60 Bible Verses About Trusting God's Plan
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
-
5 Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote
wala usizitegemee akili zako mwenyewe;
6 katika njia zako zote mkiri yeye,
naye atayanyoosha mapito yako.
7 Usiwe mwenye hekima machoni pako mwenyewe;
mche Bwana ukajiepushe na uovu.
-
26 Vivyo hivyo, Roho hutusaidia katika udhaifu wetu, kwa sababu hatujui kuomba ipasavyo. Lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa uchungu usioweza kutamkwa. 27 Naye Mungu aichunguzaye mioyo, anaijua nia ya Roho, kwa sababu Roho huwaombea watakatifu sawasawa na mapenzi ya Mungu.
28 Nasi tunajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hutenda kazi pamoja na wote wampendao, katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. 29 Maana wale Mungu aliowajua tangu mwanzo, pia aliwachagua tangu mwanzo, wapate kufanana na mfano wa Mwanawe, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. 30 Nao wale Mungu aliotangulia kuwachagua, akawaita, wale aliowaita pia akawahesabia haki, nao wale aliowahesabia haki, pia akawatukuza.
-
4 Jifurahishe katika Bwana
naye atakupa haja za moyo wako.
5 Mkabidhi Bwana njia yako,
mtumaini yeye, naye atatenda hili:
6 Yeye atafanya haki yako ingʼae kama mapambazuko,
na hukumu ya shauri lako kama jua la adhuhuri.
-
1 Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, na udhahiri wa mambo yasiyoonekana. 2 Maana baba zetu wa kale walipongezwa kwa haya.
3 Kwa imani tunafahamu kwamba ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu, vitu vyote vinavyoonekana havikuumbwa kutoka kwa vitu vinavyoonekana.
4 Kwa imani Abeli alimtolea Mungu dhabihu bora zaidi kuliko Kaini. Kwa imani alishuhudiwa kuwa mwenye haki, Mungu mwenyewe akazishuhudia sadaka zake. Kwa imani bado ananena ingawa amekufa.
5 Kwa imani Enoki alitwaliwa kutoka maisha haya, kiasi kwamba hakuonja mauti. Hakuonekana, kwa sababu Mungu alikuwa amemchukua. Kwa kuwa kabla hajatwaliwa alikuwa ameshuhudiwa kuwa ni mtu aliyempendeza Mungu. 6 Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza Mungu, kwa maana yeyote anayemjia Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko na ya kuwa huwapa thawabu wale wamtafutao kwa bidii.
7 Kwa imani, Noa alipoonywa na Mungu kuhusu mambo ambayo hayajaonekana bado, kwa kumcha Mungu alitengeneza safina ili kuokoa jamaa yake. Kwa imani yake aliuhukumu ulimwengu na akawa mrithi wa haki ipatikanayo kwa imani.
8 Kwa imani Abrahamu, alipoitwa aende mahali ambapo Mungu angempa baadaye kuwa urithi, alitii na akaenda, ingawa hakujua anakokwenda. 9 Kwa imani alifanya maskani yake katika nchi ya ahadi kama mgeni katika nchi ya kigeni; aliishi katika mahema, kama Isaki na Yakobo walivyofanya, waliokuwa pia warithi pamoja naye wa ahadi ile ile. 10 Kwa maana alikuwa akiutazamia mji wenye misingi ya kudumu ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu.
11 Kwa imani Abrahamu, ingawa alikuwa mzee wa umri, naye Sara mwenyewe aliyekuwa tasa, alipokea uwezo wa kuwa baba kwa sababu alimhesabu Mungu aliyemwahidi kuwa mwaminifu na kwamba angetimiza ahadi yake. 12 Hivyo kutokana na huyu huyu ambaye alikuwa sawa na mfu, wakazaliwa wazao wengi kama nyota za mbinguni na kama mchanga wa pwani usiohesabika.
13 Watu hawa wote wakafa katika imani bila kuzipokea zile ahadi, lakini waliziona kwa mbali na kuzishangilia. Nao walikubali kwamba walikuwa wageni na wasiokuwa na maskani hapa duniani. 14 Watu wasemao mambo kama haya, wanaonyesha wazi kwamba wanatafuta nchi yao wenyewe. 15 Kwa kweli kama wangekuwa wanafikiri kuhusu nchi waliyoiacha, wangalipata nafasi ya kurudi huko. 16 Lakini badala yake walitamani nchi iliyo bora zaidi, yaani nchi ya mbinguni. Kwa hiyo Mungu haoni aibu kuitwa Mungu wao, kwa kuwa amekwisha kuandaa mji kwa ajili yao.
17 Kwa imani Abrahamu, alipojaribiwa na Mungu, alimtoa Isaki kuwa dhabihu. Yeye aliyekuwa amezipokea ahadi za Mungu alikuwa tayari kumtoa mwanawe, aliyekuwa mwanawe pekee awe dhabihu. 18 Ingawa Mungu alikuwa amemwambia Abrahamu, “Uzao wako utahesabiwa kupitia kwa Isaki,” 19 Abrahamu alihesabu kuwa Mungu angaliweza kumfufua Isaki kutoka kwa wafu. Na kwa kusema kwa mfano, alimpata tena Isaki kutoka kwa wafu.
20 Kwa imani Isaki alimbariki Yakobo na Esau kuhusu maisha yao ya baadaye.
21 Kwa imani Yakobo alipokuwa anakufa, alimbariki kila mmoja wa mtoto wa Yosefu, akamwabudu Mungu akiwa ameegemea juu ya kichwa cha fimbo yake.
22 Kwa imani, Yosefu alipokaribia mwisho wa maisha yake, alinena habari za kutoka kwa wana wa Israeli huko Misri na akatoa maagizo kuhusu mifupa yake.
23 Kwa imani, wazazi wa Mose walimficha kwa miezi mitatu baada ya kuzaliwa, kwa sababu waliona kuwa si mtoto wa kawaida, wala hawakuiogopa amri ya mfalme.
24 Kwa imani, Mose alipokuwa mtu mzima, alikataa kuitwa mwana wa binti Farao. 25 Akachagua kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha kwa anasa za dhambi kwa kitambo kidogo tu. 26 Aliona kushutumiwa kwa ajili ya Kristo ni utajiri mkubwa zaidi kuliko hazina za Misri, maana alikuwa anatazamia kupata thawabu baadaye. 27 Kwa imani Mose aliondoka Misri bila kuogopa ghadhabu ya mfalme. Alivumilia kwa sababu alimwona yeye asiyeonekana kwa macho. 28 Kwa imani akaadhimisha Pasaka na kunyunyiza damu, ili yule mwenye kuwaangamiza wazaliwa wa kwanza asiwaguse wazaliwa wa Israeli.
29 Kwa imani, watu walivuka Bahari ya Shamu kama vile juu ya nchi kavu; lakini Wamisri walipojaribu kufanya hivyo, walitoswa ndani ya maji.
30 Kwa imani kuta za Yeriko zilianguka, baada ya watu kuzizunguka kwa siku saba.
31 Kwa imani, Rahabu, yule kahaba, hakuangamizwa pamoja na wale waliomwasi Mungu, kwa kuwa aliwakaribisha wale wapelelezi.
32 Basi niseme nini zaidi? Sina wakati wa kusema habari za Gideoni, Baraka, Samsoni, Yeftha, Daudi, Samweli na manabii, 33 ambao kwa imani walishinda milki za wafalme, walitekeleza haki, na wakapokea ahadi za Mungu; walifunga vinywa vya simba, 34 wakazima makali ya miali ya moto, na wakaepuka kuuawa kwa upanga; udhaifu wao uligeuka kuwa nguvu; pia walikuwa hodari vitani na kuyafukuza majeshi ya wageni. 35 Wanawake walipokea watu wao waliokuwa wamekufa, wakafufuliwa. Lakini wengine waliteswa, nao wakakataa kufunguliwa, ili wapate ufufuo ulio bora zaidi. 36 Wengine walidhihakiwa na kupigwa, hata walifungwa minyororo na kutiwa gerezani. 37 Walipigwa kwa mawe; walipasuliwa vipande viwili kwa msumeno; waliuawa kwa upanga. Walizungukazunguka wakiwa wamevaa ngozi za kondoo na mbuzi, wakiwa maskini, wakiteswa na kutendwa mabaya, 38 watu ambao ulimwengu haukustahili kuwa nao. Walizunguka majangwani na milimani, katika mapango na katika mahandaki ardhini.
39 Hawa wote walishuhudiwa vyema kwa sababu ya imani yao, lakini hakuna hata mmoja wao aliyepokea yale yaliyoahidiwa. 40 Kwa kuwa Mungu alikuwa ametangulia kutuwekea kitu kilicho bora zaidi ili wao wasikamilishwe pasipo sisi.
-
5 Hili ndilo asemalo Bwana:
“Amelaaniwa yeye amtegemeaye mwanadamu,
ategemeaye mwenye mwili
kwa ajili ya nguvu zake,
ambaye moyo wake
umemwacha Bwana.
6 Atakuwa kama kichaka cha jangwani;
hataona mafanikio yatakapokuja.
Ataishi katika sehemu zisizo na maji,
katika nchi ya chumvi ambapo
hakuna yeyote aishiye humo.
7 “Lakini amebarikiwa mtu ambaye tumaini lake ni katika Bwana,
ambaye matumaini yake ni katika Bwana.
8 Atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji
uenezao mizizi yake karibu na kijito cha maji.
Hauogopi wakati wa joto ujapo;
majani yake ni mabichi daima.
Hauna hofu katika mwaka wa ukame
na hautaacha kuzaa matunda.”
-
1 Mipango ya moyoni ni ya mwanadamu,
bali jibu la ulimi hutoka kwa Bwana.
2 Njia zote za mtu huonekana safi machoni pake mwenyewe,
bali makusudi hupimwa na Bwana.
3 Mkabidhi Bwana lolote ufanyalo,
nayo mipango yako itafanikiwa.
4 Bwana hufanya kila kitu kwa kusudi lake mwenyewe;
hata waovu kwa siku ya maangamizi.
-
3 Utamlinda katika amani kamilifu
yeye ambaye moyo wake ni thabiti
kwa sababu anakutumaini wewe.
4 Mtumaini Bwana milele,
kwa kuwa Bwana, Bwana, ni Mwamba wa milele.
-
4 Hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, awaambialo wale wote niliowapeleka kutoka Yerusalemu kwenda uhamishoni Babeli: 5 “Jengeni nyumba na mstarehe, pandeni bustani na mle mazao yake. 6 Oeni wake na mzae wana na binti, waozeni wana wenu wake, nanyi watoeni binti zenu waolewe, ili nao pia wazae wana na binti. Ongezekeni idadi yenu huko, wala msipungue. 7 Pia tafuteni amani na mafanikio ya mji ambamo nimewapeleka uhamishoni. Mwombeni Bwana kwa ajili ya mji huo, kwa sababu ukistawi, ninyi pia mtastawi.”
8 Naam, hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: “Msikubali manabii na wabashiri walioko miongoni mwenu wawadanganye. Msisikilize ndoto ambazo mmewatia moyo kuota. 9 Wanawatabiria ninyi uongo kwa jina langu. Sikuwatuma,” asema Bwana.
10 Hili ndilo asemalo Bwana: “Miaka sabini itakapotimia kwa ajili ya Babeli, nitakuja kwenu na kutimiza ahadi yangu ya rehema ya kuwarudisha mahali hapa. 11 Kwa maana ninajua mipango niliyo nayo kwa ajili yenu,” asema Bwana, “ni mipango ya kuwafanikisha na wala si ya kuwadhuru, ni mipango ya kuwapa tumaini katika siku zijazo. 12 Kisha mtaniita, na mtakuja na kuniomba, nami nitawasikiliza. 13 Mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote. 14 Nitaonekana kwenu,” asema Bwana, “nami nitawarudisha watu wenu waliotekwa. Nitawakusanya kutoka mataifa yote na mahali pote nilipokuwa nimewafukuzia, nami nitawarudisha mahali ambapo nilikuwa nimewatoa walipochukuliwa uhamishoni,” asema Bwana.
-
3 Wakati ninapoogopa,
nitakutumaini wewe.
4 Katika Mungu, ambaye neno lake ninalisifu,
katika Mungu ninatumaini; sitaogopa.
Mwanadamu apatikanaye na kufa,
atanitenda nini?
-
9 Bwana ni kimbilio la watu wanaoonewa,
ni ngome imara wakati wa shida.
10 Wote wanaolijua jina lako watakutumaini wewe,
kwa maana wewe Bwana,
hujawaacha kamwe wakutafutao.
-
8 “Kwa kuwa mawazo yangu si mawazo yenu,
wala njia zenu si njia zangu,”
asema Bwana.
9 “Kama vile mbingu zilivyo juu kuliko dunia,
ndivyo njia zangu zilivyo juu kuliko njia zenu
na mawazo yangu kuliko mawazo yenu.
10 Kama vile mvua na theluji
ishukavyo kutoka mbinguni,
nayo hairudi tena huko
bila kunywesha dunia
na kuichipusha na kuistawisha,
hivyo hutoa mbegu kwa mpanzi
na mkate kwa mlaji,
11 ndivyo lilivyo neno langu lile litokalo kinywani mwangu:
Halitanirudia tupu,
bali litatimiliza lile nililokusudia
na litafanikiwa katika kusudi lile nililolituma.
-
5 Hakuna mtu yeyote atakayeweza kushindana na wewe siku zote za maisha yako. Kama vile nilivyokuwa pamoja na Mose, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe, sitakuacha wala sitakupungukia.
6 “Uwe hodari na shujaa, kwa sababu wewe ndiwe utakayewaongoza watu hawa kuirithi nchi niliyowaapia baba zao kuwapa. 7 Uwe hodari na uwe na ushujaa mwingi. Uwe na bidii kutii sheria yote aliyokupa Mose mtumishi wangu, usiiache kwa kugeuka kuelekea kuume au kushoto, ili upate kufanikiwa popote uendako. 8 Usiache Kitabu hiki cha Sheria kiondoke kinywani mwako; yatafakari maneno yake usiku na mchana, ili upate kuwa mwangalifu kufanya kila kitu sawasawa na yote yaliyoandikwa ndani yake. Ndipo utakapofanikiwa na kisha utastawi. 9 Je, si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na shujaa. Usihofu wala usivunjike moyo, kwa kuwa Bwana Mungu wako atakuwa pamoja nawe kokote uendako.”
-
7 Bwana ni nguvu zangu na ngao yangu,
moyo wangu umemtumaini yeye,
nami nimesaidiwa.
Moyo wangu unarukaruka kwa furaha
nami nitamshukuru kwa wimbo.
-
25 “Kwa hiyo nawaambia, msisumbukie maisha yenu kwamba mtakula nini au mtakunywa nini; au msumbukie miili yenu kwamba mtavaa nini. Je, maisha si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi? 26 Waangalieni ndege wa angani; wao hawapandi wala hawavuni au kuweka ghalani, lakini Baba yenu wa mbinguni huwalisha. Je, ninyi si wa thamani zaidi kuliko hao ndege? 27 Ni nani miongoni mwenu ambaye kwa kujitaabisha kwake anaweza kujiongezea hata saa moja zaidi katika maisha yake?
28 “Nanyi kwa nini mnajitaabisha kwa ajili ya mavazi? Fikirini maua ya shambani yameavyo. Hayafanyi kazi wala hayafumi. 29 Lakini nawaambia, hata Solomoni katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo ya hayo maua. 30 Basi ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya shambani, ambayo leo yapo na kesho yanatupwa motoni, je, hatawavika ninyi vizuri zaidi, enyi wa imani haba? 31 Kwa hiyo msiwe na wasiwasi, mkisema, ‘Tutakula nini?’ au ‘Tutakunywa nini?’ au ‘Tutavaa nini?’ 32 Watu wasiomjua Mungu ndio wanaoshindania hayo, lakini Baba yenu wa mbinguni anafahamu kuwa mnahitaji haya yote. 33 Lakini utafuteni kwanza Ufalme wa Mungu na haki yake, na haya yote atawapa pia. 34 Kwa hiyo msiwe na wasiwasi kuhusu kesho, kwa sababu kesho itajitaabikia yenyewe. Yatosha kwa siku masumbufu yake.
-
16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. 17 Kwa maana Mungu hakumtuma Mwanawe kuuhukumu ulimwengu, bali kupitia kwake ulimwengu upate kuokolewa. 18 Yeyote amwaminiye hahukumiwi, lakini asiyeamini amekwisha kuhukumiwa, kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu.
-
2 Hakika Mungu ni wokovu wangu;
nitamtumaini wala sitaogopa.
Bwana, Bwana, ni nguvu zangu na wimbo wangu;
amekuwa wokovu wangu.”
-
19 Naye Mungu wangu atawajaza ninyi na kila mnachohitaji kwa kadiri ya utajiri wake katika utukufu ndani ya Kristo Yesu.
-
13 Nami bado nina tumaini hili:
nitauona wema wa Bwana
katika nchi ya walio hai.
14 Mngojee Bwana,
uwe hodari na mwenye moyo mkuu,
nawe, umngojee Bwana.
-
7 Wokovu wangu na heshima yangu viko kwa Mungu,
ndiye mwamba wangu wenye nguvu
na kimbilio langu.
8 Enyi watu, mtumainini yeye wakati wote,
miminieni mioyo yenu kwake,
kwa kuwa Mungu ni kimbilio letu.
-
10 Hivyo usiogope, kwa maana niko pamoja nawe;
usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako.
Nitakutia nguvu na kukusaidia;
nitakutegemeza kwa mkono wa kuume wa haki yangu.
11 “Wote walioona hasira dhidi yako
hakika wataaibika na kutahayarika,
wale wakupingao
watakuwa kama vile si kitu, na kuangamia.
12 Ingawa utawatafuta adui zako,
hutawaona.
Wale wanaopigana vita dhidi yako
watakuwa kama vile si kitu kabisa.
-
1 Yesu akawaambia, “Msifadhaike mioyoni mwenu, mnamwamini Mungu, niaminini na mimi pia. 2 Nyumbani kwa Baba yangu kuna makao mengi. Kama sivyo, ningeliwaambia. Naenda kuwaandalia makao. 3 Nami nikienda na kuwaandalia makao, nitarudi tena na kuwachukua mkae pamoja nami, ili mahali nilipo, nanyi mpate kuwepo.
-
7 Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi. Kwa kuwa kile apandacho mtu ndicho atakachovuna. 8 Apandaye kwa mwili, katika mwili wake atavuna uharibifu, lakini yeye apandaye katika Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele. 9 Hivyo, tusichoke katika kutenda mema, kwa kuwa tutavuna kwa wakati wake tusipokata tamaa. 10 Kwa hiyo, kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema, hasa wale wa jamaa ya waaminio.
-
23 Kama Bwana akipendezwa na njia ya mtu,
yeye huimarisha hatua zake,
24 ajapojikwaa, hataanguka,
kwa maana Bwana
humtegemeza kwa mkono wake.
-
1 Yeye akaaye mahali pa salama pake Yeye Aliye Juu Sana,
atadumu katika uvuli wake Mwenyezi.
2 Nitasema kumhusu Bwana, “Yeye ndiye kimbilio langu na ngome yangu,
Mungu wangu, ambaye ninamtumaini.”
-
6 Hakika hatatikisika kamwe,
mtu mwenye haki atakumbukwa milele.
7 Hataogopa habari mbaya,
moyo wake ni thabiti, ukimtegemea Bwana.
8 Moyo wake ni salama, hatakuwa na hofu,
mwishoni ataona ushindi dhidi ya adui zake.
-
8 Ni bora kumkimbilia Bwana
kuliko kumtumainia mwanadamu.
9 Ni bora kumkimbilia Bwana
kuliko kuwatumainia wakuu.
-
22 Yesu akawajibu, “Mwaminini Mungu. 23 Amin, nawaambia, mtu yeyote atakayeuambia mlima huu, ‘Ngʼoka ukatupwe baharini,’ wala asione shaka moyoni mwake, bali aamini kwamba hayo asemayo yametukia, atatimiziwa. 24 Kwa sababu hiyo nawaambia, yoyote mtakayoyaomba mkisali, aminini ya kwamba mmeyapokea, nayo yatakuwa yenu.
-
1 Kwa hiyo, ndugu zangu, nawasihi kwa rehema zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu na inayompendeza Mungu, hii ndiyo ibada yenu yenye maana. 2 Msifuatishe tena mfano wa ulimwengu huu, bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu. Ndipo mtaweza kuonja na kuhakikisha ni nini mapenzi ya Mungu yaliyo mema, yanayopendeza machoni pake na ukamilifu.
-
5 Yalindeni maisha yenu msiwe na tabia ya kupenda fedha, bali mridhike na vile mlivyo navyo, kwa sababu Mungu amesema,
“Kamwe sitakuacha,
wala sitakupungukia.”
-
1 Wapenzi, huu ndio waraka wangu wa pili ninaowaandikia. Katika nyaraka hizi mbili ninajaribu kuziamsha nia zenu safi kwa mawazo makamilifu. 2 Nataka ninyi mkumbuke maneno yaliyosemwa zamani na manabii watakatifu na ile amri ya Bwana na Mwokozi mliyopewa kupitia kwa mitume wenu.
3 Kwanza kabisa, ni lazima mfahamu ya kwamba siku za mwisho watakuja watu wenye dhihaka, wakidhihaki na kuzifuata tamaa zao mbaya. 4 Watasema, “Iko wapi ile ahadi ya kuja kwake? Tangu baba zetu walipofariki, kila kitu kinaendelea kama kilivyokuwa tangu mwanzo wa kuumbwa.” 5 Lakini wao kwa makusudi hupuuza ukweli huu, ya kwamba kwa neno la Mungu mbingu zilikuwepo tangu zamani, nayo dunia ilifanyizwa kutoka ndani ya maji na kwa maji. 6 Ulimwengu wa wakati ule uligharikishwa kwa hayo maji na kuangamizwa. 7 Lakini kwa neno lilo hilo, mbingu za sasa na dunia zimewekwa akiba kwa ajili ya moto, zikihifadhiwa hadi siku ile ya hukumu na ya kuangamizwa kwa watu wasiomcha Mungu.
8 Lakini wapenzi, msisahau neno hili: kwamba kwa Bwana, siku moja ni kama miaka elfu, na miaka elfu ni kama siku moja. 9 Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama watu wengine wanavyokudhani kukawia. Badala yake, yeye anawavumilia ninyi, maana hataki mtu yeyote aangamie, bali kila mtu afikilie toba.
10 Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwizi. Ndipo mbingu zitatoweka kwa kishindo kikuu; navyo vitu vya asili vitateketezwa kwa moto, nayo dunia na kila kitu kilichomo ndani yake kitaunguzwa.
11 Kwa kuwa vitu vyote vitaharibiwa namna hii, je, ninyi imewapasa kuwa watu wa namna gani? Inawapasa kuishi maisha matakatifu na ya kumcha Mungu, 12 mkingojea na kuhimiza kuja kwa hiyo siku ya Mungu. Siku hiyo italeta mbingu kuchomwa moto na kutoweka, na vitu vya asili vitayeyuka kwa moto. 13 Lakini kufuatana na ahadi yake, sisi tunatazamia mbingu mpya na dunia mpya, ambayo haki hukaa ndani yake.
-
11 Huu ndio ushuhuda: kwamba Mungu ametupa uzima wa milele, nao huo uzima umo katika Mwanawe. 12 Aliye naye Mwana wa Mungu anao uzima, yeye asiye na Mwana wa Mungu hana uzima.
13 Nawaandikia mambo haya ninyi mnaoliamini Jina la Mwana wa Mungu ili mpate kujua ya kuwa mnao uzima wa milele. 14 Huu ndio ujasiri tulio nao tunapomkaribia Mungu, kwamba kama tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia. 15 Nasi kama tunajua atusikia, lolote tuombalo, tunajua ya kwamba tumekwisha kupata zile haja tulizomwomba.
-
Sehemu Ya Tano
1 Ndipo Ayubu akamjibu Bwana:
2 “Ninajua ya kuwa unaweza kufanya mambo yote,
wala hakuna mpango wako unaoweza kuzuilika.
3 Uliuliza, ‘Ni nani huyu afichaye mashauri yangu bila maarifa?’
Hakika nilisema juu ya mambo niliyokuwa siyaelewi,
mambo ya ajabu mno kwangu mimi kuyajua.
4 “Ulisema, ‘Sikiliza sasa, nami nitanena;
nitakuuliza swali, nawe yakupasa kunijibu.’
5 Masikio yangu yalikuwa yamesikia habari zako,
lakini sasa macho yangu yamekuona.
6 Kwa hiyo najidharau mwenyewe,
na kutubu katika mavumbi na majivu.”
-
18 Bwana yu karibu na wote wamwitao,
karibu na wote wamwitao kwa uaminifu.
-
20 Yeyote anayekubali mafundisho hustawi,
tena amebarikiwa yeye anayemtumaini Bwana.
21 Wenye hekima moyoni huitwa wenye ufahamu,
na maneno ya kupendeza huchochea mafundisho.
22 Ufahamu ni chemchemi ya uzima kwa wale walio nao,
bali upumbavu huleta adhabu kwa wapumbavu.
-
25 Kuwaogopa watu huwa ni mtego,
bali yeyote amtumainiaye Bwana atakuwa salama.
-
28 Je wewe, hufahamu?
Je wewe, hujasikia?
Bwana ni Mungu wa milele,
Muumba wa miisho ya dunia.
Hatachoka wala kulegea,
wala hakuna hata mmoja
awezaye kuupima ufahamu wake.
29 Huwapa nguvu waliolegea
na huongeza nguvu za wadhaifu.
30 Hata vijana huchoka na kulegea,
nao vijana wanaume hujikwaa na kuanguka,
31 bali wale wamtumainio Bwana
atafanya upya nguvu zao.
Watapaa juu kwa mbawa kama tai;
watapiga mbio wala hawatachoka,
watatembea kwa miguu wala hawatazimia.
-
1 Lakini sasa hili ndilo asemalo Bwana,
yeye aliyekuumba, ee Yakobo,
yeye aliyekuhuluku, ee Israeli:
“Usiogope kwa maana nimekukomboa,
nimekuita wewe kwa jina lako, wewe u wangu.
2 Unapopita kwenye maji makuu,
nitakuwa pamoja nawe,
unapopita katika mito ya maji,
hayatakugharikisha.
Utakapopita katika moto,
hutaungua,
miali ya moto haitakuunguza.
3 Kwa kuwa Mimi ndimi Bwana, Mungu wako,
yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, Mwokozi wako.
Ninaitoa Misri kuwa fidia yako,
Kushi na Seba badala yako.
4 Kwa kuwa wewe ni wa thamani na wa kuheshimiwa machoni pangu,
nami kwa kuwa ninakupenda,
nitatoa watu badala yako
na mataifa badala ya maisha yako.
5 Usiogope, kwa kuwa mimi nipo pamoja nawe,
nitawaleta watoto wako kutoka mashariki,
na kukukusanya kutoka magharibi.
6 Nitaiambia kaskazini, ‘Watoe!’
nayo kusini, ‘Usiwazuie.’
Walete wana wangu kutoka mbali,
na binti zangu kutoka miisho ya dunia:
-
5 “Kabla sijakuumba ndani ya tumbo la mama yako, nilikujua;
kabla hujazaliwa nilikutenga kwa kazi maalum;
nilikuweka uwe nabii kwa mataifa.”
6 Nami nikasema, “Aa, Bwana Mwenyezi, sijui kusema, kwani mimi ni mtoto mdogo tu.”
7 Lakini Bwana akaniambia, “Usiseme, ‘Mimi ni mtoto mdogo tu.’ Utaenda popote nitakapokutuma na kunena lolote nitakalokuagiza. 8 Usiwaogope, kwa maana niko pamoja nawe nikuokoe,” asema Bwana.
-
18 Yesu akawajia na kusema, “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. 19 Kwa sababu hii, enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, 20 nanyi wafundisheni kuyashika mambo yote niliyowaamuru ninyi. Hakika mimi niko pamoja nanyi siku zote, hadi mwisho wa nyakati.”
-
26 Lakini huyo Msaidizi, yaani, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwenu kwa Jina langu, atawafundisha mambo yote na kuwakumbusha yote niliyowaambia.
-
5 Mose anaandika kuhusu haki ile itokanayo na sheria, kwamba, “Mtu atendaye matendo hayo ataishi kwa hayo.” 6 Lakini ile haki itokanayo na imani husema hivi: “Usiseme moyoni mwako, ‘Ni nani atakayepanda mbinguni?’ ” (yaani ili kumleta Kristo chini) 7 “au ‘Ni nani atashuka kwenda kuzimu?’ ” (yaani ili kumleta Kristo kutoka kwa wafu.) 8 Lakini andiko lasemaje? “Lile neno liko karibu nawe, liko kinywani mwako na moyoni mwako,” yaani, lile neno la imani tunalolihubiri. 9 Kwa sababu kama ukikiri kwa kinywa chako kwamba “Yesu ni Bwana,” na kuamini moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, utaokoka. 10 Kwa maana kwa moyo mtu huamini na hivyo kuhesabiwa haki, tena kwa kinywa mtu hukiri na hivyo kupata wokovu. 11 Kama yasemavyo Maandiko, “Yeyote amwaminiye hataaibika kamwe.” 12 Kwa maana hakuna tofauti kati ya Myahudi na Myunani, yeye ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao. 13 Kwa maana, “Kila mtu atakayeliitia Jina la Bwana, ataokolewa.”
14 Lakini watamwitaje yeye ambaye hawajamwamini? Nao watawezaje kumwamini yeye ambaye hawajamsikia? Tena watamsikiaje bila mtu kuwahubiria? 15 Nao watahubirije wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, “Tazama jinsi ilivyo mizuri miguu yao wale wanaohubiri habari njema!”
16 Lakini si wote waliotii Habari Njema. Kwa maana Isaya asema, “Bwana, ni nani aliyeamini ujumbe wetu?” 17 Basi, imani chanzo chake ni kusikia, na kusikia huja kwa neno la Kristo.
-
13 Mungu wa tumaini awajaze ninyi furaha yote na amani katika kumwamini, ili mpate kujawa na tumaini tele kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.
-
6 Kwa hiyo siku zote tunalo tumaini, hata ingawa tunajua kwamba wakati tukiwa katika mwili huu, tuko mbali na Bwana, 7 kwa maana twaenenda kwa imani wala si kwa kuona. 8 Naam, tunalo tumaini na ingekuwa bora zaidi kuuacha mwili huu na kwenda kukaa na Bwana. 9 Kwa hiyo, kama tuko katika mwili huu au tuko mbali nao, lengo letu ni kumpendeza Bwana. 10 Kwa kuwa sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mmoja apate kulipwa kwa ajili ya yale ambayo yametendwa katika mwili wake, yakiwa mema au mabaya.
-
1 Kwa habari zenu, mlikuwa wafu katika makosa na dhambi zenu, 2 ambazo mlizitenda mlipofuatisha namna ya ulimwengu huu na za yule mtawala wa ufalme wa anga, yule roho atendaye kazi sasa ndani ya wale wasiotii. 3 Sisi sote pia tuliishi katikati yao hapo zamani, tukitimiza tamaa za asili yetu ya dhambi na kufuata tamaa zake na mawazo yake. Nasi kwa asili tulikuwa wana wa ghadhabu, kama mtu mwingine yeyote. 4 Lakini Mungu kwa upendo wake mwingi kwetu sisi, ambaye ni mwingi wa rehema, 5 hata tulipokuwa wafu kwa ajili ya makosa yetu, alitufanya tuwe hai pamoja na Kristo Yesu, yaani, mmeokolewa kwa neema. 6 Mungu alitufufua pamoja na Kristo na kutuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho katika Kristo Yesu, 7 ili katika ule ulimwengu ujao apate kuonyesha wingi wa neema yake isiyopimika, iliyodhihirishwa kwetu kwa wema wake ndani ya Kristo Yesu. 8 Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani, wala si kwa matendo yenu mema. Hii ni zawadi kutoka kwa Mungu, 9 si kwa matendo, ili mtu yeyote asije akajisifu. 10 Kwa maana sisi ni kazi ya mikono ya Mungu, tulioumbwa katika Kristo Yesu, ili tupate kutenda matendo mema, ambayo Mungu alitangulia kuyaandaa tupate kuishi katika hayo.
-
6 Msijisumbue kwa jambo lolote, bali katika kila jambo kwa kuomba na kusihi pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. 7 Nayo amani ya Mungu, inayopita fahamu zote, itailinda mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.
-
16 Furahini siku zote; 17 ombeni bila kukoma; 18 shukuruni kwa kila jambo, kwa maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu kwa ajili yenu katika Kristo Yesu.
-
5 Kama mtu yeyote miongoni mwenu amepungukiwa na hekima na amwombe Mungu, yeye awapaye watu wote kwa ukarimu wala hana kinyongo, naye atapewa. 6 Lakini anapoomba, lazima aamini wala asiwe na shaka, kwa sababu mtu aliye na shaka ni kama wimbi la bahari, lililochukuliwa na upepo na kutupwa huku na huku. 7 Mtu kama huyo asidhani ya kuwa atapata kitu chochote kutoka kwa Bwana. 8 Yeye ni mtu mwenye nia mbili, mwenye kusitasita katika njia zake zote.
-
Zaburi ya Daudi.
1 Kwako wewe, Ee Bwana,
nainua nafsi yangu,
2 ni wewe ninayekutumainia,
Ee Mungu wangu.
Usiniache niaibike,
wala usiache adui zangu wakanishinda.
3 Kamwe hakuna hata mmoja anayekutegemea
atakayeaibishwa,
bali wataaibishwa
wafanyao hila bila sababu.
-
10 “Tulieni, mjue ya kwamba mimi ndimi Mungu;
nitatukuzwa katikati ya mataifa,
nitatukuzwa katika dunia.”
-
8 Asubuhi uniletee neno la upendo wako usiokoma,
kwa kuwa nimeweka tumaini langu kwako.
Nionyeshe njia nitakayoiendea,
kwa kuwa kwako nainua nafsi yangu.
-
13 Ufalme wako ni ufalme wa milele,
mamlaka yako hudumu vizazi vyote.
Bwana ni mwaminifu kwa ahadi zake zote
na mwenye upendo kwa vyote alivyovifanya.
14 Bwana huwategemeza wote waangukao,
na huwainua wote waliolemewa na mizigo yao.
15 Macho yao wote yanakutazama wewe,
nawe huwapa chakula chao wakati wake.
-
9 Kumbukeni mambo yaliyopita, yale ya zamani za kale;
mimi ndimi Mungu, wala hakuna mwingine;
mimi ndimi Mungu,
wala hakuna mwingine aliye kama mimi.
10 Ni mimi nitangazaye mwisho tangu mwanzo,
naam, tangu zamani za kale,
mambo ambayo hayajatendeka.
Ninasema: Kusudi langu ndilo litakalosimama,
nami nitatenda mapenzi yangu yote.
11 Kutoka mashariki ninaita ndege awindaye;
kutoka nchi ya mbali,
mtu atakayetimiza kusudi langu.
Lile ambalo nimelisema, ndilo nitakalolitimiza;
lile nililolipanga, ndilo nitakalolitenda.
-
9 “Hivi basi, ndivyo iwapasavyo kuomba:
“ ‘Baba yetu uliye mbinguni,
Jina lako litukuzwe.
10 Ufalme wako uje.
Mapenzi yako yafanyike
hapa duniani kama huko mbinguni.
11 Utupatie riziki yetu
ya kila siku.
12 Utusamehe deni zetu,
kama sisi nasi tulivyokwisha
kuwasamehe wadeni wetu.
13 Usitutie majaribuni,
bali utuokoe kutoka kwa yule mwovu
[kwa kuwa Ufalme ni wako, na nguvu,
na utukufu, hata milele. Amen].’
-
32 Ikiwa Mungu hakumhurumia Mwanawe, bali alimtoa kwa ajili yetu sote, atakosaje basi kutupatia vitu vyote kwa ukarimu pamoja naye? 33 Ni nani atakayewashtaki wale ambao Mungu amewateua? Ni Mungu mwenyewe ndiye mwenye kuwahesabia haki. 34 Ni nani basi atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu aliyekufa, naam, zaidi ya hayo, aliyefufuliwa kutoka kwa wafu, yuko mkono wa kuume wa Mungu, naye pia anatuombea. 35 Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je, ni shida au taabu au mateso au njaa au uchi au hatari au upanga? 36 Kama ilivyoandikwa:
“Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa;
tumehesabiwa kama kondoo wa kuchinjwa.”
37 Lakini katika mambo haya yote tunashinda, naam na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. 38 Kwa maana nimekwisha kujua kwa hakika ya kuwa sio mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuja, wala wenye uwezo, 39 wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kingine chochote zitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu, Bwana wetu.
-
3 Ahimidiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki sisi kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho ndani ya Kristo. 4 Kwa maana alituchagua katika yeye kabla ya kuumbwa ulimwengu ili tuwe watakatifu na bila lawama mbele zake. Kwa upendo 5 alitangulia kutuchagua tuwe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo kwa furaha yake na mapenzi yake mwenyewe. 6 Kwa hiyo tunamsifu Mungu kwa huruma zake kuu alizotumiminia sisi katika Mwanawe Mpendwa. 7 Ndani yake tunao ukombozi kwa njia ya damu yake, yaani, msamaha wa dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake 8 aliyotumiminia kwa wingi, kwa hekima yote na maarifa yote. 9 Naye alitujulisha siri ya mapenzi yake sawasawa na uradhi wa mapenzi yake, ambayo alikusudia katika Kristo, 10 ili yapate kutimizwa wakati mkamilifu utakapowadia, yaani, kuvitia vitu vyote vya mbinguni na vya duniani pamoja, chini ya kiongozi mmoja, ndiye Kristo.
11 Katika Kristo sisi nasi tumepata urithi, tukisha kuchaguliwa sawasawa na kusudi la Mungu, yeye ambaye hufanya mambo yote kulingana na kusudi la mapenzi yake, 12 ili kwamba, sisi tuliokuwa wa kwanza kuweka tumaini katika Kristo, tupate kuishi kwa sifa ya utukufu wake. 13 Ninyi pia mliingia ndani ya Kristo mliposikia Neno la kweli, Injili ya wokovu wenu. Mkiisha kuamini, ndani yake mlitiwa muhuri, yaani, Roho Mtakatifu mliyeahidiwa, 14 yeye ambaye ni amana yetu akituhakikishia urithi wetu hadi ukombozi wa wale walio milki ya Mungu kwa sifa ya utukufu wake.
-
11 Ndiye aliweka wengine kuwa mitume, wengine kuwa manabii, wengine kuwa wainjilisti, wengine kuwa wachungaji na walimu, 12 kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu kwa ajili ya kazi za huduma, ili kwamba mwili wa Kristo upate kujengwa 13 mpaka sote tutakapoufikia umoja katika imani na katika kumjua sana Mwana wa Mungu na kuwa watu wazima kwa kufikia kimo cha ukamilifu wa Kristo.
14 Ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwatupwa huku na huku na kuchukuliwa na kila upepo wa mafundisho kwa hila za watu, kwa ujanja, kwa kufuata njia zao za udanganyifu. 15 Badala yake, tukiambiana kweli kwa upendo, katika mambo yote tukue, hata tumfikie yeye aliye kichwa, yaani, Kristo. 16 Kutoka kwake, mwili wote ukiwa umeungamanishwa na kushikamanishwa pamoja kwa msaada wa kila kiungo, hukua na kujijenga wenyewe katika upendo, wakati kila kiungo kinafanya kazi yake.
-
6 Nina hakika kwamba yeye aliyeianza kazi njema mioyoni mwenu, ataiendeleza na kuikamilisha hata siku ya Kristo Yesu.
-
11 Sisemi hivyo kwa vile nina mahitaji, la! Kwa maana nimejifunza kuridhika katika hali yoyote. 12 Ninajua kupungukiwa, pia ninajua kuwa na vingi. Nimejifunza siri ya kuridhika katika kila hali, wakati wa kushiba na wakati wa kuona njaa, wakati wa kuwa na vingi na wakati wa kupungukiwa. 13 Naweza kuyafanya mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.
-
6 Kwa hiyo tunaweza kusema kwa ujasiri,
“Bwana ni msaada wangu; sitaogopa.
Mwanadamu anaweza kunitenda nini?”
-
6 Basi, nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake. 7 Mtwikeni yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana na mambo yenu.
8 Mwe na kiasi na kukesha, maana adui yenu ibilisi huzungukazunguka kama simba angurumaye akitafuta mtu ili apate kummeza. 9 Mpingeni, mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kwamba mateso kama hayo yanawapata ndugu zenu pote duniani.
10 Nanyi mkiisha kuteswa kwa kitambo kidogo, Mungu wa neema yote, aliyewaita kuingia katika utukufu wake wa milele ndani ya Kristo, yeye mwenyewe atawarejesha na kuwatia nguvu, akiwaimarisha na kuwathibitisha. 11 Uweza una yeye milele na milele. Amen.
Shows Read in context, Share and Copy.