101 Bible Verses About Hatred

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Hatred
  1. 18 “Kama ulimwengu ukiwachukia ninyi, kumbukeni kwamba ulinichukia mimi kabla yenu. 19 Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungeliwapenda kama vile unavyowapenda walio wake. Kwa sababu ninyi si wa ulimwengu, lakini mimi nimewachagua kutoka ulimwengu, hii ndiyo sababu ulimwengu unawachukia. 20 Kumbukeni lile neno nililowaambia, ‘Hakuna mtumishi aliye mkuu kuliko bwana wake.’ Kama wamenitesa mimi, nanyi pia watawatesa. Kama wamelishika neno langu, watalishika na neno lenu pia. 21 Watawatendea ninyi haya yote kwa ajili ya Jina langu, kwa sababu hawamjui yeye aliyenituma. 22 Kama sikuja na kusema nao wasingalikuwa na hatia ya dhambi. Lakini sasa hawana udhuru kwa ajili ya dhambi zao. 23 Yeyote anayenichukia mimi, anamchukia pia na Baba yangu. 24 Kama sikuwa nimefanya miujiza ambayo haijapata kufanywa na mtu mwingine yeyote, wasingalikuwa na hatia ya dhambi. Lakini sasa wameiona miujiza hii na bado wakatuchukia mimi na Baba yangu. 25 Lakini hii ni kutimiza lile neno lililoandikwa kwenye Sheria kwamba, ‘Walinichukia pasipo sababu.’

  2. 43 “Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Mpende jirani yako na umchukie adui yako.’ 44 Lakini ninawaambia: Wapendeni adui zenu na waombeeni wanaowatesa ninyi, 45 ili mpate kuwa watoto wa Baba yenu aliye mbinguni. Kwa maana yeye huwaangazia jua lake watu waovu na watu wema, naye huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. 46 Kama mkiwapenda tu wale wanaowapenda, mtapata thawabu gani? Je, hata watoza ushuru hawafanyi hivyo? 47 Nanyi kama mkiwasalimu ndugu zenu tu, je, mnafanya nini zaidi ya wengine? Je, hata watu wasiomjua Mungu, hawafanyi hivyo? 48 Kwa hiyo kuweni wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.

  3. 27 “Lakini nawaambia ninyi mnaonisikia: Wapendeni adui zenu. Watendeeni mema wanaowachukia. 28 Wabarikini wale wanaowalaani, waombeeni wale wanaowatendea mabaya. 29 Kama mtu akikupiga shavu moja, mgeuzie na la pili pia. Mtu akikunyangʼanya koti lako, usimzuie kuchukua joho pia. 30 Mpe kila akuombaye, na kama mtu akichukua mali yako usitake akurudishie.

  4. 8 Yeye atendaye dhambi ni wa ibilisi, kwa sababu ibilisi amekuwa akitenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili aziangamize kazi za ibilisi. 9 Yeyote aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wa Mungu wakaa ndani yake, wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa na Mungu. 10 Kwa jinsi hii tunaweza kujua dhahiri watoto wa Mungu na pia watoto wa ibilisi. Yeyote asiyetenda haki hatokani na Mungu, wala yeye asiyempenda ndugu yake.

    11 Hili ndilo neno mlilolisikia tangu mwanzo: Kwamba imetupasa tupendane sisi kwa sisi. 12 Msiwe kama Kaini aliyekuwa wa yule mwovu akamuua ndugu yake. Basi kwa nini alimuua? Ni kwa sababu matendo yake Kaini yalikuwa mabaya na ya ndugu yake yalikuwa ya haki. 13 Ndugu zangu, ninyi msistaajabu kama ulimwengu ukiwachukia. 14 Sisi tunajua ya kwamba tumepita mautini kuingia uzimani, kwa sababu tunawapenda ndugu. Kila asiyempenda ndugu yake akaa mautini. 15 Yeyote amchukiaye ndugu yake ni muuaji, nanyi mwajua ya kwamba muuaji hana uzima wa milele ndani yake.

    16 Kwa namna hii twaweza kulijua pendo la Mungu: Kwa sababu Yesu Kristo aliutoa uhai wake kwa ajili yetu. Nasi imetupasa kuutoa uhai kwa ajili ya hao ndugu. 17 Ikiwa mtu anavyo vitu vya ulimwengu huu na akamwona ndugu yake ni mhitaji lakini asimhurumie, upendo wa Mungu wakaaje ndani ya mtu huyo? 18 Watoto wapendwa, tusipende kwa maneno au kwa ulimi bali kwa tendo na kweli.

  5. 7 Wapendwa, siwaandikii ninyi amri mpya bali ile ya zamani, ambayo mmekuwa nayo tangu mwanzo. Amri hii ya zamani ni lile neno mlilosikia. 8 Lakini nawaandikia amri mpya, yaani, lile neno lililo kweli ndani yake na ndani yenu, kwa sababu giza linapita na ile nuru ya kweli tayari inangʼaa.

    9 Yeyote anayesema yumo nuruni lakini anamchukia ndugu yake bado yuko gizani. 10 Yeye ampendaye ndugu yake anakaa nuruni, wala hakuna kitu chochote ndani yake cha kumkwaza. 11 Lakini yeyote amchukiaye ndugu yake, yuko gizani na anaenenda gizani, wala hajui anakokwenda, kwa sababu giza limempofusha macho.

  6. 19 Basi matendo ya mwili ni dhahiri nayo ni haya: Uasherati, uchafu, ufisadi, 20 kuabudu sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, 21 husuda, ulevi, ulafi na mambo mengine yanayofanana na hayo. Nawaonya, kama nilivyokwisha kuwaonya kabla, kwamba watu watendao mambo kama hayo, hawataurithi Ufalme wa Mungu.

    22 Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, 23 upole na kiasi. Katika mambo kama haya hakuna sheria.

  7. 10 Wale wanaompenda Bwana na wauchukie uovu,

    kwa maana yeye hulinda maisha ya waaminifu wake

    na kuwaokoa kutoka mkononi mwa mwovu.

  8. 12 Chuki huchochea faraka,

    lakini upendo husitiri mabaya yote.

  9. 17 Tazama jinsi yalivyo ya thamani mawazo yako kwangu, Ee Mungu!

    Jinsi jumla yake ilivyo kubwa!

    18 Kama ningezihesabu,

    zingekuwa nyingi kuliko mchanga.

    Niamkapo,

    bado niko pamoja nawe.

    19 Laiti ungewachinja waovu, Ee Mungu!

    Ondokeni kwangu, ninyi wamwaga damu!

    20 Wanazungumza juu yako wakiwa na kusudi baya,

    adui zako wanatumia vibaya jina lako.

    21 Ee Bwana, je, nisiwachukie wanaokuchukia?

    Nisiwachukie sana wanaoinuka dhidi yako?

    22 Sina kitu zaidi ya chuki dhidi yao,

    ninawahesabu ni adui zangu.

    23 Ee Mungu, nichunguze, uujue moyo wangu,

    nijaribu na ujue mawazo yangu.

    24 Uone kama kuna njia iletayo machukizo ndani yangu,

    uniongoze katika njia ya milele.

  10. 19 Twampenda yeye kwa sababu yeye alitupenda kwanza. 20 Ikiwa mtu atasema, “Nampenda Mungu,” lakini anamchukia ndugu yake, yeye ni mwongo. Kwa maana kila mtu asiyempenda ndugu yake ambaye anamwona, atampendaje Mungu asiyemuona? 21 Naye ametupa amri hii: Yeyote anayempenda Mungu lazima pia ampende ndugu yake.

  11. 13 Kumcha Bwana ni kuchukia uovu;

    ninachukia kiburi na majivuno,

    tabia mbaya na mazungumzo potovu.

  12. 22 Watu wote watawachukia kwa ajili ya Jina langu. Lakini yule atakayevumilia hadi mwisho ataokolewa.

  13. 4 Wewe si Mungu unayefurahia uovu,

    kwako mtu mwovu hataishi.

    5 Wenye kiburi hawawezi kusimama mbele yako,

    unawachukia wote watendao mabaya.

    6 Unawaangamiza wasemao uongo.

    Bwana huwachukia

    wamwagao damu na wadanganyifu.

  14. 24 Mtu mwenye nia ya kudhuru wengine hujificha kwa maneno ya midomo yake,

    lakini moyoni mwake huficha udanganyifu.

    25 Ingawa maneno yake huvutia, usimwamini,

    kwa maana machukizo saba hujaza moyo wake.

    26 Nia yake ya kudhuru wengine inaweza kufichwa na udanganyifu,

    lakini uovu wake utafichuliwa kwenye kusanyiko.

  15. 16 Kuna vitu sita anavyovichukia Bwana,

    naam, viko saba vilivyo chukizo kwake:

    17 macho ya kiburi,

    ulimi udanganyao,

    mikono imwagayo damu isiyo na hatia,

    18 moyo uwazao mipango miovu,

    miguu iliyo myepesi kukimbilia uovu,

    19 shahidi wa uongo ambaye humwaga uongo,

    na mtu ambaye huchochea fitina kati ya ndugu.

  16. 9 “Ndipo mtasalitiwa, ili mteswe na kuuawa, nanyi mtachukiwa na mataifa yote kwa ajili yangu. 10 Wakati huo, wengi wataacha imani yao, nao watasalitiana kila mmoja na mwenzake na kuchukiana. 11 Watatokea manabii wengi wa uongo, nao watawadanganya watu wengi. 12 Kwa sababu ya kuongezeka kwa uovu upendo wa watu wengi utapoa, 13 lakini yule atakayevumilia hadi mwisho ataokolewa.

  17. 26 “Mtu yeyote anayekuja kwangu hawezi kuwa mwanafunzi wangu kama hatanipenda mimi zaidi ya baba yake na mama yake, mke wake na watoto wake, ndugu zake na dada zake, naam, hata maisha yake mwenyewe. 27 Yeyote asiyeuchukua msalaba wake na kunifuata hawezi kuwa mwanafunzi wangu.

  18. 17 “ ‘Usimchukie ndugu yako moyoni mwako. Karipia jirani yako kwa uwazi ili usishiriki hatia yake.

    18 “ ‘Usijilipizie kisasi wala kuwa na kinyongo dhidi ya mmoja wa jamaa yako, lakini mpende jirani yako kama unavyojipenda wewe mwenyewe. Mimi ndimi Bwana.

  19. 3 Sitaweka mbele ya macho yangu

    kitu kiovu.

    Ninayachukia matendo ya watu wasio na imani;

    hawatashikamana nami.

  20. 104 Ninapata ufahamu kutoka mausia yako,

    kwa hiyo ninachukia kila njia ya upotovu.

  21. 19 Tazama adui zangu walivyo wengi,

    pia uone jinsi wanavyonichukia vikali!

  22. 163 Ninachukia na kuchukizwa sana na uongo,

    lakini napenda sheria yako.

  23. 17 Afadhali chakula cha mboga mahali palipo na upendo

    kuliko nyama ya ndama iliyonona pamoja na chuki.

  24. 14 Tafuteni mema, wala si mabaya,

    ili mpate kuishi.

    Ndipo Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote atakuwa pamoja nanyi,

    kama msemavyo yupo nanyi.

    15 Yachukieni maovu, yapendeni mema;

    dumisheni haki mahakamani.

    Yamkini Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote

    atawahurumia mabaki ya Yosefu.

  25. 6 Si kwamba Neno la Mungu limeshindwa. Kwa maana si kila Mwisraeli ambaye ni wa uzao utokanao na Israeli ni Mwisraeli halisi. 7 Wala hawakuwi wazao wa Abrahamu kwa sababu wao ni watoto wake, lakini: “Uzao wako utahesabiwa kupitia kwake Isaki.” 8 Hii ina maana kwamba, si watoto waliozaliwa kimwili walio watoto wa Mungu, bali ni watoto wa ahadi wanaohesabiwa kuwa uzao wa Abrahamu. 9 Kwa maana ahadi yenyewe ilisema, “Nitakurudia tena wakati kama huu, naye Sara atapata mtoto wa kiume.”

    10 Wala si hivyo tu, bali pia watoto aliowazaa Rebeka walikuwa na baba huyo huyo mmoja, yaani, baba yetu Isaki. 11 Lakini, hata kabla hao mapacha hawajazaliwa au kufanya jambo lolote jema au baya, ili kwamba kusudi la Mungu la kuchagua lipate kusimama, 12 si kwa matendo, bali kwa yeye mwenye kuita, Rebeka aliambiwa, “Yule mkubwa atamtumikia yule mdogo.” 13 Kama vile ilivyoandikwa, “Nimempenda Yakobo, lakini nimemchukia Esau.”

    14 Tuseme nini basi? Je, Mungu ni dhalimu? La, hasha! 15 Kwa maana Mungu alimwambia Mose,

    “Nitamrehemu yeye nimrehemuye,

    na pia nitamhurumia yeye nimhurumiaye.”

  26. 3 Maana sisi wenyewe wakati fulani tulikuwa wajinga, wasiotii, tukiwa watumwa wa tamaa mbaya na anasa za kila aina. Tuliishi katika uovu na wivu, tukichukiwa na kuchukiana sisi kwa sisi.

  27. 7 Ulimwengu hauwezi kuwachukia ninyi, lakini unanichukia mimi kwa sababu ninawashuhudia kwamba matendo yao ni maovu.

  28. 6 Lakini una jambo hili kwa upande wako: Unayachukia matendo ya Wanikolai, ambayo nami pia nayachukia.

  29. 3 Basi, Israeli akampenda Yosefu kuliko yeyote miongoni mwa kaka zake, kwani ni mwanawe wa uzeeni, akamshonea joho lililorembwa vizuri sana. 4 Ndugu zake walipoona kwamba baba yao anampenda Yosefu kuliko yeyote mwingine miongoni mwao, walimchukia na hawakusema naye neno lolote jema.

    5 Yosefu akaota ndoto, naye alipowaeleza ndugu zake, wakamchukia zaidi. 6 Akawaambia, “Sikilizeni ndoto niliyoota: 7 Tulikuwa tukifunga miganda ya nafaka shambani, ghafula mganda wangu ukasimama wima, wakati miganda yenu ikiuzunguka na kuuinamia.”

    8 Ndugu zake wakamwambia, “Wewe unakusudia kututawala? Hivi kweli wewe utatutawala sisi?” Wakaongeza kumchukia zaidi kwa sababu ya ndoto yake pamoja na yale aliyowaambia.

  30. 19 Usiwaache wale wanaonisimanga,

    wale ambao ni adui zangu bila sababu;

    usiwaache wale ambao ni adui zangu bila sababu

    wakonyeze jicho kwa hila.

  31. 18 Yeye afichaye chuki yake ana midomo ya uongo,

    na yeyote anayeeneza uchonganishi ni mpumbavu.

  32. 28 Nao kwa kuwa hawakuona umuhimu wa kudumisha ufahamu wa Mungu, yeye akawaachilia wafuate akili za upotovu, watende mambo yale yasiyostahili kutendwa. 29 Wakiwa wamejawa na udhalimu wa kila namna, uasherati, uovu, tamaa mbaya na hila. Wamejawa na husuda, uuaji, ugomvi, udanganyifu, hadaa na nia mbaya. Wao pia ni wasengenyaji, 30 wasingiziaji, wanaomchukia Mungu, wajeuri, wenye kiburi na majivuno, wenye hila, wasiotii wazazi wao, 31 wajinga, wasioamini, wasio na huruma na wakatili. 32 Ingawa wanafahamu sheria ya haki ya Mungu kwamba watu wanaofanya mambo kama hayo wanastahili mauti, si kwamba wanaendelea kutenda hayo tu, bali pia wanakubaliana na wale wanaoyatenda.

  33. 9 Upendo lazima usiwe na unafiki. Chukieni lililo ovu, shikamaneni na lililo jema.

  34. 3 Wamenizunguka kwa maneno ya chuki,

    wananishambulia bila sababu.

    4 Wanachonilipa badala ya urafiki wangu ni kunishtaki,

    lakini mimi ninawaombea.

    5 Wananilipiza mabaya kwa mema,

    chuki badala ya urafiki wangu.

  35. 16 “Ninachukia kuachana,” asema Bwana, Mungu wa Israeli, “pia nachukia mtu anayejivika jeuri kama vazi,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.

    Kwa hiyo jihadharini wenyewe katika roho zenu, wala msije mkavunja uaminifu.

  36. 14 Nimewapa neno lako, nao ulimwengu umewachukia kwa kuwa wao si wa ulimwengu kama mimi nisivyo wa ulimwengu huu.

  37. 7 Unaipenda haki na kuchukia uovu;

    kwa hiyo Mungu, Mungu wako,

    amekuweka juu ya wenzako,

    kwa kukupaka mafuta ya furaha.

  38. 128 na kwa sababu naona maagizo yako yote ni adili,

    nachukia kila njia potovu.

  39. 16 Kaeni kwa amani ninyi kwa ninyi. Msijivune, bali mwe tayari kushirikiana na wanyonge. Wala msiwe watu wenye kujivuna kwamba mnajua kila kitu.

    17 Msimlipe mtu yeyote ovu kwa ovu. Jitahidini ili mtende yaliyo mema machoni pa watu wote. 18 Kama ikiwezekana, kwa upande wenu kaeni kwa amani na watu wote. 19 Wapendwa, msilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu, maana imeandikwa: “Ni juu yangu kulipiza kisasi, nitalipiza,” asema Bwana. 20 Badala yake:

    “Kama adui yako ana njaa, mlishe;

    kama ana kiu, mpe kinywaji.

    Kwa kufanya hivyo,

    unaweka makaa ya moto yanayowaka kichwani pake.”

    21 Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema.

  40. 2 Bwana asema, “Nimewapenda ninyi.”

    “Lakini ninyi mnauliza, ‘Wewe umetupendaje?’ ”

    Bwana asema, “Je, Esau hakuwa ndugu yake Yakobo? Hata hivyo nimempenda Yakobo, 3 lakini nikamchukia Esau, nami nimeifanya milima yake kuwa ukiwa, na urithi wake nimewapa mbweha wa jangwani.”

    4 Edomu anaweza kusema, “Ingawa tumepondapondwa, tutajenga upya magofu.”

    Lakini hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote asemalo: “Wanaweza kujenga, lakini nitabomoa. Wataitwa Nchi Ovu, watu ambao siku zote wapo chini ya ghadhabu ya Bwana. 5 Mtayaona kwa macho yenu wenyewe na kusema, ‘Bwana ni mkuu, hata nje ya mipaka ya Israeli!’

  41. 5 Usivisujudie wala kuviabudu; kwa kuwa Mimi, Bwana Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu, ninayewaadhibu watoto kwa ajili ya dhambi za baba zao hadi kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao,

  42. 4 Bwana yuko ndani ya Hekalu lake takatifu;

    Bwana yuko kwenye kiti chake cha enzi mbinguni.

    Huwaangalia wana wa watu,

    macho yake yanawajaribu.

    5 Bwana huwajaribu wenye haki,

    lakini waovu na wanaopenda jeuri,

    nafsi yake huwachukia.

    6 Atawanyeshea waovu makaa ya moto mkali

    na kiberiti kinachowaka,

    upepo wenye joto kali ndio fungu lao.

    7 Kwa kuwa Bwana ni mwenye haki,

    yeye hupenda haki.

    Wanyofu watauona uso wake.

  43. 10 Watu wamwagao damu humchukia mtu mwadilifu

    na hutafuta kumuua mtu mnyofu.

  44. 16 Haya ndiyo mtakayoyafanya: Semeni kweli kila mtu kwa mwenzake, na mtoe hukumu ya kweli na haki kwenye mahakama zenu, 17 usipange mabaya dhidi ya jirani yako, wala msipende kuapa kwa uongo. Nayachukia yote haya,” asema Bwana.

  45. 19 Hii ndiyo hukumu kwamba: Nuru imekuja ulimwenguni, nao watu wakapenda giza kuliko nuru kwa sababu matendo yao ni maovu. 20 Kwa kuwa kila atendaye maovu huchukia nuru, wala haji kwenye nuru ili matendo yake maovu yasifichuliwe. 21 Lakini yule aishiye kwa ukweli huja kwenye nuru, ili ionekane wazi kwamba matendo yake yametendeka katika Mungu.”

  46. 9 Umependa haki na kuchukia uovu;

    kwa hiyo Mungu, Mungu wako,

    amekuweka juu ya wenzako

    kwa kukupaka mafuta ya furaha.”

  47. 41 Esau akawa na kinyongo dhidi ya Yakobo kwa ajili ya baraka ambazo baba yake alikuwa amembariki. Akasema moyoni mwake, “Siku za kuomboleza kwa ajili ya baba yangu zimekaribia, ndipo nitamuua ndugu yangu Yakobo.”

    42 Rebeka alipokwisha kuambiwa yale aliyoyasema Esau mwanawe mkubwa, alimwita Yakobo mwanawe mdogo, akamwambia, “Ndugu yako Esau anajifariji kwa wazo la kukuua. 43 Sasa basi, mwanangu, fanya nisemalo: Kimbilia haraka kwa Labani ndugu yangu kule Harani. 44 Ukae naye kwa muda mpaka ghadhabu ya ndugu yako itulie. 45 Wakati ndugu yako atakapokuwa hana hasira nawe tena na amesahau uliyomtendea, nitakupelekea ujumbe urudi. Kwa nini niwapoteze wote wawili kwa siku moja?”

  48. 8 Mfalme wa Israeli akamjibu Yehoshafati, “Bado yupo mtu mmoja ambaye kupitia yeye twaweza kumuuliza shauri la Bwana, lakini namchukia kwa sababu huwa hatabiri jambo lolote jema kunihusu mimi, lakini kila mara hunitabiria mabaya tu. Yeye ni Mikaya mwana wa Imla.”

    Yehoshafati akajibu, “Mfalme hapaswi kusema hivyo.”

  49. 6 Ninawachukia wale wanaongʼangʼania sanamu batili;

    mimi ninamtumaini Bwana.

  50. 1 Kuna wakati kwa ajili ya kila jambo,

    nayo majira kwa kila tendo chini ya mbingu:

    2 wakati wa kuzaliwa na wakati wa kufa,

    wakati wa kupanda na wakati wa kungʼoa yaliyopandwa,

    3 wakati wa kuua na wakati wa kuponya,

    wakati wa kubomoa,

    na wakati wa kujenga,

    4 wakati wa kulia na wakati wa kucheka,

    wakati wa kuomboleza na wakati wa kucheza,

    5 wakati wa kutawanya mawe na wakati wa kukusanya mawe,

    wakati wa kukumbatia na wakati wa kutokumbatia,

    6 wakati wa kutafuta na wakati wa kupoteza,

    wakati wa kuweka na wakati wa kutupa,

    7 wakati wa kurarua na wakati wa kushona,

    wakati wa kunyamaza na wakati wa kuzungumza,

    8 wakati wa kupenda na wakati wa kuchukia,

    wakati wa vita na wakati wa amani.

  51. 4 Siketi pamoja na watu wadanganyifu,

    wala siandamani na wanafiki,

    5 ninachukia kusanyiko la watenda mabaya

    na ninakataa kuketi pamoja na waovu.

  52. 21 “Ninachukia, ninazidharau sikukuu zenu za dini;

    siwezi kuvumilia makusanyiko yenu.

    22 Hata ingawa mnaniletea sadaka zenu za kuteketezwa na sadaka za nafaka,

    sitazikubali.

    Ingawa mnaniletea sadaka nzuri za amani,

    sitazitambua.

    23 Niondoleeni kelele za nyimbo zenu!

    Sitasikiliza sauti za vinubi vyenu.

    24 Lakini acheni haki itiririke kama mto,

    na uadilifu uwe kama kijito kisichokauka!

    25 “Je, mliniletea dhabihu na sadaka

    kwa miaka arobaini kule jangwani,

    ee nyumba ya Israeli?

    26 Mmeyainua madhabahu ya mfalme wenu,

    Sikuthi mungu wenu mtawala,

    na Kiuni mungu wenu wa nyota,

    ambao mliwatengeneza wenyewe.

    27 Kwa sababu hiyo nitawapeleka uhamishoni mbali kupita Dameski,”

    asema Bwana, ambaye jina lake ni Mungu Mwenye Nguvu Zote.

  53. 68 “Ahimidiwe Bwana, Mungu wa Israeli,

    kwa kuwa amewajilia watu wake na kuwakomboa.

    69 Naye ametusimamishia pembe ya wokovu

    katika nyumba ya Daudi mtumishi wake,

    70 kama alivyonena kwa vinywa vya manabii

    wake watakatifu tangu zamani,

    71 kwamba atatuokoa kutoka kwa adui zetu,

    na kutoka mikononi mwao wote watuchukiao:

  54. 7 Yefta akawaambia, “Je, hamkunichukia mimi na kunifukuza katika nyumba ya baba yangu? Kwa nini mnanijia sasa, wakati mna matatizo.”

  55. 2 Yehu mwonaji, mwana wa Hanani, akapanda kwenda kuonana naye akamwambia Mfalme Yehoshafati, “Je, utawasaidia waovu na kuwapenda wale wanaomchukia Bwana? Kwa sababu ya jambo hili, ghadhabu ya Bwana iko juu yako. 3 Hata hivyo, kuna mema yaliyoonekana kwako, kwa kuwa umeondoa katika nchi nguzo za Ashera na umeukaza moyo wako katika kumtafuta Mungu.”

  56. 21 Ubaya utamuua mtu mwovu,

    nao adui za mwenye haki watahukumiwa.

  57. 21 “Mmesikia walivyoambiwa watu wa zamani kwamba, ‘Usiue. Yeyote atakayeua atapaswa hukumu.’ 22 Lakini mimi nawaambia kwamba, yeyote atakayemkasirikia ndugu yake, atapaswa hukumu. Tena, yeyote atakayemwambia ndugu yake, ‘Raka,’ atapaswa kujibu kwa Baraza la Wayahudi. Lakini yeyote atakayesema ‘Wewe mpumbavu!’ atapaswa hukumu ya moto wa jehanamu.

    23 “Kwa hiyo, kama unatoa sadaka yako madhabahuni, ukakumbuka kuwa ndugu yako ana kitu dhidi yako, 24 iache sadaka yako hapo mbele ya madhabahu. Enda kwanza ukapatane na ndugu yako; kisha urudi na ukatoe sadaka yako.

    25 “Patana na mshtaki wako upesi wakati uwapo njiani pamoja naye kwenda mahakamani, ili mshtaki wako asije akakutia mikononi mwa hakimu, naye hakimu akakutia mikononi mwa askari, nawe ukatupwa gerezani. 26 Amin, nakuambia, hautatoka humo hadi uwe umelipa senti ya mwisho.

  58. 12 Kulipopambazuka Wayahudi wakafanya shauri pamoja na kujifunga kwa kiapo kwamba hawatakula wala kunywa mpaka wawe wamemuua Paulo. 13 Waliofanya mpango huo walikuwa zaidi ya watu arobaini. 14 Wakawaendea viongozi wa makuhani na wazee na kusema, “Tumejifunga pamoja kwa kiapo kwamba hatutakula wala kunywa mpaka tuwe tumemuua Paulo. 15 Hivyo basi, wewe pamoja na baraza, inawapasa mkamjulishe jemadari ili amteremshe Paulo kwenu, mjifanye kama mnataka kufanya uchunguzi wa kina zaidi wa shauri lake. Nasi tuko tayari kumuua kabla hajafika hapa.”

  59. 41 wakati ninapounoa upanga wangu unaometameta

    na mkono wangu unapoushika ili kutoa hukumu,

    nitalipiza kisasi juu ya adui zangu

    na kuwalipiza wale wanaonichukia.

  60. 22 Absalomu hakusema neno lolote na Amnoni, likiwa zuri au baya, kwa kuwa alimchukia Amnoni kwa sababu alikuwa amemtia aibu Tamari, dada yake.

  61. 5 Mwenye haki huchukia uongo,

    bali waovu huleta aibu na fedheha.

  62. 13 Acheni kuniletea sadaka zisizokuwa na maana!

    Uvumba wenu ni chukizo kwangu.

    Miandamo ya Mwezi, Sabato na makusanyiko ya ibada:

    siwezi kuvumilia makusanyiko yenu maovu.

    14 Sikukuu zenu za Miandamo ya Mwezi, na sikukuu zenu zilizoamriwa:

    moyo wangu unazichukia.

    Zimekuwa mzigo kwangu,

    nimechoka kuzivumilia.

  63. 8 “Kwa maana Mimi, Bwana, napenda haki,

    na ninachukia unyangʼanyi na uovu.

    Katika uaminifu wangu nitawapa malipo yao

    na kufanya agano la milele nao.

  64. 24 “Hakuna mtu awezaye kuwatumikia mabwana wawili. Kwa kuwa atamchukia huyu na kumpenda yule mwingine, au atashikamana sana na huyu na kumdharau yule mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu pamoja na Mali.

  65. 3 Basi viongozi wa makuhani na wazee wa watu wakakusanyika katika jumba la utawala la kuhani mkuu, jina lake Kayafa. 4 Wakafanya shauri ili kumkamata Yesu kwa siri na kumuua.

  66. 13 Watu wote watawachukia kwa ajili ya Jina langu. Lakini yule atakayevumilia hadi mwisho ataokolewa.

  67. 16 Mtasalitiwa hata na wazazi, ndugu, jamaa na marafiki, na baadhi yenu watawaua. 17 Mtachukiwa na watu wote kwa ajili ya Jina langu. 18 Lakini hapatakuwa na unywele mmoja wa kichwa chenu utakaoangamia. 19 Kwa kuvumilia mtaokoa roho zenu.

  68. 6 Kwa maana hata tulipokuwa dhaifu, wakati ulipowadia, Kristo alikufa kwa ajili yetu sisi wenye dhambi. 7 Hakika, ni vigumu mtu yeyote kufa kwa ajili ya mwenye haki, ingawa inawezekana mtu akathubutu kufa kwa ajili ya mtu mwema. 8 Lakini Mungu anaudhihirisha upendo wake kwetu kwamba: Tulipokuwa tungali wenye dhambi, Kristo alikufa kwa ajili yetu.

    9 Basi, kwa kuwa sasa tumehesabiwa haki kwa damu yake, si zaidi sana tutaokolewa kutoka ghadhabu ya Mungu kupitia kwake! 10 Kwa kuwa kama tulipokuwa adui wa Mungu tulipatanishwa naye kwa njia ya kifo cha Mwanawe, si zaidi sana tukiisha kupatanishwa, tutaokolewa kwa uzima wake.

  69. 5 Kwa hiyo, ueni kabisa chochote kilicho ndani yenu cha asili ya kidunia: yaani uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya na ulafi, ambayo ndiyo ibada ya sanamu. 6 Kwa sababu ya mambo haya, ghadhabu ya Mungu inakuja. 7 Ninyi pia zamani mlienenda katika mambo haya mlipoishi maisha hayo. 8 Lakini sasa yawekeni mbali nanyi mambo kama haya yote: yaani hasira, ghadhabu, uovu, masingizio na lugha chafu kutoka midomoni mwenu. 9 Msiambiane uongo, kwa maana mmevua kabisa utu wenu wa kale pamoja na matendo yake, 10 nanyi mmevaa utu mpya, unaofanywa upya katika ufahamu sawasawa na mfano wa Muumba wake. 11 Hapa hakuna Myunani wala Myahudi, aliyetahiriwa wala asiyetahiriwa, asiyestaarabika wala aliyestaarabika, mtumwa wala mtu huru, bali Kristo ni yote, na ndani ya wote.

  70. 21 Lakini uchague watu wenye uwezo miongoni mwa watu wote, watu wanaomwogopa Mungu, watu waaminifu wanaochukia mali ya dhuluma, uwateuwe wawe maafisa juu ya maelfu, mamia, hamsini na makumi.

  71. 9 Basi ujue kwamba Bwana Mungu wako ndiye Mungu; ni Mungu mwaminifu, anayetunza Agano la upendo kwa maelfu ya vizazi vya wale wanaompenda na kuzishika amri zake. 10 Lakini

    kwa wale wanaomchukia

    atawalipiza kwenye nyuso zao

    kwa maangamizi;

    hatachelewa kuwalipiza kwenye nyuso zao

    wale wamchukiao.

  72. 31 Kamwe msimwabudu Bwana Mungu wenu kwa njia wanayoabudu miungu yao, kwa sababu katika kuabudu miungu yao, wanafanya aina zote za machukizo anayoyachukia Bwana. Hata huwateketeza wana wao na binti zao kwa moto kama kafara kwa miungu yao.

  73. 16 Lakini kwake mtu mwovu, Mungu asema:

    “Una haki gani kunena sheria zangu

    au kuchukua agano langu midomoni mwako?

    17 Unachukia mafundisho yangu

    na kuyatupa maneno yangu nyuma yako.

    18 Unapomwona mwizi, unaungana naye,

    unapiga kura yako pamoja na wazinzi.

    19 Unakitumia kinywa chako kwa mabaya

    na kuuongoza ulimi wako kwa hila.

    20 Wanena daima dhidi ya ndugu yako

    na kumsingizia mwana wa mama yako.

  74. 15 Wale wanaomchukia Bwana wangalinyenyekea mbele zake,

    na adhabu yao ingedumu milele.

  75. 28 Ulimi wa uongo, huwachukia wale unaowaumiza,

    nacho kinywa cha kujipendekeza hutenda uharibifu.

  76. 3 Alidharauliwa na kukataliwa na wanadamu,

    mtu wa huzuni nyingi, ajuaye mateso.

    Kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao,

    alidharauliwa, wala hatukumhesabu kuwa kitu.

  77. 5 Sikieni neno la Bwana,

    ninyi mtetemekao kwa neno lake:

    “Ndugu zenu wanaowachukia ninyi

    na kuwatenga ninyi kwa sababu ya Jina langu, wamesema,

    ‘Bwana na atukuzwe,

    ili tupate kuona furaha yenu!’

    Hata sasa wataaibika.

  78. 15 “Kwa sababu ya uovu wao wote huko Gilgali,

    niliwachukia huko.

    Kwa sababu ya matendo yao ya dhambi,

    nitawafukuza katika nyumba yangu.

    Sitawapenda tena,

    viongozi wao wote ni waasi.

  79. 31 Ondoeni kabisa uchungu, ghadhabu, hasira, makelele na masingizio pamoja na kila aina ya uovu. 32 Kuweni wafadhili na wenye kuhurumiana ninyi kwa ninyi, mkisameheana, kama vile naye Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.

  80. 4 Ninyi wanaume na wanawake wazinzi, hamjui ya kwamba urafiki na dunia ni uadui na Mungu? Kwa hiyo mtu yeyote anayetaka kuwa rafiki wa dunia hufanyika adui wa Mungu.

  81. 30 Pia Yakobo akakutana na Raheli kimwili, naye akampenda Raheli zaidi kuliko Lea. Yakobo akamtumikia Labani kwa miaka mingine saba.

    31 Bwana alipoona kwamba Lea hapendwi, akampa watoto, lakini Raheli alikuwa tasa.

  82. 5 Ukiona punda wa mtu anayekuchukia ameanguka na mzigo wake, usimwache hapo alipoangukia; hakikisha kuwa umemsaidia.

  83. 15 Bwana atawakinga na kila ugonjwa. Mungu hatatia juu yenu ugonjwa wowote mbaya mlioufahamu huko Misri, lakini atatia ugonjwa juu ya wale wote wanaokuchukia.

  84. 19 Wengi ni wale ambao ni adui zangu hodari,

    wale wanaonichukia bila sababu ni wengi.

  85. 7 bali wewe unatupa ushindi juu ya adui zetu,

    unawaaibisha watesi wetu.

  86. 4 Wale wanaonichukia bila sababu

    ni wengi kuliko nywele za kichwa changu;

    wengi ni adui kwangu bila sababu,

    wale wanaotafuta kuniangamiza.

    Ninalazimishwa kurudisha

    kitu ambacho sikuiba.

  87. 23 Nitawaponda adui zake mbele zake

    na kuwaangamiza watesi wake.

  88. 29 Kwa kuwa walichukia maarifa,

    wala hawakuchagua kumcha Bwana,

    30 kwa kuwa hawakukubali mashauri yangu,

    na kukataa maonyo yangu,

    31 watakula matunda ya njia zao,

    na watashibishwa matunda ya hila zao.

  89. 8 Bwana huchukia sana dhabihu za waovu,

    bali maombi ya wanyofu humfurahisha Mungu.

    9 Bwana huchukia sana njia ya waovu,

    bali huwapenda wale wafuatao haki.

  90. 17 Ingiza mguu wako nyumbani kwa jirani yako mara chache,

    ukizidisha, atakukinai na atakuchukia.

  91. 9 “ ‘Je, mtaiba na kuua, mtazini na kuapa kwa uongo, na kufukiza uvumba kwa Baali, na kufuata miungu mingine ambayo hamkuijua, 10 kisha mje na kusimama mbele yangu katika nyumba hii inayoitwa kwa Jina langu, mkisema, “Tuko salama.” Salama kwa kufanya mambo haya yote ya kuchukiza?

  92. 8 Urithi wangu umekuwa kwangu

    kama simba wa msituni.

    Huningurumia mimi,

    kwa hiyo ninamchukia.

  93. 10 mnamchukia yule akemeaye mahakamani,

    na kumdharau yule ambaye husema kweli.

  94. 14 Kwa kuwa kama mkiwasamehe watu wengine wanapowakosea, Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi pia. 15 Lakini msipowasamehe watu wengine makosa yao, naye Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.

  95. 22 Wahurumieni walio na mashaka; 23 wengine waokoeni kwa kuwanyakua kutoka kwenye moto; nao wengine wahurumieni mkiwa na hofu, mkichukia hata vazi lenye mawaa na kutiwa unajisi na mwili.

  96. 113 Ninachukia watu wa nia mbili,

    lakini ninapenda sheria yako.

  97. 14 Kwa maana tunajua kwamba sheria ni ya kiroho, lakini mimi ni wa kimwili nikiwa nimeuzwa kwenye utumwa wa dhambi. 15 Sielewi nitendalo, kwa maana lile ninalotaka kulitenda, silitendi, lakini ninatenda lile ninalolichukia. 16 Basi kama ninatenda lile nisilotaka kutenda, ni kwamba ninakubali kuwa sheria ni njema. 17 Lakini, kwa kweli si mimi tena nitendaye lile nisilotaka bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu. 18 Kwa maana ninafahamu kwamba hakuna jema lolote likaalo ndani yangu, yaani, katika asili yangu ya dhambi. Kwa kuwa nina shauku ya kutenda lililo jema, lakini siwezi kulitenda. 19 Sitendi lile jema nitakalo kutenda, bali lile baya nisilolitaka, ndilo nitendalo.

  98. 22 Bwana anachukia sana midomo idanganyayo,

    bali hufurahia watu ambao ni wa kweli.

  99. 34 Mafarisayo waliposikia kwamba Yesu alikuwa amewanyamazisha Masadukayo, Mafarisayo wakakusanyika pamoja. 35 Mmoja wao, mtaalamu wa sheria, akamuuliza swali ili kumjaribu, akisema, 36 “Mwalimu, ni amri ipi katika Sheria iliyo kuu kuliko zote?”

    37 Yesu akamjibu, “ ‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote na kwa akili zako zote.’ 38 Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. 39 Nayo ya pili ni kama hiyo, nayo ni hii: ‘Mpende jirani yako kama nafsi yako.’ 40 Amri hizi mbili ndizo msingi wa Sheria na Manabii.”

  100. 2 Yafikirini mambo yaliyo juu, wala si ya duniani.

  101. 3 Kila mmoja mwenye matumaini haya ndani yake hujitakasa, kama vile yeye alivyo mtakatifu.