41 Bible Verses About Courage

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Courage
  1. 5 Hakuna mtu yeyote atakayeweza kushindana na wewe siku zote za maisha yako. Kama vile nilivyokuwa pamoja na Mose, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe, sitakuacha wala sitakupungukia.

    6 “Uwe hodari na shujaa, kwa sababu wewe ndiwe utakayewaongoza watu hawa kuirithi nchi niliyowaapia baba zao kuwapa. 7 Uwe hodari na uwe na ushujaa mwingi. Uwe na bidii kutii sheria yote aliyokupa Mose mtumishi wangu, usiiache kwa kugeuka kuelekea kuume au kushoto, ili upate kufanikiwa popote uendako. 8 Usiache Kitabu hiki cha Sheria kiondoke kinywani mwako; yatafakari maneno yake usiku na mchana, ili upate kuwa mwangalifu kufanya kila kitu sawasawa na yote yaliyoandikwa ndani yake. Ndipo utakapofanikiwa na kisha utastawi. 9 Je, si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na shujaa. Usihofu wala usivunjike moyo, kwa kuwa Bwana Mungu wako atakuwa pamoja nawe kokote uendako.”

    10 Ndipo Yoshua akawaagiza maafisa wa watu akisema, 11 “Pitieni katika kambi yote mkawaambie watu, ‘Wekeni tayari mahitaji yenu. Siku tatu kuanzia sasa mtavuka hii Yordani ili kuingia na kuimiliki nchi ambayo Bwana Mungu wenu anawapa iwe yenu wenyewe.’ ”

  2. 6 Kuweni imara na moyo wa ushujaa. Msiogope wala msifadhaike kwa sababu yao, kwa kuwa Bwana Mungu wenu anakwenda pamoja nanyi; kamwe hatawaacha wala hatawatupa ninyi.”

    7 Kisha Mose akamwita Yoshua na akamwambia mbele ya Israeli wote, “Uwe imara na moyo wa ushujaa, kwa kuwa ni lazima uende na watu hawa katika nchi ile Bwana aliyowaapia baba zao kuwapa, nawe ni lazima uwagawie kama urithi wao. 8 Bwana mwenyewe atakutangulia naye atakuwa pamoja nawe; kamwe hatakuacha wala hatakutupa. Usiogope, wala usifadhaike.”

  3. 16 Shadraki, Meshaki na Abednego wakamjibu mfalme, “Ee Nebukadneza, hatuhitaji kujitetea mbele zako kuhusu jambo hili. 17 Ikiwa tutatupwa ndani ya tanuru iwakayo moto, Mungu tunayemtumikia anaweza kutuokoa na moto, naye atatuokoa kutoka mkononi mwako, ee mfalme. 18 Lakini hata ikiwa hatatuokoa, ee mfalme, tunataka ufahamu kwamba, hatutaitumikia miungu yako wala kuiabudu sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.”

  4. Zaburi ya Daudi.

    1 Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu,

    nimwogope nani?

    Bwana ni ngome ya uzima wangu,

    nimhofu nani?

    2 Waovu watakaposogea dhidi yangu

    ili wanile nyama yangu,

    adui zangu na watesi wangu watakaponishambulia,

    watajikwaa na kuanguka.

    3 Hata jeshi linizunguke pande zote,

    moyo wangu hautaogopa;

    hata vita vitokee dhidi yangu,

    hata hapo nitakuwa na ujasiri.

  5. 10 Hivyo usiogope, kwa maana niko pamoja nawe;

    usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako.

    Nitakutia nguvu na kukusaidia;

    nitakutegemeza kwa mkono wa kuume wa haki yangu.

    11 “Wote walioona hasira dhidi yako

    hakika wataaibika na kutahayarika,

    wale wakupingao

    watakuwa kama vile si kitu, na kuangamia.

    12 Ingawa utawatafuta adui zako,

    hutawaona.

    Wale wanaopigana vita dhidi yako

    watakuwa kama vile si kitu kabisa.

    13 Kwa maana Mimi ndimi Bwana, Mungu wako,

    nikushikaye mkono wako wa kuume

    na kukuambia, Usiwe na hofu,

    nitakusaidia.

    14 Usiogope, ee Yakobo uliye mdudu,

    ee Israeli uliye mdogo,

    kwa kuwa Mimi mwenyewe nitakusaidia,” asema Bwana,

    Mkombozi wako, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli.

  6. 11 Nifundishe njia yako, Ee Bwana,

    niongoze katika njia iliyonyooka

    kwa sababu ya watesi wangu.

    12 Usiniachilie kwa nia za adui zangu,

    kwa maana mashahidi wa uongo

    wameinuka dhidi yangu,

    wakipumua ujeuri.

    13 Nami bado nina tumaini hili:

    nitauona wema wa Bwana

    katika nchi ya walio hai.

    14 Mngojee Bwana,

    uwe hodari na mwenye moyo mkuu,

    nawe, umngojee Bwana.

  7. 13 Kesheni, simameni imara katika imani, fanyeni kiume, kuweni mashujaa kuweni hodari.

  8. 7 Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali roho ya nguvu, ya upendo na ya moyo wa kiasi.

  9. 20 Daudi pia akamwambia Solomoni mwanawe, “Uwe hodari na moyo mkuu, ukafanye kazi hii. Usiogope wala usifadhaike, kwa maana Bwana aliye Mungu, Mungu wangu yu pamoja nawe. Hatakuacha wala hatakupungukia mpaka kazi hii yote kwa ajili ya utumishi wa Hekalu la Bwana itakapokamilika.

  10. 11 “Sasa, mwanangu, Bwana awe pamoja nawe, nawe uwe na mafanikio upate kuijenga nyumba ya Bwana Mungu wako, kama alivyosema utafanya. 12 Bwana na akupe hekima na ufahamu wakati atakuweka juu ya Israeli, ili uweze kuishika sheria ya Bwana Mungu wako. 13 Ndipo utakapofanikiwa, ikiwa utakuwa na bidii kutii amri na sheria Bwana alizompa Mose kwa ajili ya Israeli. Uwe hodari na ushujaa. Usiogope wala usikate tamaa.

  11. 24 Kuweni hodari na mjipe moyo,

    ninyi nyote mnaomtumaini Bwana.

  12. 12 Basi, ndugu zangu, nataka mjue kwamba mambo yale yaliyonipata kwa kweli yamesaidia sana kueneza Injili. 13 Matokeo yake ni kwamba imejulikana wazi kwa walinzi wote wa jumba la kifalme na kwa wengine wote kuwa nimefungwa kwa ajili ya Kristo. 14 Kwa sababu ya vifungo vyangu, ndugu wengi katika Bwana wametiwa moyo kuhubiri neno la Mungu kwa ujasiri zaidi na bila woga.

  13. 33 Nimewaambia mambo haya, ili mpate kuwa na amani mkiwa ndani yangu. Ulimwenguni mtapata dhiki. Lakini jipeni moyo, kwa maana mimi nimeushinda ulimwengu.”

  14. 25 Yoshua akawaambia, “Msiogope, wala msivunjike moyo. Kuweni hodari na wenye ushujaa. Hili ndilo Bwana atakalowatendea adui zenu wote mnaokwenda kupigana nao.”

  15. 5 Yalindeni maisha yenu msiwe na tabia ya kupenda fedha, bali mridhike na vile mlivyo navyo, kwa sababu Mungu amesema,

    “Kamwe sitakuacha,

    wala sitakupungukia.”

    6 Kwa hiyo tunaweza kusema kwa ujasiri,

    “Bwana ni msaada wangu; sitaogopa.

    Mwanadamu anaweza kunitenda nini?”

  16. 12 Uwe hodari na tupigane kwa ujasiri kwa ajili ya watu wetu na miji ya Mungu wetu. Bwana atafanya lile lililo jema machoni pake.”

  17. Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Njiwa mkimya wa mbali.” Utenzi wa Daudi. Baada ya kukamatwa na Wafilisti huko Gathi.

    1 Ee Mungu unihurumie, maana watu wananifuatia vikali;

    mchana kutwa wanazidisha mashambulizi yao.

    2 Wasingiziaji wangu wananifuatia mchana kutwa,

    wengi wananishambulia kwa kiburi chao.

    3 Wakati ninapoogopa,

    nitakutumaini wewe.

    4 Katika Mungu, ambaye neno lake ninalisifu,

    katika Mungu ninatumaini; sitaogopa.

    Mwanadamu apatikanaye na kufa,

    atanitenda nini?

  18. 1 Mtu mwovu hukimbia ingawa hakuna yeyote anayemfukuza,

    bali wenye haki ni wajasiri kama simba.

  19. 18 Kisha wakawaita tena ndani na kuwaamuru wasiseme wala kufundisha kamwe kwa hili jina la Yesu.

    19 Lakini Petro na Yohana wakajibu, “Amueni ninyi wenyewe iwapo ni haki mbele za Mungu kuwatii ninyi kuliko kumtii Mungu. 20 Lakini sisi hatuwezi kuacha kusema yale tuliyoyaona na kuyasikia.”

  20. 18 Katika pendo hakuna hofu. Lakini pendo lililo kamili huitupa nje hofu, kwa sababu hofu inahusika na adhabu. Kila mwenye hofu hakukamilika katika pendo.

  21. 22 Hivyo Mose akaandika wimbo huu siku ile na akawafundisha Waisraeli.

    23 Bwana akampa Yoshua mwana wa Nuni agizo hili: “Uwe hodari na shujaa, kwa kuwa utawaleta Waisraeli katika nchi niliyowaahidi kwa kiapo, nami mwenyewe nitakuwa pamoja nawe.”

  22. 7 “Kuweni hodari na wenye moyo mkuu. Msiogope, msifadhaike wala msikate tamaa kwa sababu ya mfalme wa Ashuru na hili jeshi kubwa lililo pamoja naye, kwa kuwa aliye pamoja nasi ni mkuu kuliko aliye pamoja naye. 8 Kwake uko mkono wa mwili tu, bali kwetu yuko Bwana Mungu wetu kutusaidia na kutupigania vita vyetu.” Nao watu wakatiwa moyo kutokana na maneno aliyowaambia Hezekia mfalme wa Yuda.

  23. 27 Lakini lolote litakalotukia, mwenende kama ipasavyo Injili ya Kristo, ili kwamba nikija na kuwaona au ikiwa sipo, nipate kusikia haya juu yenu: Kuwa mnasimama imara katika roho moja, mkiishindania imani ya Injili kwa umoja, 28 wala msitishwe na wale wanaowapinga. Hii ni ishara kwao kuwa wataangamia, lakini ninyi mtaokolewa, na hii ni kazi ya Mungu.

  24. 45 Daudi akamwambia yule Mfilisti. “Wewe unanijia na upanga, mkuki na fumo, lakini mimi ninakujia kwa jina la Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa majeshi ya Israeli, ambaye wewe umemtukana. 46 Siku hii leo Bwana atakutia mkononi mwangu, nami nitakupiga na kukukata kichwa chako. Leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya jeshi la Wafilisti, nayo dunia yote itajua kuwa yuko Mungu katika Israeli. 47 Wale wote waliokusanyika hapa watajua kuwa Bwana haokoi kwa upanga wala kwa mkuki; kwa kuwa vita ni vya Bwana, naye atawatia wote mikononi mwetu.”

  25. 1 Wakati Ezra alipokuwa anaomba na kuungama, huku akilia na kujitupa chini mbele ya nyumba ya Mungu, umati mkubwa wa Waisraeli, wanaume, wanawake na watoto walikusanyika kumzunguka. Nao pia wakalia sana. 2 Kisha Shekania mwana wa Yehieli, mmoja wa wazao wa Elamu, akamwambia Ezra, “Tumekosa uaminifu kwa Mungu wetu kwa kuoa wanawake wa kigeni kutoka mataifa yanayotuzunguka. Lakini pamoja na hili, bado liko tumaini kwa ajili ya Israeli. 3 Sasa na tufanye agano mbele za Mungu wetu kuwafukuza hawa wanawake wote pamoja na watoto wao, kulingana na maonyo ya bwana wangu pamoja na wale ambao wanaogopa amri za Mungu wetu. Hili na lifanyike sawasawa na hii Sheria. 4 Inuka, suala hili lipo mikononi mwako. Sisi tutaungana nawe, uwe na ujasiri ukatende hili.”

  26. 26 Lakini huyo Msaidizi, yaani, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwenu kwa Jina langu, atawafundisha mambo yote na kuwakumbusha yote niliyowaambia. 27 Amani nawaachia, amani yangu nawapa, amani hii niwapayo si kama ile ulimwengu utoayo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiogope.

    28 “Mlinisikia nikisema, ‘Ninakwenda zangu, lakini nitarudi tena.’ Kama kweli mngelinipenda mngelifurahi kwa kuwa naenda kwa Baba, kwani Baba ni mkuu kuniliko mimi. 29 Nimewaambia mambo haya kabla hayajatukia, ili yatakapotukia mpate kuamini. 30 Sitasema nanyi zaidi, kwa sababu yule mkuu wa ulimwengu huu anakuja, naye hana kitu kwangu, 31 lakini ulimwengu upate kujua kuwa ninampenda Baba, nami hufanya vile Baba alivyoniamuru.

    “Haya inukeni; twendeni zetu.

  27. 19 kwa maana ninajua kwamba kwa maombi yenu na kwa msaada unaotolewa na Roho wa Yesu Kristo, yale yaliyonipata mimi yatageuka kuwa wokovu wangu. 20 Ninatarajia kwa shauku kubwa na kutumaini kwamba sitaaibika kwa njia yoyote, bali nitakuwa na ujasiri wa kutosha ili sasa kama wakati mwingine wowote, Kristo atukuzwe katika mwili wangu, ikiwa ni kwa kuishi au kwa kufa. 21 Kwa maana kwangu mimi, kuishi ni Kristo, na kufa ni faida.

  28. 11 Tuliposikia juu ya hili, mioyo yetu iliyeyuka na kila mmoja alikosa ujasiri kwa sababu yenu, kwa maana Bwana Mungu wenu ni Mungu juu mbinguni na duniani chini.

  29. 2 Hakika Mungu ni wokovu wangu;

    nitamtumaini wala sitaogopa.

    Bwana, Bwana, ni nguvu zangu na wimbo wangu;

    amekuwa wokovu wangu.”

  30. 26 “Kwa hiyo msiwaogope hao, kwa maana hakuna kilichofichika ambacho hakitafunuliwa, wala hakuna siri ambayo haitajulikana. 27 Ninalowaambia gizani, ninyi lisemeni mchana peupe. Na lile mnalosikia likinongʼonwa masikioni mwenu, lihubirini juu ya nyumba. 28 Msiwaogope wale wauao mwili lakini hawawezi kuua roho. Afadhali mwogopeni yeye awezaye kuiangamiza roho na mwili katika jehanamu. 29 Je, shomoro wawili hawauzwi kwa senti moja tu? Lakini hakuna hata mmoja wao atakayeanguka chini pasipo Baba yenu kujua. 30 Hata nywele za vichwa vyenu zote zimehesabiwa. 31 Hivyo msiogope; kwa maana ninyi ni wa thamani kubwa kuliko shomoro wengi.

  31. 27 Lakini mara Yesu akasema nao, akawaambia, “Jipeni moyo! Ni mimi. Msiogope.”

  32. 9 kama leo tukihojiwa kwa habari ya mambo mema aliyotendewa yule kiwete na kuulizwa jinsi alivyoponywa, 10 ijulikane kwenu nyote na kwa watu wote wa Israeli kwamba: Ni kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulubisha lakini Mungu akamfufua kutoka kwa wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama mbele yenu akiwa mzima kabisa. 11 Huyu ndiye

    “ ‘jiwe ambalo ninyi wajenzi mlilikataa,

    ambalo limekuwa jiwe kuu la pembeni.’

    12 Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hakuna jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.”

    13 Wale viongozi na wazee walipoona ujasiri wa Petro na Yohana na kujua ya kuwa walikuwa watu wa kawaida, wasio na elimu, walishangaa sana, wakatambua kwamba hawa watu walikuwa na Yesu.

  33. 11 Usiku uliofuata, Bwana akasimama karibu naye akamwambia, “Jipe moyo! Kama vile ulivyonishuhudia hapa Yerusalemu, hivyo imekupasa kunishuhudia huko Rumi pia.”

  34. Zaburi ya Daudi.

    1 Bwana ndiye mchungaji wangu,

    sitapungukiwa na kitu.

    2 Hunilaza katika malisho

    ya majani mabichi,

    kando ya maji matulivu huniongoza,

    3 hunihuisha nafsi yangu.

    Huniongoza katika njia za haki

    kwa ajili ya jina lake.

    4 Hata kama nikipita katikati

    ya bonde la uvuli wa mauti,

    sitaogopa mabaya,

    kwa maana wewe upo pamoja nami;

    fimbo yako na mkongojo wako

    vyanifariji.

  35. 10 Basi Danieli alipofahamu kuwa amri ile imetangazwa, alikwenda nyumbani kwenye chumba chake cha ghorofani ambako madirisha yalifunguka kuelekea Yerusalemu. Akapiga magoti na kuomba mara tatu kwa siku, akimshukuru Mungu wake kama alivyokuwa akifanya mwanzoni.

  36. 25 “Pamoja na jeshi kubwa atachochea nguvu zake na ushujaa wake dhidi ya mfalme wa Kusini. Mfalme wa Kusini atafanya vita na jeshi lenye nguvu sana, lakini hataweza kusimama kwa sababu ya kwa hila zilizofanywa dhidi yake.

  37. 6 Kwa hiyo siku zote tunalo tumaini, hata ingawa tunajua kwamba wakati tukiwa katika mwili huu, tuko mbali na Bwana, 7 kwa maana twaenenda kwa imani wala si kwa kuona. 8 Naam, tunalo tumaini na ingekuwa bora zaidi kuuacha mwili huu na kwenda kukaa na Bwana.

  38. 10 Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake.

  39. 14 Kwa kuwa tunaye Kuhani Mkuu kuliko wote ambaye ameingia mbinguni, Yesu Mwana wa Mungu, basi na tushikamane sana kwa uthabiti na ule ukiri wa imani yetu. 15 Kwa kuwa hatuna Kuhani Mkuu asiyeweza kuchukuliana na sisi katika udhaifu wetu, lakini tunaye mmoja ambaye alijaribiwa kwa kila namna, kama vile sisi tujaribiwavyo: lakini yeye hakutenda dhambi. 16 Basi na tukikaribie kiti cha rehema kwa ujasiri, ili tupewe rehema na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.

  40. 49 lakini walipomwona akitembea juu ya maji, wakadhani ni mzimu. Wakapiga yowe, 50 kwa sababu wote walipomwona waliogopa.

    Mara Yesu akasema nao, akawaambia, “Jipeni moyo! Ni mimi. Msiogope!”

  41. 28 “Tuliwaonya kwa nguvu msifundishe kwa jina hili, lakini ninyi mmeijaza Yerusalemu yote mafundisho yenu na tena mmekusudia kuleta damu ya mtu huyu juu yetu.”

    29 Petro na wale mitume wengine wakajibu, “Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu. 30 Mungu wa baba zetu alimfufua Yesu kutoka kwa wafu, ambaye ninyi mlimuua kwa kumtundika kwenye msalaba. 31 Mungu alimtukuza, akamweka mkono wake wa kuume kuwa Kiongozi na Mwokozi ili awape Israeli toba na msamaha wa dhambi. 32 Nasi tu mashahidi wa mambo haya, vivyo hivyo na Roho Mtakatifu ambaye Mungu amewapa wale wanaomtii.”