41 Bible Verses About Free Will

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Free Will
  1. 3 Ahimidiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki sisi kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho ndani ya Kristo. 4 Kwa maana alituchagua katika yeye kabla ya kuumbwa ulimwengu ili tuwe watakatifu na bila lawama mbele zake. Kwa upendo 5 alitangulia kutuchagua tuwe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo kwa furaha yake na mapenzi yake mwenyewe. 6 Kwa hiyo tunamsifu Mungu kwa huruma zake kuu alizotumiminia sisi katika Mwanawe Mpendwa. 7 Ndani yake tunao ukombozi kwa njia ya damu yake, yaani, msamaha wa dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake 8 aliyotumiminia kwa wingi, kwa hekima yote na maarifa yote. 9 Naye alitujulisha siri ya mapenzi yake sawasawa na uradhi wa mapenzi yake, ambayo alikusudia katika Kristo, 10 ili yapate kutimizwa wakati mkamilifu utakapowadia, yaani, kuvitia vitu vyote vya mbinguni na vya duniani pamoja, chini ya kiongozi mmoja, ndiye Kristo.

    11 Katika Kristo sisi nasi tumepata urithi, tukisha kuchaguliwa sawasawa na kusudi la Mungu, yeye ambaye hufanya mambo yote kulingana na kusudi la mapenzi yake, 12 ili kwamba, sisi tuliokuwa wa kwanza kuweka tumaini katika Kristo, tupate kuishi kwa sifa ya utukufu wake.

  2. 15 Tazama, naweka mbele yako leo uzima na mafanikio, mauti na maangamizo. 16 Ninakuamuru leo kwamba umpende Bwana Mungu wako, utembee katika njia zake, na kutunza maagizo yake, amri na sheria zake; ndipo utakapoishi na kuongezeka, naye Bwana Mungu wako atakubariki katika nchi unayoingia kuimiliki.

    17 Lakini kama moyo wako ukigeukia mbali ukawa huna utii, kama umevutwa kuisujudia miungu mingine na kuiabudu, 18 nakutangazia leo hii kwamba hakika utaangamizwa. Hutaishi maisha marefu katika nchi unayovuka Yordani kuiingia na kuimiliki.

    19 Leo ninaziita mbingu na nchi kama mashahidi dhidi yako kwamba nimeweka mbele yako uzima na mauti, baraka na laana. Basi sasa chagueni uzima, ili wewe na watoto wako mpate kuishi, 20 na ili upate kumpenda Bwana Mungu wako, uisikilize sauti yake na kuambatana naye. Kwa kuwa Bwana ndiye uzima wako, na atakupa wingi wa siku ili upate kuishi katika nchi aliyoapa kuwapa baba zako Abrahamu, Isaki na Yakobo.

  3. 16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. 17 Kwa maana Mungu hakumtuma Mwanawe kuuhukumu ulimwengu, bali kupitia kwake ulimwengu upate kuokolewa. 18 Yeyote amwaminiye hahukumiwi, lakini asiyeamini amekwisha kuhukumiwa, kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu. 19 Hii ndiyo hukumu kwamba: Nuru imekuja ulimwenguni, nao watu wakapenda giza kuliko nuru kwa sababu matendo yao ni maovu. 20 Kwa kuwa kila atendaye maovu huchukia nuru, wala haji kwenye nuru ili matendo yake maovu yasifichuliwe. 21 Lakini yule aishiye kwa ukweli huja kwenye nuru, ili ionekane wazi kwamba matendo yake yametendeka katika Mungu.”

  4. 10 Wala si hivyo tu, bali pia watoto aliowazaa Rebeka walikuwa na baba huyo huyo mmoja, yaani, baba yetu Isaki. 11 Lakini, hata kabla hao mapacha hawajazaliwa au kufanya jambo lolote jema au baya, ili kwamba kusudi la Mungu la kuchagua lipate kusimama, 12 si kwa matendo, bali kwa yeye mwenye kuita, Rebeka aliambiwa, “Yule mkubwa atamtumikia yule mdogo.” 13 Kama vile ilivyoandikwa, “Nimempenda Yakobo, lakini nimemchukia Esau.”

    14 Tuseme nini basi? Je, Mungu ni dhalimu? La, hasha! 15 Kwa maana Mungu alimwambia Mose,

    “Nitamrehemu yeye nimrehemuye,

    na pia nitamhurumia yeye nimhurumiaye.”

    16 Kwa hiyo haitegemei kutaka kwa mwanadamu au jitihada, bali hutegemea huruma ya Mungu. 17 Kwa maana Maandiko yamwambia Farao, “Nilikuinua kwa kusudi hili hasa, ili nipate kuonyesha uweza wangu juu yako, na ili Jina langu lipate kutangazwa duniani yote.”

    18 Kwa hiyo basi, Mungu humhurumia yeye atakaye kumhurumia na humfanya mgumu yeye atakaye kumfanya mgumu.

    19 Basi mtaniambia, “Kama ni hivyo, kwa nini basi bado Mungu anatulaumu? Kwa maana ni nani awezaye kupinga mapenzi yake?” 20 Lakini, ewe mwanadamu, u nani wewe ushindane na Mungu? “Je, kilichoumbwa chaweza kumwambia yeye aliyekiumba, ‘Kwa nini umeniumba hivi?’ ” 21 Je, mfinyanzi hana haki ya kufinyanga kutoka bonge moja vyombo vya udongo, vingine kwa matumizi ya heshima na vingine kwa matumizi ya kawaida?

    22 Iweje basi, kama Mungu kwa kutaka kuonyesha ghadhabu yake na kufanya uweza wake ujulikane, amevumilia kwa uvumilivu mwingi vile vyombo vya ghadhabu vilivyoandaliwa kwa uharibifu? 23 Iweje basi, kama yeye alitenda hivi ili kufanya wingi wa utukufu wake ujulikane kwa vile vyombo vya rehema yake, alivyotangulia kuvitengeneza kwa ajili ya utukufu wake, 24 yaani pamoja na sisi, ambao pia alituita, si kutoka kwa Wayahudi peke yao, bali pia kutoka kwa watu wa Mataifa?

  5. 44 Hakuna mtu awezaye kuja kwangu kama asipovutwa na Baba aliyenituma, nami nitamfufua siku ya mwisho.

  6. 5 Mose anaandika kuhusu haki ile itokanayo na sheria, kwamba, “Mtu atendaye matendo hayo ataishi kwa hayo.” 6 Lakini ile haki itokanayo na imani husema hivi: “Usiseme moyoni mwako, ‘Ni nani atakayepanda mbinguni?’ ” (yaani ili kumleta Kristo chini) 7 “au ‘Ni nani atashuka kwenda kuzimu?’ ” (yaani ili kumleta Kristo kutoka kwa wafu.) 8 Lakini andiko lasemaje? “Lile neno liko karibu nawe, liko kinywani mwako na moyoni mwako,” yaani, lile neno la imani tunalolihubiri. 9 Kwa sababu kama ukikiri kwa kinywa chako kwamba “Yesu ni Bwana,” na kuamini moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, utaokoka. 10 Kwa maana kwa moyo mtu huamini na hivyo kuhesabiwa haki, tena kwa kinywa mtu hukiri na hivyo kupata wokovu. 11 Kama yasemavyo Maandiko, “Yeyote amwaminiye hataaibika kamwe.” 12 Kwa maana hakuna tofauti kati ya Myahudi na Myunani, yeye ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao. 13 Kwa maana, “Kila mtu atakayeliitia Jina la Bwana, ataokolewa.”

    14 Lakini watamwitaje yeye ambaye hawajamwamini? Nao watawezaje kumwamini yeye ambaye hawajamsikia? Tena watamsikiaje bila mtu kuwahubiria? 15 Nao watahubirije wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, “Tazama jinsi ilivyo mizuri miguu yao wale wanaohubiri habari njema!”

    16 Lakini si wote waliotii Habari Njema. Kwa maana Isaya asema, “Bwana, ni nani aliyeamini ujumbe wetu?” 17 Basi, imani chanzo chake ni kusikia, na kusikia huja kwa neno la Kristo.

  7. 13 Ndugu zangu, ninyi mliitwa ili mwe huru, hivyo msitumie uhuru wenu kama fursa ya kufuata tamaa za mwili, bali tumikianeni ninyi kwa ninyi kwa upendo. 14 Kwa maana sheria yote hukamilika katika amri moja: “Mpende jirani yako kama nafsi yako.” 15 Kama mkiumana na kutafunana, angalieni, msije mkaangamizana.

    16 Kwa hiyo nasema, enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili. 17 Kwa maana mwili hutamani yale yaliyo kinyume na Roho, naye Roho hutamani yale yaliyo kinyume na mwili. Roho na mwili hupingana na kwa sababu hiyo hamwezi kufanya mnayotaka.

  8. 12 Bali wote waliompokea, aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake. 13 Hawa ndio wasiozaliwa kwa damu, wala kwa mapenzi ya mwili au kwa mapenzi ya mtu, bali kwa mapenzi ya Mungu.

  9. 20 Kwa maana tangu kuumbwa kwa ulimwengu, asili ya Mungu asiyeonekana kwa macho, yaani, uweza wake wa milele na asili yake ya Uungu, imeonekana waziwazi, ikitambuliwa kutokana na yale aliyoyafanya ili wanadamu wasiwe na udhuru.

    21 Kwa maana ingawa walimjua Mungu, hawakumtukuza yeye kama ndiye Mungu wala hawakumshukuru, bali fikira zao zimekuwa batili na mioyo yao ya ujinga ikatiwa giza. 22 Ingawa walijidai kuwa wenye hekima, wakawa wajinga 23 na kubadili utukufu wa Mungu aishiye milele kwa sanamu zilizofanywa zifanane na mwanadamu ambaye hufa, na mfano wa ndege, wanyama na viumbe vitambaavyo.

    24 Kwa hiyo, Mungu akawaacha wazifuate tamaa mbaya za mioyo yao katika uasherati, hata wakavunjiana heshima miili yao wao kwa wao. 25 Kwa sababu waliibadili kweli ya Mungu kuwa uongo, wakaabudu na kutumikia kiumbe badala ya Muumba, ahimidiwaye milele! Amen.

  10. 15 Bwana Mungu akamchukua huyo mtu, akamweka kwenye Bustani ya Edeni ailime na kuitunza. 16 Bwana Mungu akamwagiza huyo mtu, akamwambia, “Uko huru kula matunda ya mti wowote katika bustani, 17 lakini kamwe usile matunda ya mti wa kujua mema na mabaya, kwa maana siku utakapokula matunda yake, hakika utakufa.”

  11. 9 Moyo wa mtu huifikiri njia yake,

    bali Bwana huelekeza hatua zake.

  12. 16 Je, hamjui kwamba mnapojitoa kwa mtu yeyote kama watumwa watiifu, ninyi ni watumwa wa yule mnayemtii, aidha watumwa wa dhambi, ambayo matokeo yake ni mauti, au watumwa wa utii ambao matokeo yake ni haki? 17 Lakini Mungu ashukuriwe kwa kuwa ninyi ambao kwanza mlikuwa watumwa wa dhambi, mmekuwa watii kutoka moyoni kwa mafundisho mliyopewa. 18 Nanyi, mkiisha kuwekwa huru mbali na dhambi, mmekuwa watumwa wa haki.

    19 Ninasema kwa namna ya kibinadamu kwa sababu ya udhaifu wenu wa hali ya asili. Kama vile mlivyokuwa mkivitoa viungo vya miili yenu kama watumwa wa mambo machafu na uovu uliokuwa ukiongezeka zaidi, hivyo sasa vitoeni viungo vyenu kama watumwa wa haki inayowaelekeza mpate kutakaswa. 20 Mlipokuwa watumwa wa dhambi, mlikuwa hamtawaliwi na haki.

  13. 5 Kwa maana wale wanaoishi kwa kuufuata mwili huziweka nia zao katika vitu vya mwili, lakini wale wanaoishi kwa kufuata Roho, huziweka nia zao katika mambo ya Roho. 6 Kwa maana kuwa na nia ya mwili ni mauti, bali kuwa na nia inayoongozwa na Roho ni uzima na amani. 7 Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui na Mungu, kwa maana haiitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii. 8 Wale wanaotawaliwa na mwili, hawawezi kumpendeza Mungu.

  14. 14 “Sasa basi mcheni Bwana na kumtumikia kwa uaminifu wote. Itupeni mbali miungu ambayo baba zenu waliiabudu huko ngʼambo ya Mto Frati na huko Misri, nanyi mtumikieni Bwana. 15 Lakini msipoona vyema kumtumikia Bwana, chagueni hivi leo mtakayemtumikia, kama ni miungu ile ambayo baba zenu waliitumikia ngʼambo Frati, au miungu ya Waamori, ambao mnakaa katika nchi yao. Lakini mimi na nyumba yangu, tutamtumikia Bwana.”

  15. 28 Nasi tunajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hutenda kazi pamoja na wote wampendao, katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. 29 Maana wale Mungu aliowajua tangu mwanzo, pia aliwachagua tangu mwanzo, wapate kufanana na mfano wa Mwanawe, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi.

  16. 22 Zikimbie tamaa mbaya za ujana, ufuate haki, imani, upendo na amani pamoja na wale wamwitao Bwana kwa moyo safi. 23 Jiepushe na mabishano ya kipumbavu na yasiyo na maana, kwa kuwa wajua ya kwamba hayo huzaa magomvi. 24 Tena haimpasi mtumishi wa Bwana kuwa mgomvi, bali inampasa awe mwema kwa kila mtu, awezaye kufundisha, tena mvumilivu. 25 Inampasa kuwaonya kwa upole wale wanaopingana naye, kwa matumaini kwamba Mungu atawajalia kutubu na kuijua kweli, 26 ili fahamu zao ziwarudie tena, nao waponyoke katika mtego wa ibilisi ambaye amewateka wapate kufanya mapenzi yake.

  17. 9 Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama watu wengine wanavyokudhani kukawia. Badala yake, yeye anawavumilia ninyi, maana hataki mtu yeyote aangamie, bali kila mtu afikilie toba.

  18. 8 “Kwa kuwa mawazo yangu si mawazo yenu,

    wala njia zenu si njia zangu,”

    asema Bwana.

    9 “Kama vile mbingu zilivyo juu kuliko dunia,

    ndivyo njia zangu zilivyo juu kuliko njia zenu

    na mawazo yangu kuliko mawazo yenu.

  19. 27 Ni kweli Herode na Pontio Pilato pamoja na watu wa Mataifa na Waisraeli, walikusanyika katika mji huu dhidi ya mwanao mtakatifu Yesu uliyemtia mafuta. 28 Wao wakafanya yale ambayo uweza wako na mapenzi yako yalikuwa yamekusudia yatokee tangu zamani.

  20. 17 Roho na bibi arusi wanasema, “Njoo!” Naye asikiaye na aseme, “Njoo!” Yeyote mwenye kiu na aje, na kila anayetaka na anywe maji ya uzima bure.

  21. 21 Bwana akamwambia Mose, “Utakaporudi Misri, hakikisha kwamba utafanya mbele ya Farao maajabu yote niliyokupa uwezo wa kuyafanya. Lakini nitafanya moyo wake kuwa mgumu ili kwamba asiwaruhusu watu waende.

  22. 16 Si ninyi mlionichagua, bali mimi ndiye niliyewachagua ninyi na kuwaweka mwende mkazae matunda, na matunda yenu yapate kudumu. Ili nalo lolote mtakalomwomba Baba katika Jina langu, awape ninyi.

  23. 48 Watu wa Mataifa waliposikia haya wakafurahi na kulitukuza neno la Bwana; nao wote waliokuwa wamekusudiwa uzima wa milele wakaamini.

    49 Neno la Bwana likaenea katika eneo lile lote.

  24. 10 Kwa kuwa sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mmoja apate kulipwa kwa ajili ya yale ambayo yametendwa katika mwili wake, yakiwa mema au mabaya.

  25. 1 Awali ya yote, nasihi kwamba dua, sala, maombezi na shukrani zifanyike kwa ajili ya watu wote: 2 kwa ajili ya wafalme na wale wote wenye mamlaka, ili tupate kuishi kwa amani na utulivu, katika uchaji wote wa Mungu na utakatifu. 3 Jambo hili ni jema, tena linapendeza machoni pa Mungu Mwokozi wetu, 4 anayetaka watu wote waokolewe na wafikie kuijua kweli. 5 Kwa maana kuna Mungu mmoja na mpatanishi mmoja kati ya Mungu na wanadamu, yaani mwanadamu Kristo Yesu, 6 aliyejitoa mwenyewe kuwa fidia kwa ajili ya wanadamu wote: jambo hili lilishuhudiwa kwa wakati wake ufaao.

  26. 12 Heri mtu anayevumilia wakati wa majaribu, kwa sababu akiisha kushinda hilo jaribio atapewa taji la uzima Mungu alilowaahidia wale wampendao.

    13 Mtu anapojaribiwa asiseme, “Ninajaribiwa na Mungu.” Kwa maana Mungu hawezi kujaribiwa na maovu wala yeye hamjaribu mtu yeyote. 14 Lakini kila mtu hujaribiwa wakati anapovutwa na kudanganywa na tamaa zake mwenyewe zilizo mbaya. 15 Basi ile tamaa mbaya ikishachukua mimba, huzaa dhambi, nayo ile dhambi ikikomaa, huzaa mauti.

  27. 26 Tazama, leo ninaweka mbele yenu baraka na laana: 27 baraka kama mtatii maagizo ya Bwana Mungu wenu, ambayo ninawapa leo; 28 laana kama hamtatii maagizo ya Bwana Mungu wenu na kuacha njia ambayo ninawaamuru leo kwa kufuata miungu mingine, ambayo hamkuijua.

  28. 19 “Lakini mnauliza, ‘Kwa nini mwana asiadhibiwe kwa uovu wa baba yake?’ Kwa vile mwana ametenda yaliyo haki na sawa na amekuwa mwangalifu kuzishika amri zangu zote, hakika ataishi. 20 Roho itendayo dhambi ndiyo itakayokufa. Mwana hataadhibiwa kwa ajili ya makosa ya baba yake, wala baba hataadhibiwa kwa ajili ya makosa ya mwanawe. Haki ya mtu mwenye haki itahesabiwa juu yake na uovu wa mtu mwovu utalipizwa juu yake.

    21 “Lakini mtu mwovu akiacha dhambi zake zote alizozitenda na kushika amri zangu zote na kufanya lililo haki na sawa, hakika ataishi, hatakufa. 22 Hakuna kosa lolote alilotenda litakalokumbukwa juu yake. Kwa ajili ya mambo ya haki aliyoyatenda, ataishi. 23 Je, mimi ninafurahia kifo cha mtu mwovu? Asema Bwana Mwenyezi. Je, si mimi ninafurahi wanapogeuka kutoka njia zao mbaya na kuishi?

    24 “Lakini kama mtu mwenye haki akiacha haki yake na kutenda dhambi na kufanya mambo ya machukizo ambayo mtu mwovu hufanya, Je, ataishi? Hakuna hata mojawapo ya matendo ya haki aliyotenda litakalokumbukwa. Kwa sababu ya kukosa uaminifu kwake anayo hatia na kwa sababu ya dhambi alizozitenda, atakufa.

    25 “Lakini mnasema, ‘Njia ya Bwana si ya haki.’ Sikia, ee nyumba ya Israeli: Njia yangu siyo iliyo ya haki? Je, si njia zenu ndizo ambazo si za haki? 26 Kama mtu mwenye haki akiacha haki yake na kutenda dhambi, atakufa kwa ajili ya dhambi yake, kwa sababu ya dhambi alizotenda, atakufa. 27 Lakini mtu mwovu akigeuka kutoka maovu aliyoyatenda na kufanya yaliyo haki na sawa, ataokoa maisha yake. 28 Kwa kuwa anayafikiria na kugeuka kutoka makosa yake yote aliyoyatenda na kuyaacha, hakika ataishi, hatakufa. 29 Lakini nyumba ya Israeli inasema, ‘Njia za Bwana si haki.’ Je, njia zangu si za haki, ee nyumba ya Israeli? Je, si njia zenu ndizo ambazo si za haki?”

    30 “Kwa hiyo, ee nyumba ya Israeli, nitawahukumu, kila mmoja sawasawa na njia zake, asema Bwana Mwenyezi. Tubuni! Geukeni kutoka makosa yenu yote, ndipo dhambi haitakuwa anguko lenu. 31 Tupilieni mbali makosa yenu yote mliyoyatenda, nanyi mpate moyo mpya na roho mpya. Kwa nini mfe, ee nyumba ya Israeli? 32 Kwa maana sifurahii kifo cha mtu awaye yote afaye katika uovu, asema Bwana Mwenyezi. Tubuni basi, mkaishi!

  29. 34 Ndipo akauita ule umati wa watu pamoja na wanafunzi wake, akasema, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, ni lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake, anifuate.

  30. 12 Hivyo basi kila mmoja wetu atatoa habari zake mwenyewe kwa Mungu.

  31. 13 Hakuna jaribu lolote lililowapata ambalo si la kawaida kwa wanadamu. Naye Mungu ni mwaminifu; hataruhusu mjaribiwe kupita mnavyoweza. Lakini mnapojaribiwa atawapa njia ya kutokea ili mweze kustahimili.

  32. 1 Kristo alitupa uhuru, akataka tubaki huru. Hivyo simameni imara wala msikubali tena kulemewa na kongwa la utumwa.

  33. 17 Hivyo nawaambia hivi, nami nasisitiza katika Bwana kwamba, msiishi tena kama watu wa Mataifa waishivyo, katika ubatili wa mawazo yao. 18 Watu hao akili zao zimetiwa giza na wametengwa mbali na uzima wa Mungu kwa sababu ya ujinga wao kutokana na ugumu wa mioyo yao. 19 Wakiisha kufa ganzi, wamejitia katika mambo ya ufisadi na kupendelea kila aina ya uchafu, wakiendelea kutamani zaidi.

  34. 15 Lakini Farao alipoona pametokea nafuu, akaushupaza moyo wake na hakuwasikiliza Mose na Aroni, kama vile Bwana alivyokuwa amesema.

  35. 16 Baba wasiuawe kwa ajili ya watoto wao, wala watoto wasiuawe kwa ajili ya baba zao; kila mmoja atakufa kwa ajili ya dhambi yake mwenyewe.

  36. 19 Hakuna mji wowote katika eneo hili uliofanya mkataba wa amani na Israeli, isipokuwa hao Wahivi wa Gibeoni. Wengine wote walishindwa katika vita. 20 Kwa maana Bwana mwenyewe ndiye aliifanya mioyo yao iwe migumu, ili kupigana vita dhidi ya Israeli ili apate kuwafutilia mbali pasipo huruma, kama Bwana alivyomwagiza Mose.

    21 Wakati huo Yoshua akaenda kuwaangamiza Waanaki kutoka nchi ya vilima: kuanzia Hebroni, Debiri na Anabu, na kutoka nchi yote ya vilima ya Yuda na kutoka nchi yote ya vilima ya Israeli. Yoshua akawaangamiza kabisa pamoja na miji yao. 22 Hawakubaki Waanaki wowote katika nchi ya Israeli, ila tu katika nchi ya Gaza, Gathi na Ashdodi.

  37. 1 Mwanzoni mwa utawala wa Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda, neno hili lilikuja kutoka kwa Bwana: 2 “Hili ndilo Bwana asemalo: Simama katika ua wa nyumba ya Bwana na useme na watu wote wa miji ya Yuda wanaokuja kuabudu katika nyumba ya Bwana. Waambie kila kitu nitakachokuamuru, usipunguze neno. 3 Huenda watasikiliza, na kila mmoja akageuka kutoka njia yake mbaya. Kisha nitawahurumia na kuacha kuwaletea maafa niliyokuwa ninapanga kwa sababu ya maovu waliyofanya. 4 Waambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana: Ikiwa hamtanisikiliza na kuifuata sheria yangu ambayo nimeiweka mbele yenu, 5 nanyi ikiwa hamtayasikiliza maneno ya watumishi wangu manabii, ambao nimewatuma kwenu tena na tena (ijapokuwa hamkuwasikiliza), 6 ndipo nitaifanya nyumba hii kama Shilo na mji huu kuwa kitu cha kulaaniwa na mataifa yote ya dunia.’ ”

  38. 14 “Mimi ndimi mchungaji mwema. Ninawajua kondoo wangu nao kondoo wangu wananijua. 15 Kama vile Baba anavyonijua mimi, nami ninavyomjua Baba, nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo. 16 Ninao kondoo wengine ambao si wa zizi hili, inanipasa kuwaleta, nao wataisikia sauti yangu, hivyo patakuwa na kundi moja na mchungaji mmoja. 17 Baba yangu ananipenda kwa kuwa ninautoa uhai wangu ili niupate tena. 18 Hakuna mtu aniondoleaye uhai wangu, bali ninautoa kwa hiari yangu mwenyewe. Ninao uwezo wa kuutoa uhai wangu na pia ninao uwezo wa kuutwaa tena. Amri hii nimepewa na Baba yangu.”

  39. 7 Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi. Kwa kuwa kile apandacho mtu ndicho atakachovuna. 8 Apandaye kwa mwili, katika mwili wake atavuna uharibifu, lakini yeye apandaye katika Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele.

  40. 9 Kuja kwa yule mwasi kutaonekana kana kwamba ni kutenda kazi kwake Shetani ambaye hutumia nguvu zote, ishara, maajabu ya uongo, 10 na kila aina ya uovu kwa wale wanaoangamia kwa sababu walikataa kuipenda kweli wapate kuokolewa. 11 Kwa sababu hii, Mungu ameruhusu watawaliwe na nguvu ya udanganyifu, ili waendelee kuamini uongo, 12 na wahukumiwe wote ambao hawakuiamini ile kweli, bali wamefurahia uovu.

  41. 20 Tazama! Nasimama mlangoni nabisha. Kama mtu yeyote akisikia sauti yangu na kufungua mlango, nitaingia ndani na kula pamoja naye, naye pamoja nami.