46 Bible Verses About Going to Heaven
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
-
1 Kisha nikaona mbingu mpya na nchi mpya, kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza vimekwisha kupita, wala hapakuwepo na bahari tena. 2 Nikaona Mji Mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, ukiwa umeandaliwa kama bibi arusi aliyepambwa kwa ajili ya mumewe. 3 Nami nikasikia sauti kubwa kutoka kile kiti cha enzi ikisema, “Sasa makao ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atakaa pamoja nao. Yeye atakuwa Mungu wao nao watakuwa watu wake, naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao. 4 Atafuta kila chozi kutoka macho yao. Mauti haitakuwepo tena, wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu, kwa maana mambo ya kwanza yamekwisha kupita.”
5 Naye yule aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi akasema, “Tazama, nayafanya mambo yote kuwa mapya!” Kisha akasema, “Andika haya, maana maneno haya ni ya kuaminika tena ni kweli.”
6 Akaniambia, “Imekwisha kuwa. Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. Yeye aonaye kiu nitampa kunywa kutoka chemchemi ya maji ya uzima bila gharama yoyote. 7 Yeye ashindaye atayarithi haya yote, nami nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu. 8 Lakini waoga, wasioamini, wachafu, wauaji, wazinzi, wachawi, waabudu sanamu, pamoja na waongo wote, mahali pao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili.”
-
1 Yesu akawaambia, “Msifadhaike mioyoni mwenu, mnamwamini Mungu, niaminini na mimi pia. 2 Nyumbani kwa Baba yangu kuna makao mengi. Kama sivyo, ningeliwaambia. Naenda kuwaandalia makao. 3 Nami nikienda na kuwaandalia makao, nitarudi tena na kuwachukua mkae pamoja nami, ili mahali nilipo, nanyi mpate kuwepo. 4 Ninyi mnajua njia ya kufika ninakokwenda.”
5 Tomaso akamwambia, “Bwana, sisi hatujui unakokwenda, tutaijuaje njia?”
6 Yesu akawaambia, “Mimi ndimi njia na kweli na uzima. Mtu hawezi kuja kwa Baba isipokuwa kwa kupitia kwangu.
-
20 Lakini uenyeji wetu uko mbinguni. Nasi tunamngoja kwa shauku Mwokozi kutoka huko, yaani, Bwana Yesu Kristo, 21 atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, ili upate kufanana na mwili wake wa utukufu, kwa uweza ule ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote chini yake.
-
4 Lakini Mungu kwa upendo wake mwingi kwetu sisi, ambaye ni mwingi wa rehema, 5 hata tulipokuwa wafu kwa ajili ya makosa yetu, alitufanya tuwe hai pamoja na Kristo Yesu, yaani, mmeokolewa kwa neema. 6 Mungu alitufufua pamoja na Kristo na kutuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho katika Kristo Yesu, 7 ili katika ule ulimwengu ujao apate kuonyesha wingi wa neema yake isiyopimika, iliyodhihirishwa kwetu kwa wema wake ndani ya Kristo Yesu. 8 Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani, wala si kwa matendo yenu mema. Hii ni zawadi kutoka kwa Mungu, 9 si kwa matendo, ili mtu yeyote asije akajisifu.
-
1 Kwa maana twajua kama hema yetu ya dunia tunayoishi ikiharibiwa, tunalo jengo kutoka kwa Mungu, nyumba iliyo ya milele kule mbinguni, isiyojengwa kwa mikono ya wanadamu. 2 Katika hema hii twalia kwa uchungu, tukitamani kuvikwa makao yetu ya mbinguni, 3 kwa kuwa tukiisha kuvikwa hatutaonekana tena kuwa uchi. 4 Kwa kuwa tukiwa bado katika hema hii twalia kwa uchungu na kulemewa, kwa sababu hatutaki kuvuliwa bali kuvikwa makao yetu ya mbinguni ili kwamba kile kipatikanacho na mauti kimezwe na uzima. 5 Basi Mungu ndiye alitufanya kwa ajili ya jambo lilo hilo naye ametupa Roho Mtakatifu kuwa amana, akituhakikishia ahadi ya kile kijacho.
6 Kwa hiyo siku zote tunalo tumaini, hata ingawa tunajua kwamba wakati tukiwa katika mwili huu, tuko mbali na Bwana, 7 kwa maana twaenenda kwa imani wala si kwa kuona. 8 Naam, tunalo tumaini na ingekuwa bora zaidi kuuacha mwili huu na kwenda kukaa na Bwana. 9 Kwa hiyo, kama tuko katika mwili huu au tuko mbali nao, lengo letu ni kumpendeza Bwana.
-
16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. 17 Kwa maana Mungu hakumtuma Mwanawe kuuhukumu ulimwengu, bali kupitia kwake ulimwengu upate kuokolewa. 18 Yeyote amwaminiye hahukumiwi, lakini asiyeamini amekwisha kuhukumiwa, kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu. 19 Hii ndiyo hukumu kwamba: Nuru imekuja ulimwenguni, nao watu wakapenda giza kuliko nuru kwa sababu matendo yao ni maovu. 20 Kwa kuwa kila atendaye maovu huchukia nuru, wala haji kwenye nuru ili matendo yake maovu yasifichuliwe. 21 Lakini yule aishiye kwa ukweli huja kwenye nuru, ili ionekane wazi kwamba matendo yake yametendeka katika Mungu.”
-
13 Watu hawa wote wakafa katika imani bila kuzipokea zile ahadi, lakini waliziona kwa mbali na kuzishangilia. Nao walikubali kwamba walikuwa wageni na wasiokuwa na maskani hapa duniani. 14 Watu wasemao mambo kama haya, wanaonyesha wazi kwamba wanatafuta nchi yao wenyewe. 15 Kwa kweli kama wangekuwa wanafikiri kuhusu nchi waliyoiacha, wangalipata nafasi ya kurudi huko. 16 Lakini badala yake walitamani nchi iliyo bora zaidi, yaani nchi ya mbinguni. Kwa hiyo Mungu haoni aibu kuitwa Mungu wao, kwa kuwa amekwisha kuandaa mji kwa ajili yao.
-
13 Lakini ndugu, hatutaki mkose kujua kuhusu wale waliolala mauti, ili msihuzunike kama watu wengine wasiokuwa na tumaini. 14 Kwa kuwa tunaamini kwamba Yesu alikufa na kufufuka, na kwa hivyo, Mungu kwa njia ya Yesu atawafufua pamoja naye wale waliolala mautini ndani yake. 15 Kulingana na neno la Bwana mwenyewe, tunawaambia kwamba sisi ambao bado tuko hai, tuliobaki hadi kuja kwake Bwana, hakika hatutawatangulia waliolala mauti. 16 Kwa maana Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni, akitoa amri kwa sauti kuu, pamoja na sauti ya malaika mkuu, na sauti ya tarumbeta ya Mungu. Nao waliokufa wakiwa katika Kristo watafufuka kwanza. 17 Baada ya hilo sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu ili kumlaki Bwana hewani, hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele. 18 Kwa hiyo farijianeni kwa maneno haya.
-
1 Kisha yule malaika akanionyesha mto wa maji ya uzima, maangavu kama kioo yakitiririka kutoka kwenye kile kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana-Kondoo, 2 kupitia katikati ya barabara kuu ya huo mji. Kwenye kila upande wa huo mto kulikuwa na mti wa uzima utoao matunda ya aina kumi na mbili, ukizaa matunda yake kila mwezi. Nayo majani ya mti huo ni kwa ajili ya uponyaji wa mataifa. 3 Katika mji huo hakutakuwa tena na laana, bali kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana-Kondoo kitakuwamo humo na watumishi wake watamtumikia, 4 nao watamwona uso wake na Jina lake litakuwa kwenye vipaji vya nyuso zao. 5 Usiku hautakuwako tena, wala hawatahitaji mwanga wa taa au wa jua, kwa maana Bwana Mungu atakuwa nuru yao, nao watatawala milele na milele.
-
39 Mmoja wa wale wahalifu waliosulubiwa pamoja naye akamtukana, akasema: “Wewe si ndiye Kristo? Jiokoe mwenyewe na utuokoe na sisi.”
40 Lakini yule mhalifu mwingine akamkemea mwenzake, akasema, “Je, wewe humwogopi Mungu, wakati uko kwenye adhabu iyo hiyo? 41 Sisi tumehukumiwa kwa haki kwa kuwa tunapata tunayostahili kwa ajili ya matendo yetu. Lakini huyu mtu hajafanya kosa lolote.”
42 Kisha akasema, “Yesu, unikumbuke utakapokuja katika Ufalme wako.”
43 Yesu akamjibu, “Amin, nakuambia, leo hii utakuwa pamoja nami Paradiso.”
44 Ilikuwa kama saa sita mchana, nalo giza likafunika nchi yote hadi saa tisa,
-
9 Baada ya kusema mambo haya, walipokuwa wanatazama, akachukuliwa juu mbinguni mbele ya macho yao na wingu likampokea wasimwone tena.
10 Walipokuwa bado wakikaza macho yao kuelekea juu alipokuwa akienda zake Mbinguni, tazama ghafula, wanaume wawili waliovaa mavazi meupe wakasimama karibu nao, 11 wakasema, “Enyi watu wa Galilaya, mbona mnasimama mkitazama juu angani? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda Mbinguni, atarudi tena jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake Mbinguni.”
-
21 Kwa maana kwangu mimi, kuishi ni Kristo, na kufa ni faida. 22 Kama nitaendelea kuishi katika mwili, kwangu hili ni kwa ajili ya matunda ya kazi. Lakini sijui nichague lipi? Mimi sijui! 23 Ninavutwa kati ya mambo mawili: Ninatamani kuondoka nikakae pamoja na Kristo, jambo hilo ni bora zaidi. 24 Lakini kwa sababu yenu ni muhimu zaidi mimi nikiendelea kuishi katika mwili.
-
10 Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwizi. Ndipo mbingu zitatoweka kwa kishindo kikuu; navyo vitu vya asili vitateketezwa kwa moto, nayo dunia na kila kitu kilichomo ndani yake kitaunguzwa.
11 Kwa kuwa vitu vyote vitaharibiwa namna hii, je, ninyi imewapasa kuwa watu wa namna gani? Inawapasa kuishi maisha matakatifu na ya kumcha Mungu, 12 mkingojea na kuhimiza kuja kwa hiyo siku ya Mungu. Siku hiyo italeta mbingu kuchomwa moto na kutoweka, na vitu vya asili vitayeyuka kwa moto. 13 Lakini kufuatana na ahadi yake, sisi tunatazamia mbingu mpya na dunia mpya, ambayo haki hukaa ndani yake.
14 Kwa sababu hii, wapenzi, kwa kuwa mnatazamia mambo haya, fanyeni bidii ili awakute katika amani, bila mawaa wala dosari.
-
2 Namjua mtu mmoja katika Kristo ambaye miaka kumi na minne iliyopita alichukuliwa juu hadi mbingu ya tatu. Kama ni katika mwili au nje ya mwili, sijui, Mungu ajua. 3 Nami najua ya kwamba mtu huyu, kwamba ni katika mwili au nje ya mwili mimi sijui, lakini Mungu ajua, 4 alinyakuliwa hadi Paradiso. Huko alisikia mambo yasiyoelezeka, mambo ambayo binadamu hana ruhusa ya kuyasimulia.
-
2 Huyu alimjia Yesu usiku akamwambia, “Rabi, tunajua kuwa wewe ni mwalimu uliyetumwa na Mungu, kwa maana hakuna mtu awezaye kufanya miujiza hii uifanyayo wewe, kama Mungu hayuko pamoja naye.”
3 Yesu akamjibu, “Amin, amin nakuambia, hakuna mtu anayeweza kuuona Ufalme wa Mungu kama hajazaliwa mara ya pili.”
4 Nikodemo akauliza, “Awezaje mtu kuzaliwa wakati akiwa mzee? Hakika hawezi kuingia mara ya pili kwenye tumbo la mama yake ili azaliwe!”
5 Yesu akamwambia, “Amin, amin nakuambia, hakuna mtu yeyote anayeweza kuingia Ufalme wa Mungu kama hajazaliwa kwa maji na kwa Roho.
-
12 Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hakuna jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.”
-
10 Naye ibilisi aliyewadanganya akatupwa katika ziwa la moto na kiberiti walikokuwa wametupwa yule mnyama na yule nabii wa uongo. Watateswa humo usiku na mchana, milele na milele.
11 Kisha nikaona kiti kikubwa cheupe cha enzi pamoja na yeye aliyeketi juu yake. Dunia na mbingu zikaukimbia uso wake wala mahali pao hapakuonekana. 12 Nami nikawaona wafu wakubwa na wadogo, wakiwa wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi na vitabu vikafunguliwa. Pia kitabu kingine kikafunguliwa ambacho ni kitabu cha uzima. Hao wafu wakahukumiwa sawasawa na matendo yao kama yalivyoandikwa ndani ya hivyo vitabu. 13 Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake, nayo mauti na Kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake. Kila mtu akahukumiwa kulingana na yale aliyoyatenda. 14 Kisha mauti na Kuzimu zikatupwa katika ziwa la moto. Hii ndio mauti ya pili, yaani, hilo ziwa la moto. 15 Iwapo mtu jina lake halikuonekana katika kile kitabu cha uzima, alitupwa ndani ya lile ziwa la moto.
-
19 “Msijiwekee hazina duniani, mahali ambapo nondo na kutu huharibu, nao wevi huvunja na kuiba. 20 Lakini jiwekeeni hazina mbinguni, mahali ambapo nondo na kutu haviharibu, wala wevi hawavunji na kuiba. 21 Kwa sababu mahali hazina yako ilipo, hapo ndipo pia moyo wako utakapokuwa.
-
13 “Ingieni kupitia mlango mwembamba, kwa maana lango ni pana na njia ni pana ielekeayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa kupitia lango hilo. 14 Lakini mlango ni mwembamba na njia ni finyu ielekeayo kwenye uzima, nao ni wachache tu waionao.
-
13 Hakuna mtu yeyote aliyekwenda mbinguni isipokuwa yeye aliyeshuka kutoka mbinguni, yaani, Mwana wa Adamu.
-
22 Lakini ninyi mmekuja Mlima Sayuni, Yerusalemu ya mbinguni, mji wa Mungu aliye hai. Mmekuja penye kusanyiko kubwa la malaika maelfu kwa maelfu wasiohesabika wanaoshangilia, 23 kwenye kanisa la wazaliwa wa kwanza wa Mungu, ambao majina yao yameandikwa mbinguni. Mmekuja kwa Mungu, mhukumu wa watu wote, kwenye roho za wenye haki waliokamilishwa, 24 kwa Yesu mpatanishi wa agano jipya, na kwa damu iliyonyunyizwa, ile inenayo mambo mema kuliko damu ya Abeli.
-
13 Kisha mmoja wa wale wazee ishirini na wanne akaniuliza, “Ni nani hawa waliovaa mavazi meupe, nao wametoka wapi?”
14 Nikamjibu, “Bwana, wewe wajua.”
Naye akasema, “Hawa ni wale waliotoka katika ile dhiki kuu, nao wamefua mavazi yao katika damu ya Mwana-Kondoo na kuyafanya meupe kabisa. 15 Kwa hiyo,
“Wako mbele ya kiti cha enzi cha Mungu
na kumtumikia usiku na mchana
katika hekalu lake;
naye aketiye katika kile kiti cha enzi
atatanda hema yake juu yao.
16 Kamwe hawataona njaa
wala kiu tena.
Jua halitawapiga
wala joto lolote liunguzalo.
17 Kwa maana Mwana-Kondoo
aliyeko katikati ya kile kiti cha enzi
atakuwa Mchungaji wao;
naye atawaongoza kwenda
kwenye chemchemi za maji yaliyo hai.
Naye Mungu atafuta kila chozi
kutoka macho yao.”
-
22 Sikuona Hekalu ndani ya huo mji kwa sababu Bwana Mungu Mwenyezi na Mwana-Kondoo ndio hekalu lake. 23 Ule mji hauhitaji jua wala mwezi kuuangazia, kwa sababu utukufu wa Mungu ndio nuru yake na Mwana-Kondoo ndiye taa yake. 24 Mataifa yatatembea yakiangaziwa na nuru yake na wafalme wa duniani wataleta fahari yao ndani yake. 25 Malango yake hayatafungwa kamwe, kwa maana hakutakuwa na usiku humo. 26 Utukufu na heshima za mataifa zitaletwa humo. 27 Lakini kitu kichafu hakitaingia humo kamwe, wala mtu yeyote atendaye mambo ya aibu au ya udanganyifu. Bali watakaoingia humo ni wale tu ambao majina yao yameandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo.
-
21 “Si kila mtu aniambiaye, ‘Bwana, Bwana,’ atakayeingia katika Ufalme wa Mbinguni, bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. 22 Wengi wataniambia siku ile, ‘Bwana, Bwana, hatukutoa unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo wachafu na kufanya miujiza mingi?’ 23 Ndipo nitakapowaambia wazi, ‘Sikuwajua kamwe. Ondokeni kwangu, ninyi watenda maovu!’
-
13 Kisha watoto wadogo wakaletwa kwa Yesu ili aweke mikono yake juu yao na awaombee. Lakini wanafunzi wake wakawakemea wale waliowaleta.
14 Yesu akasema, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana Ufalme wa Mbinguni ni wa wale walio kama hawa.”
-
31 “Mwana wa Adamu atakapokuja katika utukufu wake na malaika wote watakatifu pamoja naye, ndipo atakapoketi juu ya kiti cha enzi cha utukufu wake. 32 Mataifa yote watakusanyika mbele zake, naye atawatenga kama mchungaji anavyotenga kondoo na mbuzi. 33 Atawaweka kondoo upande wake wa kuume, na mbuzi upande wake wa kushoto.
34 “Ndipo Mfalme atawaambia wale walioko upande wake wa kuume, ‘Njooni, ninyi mliobarikiwa na Baba yangu; urithini Ufalme ulioandaliwa kwa ajili yenu tangu kuumbwa kwa ulimwengu. 35 Kwa maana nilikuwa na njaa mkanipa chakula, nilikuwa na kiu mkaninywesha, nilikuwa mgeni mkanikaribisha, 36 nilikuwa uchi mkanivika, nilikuwa mgonjwa mkanitunza, nami nilikuwa kifungoni mkaja kunitembelea.’
37 “Ndipo wale wenye haki watakapomjibu, ‘Bwana, ni lini tulikuona ukiwa na njaa tukakulisha, au ukiwa na kiu tukakunywesha? 38 Lini tulikuona ukiwa mgeni tukakukaribisha, au ukiwa uchi tukakuvika? 39 Tena ni lini tulikuona ukiwa mgonjwa tukakutunza, au ukiwa kifungoni tukakutembelea?’
40 “Naye Mfalme atawajibu, ‘Amin nawaambia, kwa jinsi mlivyomtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.’
41 “Kisha atawaambia wale walio upande wake wa kushoto, ‘Ondokeni kwangu, ninyi mliolaaniwa, nendeni kwenye moto wa milele ulioandaliwa kwa ajili ya ibilisi na malaika zake. 42 Kwa maana nilikuwa na njaa hamkunipa chakula, nilikuwa na kiu hamkuninywesha, 43 nilikuwa mgeni nanyi hamkunikaribisha, nilikuwa uchi hamkunivika, nilikuwa mgonjwa hamkunitunza, na nilikuwa gerezani nanyi hamkuja kunitembelea.’
44 “Ndipo wao pia watajibu, ‘Bwana ni lini tulikuona ukiwa na njaa au kiu, au ukiwa mgeni au uchi, au ukiwa mgonjwa na kifungoni na hatukukuhudumia?’
45 “Naye atawajibu, ‘Amin nawaambia, kwa jinsi ambavyo hamkumtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu walio wadogo, hamkunitendea mimi.’
46 “Ndipo hawa watakapoingia kwenye adhabu ya milele, lakini wale wenye haki wataingia katika uzima wa milele.”
-
25 Ilipokaribia usiku wa manane, Paulo na Sila walikuwa wakiomba na kuimba nyimbo za kumsifu Mungu, nao wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza. 26 Ghafula pakatokea tetemeko kubwa la ardhi, hata msingi wa gereza ukatikisika. Mara milango ya gereza ikafunguka na ile minyororo iliyowafunga kila mmoja ikafunguka. 27 Yule mkuu wa gereza alipoamka na kuona milango ya gereza iko wazi, akachomoa upanga wake akataka kujiua, akidhani ya kuwa wafungwa wote wametoroka. 28 Lakini Paulo akapiga kelele kwa sauti kubwa, akasema, “Usijidhuru kwa maana sisi sote tuko hapa!”
29 Yule askari wa gereza akaagiza taa ziletwe, akaingia ndani ya kile chumba cha gereza, akapiga magoti akitetemeka mbele ya Paulo na Sila. 30 Kisha akawaleta nje akisema, “Bwana zangu, nifanye nini nipate kuokoka?”
31 Wakamjibu, “Mwamini Bwana Yesu Kristo, nawe utaokoka, pamoja na watu wa nyumbani mwako.” 32 Wakamwambia neno la Bwana yeye pamoja na wote waliokuwako nyumbani mwake. 33 Wakati ule ule, yule mkuu wa gereza akawachukua, akawaosha majeraha yao, kisha akabatizwa yeye pamoja na wote waliokuwa nyumbani mwake bila kuchelewa. 34 Akawapandisha nyumbani mwake akawaandalia chakula, yeye pamoja na nyumba yake yote wakafurahi sana kwa kuwa sasa walikuwa wamemwamini Mungu.
-
5 Mose anaandika kuhusu haki ile itokanayo na sheria, kwamba, “Mtu atendaye matendo hayo ataishi kwa hayo.” 6 Lakini ile haki itokanayo na imani husema hivi: “Usiseme moyoni mwako, ‘Ni nani atakayepanda mbinguni?’ ” (yaani ili kumleta Kristo chini) 7 “au ‘Ni nani atashuka kwenda kuzimu?’ ” (yaani ili kumleta Kristo kutoka kwa wafu.) 8 Lakini andiko lasemaje? “Lile neno liko karibu nawe, liko kinywani mwako na moyoni mwako,” yaani, lile neno la imani tunalolihubiri. 9 Kwa sababu kama ukikiri kwa kinywa chako kwamba “Yesu ni Bwana,” na kuamini moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, utaokoka. 10 Kwa maana kwa moyo mtu huamini na hivyo kuhesabiwa haki, tena kwa kinywa mtu hukiri na hivyo kupata wokovu. 11 Kama yasemavyo Maandiko, “Yeyote amwaminiye hataaibika kamwe.” 12 Kwa maana hakuna tofauti kati ya Myahudi na Myunani, yeye ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao. 13 Kwa maana, “Kila mtu atakayeliitia Jina la Bwana, ataokolewa.”
14 Lakini watamwitaje yeye ambaye hawajamwamini? Nao watawezaje kumwamini yeye ambaye hawajamsikia? Tena watamsikiaje bila mtu kuwahubiria? 15 Nao watahubirije wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, “Tazama jinsi ilivyo mizuri miguu yao wale wanaohubiri habari njema!”
16 Lakini si wote waliotii Habari Njema. Kwa maana Isaya asema, “Bwana, ni nani aliyeamini ujumbe wetu?” 17 Basi, imani chanzo chake ni kusikia, na kusikia huja kwa neno la Kristo.
-
1 Basi, kwa kuwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu, Kristo alikoketi mkono wa kuume wa Mungu. 2 Yafikirini mambo yaliyo juu, wala si ya duniani. 3 Kwa maana ninyi mlikufa, nao uhai wenu sasa umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu. 4 Wakati Kristo, aliye uzima wenu, atakapotokea, ndipo nanyi mtakapotokea pamoja naye katika utukufu.
-
7 “Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye, nitampa haki ya kula matunda toka kwa mti wa uzima, ambao uko katika paradiso ya Mungu.
-
4 Bwana yuko ndani ya Hekalu lake takatifu;
Bwana yuko kwenye kiti chake cha enzi mbinguni.
Huwaangalia wana wa watu,
macho yake yanawajaribu.
5 Bwana huwajaribu wenye haki,
lakini waovu na wanaopenda jeuri,
nafsi yake huwachukia.
6 Atawanyeshea waovu makaa ya moto mkali
na kiberiti kinachowaka,
upepo wenye joto kali ndio fungu lao.
7 Kwa kuwa Bwana ni mwenye haki,
yeye hupenda haki.
Wanyofu watauona uso wake.
-
2 Wengi ambao wamelala kwenye mavumbi wataamka, baadhi yao kwa uzima wa milele, wengine kwa aibu na kudharauliwa milele.
-
5 Yesu alipoingia Kapernaumu, jemadari mmoja alimjia, kumwomba msaada, 6 akisema, “Bwana, mtumishi wangu amelala nyumbani na amepooza, tena ana maumivu makali ya kutisha.”
7 Yesu akamwambia, “Nitakuja na kumponya.”
8 Lakini yule jemadari akamwambia, “Bwana, mimi sistahili wewe kuingia chini ya dari yangu. Lakini sema neno tu, naye mtumishi wangu atapona. 9 Kwa kuwa mimi mwenyewe ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, nikiwa na askari chini yangu. Nikimwambia huyu, ‘Nenda,’ yeye huenda; na mwingine nikimwambia, ‘Njoo,’ yeye huja. Nikimwambia mtumishi wangu, ‘Fanya hivi,’ yeye hufanya.”
10 Yesu aliposikia maneno haya, alishangaa, akawaambia wale waliomfuata, “Amin, nawaambia, hata katika Israeli sijapata kuona yeyote mwenye imani kubwa namna hii. 11 Ninawaambia kwamba wengi watatoka mashariki na magharibi, nao wataketi karamuni pamoja na Abrahamu, Isaki na Yakobo katika Ufalme wa Mbinguni. 12 Lakini warithi wa Ufalme watatupwa katika giza la nje, ambako kutakuwako kilio na kusaga meno.”
13 Kisha Yesu akamwambia yule jemadari, “Nenda na iwe kwako sawasawa na imani yako.” Naye yule mtumishi akapona saa ile ile.
-
19 “Palikuwa na mtu mmoja tajiri aliyevaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi, ambaye aliishi kwa anasa kila siku. 20 Hapo penye mlango wake aliishi maskini mmoja, jina lake Lazaro, mwenye vidonda mwili mzima. 21 Huyo Lazaro alitamani kujishibisha kwa makombo yaliyoanguka kutoka mezani kwa yule tajiri. Hata mbwa walikuwa wakija na kuramba vidonda vyake.
22 “Wakati ukafika yule maskini akafa, nao malaika wakamchukua akae pamoja na Abrahamu. Yule tajiri naye akafa na akazikwa. 23 Kule kuzimu alipokuwa akiteseka, alitazama juu, akamwona Abrahamu kwa mbali, naye Lazaro alikuwa karibu yake. 24 Hivyo yule tajiri akamwita, ‘Baba Abrahamu, nihurumie na umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake ndani ya maji aupoze ulimi wangu, kwa sababu nina maumivu makuu kwenye moto huu.’
25 “Lakini Abrahamu akamjibu, ‘Mwanangu, kumbuka kwamba wakati wa uhai wako ulipata mambo mazuri, lakini Lazaro alipata mambo mabaya. Lakini sasa anafarijiwa hapa na wewe uko katika maumivu makuu. 26 Zaidi ya hayo, kati yetu na ninyi huko kumewekwa shimo kubwa, ili wale wanaotaka kutoka huku kuja huko wasiweze, wala mtu yeyote asiweze kuvuka kutoka huko kuja kwetu.’
27 “Akasema, ‘Basi, nakuomba, umtume Lazaro aende nyumbani kwa baba yangu, 28 maana ninao ndugu watano. Awaonye, ili wasije nao wakafika mahali hapa pa mateso.’
29 “Abrahamu akamjibu, ‘Ndugu zako wana Maandiko ya Mose na Manabii, wawasikilize hao.’
30 “Yule tajiri akasema, ‘Hapana, baba Abrahamu, lakini mtu kutoka kwa wafu akiwaendea, watatubu.’
31 “Abrahamu akamwambia, ‘Kama wasipowasikiliza Mose na Manabii, hawataweza kushawishika hata kama mtu akifufuka kutoka kwa wafu.’ ”
-
36 Yeyote anayemwamini Mwana ana uzima wa milele, lakini yeye asiyemwamini Mwana hatauona uzima, bali ghadhabu ya Mungu itakuwa juu yake.”
-
26 Kama tukiendelea kutenda dhambi kwa makusudi baada ya kupokea ufahamu wa ile kweli, haibaki tena dhabihu kwa ajili ya dhambi. 27 Lakini kinachobaki ni kungoja kwa hofu hukumu ya moto uwakao, utakaowaangamiza adui za Mungu. 28 Yeyote aliyeikataa sheria ya Mose alikufa pasipo huruma kwa ushahidi wa watu wawili au watatu. 29 Je, mnadhani ni adhabu kali kiasi gani anayostahili kupewa mtu aliyemkanyaga Mwana wa Mungu chini ya nyayo zake, yeye aliyeifanya damu ya Agano iliyomtakasa kuwa kitu najisi na kumtendea maovu Roho wa neema? 30 Kwa kuwa tunamjua yeye aliyesema, “Ni juu yangu kulipiza kisasi; nitalipiza.” Tena asema, “Bwana atawahukumu watu wake.” 31 Ni jambo la kutisha kuanguka mikononi mwa Mungu aliye hai.
-
2 Wapendwa, sasa tu wana wa Mungu, lakini bado haijadhihirika tutakavyokuwa, lakini twajua ya kwamba yeye atakapodhihirishwa, tutafanana naye, kwa maana tutamwona kama alivyo. 3 Kila mmoja mwenye matumaini haya ndani yake hujitakasa, kama vile yeye alivyo mtakatifu.
-
29 Lakini ninawaambia, tangu sasa sitakunywa tena katika uzao huu wa mzabibu, hadi siku ile nitakapounywa mpya pamoja nanyi katika Ufalme wa Baba yangu.”
-
24 “Amin, amin nawaambia, yeyote anayesikia maneno yangu na kumwamini yeye aliyenituma, anao uzima wa milele, naye hatahukumiwa, bali amepita kutoka mautini, na kuingia uzimani.
-
32 “Kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, mimi nami nitamkiri yeye mbele za Baba yangu aliye mbinguni. 33 Lakini yeyote atakayenikana mimi mbele ya watu, mimi nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni.”
-
40 “Kama vile magugu yangʼolewavyo na kuchomwa motoni, ndivyo itakavyokuwa wakati wa mwisho wa dunia. 41 Mwana wa Adamu atawatuma malaika zake, nao watakusanya kutoka Ufalme wake kila kitu kinachosababisha dhambi na watenda maovu wote. 42 Nao watawatupa katika tanuru la moto ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno. 43 Ndipo wenye haki watangʼaa kama jua katika Ufalme wa Baba yao. Yeye aliye na masikio, na asikie.
-
1 Wakati huo, wanafunzi wakamjia Yesu na kumuuliza, “Je, nani aliye mkuu kuliko wote katika Ufalme wa Mbinguni?”
2 Yesu akamwita mtoto mdogo na kumsimamisha katikati yao. 3 Naye akasema: “Amin, nawaambia, msipookoka na kuwa kama watoto wadogo, kamwe hamtaingia katika Ufalme wa Mbinguni. 4 Kwa hiyo mtu yeyote anyenyekeaye kama huyu mtoto, ndiye aliye mkuu kuliko wote katika Ufalme wa Mbinguni.
-
21 Yesu akamwambia, “Kama ukitaka kuwa mkamilifu, nenda, ukauze vitu vyote ulivyo navyo, na hizo fedha uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.”
22 Yule kijana aliposikia hayo, akaenda zake kwa huzuni, kwa sababu alikuwa na mali nyingi.
-
39 Haya ndiyo mapenzi yake yeye aliyenituma, kwamba, nisimpoteze hata mmoja wa wale alionipa, bali niwafufue siku ya mwisho. 40 Kwa maana mapenzi ya Baba yangu ni kwamba kila mmoja amtazamaye, Mwana na kumwamini awe na uzima wa milele, nami nitawafufua siku ya mwisho.”
-
50 Ndugu zangu nisemalo ni hili: nyama na damu haviwezi kuurithi ufalme wa Mungu, wala kuharibika kurithi kutokuharibika. 51 Sikilizeni, nawaambia siri: Sote hatutalala, lakini sote tutabadilishwa 52 ghafula, kufumba na kufumbua, parapanda ya mwisho itakapolia. Kwa kuwa parapanda italia, nao wafu watafufuliwa na miili isiyoharibika, nasi tutabadilishwa. 53 Kwa maana mwili huu wa kuharibika lazima uvae kutokuharibika, nao huu wa kufa lazima uvae kutokufa. 54 Kwa hiyo, mwili huu wa kuharibika utakapovaa kutokuharibika, nao huu mwili wa kufa utakapovaa kutokufa, ndipo lile neno lililoandikwa litakapotimia: “Mauti imemezwa kwa kushinda.”
-
19 Basi matendo ya mwili ni dhahiri nayo ni haya: Uasherati, uchafu, ufisadi, 20 kuabudu sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, 21 husuda, ulevi, ulafi na mambo mengine yanayofanana na hayo. Nawaonya, kama nilivyokwisha kuwaonya kabla, kwamba watu watendao mambo kama hayo, hawataurithi Ufalme wa Mungu.
22 Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, 23 upole na kiasi. Katika mambo kama haya hakuna sheria.
Shows Read in context, Share and Copy.