78 Bible Verses About Being Happy

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Being Happy
  1. 4 Furahini katika Bwana siku zote, tena nasema furahini! 5 Upole wenu na ujulikane na watu wote. Bwana yu karibu. 6 Msijisumbue kwa jambo lolote, bali katika kila jambo kwa kuomba na kusihi pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. 7 Nayo amani ya Mungu, inayopita fahamu zote, itailinda mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.

    8 Hatimaye, ndugu zangu, mambo yote yaliyo ya kweli, yoyote yaliyo na sifa njema, yoyote yaliyo ya haki, yoyote yaliyo safi, yoyote ya kupendeza, yoyote yenye staha, ukiwepo uzuri wowote, pakiwepo chochote kinachostahili kusifiwa, tafakarini mambo hayo. 9 Mambo yote mliyojifunza au kuyapokea au kuyasikia kutoka kwangu, au kuyaona kwangu, yatendeni hayo. Naye Mungu wa amani atakuwa pamoja nanyi.

    10 Nina furaha kubwa katika Bwana kwamba hatimaye mmeanza upya kushughulika tena na maisha yangu. Kweli mmekuwa mkinifikiria lakini mlikuwa hamjapata nafasi ya kufanya hivyo. 11 Sisemi hivyo kwa vile nina mahitaji, la! Kwa maana nimejifunza kuridhika katika hali yoyote. 12 Ninajua kupungukiwa, pia ninajua kuwa na vingi. Nimejifunza siri ya kuridhika katika kila hali, wakati wa kushiba na wakati wa kuona njaa, wakati wa kuwa na vingi na wakati wa kupungukiwa. 13 Naweza kuyafanya mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.

  2. 7 Nitamsifu Bwana ambaye hunishauri,

    hata wakati wa usiku moyo wangu hunifundisha.

    8 Nimemweka Bwana mbele yangu daima.

    Kwa sababu yuko mkono wangu wa kuume,

    sitatikisika.

    9 Kwa hiyo moyo wangu unafurahia, na ulimi wangu unashangilia;

    mwili wangu nao utapumzika salama,

    10 kwa maana hutaniacha kaburini,

    wala hutamwacha Mtakatifu Wako kuona uharibifu.

    11 Umenijulisha njia ya uzima;

    utanijaza na furaha mbele zako,

    pamoja na furaha za milele

    katika mkono wako wa kuume.

  3. 13 Mungu wa tumaini awajaze ninyi furaha yote na amani katika kumwamini, ili mpate kujawa na tumaini tele kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.

  4. 20 Yeyote anayekubali mafundisho hustawi,

    tena amebarikiwa yeye anayemtumaini Bwana.

  5. 12 Wapenzi, msione ajabu kwa yale mateso yanayotukia miongoni mwenu, kana kwamba ni kitu kigeni kinachowapata. 13 Bali furahini kuwa mnashiriki katika mateso ya Kristo, ili mpate kufurahi zaidi wakati utukufu wake utakapofunuliwa. 14 Kama mkitukanwa kwa ajili ya jina la Kristo, mmebarikiwa, kwa sababu Roho wa utukufu na wa Mungu anakaa juu yenu.

  6. 1 Kwa sababu hii, kwa kuwa tumezungukwa na wingu kubwa namna hii la mashahidi, basi na tuweke kando kila kitu kinachotuzuia na ile dhambi inayotuzinga kwa urahisi, nasi tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa kwa ajili yetu. 2 Basi na tumtazame sana Yesu mwanzilishi na mkamilishaji wa imani yetu, yeye ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake alistahimili msalaba, bila kujali aibu ya huo msalaba, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu. 3 Mtafakarini sana yeye aliyestahimili upinzani mkuu namna hii kutoka kwa watu wenye dhambi, ili kwamba msije mkachoka na kukata tamaa.

  7. 3 Mtumaini Bwana na utende yaliyo mema;

    Kaa katika nchi ukafurahie malisho salama.

    4 Jifurahishe katika Bwana

    naye atakupa haja za moyo wako.

  8. 16 Kisha akawaambia mfano huu: “Shamba la mtu mmoja tajiri lilizaa sana. 17 Akawaza moyoni mwake, ‘Nifanye nini? Sina mahali pa kuhifadhi mavuno yangu.’

    18 “Ndipo huyo tajiri akasema, ‘Nitafanya hivi: Nitabomoa ghala zangu za nafaka na kujenga nyingine kubwa zaidi na huko nitayahifadhi mavuno yangu yote na vitu vyangu. 19 Nami nitaiambia nafsi yangu, “Nafsi, unavyo vitu vingi vizuri ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi. Pumzika; kula, unywe, ufurahi.” ’

    20 “Lakini Mungu akamwambia, ‘Mpumbavu wewe! Usiku huu uhai wako unatakiwa. Sasa hivyo vitu ulivyojiwekea akiba vitakuwa vya nani?’

  9. 10 Mkizishika amri zangu mtakaa katika pendo langu, kama mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake. 11 Nimewaambia mambo haya ili furaha yangu iwe ndani yenu na furaha yenu iwe kamili. 12 Amri yangu ndiyo hii: Mpendane kama mimi nilivyowapenda ninyi.

  10. 13 Heri mtu yule aonaye hekima,

    mtu yule apataye ufahamu,

    14 kwa maana hekima ana faida kuliko fedha

    na mapato yake ni bora kuliko ya dhahabu safi.

    15 Hekima ana thamani kuliko marijani;

    hakuna chochote unachokitamani

    kinachoweza kulinganishwa naye.

    16 Maisha marefu yako katika mkono wake wa kuume;

    katika mkono wake wa kushoto

    kuna utajiri na heshima.

    17 Njia zake zinapendeza,

    mapito yake yote ni amani.

    18 Yeye ni mti wa uzima kwa wale wanaomkumbatia;

    wale wamshikao watabarikiwa.

  11. 20 Amin, amin nawaambia, ninyi mtalia na kuomboleza, lakini ulimwengu utafurahi. Ninyi mtahuzunika, lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha. 21 Mwanamke anapokuwa na utungu wa kuzaa huwa na maumivu kwa sababu saa yake imewadia. Lakini mtoto akiisha kuzaliwa, yule mwanamke husahau maumivu hayo kwa sababu ya furaha ya kuzaliwa mtoto ulimwenguni. 22 Hivyo ninyi mna maumivu sasa, lakini nitawaona tena, nayo mioyo yenu itafurahi na furaha yenu hakuna awaondoleaye.

  12. 2 Ndugu zangu, hesabuni kuwa ni furaha tupu mnapopatwa na majaribu mbalimbali, 3 kwa sababu mnajua ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi. 4 Saburi na iwe na kazi timilifu, ili mpate kuwa wakamilifu, mmekamilishwa, bila kupungukiwa na kitu chochote. 5 Kama mtu yeyote miongoni mwenu amepungukiwa na hekima na amwombe Mungu, yeye awapaye watu wote kwa ukarimu wala hana kinyongo, naye atapewa.

  13. 22 Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, 23 upole na kiasi. Katika mambo kama haya hakuna sheria.

  14. 17 Mrudi mwanao, naye atakupa amani,

    atakufurahisha nafsi yako.

  15. Wimbo wa kwenda juu.

    1 Heri ni wale wote wamchao Bwana,

    waendao katika njia zake.

    2 Utakula matunda ya kazi yako;

    baraka na mafanikio vitakuwa vyako.

  16. 10 Nehemia akasema, “Nendeni mkafurahie chakula kizuri na vinywaji vitamu, na mpeleke sehemu kwa wale ambao hawana chochote cha kula. Siku hii ni takatifu kwa Bwana. Msihuzunike, kwa kuwa furaha ya Bwana ni nguvu zenu.”

  17. 22 Msikilize baba yako, aliyekuzaa,

    wala usimdharau mama yako atakapokuwa mzee.

    23 Nunua kweli wala usiiuze,

    pata hekima, adabu na ufahamu.

    24 Baba wa mwenye haki ana furaha kubwa,

    naye aliye na mwana mwenye hekima humfurahia.

    25 Baba yako na mama yako na wafurahi,

    mama aliyekuzaa na ashangilie!

  18. 12 Ninajua kwamba hakuna kitu bora kwa wanadamu kuliko kuwa na furaha na kutenda mema wakati wanapoishi. 13 Tena ni karama ya Mungu kila mtu apate kula na kunywa na kujiburudisha kwa mema katika kazi yake yote.

  19. 7 Nenda, kula chakula chako kwa furaha, unywe divai yako kwa moyo wa shangwe, kwa maana sasa Mungu anakubali unachofanya. 8 Daima uvae nguo nyeupe na daima upake kichwa chako mafuta. 9 Furahia maisha na mke wako, umpendaye, siku zote za maisha ya ubatili uliyopewa na Mungu chini ya jua, siku zote za ubatili. Kwa maana hili ndilo fungu lako katika maisha na katika kazi yako ya taabu chini ya jua. 10 Lolote mkono wako upatalo kufanya, fanya kwa nguvu zako zote, kwa kuwa huko kuzimu, unakokwenda, hakuna kufanya kazi wala mipango wala maarifa wala hekima.

  20. 1 Kwa hiyo, kwa kuwa tumekwisha kuhesabiwa haki kwa imani, tuna amani na Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, 2 ambaye kwa kupitia kwake tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo ndani yake sasa tunasimama, nasi twafurahia katika tumaini letu la kushiriki utukufu wa Mungu. 3 Si hivyo tu, bali twafurahi pia katika mateso, kwa sababu tunajua kuwa mateso huleta saburi, 4 nayo saburi huleta uthabiti wa moyo, na uthabiti wa moyo huleta tumaini, 5 wala tumaini halitukatishi tamaa, kwa sababu Mungu amekwisha kumimina pendo lake mioyoni mwetu kwa njia ya Roho Mtakatifu ambaye ametupatia.

    6 Kwa maana hata tulipokuwa dhaifu, wakati ulipowadia, Kristo alikufa kwa ajili yetu sisi wenye dhambi. 7 Hakika, ni vigumu mtu yeyote kufa kwa ajili ya mwenye haki, ingawa inawezekana mtu akathubutu kufa kwa ajili ya mtu mwema. 8 Lakini Mungu anaudhihirisha upendo wake kwetu kwamba: Tulipokuwa tungali wenye dhambi, Kristo alikufa kwa ajili yetu.

    9 Basi, kwa kuwa sasa tumehesabiwa haki kwa damu yake, si zaidi sana tutaokolewa kutoka ghadhabu ya Mungu kupitia kwake! 10 Kwa kuwa kama tulipokuwa adui wa Mungu tulipatanishwa naye kwa njia ya kifo cha Mwanawe, si zaidi sana tukiisha kupatanishwa, tutaokolewa kwa uzima wake. 11 Lakini zaidi ya hayo, pia tunafurahi katika Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kupitia kwake tumepata upatanisho.

  21. 6 Katika hili mnafurahi sana, ingawa sasa kwa kitambo kidogo mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna nyingi. 7 Haya yamewajia ili kwamba imani yenu, iliyo ya thamani kuliko dhahabu ipoteayo, ingawa hujaribiwa kwa moto, ionekane kuwa halisi na imalizie katika sifa, utukufu na heshima wakati Yesu Kristo atadhihirishwa. 8 Ingawa hamjamwona, mnampenda; tena ingawa sasa hammwoni, mnamwamini na kujawa na furaha isiyoneneka yenye utukufu usioelezeka. 9 Maana mnaupokea wokovu wa roho zenu, ambao ndio lengo la imani yenu.

  22. 15 Heri watu ambao hili ni kweli;

    heri wale ambao Bwana ni Mungu wao.

  23. 13 Hata katika kicheko moyo waweza kuuma,

    nayo furaha yaweza kuishia katika majonzi.

  24. 13 Moyo wenye furaha hufanya uso uchangamke,

    bali maumivu ya moyoni huponda roho.

  25. 14 Yeye atakuwa furaha na shangwe kwako, nao watu wengi watashangilia kwa sababu ya kuzaliwa kwake.

  26. 14 Lakini mmebarikiwa hata kama ikiwalazimu kuteseka kwa ajili ya haki. “Msiogope vitisho vyao, wala msiwe na wasiwasi.”

  27. 22 Moyo wenye furaha ni dawa nzuri,

    bali roho iliyopondeka hukausha mifupa.

  28. 16 Furahini siku zote; 17 ombeni bila kukoma; 18 shukuruni kwa kila jambo, kwa maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu kwa ajili yenu katika Kristo Yesu.

  29. 5 Kama mtu ameoa karibuni, kamwe asipelekwe vitani au kupewa wajibu mwingine wowote. Kwa mwaka mmoja atakuwa huru kubaki nyumbani ili amfurahishe mke aliyemwoa.

  30. 17 “Heri mtu yule ambaye Mungu humrudi;

    kwa hiyo usidharau adhabu yake Mwenyezi.

  31. 17 Kwa maana Ufalme wa Mungu si kula na kunywa, bali ni haki, amani na furaha katika Roho Mtakatifu.

  32. 11 Kama mnavyojua, tunawahesabu kuwa wabarikiwa wale waliovumilia. Mmesikia habari za uvumilivu wake Ayubu na mmeona kile ambacho hatimaye Bwana alimtendea. Bwana ni mwingi wa huruma, na amejaa rehema.

  33. KITABU CHA KWANZA

    1 Heri mtu yule ambaye

    haendi katika shauri la watu waovu,

    wala hasimami katika njia ya wenye dhambi,

    au kuketi katika baraza la wenye mizaha.

    2 Bali huifurahia sheria ya Bwana,

    naye huitafakari hiyo sheria usiku na mchana.

    3 Mtu huyo ni kama mti uliopandwa

    kando ya vijito vya maji,

    ambao huzaa matunda kwa majira yake

    na majani yake hayanyauki.

    Lolote afanyalo hufanikiwa.

    4 Sivyo walivyo waovu!

    Wao ni kama makapi

    yapeperushwayo na upepo.

  34. 15 Siku zote za wanaoonewa ni za taabu,

    bali moyo mchangamfu una karamu ya kudumu.

  35. 2 Hakika Mungu ni wokovu wangu;

    nitamtumaini wala sitaogopa.

    Bwana, Bwana, ni nguvu zangu na wimbo wangu;

    amekuwa wokovu wangu.”

    3 Kwa furaha mtachota maji

    kutoka visima vya wokovu.

    4 Katika siku hiyo mtasema:

    “Mshukuruni Bwana, mliitie jina lake;

    julisheni miongoni mwa mataifa yale aliyoyafanya,

    tangazeni kuwa jina lake limetukuka.

    5 Mwimbieni Bwana, kwa kuwa ametenda mambo makuu,

    hili na lijulikane duniani kote.

    6 Pazeni sauti mwimbe kwa furaha, watu wa Sayuni,

    kwa maana mkuu ni yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli miongoni mwenu.”

  36. 13 Je, mtu yeyote miongoni mwenu amepatwa na taabu? Basi inampasa aombe. Je, kuna yeyote mwenye furaha? Basi na aimbe nyimbo za kusifu.

  37. 6 Sara akasema, “Mungu ameniletea kicheko, kila mmoja atakayesikia jambo hili atacheka pamoja nami.”

  38. 5 Kutokana na ushindi uliompa, utukufu wake ni mkubwa,

    umeweka juu yake fahari na utukufu.

    6 Hakika umempa baraka za milele,

    umemfanya awe na furaha

    kwa shangwe ya uwepo wako.

    7 Kwa kuwa mfalme anamtumaini Bwana;

    kwa upendo usiokoma wa Aliye Juu Sana hatatikiswa.

  39. 3 Wana ni urithi utokao kwa Bwana,

    watoto ni zawadi kutoka kwake.

    4 Kama mishale mikononi mwa shujaa

    ndivyo walivyo wana awazaao mtu katika ujana wake.

    5 Heri mtu ambaye podo lake

    limejazwa nao.

    Hawataaibishwa wanaposhindana

    na adui zao langoni.

  40. 15 Wewe unafahamu, Ee Bwana,

    unikumbuke na unitunze mimi.

    Lipiza kisasi juu ya watesi wangu.

    Kwa uvumilivu wako usiniondolee mbali;

    kumbuka jinsi ninavyoshutumiwa.

    16 Maneno yako yalipokuja, niliyala;

    yakawa shangwe yangu

    na furaha ya moyo wangu,

    kwa kuwa nimeitwa kwa jina lako,

    Ee Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote.

  41. 9 Je, tutawezaje kumshukuru Mungu kiasi cha kutosha kwa ajili yenu, kutokana na furaha tuliyo nayo mbele za Mungu wetu kwa sababu yenu? 10 Usiku na mchana tunaomba kwa bidii ili tupate kuwaona tena na kujaza kile kilichopungua katika imani yenu.

  42. 2 Vinywa vyetu vilijaa kicheko,

    ndimi zetu zilijaa nyimbo za shangwe.

    Ndipo iliposemwa miongoni mwa mataifa,

    “Bwana amewatendea mambo makuu.”

    3 Bwana ametutendea mambo makuu,

    nasi tumejaa furaha.

  43. 1 Nikafikiri moyoni mwangu, “Haya basi, nitakujaribu kwa anasa nione ni lipi lililo jema.” Lakini hilo nalo likaonekana ni ubatili. 2 Nikasema, “Kicheko nacho ni upumbavu. Nayo matokeo ya anasa ni nini?”

  44. 26 Kwa yule mtu anayempendeza Mungu, Mungu humpa hekima, maarifa na furaha, bali kwa mwenye dhambi Mungu humpa kazi ya kukusanya na kuhifadhi utajiri ili Mungu ampe yule anayempenda. Hili nalo pia ni ubatili, ni kukimbiza upepo.

  45. 9 Furahi ewe kijana, wakati ungali kijana,

    moyo wako na ukupe furaha

    katika siku za ujana wako.

    Fuata njia za moyo wako

    na chochote macho yako yaonayo,

    lakini ujue kwamba kwa ajili ya haya yote

    Mungu atakuleta hukumuni.

  46. 21 “Bwana wake akamwambia, ‘Umefanya vizuri sana, mtumishi mwema na mwaminifu! Umekuwa mwaminifu kwa vitu vichache; nami nitakuweka kuwa msimamizi wa vitu vingi. Njoo ushiriki katika furaha ya bwana wako!’

  47. 14 Wabarikini wale wanaowatesa, barikini wala msilaani. 15 Furahini pamoja na wenye kufurahi, lieni pamoja na wale waliao. 16 Kaeni kwa amani ninyi kwa ninyi. Msijivune, bali mwe tayari kushirikiana na wanyonge. Wala msiwe watu wenye kujivuna kwamba mnajua kila kitu.

  48. 6 Lakini utauwa na kuridhika ni faida kubwa. 7 Kwa kuwa hatukuja humu duniani na kitu chochote, wala hatuwezi kutoka humu na kitu. 8 Lakini kama tuna chakula na mavazi, tutaridhika navyo. 9 Lakini wale watu wanaotamani kuwa na mali kwa haraka huanguka kwenye majaribu, na wamenaswa na tamaa nyingi za kipumbavu zenye kudhuru, zinazowazamisha watu katika uharibifu na maangamizi. 10 Kwa maana kupenda fedha ndiyo shina moja la maovu ya kila namna. Baadhi ya watu wakitamani fedha, wameiacha imani na kujichoma wenyewe kwa maumivu mengi.

  49. 9 Humjalia mwanamke tasa kutulia nyumbani mwake,

    akiwa mama watoto mwenye furaha.

    Msifuni Bwana.

  50. 20 Bwana huwachukia sana watu wenye moyo wa upotovu,

    bali hupendezwa na wale ambao njia zao hazina lawama.

  51. 10 Ninafurahia sana katika Bwana,

    nafsi yangu inashangilia katika Mungu wangu.

    Kwa maana amenivika mavazi ya wokovu,

    na kunipamba kwa joho la haki,

    kama vile bwana arusi apambavyo

    kichwa chake kama kuhani,

    na kama bibi arusi ajipambavyo

    kwa vito vyake vya thamani.

  52. 5 Yona akatoka nje akaketi mahali upande wa mashariki wa mji. Hapo akajitengenezea kibanda, akaketi kwenye kivuli chake na kungojea ni nini kitakachotokea katika mji. 6 Ndipo Bwana, Mungu akaweka tayari mzabibu na kuufanya uote, kumpa Yona kivuli kilichomfunika kichwa ili kuondoa taabu yake, naye Yona akafurahi sana kwa ajili ya ule mzabibu. 7 Lakini kesho yake asubuhi na mapema Mungu akaamuru buu, autafune mzabibu huo nao ukanyauka. 8 Wakati jua lilipochomoza, Mungu akautuma upepo wa hari wa mashariki, nalo jua likawaka juu ya kichwa cha Yona mpaka akazimia. Akatamani kufa, naye akasema, “Ni afadhali mimi nife kuliko kuishi.”

    9 Lakini Mungu alimwambia Yona, “Je, unayo haki kukasirika kuhusu mzabibu huo?”

    Akasema, “Ndiyo, ninayo haki. Nimekasirika kiasi cha kufa.”

    10 Lakini Bwana akamwambia, “Wewe unakasirika kwa ajili ya mzabibu huu, nawe hukuusababisha kuota wala kuutunza. Uliota usiku mmoja, nao ukafa usiku mmoja. 11 Lakini Ninawi ina zaidi ya watu 120,000 ambao hawawezi kupambanua kulia au kushoto, pamoja na ngʼombe wengi. Je, hainipasi kufikiri juu ya mji ule mkubwa?”

  53. 11 “Heri ninyi watu watakapowashutumu, na kuwatesa na kunena dhidi yenu mabaya ya aina zote kwa uongo kwa ajili yangu. 12 Furahini na kushangilia kwa maana thawabu yenu ni kubwa mbinguni, kwa kuwa hivyo ndivyo walivyowatesa manabii waliokuwa kabla yenu.

  54. 10 Lakini malaika akawaambia: “Msiogope. Kwa maana tazama nawaletea habari njema za furaha itakayokuwa kwa watu wote.

  55. 20 Akawatazama wanafunzi wake, akasema:

    “Mmebarikiwa ninyi mlio maskini,

    kwa sababu Ufalme wa Mungu ni wenu.

    21 Mmebarikiwa ninyi mlio na njaa sasa,

    kwa sababu mtashibishwa.

    Mmebarikiwa ninyi mnaolia sasa,

    kwa sababu mtacheka.

    22 Mmebarikiwa ninyi, watu watakapowachukia,

    watakapowatenga na kuwatukana

    na kulikataa jina lenu kama neno ovu,

    kwa ajili ya Mwana wa Adamu.

    23 “Furahini na kurukaruka kwa shangwe, kwa sababu thawabu yenu ni kubwa mbinguni, kwa kuwa hivyo ndivyo baba zao walivyowatenda manabii.

  56. 21 Siku ya pili yake wakamtolea Bwana dhabihu na sadaka za kuteketezwa: mafahali 1,000, kondoo dume 1,000 na wana-kondoo dume 1,000, pamoja na sadaka za kinywaji na sadaka nyingine nyingi sana kwa ajili ya Israeli. 22 Wakala na kunywa kwa furaha kubwa mbele za Bwana siku ile.

    Wakamtawaza Solomoni mwana wa Daudi mara ya pili kuwa mfalme, wakamtia mafuta kwa ajili ya Bwana ili awe mfalme na Sadoki kuwa kuhani. 23 Solomoni akaketi kwenye kiti cha enzi cha Bwana kuwa mfalme mahali pa Daudi baba yake. Akafanikiwa sana na Israeli wote wakamtii. 24 Maafisa wote na mashujaa, pamoja na wana wote wa Daudi, wakaahidi kumtii Mfalme Solomoni.

    25 Bwana akamtukuza sana Solomoni mbele ya Israeli wote na kumvika fahari ya kifalme ambayo hakuna mfalme yeyote wa Israeli kabla yake aliwahi kuwa nayo.

  57. 6 Bwana asifiwe,

    kwa maana amesikia kilio changu

    nikimwomba anihurumie.

    7 Bwana ni nguvu zangu na ngao yangu,

    moyo wangu umemtumaini yeye,

    nami nimesaidiwa.

    Moyo wangu unarukaruka kwa furaha

    nami nitamshukuru kwa wimbo.

    8 Bwana ni nguvu ya watu wake,

    ngome ya wokovu kwa mpakwa mafuta wake.

  58. 4 Ndipo nitakwenda madhabahuni pa Mungu,

    kwa Mungu, furaha yangu na shangwe yangu.

    Nitakusifu kwa kinubi,

    Ee Mungu, Mungu wangu.

  59. 5 Wapandao kwa machozi

    watavuna kwa nyimbo za shangwe.

    6 Yeye azichukuaye mbegu zake

    kwenda kupanda, huku akilia,

    atarudi kwa nyimbo za shangwe,

    akichukua miganda ya mavuno yake.

  60. 30 Mtazamo wa tabasamu huleta furaha moyoni,

    nazo habari njema huipa mifupa afya.

  61. 33 Nimewaambia mambo haya, ili mpate kuwa na amani mkiwa ndani yangu. Ulimwenguni mtapata dhiki. Lakini jipeni moyo, kwa maana mimi nimeushinda ulimwengu.”

  62. 25 Lakini nadhani ni muhimu kumtuma tena kwenu Epafrodito, ndugu yangu na mtendakazi pamoja nami, aliye askari mwenzangu, ambaye pia ni mjumbe wenu mliyemtuma ili ashughulike na mahitaji yangu. 26 Kwa maana amekuwa akiwaonea sana shauku ninyi nyote, akiwa na wasiwasi kwa kuwa mlisikia kwamba alikuwa mgonjwa. 27 Kweli alikuwa mgonjwa, tena karibu ya kufa. Lakini Mungu alimhurumia, wala si yeye tu, bali hata na mimi alinihurumia, nisipatwe na huzuni juu ya huzuni. 28 Kwa hiyo mimi ninafanya bidii kumtuma kwenu ili mtakapomwona kwa mara nyingine, mpate kufurahi, nami wasiwasi wangu upungue. 29 Kwa hiyo mpokeeni katika Bwana kwa furaha kubwa, nanyi wapeni heshima watu kama hawa, 30 kwa sababu alikaribia kufa kwa ajili ya kazi ya Kristo, akihatarisha maisha yake ili aweze kunihudumia vile ninyi hamkuweza.

  63. 19 Naye Mungu wangu atawajaza ninyi na kila mnachohitaji kwa kadiri ya utajiri wake katika utukufu ndani ya Kristo Yesu.

  64. 5 Kwa maana hasira yake ni ya muda mfupi,

    bali upendo wake hudumu siku zote.

    Inawezekana kilio kiwepo usiku kucha,

    lakini asubuhi kukawa na furaha.

  65. 8 Ee Mungu wangu,

    natamani kuyafanya mapenzi yako;

    sheria yako iko ndani ya moyo wangu.”

  66. 11 Mbingu na zishangilie, nchi na ifurahi;

    bahari na ivume, na vyote vilivyomo ndani yake;

    12 mashamba na yashangilie,

    pamoja na vyote vilivyomo ndani yake.

    Kisha miti yote ya msituni itaimba kwa furaha;

    13 itaimba mbele za Bwana kwa maana anakuja,

    anakuja kuihukumu dunia.

    Ataihukumu dunia kwa haki,

    na mataifa katika kweli yake.

  67. 28 Tarajio la mwenye haki ni furaha,

    bali matumaini ya mwovu huwa si kitu.

  68. 15 Kwa hiyo mimi ninasifu kufurahia maisha, kwa sababu hakuna kitu bora zaidi kwa mwanadamu chini ya jua kuliko kula, kunywa na kufurahi. Kisha furaha itafuatana naye kazini mwake siku zote za maisha yake ambazo amepewa na Mungu chini ya jua.

  69. 15 Furaha imeondoka mioyoni mwetu,

    kucheza kwetu kumegeuka maombolezo.

  70. 44 “Ufalme wa Mbinguni unafanana na hazina iliyofichwa shambani, ambayo mtu mmoja alipoiona akaificha tena. Kisha katika furaha yake, akaenda akauza vyote alivyokuwa navyo, akalinunua lile shamba.”

    45 “Tena, Ufalme wa Mbinguni unafanana na mfanyabiashara aliyekuwa akitafuta lulu safi. 46 Alipoipata lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda akauza vyote alivyokuwa navyo akainunua.”

  71. 25 “Lakini Abrahamu akamjibu, ‘Mwanangu, kumbuka kwamba wakati wa uhai wako ulipata mambo mazuri, lakini Lazaro alipata mambo mabaya. Lakini sasa anafarijiwa hapa na wewe uko katika maumivu makuu.

  72. 52 Wanafunzi wakajawa na furaha na Roho Mtakatifu.

  73. 3 Kwa ajili ya neema niliyopewa nawaambia kila mmoja miongoni mwenu, asijidhanie kuwa bora kuliko impasavyo, bali afikiri kwa busara kwa kulingana na kipimo cha imani Mungu aliyompa. 4 Kama vile katika mwili mmoja tulivyo na viungo vingi, navyo viungo vyote havina kazi moja, 5 vivyo hivyo na sisi tulio wengi, tu mwili mmoja katika Kristo, nasi kila mmoja ni kiungo cha mwenzake. 6 Tuna karama zilizotofautiana kila mmoja kutokana na neema tuliyopewa. Kama ni unabii na tutoe unabii kwa kadiri ya imani. 7 Kama ni kuhudumu na tuhudumu, mwenye kufundisha na afundishe, 8 kama ni kutia moyo na atie moyo, kama ni kuchangia kwa ajili ya mahitaji ya wengine na atoe kwa ukarimu, kama ni uongozi na aongoze kwa bidii, kama ni kuhurumia wengine na afanye hivyo kwa furaha.

  74. 13 Kwa ajili ya haya tumefarijika.

    Zaidi ya kule sisi kutiwa moyo, tulifurahi sana kumwona Tito alivyo na furaha, kwa sababu roho yake imeburudishwa na ninyi nyote.

  75. 17 Waagize wale ambao ni matajiri wa ulimwengu huu waache kujivuna, wala wasiweke tumaini lao katika mali ambayo si ya hakika, bali waweke tumaini lao katika Mungu ambaye hutupatia vitu vyote kwa wingi ili tuvifurahie. 18 Waagize watende mema, wawe matajiri katika matendo mema, pia wawe wakarimu na walio tayari kushiriki mali zao na wengine. 19 Kwa njia hii watajiwekea hazina kama msingi kwa ajili ya wakati ujao na hivyo watajipatia uzima, yaani, ule uzima ambao ni wa kweli.

  76. 5 Yalindeni maisha yenu msiwe na tabia ya kupenda fedha, bali mridhike na vile mlivyo navyo, kwa sababu Mungu amesema,

    “Kamwe sitakuacha,

    wala sitakupungukia.”

    6 Kwa hiyo tunaweza kusema kwa ujasiri,

    “Bwana ni msaada wangu; sitaogopa.

    Mwanadamu anaweza kunitenda nini?”

  77. 12 Mtatoka nje kwa furaha

    na kuongozwa kwa amani;

    milima na vilima

    vitapaza sauti kwa nyimbo mbele yenu,

    nayo miti yote ya shambani

    itapiga makofi.

  78. 9 Kwa sababu hii, tangu siku ile tuliposikia habari zenu, hatujakoma kuomba kwa ajili yenu na kumsihi Mungu awajaze ninyi maarifa ya mapenzi yake katika hekima yote ya kiroho na ufahamu. 10 Nasi tunaomba haya ili mpate kuishi maisha yanayostahili mbele za Bwana, na mpate kumpendeza kwa kila namna: mkizaa matunda kwa kila kazi njema, mkikua katika kumjua Mungu, 11 mkiwa mmetiwa nguvu kwa uwezo wote kwa kadiri ya nguvu yake yenye utukufu, ili mpate kuwa na wingi wa saburi na uvumilivu. Nanyi kwa furaha 12 mkimshukuru Baba, ambaye amewastahilisha kushiriki katika urithi wa watakatifu katika ufalme wa nuru. 13 Kwa maana ametuokoa kutoka ufalme wa giza na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wake mpendwa, 14 ambaye katika yeye tunao ukombozi, yaani msamaha wa dhambi.