65 Bible Verses About God's Plan

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About God's Plan
  1. 10 Hili ndilo asemalo Bwana: “Miaka sabini itakapotimia kwa ajili ya Babeli, nitakuja kwenu na kutimiza ahadi yangu ya rehema ya kuwarudisha mahali hapa. 11 Kwa maana ninajua mipango niliyo nayo kwa ajili yenu,” asema Bwana, “ni mipango ya kuwafanikisha na wala si ya kuwadhuru, ni mipango ya kuwapa tumaini katika siku zijazo. 12 Kisha mtaniita, na mtakuja na kuniomba, nami nitawasikiliza. 13 Mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote. 14 Nitaonekana kwenu,” asema Bwana, “nami nitawarudisha watu wenu waliotekwa. Nitawakusanya kutoka mataifa yote na mahali pote nilipokuwa nimewafukuzia, nami nitawarudisha mahali ambapo nilikuwa nimewatoa walipochukuliwa uhamishoni,” asema Bwana.

  2. 3 Ahimidiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki sisi kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho ndani ya Kristo. 4 Kwa maana alituchagua katika yeye kabla ya kuumbwa ulimwengu ili tuwe watakatifu na bila lawama mbele zake. Kwa upendo 5 alitangulia kutuchagua tuwe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo kwa furaha yake na mapenzi yake mwenyewe. 6 Kwa hiyo tunamsifu Mungu kwa huruma zake kuu alizotumiminia sisi katika Mwanawe Mpendwa. 7 Ndani yake tunao ukombozi kwa njia ya damu yake, yaani, msamaha wa dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake 8 aliyotumiminia kwa wingi, kwa hekima yote na maarifa yote. 9 Naye alitujulisha siri ya mapenzi yake sawasawa na uradhi wa mapenzi yake, ambayo alikusudia katika Kristo, 10 ili yapate kutimizwa wakati mkamilifu utakapowadia, yaani, kuvitia vitu vyote vya mbinguni na vya duniani pamoja, chini ya kiongozi mmoja, ndiye Kristo.

  3. 27 Naye Mungu aichunguzaye mioyo, anaijua nia ya Roho, kwa sababu Roho huwaombea watakatifu sawasawa na mapenzi ya Mungu.

    28 Nasi tunajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hutenda kazi pamoja na wote wampendao, katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. 29 Maana wale Mungu aliowajua tangu mwanzo, pia aliwachagua tangu mwanzo, wapate kufanana na mfano wa Mwanawe, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. 30 Nao wale Mungu aliotangulia kuwachagua, akawaita, wale aliowaita pia akawahesabia haki, nao wale aliowahesabia haki, pia akawatukuza.

  4. 10 Bwana huzuia mipango ya mataifa,

    hupinga makusudi ya mataifa.

    11 Lakini mipango ya Bwana inasimama imara milele,

    makusudi ya moyo wake kwa vizazi vyote.

  5. 5 Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote

    wala usizitegemee akili zako mwenyewe;

    6 katika njia zako zote mkiri yeye,

    naye atayanyoosha mapito yako.

  6. 24 Bwana Mwenye Nguvu Zote ameapa,

    “Hakika, kama vile nilivyopanga, ndivyo itakavyokuwa,

    nami kama nilivyokusudia, ndivyo itakavyosimama.

    25 Nitamponda Mwashuru katika nchi yangu,

    juu ya milima yangu nitawakanyagia chini.

    Nira yake itaondolewa kutoka kwa watu wangu,

    nao mzigo wake utaondolewa kutoka mabegani mwao.”

    26 Huu ndio mpango uliokusudiwa kwa ajili ya ulimwengu wote,

    huu ni mkono ulionyooshwa juu ya mataifa yote.

    27 Kwa kuwa Bwana Mwenye Nguvu Zote amekusudia,

    ni nani awezaye kumzuia?

    Mkono wake umenyooshwa,

    ni nani awezaye kuurudisha?

  7. 16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. 17 Kwa maana Mungu hakumtuma Mwanawe kuuhukumu ulimwengu, bali kupitia kwake ulimwengu upate kuokolewa.

  8. 1 Kwa hiyo, ndugu zangu, nawasihi kwa rehema zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu na inayompendeza Mungu, hii ndiyo ibada yenu yenye maana. 2 Msifuatishe tena mfano wa ulimwengu huu, bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu. Ndipo mtaweza kuonja na kuhakikisha ni nini mapenzi ya Mungu yaliyo mema, yanayopendeza machoni pake na ukamilifu.

  9. 22 “Enyi Waisraeli, sikilizeni maneno haya nisemayo: Yesu wa Nazareti alikuwa mtu aliyethibitishwa kwenu na Mungu kwa miujiza, maajabu na ishara, ambayo Mungu alitenda miongoni mwenu kupitia kwake, kama ninyi wenyewe mjuavyo. 23 Huyu mtu akiisha kutolewa kwa shauri la Mungu lililokusudiwa kwa kujua kwake Mungu tangu zamani, ninyi, kwa mikono ya watu wabaya, mlimuua kwa kumgongomea msalabani. 24 Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu akamwondolea uchungu wa mauti, kwa sababu haikuwezekana yeye kushikiliwa na nguvu za mauti.

  10. 21 Kuna mipango mingi ndani ya moyo wa mtu,

    lakini kusudi la Bwana ndilo litakalosimama.

  11. 9 Moyo wa mtu huifikiri njia yake,

    bali Bwana huelekeza hatua zake.

  12. 6 Mtafuteni Bwana maadamu anapatikana;

    mwiteni maadamu yu karibu.

    7 Mtu mwovu na aiache njia yake,

    na mtu mbaya na ayaache mawazo yake.

    Yeye na amrudie Bwana, naye atamrehemu,

    arudi kwa Mungu wetu, kwa kuwa atamsamehe bure kabisa.

    8 “Kwa kuwa mawazo yangu si mawazo yenu,

    wala njia zenu si njia zangu,”

    asema Bwana.

    9 “Kama vile mbingu zilivyo juu kuliko dunia,

    ndivyo njia zangu zilivyo juu kuliko njia zenu

    na mawazo yangu kuliko mawazo yenu.

    10 Kama vile mvua na theluji

    ishukavyo kutoka mbinguni,

    nayo hairudi tena huko

    bila kunywesha dunia

    na kuichipusha na kuistawisha,

    hivyo hutoa mbegu kwa mpanzi

    na mkate kwa mlaji,

    11 ndivyo lilivyo neno langu lile litokalo kinywani mwangu:

    Halitanirudia tupu,

    bali litatimiliza lile nililokusudia

    na litafanikiwa katika kusudi lile nililolituma.

  13. 5 “Mtanilinganisha na nani, au mtanihesabu kuwa sawa na nani?

    Ni nani mtakayenifananisha naye ili tuweze kulinganishwa?

    6 Wengine humwaga dhahabu kutoka kwenye mifuko yao,

    na kupima fedha kwenye mizani;

    huajiri mfua dhahabu kutengeneza mungu,

    kisha huisujudia na kuiabudu.

    7 Huiinua mabegani na kuichukua;

    huiweka mahali pake, papo hapo ndipo isimamapo.

    Wala haiwezi kusogea kutoka mahali pale.

    Ingawa mtu huililia, haimjibu;

    haiwezi kumwokoa kwenye taabu zake.

    8 “Kumbukeni hili, litieni akilini,

    liwekeni moyoni, enyi waasi.

    9 Kumbukeni mambo yaliyopita, yale ya zamani za kale;

    mimi ndimi Mungu, wala hakuna mwingine;

    mimi ndimi Mungu,

    wala hakuna mwingine aliye kama mimi.

    10 Ni mimi nitangazaye mwisho tangu mwanzo,

    naam, tangu zamani za kale,

    mambo ambayo hayajatendeka.

    Ninasema: Kusudi langu ndilo litakalosimama,

    nami nitatenda mapenzi yangu yote.

    11 Kutoka mashariki ninaita ndege awindaye;

    kutoka nchi ya mbali,

    mtu atakayetimiza kusudi langu.

    Lile ambalo nimelisema, ndilo nitakalolitimiza;

    lile nililolipanga, ndilo nitakalolitenda.

  14. 15 Kwa hiyo angalieni sana jinsi mnavyoenenda, si kama watu wasio na hekima, bali kama wenye hekima, 16 mkiukomboa wakati, kwa sababu nyakati hizi ni za uovu. 17 Kwa hiyo msiwe wajinga, bali mpate kujua nini mapenzi ya Bwana.

  15. 13 Basi sikilizeni ninyi msemao, “Leo au kesho tutakwenda katika mji huu ama ule tukae humo mwaka mmoja, tufanye biashara na kupata faida.” 14 Lakini hamjui hata litakalotukia kesho. Maisha yenu ni nini? Ninyi ni ukungu ambao huonekana kwa kitambo kidogo kisha hutoweka. 15 Badala yake, inawapasa kusema, “Kama Bwana akipenda, tutaishi na kufanya hili ama lile.” 16 Kama ilivyo sasa, mnajisifu na kujigamba. Kujisifu kwa namna hiyo ni uovu. 17 Basi mtu yeyote anayejua jema limpasalo kutenda, lakini asilitende, mtu huyo anatenda dhambi.

  16. 8 Lakini wapenzi, msisahau neno hili: kwamba kwa Bwana, siku moja ni kama miaka elfu, na miaka elfu ni kama siku moja. 9 Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama watu wengine wanavyokudhani kukawia. Badala yake, yeye anawavumilia ninyi, maana hataki mtu yeyote aangamie, bali kila mtu afikilie toba.

  17. 6 Lakini miongoni mwa watu waliokomaa twanena hekima, wala si hekima ya ulimwengu huu au ya watawala wa dunia hii wanaobatilika. 7 Sisi tunanena hekima ya Mungu ambayo ni siri, tena iliyofichika, ambayo Mungu aliikusudia kabla ya ulimwengu kuwepo, kwa ajili ya utukufu wetu. 8 Hakuna hata mtawala mmoja wa nyakati hizi aliyeelewa jambo hili. Kwa maana kama wangelielewa, wasingemsulubisha Bwana wa utukufu. 9 Lakini ni kama ilivyoandikwa:

    “Hakuna jicho limepata kuona,

    wala sikio limepata kusikia,

    wala hayakuingia moyoni wowote,

    yale Mungu amewaandalia

    wale wampendao”:

    10 Lakini mambo haya Mungu ametufunulia kwa Roho wake.

    Roho huchunguza kila kitu, hata mambo ya ndani sana ya Mungu.

  18. 2 “Ninajua ya kuwa unaweza kufanya mambo yote,

    wala hakuna mpango wako unaoweza kuzuilika.

  19. 16 Furahini siku zote; 17 ombeni bila kukoma; 18 shukuruni kwa kila jambo, kwa maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu kwa ajili yenu katika Kristo Yesu.

  20. 5 “Kabla sijakuumba ndani ya tumbo la mama yako, nilikujua;

    kabla hujazaliwa nilikutenga kwa kazi maalum;

    nilikuweka uwe nabii kwa mataifa.”

    6 Nami nikasema, “Aa, Bwana Mwenyezi, sijui kusema, kwani mimi ni mtoto mdogo tu.”

    7 Lakini Bwana akaniambia, “Usiseme, ‘Mimi ni mtoto mdogo tu.’ Utaenda popote nitakapokutuma na kunena lolote nitakalokuagiza. 8 Usiwaogope, kwa maana niko pamoja nawe nikuokoe,” asema Bwana.

  21. 1 Hatimaye, ndugu, tuliwaomba na kuwasihi katika Bwana Yesu kwamba, kama mlivyojifunza kutoka kwetu jinsi iwapasavyo kuishi ili kumpendeza Mungu, kama vile mnavyoishi, imewapasa mzidi sana kufanya hivyo. 2 Kwa kuwa mnajua ni maagizo gani tuliyowapa kwa mamlaka ya Bwana Yesu.

    3 Mapenzi ya Mungu ni kwamba ninyi mtakaswe, ili kwamba mjiepushe na zinaa, 4 ili kwamba kila mmoja wenu ajifunze kuutawala mwili wake mwenyewe katika utakatifu na heshima, 5 si kwa tamaa mbaya kama watu wa Mataifa wasiomjua Mungu. 6 Katika jambo hili mtu asimkosee ndugu yake wala kumlaghai. Kwa kuwa Bwana ni mlipiza kisasi katika mambo haya yote, kama vile tulivyokwisha kuwaambia mapema na kuwaonya vikali. 7 Kwa maana Mungu hakutuitia uchafu, bali utakatifu. 8 Kwa hiyo, mtu yeyote anayekataa mafundisho haya hamkatai mwanadamu, bali anamkataa Mungu anayewapa ninyi Roho wake Mtakatifu.

    9 Sasa kuhusu upendo wa ndugu hamna haja mtu yeyote kuwaandikia, kwa maana ninyi wenyewe mmefundishwa na Mungu kupendana. 10 Nanyi kwa kweli mnawapenda ndugu wote katika Makedonia nzima. Lakini ndugu, tunawasihi mzidi sana kuwapenda.

    11 Jitahidini kuishi maisha ya utulivu, kila mtu akijishughulisha na mambo yake mwenyewe na kufanya kazi kwa mikono yake, kama vile tulivyowaagiza, 12 ili maisha yenu ya kila siku yajipatie heshima kutoka kwa watu walio nje, ili msimtegemee mtu yeyote.

  22. 4 Mnapokuja kwake, yeye aliye Jiwe lililo hai, lililokataliwa na wanadamu bali kwa Mungu ni teule na la thamani kwake, 5 ninyi nanyi, kama mawe yaliyo hai, mnajengwa kuwa nyumba ya kiroho, ili mpate kuwa ukuhani mtakatifu, mkitoa dhabihu za kiroho zinazokubaliwa na Mungu kwa njia ya Yesu Kristo. 6 Kwa maana imeandikwa katika Maandiko:

    “Tazama, naweka katika Sayuni,

    jiwe la pembeni teule lenye thamani,

    na yeyote atakayemwamini

    hataaibika kamwe.”

    7 Kwenu ninyi mnaoamini, jiwe hili ni la thamani. Lakini kwao wasioamini,

    “Jiwe walilolikataa waashi

    limekuwa jiwe kuu la pembeni,”

    8 tena,

    “Jiwe lenye kuwafanya watu wajikwae,

    na mwamba wa kuwaangusha.”

    Wanajikwaa kwa sababu hawakulitii lile neno, kama walivyowekewa tangu zamani.

    9 Lakini ninyi ni taifa teule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu walio milki ya Mungu, mlioitwa ili kutangaza sifa zake yeye aliyewaita kutoka gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu. 10 Mwanzo ninyi mlikuwa si taifa, lakini sasa ninyi ni taifa la Mungu. Mwanzo mlikuwa hamjapata rehema, lakini sasa mmepata rehema.

    11 Wapenzi, ninawasihi, mkiwa kama wageni na wapitaji hapa ulimwenguni, epukeni tamaa mbaya za mwili ambazo hupigana vita na roho zenu. 12 Kuweni na mwenendo mzuri mbele ya watu wasiomjua Mungu, ili kama wanawasingizia kuwa watenda mabaya, wayaone matendo yenu mema nao wamtukuze Mungu siku atakapokuja kwetu.

  23. 8 Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea;

    nitakushauri na kukuangalia.

  24. 38 Kwa kuwa nimeshuka kutoka mbinguni si ili kufanya mapenzi yangu, bali mapenzi yake yeye aliyenituma. 39 Haya ndiyo mapenzi yake yeye aliyenituma, kwamba, nisimpoteze hata mmoja wa wale alionipa, bali niwafufue siku ya mwisho. 40 Kwa maana mapenzi ya Baba yangu ni kwamba kila mmoja amtazamaye, Mwana na kumwamini awe na uzima wa milele, nami nitawafufua siku ya mwisho.”

  25. 10 Kwa maana sisi ni kazi ya mikono ya Mungu, tulioumbwa katika Kristo Yesu, ili tupate kutenda matendo mema, ambayo Mungu alitangulia kuyaandaa tupate kuishi katika hayo.

  26. 3 Ninamshukuru Mungu wangu kila niwakumbukapo ninyi. 4 Katika maombi yangu yote daima nimekuwa nikiwaombea ninyi nyote kwa furaha, 5 kwa sababu ya kushiriki kwenu katika kueneza Injili, tangu siku ya kwanza hadi leo. 6 Nina hakika kwamba yeye aliyeianza kazi njema mioyoni mwenu, ataiendeleza na kuikamilisha hata siku ya Kristo Yesu.

  27. 26 Ndipo Mungu akasema, “Tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu, wakatawale juu ya samaki wa baharini na ndege wa angani, juu ya mifugo, juu ya dunia yote, na juu ya viumbe wote watambaao juu ya nchi.”

    27 Kwa hiyo Mungu akamuumba mtu kwa mfano wake mwenyewe,

    kwa mfano wa Mungu alimuumba;

    mwanaume na mwanamke aliwaumba.

    28 Mungu akawabariki na akawaambia, “Zaeni na mkaongezeke, mkaijaze tena dunia na kuitiisha. Mkatawale samaki wa baharini, ndege wa angani, na kila kiumbe hai kiendacho juu ya ardhi.”

    29 Kisha Mungu akasema, “Nimewapa kila mche utoao mbegu juu ya uso wa dunia yote, na kila mti wenye matunda yenye mbegu ndani yake. Vitakuwa chakula chenu. 30 Nao wanyama wote wa dunia, ndege wote wa angani, na viumbe vyote viendavyo juu ya ardhi: yaani kila kiumbe chenye pumzi ya uhai, ninawapa kila mche wa kijani kuwa chakula.” Ikawa hivyo.

    31 Mungu akaona vyote alivyoumba, na tazama, ilikuwa vizuri sana. Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya sita.

  28. 12 Bali wote waliompokea, aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake. 13 Hawa ndio wasiozaliwa kwa damu, wala kwa mapenzi ya mwili au kwa mapenzi ya mtu, bali kwa mapenzi ya Mungu.

  29. 13 Lakini Paulo akajibu, “Kwa nini mnalia na kunivunja moyo? Mimi niko tayari si kufungwa tu, bali hata kufa huko Yerusalemu kwa ajili ya jina la Bwana Yesu.” 14 Alipokuwa hashawishiki, tukaacha kumsihi, tukasema, “Mapenzi ya Bwana na yatendeke.”

  30. 20 Yuko wapi mwenye hekima? Yuko wapi msomi? Yuko wapi mwanafalsafa wa nyakati hizi? Je, Mungu hakufanya hekima ya ulimwengu huu kuwa upumbavu? 21 Kwa kuwa katika hekima ya Mungu, ulimwengu kwa hekima yake haukumjua yeye, ilimpendeza Mungu kuwaokoa wale walioamini kwa upuzi wa lile neno lililohubiriwa. 22 Wayahudi wanadai ishara za miujiza na Wayunani wanatafuta hekima. 23 Lakini sisi tunamhubiri Kristo aliyesulubiwa: yeye kwa Wayahudi ni kikwazo na kwa Wayunani ni upuzi. 24 Lakini kwa wale ambao Mungu amewaita, Wayahudi na pia Wayunani, Kristo ndiye nguvu ya Mungu na pia hekima ya Mungu. 25 Kwa maana upumbavu wa Mungu una hekima zaidi kuliko hekima ya wanadamu, nao udhaifu wa Mungu una nguvu kuliko nguvu ya wanadamu.

    26 Ndugu zangu, kumbukeni mlivyokuwa mlipoitwa. Kwa kipimo cha kibinadamu, si wengi wenu mliokuwa na hekima. Si wengi mliokuwa na ushawishi, si wengi mliozaliwa katika jamaa zenye vyeo. 27 Lakini Mungu alivichagua vitu vipumbavu vya ulimwengu ili awaaibishe wenye hekima, Mungu alivichagua vitu dhaifu vya ulimwengu ili awaaibishe wenye nguvu. 28 Alivichagua vitu vya chini na vinavyodharauliwa vya dunia hii, vitu ambavyo haviko, ili avibatilishe vile vilivyoko, 29 ili mtu yeyote asijisifu mbele zake. 30 Bali kwa yeye ninyi mmepata kuwa katika Kristo Yesu, aliyefanyika kwetu hekima itokayo kwa Mungu, yaani haki, na utakatifu na ukombozi. 31 Hivyo, kama ilivyoandikwa: “Yeye ajisifuye na ajisifu katika Bwana.”

  31. 23 Kama Bwana akipendezwa na njia ya mtu,

    yeye huimarisha hatua zake,

    24 ajapojikwaa, hataanguka,

    kwa maana Bwana

    humtegemeza kwa mkono wake.

  32. 26 Lakini huyo Msaidizi, yaani, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwenu kwa Jina langu, atawafundisha mambo yote na kuwakumbusha yote niliyowaambia.

  33. 5 Kwa hiyo, Kristo alipokuja duniani, alisema:

    “Dhabihu na sadaka hukuzitaka,

    bali mwili uliniandalia;

    6 sadaka za kuteketezwa na za dhambi

    hukupendezwa nazo.

    7 Ndipo niliposema, ‘Mimi hapa, nimekuja,

    imeandikwa kunihusu katika kitabu:

    Nimekuja kuyafanya mapenzi yako, Ee Mungu.’ ”

    8 Kwanza alisema, “Dhabihu na sadaka, sadaka za kuteketezwa na za dhambi hukuzitaka, wala hukupendezwa nazo” (ingawa sheria iliagiza zitolewe). 9 Kisha akasema “Mimi hapa, nimekuja kuyafanya mapenzi yako.” Aondoa lile Agano la kwanza ili kuimarisha la pili. 10 Katika mapenzi hayo sisi tumetakaswa na kufanywa watakatifu kwa njia ya sadaka ya mwili wa Yesu Kristo alioutoa mara moja tu.

  34. 20 Basi Mungu wa amani, ambaye kwa damu ya Agano la milele alimleta tena kutoka kwa wafu Bwana wetu Yesu, yule Mchungaji Mkuu wa kondoo, 21 awafanye ninyi wakamilifu mkiwa mmekamilishwa katika kila jambo jema ili mpate kutenda mapenzi yake, naye atende ndani yetu kile kinachompendeza machoni Pake, kwa njia ya Yesu Kristo, ambaye utukufu una yeye milele na milele. Amen.

  35. 15 Kwa maana ni mapenzi ya Mungu kwamba kwa kutenda mema mnyamazishe maneno ya kijinga ya watu wapumbavu.

  36. 14 Huu ndio ujasiri tulio nao tunapomkaribia Mungu, kwamba kama tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia.

  37. 20 Mlikusudia kunidhuru, lakini Mungu alikusudia mema, ili litimie hili linalofanyika sasa, kuokoa maisha ya watu wengi.

  38. 8 Amekuonyesha yaliyo mema, ee mwanadamu.

    Bwana anataka nini kwako?

    Ila kutenda kwa haki na kupenda rehema,

    na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako.

  39. 31 Wakati huo wanafunzi wake walikuwa wakimsihi, “Rabi, kula angalau chochote.”

    32 Lakini yeye akawajibu, “Mimi ninacho chakula ambacho ninyi hamkifahamu.”

    33 Basi wanafunzi wakaanza kuulizana, “Kuna mtu ambaye amemletea chakula?” 34 Lakini Yesu akawajibu, “Chakula changu ni kufanya mapenzi ya Mungu ambaye amenituma na kuikamilisha kazi yake.

  40. 30 “Mimi siwezi kufanya jambo lolote peke yangu. Ninavyosikia ndivyo ninavyohukumu, nayo hukumu yangu ni ya haki kwa kuwa sitafuti kufanya mapenzi yangu mwenyewe, bali mapenzi yake yeye aliyenituma.

  41. 3 Neema iwe nanyi na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana wetu Yesu Kristo, 4 aliyejitoa kwa ajili ya dhambi zetu ili apate kutuokoa katika ulimwengu huu wa sasa ulio mbaya, sawasawa na mapenzi yake yeye aliye Mungu na Baba yetu. 5 Utukufu una yeye milele na milele. Amen.

  42. 4 Mtu yeyote asemaye kuwa, “Ninamjua,” lakini hazishiki amri zake, ni mwongo, wala ndani ya mtu huyo hamna kweli. 5 Lakini mtu yeyote anayelitii neno lake, upendo wa Mungu umekamilika ndani yake kweli kweli. Katika hili twajua kuwa tumo ndani yake. 6 Yeyote anayesema anakaa ndani yake hana budi kuenenda kama Yesu alivyoenenda.

  43. 33 Akawauliza, “Mama yangu na ndugu zangu ni nani?”

    34 Kisha akawatazama wale watu waliokuwa wameketi kumzunguka pande zote, akasema, “Hawa ndio mama yangu na ndugu zangu. 35 Mtu yeyote anayetenda mapenzi ya Mungu, huyo ndiye ndugu yangu, na dada yangu na mama yangu.”

  44. 25 Ndugu zangu, ili msije mkajidai kuwa wenye hekima kuliko mlivyo, nataka mfahamu siri hii: Ugumu umewapata Israeli kwa sehemu hadi idadi ya watu wa Mataifa watakaoingia itimie. 26 Hivyo Israeli wote wataokolewa. Kama ilivyoandikwa:

    “Mkombozi atakuja kutoka Sayuni;

    ataondoa kutokumcha Mungu katika Yakobo.

    27 Hili ndilo agano langu nao

    nitakapoziondoa dhambi zao.”

    28 Kwa habari ya Injili, wao ni adui wa Mungu kwa ajili yenu, lakini kuhusu kule kuteuliwa kwao ni wapendwa, kwa ajili ya mababa zao wa zamani, 29 kwa maana akishawapa watu karama, Mungu haziondoi, wala wito wake. 30 Kama vile ninyi wakati fulani mlivyokuwa waasi kwa Mungu lakini sasa mmepata rehema kwa sababu ya kutokutii kwao, 31 hivyo nao Waisraeli wamekuwa waasi ili kwamba wao nao sasa waweze kupata rehema kwa ajili ya rehema za Mungu kwenu. 32 Kwa maana Mungu amewafunga wanadamu wote kwenye kuasi ili apate kuwarehemu wote.

    33 Tazama jinsi kilivyo kina cha utajiri

    wa hekima na maarifa ya Mungu!

    Tazama jinsi ambavyo hukumu zake hazichunguziki,

    na ambavyo njia zake zisivyotafutikana!

    34 “Ni nani aliyeyafahamu mawazo ya Bwana?

    Au ni nani ambaye amekuwa mshauri wake?”

    35 “Au ni nani aliyempa chochote

    ili arudishiwe?”

    36 Kwa maana vitu vyote vyatoka kwake, viko kwake na kwa ajili yake.

    Utukufu ni wake milele! Amen.

  45. 35 Kwa hiyo msiutupe ujasiri wenu, kwa maana una thawabu kubwa mno. 36 Inawapasa kuvumilia ili mkiisha kufanya mapenzi ya Mungu mpate kile alichoahidi. 37 Kwa kuwa bado kitambo kidogo tu,

    “Yeye ajaye atakuja wala hatakawia.

    38 Lakini mwenye haki wangu

    ataishi kwa imani.

    Naye kama akisitasita,

    sina furaha naye.”

  46. 14 Hivyo Bwana Mungu akamwambia nyoka, “Kwa kuwa umefanya hili,

    “Umelaaniwa kuliko wanyama wote

    wa kufugwa na wa porini!

    Utatambaa kwa tumbo lako

    na kula mavumbi

    siku zote za maisha yako.

    15 Nami nitaweka uadui

    kati yako na huyo mwanamke,

    na kati ya uzao wako na wake,

    yeye atakuponda kichwa,

    nawe utamuuma kisigino.”

  47. 15 Tazama, naweka mbele yako leo uzima na mafanikio, mauti na maangamizo. 16 Ninakuamuru leo kwamba umpende Bwana Mungu wako, utembee katika njia zake, na kutunza maagizo yake, amri na sheria zake; ndipo utakapoishi na kuongezeka, naye Bwana Mungu wako atakubariki katika nchi unayoingia kuimiliki.

    17 Lakini kama moyo wako ukigeukia mbali ukawa huna utii, kama umevutwa kuisujudia miungu mingine na kuiabudu, 18 nakutangazia leo hii kwamba hakika utaangamizwa. Hutaishi maisha marefu katika nchi unayovuka Yordani kuiingia na kuimiliki.

    19 Leo ninaziita mbingu na nchi kama mashahidi dhidi yako kwamba nimeweka mbele yako uzima na mauti, baraka na laana. Basi sasa chagueni uzima, ili wewe na watoto wako mpate kuishi, 20 na ili upate kumpenda Bwana Mungu wako, uisikilize sauti yake na kuambatana naye. Kwa kuwa Bwana ndiye uzima wako, na atakupa wingi wa siku ili upate kuishi katika nchi aliyoapa kuwapa baba zako Abrahamu, Isaki na Yakobo.

  48. 20 Mhimidini Bwana, enyi malaika zake,

    ninyi mlio mashujaa mnaozitii amri zake,

    ninyi mnaotii neno lake.

    21 Mhimidini Bwana, ninyi jeshi lake lote la mbinguni,

    ninyi watumishi wake mnaofanya mapenzi yake.

  49. 13 Kwa maana wewe ndiwe uliyeumba utu wangu wa ndani;

    uliniunga pamoja tumboni mwa mama yangu.

    14 Ninakusifu kwa sababu nimeumbwa

    kwa namna ya ajabu na ya kutisha;

    kazi zako ni za ajabu,

    ninajua hayo kikamilifu.

    15 Umbile langu halikufichika kwako,

    nilipoumbwa mahali pa siri.

    Nilipoungwa pamoja kwa ustadi katika vilindi vya nchi,

    16 macho yako yaliniona kabla mwili wangu haujakamilika.

    Siku zangu zote ulizonipangia

    ziliandikwa katika kitabu chako

    kabla haijakuwepo hata moja.

    17 Tazama jinsi yalivyo ya thamani mawazo yako kwangu, Ee Mungu!

    Jinsi jumla yake ilivyo kubwa!

  50. 10 Nifundishe kufanya mapenzi yako,

    kwa maana wewe ndiwe Mungu wangu,

    Roho wako mwema na aniongoze

    katika nchi tambarare.

  51. 21 “Si kila mtu aniambiaye, ‘Bwana, Bwana,’ atakayeingia katika Ufalme wa Mbinguni, bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.

  52. 50 Kwa maana yeyote afanyaye mapenzi ya Baba yangu wa mbinguni, huyo ndiye ndugu yangu, na dada yangu na mama yangu.”

  53. 10 “Angalia ili usimdharau mmojawapo wa hawa wadogo, kwa maana nawaambia, malaika wao mbinguni daima wanauona uso wa Baba yangu aliye mbinguni. [ 11 Kwa maana Mwana wa Adamu alikuja kuokoa kile kilichopotea.]

    12 “Mwaonaje? Ikiwa mtu ana kondoo mia moja, na mmoja wao akapotea, je, hatawaacha wale tisini na tisa vilimani na kwenda kumtafuta huyo mmoja aliyepotea? 13 Naye akishampata, amin, nawaambia, hufurahi zaidi kwa ajili ya huyo kondoo mmoja kuliko wale tisini na tisa ambao hawakupotea. 14 Vivyo hivyo, Baba yenu wa mbinguni hapendi hata mmojawapo wa hawa wadogo apotee.

  54. 39 Akaenda mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akaomba akisema, “Baba yangu, kama inawezekana, kikombe hiki na kiniondokee. Lakini si kama nipendavyo mimi, bali kama upendavyo wewe.”

    40 Kisha akarudi kwa wanafunzi wake, akawakuta wamelala. Akamuuliza Petro, “Je, ninyi hamkuweza kukesha pamoja nami hata kwa saa moja?

  55. 42 Akaenda tena mara ya pili na kuomba, “Baba yangu, kama haiwezekani kikombe hiki kiniepuke nisikinywe, basi mapenzi yako yafanyike.”

  56. 42 akisema, “Baba, kama ni mapenzi yako, niondolee kikombe hiki. Lakini si kama nipendavyo, bali mapenzi yako yatendeke.”

  57. 22 Baada ya kumwondoa Sauli katika ufalme, akawainulia Daudi kuwa mfalme wao. Mungu pia alimshuhudia, akisema, ‘Nimemwona Daudi mwana wa Yese, mtu anayeupendeza moyo wangu, atakayetimiza mapenzi yangu yote.’

  58. 3 Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo! Kwa rehema zake kuu ametuzaa sisi mara ya pili katika tumaini lenye uzima kupitia kwa kufufuka kwa Yesu Kristo kutoka kwa wafu, 4 ili tuupate urithi usioharibika, usio na uchafu, ule usionyauka: uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu, 5 ninyi ambao mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani, hadi uje ule wokovu ulio tayari kufunuliwa nyakati za mwisho. 6 Katika hili mnafurahi sana, ingawa sasa kwa kitambo kidogo mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna nyingi. 7 Haya yamewajia ili kwamba imani yenu, iliyo ya thamani kuliko dhahabu ipoteayo, ingawa hujaribiwa kwa moto, ionekane kuwa halisi na imalizie katika sifa, utukufu na heshima wakati Yesu Kristo atadhihirishwa. 8 Ingawa hamjamwona, mnampenda; tena ingawa sasa hammwoni, mnamwamini na kujawa na furaha isiyoneneka yenye utukufu usioelezeka. 9 Maana mnaupokea wokovu wa roho zenu, ambao ndio lengo la imani yenu.

    10 Kwa habari ya wokovu huu, wale manabii waliosema kuhusu neema ambayo ingewajia ninyi, walitafuta kwa bidii na kwa uangalifu mkubwa, 11 wakijaribu kujua ni wakati upi na katika mazingira gani ambayo Roho wa Kristo aliyekuwa ndani yao alionyesha, alipotabiri kuhusu mateso ya Kristo na utukufu ule ambao ungefuata. 12 Walidhihirishiwa kwamba walikuwa hawajihudumii wao wenyewe, bali waliwahudumia ninyi, waliponena kuhusu mambo hayo, ambayo sasa yamehubiriwa kwenu na wale waliowahubiria ninyi Injili kwa Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni. Hata malaika wanatamani kuyafahamu mambo haya.

  59. 19 Kwa hiyo, wale wanaoteswa kulingana na mapenzi ya Mungu, wajikabidhi kwa Muumba wao aliye mwaminifu, huku wakizidi kutenda mema.

  60. 5 Huyo mnyama akapewa kusema maneno ya kiburi na kukufuru na kutumia mamlaka yake kwa muda wa miezi arobaini na miwili. 6 Akafungua kinywa chake ili kumkufuru Mungu, akilitukana Jina lake na mahali aishipo na wale wakaao mbinguni. 7 Pia akaruhusiwa kufanya vita na watakatifu na kuwashinda. Akapewa uwezo juu ya watu wa kila kabila, jamaa, lugha na taifa. 8 Nao watu wote waishio duniani watamwabudu huyo mnyama, yaani, wale wote ambao majina yao hayakuandikwa kwenye kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo aliyechinjwa tangu kuumbwa kwa ulimwengu.

  61. 4 Ndipo Yosefu akawaambia ndugu zake, “Sogeeni karibu nami.” Waliposogea, akasema, “Mimi ni ndugu yenu Yosefu, yule ambaye mlimuuza Misri! 5 Sasa, msihuzunike wala msijichukie wenyewe kwa kuniuza huku, kwa sababu ilikuwa ni ili kuokoa maisha ya watu ndiyo sababu Mungu alinituma niwatangulie ninyi. 6 Kwa miaka miwili sasa imekuwepo njaa katika nchi, pia kwa miaka mitano ijayo hapatakuwepo kulima wala kuvuna. 7 Lakini Mungu alinitanguliza mbele yenu ili kuhifadhi mabaki kwa ajili yenu katika nchi, na kuokoa maisha yenu kwa wokovu mkuu.

    8 “Kwa hiyo basi, si ninyi mlionileta huku, bali ni Mungu. Alinifanya kuwa baba kwa Farao, bwana wa watu wa nyumbani mwake wote, na mtawala wa Misri yote.

  62. 8 Ee Mungu wangu,

    natamani kuyafanya mapenzi yako;

    sheria yako iko ndani ya moyo wangu.”

  63. 6 Mbwa mwitu ataishi pamoja na mwana-kondoo,

    naye chui atalala pamoja na mbuzi,

    ndama, mwana simba na ngʼombe wa mwaka mmoja watakaa pamoja,

    naye mtoto mdogo atawaongoza.

    7 Ngʼombe na dubu watalisha pamoja,

    watoto wao watalala pamoja,

    na simba atakula majani makavu kama maksai.

    8 Mtoto mchanga atacheza karibu na shimo la nyoka,

    naye mtoto mdogo ataweka mkono wake

    kwenye kiota cha fira.

    9 Hawatadhuru wala kuharibu

    juu ya mlima wangu mtakatifu wote,

    kwa kuwa dunia itajawa na kumjua Bwana

    kama maji yajazavyo bahari.

  64. 29 Je, shomoro wawili hawauzwi kwa senti moja tu? Lakini hakuna hata mmoja wao atakayeanguka chini pasipo Baba yenu kujua. 30 Hata nywele za vichwa vyenu zote zimehesabiwa. 31 Hivyo msiogope; kwa maana ninyi ni wa thamani kubwa kuliko shomoro wengi.

  65. 13 Mungu alipompa Abrahamu ahadi yake, kwa kuwa hakuwepo mwingine aliyekuwa mkuu kuliko yeye ambaye angeweza kuapa kwa jina lake, aliapa kwa nafsi yake, 14 akisema, “Hakika nitakubariki na kukupa wazao wengi.” 15 Abrahamu naye, baada ya kungoja kwa saburi, alipokea kile kilichoahidiwa.

    16 Wanadamu huapa kwa yeye aliye mkuu kuwaliko, nacho kiapo hicho huthibitisha kile kilichosemwa na hivyo humaliza mabishano yote. 17 Mungu alipotaka kuonyesha kwa udhahiri zaidi ile asili ya kutokubadilika kwa ahadi yake kwa warithi wa ahadi, aliithitibisha kwa kiapo. 18 Mungu alifanya hivyo ili kwa vitu viwili visivyobadilika, yaani ahadi yake na kiapo chake, ambavyo kwavyo Mungu hawezi kusema uongo, sisi ambao tumemkimbilia ili tulishike lile tumaini lililowekwa mbele yetu tuwe na faraja thabiti. 19 Tunalo tumaini hili kama nanga ya roho iliyo imara na thabiti. Tumaini hili huingia katika sehemu takatifu iliyopo nyuma ya pazia, 20 mahali ambapo Yesu mtangulizi wetu aliingia kwa niaba yetu. Yeye amekuwa Kuhani Mkuu milele, kwa mfano wa Melkizedeki.