43 Bible Verses About Friends
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
-
12 Amri yangu ndiyo hii: Mpendane kama mimi nilivyowapenda ninyi. 13 Hakuna mtu mwenye upendo mkuu kuliko huu, mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. 14 Ninyi ni rafiki zangu mkifanya ninayowaamuru. 15 Siwaiti ninyi watumishi tena, kwa sababu watumishi hawajui bwana wao analofanya, bali nimewaita ninyi rafiki, kwa maana nimewajulisha mambo yote niliyoyasikia kutoka kwa Baba yangu.
-
5 Afadhali karipio la wazi
kuliko upendo uliofichika.
6 Majeraha kutoka kwa rafiki yaonyesha uaminifu,
bali kubusu kwa adui ni kwingi sana.
7 Yeye aliyeshiba huchukia kabisa asali,
bali kwa mwenye njaa
hata kile kilicho kichungu
kwake ni kitamu.
8 Kama ndege atangatangavyo mbali na kiota chake,
ndivyo alivyo mtu atangatangaye
mbali na nyumbani mwake.
9 Manukato na uvumba huleta furaha moyoni,
nao uzuri wa rafiki huchipuka
kutoka kwenye ushauri wake wa uaminifu.
10 Usimwache rafiki yako wala rafiki wa baba yako,
tena usiende nyumbani mwa ndugu yako
wakati umepatwa na maafa.
Bora jirani wa karibu
kuliko ndugu aliye mbali.
-
24 Mtu mwenye marafiki wengi wanaweza kumharibu,
bali yuko rafiki aambatanaye na mtu kwa karibu kuliko ndugu.
-
17 Rafiki hupenda wakati wote
naye ndugu amezaliwa kwa ajili ya wakati wa shida.
18 Mtu mjinga hupana mkono ili kuweka rehani,
naye huweka dhamana kwa jirani yake.
-
9 Wawili ni afadhali kuliko mmoja,
kwa sababu wana malipo mazuri kwa kazi yao:
10 Kama mmoja akianguka,
mwenzake atamwinua.
Lakini ni jambo la kuhuzunisha
kwa mtu yule aangukaye
naye hana wa kumwinua!
11 Pia, kama wawili wakilala pamoja
watapashana joto.
Lakini ni vipi mtu aweza
kujipasha joto mwenyewe?
12 Ingawa mtu mmoja aweza kushindwa,
watu wawili wanaweza
kumkabili adui na kumshinda.
Kamba ya nyuzi tatu
haikatiki kwa urahisi.
-
17 Kama vile chuma kinoavyo chuma,
ndivyo mtu amnoavyo mwenzake.
-
12 Kwa hiyo, kwa kuwa ninyi mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao sana, jivikeni moyo wa huruma, utu wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu. 13 Vumilianeni na kusameheana mtu akiwa na lalamiko lolote dhidi ya mwenzake. Sameheaneni kama vile Bwana alivyowasamehe ninyi. 14 Zaidi ya maadili haya yote jivikeni upendo, ambao ndio unaofunga kila kitu pamoja katika umoja mkamilifu.
15 Amani ya Kristo na itawale mioyoni mwenu, kwa kuwa ninyi kama viungo vya mwili mmoja mmeitiwa amani. Tena kuweni watu wa shukrani. 16 Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu, mkifundishana na kuonyana katika hekima yote, mkimwimbia Mungu zaburi, nyimbo na tenzi za rohoni, huku mkiwa na shukrani mioyoni mwenu.
-
1 Baada ya Daudi kumaliza kuongea na Sauli, roho ya Yonathani ikaambatana na roho ya Daudi, naye akampenda kama nafsi yake mwenyewe. 2 Kuanzia siku ile Sauli akamchukua Daudi naye hakumruhusu kurudi nyumbani kwa baba yake. 3 Yonathani akafanya agano na Daudi kwa sababu alimpenda kama nafsi yake mwenyewe. 4 Yonathani akavua joho alilokuwa amevaa na kumpa Daudi, pamoja na koti lake, silaha zake, hata pamoja na upanga wake, upinde wake na mshipi wake.
5 Lolote Sauli alilomtuma Daudi kufanya, alitenda kwa hekima, hata Sauli akampa cheo cha juu katika jeshi. Jambo hili likawapendeza watu wote, hata maafisa wa Sauli pia.
-
24 Usifanye urafiki na mtu mwenye hasira ya haraka,
usishirikiane na yule aliye mwepesi kukasirika,
25 la sivyo utajifunza njia zake
na kujiingiza mwenyewe kwenye mtego.
26 Usiwe mwenye kupana mikono katika rehani,
au kuweka dhamana kwa ajili ya madeni.
27 Kama ukikosa njia ya kulipa,
kitanda chako
kitachukuliwa ukiwa umekilalia.
-
20 Yeye atembeaye na mwenye hekima atapata hekima,
bali rafiki wa mpumbavu hupata madhara.
-
28 Mtu mpotovu huchochea ugomvi,
nayo maongezi ya upuzi hutenganisha marafiki wa karibu.
-
33 Msidanganyike: “Ushirika na watu wabaya huharibu tabia njema.”
-
1 Ndugu zangu, ikiwa mtu ameghafilika akatenda dhambi, basi ninyi mlio wa rohoni, mrejesheni upya mtu huyo kwa roho ya upole. Lakini jihadharini, ili ninyi wenyewe msije mkajaribiwa. 2 Chukulianeni mizigo ninyi kwa ninyi, nanyi kwa njia hii mtatimiza sheria ya Kristo.
-
9 Yeye anayesamehe kosa hudumisha upendo,
bali yeyote arudiaye jambo hutenganisha marafiki wa karibu.
-
26 Mtu mwenye haki ni mwangalifu katika urafiki,
bali njia ya waovu huwapotosha.
27 Mtu mvivu haoki mawindo yake,
bali mtu mwenye bidii ana mali za thamani.
-
4 Ninyi wanaume na wanawake wazinzi, hamjui ya kwamba urafiki na dunia ni uadui na Mungu? Kwa hiyo mtu yeyote anayetaka kuwa rafiki wa dunia hufanyika adui wa Mungu.
-
9 Upendo lazima usiwe na unafiki. Chukieni lililo ovu, shikamaneni na lililo jema. 10 Pendaneni ninyi kwa ninyi kwa upendo wa ndugu. Waheshimuni na kuwatanguliza wengine. 11 Msiwe wavivu, bali mwe na bidii katika roho mkimtumikia Bwana.
-
9 Kwa maana Mungu hakutuita ili tupate ghadhabu bali tupate wokovu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. 10 Yeye alikufa kwa ajili yetu ili hata kama tuko macho au tumelala, tupate kuishi pamoja naye. 11 Kwa hiyo farijianeni na kujengana, kama vile mnavyofanya sasa.
-
16 Lakini Ruthu akajibu, “Usinisihi nikuache au niache kukufuata. Utakakokwenda nami nitakwenda, na wewe utakapoishi nitaishi. Watu wako watakuwa watu wangu, na Mungu wako atakuwa Mungu wangu. 17 Pale utakapofia nami nitafia hapo, na papo hapo nitazikwa. Bwana na aniadhibu vikali, kama kitu kingine chochote kitanitenga nawe isipokuwa kifo.” 18 Naomi alipotambua kwamba Ruthu amenuia kufuatana naye, hakuendelea kumsihi tena.
-
11 Basi marafiki watatu wa Ayubu, ndio Elifazi Mtemani, na Bildadi Mshuhi na Sofari Mnaamathi, waliposikia juu ya taabu yote iliyompata Ayubu, wakajipanga toka manyumbani mwao, nao wakakutana pamoja kwa makubaliano kwenda kumtuliza katika taabu hiyo na kumfariji. 12 Walipomwona kwa mbali, ilikuwa vigumu kumtambua. Wakaanza kulia kwa sauti kubwa, wakayararua majoho yao na kujirushia mavumbi juu ya vichwa vyao. 13 Kisha wakaketi chini kwenye udongo pamoja na Ayubu kwa siku saba usiku na mchana. Hakuna yeyote aliyesema naye neno, kwa sababu waliona jinsi mateso yake yalivyokuwa makubwa.
-
20 Mwombezi wangu ni rafiki yangu
macho yangu yamwagapo machozi kwa Mungu;
21 kwa niaba ya mtu anamsihi Mungu
kama mtu anavyosihi kwa ajili ya rafiki yake.
-
8 Zaidi ya yote, dumuni katika upendo kwa maana upendo husitiri wingi wa dhambi. 9 Kuweni wakarimu kila mtu na mwenzake pasipo manungʼuniko. 10 Kila mmoja na atumie kipawa chochote alichopewa kuwahudumia wengine, kama mawakili waaminifu wa neema mbalimbali za Mungu.
-
Wimbo wa kwenda juu. Wa Daudi.
1 Tazama jinsi ilivyo vyema na kupendeza
wakati ndugu wanapoishi pamoja katika umoja!
-
46 Inukeni, twende zetu! Tazameni, msaliti wangu yuaja!”
47 Alipokuwa bado anazungumza, Yuda, mmoja wa wale Kumi na Wawili, akafika. Alikuwa amefuatana na umati mkubwa wa watu wenye panga na marungu, waliokuwa wametumwa na viongozi wa makuhani na wazee wa watu. 48 Basi msaliti alikuwa amewapa hao watu ishara, kwamba: “Yule nitakayembusu ndiye. Mkamateni.” 49 Mara Yuda akamjia Yesu na kumsalimu, “Salamu, Rabi!” Akambusu.
50 Yesu akamwambia, “Rafiki, fanya kile ulichokuja kufanya hapa.”
Kisha wale watu wakasogea mbele, wakamkamata Yesu.
-
10 Kila mara watu walipoona hiyo nguzo ya wingu ikiwa imesimama kwenye ingilio la hema, wote walisimama wakaabudu, kila mmoja kwenye ingilio la hema lake. 11 Bwana angezungumza na Mose uso kwa uso, kama vile mtu azungumzavyo na rafiki yake. Kisha Mose angerudi kambini, lakini msaidizi wake kijana Yoshua mwana wa Nuni hakuondoka mle Hemani.
-
12 Kama aliyenitukana ni adui yangu, ningevumilia,
kama mtu mwovu angejiinua dhidi yangu,
ningejificha asinione.
13 Kumbe ni wewe, mwenzangu,
mshiriki na rafiki yangu wa karibu,
14 ambaye awali tulifurahia ushirika mzuri,
tulipokuwa tukienda na umati hekaluni mwa Mungu.
-
42 Nao wakawa wanadumu katika mafundisho ya mitume, katika ushirika, katika kumega mkate na katika kusali. 43 Kila mtu akaingiwa na hofu ya Mungu, nayo miujiza mingi na ishara zikafanywa na mitume. 44 Walioamini wote walikuwa mahali pamoja, nao walikuwa na kila kitu shirika. 45 Waliuza mali zao na vitu walivyokuwa navyo, kila mtu akagawiwa kadiri ya mahitaji yake. 46 Siku zote kwa moyo mmoja walikutana ndani ya ukumbi wa Hekalu, wakimega mkate nyumba kwa nyumba, wakila chakula chao kwa furaha na moyo mweupe, 47 wakimsifu Mungu na kuwapendeza watu wote. Kila siku Bwana akaliongeza kanisa wale waliokuwa wakiokolewa.
-
1 Kama kukiwa na jambo lolote la kutia moyo katika kuunganishwa na Kristo, kukiwa faraja yoyote katika upendo wake, kukiwa na ushirika wowote na Roho, kukiwa na wema wowote na huruma, 2 basi ikamilisheni furaha yangu kwa kuwa na nia moja, mkiwa na upendo huo moja, mkiwa wa roho na kusudi moja. 3 Msitende jambo lolote kwa nia ya kujitukuza wala kujivuna, bali kwa unyenyekevu kila mtu amhesabu mwingine bora kuliko nafsi yake. 4 Kila mmoja wenu asiangalie faida yake mwenyewe tu, bali pia ajishughulishe kwa faida ya wengine.
-
24 Tuangaliane na kuhimizana sisi kwa sisi katika upendo na katika kutenda mema. 25 Wala tusiache kukutana pamoja, kama wengine walivyo na desturi, bali tuhimizane sisi kwa sisi kadiri tuonavyo Siku ile inakaribia.
-
23 Kwa njia hiyo yakatimizwa yale Maandiko yasemayo, “Abrahamu alimwamini Mungu na ikahesabiwa kwake kuwa haki,” naye akaitwa rafiki wa Mungu.
-
10 Baada ya Ayubu kuwaombea rafiki zake, Bwana akamwondoa kwenye uteka, akamfanikisha tena naye akampa mara mbili ya vile alivyokuwa navyo hapo mwanzoni.
-
9 Hata rafiki yangu wa karibu niliyemwamini,
yule aliyekula chakula changu
ameniinulia kisigino chake.
-
8 “Lakini wewe, ee Israeli, mtumishi wangu,
Yakobo, niliyemchagua,
ninyi wazao wa Abrahamu rafiki yangu,
-
15 “Kama ndugu yako akikukosea, nenda ukamwonyeshe kosa lake, kati yenu ninyi wawili peke yenu. Kama akikusikiliza, utakuwa umempata tena ndugu yako.
-
27 “Lakini nawaambia ninyi mnaonisikia: Wapendeni adui zenu. Watendeeni mema wanaowachukia. 28 Wabarikini wale wanaowalaani, waombeeni wale wanaowatendea mabaya. 29 Kama mtu akikupiga shavu moja, mgeuzie na la pili pia. Mtu akikunyangʼanya koti lako, usimzuie kuchukua joho pia. 30 Mpe kila akuombaye, na kama mtu akichukua mali yako usitake akurudishie. 31 Watendeeni wengine kama ambavyo mngetaka wawatendee ninyi.
-
4 Upendo huvumilia, upendo hufadhili, upendo hauoni wivu, hauna majivuno, hauna kiburi. 5 Haukosi kuwa na adabu, hautafuti mambo yake, haukasiriki upesi, hauweki kumbukumbu ya mabaya. 6 Upendo haufurahii mabaya bali hufurahi pamoja na kweli. 7 Upendo huvumilia yote, huamini yote, hutumaini yote, hustahimili yote.
-
3 Je, watu wawili hutembea pamoja
wasipokubaliana kufanya hivyo?
-
16 Katika utetezi wangu wa mara ya kwanza, hakuna hata mmoja aliyeniunga mkono, bali kila mmoja aliniacha. Namwomba Mungu wasihesabiwe hatia kwa jambo hilo.
-
6 Kama ndugu yako hasa, au mwanao au binti yako, au mke umpendaye, au rafiki yako wa karibu sana akikushawishi kwa siri, akisema, “Na twende tukaabudu miungu mingine” (miungu ambayo ninyi wala baba zenu hamkuifahamu, 7 miungu ya watu wanaowazunguka, ikiwa karibu au mbali, kutoka mwisho mmoja wa nchi mpaka mwingine), 8 usikubali wala usimsikilize. Usimhurumie! Usimwache wala usimkinge. 9 Hakika ni lazima auawe. Ni lazima mkono wako uwe wa kwanza katika kumuua kisha mikono ya watu wengine wote. 10 Mpigeni kwa mawe mpaka afe, kwa sababu alijaribu kuwageuza mtoke kwa Bwana Mungu wenu ambaye aliwatoa Misri, kutoka nchi ya utumwa. 11 Kisha Israeli wote watasikia na kuogopa, wala hakuna mmoja miongoni mwenu atakayefanya uovu tena.
-
19 Mwana wa Adamu alikuja akila na kunywa, nao wanasema, ‘Tazameni huyu mlafi na mlevi, rafiki wa watoza ushuru na “wenye dhambi.” ’ Lakini hekima huthibitishwa kuwa kweli kwa matendo yake.”
-
5 Kisha akawaambia, “Ni nani miongoni mwenu mwenye rafiki yake, naye akamwendea usiku wa manane na kumwambia, ‘Rafiki, nikopeshe mikate mitatu. 6 Kwa sababu rafiki yangu amekuja kutoka safarini, nami sina kitu cha kumpa.’
7 “Kisha yule aliyeko ndani amjibu, ‘Usinisumbue. Mlango umefungwa, nami na watoto wangu tumelala. Siwezi kuamka nikupe chochote.’ 8 Nawaambia, ingawa huyo mtu hataamka na kumpa hiyo mikate kwa sababu ni rafiki yake, lakini kwa sababu ya kuendelea kwake kuomba, ataamka na kumpa kiasi anachohitaji.
-
15 Furahini pamoja na wenye kufurahi, lieni pamoja na wale waliao.
-
16 Kwa namna hii twaweza kulijua pendo la Mungu: Kwa sababu Yesu Kristo aliutoa uhai wake kwa ajili yetu. Nasi imetupasa kuutoa uhai kwa ajili ya hao ndugu. 17 Ikiwa mtu anavyo vitu vya ulimwengu huu na akamwona ndugu yake ni mhitaji lakini asimhurumie, upendo wa Mungu wakaaje ndani ya mtu huyo? 18 Watoto wapendwa, tusipende kwa maneno au kwa ulimi bali kwa tendo na kweli.
Shows Read in context, Share and Copy.