaye Kuhani Mkuu juu ya nyumba ya Mungu, 22 sisi na tumkaribie Mungu kwa moyo mnyofu kwa imani timilifu, mioyo yetu ikiwa imenyunyizwa damu ya Kristo na kuwa safi kutokana na dhamiri mbaya nayo miili yetu ikiwa imeoshwa kwa maji safi. 23 Tushike kwa uthabiti lile tumaini la ukiri wetu bila kuyumbayumba, kwa maana yeye aliyeahidi ni mwaminifu.

  24. 23 Katika siku hiyo hamtaniuliza neno lolote. Amin, amin nawaambia, kama mkimwomba Baba jambo lolote kwa jina langu, yeye atawapa. 24 Mpaka sasa hamjaomba jambo lolote kwa Jina langu. Ombeni nanyi mtapewa, ili furaha yenu ipate kuwa kamili.

  25. 5 Kisha Samweli akasema, “Wakusanyeni Israeli wote huko Mispa, nami nitawaombea ninyi kwa Bwana.” 6 Walipokwisha kukutanika huko Mispa, walichota maji na kuyamimina mbele za Bwana. Siku hiyo walifunga na wakaungama, wakisema, “Tumetenda dhambi dhidi ya Bwana.” Naye Samweli alikuwa kiongozi wa Israeli huko Mispa.

    7 Wafilisti waliposikia kwamba Israeli wamekusanyika huko Mispa, watawala wa Wafilisti wakapanda ili kuwashambulia. Waisraeli waliposikia habari hiyo, waliogopa kwa sababu ya Wafilisti. 8 Wakamwambia Samweli, “Usiache kumlilia Bwana, Mungu wetu, kwa ajili yetu, ili apate kutuokoa na mikono ya Wafilisti.” 9 Kisha Samweli akamchukua mwana-kondoo anyonyaye na kumtoa mzima kama sadaka ya kuteketezwa kwa Bwana. Akamlilia Bwana kwa niaba ya Israeli, naye Bwana akamjibu.

    10 Samweli alipokuwa anatoa hiyo dhabihu ya kuteketezwa, Wafilisti wakasogea karibu ili kupigana vita na Israeli. Lakini siku ile Bwana alinguruma kwa ngurumo kubwa dhidi ya Wafilisti na kuwafanya wafadhaike na kutetemeka hivi kwamba walikimbizwa mbele ya Waisraeli.

  26. 2 Dumuni sana katika maombi, mkikesha katika hayo pamoja na kushukuru. 3 Pia tuombeeni na sisi ili Mungu atufungulie mlango wa kunena, ili tupate kuitangaza siri ya Kristo, ambayo kwa ajili yake pia mimi nimefungwa. 4 Ombeni ili nipate kuitangaza Injili kwa udhahiri kama ipasavyo kunena.

  27. 7 Ili kunizuia nisijivune kwa sababu ya ufunuo huu mkuu, nilipewa mwiba katika mwili wangu, mjumbe wa Shetani, ili anitese. 8 Kwa habari ya jambo hili nilimsihi Bwana mara tatu aniondolee mwiba huu. 9 Lakini aliniambia, “Neema yangu inakutosha, kwa kuwa uweza wangu hukamilika katika udhaifu.” Kwa hiyo nitajisifu kwa furaha zaidi kuhusu udhaifu wangu, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. 10 Hii ndiyo sababu, kwa ajili ya Kristo, nafurahia udhaifu, katika kutukanwa, katika taabu, katika mateso na katika shida, kwa maana ninapokuwa dhaifu, ndipo nina nguvu.

  28. 16 Lakini ninamwita Mungu,

    naye Bwana huniokoa.

    17 Jioni, asubuhi na adhuhuri

    ninalia kwa huzuni,

    naye husikia sauti yangu.

    18 Huniokoa nikawa salama katika vita

    vilivyopangwa dhidi yangu,

    ingawa watu wengi hunipinga.

    19 Mungu anayemiliki milele,

    atawasikia na kuwaadhibu,

    watu ambao hawabadilishi njia zao,

    wala hawana hofu ya Mungu.

    20 Mwenzangu hushambulia rafiki zake,

    naye huvunja agano lake.

    21 Mazungumzo yake ni laini kama siagi,

    hata hivyo vita vimo moyoni mwake.

    Maneno yake ni mororo kuliko mafuta,

    hata hivyo ni upanga mkali uliofutwa.

  29. 32 Jioni ile baada ya jua kutua, watu wakamletea Yesu wagonjwa wote na waliopagawa na pepo wachafu. 33 Mji wote ukakusanyika mbele ya nyumba hiyo. 34 Yesu akawaponya watu wengi waliokuwa na magonjwa ya aina mbalimbali. Akawatoa pepo wachafu wengi, lakini hakuwaacha hao pepo wachafu waseme, kwa sababu walimjua yeye ni nani.

    35 Alfajiri na mapema sana kulipokuwa bado kuna giza, Yesu akaamka, akaondoka, akaenda mahali pa faragha ili kuomba. 36 Simoni na wenzake wakaenda kumtafuta, 37 nao walipomwona, wakamwambia, “Kila mtu anakutafuta!”

  30. 1 Awali ya yote, nasihi kwamba dua, sala, maombezi na shukrani zifanyike kwa ajili ya watu wote: 2 kwa ajili ya wafalme na wale wote wenye mamlaka, ili tupate kuishi kwa amani na utulivu, katika uchaji wote wa Mungu na utakatifu. 3 Jambo hili ni jema, tena linapendeza machoni pa Mungu Mwokozi wetu, 4 anayetaka watu wote waokolewe na wafikie kuijua kweli.

  31. 9 Bwana akamwambia Mose, “Nimeona watu hawa, nao ni watu wenye shingo ngumu. 10 Sasa niache ili hasira yangu ipate kuwaka dhidi yao, nami nipate kuwaangamiza. Kisha nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa.”

    11 Lakini Mose akamsihi Bwana Mungu wake, akasema, “Ee Bwana, kwa nini hasira yako iwake dhidi ya watu wako, wale uliowatoa Misri kwa uweza mkuu na mkono wenye nguvu? 12 Kwa nini Wamisri waseme, ‘Ni kwa nia mbaya aliwatoa Misri, ili awaue milimani na kuwafuta usoni mwa dunia’? Achilia mbali hasira yako kali, waonee huruma na usilete maafa juu ya watu wako. 13 Wakumbuke watumishi wako Abrahamu, Isaki na Israeli, ambao uliwaapia kwa nafsi yako mwenyewe: ‘Nitawafanya uzao wako kuwa wengi kama nyota za angani, nami nitawapa wazao wako nchi hii yote ambayo niliwaahidia, nayo itakuwa urithi wao milele.’ ” 14 Kisha Bwana akawaonea huruma, wala hakuleta juu ya watu wake maafa aliyokuwa amekusudia.

  32. 59 Walipokuwa wakimpiga mawe, Stefano aliomba, “Bwana Yesu, pokea roho yangu.” 60 Kisha akapiga magoti, akalia kwa sauti kubwa akasema, “Bwana usiwahesabie dhambi hii.” Baada ya kusema hayo, akalala.

  33. 8 Nataka kila mahali wanaume wasali wakiinua mikono mitakatifu pasipo hasira wala kugombana.

  34. 5 Ndipo wakati wa kutoa dhabihu ya jioni nikainuka kutoka kujidhili kwangu nikiwa na koti na joho langu lililoraruka, nikapiga magoti mikono yangu ikiwa imeinuliwa kwa Bwana Mungu wangu. 6 Nami nikaomba:

    “Ee Mungu wangu, natahayari na kuona aibu kukuinulia uso wangu Mungu wangu, kwa sababu dhambi zetu zimejikusanya hata kupita juu ya vichwa vyetu na hatia yetu imefika mbinguni.

  35. 17 Bwana ni mwenye haki katika njia zake zote,

    na mwenye upendo kwa vyote alivyovifanya.

    18 Bwana yu karibu na wote wamwitao,

    karibu na wote wamwitao kwa uaminifu.

    19 Huwatimizia wamchao matakwa yao,

    husikia kilio chao na kuwaokoa.

    20 Bwana huwalinda wote wampendao,

    bali waovu wote atawaangamiza.

  36. 15 Kwa sababu hii, tangu niliposikia juu ya imani yenu katika Bwana Yesu na upendo wenu kwa watakatifu wote, 16 sijaacha kumshukuru Mungu kwa ajili yenu, nikiwakumbuka katika maombi yangu. 17 Nazidi kumwomba Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awajalieni ninyi roho ya hekima na ya ufunuo, ili mpate kumjua zaidi. 18 Ninaomba pia kwamba macho ya mioyo yenu yatiwe nuru ili mpate kujua tumaini mliloitiwa, utajiri wa urithi wa utukufu wake kwa watakatifu 19 na uweza wake mkuu usiolinganishwa kwa ajili yetu sisi tuaminio. Uweza huo unaofanya kazi ndani yetu, ni sawa na ile nguvu kuu mno 20 aliyoitumia katika Kristo alipomfufua kutoka kwa wafu, na akamketisha mkono wake wa kuume huko mbinguni, 21 juu sana kuliko falme zote na mamlaka, enzi na milki, na juu ya kila jina litajwalo, si katika ulimwengu huu tu, bali katika ule ujao pia.

  37. 19 Eliya akamjibu, “Nipe mwanao.” Eliya akampokea kutoka kifuani mwake, akambeba mpaka chumba cha juu alipokuwa anaishi, akamlaza kitandani mwake. 20 Kisha akamlilia Bwana, akasema “Ee Bwana Mungu wangu, je, pia umeleta msiba juu ya mjane huyu ninayeishi pamoja naye, kwa kusababisha mwanawe kufa?” 21 Kisha akajinyoosha juu ya kijana mara tatu na kumlilia Bwana, akisema, “Ee Bwana Mungu wangu, nakuomba roho ya huyu kijana imrudie!”

    22 Bwana akasikia kilio cha Eliya, na roho ya kijana ikamrudia, naye akafufuka. 23 Eliya akamtwaa kijana na kumbeba kutoka chumbani mwake akamshusha kumpeleka kwenye nyumba. Akampa mama yake na kusema, “Tazama, mwanao yu hai!”

  38. 15 Mnaponyoosha mikono yenu katika maombi,

    nitaficha macho yangu nisiwaone;

    hata mkiomba maombi mengi

    sitasikiliza.

    Mikono yenu imejaa damu;

    16 jiosheni na mkajitakase.

    Yaondoeni matendo yenu maovu

    mbele zangu!

    Acheni kutenda mabaya,

    17 jifunzeni kutenda mema!

    Tafuteni haki,

    watieni moyo walioonewa.

    Teteeni shauri la yatima,

    wateteeni wajane.

  39. 13 Walipowasili mjini Yerusalemu, walikwenda ghorofani kwenye chumba walichokuwa wakiishi. Wale waliokuwepo walikuwa: Petro, Yohana, Yakobo, Andrea, Filipo, Tomaso, Bartholomayo, Mathayo, Yakobo mwana wa Alfayo, Simoni Zelote na Yuda mwana wa Yakobo. 14 Hawa wote waliungana pamoja katika maombi. Pamoja nao walikuwepo wanawake kadha, na Maria mama yake Yesu, pamoja na ndugu zake Yesu.

  40. 4 Niliposikia mambo haya, niliketi, nikalia. Kwa siku kadhaa niliomboleza na kufunga na kuomba mbele za Mungu wa mbinguni. 5 Kisha nikasema:

    “Ee Bwana, Mungu wa mbinguni, mkuu na mwenye kuogofya, ambaye hulishika agano lake la upendo na wale wampendao na kutii amri zake, 6 tega masikio yako, na ufungue macho yako, ili usikie maombi ya mtumishi wako anayoomba mbele yako usiku na mchana kwa ajili ya watumishi wako, watu wa Israeli. Ninaungama dhambi zetu sisi Waisraeli, pamoja na zangu na za nyumba ya baba yangu, tulizotenda dhidi yako. 7 Tumetenda uovu sana mbele zako. Hatukutii amri, maagizo na sheria ulizompa Mose mtumishi wako.

  41. 21 Wapendwa, kama mioyo yetu haituhukumu, tunao ujasiri mbele za Mungu, 22 lolote tuombalo, twalipokea kutoka kwake, kwa sababu tumezitii amri zake na kutenda yale yanayompendeza.

  42. 20 Basi, nilipokuwa bado nikinena na kuomba, nikiungama dhambi yangu na dhambi ya watu wangu Israeli, na nikifanya maombi yangu kwa Bwana Mungu wangu kwa ajili ya mlima wake mtakatifu, 21 wakati nilipokuwa bado katika maombi, Gabrieli, yule mtu niliyekuwa nimemwona katika maono hapo awali, alinijia kwa kasi karibu wakati wa kutoa dhabihu ya jioni. 22 Akanielimisha na kuniambia, “Danieli, sasa nimekuja kukupa akili na ufahamu. 23 Mara ulipoanza kuomba, jibu lilitolewa, ambalo nimekuja kukupasha habari, kwa maana wewe unapendwa sana. Kwa hiyo, tafakari ujumbe huu na uelewe maono haya:

  43. 14 Hezekia akapokea barua kutoka kwa wale wajumbe, naye akaisoma. Kisha akapanda katika Hekalu la Bwana, akaikunjua mbele za Bwana. 15 Naye Hezekia akamwomba Bwana akisema: “Ee Bwana, Mungu wa Israeli, uketiye juu ya kiti cha enzi kati ya makerubi, wewe peke yako ndiwe Mungu juu ya falme zote za dunia. Wewe umeumba mbingu na nchi. 16 Tega sikio, Ee Bwana, usikie; fungua macho yako, Ee Bwana, uone; sikiliza maneno ambayo Senakeribu ametuma kumtukana Mungu aliye hai.

    17 “Ni kweli, Ee Bwana, kwamba wafalme wa Ashuru wameyaangamiza mataifa haya na nchi zao. 18 Wameitupa miungu yao kwenye moto na kuiangamiza, kwa kuwa haikuwa miungu, bali miti na mawe tu iliyotengenezwa kwa mikono ya wanadamu. 19 Sasa basi, Ee Bwana Mungu wetu, tuokoe kutoka mkononi mwake, ili falme zote duniani zipate kujua kwamba wewe peke yako, Ee Bwana, ndiwe Mungu.”

    20 Kisha Isaya mwana wa Amozi akapeleka ujumbe kwa Hezekia, akasema: “Hili ndilo asemalo Bwana, Mungu wa Israeli: Nimesikia maombi yako kuhusu Senakeribu mfalme wa Ashuru.

  44. 5 Kwa hiyo Petro akawekwa gerezani, lakini kanisa lilikuwa likimwombea kwa Mungu kwa bidii.

    6 Usiku ule kabla ya siku ambayo Herode Agripa alikuwa amekusudia kumtoa na kumfanyia mashtaka, Petro alikuwa amelala kati ya askari wawili, akiwa amefungwa kwa minyororo miwili. Nao walinzi wa zamu walikuwa wakilinda penye lango la gereza. 7 Ghafula malaika wa Bwana akatokea na nuru ikamulika mle ndani ya gereza. Yule malaika akampiga Petro ubavuni na kumwamsha, akisema, “Ondoka upesi!” Mara ile minyororo ikaanguka kutoka mikononi mwa Petro.

    8 Yule malaika akamwambia, “Vaa nguo zako na viatu vyako.” Petro akafanya hivyo. Kisha akamwambia, “Jifunge vazi lako na unifuate.”

  45. 4 Mfalme ni mwenye nguvu na hupenda haki,

    wewe umethibitisha adili;

    katika Yakobo umefanya

    yaliyo haki na sawa.

    5 Mtukuzeni Bwana Mungu wetu,

    na mkaabudu katika mahali pa kuwekea miguu yake;

    yeye ni mtakatifu.

    6 Mose na Aroni walikuwa miongoni mwa makuhani wake,

    Samweli alikuwa miongoni mwa walioliitia jina lake;

    walimwita Bwana,

    naye aliwajibu.

    7 Alizungumza nao kutoka nguzo ya wingu;

    walizishika sheria zake na amri alizowapa.

    8 Ee Bwana, wetu,

    ndiwe uliyewajibu,

    kwa Israeli ulikuwa Mungu mwenye kusamehe,

    ingawa uliadhibu matendo yao mabaya.

  46. 9 Ndipo utaita, naye Bwana atajibu,

    utalia kuomba msaada,

    naye atasema: Mimi hapa.

    “Kama ukiiondoa nira ya udhalimu,

    na kunyoosha kidole na kuzungumza maovu,

    10 nanyi kama mkimkunjulia mtu mwenye njaa nafsi zenu

    na kutosheleza mahitaji ya walioonewa,

    ndipo nuru yenu itakapongʼaa gizani,

    nao usiku wenu utakuwa kama adhuhuri.

    11 Bwana atakuongoza siku zote,

    atayatosheleza mahitaji yako katika nchi kame,

    naye ataitia nguvu mifupa yako.

    Utakuwa kama bustani iliyonyweshwa vizuri,

    kama chemchemi ambayo maji yake hayakauki kamwe.

  47. 24 Kabla hawajaita, nitajibu,

    nao wakiwa katika kunena, nitasikia.

  48. 5 Bwana akamtokea Solomoni huko Gibeoni wakati wa usiku katika ndoto, naye Mungu akasema, “Omba lolote utakalo nikupe.”

    6 Solomoni akajibu, “Umemfanyia mtumishi wako, baba yangu Daudi, fadhili nyingi, kwa kuwa alikuwa mwaminifu kwako na mwenye haki, tena mnyofu wa moyo. Nawe umemzidishia fadhili hii kuu kwani umempa mwana wa kuketi kwenye kiti chake cha ufalme, kama ilivyo leo.

    7 “Sasa, Ee Bwana Mungu wangu, umemfanya mtumishi wako mfalme badala ya baba yangu Daudi. Lakini mimi ni mtoto mdogo tu, wala sijui jinsi ya kutekeleza wajibu wangu. 8 Mtumishi wako yuko hapa miongoni mwa watu uliowachagua: taifa kubwa, watu wengi wasioweza kuhesabika wala kutoa idadi yao. 9 Hivyo mpe mtumishi wako moyo wa ufahamu ili kutawala watu wako na kupambanua kati ya mema na mabaya. Kwa maana, ni nani awezaye kutawala watu wako hawa walio wengi hivi?”

  49. 36 Wakati wa kutoa dhabihu ya jioni, nabii Eliya akasogea mbele na kuomba, akisema: “Ee Bwana, Mungu wa Abrahamu, na Isaki na Israeli, ijulikane leo kwamba wewe ndiye Mungu katika Israeli na ya kwamba mimi ni mtumishi wako na nimefanya mambo haya yote kwa neno lako. 37 Unijibu mimi, Ee Bwana, nijibu mimi, ili watu hawa wajue kwamba wewe, Ee Bwana, ndiwe Mungu, na kwamba unaigeuza mioyo yao ikurudie tena.”

    38 Kisha moto wa Bwana ukashuka na kuiteketeza ile dhabihu, zile kuni, yale mawe, ule udongo, na pia kuramba yale maji yaliyokuwa ndani ya handaki.

  50. 1 Baada ya Yesu kusema haya, alitazama kuelekea mbinguni akawaombea na kusema:

    “Baba, saa imewadia. Umtukuze Mwanao, ili Mwanao apate kukutukuza wewe.

  51. 22 Umati wa watu waliokuwepo wakajiunga katika kuwashambulia Paulo na Sila na wale mahakimu wakaamuru wavuliwe nguo zao na wachapwe viboko. 23 Baada ya kuwachapa sana, wakawatupa gerezani na kumwagiza mkuu wa gereza awalinde kikamilifu. 24 Kufuata maelekezo haya, yule mkuu wa gereza akawaweka katika chumba cha ndani sana mle gerezani, na akawafunga miguu yao kwa minyororo.

    25 Ilipokaribia usiku wa manane, Paulo na Sila walikuwa wakiomba na kuimba nyimbo za kumsifu Mungu, nao wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza. 26 Ghafula pakatokea tetemeko kubwa la ardhi, hata msingi wa gereza ukatikisika. Mara milango ya gereza ikafunguka na ile minyororo iliyowafunga kila mmoja ikafunguka.

  52. 9 Kwa sababu hii, tangu siku ile tuliposikia habari zenu, hatujakoma kuomba kwa ajili yenu na kumsihi Mungu awajaze ninyi maarifa ya mapenzi yake katika hekima yote ya kiroho na ufahamu. 10 Nasi tunaomba haya ili mpate kuishi maisha yanayostahili mbele za Bwana, na mpate kumpendeza kwa kila namna: mkizaa matunda kwa kila kazi njema, mkikua katika kumjua Mungu, 11 mkiwa mmetiwa nguvu kwa uwezo wote kwa kadiri ya nguvu yake yenye utukufu, ili mpate kuwa na wingi wa saburi na uvumilivu. Nanyi kwa furaha 12 mkimshukuru Baba, ambaye amewastahilisha kushiriki katika urithi wa watakatifu katika ufalme wa nuru. 13 Kwa maana ametuokoa kutoka ufalme wa giza na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wake mpendwa, 14 ambaye katika yeye tunao ukombozi, yaani msamaha wa dhambi.

  53. 6 Katika shida yangu nalimwita Bwana,

    nilimlilia Mungu wangu anisaidie.

    Kutoka hekaluni mwake alisikia sauti yangu,

    kilio changu kikafika mbele zake,

    masikioni mwake.

  54. 34 Yesu akasema, “Baba, wasamehe, kwa maana hawajui walitendalo!” Wakagawana nguo zake kwa kupiga kura.

  55. 2 Walipokuwa wakimwabudu Bwana na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, “Nitengeeni Sauli na Barnaba kwa kazi ile maalum niliyowaitia.” 3 Ndipo baada ya kufunga na kuomba, wakawawekea mikono yao na wakawatuma waende zao.

  56. 18 Tuombeeni. Tuna hakika kuwa tunayo dhamiri safi na shauku ya kuishi kwa uadilifu kwa kila njia. 19 Ninawasihi zaidi mniombee ili nipate kurudishwa kwenu upesi.

    20 Basi Mungu wa amani, ambaye kwa damu ya Agano la milele alimleta tena kutoka kwa wafu Bwana wetu Yesu, yule Mchungaji Mkuu wa kondoo, 21 awafanye ninyi wakamilifu mkiwa mmekamilishwa katika kila jambo jema ili mpate kutenda mapenzi yake, naye atende ndani yetu kile kinachompendeza machoni Pake, kwa njia ya Yesu Kristo, ambaye utukufu una yeye milele na milele. Amen.

  57. 25 Nilianguka kifudifudi mbele za Bwana kwa zile siku arobaini usiku na mchana kwa sababu Bwana alikuwa amesema angewaangamiza ninyi. 26 Nilimwomba Bwana na kusema, “Ee Bwana Mwenyezi, usiangamize watu wako, urithi wako mwenyewe ule ulioukomboa kwa uweza wako mkuu na kuwatoa katika nchi ya Misri kwa mkono wenye nguvu. 27 Wakumbuke watumishi wako Abrahamu, Isaki na Yakobo. Usiangalie ukaidi wa watu hawa, uovu wao wala dhambi yao. 28 Watu wa nchi ile uliyotutoa sisi wasije wakasema, ‘Ni kwa sababu Bwana hakuweza kuwachukua mpaka nchi aliyokuwa amewaahidia, kwa sababu aliwachukia, akawaleta ili aje kuwaua jangwani.’ 29 Bali wao ni watu wako, urithi wako ule ulioutoa Misri kwa uweza wako mkuu na kwa mkono wako ulionyooka.”

  58. 6 Mtafuteni Bwana maadamu anapatikana;

    mwiteni maadamu yu karibu.

  59. 21 Yesu akamjibu, “Mwanamke, niamini, wakati unakuja ambapo hamtamwabudu Baba katika mlima huu, wala huko Yerusalemu. 22 Ninyi Wasamaria mnaabudu msichokijua. Sisi Wayahudi tunamwabudu Mungu tunayemjua kwa sababu wokovu unatoka kwa Wayahudi. 23 Lakini saa yaja, tena ipo, ambapo wale waabuduo halisi, watamwabudu Baba katika roho na kweli. Watu wanaoabudu namna hii, ndio Baba anawatafuta. 24 Mungu ni Roho na wote wanaomwabudu imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.”

  60. 31 Walipokwisha kuomba, mahali walipokuwa wamekutanika pakatikiswa, wote wakajazwa na Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri.

    32 Wale walioamini wote walikuwa na moyo mmoja na nia moja. Wala hakuna hata mmoja aliyesema chochote alichokuwa nacho ni mali yake mwenyewe, lakini walishirikiana kila kitu walichokuwa nacho.

  61. 6 Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza Mungu, kwa maana yeyote anayemjia Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko na ya kuwa huwapa thawabu wale wamtafutao kwa bidii.

  62. 42 Kisha akasema, “Yesu, unikumbuke utakapokuja katika Ufalme wako.”

    43 Yesu akamjibu, “Amin, nakuambia, leo hii utakuwa pamoja nami Paradiso.”

  63. 15 Kwa maana hamkupokea roho ya utumwa iwaleteayo tena hofu, bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambaye kwa yeye twalia, “Abba, yaani, Baba,” 16 Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu ya kwamba sisi tu watoto wa Mungu.