68 Bible Verses About Redemption

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Redemption
  1. 13 Kwa hiyo, tayarisheni nia zenu kwa kazi; mwe na kiasi, mkitumainia kikamilifu ile neema mtakayopewa Yesu Kristo atakapodhihirishwa. 14 Kama watoto watiifu, msifuate tamaa zenu mbaya wakati mlipoishi kwa ujinga. 15 Bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, nanyi kuweni watakatifu katika mwenendo wenu wote. 16 Kwa maana imeandikwa: “Kuweni watakatifu, kwa kuwa mimi ni mtakatifu.”

    17 Kwa sababu mnamwita Baba ahukumuye kila mtu kulingana na matendo yake pasipo upendeleo, enendeni kwa hofu ya kumcha Mungu wakati wenu wa kukaa hapa duniani kama wageni. 18 Kwa maana mnafahamu kwamba mlikombolewa kutoka mwenendo wenu usiofaa ambao mliurithi kutoka kwa baba zenu, si kwa vitu viharibikavyo kama fedha na dhahabu, 19 bali kwa damu ya thamani ya Kristo, yule Mwana-Kondoo asiye na dosari wala doa. 20 Yeye alichaguliwa kabla ya kuwekwa kwa misingi ya ulimwengu, lakini akadhihirishwa katika siku hizi za mwisho kwa ajili yenu. 21 Kupitia kwake mmemwamini Mungu, aliyemfufua kutoka kwa wafu na akampa utukufu, ili imani yenu na tumaini lenu ziwe kwa Mungu.

  2. 3 Ahimidiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki sisi kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho ndani ya Kristo. 4 Kwa maana alituchagua katika yeye kabla ya kuumbwa ulimwengu ili tuwe watakatifu na bila lawama mbele zake. Kwa upendo 5 alitangulia kutuchagua tuwe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo kwa furaha yake na mapenzi yake mwenyewe. 6 Kwa hiyo tunamsifu Mungu kwa huruma zake kuu alizotumiminia sisi katika Mwanawe Mpendwa. 7 Ndani yake tunao ukombozi kwa njia ya damu yake, yaani, msamaha wa dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake 8 aliyotumiminia kwa wingi, kwa hekima yote na maarifa yote. 9 Naye alitujulisha siri ya mapenzi yake sawasawa na uradhi wa mapenzi yake, ambayo alikusudia katika Kristo, 10 ili yapate kutimizwa wakati mkamilifu utakapowadia, yaani, kuvitia vitu vyote vya mbinguni na vya duniani pamoja, chini ya kiongozi mmoja, ndiye Kristo.

  3. 21 Lakini sasa, haki itokayo kwa Mungu imedhihirishwa pasipo sheria, ambayo Sheria na Manabii wanaishuhudia. 22 Haki hii itokayo kwa Mungu hupatikana kwa Yesu Kristo kwa wote wamwaminio. Kwa maana hapo hakuna tofauti, 23 kwa kuwa wote wametenda dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu, 24 wanahesabiwa haki bure kwa neema yake kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu. 25 Yeye ambaye Mungu alimtoa awe dhabihu ya upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake. Alifanya hivi ili kuonyesha haki yake, kwa sababu kwa ustahimili wake aliziachilia zile dhambi zilizotangulia kufanywa. 26 Alifanya hivyo ili kuonyesha haki yake wakati huu, ili yeye awe mwenye haki na mwenye kumhesabia haki yule anayemwamini Yesu.

    27 Basi, kujivuna kuko wapi? Kumewekwa mbali. Kwa sheria gani? Je, ni kwa ile ya matendo? La hasha, bali kwa ile sheria ya imani. 28 Kwa maana twaona kwamba mwanadamu huhesabiwa haki kwa njia ya imani wala si kwa matendo ya sheria.

  4. 15 Yeye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. 16 Kwake yeye vitu vyote vilivyoko mbinguni na juu ya nchi viliumbwa: vitu vinavyoonekana na visivyoonekana, viwe ni viti vya enzi au falme, au wenye mamlaka au watawala; vitu vyote viliumbwa na yeye na kwa ajili yake. 17 Yeye alikuwepo kabla ya vitu vyote, na katika yeye vitu vyote vinashikamana pamoja. 18 Yeye ndiye kichwa cha mwili, yaani kanisa, naye ndiye mwanzo na mzaliwa wa kwanza kutoka kwa wafu, ili yeye awe mkuu katika vitu vyote. 19 Kwa kuwa ilimpendeza Mungu kwamba utimilifu wake wote ukae ndani yake, 20 na kwa njia yake aweze kuvipatanisha vitu vyote na yeye mwenyewe, viwe ni vitu vilivyo duniani au vilivyo mbinguni, kwa kufanya amani kwa damu yake, iliyomwagika msalabani.

    21 Hapo kwanza mlikuwa mmetengana na Mungu, na mlikuwa adui zake katika nia zenu kwa sababu ya mienendo yenu mibaya. 22 Lakini sasa Mungu amewapatanisha ninyi kwa njia ya mwili wa Kristo kupitia mauti, ili awalete mbele zake mkiwa watakatifu, bila dosari wala lawama,

  5. 11 Kwa maana neema ya Mungu ambayo inawaokoa wanadamu wote imefunuliwa. 12 Nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia, ili tupate kuishi maisha ya kiasi, ya haki na ya utaua katika ulimwengu huu wa sasa, 13 huku tukilitazamia tumaini lenye baraka na ufunuo wa utukufu wa Mungu wetu Mkuu, aliye Mwokozi wetu Yesu Kristo. 14 Ndiye alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, ili atukomboe kutoka uovu wote na kujisafishia watu kuwa mali yake Mwenyewe, yaani, wale walio na juhudi katika kutenda mema.

  6. 11 Kristo alipokuja akiwa Kuhani Mkuu wa mambo mema ambayo tayari yameshawasili, alipitia kwenye hema iliyo kuu zaidi na bora zaidi, ambayo haikutengenezwa kwa mikono ya binadamu, hii ni kusema, ambayo si sehemu ya uumbaji huu. 12 Hakuingia kwa njia ya damu ya mbuzi na ya ndama; lakini aliingia Patakatifu pa Patakatifu mara moja tu kwa damu yake mwenyewe, akiisha kupata ukombozi wa milele. 13 Damu ya mbuzi na ya mafahali, na majivu ya mitamba walivyonyunyiziwa wale waliokuwa najisi kwa taratibu za kiibada viliwatakasa, hata kuwaondolea uchafu wa nje. 14 Basi ni zaidi aje damu ya Kristo, ambaye kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na waa, itatusafisha dhamiri zetu kutokana na matendo yaletayo mauti, ili tupate kumtumikia Mungu aliye hai!

    15 Kwa sababu hii Kristo ni mpatanishi wa agano jipya, ili kwamba wale walioitwa waweze kupokea ile ahadi ya urithi wa milele: kwa vile yeye alikufa awe ukombozi wao kutoka kwa dhambi walizozitenda chini ya agano la kwanza.

  7. 1 Lile nisemalo ni kwamba wakati wote mrithi bado ni mtoto, hana tofauti na mtumwa, ingawa ndiye mmiliki wa mali yote. 2 Yeye huwa yuko chini ya uangalizi wa walezi na wadhamini mpaka ufike wakati uliowekwa na baba yake. 3 Vivyo hivyo na sisi, tulipokuwa bado watoto wadogo, tulikuwa utumwani chini ya taratibu za kawaida za ulimwengu. 4 Lakini ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe, ambaye alizaliwa na mwanamke, akazaliwa chini ya sheria, 5 kusudi awakomboe wale waliokuwa chini ya sheria, ili tupate kupokea zile haki kamili za kufanywa watoto wa Mungu. 6 Kwa sababu ninyi ni watoto wa Mungu, Mungu amemtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, anayelia, “Abba, Baba.” 7 Kwa hiyo, wewe si mtumwa tena, bali ni mtoto, kwa kuwa wewe ni mtoto, Mungu amekufanya wewe pia kuwa mrithi kwa kupitia Kristo.

  8. 13 Kristo alitukomboa kutoka laana ya sheria kwa kufanyika laana kwa ajili yetu, kwa maana imeandikwa, “Amelaaniwa yeye aangikwaye juu ya mti.” 14 Alitukomboa ili kwamba baraka aliyopewa Abrahamu ipate kuwafikia watu wa Mataifa kwa njia ya Kristo Yesu, ili kwa imani tupate kupokea ile ahadi ya Roho.

  9. 18 Nayahesabu mateso yetu ya wakati huu kuwa si kitu kulinganisha na utukufu utakaodhihirishwa kwetu. 19 Kwa maana viumbe vyote vinangoja kwa shauku kudhihirishwa kwa watoto wa Mungu. 20 Kwa kuwa viumbe vyote viliwekwa chini ya ubatili, si kwa chaguo lao, bali kwa mapenzi yake yeye aliyevitiisha katika tumaini, 21 ili kwamba viumbe vyote vipate kuwekwa huru kutoka kwa utumwa wa kuharibika na kupewa uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu.

    22 Kwa maana twajua ya kuwa hata sasa viumbe vyote vimekuwa vikilia kwa maumivu kama utungu wa mwanamke wakati wa kuzaa. 23 Wala si hivyo viumbe peke yao, bali hata sisi ambao ndio matunda ya kwanza ya Roho, kwa ndani tunalia kwa uchungu tukisubiri kwa shauku kufanywa wana wa Mungu, yaani, ukombozi wa miili yetu.

  10. 1 Lakini sasa hili ndilo asemalo Bwana,

    yeye aliyekuumba, ee Yakobo,

    yeye aliyekuhuluku, ee Israeli:

    “Usiogope kwa maana nimekukomboa,

    nimekuita wewe kwa jina lako, wewe u wangu.

    2 Unapopita kwenye maji makuu,

    nitakuwa pamoja nawe,

    unapopita katika mito ya maji,

    hayatakugharikisha.

    Utakapopita katika moto,

    hutaungua,

    miali ya moto haitakuunguza.

    3 Kwa kuwa Mimi ndimi Bwana, Mungu wako,

    yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, Mwokozi wako.

    Ninaitoa Misri kuwa fidia yako,

    Kushi na Seba badala yako.

    4 Kwa kuwa wewe ni wa thamani na wa kuheshimiwa machoni pangu,

    nami kwa kuwa ninakupenda,

    nitatoa watu badala yako

    na mataifa badala ya maisha yako.

  11. 8 Alipokwisha kukitwaa kile kitabu, wale viumbe wenye uhai wanne pamoja na wale wazee ishirini na wanne wakaanguka mbele ya yule Mwana-Kondoo. Kila mmoja wao alikuwa na kinubi, nao walikuwa wameshika mabakuli ya dhahabu yaliyojaa uvumba, ambayo ni maombi ya watakatifu. 9 Nao wakaimba wimbo mpya, wakisema:

    “Wewe unastahili kukitwaa kitabu

    na kuzivunja lakiri zake,

    kwa sababu ulichinjwa

    na kwa damu yako ukamnunulia Mungu watu

    kutoka kila kabila, kila lugha,

    kila jamaa na kila taifa.

    10 Wewe umewafanya hawa wawe ufalme na makuhani

    wa kumtumikia Mungu wetu,

    nao watatawala duniani.”

    11 Kisha nikatazama, nikasikia sauti za malaika wengi wakiwa wamekizunguka kile kiti cha enzi, pamoja na wale viumbe wenye uhai wanne na wale wazee ishirini na wanne. Idadi yao ilikuwa kumi elfu mara kumi elfu na maelfu ya maelfu. 12 Nao waliimba kwa sauti kuu, wakisema:

    “Anastahili Mwana-Kondoo, yeye aliyechinjwa,

    kupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu

    na heshima na utukufu na sifa!”

    13 Kisha nikasikia kila kiumbe mbinguni na duniani, chini ya nchi na baharini na vyote vilivyomo ndani yake vikiimba:

    “Sifa na heshima na utukufu na uweza

    ni vyake yeye aketiye juu ya hicho kiti cha enzi

    na kwa Mwana-Kondoo,

    milele na milele!”

    14 Wale viumbe wenye uhai wanne wakasema, “Amen!” Nao wale wazee ishirini na wanne wakaanguka kifudifudi wakaabudu.

  12. 24 Katika nchi yote mtakayoshika kuwa milki yenu, ni lazima mtoe ukombozi wa ardhi.

    25 “ ‘Ikiwa mmoja wa wazawa wa nchi yako amekuwa maskini na akauza baadhi ya mali yake, ndugu yake wa karibu atakuja na kukomboa kile ndugu yako alichokiuza. 26 Iwapo mtu huyo hana jamaa wa karibu wa kukomboa mali hiyo kwa ajili yake, lakini yeye mwenyewe akafanikiwa na kupata mali itoshayo kuikomboa, 27 ataamua tena thamani yake kwa miaka tangu alipoiuza, na kurudisha kiasi kilichobaki cha thamani kwa mtu ambaye alikuwa amemuuzia mali hiyo, naye ataweza kuirudia mali yake. 28 Lakini kama hatapata njia ya kumlipa mnunuzi, ile mali aliyouza itabaki kumilikiwa na mnunuzi mpaka Mwaka wa Yubile. Mali hiyo itarudishwa mwaka wa Yubile, naye ataweza kuirudia mali yake.

  13. 25 Ninajua kwamba Mkombozi wangu yu hai,

    naye kwamba mwishoni atasimama juu ya nchi.

    26 Nami baada ya ngozi yangu kuharibiwa,

    bado nikiwa na mwili huu nitamwona Mungu;

    27 mimi nitamwona kwa macho yangu mwenyewe:

    mimi, wala si mwingine.

    Tazama jinsi moyo wangu unavyomtamani sana!

  14. 16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. 17 Kwa maana Mungu hakumtuma Mwanawe kuuhukumu ulimwengu, bali kupitia kwake ulimwengu upate kuokolewa. 18 Yeyote amwaminiye hahukumiwi, lakini asiyeamini amekwisha kuhukumiwa, kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu.

  15. 7 Hakuna mwanadamu awaye yote

    awezaye kuukomboa uhai wa mwingine,

    au kumpa Mungu fidia kwa ajili yake.

    8 Fidia ya uhai ni gharama kubwa,

    hakuna malipo yoyote yanayotosha,

    9 ili kwamba aishi milele

    na asione uharibifu.

  16. 30 Wala msimhuzunishe Roho Mtakatifu wa Mungu, ambaye kwake mlitiwa muhuri kwa ajili ya siku ya ukombozi. 31 Ondoeni kabisa uchungu, ghadhabu, hasira, makelele na masingizio pamoja na kila aina ya uovu.

  17. 6 “Kwa hiyo, waambie Waisraeli: ‘Mimi ndimi Bwana, nami nitawatoa mtoke katika kongwa la Wamisri. Nitawaweka huru mtoke kuwa watumwa wao, nami nitawakomboa kwa mkono ulionyooshwa pamoja na matendo makuu ya hukumu. 7 Nitawatwaa mwe watu wangu mwenyewe, nami nitakuwa Mungu wenu. Ndipo mtajua kuwa mimi ndimi Bwana Mungu wenu, niliyewatoa chini ya kongwa la Wamisri. 8 Nami nitawaleta mpaka nchi niliyoapa kwa mkono ulioinuliwa kumpa Abrahamu, Isaki na Yakobo. Nitawapa iwe milki yenu. Mimi ndimi Bwana.’ ”

  18. 44 Bwana akamwambia Mose, 45 “Watwae Walawi badala ya wazaliwa wa kwanza wote wa Israeli, nayo mifugo ya Walawi badala ya mifugo yao. Walawi watakuwa wangu. Mimi ndimi Bwana. 46 Ili kukomboa wazao wa kwanza 273 wa Waisraeli ambao wamezidi hesabu ya Walawi, 47 kusanya shekeli tano kwa kila mmoja, kufuatana na shekeli ya mahali patakatifu, ambayo ina uzito wa gera ishirini. 48 Mpe Aroni na wanawe hizo fedha kwa ajili ya ukombozi wa idadi ya Waisraeli waliozidi.”

    49 Kwa hiyo Mose akakusanya fedha za ukombozi kutoka kwa wale ambao hesabu yao ilizidi wale waliokombolewa na Walawi. 50 Kutokana na wazaliwa wa kwanza wa Waisraeli alikusanya fedha yenye uzito wa shekeli 1,365 kufuatana na shekeli ya mahali patakatifu. 51 Mose akampa Aroni na wanawe ile fedha ya ukombozi, kama alivyoamriwa na neno la Bwana.

  19. 21 “Ee Yakobo, kumbuka mambo haya,

    ee Israeli, kwa kuwa wewe ni mtumishi wangu.

    Nimekuumba wewe, wewe ni mtumishi wangu.

    Ee Israeli, sitakusahau.

    22 Nimeyafuta makosa yako kama wingu,

    dhambi zako kama ukungu wa asubuhi.

    Nirudie mimi,

    kwa kuwa nimekukomboa wewe.”

    23 Enyi mbingu, imbeni kwa furaha,

    kwa maana Bwana amefanya jambo hili.

    Ee vilindi vya dunia, piga kelele.

    Enyi milima, pazeni sauti kwa nyimbo,

    enyi misitu na miti yenu yote,

    kwa maana Bwana amemkomboa Yakobo,

    ameuonyesha utukufu wake katika Israeli.

  20. 25 Lakini Yesu akawaita wote pamoja na kuwaambia, “Mnafahamu kuwa watawala wa watu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, nao wenye vyeo huonyesha mamlaka yao. 26 Isiwe hivyo kwenu. Badala yake, yeyote anayetaka kuwa mkuu miongoni mwenu hana budi kuwa mtumishi wenu, 27 naye anayetaka kuwa wa kwanza miongoni mwenu hana budi kuwa mtumwa wenu: 28 kama vile ambavyo Mwana wa Adamu hakuja ili kutumikiwa, bali kutumika na kuutoa uhai wake uwe fidia kwa ajili ya wengi.”

  21. 28 Jilindeni nafsi zenu na mlilinde lile kundi lote ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi wake. Lichungeni kanisa lake Mungu alilolinunua kwa damu yake mwenyewe.

  22. 1 Kisha Hana akaomba na kusema:

    “Moyo wangu wamshangilia Bwana,

    katika Bwana pembe yangu imeinuliwa juu.

    Kinywa changu chajisifu juu ya adui zangu,

    kwa kuwa naufurahia wokovu wako.

  23. 11 “Baada ya Bwana kukuingiza katika nchi ya Wakanaani na kukupa nchi hiyo, kama alivyokuahidi kwa kiapo na kwa baba zako, 12 inakupasa kumtolea Bwana mzaliwa wa kwanza wa kila tumbo. Wazaliwa wote wa kwanza wa kiume wa mifugo yako ni mali ya Bwana. 13 Kila mzaliwa wa kwanza wa punda utamkomboa kwa mwana-kondoo, lakini kama hukumkomboa, utamvunja shingo yake. Kila mzaliwa wa kwanza mwanaume miongoni mwa wana wenu utamkomboa.

    14 “Katika siku zijazo, mwanao akikuuliza, ‘Hii ina maana gani?’ Mwambie, ‘Kwa mkono wenye nguvu Bwana alitutoa katika nchi ya Misri, kutoka nchi ya utumwa. 15 Farao alipokataa kwa ukaidi kuturuhusu kuondoka, Bwana aliua kila mzaliwa wa kwanza wa Wamisri, mwanadamu na wa mnyama. Hii ndiyo sababu ninatoa dhabihu kwa Bwana mzaliwa wa kwanza wa kiume, wa kila tumbo na kumkomboa kila mzaliwa wa kwanza wa wana wangu.’ 16 Jambo hili litakuwa kama ishara kwenye mkono wako na kama alama kwenye paji la uso wako, kwamba Bwana alikutoa katika nchi ya Misri kwa mkono wake wenye nguvu.”

  24. 5 Kwa maana kuna Mungu mmoja na mpatanishi mmoja kati ya Mungu na wanadamu, yaani mwanadamu Kristo Yesu, 6 aliyejitoa mwenyewe kuwa fidia kwa ajili ya wanadamu wote: jambo hili lilishuhudiwa kwa wakati wake ufaao. 7 Nami kwa kusudi hili nimewekwa niwe mhubiri na mtume (nasema kweli katika Kristo wala sisemi uongo), mwalimu wa watu wa Mataifa katika imani na kweli.

  25. 6 Kwa maana hata tulipokuwa dhaifu, wakati ulipowadia, Kristo alikufa kwa ajili yetu sisi wenye dhambi. 7 Hakika, ni vigumu mtu yeyote kufa kwa ajili ya mwenye haki, ingawa inawezekana mtu akathubutu kufa kwa ajili ya mtu mwema. 8 Lakini Mungu anaudhihirisha upendo wake kwetu kwamba: Tulipokuwa tungali wenye dhambi, Kristo alikufa kwa ajili yetu.

    9 Basi, kwa kuwa sasa tumehesabiwa haki kwa damu yake, si zaidi sana tutaokolewa kutoka ghadhabu ya Mungu kupitia kwake! 10 Kwa kuwa kama tulipokuwa adui wa Mungu tulipatanishwa naye kwa njia ya kifo cha Mwanawe, si zaidi sana tukiisha kupatanishwa, tutaokolewa kwa uzima wake. 11 Lakini zaidi ya hayo, pia tunafurahi katika Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kupitia kwake tumepata upatanisho.

  26. 7 Ee Israeli, mtumaini Bwana,

    maana kwa Bwana kuna upendo usiokoma,

    na kwake kuna ukombozi kamili.

    8 Yeye mwenyewe ataikomboa Israeli

    kutoka dhambi zao zote.

  27. 45 Kwa kuwa hata Mwana wa Adamu hakuja ili kutumikiwa, bali kutumika na kuutoa uhai wake uwe fidia kwa ajili ya wengi.”

  28. 25 “Kutakuwa na ishara katika jua, mwezi na nyota. Hapa duniani, mataifa yatakuwa katika dhiki na fadhaa kutokana na ngurumo na misukosuko ya bahari. 26 Watu watazimia roho kutokana na hofu kuu na kuyaona yale mambo yanayotokea duniani, kwa maana nguvu za angani zitatikisika. 27 Wakati huo ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija mawinguni pamoja na uweza na utukufu mkuu. 28 Mambo haya yatakapoanza kutendeka, simameni na mkaviinue vichwa vyenu, kwa sababu ukombozi wenu umekaribia.”

  29. 68 “Ahimidiwe Bwana, Mungu wa Israeli,

    kwa kuwa amewajilia watu wake na kuwakomboa.

    69 Naye ametusimamishia pembe ya wokovu

    katika nyumba ya Daudi mtumishi wake,

    70 kama alivyonena kwa vinywa vya manabii

    wake watakatifu tangu zamani,

    71 kwamba atatuokoa kutoka kwa adui zetu,

    na kutoka mikononi mwao wote watuchukiao:

    72 ili kuonyesha rehema kwa baba zetu

    na kukumbuka Agano lake takatifu,

    73 kiapo alichomwapia baba yetu Abrahamu:

    74 kutuokoa kutoka mikononi mwa adui zetu,

    tupate kumtumikia yeye pasipo hofu

    75 katika utakatifu na haki mbele zake,

    siku zetu zote.

  30. 22 Kwa maana yeyote aliyeitwa katika Bwana akiwa mtumwa yeye ni mtu huru kwa Bwana, kama vile yeyote aliyekuwa huru alipoitwa yeye ni mtumwa wa Kristo. 23 Mlinunuliwa kwa gharama; msiwe watumwa wa wanadamu.

  31. 3 Nao wakaimba wimbo mpya mbele ya hicho kiti cha enzi na mbele ya wale viumbe wanne wenye uhai na wale wazee. Hakuna mtu yeyote aliyeweza kujifunza wimbo huo isipokuwa hao 144,000 waliokuwa wamekombolewa kutoka duniani. 4 Hawa ndio wale ambao hawakujitia unajisi kwa wanawake, kwa kuwa wao ni bikira. Wao humfuata Mwana-Kondoo kila aendako. Hawa wamekombolewa kutoka miongoni mwa wanadamu wakawa malimbuko kwa Mungu na kwa Mwana-Kondoo.

  32. KITABU CHA TANO

    1 Mshukuruni Bwana, kwa kuwa yeye ni mwema,

    upendo wake wadumu milele.

    2 Waliokombolewa wa Bwana na waseme hivi,

    wale aliowaokoa kutoka mkono wa adui,

    3 wale aliowakusanya kutoka nchi mbalimbali,

    kutoka mashariki na magharibi,

    kutoka kaskazini na kusini.

  33. 9 Aliwapa watu wake ukombozi,

    aliamuru agano lake milele:

    jina lake ni takatifu na la kuogopwa.

  34. 2 Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,

    wala usisahau wema wake wote,

    3 akusamehe dhambi zako zote,

    akuponya magonjwa yako yote,

    4 aukomboa uhai wako na kaburi,

    akuvika taji ya upendo na huruma,

    5 atosheleza mahitaji yako kwa vitu vyema,

    ili ujana wako uhuishwe kama wa tai.

  35. 15 Ni nini basi? Je, tutende dhambi kwa kuwa hatuko chini ya sheria bali chini ya neema? La, hasha! 16 Je, hamjui kwamba mnapojitoa kwa mtu yeyote kama watumwa watiifu, ninyi ni watumwa wa yule mnayemtii, aidha watumwa wa dhambi, ambayo matokeo yake ni mauti, au watumwa wa utii ambao matokeo yake ni haki? 17 Lakini Mungu ashukuriwe kwa kuwa ninyi ambao kwanza mlikuwa watumwa wa dhambi, mmekuwa watii kutoka moyoni kwa mafundisho mliyopewa. 18 Nanyi, mkiisha kuwekwa huru mbali na dhambi, mmekuwa watumwa wa haki.

  36. 5 Ninaikabidhi roho yangu mikononi mwako,

    unikomboe Ee Bwana, uliye Mungu wa kweli.

  37. 15 Lakini Mungu atakomboa uhai wangu na kaburi,

    hakika atanichukua kwake.

  38. 57 Ulikuja karibu nilipokuita,

    nawe ukasema, “Usiogope.”

    58 Ee Bwana, ulichukua shauri langu,

    ukaukomboa uhai wangu.

  39. 3 Sisi sote pia tuliishi katikati yao hapo zamani, tukitimiza tamaa za asili yetu ya dhambi na kufuata tamaa zake na mawazo yake. Nasi kwa asili tulikuwa wana wa ghadhabu, kama mtu mwingine yeyote. 4 Lakini Mungu kwa upendo wake mwingi kwetu sisi, ambaye ni mwingi wa rehema, 5 hata tulipokuwa wafu kwa ajili ya makosa yetu, alitufanya tuwe hai pamoja na Kristo Yesu, yaani, mmeokolewa kwa neema. 6 Mungu alitufufua pamoja na Kristo na kutuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho katika Kristo Yesu, 7 ili katika ule ulimwengu ujao apate kuonyesha wingi wa neema yake isiyopimika, iliyodhihirishwa kwetu kwa wema wake ndani ya Kristo Yesu. 8 Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani, wala si kwa matendo yenu mema. Hii ni zawadi kutoka kwa Mungu, 9 si kwa matendo, ili mtu yeyote asije akajisifu. 10 Kwa maana sisi ni kazi ya mikono ya Mungu, tulioumbwa katika Kristo Yesu, ili tupate kutenda matendo mema, ambayo Mungu alitangulia kuyaandaa tupate kuishi katika hayo.

  40. 3 Kisha akamwambia yule jamaa wa karibu wa kukomboa, “Naomi, aliyerudi hapa kutoka nchi ya Moabu, anauza sehemu ya ardhi iliyokuwa mali ya ndugu yetu Elimeleki. 4 Nami niliwaza nikujulishe wewe na kukuambia uinunue mbele ya hawa waliopo hapa, na mbele ya wazee wa watu wangu. Kama wewe utaikomboa, haya fanya hivyo. Lakini kama hutaikomboa, uniambie, ili nijue. Kwa kuwa hakuna mtu mwingine mwenye haki ya kuikomboa ila wewe na baada yako ni mimi.”

    Naye akasema, “Nitaikomboa mimi.”

    5 Ndipo Boazi akasema “Siku utakaponunua hiyo ardhi kutoka kwa Naomi na Ruthu, Mmoabu, itakubidi kumchukua pia huyo mjane, ili kudumisha jina la marehemu pamoja na mali yake.”

    6 Aliposikia hili, yule jamaa wa karibu wa kukomboa akasema, “Basi mimi sitaweza kuikomboa, kwa sababu inaonekana nitauhatarisha urithi wangu. Wewe ikomboe mwenyewe. Mimi sitaweza.”

  41. 14 “Nitawakomboa watu hawa kutoka nguvu za kaburi,

    nitawakomboa kutoka mautini.

    Yako wapi, ee mauti, mateso yako?

    Uko wapi, ee kuzimu, uharibifu wako?

    “Sitakuwa na huruma,

  42. 38 Wakati huo huo, Ana alikuja akaanza kusifu, akimshukuru Mungu na kusema habari za huyo mtoto kwa watu wote waliokuwa wakitarajia ukombozi wa Yerusalemu.

  43. 9 Lakini ninyi ni taifa teule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu walio milki ya Mungu, mlioitwa ili kutangaza sifa zake yeye aliyewaita kutoka gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu.

  44. 19 “Mzaliwa wa kwanza wa kila tumbo ni mali yangu, pamoja na wazaliwa wa kwanza wote wa kiume wa mifugo yako, ikiwa ni wa ngʼombe au wa kondoo au mbuzi. 20 Utakomboa mzaliwa wa kwanza wa punda kwa mwana-kondoo, lakini kama humkomboi, utavunja shingo yake. Utakomboa wazaliwa wako wa kwanza wote wa kiume.

    “Mtu yeyote asije mbele zangu mikono mitupu.

  45. 23 Naye ni nani aliye kama watu wako Israeli, taifa pekee duniani ambalo Mungu alitoka kwenda kulikomboa kwa ajili yake mwenyewe, na kujifanyia jina mwenyewe, kwa kufanya maajabu makubwa na ya kutisha kwa kuwafukuza mataifa na miungu yao mbele ya watu wako, ambao uliwakomboa kutoka Misri? 24 Umeimarisha watu wako Israeli hasa kama watu wako mwenyewe milele, nawe, Ee Bwana, umekuwa Mungu wao.

  46. 15 Kwa mkono wako wenye nguvu umewakomboa watu wako,

    uzao wa Yakobo na Yosefu.

  47. 3 Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana:

    “Mliuzwa pasipo malipo,

    nanyi mtakombolewa bila fedha.”

  48. 11 Bali mimi ninaishi maisha yasiyo na lawama;

    nikomboe na unihurumie.

  49. 9 Alikemea Bahari ya Shamu, nayo ikakauka,

    akawaongoza katika vilindi vyake kama vile jangwani.

    10 Aliwaokoa mikononi mwa adui;

    kutoka mikononi mwa adui aliwakomboa.

    11 Maji yaliwafunika adui zao,

    hakunusurika hata mmoja.

  50. 7 Hili ndilo asemalo Bwana,

    yeye Mkombozi na Aliye Mtakatifu wa Israeli,

    kwake yeye aliyedharauliwa na kuchukiwa na taifa,

    kwa mtumishi wa watawala:

    “Wafalme watakuona na kusimama,

    wakuu wataona na kuanguka kifudifudi,

    kwa sababu ya Bwana, aliye mwaminifu,

    yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, aliyekuchagua wewe.”

  51. 9 Katika taabu zao zote naye alitaabika,

    na malaika wa uso wake akawaokoa.

    Katika upendo wake na rehema zake aliwakomboa,

    akawainua na kuwachukua siku zote zilizopita.

  52. 1 Watoto wangu wapendwa, nawaandikia haya ili msitende dhambi. Lakini kama mtu yeyote akitenda dhambi, tunaye Mwombezi kwa Baba: ndiye Yesu Kristo, Mwenye Haki. 2 Yeye ndiye dhabihu ya upatanisho kwa ajili ya dhambi zetu, wala si kwa ajili ya dhambi zetu tu, bali pia kwa ajili ya dhambi za ulimwengu wote.

  53. 11 “Ni nani miongoni mwa miungu aliye kama wewe, Ee Bwana?

    Ni nani kama Wewe:

    uliyetukuka katika utakatifu,

    utishaye katika utukufu,

    ukitenda maajabu?

    12 Uliunyoosha mkono wako wa kuume

    na nchi ikawameza.

    13 “Katika upendo wako usiokoma utawaongoza

    watu uliowakomboa.

    Katika nguvu zako utawaongoza

    mpaka makao yako matakatifu.

  54. 7 Bwana hakuweka upendo wake juu yenu na kuwachagua kwa sababu mlikuwa wengi mno kuliko watu wengine, kwa maana ninyi ndio mliokuwa wachache sana kuliko mataifa yote. 8 Lakini ni kwa sababu Bwana aliwapenda ninyi na kutunza kiapo alichowaapia babu zenu kwamba atawatoa ninyi kwa mkono wenye nguvu na kuwakomboa kutoka nchi ya utumwa, kutoka nguvu za Farao mfalme wa Misri.

  55. 22 Ee Mungu, wakomboe Israeli,

    katika shida zao zote!

  56. 11 Wale waliolipiwa fidia na Bwana watarudi.

    Wataingia Sayuni wakiimba;

    furaha ya milele itakuwa taji juu ya vichwa vyao.

    Furaha na shangwe zitawapata,

    huzuni na kulia kwa uchungu kutatoweka.

  57. 21 “Nitakuokoa kutoka mikono ya waovu,

    na kukukomboa kutoka makucha ya watu wakatili.”

  58. 11 Kwa kuwa Bwana atamlipia fidia Yakobo

    na kuwakomboa mkononi mwa walio na nguvu kuliko wao.

  59. 20 Nimesulubiwa pamoja na Kristo, wala si mimi tena ninayeishi, bali Kristo ndiye aishiye ndani yangu. Uhai nilio nao sasa katika mwili, ninaishi kwa imani ya Mwana wa Mungu, aliyenipenda na kujitoa kwa ajili yangu.

  60. 9 Akauliza, “Wewe ni nani?”

    Akajibu, “Ni mimi Ruthu, mjakazi wako. Uitande nguo yako juu yangu, kwa sababu wewe ndiwe jamaa wa karibu wa kutukomboa.”

  61. 21 Naye ni nani aliye kama watu wako Israeli: taifa pekee duniani ambalo Mungu wake alitoka kwenda kulikomboa kwa ajili yake mwenyewe na kujifanyia jina kwa ajili yake mwenyewe, kwa kufanya maajabu makubwa na ya kutisha kwa kuwafukuza mataifa mbele ya watu wako, ambao uliwakomboa kutoka Misri? 22 Uliwafanya watu wako Israeli kuwa watu wako wewe mwenyewe milele, nawe, Ee Bwana Mungu, umekuwa Mungu wao.

  62. 26 Inuka na utusaidie,

    utukomboe kwa sababu ya upendo wako usio na mwisho.

  63. 17 Usimfiche mtumishi wako uso wako,

    uharakishe kunijibu, kwa sababu niko katika shida.

    18 Njoo karibu uniokoe,

    nikomboe kwa sababu ya adui zangu.

  64. 23 Midomo yangu itapaza sauti kwa furaha

    ninapokuimbia sifa,

    mimi, ambaye umenikomboa.

  65. 34 Kila mara Mungu alipowaua baadhi yao,

    waliosalia walimtafuta,

    walimgeukia tena kwa shauku.

    35 Walikumbuka kwamba Mungu alikuwa Mwamba wao,

    kwamba Mungu Aliye Juu Sana alikuwa Mkombozi wao.

  66. 5 Kwa maana Muumba wako ndiye mume wako,

    Bwana Mwenye Nguvu Zote ndilo jina lake,

    yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli ni Mkombozi wako,

    yeye anaitwa Mungu wa dunia yote.

    6 Bwana atakuita urudi

    kana kwamba ulikuwa mke aliyeachwa na kuhuzunishwa rohoni;

    kama mke aliyeolewa bado angali kijana

    na kukataliwa,” asema Mungu wako.

    7 “Kwa kitambo kidogo nilikuacha,

    lakini kwa huruma nyingi nitakurudisha.

    8 Katika ukali wa hasira

    nilikuficha uso wangu kwa kitambo,

    lakini kwa fadhili za milele

    nitakuwa na huruma juu yako,”

    asema Bwana Mkombozi wako.

  67. 21 Hivyo naiona sheria ikitenda kazi. Ninapotaka kutenda jema, jambo baya liko papo hapo. 22 Kwa maana katika utu wangu wa ndani naifurahia sheria ya Mungu. 23 Lakini ninaona kuna sheria nyingine inayotenda kazi katika viungo vya mwili wangu inayopigana vita dhidi ya ile sheria ya akili yangu. Sheria hii inanifanya mateka wa ile sheria ya dhambi inayofanya kazi katika viungo vya mwili wangu.

    24 Ole wangu mimi maskini! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti?

    25 Ashukuriwe Mungu kwa njia ya Yesu Kristo Bwana wetu! Hivyo basi, mimi mwenyewe kwa akili zangu ni mtumwa wa sheria ya Mungu, lakini katika asili ya dhambi ni mtumwa wa sheria ya dhambi.

  68. 1 Kisha yule malaika akanionyesha mto wa maji ya uzima, maangavu kama kioo yakitiririka kutoka kwenye kile kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana-Kondoo, 2 kupitia katikati ya barabara kuu ya huo mji. Kwenye kila upande wa huo mto kulikuwa na mti wa uzima utoao matunda ya aina kumi na mbili, ukizaa matunda yake kila mwezi. Nayo majani ya mti huo ni kwa ajili ya uponyaji wa mataifa. 3 Katika mji huo hakutakuwa tena na laana, bali kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana-Kondoo kitakuwamo humo na watumishi wake watamtumikia, 4 nao watamwona uso wake na Jina lake litakuwa kwenye vipaji vya nyuso zao. 5 Usiku hautakuwako tena, wala hawatahitaji mwanga wa taa au wa jua, kwa maana Bwana Mungu atakuwa nuru yao, nao watatawala milele na milele.