81 Bible Verses About Joy

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Joy
  1. 22 Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, 23 upole na kiasi. Katika mambo kama haya hakuna sheria.

  2. Wimbo wa kwenda juu.

    1 Bwana alipowarejeza mateka Sayuni,

    tulikuwa kama watu walioota ndoto.

    2 Vinywa vyetu vilijaa kicheko,

    ndimi zetu zilijaa nyimbo za shangwe.

    Ndipo iliposemwa miongoni mwa mataifa,

    “Bwana amewatendea mambo makuu.”

    3 Bwana ametutendea mambo makuu,

    nasi tumejaa furaha.

    4 Ee Bwana, turejeshee watu wetu waliotekwa,

    kama vijito katika Negebu.

    5 Wapandao kwa machozi

    watavuna kwa nyimbo za shangwe.

    6 Yeye azichukuaye mbegu zake

    kwenda kupanda, huku akilia,

    atarudi kwa nyimbo za shangwe,

    akichukua miganda ya mavuno yake.

  3. 7 Ninyi mkikaa ndani yangu na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni lolote mtakalo, nanyi mtatendewa. 8 Kwa hiyo Baba yangu hutukuzwa, kwa vile mzaavyo matunda mengi, nanyi mtakuwa wanafunzi wangu.

    9 “Kama vile Baba alivyonipenda mimi, hivyo ndivyo mimi nilivyowapenda ninyi. Basi kaeni katika pendo langu. 10 Mkizishika amri zangu mtakaa katika pendo langu, kama mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake. 11 Nimewaambia mambo haya ili furaha yangu iwe ndani yenu na furaha yenu iwe kamili.

  4. 20 Amin, amin nawaambia, ninyi mtalia na kuomboleza, lakini ulimwengu utafurahi. Ninyi mtahuzunika, lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha. 21 Mwanamke anapokuwa na utungu wa kuzaa huwa na maumivu kwa sababu saa yake imewadia. Lakini mtoto akiisha kuzaliwa, yule mwanamke husahau maumivu hayo kwa sababu ya furaha ya kuzaliwa mtoto ulimwenguni. 22 Hivyo ninyi mna maumivu sasa, lakini nitawaona tena, nayo mioyo yenu itafurahi na furaha yenu hakuna awaondoleaye. 23 Katika siku hiyo hamtaniuliza neno lolote. Amin, amin nawaambia, kama mkimwomba Baba jambo lolote kwa jina langu, yeye atawapa. 24 Mpaka sasa hamjaomba jambo lolote kwa Jina langu. Ombeni nanyi mtapewa, ili furaha yenu ipate kuwa kamili.

  5. 3 Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo! Kwa rehema zake kuu ametuzaa sisi mara ya pili katika tumaini lenye uzima kupitia kwa kufufuka kwa Yesu Kristo kutoka kwa wafu, 4 ili tuupate urithi usioharibika, usio na uchafu, ule usionyauka: uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu, 5 ninyi ambao mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani, hadi uje ule wokovu ulio tayari kufunuliwa nyakati za mwisho. 6 Katika hili mnafurahi sana, ingawa sasa kwa kitambo kidogo mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna nyingi. 7 Haya yamewajia ili kwamba imani yenu, iliyo ya thamani kuliko dhahabu ipoteayo, ingawa hujaribiwa kwa moto, ionekane kuwa halisi na imalizie katika sifa, utukufu na heshima wakati Yesu Kristo atadhihirishwa. 8 Ingawa hamjamwona, mnampenda; tena ingawa sasa hammwoni, mnamwamini na kujawa na furaha isiyoneneka yenye utukufu usioelezeka. 9 Maana mnaupokea wokovu wa roho zenu, ambao ndio lengo la imani yenu.

  6. 8 Nimemweka Bwana mbele yangu daima.

    Kwa sababu yuko mkono wangu wa kuume,

    sitatikisika.

    9 Kwa hiyo moyo wangu unafurahia, na ulimi wangu unashangilia;

    mwili wangu nao utapumzika salama,

    10 kwa maana hutaniacha kaburini,

    wala hutamwacha Mtakatifu Wako kuona uharibifu.

    11 Umenijulisha njia ya uzima;

    utanijaza na furaha mbele zako,

    pamoja na furaha za milele

    katika mkono wako wa kuume.

  7. 2 Ndugu zangu, hesabuni kuwa ni furaha tupu mnapopatwa na majaribu mbalimbali, 3 kwa sababu mnajua ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi. 4 Saburi na iwe na kazi timilifu, ili mpate kuwa wakamilifu, mmekamilishwa, bila kupungukiwa na kitu chochote.

  8. 13 Mungu wa tumaini awajaze ninyi furaha yote na amani katika kumwamini, ili mpate kujawa na tumaini tele kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.

  9. 4 Furahini katika Bwana siku zote, tena nasema furahini! 5 Upole wenu na ujulikane na watu wote. Bwana yu karibu. 6 Msijisumbue kwa jambo lolote, bali katika kila jambo kwa kuomba na kusihi pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. 7 Nayo amani ya Mungu, inayopita fahamu zote, itailinda mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.

  10. 3 Ndipo Yesu akawaambia mfano huu: 4 “Ikiwa mmoja wenu ana kondoo mia moja, naye akapoteza mmoja wao, je, hawaachi wale tisini na tisa nyikani na kwenda kumtafuta huyo aliyepotea mpaka ampate? 5 Naye akishampata, humbeba mabegani mwake kwa furaha 6 na kwenda nyumbani. Kisha huwaita rafiki zake na majirani, na kuwaambia, ‘Furahini pamoja nami; nimempata kondoo wangu aliyepotea.’ 7 Nawaambieni, vivyo hivyo kutakuwa na furaha zaidi mbinguni kwa sababu ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa wenye haki tisini na tisa ambao hawana haja ya kutubu.”

    8 “Au ikiwa mwanamke ana sarafu za fedha kumi, naye akapoteza moja, je, hawashi taa na kufagia nyumba na kuitafuta kwa bidii mpaka aipate? 9 Naye akiisha kuipata, huwaita rafiki zake na majirani na kuwaambia, ‘Furahini pamoja nami; nimeipata ile sarafu yangu ya fedha iliyopotea.’ 10 Vivyo hivyo, nawaambia, kuna furaha mbele ya malaika wa Mungu juu ya mwenye dhambi mmoja atubuye.”

  11. 44 “Ufalme wa Mbinguni unafanana na hazina iliyofichwa shambani, ambayo mtu mmoja alipoiona akaificha tena. Kisha katika furaha yake, akaenda akauza vyote alivyokuwa navyo, akalinunua lile shamba.”

  12. 16 Furahini siku zote; 17 ombeni bila kukoma; 18 shukuruni kwa kila jambo, kwa maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu kwa ajili yenu katika Kristo Yesu.

  13. 17 Kwa maana Ufalme wa Mungu si kula na kunywa, bali ni haki, amani na furaha katika Roho Mtakatifu. 18 Kwa sababu mtu yeyote anayemtumikia Kristo kwa jinsi hii, anampendeza Mungu na kukubaliwa na wanadamu.

  14. 17 Wale sabini na wawili wakarudi kwa furaha, na kusema, “Bwana, hata pepo wachafu wanatutii kwa jina lako.”

    18 Yesu akawaambia, “Nilimwona Shetani akianguka kutoka mbinguni kama umeme wa radi. 19 Tazama nimewapa mamlaka ya kukanyaga nyoka na nge na juu ya nguvu zote za adui; wala hakuna kitu chochote kitakachowadhuru. 20 Basi, msifurahi kwa kuwa pepo wachafu wanawatii, bali furahini kwa kuwa majina yenu yameandikwa mbinguni.”

    21 Wakati huo Yesu akashangilia katika Roho Mtakatifu, akasema, “Nakuhimidi Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa umewaficha mambo haya wenye hekima na wenye elimu, nawe ukawafunulia watoto wadogo. Naam, Baba, kwa kuwa hivyo ndivyo ilivyokupendeza.

    22 “Nimekabidhiwa vitu vyote na Baba yangu. Hakuna mtu amjuaye Mwana ni nani ila Baba, wala hakuna amjuaye Baba ni nani ila Mwana na yeyote ambaye Mwana anapenda kumfunulia.”

  15. 8 Katika eneo lile walikuwako wachungaji waliokuwa wakikaa mashambani, wakilinda makundi yao ya kondoo usiku. 9 Ghafula tazama, malaika wa Bwana akawatokea, nao utukufu wa Bwana ukawangʼaria kotekote, wakaingiwa na hofu. 10 Lakini malaika akawaambia: “Msiogope. Kwa maana tazama nawaletea habari njema za furaha itakayokuwa kwa watu wote. 11 Leo katika mji wa Daudi kwa ajili yenu amezaliwa Mwokozi, ndiye Kristo Bwana.

  16. 6 Nanyi mkawa wafuasi wetu na wa Bwana, ingawa mlipata mateso mengi, mlilipokea lile Neno kwa furaha katika Roho Mtakatifu. 7 Hivyo ninyi mkawa kielelezo kwa waumini wote katika Makedonia na Akaya.

  17. 1 Kwa hiyo, kwa kuwa tumekwisha kuhesabiwa haki kwa imani, tuna amani na Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, 2 ambaye kwa kupitia kwake tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo ndani yake sasa tunasimama, nasi twafurahia katika tumaini letu la kushiriki utukufu wa Mungu. 3 Si hivyo tu, bali twafurahi pia katika mateso, kwa sababu tunajua kuwa mateso huleta saburi, 4 nayo saburi huleta uthabiti wa moyo, na uthabiti wa moyo huleta tumaini, 5 wala tumaini halitukatishi tamaa, kwa sababu Mungu amekwisha kumimina pendo lake mioyoni mwetu kwa njia ya Roho Mtakatifu ambaye ametupatia.

  18. 13 “Lakini sasa naja kwako, nami ninasema mambo haya wakati bado nikiwa ulimwenguni, ili wawe na furaha yangu kamili ndani yao. 14 Nimewapa neno lako, nao ulimwengu umewachukia kwa kuwa wao si wa ulimwengu kama mimi nisivyo wa ulimwengu huu. 15 Siombi kwamba uwaondoe ulimwenguni, bali uwalinde dhidi ya yule mwovu. 16 Wao si wa ulimwengu huu, kama vile mimi nisivyo wa ulimwengu.

  19. 12 Kuweni na furaha katika tumaini, katika dhiki kuweni na saburi, dumuni katika maombi.

  20. 1 Kama kukiwa na jambo lolote la kutia moyo katika kuunganishwa na Kristo, kukiwa faraja yoyote katika upendo wake, kukiwa na ushirika wowote na Roho, kukiwa na wema wowote na huruma, 2 basi ikamilisheni furaha yangu kwa kuwa na nia moja, mkiwa na upendo huo moja, mkiwa wa roho na kusudi moja.

  21. 17 Ingawa mtini hauchanui maua

    na hakuna zabibu juu ya mizabibu,

    ingawaje mzeituni hauzai,

    na hata mashamba hayatoi chakula,

    iwapo hakuna kondoo katika banda,

    wala ngʼombe katika zizi,

    18 hata hivyo nitashangilia katika Bwana,

    nitamfurahia Mungu Mwokozi wangu.

    19 Bwana Mwenyezi ni nguvu yangu;

    huifanya miguu yangu kama miguu ya ayala,

    huniwezesha kupita juu ya vilima.

    Kwa kiongozi wa uimbaji. Kwa vinanda vyangu vya nyuzi.

  22. 11 “Heri ninyi watu watakapowashutumu, na kuwatesa na kunena dhidi yenu mabaya ya aina zote kwa uongo kwa ajili yangu. 12 Furahini na kushangilia kwa maana thawabu yenu ni kubwa mbinguni, kwa kuwa hivyo ndivyo walivyowatesa manabii waliokuwa kabla yenu.

  23. 52 Wanafunzi wakajawa na furaha na Roho Mtakatifu.

  24. 4 Mara nyingi najivuna kwa ajili yenu; naona fahari juu yenu. Nimejawa na faraja. Nina furaha kupita kiasi katika mateso yetu yote.

  25. 1 Hatimaye, ndugu zangu, furahini katika Bwana! Mimi kuwaandikia mambo yale yale hakuniudhi, kwa maana ni kinga kwa ajili yenu.

    2 Jihadharini na mbwa, wale watenda maovu, jihadharini na wale wajikatao miili yao, wasemao ili kuokoka ni lazima kutahiriwa. 3 Kwa maana sisi ndio tulio tohara, sisi tumwabuduo Mungu katika Roho, tunaona fahari katika Kristo Yesu, ambao hatuweki tumaini letu katika mwili,

  26. 12 Wapenzi, msione ajabu kwa yale mateso yanayotukia miongoni mwenu, kana kwamba ni kitu kigeni kinachowapata. 13 Bali furahini kuwa mnashiriki katika mateso ya Kristo, ili mpate kufurahi zaidi wakati utukufu wake utakapofunuliwa. 14 Kama mkitukanwa kwa ajili ya jina la Kristo, mmebarikiwa, kwa sababu Roho wa utukufu na wa Mungu anakaa juu yenu.

  27. 11 Lakini wote wakimbiliao kwako na wafurahi,

    waimbe kwa shangwe daima.

    Ueneze ulinzi wako juu yao,

    ili wale wapendao jina lako

    wapate kukushangilia.

  28. 3 Hatuweki kitu cha kukwaza katika njia ya mtu yeyote, ili huduma yetu isionekane kuwa na lawama. 4 Bali kama watumishi wa Mungu tuonyeshe kwa kila njia: katika saburi nyingi; katika dhiki, katika misiba, na katika shida; 5 katika kupigwa, katika kufungwa gerezani na katika ghasia; katika kazi ngumu, katika kukesha na katika kufunga; 6 katika utakatifu, katika ufahamu, katika uvumilivu, na katika utu wema; katika Roho Mtakatifu na upendo wa kweli; 7 katika maneno ya kweli na katika nguvu za Mungu, kwa silaha za haki za mkono wa kuume na za mkono wa kushoto; 8 katika utukufu na katika kudharauliwa; katika sifa mbaya na katika sifa nzuri; tukiwa kama wadanganyaji, lakini tukiwa wakweli; 9 tukiwa maarufu, lakini tukihesabiwa kama tusiojulikana; tukiwa kama wanaokufa, lakini tunaishi; tukipigwa, lakini hatuuawi; 10 tukiwa kama wenye huzuni, lakini siku zote tukifurahi; tukionekana maskini, lakini tukitajirisha wengi; tukiwa kama wasio na kitu, lakini tuna vitu vyote.

  29. 5 Kwa maana hasira yake ni ya muda mfupi,

    bali upendo wake hudumu siku zote.

    Inawezekana kilio kiwepo usiku kucha,

    lakini asubuhi kukawa na furaha.

  30. 3 Ninamshukuru Mungu wangu kila niwakumbukapo ninyi. 4 Katika maombi yangu yote daima nimekuwa nikiwaombea ninyi nyote kwa furaha, 5 kwa sababu ya kushiriki kwenu katika kueneza Injili, tangu siku ya kwanza hadi leo. 6 Nina hakika kwamba yeye aliyeianza kazi njema mioyoni mwenu, ataiendeleza na kuikamilisha hata siku ya Kristo Yesu.

  31. 6 Wengi wanauliza, “Ni nani awezaye

    kutuonyesha jema lolote?”

    Ee Bwana, tuangazie nuru ya uso wako.

    7 Wewe umejaza moyo wangu kwa furaha kubwa

    kuliko watu waliopata nafaka na divai kwa wingi.

    8 Nitajilaza chini na kulala kwa amani,

    kwa kuwa wewe peke yako, Ee Bwana,

    waniwezesha kukaa kwa salama.

  32. 18 Niliposema, “Mguu wangu unateleza,”

    Ee Bwana, upendo wako ulinishikilia.

    19 Wakati wasiwasi ulipokuwa mwingi ndani yangu,

    faraja yako ilinipa furaha nafsini mwangu.

  33. 25 Kwa maana Daudi asema kumhusu yeye:

    “ ‘Nalimwona Bwana mbele yangu daima.

    Kwa sababu yuko mkono wangu wa kuume,

    sitatikisika.

    26 Kwa hiyo moyo wangu unafurahia,

    na ulimi wangu unashangilia;

    mwili wangu nao utapumzika kwa tumaini.

    27 Kwa maana hutaniacha kaburini,

    wala hutamwacha Aliye Mtakatifu wako kuona uharibifu.

    28 Umenionyesha njia za uzima,

    utanijaza na furaha mbele zako.’

  34. 15 Furahini pamoja na wenye kufurahi, lieni pamoja na wale waliao.

  35. 12 Unirudishie tena furaha ya wokovu wako,

    unipe roho ya utii, ili initegemeze.

    13 Ndipo nitakapowafundisha wakosaji njia zako,

    na wenye dhambi watakugeukia wewe.

  36. 15 Wewe unafahamu, Ee Bwana,

    unikumbuke na unitunze mimi.

    Lipiza kisasi juu ya watesi wangu.

    Kwa uvumilivu wako usiniondolee mbali;

    kumbuka jinsi ninavyoshutumiwa.

    16 Maneno yako yalipokuja, niliyala;

    yakawa shangwe yangu

    na furaha ya moyo wangu,

    kwa kuwa nimeitwa kwa jina lako,

    Ee Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote.

  37. 24 Kwake yeye awezaye kuwalinda ninyi msianguke na kuwaleta mbele za utukufu wake mkuu bila dosari na kwa furaha ipitayo kiasi: 25 kwake yeye Mungu pekee Mwokozi wetu, kwa Yesu Kristo Bwana wetu, utukufu, ukuu, uweza na mamlaka ni vyake tangu milele, sasa na hata milele! Amen.

  38. 11 Shangilieni katika Bwana na mfurahi, enyi wenye haki!

    Imbeni, nyote mlio wanyofu wa moyo!

  39. Zaburi ya shukrani.

    1 Mpigieni Bwana kelele za shangwe, dunia yote.

    2 Mwabuduni Bwana kwa furaha;

    njooni mbele zake kwa nyimbo za shangwe.

  40. 7 Upendo wako umenifurahisha mno na kunitia moyo, kwa sababu wewe ndugu, umeiburudisha mioyo ya watakatifu.

  41. 10 Ninafurahia sana katika Bwana,

    nafsi yangu inashangilia katika Mungu wangu.

    Kwa maana amenivika mavazi ya wokovu,

    na kunipamba kwa joho la haki,

    kama vile bwana arusi apambavyo

    kichwa chake kama kuhani,

    na kama bibi arusi ajipambavyo

    kwa vito vyake vya thamani.

  42. 13 Lakini malaika akamwambia, “Usiogope, Zekaria, kwa maana Mungu amesikia maombi yako. Mkeo Elizabeti atakuzalia mtoto wa kiume, nawe utamwita jina lake Yohana. 14 Yeye atakuwa furaha na shangwe kwako, nao watu wengi watashangilia kwa sababu ya kuzaliwa kwake. 15 Kwa kuwa atakuwa mkuu mbele za Bwana, kamwe hataonja mvinyo wala kinywaji chochote cha kulevya, naye atajazwa Roho Mtakatifu hata kabla ya kuzaliwa kwake.

  43. 22 Mmebarikiwa ninyi, watu watakapowachukia,

    watakapowatenga na kuwatukana

    na kulikataa jina lenu kama neno ovu,

    kwa ajili ya Mwana wa Adamu.

    23 “Furahini na kurukaruka kwa shangwe, kwa sababu thawabu yenu ni kubwa mbinguni, kwa kuwa hivyo ndivyo baba zao walivyowatenda manabii.

  44. 52 Kisha wakamwabudu na kurudi Yerusalemu wakiwa wamejawa na furaha kuu. 53 Nao wakadumu ndani ya Hekalu wakimtukuza Mungu. Amen.

  45. 41 Nao mitume wakatoka nje ya baraza, wakiwa wamejaa furaha kwa sababu wamehesabiwa kustahili kupata aibu kwa ajili ya jina la Yesu. 42 Kila siku, Hekaluni na nyumba kwa nyumba, hawakuacha kufundisha na kuhubiri habari njema kwamba Yesu ndiye Kristo.

  46. 1 Kwa hiyo, ndugu zangu, ninaowapenda na ambao ninawaonea shauku, ninyi mlio furaha yangu na taji yangu, hivi ndivyo iwapasavyo kusimama imara katika Bwana, ninyi wapenzi wangu.

  47. 17 Watiini viongozi wenu na kujinyenyekeza chini ya mamlaka yao. Kwa maana wao wanakesha kwa ajili yenu kama watu watakaopaswa kutoa hesabu. Watiini ili wafanye kazi yao kwa furaha, wala si kama mzigo, maana hiyo haitakuwa na faida kwenu.

  48. 7 Bwana ni nguvu zangu na ngao yangu,

    moyo wangu umemtumaini yeye,

    nami nimesaidiwa.

    Moyo wangu unarukaruka kwa furaha

    nami nitamshukuru kwa wimbo.

  49. 23 Mtu hupata furaha katika kutoa jibu linalofaa:

    je, ni zuri namna gani neno lililotoka kwa wakati wake!

  50. 2 Watu wanaotembea katika giza

    wameona nuru kuu,

    wale wanaoishi katika nchi ya uvuli wa mauti,

    nuru imewazukia.

    3 Umelikuza taifa,

    na kuzidisha furaha yao,

    wanafurahia mbele zako,

    kama watu wanavyofurahia wakati wa mavuno,

    kama watu wafurahivyo

    wagawanyapo nyara.

    4 Kama vile siku ya kushindwa kwa Wamidiani,

    umevunja nira iliyowalemea,

    ile gongo mabegani mwao na

    fimbo yake yeye aliyewaonea.

    5 Kila kiatu cha askari kilichotumiwa vitani,

    na kila vazi lililovingirishwa katika damu

    vitawekwa kwa ajili ya kuchomwa,

    vitakuwa kuni za kuwasha moto.

    6 Kwa maana, kwa ajili yetu mtoto amezaliwa,

    tumepewa mtoto mwanaume,

    nao utawala utakuwa mabegani mwake.

    Naye ataitwa

    Mshauri wa Ajabu, Mungu Mwenye Nguvu,

    Baba wa Milele, Mfalme wa Amani.

    7 Kuongezeka kwa utawala wake na amani

    hakutakuwa na mwisho.

    Atatawala katika kiti cha enzi cha Daudi

    na juu ya ufalme wake,

    akiuthibitisha na kuutegemeza

    kwa haki na kwa adili,

    tangu wakati huo na hata milele.

    Wivu wa Bwana Mwenye Nguvu Zote

    utatimiza haya.

  51. 10 waliokombolewa na Bwana watarudi.

    Wataingia Sayuni wakiimba;

    furaha ya milele itakuwa juu ya vichwa vyao.

    Watapata furaha na shangwe;

    huzuni na majonzi vitakimbia.

  52. 14 Imba, ee Binti Sayuni;

    paza sauti, ee Israeli!

    Furahi na kushangilia kwa moyo wako wote,

    ee Binti Yerusalemu!

    15 Bwana amekuondolea adhabu yako,

    amewarudisha nyuma adui zako.

    Bwana, Mfalme wa Israeli, yu pamoja nawe;

    kamwe hutaogopa tena madhara yoyote.

    16 Katika siku hiyo watauambia Yerusalemu,

    “Usiogope, ee Sayuni;

    usiiache mikono yako ilegee.

    17 Bwana Mungu wako yu pamoja nawe,

    yeye ni mwenye nguvu kuokoa.

    Atakufurahia kwa furaha kubwa,

    atakutuliza kwa pendo lake,

    atakufurahia kwa kuimba.”

  53. 10 Walipoiona ile nyota wakajawa na furaha kubwa mno. 11 Walipoingia ndani ya ile nyumba, wakamwona mtoto pamoja na Maria mama yake, wakamsujudu na kumwabudu yule mtoto Yesu. Ndipo wakafungua hazina zao, wakamtolea zawadi za dhahabu, uvumba na manemane.

  54. 21 “Bwana wake akamwambia, ‘Umefanya vizuri sana, mtumishi mwema na mwaminifu! Umekuwa mwaminifu kwa vitu vichache; nami nitakuweka kuwa msimamizi wa vitu vingi. Njoo ushiriki katika furaha ya bwana wako!’

  55. 27 Yohana akawajibu, “Hakuna mtu yeyote awezaye kupata kitu chochote isipokuwa kile tu alichopewa kutoka mbinguni. 28 Ninyi wenyewe ni mashahidi wangu kwamba nilisema, ‘Mimi si Kristo, ila nimetumwa nimtangulie.’ 29 Bibi arusi ni wa bwana arusi. Lakini rafiki yake bwana arusi anayesimama karibu naye na kusikiliza kutoka kwake, hufurahi sana aisikiapo sauti ya bwana arusi. Kwa sababu hii furaha yangu imekamilika. 30 Yeye hana budi kuwa mkuu zaidi na mimi nizidi kuwa mdogo.”

  56. 34 Mliwahurumia wale waliokuwa kifungoni, mkikubali kwa furaha kunyangʼanywa mali zenu kwa maana mlijua kwamba mnayo mali iliyo bora zaidi idumuyo.

  57. 3 Ilinifurahisha sana baadhi ya ndugu walipokuja na kutueleza juu ya uaminifu wako katika kweli na jinsi unavyoendelea kuenenda katika hiyo kweli. 4 Sina furaha kubwa kuliko hii, kusikia kwamba watoto wangu wanaenenda katika kweli.

  58. 1 Njooni, tumwimbie Bwana kwa furaha;

    tumfanyie kelele za shangwe

    Mwamba wa wokovu wetu.

    2 Tuje mbele zake kwa shukrani,

    tumtukuze kwa vinanda na nyimbo.

  59. 28 Tarajio la mwenye haki ni furaha,

    bali matumaini ya mwovu huwa si kitu.

  60. 24 Baba wa mwenye haki ana furaha kubwa,

    naye aliye na mwana mwenye hekima humfurahia.

    25 Baba yako na mama yako na wafurahi,

    mama aliyekuzaa na ashangilie!

  61. 12 Mtatoka nje kwa furaha

    na kuongozwa kwa amani;

    milima na vilima

    vitapaza sauti kwa nyimbo mbele yenu,

    nayo miti yote ya shambani

    itapiga makofi.

    13 Badala ya kichaka cha miiba

    itaota miti ya misunobari,

    na badala ya michongoma

    utaota mhadasi.

    Hili litakuwa jambo la kumpatia Bwana jina,

    kwa ajili ya ishara ya milele,

    ambayo haitaharibiwa.”

  62. 46 Siku zote kwa moyo mmoja walikutana ndani ya ukumbi wa Hekalu, wakimega mkate nyumba kwa nyumba, wakila chakula chao kwa furaha na moyo mweupe, 47 wakimsifu Mungu na kuwapendeza watu wote. Kila siku Bwana akaliongeza kanisa wale waliokuwa wakiokolewa.

  63. 6 Watu walipokuwa wanarudi nyumbani baada ya Daudi kumuua yule Mfilisti, wanawake wakaja kutoka pande zote za miji ya Israeli kumlaki Mfalme Sauli kwa kuimba na kucheza, kwa nyimbo za furaha na kwa matari na zeze.

    7 Walipokuwa wanacheza, wakaimba:

    “Sauli amewaua elfu zake,

    naye Daudi makumi elfu yake.”

  64. 6 Kisha kichwa changu kitainuliwa

    juu ya adui zangu wanaonizunguka.

    Katika maskani yake nitatoa dhabihu kwa kelele za shangwe;

    nitamwimbia Bwana na kumsifu.

  65. 11 Uligeuza maombolezo yangu kuwa kucheza,

    ulinivua nguo za gunia ukanivika shangwe,

    12 ili moyo wangu uweze kukusifu na usikae kimya.

    Ee Bwana Mungu wangu, nitakushukuru milele.

  66. 10 Sikujinyima kitu chochote ambacho macho yangu yalikitamani,

    hakuna anasa ambayo niliunyima moyo wangu.

    Moyo wangu ulifurahia kazi zangu zote,

    hii ilikuwa thawabu ya kazi zangu zote.

    11 Hata hivyo nilipokuja kuangalia yote ambayo

    mikono yangu ilikuwa imefanya

    na yale niliyotaabika kukamilisha,

    kila kitu kilikuwa ni ubatili, ni kukimbiza upepo;

    hapakuwa na faida yoyote chini ya jua.

  67. 9 Watu wakafurahi kwa sababu ya itikio la hiari la viongozi wao, kwa kuwa walikuwa wametoa kwa hiari na kwa moyo wote kwa Bwana. Mfalme Daudi pia akafurahi sana.

  68. 111 Sheria zako ni urithi wangu milele,

    naam ni furaha ya moyo wangu.

  69. 46 Naye Maria akasema:

    “Moyo wangu wamwadhimisha Bwana,

    47 nayo roho yangu inamfurahia

    Mungu Mwokozi wangu,

    48 kwa kuwa ameangalia kwa fadhili

    unyonge wa mtumishi wake.

    Hakika tangu sasa vizazi vyote vitaniita aliyebarikiwa,

    49 kwa maana yeye Mwenye Nguvu

    amenitendea mambo ya ajabu:

    jina lake ni takatifu.

  70. 33 Nimewaambia mambo haya, ili mpate kuwa na amani mkiwa ndani yangu. Ulimwenguni mtapata dhiki. Lakini jipeni moyo, kwa maana mimi nimeushinda ulimwengu.”

  71. 28 Nasi tunajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hutenda kazi pamoja na wote wampendao, katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. 29 Maana wale Mungu aliowajua tangu mwanzo, pia aliwachagua tangu mwanzo, wapate kufanana na mfano wa Mwanawe, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. 30 Nao wale Mungu aliotangulia kuwachagua, akawaita, wale aliowaita pia akawahesabia haki, nao wale aliowahesabia haki, pia akawatukuza.

  72. 17 Lakini hata kama nikimiminwa kama sadaka ya kinywaji kwenye dhabihu na huduma itokayo katika imani yenu, mimi ninafurahi na kushangilia pamoja nanyi nyote. 18 Vivyo hivyo, ninyi nanyi imewapasa kufurahi na kushangilia pamoja nami.

  73. 8 Lakini kwa habari za Mwana asema,

    “Kiti chako cha enzi, Ee Mungu,

    kitadumu milele na milele,

    nayo haki itakuwa fimbo ya utawala

    ya ufalme wako.

    9 Umependa haki na kuchukia uovu;

    kwa hiyo Mungu, Mungu wako,

    amekuweka juu ya wenzako

    kwa kukupaka mafuta ya furaha.”

  74. Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.

    1 Ee Bwana, mfalme huzifurahia nguvu zako.

    Tazama jinsi ilivyo kuu furaha yake

    kwa ushindi unaompa!

  75. 1 Mwimbieni Bwana kwa furaha, enyi wenye haki;

    kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo.

    2 Msifuni Bwana kwa kinubi,

    mwimbieni sifa kwa zeze la nyuzi kumi.

    3 Mwimbieni wimbo mpya;

    pigeni kwa ustadi, na mpaze sauti za shangwe.

  76. 8 Unipe kusikia furaha na shangwe,

    mifupa uliyoiponda na ifurahi.

  77. 23 Midomo yangu itapaza sauti kwa furaha

    ninapokuimbia sifa,

    mimi, ambaye umenikomboa.

  78. 22 Jiwe walilolikataa waashi,

    limekuwa jiwe kuu la pembeni.

    23 Bwana ametenda hili,

    nalo ni la kushangaza machoni petu.

    24 Hii ndiyo siku Bwana aliyoifanya,

    tushangilie na kufurahi ndani yake.

  79. 8 Hata kama mtu ataishi miaka mingi kiasi gani,

    na aifurahie yote.

    Lakini na akumbuke siku za giza,

    kwa maana zitakuwa nyingi.

    Kila kitu kitakachokuja ni ubatili.

    9 Furahi ewe kijana, wakati ungali kijana,

    moyo wako na ukupe furaha

    katika siku za ujana wako.

    Fuata njia za moyo wako

    na chochote macho yako yaonayo,

    lakini ujue kwamba kwa ajili ya haya yote

    Mungu atakuleta hukumuni.

  80. 7 Ili kunizuia nisijivune kwa sababu ya ufunuo huu mkuu, nilipewa mwiba katika mwili wangu, mjumbe wa Shetani, ili anitese. 8 Kwa habari ya jambo hili nilimsihi Bwana mara tatu aniondolee mwiba huu. 9 Lakini aliniambia, “Neema yangu inakutosha, kwa kuwa uweza wangu hukamilika katika udhaifu.” Kwa hiyo nitajisifu kwa furaha zaidi kuhusu udhaifu wangu, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. 10 Hii ndiyo sababu, kwa ajili ya Kristo, nafurahia udhaifu, katika kutukanwa, katika taabu, katika mateso na katika shida, kwa maana ninapokuwa dhaifu, ndipo nina nguvu.

  81. 13 Je, mtu yeyote miongoni mwenu amepatwa na taabu? Basi inampasa aombe. Je, kuna yeyote mwenye furaha? Basi na aimbe nyimbo za kusifu.