82 Bible Verses About Fear and Worry

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Fear and Worry
  1. 4 Furahini katika Bwana siku zote, tena nasema furahini! 5 Upole wenu na ujulikane na watu wote. Bwana yu karibu. 6 Msijisumbue kwa jambo lolote, bali katika kila jambo kwa kuomba na kusihi pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. 7 Nayo amani ya Mungu, inayopita fahamu zote, itailinda mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.

    8 Hatimaye, ndugu zangu, mambo yote yaliyo ya kweli, yoyote yaliyo na sifa njema, yoyote yaliyo ya haki, yoyote yaliyo safi, yoyote ya kupendeza, yoyote yenye staha, ukiwepo uzuri wowote, pakiwepo chochote kinachostahili kusifiwa, tafakarini mambo hayo. 9 Mambo yote mliyojifunza au kuyapokea au kuyasikia kutoka kwangu, au kuyaona kwangu, yatendeni hayo. Naye Mungu wa amani atakuwa pamoja nanyi.

  2. 6 Basi, nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake. 7 Mtwikeni yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana na mambo yenu.

  3. 8 “Lakini wewe, ee Israeli, mtumishi wangu,

    Yakobo, niliyemchagua,

    ninyi wazao wa Abrahamu rafiki yangu,

    9 nilikuchukua toka miisho ya dunia,

    nilikuita kutoka pembe zake za mbali.

    Nilisema, ‘Wewe ni mtumishi wangu’;

    nimekuchagua, wala sikukukataa.

    10 Hivyo usiogope, kwa maana niko pamoja nawe;

    usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako.

    Nitakutia nguvu na kukusaidia;

    nitakutegemeza kwa mkono wa kuume wa haki yangu.

    11 “Wote walioona hasira dhidi yako

    hakika wataaibika na kutahayarika,

    wale wakupingao

    watakuwa kama vile si kitu, na kuangamia.

    12 Ingawa utawatafuta adui zako,

    hutawaona.

    Wale wanaopigana vita dhidi yako

    watakuwa kama vile si kitu kabisa.

    13 Kwa maana Mimi ndimi Bwana, Mungu wako,

    nikushikaye mkono wako wa kuume

    na kukuambia, Usiwe na hofu,

    nitakusaidia.

    14 Usiogope, ee Yakobo uliye mdudu,

    ee Israeli uliye mdogo,

    kwa kuwa Mimi mwenyewe nitakusaidia,” asema Bwana,

    Mkombozi wako, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli.

  4. 4 Nilimtafuta Bwana naye akanijibu,

    akaniokoa kwenye hofu zangu zote.

    5 Wale wamtazamao hutiwa nuru,

    nyuso zao hazifunikwi na aibu kamwe.

    6 Maskini huyu alimwita Bwana, naye akamsikia,

    akamwokoa katika taabu zake zote.

    7 Malaika wa Bwana hufanya kituo

    akiwazunguka wale wamchao,

    naye huwaokoa.

    8 Onjeni mwone kwamba Bwana ni mwema,

    heri mtu yule anayemkimbilia.

    9 Mcheni Bwana enyi watakatifu wake,

    kwa maana wale wamchao

    hawapungukiwi na chochote.

  5. 26 Lakini huyo Msaidizi, yaani, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwenu kwa Jina langu, atawafundisha mambo yote na kuwakumbusha yote niliyowaambia. 27 Amani nawaachia, amani yangu nawapa, amani hii niwapayo si kama ile ulimwengu utoayo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiogope.

    28 “Mlinisikia nikisema, ‘Ninakwenda zangu, lakini nitarudi tena.’ Kama kweli mngelinipenda mngelifurahi kwa kuwa naenda kwa Baba, kwani Baba ni mkuu kuniliko mimi.

  6. 26 Vivyo hivyo, Roho hutusaidia katika udhaifu wetu, kwa sababu hatujui kuomba ipasavyo. Lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa uchungu usioweza kutamkwa. 27 Naye Mungu aichunguzaye mioyo, anaijua nia ya Roho, kwa sababu Roho huwaombea watakatifu sawasawa na mapenzi ya Mungu.

    28 Nasi tunajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hutenda kazi pamoja na wote wampendao, katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.

  7. Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Njiwa mkimya wa mbali.” Utenzi wa Daudi. Baada ya kukamatwa na Wafilisti huko Gathi.

    1 Ee Mungu unihurumie, maana watu wananifuatia vikali;

    mchana kutwa wanazidisha mashambulizi yao.

    2 Wasingiziaji wangu wananifuatia mchana kutwa,

    wengi wananishambulia kwa kiburi chao.

    3 Wakati ninapoogopa,

    nitakutumaini wewe.

    4 Katika Mungu, ambaye neno lake ninalisifu,

    katika Mungu ninatumaini; sitaogopa.

    Mwanadamu apatikanaye na kufa,

    atanitenda nini?

  8. 24 “Hakuna mtu awezaye kuwatumikia mabwana wawili. Kwa kuwa atamchukia huyu na kumpenda yule mwingine, au atashikamana sana na huyu na kumdharau yule mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu pamoja na Mali.

    25 “Kwa hiyo nawaambia, msisumbukie maisha yenu kwamba mtakula nini au mtakunywa nini; au msumbukie miili yenu kwamba mtavaa nini. Je, maisha si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi? 26 Waangalieni ndege wa angani; wao hawapandi wala hawavuni au kuweka ghalani, lakini Baba yenu wa mbinguni huwalisha. Je, ninyi si wa thamani zaidi kuliko hao ndege? 27 Ni nani miongoni mwenu ambaye kwa kujitaabisha kwake anaweza kujiongezea hata saa moja zaidi katika maisha yake?

    28 “Nanyi kwa nini mnajitaabisha kwa ajili ya mavazi? Fikirini maua ya shambani yameavyo. Hayafanyi kazi wala hayafumi. 29 Lakini nawaambia, hata Solomoni katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo ya hayo maua. 30 Basi ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya shambani, ambayo leo yapo na kesho yanatupwa motoni, je, hatawavika ninyi vizuri zaidi, enyi wa imani haba? 31 Kwa hiyo msiwe na wasiwasi, mkisema, ‘Tutakula nini?’ au ‘Tutakunywa nini?’ au ‘Tutavaa nini?’ 32 Watu wasiomjua Mungu ndio wanaoshindania hayo, lakini Baba yenu wa mbinguni anafahamu kuwa mnahitaji haya yote. 33 Lakini utafuteni kwanza Ufalme wa Mungu na haki yake, na haya yote atawapa pia. 34 Kwa hiyo msiwe na wasiwasi kuhusu kesho, kwa sababu kesho itajitaabikia yenyewe. Yatosha kwa siku masumbufu yake.

  9. 6 Kwa sababu hii nakukumbusha uchochee ile karama ya Mungu, iliyowekwa ndani yako nilipokuwekea mikono yangu. 7 Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali roho ya nguvu, ya upendo na ya moyo wa kiasi.

  10. 16 Hivyo nasi twajua na kulitumainia pendo la Mungu alilo nalo kwa ajili yetu.

    Mungu ni Upendo. Kila akaaye katika upendo hukaa ndani ya Mungu na Mungu hukaa ndani yake. 17 Kwa njia hii, pendo hukamilishwa miongoni mwetu ili tupate kuwa na ujasiri katika siku ya hukumu, kwa sababu kama alivyo ndivyo tulivyo sisi katika ulimwengu huu. 18 Katika pendo hakuna hofu. Lakini pendo lililo kamili huitupa nje hofu, kwa sababu hofu inahusika na adhabu. Kila mwenye hofu hakukamilika katika pendo.

    19 Twampenda yeye kwa sababu yeye alitupenda kwanza.

  11. Zaburi ya Daudi.

    1 Bwana ndiye mchungaji wangu,

    sitapungukiwa na kitu.

    2 Hunilaza katika malisho

    ya majani mabichi,

    kando ya maji matulivu huniongoza,

    3 hunihuisha nafsi yangu.

    Huniongoza katika njia za haki

    kwa ajili ya jina lake.

    4 Hata kama nikipita katikati

    ya bonde la uvuli wa mauti,

    sitaogopa mabaya,

    kwa maana wewe upo pamoja nami;

    fimbo yako na mkongojo wako

    vyanifariji.

  12. 22 Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake: “Kwa hiyo nawaambia, msisumbukie maisha yenu kwamba mtakula nini; au msumbukie miili yenu kwamba mtavaa nini. 23 Maisha ni zaidi ya chakula, na mwili ni zaidi ya mavazi. 24 Fikirini ndege! Wao hawapandi wala hawavuni, hawana ghala wala popote pa kuhifadhi nafaka; lakini Mungu huwalisha. Ninyi ni wa thamani zaidi kuliko ndege! 25 Ni nani miongoni mwenu ambaye kwa kujitaabisha kwake anaweza kujiongezea hata saa moja zaidi katika maisha yake? 26 Kama hamwezi kufanya jambo dogo kama hilo, kwa nini basi kuyasumbukia hayo mengine?

    27 “Angalieni maua jinsi yameavyo: Hayafanyi kazi wala hayafumi. Lakini nawaambia, hata Solomoni katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo ya hayo maua. 28 Basi ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya shambani, ambayo leo yapo, na kesho yanatupwa motoni, si atawavika ninyi vizuri zaidi, enyi wa imani haba! 29 Wala msisumbuke mioyoni mwenu mtakula nini au mtakunywa nini. Msiwe na wasiwasi juu ya haya. 30 Watu wa mataifa ya duniani husumbuka sana kuhusu vitu hivi vyote, lakini Baba yenu anafahamu kuwa mnahitaji haya yote. 31 Bali utafuteni Ufalme wa Mungu, na haya yote atawapa pia.

    32 “Msiogope enyi kundi dogo, kwa maana Baba yenu ameona vyema kuwapa ninyi Ufalme. 33 Uzeni mali zenu mkawape maskini. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, mkajiwekee hazina mbinguni isiyokwisha, mahali ambapo mwizi hakaribii wala nondo haharibu. 34 Kwa sababu mahali hazina yako ilipo, hapo ndipo moyo wako utakapokuwa pia.

  13. 5 Yalindeni maisha yenu msiwe na tabia ya kupenda fedha, bali mridhike na vile mlivyo navyo, kwa sababu Mungu amesema,

    “Kamwe sitakuacha,

    wala sitakupungukia.”

    6 Kwa hiyo tunaweza kusema kwa ujasiri,

    “Bwana ni msaada wangu; sitaogopa.

    Mwanadamu anaweza kunitenda nini?”

  14. 1 Lakini sasa hili ndilo asemalo Bwana,

    yeye aliyekuumba, ee Yakobo,

    yeye aliyekuhuluku, ee Israeli:

    “Usiogope kwa maana nimekukomboa,

    nimekuita wewe kwa jina lako, wewe u wangu.

    2 Unapopita kwenye maji makuu,

    nitakuwa pamoja nawe,

    unapopita katika mito ya maji,

    hayatakugharikisha.

    Utakapopita katika moto,

    hutaungua,

    miali ya moto haitakuunguza.

    3 Kwa kuwa Mimi ndimi Bwana, Mungu wako,

    yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, Mwokozi wako.

    Ninaitoa Misri kuwa fidia yako,

    Kushi na Seba badala yako.

    4 Kwa kuwa wewe ni wa thamani na wa kuheshimiwa machoni pangu,

    nami kwa kuwa ninakupenda,

    nitatoa watu badala yako

    na mataifa badala ya maisha yako.

    5 Usiogope, kwa kuwa mimi nipo pamoja nawe,

    nitawaleta watoto wako kutoka mashariki,

    na kukukusanya kutoka magharibi.

  15. Zaburi ya Daudi.

    1 Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu,

    nimwogope nani?

    Bwana ni ngome ya uzima wangu,

    nimhofu nani?

    2 Waovu watakaposogea dhidi yangu

    ili wanile nyama yangu,

    adui zangu na watesi wangu watakaponishambulia,

    watajikwaa na kuanguka.

    3 Hata jeshi linizunguke pande zote,

    moyo wangu hautaogopa;

    hata vita vitokee dhidi yangu,

    hata hapo nitakuwa na ujasiri.

  16. 17 Kama Bwana asingelinisaidia upesi,

    ningelikuwa ninaishi katika ukimya wa kifo.

    18 Niliposema, “Mguu wangu unateleza,”

    Ee Bwana, upendo wako ulinishikilia.

    19 Wakati wasiwasi ulipokuwa mwingi ndani yangu,

    faraja yako ilinipa furaha nafsini mwangu.

    20 Je, kiti cha utawala wa udhalimu kitajiunga nawe,

    ule utawala uletao taabu kutokana na sheria zake?

  17. 5 Hakuna mtu yeyote atakayeweza kushindana na wewe siku zote za maisha yako. Kama vile nilivyokuwa pamoja na Mose, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe, sitakuacha wala sitakupungukia.

    6 “Uwe hodari na shujaa, kwa sababu wewe ndiwe utakayewaongoza watu hawa kuirithi nchi niliyowaapia baba zao kuwapa. 7 Uwe hodari na uwe na ushujaa mwingi. Uwe na bidii kutii sheria yote aliyokupa Mose mtumishi wangu, usiiache kwa kugeuka kuelekea kuume au kushoto, ili upate kufanikiwa popote uendako. 8 Usiache Kitabu hiki cha Sheria kiondoke kinywani mwako; yatafakari maneno yake usiku na mchana, ili upate kuwa mwangalifu kufanya kila kitu sawasawa na yote yaliyoandikwa ndani yake. Ndipo utakapofanikiwa na kisha utastawi. 9 Je, si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na shujaa. Usihofu wala usivunjike moyo, kwa kuwa Bwana Mungu wako atakuwa pamoja nawe kokote uendako.”

  18. 22 Mtwike Bwana fadhaa zako,

    naye atakutegemeza,

    hatamwacha kamwe mwenye haki wake aanguke.

    23 Lakini wewe, Ee Mungu,

    utawashusha waovu katika shimo la uharibifu.

    Wenye kiu ya kumwaga damu na wenye hila,

    hawataishi nusu ya siku zao.

    Lakini mimi ninakutumaini wewe.

  19. 28 “Njooni kwangu, ninyi nyote mnaotaabika na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. 29 Jifungeni nira yangu, mjifunze kutoka kwangu, kwa maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtapata raha nafsini mwenu. 30 Kwa maana nira yangu ni laini na mzigo wangu ni mwepesi.”

  20. 5 Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote

    wala usizitegemee akili zako mwenyewe;

    6 katika njia zako zote mkiri yeye,

    naye atayanyoosha mapito yako.

    7 Usiwe mwenye hekima machoni pako mwenyewe;

    mche Bwana ukajiepushe na uovu.

    8 Hii itakuletea afya mwilini mwako,

    na mafuta kwenye mifupa yako.

  21. 35 Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je, ni shida au taabu au mateso au njaa au uchi au hatari au upanga? 36 Kama ilivyoandikwa:

    “Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa;

    tumehesabiwa kama kondoo wa kuchinjwa.”

    37 Lakini katika mambo haya yote tunashinda, naam na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. 38 Kwa maana nimekwisha kujua kwa hakika ya kuwa sio mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuja, wala wenye uwezo, 39 wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kingine chochote zitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu, Bwana wetu.

  22. 25 Moyo wa wasiwasi humlemea mtu,

    bali neno la huruma humfurahisha.

  23. Kwa mwimbishaji. Zaburi ya wana wa Kora. Mtindo wa alamothi.

    1 Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu,

    msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso.

    2 Kwa hiyo hatutaogopa, hata kama dunia ikiondolewa

    nayo milima ikiangukia moyoni mwa bahari.

    3 Hata kama maji yake yatanguruma na kuumuka,

    milima nayo ikitetemeka kwa mawimbi yake.

  24. 12 Kwa maana macho ya Bwana

    huwaelekea wenye haki,

    na masikio yake yako makini

    kusikiliza maombi yao.

    Bali uso wa Bwana uko kinyume

    na watendao maovu.”

    13 Basi, ni nani atakayewadhuru mkiwa wenye juhudi katika kutenda mema? 14 Lakini mmebarikiwa hata kama ikiwalazimu kuteseka kwa ajili ya haki. “Msiogope vitisho vyao, wala msiwe na wasiwasi.” 15 Bali mtakaseni Kristo kuwa Bwana mioyoni mwenu. Siku zote mwe tayari kumjibu mtu yeyote atakayewauliza kuhusu sababu ya tumaini lililomo ndani yenu. Lakini fanyeni hivyo kwa upole na kwa heshima, 16 mkizitunza dhamiri zenu ziwe safi, ili wale wasemao mabaya dhidi ya mwenendo wenu mzuri katika Kristo waaibike kwa ajili ya masingizio yao.

    17 Kwa maana ni afadhali kupata mateso kwa ajili ya kutenda mema, kama kuteseka huko ndiyo mapenzi ya Mungu, kuliko kuteseka kwa kutenda maovu.

  25. 26 “Kwa hiyo msiwaogope hao, kwa maana hakuna kilichofichika ambacho hakitafunuliwa, wala hakuna siri ambayo haitajulikana. 27 Ninalowaambia gizani, ninyi lisemeni mchana peupe. Na lile mnalosikia likinongʼonwa masikioni mwenu, lihubirini juu ya nyumba. 28 Msiwaogope wale wauao mwili lakini hawawezi kuua roho. Afadhali mwogopeni yeye awezaye kuiangamiza roho na mwili katika jehanamu. 29 Je, shomoro wawili hawauzwi kwa senti moja tu? Lakini hakuna hata mmoja wao atakayeanguka chini pasipo Baba yenu kujua. 30 Hata nywele za vichwa vyenu zote zimehesabiwa. 31 Hivyo msiogope; kwa maana ninyi ni wa thamani kubwa kuliko shomoro wengi.

  26. Zaburi ya Daudi.

    1 Usisumbuke kwa ajili ya watendao maovu,

    wala usiwaonee wivu watendao mabaya,

    2 kwa maana kama majani watanyauka mara,

    kama mimea ya kijani watakufa mara.

    3 Mtumaini Bwana na utende yaliyo mema;

    Kaa katika nchi ukafurahie malisho salama.

    4 Jifurahishe katika Bwana

    naye atakupa haja za moyo wako.

    5 Mkabidhi Bwana njia yako,

    mtumaini yeye, naye atatenda hili:

    6 Yeye atafanya haki yako ingʼae kama mapambazuko,

    na hukumu ya shauri lako kama jua la adhuhuri.

    7 Tulia mbele za Bwana

    na umngojee kwa uvumilivu;

    usisumbuke watu wanapofanikiwa katika njia zao,

    wanapotekeleza mipango yao miovu.

    8 Epuka hasira na uache ghadhabu,

    usihangaike: itakuongoza tu kutenda uovu.

    9 Kwa maana waovu watakatiliwa mbali,

    bali wale wanaomtumaini Bwana watairithi nchi.

  27. 3 Itieni nguvu mikono iliyo dhaifu,

    yafanyeni imara magoti yaliyolegea,

    4 waambieni wale wenye mioyo ya hofu,

    “Kuweni hodari, msiogope;

    tazama, Mungu wenu atakuja,

    pamoja na malipo ya Mungu,

    atakuja na kuwaokoa ninyi.”

  28. 5 Wakati wa maumivu yangu makuu nilimlilia Bwana,

    naye akanijibu kwa kuniweka huru.

    6 Bwana yuko pamoja nami, sitaogopa.

    Mwanadamu anaweza kunitenda nini?

    7 Bwana yuko pamoja nami,

    yeye ni msaidizi wangu.

    Nitawatazama adui zangu

    wakiwa wameshindwa.

    8 Ni bora kumkimbilia Bwana

    kuliko kumtumainia mwanadamu.

  29. 11 Kwa maana ninajua mipango niliyo nayo kwa ajili yenu,” asema Bwana, “ni mipango ya kuwafanikisha na wala si ya kuwadhuru, ni mipango ya kuwapa tumaini katika siku zijazo. 12 Kisha mtaniita, na mtakuja na kuniomba, nami nitawasikiliza. 13 Mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote. 14 Nitaonekana kwenu,” asema Bwana, “nami nitawarudisha watu wenu waliotekwa. Nitawakusanya kutoka mataifa yote na mahali pote nilipokuwa nimewafukuzia, nami nitawarudisha mahali ambapo nilikuwa nimewatoa walipochukuliwa uhamishoni,” asema Bwana.

  30. 1 Yesu akawaambia, “Msifadhaike mioyoni mwenu, mnamwamini Mungu, niaminini na mimi pia. 2 Nyumbani kwa Baba yangu kuna makao mengi. Kama sivyo, ningeliwaambia. Naenda kuwaandalia makao. 3 Nami nikienda na kuwaandalia makao, nitarudi tena na kuwachukua mkae pamoja nami, ili mahali nilipo, nanyi mpate kuwepo. 4 Ninyi mnajua njia ya kufika ninakokwenda.”

  31. 6 Kuweni imara na moyo wa ushujaa. Msiogope wala msifadhaike kwa sababu yao, kwa kuwa Bwana Mungu wenu anakwenda pamoja nanyi; kamwe hatawaacha wala hatawatupa ninyi.”

  32. 5 Hili ndilo asemalo Bwana:

    “Amelaaniwa yeye amtegemeaye mwanadamu,

    ategemeaye mwenye mwili

    kwa ajili ya nguvu zake,

    ambaye moyo wake

    umemwacha Bwana.

    6 Atakuwa kama kichaka cha jangwani;

    hataona mafanikio yatakapokuja.

    Ataishi katika sehemu zisizo na maji,

    katika nchi ya chumvi ambapo

    hakuna yeyote aishiye humo.

    7 “Lakini amebarikiwa mtu ambaye tumaini lake ni katika Bwana,

    ambaye matumaini yake ni katika Bwana.

    8 Atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji

    uenezao mizizi yake karibu na kijito cha maji.

    Hauogopi wakati wa joto ujapo;

    majani yake ni mabichi daima.

    Hauna hofu katika mwaka wa ukame

    na hautaacha kuzaa matunda.”

  33. 11 Sisemi hivyo kwa vile nina mahitaji, la! Kwa maana nimejifunza kuridhika katika hali yoyote. 12 Ninajua kupungukiwa, pia ninajua kuwa na vingi. Nimejifunza siri ya kuridhika katika kila hali, wakati wa kushiba na wakati wa kuona njaa, wakati wa kuwa na vingi na wakati wa kupungukiwa. 13 Naweza kuyafanya mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.

  34. 23 Naye alipoingia kwenye mashua, wanafunzi wake wakamfuata. 24 Ghafula, kukainuka dhoruba kali baharini hata mashua ikaanza kufunikwa na mawimbi, lakini Yesu alikuwa amelala usingizi. 25 Wanafunzi wake wakamwendea na kumwamsha, wakisema, “Bwana, tuokoe! Tunazama!”

    26 Naye Yesu akawaambia, “Kwa nini mnaogopa, enyi wa imani haba?” Kisha akaamka na kukemea dhoruba na mawimbi, nako kukawa shwari kabisa.

    27 Wale watu wakashangaa, wakisema, “Ni mtu wa namna gani huyu? Hata upepo na mawimbi vinamtii!”

  35. 14 Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio watoto wa Mungu. 15 Kwa maana hamkupokea roho ya utumwa iwaleteayo tena hofu, bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambaye kwa yeye twalia, “Abba, yaani, Baba,” 16 Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu ya kwamba sisi tu watoto wa Mungu. 17 Hivyo, ikiwa sisi ni watoto, basi tu warithi, warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo, naam, tukiteswa pamoja naye tupate pia kutukuzwa pamoja naye.

    18 Nayahesabu mateso yetu ya wakati huu kuwa si kitu kulinganisha na utukufu utakaodhihirishwa kwetu. 19 Kwa maana viumbe vyote vinangoja kwa shauku kudhihirishwa kwa watoto wa Mungu.

  36. 4 “Nawaambieni rafiki zangu, msiwaogope wale wauao mwili, lakini baada ya hilo hawawezi kufanya lolote zaidi. 5 Lakini nitawaambia nani wa kumwogopa: Mwogopeni yule ambaye baada ya kuua mwili, ana mamlaka ya kuwatupa motoni. Naam, nawaambia, mwogopeni huyo! 6 Mnajua kwamba shomoro watano huuzwa kwa senti mbili? Lakini Mungu hamsahau hata mmoja wao. 7 Naam, hata nywele za vichwa vyenu zote zimehesabiwa. Hivyo msiogope, kwa maana ninyi ni wa thamani kubwa kuliko shomoro wengi.

    8 “Ninawaambia kwamba yeyote atakayenikiri mbele ya watu, Mwana wa Adamu naye atamkiri mbele za malaika wa Mungu. 9 Lakini yeye atakayenikana mimi mbele ya watu, Mwana wa Adamu naye atamkana mbele ya malaika wa Mungu.

  37. 7 Hataogopa habari mbaya,

    moyo wake ni thabiti, ukimtegemea Bwana.

    8 Moyo wake ni salama, hatakuwa na hofu,

    mwishoni ataona ushindi dhidi ya adui zake.

  38. 18 Watu walipoona ngurumo na radi, na kusikia mlio wa tarumbeta, na kuuona mlima katika moshi, walitetemeka kwa woga. Wakasimama mbali 19 na wakamwambia Mose, “Sema nasi wewe mwenyewe, nasi tutakusikiliza. Lakini usimwache Mungu aseme nasi, la sivyo tutakufa.”

    20 Mose akawaambia watu, “Msiogope! Mungu amekuja kuwajaribu, ili kwamba hofu ya Mungu iwakalie, msitende dhambi.”

  39. 10 “Tulieni, mjue ya kwamba mimi ndimi Mungu;

    nitatukuzwa katikati ya mataifa,

    nitatukuzwa katika dunia.”

    11 Bwana Mwenye Nguvu Zote yu pamoja nasi;

    Mungu wa Yakobo ni ngome yetu.

  40. Wimbo wa kwenda juu.

    1 Nayainua macho yangu nitazame vilima,

    msaada wangu utatoka wapi?

    2 Msaada wangu hutoka kwa Bwana,

    Muumba wa mbingu na dunia.

  41. 30 Hata vijana huchoka na kulegea,

    nao vijana wanaume hujikwaa na kuanguka,

    31 bali wale wamtumainio Bwana

    atafanya upya nguvu zao.

    Watapaa juu kwa mbawa kama tai;

    watapiga mbio wala hawatachoka,

    watatembea kwa miguu wala hawatazimia.

  42. 22 Ile mbegu iliyopandwa katika miiba ni yule mtu alisikiaye neno, lakini masumbufu ya maisha haya na udanganyifu wa mali hulisonga lile neno na kulifanya lisizae matunda.

  43. 7 Kisha Mose akamwita Yoshua na akamwambia mbele ya Israeli wote, “Uwe imara na moyo wa ushujaa, kwa kuwa ni lazima uende na watu hawa katika nchi ile Bwana aliyowaapia baba zao kuwapa, nawe ni lazima uwagawie kama urithi wao. 8 Bwana mwenyewe atakutangulia naye atakuwa pamoja nawe; kamwe hatakuacha wala hatakutupa. Usiogope, wala usifadhaike.”

  44. 1 Yeye akaaye mahali pa salama pake Yeye Aliye Juu Sana,

    atadumu katika uvuli wake Mwenyezi.

    2 Nitasema kumhusu Bwana, “Yeye ndiye kimbilio langu na ngome yangu,

    Mungu wangu, ambaye ninamtumaini.”

    3 Hakika yeye ataniokoa na mtego wa mwindaji,

    na maradhi ya kuambukiza ya kuua.

    4 Atakufunika kwa manyoya yake,

    chini ya mbawa zake utapata kimbilio,

    uaminifu wake utakuwa ngao na kinga yako.

    5 Hutaogopa vitisho vya usiku,

    wala mshale urukao mchana,

    6 wala maradhi ya kuambukiza

    yanayonyemelea gizani,

    wala tauni iharibuyo adhuhuri.

  45. 16 Basi, Bwana wa amani mwenyewe awapeni amani nyakati zote na kwa kila njia. Bwana awe nanyi nyote.

  46. 13 Utamcha Bwana Mungu wako, na umtumikie yeye peke yake na kuapa kwa jina lake. 14 Usifuate miungu mingine, miungu ya mataifa yanayokuzunguka; 15 kwa kuwa Bwana Mungu wako, ambaye yuko katikati yako, ni Mungu mwenye wivu na hasira yake itawaka dhidi yako, naye atakuangamiza kutoka uso wa nchi.

  47. 39 Akaamka, akaukemea ule upepo, akayaambia yale mawimbi, “Uwe kimya! Tulia!” Ule upepo ukatulia, kukawa shwari kabisa.

    40 Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kwa nini mnaogopa hivyo? Je, bado hamna imani?”

    41 Nao wakawa wameogopa sana, wakaulizana, “Ni nani huyu ambaye hata upepo na mawimbi vinamtii?”

  48. 32 Saa inakuja, naam, imekwisha kuwadia, mtakapotawanyika kila mmoja kwenda nyumbani kwake na kuniacha peke yangu. Lakini mimi siko peke yangu kwa sababu Baba yu pamoja nami. 33 Nimewaambia mambo haya, ili mpate kuwa na amani mkiwa ndani yangu. Ulimwenguni mtapata dhiki. Lakini jipeni moyo, kwa maana mimi nimeushinda ulimwengu.”

  49. 17 Nilipomwona, nilianguka miguuni pake kama aliyekufa. Ndipo akauweka mkono wake wa kuume juu yangu na kusema: “Usiogope, Mimi ndiye wa Kwanza na wa Mwisho. 18 Mimi ni Yeye Aliye Hai, niliyekuwa nimekufa, na tazama, ni hai milele na milele! Nami ninazo funguo za mauti na kuzimu.

  50. 40 Lakini Martha alikuwa akihangaika na maandalizi yote yaliyokuwa yafanyike. Martha akaja kwa Yesu na kumuuliza, “Bwana, hujali kwamba ndugu yangu ameniachia kazi zote mwenyewe? Basi mwambie anisaidie.”

    41 Lakini Bwana akamjibu, “Martha, Martha, mbona unasumbuka na kuhangaika na mengi? 42 Lakini kunahitajika kitu kimoja tu. Maria amechagua kile kilicho bora, wala hakuna mtu atakayemwondolea.”

  51. 32 Ningetaka msiwe na masumbufu. Mwanaume ambaye hajaoa anajishughulisha na mambo ya Bwana, jinsi ya kumpendeza Bwana. 33 Lakini mwanaume aliyeoa anajishughulisha na mambo ya dunia, jinsi ya kumfurahisha mkewe, 34 na mawazo yake yamegawanyika. Mwanamke asiyeolewa hujishughulisha na mambo ya Bwana: lengo lake ni awe mtakatifu kimwili na kiroho. Lakini yule aliyeolewa hujishughulisha na mambo ya dunia, jinsi atakavyoweza kumfurahisha mumewe.

  52. 12 Ni nani basi, mtu yule anayemcha Bwana?

    Atamfundisha katika njia

    atakayoichagua kwa ajili yake.

    13 Mtu huyo atafanikiwa maishani mwake,

    nao wazao wake watairithi nchi.

    14 Siri ya Bwana iko kwa wale wamchao,

    yeye huwajulisha agano lake.

  53. 10 Kumcha Bwana ndicho chanzo cha hekima,

    wote wanaozifuata amri zake wana busara.

    Sifa zake zadumu milele.

  54. 26 Yeye amchaye Bwana ana ngome salama,

    na kwa watoto wake itakuwa kimbilio.

    27 Kumcha Bwana ni chemchemi ya uzima,

    ili kumwepusha mtu na mitego ya mauti.

  55. 15 Bwana amekuondolea adhabu yako,

    amewarudisha nyuma adui zako.

    Bwana, Mfalme wa Israeli, yu pamoja nawe;

    kamwe hutaogopa tena madhara yoyote.

    16 Katika siku hiyo watauambia Yerusalemu,

    “Usiogope, ee Sayuni;

    usiiache mikono yako ilegee.

    17 Bwana Mungu wako yu pamoja nawe,

    yeye ni mwenye nguvu kuokoa.

    Atakufurahia kwa furaha kubwa,

    atakutuliza kwa pendo lake,

    atakufurahia kwa kuimba.”

  56. 36 Aliposikia hayo waliyosema, Yesu akamwambia huyo kiongozi wa sinagogi, “Usiogope. Amini tu.”

  57. 48 Akawaona wanafunzi wake wanahangaika na kupiga makasia kwa nguvu, kwa sababu upepo ulikuwa wa mbisho. Wakati wa zamu ya nne ya usiku, Yesu akawaendea wanafunzi wake, akiwa anatembea juu ya maji. Alikuwa karibu kuwapita, 49 lakini walipomwona akitembea juu ya maji, wakadhani ni mzimu. Wakapiga yowe, 50 kwa sababu wote walipomwona waliogopa.

    Mara Yesu akasema nao, akawaambia, “Jipeni moyo! Ni mimi. Msiogope!” 51 Akapanda ndani ya mashua nao, na ule upepo ukakoma! Wakashangaa kabisa,

  58. 22 Msiwaogope, Bwana Mungu wenu atapigana kwa ajili yenu.”

  59. 1 Msifuni Bwana.

    Heri mtu yule amchaye Bwana,

    mtu yule apendezwaye sana na amri zake.

  60. 10 “Kumcha Bwana ndicho chanzo cha hekima,

    na kumjua Aliye Mtakatifu ni ufahamu.

  61. 11 “Watakapowapeleka katika masinagogi, na mbele ya watawala na wenye mamlaka, msiwe na wasiwasi kuhusu namna mtakavyojitetea au mtakavyosema. 12 Kwa maana Roho Mtakatifu atawafundisha wakati huo huo mnachopaswa kusema.”

  62. 22 Mtu atapata nini kwa taabu yote na kuhangaika kwa bidii katika kazi anayotaabikia chini ya jua? 23 Siku zake zote kazi yake ni maumivu na masikitiko, hata usiku akili yake haipati mapumziko. Hili nalo pia ni ubatili.

  63. 12 Kwa hiyo, wapenzi wangu, kama vile ambavyo mmekuwa mkitii siku zote, si tu wakati nikiwa pamoja nanyi, bali sasa zaidi sana nisipokuwepo, utimizeni wokovu wenu kwa kuogopa na kutetemeka,

  64. 26 Kama tukiendelea kutenda dhambi kwa makusudi baada ya kupokea ufahamu wa ile kweli, haibaki tena dhabihu kwa ajili ya dhambi. 27 Lakini kinachobaki ni kungoja kwa hofu hukumu ya moto uwakao, utakaowaangamiza adui za Mungu.

  65. 15 Kesho yake asubuhi na mapema, mtumishi wa mtu wa Mungu alipoamka na kutoka nje, jeshi, pamoja na farasi na magari ya vita, likawa limeuzunguka mji. Mtumishi wake akasema, “Ole wetu, bwana wangu! Tutafanya nini?”

    16 Nabii akajibu, “Usiogope. Wale walio pamoja nasi ni wengi zaidi kuliko wale walio pamoja nao.”

    17 Kisha Elisha akaomba, “Ee Bwana, mfumbue macho huyu mtumishi ili apate kuona.” Ndipo Bwana akayafumbua macho ya yule mtumishi, naye akatazama na kuona vilima vimejaa farasi na magari ya moto, yamemzunguka Elisha pande zote.

  66. 26 Wanafunzi wake walipomwona akitembea juu ya maji, waliingiwa na hofu kuu, wakasema, “Ni mzimu.” Wakapiga yowe kwa kuogopa.

    27 Lakini mara Yesu akasema nao, akawaambia, “Jipeni moyo! Ni mimi. Msiogope.”

  67. 3 Lakini wewe, Ee Bwana, ni ngao pande zote;

    umeniwekea utukufu na kuinua kichwa changu.

    4 Ninamlilia Bwana kwa sauti kuu,

    naye ananijibu kutoka mlima wake mtakatifu.

    5 Ninajilaza na kupata usingizi;

    naamka tena, kwa maana Bwana hunitegemeza.

    6 Sitaogopa makumi elfu ya adui,

    wanaojipanga dhidi yangu kila upande.

  68. 13 Kama baba alivyo na huruma kwa watoto wake,

    ndivyo Bwana anavyowahurumia wale wanaomcha;

  69. 13 Hii ndiyo jumla ya maneno;

    yote yamekwisha sikiwa:

    Mche Mungu, nawe uzishike amri zake,

    maana kwa jumla ndiyo impasayo mtu.

    14 Kwa maana Mungu ataleta hukumuni kila kazi,

    pamoja na kila neno la siri,

    likiwa jema au baya.

  70. 14 Lakini kusudieni mioyoni mwenu msisumbuke awali kuhusu mtakalosema mbele ya mashtaka. 15 Kwa maana nitawapa maneno na hekima ambayo hakuna hata adui yenu mmoja atakayeweza kushindana nayo wala kuipinga.

  71. 19 Naye Mungu wangu atawajaza ninyi na kila mnachohitaji kwa kadiri ya utajiri wake katika utukufu ndani ya Kristo Yesu.

  72. 1 Baada ya jambo hili, neno la Bwana likamjia Abramu katika maono:

    “Usiogope, Abramu.

    Mimi ni ngao yako,

    na thawabu yako kubwa sana.”

  73. 12 Zekaria alipomwona huyo malaika, akafadhaika sana, akajawa na hofu. 13 Lakini malaika akamwambia, “Usiogope, Zekaria, kwa maana Mungu amesikia maombi yako. Mkeo Elizabeti atakuzalia mtoto wa kiume, nawe utamwita jina lake Yohana.

  74. 28 Zaidi ya hayo yote, nakabiliwa na mzigo wa wajibu wangu kwa makanisa yote.

  75. 10 Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. 11 Vaeni silaha zote za Mungu ili kwamba mweze kuzipinga hila za ibilisi. 12 Kwa maana kushindana kwetu si juu ya nyama na damu, bali dhidi ya falme, mamlaka, dhidi ya wakuu wa giza na majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. 13 Kwa hiyo vaeni silaha zote za Mungu ili mweze kushindana siku ya uovu itakapokuja nanyi mkiisha kufanya yote, simameni imara.

  76. 11 Mtumikieni Bwana kwa hofu

    na mshangilie kwa kutetemeka.

  77. 4 Wale walinzi wa kaburi walimwogopa sana, wakatetemeka hata wakawa kama wafu.

  78. 23 Kumcha Bwana huongoza kwenye uzima,

    kisha mtu hupumzika akiwa ameridhika,

    bila kuguswa na shida.

  79. 57 Ulikuja karibu nilipokuita,

    nawe ukasema, “Usiogope.”

    58 Ee Bwana, ulichukua shauri langu,

    ukaukomboa uhai wangu.

  80. 20 Lakini mara alipoazimu kufanya jambo hili, malaika wa Bwana akamtokea katika ndoto na kusema, “Yosefu mwana wa Daudi, usiogope kumchukua Maria awe mke wako, kwa maana mimba aliyo nayo ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu.

  81. 5 Visiwa vimeliona na kuogopa,

    miisho ya dunia inatetemeka.

    Wanakaribia na kuja mbele,

  82. 25 “Kutakuwa na ishara katika jua, mwezi na nyota. Hapa duniani, mataifa yatakuwa katika dhiki na fadhaa kutokana na ngurumo na misukosuko ya bahari. 26 Watu watazimia roho kutokana na hofu kuu na kuyaona yale mambo yanayotokea duniani, kwa maana nguvu za angani zitatikisika. 27 Wakati huo ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija mawinguni pamoja na uweza na utukufu mkuu. 28 Mambo haya yatakapoanza kutendeka, simameni na mkaviinue vichwa vyenu, kwa sababu ukombozi wenu umekaribia.”