37 Bible Verses About God's Beautiful Creation
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
-
1 Hapo mwanzo Mungu aliumba mbingu na dunia. 2 Wakati huu dunia ilikuwa haina umbo, tena ilikuwa tupu. Giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji, naye Roho wa Mungu alikuwa ametulia juu ya maji.
3 Mungu akasema, “Iwepo nuru,” nayo nuru ikawepo. 4 Mungu akaona ya kuwa nuru ni njema, ndipo Mungu akatenganisha nuru na giza. 5 Mungu akaiita nuru “mchana,” na giza akaliita “usiku.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya kwanza.
6 Mungu akasema, “Iwepo nafasi kati ya maji igawe maji na maji.” 7 Kwa hiyo Mungu akafanya nafasi, akatenganisha maji yaliyo chini ya hiyo nafasi na maji yaliyo juu yake. Ikawa hivyo. 8 Mungu akaiita hiyo nafasi “anga.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya pili.
9 Mungu akasema, “Maji yaliyopo chini ya anga na yakusanyike mahali pamoja, pawepo na nchi kavu.” Ikawa hivyo. 10 Mungu akaiita nchi kavu “ardhi,” nalo lile kusanyiko la maji akaliita “bahari.” Mungu akaona kuwa ni vyema.
11 Kisha Mungu akasema, “Ardhi na itoe mimea: miche itoayo mbegu, miti juu ya nchi itoayo matunda yenye mbegu ndani yake, kila mmea kulingana na aina zake mbalimbali.” Ikawa hivyo. 12 Ardhi ikachipua mimea: Mimea itoayo mbegu kulingana na aina zake, na miti itoayo matunda yenye mbegu kulingana na aina zake. Mungu akaona ya kuwa hili ni jema. 13 Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya tatu.
14 Mungu akasema, “Iwepo mianga kwenye nafasi ya anga ili itenganishe usiku na mchana, nayo iwe alama ya kutambulisha majira mbalimbali, siku na miaka, 15 nayo iwe mianga kwenye nafasi ya anga ya kutia nuru juu ya dunia.” Ikawa hivyo. 16 Mungu akafanya mianga miwili mikubwa: mwanga mkubwa utawale mchana, na mwanga mdogo utawale usiku. Pia Mungu akafanya nyota. 17 Mungu akaiweka katika nafasi ya anga iangaze dunia, 18 itawale usiku na mchana, na ikatenganishe nuru na giza. Mungu akaona kuwa hili ni jema. 19 Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya nne.
20 Mungu akasema, “Kuwepo na viumbe hai tele kwenye maji, nao ndege waruke juu ya dunia katika nafasi ya anga.” 21 Kwa hiyo Mungu akaumba viumbe wakubwa wa baharini na kila kiumbe hai kiendacho majini kulingana na aina zake, na kila ndege mwenye mabawa kulingana na aina yake. Mungu akaona kuwa hili ni jema. 22 Mungu akavibariki, akasema, “Zaeni mwongezeke, mkayajaze maji ya bahari, nao ndege waongezeke katika dunia.” 23 Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya tano.
24 Mungu akasema, “Ardhi na itoe viumbe hai kulingana na aina zake: wanyama wa kufugwa, viumbe vitambaavyo ardhini na wanyama pori, kila mnyama kulingana na aina yake.” Ikawa hivyo. 25 Mungu akafanya wanyama pori kulingana na aina zake, wanyama wa kufugwa kulingana na aina zake, na viumbe vyote vitambaavyo juu ya ardhi kulingana na aina zake. Mungu akaona kuwa hili ni jema.
26 Ndipo Mungu akasema, “Tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu, wakatawale juu ya samaki wa baharini na ndege wa angani, juu ya mifugo, juu ya dunia yote, na juu ya viumbe wote watambaao juu ya nchi.”
27 Kwa hiyo Mungu akamuumba mtu kwa mfano wake mwenyewe,
kwa mfano wa Mungu alimuumba;
mwanaume na mwanamke aliwaumba.
28 Mungu akawabariki na akawaambia, “Zaeni na mkaongezeke, mkaijaze tena dunia na kuitiisha. Mkatawale samaki wa baharini, ndege wa angani, na kila kiumbe hai kiendacho juu ya ardhi.”
29 Kisha Mungu akasema, “Nimewapa kila mche utoao mbegu juu ya uso wa dunia yote, na kila mti wenye matunda yenye mbegu ndani yake. Vitakuwa chakula chenu. 30 Nao wanyama wote wa dunia, ndege wote wa angani, na viumbe vyote viendavyo juu ya ardhi: yaani kila kiumbe chenye pumzi ya uhai, ninawapa kila mche wa kijani kuwa chakula.” Ikawa hivyo.
31 Mungu akaona vyote alivyoumba, na tazama, ilikuwa vizuri sana. Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya sita.
-
Kwa mwimbishaji. Mtindo wa gitithi. Zaburi ya Daudi.
1 Ee Bwana, Bwana wetu,
tazama jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote!
Umeuweka utukufu wako
juu ya mbingu.
2 Midomoni mwa watoto wachanga na wanyonyao
umeamuru sifa,
kwa sababu ya watesi wako,
kumnyamazisha adui na mlipiza kisasi.
3 Nikiziangalia mbingu zako,
kazi ya vidole vyako,
mwezi na nyota,
ulizoziratibisha,
4 mwanadamu ni kitu gani hata unamfikiria,
binadamu ni nani hata unamjali?
5 Umemfanya chini kidogo kuliko viumbe wa mbinguni,
ukamvika taji ya utukufu na heshima.
6 Umemfanya mtawala juu ya kazi za mikono yako;
umeweka vitu vyote chini ya miguu yake.
7 Mifugo na makundi yote pia,
naam, na wanyama wa kondeni,
8 ndege wa angani na samaki wa baharini,
naam, kila kiogeleacho katika njia za bahari.
9 Ee Bwana, Bwana wetu,
tazama jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote!
-
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.
1 Mbingu zinatangaza utukufu wa Mungu,
anga zahubiri kazi ya mikono yake.
2 Siku baada ya siku zinatoa habari,
usiku baada ya usiku zinatangaza maarifa.
3 Hakuna msemo wala lugha,
ambapo sauti zao hazisikiki.
4 Sauti yao imeenea duniani pote,
nayo maneno yao yameenea
hadi miisho ya ulimwengu.
Katika mbingu amepiga hema kwa ajili ya jua,
5 linafanana na bwana arusi
akitoka chumbani mwake,
kama shujaa afurahiavyo
kukamilisha kushindana kwake.
6 Huchomoza upande mmoja wa mbingu,
na kufanya mzunguko wake
hadi upande mwingine.
Hakuna kilichojificha joto lake.
-
18 Ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni dhidi ya uasi wote na uovu wa wanadamu ambao huipinga kweli kwa uovu wao, 19 kwa maana yote yanayoweza kujulikana kumhusu Mungu ni dhahiri kwao, kwa sababu Mungu mwenyewe ameyadhihirisha kwao. 20 Kwa maana tangu kuumbwa kwa ulimwengu, asili ya Mungu asiyeonekana kwa macho, yaani, uweza wake wa milele na asili yake ya Uungu, imeonekana waziwazi, ikitambuliwa kutokana na yale aliyoyafanya ili wanadamu wasiwe na udhuru.
21 Kwa maana ingawa walimjua Mungu, hawakumtukuza yeye kama ndiye Mungu wala hawakumshukuru, bali fikira zao zimekuwa batili na mioyo yao ya ujinga ikatiwa giza. 22 Ingawa walijidai kuwa wenye hekima, wakawa wajinga 23 na kubadili utukufu wa Mungu aishiye milele kwa sanamu zilizofanywa zifanane na mwanadamu ambaye hufa, na mfano wa ndege, wanyama na viumbe vitambaavyo.
-
Zaburi ya Daudi.
1 Dunia ni mali ya Bwana, na vyote vilivyomo ndani yake,
ulimwengu, na wote waishio ndani yake,
2 maana aliiwekea misingi yake baharini
na kuifanya imara juu ya maji.
-
1 Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.
Ee Bwana Mungu wangu, wewe ni mkuu sana,
umejivika utukufu na enzi.
2 Amejifunika katika nuru kama vile kwa vazi,
amezitandaza mbingu kama hema
3 na kuziweka nguzo za orofa yake juu ya maji.
Huyafanya mawingu kuwa gari lake,
na hupanda kwenye mbawa za upepo.
4 Huzifanya pepo kuwa wajumbe wake,
miali ya moto watumishi wake.
5 Ameiweka dunia kwenye misingi yake,
haiwezi kamwe kuondoshwa.
6 Uliifunika kwa kilindi kama kwa vazi,
maji yalisimama juu ya milima.
7 Lakini kwa kukemea kwako maji yalikimbia,
kwa sauti ya radi yako yakatoroka,
8 yakapanda milima, yakateremka mabondeni,
hadi mahali pale ulipoyakusudia.
9 Uliyawekea mpaka ambao hayawezi kuuvuka,
kamwe hayataifunika dunia tena.
10 Huzifanya chemchemi zimwage maji mabondeni,
hutiririka kati ya milima.
11 Huwapa maji wanyama wote wa kondeni,
punda-mwitu huzima kiu yao.
12 Ndege wa angani hufanya viota kando ya maji,
huimba katikati ya matawi.
13 Huinyeshea milima kutoka orofa zake,
dunia inatoshelezwa kwa matunda ya kazi yake.
14 Huyafanya majani ya mifugo yaote,
na mimea kwa watu kulima,
wajipatie chakula kutoka ardhini:
15 divai ya kuufurahisha moyo wa mwanadamu,
mafuta kwa ajili ya kungʼarisha uso wake,
na mkate wa kutia mwili nguvu.
16 Miti ya Bwana inanyeshewa vizuri,
mierezi ya Lebanoni aliyoipanda.
17 Humo ndege hufanya viota vyao,
korongo ana nyumba yake kwenye msunobari.
18 Milima mirefu ni makao ya mbuzi-mwitu,
majabali ni kimbilio la pelele.
19 Mwezi hugawanya majira,
na jua hutambua wakati wake wa kutua.
20 Unaleta giza, kunakuwa usiku,
wanyama wote wa mwituni huzurura.
21 Simba hunguruma kwa mawindo yao,
na kutafuta chakula chao kutoka kwa Mungu.
22 Jua huchomoza, nao huondoka,
hurudi na kulala katika mapango yao.
23 Kisha mwanadamu huenda kazini mwake,
katika kazi yake mpaka jioni.
24 Ee Bwana, jinsi matendo yako yalivyo mengi!
Kwa hekima ulizifanya zote,
dunia imejaa viumbe vyako.
25 Pale kuna bahari, kubwa na yenye nafasi tele,
imejaa viumbe visivyo na idadi,
vitu vyenye uhai vikubwa na vidogo.
26 Huko meli huenda na kurudi,
pia Lewiathani, uliyemuumba acheze ndani yake.
27 Hawa wote wanakutazamia wewe,
uwape chakula chao kwa wakati wake.
28 Wakati unapowapa,
wanakikusanya,
unapofumbua mkono wako,
wao wanashibishwa mema.
29 Unapoficha uso wako,
wanapata hofu,
unapoondoa pumzi yao,
wanakufa na kurudi mavumbini.
30 Unapopeleka Roho wako,
wanaumbwa,
nawe huufanya upya uso wa dunia.
31 Utukufu wa Bwana na udumu milele,
Bwana na azifurahie kazi zake:
32 yeye aitazamaye dunia, nayo ikatetemeka,
aigusaye milima, nayo ikatoa moshi.
33 Nitamwimbia Bwana maisha yangu yote;
nitaimba sifa kwa Mungu wangu muda wote ninaoishi.
34 Kutafakari kwangu na kumpendeze yeye,
ninapofurahi katika Bwana.
35 Lakini wenye dhambi na watoweke katika dunia
na waovu wasiwepo tena.
Ee nafsi yangu, msifu Bwana.
Msifuni Bwana.
-
24 “Mungu aliyeumba dunia na vyote vilivyomo ndani yake, yeye ndiye Bwana wa mbingu na nchi, hakai katika mahekalu yaliyojengwa kwa mikono ya wanadamu. 25 Wala hatumikiwi na mikono ya wanadamu kana kwamba anahitaji chochote, kwa sababu yeye mwenyewe ndiye awapaye watu wote uhai na pumzi na vitu vyote. 26 Kutoka kwa mtu mmoja, yeye aliumba mataifa yote ya wanadamu ili waikalie dunia yote, naye akaweka nyakati za kuishi. 27 Mungu alifanya hivyo ili wanadamu wamtafute na huenda wakamfikia ingawa kwa kupapasapapasa ijapokuwa kwa kweli hakai mbali na kila mmoja wetu. 28 ‘Kwa kuwa katika yeye tunaishi, tunatembea na kuwa na uzima wetu.’ Kama baadhi ya watunga mashairi wenu walivyosema, ‘Sisi ni watoto wake.’
29 “Kwa kuwa sisi ni watoto wa Mungu, haitupasi kudhani kuwa uungu ni kama sanamu ya dhahabu au ya fedha au ya jiwe, mfano uliotengenezwa kwa ubunifu na ustadi wa mwanadamu.
-
7 “Lakini ulizeni wanyama, nao watawafundisha,
au ndege wa angani, nao watawaambia;
8 au zungumzeni na dunia, nayo itawafundisha,
au acheni samaki wa baharini wawape taarifa.
9 Ni nani miongoni mwa hawa wote asiyejua
kwamba mkono wa Bwana ndio uliofanya hili?
10 Mkononi mwake kuna uhai wa kila kiumbe,
na pumzi ya wanadamu wote.
-
1 Hapo mwanzo alikuwako Neno, huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. 2 Tangu mwanzo huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu.
3 Vitu vyote viliumbwa kwa yeye, wala pasipo yeye hakuna chochote kilichoumbwa ambacho kimeumbwa.
-
4 Haya ndiyo maelezo ya mbingu na dunia wakati zilipoumbwa.
Bwana Mungu alipoziumba mbingu na dunia, 5 hapakuwepo na mche wa shambani uliokuwa umejitokeza ardhini, wala hapakuwepo na mmea wa shamba uliokuwa umeota, kwa kuwa Bwana Mungu alikuwa hajanyeshea mvua juu ya nchi, na hapakuwepo mtu wa kuilima ardhi, 6 lakini umande ulitokeza kutoka ardhini na kunyesha uso wote wa nchi: 7 Bwana Mungu alimuumba mtu kutoka mavumbi ya ardhi, akampulizia pumzi ya uhai puani mwake, naye mtu akawa kiumbe hai.
8 Basi Bwana Mungu alikuwa ameotesha bustani upande wa mashariki, katika Edeni, huko akamweka huyo mtu aliyemuumba. 9 Bwana Mungu akafanya aina zote za miti ziote kutoka ardhini, miti yenye kupendeza macho na mizuri kwa chakula. Katikati ya bustani ulikuwepo mti wa uzima na mti wa kujua mema na mabaya.
-
12 Mimi ndiye niliyeumba dunia
na kumuumba mwanadamu juu yake.
Mikono yangu mwenyewe ndiyo iliyozitanda mbingu,
nikayapanga majeshi yake yote ya angani.
-
11 “Bwana wetu na Mungu wetu,
wewe unastahili kupokea utukufu
na heshima na uweza,
kwa maana ndiwe uliyeviumba vitu vyote,
na kwa mapenzi yako viliumbwa
na vimekuwako.”
-
5 Bwana hupenda uadilifu na haki;
dunia imejaa upendo wake usiokoma.
6 Kwa neno la Bwana mbingu ziliumbwa,
jeshi lao la angani kwa pumzi ya kinywa chake.
7 Ameyakusanya maji ya bahari
kama kwenye chungu;
vilindi vya bahari
ameviweka katika ghala.
8 Dunia yote na imwogope Bwana,
watu wote wa dunia wamche.
9 Kwa maana Mungu alisema, na ikawa,
aliamuru na ikasimama imara.
-
3 Kwa kuwa Bwana ni Mungu mkuu,
mfalme mkuu juu ya miungu yote.
4 Mkononi mwake mna vilindi vya dunia,
na vilele vya milima ni mali yake.
5 Bahari ni yake, kwani ndiye aliifanya,
na mikono yake iliumba nchi kavu.
-
13 Kwa maana wewe ndiwe uliyeumba utu wangu wa ndani;
uliniunga pamoja tumboni mwa mama yangu.
14 Ninakusifu kwa sababu nimeumbwa
kwa namna ya ajabu na ya kutisha;
kazi zako ni za ajabu,
ninajua hayo kikamilifu.
15 Umbile langu halikufichika kwako,
nilipoumbwa mahali pa siri.
Nilipoungwa pamoja kwa ustadi katika vilindi vya nchi,
16 macho yako yaliniona kabla mwili wangu haujakamilika.
Siku zangu zote ulizonipangia
ziliandikwa katika kitabu chako
kabla haijakuwepo hata moja.
-
19 Kwa maana viumbe vyote vinangoja kwa shauku kudhihirishwa kwa watoto wa Mungu. 20 Kwa kuwa viumbe vyote viliwekwa chini ya ubatili, si kwa chaguo lao, bali kwa mapenzi yake yeye aliyevitiisha katika tumaini, 21 ili kwamba viumbe vyote vipate kuwekwa huru kutoka kwa utumwa wa kuharibika na kupewa uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu.
22 Kwa maana twajua ya kuwa hata sasa viumbe vyote vimekuwa vikilia kwa maumivu kama utungu wa mwanamke wakati wa kuzaa.
-
10 Kwa maana sisi ni kazi ya mikono ya Mungu, tulioumbwa katika Kristo Yesu, ili tupate kutenda matendo mema, ambayo Mungu alitangulia kuyaandaa tupate kuishi katika hayo.
-
Zaburi ya Asafu.
1 Mwenye Nguvu, Mungu, Bwana,
asema na kuiita dunia,
tangu mawio ya jua
hadi mahali pake liendapo kutua.
2 Kutoka Sayuni, penye uzuri mkamilifu,
Mungu anaangaza.
3 Mungu wetu anakuja na hatakaa kimya,
moto uteketezao unamtangulia,
akiwa amezungukwa na tufani kali.
4 Anaziita mbingu zilizo juu,
na nchi, ili aweze kuwahukumu watu wake:
5 “Nikusanyieni watu wangu waliowekwa wakfu,
waliofanya agano nami kwa dhabihu.”
6 Nazo mbingu zinatangaza haki yake,
kwa maana Mungu mwenyewe ni hakimu.
-
1 Msifuni Bwana.
Msifuni Bwana kutoka mbinguni,
msifuni juu vileleni.
2 Msifuni, enyi malaika wake wote,
msifuni yeye, enyi jeshi lake lote la mbinguni.
3 Msifuni yeye, enyi jua na mwezi,
msifuni yeye, enyi nyota zote zingʼaazo.
4 Msifuni yeye, enyi mbingu zilizo juu sana,
na ninyi maji juu ya anga.
5 Vilisifu jina la Bwana
kwa maana aliamuru navyo vikaumbwa.
6 Aliviweka mahali pake milele na milele,
alitoa amri ambayo haibadiliki milele.
7 Mtukuzeni Bwana kutoka duniani,
ninyi viumbe vikubwa vya baharini na vilindi vyote vya bahari,
8 umeme wa radi na mvua ya mawe, theluji na mawingu,
pepo za dhoruba zinazofanya amri zake,
9 ninyi milima na vilima vyote,
miti ya matunda na mierezi yote,
10 wanyama wa mwituni na mifugo yote,
viumbe vidogo na ndege warukao,
11 wafalme wa dunia na mataifa yote,
ninyi wakuu na watawala wote wa dunia,
12 wanaume vijana na wanawali,
wazee na watoto.
13 Wote na walisifu jina la Bwana,
kwa maana jina lake pekee limetukuka,
utukufu wake uko juu ya nchi na mbingu.
14 Amewainulia watu wake pembe,
sifa ya watakatifu wake wote,
ya Israeli, watu walio karibu na moyo wake.
Msifuni Bwana.
-
11 Amefanya kila kitu kiwe kizuri kwa wakati wake. Pia ameiweka hiyo milele katika mioyo ya wanadamu, wala hawawezi kutambua kwa kina yale ambayo Mungu amefanya tangu mwanzo hadi mwisho.
-
5 Kwa uwezo wangu mkuu na kwa mkono wangu ulionyooshwa nimeumba dunia na watu wake na wanyama walioko ndani yake, nami humpa yeyote inipendezavyo.
-
28 “Nanyi kwa nini mnajitaabisha kwa ajili ya mavazi? Fikirini maua ya shambani yameavyo. Hayafanyi kazi wala hayafumi. 29 Lakini nawaambia, hata Solomoni katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo ya hayo maua. 30 Basi ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya shambani, ambayo leo yapo na kesho yanatupwa motoni, je, hatawavika ninyi vizuri zaidi, enyi wa imani haba? 31 Kwa hiyo msiwe na wasiwasi, mkisema, ‘Tutakula nini?’ au ‘Tutakunywa nini?’ au ‘Tutavaa nini?’ 32 Watu wasiomjua Mungu ndio wanaoshindania hayo, lakini Baba yenu wa mbinguni anafahamu kuwa mnahitaji haya yote.
-
29 Je, shomoro wawili hawauzwi kwa senti moja tu? Lakini hakuna hata mmoja wao atakayeanguka chini pasipo Baba yenu kujua. 30 Hata nywele za vichwa vyenu zote zimehesabiwa. 31 Hivyo msiogope; kwa maana ninyi ni wa thamani kubwa kuliko shomoro wengi.
-
7 Hutandaza anga la kaskazini mahali patupu;
naye huiningʼiniza dunia mahali pasipo na kitu.
8 Huyafungia maji kwenye mawingu yake,
hata hivyo mawingu hayapasuki kwa uzito wake.
9 Huufunika uso wa mwezi mpevu,
akitandaza mawingu juu yake.
10 Amechora mstari wa upeo juu ya uso wa maji,
ameweka mpaka wa nuru na giza.
11 Nguzo za mbingu nazo zatetemeka,
zinatishika anapozikemea.
12 Kwa nguvu zake aliisukasuka bahari;
kwa hekima yake alimkata Rahabu vipande vipande.
13 Aliisafisha anga kwa pumzi yake;
kwa mkono wake alimchoma joka aendaye mbio.
14 Haya ni mambo madogo tu katika matendo yake;
tazama jinsi ulivyo mdogo mnongʼono tunaousikia kumhusu!
Ni nani basi awezaye kuelewa
ngurumo za nguvu zake?”
-
11 Huyasheheneza mawingu kwa maji,
naye husambaza umeme wake wa radi kupitia hayo.
12 Nayo mawingu huzungukazunguka pande zote kwa amri yake,
juu ya uso wa dunia yote,
kufanya lolote ayaamuruyo.
13 Huleta mawingu ili kuadhibu wanadamu,
au kuinyeshea dunia yake na kuonyesha upendo wake.
14 “Ayubu, sikiliza hili;
nyamaza na uyafikiri maajabu ya Mungu.
15 Je, unajua jinsi Mungu anavyoyaongoza mawingu,
na kufanya umeme wake wa radi utoe mwanga?
16 Je, wajua jinsi mawingu yanavyokaa yakiwa yametulia,
hayo maajabu yake yeye aliye mkamilifu katika maarifa?
-
11 Mbingu ni zako, nayo nchi pia ni yako,
uliuwekea ulimwengu msingi
pamoja na vyote vilivyomo.
-
15 Bwana Mungu akamchukua huyo mtu, akamweka kwenye Bustani ya Edeni ailime na kuitunza.
-
11 Mbingu na zishangilie, nchi na ifurahi;
bahari na ivume, na vyote vilivyomo ndani yake;
12 mashamba na yashangilie,
pamoja na vyote vilivyomo ndani yake.
Kisha miti yote ya msituni itaimba kwa furaha;
13 itaimba mbele za Bwana kwa maana anakuja,
anakuja kuihukumu dunia.
Ataihukumu dunia kwa haki,
na mataifa katika kweli yake.
-
13 Atoapo sauti yake, maji yaliyo katika mbingu hunguruma;
huyafanya mawingu yainuke kutoka miisho ya dunia.
Hupeleka umeme wa radi pamoja na mvua,
naye huuleta upepo kutoka ghala zake.
-
8 (yeye ambaye alifanya Kilimia na Orioni,
ambaye hugeuza giza kuwa mapambazuko
na mchana kuwa usiku,
ambaye huyaita maji ya bahari
na kuyamwaga juu ya uso wa nchi:
Bwana ndilo jina lake;
9 yeye hufanya maangamizo kwenye ngome
na kufanya mji uliozungushiwa ngome kuwa ukiwa),
-
27 “Angalieni maua jinsi yameavyo: Hayafanyi kazi wala hayafumi. Lakini nawaambia, hata Solomoni katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo ya hayo maua.
-
6 Wewe peke yako ndiwe Bwana. Uliziumba mbingu, hata mbingu za mbingu na jeshi lote la mbinguni, dunia na vyote vilivyo ndani yake, na pia bahari na vyote vilivyomo ndani yake. Huvipa vitu vyote uhai, nalo jeshi la mbinguni linakuabudu wewe.
-
1 Tazama, Bwana ataifanya dunia kuwa ukiwa
na kuiharibu,
naye atauharibu uso wake
na kutawanya wakaao ndani yake:
2 ndivyo itakavyokuwa
kwa makuhani na kwa watu,
kwa bwana na kwa mtumishi,
kwa bibi na kwa mtumishi wake wa kike,
kwa muuzaji na kwa mnunuzi,
kwa mkopaji na kwa mkopeshaji,
kwa mdaiwa na kwa mdai.
3 Dunia itaharibiwa kabisa
na kutekwa nyara kabisa.
Bwana amesema neno hili.
4 Dunia inakauka na kunyauka,
dunia inanyongʼonyea na kunyauka,
waliotukuzwa wa dunia wananyongʼonyea.
5 Dunia imetiwa unajisi na watu wake;
wameacha kutii sheria,
wamevunja amri
na kuvunja agano la milele.
6 Kwa hiyo laana inaiteketeza dunia,
watu wake lazima waichukue hatia yao.
Kwa hiyo wakazi wa dunia wameteketezwa,
nao waliosalia ni wachache sana.
-
28 Je wewe, hufahamu?
Je wewe, hujasikia?
Bwana ni Mungu wa milele,
Muumba wa miisho ya dunia.
Hatachoka wala kulegea,
wala hakuna hata mmoja
awezaye kuupima ufahamu wake.
-
17 “Tazama, nitaumba
mbingu mpya na dunia mpya.
Mambo ya zamani hayatakumbukwa,
wala hayatakuja akilini.
18 Lakini furahini na kushangilia daima
katika hivi nitakavyoumba,
kwa kuwa nitaumba Yerusalemu uwe wa kupendeza,
nao watu wake wawe furaha.
-
6 Ndipo Bwana, Mungu akaweka tayari mzabibu na kuufanya uote, kumpa Yona kivuli kilichomfunika kichwa ili kuondoa taabu yake, naye Yona akafurahi sana kwa ajili ya ule mzabibu. 7 Lakini kesho yake asubuhi na mapema Mungu akaamuru buu, autafune mzabibu huo nao ukanyauka. 8 Wakati jua lilipochomoza, Mungu akautuma upepo wa hari wa mashariki, nalo jua likawaka juu ya kichwa cha Yona mpaka akazimia. Akatamani kufa, naye akasema, “Ni afadhali mimi nife kuliko kuishi.”
9 Lakini Mungu alimwambia Yona, “Je, unayo haki kukasirika kuhusu mzabibu huo?”
Akasema, “Ndiyo, ninayo haki. Nimekasirika kiasi cha kufa.”
10 Lakini Bwana akamwambia, “Wewe unakasirika kwa ajili ya mzabibu huu, nawe hukuusababisha kuota wala kuutunza. Uliota usiku mmoja, nao ukafa usiku mmoja. 11 Lakini Ninawi ina zaidi ya watu 120,000 ambao hawawezi kupambanua kulia au kushoto, pamoja na ngʼombe wengi. Je, hainipasi kufikiri juu ya mji ule mkubwa?”
-
6 Mnajua kwamba shomoro watano huuzwa kwa senti mbili? Lakini Mungu hamsahau hata mmoja wao.
Shows Read in context, Share and Copy.