75 Bible Verses About Vanity
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
-
1 Maneno ya Mhubiri, mwana wa Daudi, mfalme huko Yerusalemu:
2 “Ubatili mtupu! Ubatili mtupu!”
Mhubiri anasema.
“Ubatili mtupu!
Kila kitu ni ubatili.”
3 Mwanadamu anafaidi nini kutokana na kazi yake yote
anayotaabikia chini ya jua?
4 Vizazi huja na vizazi hupita,
lakini dunia inadumu milele.
5 Jua huchomoza na jua huzama,
nalo huharakisha kurudi mawioni.
6 Upepo huvuma kuelekea kusini
na kugeukia kaskazini,
hurudia mzunguko huo huo,
daima ukirudia njia yake.
7 Mito yote hutiririka baharini,
hata hivyo bahari kamwe haijai.
Mahali mito inapotoka,
huko hurudi tena.
8 Vitu vyote vinachosha,
zaidi kuliko mtu anavyoweza kusema.
Jicho kamwe halitosheki kutazama,
wala sikio halishibi kusikia.
9 Kile kilichokuwepo kitakuwepo tena,
kile kilichofanyika kitafanyika tena,
hakuna kilicho kipya chini ya jua.
10 Kuna kitu chochote ambacho mtu anaweza kusema,
“Tazama! Kitu hiki ni kipya”?
Kilikuwepo tangu zamani za kale,
kilikuwepo kabla ya wakati wetu.
11 Hakuna kumbukumbu ya watu wa zamani,
hata na wale ambao hawajaja bado
hawatakumbukwa
na wale watakaofuata baadaye.
-
12 Mimi, Mhubiri, nilikuwa mfalme wa Israeli katika Yerusalemu. 13 Nilitumia muda wangu wote kujifunza na kuvumbua kwa hekima yote yanayofanyika chini ya mbingu. Jinsi gani Mungu ameweka mzigo mzito juu ya wanadamu! 14 Nimeshaona mambo yote yanayotendeka chini ya jua, hayo yote ni ubatili, hii ni kukimbiza upepo.
15 Kilichopindika hakiwezi kunyooshwa,
kile ambacho hakipo haiwezekani kukihesabu.
16 Niliwaza mwenyewe, “Tazama, nimekua na kuongezeka katika hekima kuliko yeyote aliyewahi kutawala Yerusalemu kabla yangu. Nimekuwa na uzoefu mkubwa wa hekima na maarifa.” 17 Ndipo nilipojitahidi kufahamu kutofautisha hekima, wazimu na upumbavu, lakini nikatambua hata hili nalo ni kukimbiza upepo.
18 Kwa kuwa hekima nyingi huleta huzuni kubwa;
maarifa yanapoongezeka, masikitiko yanaongezeka.
-
1 Nikafikiri moyoni mwangu, “Haya basi, nitakujaribu kwa anasa nione ni lipi lililo jema.” Lakini hilo nalo likaonekana ni ubatili. 2 Nikasema, “Kicheko nacho ni upumbavu. Nayo matokeo ya anasa ni nini?” 3 Nikajaribu kujifurahisha kwa mvinyo na kukumbatia upumbavu, huku bado akili yangu inaniongoza kwa hekima. Nilitaka kuona ni lipi bora watu wafanye kwa siku chache wanazoishi chini ya mbingu.
4 Nikafanya miradi mikubwa: Nikajijengea majumba na kulima mashamba ya mizabibu. 5 Nikatengeneza bustani na viwanja vya starehe nikaotesha huko kila aina ya miti ya matunda. 6 Nikajenga mabwawa ya kukusanya maji ya kunyweshea hii miti iliyokuwa inastawi vizuri. 7 Nikanunua watumwa wa kiume na wa kike na watumwa wengine walizaliwa nyumbani mwangu. Pia nilikuwa na makundi ya ngʼombe, kondoo na mbuzi kuliko mtu yeyote aliyewahi kuishi Yerusalemu kabla yangu. 8 Nikajikusanyia fedha na dhahabu, hazina za wafalme na za majimbo. Nikajipatia waimbaji wanaume na wanawake, nazo nyumba za masuria: vitu ambavyo moyo wa mwanadamu hufurahia. 9 Nikawa maarufu sana kuliko mtu mwingine yeyote aliyepata kuishi Yerusalemu kabla yangu. Katika haya yote bado nikawa nina hekima.
10 Sikujinyima kitu chochote ambacho macho yangu yalikitamani,
hakuna anasa ambayo niliunyima moyo wangu.
Moyo wangu ulifurahia kazi zangu zote,
hii ilikuwa thawabu ya kazi zangu zote.
11 Hata hivyo nilipokuja kuangalia yote ambayo
mikono yangu ilikuwa imefanya
na yale niliyotaabika kukamilisha,
kila kitu kilikuwa ni ubatili, ni kukimbiza upepo;
hapakuwa na faida yoyote chini ya jua.
-
12 Kisha nikageuza mawazo yangu kufikiria hekima,
wazimu na upumbavu.
Ni nini zaidi mtu anayetawala baada ya mfalme
anachoweza kufanya ambacho hakijafanywa?
13 Nikaona kuwa hekima ni bora kuliko upumbavu,
kama vile nuru ilivyo bora kuliko giza.
14 Mtu mwenye hekima ana macho katika kichwa chake,
lakini mpumbavu anatembea gizani;
lakini nikaja kuona kwamba
wote wawili hatima yao inafanana.
15 Kisha nikafikiri moyoni mwangu,
“Hatima ya mpumbavu itanipata mimi pia.
Nitafaidi nini basi kwa kuwa na hekima?”
Nikasema moyoni mwangu,
“Hili nalo ni ubatili.”
16 Kwa maana kwa mtu mwenye hekima,
kama ilivyo kwa mpumbavu,
hatakumbukwa kwa muda mrefu,
katika siku zijazo wote watasahaulika.
Kama vile ilivyo kwa mpumbavu,
mtu mwenye hekima pia lazima atakufa!
17 Kwa hiyo nikachukia maisha, kwa sababu kazi inayofanyika chini ya jua ilikuwa masikitiko kwangu. Yote hayo ni ubatili, ni kukimbiza upepo. 18 Nikachukia kila kitu nilichokuwa nimetaabikia chini ya jua, kwa sababu ni lazima nimwachie yule ajaye baada yangu. 19 Nani ajuaye kama atakuwa ni mtu mwenye hekima au mpumbavu? Lakini hata hivyo yeye ndiye atakayetawala kazi zote ambazo nimemiminia juhudi na ustadi chini ya jua. Hili nalo ni ubatili. 20 Kwa hiyo moyo wangu ukaanza kukata tamaa juu ya kazi yangu yote niliyoifanya kwa taabu chini ya jua. 21 Kwa kuwa mtu anaweza kufanya kazi yake kwa hekima, maarifa na ustadi, kisha analazimika kuacha vyote alivyo navyo kwa mtu mwingine ambaye hajavifanyia kazi. Hili nalo pia ni ubatili tena ni balaa kubwa. 22 Mtu atapata nini kwa taabu yote na kuhangaika kwa bidii katika kazi anayotaabikia chini ya jua? 23 Siku zake zote kazi yake ni maumivu na masikitiko, hata usiku akili yake haipati mapumziko. Hili nalo pia ni ubatili.
24 Hakuna kitu bora anachoweza kufanya mtu zaidi ya kula na kunywa na kuridhika katika kazi yake. Hili nalo pia, ninaona, latokana na mkono wa Mungu, 25 kwa sababu pasipo yeye, ni nani awezaye kula na kufurahi? 26 Kwa yule mtu anayempendeza Mungu, Mungu humpa hekima, maarifa na furaha, bali kwa mwenye dhambi Mungu humpa kazi ya kukusanya na kuhifadhi utajiri ili Mungu ampe yule anayempenda. Hili nalo pia ni ubatili, ni kukimbiza upepo.
-
1 Nikatazama tena nikaona uonevu wote uliokuwa unafanyika chini ya jua:
Nikaona machozi ya walioonewa,
wala hawana wa kuwafariji;
uwezo ulikuwa upande wa wale wanaowaonea,
wala hawana wa kuwafariji.
2 Nami nikasema kwamba wafu,
waliokwisha kufa,
wana furaha kuliko watu walio hai,
ambao bado wanaishi.
3 Lakini aliye bora kuliko hao wawili
ni yule ambaye hajazaliwa bado,
ambaye hajaona ule uovu
unaofanyika chini ya jua.
4 Tena nikaona kuwa kazi zote na mafanikio yote huchipuka kutokana na wivu wa mtu kwa jirani yake. Hili nalo ni ubatili, ni kukimbiza upepo.
5 Mpumbavu hukunja mikono yake
na kujiangamiza mwenyewe.
6 Afadhali konzi moja pamoja
na utulivu kuliko konzi mbili pamoja na taabu
na kukimbiza upepo.
7 Tena nikaona kitu kingine kilicho ubatili chini ya jua:
8 Kulikuwepo mwanadamu aliye peke yake,
hakuwa na mwana wala ndugu.
Hapakuwa na mwisho wa kazi yake,
hata hivyo macho yake
hayakutosheka na utajiri wake.
Aliuliza, “Ninajitaabisha hivi kwa ajili ya nani,
nami kwa nini ninajinyima kufurahia?”
Hili pia ni ubatili,
ni shughuli yenye taabu!
-
7 Nuru ni tamu,
tena inafurahisha macho kuona jua.
8 Hata kama mtu ataishi miaka mingi kiasi gani,
na aifurahie yote.
Lakini na akumbuke siku za giza,
kwa maana zitakuwa nyingi.
Kila kitu kitakachokuja ni ubatili.
9 Furahi ewe kijana, wakati ungali kijana,
moyo wako na ukupe furaha
katika siku za ujana wako.
Fuata njia za moyo wako
na chochote macho yako yaonayo,
lakini ujue kwamba kwa ajili ya haya yote
Mungu atakuleta hukumuni.
10 Kwa hiyo basi, ondoa wasiwasi moyoni mwako
na utupilie mbali masumbufu ya mwili wako,
kwa kuwa ujana na nguvu ni ubatili.
-
4 “Ee Bwana, nijulishe mwisho wa maisha yangu
na hesabu ya siku zangu;
nijalie kujua jinsi maisha yangu
yanavyopita upesi.
5 Umefanya maisha yangu mafupi kama pumzi;
muda wangu wa kuishi ni kama
hauna thamani kwako.
Maisha ya kila mwanadamu
ni kama pumzi.
6 Hakika kila binadamu ni kama njozi
aendapo huku na huko:
hujishughulisha na mengi lakini ni ubatili;
anakusanya mali nyingi,
wala hajui ni nani atakayeifaidi.
-
18 Nayahesabu mateso yetu ya wakati huu kuwa si kitu kulinganisha na utukufu utakaodhihirishwa kwetu. 19 Kwa maana viumbe vyote vinangoja kwa shauku kudhihirishwa kwa watoto wa Mungu. 20 Kwa kuwa viumbe vyote viliwekwa chini ya ubatili, si kwa chaguo lao, bali kwa mapenzi yake yeye aliyevitiisha katika tumaini, 21 ili kwamba viumbe vyote vipate kuwekwa huru kutoka kwa utumwa wa kuharibika na kupewa uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu.
22 Kwa maana twajua ya kuwa hata sasa viumbe vyote vimekuwa vikilia kwa maumivu kama utungu wa mwanamke wakati wa kuzaa. 23 Wala si hivyo viumbe peke yao, bali hata sisi ambao ndio matunda ya kwanza ya Roho, kwa ndani tunalia kwa uchungu tukisubiri kwa shauku kufanywa wana wa Mungu, yaani, ukombozi wa miili yetu.
-
1 Mkumbuke Muumba wako
siku za ujana wako,
kabla hazijaja siku za taabu,
wala haijakaribia miaka utakaposema,
“Mimi sifurahii hiyo”:
2 kabla jua na nuru,
nao mwezi na nyota havijatiwa giza,
kabla ya kurudi mawingu baada ya mvua;
3 siku ile walinzi wa nyumba watakapotetemeka,
nao watu wenye nguvu watakapojiinamisha,
wakati wasagao watakapokoma kwa sababu ya uchache,
nao wachunguliao madirishani kutiwa giza;
4 wakati milango ya kuingia barabarani itakapofungwa
na sauti ya kusaga kufifia;
wakati watu wataamshwa kwa sauti ya ndege,
lakini nyimbo zao zote zikififia;
5 wakati watu watakapoogopa kilichoinuka juu
na hatari zitakazokuwepo barabarani;
wakati mlozi utakapochanua maua
na panzi kujikokota
nawe usiwe na shauku ya kitu chochote.
Ndipo mwanadamu aiendea nyumba yake ya milele
nao waombolezaji wakizunguka barabarani.
6 Mkumbuke Muumba wako: kabla haijakatika kamba ya fedha,
au bakuli la dhahabu halijavunjika;
kabla mtungi kuvunjika kwenye chemchemi,
au gurudumu kuvunjika kisimani,
7 nayo mavumbi kurudi ardhini yalikotoka,
na roho kurudi kwa Mungu aliyeitoa.
8 Mhubiri asema, “Ubatili! Ubatili!
Kila kitu ni ubatili!”
9 Mhubiri hakuwa tu na hekima, bali aliwagawia watu maarifa pia. Alitafakari na kutafiti na akaweka katika utaratibu mithali nyingi. 10 Mhubiri alitafiti ili kupata maneno sahihi na kila alichoandika kilikuwa sawa na kweli.
11 Maneno ya wenye hekima ni kama mchokoro, mithali zao zilizokusanywa pamoja ni kama misumari iliyogongomewa ikawa imara, yaliyotolewa na Mchungaji mmoja. 12 Tena zaidi ya hayo, mwanangu, kubali maonyo, hakuna mwisho wa kutunga vitabu vingi, nako kusoma sana huuchosha mwili.
13 Hii ndiyo jumla ya maneno;
yote yamekwisha sikiwa:
Mche Mungu, nawe uzishike amri zake,
maana kwa jumla ndiyo impasayo mtu.
14 Kwa maana Mungu ataleta hukumuni kila kazi,
pamoja na kila neno la siri,
likiwa jema au baya.
-
1 Nimeona ubaya mwingine chini ya jua, nao unalemea sana wanadamu: 2 Mungu humpa mwanadamu utajiri, mali na heshima, hivyo hakukosa chochote moyo wake unachokitamani. Lakini Mungu hamwezeshi kuvifurahia, badala yake mgeni ndiye anayevifurahia. Hili ni ubatili, ni ubaya unaosikitisha.
3 Mtu anaweza kuwa na watoto mia moja naye akaishi miaka mingi, lakini haidhuru kuwa ataishi muda mrefu kiasi gani, kama hawezi kufurahia mafanikio yake na kwamba hapati mazishi ya heshima, ninasema afadhali mtoto aliyezaliwa akiwa amekufa kuliko yeye. 4 Kuzaliwa kwake hakuna maana, huondokea gizani na gizani jina lake hufunikwa. 5 Ingawa hakuwahi kuliona jua wala kujua kitu chochote, yeye ana pumziko zaidi kuliko mtu huyo, 6 Hata kama huyo mtu ataishi miaka elfu mara mbili na zaidi, lakini akashindwa kufurahia mafanikio yake, je, wote hawaendi sehemu moja?
7 Juhudi zote za binadamu ni kwa ajili ya kinywa chake,
hata hivyo hamu yake kamwe haitoshelezwi.
8 Mtu mwenye hekima ana faida gani
zaidi ya mpumbavu?
Mtu maskini anapata faida gani
kwa kujua jinsi ya kujistahi
mbele ya watu wengine?
9 Ni bora kile ambacho jicho linakiona
kuliko hamu isiyotoshelezwa.
Hili nalo ni ubatili,
ni kukimbiza upepo.
10 Lolote lililopo limekwisha kupewa jina,
naye mwanadamu alivyo ameshajulikana;
hakuna mtu awezaye kushindana
na mwenye nguvu kuliko yeye.
11 Maneno yanavyokuwa mengi,
ndivyo yanavyokosa maana,
Je, hilo linamfaidia vipi yeyote?
12 Kwa maana ni nani anayejua lililo jema kwa ajili ya maisha ya mwanadamu, katika siku chache na za ubatili anazopita kama kivuli? Ni nani awezaye kumwambia yatakayotokea chini ya jua baada ya yeye kuondoka?
-
10 Yeyote apendaye fedha kamwe
hatosheki na fedha;
yeyote apendaye utajiri kamwe
hatosheki na kipato chake.
Hili nalo pia ni ubatili.
-
11 Unakemea na kuadhibu wanadamu
kwa ajili ya dhambi zao;
unaharibu utajiri wao kama nondo aharibuvyo:
kila mwanadamu ni kama pumzi tu.
-
30 Kujipamba ili kuvutia ni udanganyifu na uzuri unapita upesi,
bali mwanamke anayemcha Bwana atasifiwa.
-
17 Hivyo nawaambia hivi, nami nasisitiza katika Bwana kwamba, msiishi tena kama watu wa Mataifa waishivyo, katika ubatili wa mawazo yao. 18 Watu hao akili zao zimetiwa giza na wametengwa mbali na uzima wa Mungu kwa sababu ya ujinga wao kutokana na ugumu wa mioyo yao.
-
3 Ee Bwana, mwanadamu ni nini hata umjali,
Binadamu ni nini hata umfikirie?
4 Mwanadamu ni kama pumzi,
siku zake ni kama kivuli kinachopita.
-
15 Walizikataa amri zake, na agano alilokuwa amelifanya na baba zao, na maonyo aliyokuwa amewapa. Wakafuata sanamu zisizofaa, nao wenyewe wakawa hawafai. Wakayaiga mataifa yaliyowazunguka, ingawa Bwana alikuwa amewaonya akiwaambia, “Msifanye kama wanavyofanya,” nao wakafanya mambo ambayo Bwana alikuwa amewakataza wasifanye.
-
37 Geuza macho yangu kutoka kwenye mambo yasiyofaa,
uyahifadhi maisha yangu sawasawa na neno lako.
-
11 Fedha isiyo ya halali hupungua,
bali yeye akusanyaye fedha kidogo kidogo huongezeka.
12 Kilichotarajiwa kikikawia kuja moyo huugua,
bali tumaini lililotimizwa ni mti wa uzima.
-
5 Hivi ndivyo asemavyo Bwana:
“Je, baba zenu waliona kosa gani kwangu,
hata wakatangatanga mbali nami hivyo?
Walifuata sanamu zisizofaa,
nao wenyewe wakawa hawafai.
-
17 Watu hawa ni chemchemi zisizo na maji, na ukungu upeperushwao na tufani. Giza nene limewekwa tayari kwa ajili yao. 18 Kwa maana wao hunena maneno makuu mno ya kiburi cha bure, na kwa kuvutia tamaa mbaya za asili ya mwili, huwashawishi watu ambao ndipo tu wamejiondoa miongoni mwa wale wanaoishi katika ufisadi. 19 Huwaahidi uhuru hao waliowanasa, wakati wao wenyewe ni watumwa wa ufisadi: kwa maana mtu ni mtumwa wa kitu chochote kinachomtawala. 20 Kama wameukimbia upotovu wa dunia kwa kumjua Bwana wetu na Mwokozi Yesu Kristo, kisha wakanaswa tena humo na kushindwa, hali yao ya mwisho ni mbaya zaidi kuliko ile ya kwanza. 21 Ingelikuwa afadhali kwao kama wasingeliijua kamwe njia ya haki, kuliko kuijua kisha wakaiacha ile amri takatifu waliyokabidhiwa. 22 Imetukia kwao sawasawa na ile mithali ya kweli isemayo: “Mbwa huyarudia matapiko yake mwenyewe,” tena, “Nguruwe aliyeoshwa hurudi kugaagaa matopeni.”
-
2 Enyi watu, mtabadilisha utukufu wangu
kuwa aibu mpaka lini?
Mtapenda udanganyifu
na kufuata miungu ya uongo mpaka lini?
-
8 Sikizeni, enyi wajinga miongoni mwa watu;
enyi wapumbavu, lini mtakuwa na hekima?
9 Je, aliyeweka sikio asisikie?
Aliyeumba jicho asione?
10 Je, anayeadhibisha mataifa asiadhibu?
Je, awafundishaye wanadamu asiwe na maarifa?
11 Bwana anajua mawazo ya mwanadamu;
anajua kwamba ni ubatili.
-
8 Uutenge mbali nami udanganyifu na uongo;
usinipe umaskini wala utajiri,
bali unipe chakula cha kunitosha kila siku.
-
19 Ee Bwana, nguvu zangu na ngome yangu,
kimbilio langu wakati wa taabu,
kwako mataifa yatakujia
kutoka miisho ya dunia na kusema,
“Baba zetu hawakuwa na chochote zaidi ya miungu ya uongo,
sanamu zisizofaa kitu
ambazo hazikuwafaidia lolote.
-
16 Ninayachukia maisha yangu; nisingetamani kuendelea kuishi.
Niache; siku zangu ni ubatili.
-
7 Kinywa chake kimejaa laana, uongo na vitisho;
shida na ubaya viko chini ya ulimi wake.
-
6 Ninawachukia wale wanaongʼangʼania sanamu batili;
mimi ninamtumaini Bwana.
-
16 Hapakuwa na kikomo cha watu wote aliowatawala. Lakini wale waliokuja baadaye hawakufurahia kazi ya yule aliyepokea ufalme. Hili nalo pia ni ubatili, ni kukimbiza upepo.
-
9 Wote wachongao sanamu ni ubatili,
navyo vitu wanavyovithamini havifai kitu.
Wale ambao wanazitetea ni vipofu,
ni wajinga, nao waaibika.
10 Ni nani atengenezaye mungu na kusubu sanamu,
ambayo haiwezi kumfaidia kitu chochote?
11 Yeye pamoja na wenziwe wa aina yake wataaibishwa,
mafundi wao si kitu ila ni wanadamu tu.
Wote wakusanyike pamoja na kuwa na msimamo wao,
watashushwa chini kwa hofu na kwa fedheha.
-
6 Kila anapokuja mtu kunitazama,
huzungumza uongo,
huku moyo wake hukusanya masingizio;
kisha huondoka na kuyasambaza huku na huko.
-
9 Binadamu wa ngazi ya chini ni pumzi tu,
nao wa ngazi ya juu ni uongo tu;
wakipimwa kwenye mizani, si chochote;
wote kwa pamoja ni pumzi tu.
-
33 Kwa hiyo akamaliza siku zao katika ubatili
na miaka yao katika vitisho.
-
6 Mali iliyopatikana kwa ulimi wa uongo
ni mvuke upitao upesi na mtego wa kufisha.
-
13 Utakapolia kwa kuhitaji msaada,
sanamu zako ulizojikusanyia na zikuokoe!
Upepo utazipeperusha zote,
pumzi peke yake itazipeperusha,
Lakini mtu atakayenifanya kimbilio lake,
atairithi nchi
na kuumiliki mlima wangu mtakatifu.”
-
6 Watu wengine wamepotoka kutoka haya na kugeukia majadiliano yasiyo na maana kwa kuwa, 7 wanataka kuwa walimu wa sheria, lakini hawajui mambo yale wanayosema wala hayo wanayoyatumainia kwa uthabiti.
-
31 Asijidanganye mwenyewe kutumainia ubatili,
kwa kuwa hatapata malipo yoyote.
-
1 Kwa nini mataifa wanashauriana kufanya mabaya,
na kabila za watu kula njama bure?
-
7 Nenda, kula chakula chako kwa furaha, unywe divai yako kwa moyo wa shangwe, kwa maana sasa Mungu anakubali unachofanya. 8 Daima uvae nguo nyeupe na daima upake kichwa chako mafuta. 9 Furahia maisha na mke wako, umpendaye, siku zote za maisha ya ubatili uliyopewa na Mungu chini ya jua, siku zote za ubatili. Kwa maana hili ndilo fungu lako katika maisha na katika kazi yako ya taabu chini ya jua. 10 Lolote mkono wako upatalo kufanya, fanya kwa nguvu zako zote, kwa kuwa huko kuzimu, unakokwenda, hakuna kufanya kazi wala mipango wala maarifa wala hekima.
-
29 Tazama, wote ni ubatili!
Matendo yao ni bure;
vinyago vyao ni upepo mtupu na machafuko.
-
18 Ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni dhidi ya uasi wote na uovu wa wanadamu ambao huipinga kweli kwa uovu wao, 19 kwa maana yote yanayoweza kujulikana kumhusu Mungu ni dhahiri kwao, kwa sababu Mungu mwenyewe ameyadhihirisha kwao. 20 Kwa maana tangu kuumbwa kwa ulimwengu, asili ya Mungu asiyeonekana kwa macho, yaani, uweza wake wa milele na asili yake ya Uungu, imeonekana waziwazi, ikitambuliwa kutokana na yale aliyoyafanya ili wanadamu wasiwe na udhuru.
21 Kwa maana ingawa walimjua Mungu, hawakumtukuza yeye kama ndiye Mungu wala hawakumshukuru, bali fikira zao zimekuwa batili na mioyo yao ya ujinga ikatiwa giza. 22 Ingawa walijidai kuwa wenye hekima, wakawa wajinga 23 na kubadili utukufu wa Mungu aishiye milele kwa sanamu zilizofanywa zifanane na mwanadamu ambaye hufa, na mfano wa ndege, wanyama na viumbe vitambaavyo.
-
8 Kwa maana mazoezi ya mwili yana faida kwa sehemu, lakini utauwa una faida katika mambo yote, yaani, unayo ahadi ya uzima wa sasa na ya ule ujao.
-
2 Mnajisumbua bure kuamka mapema
na kuchelewa kulala,
mkitaabikia chakula:
kwa maana yeye huwapa usingizi wapenzi wake.
-
19 Yeye alimaye shamba lake atakuwa na chakula tele,
bali yule afuataye mambo ya upuzi atakuwa na umaskini wa kumtosha.
-
13 Tafakari kile Mungu alichokitenda:
Nani awezaye kunyoosha
kile ambacho yeye amekipinda?
14 Nyakati zikiwa nzuri, ufurahi,
lakini nyakati zikiwa mbaya, tafakari:
Mungu amefanya hiyo moja,
naam, sanjari na hiyo nyingine.
Kwa hiyo, mwanadamu hawezi kugundua
kitu chochote kuhusu maisha yake ya baadaye.
15 Katika maisha haya yangu ya ubatili nimeshaona haya mawili:
mtu mwadilifu akiangamia katika uadilifu wake,
naye mtu mwovu akiishi maisha marefu katika uovu wake.
-
10 Ndipo pia, nikaona waovu wakizikwa, wale ambao walizoea kuingia na kutoka mahali patakatifu na kupewa sifa katika mji ambapo walikuwa wamefanya haya. Hili nalo ni ubatili.
11 Wakati hukumu juu ya tendo ovu haitekelezwi upesi, mioyo ya watu hujaa mipango ya kutenda maovu. 12 Ingawa mtu mwovu hufanya maovu mia moja na akaendelea kuishi maisha marefu, najua kwamba itakuwa bora zaidi kwa watu wanaomwogopa Mungu, wamchao Mungu. 13 Lakini kwa sababu waovu hawamwogopi Mungu, hawatafanikiwa, maisha yao hayatarefuka kama kivuli.
14 Kuna kitu kingine ambacho ni ubatili kinachotokea duniani: Watu waadilifu kupata yale yanayowastahili waovu, nao waovu kupata yale yanayowastahili waadilifu. Hili nalo pia, nasema ni ubatili. 15 Kwa hiyo mimi ninasifu kufurahia maisha, kwa sababu hakuna kitu bora zaidi kwa mwanadamu chini ya jua kuliko kula, kunywa na kufurahi. Kisha furaha itafuatana naye kazini mwake siku zote za maisha yake ambazo amepewa na Mungu chini ya jua.
16 Nilipotafakari akilini mwangu ili nijue hekima na kuangalia kazi ya mwanadamu duniani, jinsi ambavyo macho yake hayapati usingizi mchana wala usiku, 17 ndipo nikaona yale yote ambayo Mungu ameyafanya. Hakuna yeyote awezaye kuelewa yale yanayotendeka chini ya jua. Licha ya juhudi zake zote za kutafuta, mtu hawezi kugundua maana yake. Hata ingawa mtu mwenye hekima anadai kuwa anafahamu, kwa hakika hawezi kutambua.
-
13 Watapanda ngano lakini watavuna miiba;
watajitaabisha lakini hawatafaidi chochote.
Kwa hiyo beba aibu ya mavuno yako
kwa sababu ya hasira kali ya Bwana Mungu.”
-
20 tena, “Bwana anajua kwamba mawazo ya wenye hekima ni ubatili.”
-
3 Kama nikitoa mali yote niliyo nayo na kama nikijitolea mwili wangu uchomwe moto, kama sina upendo, hainifaidi kitu.
-
20 Timotheo, linda kile kilichowekwa amana kwako. Epuka majadiliano yasiyo ya utauwa na mabishano ambayo kwa uongo huitwa elimu, 21 ambayo wengine kwa kujidai kuwa nayo wameiacha imani.
Neema iwe nanyi. Amen.
-
14 Endelea kuwakumbusha mambo haya ukiwaonya mbele za Bwana waache kushindana kwa maneno ambayo hayana faida yoyote bali huwaangamiza tu wale wanaoyasikia. 15 Jitahidi kujionyesha kwa Mungu kuwa umekubaliwa naye, mtendakazi asiye na sababu ya kuona aibu, ukilitumia kwa usahihi neno la kweli. 16 Jiepushe na maneno mabaya, yasiyo na maana, yasiyo ya utauwa, kwa maana hayo huzidi kuwatosa watu katika kukosa heshima kwa Mungu. 17 Mafundisho yao yataenea kama kidonda kisichopona. Miongoni mwao wamo Himenayo na Fileto 18 ambao wameiacha kweli, wakisema kwamba ufufuo wa wafu umekwisha kuwako, nao huharibu imani ya baadhi ya watu. 19 Lakini msingi wa Mungu ulio imara umesimama, ukiwa na muhuri wenye maandishi haya: “Bwana anawajua walio wake”; tena, “Kila alitajaye jina la Bwana, na auache uovu.”
20 Katika nyumba kubwa si kwamba kuna vyombo vya dhahabu na fedha tu, bali pia vimo vyombo vya miti na vya udongo; vingine kwa matumizi maalum, na vingine kwa matumizi ya kawaida. 21 Basi ikiwa mtu amejitakasa na kujitenga na hayo niliyoyataja, atakuwa chombo maalum, kilichotengwa na ambacho kinamfaa mwenye nyumba, kimeandaliwa tayari kwa kila kazi njema.
22 Zikimbie tamaa mbaya za ujana, ufuate haki, imani, upendo na amani pamoja na wale wamwitao Bwana kwa moyo safi. 23 Jiepushe na mabishano ya kipumbavu na yasiyo na maana, kwa kuwa wajua ya kwamba hayo huzaa magomvi. 24 Tena haimpasi mtumishi wa Bwana kuwa mgomvi, bali inampasa awe mwema kwa kila mtu, awezaye kufundisha, tena mvumilivu. 25 Inampasa kuwaonya kwa upole wale wanaopingana naye, kwa matumaini kwamba Mungu atawajalia kutubu na kuijua kweli, 26 ili fahamu zao ziwarudie tena, nao waponyoke katika mtego wa ibilisi ambaye amewateka wapate kufanya mapenzi yake.
-
9 Lakini jiepushe na maswali ya kipuzi, mambo ya koo, mabishano na ugomvi kuhusu sheria, kwa sababu hayana faida, tena ni ubatili. 10 Mtu anayesababisha mafarakano, mwonye mara ya kwanza, kisha mwonye mara ya pili. Baada ya hapo, usihusike naye tena. 11 Kwa kuwa unajua kwamba mtu kama huyo amepotoka na tena ni mwenye dhambi. Yeye amejihukumu mwenyewe.
-
13 Kwa hiyo, tayarisheni nia zenu kwa kazi; mwe na kiasi, mkitumainia kikamilifu ile neema mtakayopewa Yesu Kristo atakapodhihirishwa. 14 Kama watoto watiifu, msifuate tamaa zenu mbaya wakati mlipoishi kwa ujinga. 15 Bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, nanyi kuweni watakatifu katika mwenendo wenu wote. 16 Kwa maana imeandikwa: “Kuweni watakatifu, kwa kuwa mimi ni mtakatifu.”
17 Kwa sababu mnamwita Baba ahukumuye kila mtu kulingana na matendo yake pasipo upendeleo, enendeni kwa hofu ya kumcha Mungu wakati wenu wa kukaa hapa duniani kama wageni. 18 Kwa maana mnafahamu kwamba mlikombolewa kutoka mwenendo wenu usiofaa ambao mliurithi kutoka kwa baba zenu, si kwa vitu viharibikavyo kama fedha na dhahabu, 19 bali kwa damu ya thamani ya Kristo, yule Mwana-Kondoo asiye na dosari wala doa. 20 Yeye alichaguliwa kabla ya kuwekwa kwa misingi ya ulimwengu, lakini akadhihirishwa katika siku hizi za mwisho kwa ajili yenu. 21 Kupitia kwake mmemwamini Mungu, aliyemfufua kutoka kwa wafu na akampa utukufu, ili imani yenu na tumaini lenu ziwe kwa Mungu.
22 Basi kwa kuwa mmejitakasa nafsi zenu kwa kuitii ile kweli hata mkawa na upendo wa ndugu usio na unafiki, basi pendaneni kwa dhati kutoka moyoni. 23 Kwa maana mmezaliwa upya, si kwa mbegu ile iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika, kupitia kwa neno la Mungu lililo hai na linalodumu milele. 24 Maana,
“Wanadamu wote ni kama majani,
nao utukufu wao ni kama maua ya kondeni;
majani hunyauka na maua huanguka,
25 lakini neno la Bwana ladumu milele.”
Hili ndilo neno lililohubiriwa kwenu.
-
15 Msiupende ulimwengu wala mambo yaliyo ulimwenguni. Kama mtu yeyote akiupenda ulimwengu, upendo wa Baba haumo ndani yake. 16 Kwa maana kila kitu kilichomo ulimwenguni, yaani tamaa ya mwili, tamaa ya macho na kiburi cha uzima, havitokani na Baba bali hutokana na ulimwengu. 17 Nao ulimwengu unapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu milele.
-
11 Tuletee msaada dhidi ya adui,
kwa maana msaada wa mwanadamu haufai kitu.
-
11 Yeye alimaye shamba lake atakuwa na chakula tele,
bali yeye afuataye mambo ya upuzi hana akili.
-
16 Pia nikaona kitu kingine tena chini ya jua:
Mahali pa kutolea hukumu,
uovu ulikuwepo,
mahali pa kupatia haki,
uovu ulikuwepo.
17 Nikafikiri moyoni mwangu,
“Mungu atawaleta hukumuni
wote wawili wenye haki na waovu,
kwa maana kutakuwako na wakati kwa ajili ya kila jambo,
wakati kwa ajili ya kila tendo.”
18 Pia nikafikiri, “Kuhusu wanadamu, Mungu huwajaribu ili wajione kwamba wao ni kama wanyama. 19 Hatima ya mwanadamu ni kama ile ya wanyama; wote wana mwisho unaofanana: Jinsi anavyokufa mnyama, ndivyo anavyokufa mwanadamu. Wote wana pumzi inayofanana; mwanadamu hana cha zaidi kuliko mnyama. Kila kitu ni ubatili. 20 Wote huenda mahali panapofanana; wote hutoka mavumbini, mavumbini wote hurudi. 21 Ni nani ajuaye kama roho ya mtu huenda juu na roho ya mnyama hushuka chini ardhini?”
22 Kwa hiyo nikaona kwamba hakuna kitu kilicho bora zaidi kwa mwanadamu kuliko kuifurahia kazi yake, kwa sababu hilo ndilo fungu lake. Kwa maana ni nani awezaye kumrudisha ili aje kuona kile kitakachotendeka baada yake?
-
6 Kama ilivyo kuvunjika kwa miiba chini ya sufuria,
ndivyo kilivyo kicheko cha wapumbavu.
Hili nalo pia ni ubatili.
-
13 Acheni kuniletea sadaka zisizokuwa na maana!
Uvumba wenu ni chukizo kwangu.
Miandamo ya Mwezi, Sabato na makusanyiko ya ibada:
siwezi kuvumilia makusanyiko yenu maovu.
-
32 Kweli, niko kinyume na hao wanaotabiri ndoto za uongo,” asema Bwana. “Wanazisimulia na kuwapotosha watu wangu kwa uongo wao bila kujali, lakini sikuwatuma wala sikuwaamuru. Hawawafaidi watu hawa hata kidogo,” asema Bwana.
-
13 “Mmesema vitu vigumu dhidi yangu,” asema Bwana.
“Hata hivyo mnauliza, ‘Tumesema nini dhidi yako?’
14 “Mmesema, ‘Ni bure kumtumikia Mungu. Tumepata faida gani kwa kushika maagizo yake na kwenda kama waombolezaji mbele za Bwana Mwenye Nguvu Zote? 15 Lakini sasa wenye kiburi wanabarikiwa. Hakika watenda mabaya wanastawi, pia hata wale wanaoshindana na Mungu ndio wanaosalimika.’ ”
16 Ndipo wale waliomcha Bwana wakasemezana wao kwa wao, naye Bwana akasikiliza na akasikia. Kitabu cha kumbukumbu kikaandikwa mbele yake kuhusu wale ambao walimcha Bwana na kuliheshimu jina lake.
17 “Nao watakuwa watu wangu,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote, “katika siku ile nitakapowafanya watu kuwa hazina yangu. Nitawahurumia, kama vile kwa huruma mtu amhurumiavyo mwanawe anayemtumikia. 18 Kwa mara nyingine tena utaona tofauti kati ya wenye haki na waovu, kati ya wale wanaomtumikia Mungu na wale wasiomtumikia.
-
7 Nanyi mnaposali msiseme maneno kama wafanyavyo watu wasiomjua Mungu. Kwa maana wao hudhani kwamba watasikiwa kwa sababu ya wingi wa maneno yao.
-
23 Punde Petro na Yohana walipoachiliwa, walirudi kwa waumini wenzao wakawaeleza waliyoambiwa na viongozi wa makuhani na wazee. 24 Watu waliposikia hayo, wakainua sauti zao, wakamwomba Mungu kwa pamoja, wakisema, “Bwana Mwenyezi, uliyeziumba mbingu na nchi na bahari, na vitu vyote vilivyomo. 25 Wewe ulisema kwa Roho Mtakatifu kupitia kwa kinywa cha baba yetu Daudi, mtumishi wako, ukasema:
“ ‘Mbona mataifa wanaghadhibika,
na kabila za watu zinawaza ubatili?
26 Wafalme wa dunia wamejipanga,
na watawala wanakusanyika pamoja
dhidi ya Bwana
na dhidi ya Mpakwa Mafuta wake.’
27 Ni kweli Herode na Pontio Pilato pamoja na watu wa Mataifa na Waisraeli, walikusanyika katika mji huu dhidi ya mwanao mtakatifu Yesu uliyemtia mafuta. 28 Wao wakafanya yale ambayo uweza wako na mapenzi yako yalikuwa yamekusudia yatokee tangu zamani. 29 Sasa, Bwana angalia vitisho vyao na utuwezeshe sisi watumishi wako kulinena neno lako kwa ujasiri mkuu. 30 Nyoosha mkono wako ili kuponya wagonjwa na kutenda ishara na miujiza kwa jina la Mwanao mtakatifu Yesu.”
31 Walipokwisha kuomba, mahali walipokuwa wamekutanika pakatikiswa, wote wakajazwa na Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri.
-
1 Kwa hiyo, ndugu zangu, nawasihi kwa rehema zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu na inayompendeza Mungu, hii ndiyo ibada yenu yenye maana. 2 Msifuatishe tena mfano wa ulimwengu huu, bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu. Ndipo mtaweza kuonja na kuhakikisha ni nini mapenzi ya Mungu yaliyo mema, yanayopendeza machoni pake na ukamilifu.
-
9 Msichukuliwe na kila aina ya mafundisho ya kigeni. Ni vyema mioyo yenu iimarishwe kwa neema, wala si kwa sheria kuhusu utaratibu wa vyakula, ambavyo havina faida kwa wale wanaozishika hizo sheria.
-
14 Ndugu zangu, yafaa nini ikiwa mtu atadai kuwa anayo imani lakini hana matendo? Je, imani kama hiyo yaweza kumwokoa?
-
2 Hazina zilizopatikana kwa njia mbaya hazifai,
lakini uadilifu huokoa kutoka mautini.
-
12 Nitaifunua haki yako na matendo yako,
nayo hayatakufaidi.
-
8 Lakini tazama, mnatumainia maneno ya udanganyifu yasiyo na maana.
-
14 Hivyo Bwana Mungu akamwambia nyoka, “Kwa kuwa umefanya hili,
“Umelaaniwa kuliko wanyama wote
wa kufugwa na wa porini!
Utatambaa kwa tumbo lako
na kula mavumbi
siku zote za maisha yako.
15 Nami nitaweka uadui
kati yako na huyo mwanamke,
na kati ya uzao wako na wake,
yeye atakuponda kichwa,
nawe utamuuma kisigino.”
16 Kwa mwanamke akasema,
“Nitakuzidishia sana utungu wakati wa kuzaa kwako;
kwa utungu utazaa watoto.
Tamaa yako itakuwa kwa mumeo
naye atakutawala.”
17 Kwa Adamu akasema, “Kwa sababu umemsikiliza mke wako na ukala kutoka kwenye mti niliokuamuru, ‘Msile tunda lake,’
“Ardhi imelaaniwa kwa sababu yako,
kwa kazi ngumu utakula chakula kitokacho humo
siku zote za maisha yako.
18 Itazaa miiba na mibaruti kwa ajili yako,
nawe utakula mimea ya shambani.
19 Kwa jasho la uso wako
utakula chakula chako
hadi utakaporudi ardhini,
kwa kuwa ulitwaliwa kutoka humo,
kwa kuwa wewe u mavumbi
na mavumbini wewe utarudi.”
-
47 Kumbuka jinsi maisha yangu yanavyopita haraka.
Ni kwa ubatili kiasi gani umemuumba mwanadamu!
-
3 Kwa maana desturi za mataifa hazina maana,
wanakata mti msituni,
na fundi anauchonga kwa patasi.
4 Wanaparemba kwa fedha na dhahabu,
wanakikaza kwa nyundo na misumari ili kisitikisike.
5 Sanamu zao ni kama sanamu
iliyowekwa shambani la matango kutishia ndege
nazo haziwezi kuongea;
sharti zibebwe
sababu haziwezi kutembea.
Usiziogope; haziwezi kudhuru,
wala kutenda lolote jema.”
-
15 “Enyi watu, kwa nini mnafanya mambo haya? Sisi ni wanadamu tu kama ninyi! Tunawaletea habari njema, tukiwaambia kwamba mgeuke mtoke katika mambo haya yasiyofaa, mmwelekee Mungu aliye hai, aliyeziumba mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo. 16 Zamani aliwaachia mataifa waishi walivyotaka.
-
10 Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo na neema yake kwangu haikuwa kitu bure. Bali nilizidi sana kufanya kazi kuliko mitume wote, lakini haikuwa mimi, bali ni ile neema ya Mungu iliyokuwa pamoja nami.
-
17 Kwa hiyo kama mtu akiwa ndani ya Kristo, amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita, tazama, yamekuwa mapya.
-
15 Kwa maana katika Kristo Yesu, kutahiriwa au kutokutahiriwa si kitu, bali kule kuwa kiumbe kipya ni kila kitu!
Shows Read in context, Share and Copy.