62 Bible Verses About Victory

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Victory
  1. 54 Kwa hiyo, mwili huu wa kuharibika utakapovaa kutokuharibika, nao huu mwili wa kufa utakapovaa kutokufa, ndipo lile neno lililoandikwa litakapotimia: “Mauti imemezwa kwa kushinda.”

    55 “Kuko wapi, ee mauti, kushinda kwako?

    Uko wapi, ee mauti, uchungu wako?”

    56 Uchungu wa mauti ni dhambi na nguvu ya dhambi ni sheria. 57 Lakini ashukuriwe Mungu, yeye atupaye ushindi kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo.

    58 Kwa hiyo, ndugu zangu wapenzi, simameni imara, msitikisike, mzidi sana katika kuitenda kazi ya Bwana, kwa maana mnajua ya kuwa, kazi yenu katika Bwana si bure.

  2. 1 Kila mtu anayeamini kwamba Yesu ndiye Kristo amezaliwa na Mungu, na yeyote ampendaye Baba humpenda pia mtoto aliyezaliwa naye. 2 Hivi ndivyo tunavyojua kwamba tunawapenda watoto wa Mungu, kwa kumpenda Mungu na kuzitii amri zake. 3 Huku ndiko kumpenda Mungu, yaani, kuzitii amri zake. Nazo amri zake si nzito. 4 Kwa maana kila aliyezaliwa na Mungu huushinda ulimwengu. Huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, yaani, hiyo imani yetu. 5 Ni nani yule aushindaye ulimwengu? Ni yule tu aaminiye kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu.

  3. 35 Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je, ni shida au taabu au mateso au njaa au uchi au hatari au upanga? 36 Kama ilivyoandikwa:

    “Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa;

    tumehesabiwa kama kondoo wa kuchinjwa.”

    37 Lakini katika mambo haya yote tunashinda, naam na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. 38 Kwa maana nimekwisha kujua kwa hakika ya kuwa sio mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuja, wala wenye uwezo, 39 wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kingine chochote zitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu, Bwana wetu.

  4. 33 Nimewaambia mambo haya, ili mpate kuwa na amani mkiwa ndani yangu. Ulimwenguni mtapata dhiki. Lakini jipeni moyo, kwa maana mimi nimeushinda ulimwengu.”

  5. 22 Kwa maana kama vile katika Adamu watu wote wanakufa, vivyo hivyo katika Kristo wote watafanywa hai. 23 Lakini kila mmoja kwa wakati wake: Kristo, tunda la kwanza kisha, wale walio wake, wakati atakapokuja. 24 Ndipo mwisho utafika, wakati atakapomkabidhi Mungu Baba ufalme, akiisha angamiza kila utawala na kila mamlaka na nguvu. 25 Kwa maana lazima Kristo atawale mpaka awe amewaweka adui zake wote chini ya miguu yake. 26 Adui wa mwisho atakayeangamizwa ni mauti. 27 Kwa maana Mungu “ameweka vitu vyote chini ya miguu yake.” Lakini isemapo kwamba “vitu vyote” vimewekwa chini yake, ni wazi kwamba Mungu aliyetiisha vitu vyote chini ya Kristo hayumo miongoni mwa hivyo vilivyotiishwa. 28 Atakapokuwa amekwisha kuyafanya haya, ndipo Mwana mwenyewe atatiishwa chini yake yeye aliyetiisha vitu vyote, ili Mungu awe yote katika yote.

  6. 1 Mtakapokwenda vitani kupigana na adui zenu na mkaona farasi na magari ya vita na jeshi kubwa kuliko lenu, msiwaogope, kwa sababu Bwana Mungu wenu aliyewatoa kutoka Misri, atakuwa pamoja nanyi. 2 Wakati mtakapokaribia kwenda vitani, kuhani atakuja mbele na kuhutubia jeshi. 3 Atasema: “Sikia, ee Israeli, leo unakwenda vitani kupigana na adui zako. Usife moyo wala usiogope, usitishwe wala usitiwe hofu mbele yao. 4 Kwa kuwa Bwana Mungu wenu ndiye huenda pamoja nanyi kuwapigania dhidi ya adui zenu na kuwapatia ushindi.”

  7. 13 Mlipokuwa wafu katika dhambi zenu na kutokutahiriwa katika asili yenu ya dhambi, Mungu aliwafanya mwe hai pamoja na Kristo. Alitusamehe dhambi zetu zote, 14 akiisha kuifuta ile hati yenye mashtaka yaliyokuwa yanatukabili, pamoja na maagizo yake. Aliiondoa isiwepo tena, akiigongomea kwenye msalaba wake. 15 Mungu akiisha kuzivua enzi na mamlaka, alizifanya kuwa kitu cha fedheha hadharani kwa kuziburura kwa ujasiri, akizishinda katika msalaba wa Kristo.

  8. 7 Basi palikuwa na vita mbinguni: Mikaeli na malaika zake wakapigana na hilo joka, nalo joka pamoja na malaika zake likapigana nao. 8 Lakini joka na malaika zake wakashindwa, na hapakuwa tena na nafasi yao huko mbinguni. 9 Lile joka kuu likatupwa chini, yule nyoka wa zamani aitwaye ibilisi au Shetani, aupotoshaye ulimwengu wote. Akatupwa chini duniani, yeye pamoja na malaika zake.

    10 Kisha nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema:

    “Sasa wokovu na uweza na Ufalme wa Mungu wetu umekuja

    na mamlaka ya Kristo wake.

    Kwa kuwa ametupwa chini

    mshtaki wa ndugu zetu,

    anayewashtaki mbele za Mungu

    usiku na mchana.

    11 Nao wakamshinda

    kwa damu ya Mwana-Kondoo

    na kwa neno la ushuhuda wao.

    Wala wao hawakuyapenda maisha yao

    hata kufa.

  9. 5 Kwa maana ikiwa tumeungana naye katika mauti yake, bila shaka tutaungana naye katika ufufuo wake. 6 Kwa maana twajua kwamba utu wetu wa kale ulisulubiwa pamoja naye ili ule mwili wa dhambi upate kuangamizwa, nasi tusiendelee kuwa tena watumwa wa dhambi. 7 Kwa maana mtu yeyote aliyekufa amehesabiwa haki mbali na dhambi.

    8 Basi ikiwa tulikufa pamoja na Kristo, tunaamini kwamba pia tutaishi pamoja naye. 9 Kwa maana tunajua kwamba Kristo, kwa sababu alifufuliwa kutoka kwa wafu, hawezi kufa tena; mauti haina tena mamlaka juu yake. 10 Kifo alichokufa, aliifia dhambi mara moja tu, lakini uzima alio nao anamwishia Mungu.

    11 Vivyo hivyo, jihesabuni wafu katika dhambi lakini mlio hai kwa Mungu katika Kristo Yesu. 12 Kwa hiyo, msiruhusu dhambi itawale ndani ya miili yenu, ipatikanayo na kufa, ili kuwafanya mzitii tamaa mbaya. 13 Wala msivitoe viungo vya miili yenu vitumike kama vyombo vya uovu vya kutenda dhambi, bali jitoeni kwa Mungu, kama watu waliotolewa kutoka mautini kuingia uzimani. Nanyi vitoeni viungo vya miili yenu kwake kama vyombo vya haki. 14 Kwa maana dhambi haitakuwa na mamlaka juu yenu, kwa sababu hampo chini ya sheria, bali chini ya neema.

  10. 10 Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. 11 Vaeni silaha zote za Mungu ili kwamba mweze kuzipinga hila za ibilisi. 12 Kwa maana kushindana kwetu si juu ya nyama na damu, bali dhidi ya falme, mamlaka, dhidi ya wakuu wa giza na majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. 13 Kwa hiyo vaeni silaha zote za Mungu ili mweze kushindana siku ya uovu itakapokuja nanyi mkiisha kufanya yote, simameni imara.

  11. 14 Kwa kuwa tunaye Kuhani Mkuu kuliko wote ambaye ameingia mbinguni, Yesu Mwana wa Mungu, basi na tushikamane sana kwa uthabiti na ule ukiri wa imani yetu. 15 Kwa kuwa hatuna Kuhani Mkuu asiyeweza kuchukuliana na sisi katika udhaifu wetu, lakini tunaye mmoja ambaye alijaribiwa kwa kila namna, kama vile sisi tujaribiwavyo: lakini yeye hakutenda dhambi. 16 Basi na tukikaribie kiti cha rehema kwa ujasiri, ili tupewe rehema na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.

  12. 24 Je, hamjui kwamba katika mashindano ya mbio wote wanaoshindana hukimbia, lakini ni mmoja wao tu apewaye tuzo? Kwa hiyo kimbieni katika mashindano kwa jinsi ambavyo mtapata tuzo.

    25 Kila mmoja anayeshiriki katika mashindano hufanya mazoezi makali. Wao hufanya hivyo ili wapokee taji isiyodumu, lakini sisi tunafanya hivyo ili kupata taji idumuyo milele. 26 Kwa hiyo mimi sikimbii kama mtu akimbiaye bila lengo, sipigani kama mtu anayepiga hewa, 27 la, bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha ili nikiisha kuwahubiria wengine, mimi nisiwe mtu wa kukataliwa.

  13. 7 Ili kunizuia nisijivune kwa sababu ya ufunuo huu mkuu, nilipewa mwiba katika mwili wangu, mjumbe wa Shetani, ili anitese. 8 Kwa habari ya jambo hili nilimsihi Bwana mara tatu aniondolee mwiba huu. 9 Lakini aliniambia, “Neema yangu inakutosha, kwa kuwa uweza wangu hukamilika katika udhaifu.” Kwa hiyo nitajisifu kwa furaha zaidi kuhusu udhaifu wangu, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. 10 Hii ndiyo sababu, kwa ajili ya Kristo, nafurahia udhaifu, katika kutukanwa, katika taabu, katika mateso na katika shida, kwa maana ninapokuwa dhaifu, ndipo nina nguvu.

  14. 4 Watoto wapendwa, ninyi mmetokana na Mungu, nanyi mmewashinda kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika ulimwengu.

  15. 45 Daudi akamwambia yule Mfilisti. “Wewe unanijia na upanga, mkuki na fumo, lakini mimi ninakujia kwa jina la Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa majeshi ya Israeli, ambaye wewe umemtukana. 46 Siku hii leo Bwana atakutia mkononi mwangu, nami nitakupiga na kukukata kichwa chako. Leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya jeshi la Wafilisti, nayo dunia yote itajua kuwa yuko Mungu katika Israeli. 47 Wale wote waliokusanyika hapa watajua kuwa Bwana haokoi kwa upanga wala kwa mkuki; kwa kuwa vita ni vya Bwana, naye atawatia wote mikononi mwetu.”

  16. 17 Wale sabini na wawili wakarudi kwa furaha, na kusema, “Bwana, hata pepo wachafu wanatutii kwa jina lako.”

    18 Yesu akawaambia, “Nilimwona Shetani akianguka kutoka mbinguni kama umeme wa radi. 19 Tazama nimewapa mamlaka ya kukanyaga nyoka na nge na juu ya nguvu zote za adui; wala hakuna kitu chochote kitakachowadhuru. 20 Basi, msifurahi kwa kuwa pepo wachafu wanawatii, bali furahini kwa kuwa majina yenu yameandikwa mbinguni.”

  17. 13 Naweza kuyafanya mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.

  18. 31 Tuseme nini basi kuhusu haya? Ikiwa Mungu yuko upande wetu, ni nani awezaye kuwa kinyume chetu?

  19. 3 Sio kwa upanga wao waliipata nchi,

    wala si mkono wao uliwapatia ushindi;

    ilikuwa ni kitanga cha mkono wako wa kuume,

    na nuru ya uso wako,

    kwa kuwa uliwapenda.

    4 Wewe ni mfalme wangu na Mungu wangu,

    unayeamuru ushindi kwa Yakobo.

    5 Kwa uwezo wako tunawasukuma nyuma watesi wetu;

    kwa jina lako tunawakanyaga adui zetu.

    6 Siutumaini upinde wangu,

    upanga wangu hauniletei ushindi;

    7 bali wewe unatupa ushindi juu ya adui zetu,

    unawaaibisha watesi wetu.

  20. 11 Tuletee msaada dhidi ya adui,

    kwa maana msaada wa mwanadamu haufai kitu.

    12 Kwa msaada wa Mungu tutapata ushindi,

    naye atawaponda adui zetu.

  21. 12 “Zile pembe kumi ulizoziona ni wafalme kumi ambao bado hawajapokea ufalme, lakini watapokea mamlaka kuwa wafalme kwa saa moja pamoja na yule mnyama. 13 Hawa wana nia moja, nao watamwachia yule mnyama nguvu zao na mamlaka yao. 14 Watafanya vita na Mwana-Kondoo, lakini Mwana-Kondoo atawashinda kwa sababu yeye ni Bwana wa mabwana na Mfalme wa wafalme. Yeye atakuwa pamoja na watu wake walioitwa ambao ni wateule wake na wafuasi wake waaminifu.”

  22. 31 Farasi huandaliwa kwa ajili ya siku ya vita,

    bali ushindi huwa kwa Bwana.

  23. 8 Yeye atendaye dhambi ni wa ibilisi, kwa sababu ibilisi amekuwa akitenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili aziangamize kazi za ibilisi.

  24. 6 Akaniambia, “Imekwisha kuwa. Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. Yeye aonaye kiu nitampa kunywa kutoka chemchemi ya maji ya uzima bila gharama yoyote. 7 Yeye ashindaye atayarithi haya yote, nami nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu.

  25. 13 Hakuna jaribu lolote lililowapata ambalo si la kawaida kwa wanadamu. Naye Mungu ni mwaminifu; hataruhusu mjaribiwe kupita mnavyoweza. Lakini mnapojaribiwa atawapa njia ya kutokea ili mweze kustahimili.

  26. 14 Lakini Mungu ashukuriwe, yeye ambaye siku zote hutufanya tuandamane kwa ushindi tukiwa ndani ya Kristo. Naye kupitia kwetu hueneza kila mahali harufu nzuri ya kumjua yeye.

  27. 13 Lakini ndugu, hatutaki mkose kujua kuhusu wale waliolala mauti, ili msihuzunike kama watu wengine wasiokuwa na tumaini. 14 Kwa kuwa tunaamini kwamba Yesu alikufa na kufufuka, na kwa hivyo, Mungu kwa njia ya Yesu atawafufua pamoja naye wale waliolala mautini ndani yake. 15 Kulingana na neno la Bwana mwenyewe, tunawaambia kwamba sisi ambao bado tuko hai, tuliobaki hadi kuja kwake Bwana, hakika hatutawatangulia waliolala mauti. 16 Kwa maana Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni, akitoa amri kwa sauti kuu, pamoja na sauti ya malaika mkuu, na sauti ya tarumbeta ya Mungu. Nao waliokufa wakiwa katika Kristo watafufuka kwanza. 17 Baada ya hilo sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu ili kumlaki Bwana hewani, hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele. 18 Kwa hiyo farijianeni kwa maneno haya.

  28. 41 Lakini Mose akasema, “Kwa nini hamtii amri ya Bwana? Jambo hili halitafanikiwa! 42 Msipande juu, kwa kuwa Bwana hayupo pamoja nanyi. Mtashindwa na adui zenu, 43 kwa kuwa Waamaleki na Wakanaani watapambana nanyi huko. Kwa sababu mmemwacha Bwana, hatakuwa pamoja nanyi, ninyi mtaanguka kwa upanga.”

  29. 2 Kisha Bwana akamwambia Yoshua, “Tazama, nimeitia Yeriko mikononi mwako, pamoja na mfalme wake na watu wake wa vita. 3 Zunguka mji mara moja pamoja na watu wote wenye silaha. Fanya hivi kwa siku sita. 4 Uwe na makuhani saba wakibeba mabaragumu ya pembe za kondoo dume mbele ya Sanduku. Siku ya saba, mzunguke mji mara saba, nao makuhani wakipiga baragumu hizo. 5 Utakapowasikia wamepaliza sauti kubwa ya baragumu, watu wote wapige kelele kwa sauti kuu, kisha ukuta wa mji utaanguka na watu watapanda, kila mtu akiendelea mbele.”

  30. 36 Wakati wa kutoa dhabihu ya jioni, nabii Eliya akasogea mbele na kuomba, akisema: “Ee Bwana, Mungu wa Abrahamu, na Isaki na Israeli, ijulikane leo kwamba wewe ndiye Mungu katika Israeli na ya kwamba mimi ni mtumishi wako na nimefanya mambo haya yote kwa neno lako. 37 Unijibu mimi, Ee Bwana, nijibu mimi, ili watu hawa wajue kwamba wewe, Ee Bwana, ndiwe Mungu, na kwamba unaigeuza mioyo yao ikurudie tena.”

    38 Kisha moto wa Bwana ukashuka na kuiteketeza ile dhabihu, zile kuni, yale mawe, ule udongo, na pia kuramba yale maji yaliyokuwa ndani ya handaki.

    39 Wakati watu wote walipoona hili, wakaanguka kifudifudi na kulia, “Bwana: yeye ndiye Mungu! Bwana: yeye ndiye Mungu!”

  31. 21 Hivyo naiona sheria ikitenda kazi. Ninapotaka kutenda jema, jambo baya liko papo hapo. 22 Kwa maana katika utu wangu wa ndani naifurahia sheria ya Mungu. 23 Lakini ninaona kuna sheria nyingine inayotenda kazi katika viungo vya mwili wangu inayopigana vita dhidi ya ile sheria ya akili yangu. Sheria hii inanifanya mateka wa ile sheria ya dhambi inayofanya kazi katika viungo vya mwili wangu.

    24 Ole wangu mimi maskini! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti?

    25 Ashukuriwe Mungu kwa njia ya Yesu Kristo Bwana wetu! Hivyo basi, mimi mwenyewe kwa akili zangu ni mtumwa wa sheria ya Mungu, lakini katika asili ya dhambi ni mtumwa wa sheria ya dhambi.

  32. 20 Mungu wa amani atamponda Shetani chini ya miguu yenu upesi.

    Neema ya Bwana wetu Yesu iwe nanyi. Amen.

  33. 7 Lakini tunayo hazina hii katika vyombo vya udongo, ili ijulikane wazi kwamba uwezo huu wa ajabu unatoka kwa Mungu wala si kwetu. 8 Twataabika kila upande lakini hatuangamizwi; twaona wasiwasi lakini hatukati tamaa; 9 twateswa lakini hatuachwi; twatupwa chini lakini hatupondwi. 10 Siku zote twachukua katika mwili kufa kwake Yesu ili kwamba uzima wa Yesu uweze kudhihirika katika miili yetu. 11 Kwa maana sisi tulio hai siku zote tumetolewa tufe kwa ajili ya Yesu, ili kwamba uzima wake upate kudhihirishwa katika mwili wetu upatikanao na mauti. 12 Hivyo basi, mauti inatenda kazi ndani yetu, bali uzima unatenda kazi ndani yenu.

  34. 12 Heri mtu anayevumilia wakati wa majaribu, kwa sababu akiisha kushinda hilo jaribio atapewa taji la uzima Mungu alilowaahidia wale wampendao.

  35. 1 Ndipo Mose na Waisraeli wakamwimbia Bwana wimbo huu:

    “Nitamwimbia Bwana,

    kwa kuwa ametukuzwa sana.

    Farasi na mpanda farasi

    amewatosa baharini.

  36. 20 “Tazama, ninamtuma malaika akutangulie mbele yako akulinde njiani na kukuleta mpaka mahali nilipoandaa. 21 Mtamtii na kusikiliza kile anachokisema. Usiasi dhidi yake; hatakusamehe uasi wako, kwa maana Jina langu limo ndani yake. 22 Kama ukitii kweli kweli kile asemacho na kufanya yote nisemayo, nitakuwa adui wa adui zako, na nitawapinga wale wakupingao. 23 Malaika wangu atatangulia mbele yako na kukuleta katika nchi ya Waamori, Wahiti, Waperizi, Wakanaani, Wahivi na Wayebusi, nami nitawafutilia mbali.

  37. 11 Ukuu na uweza, ni vyako, Ee Bwana,

    na utukufu na enzi na uzuri,

    kwa kuwa kila kilichoko mbinguni na duniani

    ni chako wewe.

    Ee Bwana, ufalme ni wako;

    umetukuzwa kuwa mkuu juu ya yote.

  38. 25 Yesu akamwambia, “Mimi ndiye huo ufufuo na uzima. Yeye aniaminiye mimi, hata akifa atakuwa anaishi 26 na yeyote aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je, unasadiki haya?”

  39. 35 Hunipa ngao yako ya ushindi,

    nao mkono wako wa kuume hunitegemeza,

    unajishusha chini ili kuniinua.

  40. 28 Nasi tunajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hutenda kazi pamoja na wote wampendao, katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.

  41. 7 Nimevipiga vita vizuri, mashindano nimeyamaliza, imani nimeilinda. 8 Sasa nimewekewa taji ya haki ambayo Bwana, mwamuzi wa haki, atanitunukia siku ile: wala si mimi tu, bali pia wote ambao wamengoja kwa shauku kudhihirishwa kwake.

  42. 13 Ndipo utakapofanikiwa, ikiwa utakuwa na bidii kutii amri na sheria Bwana alizompa Mose kwa ajili ya Israeli. Uwe hodari na ushujaa. Usiogope wala usikate tamaa.

  43. 20 Ndipo Roho wa Bwana akaja juu ya Zekaria mwana wa Yehoyada kuhani. Akasimama mbele ya watu akasema, “Hili ndilo asemalo Mungu, ‘Kwa nini mnakataa kuzitii amri za Bwana? Hamtafanikiwa kwa kuwa mmemwacha Bwana, yeye naye amewaacha ninyi.’ ”

  44. 7 Wengine wanatumaini magari ya vita, na wengine farasi,

    bali sisi tutalitumainia jina la Bwana, Mungu wetu.

  45. 8 Moyo wake ni salama, hatakuwa na hofu,

    mwishoni ataona ushindi dhidi ya adui zake.

  46. 3 Usiweke tumaini lako kwa wakuu,

    kwa wanadamu ambao hufa,

    ambao hawawezi kuokoa.

  47. 14 Nakaza mwendo nifikie ile alama ya ushindi iliyowekwa ili nipate tuzo ya mwito mkuu wa Mungu ambao nimeitiwa huko juu mbinguni katika Kristo Yesu.

  48. 6 Msijisumbue kwa jambo lolote, bali katika kila jambo kwa kuomba na kusihi pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. 7 Nayo amani ya Mungu, inayopita fahamu zote, itailinda mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.

  49. 6 Kwa hiyo tunaweza kusema kwa ujasiri,

    “Bwana ni msaada wangu; sitaogopa.

    Mwanadamu anaweza kunitenda nini?”

  50. 17 Nilipomwona, nilianguka miguuni pake kama aliyekufa. Ndipo akauweka mkono wake wa kuume juu yangu na kusema: “Usiogope, Mimi ndiye wa Kwanza na wa Mwisho. 18 Mimi ni Yeye Aliye Hai, niliyekuwa nimekufa, na tazama, ni hai milele na milele! Nami ninazo funguo za mauti na kuzimu.

  51. 8 Waamaleki wakaja na kuwashambulia Waisraeli huko Refidimu. 9 Mose akamwambia Yoshua, “Chagua baadhi ya watu wetu na uende kupigana na Waamaleki. Kesho nitasimama juu ya kilima nikiwa na fimbo ya Mungu mkononi mwangu.”

    10 Kwa hiyo Yoshua akapigana na Waamaleki kama Mose alivyomwagiza, nao Mose, Aroni na Huri wakapanda juu ya kilima. 11 Ikawa wakati wote Mose alipokuwa amenyanyua mikono yake, Waisraeli walikuwa wakishinda, lakini kila aliposhusha mikono yake Waamaleki walishinda. 12 Mikono ya Mose ilipochoka, wakachukua jiwe na kumpa alikalie. Aroni na Huri wakaishikilia juu mikono ya Mose, mmoja upande huu na mwingine upande huu. Wakaitegemeza mikono yake ikabaki thabiti mpaka jua lilipozama. 13 Kwa hiyo Yoshua akalishinda jeshi la Waamaleki kwa upanga.

  52. 8 Bwana akamwambia Yoshua, “Usiwaogope watu hao, nimewatia mkononi mwako. Hakuna yeyote atakayeweza kushindana nawe.”

  53. 8 yeye atameza mauti milele.

    Bwana Mwenyezi atafuta machozi katika nyuso zote;

    ataondoa aibu ya watu wake duniani kote.

    Bwana amesema hili.

  54. 13 Usitutie majaribuni,

    bali utuokoe kutoka kwa yule mwovu

    [kwa kuwa Ufalme ni wako, na nguvu,

    na utukufu, hata milele. Amen].’

  55. 23 Wakati huo huo katika sinagogi lao palikuwa na mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu, 24 naye akapiga kelele akisema, “Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Ninakujua wewe ni nani. Wewe ndiwe Aliye Mtakatifu wa Mungu!”

    25 Lakini Yesu akamkemea, akamwambia, “Nyamaza kimya! Nawe umtoke!” 26 Yule pepo mchafu akamtikisatikisa huyo mtu kwa nguvu, kisha akamtoka akipiga kelele kwa sauti kubwa.

    27 Watu wote wakashangaa, hata wakaulizana wao kwa wao, “Haya ni mambo gani? Ni mafundisho mapya, tena yenye mamlaka! Anaamuru hata pepo wachafu, nao wanamtii!”

  56. 33 Ndani ya sinagogi palikuwa na mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu. Naye akapiga kelele kwa nguvu akisema, 34 “Tuache! Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Ninakujua wewe ni nani. Wewe ndiwe Aliye Mtakatifu wa Mungu!”

    35 Basi Yesu akamkemea yule pepo mchafu, akisema, “Nyamaza kimya! Nawe umtoke!” Yule pepo mchafu akamwangusha yule mtu chini mbele yao wote, akatoka pasipo kumdhuru. 36 Watu wote wakashangaa, wakaambiana, “Mafundisho haya ni ya namna gani? Anawaamuru pepo wachafu kwa mamlaka na nguvu, nao wanatoka!”

  57. 20 Zaidi ya hayo, sheria ilikuja, ili uvunjaji wa sheria uongezeke. Lakini dhambi ilipoongezeka, neema iliongezeka zaidi, 21 ili kwamba kama vile dhambi ilivyotawala kwa njia ya mauti, vivyo hivyo neema iweze kutawala kwa njia ya kuhesabiwa haki hata kuleta uzima wa milele katika Yesu Kristo Bwana wetu.

  58. 11 Kwa maana neema ya Mungu ambayo inawaokoa wanadamu wote imefunuliwa. 12 Nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia, ili tupate kuishi maisha ya kiasi, ya haki na ya utaua katika ulimwengu huu wa sasa, 13 huku tukilitazamia tumaini lenye baraka na ufunuo wa utukufu wa Mungu wetu Mkuu, aliye Mwokozi wetu Yesu Kristo. 14 Ndiye alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, ili atukomboe kutoka uovu wote na kujisafishia watu kuwa mali yake Mwenyewe, yaani, wale walio na juhudi katika kutenda mema.

  59. 1 Yakobo, mtumwa wa Mungu na wa Bwana Yesu Kristo:

    Kwa makabila kumi na mawili yaliyotawanyika ulimwenguni:

    Salamu.

    2 Ndugu zangu, hesabuni kuwa ni furaha tupu mnapopatwa na majaribu mbalimbali, 3 kwa sababu mnajua ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi. 4 Saburi na iwe na kazi timilifu, ili mpate kuwa wakamilifu, mmekamilishwa, bila kupungukiwa na kitu chochote. 5 Kama mtu yeyote miongoni mwenu amepungukiwa na hekima na amwombe Mungu, yeye awapaye watu wote kwa ukarimu wala hana kinyongo, naye atapewa.

  60. 9 Lakini ninyi ni taifa teule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu walio milki ya Mungu, mlioitwa ili kutangaza sifa zake yeye aliyewaita kutoka gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu.

  61. 1 Simoni Petro, mtumishi na mtume wa Yesu Kristo:

    Kwa wale ambao kwa njia ya haki ya Mungu na Mwokozi wetu Yesu Kristo mmepokea imani iliyo na thamani kama yetu:

    2 Neema na amani iwe kwenu kwa wingi katika kumjua Mungu na Yesu Bwana wetu.

    3 Uweza wake wa uungu umetupatia mambo yote tunayohitaji kwa ajili ya uzima na uchaji wa Mungu, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe. 4 Kwa sababu hiyo, ametukirimia ahadi zake kuu na za thamani kupitia mambo haya, ili kupitia hayo mpate kuwa washiriki wa asili ya uungu, na kuokoka kutoka upotovu ulioko duniani unaosababishwa na tamaa mbaya.

  62. 2 Nikaona kile kilichoonekana kama bahari ya kioo iliyochanganyikana na moto. Kando ya hiyo bahari, walikuwa wamesimama wale watu waliomshinda yule mnyama na sanamu yake pamoja na tarakimu ya jina lake. Mikononi mwao walikuwa wameshika vinubi walivyopewa na Mungu.