61 Bible Verses About Water

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Water
  1. 37 Siku ile ya mwisho ya Sikukuu, siku ile kuu, wakati Yesu akiwa amesimama huko, akapaza sauti yake akasema, “Kama mtu yeyote anaona kiu na aje kwangu anywe. 38 Yeyote aniaminiye mimi, kama Maandiko yasemavyo, vijito vya maji ya uzima vitatiririka ndani mwake.”

  2. 10 Yesu akajibu akamwambia, “Kama ungelijua karama ya Mungu, naye ni nani anayekuambia, Nipe maji ninywe, wewe ungelimwomba yeye, naye angelikupa maji yaliyo hai.”

    11 Yule mwanamke akamjibu, “Bwana, wewe huna chombo cha kutekea maji na kisima hiki ni kirefu. Hayo maji ya uzima utayapata wapi? 12 Kwani wewe ni mkuu kuliko baba yetu Yakobo ambaye alitupatia kisima hiki, ambacho yeye pamoja na watoto wake na mifugo yake walikitumia?”

    13 Yesu akamjibu, “Kila mtu anayekunywa maji ya kisima hiki ataona kiu tena. 14 Lakini yeyote anywaye maji nitakayompa hataona kiu kamwe. Maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujika uzima wa milele.”

    15 Yule mwanamke akamwambia, “Bwana, tafadhali nipe maji hayo ili nisipate kiu tena na wala nisije tena hapa kuteka maji!”

  3. 17 Roho na bibi arusi wanasema, “Njoo!” Naye asikiaye na aseme, “Njoo!” Yeyote mwenye kiu na aje, na kila anayetaka na anywe maji ya uzima bure.

  4. 1 Kisha yule malaika akanionyesha mto wa maji ya uzima, maangavu kama kioo yakitiririka kutoka kwenye kile kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana-Kondoo, 2 kupitia katikati ya barabara kuu ya huo mji. Kwenye kila upande wa huo mto kulikuwa na mti wa uzima utoao matunda ya aina kumi na mbili, ukizaa matunda yake kila mwezi. Nayo majani ya mti huo ni kwa ajili ya uponyaji wa mataifa. 3 Katika mji huo hakutakuwa tena na laana, bali kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana-Kondoo kitakuwamo humo na watumishi wake watamtumikia, 4 nao watamwona uso wake na Jina lake litakuwa kwenye vipaji vya nyuso zao. 5 Usiku hautakuwako tena, wala hawatahitaji mwanga wa taa au wa jua, kwa maana Bwana Mungu atakuwa nuru yao, nao watatawala milele na milele.

  5. 24 “ ‘Kwa kuwa nitawaondoa ninyi toka mataifa, nitawakusanya kutoka nchi zote na kuwarudisha kwenye nchi yenu wenyewe. 25 Nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtakuwa safi, nitawatakasa kutoka uchafu wenu wote na kutoka sanamu zenu zote. 26 Nitawapa moyo mpya na kuweka roho mpya ndani yenu, nitaondoa ndani yenu moyo wenu wa jiwe na kuwapa moyo wa nyama. 27 Nami nitaweka Roho yangu ndani yenu na kuwafanya ninyi mfuate amri zangu na kuwafanya kuwa waangalifu kuzishika sheria zangu.

  6. 1 Basi palikuwa na mtu mmoja Farisayo, jina lake Nikodemo, mmoja wa Baraza la Wayahudi lililotawala. 2 Huyu alimjia Yesu usiku akamwambia, “Rabi, tunajua kuwa wewe ni mwalimu uliyetumwa na Mungu, kwa maana hakuna mtu awezaye kufanya miujiza hii uifanyayo wewe, kama Mungu hayuko pamoja naye.”

    3 Yesu akamjibu, “Amin, amin nakuambia, hakuna mtu anayeweza kuuona Ufalme wa Mungu kama hajazaliwa mara ya pili.”

    4 Nikodemo akauliza, “Awezaje mtu kuzaliwa wakati akiwa mzee? Hakika hawezi kuingia mara ya pili kwenye tumbo la mama yake ili azaliwe!”

    5 Yesu akamwambia, “Amin, amin nakuambia, hakuna mtu yeyote anayeweza kuingia Ufalme wa Mungu kama hajazaliwa kwa maji na kwa Roho.

  7. 19 Kwa hiyo, ndugu zangu, kwa kuwa tunao ujasiri wa kupaingia Patakatifu pa Patakatifu kwa damu ya Yesu, 20 kwa njia mpya iliyo hai tuliyofunguliwa kwa ajili yetu kupitia kwenye lile pazia, yaani, mwili wake, 21 basi kwa kuwa tunaye Kuhani Mkuu juu ya nyumba ya Mungu, 22 sisi na tumkaribie Mungu kwa moyo mnyofu kwa imani timilifu, mioyo yetu ikiwa imenyunyizwa damu ya Kristo na kuwa safi kutokana na dhamiri mbaya nayo miili yetu ikiwa imeoshwa kwa maji safi. 23 Tushike kwa uthabiti lile tumaini la ukiri wetu bila kuyumbayumba, kwa maana yeye aliyeahidi ni mwaminifu.

  8. 13 Kisha mmoja wa wale wazee ishirini na wanne akaniuliza, “Ni nani hawa waliovaa mavazi meupe, nao wametoka wapi?”

    14 Nikamjibu, “Bwana, wewe wajua.”

    Naye akasema, “Hawa ni wale waliotoka katika ile dhiki kuu, nao wamefua mavazi yao katika damu ya Mwana-Kondoo na kuyafanya meupe kabisa. 15 Kwa hiyo,

    “Wako mbele ya kiti cha enzi cha Mungu

    na kumtumikia usiku na mchana

    katika hekalu lake;

    naye aketiye katika kile kiti cha enzi

    atatanda hema yake juu yao.

    16 Kamwe hawataona njaa

    wala kiu tena.

    Jua halitawapiga

    wala joto lolote liunguzalo.

    17 Kwa maana Mwana-Kondoo

    aliyeko katikati ya kile kiti cha enzi

    atakuwa Mchungaji wao;

    naye atawaongoza kwenda

    kwenye chemchemi za maji yaliyo hai.

    Naye Mungu atafuta kila chozi

    kutoka macho yao.”

  9. 5 Kwa nini mmetupandisha kutoka Misri mpaka mahali hapa pa kutisha? Hapa hakuna nafaka wala tini, zabibu au makomamanga. Wala hapa hakuna maji ya kunywa!”

    6 Mose na Aroni wakaondoka pale kwenye kusanyiko mpaka kwenye mlango wa Hema la Kukutania na kuanguka kifudifudi, nao utukufu wa Bwana ukawatokea. 7 Bwana akamwambia Mose, 8 “Chukua ile fimbo, na wewe na ndugu yako Aroni mkusanye kusanyiko pamoja. Nena na ule mwamba mbele ya macho yao, nao utatoa maji yake. Utatoa maji kutoka huo mwamba kwa ajili ya jumuiya ili wao na mifugo yao waweze kunywa.”

    9 Kwa hiyo Mose akaichukua hiyo fimbo kutoka pale ilipokuwa mbele za Bwana kama alivyomwagiza. 10 Mose na Aroni wakakusanya kusanyiko pamoja mbele ya huo mwamba, naye Mose akawaambia, “Sikilizeni, enyi waasi. Je, ni lazima tuwatoleeni maji kutoka mwamba huu?” 11 Ndipo Mose akainua mkono wake na kuupiga mwamba mara mbili kwa fimbo yake. Maji yakabubujika, nayo jumuiya na mifugo yao wakanywa.

  10. 15 Alipasua miamba jangwani

    na akawapa maji tele kama bahari,

    16 alitoa vijito kutoka kwenye jabali lililochongoka,

    akayafanya maji yatiririke kama mito.

    17 Lakini waliendelea kutenda dhambi dhidi yake,

    wakiasi jangwani dhidi ya Aliye Juu Sana.

    18 Kwa makusudi walimjaribu Mungu,

    wakidai vyakula walivyovitamani.

    19 Walinena dhidi ya Mungu, wakisema,

    “Je, Mungu aweza kuandaa meza jangwani?

    20 Alipopiga mwamba, maji yalitoka kwa nguvu,

    vijito vikatiririka maji mengi.

    Lakini je, aweza kutupa chakula pia?

    Je, anaweza kuwapa watu wake nyama?”

  11. 6 “Je, hii si ndiyo aina ya mfungo niliyoichagua:

    kufungua minyororo ya udhalimu,

    na kufungua kamba za nira,

    kuwaweka huru walioonewa,

    na kuvunja kila nira?

    7 Je, sio kushirikiana chakula chako na wenye njaa

    na kuwapatia maskini wasiokuwa na makao hifadhi,

    unapomwona aliye uchi, umvike,

    wala si kumkimbia mtu wa nyama na damu yako mwenyewe?

    8 Ndipo nuru yako itajitokeza kama mapambazuko

    na uponyaji wako utatokea upesi;

    ndipo haki yako itakapokutangulia mbele yako,

    na utukufu wa Bwana utakuwa mlinzi nyuma yako.

    9 Ndipo utaita, naye Bwana atajibu,

    utalia kuomba msaada,

    naye atasema: Mimi hapa.

    “Kama ukiiondoa nira ya udhalimu,

    na kunyoosha kidole na kuzungumza maovu,

    10 nanyi kama mkimkunjulia mtu mwenye njaa nafsi zenu

    na kutosheleza mahitaji ya walioonewa,

    ndipo nuru yenu itakapongʼaa gizani,

    nao usiku wenu utakuwa kama adhuhuri.

    11 Bwana atakuongoza siku zote,

    atayatosheleza mahitaji yako katika nchi kame,

    naye ataitia nguvu mifupa yako.

    Utakuwa kama bustani iliyonyweshwa vizuri,

    kama chemchemi ambayo maji yake hayakauki kamwe.

  12. 6 Akaniambia, “Imekwisha kuwa. Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. Yeye aonaye kiu nitampa kunywa kutoka chemchemi ya maji ya uzima bila gharama yoyote. 7 Yeye ashindaye atayarithi haya yote, nami nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu. 8 Lakini waoga, wasioamini, wachafu, wauaji, wazinzi, wachawi, waabudu sanamu, pamoja na waongo wote, mahali pao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili.”

  13. 1 Katika siku ile utasema:

    “Nitakusifu wewe, Ee Bwana.

    Ingawa ulinikasirikia,

    hasira yako imegeukia mbali

    nawe umenifariji.

    2 Hakika Mungu ni wokovu wangu;

    nitamtumaini wala sitaogopa.

    Bwana, Bwana, ni nguvu zangu na wimbo wangu;

    amekuwa wokovu wangu.”

    3 Kwa furaha mtachota maji

    kutoka visima vya wokovu.

  14. 1 “Njooni, ninyi nyote wenye kiu,

    njooni kwenye maji;

    nanyi ambao hamna fedha,

    njooni, nunueni na mle!

    Njooni, nunueni divai na maziwa

    bila fedha na bila gharama.

    2 Kwa nini kutumia fedha kwa kitu ambacho si chakula,

    na kutaabikia kitu kisichoshibisha?

    Sikilizeni, nisikilizeni mimi na mle kilicho kizuri,

    nazo nafsi zenu zitafurahia utajiri wa unono.

    3 Tegeni sikio mje kwangu,

    nisikieni mimi, ili nafsi zenu zipate kuishi.

    Nitafanya agano la milele nanyi,

    pendo la uaminifu nililomwahidi Daudi.

  15. 25 Ninyi waume, wapendeni wake zenu, kama vile Kristo alivyolipenda Kanisa akajitoa kwa ajili yake 26 kusudi alifanye takatifu, akilitakasa kwa kuliosha kwa maji katika Neno lake, 27 apate kujiletea Kanisa tukufu lisilo na doa wala kunyanzi au waa lolote, bali takatifu na lisilo na hatia.

  16. 8 Hili ndilo asemalo Bwana:

    “Wakati wangu uliokubalika nitakujibu,

    nami katika siku ya wokovu nitakusaidia;

    nitakuhifadhi, nami nitakufanya

    kuwa agano kwa ajili ya watu,

    ili kurudisha nchi

    na kugawanyia urithi tena wale waliokuwa ukiwa,

    9 kuwaambia mateka, ‘Tokeni nje,’

    nao wale walio gizani, ‘Kuweni huru!’

    “Watajilisha kando ya barabara

    na kupata malisho yao juu ya kila kilima kilicho kitupu.

    10 Hawataona njaa wala kuona kiu,

    wala hari ya jangwani au jua halitawapiga.

    Yeye mwenye huruma juu yao atawaonyesha njia,

    na kuwaongoza kando ya chemchemi za maji.

  17. 13 “Watu wangu wametenda dhambi mbili:

    Wameniacha mimi,

    niliye chemchemi ya maji yaliyo hai,

    nao wamejichimbia visima vyao wenyewe,

    visima vilivyobomoka, visivyoweza kuhifadhi maji.

  18. 6 Mungu akasema, “Iwepo nafasi kati ya maji igawe maji na maji.” 7 Kwa hiyo Mungu akafanya nafasi, akatenganisha maji yaliyo chini ya hiyo nafasi na maji yaliyo juu yake. Ikawa hivyo.

  19. 2 Unapopita kwenye maji makuu,

    nitakuwa pamoja nawe,

    unapopita katika mito ya maji,

    hayatakugharikisha.

    Utakapopita katika moto,

    hutaungua,

    miali ya moto haitakuunguza.

  20. 5 Mama yake akawaambia wale watumishi, “Lolote atakalowaambia, fanyeni.”

    6 Basi ilikuwepo mitungi sita ya kuhifadhia maji iliyotengenezwa kwa mawe kwa ajili ya kujitakasa kwa desturi ya Kiyahudi; kila mtungi ungeweza kuchukua vipipa viwili au vitatu.

    7 Yesu akawaambia wale watumishi, “Ijazeni hiyo mitungi maji.” Nao wakaijaza ile mitungi mpaka juu.

    8 Kisha akawaambia, “Sasa choteni hayo maji kidogo, mpelekeeni mkuu wa meza.”

    Hivyo wakachota, wakampelekea. 9 Yule mkuu wa meza akayaonja yale maji ambayo yalikuwa yamebadilika kuwa divai. Hakujua divai hiyo ilikotoka ingawa wale watumishi waliochota yale maji wao walifahamu. Basi akamwita bwana arusi kando 10 akamwambia, “Watu wote hutoa kwanza divai nzuri, kisha huleta ile divai hafifu wageni wakisha kunywa vya kutosha, lakini wewe umeiweka ile nzuri kupita zote mpaka sasa.”

    11 Huu, ndio uliokuwa muujiza wa kwanza Yesu aliofanya Kana ya Galilaya. Hivyo Yesu alidhihirisha utukufu wake, nao wanafunzi wake wakamwamini.

  21. 17 “Alinyoosha mkono kutoka juu na kunishika;

    alinitoa kutoka kilindi cha maji makuu.

    18 Aliniokoa kutoka adui wangu mwenye nguvu nyingi,

    kutoka adui zangu waliokuwa na nguvu nyingi kuliko mimi.

  22. 9 Mungu akasema, “Maji yaliyopo chini ya anga na yakusanyike mahali pamoja, pawepo na nchi kavu.” Ikawa hivyo. 10 Mungu akaiita nchi kavu “ardhi,” nalo lile kusanyiko la maji akaliita “bahari.” Mungu akaona kuwa ni vyema.

  23. 25 Ni nani aliyepasua mifereji kwa ajili ya maji mengi ya mvua yaendayo kasi

    na njia ya umeme wa radi,

    26 ili kusababisha mvua kunyeshea mahali pasipokaliwa na mtu,

    jangwa lisilo na yeyote ndani yake,

    27 ili kuitosheleza nchi ya ukiwa na jangwa,

    na majani yaanze kumea ndani yake?

    28 Je, mvua ina baba?

    Ni nani baba azaaye matone ya umande?

    29 Barafu inatoka tumbo la nani?

    Ni nani azaaye ukungu kutoka mbinguni,

    30 wakati maji yawapo magumu kama jiwe,

    wakati uso wa vilindi vya maji unapoganda?

  24. 13 Ee Bwana, uliye tumaini la Israeli,

    wote wakuachao wataaibika.

    Wale wanaogeukia mbali nawe wataandikwa mavumbini

    kwa sababu wamemwacha Bwana,

    chemchemi ya maji yaliyo hai.

  25. 1 Hapo mwanzo Mungu aliumba mbingu na dunia. 2 Wakati huu dunia ilikuwa haina umbo, tena ilikuwa tupu. Giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji, naye Roho wa Mungu alikuwa ametulia juu ya maji.

    3 Mungu akasema, “Iwepo nuru,” nayo nuru ikawepo.

  26. 17 Kisha Bwana akamwambia Mose, 18 “Tengeneza sinia la shaba lenye kitako cha shaba kwa ajili ya kunawia. Liweke kati ya Hema la Kukutania na madhabahu, kisha uweke maji ndani yake. 19 Aroni na wanawe watanawa mikono na miguu yao kwa maji yatokayo katika hilo sinia. 20 Wakati wowote wanapoingia katika Hema la Kukutania, watanawa kwa maji ili kwamba wasije wakafa. Pia, wanapokaribia madhabahu ili kuhudumu kwa kuleta sadaka zilizotolewa kwa Bwana kwa moto, 21 watanawa mikono na miguu yao ili kwamba wasije wakafa. Hii itakuwa ni amri ya kudumu kwa ajili ya Aroni na wazao wake kwa vizazi vijavyo.”

  27. 7 Baada ya hayo, kuhani lazima afue nguo zake, na aoge mwili wake kwa maji. Kisha anaweza kurudi kambini, lakini atakuwa najisi kwa kawaida ya ibada mpaka jioni. 8 Mtu amchomaye huyo mtamba lazima naye pia afue nguo zake na kuoga kwa maji, naye pia atakuwa najisi mpaka jioni.

    9 “Mtu ambaye ni safi atakusanya majivu ya mtamba huyo na kuyaweka mahali ambapo ni safi nje ya kambi kwa taratibu za kiibada. Yatahifadhiwa na jumuiya ya Kiisraeli kwa matumizi katika maji ya utakaso; ni kwa ajili ya kutakasa kutoka dhambini.

  28. Zaburi ya Daudi.

    1 Bwana ndiye mchungaji wangu,

    sitapungukiwa na kitu.

    2 Hunilaza katika malisho

    ya majani mabichi,

    kando ya maji matulivu huniongoza,

  29. 15 Kunywa maji kutoka kwenye kisima chako mwenyewe,

    maji yanayotiririka kutoka kwenye kisima chako mwenyewe.

    16 Je, chemchemi zako zifurike katika barabara za mji

    na vijito vyako vya maji viwanjani?

    17 Na viwe vyako mwenyewe,

    kamwe visishirikishwe wageni.

    18 Chemchemi yako na ibarikiwe

    na umfurahie mke wa ujana wako.

    19 Kulungu jike apendaye, kulungu mzuri:

    matiti yake na yakutosheleze siku zote,

    nawe utekwe daima na upendo wake.

    20 Kwa nini mwanangu, utekwe na mwanamke kahaba?

    Kwa nini ukumbatie kifua cha mke wa mwanaume mwingine?

  30. 4 Maneno ya kinywa cha mwanadamu ni kina cha maji,

    bali chemchemi ya hekima ni kijito kinachobubujika.

  31. 15 Daudi akatamani maji, akasema, “Laiti mtu angenipatia maji ya kunywa kutoka kisima kilicho karibu na lango la Bethlehemu!” 16 Basi mashujaa hao watatu wakapenya katikati ya Wafilisti, wakaenda kuchota maji kutoka kwa kisima kilicho karibu na lango la Bethlehemu, wakamletea Daudi. Lakini Daudi akakataa kuyanywa. Badala yake, aliyamimina mbele za Bwana.

  32. 18 “Katika siku hiyo milima itadondosha divai mpya,

    na vilima vitatiririka maziwa;

    mabonde yote ya Yuda yatatiririka maji.

    Chemchemi itatiririka kutoka kwenye nyumba ya Bwana

    na kunywesha Bonde la Shitimu.

  33. 40 “Mtu yeyote atakayewapokea ninyi atakuwa amenipokea mimi, na yeyote atakayenipokea mimi atakuwa amempokea yeye aliyenituma. 41 Mtu yeyote anayempokea nabii kwa kuwa ni nabii atapokea thawabu ya nabii, naye mtu anayempokea mwenye haki kwa kuwa ni mwenye haki atapokea thawabu ya mwenye haki. 42 Kama yeyote akimpa hata kikombe cha maji baridi mmoja wa hawa wadogo kwa kuwa ni mwanafunzi wangu, amin, nawaambia, hataikosa thawabu yake.”

  34. 5 Mama yao amekosa uaminifu

    na amewachukua mimba katika aibu.

    Gomeri alisema, ‘Nitawaendea wapenzi wangu,

    ambao hunipa chakula changu

    na maji yangu,

    sufu yangu na kitani yangu, mafuta yangu

    na kinywaji changu.’

  35. 25 Wakati wa zamu ya nne ya usiku, Yesu akawaendea wanafunzi wake akiwa anatembea juu ya maji. 26 Wanafunzi wake walipomwona akitembea juu ya maji, waliingiwa na hofu kuu, wakasema, “Ni mzimu.” Wakapiga yowe kwa kuogopa.

    27 Lakini mara Yesu akasema nao, akawaambia, “Jipeni moyo! Ni mimi. Msiogope.”

    28 Petro akamjibu, “Bwana, ikiwa ni wewe, niambie nije kwako nikitembea juu ya maji.”

    29 Yesu akamwambia, “Njoo.”

    Basi Petro akatoka kwenye chombo, akatembea juu ya maji kumwelekea Yesu.

  36. 11 Je, chemchemi yaweza kutoa katika tundu moja maji matamu na maji ya chumvi? 12 Je, ndugu zangu, mtini waweza kuzaa zeituni, au mzabibu kuzaa tini? Wala chemchemi ya maji ya chumvi haiwezi kutoa maji matamu.

  37. 1 Kisha nikasikia sauti kubwa kutoka mle Hekaluni ikiwaambia wale malaika saba, “Nendeni, mkayamwage duniani hayo mabakuli saba ya ghadhabu ya Mungu.”

    2 Malaika wa kwanza akaenda akalimwaga hilo bakuli lake juu ya nchi. Majipu mabaya yenye maumivu makali yakawapata wale watu wote waliokuwa na chapa ya yule mnyama na walioabudu sanamu yake.

    3 Malaika wa pili akalimwaga bakuli lake baharini, nayo ikabadilika kuwa damu kama ya mtu aliyekufa na kila kiumbe hai kilichokuwa ndani ya bahari kikafa.

    4 Malaika wa tatu akalimwaga bakuli lake katika mito na chemchemi za maji, nazo zikawa damu. 5 Ndipo nikamsikia malaika msimamizi wa maji akisema:

    “Wewe una haki katika hukumu hizi ulizotoa,

    wewe uliyeko, uliyekuwako, Uliye Mtakatifu,

    kwa sababu umehukumu hivyo;

    6 kwa kuwa walimwaga damu ya watakatifu wako

    na manabii wako,

    nawe umewapa damu wanywe

    kama walivyostahili.”

  38. 19 Watumishi wa Isaki wakachimba katika lile bonde wakagundua huko kisima chenye maji safi. 20 Lakini wachungaji wa Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaki wakisema, “Maji haya ni yetu!” Ndipo akakiita kile kisima Eseki, kwa sababu waligombana naye. 21 Kisha wakachimba kisima kingine, lakini hata hicho pia wakakigombania, akakiita Sitna. 22 Akaondoka huko, akachimba kisima kingine, wala hakuna yeyote aliyekigombania. Akakiita Rehobothi, akisema, “Sasa Bwana ametufanyia nafasi, nasi tutastawi katika nchi.”

  39. 21 Ndipo Mose akanyoosha mkono wake juu ya bahari, naye Bwana akayasukuma maji ya bahari nyuma kwa upepo mkali wa mashariki usiku ule wote na kupafanya nchi kavu. Maji yakagawanyika, 22 nao Waisraeli wakapita baharini mahali pakavu, maji yakiwa ukuta upande wao wa kuume na upande wao wa kushoto.

  40. 7 Kwa kuwa Bwana Mungu wenu anawaleta katika nchi nzuri, nchi yenye vijito na mabwawa ya maji, yenye chemchemi zinazotiririka mabondeni na katika vilima; 8 nchi yenye ngano na shayiri, mizabibu na mitini, mikomamanga, mafuta ya zeituni na asali; 9 nchi ambayo chakula hakitapungua na hamtakosa chochote; nchi ambayo miamba yake ni chuma na mnaweza kuchimba shaba kutoka kwenye vilima.

    10 Wakati mtakapokwisha kula na kushiba, msifuni Bwana Mungu wenu kwa ajili ya nchi nzuri aliyowapa.

  41. 7 Hukumpa maji aliyechoka,

    nawe ulimnyima chakula mwenye njaa,

  42. 10 Mto wa kunyeshea bustani ulitiririka toka Edeni, kuanzia hapa ukagawanyika kuwa mito minne. 11 Mto wa kwanza uliitwa Pishoni, nao huzunguka nchi yote ya Havila ambako kuna dhahabu. 12 (Dhahabu ya nchi hiyo ni nzuri, bedola na vito shohamu pia hupatikana huko.) 13 Jina la mto wa pili ni Gihoni, ambao huzunguka nchi yote ya Kushi. 14 Jina la mto wa tatu ni Tigrisi, unaopita mashariki ya Ashuru. Mto wa nne ni Frati.

  43. 11 Katika siku ya kumi na saba ya mwezi wa pili mwaka wa 600 wa kuishi kwake Noa, siku hiyo ndipo chemchemi zote hata zilizo chini sana ya ardhi zilibubujika kwa nguvu, na malango ya mafuriko ya mbinguni yakafunguliwa. 12 Mvua ikanyesha juu ya nchi siku arobaini usiku na mchana.

  44. 22 Kisha Mose akawaongoza Israeli kutoka Bahari ya Shamu na kuingia katika Jangwa la Shuri. Kwa siku tatu walisafiri jangwani bila kupata maji. 23 Walipofika Mara, hawakuweza kunywa maji yake kwa sababu yalikuwa machungu. (Ndiyo sababu mahali hapo panaitwa Mara) 24 Kwa hiyo watu wakamnungʼunikia Mose, wakisema, “Tunywe nini?”

    25 Ndipo Mose akamlilia Bwana, naye Bwana akamwonyesha kipande cha mti. Akakitupa ndani ya maji, nayo maji yakawa matamu.

    Huko Bwana akawapa amri na sheria na huko akawajaribu. 26 Mungu akasema, “Kama mkisikiliza kwa bidii sauti ya Bwana Mungu wenu na kuyafanya yaliyo sawa machoni pake, kama mkiyatii maagizo yake na kuzishika amri zake zote, sitaleta juu yenu ugonjwa wowote niliowaletea Wamisri, kwa kuwa Mimi ndimi Bwana, niwaponyaye.”

    27 Kisha wakafika Elimu, mahali palipokuwa na chemchemi kumi na mbili, na miti sabini ya mitende, wakapiga kambi huko karibu na maji.

  45. 19 Watu wa mji wakamwambia Elisha, “Tazama, bwana wetu, mahali mji huu ulipojengwa ni pazuri, kama bwana wangu aonavyo, lakini maji yake ni mabaya, na nchi haizai.”

    20 Akasema, “Nileteeni bakuli mpya, mweke chumvi ndani yake.” Kwa hiyo wakamletea.

    21 Kisha akaenda kwenye chemchemi na kuitupa ile chumvi ndani yake, akisema, “Hili ndilo asemalo Bwana: ‘Nimeyaponya maji haya. Kamwe hayatasababisha mauti tena wala kutozaa.’ ” 22 Nayo yale maji yakaponywa mpaka leo, sawasawa na neno la Elisha alilokuwa amesema.

  46. KITABU CHA PILI

    Kwa mwimbishaji. Utenzi wa wana wa Kora.

    1 Kama vile ayala aoneavyo shauku vijito vya maji,

    ndivyo nafsi yangu ikuoneavyo shauku, Ee Mungu.

    2 Nafsi yangu inamwonea Mungu kiu, Mungu aliye hai.

    Ni lini nitaweza kwenda kukutana na Mungu?

    3 Machozi yangu yamekuwa chakula changu

    usiku na mchana,

    huku watu wakiniambia mchana kutwa,

    “Yuko wapi Mungu wako?”

    4 Mambo haya nayakumbuka

    ninapoimimina nafsi yangu:

    Jinsi nilivyokuwa nikienda na umati wa watu,

    nikiongoza maandamano kuelekea kwenye nyumba ya Mungu,

    kwa kelele za shangwe na za shukrani

    katikati ya umati uliosherehekea.

    5 Ee nafsi yangu, kwa nini unasononeka?

    Kwa nini unafadhaika hivyo ndani yangu?

    Weka tumaini lako kwa Mungu,

    kwa sababu bado nitamsifu,

    Mwokozi wangu na

  47. 5 Makusudi ya moyo wa mwanadamu ni maji yenye kina,

    lakini mtu mwenye ufahamu huyachota.

  48. 6 Huko ndiko kulikokuwa na kile kisima cha Yakobo. Naye Yesu alikuwa amechoka kwa kuwa alikuwa ametoka safarini. Akaketi karibu na hicho kisima. Ilikuwa yapata saa sita mchana.

  49. 8 Malaika wa pili akaipiga tarumbeta yake na kitu kama mlima mkubwa unaowaka moto kikatupwa baharini. Theluthi ya bahari ikawa damu, 9 theluthi ya viumbe vyenye uhai viishivyo baharini vikafa na theluthi ya meli zikaharibiwa.

    10 Malaika wa tatu akaipiga tarumbeta yake, na nyota kubwa iliyokuwa ikiwaka kama taa ikaanguka toka angani, ikaangukia theluthi ya mito na chemchemi za maji. 11 Nyota hiyo inaitwa Uchungu. Theluthi ya maji yakawa machungu na watu wengi wakafa kutokana na maji hayo kwa maana yalikuwa machungu.

  50. 20 Mungu akasema, “Kuwepo na viumbe hai tele kwenye maji, nao ndege waruke juu ya dunia katika nafasi ya anga.” 21 Kwa hiyo Mungu akaumba viumbe wakubwa wa baharini na kila kiumbe hai kiendacho majini kulingana na aina zake, na kila ndege mwenye mabawa kulingana na aina yake. Mungu akaona kuwa hili ni jema.

  51. 14 Kesho yake asubuhi na mapema, Abrahamu akachukua chakula na kiriba cha maji, akampa Hagari. Akaviweka mabegani mwa Hagari, akamwondoa pamoja na kijana. Hagari akashika njia, akatangatanga katika jangwa la Beer-Sheba.

    15 Maji yalipokwisha kwenye kiriba, akamwacha kijana chini ya mojawapo ya vichaka. 16 Kisha akajiendea zake akaketi karibu, umbali wa kutupa mshale, akawaza, “Siwezi kumwangalia kijana akifa.” Ikawa alipokuwa ameketi pale karibu, akaanza kulia kwa huzuni.

    17 Mungu akamsikia kijana akilia, malaika wa Mungu akamwita Hagari kutoka mbinguni na kumwambia, “Kuna nini Hagari? Usiogope, Mungu amesikia kijana analia akiwa amelala pale. 18 Mwinue kijana na umshike mkono, kwa maana nitamfanya kuwa taifa kubwa.”

    19 Ndipo Mungu akamfumbua Hagari macho yake naye akaona kisima cha maji. Hivyo akaenda akajaza kiriba maji na kumpa kijana anywe.

  52. 1 Jumuiya yote ya Israeli ikaondoka kutoka Jangwa la Sini, ikisafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine kama Bwana alivyoagiza. Wakapiga kambi huko Refidimu, lakini hapakuwa na maji ya watu kunywa. 2 Kwa hiyo wakagombana na Mose wakisema, “Tupe maji ya kunywa.”

    Mose akajibu, “Mbona mnagombana nami? Kwa nini mnamjaribu Bwana?”

    3 Lakini watu walikuwa na kiu huko, wakanungʼunika dhidi ya Mose, wakisema, “Kwa nini ulitutoa kule Misri, ukatuleta hapa utuue kwa kiu sisi, watoto wetu na mifugo yetu?”

    4 Kisha Mose akamlilia Bwana, akasema, “Niwafanyie nini watu hawa? Sasa wanakaribia kunipiga kwa mawe.”

    5 Bwana akamjibu Mose, “Pita mbele ya watu. Wachukue pamoja nawe baadhi ya wazee wa Israeli, ichukue mkononi mwako ile fimbo uliyopiga nayo Mto Naili, nawe uende. 6 Huko nitasimama mbele yako karibu na mwamba wa Horebu. Uupige mwamba na maji yatatoka ndani yake kwa ajili ya watu kunywa.” Kwa hiyo Mose akafanya haya mbele ya wazee wa Israeli. 7 Naye akapaita mahali pale Masa, na Meriba kwa sababu Waisraeli waligombana na kumjaribu Bwana wakisema, “Je, Bwana yu pamoja nasi au la?”

  53. 14 Basi, watu walipovunja kambi ili kuvuka Yordani, makuhani wakiwa wamebeba Sanduku la Agano waliwatangulia. 15 Wakati huu ulikuwa wakati wa mavuno, nao Mto Yordani ulikuwa umefurika hadi kwenye kingo zake. Ilikuwa kawaida ya Yordani kufurika nyakati zote za mavuno. Mara tu makuhani wale waliokuwa wamebeba Sanduku la Agano walipofika mtoni na nyayo zao kuzama ndani ya yale maji, 16 maji hayo yaliyotiririka kutoka upande wa juu yaliacha kutiririka yakasimama kama chuguu mbali kabisa nao, kwenye mji ulioitwa Adamu kwenye eneo la Sarethani, wakati yale maji yaliyokuwa yanatiririka kuingia kwenye Bahari ya Araba (yaani Bahari ya Chumvi), yalitindika kabisa. Hivyo watu wakavuka kukabili Yeriko.

    17 Wale makuhani waliobeba Sanduku la Agano la Bwana, wakasimama imara mahali pakavu katikati ya Mto Yordani, wakati Waisraeli wote wakiwa wanapita hadi taifa lote likaisha kuvuka mahali pakavu.

  54. KITABU CHA KWANZA

    1 Heri mtu yule ambaye

    haendi katika shauri la watu waovu,

    wala hasimami katika njia ya wenye dhambi,

    au kuketi katika baraza la wenye mizaha.

    2 Bali huifurahia sheria ya Bwana,

    naye huitafakari hiyo sheria usiku na mchana.

    3 Mtu huyo ni kama mti uliopandwa

    kando ya vijito vya maji,

    ambao huzaa matunda kwa majira yake

    na majani yake hayanyauki.

    Lolote afanyalo hufanikiwa.

  55. 9 Waitunza nchi na kuinyeshea,

    waitajirisha kwa wingi.

    Vijito vya Mungu vimejaa maji

    ili kuwapa watu nafaka,

    kwa maana wewe umeviamuru.

    10 Umeilowesha mifereji yake

    na kusawazisha kingo zake;

    umeilainisha kwa manyunyu

    na kuibariki mimea yake.

    11 Umeuvika mwaka taji ya baraka,

    magari yako yanafurika kwa wingi.

    12 Mbuga za majani za jangwani umezineemesha;

    vilima vimevikwa furaha.

  56. 17 “Maji yaliyoibiwa ni matamu;

    chakula kinacholiwa sirini ni kitamu!”

  57. 3 Tumkubali Bwana,

    tukaze kumkubali yeye.

    Kutokea kwake ni hakika kama vile

    kuchomoza kwa jua;

    atatujia kama mvua za masika,

    kama vile mvua za vuli

    ziinyweshavyo nchi.”

  58. 11 “Mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba. Lakini nyuma yangu anakuja yeye aliye na uwezo kuliko mimi, ambaye sistahili hata kuvichukua viatu vyake. Yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto.

  59. 13 Kisha Yesu akaja kutoka Galilaya mpaka Mto Yordani ili Yohana ambatize. 14 Lakini Yohana akajitahidi kumzuia, akimwambia, “Mimi ninahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu nikubatize?”

    15 Lakini Yesu akamjibu, “Kubali hivi sasa, kwa maana ndivyo itupasavyo kwa njia hii kuitimiza haki yote.” Hivyo Yohana akakubali.

    16 Naye Yesu alipokwisha kubatizwa, mara alipotoka ndani ya maji, ghafula mbingu zikafunguka, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua na kutulia juu yake. 17 Nayo sauti kutoka mbinguni ikasema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa, ambaye ninapendezwa sana naye.”

  60. 41 Amin, nawaambia, yeyote awapaye ninyi kikombe cha maji kwa Jina langu kwa sababu ninyi ni mali ya Kristo, hakika hataikosa thawabu yake.”

  61. 36 Walipokuwa wakiendelea na safari wakafika mahali palipokuwa na maji, yule towashi akamuuliza Filipo, “Tazama, hapa kuna maji. Kitu gani kitanizuia nisibatizwe?” [ 37 Filipo akamwambia, “Kama ukiamini kwa moyo wako wote unaweza kubatizwa.” Akajibu, “Naamini kuwa Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu.”] 38 Naye akaamuru lile gari lisimamishwe. Wakateremka kwenye maji wote wawili, yule towashi na Filipo, naye Filipo akambatiza. 39 Nao walipopanda kutoka kwenye maji, ghafula Roho wa Bwana akamnyakua Filipo, naye towashi hakumwona tena, lakini akaenda zake akifurahi.