90 Bible Verses About Worshiping God
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
-
21 Yesu akamjibu, “Mwanamke, niamini, wakati unakuja ambapo hamtamwabudu Baba katika mlima huu, wala huko Yerusalemu. 22 Ninyi Wasamaria mnaabudu msichokijua. Sisi Wayahudi tunamwabudu Mungu tunayemjua kwa sababu wokovu unatoka kwa Wayahudi. 23 Lakini saa yaja, tena ipo, ambapo wale waabuduo halisi, watamwabudu Baba katika roho na kweli. Watu wanaoabudu namna hii, ndio Baba anawatafuta. 24 Mungu ni Roho na wote wanaomwabudu imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.”
-
1 Njooni, tumwimbie Bwana kwa furaha;
tumfanyie kelele za shangwe
Mwamba wa wokovu wetu.
2 Tuje mbele zake kwa shukrani,
tumtukuze kwa vinanda na nyimbo.
3 Kwa kuwa Bwana ni Mungu mkuu,
mfalme mkuu juu ya miungu yote.
4 Mkononi mwake mna vilindi vya dunia,
na vilele vya milima ni mali yake.
5 Bahari ni yake, kwani ndiye aliifanya,
na mikono yake iliumba nchi kavu.
6 Njooni, tusujudu, tumwabudu,
tupige magoti mbele za Bwana Muumba wetu,
7 kwa maana yeye ndiye Mungu wetu,
na sisi ni watu wa malisho yake,
kondoo chini ya utunzaji wake.
Kama mkiisikia sauti yake leo,
-
1 Kwa hiyo, ndugu zangu, nawasihi kwa rehema zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu na inayompendeza Mungu, hii ndiyo ibada yenu yenye maana.
-
Zaburi ya shukrani.
1 Mpigieni Bwana kelele za shangwe, dunia yote.
2 Mwabuduni Bwana kwa furaha;
njooni mbele zake kwa nyimbo za shangwe.
3 Jueni kwamba Bwana ndiye Mungu.
Yeye ndiye alituumba, sisi tu mali yake;
sisi tu watu wake,
kondoo wa malisho yake.
4 Ingieni malangoni mwake kwa shukrani
na katika nyua zake kwa kusifu,
mshukuruni yeye na kulisifu jina lake.
-
Zaburi ya Daudi.
1 Mpeni Bwana, enyi mashujaa,
mpeni Bwana utukufu na nguvu.
2 Mpeni Bwana utukufu unaostahili jina lake;
mwabuduni Bwana katika uzuri wa utakatifu wake.
-
8 Mpeni Bwana utukufu unaostahili jina lake;
leteni sadaka na mje katika nyua zake.
9 Mwabuduni Bwana katika uzuri wa utakatifu wake;
dunia yote na itetemeke mbele zake.
-
8 Kila mmoja wa hawa viumbe wanne wenye uhai alikuwa na mabawa sita, na kujawa na macho pande zote hadi chini ya mabawa. Usiku na mchana hawaachi kusema:
“Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu,
ni Bwana Mungu Mwenyezi,
aliyekuwako, aliyeko na atakayekuja.”
9 Kila mara viumbe hao wanne wenye uhai wanapomtukuza, kumheshimu na kumshukuru yeye aketiye kwenye kile kiti cha enzi, tena aishiye milele na milele, 10 wale wazee ishirini na wanne huanguka mbele zake aketiye kwenye kiti cha enzi na kumwabudu yeye aliye hai milele na milele. Huziweka taji zao mbele ya kiti cha enzi, wakisema:
11 “Bwana wetu na Mungu wetu,
wewe unastahili kupokea utukufu
na heshima na uweza,
kwa maana ndiwe uliyeviumba vitu vyote,
na kwa mapenzi yako viliumbwa
na vimekuwako.”
-
14 Zaidi ya maadili haya yote jivikeni upendo, ambao ndio unaofunga kila kitu pamoja katika umoja mkamilifu.
15 Amani ya Kristo na itawale mioyoni mwenu, kwa kuwa ninyi kama viungo vya mwili mmoja mmeitiwa amani. Tena kuweni watu wa shukrani. 16 Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu, mkifundishana na kuonyana katika hekima yote, mkimwimbia Mungu zaburi, nyimbo na tenzi za rohoni, huku mkiwa na shukrani mioyoni mwenu. 17 Lolote mfanyalo, ikiwa ni kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba katika yeye.
-
28 Kwa hiyo, kwa kuwa tunapokea ufalme ambao hauwezi kutetemeshwa, basi na tuwe na shukrani, na hivyo tumwabudu Mungu kwa namna inayompendeza, kwa unyenyekevu na uchaji, 29 kwa kuwa “Mungu wetu ni moto ulao.”
-
15 Basi kwa njia ya Yesu, tuzidi kumtolea Mungu dhabihu ya sifa, yaani matunda ya midomo inayolikiri Jina lake. 16 Na msiache kutenda mema na kushirikiana vile vitu mlivyo navyo, kwa kuwa dhabihu kama hizo ndizo zinazompendeza Mungu.
-
5 Nao Walawi Yeshua, Kadmieli, Bani, Hashabnea, Sherebia, Hodia, Shebania na Pethahia wakasema: “Simameni mkamsifu Bwana Mungu wenu, yeye ambaye ni Mungu tangu milele hata milele.
“Libarikiwe jina lake tukufu, litukuzwe juu ya baraka zote na sifa. 6 Wewe peke yako ndiwe Bwana. Uliziumba mbingu, hata mbingu za mbingu na jeshi lote la mbinguni, dunia na vyote vilivyo ndani yake, na pia bahari na vyote vilivyomo ndani yake. Huvipa vitu vyote uhai, nalo jeshi la mbinguni linakuabudu wewe.
-
29 mpeni Bwana utukufu
unaostahili jina lake.
Leteni sadaka na mje katika nyua zake;
mwabuduni Bwana katika uzuri wa utakatifu wake.
-
17 Kwa hiyo msiwe wajinga, bali mpate kujua nini mapenzi ya Bwana. 18 Pia msilewe kwa mvinyo, ambamo ndani yake mna upotovu, bali mjazwe Roho. 19 Msemezane ninyi kwa ninyi kwa zaburi, nyimbo na tenzi za rohoni, mkimwimbia na kumsifu Bwana mioyoni mwenu, 20 siku zote mkimshukuru Mungu Baba kwa kila jambo katika Jina la Bwana wetu Yesu Kristo.
21 Nyenyekeaneni ninyi kwa ninyi kwa heshima kwa ajili ya Kristo.
-
9 Kwa hiyo, Mungu alimtukuza juu sana,
na kumpa Jina lililo kuu kuliko kila jina,
10 ili kwa Jina la Yesu, kila goti lipigwe,
la vitu vya mbinguni, na vya duniani,
na vya chini ya nchi,
11 na kila ulimi ukiri ya kwamba
Yesu Kristo ni Bwana,
kwa utukufu wa Mungu Baba.
-
3 Ahimidiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki sisi kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho ndani ya Kristo. 4 Kwa maana alituchagua katika yeye kabla ya kuumbwa ulimwengu ili tuwe watakatifu na bila lawama mbele zake. Kwa upendo 5 alitangulia kutuchagua tuwe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo kwa furaha yake na mapenzi yake mwenyewe. 6 Kwa hiyo tunamsifu Mungu kwa huruma zake kuu alizotumiminia sisi katika Mwanawe Mpendwa.
-
9 Baada ya hili nikatazama na hapo mbele yangu palikuwa na umati mkubwa wa watu ambao hakuna yeyote awezaye kuuhesabu, kutoka kila taifa, kila kabila, kila jamaa na kila lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi na mbele ya Mwana-Kondoo. Walikuwa wamevaa mavazi meupe na wakiwa wameshika matawi ya mitende mikononi mwao. 10 Nao walikuwa wakipiga kelele kwa sauti kubwa wakisema:
“Wokovu una Mungu wetu,
yeye aketiye kwenye kiti cha enzi,
na Mwana-Kondoo!”
11 Malaika wote walikuwa wamesimama kukizunguka kile kiti cha enzi na wale wazee ishirini na wanne na wale viumbe wanne wenye uhai. Wakaanguka kifudifudi mbele ya hicho kiti cha enzi na kumwabudu Mungu, 12 wakisema:
“Amen!
Sifa na utukufu
na hekima na shukrani na heshima
na uweza na nguvu
viwe kwa Mungu wetu milele na milele.
Amen!”
-
8 Mimi, Yohana, ndiye niliyesikia na kuyaona mambo haya. Nami nilipokwisha kuyasikia na kuyaona, nilianguka chini nikasujudu miguuni pa yule malaika aliyekuwa akinionyesha mambo hayo. 9 Lakini yeye akaniambia, “Usifanye hivyo! Mimi ni mtumishi pamoja nawe na ndugu zako manabii na wote wanaoyashika maneno ya kitabu hiki. Msujudie Mungu!”
-
9 Nao wakaimba wimbo mpya, wakisema:
“Wewe unastahili kukitwaa kitabu
na kuzivunja lakiri zake,
kwa sababu ulichinjwa
na kwa damu yako ukamnunulia Mungu watu
kutoka kila kabila, kila lugha,
kila jamaa na kila taifa.
10 Wewe umewafanya hawa wawe ufalme na makuhani
wa kumtumikia Mungu wetu,
nao watatawala duniani.”
11 Kisha nikatazama, nikasikia sauti za malaika wengi wakiwa wamekizunguka kile kiti cha enzi, pamoja na wale viumbe wenye uhai wanne na wale wazee ishirini na wanne. Idadi yao ilikuwa kumi elfu mara kumi elfu na maelfu ya maelfu. 12 Nao waliimba kwa sauti kuu, wakisema:
“Anastahili Mwana-Kondoo, yeye aliyechinjwa,
kupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu
na heshima na utukufu na sifa!”
13 Kisha nikasikia kila kiumbe mbinguni na duniani, chini ya nchi na baharini na vyote vilivyomo ndani yake vikiimba:
“Sifa na heshima na utukufu na uweza
ni vyake yeye aketiye juu ya hicho kiti cha enzi
na kwa Mwana-Kondoo,
milele na milele!”
14 Wale viumbe wenye uhai wanne wakasema, “Amen!” Nao wale wazee ishirini na wanne wakaanguka kifudifudi wakaabudu.
-
7 Bwana akamtokea Abramu, akamwambia, “Nitawapa uzao wako nchi hii.” Hivyo hapa akamjengea madhabahu Bwana aliyekuwa amemtokea.
8 Kutoka huko Abramu akasafiri kuelekea kwenye vilima mashariki ya Betheli, naye akapiga hema huko, Betheli ikiwa upande wa magharibi na Ai upande wa mashariki. Huko alimjengea Bwana madhabahu na akaliitia jina la Bwana.
-
1 Ndipo Mungu akasema maneno haya yote:
2 “Mimi ndimi Bwana Mungu wako, niliyekutoa Misri, kutoka nchi ya utumwa.
3 Usiwe na miungu mingine ila mimi.
4 Usijitengenezee sanamu katika umbo la kitu chochote kilicho juu mbinguni, au duniani chini, au ndani ya maji. 5 Usivisujudie wala kuviabudu; kwa kuwa Mimi, Bwana Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu, ninayewaadhibu watoto kwa ajili ya dhambi za baba zao hadi kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao, 6 lakini ninaonyesha upendo kwa maelfu ya vizazi vya wale wanipendao na kuzishika amri zangu.
-
1 Nadabu na Abihu, wana wa Aroni, wakachukua vyetezo vyao, wakaweka moto ndani yake na kuongeza uvumba; kisha wakamtolea Bwana moto usio halali, kinyume na agizo la Mungu. 2 Hivyo moto ukaja kutoka kwa uwepo wa Bwana na kuwaramba, nao wakafa mbele za Bwana. 3 Kisha Mose akamwambia Aroni, “Hili ndilo alilonena Bwana wakati aliposema:
“ ‘Miongoni mwa wale watakaonikaribia
nitajionyesha kuwa mtakatifu;
machoni pa watu wote
nitaheshimiwa.’ ”
Aroni akanyamaza.
-
1 Katika siku ya ishirini na nne ya mwezi ule ule, Waisraeli walikusanyika pamoja, wakifunga na kuvaa nguo za gunia na kujitia mavumbi vichwani mwao. 2 Wale wa uzao wa Israeli walijitenga na wageni wote. Wakasimama mahali pao, na kuungama dhambi zao na uovu wa baba zao. 3 Wakasimama pale walipokuwa, wakasoma kutoka kwenye kile Kitabu cha Sheria ya Bwana Mungu wao kwa muda wa robo siku, na wakatumia robo nyingine kwa kuungama dhambi na kumwabudu Bwana Mungu wao.
-
Zaburi ya Daudi. Wakati alipokuwa katika Jangwa la Yuda.
1 Ee Mungu, wewe ni Mungu wangu,
nakutafuta kwa moyo wote;
nafsi yangu inakuonea kiu,
mwili wangu unakuonea wewe shauku,
katika nchi kame na iliyochoka
mahali ambapo hapana maji.
2 Nimekuona katika mahali patakatifu
na kuuona uwezo wako na utukufu wako.
3 Kwa sababu upendo wako ni bora kuliko uhai,
midomo yangu itakuadhimisha.
4 Nitakusifu siku zote za maisha yangu,
na kwa jina lako nitainua mikono yangu.
-
13 Bwana anasema:
“Watu hawa hunikaribia kwa vinywa vyao
na kuniheshimu kwa midomo yao,
lakini mioyo yao iko mbali nami.
Ibada yao kwangu inatokana na maagizo
waliyofundishwa na wanadamu.
14 Kwa hiyo mara nyingine tena nitawashangaza watu hawa,
kwa ajabu juu ya ajabu.
Hekima ya wenye hekima itapotea,
nayo akili ya wenye akili itatoweka.”
-
42 Nao wakawa wanadumu katika mafundisho ya mitume, katika ushirika, katika kumega mkate na katika kusali. 43 Kila mtu akaingiwa na hofu ya Mungu, nayo miujiza mingi na ishara zikafanywa na mitume. 44 Walioamini wote walikuwa mahali pamoja, nao walikuwa na kila kitu shirika. 45 Waliuza mali zao na vitu walivyokuwa navyo, kila mtu akagawiwa kadiri ya mahitaji yake. 46 Siku zote kwa moyo mmoja walikutana ndani ya ukumbi wa Hekalu, wakimega mkate nyumba kwa nyumba, wakila chakula chao kwa furaha na moyo mweupe, 47 wakimsifu Mungu na kuwapendeza watu wote. Kila siku Bwana akaliongeza kanisa wale waliokuwa wakiokolewa.
-
7 Ninyi wanafiki! Isaya alikuwa sawa alipotabiri juu yenu kwamba:
8 “ ‘Watu hawa huniheshimu kwa midomo yao,
lakini mioyo yao iko mbali nami.
9 Huniabudu bure;
nayo mafundisho yao
ni maagizo ya wanadamu tu.’ ”
-
8 Yesu akamjibu, “Imeandikwa: ‘Mwabudu Bwana Mungu wako na umtumikie yeye peke yake.’ ”
-
29 Mose na Aroni wakawakusanya wazee wote wa Waisraeli, 30 naye Aroni akawaambia kila kitu Bwana alichokuwa amemwambia Mose. Pia akafanya ishara mbele ya watu, 31 nao wakaamini. Nao waliposikia kuwa Bwana anajishughulisha nao, na kwamba ameona mateso yao, walisujudu na kuabudu.
-
31 Mbingu na zishangilie, nchi na ifurahi;
semeni katikati ya mataifa, “Bwana anatawala!”
32 Bahari na ivume, na vyote vilivyomo ndani yake;
mashamba na yashangilie, na vyote vilivyomo ndani yake.
33 Kisha miti ya msituni itaimba,
itaimba kwa furaha mbele za Bwana,
kwa maana anakuja kuihukumu dunia.
34 Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema;
upendo wake wadumu milele.
35 Mlilieni, “Ee Mungu Mwokozi wetu, tuokoe.
Tukusanye tena na utukomboe kutoka kwa mataifa,
ili tuweze kulishukuru jina lako takatifu,
na kushangilia katika sifa zako.”
36 Atukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli,
tangu milele na hata milele.
Nao watu wote wakasema, “Amen,” na “Msifuni Bwana.”
-
3 Waisraeli wote walipoona moto ukishuka na utukufu wa Bwana ukiwa juu ya Hekalu, wakapiga magoti sakafuni wakasujudu nyuso zao mpaka chini, nao wakamwabudu na kumshukuru Bwana wakisema,
“Yeye ni mwema;
upendo wake unadumu milele.”
-
22 Nitalitangaza jina lako kwa ndugu zangu,
katika kusanyiko nitakusifu wewe.
23 Ninyi ambao mnamcha Bwana, msifuni!
Ninyi nyote wazao wote wa Yakobo, mheshimuni yeye!
Mcheni yeye, ninyi wazao wote wa Israeli!
-
Kwa mwimbishaji. Wimbo. Zaburi.
1 Mpigieni Mungu kelele za shangwe, dunia yote!
2 Imbeni utukufu wa jina lake;
mpeni sifa zake kwa utukufu!
3 Mwambieni Mungu, “Jinsi gani yalivyo ya kutisha matendo yako!
Uwezo wako ni mkuu mno kiasi kwamba
adui wananyenyekea mbele zako.
4 Dunia yote yakusujudia,
wanakuimbia wewe sifa,
wanaliimbia sifa jina lako.”
-
24 Kufuata maelekezo haya, yule mkuu wa gereza akawaweka katika chumba cha ndani sana mle gerezani, na akawafunga miguu yao kwa minyororo.
25 Ilipokaribia usiku wa manane, Paulo na Sila walikuwa wakiomba na kuimba nyimbo za kumsifu Mungu, nao wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza. 26 Ghafula pakatokea tetemeko kubwa la ardhi, hata msingi wa gereza ukatikisika. Mara milango ya gereza ikafunguka na ile minyororo iliyowafunga kila mmoja ikafunguka.
-
14 Usiabudu mungu mwingine, kwa kuwa Bwana, ambaye jina lake ni Wivu, ni Mungu mwenye wivu.
-
Wimbo wa Sifa. Wa Daudi.
1 Nitakutukuza wewe, Mungu wangu Mfalme,
nitalisifu jina lako milele na milele.
2 Kila siku nitakusifu
na kulitukuza jina lako milele na milele.
3 Bwana ni mkuu, anayestahili kusifiwa sana,
ukuu wake haupimiki.
4 Kizazi kimoja kitasifia kazi zako kwa kizazi kingine,
watasimulia matendo yako makuu.
-
3 Msifuni kwa mvumo wa tarumbeta,
msifuni kwa kinubi na zeze,
4 msifuni kwa matari na kucheza,
msifuni kwa kinanda cha nyuzi na filimbi,
5 msifuni kwa matoazi yaliayo,
msifuni kwa matoazi yavumayo sana.
6 Kila chenye pumzi na kimsifu Bwana.
Msifuni Bwana!
-
8 Kwa mara nyingine, ibilisi akamchukua Yesu mpaka kwenye kilele cha mlima mrefu na kumwonyesha falme zote za dunia na fahari zake, 9 kisha akamwambia, “Nitakupa hivi vyote kama ukinisujudia na kuniabudu.”
10 Yesu akamwambia, “Ondoka mbele yangu, Shetani! Kwa maana imeandikwa, ‘Mwabudu Bwana Mungu wako, na umtumikie yeye peke yake.’ ”
-
52 Kisha wakamwabudu na kurudi Yerusalemu wakiwa wamejawa na furaha kuu. 53 Nao wakadumu ndani ya Hekalu wakimtukuza Mungu. Amen.
-
1 Mwimbieni Bwana wimbo mpya;
mwimbieni Bwana dunia yote.
2 Mwimbieni Bwana, lisifuni jina lake;
tangazeni wokovu wake siku baada ya siku.
3 Tangazeni utukufu wake katikati ya mataifa,
matendo yake ya ajabu miongoni mwa mataifa yote.
4 Kwa kuwa Bwana ni mkuu mwenye kustahili kusifiwa kuliko wote;
yeye ni wa kuogopwa kuliko miungu yote.
5 Kwa maana miungu yote ya mataifa ni sanamu,
lakini Bwana aliziumba mbingu.
6 Fahari na enzi viko mbele yake;
nguvu na utukufu vimo patakatifu pake.
-
10 Basi Danieli alipofahamu kuwa amri ile imetangazwa, alikwenda nyumbani kwenye chumba chake cha ghorofani ambako madirisha yalifunguka kuelekea Yerusalemu. Akapiga magoti na kuomba mara tatu kwa siku, akimshukuru Mungu wake kama alivyokuwa akifanya mwanzoni.
-
3 Kwa maana sisi ndio tulio tohara, sisi tumwabuduo Mungu katika Roho, tunaona fahari katika Kristo Yesu, ambao hatuweki tumaini letu katika mwili,
-
3 Nao wakaimba wimbo wa Mose, mtumishi wa Mungu, na wimbo wa Mwana-Kondoo, wakisema:
“Bwana Mungu Mwenyezi,
matendo yako ni makuu na ya ajabu.
Njia zako wewe ni za haki na za kweli,
Mfalme wa nyakati zote!
4 Ni nani ambaye hatakuogopa wewe Bwana
na kulitukuza jina lako?
Kwa kuwa wewe peke yako ndiwe mtakatifu.
Mataifa yote yatakuja
na kuabudu mbele zako,
kwa kuwa matendo yako ya haki
yamedhihirishwa.”
-
20 Ndipo Ayubu akasimama, akararua joho lake na kunyoa nywele zake. Kisha akaanguka chini katika kuabudu 21 na kusema:
“Nilitoka tumboni mwa mama yangu uchi,
nami nitaondoka uchi,
Bwana alinipa, naye Bwana ameviondoa,
jina la Bwana litukuzwe.”
-
8 Ee Bwana, katikati ya miungu hakuna kama wewe,
hakuna matendo ya kulinganishwa na yako.
9 Ee Bwana, mataifa yote uliyoyafanya
yatakuja na kuabudu mbele zako;
wataliletea utukufu jina lako.
10 Kwa maana wewe ni mkuu, na unafanya mambo ya ajabu;
wewe peke yako ndiwe Mungu.
-
5 Mtukuzeni Bwana Mungu wetu,
na mkaabudu katika mahali pa kuwekea miguu yake;
yeye ni mtakatifu.
-
6 Yesu akawajibu, “Nabii Isaya alisema ukweli alipotabiri juu yenu, ninyi wanafiki. Kama ilivyoandikwa:
“ ‘Watu hawa huniheshimu kwa midomo yao,
lakini mioyo yao iko mbali nami.
7 Huniabudu bure,
nayo mafundisho yao ni maagizo ya wanadamu tu.’
-
9 Lakini ninyi ni taifa teule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu walio milki ya Mungu, mlioitwa ili kutangaza sifa zake yeye aliyewaita kutoka gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu.
-
4 Wale wazee ishirini na wanne pamoja na wale viumbe wanne wenye uhai wakaanguka kifudifudi, wakamwabudu Mungu, aliyekuwa ameketi kwenye kile kiti cha enzi. Wakasema kwa sauti kuu:
“Amen, Haleluya!”
5 Kisha sauti ikatoka katika kile kiti cha enzi, ikisema:
“Msifuni Mungu wetu,
ninyi watumishi wake wote,
ninyi nyote mnaomcha,
wadogo kwa wakubwa!”
6 Kisha nikasikia sauti kama ya umati mkubwa, kama sauti ya maji mengi yaendayo kasi na kama ngurumo kubwa ya radi wakipiga kelele wakisema:
“Haleluya!
Kwa maana Bwana Mungu wetu Mwenyezi anatawala.
7 Tufurahi, tushangilie
na kumpa utukufu!
Kwa maana arusi ya Mwana-Kondoo imewadia
na bibi arusi wake amejiweka tayari.
-
20 Kisha Miriamu yule nabii mke, ndugu yake Aroni, akachukua matari mkononi mwake na wanawake wote wakamfuata na matari yao wakicheza. 21 Miriamu akawaimbia:
“Mwimbieni Bwana,
kwa maana ametukuka sana.
Farasi na mpanda farasi
amewatosa baharini.”
-
27 Hezekia akatoa amri ya kutoa sadaka ya kuteketezwa madhabahuni. Walipoanza kutoa sadaka, wakaanza pia kumwimbia Bwana pamoja na tarumbeta na zile ala za uimbaji za Daudi mfalme wa Israeli. 28 Kusanyiko lote wakaabudu kwa kusujudu, wakati waimbaji wakiwa wanaimba na wenye tarumbeta wakipiga tarumbeta zao. Yote haya yaliendelea mpaka walipomaliza kutoa ile dhabihu ya sadaka ya kuteketezwa.
29 Kutoa sadaka kulipomalizika, mfalme na kila mtu aliyekuwepo pamoja naye wakapiga magoti na kuabudu. 30 Mfalme Hezekia na maafisa wake wakawaamuru Walawi kumsifu Bwana kwa maneno ya Daudi na ya Asafu mwonaji. Hivyo wakaimba sifa kwa furaha nao wakainamisha vichwa vyao na kuabudu.
-
Zaburi ya Daudi, alipojifanya mwendawazimu mbele ya Abimeleki, ambaye alimfukuza, naye akaondoka.
1 Nitamtukuza Bwana nyakati zote,
sifa zake zitakuwa midomoni mwangu siku zote.
2 Nafsi yangu itajisifu katika Bwana,
walioonewa watasikia na wafurahi.
3 Mtukuzeni Bwana pamoja nami,
naam, na tulitukuze jina lake pamoja.
-
3 Na walisifu jina lake kwa kucheza
na wampigie muziki kwa matari na kinubi.
-
20 Mkutanikapo pamoja si chakula cha Bwana mnachokula, 21 kwa kuwa mnapokula, kila mmoja wenu anakula bila kuwangoja wengine. Mmoja hukaa njaa na mwingine analewa. 22 Je, hamna nyumbani kwenu ambako mnaweza kula na kunywa? Au mnalidharau kanisa la Mungu na kuwadhalilisha wale wasio na kitu? Niwaambie nini? Je, niwasifu juu ya jambo hili? La, hasha!
23 Kwa maana mimi nilipokea kutoka kwa Bwana yale niliyowapa ninyi, kwamba Bwana Yesu, usiku ule aliposalitiwa, alitwaa mkate, 24 naye akiisha kushukuru, akaumega, akasema, “Huu ndio mwili wangu, uliotolewa kwa ajili yenu. Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.” 25 Vivyo hivyo baada ya kula, akakitwaa kikombe, akisema, “Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu. Fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu.” 26 Maana kila mlapo mkate huu na kunywea kikombe hiki, mnatangaza mauti ya Bwana mpaka ajapo.
27 Kwa hiyo, mtu yeyote alaye mkate huo au kukinywea kikombe hicho cha Bwana isivyostahili, atakuwa na hatia ya dhambi juu ya mwili na damu ya Bwana. 28 Inampasa mtu ajichunguze mwenyewe, kabla ya kula mkate na kukinywea kikombe.
-
6 Kisha nikamwona malaika mwingine akiruka juu angani, naye alikuwa na Injili ya milele ya kuwatangazia wale waishio duniani, yaani, kwa kila taifa, kabila, lugha na jamaa. 7 Akasema kwa sauti kubwa, “Mcheni Mungu na kumpa utukufu, kwa maana saa ya hukumu yake imewadia. Mwabuduni yeye aliyeziumba mbingu, dunia, bahari na chemchemi za maji.”
-
9 Ndipo malaika akaniambia, “Andika: ‘Wamebarikiwa wale walioalikwa kwenye karamu ya arusi ya Mwana-Kondoo!’ ” Naye akaongeza kusema, “Haya ndiyo maneno ya kweli ya Mungu.”
10 Ndipo nikaanguka kifudifudi miguuni pake ili kumwabudu, lakini yeye akaniambia, “Usifanye hivyo! Mimi pia ni mtumishi mwenzako pamoja na ndugu zako walio na ushuhuda wa Yesu. Mwabudu Mungu! Maana ushuhuda wa Yesu ndio roho ya unabii.”
-
9 Kila mara Mose alipoingia ndani ya hema, nguzo ya wingu ingeshuka chini na kukaa kwenye ingilio, wakati Mungu akizungumza na Mose. 10 Kila mara watu walipoona hiyo nguzo ya wingu ikiwa imesimama kwenye ingilio la hema, wote walisimama wakaabudu, kila mmoja kwenye ingilio la hema lake.
-
4 Sikia, ee Israeli: Bwana Mungu wako, Bwana ni mmoja. 5 Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote. 6 Amri hizi ninazokupa leo zitakuwa katika moyo wako. 7 Wafundishe watoto wako kwa bidii. Nena kuhusu amri hizi uketipo nyumbani na wakati utembeapo njiani, ulalapo na uamkapo. 8 Zifunge kama alama juu ya mkono wako, na uzifunge juu ya paji la uso wako. 9 Ziandike kwenye miimo ya milango ya nyumba yako na juu ya malango yako.
-
22 Lakini Samweli akajibu:
“Je, Bwana anafurahia sadaka za kuteketezwa na dhabihu
kama vile kuitii sauti ya Bwana?
Kutii ni bora zaidi kuliko dhabihu,
nako kusikia ni bora
kuliko mafuta ya kondoo dume.
-
Kwa mwimbishaji. Mtindo wa muth-labeni. Zaburi ya Daudi.
1 Ee Bwana, nitakutukuza kwa moyo wangu wote,
nitayasimulia matendo yako yote ya ajabu.
2 Nitafurahi na kushangilia ndani yako.
Nitaliimbia sifa jina lako, Ewe Uliye Juu Sana.
-
11 Uligeuza maombolezo yangu kuwa kucheza,
ulinivua nguo za gunia ukanivika shangwe,
12 ili moyo wangu uweze kukusifu na usikae kimya.
Ee Bwana Mungu wangu, nitakushukuru milele.
-
4 Ndipo nitakwenda madhabahuni pa Mungu,
kwa Mungu, furaha yangu na shangwe yangu.
Nitakusifu kwa kinubi,
Ee Mungu, Mungu wangu.
-
Zaburi ya Daudi.
1 Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.
Vyote vilivyomo ndani yangu
vilihimidi jina lake takatifu.
-
16 Furahini siku zote; 17 ombeni bila kukoma; 18 shukuruni kwa kila jambo, kwa maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu kwa ajili yenu katika Kristo Yesu.
-
12 Na sasa, ee Israeli, Bwana Mungu wako anataka nini kwako ila kumcha Bwana Mungu wako, kwenda katika njia zake, kumpenda na kumtumikia Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote, 13 na kuyashika maagizo ya Bwana na amri zake ninazokupa leo kwa mafanikio yako mwenyewe?
-
15 Gideoni alipoisikia hiyo ndoto na tafsiri yake, akamwabudu Mungu. Akarudi kwenye kambi ya Israeli na kusema, “Inukeni! Bwana amelitia jeshi la Wamidiani mikononi mwenu.”
-
11 Basi makuhani wakaondoka hapo Mahali Patakatifu. Makuhani wote waliokuwa huko walikuwa wamejiweka wakfu, bila kujali migawanyo yao. 12 Walawi wote waliokuwa waimbaji, yaani, Asafu, Hemani, Yeduthuni, wana wa ndugu zao, walisimama upande wa mashariki wa madhabahu, wakiwa wamevaa kitani safi huku wakipiga matoazi, vinubi na zeze. Walikuwa pamoja na makuhani 120 wakipiga tarumbeta. 13 Wapiga tarumbeta na waimbaji wakaungana katika sauti linganifu, ikawa kama vile ni sauti moja, wakimsifu na kumshukuru Bwana, nao alipoinua sauti zao pamoja na tarumbeta na matoazi na vyombo vingine vya uimbaji, wakamsifu Bwana wakisema:
“Yeye ni mwema;
upendo wake unadumu milele.”
Ndipo Hekalu la Bwana likajazwa na wingu, 14 nao makuhani hawakuweza kufanya huduma yao kwa sababu ya lile wingu, kwa kuwa utukufu wa Bwana ulijaza Hekalu la Mungu.
-
15 Sasa macho yangu yatafumbuka na masikio yangu yatasikiliza kwa makini maombi yaombwayo mahali hapa. 16 Kwa maana sasa nimechagua na kutakasa Hekalu hili ili kwamba Jina langu lipate kuwa huko milele. Macho yangu na moyo wangu utakuwepo huko daima.
-
5 Ezra akakifungua kile kitabu. Watu wote waliweza kumwona kwa sababu alikuwa amesimama juu zaidi, naye alipokifungua watu wote wakasimama. 6 Ezra akamsifu Bwana, Mungu mkuu, nao watu wote wakainua mikono yao na kuitikia, “Amen! Amen!” Kisha wakasujudu na kumwabudu Bwana hali nyuso zao zikigusa ardhi.
-
25 Kwako wewe hutoka kiini cha sifa zangu katika kusanyiko kubwa,
nitatimiza nadhiri zangu mbele ya wale wakuchao wewe.
26 Maskini watakula na kushiba,
wale wamtafutao Bwana watamsifu:
mioyo yenu na iishi milele!
27 Miisho yote ya dunia itakumbuka
na kumgeukia Bwana,
nazo jamaa zote za mataifa
watasujudu mbele zake,
28 kwa maana ufalme ni wa Bwana
naye hutawala juu ya mataifa.
-
3 Nani awezaye kuupanda mlima wa Bwana?
Ni nani awezaye kusimama patakatifu pake?
4 Ni yule mwenye mikono safi na moyo mweupe,
yule ambaye hakuinulia sanamu nafsi yake
au kuapa kwa kitu cha uongo.
5 Huyo atapokea baraka kutoka kwa Bwana,
na hukumu ya haki kutoka kwa Mungu Mwokozi wake.
6 Hiki ndicho kizazi cha wale wamtafutao,
wale wautafutao uso wako, Ee Mungu wa Yakobo.
-
1 Mshukuruni Bwana, liitieni jina lake,
wajulisheni mataifa yale aliyoyatenda.
2 Mwimbieni yeye, mwimbieni yeye sifa,
waambieni matendo yake yote ya ajabu.
3 Lishangilieni jina lake takatifu,
mioyo ya wale wamtafutao Bwana na ifurahi.
4 Mtafuteni Bwana na nguvu zake,
utafuteni uso wake siku zote.
5 Kumbuka matendo ya ajabu aliyoyafanya,
miujiza yake na hukumu alizozitamka,
6 enyi wazao wa Abrahamu mtumishi wake,
enyi wana wa Yakobo, wateule wake.
-
1 Ee Bwana, wewe ni Mungu wangu,
nitakutukuza na kulisifu jina lako,
kwa maana katika ukamilifu wa uaminifu
umetenda mambo ya ajabu,
mambo yaliyokusudiwa tangu zamani.
-
6 Wageni wanaoambatana na Bwana
ili kumtumikia,
kulipenda jina la Bwana,
na kumwabudu yeye,
wote washikao Sabato bila kuinajisi
na ambao hushika sana agano langu:
7 hawa nitawaleta kwenye mlima wangu mtakatifu
na kuwapa furaha ndani ya nyumba yangu ya sala.
Sadaka zao za kuteketeza na dhabihu zao
zitakubalika juu ya madhabahu yangu;
kwa maana nyumba yangu itaitwa
nyumba ya sala kwa mataifa yote.”
-
28 Ndipo Nebukadneza akasema, “Ahimidiwe Mungu wa Shadraki, Meshaki na Abednego, ambaye amemtuma malaika wake na kuwaokoa watumishi wake. Walimtumaini na kukaidi amri ya mfalme, nao wakawa tayari kufa kuliko kutumikia au kuabudu mungu mwingine yeyote isipokuwa Mungu wao.
-
5 ninyi nanyi, kama mawe yaliyo hai, mnajengwa kuwa nyumba ya kiroho, ili mpate kuwa ukuhani mtakatifu, mkitoa dhabihu za kiroho zinazokubaliwa na Mungu kwa njia ya Yesu Kristo.
-
10 Wajenzi walipoweka msingi wa Hekalu la Bwana, makuhani wakiwa wamevalia mavazi yao wakiwa na tarumbeta na Walawi (wana wa Asafu) wakiwa na matoazi, walishika nafasi zao za kumtukuza Bwana, kama ilivyoagizwa na Daudi mfalme wa Israeli. 11 Waliimba nyimbo za sifa na za shukrani kwa Bwana hivi:
“Yeye ni mwema;
upendo wake kwa Israeli
wadumu milele.”
Watu wote wakapaza sauti kubwa za sifa kwa Bwana, kwa sababu msingi wa nyumba ya Bwana ulikuwa umewekwa. 12 Lakini wengi wa makuhani wazee, Walawi na viongozi wa jamaa waliokuwa wameona Hekalu la mwanzoni, walilia kwa sauti walipoona msingi wa Hekalu hili ukiwekwa, huku wengine wengi wakipiga kelele kwa furaha. 13 Hakuna mtu ambaye angeweza kutofautisha sauti hizo za furaha na za kilio, kwa sababu watu walipiga kelele sana. Nayo hiyo sauti ikasikika mbali.
-
2 Nitasujudu nikielekea Hekalu lako takatifu,
nami nitalisifu jina lako
kwa ajili ya upendo wako
na uaminifu,
kwa kuwa umelikuza jina lako na neno lako
juu ya vitu vyote.
-
21 “Ninachukia, ninazidharau sikukuu zenu za dini;
siwezi kuvumilia makusanyiko yenu.
22 Hata ingawa mnaniletea sadaka zenu za kuteketezwa na sadaka za nafaka,
sitazikubali.
Ingawa mnaniletea sadaka nzuri za amani,
sitazitambua.
23 Niondoleeni kelele za nyimbo zenu!
Sitasikiliza sauti za vinubi vyenu.
24 Lakini acheni haki itiririke kama mto,
na uadilifu uwe kama kijito kisichokauka!
-
6 Nimjie Bwana na kitu gani na kusujudu
mbele za Mungu aliyetukuka?
Je, nije mbele zake na sadaka za kuteketezwa,
nije na ndama za mwaka mmoja?
7 Je, Bwana atafurahishwa na kondoo dume elfu,
au mito elfu kumi ya mafuta?
Je, nimtoe mzaliwa wangu wa kwanza kwa ajili ya kosa langu,
mtoto wangu mwenyewe
kwa ajili ya dhambi ya nafsi yangu?
8 Amekuonyesha yaliyo mema, ee mwanadamu.
Bwana anataka nini kwako?
Ila kutenda kwa haki na kupenda rehema,
na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako.
-
16 Nilisikia na moyo wangu ukagonga kwa nguvu,
midomo yangu ikatetemeka kwa hofu niliposikia sauti;
uchakavu ukanyemelea mifupa yangu,
na miguu yangu ikatetemeka.
Hata hivyo nitasubiri kwa uvumilivu siku ya maafa
kuyajilia mataifa yaliyotuvamia.
17 Ingawa mtini hauchanui maua
na hakuna zabibu juu ya mizabibu,
ingawaje mzeituni hauzai,
na hata mashamba hayatoi chakula,
iwapo hakuna kondoo katika banda,
wala ngʼombe katika zizi,
18 hata hivyo nitashangilia katika Bwana,
nitamfurahia Mungu Mwokozi wangu.
-
18 Ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni dhidi ya uasi wote na uovu wa wanadamu ambao huipinga kweli kwa uovu wao, 19 kwa maana yote yanayoweza kujulikana kumhusu Mungu ni dhahiri kwao, kwa sababu Mungu mwenyewe ameyadhihirisha kwao. 20 Kwa maana tangu kuumbwa kwa ulimwengu, asili ya Mungu asiyeonekana kwa macho, yaani, uweza wake wa milele na asili yake ya Uungu, imeonekana waziwazi, ikitambuliwa kutokana na yale aliyoyafanya ili wanadamu wasiwe na udhuru.
21 Kwa maana ingawa walimjua Mungu, hawakumtukuza yeye kama ndiye Mungu wala hawakumshukuru, bali fikira zao zimekuwa batili na mioyo yao ya ujinga ikatiwa giza. 22 Ingawa walijidai kuwa wenye hekima, wakawa wajinga 23 na kubadili utukufu wa Mungu aishiye milele kwa sanamu zilizofanywa zifanane na mwanadamu ambaye hufa, na mfano wa ndege, wanyama na viumbe vitambaavyo.
24 Kwa hiyo, Mungu akawaacha wazifuate tamaa mbaya za mioyo yao katika uasherati, hata wakavunjiana heshima miili yao wao kwa wao. 25 Kwa sababu waliibadili kweli ya Mungu kuwa uongo, wakaabudu na kutumikia kiumbe badala ya Muumba, ahimidiwaye milele! Amen.
-
26 Basi tuseme nini ndugu zangu? Mnapokutana pamoja, kila mmoja ana wimbo, au neno la mafundisho, au ufunuo, lugha mpya au atatafsiri. Mambo yote yatendeke kwa ajili ya kulijenga kanisa. 27 Kama mtu yeyote akinena kwa lugha, basi waseme watu wawili au watatu si zaidi, mmoja baada ya mwingine na lazima awepo mtu wa kutafsiri. 28 Lakini kama hakuna mtu wa kutafsiri, hao watu na wanyamaze kimya kanisani na wanene na nafsi zao wenyewe na Mungu.
29 Manabii wawili au watatu wanene na wengine wapime yale yasemwayo. 30 Kama mtu yeyote aliyeketi karibu, akipata ufunuo, basi yule wa kwanza na anyamaze. 31 Kwa maana wote mnaweza kutoa unabii, mmoja baada ya mwingine, ili kila mtu apate kufundishwa na kutiwa moyo. 32 Roho za manabii huwatii manabii. 33 Kwa maana Mungu si Mungu wa machafuko bali ni Mungu wa amani.
Kama ilivyo katika makusanyiko yote ya watakatifu, 34 wanawake wanapaswa kuwa kimya kanisani. Hawaruhusiwi kusema, bali wanyenyekee kama sheria isemavyo. 35 Kama wakitaka kuuliza kuhusu jambo lolote, wawaulize waume zao nyumbani. Kwa maana ni aibu kwa mwanamke kuzungumza kanisani.
36 Je, neno la Mungu lilianzia kwenu? Au ni ninyi tu ambao neno la Mungu limewafikia? 37 Kama mtu yeyote akidhani kwamba yeye ni nabii, au ana karama za rohoni, basi na akubali kwamba haya ninayoandika ni maagizo kutoka kwa Bwana. 38 Kama mtu akipuuza jambo hili yeye mwenyewe atapuuzwa.
39 Kwa hiyo ndugu zangu, takeni sana kutoa unabii na msikataze watu kusema kwa lugha. 40 Lakini kila kitu kitendeke kwa heshima na kwa utaratibu.
-
25 Kwa kuwa Bwana ni mkuu,
mwenye kustahili kusifiwa kuliko wote;
yeye ni wa kuogopwa kuliko miungu yote.
-
3 Hata hivyo umesimikwa katika kiti cha enzi kama Uliye Mtakatifu;
wewe ni sifa ya Israeli.
-
Wimbo. Zaburi ya wana wa Kora.
1 Bwana ni mkuu, anayestahili kusifiwa sana,
katika mji wa Mungu wetu,
mlima wake mtakatifu.
-
9 Nitakusifu wewe, Ee Bwana, katikati ya mataifa;
nitaimba habari zako, katikati ya jamaa za watu.
-
4 Mwimbieni Mungu, liimbieni sifa jina lake,
mtukuzeni yeye aendeshwaye juu ya mawingu:
jina lake ni Bwana,
furahini mbele zake.
5 Baba wa yatima, mtetezi wa wajane,
ni Mungu katika makao yake matakatifu.
-
8 Kinywa changu kimejazwa sifa zako,
nikitangaza utukufu wako mchana kutwa.
-
1 Msifuni Bwana.
Msifuni Bwana kutoka mbinguni,
msifuni juu vileleni.
2 Msifuni, enyi malaika wake wote,
msifuni yeye, enyi jeshi lake lote la mbinguni.
3 Msifuni yeye, enyi jua na mwezi,
msifuni yeye, enyi nyota zote zingʼaazo.
4 Msifuni yeye, enyi mbingu zilizo juu sana,
na ninyi maji juu ya anga.
5 Vilisifu jina la Bwana
kwa maana aliamuru navyo vikaumbwa.
-
37 Yesu akamjibu, “ ‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote na kwa akili zako zote.’ 38 Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. 39 Nayo ya pili ni kama hiyo, nayo ni hii: ‘Mpende jirani yako kama nafsi yako.’
Shows Read in context, Share and Copy.