108 Bible Verses About Protection

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Protection
  1. 1 Yeye akaaye mahali pa salama pake Yeye Aliye Juu Sana,

    atadumu katika uvuli wake Mwenyezi.

    2 Nitasema kumhusu Bwana, “Yeye ndiye kimbilio langu na ngome yangu,

    Mungu wangu, ambaye ninamtumaini.”

    3 Hakika yeye ataniokoa na mtego wa mwindaji,

    na maradhi ya kuambukiza ya kuua.

    4 Atakufunika kwa manyoya yake,

    chini ya mbawa zake utapata kimbilio,

    uaminifu wake utakuwa ngao na kinga yako.

    5 Hutaogopa vitisho vya usiku,

    wala mshale urukao mchana,

    6 wala maradhi ya kuambukiza

    yanayonyemelea gizani,

    wala tauni iharibuyo adhuhuri.

    7 Ijapo watu elfu wataangukia kando yako,

    kumi elfu mkono wako wa kuume,

    lakini haitakukaribia wewe.

    8 Utatazama tu kwa macho yako

    na kuona adhabu ya waovu.

    9 Kama ukimfanya Aliye Juu Sana kuwa makao yako:

    naam, Bwana ambaye ni kimbilio langu,

    10 basi hakuna madhara yatakayokupata wewe,

    hakuna maafa yataikaribia hema yako.

    11 Kwa kuwa atawaagiza malaika zake kwa ajili yako,

    wakulinde katika njia zako zote.

    12 Mikononi mwao watakuinua,

    ili usijikwae mguu wako kwenye jiwe.

  2. Zaburi ya Daudi.

    1 Bwana ndiye mchungaji wangu,

    sitapungukiwa na kitu.

    2 Hunilaza katika malisho

    ya majani mabichi,

    kando ya maji matulivu huniongoza,

    3 hunihuisha nafsi yangu.

    Huniongoza katika njia za haki

    kwa ajili ya jina lake.

    4 Hata kama nikipita katikati

    ya bonde la uvuli wa mauti,

    sitaogopa mabaya,

    kwa maana wewe upo pamoja nami;

    fimbo yako na mkongojo wako

    vyanifariji.

  3. Wimbo wa kwenda juu.

    1 Nayainua macho yangu nitazame vilima,

    msaada wangu utatoka wapi?

    2 Msaada wangu hutoka kwa Bwana,

    Muumba wa mbingu na dunia.

    3 Hatauacha mguu wako uteleze,

    yeye akulindaye hatasinzia,

    4 hakika, yeye alindaye Israeli

    hatasinzia wala hatalala usingizi.

    5 Bwana anakulinda,

    Bwana ni uvuli wako mkono wako wa kuume,

    6 jua halitakudhuru mchana,

    wala mwezi wakati wa usiku.

    7 Bwana atakukinga na madhara yote,

    atayalinda maisha yako,

    8 Bwana atakulinda unapoingia na unapotoka,

    tangu sasa na hata milele.

  4. 10 Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. 11 Vaeni silaha zote za Mungu ili kwamba mweze kuzipinga hila za ibilisi. 12 Kwa maana kushindana kwetu si juu ya nyama na damu, bali dhidi ya falme, mamlaka, dhidi ya wakuu wa giza na majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. 13 Kwa hiyo vaeni silaha zote za Mungu ili mweze kushindana siku ya uovu itakapokuja nanyi mkiisha kufanya yote, simameni imara. 14 Kwa hiyo simameni imara mkiwa mmejifunga kweli kiunoni na kuvaa dirii ya haki kifuani, 15 nayo miguu yenu ifungiwe utayari tuupatao kwa Injili ya amani. 16 Zaidi ya haya yote, twaeni ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu. 17 Vaeni chapeo ya wokovu na mchukue upanga wa Roho, ambao ni Neno la Mungu.

  5. 3 Lakini Bwana ni mwaminifu, naye atawaimarisha ninyi na kuwalinda kutokana na yule mwovu. 4 Nasi tuna tumaini katika Bwana ya kuwa mnafanya na mtaendelea kufanya yale tuliyowaagiza. 5 Bwana aiongoze mioyo yenu katika upendo wa Mungu na katika saburi ya Kristo.

  6. Kwa mwimbishaji. Zaburi ya wana wa Kora. Mtindo wa alamothi.

    1 Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu,

    msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso.

    2 Kwa hiyo hatutaogopa, hata kama dunia ikiondolewa

    nayo milima ikiangukia moyoni mwa bahari.

  7. 3 Lakini wewe, Ee Bwana, ni ngao pande zote;

    umeniwekea utukufu na kuinua kichwa changu.

    4 Ninamlilia Bwana kwa sauti kuu,

    naye ananijibu kutoka mlima wake mtakatifu.

    5 Ninajilaza na kupata usingizi;

    naamka tena, kwa maana Bwana hunitegemeza.

  8. 10 Hivyo usiogope, kwa maana niko pamoja nawe;

    usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako.

    Nitakutia nguvu na kukusaidia;

    nitakutegemeza kwa mkono wa kuume wa haki yangu.

    11 “Wote walioona hasira dhidi yako

    hakika wataaibika na kutahayarika,

    wale wakupingao

    watakuwa kama vile si kitu, na kuangamia.

    12 Ingawa utawatafuta adui zako,

    hutawaona.

    Wale wanaopigana vita dhidi yako

    watakuwa kama vile si kitu kabisa.

  9. 11 Lakini wote wakimbiliao kwako na wafurahi,

    waimbe kwa shangwe daima.

    Ueneze ulinzi wako juu yao,

    ili wale wapendao jina lako

    wapate kukushangilia.

  10. 7 Wewe ndiwe mahali pangu pa kujificha,

    utaniepusha na taabu

    na kunizunguka kwa nyimbo za wokovu.

  11. 10 Jina la Bwana ni ngome imara,

    wenye haki huikimbilia na kuwa salama.

    11 Mali ya tajiri ni mji wake wenye ngome,

    wanaudhania kuwa ukuta usioweza kurukwa.

    12 Kabla ya anguko moyo wa mtu hujaa kiburi,

    bali unyenyekevu hutangulia heshima.

  12. 17 Hakuna silaha itakayofanyizwa dhidi yako

    itakayofanikiwa,

    nawe utauthibitisha kuwa mwongo

    kila ulimi utakaokushtaki.

    Huu ndio urithi wa watumishi wa Bwana

    na hii ndiyo haki yao itokayo kwangu,”

    asema Bwana.

  13. 28 nami ninawapa uzima wa milele, hawataangamia kamwe wala hakuna mtu atakayewapokonya kutoka mikono yangu. 29 Baba yangu aliyenipa hawa ni mkuu kuliko wote na hakuna awezaye kuwapokonya kutoka mikononi mwake. 30 Mimi na Baba yangu tu umoja.”

  14. 16 Katika utetezi wangu wa mara ya kwanza, hakuna hata mmoja aliyeniunga mkono, bali kila mmoja aliniacha. Namwomba Mungu wasihesabiwe hatia kwa jambo hilo. 17 Lakini Bwana alisimama upande wangu akanitia nguvu, ili kupitia kwangu lile Neno lihubiriwe kwa ukamilifu, watu wote Mataifa wapate kulisikia. Mimi niliokolewa kutoka kinywa cha simba. 18 Bwana ataniokoa katika kila shambulio baya na kunileta salama katika Ufalme wake wa mbinguni. Atukuzwe yeye milele na milele. Amen.

  15. 13 Hakuna jaribu lolote lililowapata ambalo si la kawaida kwa wanadamu. Naye Mungu ni mwaminifu; hataruhusu mjaribiwe kupita mnavyoweza. Lakini mnapojaribiwa atawapa njia ya kutokea ili mweze kustahimili.

  16. 6 Kuweni imara na moyo wa ushujaa. Msiogope wala msifadhaike kwa sababu yao, kwa kuwa Bwana Mungu wenu anakwenda pamoja nanyi; kamwe hatawaacha wala hatawatupa ninyi.”

  17. 7 Malaika wa Bwana hufanya kituo

    akiwazunguka wale wamchao,

    naye huwaokoa.

    8 Onjeni mwone kwamba Bwana ni mwema,

    heri mtu yule anayemkimbilia.

    9 Mcheni Bwana enyi watakatifu wake,

    kwa maana wale wamchao

    hawapungukiwi na chochote.

  18. 23 Mungu mwenyewe, Mungu wa amani, awatakase ninyi kabisa. Nanyi mhifadhiwe roho zenu, nafsi zenu na miili yenu, bila kuwa na lawama katika Bwana wetu Yesu Kristo. 24 Yeye aliyewaita ni mwaminifu naye atafanya hayo.

  19. 13 Mose akawajibu Waisraeli, “Msiogope. Simameni imara, nanyi mtauona wokovu Bwana atakaowapatia leo. Hao Wamisri mnaowaona leo kamwe hamtawaona tena. 14 Bwana atawapigania ninyi, nanyi mnatakiwa kutulia tu.”

  20. 1 Lakini sasa hili ndilo asemalo Bwana,

    yeye aliyekuumba, ee Yakobo,

    yeye aliyekuhuluku, ee Israeli:

    “Usiogope kwa maana nimekukomboa,

    nimekuita wewe kwa jina lako, wewe u wangu.

    2 Unapopita kwenye maji makuu,

    nitakuwa pamoja nawe,

    unapopita katika mito ya maji,

    hayatakugharikisha.

    Utakapopita katika moto,

    hutaungua,

    miali ya moto haitakuunguza.

    3 Kwa kuwa Mimi ndimi Bwana, Mungu wako,

    yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, Mwokozi wako.

    Ninaitoa Misri kuwa fidia yako,

    Kushi na Seba badala yako.

  21. 6 Bwana yuko pamoja nami, sitaogopa.

    Mwanadamu anaweza kunitenda nini?

    7 Bwana yuko pamoja nami,

    yeye ni msaidizi wangu.

    Nitawatazama adui zangu

    wakiwa wameshindwa.

    8 Ni bora kumkimbilia Bwana

    kuliko kumtumainia mwanadamu.

    9 Ni bora kumkimbilia Bwana

    kuliko kuwatumainia wakuu.

  22. 7 Uonyeshe ajabu ya upendo wako mkuu,

    wewe uokoaye kwa mkono wako wa kuume

    wale wanaokukimbilia kutokana na adui zao.

    8 Nilinde kama mboni ya jicho lako,

    unifiche chini ya kivuli cha mbawa zako

    9 kutokana na waovu wanaonishambulia,

    kutokana na adui wauaji wanaonizunguka.

    10 Huifunga mioyo yao iliyo migumu,

    vinywa vyao hunena kwa majivuno.

  23. 17 Wenye haki hulia, naye Bwana huwasikia,

    huwaokoa katika taabu zao zote.

    18 Bwana yu karibu na waliovunjika moyo,

    na huwaokoa waliopondeka roho.

    19 Mwenye haki ana mateso mengi,

    lakini Bwana humwokoa nayo yote,

    20 huhifadhi mifupa yake yote,

    hata mmoja hautavunjika.

  24. 7 Nijapopita katikati ya shida,

    wewe unayahifadhi maisha yangu,

    unanyoosha mkono wako dhidi ya hasira ya adui zangu,

    kwa mkono wako wa kuume unaniokoa.

  25. 3 Mungu wangu ni mwamba wangu,

    ambaye kwake ninakimbilia,

    ngao yangu na pembe ya wokovu wangu.

    Yeye ni ngome yangu, kimbilio langu

    na mwokozi wangu,

    huniokoa kutoka kwa watu wenye jeuri.

    4 Ninamwita Bwana, anayestahili kusifiwa,

    nami ninaokolewa kutoka kwa adui zangu.

  26. Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Usiharibu!” Utenzi wa Daudi. Baada ya kumponyoka Sauli pangoni.

    1 Unihurumie, Ee Mungu, unihurumie,

    kwa maana nafsi yangu inakukimbilia.

    Chini ya uvuli wa mbawa zako nitakimbilia

    mpaka maafa yapite.

  27. 114 Wewe ni kimbilio langu na ngao yangu,

    nimeweka tumaini langu katika neno lako.

  28. 1 Hatimaye, ndugu zangu, furahini katika Bwana! Mimi kuwaandikia mambo yale yale hakuniudhi, kwa maana ni kinga kwa ajili yenu.

    2 Jihadharini na mbwa, wale watenda maovu, jihadharini na wale wajikatao miili yao, wasemao ili kuokoka ni lazima kutahiriwa. 3 Kwa maana sisi ndio tulio tohara, sisi tumwabuduo Mungu katika Roho, tunaona fahari katika Kristo Yesu, ambao hatuweki tumaini letu katika mwili,

  29. 14 Bwana asema, “Kwa kuwa ananipenda, nitamwokoa;

    nitamlinda, kwa kuwa analikiri Jina langu.

    15 Ataniita, nami nitamjibu;

    nitakuwa pamoja naye katika taabu,

    nitamwokoa na kumheshimu.

    16 Kwa siku nyingi nitamshibisha

    na kumwonyesha wokovu wangu.”

  30. Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi mtumishi wa Bwana aliyomwimbia Bwana wakati Bwana alipomwokoa mikononi mwa adui zake wote, na pia mkononi mwa Sauli. Alisema hivi:

    1 Nakupenda wewe, Ee Bwana,

    nguvu yangu.

    2 Bwana ni mwamba wangu,

    ngome yangu na mwokozi wangu,

    Mungu wangu ni mwamba,

    ambaye kwake ninakimbilia.

    Yeye ni ngao yangu na pembe ya wokovu wangu,

    ngome yangu.

  31. 16 Lakini mimi nitaziimba nguvu zako,

    asubuhi nitaimba juu ya upendo wako;

    kwa maana wewe ndiwe ngome yangu

    na kimbilio langu wakati wa shida.

  32. 4 Hata mpaka wakati wa uzee wenu na mvi, Mimi ndiye,

    Mimi ndiye nitakayewasaidia ninyi.

    Nimewahuluku, nami nitawabeba,

    nitawasaidia ninyi na kuwaokoa.

  33. 31 Tuseme nini basi kuhusu haya? Ikiwa Mungu yuko upande wetu, ni nani awezaye kuwa kinyume chetu? 32 Ikiwa Mungu hakumhurumia Mwanawe, bali alimtoa kwa ajili yetu sote, atakosaje basi kutupatia vitu vyote kwa ukarimu pamoja naye? 33 Ni nani atakayewashtaki wale ambao Mungu amewateua? Ni Mungu mwenyewe ndiye mwenye kuwahesabia haki.

  34. 6 Kwa hiyo tunaweza kusema kwa ujasiri,

    “Bwana ni msaada wangu; sitaogopa.

    Mwanadamu anaweza kunitenda nini?”

  35. 7 Basi mtiini Mungu. Mpingeni ibilisi, naye atawakimbia. 8 Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu ninyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu ninyi wenye nia mbili.

  36. Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Usiharibu!” Utenzi wa Daudi. Wakati Sauli alipotuma wapelelezi nyumbani mwa Daudi ili wamuue.

    1 Ee Mungu, uniokoe na adui zangu,

    unilinde kutokana na hao wanaoinuka dhidi yangu.

  37. 7 Bwana ni Mwema,

    kimbilio wakati wa taabu.

    Huwatunza wale wanaomtegemea,

  38. 15 Siombi kwamba uwaondoe ulimwenguni, bali uwalinde dhidi ya yule mwovu.

  39. Utenzi wa Daudi.

    1 Ee Mungu, uniweke salama,

    kwa maana kwako nimekimbilia.

    2 Nilimwambia Bwana, “Wewe ndiwe Bwana wangu;

    pasipo wewe sina jambo jema.”

  40. 30 Kuhusu Mungu, njia yake ni kamilifu,

    neno la Bwana halina dosari.

    Yeye ni ngao kwa wote

    wanaokimbilia kwake.

    31 Kwa maana ni nani aliye Mungu

    zaidi ya Bwana?

    Ni nani aliye Mwamba

    isipokuwa Mungu wetu?

    32 Mungu ndiye anivikaye nguvu

    na kufanya njia yangu kuwa kamilifu.

  41. 22 Bwana huwakomboa watumishi wake,

    yeyote anayemkimbilia yeye

    hatahukumiwa kamwe.

  42. 7 Ili kunizuia nisijivune kwa sababu ya ufunuo huu mkuu, nilipewa mwiba katika mwili wangu, mjumbe wa Shetani, ili anitese. 8 Kwa habari ya jambo hili nilimsihi Bwana mara tatu aniondolee mwiba huu. 9 Lakini aliniambia, “Neema yangu inakutosha, kwa kuwa uweza wangu hukamilika katika udhaifu.” Kwa hiyo nitajisifu kwa furaha zaidi kuhusu udhaifu wangu, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. 10 Hii ndiyo sababu, kwa ajili ya Kristo, nafurahia udhaifu, katika kutukanwa, katika taabu, katika mateso na katika shida, kwa maana ninapokuwa dhaifu, ndipo nina nguvu.

  43. 5 Yalindeni maisha yenu msiwe na tabia ya kupenda fedha, bali mridhike na vile mlivyo navyo, kwa sababu Mungu amesema,

    “Kamwe sitakuacha,

    wala sitakupungukia.”

  44. 5 Ndipo ibilisi akamchukua Yesu mpaka mji mtakatifu na kumweka juu ya mnara mrefu wa Hekalu, 6 akamwambia, “Kama wewe ndiwe Mwana wa Mungu jitupe chini. Kwa kuwa imeandikwa:

    “ ‘Atakuagizia malaika zake,

    nao watakuchukua mikononi mwao

    ili usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.’ ”

    7 Yesu akamjibu, “Pia imeandikwa: ‘Usimjaribu Bwana Mungu wako.’ ”

  45. 42 Mfilisti akamwangalia Daudi kote na kumwona kuwa ni kijana tu, mwekundu na mzuri wa kupendeza, naye akamdharau. 43 Akamwambia Daudi, “Je, mimi ni mbwa, hata unanijia na fimbo?” Yule Mfilisti akamlaani Daudi kwa miungu yake. 44 Tena Mfilisti akamwambia, “Njoo hapa, nami nitawapa ndege wa angani na wanyama wa mwituni nyama yako.”

    45 Daudi akamwambia yule Mfilisti. “Wewe unanijia na upanga, mkuki na fumo, lakini mimi ninakujia kwa jina la Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa majeshi ya Israeli, ambaye wewe umemtukana. 46 Siku hii leo Bwana atakutia mkononi mwangu, nami nitakupiga na kukukata kichwa chako. Leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya jeshi la Wafilisti, nayo dunia yote itajua kuwa yuko Mungu katika Israeli. 47 Wale wote waliokusanyika hapa watajua kuwa Bwana haokoi kwa upanga wala kwa mkuki; kwa kuwa vita ni vya Bwana, naye atawatia wote mikononi mwetu.”

    48 Yule Mfilisti aliposogea karibu ili kumshambulia, Daudi akaenda mbio kuelekea safu ya vita kukutana naye. 49 Daudi akatia mkono wake mfukoni na kuchukua jiwe, akalirusha kwa kombeo, nalo likampiga yule Mfilisti kwenye paji la uso. Lile jiwe likaingia kipajini mwa uso, akaanguka chini kifudifudi.

  46. 9 Kwa kuwa macho ya Bwana hukimbiakimbia duniani kote ili kujionyesha mwenye nguvu kwa ajili ya wale ambao mioyo yao inamtegemea kwa ukamilifu. Umefanya jambo la upumbavu na kuanzia sasa na kuendelea utakuwa na vita.”

  47. 5 “Kwa sababu ya uonevu wa wanyonge

    na kulia kwa uchungu kwa wahitaji,

    nitainuka sasa,” asema Bwana.

    “Nitawalinda kutokana na wale

    wenye nia mbaya juu yao.”

  48. 35 Hunipa ngao yako ya ushindi,

    nao mkono wako wa kuume hunitegemeza,

    unajishusha chini ili kuniinua.

    36 Huyapanua mapito yangu,

    ili miguu yangu isiteleze.

  49. 7 Kwa sababu wewe ndiwe msaada wangu,

    chini ya uvuli wa mbawa zako naimba.

    8 Nafsi yangu inaambatana nawe,

    mkono wako wa kuume hunishika.

    9 Wale wanaotafuta uhai wangu wataharibiwa,

    watakwenda chini kwenye vilindi vya dunia.

  50. 4 Ee Bwana, niepushe na mikono ya waovu;

    nilinde na watu wenye jeuri

    wanaopanga kunikwaza miguu yangu.

  51. 3 “Wekeni tayari ngao zenu, kubwa na ndogo,

    mtoke kwa ajili ya vita!

    4 Fungieni farasi lijamu,

    pandeni farasi!

    Shikeni nafasi zenu

    mkiwa mmevaa chapeo!

    Isugueni mikuki yenu,

    vaeni dirii vifuani!

  52. 28 Nasi tunajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hutenda kazi pamoja na wote wampendao, katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.

  53. 4 Furahini katika Bwana siku zote, tena nasema furahini! 5 Upole wenu na ujulikane na watu wote. Bwana yu karibu. 6 Msijisumbue kwa jambo lolote, bali katika kila jambo kwa kuomba na kusihi pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. 7 Nayo amani ya Mungu, inayopita fahamu zote, itailinda mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.

  54. 4 Watoto wapendwa, ninyi mmetokana na Mungu, nanyi mmewashinda kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika ulimwengu.

  55. 10 Kwa kuwa umeshika amri yangu ya kuvumilia katika saburi, nitakulinda katika saa ya kujaribiwa inayokuja ulimwenguni pote, ili kuwajaribu wote wakaao duniani.

  56. 1 Mtakapokwenda vitani kupigana na adui zenu na mkaona farasi na magari ya vita na jeshi kubwa kuliko lenu, msiwaogope, kwa sababu Bwana Mungu wenu aliyewatoa kutoka Misri, atakuwa pamoja nanyi. 2 Wakati mtakapokaribia kwenda vitani, kuhani atakuja mbele na kuhutubia jeshi. 3 Atasema: “Sikia, ee Israeli, leo unakwenda vitani kupigana na adui zako. Usife moyo wala usiogope, usitishwe wala usitiwe hofu mbele yao. 4 Kwa kuwa Bwana Mungu wenu ndiye huenda pamoja nanyi kuwapigania dhidi ya adui zenu na kuwapatia ushindi.”

  57. 5 Hakuna mtu yeyote atakayeweza kushindana na wewe siku zote za maisha yako. Kama vile nilivyokuwa pamoja na Mose, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe, sitakuacha wala sitakupungukia.

  58. 9 Je, si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na shujaa. Usihofu wala usivunjike moyo, kwa kuwa Bwana Mungu wako atakuwa pamoja nawe kokote uendako.”

  59. 8 Nimemweka Bwana mbele yangu daima.

    Kwa sababu yuko mkono wangu wa kuume,

    sitatikisika.

  60. Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.

    1 Heri mtu yule anayemjali mnyonge,

    Bwana atamwokoa wakati wa shida.

    2 Bwana atamlinda na kuyahifadhi maisha yake,

    atambariki katika nchi

    na hatamwacha katika tamaa ya adui zake.

  61. Kwa mwimbishaji. Kwa ala za nyuzi za uimbaji. Zaburi ya Daudi.

    1 Ee Mungu, sikia kilio changu,

    usikilize maombi yangu.

    2 Kutoka miisho ya dunia ninakuita,

    ninaita huku moyo wangu unadhoofika;

    uniongoze kwenye mwamba

    ule ulio juu kuliko mimi.

    3 Kwa kuwa umekuwa kimbilio langu,

    ngome imara dhidi ya adui.

    4 Natamani kukaa hemani mwako milele,

    na kukimbilia chini ya uvuli wa mbawa zako.

  62. 2 Yeye peke yake ndiye mwamba wangu na wokovu wangu;

    yeye ni ngome yangu, sitatikisika kamwe.

  63. 25 Usiogope maafa ya ghafula

    au maangamizi yanayowapata waovu,

    26 kwa kuwa Bwana atakuwa tumaini lako

    na kuepusha mguu wako kunaswa katika mtego.

  64. 5 Pata hekima, pata ufahamu;

    usiyasahau maneno yangu wala usiyaache.

    6 Usimwache hekima naye atakuweka salama;

    mpende, naye atakulinda.

    7 Hekima ni bora kuliko vitu vyote; kwa hiyo jipe hekima.

    Hata ikikugharimu vyote ulivyo navyo, pata ufahamu.

    8 Mstahi, naye atakukweza;

    mkumbatie, naye atakuheshimu.

    9 Atakuvika shada la neema kichwani mwako

    na kukupa taji ya utukufu.”

  65. 23 Kumcha Bwana huongoza kwenye uzima,

    kisha mtu hupumzika akiwa ameridhika,

    bila kuguswa na shida.

  66. 5 “Kila neno la Mungu ni kamilifu;

    yeye ni ngao kwa wale wanaomkimbilia.

  67. 17 jifunzeni kutenda mema!

    Tafuteni haki,

    watieni moyo walioonewa.

    Teteeni shauri la yatima,

    wateteeni wajane.

  68. 17 Bwana Mungu wako yu pamoja nawe,

    yeye ni mwenye nguvu kuokoa.

    Atakufurahia kwa furaha kubwa,

    atakutuliza kwa pendo lake,

    atakufurahia kwa kuimba.”

  69. 19 Tazama nimewapa mamlaka ya kukanyaga nyoka na nge na juu ya nguvu zote za adui; wala hakuna kitu chochote kitakachowadhuru.

  70. 16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. 17 Kwa maana Mungu hakumtuma Mwanawe kuuhukumu ulimwengu, bali kupitia kwake ulimwengu upate kuokolewa.

  71. 24 Kwake yeye awezaye kuwalinda ninyi msianguke na kuwaleta mbele za utukufu wake mkuu bila dosari na kwa furaha ipitayo kiasi: 25 kwake yeye Mungu pekee Mwokozi wetu, kwa Yesu Kristo Bwana wetu, utukufu, ukuu, uweza na mamlaka ni vyake tangu milele, sasa na hata milele! Amen.

  72. Wimbo wa kwenda juu. Wa Solomoni.

    1 Bwana asipoijenga nyumba,

    wajengao hufanya kazi bure.

    Bwana asipoulinda mji,

    walinzi wakesha bure.

  73. 15 Niko pamoja nawe nami nitakulinda kila uendako na nitakurudisha katika nchi hii. Sitakuacha mpaka nitakapofanya hayo niliyokuahidi.”

  74. 37 Atasema: “Sasa iko wapi miungu yao,

    mwamba walioukimbilia,

    38 miungu wale waliokula mafuta ya dhabihu zao

    na kunywa mvinyo wa sadaka zao za vinywaji?

    Wainuke basi, wawasaidie!

    Wawapeni basi ulinzi!

    39 “Tazama basi, Mimi mwenyewe, Mimi Ndiye!

    Hakuna mungu mwingine ila Mimi.

    Mimi ninaua na Mimi ninafufua,

    Mimi nimejeruhi na Mimi nitaponya,

    wala hakuna awezaye kuokoa kutoka mkononi mwangu.

  75. 38 Ndipo Sauli akamvika Daudi silaha zake mwenyewe za vita. Akamvika dirii na chapeo ya shaba kichwani mwake.

  76. Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.

    1 Bwana na akujibu unapokuwa katika dhiki,

    jina la Mungu wa Yakobo na liwe kinga yako.

  77. 15 Macho ya Bwana huwaelekea wenye haki,

    na masikio yake yako makini kusikiliza kilio chao.

  78. 3 Wakati ninapoogopa,

    nitakutumaini wewe.

    4 Katika Mungu, ambaye neno lake ninalisifu,

    katika Mungu ninatumaini; sitaogopa.

    Mwanadamu apatikanaye na kufa,

    atanitenda nini?

  79. Wimbo wa kwenda juu.

    1 Wale wamtumainio Bwana ni kama mlima Sayuni,

    ambao hauwezi kutikisika, bali wadumu milele.

    2 Kama milima inavyozunguka Yerusalemu,

    ndivyo Bwana anavyowazunguka watu wake

    sasa na hata milele.

  80. 19 Huwatimizia wamchao matakwa yao,

    husikia kilio chao na kuwaokoa.

  81. 33 Lakini yeyote anisikilizaye ataishi kwa usalama,

    atatulia, bila kuwa na hofu ya madhara.”

  82. 21 Hakuna dhara linalompata mwenye haki,

    bali waovu wana taabu nyingi.

  83. 26 Yeye amchaye Bwana ana ngome salama,

    na kwa watoto wake itakuwa kimbilio.

  84. 12 Mtu mwenye busara huona hatari na kujificha,

    bali mjinga huendelea mbele nayo ikamtesa.

  85. 1 Katika siku ile, wimbo huu utaimbwa katika nchi ya Yuda:

    Tuna mji ulio na nguvu,

    Mungu huufanya wokovu kuwa kuta zake na maboma yake.

    2 Fungua malango ili taifa lenye haki lipate kuingia,

    taifa lile lidumishalo imani.

    3 Utamlinda katika amani kamilifu

    yeye ambaye moyo wake ni thabiti

    kwa sababu anakutumaini wewe.

    4 Mtumaini Bwana milele,

    kwa kuwa Bwana, Bwana, ni Mwamba wa milele.

    5 Huwashusha wale wajikwezao,

    huushusha chini mji wenye kiburi,

    huushusha hadi ardhini

    na kuutupa chini mavumbini.

    6 Miguu huukanyaga chini,

    miguu ya hao walioonewa,

    hatua za hao maskini.

  86. 16 Mtasalitiwa hata na wazazi, ndugu, jamaa na marafiki, na baadhi yenu watawaua. 17 Mtachukiwa na watu wote kwa ajili ya Jina langu. 18 Lakini hapatakuwa na unywele mmoja wa kichwa chenu utakaoangamia. 19 Kwa kuvumilia mtaokoa roho zenu.

  87. 33 Nimewaambia mambo haya, ili mpate kuwa na amani mkiwa ndani yangu. Ulimwenguni mtapata dhiki. Lakini jipeni moyo, kwa maana mimi nimeushinda ulimwengu.”

  88. 11 Mimi sasa simo tena ulimwenguni, lakini wao bado wamo ulimwenguni, nami naja kwako. Baba Mtakatifu, uwalinde kwa uweza wa jina lako ulilonipa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo wamoja. 12 Nilipokuwa pamoja nao, niliwalinda, wakawa salama kwa lile jina ulilonipa. Hakuna hata mmoja aliyepotea, isipokuwa yule aliyekusudiwa upotevu, ili Maandiko yapate kutimia.

  89. 19 Wapendwa, msilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu, maana imeandikwa: “Ni juu yangu kulipiza kisasi, nitalipiza,” asema Bwana.

  90. 13 Naweza kuyafanya mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.

  91. 8 Kama mtu hawatunzi wale wa jamaa yake, hasa wale wa nyumbani mwake mwenyewe, ameikana imani, tena ni mbaya kuliko yeye asiyeamini.

  92. 19 Sisi twajua kuwa tu watoto wa Mungu na ya kwamba ulimwengu wote uko chini ya utawala wa yule mwovu.

  93. 32 Kwa maana ni nani aliye Mungu

    zaidi ya Bwana?

    Ni nani aliye Mwamba

    isipokuwa Mungu wetu?

  94. Ombolezo la Daudi kwa Bwana kwa sababu ya Kushi, Mbenyamini.

    1 Ee Bwana, Mungu wangu, ninakukimbilia wewe,

    uniokoe na kunikomboa na wote wanaonifuatia,

  95. 9 Ee Mungu mwenye haki,

    uchunguzaye mawazo na mioyo,

    komesha ghasia za waovu

    na ufanye wenye haki waishi kwa amani.

  96. 9 Bwana ni kimbilio la watu wanaoonewa,

    ni ngome imara wakati wa shida.

    10 Wote wanaolijua jina lako watakutumaini wewe,

    kwa maana wewe Bwana,

    hujawaacha kamwe wakutafutao.

  97. Zaburi ya Daudi.

    1 Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu,

    nimwogope nani?

    Bwana ni ngome ya uzima wangu,

    nimhofu nani?

  98. 19 Tazama jinsi ulivyo mkuu wema wako,

    uliowawekea akiba wakuchao,

    ambao huwapa wale wakukimbiliao

    machoni pa watu.

  99. 11 Ee Bwana, usizuilie huruma zako,

    upendo wako na kweli yako daima vinilinde.

    12 Kwa maana taabu zisizo na hesabu zimenizunguka,

    dhambi zangu zimenikamata, hata nisiweze kuona.

    Zimekuwa nyingi kuliko nywele za kichwa changu,

    nao moyo unazimia ndani yangu.

    13 Ee Bwana, uwe radhi kuniokoa;

    Ee Bwana, njoo hima unisaidie.

  100. 7 Wokovu wangu na heshima yangu viko kwa Mungu,

    ndiye mwamba wangu wenye nguvu

    na kimbilio langu.

    8 Enyi watu, mtumainini yeye wakati wote,

    miminieni mioyo yenu kwake,

    kwa kuwa Mungu ni kimbilio letu.

  101. 12 Kwa maana atamwokoa mhitaji anayemlilia,

    aliyeonewa asiye na wa kumsaidia.

    13 Atawahurumia wanyonge na wahitaji

    na kuwaokoa wahitaji kutoka mauti.

    14 Atawaokoa kutoka uonevu na ukatili,

    kwani damu yao ni ya thamani machoni pake.

  102. 10 Wale wanaompenda Bwana na wauchukie uovu,

    kwa maana yeye hulinda maisha ya waaminifu wake

    na kuwaokoa kutoka mkononi mwa mwovu.

  103. Wimbo wa kwenda juu. Wa Daudi.

    1 Kama Bwana asingalikuwa upande wetu;

    Israeli na aseme sasa:

    2 kama Bwana asingalikuwa upande wetu,

    wakati watu walipotushambulia,

    3 wakati hasira yao ilipowaka dhidi yetu,

    wangalitumeza tungali hai,

    4 mafuriko yangalitugharikisha,

    maji mengi yangalitufunika,

    5 maji yaendayo kasi

    yangalituchukua.

  104. 7 Anahifadhi ushindi kwa ajili ya mwadilifu,

    yeye ni ngao kwa wale wasio na lawama,

    8 kwa kuwa hulinda mwenendo wa mwenye haki

    na kuhifadhi njia ya waaminifu wake.

  105. 5 Sasa nitawaambia lile nitakalolitendea

    shamba langu la mizabibu:

    Nitaondoa uzio wake,

    nalo litaharibiwa,

    nitabomoa ukuta wake,

    nalo litakanyagwa.

    6 Nitalifanya nchi ya ukiwa isiyokaliwa na watu,

    halitakatiwa matawi wala kulimwa,

    nayo michongoma na miiba itamea huko,

    nitaamuru mawingu yasinyeshe mvua juu yake.”

    7 Shamba la mzabibu la Bwana Mwenye Nguvu Zote

    ni nyumba ya Israeli,

    na watu wa Yuda

    ni bustani yake ya kumpendeza.

    Alitazamia haki, lakini akaona umwagaji damu,

    alitazamia uadilifu, lakini akasikia vilio vya taabu.

  106. 1 “Katika wakati huo Mikaeli, mtawala mkuu ambaye huwalinda watu wako, atainuka. Kutakuwako wakati wa taabu ambao haujatokea tangu mwanzo wa mataifa hadi wakati huo. Lakini wakati huo, watu wako, kila mmoja ambaye jina lake litakutwa limeandikwa kwenye kitabu, ataokolewa.

  107. 13 Usitutie majaribuni,

    bali utuokoe kutoka kwa yule mwovu

    [kwa kuwa Ufalme ni wako, na nguvu,

    na utukufu, hata milele. Amen].’

  108. 28 Msiwaogope wale wauao mwili lakini hawawezi kuua roho. Afadhali mwogopeni yeye awezaye kuiangamiza roho na mwili katika jehanamu. 29 Je, shomoro wawili hawauzwi kwa senti moja tu? Lakini hakuna hata mmoja wao atakayeanguka chini pasipo Baba yenu kujua. 30 Hata nywele za vichwa vyenu zote zimehesabiwa. 31 Hivyo msiogope; kwa maana ninyi ni wa thamani kubwa kuliko shomoro wengi.