54 Bible Verses About Finances

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Finances
  1. 10 “Yeyote aliye mwaminifu katika mambo madogo, pia ni mwaminifu hata katika mambo makubwa, naye mtu ambaye si mwaminifu katika mambo madogo pia si mwaminifu katika mambo makubwa. 11 Ikiwa hamkuwa waaminifu katika mali ya kidunia, ni nani atakayewaaminia mali ya kweli? 12 Nanyi kama hamkuwa waaminifu na mali ya mtu mwingine, ni nani atakayewapa iliyo yenu wenyewe?

    13 “Hakuna mtumishi awezaye kuwatumikia mabwana wawili. Kwa kuwa atamchukia huyu na kumpenda yule mwingine, au atashikamana sana na huyu na kumdharau yule mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu pamoja na Mali.”

  2. 6 Lakini utauwa na kuridhika ni faida kubwa. 7 Kwa kuwa hatukuja humu duniani na kitu chochote, wala hatuwezi kutoka humu na kitu. 8 Lakini kama tuna chakula na mavazi, tutaridhika navyo. 9 Lakini wale watu wanaotamani kuwa na mali kwa haraka huanguka kwenye majaribu, na wamenaswa na tamaa nyingi za kipumbavu zenye kudhuru, zinazowazamisha watu katika uharibifu na maangamizi. 10 Kwa maana kupenda fedha ndiyo shina moja la maovu ya kila namna. Baadhi ya watu wakitamani fedha, wameiacha imani na kujichoma wenyewe kwa maumivu mengi.

    11 Lakini wewe, mtu wa Mungu, yakimbie mambo haya yote. Fuata haki, utauwa, imani, upendo, saburi na upole.

  3. 6 Kumbukeni kwamba: Yeyote apandaye kwa uchache pia atavuna kwa uchache, naye apandaye kwa ukarimu pia atavuna kwa ukarimu. 7 Kila mtu atoe kama anavyokusudia moyoni mwake, si kwa uchoyo au kwa kulazimishwa, kwa maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo mkunjufu. 8 Naye Mungu aweza kuwapa kila baraka kwa wingi, ili katika mambo yote kila wakati, mwe na kila kitu mnachohitaji, ili mweze kushiriki kwa wingi katika kila kazi njema. 9 Kama ilivyoandikwa:

    “Ametawanya vipawa vyake kwa ukarimu

    akawapa maskini;

    haki yake hudumu milele.”

    10 Yeye ampaye mpanzi mbegu kwa ajili ya kupanda na mkate kuwa chakula, atawapa na kuzizidisha mbegu zenu za kupanda na kuongeza mavuno ya haki yenu. 11 Mtatajirishwa kwa kila namna ili mpate kuwa wakarimu kila wakati, na kupitia kwetu, ukarimu wenu utamletea Mungu shukrani.

  4. 19 Naye Mungu wangu atawajaza ninyi na kila mnachohitaji kwa kadiri ya utajiri wake katika utukufu ndani ya Kristo Yesu.

  5. 19 “Msijiwekee hazina duniani, mahali ambapo nondo na kutu huharibu, nao wevi huvunja na kuiba. 20 Lakini jiwekeeni hazina mbinguni, mahali ambapo nondo na kutu haviharibu, wala wevi hawavunji na kuiba. 21 Kwa sababu mahali hazina yako ilipo, hapo ndipo pia moyo wako utakapokuwa.

  6. 17 Waagize wale ambao ni matajiri wa ulimwengu huu waache kujivuna, wala wasiweke tumaini lao katika mali ambayo si ya hakika, bali waweke tumaini lao katika Mungu ambaye hutupatia vitu vyote kwa wingi ili tuvifurahie. 18 Waagize watende mema, wawe matajiri katika matendo mema, pia wawe wakarimu na walio tayari kushiriki mali zao na wengine. 19 Kwa njia hii watajiwekea hazina kama msingi kwa ajili ya wakati ujao na hivyo watajipatia uzima, yaani, ule uzima ambao ni wa kweli.

  7. 5 Yalindeni maisha yenu msiwe na tabia ya kupenda fedha, bali mridhike na vile mlivyo navyo, kwa sababu Mungu amesema,

    “Kamwe sitakuacha,

    wala sitakupungukia.”

  8. 7 Matajiri huwatawala maskini

    naye akopaye ni mtumwa wa akopeshaye.

  9. 10 Nina furaha kubwa katika Bwana kwamba hatimaye mmeanza upya kushughulika tena na maisha yangu. Kweli mmekuwa mkinifikiria lakini mlikuwa hamjapata nafasi ya kufanya hivyo. 11 Sisemi hivyo kwa vile nina mahitaji, la! Kwa maana nimejifunza kuridhika katika hali yoyote. 12 Ninajua kupungukiwa, pia ninajua kuwa na vingi. Nimejifunza siri ya kuridhika katika kila hali, wakati wa kushiba na wakati wa kuona njaa, wakati wa kuwa na vingi na wakati wa kupungukiwa. 13 Naweza kuyafanya mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.

  10. 10 Yeyote apendaye fedha kamwe

    hatosheki na fedha;

    yeyote apendaye utajiri kamwe

    hatosheki na kipato chake.

    Hili nalo pia ni ubatili.

  11. 8 “Je, mwanadamu atamwibia Mungu? Hata hivyo mnaniibia mimi.

    “Lakini mnauliza, ‘Tunakuibia kwa namna gani?’

    “Mnaniibia zaka na dhabihu. 9 Mko chini ya laana, ninyi taifa lote, kwa sababu mnaniibia mimi. 10 Leteni zaka kamili ghalani, ili kuwe na chakula katika nyumba yangu. Nijaribuni katika hili,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote, “nanyi mwone kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni na kuwamwagieni baraka nyingi mpaka mkose nafasi ya kutosha.

  12. 30 Basi ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya shambani, ambayo leo yapo na kesho yanatupwa motoni, je, hatawavika ninyi vizuri zaidi, enyi wa imani haba? 31 Kwa hiyo msiwe na wasiwasi, mkisema, ‘Tutakula nini?’ au ‘Tutakunywa nini?’ au ‘Tutavaa nini?’ 32 Watu wasiomjua Mungu ndio wanaoshindania hayo, lakini Baba yenu wa mbinguni anafahamu kuwa mnahitaji haya yote. 33 Lakini utafuteni kwanza Ufalme wa Mungu na haki yake, na haya yote atawapa pia. 34 Kwa hiyo msiwe na wasiwasi kuhusu kesho, kwa sababu kesho itajitaabikia yenyewe. Yatosha kwa siku masumbufu yake.

  13. 8 Msidaiwe kitu na mtu yeyote, isipokuwa kupendana, kwa maana yeye ampendaye mwenzake, ameitimiza sheria.

  14. 2 Siku ya kwanza ya kila juma, kila mmoja wenu atenge kiasi cha fedha, kulingana na mapato yake na fedha hizo aziweke akiba, ili nitakapokuja pasiwe na lazima ya kufanya mchango.

  15. 17 Mnaweza kusema, “Uwezo wangu na nguvu za mikono yangu ndizo zilizonipatia utajiri huu.” 18 Lakini kumbukeni Bwana Mungu wenu, ndiye ambaye huwapa uwezo wa kupata utajiri, na hivyo kulithibitisha Agano lake, ambalo aliwaapia baba zenu, kama ilivyo leo.

  16. 9 Mheshimu Bwana kwa mali zako na

    kwa malimbuko ya mazao yako yote;

    10 ndipo ghala zako zitakapojaa hadi kufurika,

    viriba vyako vitafurika kwa mvinyo mpya.

  17. 5 Mipango ya mwenye bidii huelekeza kwenye faida,

    kama vile kwa hakika pupa huelekeza kwenye umaskini.

  18. 20 Katika nyumba ya mwenye hekima

    kuna akiba ya vyakula vizuri na mafuta,

    lakini mtu mpumbavu

    hutafuna vyote alivyo navyo.

  19. 38 Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa. Kipimo cha kujaa na kushindiliwa na kusukwasukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile mpimacho, ndicho mtakachopimiwa.”

  20. 15 Ndipo Yesu akawaambia, “Jihadharini! Jilindeni na aina zote za choyo. Kwa maana maisha ya mtu hayatokani na wingi wa mali alizo nazo.”

  21. 28 “Ni nani miongoni mwenu ambaye kama anataka kujenga nyumba, hakai kwanza chini na kufanya makisio ya gharama aone kama ana fedha za kutosha kukamilisha? 29 La sivyo, akiisha kuweka msingi, naye akiwa hana uwezo wa kuikamilisha, wote waionao wataanza kumdhihaki, 30 wakisema, ‘Mtu huyu alianza kujenga lakini hakuweza kukamilisha.’

  22. 4 Usijitaabishe ili kuupata utajiri,

    uwe na hekima kuonyesha kujizuia.

  23. 23 Hakikisha kuwa unajua hali ya makundi yako

    ya kondoo na mbuzi,

    angalia kwa bidii ngʼombe zako.

    24 Kwa kuwa utajiri haudumu milele,

    nayo taji haidumu vizazi vyote.

  24. 20 “Kisha akaja yule mtumishi mwingine, akasema, ‘Bwana, hii hapa fedha yako. Niliitunza vizuri kwenye kitambaa. 21 Nilikuogopa, kwa sababu wewe ni mtu mgumu. Unachukua ambapo hukuweka kitu, na unavuna mahali ambapo hukupanda kitu.’

    22 “Bwana wake akamjibu, ‘Nitakuhukumu kwa maneno yako mwenyewe, wewe mtumishi mwovu! Kama ulifahamu kwamba mimi ni mtu mgumu, nichukuaye mahali ambapo sikuweka kitu na kuvuna mahali ambapo sikupanda, 23 kwa nini basi hukuweka fedha zangu kwa watoa riba, ili nitakaporudi nichukue iliyo yangu na riba yake?’

    24 “Ndipo akawaambia wale waliokuwa wamesimama karibu, ‘Mnyangʼanyeni fungu lake la fedha, mkampe yule mwenye kumi.’

    25 “Wakamwambia, ‘Bwana, mbona; tayari anayo mafungu kumi!’

    26 “Akawajibu, ‘Nawaambia kwamba kila aliye na kitu, ataongezewa. Lakini yule asiye na kitu, hata alicho nacho atanyangʼanywa.

  25. 8 Kama mtu hawatunzi wale wa jamaa yake, hasa wale wa nyumbani mwake mwenyewe, ameikana imani, tena ni mbaya kuliko yeye asiyeamini.

  26. 1 Basi sikilizeni, ninyi matajiri, lieni na kuomboleza kwa ajili ya hali mbaya sana inayowajia. 2 Utajiri wenu umeoza na mavazi yenu yameliwa na nondo. 3 Dhahabu yenu na fedha yenu vimeliwa na kutu. Kutu yake itashuhudia dhidi yenu nayo itaila miili yenu kama vile moto. Mmejiwekea hazina kwa ajili ya siku za mwisho.

  27. 26 Usiwe mwenye kupana mikono katika rehani,

    au kuweka dhamana kwa ajili ya madeni.

    27 Kama ukikosa njia ya kulipa,

    kitanda chako

    kitachukuliwa ukiwa umekilalia.

  28. 24 Baada ya Yesu na wanafunzi wake kufika Kapernaumu, wakusanya kodi ya Hekalu wakamjia Petro na kumuuliza, “Je, Mwalimu wenu halipi kodi ya Hekalu?”

    25 Petro akajibu, “Ndiyo, yeye hulipa.” Petro aliporudi nyumbani, Yesu akawa wa kwanza kulizungumzia, akamuuliza, “Unaonaje Simoni? Wafalme wa dunia hupokea ushuru na kodi kutoka kwa nani? Je, ni kutoka kwa watoto wao au kutoka kwa watu wengine?”

    26 Petro akamjibu, “Kutoka kwa watu wengine.” Yesu akamwambia, “Kwa hiyo watoto wao wamesamehewa. 27 Lakini ili tusije tukawaudhi, nenda baharini ukatupe ndoana. Mchukue samaki wa kwanza utakayemvua. Fungua kinywa chake nawe utakuta humo fedha, ichukue ukalipe kodi yako na yangu.”

  29. 12 Yesu akaingia katika eneo la Hekalu na kuwafukuza wote waliokuwa wakinunua na kuuza vitu Hekaluni. Akazipindua meza za wale waliokuwa wakibadilisha fedha, na pia viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa. 13 Akawaambia, “Imeandikwa, ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala,’ lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyangʼanyi.”

  30. 22 Baraka ya Bwana hutajirisha,

    wala haichanganyi huzuni.

  31. 11 Fedha isiyo ya halali hupungua,

    bali yeye akusanyaye fedha kidogo kidogo huongezeka.

  32. 23 Kazi zote zinazofanywa kwa bidii huleta faida,

    bali mazungumzo matupu huelekea umaskini tu.

  33. 32 Wale walioamini wote walikuwa na moyo mmoja na nia moja. Wala hakuna hata mmoja aliyesema chochote alichokuwa nacho ni mali yake mwenyewe, lakini walishirikiana kila kitu walichokuwa nacho. 33 Mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwa Bwana Yesu kwa nguvu nyingi na neema ya Mungu ilikuwa juu yao wote. 34 Wala hapakuwepo mtu yeyote miongoni mwao aliyekuwa mhitaji, kwa sababu mara kwa mara wale waliokuwa na mashamba na nyumba waliviuza, wakaleta thamani ya vitu vilivyouzwa, 35 wakaiweka miguuni pa mitume, kila mtu akagawiwa kadiri ya mahitaji yake.

  34. 35 Katika kila jambo nimewaonyesha kwamba kwa njia hii ya kufanya kazi kwa bidii imetupasa kuwasaidia wadhaifu, mkikumbuka maneno ya Bwana Yesu mwenyewe jinsi alivyosema, ‘Ni heri kutoa kuliko kupokea.’ ”

  35. 7 Ikiwa kuna mtu maskini miongoni mwa ndugu zenu, katika mji wowote wa hiyo nchi ambayo Bwana Mungu wenu anawapa, msiwe na moyo mgumu wala usimfumbie mkono ndugu yako aliye maskini. 8 Afadhali fungua mikono yako na umkopeshe kwa hiari chochote anachohitaji.

  36. 21 Waovu hukopa na hawalipi,

    bali wenye haki hutoa kwa ukarimu.

  37. 4 Mikono mivivu hufanya mtu kuwa maskini

    lakini mikono yenye bidii huleta utajiri.

  38. 22 Mtu mwema huwaachia wana wa wanawe urithi,

    bali mali ya wenye dhambi imehifadhiwa

    kwa ajili ya wenye haki.

  39. 19 Yeye alimaye shamba lake atakuwa na chakula tele,

    bali yule afuataye mambo ya upuzi atakuwa na umaskini wa kumtosha.

  40. 21 Yesu akamwambia, “Kama ukitaka kuwa mkamilifu, nenda, ukauze vitu vyote ulivyo navyo, na hizo fedha uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.”

    22 Yule kijana aliposikia hayo, akaenda zake kwa huzuni, kwa sababu alikuwa na mali nyingi.

    23 Ndipo Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Amin, nawaambia, itakuwa vigumu kwa mtu tajiri kuingia katika Ufalme wa Mbinguni.

  41. 41 Kisha Yesu akaketi mkabala na sehemu ambapo sadaka zilikuwa zinawekwa na kuangalia umati wa watu wakiweka fedha zao kwenye sanduku la hazina ya Hekalu. Matajiri wengi wakaweka kiasi kikubwa cha fedha. 42 Lakini mjane mmoja maskini akaja na kuweka sarafu mbili ndogo za shaba zenye thamani ya senti mbili.

    43 Yesu akawaita wanafunzi wake, akawaambia, “Amin, nawaambia, huyu mjane maskini ameweka katika sanduku la hazina zaidi ya watu wengine wote. 44 Wengine wote wametoa kutokana na ziada ya mali zao. Lakini huyu mjane ametoa kutokana na umaskini wake, akaweka kila kitu alichokuwa nacho, hata kile alichohitaji ili kuishi.”

  42. 12 Watoza ushuru nao wakaja ili wabatizwe, wakamuuliza, “Bwana na sisi inatupasa tufanyeje?”

    13 Akawaambia, “Msichukue zaidi ya kiwango mlichopangiwa.”

    14 Askari nao wakamuuliza, “Je, nasi inatupasa tufanye nini?”

    Akawaambia, “Msimdhulumu mtu wala msimshtaki mtu kwa uongo, bali mridhike na mishahara yenu.”

  43. 16 Kisha akawaambia mfano huu: “Shamba la mtu mmoja tajiri lilizaa sana. 17 Akawaza moyoni mwake, ‘Nifanye nini? Sina mahali pa kuhifadhi mavuno yangu.’

    18 “Ndipo huyo tajiri akasema, ‘Nitafanya hivi: Nitabomoa ghala zangu za nafaka na kujenga nyingine kubwa zaidi na huko nitayahifadhi mavuno yangu yote na vitu vyangu. 19 Nami nitaiambia nafsi yangu, “Nafsi, unavyo vitu vingi vizuri ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi. Pumzika; kula, unywe, ufurahi.” ’

    20 “Lakini Mungu akamwambia, ‘Mpumbavu wewe! Usiku huu uhai wako unatakiwa. Sasa hivyo vitu ulivyojiwekea akiba vitakuwa vya nani?’

    21 “Hivyo ndivyo ilivyo kwa wale wanaojiwekea mali lakini hawajitajirishi kwa Mungu.”

  44. 10 Kwa maana hata tulipokuwa pamoja nanyi, tuliwapa amri kwamba: “Mtu yeyote asiyetaka kufanya kazi, hata kula asile.”

    11 Kwa kuwa tunasikia kwamba baadhi ya watu miongoni mwenu ni wavivu. Hawafanyi kazi bali hujishughulisha na mambo ya wengine. 12 Basi watu kama hao tunawaagiza na kuwahimiza katika Bwana Yesu Kristo, kwamba wafanye kazi kwa utulivu kwa ajili ya chakula chao wenyewe. 13 Kwa upande wenu, ndugu, ninyi kamwe msichoke katika kutenda mema.

    14 Ikiwa mtu yeyote hayatii maagizo yetu yaliyoko katika barua hii, mwangalieni sana mtu huyo. Msishirikiane naye, ili apate kuona aibu. 15 Lakini msimhesabu kuwa adui, bali mwonyeni kama ndugu.

  45. 2 lichungeni kundi la Mungu mlilokabidhiwa, mkitumika kama waangalizi, si kwa kulazimishwa bali kwa hiari, kama Mungu anavyowataka mwe; si kwa tamaa ya fedha, bali mlio na bidii katika kutumika. 3 Msijifanye mabwana juu ya wale walio chini ya uangalizi wenu, bali kuweni vielelezo kwa hilo kundi.

  46. 6 Basi, nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake. 7 Mtwikeni yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana na mambo yenu.

  47. 35 “ ‘Ikiwa mmoja wa wazawa wa nchi yako amekuwa maskini, naye akashindwa kujitegemeza mwenyewe katikati yako, msaidie kama vile ambavyo ungelimsaidia mgeni au kama mkazi wa muda, ili aweze kuendelea kuishi katikati yako. 36 Usichukue riba wala faida yoyote kutoka kwake, bali utamwogopa Mungu wako, ili mzawa wa nchi yako aweze kuendelea kuishi katikati yako. 37 Usimkopeshe fedha ili alipe na riba, wala usimuuzie chakula kwa faida.

  48. 17 Yeye amhurumiaye maskini humkopesha Bwana,

    naye atamtuza kwa aliyotenda.

  49. 17 Tuambie basi, wewe unaonaje? Je, ni halali kulipa kodi kwa Kaisari, au la?”

    18 Lakini Yesu, akijua makusudi yao mabaya, akawaambia, “Enyi wanafiki, kwa nini mnajaribu kunitega? 19 Nionyesheni hiyo sarafu inayotumika kwa kulipia kodi.” Wakamletea dinari. 20 Naye akawauliza, “Sura hii ni ya nani? Na maandishi haya ni ya nani?”

    21 Wakamjibu, “Ni vya Kaisari.”

    Basi Yesu akawaambia, “Mpeni Kaisari kilicho cha Kaisari, naye Mungu mpeni kilicho cha Mungu.”

  50. 32 “Msiogope enyi kundi dogo, kwa maana Baba yenu ameona vyema kuwapa ninyi Ufalme. 33 Uzeni mali zenu mkawape maskini. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, mkajiwekee hazina mbinguni isiyokwisha, mahali ambapo mwizi hakaribii wala nondo haharibu. 34 Kwa sababu mahali hazina yako ilipo, hapo ndipo moyo wako utakapokuwa pia.

  51. 20 Petro akamjibu, “Fedha yako na iangamie pamoja nawe, kwa sababu ulidhani unaweza kununua karama ya Mungu kwa fedha!

  52. 6 Basi, yeye afundishwaye katika neno na amshirikishe mwalimu wake mema yote.

  53. 6 Msijisumbue kwa jambo lolote, bali katika kila jambo kwa kuomba na kusihi pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu.

  54. 17 Kila kitolewacho kilicho chema na kilicho kamili, hutoka juu, na hushuka kutoka kwa Baba wa mianga, ambaye kwake hakuna kubadilika, wala kivuli cha kugeukageuka.