105 Bible Verses About Poverty

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Poverty
  1. 2 Kwa maana kama akija mtu katika kusanyiko lenu akiwa amevaa pete ya dhahabu na mavazi mazuri, pia akaingia mtu maskini mwenye mavazi yaliyochakaa, 3 nanyi mkampa heshima yule aliyevaa mavazi mazuri na kumwambia, “Keti hapa mahali pazuri,” lakini yule maskini mkamwambia, “Wewe simama pale,” au “Keti hapa sakafuni karibu na miguu yangu,” 4 je, hamjawabagua na kuwa mahakimu mioyoni mwenu mkihukumu kwa mawazo yenu maovu?

    5 Ndugu zangu, sikilizeni: Je, Mungu hakuwachagua wale walio maskini machoni pa ulimwengu kuwa matajiri katika imani na kuurithi Ufalme aliowaahidi wale wampendao? 6 Lakini ninyi mmemdharau yule aliye maskini. Je, hao matajiri si ndio wanaowadhulumu na kuwaburuta mahakamani? 7 Je, si wao wanaolikufuru Jina lile lililo bora sana mliloitiwa?

    8 Kama kweli mnaitimiza ile sheria ya kifalme inayopatikana katika Maandiko isemayo, “Mpende jirani yako kama unavyoipenda nafsi yako,” mnafanya vyema. 9 Lakini kama mnakuwa na upendeleo kwa watu, mnatenda dhambi, na sheria inawahukumu kuwa ninyi ni wakosaji.

  2. 3 “Heri walio maskini wa roho,

    maana Ufalme wa Mbinguni ni wao.

  3. 18 “Roho wa Bwana yu juu yangu,

    kwa sababu amenitia mafuta

    kuwahubiria maskini habari njema.

    Amenituma kuwatangazia wafungwa

    kufunguliwa kwao,

    na vipofu kupata kuona tena,

    kuwaweka huru wanaoonewa,

    19 na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubalika.”

  4. 21 Yesu akamwambia, “Kama ukitaka kuwa mkamilifu, nenda, ukauze vitu vyote ulivyo navyo, na hizo fedha uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.”

    22 Yule kijana aliposikia hayo, akaenda zake kwa huzuni, kwa sababu alikuwa na mali nyingi.

    23 Ndipo Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Amin, nawaambia, itakuwa vigumu kwa mtu tajiri kuingia katika Ufalme wa Mbinguni. 24 Tena nawaambia, ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita kwenye tundu la sindano kuliko mtu tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu.”

  5. 6 Kumbukeni kwamba: Yeyote apandaye kwa uchache pia atavuna kwa uchache, naye apandaye kwa ukarimu pia atavuna kwa ukarimu. 7 Kila mtu atoe kama anavyokusudia moyoni mwake, si kwa uchoyo au kwa kulazimishwa, kwa maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo mkunjufu. 8 Naye Mungu aweza kuwapa kila baraka kwa wingi, ili katika mambo yote kila wakati, mwe na kila kitu mnachohitaji, ili mweze kushiriki kwa wingi katika kila kazi njema. 9 Kama ilivyoandikwa:

    “Ametawanya vipawa vyake kwa ukarimu

    akawapa maskini;

    haki yake hudumu milele.”

    10 Yeye ampaye mpanzi mbegu kwa ajili ya kupanda na mkate kuwa chakula, atawapa na kuzizidisha mbegu zenu za kupanda na kuongeza mavuno ya haki yenu. 11 Mtatajirishwa kwa kila namna ili mpate kuwa wakarimu kila wakati, na kupitia kwetu, ukarimu wenu utamletea Mungu shukrani.

  6. 25 Sasa, niko njiani kuelekea Yerusalemu kwa ajili ya kuwahudumia watakatifu huko. 26 Kwa kuwa imewapendeza watu wa Makedonia na Akaya kufanya changizo kwa ajili ya maskini walioko miongoni mwa watakatifu huko Yerusalemu. 27 Imewapendeza kufanya hivyo, naam, kwani ni wadeni wao. Kwa maana ikiwa watu wa Mataifa wameshiriki baraka za rohoni za Wayahudi, wao ni wadeni wa Wayahudi, ili Wayahudi nao washiriki baraka zao za mambo ya mwilini.

  7. 7 Mwenye haki hujali haki kwa ajili ya maskini,

    bali mwovu hajishughulishi na hilo.

  8. 41 Kisha Yesu akaketi mkabala na sehemu ambapo sadaka zilikuwa zinawekwa na kuangalia umati wa watu wakiweka fedha zao kwenye sanduku la hazina ya Hekalu. Matajiri wengi wakaweka kiasi kikubwa cha fedha. 42 Lakini mjane mmoja maskini akaja na kuweka sarafu mbili ndogo za shaba zenye thamani ya senti mbili.

    43 Yesu akawaita wanafunzi wake, akawaambia, “Amin, nawaambia, huyu mjane maskini ameweka katika sanduku la hazina zaidi ya watu wengine wote. 44 Wengine wote wametoa kutokana na ziada ya mali zao. Lakini huyu mjane ametoa kutokana na umaskini wake, akaweka kila kitu alichokuwa nacho, hata kile alichohitaji ili kuishi.”

  9. 7 Maana ninyi wenyewe mnajua jinsi iwapasavyo kufuata mfano wetu. Sisi hatukuwa wavivu tulipokuwa pamoja nanyi, 8 wala hatukula chakula cha mtu yeyote pasipo kukilipia. Badala yake tulifanya kazi kwa bidii usiku na mchana, ili tusimlemee mtu yeyote miongoni mwenu. 9 Tulifanya hivi, si kwa sababu hatukuwa na haki ya kupata msaada kama huo, bali ndio sisi wenyewe tuwe kielelezo. 10 Kwa maana hata tulipokuwa pamoja nanyi, tuliwapa amri kwamba: “Mtu yeyote asiyetaka kufanya kazi, hata kula asile.”

    11 Kwa kuwa tunasikia kwamba baadhi ya watu miongoni mwenu ni wavivu. Hawafanyi kazi bali hujishughulisha na mambo ya wengine. 12 Basi watu kama hao tunawaagiza na kuwahimiza katika Bwana Yesu Kristo, kwamba wafanye kazi kwa utulivu kwa ajili ya chakula chao wenyewe.

  10. 17 Waagize wale ambao ni matajiri wa ulimwengu huu waache kujivuna, wala wasiweke tumaini lao katika mali ambayo si ya hakika, bali waweke tumaini lao katika Mungu ambaye hutupatia vitu vyote kwa wingi ili tuvifurahie. 18 Waagize watende mema, wawe matajiri katika matendo mema, pia wawe wakarimu na walio tayari kushiriki mali zao na wengine. 19 Kwa njia hii watajiwekea hazina kama msingi kwa ajili ya wakati ujao na hivyo watajipatia uzima, yaani, ule uzima ambao ni wa kweli.

  11. 27 Dini iliyo safi, isiyo na uchafu, inayokubalika mbele za Mungu Baba yetu, ndiyo hii: Kuwasaidia yatima na wajane katika dhiki zao na kujilinda usitiwe madoa na dunia.

  12. 19 “Palikuwa na mtu mmoja tajiri aliyevaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi, ambaye aliishi kwa anasa kila siku. 20 Hapo penye mlango wake aliishi maskini mmoja, jina lake Lazaro, mwenye vidonda mwili mzima. 21 Huyo Lazaro alitamani kujishibisha kwa makombo yaliyoanguka kutoka mezani kwa yule tajiri. Hata mbwa walikuwa wakija na kuramba vidonda vyake.

    22 “Wakati ukafika yule maskini akafa, nao malaika wakamchukua akae pamoja na Abrahamu. Yule tajiri naye akafa na akazikwa. 23 Kule kuzimu alipokuwa akiteseka, alitazama juu, akamwona Abrahamu kwa mbali, naye Lazaro alikuwa karibu yake. 24 Hivyo yule tajiri akamwita, ‘Baba Abrahamu, nihurumie na umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake ndani ya maji aupoze ulimi wangu, kwa sababu nina maumivu makuu kwenye moto huu.’

    25 “Lakini Abrahamu akamjibu, ‘Mwanangu, kumbuka kwamba wakati wa uhai wako ulipata mambo mazuri, lakini Lazaro alipata mambo mabaya. Lakini sasa anafarijiwa hapa na wewe uko katika maumivu makuu. 26 Zaidi ya hayo, kati yetu na ninyi huko kumewekwa shimo kubwa, ili wale wanaotaka kutoka huku kuja huko wasiweze, wala mtu yeyote asiweze kuvuka kutoka huko kuja kwetu.’

  13. 3 Waheshimu wanawake wajane ambao ni wajane kweli kweli. 4 Kama mjane ana watoto ama wajukuu, hawa inawapasa awali ya yote wajifunze kutimiza wajibu wao wa kumcha Mungu katika matendo kwa kuwatunza wale wa jamaa zao wenyewe, na hivyo wawarudishie wema waliowatendea wazazi wao, kwa kuwa hivi ndivyo impendezavyo Mungu.

  14. 12 Kisha Yesu akamwambia yule aliyewaalika, “Uandaapo karamu ya chakula cha mchana au cha jioni, usialike rafiki zako au ndugu zako au jamaa zako au majirani zako walio matajiri tu. Ukifanya hivyo, wao nao wanaweza kukualika kwao, nawe ukawa umelipwa kile ulichofanya na kupata thawabu yako. 13 Bali ufanyapo karamu, waalike maskini, vilema na vipofu, 14 nawe utabarikiwa kwa sababu hawa hawana uwezo wa kukulipa. Mungu atakulipa wakati wa ufufuo wa wenye haki.”

  15. 10 “Kwa muda wa miaka sita mtapanda mashamba yenu na kuvuna mazao, 11 lakini katika mwaka wa saba usiilime ardhi wala kuitumia, ili watu walio maskini miongoni mwenu waweze kupata chakula kutoka kwenye hayo mashamba, nao wanyama pori wapate chakula kwa yale mabaki watakayobakiza. Utafanya hivyo katika shamba lako la mizabibu na la mizeituni.

  16. 20 Akawatazama wanafunzi wake, akasema:

    “Mmebarikiwa ninyi mlio maskini,

    kwa sababu Ufalme wa Mungu ni wenu.

    21 Mmebarikiwa ninyi mlio na njaa sasa,

    kwa sababu mtashibishwa.

    Mmebarikiwa ninyi mnaolia sasa,

    kwa sababu mtacheka.

  17. 9 Kwa maana mnajua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba ingawa alikuwa tajiri, kwa ajili yenu alikubali kuwa maskini, ili kwa umaskini wake ninyi mpate kuwa matajiri.

  18. 13 Usiupende usingizi la sivyo utakuwa maskini,

    uwe macho nawe utakuwa na chakula cha akiba.

  19. 19 Yeye alimaye shamba lake atakuwa na chakula tele,

    bali yule afuataye mambo ya upuzi atakuwa na umaskini wa kumtosha.

  20. 1 Roho wa Bwana Mwenyezi yu juu yangu,

    kwa sababu Bwana amenitia mafuta

    kuwahubiria maskini habari njema.

    Amenituma kuwaganga waliovunjika moyo,

    kuwatangazia mateka uhuru wao,

    na hao waliofungwa

    habari za kufunguliwa kwao;

    2 kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa,

    na siku ya kisasi ya Mungu wetu,

    kuwafariji wote waombolezao,

    3 na kuwapa mahitaji

    wale wanaohuzunika katika Sayuni,

    ili kuwapa taji ya uzuri badala ya majivu,

    mafuta ya furaha badala ya maombolezo,

    vazi la sifa badala ya roho ya kukata tamaa.

    Nao wataitwa mialoni ya haki,

    pando la Bwana,

    ili kuonyesha utukufu wake.

  21. 17 Ikiwa mtu anavyo vitu vya ulimwengu huu na akamwona ndugu yake ni mhitaji lakini asimhurumie, upendo wa Mungu wakaaje ndani ya mtu huyo? 18 Watoto wapendwa, tusipende kwa maneno au kwa ulimi bali kwa tendo na kweli.

  22. 6 Ninyi watenda mabaya mnakwamisha mipango ya maskini,

    bali Bwana ndiye kimbilio lao.

  23. 10 Nitapaza sauti yangu nikisema,

    “Ni nani aliye kama wewe, Ee Bwana?

    Wewe huwaokoa maskini kutokana na wale walio na nguvu kuliko wao,

    maskini na mhitaji kutokana na wanaowanyangʼanya!”

  24. 14 Ndugu zangu, yafaa nini ikiwa mtu atadai kuwa anayo imani lakini hana matendo? Je, imani kama hiyo yaweza kumwokoa? 15 Ikiwa ndugu yako au dada hana mavazi wala chakula, 16 mmoja wenu akamwambia, “Enenda zako kwa amani, ukaote moto na kushiba,” pasipo kumpatia yale mahitaji ya mwili aliyopungukiwa, yafaa nini? 17 Vivyo hivyo, imani peke yake kama haikuambatana na matendo, imekufa.

  25. 3 Teteeni wanyonge na yatima,

    tunzeni haki za maskini na walioonewa.

    4 Mwokoeni mnyonge na mhitaji,

    wakomboeni kutoka mkononi mwa mwovu.

  26. 12 Najua kwamba Bwana huwapatia maskini haki,

    na kuitegemeza njia ya mhitaji.

  27. 22 Usiwadhulumu maskini kwa sababu ni maskini,

    wala kumdhulumu mhitaji mahakamani,

    23 kwa sababu Bwana atalichukua shauri lao

    naye atawateka wao waliowateka.

  28. 1 Ole wao wawekao sheria zisizo za haki,

    kwa wale watoao amri za kuonea,

    2 kuwanyima maskini haki zao

    na kuzuilia haki za watu wangu walioonewa,

    kuwafanya wajane mawindo yao

    na kuwanyangʼanya yatima.

    3 Mtafanya nini siku ya kutoa hesabu,

    wakati maafa yatakapokuja kutoka mbali?

    Mtamkimbilia nani awape msaada?

    Mtaacha wapi mali zenu?

  29. 21 “Usimtendee mgeni vibaya au kumwonea, kwa kuwa nanyi mlikuwa wageni huko Misri.

    22 “Usimdhulumu mjane wala yatima. 23 Kama ukifanya hivyo nao wakinililia, hakika nitasikia kilio chao. 24 Hasira yangu itawaka, nami nitawaua kwa upanga, wake zenu watakuwa wajane na watoto wenu watakuwa yatima.

    25 “Kama ukimkopesha mmojawapo wa watu wangu fedha ambaye ni mhitaji, usiwe kama mtu mkopesha fedha; usimtoze riba. 26 Kama ukichukua vazi la jirani kama rehani, ulirudishe kwake kabla jua kuzama, 27 kwa kuwa vazi lake ndilo pekee alilo nalo la kumfunika mwili wake. Ni nini kingine atajifunika nacho? Atakaponililia, nitasikia, kwa kuwa nina huruma.

  30. 6 “Usiwanyime haki watu wako walio maskini katika mashtaka yao.

  31. 9 Ametawanya vipawa vyake kwa ukarimu akawapa maskini;

    haki yake hudumu milele;

    pembe yake itatukuzwa kwa heshima.

  32. 1 Afadhali mtu maskini ambaye mwenendo wake hauna lawama,

    kuliko mpumbavu ambaye midomo yake imepotoka.

  33. 1 Heri kuchagua jina jema kuliko utajiri mwingi,

    kuheshimiwa ni bora kuliko fedha au dhahabu.

    2 Tajiri na maskini wanafanana kwa hili:

    Bwana ni Muumba wao wote.

  34. 6 Hili ndilo asemalo Bwana:

    “Kwa dhambi tatu za Israeli,

    hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu.

    Wanawauza wenye haki kwa fedha,

    na maskini kwa jozi ya viatu.

    7 Wanakanyaga juu ya vichwa vya maskini,

    kama vile juu ya mavumbi ya nchi,

    na kukataa haki kwa walioonewa.

    Baba na mwanawe hushiriki msichana mmoja,

    kwa hivyo hulinajisi Jina langu takatifu.

  35. 10 tukiwa kama wenye huzuni, lakini siku zote tukifurahi; tukionekana maskini, lakini tukitajirisha wengi; tukiwa kama wasio na kitu, lakini tuna vitu vyote.

  36. 7 Ikiwa kuna mtu maskini miongoni mwa ndugu zenu, katika mji wowote wa hiyo nchi ambayo Bwana Mungu wenu anawapa, msiwe na moyo mgumu wala usimfumbie mkono ndugu yako aliye maskini. 8 Afadhali fungua mikono yako na umkopeshe kwa hiari chochote anachohitaji. 9 Jihadhari usijiwekee wazo hili ovu: “Mwaka wa saba, mwaka wa kufuta madeni umekaribia,” usije ukaonyesha nia mbaya kwa ndugu yako mhitaji na ukaacha kumpa chochote. Anaweza kumlalamikia Bwana dhidi yako nawe utakuwa umepatikana na hatia ya dhambi. 10 Mpe kwa ukarimu na ufanye hivyo bila kinyongo moyoni, ndipo kwa sababu ya hili Bwana Mungu wenu atakubariki katika kazi zako zote na kwa kila kitu utakachokiwekea mkono wako. 11 Siku zote watakuwepo watu maskini katika nchi. Kwa hiyo ninawaamuru mwe na mikono iliyokunjuliwa kuwaelekea ndugu zenu, kuwaelekea maskini na wahitaji katika nchi yenu.

  37. 18 Yeye anayedharau maonyo hupata umaskini na aibu,

    bali yeye anayekubali maonyo huheshimiwa.

  38. 20 Maskini huepukwa hata na majirani zao,

    bali matajiri wana marafiki wengi.

    21 Yeye anayemdharau jirani yake hutenda dhambi,

    bali amebarikiwa yeye aliye na huruma kwa mhitaji.

  39. 27 Yeye ampaye maskini

    hatapungukiwa na kitu chochote,

    bali yeye awafumbiaye maskini macho

    hupata laana nyingi.

  40. 10 Walichotuomba ni kwamba tuendelee kuwakumbuka maskini, jambo ambalo ndilo nililokuwa na shauku ya kulifanya.

  41. 1 Basi sikilizeni, ninyi matajiri, lieni na kuomboleza kwa ajili ya hali mbaya sana inayowajia. 2 Utajiri wenu umeoza na mavazi yenu yameliwa na nondo. 3 Dhahabu yenu na fedha yenu vimeliwa na kutu. Kutu yake itashuhudia dhidi yenu nayo itaila miili yenu kama vile moto. Mmejiwekea hazina kwa ajili ya siku za mwisho. 4 Angalieni! Ule ujira wa vibarua waliolima mashamba yenu mliouzuia kwa hila unapiga kelele dhidi yenu na vilio vya wavunaji vimefika masikioni mwa Bwana Mwenye Nguvu Zote. 5 Mmeishi duniani kwa anasa na kwa starehe, mmejinenepesha tayari kwa siku ya kuchinjwa. 6 Mmewahukumu na kuwaua watu wenye haki, waliokuwa hawapingani nanyi.

  42. 5 Heri yeye ambaye Mungu wa Yakobo ni msaada wake,

    ambaye tumaini lake ni katika Bwana, Mungu wake,

    6 Muumba wa mbingu na nchi,

    na bahari na vyote vilivyomo ndani yake:

    Bwana anayedumu kuwa mwaminifu

    milele na milele.

    7 Naye huwapatia haki walioonewa

    na kuwapa wenye njaa chakula.

    Bwana huwaweka wafungwa huru,

    8 Bwana huwafumbua vipofu macho,

    Bwana huwainua waliolemewa na mizigo yao,

    Bwana huwapenda wenye haki.

    9 Bwana huwalinda wageni

    na kuwategemeza yatima na wajane,

    lakini hupinga njia za waovu.

  43. 10 Bado kulala kidogo, kusinzia kidogo,

    bado kukunja mikono kidogo upate kupumzika:

    11 hivyo umaskini utakuja juu yako kama mnyangʼanyi,

    na kupungukiwa kutakujia kama mtu mwenye silaha.

  44. 20 Usiwe miongoni mwa wanywao mvinyo,

    au wale walao nyama kwa pupa,

    21 kwa maana walevi na walafi huwa maskini,

    nako kusinzia huwavika matambara.

  45. 8 Neno la Bwana likamjia tena Zekaria: 9 “Hivi ndivyo asemavyo Bwana Mwenye Nguvu Zote: ‘Fanyeni hukumu za haki, onyesheni rehema na huruma ninyi kwa ninyi. 10 Msimwonee mjane wala yatima, mgeni wala maskini. Msiwaziane mabaya mioyoni mwenu ninyi kwa ninyi.’

  46. 20 Naye Yesu akamjibu, “Mbweha wana mapango, nao ndege wa angani wana viota, lakini Mwana wa Adamu hana mahali pa kulaza kichwa chake.”

  47. 11 Yohana akawaambia, “Aliye na kanzu mbili amgawie asiye nayo, naye aliye na chakula na afanye vivyo hivyo.”

  48. 16 Lakini kama mwanamke yeyote aaminiye ana wajane katika jamaa yake, inampasa awasaidie wala si kuwaacha wakililemea kanisa, ili kanisa liweze kuwasaidia wale ambao ni wajane kweli kweli.

  49. 9 Naijua dhiki yako na umaskini wako, lakini wewe ni tajiri! Nayajua masingizio ya wale wasemao kuwa ni Wayahudi lakini sio, bali wao ni sinagogi la Shetani.

  50. 9 Umewafukuza wajane mikono mitupu

    na kuzivunja nguvu za yatima.

    10 Ndiyo sababu mitego imekuzunguka pande zote,

    hatari ya ghafula inakutia hofu,

    11 ndiyo sababu ni giza sana huwezi kuona,

    tena ndiyo sababu mafuriko ya maji yamekufunika.

  51. 24 Kuna mtu atoaye kwa ukarimu, hata hivyo hupata zaidi,

    mwingine huzuia, lakini huwa maskini.

    25 Mtu mkarimu atastawi;

    yeye awaburudishaye wengine

    ataburudishwa mwenyewe.

  52. 23 Kazi zote zinazofanywa kwa bidii huleta faida,

    bali mazungumzo matupu huelekea umaskini tu.

  53. 5 Yeye anaye mdhihaki maskini huonyesha dharau kwa Muumba wake;

    yeyote afurahiaye maafa hataepuka kuadhibiwa.

  54. 17 Yeye amhurumiaye maskini humkopesha Bwana,

    naye atamtuza kwa aliyotenda.

  55. 22 Lile mtu alionealo shauku ni upendo usio na mwisho,

    afadhali kuwa maskini kuliko kuwa mwongo.

  56. 17 Mtu apendaye anasa atakuwa maskini,

    yeyote apendaye mvinyo na mafuta kamwe hatakuwa tajiri.

  57. 8 “Sema kwa ajili ya wale wasioweza kujisemea,

    kwa ajili ya haki za wote walioachwa ukiwa.

    9 Sema na uamue kwa haki,

    tetea haki za maskini na wahitaji.”

  58. 8 (yeye ambaye alifanya Kilimia na Orioni,

    ambaye hugeuza giza kuwa mapambazuko

    na mchana kuwa usiku,

    ambaye huyaita maji ya bahari

    na kuyamwaga juu ya uso wa nchi:

    Bwana ndilo jina lake;

    9 yeye hufanya maangamizo kwenye ngome

    na kufanya mji uliozungushiwa ngome kuwa ukiwa),

    10 mnamchukia yule akemeaye mahakamani,

    na kumdharau yule ambaye husema kweli.

    11 Mnamgandamiza maskini

    na kumlazimisha awape nafaka.

    Kwa hiyo, ingawa mmejenga majumba ya mawe ya fahari,

    hamtaishi ndani yake;

    ingawa mmepanda mashamba mazuri ya mizabibu,

    hamtakunywa divai yake.

    12 Kwa kuwa ninajua hesabu ya makosa yenu

    na ukubwa wa dhambi zenu.

    Mmewaonea wenye haki na kupokea rushwa

    na kuzuia haki ya maskini mahakamani.

    13 Kwa hiyo mtu mwenye busara hunyamaza kimya nyakati kama hizo,

    kwa kuwa nyakati ni mbaya.

  59. 21 “Yule mtumishi akarudi, akampa bwana wake taarifa. Ndipo yule mwenye nyumba akakasirika, akamwagiza yule mtumishi wake, akisema, ‘Nenda upesi kwenye mitaa na vichochoro vya mjini uwalete maskini, vilema, vipofu na viwete.’

  60. 8 Lakini Zakayo akasimama na kumwambia Bwana, “Tazama, Bwana! Sasa hivi nusu ya mali yangu ninawapa maskini, nami kama nimemdhulumu mtu yeyote kitu chochote, nitamrudishia mara nne ya hicho kiwango.”

  61. Mateso Na Kuenea Kwa Injili

    1 Basi ikawa katika siku hizo, wakati idadi ya wanafunzi ilipokuwa ikiongezeka sana, palitokea manungʼuniko kati ya Wayahudi wa Kiyunani, dhidi ya Waebrania kwa sababu wajane wao walisahaulika katika mgawanyo wa chakula wa kila siku.

  62. 35 Katika kila jambo nimewaonyesha kwamba kwa njia hii ya kufanya kazi kwa bidii imetupasa kuwasaidia wadhaifu, mkikumbuka maneno ya Bwana Yesu mwenyewe jinsi alivyosema, ‘Ni heri kutoa kuliko kupokea.’ ”

  63. 9 Mjane yeyote asiwekwe kwenye orodha ya wajane isipokuwa awe ametimiza umri wa miaka sitini, na ambaye alikuwa mke wa mume mmoja, 10 awe ameshuhudiwa kwa matendo yake mema, aliyewalea watoto wake vizuri, aliye mkarimu, aliyewanawisha watakatifu miguu, aliyewasaidia wenye shida na aliyejitolea kwa ajili ya matendo mema ya kila namna.

  64. 15 Nayajua matendo yako, ya kwamba wewe si baridi wala si moto. Afadhali ungelikuwa moja au lingine. 16 Hivyo kwa kuwa u vuguvugu, si baridi wala moto, nitakutapika utoke kinywani mwangu. 17 Kwa maana unasema: ‘Mimi ni tajiri, nimejilimbikizia mali, wala sihitaji kitu chochote.’ Lakini hutambui ya kwamba wewe ni mnyonge, wa kuhurumiwa, maskini, kipofu, tena uliye uchi. 18 Nakushauri ununue kutoka kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, ili upate kuwa tajiri, na mavazi meupe ili uyavae upate kuficha aibu ya uchi wako, na mafuta ya kupaka macho yako ili upate kuona.

    19 “Wale niwapendao, ninawakemea na kuwaadibisha. Hivyo uwe na bidii ukatubu. 20 Tazama! Nasimama mlangoni nabisha. Kama mtu yeyote akisikia sauti yangu na kufungua mlango, nitaingia ndani na kula pamoja naye, naye pamoja nami.

    21 “Yeye ashindaye nitampa haki ya kuketi pamoja nami kwenye kiti changu cha enzi, kama vile mimi nilivyoshinda na nikaketi pamoja na Baba yangu kwenye kiti chake cha enzi. 22 Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho ayaambia makanisa.”

  65. 17 Waovu wataishia kuzimu,

    naam, mataifa yote wanaomsahau Mungu.

    18 Lakini mhitaji hatasahaulika siku zote,

    wala matumaini ya walioonewa hayatapotea.

  66. 5 “Kwa sababu ya uonevu wa wanyonge

    na kulia kwa uchungu kwa wahitaji,

    nitainuka sasa,” asema Bwana.

    “Nitawalinda kutokana na wale

    wenye nia mbaya juu yao.”

  67. 10 Ee Mungu, watu wako waliishi huko,

    nawe kwa wingi wa utajiri wako

    uliwapa maskini mahitaji yao.

  68. 12 Kwa maana atamwokoa mhitaji anayemlilia,

    aliyeonewa asiye na wa kumsaidia.

    13 Atawahurumia wanyonge na wahitaji

    na kuwaokoa wahitaji kutoka mauti.

    14 Atawaokoa kutoka uonevu na ukatili,

    kwani damu yao ni ya thamani machoni pake.

    15 Aishi maisha marefu!

    Na apewe dhahabu ya Sheba.

    Watu wamwombee daima

    na kumbariki mchana kutwa.

  69. 31 Yeye amwoneaye maskini huonyesha dharau kwa Muumba wao,

    bali yeyote anayemhurumia mhitaji humheshimu Mungu.

  70. 6 Afadhali maskini ambaye mwenendo wake hauna lawama

    kuliko tajiri ambaye njia zake ni potovu.

  71. 16 Aliwatetea maskini na wahitaji,

    hivyo yeye akafanikiwa katika yote.

    Je, hiyo si ndiyo maana ya kunijua mimi?”

    asema Bwana.

  72. 4 Lisikieni hili, ninyi ambao mnawagandamiza wahitaji,

    na kuwaonea maskini wa nchi,

    5 mkisema,

    “Ni lini Mwezi Mwandamo utakapopita

    ili tupate kuuza nafaka,

    na Sabato itakwisha lini

    ili tuweze kuuza ngano?”

    Mkipunguza vipimo,

    na kuongeza bei,

    na kudanganya kwa mizani zisizo sawa,

    6 mkiwanunua maskini kwa fedha,

    na wahitaji kwa jozi ya viatu,

    na mkiuza hata takataka za ngano

    pamoja na ngano.

  73. 1 Basi sasa ndugu, nataka ninyi mjue kuhusu ile neema ambayo Mungu amewapa makanisa ya Makedonia. 2 Pamoja na majaribu makali na taabu walizopata, furaha waliyokuwa nayo ilikuwa kubwa, ingawa walikuwa maskini kupindukia, kwa upande wao walifurika kwa wingi wa ukarimu. 3 Kwa maana nashuhudia kwamba wao walitoa kwa kadiri wawezavyo, hata na zaidi ya uwezo wao, kwa hiari yao wenyewe, 4 wakitusihi kwa bidii wapewe fursa ya kushiriki katika huduma hii ya kuwasaidia watakatifu. 5 Wala hawakufanya tulivyotazamia, bali walijitoa wao wenyewe kwa Bwana kwanza na ndipo wakajitoa kwa ajili yetu, kufuatana na mapenzi ya Mungu.

  74. 28 Yeye ambaye amekuwa akiiba, asiibe tena, lakini lazima ajishughulishe, afanye kitu kifaacho kwa mikono yake mwenyewe, ili awe na kitu cha kuwagawia wahitaji.

  75. 1 Bwana akamtuma Nathani kwa Daudi. Alipofika kwake akamwambia, “Katika mji mmoja kulikuwepo na watu wawili, mmoja alikuwa tajiri na mwingine alikuwa maskini. 2 Yule mtu tajiri alikuwa na idadi kubwa sana ya kondoo na ngʼombe, 3 lakini yule maskini hakuwa na chochote ila kondoo jike mdogo aliyekuwa amemnunua. Akamtunza kondoo huyo, akakulia kwake pamoja na watoto wake. Kondoo huyo alishiriki chakula cha bwana wake na kunywea kikombe chake hata pia huyo kondoo alilala mikononi mwa bwana wake. Kwake alikuwa kama binti yake.

    4 “Siku moja yule tajiri akafikiwa na mgeni, lakini huyo tajiri akaacha kuchukua mmoja wa kondoo au ngʼombe wake mwenyewe amwandalie mgeni. Badala yake akachukua yule kondoo jike mdogo aliyekuwa mali ya yule maskini na kumwandalia yule mgeni wake.”

    5 Daudi akawakwa na hasira dhidi ya mtu huyo tajiri na kumwambia Nathani, “Hakika kama Bwana aishivyo, mtu huyo aliyefanya hivyo anastahili kufa! 6 Lazima alipe mara nne zaidi, kwa ajili ya kondoo huyo, kwa sababu amefanya jambo kama hilo na hakuwa na huruma.”

  76. Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.

    1 Heri mtu yule anayemjali mnyonge,

    Bwana atamwokoa wakati wa shida.

    2 Bwana atamlinda na kuyahifadhi maisha yake,

    atambariki katika nchi

    na hatamwacha katika tamaa ya adui zake.

    3 Bwana atamtegemeza awapo mgonjwa kitandani,

    atamwinua kutoka kitandani mwake.

  77. 16 Yeye amwoneaye maskini ili kujiongezea mali,

    naye ampaye tajiri zawadi, wote huwa maskini.

  78. 7 “Ninakuomba vitu viwili, Ee Bwana;

    usininyime kabla sijafa:

    8 Uutenge mbali nami udanganyifu na uongo;

    usinipe umaskini wala utajiri,

    bali unipe chakula cha kunitosha kila siku.

    9 Nisije nikawa na vingi vya kuzidi nikakukana

    na kusema, ‘Bwana ni nani?’

    Au nisije nikawa maskini nikaiba,

    nami nikaliaibisha jina la Mungu wangu.

  79. 13 Bwana anachukua nafasi yake mahakamani,

    anasimama kuhukumu watu.

    14 Bwana anaingia katika hukumu

    dhidi ya wazee na viongozi wa watu wake:

    “Ninyi ndio mlioharibu shamba langu la mizabibu,

    mali zilizonyangʼanywa maskini zimo nyumbani mwenu.

    15 Mnamaanisha nini kuwaponda watu wangu

    na kuzisaga nyuso za maskini?”

    asema Bwana, Bwana Mwenye Nguvu Zote.

  80. 32 Wale walioamini wote walikuwa na moyo mmoja na nia moja. Wala hakuna hata mmoja aliyesema chochote alichokuwa nacho ni mali yake mwenyewe, lakini walishirikiana kila kitu walichokuwa nacho. 33 Mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwa Bwana Yesu kwa nguvu nyingi na neema ya Mungu ilikuwa juu yao wote. 34 Wala hapakuwepo mtu yeyote miongoni mwao aliyekuwa mhitaji, kwa sababu mara kwa mara wale waliokuwa na mashamba na nyumba waliviuza, wakaleta thamani ya vitu vilivyouzwa, 35 wakaiweka miguuni pa mitume, kila mtu akagawiwa kadiri ya mahitaji yake.

  81. 14 “ ‘Usimlaani kiziwi, wala usiweke kikwazo mbele ya kipofu, lakini umche Mungu wako. Mimi ndimi Bwana.

    15 “ ‘Usipotoshe haki; usionyeshe kumpendelea maskini, wala upendeleo kwa mwenye cheo, bali mwamulie jirani yako kwa haki.

    16 “ ‘Usieneze uchochezi miongoni mwa watu wako.

    “ ‘Usifanye kitu chochote kile kinachohatarisha maisha ya jirani yako. Mimi ndimi Bwana.

  82. 14 Lakini wewe, Ee Mungu, unaona shida na huzuni,

    umekubali kuyapokea mkononi mwako.

    Mhanga anajisalimisha kwako,

    wewe ni msaada wa yatima.

  83. 15 Mali ya tajiri ni mji wake wenye ngome,

    bali ufukara ni maangamizi ya maskini.

  84. 30 Nilipita karibu na shamba la mvivu,

    karibu na shamba la mizabibu la mtu asiye na akili,

    31 miiba ilikuwa imeota kila mahali,

    ardhi ilikuwa imefunikwa na magugu, na

    ukuta wa mawe ulikuwa umebomoka.

    32 Nikatafakari moyoni mwangu lile nililoliona,

    nami nikajifunza somo kutokana na niliyoyaona:

    33 Bado kulala kidogo, kusinzia kidogo,

    bado kukunja mikono kidogo upate kupumzika:

    34 hivyo umaskini utakuja juu yako kama mnyangʼanyi,

    na kupungukiwa kutakujia kama mtu mwenye silaha.

  85. 17 Yesu alipokuwa anaondoka, mtu mmoja akamkimbilia, akapiga magoti mbele yake, akamuuliza, “Mwalimu mwema, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?”

    18 Yesu akamwambia, “Mbona unaniita mwema? Hakuna yeyote aliye mwema ila Mungu peke yake. 19 Unazijua amri: ‘Usiue, usizini, usiibe, usishuhudie uongo, usidanganye, waheshimu baba yako na mama yako.’ ”

    20 Akamjibu, “Mwalimu, amri hizi zote nimezishika tangu nikiwa mtoto.”

    21 Yesu akamtazama na kumpenda, akamwambia, “Umepungukiwa na kitu kimoja. Nenda ukauze kila kitu ulicho nacho uwape maskini hizo fedha, nawe utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.”

    22 Yule mtu aliposikia hayo, akasikitika sana. Akaondoka kwa huzuni kwa sababu alikuwa na mali nyingi.

  86. 22 Hivyo akawajibu wale wajumbe, “Rudini mkamwambie Yohana yote mnayoyaona na kuyasikia: Vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa na maskini wanahubiriwa habari njema.

  87. 9 Ndugu asiye na cheo kikubwa yampasa ajivunie hali hiyo maana ametukuzwa. 10 Lakini yeye aliye tajiri afurahi kwa kuwa ameshushwa, kwa sababu atatoweka kama ua la shambani. 11 Kwa maana jua kali lenye kuchoma huchomoza na kuliunguza, likayakausha majani, na ua lake likapukutika, nao uzuri wake huharibika. Vivyo hivyo tajiri naye atanyauka akiwa anaendelea na shughuli zake.

  88. 1 Mke wa mmoja wa wana wa manabii akamlilia Elisha, akamwambia, “Mtumishi wako, mume wangu, amekufa, nawe unajua alikuwa anamcha Bwana. Lakini sasa yule anayemdai anakuja kuchukua wanangu wawili kama watumwa wake.”

    2 Elisha akamjibu, “Nitawezaje kukusaidia? Niambie, una nini ndani ya nyumba yako?”

    Akasema, “Mtumishi wako hana kitu chochote kabisa, isipokuwa mafuta kidogo.”

    3 Elisha akasema, “Zunguka kwa majirani zako wote ukaombe vyombo vitupu. Usiombe vichache. 4 Kisha ingia ndani na ujifungie mlango, wewe na wanao. Mimina mafuta kwenye vyombo vyote, na kila kimoja kinapojaa, kiweke kando.”

    5 Yule mjane akaondoka na kujifungia ndani, yeye na wanawe. Wao wakamletea vyombo, naye akaendelea kumimina mafuta. 6 Vyombo vyote vilipojaa, akamwambia mwanawe, “Niletee chombo kingine.”

    Lakini mwanawe akajibu, “Hakuna chombo kingine kilichobaki.” Basi mafuta yakakoma kutiririka.

    7 Yule mwanamke akaenda akamwambia yule mtu wa Mungu, naye mtu wa Mungu akasema, “Nenda ukayauze hayo mafuta ulipe madeni yako. Wewe na wanao mnaweza kuishi kwa kile kinachosalia.”

  89. 6 Umedai dhamana kwa ndugu zako bila sababu;

    umewavua watu nguo zao, ukawaacha uchi.

    7 Hukumpa maji aliyechoka,

    nawe ulimnyima chakula mwenye njaa,

  90. 5 Wale wamtazamao hutiwa nuru,

    nyuso zao hazifunikwi na aibu kamwe.

    6 Maskini huyu alimwita Bwana, naye akamsikia,

    akamwokoa katika taabu zake zote.

  91. 4 Mikono mivivu hufanya mtu kuwa maskini

    lakini mikono yenye bidii huleta utajiri.

  92. 5 Mipango ya mwenye bidii huelekeza kwenye faida,

    kama vile kwa hakika pupa huelekeza kwenye umaskini.

  93. 4 Umekuwa kimbilio la watu maskini,

    kimbilio la mhitaji katika taabu yake,

    hifadhi wakati wa dhoruba

    na kivuli wakati wa hari.

    Kwa maana pumzi ya wakatili

    ni kama dhoruba ipigayo ukuta

  94. 41 “Kisha atawaambia wale walio upande wake wa kushoto, ‘Ondokeni kwangu, ninyi mliolaaniwa, nendeni kwenye moto wa milele ulioandaliwa kwa ajili ya ibilisi na malaika zake. 42 Kwa maana nilikuwa na njaa hamkunipa chakula, nilikuwa na kiu hamkuninywesha, 43 nilikuwa mgeni nanyi hamkunikaribisha, nilikuwa uchi hamkunivika, nilikuwa mgonjwa hamkunitunza, na nilikuwa gerezani nanyi hamkuja kunitembelea.’

    44 “Ndipo wao pia watajibu, ‘Bwana ni lini tulikuona ukiwa na njaa au kiu, au ukiwa mgeni au uchi, au ukiwa mgonjwa na kifungoni na hatukukuhudumia?’

    45 “Naye atawajibu, ‘Amin nawaambia, kwa jinsi ambavyo hamkumtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu walio wadogo, hamkunitendea mimi.’

    46 “Ndipo hawa watakapoingia kwenye adhabu ya milele, lakini wale wenye haki wataingia katika uzima wa milele.”

  95. 10 Kwa hiyo, kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema, hasa wale wa jamaa ya waaminio.

  96. 9 Sasa kuhusu upendo wa ndugu hamna haja mtu yeyote kuwaandikia, kwa maana ninyi wenyewe mmefundishwa na Mungu kupendana. 10 Nanyi kwa kweli mnawapenda ndugu wote katika Makedonia nzima. Lakini ndugu, tunawasihi mzidi sana kuwapenda.

    11 Jitahidini kuishi maisha ya utulivu, kila mtu akijishughulisha na mambo yake mwenyewe na kufanya kazi kwa mikono yake, kama vile tulivyowaagiza, 12 ili maisha yenu ya kila siku yajipatie heshima kutoka kwa watu walio nje, ili msimtegemee mtu yeyote.

  97. 9 Mtu mkarimu yeye mwenyewe atabarikiwa

    kwa kuwa hushiriki chakula chake na maskini.

  98. 3 Kama nikitoa mali yote niliyo nayo na kama nikijitolea mwili wangu uchomwe moto, kama sina upendo, hainifaidi kitu.

  99. 9 Sasa rudini haraka kwa baba yangu na mwambieni, ‘Hili ndilo mwanao Yosefu asemalo: Mungu amenifanya mimi kuwa bwana wa Misri yote. Shuka uje kwangu, wala usikawie. 10 Nawe utaishi katika nchi ya Gosheni na kuwa karibu nami, wewe, watoto wako na wajukuu wako, makundi yako ya kondoo, mbuzi na ngʼombe, pamoja na vyote ulivyo navyo. 11 Nitawatunza huko, kwa sababu bado iko miaka mingine mitano inayokuja ya njaa. La sivyo, wewe na nyumba yako na wote ulio nao mtakuwa fukara.’

  100. 9 “ ‘Wakati uvunapo mavuno ya nchi yako, usivune hadi kwenye mipaka ya shamba lako, wala usikusanye mabaki ya mavuno yako. 10 Usirudi mara ya pili katika shamba lako la mizabibu, wala usiokote zabibu zilizoanguka chini. Ziache kwa ajili ya maskini na mgeni. Mimi ndimi Bwana Mungu wako.

  101. 25 “ ‘Ikiwa mmoja wa wazawa wa nchi yako amekuwa maskini na akauza baadhi ya mali yake, ndugu yake wa karibu atakuja na kukomboa kile ndugu yako alichokiuza. 26 Iwapo mtu huyo hana jamaa wa karibu wa kukomboa mali hiyo kwa ajili yake, lakini yeye mwenyewe akafanikiwa na kupata mali itoshayo kuikomboa, 27 ataamua tena thamani yake kwa miaka tangu alipoiuza, na kurudisha kiasi kilichobaki cha thamani kwa mtu ambaye alikuwa amemuuzia mali hiyo, naye ataweza kuirudia mali yake. 28 Lakini kama hatapata njia ya kumlipa mnunuzi, ile mali aliyouza itabaki kumilikiwa na mnunuzi mpaka Mwaka wa Yubile. Mali hiyo itarudishwa mwaka wa Yubile, naye ataweza kuirudia mali yake.

    29 “ ‘Ikiwa mtu atauza nyumba iliyo ndani ya mji uliozungukwa kwa ukuta, yeye anayo haki ya kuikomboa mwaka mzima baada ya mauzo ya hiyo nyumba. Wakati huo anaweza kuikomboa. 30 Ikiwa haikukombolewa kabla ya mwaka mmoja kamili kupita, nyumba iliyo ndani ya mji uliozungukwa kwa ukuta itakuwa mali ya kudumu ya mnunuzi na wazao wake. Haitarudishwa mwaka wa Yubile.

  102. 28 Mwishoni mwa kila mwaka wa tatu, leteni zaka zote za mazao ya miaka ile na uyahifadhi kwenye miji yenu, 29 ili Walawi (ambao hawana mashamba wala urithi wao wenyewe) na wageni, yatima na wajane wanaoishi kwenye miji yenu wapate kuja kula na kushiba, ili Bwana Mungu wenu apate kuwabariki ninyi katika kazi zote za mikono yenu.

  103. 10 Unapomkopesha jirani yako chochote, usiingie nyumbani kwake kutwaa kile anachokitoa kama rehani. 11 Ukae nje na umwache huyo mtu uliyemkopesha akuletee hiyo rehani. 12 Ikiwa mtu huyo ni maskini, usiende kulala ukiwa na hiyo rehani yake katika milki yako. 13 Rudisha vazi lake kabla ya machweo ya jua ili apate kulilalia. Kisha atakushukuru na kitaonekana kama kitendo cha haki mbele za Bwana Mungu wako.

    14 Usimwonee mtu maskini na mhitaji ambaye umemwajiri, akiwa ni nduguyo Mwisraeli au mgeni anayeishi katika mojawapo ya miji yenu. 15 Mlipe ujira wake kila siku kabla ya jua kutua, kwa sababu yeye ni maskini na anautegemea ujira huo. La sivyo, anaweza kumlilia Bwana dhidi yako, nawe ukapata hatia ya dhambi.

  104. 7 Bwana humfanya mtu maskini naye hutajirisha,

    hushusha na hukweza.

    8 Humwinua maskini kutoka mavumbini

    na humwinua mhitaji kutoka lundo la majivu;

    huwaketisha pamoja na wakuu

    na kuwafanya warithi kiti cha enzi cha heshima.

    “Kwa kuwa misingi ya dunia ni ya Bwana;

    juu yake ameuweka ulimwengu.

  105. 10 “Aweza kuwa ana mwana jeuri, amwagaye damu au atendaye mojawapo ya mambo haya 11 (ingawa baba yake hakufanya mojawapo ya haya):

    “Hula katika mahali pa ibada za miungu kwenye milima.

    Humtia unajisi mke wa jirani yake.

    12 Huwaonea maskini na wahitaji.

    Hunyangʼanyana.

    Harudishi kile kilichowekwa rehani kwake.

    Huziinulia sanamu macho.

    Hufanya mambo ya machukizo.

    13 Hukopesha kwa riba na kutafuta faida ya ziada.

    Je, mtu wa namna hii ataishi? Hapana, hataishi! Kwa sababu amefanya mambo haya yote ya machukizo, hakika atauawa na damu yake itakuwa juu ya kichwa chake mwenyewe.