57 Bible Verses About Judgment
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
-
11 Kisha nikaona kiti kikubwa cheupe cha enzi pamoja na yeye aliyeketi juu yake. Dunia na mbingu zikaukimbia uso wake wala mahali pao hapakuonekana. 12 Nami nikawaona wafu wakubwa na wadogo, wakiwa wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi na vitabu vikafunguliwa. Pia kitabu kingine kikafunguliwa ambacho ni kitabu cha uzima. Hao wafu wakahukumiwa sawasawa na matendo yao kama yalivyoandikwa ndani ya hivyo vitabu. 13 Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake, nayo mauti na Kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake. Kila mtu akahukumiwa kulingana na yale aliyoyatenda. 14 Kisha mauti na Kuzimu zikatupwa katika ziwa la moto. Hii ndio mauti ya pili, yaani, hilo ziwa la moto. 15 Iwapo mtu jina lake halikuonekana katika kile kitabu cha uzima, alitupwa ndani ya lile ziwa la moto.
-
5 Lakini kwa sababu ya ukaidi wenu na mioyo yenu isiyotaka kutubu, mnajiwekea akiba ya ghadhabu dhidi yenu wenyewe kwa siku ile ya ghadhabu ya Mungu, wakati hukumu yake ya haki itakapodhihirishwa. 6 Kwa maana Mungu atamlipa kila mtu sawasawa na matendo yake. 7 Wale ambao kwa kuvumilia katika kutenda mema hutafuta utukufu, heshima na maisha yasiyoharibika, Mungu atawapa uzima wa milele. 8 Lakini kwa wale watafutao mambo yao wenyewe na wale wanaokataa kweli na kuzifuata njia mbaya, kutakuwa na ghadhabu na hasira ya Mungu. 9 Kutakuwa na taabu na dhiki kwa kila mmoja atendaye maovu, Myahudi kwanza na mtu wa Mataifa pia,
-
10 Kwa kuwa sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mmoja apate kulipwa kwa ajili ya yale ambayo yametendwa katika mwili wake, yakiwa mema au mabaya.
11 Basi, kwa kuwa tunajua kumcha Bwana, tunajitahidi kuwavuta wengine. Lakini Mungu anatufahamu dhahiri, nami natumaini kwamba tu dhahiri katika dhamiri zenu pia.
-
25 Amin, amin nawaambia, saa yaja, nayo saa ipo, wafu watakapoisikia sauti ya Mwana wa Mungu, nao watakaoisikia watakuwa hai. 26 Kama vile Baba alivyo na uzima ndani yake, vivyo hivyo amempa Mwana kuwa na uzima ndani yake. 27 Naye amempa Mwanawe mamlaka ya kuhukumu kwa kuwa yeye ni Mwana wa Adamu.
28 “Msishangae kusikia haya, kwa maana saa inakuja ambapo wale walio makaburini wataisikia sauti yake. 29 Nao watatoka nje, wale waliotenda mema watafufuka wapate uzima na wale waliotenda maovu, watafufuka wahukumiwe.
-
39 Yule adui aliyepanda magugu ni ibilisi. Mavuno ni mwisho wa dunia, nao wavunaji ni malaika.
40 “Kama vile magugu yangʼolewavyo na kuchomwa motoni, ndivyo itakavyokuwa wakati wa mwisho wa dunia. 41 Mwana wa Adamu atawatuma malaika zake, nao watakusanya kutoka Ufalme wake kila kitu kinachosababisha dhambi na watenda maovu wote. 42 Nao watawatupa katika tanuru la moto ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno. 43 Ndipo wenye haki watangʼaa kama jua katika Ufalme wa Baba yao. Yeye aliye na masikio, na asikie.
-
1 “Usihukumu ili usije ukahukumiwa. 2 Kwa maana jinsi unavyowahukumu wengine, ndivyo utakavyohukumiwa, na kwa kipimo kile upimiacho, ndicho utakachopimiwa.
3 “Mbona unatazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na wala huoni boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe? 4 Au unawezaje kumwambia ndugu yako, ‘Acha nitoe kibanzi kwenye jicho lako,’ wakati kuna boriti kwenye jicho lako mwenyewe? 5 Ewe mnafiki, ondoa boriti ndani ya jicho lako kwanza, ndipo utaweza kuona dhahiri jinsi ya kuondoa kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako.
-
30 Zamani wakati wa ujinga, Mungu alijifanya kama haoni, lakini sasa anawaamuru watu wote kila mahali watubu. 31 Kwa kuwa ameweka siku ambayo atauhukumu ulimwengu kwa haki akimtumia mtu aliyemchagua. Amewahakikishia watu wote mambo haya kwa kumfufua Kristo kutoka kwa wafu.”
-
9 Furahi ewe kijana, wakati ungali kijana,
moyo wako na ukupe furaha
katika siku za ujana wako.
Fuata njia za moyo wako
na chochote macho yako yaonayo,
lakini ujue kwamba kwa ajili ya haya yote
Mungu atakuleta hukumuni.
-
21 “Si kila mtu aniambiaye, ‘Bwana, Bwana,’ atakayeingia katika Ufalme wa Mbinguni, bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. 22 Wengi wataniambia siku ile, ‘Bwana, Bwana, hatukutoa unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo wachafu na kufanya miujiza mingi?’ 23 Ndipo nitakapowaambia wazi, ‘Sikuwajua kamwe. Ondokeni kwangu, ninyi watenda maovu!’
-
27 Kwa hiyo, mtu yeyote alaye mkate huo au kukinywea kikombe hicho cha Bwana isivyostahili, atakuwa na hatia ya dhambi juu ya mwili na damu ya Bwana. 28 Inampasa mtu ajichunguze mwenyewe, kabla ya kula mkate na kukinywea kikombe. 29 Kwa maana mtu yeyote alaye na kunywa pasipo kuutambua mwili wa Bwana, hula na kunywa hukumu juu yake mwenyewe. 30 Hii ndiyo sababu wengi miongoni mwenu ni wagonjwa na dhaifu na wengine wenu hata wamekufa. 31 Lakini kama tungejichunguza wenyewe tusingehukumiwa. 32 Tunapohukumiwa na Bwana, tunaadibishwa ili tusije tukahukumiwa pamoja na ulimwengu.
-
19 Hii ndiyo hukumu kwamba: Nuru imekuja ulimwenguni, nao watu wakapenda giza kuliko nuru kwa sababu matendo yao ni maovu. 20 Kwa kuwa kila atendaye maovu huchukia nuru, wala haji kwenye nuru ili matendo yake maovu yasifichuliwe.
-
7 Lakini kwa neno lilo hilo, mbingu za sasa na dunia zimewekwa akiba kwa ajili ya moto, zikihifadhiwa hadi siku ile ya hukumu na ya kuangamizwa kwa watu wasiomcha Mungu.
8 Lakini wapenzi, msisahau neno hili: kwamba kwa Bwana, siku moja ni kama miaka elfu, na miaka elfu ni kama siku moja. 9 Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama watu wengine wanavyokudhani kukawia. Badala yake, yeye anawavumilia ninyi, maana hataki mtu yeyote aangamie, bali kila mtu afikilie toba.
10 Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwizi. Ndipo mbingu zitatoweka kwa kishindo kikuu; navyo vitu vya asili vitateketezwa kwa moto, nayo dunia na kila kitu kilichomo ndani yake kitaunguzwa.
-
31 “Mwana wa Adamu atakapokuja katika utukufu wake na malaika wote watakatifu pamoja naye, ndipo atakapoketi juu ya kiti cha enzi cha utukufu wake. 32 Mataifa yote watakusanyika mbele zake, naye atawatenga kama mchungaji anavyotenga kondoo na mbuzi. 33 Atawaweka kondoo upande wake wa kuume, na mbuzi upande wake wa kushoto.
34 “Ndipo Mfalme atawaambia wale walioko upande wake wa kuume, ‘Njooni, ninyi mliobarikiwa na Baba yangu; urithini Ufalme ulioandaliwa kwa ajili yenu tangu kuumbwa kwa ulimwengu. 35 Kwa maana nilikuwa na njaa mkanipa chakula, nilikuwa na kiu mkaninywesha, nilikuwa mgeni mkanikaribisha, 36 nilikuwa uchi mkanivika, nilikuwa mgonjwa mkanitunza, nami nilikuwa kifungoni mkaja kunitembelea.’
37 “Ndipo wale wenye haki watakapomjibu, ‘Bwana, ni lini tulikuona ukiwa na njaa tukakulisha, au ukiwa na kiu tukakunywesha? 38 Lini tulikuona ukiwa mgeni tukakukaribisha, au ukiwa uchi tukakuvika? 39 Tena ni lini tulikuona ukiwa mgonjwa tukakutunza, au ukiwa kifungoni tukakutembelea?’
40 “Naye Mfalme atawajibu, ‘Amin nawaambia, kwa jinsi mlivyomtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.’
41 “Kisha atawaambia wale walio upande wake wa kushoto, ‘Ondokeni kwangu, ninyi mliolaaniwa, nendeni kwenye moto wa milele ulioandaliwa kwa ajili ya ibilisi na malaika zake. 42 Kwa maana nilikuwa na njaa hamkunipa chakula, nilikuwa na kiu hamkuninywesha, 43 nilikuwa mgeni nanyi hamkunikaribisha, nilikuwa uchi hamkunivika, nilikuwa mgonjwa hamkunitunza, na nilikuwa gerezani nanyi hamkuja kunitembelea.’
44 “Ndipo wao pia watajibu, ‘Bwana ni lini tulikuona ukiwa na njaa au kiu, au ukiwa mgeni au uchi, au ukiwa mgonjwa na kifungoni na hatukukuhudumia?’
45 “Naye atawajibu, ‘Amin nawaambia, kwa jinsi ambavyo hamkumtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu walio wadogo, hamkunitendea mimi.’
46 “Ndipo hawa watakapoingia kwenye adhabu ya milele, lakini wale wenye haki wataingia katika uzima wa milele.”
-
27 Kama vile mwanadamu alivyowekewa kufa mara moja tu na baada ya kufa akabili hukumu,
-
12 Kama mtu yeyote akijenga juu ya msingi huu kwa kutumia dhahabu, fedha, vito vya thamani, miti, majani au nyasi, 13 kazi yake itaonekana ilivyo, kwa kuwa Siku ile itaidhihirisha. Itadhihirishwa kwa moto, nao moto utapima ubora wa kazi ya kila mtu. 14 Kama kile alichojenga kitabaki, atapokea thawabu yake. 15 Kama kazi kitateketea, atapata hasara, ila yeye mwenyewe ataokolewa, lakini tu kama mtu aliyenusurika kwenye moto.
-
1 Kama mtu yeyote wa kwenu ana ugomvi na mwenzake, anathubutuje kuupeleka kwa wasiomcha Mungu ili kuamuliwa badala ya kuupeleka kwa watakatifu? 2 Je, hamjui kwamba watakatifu watauhukumu ulimwengu? Nanyi kama mtauhukumu ulimwengu, je, hamwezi kuamua mambo madogo madogo? 3 Hamjui kwamba tutawahukumu malaika? Je, si zaidi mambo ya maisha haya? 4 Kwa hiyo kama kuna ugomvi miongoni mwenu kuhusu mambo kama haya, chagueni kuwa waamuzi, watu ambao wanaonekana hata sio wa heshima katika kanisa. 5 Nasema hivi ili mwone aibu. Je, inawezekana kuwa miongoni mwenu hakuna mtu mwenye hekima ya kutosha kuamua ugomvi kati ya waaminio? 6 Badala yake ndugu mmoja anampeleka mwenzake mahakamani, tena mbele ya watu wasioamini!
-
36 Lakini nawaambia, katika siku ya hukumu watu watatoa hesabu kuhusu kila neno lisilo maana walilonena. 37 Kwa maana kwa maneno yako utahesabiwa haki, na kwa maneno yako utahukumiwa.”
-
14 Kwa maana Mungu ataleta hukumuni kila kazi,
pamoja na kila neno la siri,
likiwa jema au baya.
-
1 Mkaribisheni yeye ambaye imani yake ni dhaifu, lakini si kwa kugombana na kubishana juu ya mawazo yake. 2 Mtu mmoja imani yake inamruhusu kula kila kitu, lakini mwingine ambaye imani yake ni dhaifu, hula mboga tu. 3 Yeye alaye kila kitu asimdharau yeye asiyekula. Wala yeye asiyekula kila kitu asimhukumu yule alaye kila kitu, kwa maana Mungu amemkubali. 4 Wewe ni nani hata umhukumu mtumishi wa mtu mwingine? Kwa bwana wake tu anasimama au kuanguka. Naye atasimama kwa sababu Bwana anaweza kumsimamisha.
5 Mtu mmoja anaitukuza siku fulani kuwa ni bora kuliko nyingine, na mwingine anaona kuwa siku zote ni sawa. Basi kila mmoja awe na hakika na yale anayoamini.
-
1 Kwa hiyo huna udhuru wowote, wewe utoaye hukumu kwa mwingine, kwa maana katika jambo lolote unalowahukumu wengine, unajihukumu wewe mwenyewe kwa sababu wewe unayehukumu unafanya mambo hayo hayo. 2 Basi tunajua kwamba hukumu ya Mungu dhidi ya wale wafanyao mambo kama hayo ni ya kweli. 3 Hivyo wewe mwanadamu, utoapo hukumu juu yao na bado unafanya mambo yale yale, unadhani utaepuka hukumu ya Mungu?
-
6 Mungu ni mwenye haki: yeye atawalipa mateso wale wawatesao ninyi 7 na kuwapa ninyi mnaoteseka raha pamoja na sisi, wakati Bwana Yesu atakapodhihirishwa kutoka mbinguni katika mwali wa moto pamoja na malaika wake wenye nguvu. 8 Atawaadhibu wale wasiomjua Mungu na ambao hawakuitii Injili ya Bwana wetu Yesu. 9 Wataadhibiwa kwa uangamivu wa milele na kutengwa na uso wa Bwana na utukufu wa uweza wake, 10 siku hiyo atakapokuja kutukuzwa katika watakatifu wake na kustaajabiwa miongoni mwa wote walioamini. Ninyi pia mtakuwa miongoni mwa hawa kwa sababu mliamini ushuhuda wetu kwenu.
-
5 Ingawa mmekwisha kujua haya yote, nataka niwakumbushe kuwa Bwana akiisha kuwaokoa watu wake kutoka nchi ya Misri, baadaye aliwaangamiza wale ambao hawakuamini. 6 Nao malaika ambao hawakulinda nafasi zao, lakini wakayaacha makao yao, hawa amewaweka katika giza, wakiwa wamefungwa kwa minyororo ya milele kwa ajili ya hukumu Siku ile kuu. 7 Vivyo hivyo, Sodoma na Gomora na pia ile miji iliyokuwa kandokando, ambayo kwa jinsi moja na hao, walijifurahisha kwa uasherati na kufuata tamaa za mwili zisizo za asili, waliwekwa wawe mfano kwa kuadhibiwa katika moto wa milele.
-
26 Kwa maana, je, itamfaidi nini mtu kuupata ulimwengu wote, lakini akayapoteza maisha yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake? 27 Kwa maana Mwana wa Adamu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika zake, naye ndipo atakapomlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake.
-
1 “Katika wakati huo Mikaeli, mtawala mkuu ambaye huwalinda watu wako, atainuka. Kutakuwako wakati wa taabu ambao haujatokea tangu mwanzo wa mataifa hadi wakati huo. Lakini wakati huo, watu wako, kila mmoja ambaye jina lake litakutwa limeandikwa kwenye kitabu, ataokolewa. 2 Wengi ambao wamelala kwenye mavumbi wataamka, baadhi yao kwa uzima wa milele, wengine kwa aibu na kudharauliwa milele. 3 Wale wenye hekima watangʼaa kama mwanga wa mbingu, nao wale ambao huwaongoza wengi kutenda haki, watangʼaa kama nyota milele na milele.
-
26 Kama tukiendelea kutenda dhambi kwa makusudi baada ya kupokea ufahamu wa ile kweli, haibaki tena dhabihu kwa ajili ya dhambi. 27 Lakini kinachobaki ni kungoja kwa hofu hukumu ya moto uwakao, utakaowaangamiza adui za Mungu. 28 Yeyote aliyeikataa sheria ya Mose alikufa pasipo huruma kwa ushahidi wa watu wawili au watatu. 29 Je, mnadhani ni adhabu kali kiasi gani anayostahili kupewa mtu aliyemkanyaga Mwana wa Mungu chini ya nyayo zake, yeye aliyeifanya damu ya Agano iliyomtakasa kuwa kitu najisi na kumtendea maovu Roho wa neema? 30 Kwa kuwa tunamjua yeye aliyesema, “Ni juu yangu kulipiza kisasi; nitalipiza.” Tena asema, “Bwana atawahukumu watu wake.”
-
31 Watendeeni wengine kama ambavyo mngetaka wawatendee ninyi.
32 “Kama mkiwapenda tu wale wanaowapenda, mwapata sifa gani? Hata ‘wenye dhambi’ huwapenda wale wawapendao. 33 Tena mkiwatendea mema wale tu wanaowatendea ninyi mema, mwapata sifa gani? Hata ‘wenye dhambi’ hufanya vivyo hivyo. 34 Tena mnapowakopesha wale tu mnaotegemea wawalipe, mwapata sifa gani? Hata ‘wenye dhambi’ huwakopesha ‘wenye dhambi’ wenzao wakitarajia kulipwa mali yao yote. 35 Lakini wapendeni adui zenu, watendeeni mema, wakopesheni bila kutegemea kurudishiwa mlichokopesha. Ndipo thawabu yenu itakapokuwa kubwa, nanyi mtakuwa wana wa Aliye Juu Sana, kwa sababu yeye ni mwema kwa watu wasio na shukrani na kwa wale waovu. 36 Kuweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma.
37 “Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa. Msilaumu, nanyi hamtalaumiwa. Sameheni, nanyi mtasamehewa. 38 Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa. Kipimo cha kujaa na kushindiliwa na kusukwasukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile mpimacho, ndicho mtakachopimiwa.”
-
10 Kwa maana mtu yeyote anayeishika sheria yote lakini akajikwaa katika kipengele kimoja tu, ana hatia ya kuivunja sheria yote. 11 Kwa sababu yeye aliyesema, “Usizini,” alisema pia, “Usiue.” Basi kama huzini lakini unaua, umekuwa mvunjaji wa sheria.
12 Hivyo semeni na kutenda kama watu watakaohukumiwa kwa sheria ile iletayo uhuru. 13 Kwa kuwa hukumu bila huruma itatolewa kwa mtu yeyote asiyekuwa na huruma. Huruma huishinda hukumu.
-
17 Kwa njia hii, pendo hukamilishwa miongoni mwetu ili tupate kuwa na ujasiri katika siku ya hukumu, kwa sababu kama alivyo ndivyo tulivyo sisi katika ulimwengu huu. 18 Katika pendo hakuna hofu. Lakini pendo lililo kamili huitupa nje hofu, kwa sababu hofu inahusika na adhabu. Kila mwenye hofu hakukamilika katika pendo.
-
7 Bwana anatawala milele,
ameweka kiti chake cha enzi apate kuhukumu.
8 Mungu atahukumu ulimwengu kwa haki,
atatawala mataifa kwa haki.
9 Bwana ni kimbilio la watu wanaoonewa,
ni ngome imara wakati wa shida.
10 Wote wanaolijua jina lako watakutumaini wewe,
kwa maana wewe Bwana,
hujawaacha kamwe wakutafutao.
-
17 Nikafikiri moyoni mwangu,
“Mungu atawaleta hukumuni
wote wawili wenye haki na waovu,
kwa maana kutakuwako na wakati kwa ajili ya kila jambo,
wakati kwa ajili ya kila tendo.”
-
1 Kwa hiyo, sasa hakuna hukumu ya adhabu kwa wale walio ndani ya Kristo Yesu, wale ambao hawaenendi kwa kuufuata mwili bali kwa kufuata Roho. 2 Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima katika Kristo Yesu imeniweka huru mbali na sheria ya dhambi na mauti.
-
1 Nakuagiza mbele za Mungu na mbele za Kristo Yesu, atakayewahukumu watu walio hai na waliokufa wakati wa kuja kwake na ufalme wake, kwamba:
-
17 Kwa maana wakati umewadia wa hukumu kuanzia katika nyumba ya Mungu. Basi kama ikianzia kwetu sisi, mwisho wa hao wasiotii Injili ya Mungu utakuwaje? 18 Basi,
“Ikiwa ni vigumu kwa mwenye haki kuokoka,
itakuwaje kwa mtu asiyemcha Mungu na mwenye dhambi?”
-
5 Yeye ashindaye atavikwa vazi jeupe kama wao. Sitafuta jina lake kutoka kitabu cha uzima, bali nitalikiri jina lake mbele za Baba yangu na mbele za malaika wake.
-
14 Kama mtu yeyote hatawakaribisha ninyi, wala kusikiliza maneno yenu, kungʼuteni mavumbi kutoka kwenye miguu yenu mtakapokuwa mnatoka kwenye nyumba hiyo au mji huo. 15 Amin, nawaambia, itakuwa rahisi zaidi kwa miji ya Sodoma na Gomora kustahimili katika hukumu kuliko mji huo.
-
1 Kwa hiyo, tukiachana na mafundisho yale ya awali kuhusu Kristo na tukisonga mbele ili tufikie utimilifu, sio kuweka tena msingi wa mafundisho ya kuzitubia kazi zisizo na uhai na imani katika Mungu, 2 mafundisho kuhusu aina za ubatizo, kuwekea watu mikono, ufufuo wa wafu, na hukumu ya milele. 3 Mungu akitujalia tutafanya hivyo.
4 Kwa kuwa ni vigumu kwa wale ambao wakati fulani walishapata nuru, ambao walishaonja kipawa cha mbinguni, ambao wamekwisha kushiriki katika Roho Mtakatifu, 5 ambao wameonja uzuri wa Neno la Mungu na nguvu za wakati ujao, 6 kisha wakianguka, kuwarejesha tena katika toba. Kwa kuwa wanamsulubisha Mwana wa Mungu mara ya pili na kumdhalilisha hadharani, nayo ikawa hasara kwao.
-
18 Mataifa walikasirika nao
wakati wa ghadhabu yako umewadia.
Wakati umewadia wa kuwahukumu waliokufa
na kuwapa thawabu watumishi wako manabii
na watakatifu wako pamoja na wale wote
wanaoliheshimu Jina lako,
wakubwa kwa wadogo:
na kuwaangamiza wale wanaoiangamiza dunia.”
-
19 Pilato akiwa ameketi kwenye kiti cha hukumu, mkewe akampelekea ujumbe huu: “Usiwe na jambo lolote juu ya mtu huyu asiye na hatia, kwa kuwa leo nimeteseka sana katika ndoto kwa sababu yake.”
-
31 Malkia wa Kusini atasimama wakati wa hukumu na kuwahukumu watu wa kizazi hiki. Kwa kuwa yeye alikuja kutoka miisho ya dunia ili kuisikiliza hekima ya Solomoni. Na hapa yupo aliye mkuu kuliko Solomoni. 32 Siku ya hukumu, watu wa Ninawi watasimama pamoja na kizazi hiki na kukihukumu; kwa maana wao walitubu waliposikia mahubiri ya Yona. Na tazama, hapa yupo yeye aliye mkuu kuliko Yona.
-
12 Lakini wakati Galio alipokuwa msaidizi wa mwakilishi wa mtawala huko Akaya, Wayahudi waliungana kumshambulia Paulo, wakamkamata na kumpeleka mahakamani. 13 Wakamshtaki wakisema, “Mtu huyu anawashawishi watu wamwabudu Mungu kinyume cha sheria.”
14 Paulo alipotaka kujitetea, Galio akawaambia Wayahudi, “Kama ninyi Wayahudi mlikuwa mkilalamika kuhusu makosa makubwa ya uhalifu ingekuwa haki kwangu kuwasikiliza. 15 Lakini kwa kuwa linahusu maneno, majina na sheria yenu, amueni ninyi wenyewe. Mimi sitakuwa mwamuzi wa mambo haya.” 16 Akawafukuza kutoka mahakamani. 17 Ndipo wote wakamkamata Sosthene kiongozi wa sinagogi, wakampiga mbele ya mahakama, lakini Galio hakujali kitendo chao hata kidogo.
-
24 Je, hamjui kwamba katika mashindano ya mbio wote wanaoshindana hukimbia, lakini ni mmoja wao tu apewaye tuzo? Kwa hiyo kimbieni katika mashindano kwa jinsi ambavyo mtapata tuzo.
25 Kila mmoja anayeshiriki katika mashindano hufanya mazoezi makali. Wao hufanya hivyo ili wapokee taji isiyodumu, lakini sisi tunafanya hivyo ili kupata taji idumuyo milele. 26 Kwa hiyo mimi sikimbii kama mtu akimbiaye bila lengo, sipigani kama mtu anayepiga hewa, 27 la, bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha ili nikiisha kuwahubiria wengine, mimi nisiwe mtu wa kukataliwa.
-
14 Anga ikatoweka kama vile karatasi isokotwavyo, na kila mlima na kila kisiwa kikaondolewa mahali pake.
15 Ndipo wafalme wa dunia, wakuu wote, majemadari, matajiri, wenye nguvu na kila mtu, mtumwa na mtu huru, wakajificha katika mapango na kwenye miamba ya milima. 16 Wakaiita milima na miamba wakisema, “Tuangukieni, mkatufiche na uso wake yeye aketiye kwenye kiti cha enzi, na mkatuepushe na ghadhabu ya Mwana-Kondoo! 17 Kwa maana siku ile kuu ya ghadhabu yao imewadia. Je, ni nani awezaye kustahimili?”
-
10 Lakini mkiingia katika mji, nao hawakuwakaribisha, tokeni mwende katika barabara zake mkaseme: 11 ‘Hata mavumbi ya mji wenu yaliyoshikamana na miguu yetu, tunayakungʼuta dhidi yenu. Lakini mjue kwamba Ufalme wa Mungu umekaribia.’ 12 Ninawaambia, itakuwa rahisi zaidi kwa Sodoma kustahimili katika siku ile kuliko mji ule.
13 “Ole wako Korazini! Ole wako Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwenu ingefanyika Tiro na Sidoni, miji hiyo ingekuwa imetubu zamani, kwa kuvaa magunia na kujipaka majivu. 14 Lakini itakuwa rahisi zaidi kwa Tiro na Sidoni kustahimili katika siku ya hukumu, kuliko ninyi. 15 Nawe, Kapernaumu, je, utainuliwa hadi mbinguni? La hasha, utashushwa mpaka kuzimu.”
-
42 Naye alituamuru kuhubiri kwa watu wote na kushuhudia kwamba ndiye alitiwa mafuta na Mungu kuwa hakimu wa walio hai na wafu.
-
7 Lakini Bwana akamwambia Samweli, “Usitazame sura yake wala kimo chake, kwa kuwa nimemkataa. Bwana hatazami katika vile vitu mwanadamu avitazamavyo. Mwanadamu hutazama katika sura ya nje, lakini Bwana hutazama moyoni.”
-
45 Lakini kama yule mtumishi atasema moyoni mwake, ‘Bwana wangu anakawia kurudi,’ kisha akaanza kuwapiga wale watumishi wa kiume na wa kike, na kula na kunywa na kulewa. 46 Basi bwana wa mtumishi huyo atakuja siku asiyodhani na saa asiyoijua. Atamkata vipande vipande na kumweka katika sehemu moja pamoja na wale wasioamini.
47 “Yule mtumishi anayefahamu vyema mapenzi ya bwana wake na asijiandae wala kufanya kama apendavyo bwana wake, atapigwa kwa mapigo mengi. 48 Lakini yeyote ambaye hakujua naye akafanya yale yastahiliyo kupigwa, atapigwa kidogo. Yeyote aliyepewa vitu vingi, atadaiwa vingi; na yeyote aliyekabidhiwa vingi, kwake vitatakiwa vingi.
-
47 “Tena, Ufalme wa Mbinguni ni kama wavu wa kuvua samaki uliotupwa baharini ukavua samaki wa kila aina. 48 Ulipojaa, wavuvi wakavuta pwani, wakaketi na kukusanya samaki wazuri kuwaweka kwenye vyombo safi, lakini wale samaki wabaya wakawatupa. 49 Hivi ndivyo itakavyokuwa wakati wa mwisho wa dunia. Malaika watakuja na kuwatenganisha watu waovu na watu wenye haki. 50 Nao watawatupa hao waovu katika tanuru la moto ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno.”
-
30 “Mimi siwezi kufanya jambo lolote peke yangu. Ninavyosikia ndivyo ninavyohukumu, nayo hukumu yangu ni ya haki kwa kuwa sitafuti kufanya mapenzi yangu mwenyewe, bali mapenzi yake yeye aliyenituma.
-
25 Hilo na liwe mbali nawe, kufanya jambo kama hilo, kuwaua wenye haki pamoja na waovu, kuwatendea wenye haki sawasawa na waovu. Iwe mbali nawe! Je, Mwamuzi wa dunia yote hatafanya lililo sawa?”
-
2 Usimhukumu mtumishi wako,
kwa kuwa hakuna mtu anayeishi aliye mwenye haki mbele zako.
-
2 Hakuna jambo lolote lililositirika ambalo halitafunuliwa, au lililofichwa ambalo halitajulikana. 3 Kwa hiyo, lolote mlilosema gizani litasikiwa nuruni. Na kile mlichonongʼona masikioni mkiwa kwenye vyumba vya ndani, kitatangazwa juu ya paa.
4 “Nawaambieni rafiki zangu, msiwaogope wale wauao mwili, lakini baada ya hilo hawawezi kufanya lolote zaidi. 5 Lakini nitawaambia nani wa kumwogopa: Mwogopeni yule ambaye baada ya kuua mwili, ana mamlaka ya kuwatupa motoni. Naam, nawaambia, mwogopeni huyo!
-
4 La hasha! Mungu na aonekane mwenye haki, na kila mwanadamu kuwa mwongo, kama ilivyoandikwa:
“Ili uthibitike kuwa wa kweli unaponena,
na ukashinde utoapo hukumu.”
5 Ikiwa uovu wetu unathibitisha haki ya Mungu waziwazi, tuseme nini basi? Je, Mungu kuileta ghadhabu yake juu yetu ni kwamba yeye si mwenye haki? (Nanena kibinadamu.) 6 La hasha! Kama hivyo ndivyo ilivyo, Mungu angehukumuje ulimwengu?
-
13 kwa maana mkiishi kwa kuufuata mwili, mtakufa, lakini kama mkiyaua matendo ya mwili kwa Roho, mtaishi. 14 Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio watoto wa Mungu. 15 Kwa maana hamkupokea roho ya utumwa iwaleteayo tena hofu, bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambaye kwa yeye twalia, “Abba, yaani, Baba,” 16 Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu ya kwamba sisi tu watoto wa Mungu. 17 Hivyo, ikiwa sisi ni watoto, basi tu warithi, warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo, naam, tukiteswa pamoja naye tupate pia kutukuzwa pamoja naye.
-
33 Tazama jinsi kilivyo kina cha utajiri
wa hekima na maarifa ya Mungu!
Tazama jinsi ambavyo hukumu zake hazichunguziki,
na ambavyo njia zake zisivyotafutikana!
-
15 Mtu wa kiroho hubainisha mambo yote, lakini yeye mwenyewe habainishwi na mtu yeyote.
-
12 Kwa maana Neno la Mungu li hai tena lina nguvu. Lina makali kuliko upanga wowote wenye makali kuwili, hivyo linachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, viungo na mafuta yaliyo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo. 13 Wala hakuna kiumbe chochote kilichofichika machoni pa Mungu. Kila kitu kimefunuliwa na kiko wazi machoni pake yeye ambaye kwake ni lazima tutatoa hesabu.
14 Kwa kuwa tunaye Kuhani Mkuu kuliko wote ambaye ameingia mbinguni, Yesu Mwana wa Mungu, basi na tushikamane sana kwa uthabiti na ule ukiri wa imani yetu. 15 Kwa kuwa hatuna Kuhani Mkuu asiyeweza kuchukuliana na sisi katika udhaifu wetu, lakini tunaye mmoja ambaye alijaribiwa kwa kila namna, kama vile sisi tujaribiwavyo: lakini yeye hakutenda dhambi. 16 Basi na tukikaribie kiti cha rehema kwa ujasiri, ili tupewe rehema na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.
-
1 Baada ya haya nikasikia sauti kama ya umati mkubwa mbinguni wakipiga kelele wakisema:
“Haleluya!
Wokovu na utukufu na uweza ni vya Mungu wetu,
2 kwa maana hukumu zake
ni za kweli na za haki.
Amemhukumu yule kahaba mkuu
aliyeuharibu ulimwengu kwa uzinzi wake.
Mungu amemlipiza kisasi
kwa ajili ya damu ya watumishi wake.”
3 Wakasema tena kwa nguvu:
“Haleluya!
Moshi wake huyo kahaba unapanda juu
milele na milele.”
Shows Read in context, Share and Copy.