84 Bible Verses About Following God
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
-
18 Yesu alipokuwa anatembea kando ya Bahari ya Galilaya, aliwaona ndugu wawili, Simoni aitwaye Petro, na Andrea ndugu yake. Walikuwa wakizitupa nyavu zao baharini kwa kuwa wao walikuwa wavuvi. 19 Yesu akawaambia, “Njooni, nifuateni nami nitawafanya mwe wavuvi wa watu.” 20 Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata.
21 Alipoendelea mbele kutoka pale, akawaona ndugu wengine wawili, Yakobo mwana wa Zebedayo na Yohana nduguye, wakiwa wamekaa kwenye mashua pamoja na baba yao Zebedayo, wakizitengeneza nyavu zao. Yesu akawaita. 22 Nao mara wakaiacha mashua yao, pamoja na baba yao, wakamfuata.
-
16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.
-
21 “Si kila mtu aniambiaye, ‘Bwana, Bwana,’ atakayeingia katika Ufalme wa Mbinguni, bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. 22 Wengi wataniambia siku ile, ‘Bwana, Bwana, hatukutoa unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo wachafu na kufanya miujiza mingi?’ 23 Ndipo nitakapowaambia wazi, ‘Sikuwajua kamwe. Ondokeni kwangu, ninyi watenda maovu!’
24 “Kwa hiyo kila mtu ayasikiaye haya maneno yangu na kuyatenda, ni kama mtu mwenye busara aliyejenga nyumba yake kwenye mwamba. 25 Mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, na upepo ukavuma ukaipiga hiyo nyumba. Lakini haikuanguka; kwa sababu msingi wake ulikuwa kwenye mwamba. 26 Naye kila anayesikia haya maneno yangu wala asiyatende, ni kama mtu mjinga aliyejenga nyumba yake kwenye mchanga. 27 Mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, nao upepo ukavuma ukaipiga hiyo nyumba, nayo ikaanguka kwa kishindo kikubwa.”
-
18 Yesu alipoona makutano mengi wamemzunguka, aliwaamuru wanafunzi wake wavuke mpaka ngʼambo ya ziwa. 19 Kisha mwalimu mmoja wa sheria akamjia Yesu na kumwambia, “Mwalimu, nitakufuata kokote uendako.”
20 Naye Yesu akamjibu, “Mbweha wana mapango, nao ndege wa angani wana viota, lakini Mwana wa Adamu hana mahali pa kulaza kichwa chake.”
21 Mwanafunzi mwingine akamwambia, “Bwana, niruhusu kwanza nikamzike baba yangu.”
22 Lakini Yesu akamwambia, “Nifuate, uwaache wafu wawazike wafu wao.”
23 Naye alipoingia kwenye mashua, wanafunzi wake wakamfuata.
-
57 Walipokuwa njiani wakienda, mtu mmoja akamwambia Yesu, “Nitakufuata kokote uendako.”
58 Yesu akamjibu, “Mbweha wana mapango, nao ndege wa angani wana viota, lakini Mwana wa Adamu hana mahali pa kulaza kichwa chake.”
59 Yesu akamwambia mtu mwingine, “Nifuate.”
Mtu huyo akamjibu, “Bwana, niruhusu kwanza nikamzike baba yangu.”
60 Yesu akamwambia, “Waache wafu wawazike wafu wao, bali wewe nenda ukautangaze Ufalme wa Mungu.”
61 Mtu mwingine akamwambia, “Bwana, nitakufuata lakini naomba kwanza nikawaage jamaa yangu.”
62 Yesu akamwambia, “Mtu yeyote atiaye mkono wake kulima, kisha akatazama nyuma, hafai kwa Ufalme wa Mungu.”
-
26 Mtu yeyote akinitumikia lazima anifuate, nami mahali nilipo ndipo mtumishi wangu atakapokuwa. Mtu akinitumikia, Baba yangu atamheshimu.
-
13 Kwa hiyo, tayarisheni nia zenu kwa kazi; mwe na kiasi, mkitumainia kikamilifu ile neema mtakayopewa Yesu Kristo atakapodhihirishwa. 14 Kama watoto watiifu, msifuate tamaa zenu mbaya wakati mlipoishi kwa ujinga. 15 Bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, nanyi kuweni watakatifu katika mwenendo wenu wote. 16 Kwa maana imeandikwa: “Kuweni watakatifu, kwa kuwa mimi ni mtakatifu.”
-
1 Bwana akawa amemwambia Abramu, “Ondoka kutoka nchi yako, uache jamii yako na nyumba ya baba yako, uende hadi nchi nitakayokuonyesha.
2 “Mimi nitakufanya taifa kubwa
na nitakubariki,
Nitalikuza jina lako,
nawe utakuwa baraka.
3 Nitawabariki wale wanaokubariki,
na yeyote akulaaniye nitamlaani;
na kupitia kwako mataifa yote duniani
yatabarikiwa.”
4 Hivyo Abramu akaondoka kama Bwana alivyokuwa amemwambia; naye Loti akaondoka pamoja naye. Wakati Abramu alipoitwa aondoke Harani, alikuwa na miaka sabini na mitano.
-
10 Hili ndilo asemalo Bwana: “Miaka sabini itakapotimia kwa ajili ya Babeli, nitakuja kwenu na kutimiza ahadi yangu ya rehema ya kuwarudisha mahali hapa. 11 Kwa maana ninajua mipango niliyo nayo kwa ajili yenu,” asema Bwana, “ni mipango ya kuwafanikisha na wala si ya kuwadhuru, ni mipango ya kuwapa tumaini katika siku zijazo. 12 Kisha mtaniita, na mtakuja na kuniomba, nami nitawasikiliza. 13 Mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote. 14 Nitaonekana kwenu,” asema Bwana, “nami nitawarudisha watu wenu waliotekwa. Nitawakusanya kutoka mataifa yote na mahali pote nilipokuwa nimewafukuzia, nami nitawarudisha mahali ambapo nilikuwa nimewatoa walipochukuliwa uhamishoni,” asema Bwana.
-
34 Ndipo akauita ule umati wa watu pamoja na wanafunzi wake, akasema, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, ni lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake, anifuate. 35 Kwa maana yeyote anayetaka kuyaokoa maisha yake atayapoteza, lakini yeyote atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili atayaokoa. 36 Je, itamfaidi nini mtu kuupata ulimwengu wote, lakini akayapoteza maisha yake? 37 Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake? 38 Mtu yeyote akinionea aibu mimi na maneno yangu katika kizazi hiki cha uzinzi na dhambi, Mwana wa Adamu naye atamwonea aibu wakati atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu.”
-
52 Ndipo Wayahudi wakaanza kuhojiana vikali wao kwa wao wakisema, “Mtu huyu awezaje kutupatia mwili wake tuule?”
53 Hivyo Yesu akawaambia, “Amin, amin nawaambia, msipoula mwili wa Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu. 54 Mtu yeyote aulaye mwili wangu na kunywa damu yangu, anao uzima wa milele. Nami nitamfufua siku ya mwisho. 55 Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli na damu yangu ni kinywaji cha kweli. 56 Yeyote alaye mwili wangu na kunywa damu yangu, atakaa ndani yangu nami nitakaa ndani yake. 57 Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, na kama nami ninavyoishi kwa sababu ya Baba, hivyo anilaye mimi ataishi kwa sababu yangu. 58 Huu ndio mkate ushukao kutoka mbinguni, si kama ule mkate baba zenu waliokula nao wakafa. Lakini yeye aulaye mkate huu ataishi milele.” 59 Yesu alisema maneno haya alipokuwa akifundisha katika sinagogi huko Kapernaumu.
60 Wengi wa wafuasi wake waliposikia jambo hili wakasema, “Mafundisho haya ni magumu. Ni nani awezaye kuyapokea?”
61 Yesu alipojua kwamba wafuasi wake wananungʼunika kuhusu mafundisho yake, akawaambia, “Je, jambo hili limewaudhi? 62 Ingekuwaje basi kama mngemwona Mwana wa Adamu akipaa kwenda zake huko alipokuwa kwanza? 63 Roho ndiye atiaye uzima, mwili haufai kitu. Maneno haya niliyowaambia ni Roho tena ni uzima. 64 Lakini baadhi yenu hamwamini.” Kwa maana Yesu alifahamu tangu mwanzo wale ambao hawangemwamini miongoni mwao na yule ambaye angemsaliti. 65 Akaendelea kusema, “Hii ndiyo sababu niliwaambia kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu.”
66 Tangu wakati huo wafuasi wake wengi wakarejea nyuma wakaacha kumfuata.
67 Hivyo Yesu akawauliza wale wanafunzi wake kumi na wawili, “Je, ninyi pia mnataka kuondoka?”
68 Simoni Petro akamjibu, “Bwana, tuondoke twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. 69 Tunaamini na kujua kuwa wewe ndiwe Aliye Mtakatifu wa Mungu.”
-
20 Kwani ni faida gani kwa mtu kustahimili anapopigwa kwa sababu ya makosa yake? Lakini kama mkiteswa kwa sababu ya kutenda mema, nanyi mkastahimili, hili ni jambo la kusifiwa mbele za Mungu.
21 Ninyi mliitwa kwa ajili ya haya, kwa sababu Kristo naye aliteswa kwa ajili yenu, akiwaachia kielelezo, ili mzifuate nyayo zake.
22 “Yeye hakutenda dhambi,
wala hila haikuonekana kinywani mwake.”
23 Yeye alipotukanwa, hakurudisha matukano; alipoteswa, hakutishia, bali alijikabidhi kwa yeye ahukumuye kwa haki. 24 Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, ili tufe kwa mambo ya dhambi, bali tupate kuishi katika haki. Kwa kupigwa kwake, ninyi mmeponywa. 25 Kwa maana mlikuwa mmepotea kama kondoo, lakini sasa mmerudi kwa Mchungaji na Mwangalizi wa roho zenu.
-
24 Ndipo Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, ni lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake, anifuate. 25 Kwa maana yeyote anayetaka kuyaokoa maisha yake atayapoteza, lakini yeyote atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu atayapata. 26 Kwa maana, je, itamfaidi nini mtu kuupata ulimwengu wote, lakini akayapoteza maisha yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake? 27 Kwa maana Mwana wa Adamu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika zake, naye ndipo atakapomlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake.
-
16 Je, hamjui kwamba mnapojitoa kwa mtu yeyote kama watumwa watiifu, ninyi ni watumwa wa yule mnayemtii, aidha watumwa wa dhambi, ambayo matokeo yake ni mauti, au watumwa wa utii ambao matokeo yake ni haki? 17 Lakini Mungu ashukuriwe kwa kuwa ninyi ambao kwanza mlikuwa watumwa wa dhambi, mmekuwa watii kutoka moyoni kwa mafundisho mliyopewa. 18 Nanyi, mkiisha kuwekwa huru mbali na dhambi, mmekuwa watumwa wa haki.
-
12 Kisha Yesu akasema nao tena akawaambia, “Mimi ni nuru ya ulimwengu. Mtu yeyote akinifuata hatatembea gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.”
-
7 Kwa hiyo Yesu akasema nao tena akawaambia, “Amin, amin nawaambia, mimi ndimi lango la kondoo. 8 Wote walionitangulia ni wevi na wanyangʼanyi, lakini kondoo hawakuwasikia. 9 Mimi ndimi lango, yeyote anayeingia zizini kwa kupitia kwangu ataokoka, ataingia na kutoka, naye atapata malisho. 10 Mwizi huja ili aibe, kuua na kuangamiza. Mimi nimekuja ili wapate uzima kisha wawe nao tele.
11 “Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo. 12 Mtu wa kuajiriwa sio mchungaji mwenye kondoo. Amwonapo mbwa mwitu akija, yeye hukimbia na kuwaacha kondoo. Naye mbwa mwitu hulishambulia kundi na kulitawanya. 13 Yeye hukimbia kwa sababu ameajiriwa wala hawajali kondoo.
14 “Mimi ndimi mchungaji mwema. Ninawajua kondoo wangu nao kondoo wangu wananijua. 15 Kama vile Baba anavyonijua mimi, nami ninavyomjua Baba, nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo. 16 Ninao kondoo wengine ambao si wa zizi hili, inanipasa kuwaleta, nao wataisikia sauti yangu, hivyo patakuwa na kundi moja na mchungaji mmoja. 17 Baba yangu ananipenda kwa kuwa ninautoa uhai wangu ili niupate tena. 18 Hakuna mtu aniondoleaye uhai wangu, bali ninautoa kwa hiari yangu mwenyewe. Ninao uwezo wa kuutoa uhai wangu na pia ninao uwezo wa kuutwaa tena. Amri hii nimepewa na Baba yangu.”
-
5 “Mimi ni mzabibu, ninyi ni matawi. Akaaye ndani yangu, nami ndani yake, huyo huzaa sana, maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya jambo lolote. 6 Mtu yeyote asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka. Matawi kama hayo hukusanywa na kutupwa motoni, yakateketea. 7 Ninyi mkikaa ndani yangu na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni lolote mtakalo, nanyi mtatendewa. 8 Kwa hiyo Baba yangu hutukuzwa, kwa vile mzaavyo matunda mengi, nanyi mtakuwa wanafunzi wangu.
9 “Kama vile Baba alivyonipenda mimi, hivyo ndivyo mimi nilivyowapenda ninyi. Basi kaeni katika pendo langu. 10 Mkizishika amri zangu mtakaa katika pendo langu, kama mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake. 11 Nimewaambia mambo haya ili furaha yangu iwe ndani yenu na furaha yenu iwe kamili.
-
1 Igeni mfano wangu, kama ninavyouiga mfano wa Kristo.
2 Ninawasifu kwa kuwa mnanikumbuka katika kila jambo na kwa kushika mafundisho niliyowapa.
-
1 Kama kukiwa na jambo lolote la kutia moyo katika kuunganishwa na Kristo, kukiwa faraja yoyote katika upendo wake, kukiwa na ushirika wowote na Roho, kukiwa na wema wowote na huruma, 2 basi ikamilisheni furaha yangu kwa kuwa na nia moja, mkiwa na upendo huo moja, mkiwa wa roho na kusudi moja. 3 Msitende jambo lolote kwa nia ya kujitukuza wala kujivuna, bali kwa unyenyekevu kila mtu amhesabu mwingine bora kuliko nafsi yake. 4 Kila mmoja wenu asiangalie faida yake mwenyewe tu, bali pia ajishughulishe kwa faida ya wengine.
5 Kuweni na nia ile ile aliyokuwa nayo Kristo Yesu:
6 Yeye, ingawa alikuwa na asili ya Mungu hasa,
hakuona kule kuwa sawa na Mungu
kuwa kitu cha kushikilia,
7 bali alijifanya si kitu,
akachukua hali hasa na mtumwa,
naye akazaliwa katika umbo la mwanadamu.
8 Naye akiwa na umbo la mwanadamu,
alijinyenyekeza, akatii hata mauti:
naam, mauti ya msalaba!
9 Kwa hiyo, Mungu alimtukuza juu sana,
na kumpa Jina lililo kuu kuliko kila jina,
10 ili kwa Jina la Yesu, kila goti lipigwe,
la vitu vya mbinguni, na vya duniani,
na vya chini ya nchi,
11 na kila ulimi ukiri ya kwamba
Yesu Kristo ni Bwana,
kwa utukufu wa Mungu Baba.
12 Kwa hiyo, wapenzi wangu, kama vile ambavyo mmekuwa mkitii siku zote, si tu wakati nikiwa pamoja nanyi, bali sasa zaidi sana nisipokuwepo, utimizeni wokovu wenu kwa kuogopa na kutetemeka, 13 kwa maana Mungu ndiye atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu kwa kulitimiza kusudi lake jema.
14 Fanyeni mambo yote bila kunungʼunika wala kushindana, 15 ili msiwe na lawama wala hatia, bali mwe wana wa Mungu wasio na kasoro katika kizazi chenye ukaidi na kilichopotoka, ambacho ndani yake ninyi mnangʼaa kama mianga ulimwenguni. 16 Mkilishika neno la uzima, ili nipate kuona fahari siku ya Kristo kwamba sikupiga mbio wala kujitaabisha bure. 17 Lakini hata kama nikimiminwa kama sadaka ya kinywaji kwenye dhabihu na huduma itokayo katika imani yenu, mimi ninafurahi na kushangilia pamoja nanyi nyote. 18 Vivyo hivyo, ninyi nanyi imewapasa kufurahi na kushangilia pamoja nami.
-
9 Yesu alipokuwa akienda kutoka huko, alimwona mtu mmoja jina lake Mathayo akiwa ameketi forodhani mahali pa kutoza ushuru. Yesu akamwambia, “Nifuate.” Mathayo akaondoka, akamfuata.
10 Yesu alipokuwa akila chakula ndani ya nyumba ya Mathayo, watoza ushuru wengi na “wenye dhambi” wakaja kula pamoja naye na wanafunzi wake. 11 Mafarisayo walipoona mambo haya, wakawauliza wanafunzi wake, “Kwa nini Mwalimu wenu anakula pamoja na watoza ushuru na ‘wenye dhambi’?”
12 Lakini Yesu aliposikia hayo, akawaambia, “Watu wenye afya hawahitaji tabibu, lakini wale walio wagonjwa ndio wanaohitaji tabibu. 13 Nendeni mkajifunze maana ya maneno haya: ‘Nataka rehema, wala si dhabihu.’ Kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.”
-
18 Yesu akawajia na kusema, “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. 19 Kwa sababu hii, enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, 20 nanyi wafundisheni kuyashika mambo yote niliyowaamuru ninyi. Hakika mimi niko pamoja nanyi siku zote, hadi mwisho wa nyakati.”
-
16 Yesu alipokuwa akitembea kando ya Bahari ya Galilaya, aliwaona Simoni na Andrea nduguye wakizitupa nyavu zao baharini, kwa kuwa wao walikuwa wavuvi. 17 Yesu akawaambia, “Njooni, nifuateni nami nitawafanya mwe wavuvi wa watu.” 18 Mara wakaacha nyavu zao, wakamfuata.
19 Alipokwenda mbele kidogo, akamwona Yakobo mwana wa Zebedayo na Yohana nduguye, wakiwa kwenye mashua yao wakizitengeneza nyavu zao. 20 Papo hapo akawaita, nao wakamwacha Zebedayo baba yao kwenye mashua pamoja na watumishi wa kuajiriwa, nao wakamfuata Yesu.
-
23 Kisha akawaambia wote, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, ni lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake kila siku, anifuate. 24 Kwa maana yeyote anayetaka kuyaokoa maisha yake atayapoteza, lakini yeyote atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu atayaokoa. 25 Je, itamfaidi nini mtu kuupata ulimwengu wote, lakini akapoteza au kuangamiza nafsi yake?
-
3 Kisha Mose akakwea kwenda kwa Mungu, naye Bwana akamwita kutoka kwenye ule mlima akasema, “Hivi ndivyo utakavyosema na nyumba ya Yakobo na utakachowaambia watu wa Israeli: 4 ‘Ninyi wenyewe mmeona nililofanya huko Misri, jinsi nilivyowabeba kwenye mbawa za tai na kuwaleta kwangu. 5 Sasa kama mkinitii kikamilifu na kutunza Agano langu, basi ninyi mtakuwa mali yangu ya thamani kubwa miongoni mwa mataifa yote. Ijapokuwa dunia yote ni mali yangu, 6 ninyi mtakuwa kwangu ufalme wa makuhani na taifa takatifu.’ Haya ndiyo maneno utakayosema kwa wana wa Israeli.”
-
5 Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote
wala usizitegemee akili zako mwenyewe;
6 katika njia zako zote mkiri yeye,
naye atayanyoosha mapito yako.
-
37 “Yeyote ampendaye baba yake au mama yake kuliko anavyonipenda mimi, hastahili kuwa wangu. Yeyote ampendaye mwanawe au binti yake kuliko anavyonipenda mimi, hastahili kuwa wangu. 38 Tena yeyote asiyeuchukua msalaba wake na kunifuata, hastahili kuwa wangu. 39 Kwa maana yeyote anayetaka kuyaokoa maisha yake atayapoteza, lakini yeyote atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu atayapata.
-
8 Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani, wala si kwa matendo yenu mema. Hii ni zawadi kutoka kwa Mungu, 9 si kwa matendo, ili mtu yeyote asije akajisifu. 10 Kwa maana sisi ni kazi ya mikono ya Mungu, tulioumbwa katika Kristo Yesu, ili tupate kutenda matendo mema, ambayo Mungu alitangulia kuyaandaa tupate kuishi katika hayo.
11 Kwa hiyo kumbukeni kwamba ninyi ambao hapo awali mlikuwa watu wa Mataifa kwa kuzaliwa na kuitwa “wasiotahiriwa” na wale wanaojiita “waliotahiriwa” (yaani tohara ifanyikayo katika mwili kwa mikono ya wanadamu), 12 kumbukeni kwamba wakati ule mlikuwa mbali na Kristo, mkiwa mmetengwa kutoka jumuiya ya Israeli, na mkiwa wageni katika yale maagano ya ahadi, nanyi mkiwa hamna tumaini wala Mungu duniani.
-
1 Kwa hiyo, mfuateni Mungu kama watoto wapendwao, 2 mkiishi maisha ya upendo, kama vile Kristo alivyotupenda sisi akajitoa kwa ajili yetu kuwa sadaka yenye harufu nzuri na dhabihu kwa Mungu.
-
22 Noa akafanya kila kitu kama vile Mungu alivyomwamuru.
-
2 Kisha Mungu akamwambia, “Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, Isaki umpendaye, uende katika nchi ya Moria. Mtoe huko kama sadaka ya kuteketezwa juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia.”
3 Abrahamu akaamka asubuhi na mapema siku iliyofuata, akamtayarisha punda wake. Akawachukua watumishi wake wawili pamoja na Isaki mwanawe. Baada ya kuchanja kuni za kutosha kwa ajili ya hiyo sadaka ya kuteketezwa, akaondoka kuelekea mahali Mungu alipokuwa amemwambia.
-
22 Lakini Samweli akajibu:
“Je, Bwana anafurahia sadaka za kuteketezwa na dhabihu
kama vile kuitii sauti ya Bwana?
Kutii ni bora zaidi kuliko dhabihu,
nako kusikia ni bora
kuliko mafuta ya kondoo dume.
-
5 Hezekia aliweka tumaini lake kwa Bwana, Mungu wa Israeli. Hapakuwepo na mfalme mwingine wa kufanana naye miongoni mwa wafalme wa Yuda, kabla yake au baada yake. 6 Alishikamana na Bwana kwa bidii wala hakuacha kumfuata; alishika amri ambazo Bwana alikuwa amempa Mose. 7 Naye Bwana alikuwa pamoja naye, akafanikiwa katika kila alichokifanya. Aliasi dhidi ya mfalme wa Ashuru, wala hakumtumikia.
-
23 lakini niliwapa amri hii nikisema: Nitiini mimi, nami nitakuwa Mungu wenu nanyi mtakuwa watu wangu. Enendeni katika njia zote ninazowaamuru ili mpate kufanikiwa.
-
3 Yona akalitii neno la Bwana naye akaenda Ninawi. Basi Ninawi ulikuwa mji maarufu sana, ilichukua siku tatu kuuzunguka.
-
28 “Njooni kwangu, ninyi nyote mnaotaabika na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. 29 Jifungeni nira yangu, mjifunze kutoka kwangu, kwa maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtapata raha nafsini mwenu. 30 Kwa maana nira yangu ni laini na mzigo wangu ni mwepesi.”
-
16 Mtu mmoja akamjia Yesu na kumuuliza, “Mwalimu mwema, nifanye jambo gani jema ili nipate uzima wa milele?”
17 Yesu akamjibu, “Mbona unaniuliza habari ya mema? Aliye mwema ni Mmoja tu. Lakini ukitaka kuingia uzimani, zitii amri.”
18 Yule mtu akamuuliza, “Amri zipi?”
Yesu akamjibu, “Usiue, usizini, usiibe, usishuhudie uongo, 19 waheshimu baba yako na mama yako, na umpende jirani yako kama nafsi yako.”
20 Yule kijana akasema, “Hizi zote nimezishika. Je, bado nimepungukiwa na nini?”
21 Yesu akamwambia, “Kama ukitaka kuwa mkamilifu, nenda, ukauze vitu vyote ulivyo navyo, na hizo fedha uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.”
22 Yule kijana aliposikia hayo, akaenda zake kwa huzuni, kwa sababu alikuwa na mali nyingi.
23 Ndipo Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Amin, nawaambia, itakuwa vigumu kwa mtu tajiri kuingia katika Ufalme wa Mbinguni. 24 Tena nawaambia, ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita kwenye tundu la sindano kuliko mtu tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu.”
25 Wanafunzi wake waliposikia haya, walishangaa sana na kuuliza, “Ni nani basi awezaye kuokoka?”
26 Lakini Yesu akawatazama, akawaambia, “Kwa mwanadamu jambo hili haliwezekani, lakini mambo yote yanawezekana kwa Mungu.”
27 Ndipo Petro akamjibu, “Tazama, sisi tumeacha kila kitu na kukufuata! Tutapata nini basi?”
28 Yesu akawaambia, “Amin, nawaambia, wakati wa kufanywa upya vitu vyote, Mwana wa Adamu atakapoketi kwenye kiti chake kitukufu cha enzi, ninyi mlionifuata pia mtaketi katika viti vya enzi kumi na viwili, mkiyahukumu makabila kumi na mawili ya Israeli. 29 Kila mtu aliyeacha nyumba, au ndugu zake wa kiume au wa kike, baba au mama, watoto au mashamba kwa ajili yangu, atapokea mara mia zaidi ya hayo, na ataurithi uzima wa milele. 30 Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, na walio wa mwisho watakuwa wa kwanza.
-
27 Baada ya haya, Yesu alitoka na kumwona mtoza ushuru mmoja jina lake Lawi akiwa amekaa forodhani, mahali pake pa kutoza ushuru. Akamwambia, “Nifuate.” 28 Naye Lawi akaacha kila kitu, akaondoka, akamfuata.
-
28 Yesu akajibu, “Wamebarikiwa zaidi wale wanaolisikia neno la Mungu na kulitii.”
-
25 Umati mkubwa wa watu ulikuwa ukisafiri pamoja na Yesu, naye akageuka, akawaambia, 26 “Mtu yeyote anayekuja kwangu hawezi kuwa mwanafunzi wangu kama hatanipenda mimi zaidi ya baba yake na mama yake, mke wake na watoto wake, ndugu zake na dada zake, naam, hata maisha yake mwenyewe. 27 Yeyote asiyeuchukua msalaba wake na kunifuata hawezi kuwa mwanafunzi wangu.
28 “Ni nani miongoni mwenu ambaye kama anataka kujenga nyumba, hakai kwanza chini na kufanya makisio ya gharama aone kama ana fedha za kutosha kukamilisha? 29 La sivyo, akiisha kuweka msingi, naye akiwa hana uwezo wa kuikamilisha, wote waionao wataanza kumdhihaki, 30 wakisema, ‘Mtu huyu alianza kujenga lakini hakuweza kukamilisha.’
31 “Au ni mfalme gani atokaye kwenda kupigana vita na mfalme mwingine, ambaye hakai chini kwanza na kufikiri iwapo akiwa na jeshi la watu 10,000 ataweza kupigana na yule anayekuja na jeshi la watu 20,000? 32 Kama hawezi, basi wakati yule mwingine akiwa bado yuko mbali, yeye hutuma ujumbe wa watu na kuomba masharti ya amani. 33 Vivyo hivyo, yeyote miongoni mwenu ambaye hawezi kuacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.
-
15 “Kama mnanipenda, mtazishika amri zangu.
-
19 Lakini Petro na Yohana wakajibu, “Amueni ninyi wenyewe iwapo ni haki mbele za Mungu kuwatii ninyi kuliko kumtii Mungu. 20 Lakini sisi hatuwezi kuacha kusema yale tuliyoyaona na kuyasikia.”
-
27 Wakiisha kuwaleta mitume wakawaamuru kusimama mbele ya baraza ili kuhani mkuu awahoji. 28 “Tuliwaonya kwa nguvu msifundishe kwa jina hili, lakini ninyi mmeijaza Yerusalemu yote mafundisho yenu na tena mmekusudia kuleta damu ya mtu huyu juu yetu.”
29 Petro na wale mitume wengine wakajibu, “Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu. 30 Mungu wa baba zetu alimfufua Yesu kutoka kwa wafu, ambaye ninyi mlimuua kwa kumtundika kwenye msalaba. 31 Mungu alimtukuza, akamweka mkono wake wa kuume kuwa Kiongozi na Mwokozi ili awape Israeli toba na msamaha wa dhambi. 32 Nasi tu mashahidi wa mambo haya, vivyo hivyo na Roho Mtakatifu ambaye Mungu amewapa wale wanaomtii.”
-
19 Kwa maana kama vile kwa kutokutii kwa yule mtu mmoja wengi walifanywa wenye dhambi, vivyo hivyo kwa kutii kwa mtu mmoja wengi watafanywa wenye haki.
-
7 Katika siku za maisha ya Yesu hapa duniani, alimtolea maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, yeye awezaye kumwokoa na mauti, naye Mungu akamsikia kwa sababu ya kutii kwake kwa unyenyekevu. 8 Ingawa alikuwa Mwana, alijifunza utiifu kutokana na mateso aliyoyapata, 9 na akiisha kukamilishwa, akawa chanzo cha wokovu wa milele kwa wote wanaomtii. 10 Naye amewekwa na Mungu kuwa Kuhani Mkuu kwa mfano wa Melkizedeki.
-
1 Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, na udhahiri wa mambo yasiyoonekana. 2 Maana baba zetu wa kale walipongezwa kwa haya.
3 Kwa imani tunafahamu kwamba ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu, vitu vyote vinavyoonekana havikuumbwa kutoka kwa vitu vinavyoonekana.
4 Kwa imani Abeli alimtolea Mungu dhabihu bora zaidi kuliko Kaini. Kwa imani alishuhudiwa kuwa mwenye haki, Mungu mwenyewe akazishuhudia sadaka zake. Kwa imani bado ananena ingawa amekufa.
5 Kwa imani Enoki alitwaliwa kutoka maisha haya, kiasi kwamba hakuonja mauti. Hakuonekana, kwa sababu Mungu alikuwa amemchukua. Kwa kuwa kabla hajatwaliwa alikuwa ameshuhudiwa kuwa ni mtu aliyempendeza Mungu. 6 Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza Mungu, kwa maana yeyote anayemjia Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko na ya kuwa huwapa thawabu wale wamtafutao kwa bidii.
7 Kwa imani, Noa alipoonywa na Mungu kuhusu mambo ambayo hayajaonekana bado, kwa kumcha Mungu alitengeneza safina ili kuokoa jamaa yake. Kwa imani yake aliuhukumu ulimwengu na akawa mrithi wa haki ipatikanayo kwa imani.
8 Kwa imani Abrahamu, alipoitwa aende mahali ambapo Mungu angempa baadaye kuwa urithi, alitii na akaenda, ingawa hakujua anakokwenda. 9 Kwa imani alifanya maskani yake katika nchi ya ahadi kama mgeni katika nchi ya kigeni; aliishi katika mahema, kama Isaki na Yakobo walivyofanya, waliokuwa pia warithi pamoja naye wa ahadi ile ile. 10 Kwa maana alikuwa akiutazamia mji wenye misingi ya kudumu ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu.
11 Kwa imani Abrahamu, ingawa alikuwa mzee wa umri, naye Sara mwenyewe aliyekuwa tasa, alipokea uwezo wa kuwa baba kwa sababu alimhesabu Mungu aliyemwahidi kuwa mwaminifu na kwamba angetimiza ahadi yake. 12 Hivyo kutokana na huyu huyu ambaye alikuwa sawa na mfu, wakazaliwa wazao wengi kama nyota za mbinguni na kama mchanga wa pwani usiohesabika.
13 Watu hawa wote wakafa katika imani bila kuzipokea zile ahadi, lakini waliziona kwa mbali na kuzishangilia. Nao walikubali kwamba walikuwa wageni na wasiokuwa na maskani hapa duniani. 14 Watu wasemao mambo kama haya, wanaonyesha wazi kwamba wanatafuta nchi yao wenyewe. 15 Kwa kweli kama wangekuwa wanafikiri kuhusu nchi waliyoiacha, wangalipata nafasi ya kurudi huko. 16 Lakini badala yake walitamani nchi iliyo bora zaidi, yaani nchi ya mbinguni. Kwa hiyo Mungu haoni aibu kuitwa Mungu wao, kwa kuwa amekwisha kuandaa mji kwa ajili yao.
17 Kwa imani Abrahamu, alipojaribiwa na Mungu, alimtoa Isaki kuwa dhabihu. Yeye aliyekuwa amezipokea ahadi za Mungu alikuwa tayari kumtoa mwanawe, aliyekuwa mwanawe pekee awe dhabihu. 18 Ingawa Mungu alikuwa amemwambia Abrahamu, “Uzao wako utahesabiwa kupitia kwa Isaki,” 19 Abrahamu alihesabu kuwa Mungu angaliweza kumfufua Isaki kutoka kwa wafu. Na kwa kusema kwa mfano, alimpata tena Isaki kutoka kwa wafu.
20 Kwa imani Isaki alimbariki Yakobo na Esau kuhusu maisha yao ya baadaye.
21 Kwa imani Yakobo alipokuwa anakufa, alimbariki kila mmoja wa mtoto wa Yosefu, akamwabudu Mungu akiwa ameegemea juu ya kichwa cha fimbo yake.
22 Kwa imani, Yosefu alipokaribia mwisho wa maisha yake, alinena habari za kutoka kwa wana wa Israeli huko Misri na akatoa maagizo kuhusu mifupa yake.
23 Kwa imani, wazazi wa Mose walimficha kwa miezi mitatu baada ya kuzaliwa, kwa sababu waliona kuwa si mtoto wa kawaida, wala hawakuiogopa amri ya mfalme.
24 Kwa imani, Mose alipokuwa mtu mzima, alikataa kuitwa mwana wa binti Farao. 25 Akachagua kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha kwa anasa za dhambi kwa kitambo kidogo tu. 26 Aliona kushutumiwa kwa ajili ya Kristo ni utajiri mkubwa zaidi kuliko hazina za Misri, maana alikuwa anatazamia kupata thawabu baadaye. 27 Kwa imani Mose aliondoka Misri bila kuogopa ghadhabu ya mfalme. Alivumilia kwa sababu alimwona yeye asiyeonekana kwa macho. 28 Kwa imani akaadhimisha Pasaka na kunyunyiza damu, ili yule mwenye kuwaangamiza wazaliwa wa kwanza asiwaguse wazaliwa wa Israeli.
29 Kwa imani, watu walivuka Bahari ya Shamu kama vile juu ya nchi kavu; lakini Wamisri walipojaribu kufanya hivyo, walitoswa ndani ya maji.
30 Kwa imani kuta za Yeriko zilianguka, baada ya watu kuzizunguka kwa siku saba.
31 Kwa imani, Rahabu, yule kahaba, hakuangamizwa pamoja na wale waliomwasi Mungu, kwa kuwa aliwakaribisha wale wapelelezi.
32 Basi niseme nini zaidi? Sina wakati wa kusema habari za Gideoni, Baraka, Samsoni, Yeftha, Daudi, Samweli na manabii, 33 ambao kwa imani walishinda milki za wafalme, walitekeleza haki, na wakapokea ahadi za Mungu; walifunga vinywa vya simba, 34 wakazima makali ya miali ya moto, na wakaepuka kuuawa kwa upanga; udhaifu wao uligeuka kuwa nguvu; pia walikuwa hodari vitani na kuyafukuza majeshi ya wageni. 35 Wanawake walipokea watu wao waliokuwa wamekufa, wakafufuliwa. Lakini wengine waliteswa, nao wakakataa kufunguliwa, ili wapate ufufuo ulio bora zaidi. 36 Wengine walidhihakiwa na kupigwa, hata walifungwa minyororo na kutiwa gerezani. 37 Walipigwa kwa mawe; walipasuliwa vipande viwili kwa msumeno; waliuawa kwa upanga. Walizungukazunguka wakiwa wamevaa ngozi za kondoo na mbuzi, wakiwa maskini, wakiteswa na kutendwa mabaya, 38 watu ambao ulimwengu haukustahili kuwa nao. Walizunguka majangwani na milimani, katika mapango na katika mahandaki ardhini.
39 Hawa wote walishuhudiwa vyema kwa sababu ya imani yao, lakini hakuna hata mmoja wao aliyepokea yale yaliyoahidiwa. 40 Kwa kuwa Mungu alikuwa ametangulia kutuwekea kitu kilicho bora zaidi ili wao wasikamilishwe pasipo sisi.
-
15 Msiupende ulimwengu wala mambo yaliyo ulimwenguni. Kama mtu yeyote akiupenda ulimwengu, upendo wa Baba haumo ndani yake. 16 Kwa maana kila kitu kilichomo ulimwenguni, yaani tamaa ya mwili, tamaa ya macho na kiburi cha uzima, havitokani na Baba bali hutokana na ulimwengu. 17 Nao ulimwengu unapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu milele.
-
24 Lakini kwa sababu mtumishi wangu Kalebu ana roho ya tofauti na ananifuata kwa moyo wote, nitamwingiza katika nchi aliyoiendea, nao wazao wake watairithi.
-
11 ‘Kwa kuwa hawakunifuata kwa moyo wote, hakuna mtu yeyote mwenye miaka ishirini au zaidi ambaye alikuja kutoka Misri atakayeona nchi niliyoahidi kwa kiapo kwa Abrahamu, Isaki na Yakobo; 12 hakuna hata mmoja isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune, Mkenizi, na Yoshua mwana wa Nuni, kwa sababu walimfuata Bwana kwa moyo wote.’
-
8 Lakini ndugu zangu tuliopanda nao waliifanya mioyo ya watu iyeyuke kwa hofu. Bali mimi, nilimfuata Bwana Mungu wangu kwa moyo wote. 9 Hivyo katika siku ile, Mose akaniapia, ‘Nchi ambayo umeikanyaga kwa miguu yako itakuwa urithi wako na wa watoto wako milele, kwa sababu umemfuata Bwana Mungu wangu kwa moyo wote.’
-
28 Ndipo Petro akamjibu, “Tazama, tumeacha kila kitu na kukufuata wewe!”
29 Yesu akasema, “Amin, nawaambia, hakuna mtu yeyote aliyeacha nyumba, ndugu wa kiume au wa kike, au mama au baba, au watoto au mashamba kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili, 30 ambaye hatalipwa mara mia katika ulimwengu huu: nyumba, ndugu wa kiume na wa kike, mama na baba na watoto, mashamba pamoja na mateso, kisha uzima wa milele katika ulimwengu ujao. 31 Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, na wa mwisho watakuwa wa kwanza.”
-
34 Akawaambia, “Moyo wangu umejawa na huzuni kiasi cha kufa. Kaeni hapa na mkeshe.”
35 Akaenda mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akaomba kwamba kama ingewezekana saa hiyo ya mateso imwondokee. 36 Akasema, “Abba, Baba, mambo yote yawezekana kwako. Niondolee kikombe hiki. Lakini si kama nipendavyo mimi, bali vile upendavyo wewe.”
-
19 Wakati mmoja mama yake Yesu na ndugu zake walikuja kumwona, lakini hawakuweza kumfikia kwa sababu ya msongamano wa watu. 20 Mtu mmoja akamwambia, “Mama yako na ndugu zako wako nje wanataka kukuona.”
21 Yesu akamjibu, “Mama yangu na ndugu zangu ni wale wote wanaolisikia neno la Mungu na kulifanya.”
-
12 Alipomaliza kuwanawisha miguu yao, alivaa tena mavazi yake, akarudi alikokuwa ameketi, akawauliza, “Je, mmeelewa nililowafanyia? 13 Ninyi mnaniita mimi ‘Mwalimu’ na ‘Bwana,’ hii ni sawa, maana ndivyo nilivyo. 14 Kwa hiyo, ikiwa mimi niliye Bwana wenu na Mwalimu wenu nimewanawisha ninyi miguu, pia hamna budi kunawishana miguu ninyi kwa ninyi. 15 Mimi nimewawekea kielelezo kwamba imewapasa kutenda kama vile nilivyowatendea ninyi. 16 Amin, amin nawaambia, mtumishi si mkuu kuliko bwana wake, wala aliyetumwa si mkuu kuliko yule aliyemtuma. 17 Sasa kwa kuwa mmejua mambo haya, heri yenu ninyi kama mkiyatenda.
-
1 Kwa sababu hii, kwa kuwa tumezungukwa na wingu kubwa namna hii la mashahidi, basi na tuweke kando kila kitu kinachotuzuia na ile dhambi inayotuzinga kwa urahisi, nasi tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa kwa ajili yetu. 2 Basi na tumtazame sana Yesu mwanzilishi na mkamilishaji wa imani yetu, yeye ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake alistahimili msalaba, bila kujali aibu ya huo msalaba, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu.
-
3 Huku ndiko kumpenda Mungu, yaani, kuzitii amri zake. Nazo amri zake si nzito.
-
3 Usiwe na miungu mingine ila mimi.
-
33 Lakini utafuteni kwanza Ufalme wa Mungu na haki yake, na haya yote atawapa pia.
-
28 Ndipo Petro akamjibu, “Tazama, tumeacha vyote tulivyokuwa navyo tukakufuata!”
29 Yesu akajibu, “Amin, nawaambia, hakuna hata mtu aliyeacha nyumba yake, au mke, au ndugu, au wazazi au watoto kwa ajili ya Ufalme wa Mungu 30 ambaye hatapewa mara nyingi zaidi ya hivyo katika maisha haya, na hatimaye kupata uzima wa milele ujao.”
-
26 Lakini huyo Msaidizi, yaani, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwenu kwa Jina langu, atawafundisha mambo yote na kuwakumbusha yote niliyowaambia.
-
19 Yesu alisema haya ili kuashiria ni kifo cha aina gani Petro atakachomtukuza nacho Mungu. Kisha Yesu akamwambia Petro, “Nifuate!”
-
1 Kila mtu na atii mamlaka inayotawala, kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu, nazo mamlaka zilizopo zimewekwa na Mungu. 2 Kwa hiyo yeye anayeasi dhidi ya mamlaka inayotawala anaasi dhidi ya kile kilichowekwa na Mungu, nao wale wafanyao hivyo watajiletea hukumu juu yao wenyewe. 3 Kwa kuwa watawala hawawatishi watu wale wanaotenda mema bali wale wanaotenda mabaya. Je, wataka usimwogope mwenye mamlaka? Basi tenda lile lililo jema naye atakusifu. 4 Kwa maana mwenye mamlaka ni mtumishi wa Mungu kwa ajili ya mema. Lakini kama ukitenda mabaya, basi ogopa, kwa kuwa hauinui upanga bila sababu. Yeye ni mtumishi wa Mungu, mjumbe wa Mungu wa kutekeleza adhabu juu ya watenda mabaya. 5 Kwa hiyo ni lazima kutii wenye mamlaka, si kwa sababu ya kuogopa adhabu iwezayo kutolewa, bali pia kwa ajili ya dhamiri.
6 Kwa sababu hii mnalipa kodi, kwa maana watawala ni watumishi wa Mungu, ambao hutumia muda wao wote kutawala. 7 Mlipeni kila mtu kile mnachodaiwa. Kama mnadaiwa kodi lipeni kodi, kama ni ushuru, lipeni ushuru, astahiliye hofu, mhofu, astahiliye heshima, mheshimu.
-
19 Kwa maana mimi kwa njia ya sheria, nimeifia sheria ili nipate kuishi kwa ajili ya Mungu. 20 Nimesulubiwa pamoja na Kristo, wala si mimi tena ninayeishi, bali Kristo ndiye aishiye ndani yangu. Uhai nilio nao sasa katika mwili, ninaishi kwa imani ya Mwana wa Mungu, aliyenipenda na kujitoa kwa ajili yangu.
-
20 Basi Mungu wa amani, ambaye kwa damu ya Agano la milele alimleta tena kutoka kwa wafu Bwana wetu Yesu, yule Mchungaji Mkuu wa kondoo, 21 awafanye ninyi wakamilifu mkiwa mmekamilishwa katika kila jambo jema ili mpate kutenda mapenzi yake, naye atende ndani yetu kile kinachompendeza machoni Pake, kwa njia ya Yesu Kristo, ambaye utukufu una yeye milele na milele. Amen.
-
33 Fuateni yale yote ambayo Bwana Mungu wenu aliwaagiza, ili mpate kuishi, kustawi na kuziongeza siku zenu katika nchi mtakayoimiliki.
-
9 Kijana aifanye njia yake kuwa safi jinsi gani?
Ni kwa kutii, akilifuata neno lako.
10 Ninakutafuta kwa moyo wangu wote,
usiniache niende mbali na amri zako.
11 Nimelificha neno lako moyoni mwangu
ili nisikutende dhambi.
-
43 “Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Mpende jirani yako na umchukie adui yako.’ 44 Lakini ninawaambia: Wapendeni adui zenu na waombeeni wanaowatesa ninyi, 45 ili mpate kuwa watoto wa Baba yenu aliye mbinguni. Kwa maana yeye huwaangazia jua lake watu waovu na watu wema, naye huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. 46 Kama mkiwapenda tu wale wanaowapenda, mtapata thawabu gani? Je, hata watoza ushuru hawafanyi hivyo? 47 Nanyi kama mkiwasalimu ndugu zenu tu, je, mnafanya nini zaidi ya wengine? Je, hata watu wasiomjua Mungu, hawafanyi hivyo? 48 Kwa hiyo kuweni wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.
-
52 Ndipo Yesu akamwambia, “Rudisha upanga wako mahali pake, kwa maana wote watumiao upanga watakufa kwa upanga. 53 Je, unadhani siwezi kumwomba Baba yangu naye mara moja akaniletea zaidi ya majeshi kumi na mawili ya malaika? 54 Lakini je, yale Maandiko yanayotabiri kwamba ni lazima itendeke hivi yatatimiaje?”
-
14 Alipokuwa akitembea, akamwona Lawi mwana wa Alfayo ameketi forodhani mahali pa kutoza ushuru, akamwambia, “Nifuate.” Lawi akaondoka, akamfuata Yesu.
-
1 Siku moja Yesu alipokuwa amesimama karibu na Ziwa la Genesareti, watu wengi wakiwa wanasongana kumzunguka ili wapate kusikia neno la Mungu, 2 akaona mashua mbili ukingoni mwa ziwa, zikiwa zimeachwa hapo na wavuvi waliokuwa wanaosha nyavu zao. 3 Akaingia katika mojawapo ya hizo mashua ambayo ilikuwa ya Simoni, akamwomba aisogeze ndani ya maji kidogo kutoka ufuoni. Kisha akaketi na kufundisha watu akiwa mle ndani ya mashua.
4 Alipomaliza kunena, akamwambia Simoni, “Sasa peleka mashua hadi kilindini kisha mshushe nyavu zenu mkavue samaki.”
5 Simoni akamjibu, “Bwana, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha na hatukuvua chochote. Lakini, kwa neno lako nitazishusha nyavu.”
6 Nao walipozishusha nyavu zao, wakavua samaki wengi sana, nyavu zao zikajaa zikaanza kukatika. 7 Wakawaashiria wavuvi wenzao kwenye ile mashua nyingine ili waje kuwasaidia. Wakaja, wakajaza mashua zote mbili samaki hata zikaanza kuzama.
8 Simoni Petro alipoona haya yaliyotukia, alianguka miguuni mwa Yesu na kumwambia, “Bwana, ondoka kwangu. Mimi ni mtu mwenye dhambi!” 9 Kwa kuwa yeye na wavuvi wenzake walikuwa wameshangazwa sana na wingi wa samaki waliokuwa wamepata. 10 Vivyo hivyo wenzake Simoni, yaani Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, walishangazwa pia.
Ndipo Yesu akamwambia Simoni, “Usiogope, tangu sasa utakuwa mvuvi wa watu.” 11 Hivyo wakasogeza mashua zao mpaka ufuoni mwa bahari, wakaacha kila kitu na kumfuata.
-
22 Yesu aliposikia haya, akamwambia, “Bado kuna jambo moja ulilopungukiwa. Nenda ukauze kila kitu ulicho nacho, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.”
23 Aliposikia jambo hili, alisikitika sana kwa maana alikuwa mtu mwenye mali nyingi.
-
43 Siku iliyofuata Yesu aliamua kwenda Galilaya. Akamkuta Filipo, akamwambia, “Nifuate.”
44 Basi Filipo alikuwa mwenyeji wa Bethsaida, mji alikotoka Andrea na Petro. 45 Filipo naye akamkuta Nathanaeli na kumwambia, “Tumemwona yeye ambaye Mose aliandika habari zake katika Sheria na ambaye pia manabii waliandika kumhusu, yaani, Yesu wa Nazareti, mwana wa Yosefu.”
-
31 Kisha Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, “Kama mkidumu katika maneno yangu, mtakuwa wanafunzi wangu kweli kweli. 32 Ndipo mtaijua kweli nayo kweli itawaweka huru.”
-
1 “Amin, amin nawaambia, yeye asiyeingia katika zizi la kondoo kwa kupitia kwenye lango, lakini akwea kuingia ndani kwa njia nyingine, ni mwizi na mnyangʼanyi. 2 Yeye anayeingia kwa kupitia kwenye lango ndiye mchungaji wa kondoo. 3 Mlinzi humfungulia lango na kondoo huisikia sauti yake. Huwaita kondoo wake kwa majina yao na kuwatoa nje ya zizi. 4 Akiisha kuwatoa wote nje, hutangulia mbele yao na kondoo humfuata kwa kuwa wanaijua sauti yake. 5 Lakini kondoo hawatamfuata mgeni bali watamkimbia, kwa sababu hawaijui sauti ya mgeni.”
-
35 Kama mkipendana ninyi kwa ninyi, kwa njia hii, watu wote watajua kuwa ninyi ni wanafunzi wangu.”
-
6 Yesu akawaambia, “Mimi ndimi njia na kweli na uzima. Mtu hawezi kuja kwa Baba isipokuwa kwa kupitia kwangu.
-
21 Yeyote mwenye amri zangu na kuzishika ndiye anipendaye, naye anipendaye atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda na kujidhihirisha kwake.”
-
23 Yesu akamjibu, “Mtu yeyote akinipenda atalishika neno langu na Baba yangu atampenda, nasi tutakuja kwake na kufanya makao yetu kwake.
-
37 Watu waliposikia maneno haya yakawachoma mioyo yao, wakawauliza Petro na wale mitume wengine, “Ndugu zetu tufanye nini?”
38 Petro akawajibu, “Tubuni, mkabatizwe kila mmoja wenu kwa jina la Yesu Kristo, ili mpate kusamehewa dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu. 39 Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu na watoto wenu, na kwa wote walio mbali, na kila mtu ambaye Bwana Mungu wetu atamwita amjie.”
40 Petro akawaonya kwa maneno mengine mengi na kuwasihi akisema, “Jiepusheni na kizazi hiki kilichopotoka.” 41 Wale wote waliopokea ujumbe wa Petro kwa furaha wakabatizwa na siku ile waliongezeka watu wapatao 3,000.
-
28 Nasi tunajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hutenda kazi pamoja na wote wampendao, katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.
-
16 Kwa hiyo nasema, enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili. 17 Kwa maana mwili hutamani yale yaliyo kinyume na Roho, naye Roho hutamani yale yaliyo kinyume na mwili. Roho na mwili hupingana na kwa sababu hiyo hamwezi kufanya mnayotaka. 18 Lakini kama mkiongozwa na Roho, hamko chini ya sheria.
19 Basi matendo ya mwili ni dhahiri nayo ni haya: Uasherati, uchafu, ufisadi, 20 kuabudu sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, 21 husuda, ulevi, ulafi na mambo mengine yanayofanana na hayo. Nawaonya, kama nilivyokwisha kuwaonya kabla, kwamba watu watendao mambo kama hayo, hawataurithi Ufalme wa Mungu.
22 Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, 23 upole na kiasi. Katika mambo kama haya hakuna sheria. 24 Wote walio wa Kristo Yesu wameusulubisha mwili na shauku zake pamoja na tamaa zake. 25 Kwa kuwa tunaishi kwa Roho, basi, tuenende kwa Roho.
-
13 Basi sikilizeni ninyi msemao, “Leo au kesho tutakwenda katika mji huu ama ule tukae humo mwaka mmoja, tufanye biashara na kupata faida.” 14 Lakini hamjui hata litakalotukia kesho. Maisha yenu ni nini? Ninyi ni ukungu ambao huonekana kwa kitambo kidogo kisha hutoweka. 15 Badala yake, inawapasa kusema, “Kama Bwana akipenda, tutaishi na kufanya hili ama lile.” 16 Kama ilivyo sasa, mnajisifu na kujigamba. Kujisifu kwa namna hiyo ni uovu. 17 Basi mtu yeyote anayejua jema limpasalo kutenda, lakini asilitende, mtu huyo anatenda dhambi.
-
18 Kwa kuwa Kristo naye aliteswa mara moja tu kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili ya wasio haki, ili awalete ninyi kwa Mungu. Mwili wake ukauawa, lakini akafanywa hai katika Roho. 19 Baada ya kufanywa hai, alikwenda na kuzihubiria roho zilizokuwa kifungoni: 20 roho hizo ambazo zamani hazikutii, wakati ule uvumilivu wa Mungu ulipokuwa ukingoja katika siku za Noa, wakati wa kujenga safina, ambamo watu wachache tu, yaani watu wanane, waliokolewa ili wasiangamie kwa gharika. 21 Nayo maji hayo ni kielelezo cha ubatizo ambao sasa unawaokoa ninyi pia: si kwa kuondoa uchafu kwenye mwili, bali kama ahadi ya dhamiri safi kwa Mungu, kwa njia ya ufufuo wa Yesu Kristo. 22 Yeye ameingia mbinguni na amekaa mkono wa kuume wa Mungu; nao malaika, mamlaka na nguvu zote wametiishwa chini yake.
-
4 Imenipa furaha kuu kuona baadhi ya watoto wako wanaenenda katika kweli, kama vile Baba alivyotuagiza. 5 Sasa, bibi mpendwa, si kwamba ninakuandikia amri mpya, bali ile tuliyokuwa nayo tangu mwanzo. Tupendane kila mmoja na mwenzake. 6 Hili ndilo pendo, kwamba tuenende sawasawa na amri zake. Hii ndiyo amri yake kama vile mlivyosikia tangu mwanzo, kwamba mwenende katika upendo.
7 Wadanganyifu wengi, wasiokubali kwamba Yesu Kristo amekuja katika mwili, wametokea ulimwenguni. Mtu wa namna hiyo ni mdanganyifu na mpinga Kristo. 8 Jihadharini msije mkapoteza kile mlichokitenda, bali mpate kupewa thawabu kamilifu. 9 Mtu yeyote asiyedumu katika mafundisho ya Kristo, bali akayaacha, yeye hana Mungu. Yeyote anayedumu katika mafundisho ana Baba na Mwana pia. 10 Msimpokee mtu yeyote anayewajia ambaye hawaletei mafundisho haya, wala msimkaribishe nyumbani mwenu. 11 Yeyote amkaribishaye mtu wa namna hiyo anashiriki katika matendo maovu ya mtu huyo.
-
1 Kisha nikatazama na hapo mbele yangu alikuwepo Mwana-Kondoo, akiwa amesimama juu ya Mlima Sayuni. Pamoja naye walikuwa wale 144,000 wenye Jina la Mwana-Kondoo na Jina la Baba yake likiwa limeandikwa kwenye vipaji vya nyuso zao. 2 Nami nikasikia sauti kutoka mbinguni kama sauti ya maji mengi yaendayo kwa kasi na sauti kama ngurumo ya radi. Sauti hiyo niliyoisikia ilikuwa kama sauti ya wapiga vinubi wakipiga vinubi vyao. 3 Nao wakaimba wimbo mpya mbele ya hicho kiti cha enzi na mbele ya wale viumbe wanne wenye uhai na wale wazee. Hakuna mtu yeyote aliyeweza kujifunza wimbo huo isipokuwa hao 144,000 waliokuwa wamekombolewa kutoka duniani. 4 Hawa ndio wale ambao hawakujitia unajisi kwa wanawake, kwa kuwa wao ni bikira. Wao humfuata Mwana-Kondoo kila aendako. Hawa wamekombolewa kutoka miongoni mwa wanadamu wakawa malimbuko kwa Mungu na kwa Mwana-Kondoo. 5 Vinywani mwao hapakuonekana uongo, wala hawakuwa na hatia yoyote.
Shows Read in context, Share and Copy.