42 Bible Verses About Nature
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
-
26 Ndipo Mungu akasema, “Tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu, wakatawale juu ya samaki wa baharini na ndege wa angani, juu ya mifugo, juu ya dunia yote, na juu ya viumbe wote watambaao juu ya nchi.”
27 Kwa hiyo Mungu akamuumba mtu kwa mfano wake mwenyewe,
kwa mfano wa Mungu alimuumba;
mwanaume na mwanamke aliwaumba.
28 Mungu akawabariki na akawaambia, “Zaeni na mkaongezeke, mkaijaze tena dunia na kuitiisha. Mkatawale samaki wa baharini, ndege wa angani, na kila kiumbe hai kiendacho juu ya ardhi.”
29 Kisha Mungu akasema, “Nimewapa kila mche utoao mbegu juu ya uso wa dunia yote, na kila mti wenye matunda yenye mbegu ndani yake. Vitakuwa chakula chenu. 30 Nao wanyama wote wa dunia, ndege wote wa angani, na viumbe vyote viendavyo juu ya ardhi: yaani kila kiumbe chenye pumzi ya uhai, ninawapa kila mche wa kijani kuwa chakula.” Ikawa hivyo.
31 Mungu akaona vyote alivyoumba, na tazama, ilikuwa vizuri sana. Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya sita.
-
18 Ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni dhidi ya uasi wote na uovu wa wanadamu ambao huipinga kweli kwa uovu wao, 19 kwa maana yote yanayoweza kujulikana kumhusu Mungu ni dhahiri kwao, kwa sababu Mungu mwenyewe ameyadhihirisha kwao. 20 Kwa maana tangu kuumbwa kwa ulimwengu, asili ya Mungu asiyeonekana kwa macho, yaani, uweza wake wa milele na asili yake ya Uungu, imeonekana waziwazi, ikitambuliwa kutokana na yale aliyoyafanya ili wanadamu wasiwe na udhuru.
21 Kwa maana ingawa walimjua Mungu, hawakumtukuza yeye kama ndiye Mungu wala hawakumshukuru, bali fikira zao zimekuwa batili na mioyo yao ya ujinga ikatiwa giza. 22 Ingawa walijidai kuwa wenye hekima, wakawa wajinga 23 na kubadili utukufu wa Mungu aishiye milele kwa sanamu zilizofanywa zifanane na mwanadamu ambaye hufa, na mfano wa ndege, wanyama na viumbe vitambaavyo.
-
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.
1 Mbingu zinatangaza utukufu wa Mungu,
anga zahubiri kazi ya mikono yake.
2 Siku baada ya siku zinatoa habari,
usiku baada ya usiku zinatangaza maarifa.
-
Kwa mwimbishaji. Mtindo wa gitithi. Zaburi ya Daudi.
1 Ee Bwana, Bwana wetu,
tazama jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote!
Umeuweka utukufu wako
juu ya mbingu.
2 Midomoni mwa watoto wachanga na wanyonyao
umeamuru sifa,
kwa sababu ya watesi wako,
kumnyamazisha adui na mlipiza kisasi.
3 Nikiziangalia mbingu zako,
kazi ya vidole vyako,
mwezi na nyota,
ulizoziratibisha,
4 mwanadamu ni kitu gani hata unamfikiria,
binadamu ni nani hata unamjali?
5 Umemfanya chini kidogo kuliko viumbe wa mbinguni,
ukamvika taji ya utukufu na heshima.
6 Umemfanya mtawala juu ya kazi za mikono yako;
umeweka vitu vyote chini ya miguu yake.
7 Mifugo na makundi yote pia,
naam, na wanyama wa kondeni,
8 ndege wa angani na samaki wa baharini,
naam, kila kiogeleacho katika njia za bahari.
-
15 Yeye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. 16 Kwake yeye vitu vyote vilivyoko mbinguni na juu ya nchi viliumbwa: vitu vinavyoonekana na visivyoonekana, viwe ni viti vya enzi au falme, au wenye mamlaka au watawala; vitu vyote viliumbwa na yeye na kwa ajili yake. 17 Yeye alikuwepo kabla ya vitu vyote, na katika yeye vitu vyote vinashikamana pamoja. 18 Yeye ndiye kichwa cha mwili, yaani kanisa, naye ndiye mwanzo na mzaliwa wa kwanza kutoka kwa wafu, ili yeye awe mkuu katika vitu vyote. 19 Kwa kuwa ilimpendeza Mungu kwamba utimilifu wake wote ukae ndani yake, 20 na kwa njia yake aweze kuvipatanisha vitu vyote na yeye mwenyewe, viwe ni vitu vilivyo duniani au vilivyo mbinguni, kwa kufanya amani kwa damu yake, iliyomwagika msalabani.
-
5 Kwa hiyo, ueni kabisa chochote kilicho ndani yenu cha asili ya kidunia: yaani uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya na ulafi, ambayo ndiyo ibada ya sanamu. 6 Kwa sababu ya mambo haya, ghadhabu ya Mungu inakuja. 7 Ninyi pia zamani mlienenda katika mambo haya mlipoishi maisha hayo. 8 Lakini sasa yawekeni mbali nanyi mambo kama haya yote: yaani hasira, ghadhabu, uovu, masingizio na lugha chafu kutoka midomoni mwenu. 9 Msiambiane uongo, kwa maana mmevua kabisa utu wenu wa kale pamoja na matendo yake, 10 nanyi mmevaa utu mpya, unaofanywa upya katika ufahamu sawasawa na mfano wa Muumba wake. 11 Hapa hakuna Myunani wala Myahudi, aliyetahiriwa wala asiyetahiriwa, asiyestaarabika wala aliyestaarabika, mtumwa wala mtu huru, bali Kristo ni yote, na ndani ya wote.
-
19 Kwa maana viumbe vyote vinangoja kwa shauku kudhihirishwa kwa watoto wa Mungu. 20 Kwa kuwa viumbe vyote viliwekwa chini ya ubatili, si kwa chaguo lao, bali kwa mapenzi yake yeye aliyevitiisha katika tumaini, 21 ili kwamba viumbe vyote vipate kuwekwa huru kutoka kwa utumwa wa kuharibika na kupewa uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu.
22 Kwa maana twajua ya kuwa hata sasa viumbe vyote vimekuwa vikilia kwa maumivu kama utungu wa mwanamke wakati wa kuzaa. 23 Wala si hivyo viumbe peke yao, bali hata sisi ambao ndio matunda ya kwanza ya Roho, kwa ndani tunalia kwa uchungu tukisubiri kwa shauku kufanywa wana wa Mungu, yaani, ukombozi wa miili yetu.
-
10 Katikati ya mataifa semeni, “Bwana anatawala.”
Ulimwengu ameuweka imara, hauwezi kusogezwa;
atawahukumu watu kwa uadilifu.
11 Mbingu na zishangilie, nchi na ifurahi;
bahari na ivume, na vyote vilivyomo ndani yake;
12 mashamba na yashangilie,
pamoja na vyote vilivyomo ndani yake.
Kisha miti yote ya msituni itaimba kwa furaha;
13 itaimba mbele za Bwana kwa maana anakuja,
anakuja kuihukumu dunia.
Ataihukumu dunia kwa haki,
na mataifa katika kweli yake.
-
4 Haya ndiyo maelezo ya mbingu na dunia wakati zilipoumbwa.
Bwana Mungu alipoziumba mbingu na dunia, 5 hapakuwepo na mche wa shambani uliokuwa umejitokeza ardhini, wala hapakuwepo na mmea wa shamba uliokuwa umeota, kwa kuwa Bwana Mungu alikuwa hajanyeshea mvua juu ya nchi, na hapakuwepo mtu wa kuilima ardhi, 6 lakini umande ulitokeza kutoka ardhini na kunyesha uso wote wa nchi: 7 Bwana Mungu alimuumba mtu kutoka mavumbi ya ardhi, akampulizia pumzi ya uhai puani mwake, naye mtu akawa kiumbe hai.
8 Basi Bwana Mungu alikuwa ameotesha bustani upande wa mashariki, katika Edeni, huko akamweka huyo mtu aliyemuumba. 9 Bwana Mungu akafanya aina zote za miti ziote kutoka ardhini, miti yenye kupendeza macho na mizuri kwa chakula. Katikati ya bustani ulikuwepo mti wa uzima na mti wa kujua mema na mabaya.
-
7 “Lakini ulizeni wanyama, nao watawafundisha,
au ndege wa angani, nao watawaambia;
8 au zungumzeni na dunia, nayo itawafundisha,
au acheni samaki wa baharini wawape taarifa.
9 Ni nani miongoni mwa hawa wote asiyejua
kwamba mkono wa Bwana ndio uliofanya hili?
10 Mkononi mwake kuna uhai wa kila kiumbe,
na pumzi ya wanadamu wote.
-
26 Kwa sababu hii, Mungu aliwaacha wavunjiane heshima kwa kufuata tamaa zao za aibu. Hata wanawake wao wakabadili matumizi ya asili ya miili yao wakaitumia isivyokusudiwa. 27 Vivyo hivyo wanaume pia wakiacha matumizi ya asili ya wanawake wakawakiana tamaa wao kwa wao. Wanaume wakafanyiana matendo ya aibu na wanaume wengine nao wakapata katika maisha yao adhabu iliyowastahili kwa ajili ya upotovu wao.
-
1 Kwa habari zenu, mlikuwa wafu katika makosa na dhambi zenu, 2 ambazo mlizitenda mlipofuatisha namna ya ulimwengu huu na za yule mtawala wa ufalme wa anga, yule roho atendaye kazi sasa ndani ya wale wasiotii. 3 Sisi sote pia tuliishi katikati yao hapo zamani, tukitimiza tamaa za asili yetu ya dhambi na kufuata tamaa zake na mawazo yake. Nasi kwa asili tulikuwa wana wa ghadhabu, kama mtu mwingine yeyote. 4 Lakini Mungu kwa upendo wake mwingi kwetu sisi, ambaye ni mwingi wa rehema, 5 hata tulipokuwa wafu kwa ajili ya makosa yetu, alitufanya tuwe hai pamoja na Kristo Yesu, yaani, mmeokolewa kwa neema.
-
9 Moyo ni mdanganyifu kuliko vitu vyote,
ni mwovu kupita kiasi.
Ni nani awezaye kuujua?
-
17 Lakini kama baadhi ya matawi yalikatwa, nawe chipukizi la mzeituni mwitu ukapandikizwa mahali pao ili kushiriki unono pamoja na matawi mengine kutoka shina la mzeituni, 18 basi usijivune juu ya hayo matawi. Kama ukijivuna, kumbuka jambo hili: si wewe unayelishikilia shina, bali ni shina linalokushikilia wewe. 19 Basi utasema, “Matawi yale yalikatwa ili nipate kupandikizwa katika hilo shina.” 20 Hii ni kweli. Matawi hayo yalikatwa kwa sababu ya kutokuamini kwake, lakini wewe umesimama tu kwa sababu ya imani. Kwa hiyo usijivune, bali simama kwa kuogopa. 21 Kwa maana kama Mungu hakuyahurumia matawi ya asili, wala hatakuhurumia wewe.
22 Angalia basi wema na ukali wa Mungu: Kwa wale walioanguka, ukali, bali kwako wewe wema wa Mungu, kama utadumu katika wema wake. La sivyo, nawe utakatiliwa mbali. 23 Wao nao wasipodumu katika kutokuamini kwao, watapandikizwa tena kwenye shina, kwa maana Mungu anao uwezo wa kuwapandikiza tena kwenye hilo shina. 24 Ikiwa wewe ulikatwa kutoka kile ambacho kwa asili ni mzeituni mwitu na kupandikizwa kinyume cha asili kwenye mzeituni uliopandwa, si rahisi zaidi matawi haya ya asili kupandikizwa tena kwenye shina lake la mzeituni!
-
6 Kwa maana kuwa na nia ya mwili ni mauti, bali kuwa na nia inayoongozwa na Roho ni uzima na amani. 7 Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui na Mungu, kwa maana haiitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii. 8 Wale wanaotawaliwa na mwili, hawawezi kumpendeza Mungu.
-
35 Lakini mtu anaweza kuuliza, “Wafu wafufuliwaje? Watakuwa na mwili wa namna gani?” 36 Ninyi wapumbavu kiasi gani? Mpandacho hakiwi hai kama hakikufa. 37 Mpandapo, hampandi mwili ule utakao kuwa, bali mwapanda mbegu tu, pengine ya ngano au ya kitu kingine. 38 Lakini Mungu huipa mbegu umbo kama alivyokusudia mwenyewe na kila aina ya mbegu huipa umbo lake. 39 Kwa maana nyama zote si za aina moja. Binadamu wana nyama ya aina moja, wanyama wana aina nyingine, kadhalika ndege na samaki wana nyama tofauti. 40 Pia kuna miili ya mbinguni na miili ya duniani, lakini fahari wa ile miili ya mbinguni ni wa aina moja na fahari wa ile miili ya duniani ni wa aina nyingine. 41 Jua lina fahari ya aina moja, mwezi nao una fahari yake na nyota pia, nazo nyota hutofautiana katika fahari.
42 Hivyo ndivyo itakavyokuwa wakati wa ufufuo wa wafu. Ule mwili wa kuharibika uliopandwa, utafufuliwa usioharibika, 43 unapandwa katika aibu, unafufuliwa katika utukufu, unapandwa katika udhaifu, unafufuliwa katika nguvu, 44 unapandwa mwili wa asili, unafufuliwa mwili wa kiroho.
Kama kuna mwili wa asili, basi kuna mwili wa kiroho pia. 45 Kwa hiyo imeandikwa, “Mtu wa kwanza Adamu alifanyika kiumbe hai”; Adamu wa mwisho, yeye ni roho iletayo uzima. 46 Lakini si ule wa kiroho uliotangulia, bali ni ule wa asili, kisha ule wa kiroho. 47 Mtu wa kwanza aliumbwa kwa mavumbi ya ardhini, mtu wa pili alitoka mbinguni. 48 Kama vile alivyokuwa yule wa ardhini, ndivyo walivyo wale walio wa ardhini; na kwa vile alivyo mtu yule aliyetoka mbinguni, ndivyo walivyo wale walio wa mbinguni. 49 Kama vile tulivyochukua mfano wa mtu wa ardhini, ndivyo tutakavyochukua mfano wa yule mtu aliyetoka mbinguni.
50 Ndugu zangu nisemalo ni hili: nyama na damu haviwezi kuurithi ufalme wa Mungu, wala kuharibika kurithi kutokuharibika.
-
29 Je, shomoro wawili hawauzwi kwa senti moja tu? Lakini hakuna hata mmoja wao atakayeanguka chini pasipo Baba yenu kujua. 30 Hata nywele za vichwa vyenu zote zimehesabiwa. 31 Hivyo msiogope; kwa maana ninyi ni wa thamani kubwa kuliko shomoro wengi.
-
24 “Mungu aliyeumba dunia na vyote vilivyomo ndani yake, yeye ndiye Bwana wa mbingu na nchi, hakai katika mahekalu yaliyojengwa kwa mikono ya wanadamu. 25 Wala hatumikiwi na mikono ya wanadamu kana kwamba anahitaji chochote, kwa sababu yeye mwenyewe ndiye awapaye watu wote uhai na pumzi na vitu vyote. 26 Kutoka kwa mtu mmoja, yeye aliumba mataifa yote ya wanadamu ili waikalie dunia yote, naye akaweka nyakati za kuishi. 27 Mungu alifanya hivyo ili wanadamu wamtafute na huenda wakamfikia ingawa kwa kupapasapapasa ijapokuwa kwa kweli hakai mbali na kila mmoja wetu. 28 ‘Kwa kuwa katika yeye tunaishi, tunatembea na kuwa na uzima wetu.’ Kama baadhi ya watunga mashairi wenu walivyosema, ‘Sisi ni watoto wake.’
-
1 Zamani Mungu alisema na baba zetu kwa njia ya manabii mara nyingi na kwa njia mbalimbali, 2 lakini katika siku hizi za mwisho anasema nasi kwa njia ya Mwanawe, ambaye amemweka kuwa mrithi wa vitu vyote, na ambaye kupitia kwake aliuumba ulimwengu. 3 Mwana ni mngʼao wa utukufu wa Mungu na mfano halisi wa nafsi yake, akivihifadhi vitu vyote kwa neno lake lenye uweza. Akiisha kufanya utakaso kwa ajili ya dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Aliye Mkuu huko mbinguni. 4 Kwa hiyo alifanyika bora kuliko malaika, kama jina alilorithi lilivyo bora kuliko lao.
-
15 Bwana Mungu akamchukua huyo mtu, akamweka kwenye Bustani ya Edeni ailime na kuitunza.
-
14 Huyafanya majani ya mifugo yaote,
na mimea kwa watu kulima,
wajipatie chakula kutoka ardhini:
15 divai ya kuufurahisha moyo wa mwanadamu,
mafuta kwa ajili ya kungʼarisha uso wake,
na mkate wa kutia mwili nguvu.
16 Miti ya Bwana inanyeshewa vizuri,
mierezi ya Lebanoni aliyoipanda.
17 Humo ndege hufanya viota vyao,
korongo ana nyumba yake kwenye msunobari.
18 Milima mirefu ni makao ya mbuzi-mwitu,
majabali ni kimbilio la pelele.
-
26 Waangalieni ndege wa angani; wao hawapandi wala hawavuni au kuweka ghalani, lakini Baba yenu wa mbinguni huwalisha. Je, ninyi si wa thamani zaidi kuliko hao ndege? 27 Ni nani miongoni mwenu ambaye kwa kujitaabisha kwake anaweza kujiongezea hata saa moja zaidi katika maisha yake?
28 “Nanyi kwa nini mnajitaabisha kwa ajili ya mavazi? Fikirini maua ya shambani yameavyo. Hayafanyi kazi wala hayafumi. 29 Lakini nawaambia, hata Solomoni katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo ya hayo maua. 30 Basi ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya shambani, ambayo leo yapo na kesho yanatupwa motoni, je, hatawavika ninyi vizuri zaidi, enyi wa imani haba?
-
10 Lakini mambo haya Mungu ametufunulia kwa Roho wake.
Roho huchunguza kila kitu, hata mambo ya ndani sana ya Mungu. 11 Kwa maana ni nani anayejua mawazo ya mtu isipokuwa roho iliyo ndani ya huyo mtu? Vivyo hivyo hakuna mtu ajuaye mawazo ya Mungu isipokuwa Roho wa Mungu. 12 Basi hatukupokea roho ya dunia bali Roho atokaye kwa Mungu, ili tuweze kuelewa kile kipawa ambacho Mungu ametupatia bure. 13 Haya ndiyo tusemayo, si kwa maneno tuliyofundishwa kwa hekima ya wanadamu bali kwa maneno tuliyofundishwa na Roho, tukifafanua kweli za kiroho kwa maneno ya kiroho. 14 Mtu ambaye hana Roho hawezi kupokea mambo yatokayo kwa Roho wa Mungu, kwa kuwa ni upuzi kwake, naye hawezi kuyaelewa kwa sababu hayo yanaeleweka tu kwa upambanuzi wa rohoni.
-
1 Ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama watu wa kiroho, bali kama watu wa mwilini, kama watoto wachanga katika Kristo. 2 Naliwanywesha maziwa, wala si chakula kigumu, kwa kuwa hamkuwa tayari kwa hicho chakula. Naam, hata sasa hamko tayari. 3 Ninyi bado ni watu wa mwilini. Kwa kuwa bado kuna wivu na magombano miongoni mwenu, je, ninyi si watu wa mwilini? Je, si mwaendelea kama watu wa kawaida? 4 Kwa maana mmoja anaposema, “Mimi ni wa Paulo,” na mwingine, “Mimi ni wa Apolo,” je, ninyi si wanadamu wa kawaida?
-
6 Ndipo Bwana, Mungu akaweka tayari mzabibu na kuufanya uote, kumpa Yona kivuli kilichomfunika kichwa ili kuondoa taabu yake, naye Yona akafurahi sana kwa ajili ya ule mzabibu. 7 Lakini kesho yake asubuhi na mapema Mungu akaamuru buu, autafune mzabibu huo nao ukanyauka. 8 Wakati jua lilipochomoza, Mungu akautuma upepo wa hari wa mashariki, nalo jua likawaka juu ya kichwa cha Yona mpaka akazimia. Akatamani kufa, naye akasema, “Ni afadhali mimi nife kuliko kuishi.”
9 Lakini Mungu alimwambia Yona, “Je, unayo haki kukasirika kuhusu mzabibu huo?”
Akasema, “Ndiyo, ninayo haki. Nimekasirika kiasi cha kufa.”
10 Lakini Bwana akamwambia, “Wewe unakasirika kwa ajili ya mzabibu huu, nawe hukuusababisha kuota wala kuutunza. Uliota usiku mmoja, nao ukafa usiku mmoja. 11 Lakini Ninawi ina zaidi ya watu 120,000 ambao hawawezi kupambanua kulia au kushoto, pamoja na ngʼombe wengi. Je, hainipasi kufikiri juu ya mji ule mkubwa?”
-
12 Watu wote waliotenda dhambi pasipo sheria wataangamia pasipo sheria, nao wote wale waliotenda dhambi chini ya sheria watahukumiwa kwa sheria. 13 Kwa maana si wale wanaoisikia sheria ambao ni wenye haki mbele za Mungu, bali ni wale wanaoitii sheria ndio watakaohesabiwa haki. 14 (Naam, wakati wa watu wa Mataifa, ambao hawana sheria, wanapofanya kwa asili mambo yatakiwayo na sheria, wao ni sheria kwa nafsi zao wenyewe, hata ingawa hawana sheria. 15 Wao wanaonyesha kwamba lile linalotakiwa na sheria limeandikwa kwenye mioyo yao, ambayo pia dhamiri zao zikiwashuhudia, nayo mawazo yao yenye kupingana yatawashtaki au kuwatetea.) 16 Hili litatukia siku hiyo Mungu atakapozihukumu siri za wanadamu kwa njia ya Yesu Kristo, kama isemavyo Injili yangu.
-
14 Je, maumbile ya asili hayatufundishi kuwa ni aibu kwa mwanaume kuwa na nywele ndefu?
-
16 Bwana Mungu akamwagiza huyo mtu, akamwambia, “Uko huru kula matunda ya mti wowote katika bustani, 17 lakini kamwe usile matunda ya mti wa kujua mema na mabaya, kwa maana siku utakapokula matunda yake, hakika utakufa.”
-
11 Ninaweka Agano nanyi: Kamwe uhai hautafutwa tena kwa gharika, kamwe haitakuwepo tena gharika ya kuangamiza dunia.”
12 Mungu akasema, “Hii ni ishara ya Agano ninalofanya kati yangu na ninyi na kila kiumbe hai kilicho pamoja nanyi, Agano kwa vizazi vyote vijavyo: 13 Nimeweka upinde wangu wa mvua mawinguni, nao utakuwa ishara ya Agano nifanyalo kati yangu na dunia. 14 Wakati wowote ninapotanda mawingu juu ya dunia na upinde wa mvua ukijitokeza mawinguni, 15 nitakumbuka Agano langu kati yangu na ninyi na viumbe vyote vilivyo hai vya kila aina. Kamwe maji hayatakuwa tena gharika ya kuangamiza uhai wote. 16 Wakati wowote upinde wa mvua unapotokea mawinguni, nitauona na kukumbuka Agano la milele kati ya Mungu na viumbe vyote vilivyo hai vya kila aina duniani.”
-
3 Msifuni yeye, enyi jua na mwezi,
msifuni yeye, enyi nyota zote zingʼaazo.
4 Msifuni yeye, enyi mbingu zilizo juu sana,
na ninyi maji juu ya anga.
5 Vilisifu jina la Bwana
kwa maana aliamuru navyo vikaumbwa.
-
3 Dunia itaharibiwa kabisa
na kutekwa nyara kabisa.
Bwana amesema neno hili.
4 Dunia inakauka na kunyauka,
dunia inanyongʼonyea na kunyauka,
waliotukuzwa wa dunia wananyongʼonyea.
5 Dunia imetiwa unajisi na watu wake;
wameacha kutii sheria,
wamevunja amri
na kuvunja agano la milele.
6 Kwa hiyo laana inaiteketeza dunia,
watu wake lazima waichukue hatia yao.
Kwa hiyo wakazi wa dunia wameteketezwa,
nao waliosalia ni wachache sana.
-
8 “Kwa kuwa mawazo yangu si mawazo yenu,
wala njia zenu si njia zangu,”
asema Bwana.
9 “Kama vile mbingu zilivyo juu kuliko dunia,
ndivyo njia zangu zilivyo juu kuliko njia zenu
na mawazo yangu kuliko mawazo yenu.
10 Kama vile mvua na theluji
ishukavyo kutoka mbinguni,
nayo hairudi tena huko
bila kunywesha dunia
na kuichipusha na kuistawisha,
hivyo hutoa mbegu kwa mpanzi
na mkate kwa mlaji,
11 ndivyo lilivyo neno langu lile litokalo kinywani mwangu:
Halitanirudia tupu,
bali litatimiliza lile nililokusudia
na litafanikiwa katika kusudi lile nililolituma.
12 Mtatoka nje kwa furaha
na kuongozwa kwa amani;
milima na vilima
vitapaza sauti kwa nyimbo mbele yenu,
nayo miti yote ya shambani
itapiga makofi.
13 Badala ya kichaka cha miiba
itaota miti ya misunobari,
na badala ya michongoma
utaota mhadasi.
Hili litakuwa jambo la kumpatia Bwana jina,
kwa ajili ya ishara ya milele,
ambayo haitaharibiwa.”
-
44 Ninyi ni watoto wa baba yenu ibilisi, nanyi mnataka kutimiza matakwa ya baba yenu. Yeye alikuwa muuaji tangu mwanzo, wala hakushikana na kweli maana hamna kweli ndani yake. Asemapo uongo husema yaliyo yake mwenyewe kwa maana yeye ni mwongo na baba wa huo uongo. 45 Lakini kwa sababu nimewaambia kweli hamkuniamini!
-
14 Kwa maana tunajua kwamba sheria ni ya kiroho, lakini mimi ni wa kimwili nikiwa nimeuzwa kwenye utumwa wa dhambi. 15 Sielewi nitendalo, kwa maana lile ninalotaka kulitenda, silitendi, lakini ninatenda lile ninalolichukia. 16 Basi kama ninatenda lile nisilotaka kutenda, ni kwamba ninakubali kuwa sheria ni njema. 17 Lakini, kwa kweli si mimi tena nitendaye lile nisilotaka bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu. 18 Kwa maana ninafahamu kwamba hakuna jema lolote likaalo ndani yangu, yaani, katika asili yangu ya dhambi. Kwa kuwa nina shauku ya kutenda lililo jema, lakini siwezi kulitenda. 19 Sitendi lile jema nitakalo kutenda, bali lile baya nisilolitaka, ndilo nitendalo. 20 Basi kama ninatenda lile nisilotaka kutenda, si mimi tena nifanyaye hivyo, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu.
21 Hivyo naiona sheria ikitenda kazi. Ninapotaka kutenda jema, jambo baya liko papo hapo. 22 Kwa maana katika utu wangu wa ndani naifurahia sheria ya Mungu. 23 Lakini ninaona kuna sheria nyingine inayotenda kazi katika viungo vya mwili wangu inayopigana vita dhidi ya ile sheria ya akili yangu. Sheria hii inanifanya mateka wa ile sheria ya dhambi inayofanya kazi katika viungo vya mwili wangu.
24 Ole wangu mimi maskini! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti?
25 Ashukuriwe Mungu kwa njia ya Yesu Kristo Bwana wetu! Hivyo basi, mimi mwenyewe kwa akili zangu ni mtumwa wa sheria ya Mungu, lakini katika asili ya dhambi ni mtumwa wa sheria ya dhambi.
-
5 Bwana akaona jinsi uovu wa mwanadamu ulivyokuwa mkubwa duniani, na ya kuwa kila mwelekeo wa mawazo ya moyo wake wakati wote ulikuwa mbaya tu. 6 Bwana akasikitika kwamba alimuumba mwanadamu duniani, moyo wa Mungu ukajaa masikitiko.
-
25 Ni nani aliyepasua mifereji kwa ajili ya maji mengi ya mvua yaendayo kasi
na njia ya umeme wa radi,
26 ili kusababisha mvua kunyeshea mahali pasipokaliwa na mtu,
jangwa lisilo na yeyote ndani yake,
27 ili kuitosheleza nchi ya ukiwa na jangwa,
na majani yaanze kumea ndani yake?
28 Je, mvua ina baba?
Ni nani baba azaaye matone ya umande?
29 Barafu inatoka tumbo la nani?
Ni nani azaaye ukungu kutoka mbinguni,
30 wakati maji yawapo magumu kama jiwe,
wakati uso wa vilindi vya maji unapoganda?
-
24 Ee Bwana, jinsi matendo yako yalivyo mengi!
Kwa hekima ulizifanya zote,
dunia imejaa viumbe vyako.
25 Pale kuna bahari, kubwa na yenye nafasi tele,
imejaa viumbe visivyo na idadi,
vitu vyenye uhai vikubwa na vidogo.
-
5 Watasema juu ya utukufu wa fahari ya ukuu wako,
nami nitatafakari juu ya kazi zako za ajabu.
-
6 Sauti husema, “Piga kelele.”
Nami nikasema, “Nipige kelele gani?”
“Wanadamu wote ni kama majani,
nao utukufu wao wote
ni kama maua ya kondeni.
7 Majani hunyauka na maua huanguka,
kwa sababu pumzi ya Bwana huyapuliza.
Hakika wanadamu ni majani.
8 Majani hunyauka na maua huanguka,
lakini neno la Mungu wetu ladumu milele.”
-
13 Atoapo sauti yake, maji yaliyo katika mbingu hunguruma;
huyafanya mawingu yainuke kutoka miisho ya dunia.
Hupeleka umeme wa radi pamoja na mvua,
naye huuleta upepo kutoka ghala zake.
-
22 Siku moja Yesu alipanda ndani ya mashua pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, “Tuvukeni twende mpaka ngʼambo ya ziwa.” Nao wakaondoka. 23 Hivyo walipokuwa wakienda, akalala usingizi. Dhoruba kali ikatokea mle ziwani, hata mashua ikawa inajaa maji, nao walikuwa katika hatari kubwa.
24 Wanafunzi wake wakamwendea na kumwamsha, wakisema, “Bwana, Bwana, tunaangamia!”
Yeye akaamka, akaukemea ule upepo na yale mawimbi; dhoruba ikakoma, nako kukawa shwari. 25 Akawauliza wanafunzi wake, “Imani yenu iko wapi?”
Kwa woga na mshangao wakaulizana, “Huyu ni nani, ambaye anaamuru hata upepo na maji, navyo vikamtii?”
-
6 Mwili huzaa mwili, lakini Roho huzaa roho.
Shows Read in context, Share and Copy.