42 Bible Verses About Friendship and Love
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
-
12 Amri yangu ndiyo hii: Mpendane kama mimi nilivyowapenda ninyi. 13 Hakuna mtu mwenye upendo mkuu kuliko huu, mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. 14 Ninyi ni rafiki zangu mkifanya ninayowaamuru. 15 Siwaiti ninyi watumishi tena, kwa sababu watumishi hawajui bwana wao analofanya, bali nimewaita ninyi rafiki, kwa maana nimewajulisha mambo yote niliyoyasikia kutoka kwa Baba yangu. 16 Si ninyi mlionichagua, bali mimi ndiye niliyewachagua ninyi na kuwaweka mwende mkazae matunda, na matunda yenu yapate kudumu. Ili nalo lolote mtakalomwomba Baba katika Jina langu, awape ninyi. 17 Amri yangu ndiyo hii: Mpendane.
-
17 Rafiki hupenda wakati wote
naye ndugu amezaliwa kwa ajili ya wakati wa shida.
18 Mtu mjinga hupana mkono ili kuweka rehani,
naye huweka dhamana kwa jirani yake.
-
24 Mtu mwenye marafiki wengi wanaweza kumharibu,
bali yuko rafiki aambatanaye na mtu kwa karibu kuliko ndugu.
-
9 Wawili ni afadhali kuliko mmoja,
kwa sababu wana malipo mazuri kwa kazi yao:
10 Kama mmoja akianguka,
mwenzake atamwinua.
Lakini ni jambo la kuhuzunisha
kwa mtu yule aangukaye
naye hana wa kumwinua!
11 Pia, kama wawili wakilala pamoja
watapashana joto.
Lakini ni vipi mtu aweza
kujipasha joto mwenyewe?
12 Ingawa mtu mmoja aweza kushindwa,
watu wawili wanaweza
kumkabili adui na kumshinda.
Kamba ya nyuzi tatu
haikatiki kwa urahisi.
-
5 Afadhali karipio la wazi
kuliko upendo uliofichika.
6 Majeraha kutoka kwa rafiki yaonyesha uaminifu,
bali kubusu kwa adui ni kwingi sana.
-
17 Kama vile chuma kinoavyo chuma,
ndivyo mtu amnoavyo mwenzake.
-
1 Baada ya Daudi kumaliza kuongea na Sauli, roho ya Yonathani ikaambatana na roho ya Daudi, naye akampenda kama nafsi yake mwenyewe. 2 Kuanzia siku ile Sauli akamchukua Daudi naye hakumruhusu kurudi nyumbani kwa baba yake. 3 Yonathani akafanya agano na Daudi kwa sababu alimpenda kama nafsi yake mwenyewe. 4 Yonathani akavua joho alilokuwa amevaa na kumpa Daudi, pamoja na koti lake, silaha zake, hata pamoja na upanga wake, upinde wake na mshipi wake.
5 Lolote Sauli alilomtuma Daudi kufanya, alitenda kwa hekima, hata Sauli akampa cheo cha juu katika jeshi. Jambo hili likawapendeza watu wote, hata maafisa wa Sauli pia.
-
12 Kwa hiyo, kwa kuwa ninyi mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao sana, jivikeni moyo wa huruma, utu wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu. 13 Vumilianeni na kusameheana mtu akiwa na lalamiko lolote dhidi ya mwenzake. Sameheaneni kama vile Bwana alivyowasamehe ninyi. 14 Zaidi ya maadili haya yote jivikeni upendo, ambao ndio unaofunga kila kitu pamoja katika umoja mkamilifu.
-
9 Yeye anayesamehe kosa hudumisha upendo,
bali yeyote arudiaye jambo hutenganisha marafiki wa karibu.
-
23 Kwa njia hiyo yakatimizwa yale Maandiko yasemayo, “Abrahamu alimwamini Mungu na ikahesabiwa kwake kuwa haki,” naye akaitwa rafiki wa Mungu.
-
20 Yeye atembeaye na mwenye hekima atapata hekima,
bali rafiki wa mpumbavu hupata madhara.
-
10 Usimwache rafiki yako wala rafiki wa baba yako,
tena usiende nyumbani mwa ndugu yako
wakati umepatwa na maafa.
Bora jirani wa karibu
kuliko ndugu aliye mbali.
-
4 Ninyi wanaume na wanawake wazinzi, hamjui ya kwamba urafiki na dunia ni uadui na Mungu? Kwa hiyo mtu yeyote anayetaka kuwa rafiki wa dunia hufanyika adui wa Mungu.
-
28 Mtu mpotovu huchochea ugomvi,
nayo maongezi ya upuzi hutenganisha marafiki wa karibu.
-
9 Manukato na uvumba huleta furaha moyoni,
nao uzuri wa rafiki huchipuka
kutoka kwenye ushauri wake wa uaminifu.
-
10 Pendaneni ninyi kwa ninyi kwa upendo wa ndugu. Waheshimuni na kuwatanguliza wengine. 11 Msiwe wavivu, bali mwe na bidii katika roho mkimtumikia Bwana.
-
33 Msidanganyike: “Ushirika na watu wabaya huharibu tabia njema.”
-
1 Ndugu zangu, ikiwa mtu ameghafilika akatenda dhambi, basi ninyi mlio wa rohoni, mrejesheni upya mtu huyo kwa roho ya upole. Lakini jihadharini, ili ninyi wenyewe msije mkajaribiwa. 2 Chukulianeni mizigo ninyi kwa ninyi, nanyi kwa njia hii mtatimiza sheria ya Kristo.
-
11 Kwa hiyo farijianeni na kujengana, kama vile mnavyofanya sasa.
-
7 Basi Mose alikuwa na desturi ya kuchukua hema na kuliweka wakfu nje ya kambi umbali kiasi, akaliita “Hema la Kukutania.” Kila aliyekuwa akiulizia shauri kwa Bwana, angelikwenda katika Hema la Kukutania nje ya kambi. 8 Wakati wowote Mose alipokwenda kwenye Hema, watu wote waliinuka na kusimama kwenye maingilio ya mahema yao, wakimwangalia Mose mpaka aingie kwenye Hema. 9 Kila mara Mose alipoingia ndani ya hema, nguzo ya wingu ingeshuka chini na kukaa kwenye ingilio, wakati Mungu akizungumza na Mose. 10 Kila mara watu walipoona hiyo nguzo ya wingu ikiwa imesimama kwenye ingilio la hema, wote walisimama wakaabudu, kila mmoja kwenye ingilio la hema lake. 11 Bwana angezungumza na Mose uso kwa uso, kama vile mtu azungumzavyo na rafiki yake. Kisha Mose angerudi kambini, lakini msaidizi wake kijana Yoshua mwana wa Nuni hakuondoka mle Hemani.
-
20 Mwombezi wangu ni rafiki yangu
macho yangu yamwagapo machozi kwa Mungu;
21 kwa niaba ya mtu anamsihi Mungu
kama mtu anavyosihi kwa ajili ya rafiki yake.
-
24 Usifanye urafiki na mtu mwenye hasira ya haraka,
usishirikiane na yule aliye mwepesi kukasirika,
25 la sivyo utajifunza njia zake
na kujiingiza mwenyewe kwenye mtego.
26 Usiwe mwenye kupana mikono katika rehani,
au kuweka dhamana kwa ajili ya madeni.
27 Kama ukikosa njia ya kulipa,
kitanda chako
kitachukuliwa ukiwa umekilalia.
-
31 Watendeeni wengine kama ambavyo mngetaka wawatendee ninyi.
32 “Kama mkiwapenda tu wale wanaowapenda, mwapata sifa gani? Hata ‘wenye dhambi’ huwapenda wale wawapendao. 33 Tena mkiwatendea mema wale tu wanaowatendea ninyi mema, mwapata sifa gani? Hata ‘wenye dhambi’ hufanya vivyo hivyo. 34 Tena mnapowakopesha wale tu mnaotegemea wawalipe, mwapata sifa gani? Hata ‘wenye dhambi’ huwakopesha ‘wenye dhambi’ wenzao wakitarajia kulipwa mali yao yote. 35 Lakini wapendeni adui zenu, watendeeni mema, wakopesheni bila kutegemea kurudishiwa mlichokopesha. Ndipo thawabu yenu itakapokuwa kubwa, nanyi mtakuwa wana wa Aliye Juu Sana, kwa sababu yeye ni mwema kwa watu wasio na shukrani na kwa wale waovu.
-
8 Zaidi ya yote, dumuni katika upendo kwa maana upendo husitiri wingi wa dhambi. 9 Kuweni wakarimu kila mtu na mwenzake pasipo manungʼuniko. 10 Kila mmoja na atumie kipawa chochote alichopewa kuwahudumia wengine, kama mawakili waaminifu wa neema mbalimbali za Mungu.
-
16 Lakini Ruthu akajibu, “Usinisihi nikuache au niache kukufuata. Utakakokwenda nami nitakwenda, na wewe utakapoishi nitaishi. Watu wako watakuwa watu wangu, na Mungu wako atakuwa Mungu wangu. 17 Pale utakapofia nami nitafia hapo, na papo hapo nitazikwa. Bwana na aniadhibu vikali, kama kitu kingine chochote kitanitenga nawe isipokuwa kifo.” 18 Naomi alipotambua kwamba Ruthu amenuia kufuatana naye, hakuendelea kumsihi tena.
-
32 Daudi alipofika kwenye kilele cha mlima, mahali ambapo watu walikuwa wamezoea kumwabudu Mungu, Hushai, Mwariki, alikuwako huko kumlaki, joho lake likiwa limeraruka na mavumbi kichwani mwake. 33 Daudi akamwambia, “Kama ukienda pamoja nami, utakuwa mzigo kwangu. 34 Lakini ikiwa utarudi mjini na kumwambia Absalomu, ‘Nitakuwa mtumishi wako, ee mfalme; nilikuwa mtumishi wa baba yako wakati uliopita, lakini sasa nitakuwa mtumishi wako,’ basi utaweza kunisaidia kwa kupinga shauri la Ahithofeli. 35 Je, makuhani Sadoki na Abiathari hawatakuwa pamoja nawe? Waambie lolote utakalosikia katika jumba la mfalme. 36 Wana wao wawili, Ahimaasi mwana wa Sadoki na Yonathani mwana wa Abiathari, wako pamoja nao huko. Watume kwangu na lolote utakalosikia.”
37 Kwa hiyo Hushai, rafiki wa Daudi, akafika Yerusalemu wakati Absalomu alipokuwa anaingia mjini.
-
14 “Mtu anayekata tamaa angetazamia moyo wa kujitoa wa rafiki zake,
hata kama akiacha uchaji wa Mwenyezi.
-
Wimbo wa kwenda juu. Wa Daudi.
1 Tazama jinsi ilivyo vyema na kupendeza
wakati ndugu wanapoishi pamoja katika umoja!
-
26 Mtu mwenye haki ni mwangalifu katika urafiki,
bali njia ya waovu huwapotosha.
-
8 “Lakini wewe, ee Israeli, mtumishi wangu,
Yakobo, niliyemchagua,
ninyi wazao wa Abrahamu rafiki yangu,
-
5 Kisha akawaambia, “Ni nani miongoni mwenu mwenye rafiki yake, naye akamwendea usiku wa manane na kumwambia, ‘Rafiki, nikopeshe mikate mitatu. 6 Kwa sababu rafiki yangu amekuja kutoka safarini, nami sina kitu cha kumpa.’
7 “Kisha yule aliyeko ndani amjibu, ‘Usinisumbue. Mlango umefungwa, nami na watoto wangu tumelala. Siwezi kuamka nikupe chochote.’ 8 Nawaambia, ingawa huyo mtu hataamka na kumpa hiyo mikate kwa sababu ni rafiki yake, lakini kwa sababu ya kuendelea kwake kuomba, ataamka na kumpa kiasi anachohitaji.
-
24 Tuangaliane na kuhimizana sisi kwa sisi katika upendo na katika kutenda mema. 25 Wala tusiache kukutana pamoja, kama wengine walivyo na desturi, bali tuhimizane sisi kwa sisi kadiri tuonavyo Siku ile inakaribia.
-
26 Nahuzunika kwa ajili yako,
Yonathani ndugu yangu,
kwangu ulikuwa mpendwa sana.
Upendo wako kwangu ulikuwa wa ajabu,
wa ajabu zaidi kuliko ule wa wanawake.
-
7 Je, si wewe, Ee Mungu wetu, uliyewafukuza wenyeji wa nchi hii mbele ya watu wako Israeli, ukawapa wazao wa Abrahamu, rafiki yako, hata milele?
-
12 Kama aliyenitukana ni adui yangu, ningevumilia,
kama mtu mwovu angejiinua dhidi yangu,
ningejificha asinione.
13 Kumbe ni wewe, mwenzangu,
mshiriki na rafiki yangu wa karibu,
14 ambaye awali tulifurahia ushirika mzuri,
tulipokuwa tukienda na umati hekaluni mwa Mungu.
-
15 “Kama ndugu yako akikukosea, nenda ukamwonyeshe kosa lake, kati yenu ninyi wawili peke yenu. Kama akikusikiliza, utakuwa umempata tena ndugu yako. 16 Lakini kama hatakusikiliza, nenda na mtu mwingine mmoja au wawili ili kila neno lithibitishwe kwa ushahidi wa mashahidi wawili au watatu. 17 Kama akikataa kuwasikiliza hao, liambie kanisa. Naye kama akikataa hata kulisikiliza kanisa, basi awe kwenu kama mtu asiyeamini au mtoza ushuru.
18 “Amin, nawaambia, lolote mtakalolifunga duniani litakuwa limefungwa mbinguni, na lolote mtakalolifungua duniani litakuwa limefunguliwa mbinguni.
19 “Tena nawaambia, ikiwa wawili wenu watakubaliana duniani kuhusu jambo lolote watakaloomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni. 20 Kwa kuwa wanapokusanyika pamoja watu wawili au watatu kwa Jina langu, mimi niko papo hapo pamoja nao.”
-
16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. 17 Kwa maana Mungu hakumtuma Mwanawe kuuhukumu ulimwengu, bali kupitia kwake ulimwengu upate kuokolewa.
-
11 Ninatamani sana kuwaona ili nipate kuweka juu yenu karama za rohoni ili mwe imara, 12 au zaidi, ninyi pamoja nami tuweze kutiana moyo katika imani sisi kwa sisi.
-
2 Kwa Timotheo, mwanangu mpendwa:
Neema, rehema na amani itokayo kwa Mungu Baba, na kwa Kristo Yesu Bwana wetu.
3 Ninamshukuru Mungu, ninayemtumikia kwa dhamiri safi, kama walivyofanya baba zangu, ninapokukumbuka usiku na mchana katika maombi yangu. 4 Nikiyakumbuka machozi yako, ninatamani sana kukuona ili nipate kujawa na furaha.
-
16 Kwa namna hii twaweza kulijua pendo la Mungu: Kwa sababu Yesu Kristo aliutoa uhai wake kwa ajili yetu. Nasi imetupasa kuutoa uhai kwa ajili ya hao ndugu. 17 Ikiwa mtu anavyo vitu vya ulimwengu huu na akamwona ndugu yake ni mhitaji lakini asimhurumie, upendo wa Mungu wakaaje ndani ya mtu huyo? 18 Watoto wapendwa, tusipende kwa maneno au kwa ulimi bali kwa tendo na kweli. 19 Basi hivi ndivyo tutakavyoweza kujua ya kuwa sisi tu wa kweli na hivyo twaithibitisha mioyo yetu mbele za Mungu
-
7 Wapendwa, tupendane, kwa kuwa pendo latoka kwa Mungu. Kila apendaye amezaliwa na Mungu, naye anamjua Mungu.
-
16 Hivyo nasi twajua na kulitumainia pendo la Mungu alilo nalo kwa ajili yetu.
Mungu ni Upendo. Kila akaaye katika upendo hukaa ndani ya Mungu na Mungu hukaa ndani yake. 17 Kwa njia hii, pendo hukamilishwa miongoni mwetu ili tupate kuwa na ujasiri katika siku ya hukumu, kwa sababu kama alivyo ndivyo tulivyo sisi katika ulimwengu huu. 18 Katika pendo hakuna hofu. Lakini pendo lililo kamili huitupa nje hofu, kwa sababu hofu inahusika na adhabu. Kila mwenye hofu hakukamilika katika pendo.
19 Twampenda yeye kwa sababu yeye alitupenda kwanza. 20 Ikiwa mtu atasema, “Nampenda Mungu,” lakini anamchukia ndugu yake, yeye ni mwongo. Kwa maana kila mtu asiyempenda ndugu yake ambaye anamwona, atampendaje Mungu asiyemuona? 21 Naye ametupa amri hii: Yeyote anayempenda Mungu lazima pia ampende ndugu yake.
Shows Read in context, Share and Copy.