47 Bible Verses About Loyalty

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Loyalty
  1. 15 Naomi akamwambia, “Tazama, mwenzako anarejea kwa watu wake na kwa miungu yake. Rudi pamoja naye.”

    16 Lakini Ruthu akajibu, “Usinisihi nikuache au niache kukufuata. Utakakokwenda nami nitakwenda, na wewe utakapoishi nitaishi. Watu wako watakuwa watu wangu, na Mungu wako atakuwa Mungu wangu. 17 Pale utakapofia nami nitafia hapo, na papo hapo nitazikwa. Bwana na aniadhibu vikali, kama kitu kingine chochote kitanitenga nawe isipokuwa kifo.”

  2. 5 Hakuna mtu yeyote atakayeweza kushindana na wewe siku zote za maisha yako. Kama vile nilivyokuwa pamoja na Mose, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe, sitakuacha wala sitakupungukia.

  3. 17 Rafiki hupenda wakati wote

    naye ndugu amezaliwa kwa ajili ya wakati wa shida.

  4. 22 Kwa sababu ya upendo mkuu wa Bwana, hatuangamii,

    kwa kuwa huruma zake hazikomi kamwe.

    23 Ni mpya kila asubuhi,

    uaminifu wako ni mkuu.

    24 Nimeiambia nafsi yangu, “Bwana ni fungu langu,

    kwa hiyo nitamngojea.”

  5. 6 Kwa kuwa wewe ni taifa takatifu kwa Bwana Mungu wako. Bwana Mungu wako amekuchagua wewe kutoka mataifa yote juu ya uso wa dunia kuwa watu wake, hazina yake ya thamani.

    7 Bwana hakuweka upendo wake juu yenu na kuwachagua kwa sababu mlikuwa wengi mno kuliko watu wengine, kwa maana ninyi ndio mliokuwa wachache sana kuliko mataifa yote. 8 Lakini ni kwa sababu Bwana aliwapenda ninyi na kutunza kiapo alichowaapia babu zenu kwamba atawatoa ninyi kwa mkono wenye nguvu na kuwakomboa kutoka nchi ya utumwa, kutoka nguvu za Farao mfalme wa Misri. 9 Basi ujue kwamba Bwana Mungu wako ndiye Mungu; ni Mungu mwaminifu, anayetunza Agano la upendo kwa maelfu ya vizazi vya wale wanaompenda na kuzishika amri zake. 10 Lakini

    kwa wale wanaomchukia

    atawalipiza kwenye nyuso zao

    kwa maangamizi;

    hatachelewa kuwalipiza kwenye nyuso zao

    wale wamchukiao.

  6. 24 “Hakuna mtu awezaye kuwatumikia mabwana wawili. Kwa kuwa atamchukia huyu na kumpenda yule mwingine, au atashikamana sana na huyu na kumdharau yule mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu pamoja na Mali.

  7. 12 Amri yangu ndiyo hii: Mpendane kama mimi nilivyowapenda ninyi. 13 Hakuna mtu mwenye upendo mkuu kuliko huu, mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. 14 Ninyi ni rafiki zangu mkifanya ninayowaamuru. 15 Siwaiti ninyi watumishi tena, kwa sababu watumishi hawajui bwana wao analofanya, bali nimewaita ninyi rafiki, kwa maana nimewajulisha mambo yote niliyoyasikia kutoka kwa Baba yangu. 16 Si ninyi mlionichagua, bali mimi ndiye niliyewachagua ninyi na kuwaweka mwende mkazae matunda, na matunda yenu yapate kudumu. Ili nalo lolote mtakalomwomba Baba katika Jina langu, awape ninyi. 17 Amri yangu ndiyo hii: Mpendane.

  8. 26 “Mtu yeyote anayekuja kwangu hawezi kuwa mwanafunzi wangu kama hatanipenda mimi zaidi ya baba yake na mama yake, mke wake na watoto wake, ndugu zake na dada zake, naam, hata maisha yake mwenyewe. 27 Yeyote asiyeuchukua msalaba wake na kunifuata hawezi kuwa mwanafunzi wangu.

    28 “Ni nani miongoni mwenu ambaye kama anataka kujenga nyumba, hakai kwanza chini na kufanya makisio ya gharama aone kama ana fedha za kutosha kukamilisha? 29 La sivyo, akiisha kuweka msingi, naye akiwa hana uwezo wa kuikamilisha, wote waionao wataanza kumdhihaki, 30 wakisema, ‘Mtu huyu alianza kujenga lakini hakuweza kukamilisha.’

    31 “Au ni mfalme gani atokaye kwenda kupigana vita na mfalme mwingine, ambaye hakai chini kwanza na kufikiri iwapo akiwa na jeshi la watu 10,000 ataweza kupigana na yule anayekuja na jeshi la watu 20,000? 32 Kama hawezi, basi wakati yule mwingine akiwa bado yuko mbali, yeye hutuma ujumbe wa watu na kuomba masharti ya amani. 33 Vivyo hivyo, yeyote miongoni mwenu ambaye hawezi kuacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.

  9. 1 Kila mtu na atii mamlaka inayotawala, kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu, nazo mamlaka zilizopo zimewekwa na Mungu. 2 Kwa hiyo yeye anayeasi dhidi ya mamlaka inayotawala anaasi dhidi ya kile kilichowekwa na Mungu, nao wale wafanyao hivyo watajiletea hukumu juu yao wenyewe. 3 Kwa kuwa watawala hawawatishi watu wale wanaotenda mema bali wale wanaotenda mabaya. Je, wataka usimwogope mwenye mamlaka? Basi tenda lile lililo jema naye atakusifu. 4 Kwa maana mwenye mamlaka ni mtumishi wa Mungu kwa ajili ya mema. Lakini kama ukitenda mabaya, basi ogopa, kwa kuwa hauinui upanga bila sababu. Yeye ni mtumishi wa Mungu, mjumbe wa Mungu wa kutekeleza adhabu juu ya watenda mabaya. 5 Kwa hiyo ni lazima kutii wenye mamlaka, si kwa sababu ya kuogopa adhabu iwezayo kutolewa, bali pia kwa ajili ya dhamiri.

  10. 14 “Sasa basi mcheni Bwana na kumtumikia kwa uaminifu wote. Itupeni mbali miungu ambayo baba zenu waliiabudu huko ngʼambo ya Mto Frati na huko Misri, nanyi mtumikieni Bwana. 15 Lakini msipoona vyema kumtumikia Bwana, chagueni hivi leo mtakayemtumikia, kama ni miungu ile ambayo baba zenu waliitumikia ngʼambo Frati, au miungu ya Waamori, ambao mnakaa katika nchi yao. Lakini mimi na nyumba yangu, tutamtumikia Bwana.”

  11. 22 Kwa maana nimezishika njia za Bwana;

    sijatenda ubaya nikamwacha Mungu wangu.

    23 Sheria zake zote zi mbele yangu,

    wala sijayaacha maagizo yake.

    24 Nimekuwa sina hatia mbele zake,

    nami nimejilinda nisitende dhambi.

  12. 33 Petro akajibu, “Hata kama wote watakuacha, kamwe mimi sitakuacha.”

    34 Yesu akamjibu, “Amin, nakuambia, usiku huu, kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.”

    35 Lakini Petro akasisitiza, “Hata kama itabidi kufa pamoja nawe, sitakukana kamwe.” Nao wanafunzi wale wengine wote wakasema vivyo hivyo.

  13. 1 Wakumbushe watu kuwanyenyekea watawala na kuwatii wenye mamlaka, wawe tayari kutenda kila lililo jema.

  14. 24 Mtu mwenye marafiki wengi wanaweza kumharibu,

    bali yuko rafiki aambatanaye na mtu kwa karibu kuliko ndugu.

  15. 9 “Kwangu mimi jambo hili ni kama siku za Noa,

    nilipoapa kuwa maji ya Noa kamwe hayatafunika tena dunia.

    Hivyo sasa nimeapa sitawakasirikia ninyi,

    kamwe sitawakemea tena.

    10 Ijapotikisika milima, na vilima viondolewe,

    hata hivyo upendo wangu usiokoma kwenu hautatikisika,

    wala agano langu la amani halitaondolewa,”

    asema Bwana, mwenye huruma juu yenu.

  16. 10 Kwa hiyo ninavumilia mambo yote kwa ajili ya wateule wa Mungu, kusudi wao nao wapate wokovu ulio katika Kristo Yesu, pamoja na utukufu wa milele.

    11 Hili ni neno la kuaminiwa:

    Kwa maana kama tumekufa pamoja naye,

    tutaishi pia pamoja naye.

    12 Kama tukistahimili,

    pia tutatawala pamoja naye.

    Kama tukimkana yeye,

    naye atatukana sisi.

    13 Kama tusipoamini,

    yeye hudumu kuwa mwaminifu,

    kwa maana hawezi kujikana mwenyewe.

  17. 1 Baada ya Daudi kumaliza kuongea na Sauli, roho ya Yonathani ikaambatana na roho ya Daudi, naye akampenda kama nafsi yake mwenyewe. 2 Kuanzia siku ile Sauli akamchukua Daudi naye hakumruhusu kurudi nyumbani kwa baba yake. 3 Yonathani akafanya agano na Daudi kwa sababu alimpenda kama nafsi yake mwenyewe. 4 Yonathani akavua joho alilokuwa amevaa na kumpa Daudi, pamoja na koti lake, silaha zake, hata pamoja na upanga wake, upinde wake na mshipi wake.

  18. 15 “Kama mnanipenda, mtazishika amri zangu.

  19. 35 Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je, ni shida au taabu au mateso au njaa au uchi au hatari au upanga? 36 Kama ilivyoandikwa:

    “Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa;

    tumehesabiwa kama kondoo wa kuchinjwa.”

    37 Lakini katika mambo haya yote tunashinda, naam na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. 38 Kwa maana nimekwisha kujua kwa hakika ya kuwa sio mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuja, wala wenye uwezo, 39 wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kingine chochote zitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu, Bwana wetu.

  20. 23 Hii ndiyo amri yake: kwamba tuliamini Jina la Mwanawe, Yesu Kristo, na kupendana sisi kwa sisi kama yeye alivyotuamuru. 24 Wale wote wanaozishika amri zake hukaa ndani yake na yeye ndani yao. Hivi ndivyo tunavyojua kwamba anakaa ndani yetu. Nasi twajua hili kwa njia ya Roho yule aliyetupa.

  21. 4 Usijitengenezee sanamu katika umbo la kitu chochote kilicho juu mbinguni, au duniani chini, au ndani ya maji. 5 Usivisujudie wala kuviabudu; kwa kuwa Mimi, Bwana Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu, ninayewaadhibu watoto kwa ajili ya dhambi za baba zao hadi kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao, 6 lakini ninaonyesha upendo kwa maelfu ya vizazi vya wale wanipendao na kuzishika amri zangu.

  22. 7 Lakini sivyo kwa mtumishi wangu Mose;

    yeye ni mwaminifu katika nyumba yangu yote.

  23. 23 Tushike kwa uthabiti lile tumaini la ukiri wetu bila kuyumbayumba, kwa maana yeye aliyeahidi ni mwaminifu.

  24. 10 Usiogope mateso yatakayokupata. Nakuambia ibilisi atawatia baadhi yenu gerezani ili kuwajaribu, nanyi mtapata dhiki kwa muda wa siku kumi. Uwe mwaminifu hata kufa, nami nitakupa taji ya uzima.

  25. 18 Katika siku ile nitafanya Agano kwa ajili yao

    na wanyama wa kondeni, na ndege wa angani,

    na viumbe vile vitambaavyo ardhini.

    Upinde, upanga na vita,

    nitaondolea mbali katika nchi,

    ili kwamba wote waweze kukaa salama.

    19 Nitakuposa uwe wangu milele;

    nitakuposa kwa uadilifu na haki,

    kwa upendo na huruma.

    20 Nitakuposa kwa uaminifu,

    nawe utamkubali Bwana.

  26. 8 Amekuonyesha yaliyo mema, ee mwanadamu.

    Bwana anataka nini kwako?

    Ila kutenda kwa haki na kupenda rehema,

    na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako.

  27. 13 Kwa ajili ya Bwana, tiini kila mamlaka iliyowekwa na wanadamu: Kwa mfalme kwani ndiye aliye na mamlaka ya juu zaidi, 14 au kwa maafisa aliowaweka, kwa kuwa mfalme amewatuma ili kuwaadhibu wale wanaokosa, na kuwapongeza wale watendao mema.

  28. 21 Yeye afuatiaye haki na upendo

    hupata uzima, mafanikio na heshima.

  29. 3 Tegeni sikio mje kwangu,

    nisikieni mimi, ili nafsi zenu zipate kuishi.

    Nitafanya agano la milele nanyi,

    pendo la uaminifu nililomwahidi Daudi.

  30. 33 “Hili ndilo agano nitakalofanya na nyumba ya Israeli

    baada ya siku zile,” asema Bwana.

    “Nitaweka sheria yangu katika nia zao,

    na kuiandika mioyoni mwao.

    Nitakuwa Mungu wao,

    nao watakuwa watu wangu.

    34 Mtu hatamfundisha tena jirani yake,

    wala mtu kumfundisha ndugu yake akisema, ‘Mjue Bwana Mungu,’

    kwa sababu wote watanijua mimi,

    tangu aliye mdogo kabisa kwao, hadi aliye mkuu sana,”

    asema Bwana.

    “Kwa sababu nitasamehe uovu wao,

    wala sitazikumbuka dhambi zao tena.”

  31. 29 Petro na wale mitume wengine wakajibu, “Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu.

  32. 10 Njia zote za Bwana ni za upendo na uaminifu

    kwa wale wanaoshika shuhuda za agano lake.

  33. 14 Bwana asema, “Kwa kuwa ananipenda, nitamwokoa;

    nitamlinda, kwa kuwa analikiri Jina langu.

    15 Ataniita, nami nitamjibu;

    nitakuwa pamoja naye katika taabu,

    nitamwokoa na kumheshimu.

    16 Kwa siku nyingi nitamshibisha

    na kumwonyesha wokovu wangu.”

  34. 6 Watu wengi hujidai kuwa na upendo usiokoma,

    bali mtu mwaminifu ni nani awezaye kumpata?

  35. 1 Sikieni neno la Bwana, enyi Waisraeli,

    kwa sababu Bwana analo shtaka

    dhidi yenu ninyi mnaoishi katika nchi:

    “Hakuna uaminifu, hakuna upendo,

    hakuna kumjua Mungu katika nchi.

    2 Kuna kulaani tu, uongo na uuaji,

    wizi na uzinzi,

    bila kuwa na mipaka,

    nao umwagaji damu mmoja

    baada ya mwingine.

    3 Kwa sababu hii nchi huomboleza,

    wote waishio ndani mwake wanadhoofika,

    wanyama wa kondeni, ndege wa angani

    na samaki wa baharini wanakufa.

  36. 42 Yesu akamjibu, “Ni yupi basi wakili mwaminifu na mwenye busara, ambaye bwana wake atamfanya msimamizi juu ya watumishi wake wote, ili awape watumishi wengine chakula chao wakati unaofaa? 43 Heri mtumishi yule ambaye bwana wake atakaporudi atamkuta akifanya hivyo. 44 Amin nawaambia, atamweka mtumishi huyo kuwa msimamizi wa mali yake yote. 45 Lakini kama yule mtumishi atasema moyoni mwake, ‘Bwana wangu anakawia kurudi,’ kisha akaanza kuwapiga wale watumishi wa kiume na wa kike, na kula na kunywa na kulewa. 46 Basi bwana wa mtumishi huyo atakuja siku asiyodhani na saa asiyoijua. Atamkata vipande vipande na kumweka katika sehemu moja pamoja na wale wasioamini.

    47 “Yule mtumishi anayefahamu vyema mapenzi ya bwana wake na asijiandae wala kufanya kama apendavyo bwana wake, atapigwa kwa mapigo mengi. 48 Lakini yeyote ambaye hakujua naye akafanya yale yastahiliyo kupigwa, atapigwa kidogo. Yeyote aliyepewa vitu vingi, atadaiwa vingi; na yeyote aliyekabidhiwa vingi, kwake vitatakiwa vingi.

  37. 31 Kisha Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, “Kama mkidumu katika maneno yangu, mtakuwa wanafunzi wangu kweli kweli.

  38. 15 Walipokwisha kula, Yesu akamuuliza Simoni Petro, “Je, Simoni mwana wa Yohana, unanipenda kweli kuliko hawa?”

    Yeye akamjibu, “Ndiyo Bwana, wewe unajua ya kuwa ninakupenda.”

    Yesu akamwambia, “Lisha wana-kondoo wangu.”

    16 Yesu akamwambia tena, “Simoni, mwana wa Yohana, wanipenda?”

    Petro akamjibu, “Ndiyo Bwana, wewe unajua ya kuwa ninakupenda.”

    Yesu akamwambia, “Chunga kondoo zangu.”

    17 Kwa mara ya tatu Yesu akamuuliza Petro, “Simoni mwana wa Yohana, unanipenda?”

    Petro akahuzunika sana kwa kuwa Yesu alimuuliza mara ya tatu, “Unanipenda?” Akamjibu, “Bwana, wewe unajua yote, unajua ya kuwa ninakupenda.”

    Yesu akamwambia, “Lisha kondoo wangu.

  39. 42 Nao wakawa wanadumu katika mafundisho ya mitume, katika ushirika, katika kumega mkate na katika kusali.

  40. 1 Basi, watu na watuhesabu sisi kuwa tu watumishi wa Kristo na mawakili wa siri za Mungu. 2 Tena, litakiwalo ni mawakili waonekane kuwa waaminifu.

  41. 3 Naam, nakusihi wewe pia, mwenzangu mwaminifu, uwasaidie hawa wanawake, kwa sababu walijitaabisha katika kazi ya Injili pamoja nami bega kwa bega, wakiwa pamoja na Klementi na watendakazi wenzangu ambao majina yao yameandikwa katika kitabu cha uzima.

  42. 1 Wakati baraka hizi zote pamoja na laana nilizoziweka mbele yako zitakapokujia, nawe ukazitafakari moyoni popote Bwana Mungu wako atakapokutawanya miongoni mwa mataifa, 2 hapo wewe na watoto wako mtakapomrudia Bwana Mungu wako, na kumtii kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote kulingana na kila kitu ninachokuamuru leo, 3 ndipo Bwana Mungu wako atakapokurudisha kutoka utumwani na kukuhurumia, naye atakukusanya tena kutoka mataifa yote kule alikutawanya.

  43. 10 Sikuficha haki yako moyoni mwangu;

    ninasema juu ya uaminifu wako na wokovu wako.

    Sikuficha upendo wako na kweli yako

    mbele ya kusanyiko kubwa.

    11 Ee Bwana, usizuilie huruma zako,

    upendo wako na kweli yako daima vinilinde.

  44. 28 Nitadumisha upendo wangu kwake milele,

    na agano langu naye litakuwa imara.

  45. 2 “Nenda ukahubiri masikioni mwa watu wa Yerusalemu:

    “ ‘Nakumbuka moyo wako wa uchaji katika ujana wako,

    jinsi ulivyonipenda kama bibi arusi

    na kunifuata katika jangwa lile lote,

    katika nchi isiyopandwa mbegu.

  46. 57 Walipokuwa njiani wakienda, mtu mmoja akamwambia Yesu, “Nitakufuata kokote uendako.”

    58 Yesu akamjibu, “Mbweha wana mapango, nao ndege wa angani wana viota, lakini Mwana wa Adamu hana mahali pa kulaza kichwa chake.”

    59 Yesu akamwambia mtu mwingine, “Nifuate.”

    Mtu huyo akamjibu, “Bwana, niruhusu kwanza nikamzike baba yangu.”

    60 Yesu akamwambia, “Waache wafu wawazike wafu wao, bali wewe nenda ukautangaze Ufalme wa Mungu.”

    61 Mtu mwingine akamwambia, “Bwana, nitakufuata lakini naomba kwanza nikawaage jamaa yangu.”

    62 Yesu akamwambia, “Mtu yeyote atiaye mkono wake kulima, kisha akatazama nyuma, hafai kwa Ufalme wa Mungu.”

  47. 5 Basi Mose kama mtumishi alikuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Mungu, akishuhudia kwa yale ambayo yangetamkwa baadaye. 6 Lakini Kristo ni mwaminifu kama Mwana katika nyumba ya Mungu. Sisi ndio nyumba yake, kama tutashikilia sana ujasiri wetu na tumaini tunalojivunia.