36 Bible Verses About Forgiving Yourself

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Forgiving Yourself
  1. 13 Ndugu zangu, sijihesabu kuwa nimekwisha kushika. Lakini ninafanya jambo moja: Ninasahau mambo yale yaliyopita, nakaza mwendo kufikia yale yaliyo mbele. 14 Nakaza mwendo nifikie ile alama ya ushindi iliyowekwa ili nipate tuzo ya mwito mkuu wa Mungu ambao nimeitiwa huko juu mbinguni katika Kristo Yesu.

  2. 10 Kwa maana huzuni ya kimungu huleta toba iletayo wokovu na wala haina majuto. Lakini huzuni ya kidunia husababisha mauti.

  3. 6 Kama tukisema kwamba twashirikiana naye huku tukienenda gizani, twasema uongo, wala hatutendi lililo kweli. 7 Lakini tukienenda nuruni, kama yeye alivyo nuruni, twashirikiana sisi kwa sisi na damu yake Yesu, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote.

    8 Kama tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe wala kweli haimo ndani yetu. 9 Kama tukiziungama dhambi zetu, yeye ni mwaminifu na wa haki, atatusamehe dhambi zetu na kutusafisha kutoka kwenye udhalimu wote. 10 Kama tukisema hatukutenda dhambi, twamfanya yeye kuwa mwongo na neno lake halimo ndani yetu.

  4. 12 Utusamehe deni zetu,

    kama sisi nasi tulivyokwisha

    kuwasamehe wadeni wetu.

    13 Usitutie majaribuni,

    bali utuokoe kutoka kwa yule mwovu

    [kwa kuwa Ufalme ni wako, na nguvu,

    na utukufu, hata milele. Amen].’

    14 Kwa kuwa kama mkiwasamehe watu wengine wanapowakosea, Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi pia. 15 Lakini msipowasamehe watu wengine makosa yao, naye Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.

  5. 31 Ondoeni kabisa uchungu, ghadhabu, hasira, makelele na masingizio pamoja na kila aina ya uovu. 32 Kuweni wafadhili na wenye kuhurumiana ninyi kwa ninyi, mkisameheana, kama vile naye Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.

  6. 12 Kwa hiyo, kwa kuwa ninyi mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao sana, jivikeni moyo wa huruma, utu wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu. 13 Vumilianeni na kusameheana mtu akiwa na lalamiko lolote dhidi ya mwenzake. Sameheaneni kama vile Bwana alivyowasamehe ninyi.

  7. Zaburi ya Daudi. Funzo.

    1 Heri mtu yule ambaye amesamehewa makosa yake,

    ambaye dhambi zake zimefunikwa.

    2 Heri mtu yule ambaye Bwana

    hamhesabii dhambi,

    na ambaye rohoni mwake

    hamna udanganyifu.

    3 Niliponyamaza, mifupa yangu ilichakaa

    kwa kulia kwa maumivu makali mchana kutwa.

    4 Usiku na mchana

    mkono wako ulinilemea,

    nguvu zangu zilinyonywa

    kama vile katika joto la kiangazi.

    5 Kisha nilikujulisha dhambi yangu

    wala sikuficha uovu wangu.

    Nilisema, “Nitaungama

    makosa yangu kwa Bwana.”

    Ndipo uliponisamehe

    hatia ya dhambi yangu.

  8. 4 Lakini Mungu kwa upendo wake mwingi kwetu sisi, ambaye ni mwingi wa rehema, 5 hata tulipokuwa wafu kwa ajili ya makosa yetu, alitufanya tuwe hai pamoja na Kristo Yesu, yaani, mmeokolewa kwa neema. 6 Mungu alitufufua pamoja na Kristo na kutuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho katika Kristo Yesu, 7 ili katika ule ulimwengu ujao apate kuonyesha wingi wa neema yake isiyopimika, iliyodhihirishwa kwetu kwa wema wake ndani ya Kristo Yesu. 8 Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani, wala si kwa matendo yenu mema. Hii ni zawadi kutoka kwa Mungu, 9 si kwa matendo, ili mtu yeyote asije akajisifu.

  9. 3 Kwa hiyo, jilindeni.

    “Kama ndugu yako akikukosea mwonye, naye akitubu, msamehe. 4 Kama akikukosea mara saba kwa siku moja na mara saba kwa siku moja akaja kwako akisema, ‘Ninatubu,’ msamehe.”

  10. 10 yeye hatutendei kulingana na dhambi zetu

    wala hatupatilizi kwa kadiri ya maovu yetu.

    11 Kama vile mbingu zilivyo juu ya dunia sana,

    ndivyo wema wake ulivyo mwingi kwa wanaomcha;

    12 kama mashariki ilivyo mbali na magharibi,

    ndivyo Mungu alivyoziweka dhambi zetu mbali nasi.

    13 Kama baba alivyo na huruma kwa watoto wake,

    ndivyo Bwana anavyowahurumia wale wanaomcha;

    14 kwa kuwa anajua tulivyoumbwa,

    anakumbuka kwamba sisi tu mavumbi.

  11. 34 Mtu hatamfundisha tena jirani yake,

    wala mtu kumfundisha ndugu yake akisema, ‘Mjue Bwana Mungu,’

    kwa sababu wote watanijua mimi,

    tangu aliye mdogo kabisa kwao, hadi aliye mkuu sana,”

    asema Bwana.

    “Kwa sababu nitasamehe uovu wao,

    wala sitazikumbuka dhambi zao tena.”

  12. 21 Lakini sasa, haki itokayo kwa Mungu imedhihirishwa pasipo sheria, ambayo Sheria na Manabii wanaishuhudia. 22 Haki hii itokayo kwa Mungu hupatikana kwa Yesu Kristo kwa wote wamwaminio. Kwa maana hapo hakuna tofauti, 23 kwa kuwa wote wametenda dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu, 24 wanahesabiwa haki bure kwa neema yake kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu. 25 Yeye ambaye Mungu alimtoa awe dhabihu ya upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake. Alifanya hivi ili kuonyesha haki yake, kwa sababu kwa ustahimili wake aliziachilia zile dhambi zilizotangulia kufanywa. 26 Alifanya hivyo ili kuonyesha haki yake wakati huu, ili yeye awe mwenye haki na mwenye kumhesabia haki yule anayemwamini Yesu.

    27 Basi, kujivuna kuko wapi? Kumewekwa mbali. Kwa sheria gani? Je, ni kwa ile ya matendo? La hasha, bali kwa ile sheria ya imani. 28 Kwa maana twaona kwamba mwanadamu huhesabiwa haki kwa njia ya imani wala si kwa matendo ya sheria. 29 Je, Mungu ni Mungu wa Wayahudi peke yao? Je, yeye si Mungu wa watu wa Mataifa pia? Naam, yeye ni Mungu wa watu wa Mataifa pia. 30 Basi kwa kuwa tuna Mungu mmoja tu, atawahesabia haki wale waliotahiriwa kwa imani na wale wasiotahiriwa kwa imani iyo hiyo. 31 Je, basi ni kwamba tunaibatilisha sheria kwa imani hii? La, hasha! Badala yake tunaithibitisha sheria.

  13. 13 Yeye afichaye dhambi zake hatafanikiwa,

    bali yeyote aziungamaye na kuziacha hupata rehema.

  14. 25 Nanyi kila msimamapo kusali, sameheni mkiwa na neno na mtu, ili naye Baba yenu aliye mbinguni awasamehe ninyi makosa yenu. [

  15. 19 Tubuni basi mkamgeukie Mungu, dhambi zenu zifutwe, ili zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwepo kwake Bwana, 20 naye apate kumtuma Kristo, ambaye ameteuliwa kwa ajili yenu, yaani Yesu. 21 Ilimpasa mbingu zimpokee mpaka wakati wa kufanywa upya kila kitu, kama Mungu alivyoahidi zamani kupitia kwa vinywa vya manabii wake watakatifu.

  16. 1 Kwa hiyo, sasa hakuna hukumu ya adhabu kwa wale walio ndani ya Kristo Yesu, wale ambao hawaenendi kwa kuufuata mwili bali kwa kufuata Roho. 2 Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima katika Kristo Yesu imeniweka huru mbali na sheria ya dhambi na mauti.

  17. 7 Mtu mwovu na aiache njia yake,

    na mtu mbaya na ayaache mawazo yake.

    Yeye na amrudie Bwana, naye atamrehemu,

    arudi kwa Mungu wetu, kwa kuwa atamsamehe bure kabisa.

  18. 18 Ni nani Mungu kama wewe,

    ambaye anaachilia dhambi

    na kusamehe makosa

    ya mabaki ya urithi wake?

    Wewe huwi na hasira milele,

    bali unafurahia kuonyesha rehema.

    19 Utatuhurumia tena,

    utazikanyaga dhambi zetu

    chini ya nyayo zako,

    na kutupa maovu yetu yote

    katika vilindi vya bahari.

  19. 4 Yohana alikuja, akibatiza huko nyikani, akihubiri ubatizo wa toba kwa ajili ya msamaha wa dhambi. 5 Watu kutoka Uyahudi wote na sehemu zote za Yerusalemu walikuwa wakimwendea. Nao wakaziungama dhambi zao, akawabatiza katika Mto Yordani.

  20. 8 Hatimaye, ndugu zangu, mambo yote yaliyo ya kweli, yoyote yaliyo na sifa njema, yoyote yaliyo ya haki, yoyote yaliyo safi, yoyote ya kupendeza, yoyote yenye staha, ukiwepo uzuri wowote, pakiwepo chochote kinachostahili kusifiwa, tafakarini mambo hayo.

  21. 10 “Mwanadamu, sema na nyumba ya Israeli uwaambie, ‘Hili ndilo mnalosema: “Makosa yetu na dhambi zetu zimetulemea, nasi tunadhoofika kwa sababu ya hayo. Tutawezaje basi kuishi?” ’ 11 Waambie, ‘Hakika kama mimi niishivyo, asema Bwana Mwenyezi, sifurahii kifo cha watu waovu, bali kwamba wageuke kutoka njia zao mbaya wapate kuishi. Geukeni! Geukeni kutoka njia zenu mbaya! Kwa nini mkafe, ee nyumba ya Israeli?’

    12 “Kwa hiyo, mwanadamu, waambie watu wako, ‘Haki ya mtu mwenye haki haitamwokoa wakati anapoacha kutii, wala uovu wa mtu mwovu hautamsababisha yeye kuanguka anapotubu na kuacha uovu. Mtu mwenye haki, kama akitenda dhambi, hataishi kwa sababu ya uadilifu wake wa awali.’ 13 Kama nikimwambia mtu mwenye haki kwamba hakika utaishi, lakini akategemea hiyo haki yake na kutenda uovu, hakuna tendo lolote la haki alilotenda litakalokumbukwa, atakufa kwa ajili ya uovu alioutenda. 14 Nami kama nikimwambia mtu mwovu, ‘Hakika utakufa,’ kisha akageuka kutoka dhambi yake na kufanya lile lililo haki na sawa, 15 kama akirudisha kile alichochukua rehani kwa ajili ya deni, akarudisha alichoiba na kufuata amri zile ziletazo uzima, wala hafanyi uovu, hakika ataishi, hatakufa. 16 Hakuna dhambi yoyote aliyoitenda itakayokumbukwa juu yake. Ametenda lile lililo haki na sawa, hakika ataishi.

  22. 4 Utusamehe dhambi zetu,

    kwa kuwa na sisi huwasamehe wote wanaotukosea.

    Wala usitutie majaribuni

    (bali utuokoe kutoka kwa yule mwovu).’ ”

  23. 1 Kwa hiyo, kwa kuwa tumekwisha kuhesabiwa haki kwa imani, tuna amani na Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, 2 ambaye kwa kupitia kwake tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo ndani yake sasa tunasimama, nasi twafurahia katika tumaini letu la kushiriki utukufu wa Mungu. 3 Si hivyo tu, bali twafurahi pia katika mateso, kwa sababu tunajua kuwa mateso huleta saburi, 4 nayo saburi huleta uthabiti wa moyo, na uthabiti wa moyo huleta tumaini, 5 wala tumaini halitukatishi tamaa, kwa sababu Mungu amekwisha kumimina pendo lake mioyoni mwetu kwa njia ya Roho Mtakatifu ambaye ametupatia.

    6 Kwa maana hata tulipokuwa dhaifu, wakati ulipowadia, Kristo alikufa kwa ajili yetu sisi wenye dhambi. 7 Hakika, ni vigumu mtu yeyote kufa kwa ajili ya mwenye haki, ingawa inawezekana mtu akathubutu kufa kwa ajili ya mtu mwema. 8 Lakini Mungu anaudhihirisha upendo wake kwetu kwamba: Tulipokuwa tungali wenye dhambi, Kristo alikufa kwa ajili yetu.

    9 Basi, kwa kuwa sasa tumehesabiwa haki kwa damu yake, si zaidi sana tutaokolewa kutoka ghadhabu ya Mungu kupitia kwake! 10 Kwa kuwa kama tulipokuwa adui wa Mungu tulipatanishwa naye kwa njia ya kifo cha Mwanawe, si zaidi sana tukiisha kupatanishwa, tutaokolewa kwa uzima wake. 11 Lakini zaidi ya hayo, pia tunafurahi katika Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kupitia kwake tumepata upatanisho.

  24. 17 Kwa hiyo kama mtu akiwa ndani ya Kristo, amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita, tazama, yamekuwa mapya. 18 Haya yote yanatokana na Mungu, ambaye ametupatanisha sisi na nafsi yake kwa njia ya Yesu Kristo na kutupata sisi huduma ya upatanisho:

  25. 3 Ahimidiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki sisi kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho ndani ya Kristo. 4 Kwa maana alituchagua katika yeye kabla ya kuumbwa ulimwengu ili tuwe watakatifu na bila lawama mbele zake. Kwa upendo 5 alitangulia kutuchagua tuwe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo kwa furaha yake na mapenzi yake mwenyewe. 6 Kwa hiyo tunamsifu Mungu kwa huruma zake kuu alizotumiminia sisi katika Mwanawe Mpendwa.

  26. 47 Kwa hiyo, nakuambia, dhambi zake zilizokuwa nyingi zimesamehewa, kwani ameonyesha upendo mwingi. Lakini yule aliyesamehewa kidogo, hupenda kidogo.”

    48 Kisha akamwambia yule mwanamke, “Dhambi zako zimesamehewa.”

    49 Lakini wale waliokuwa wameketi pamoja naye chakulani wakaanza kusemezana wao kwa wao, “Huyu ni nani ambaye hata anasamehe dhambi?”

  27. 16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.

  28. 7 Ndani yake tunao ukombozi kwa njia ya damu yake, yaani, msamaha wa dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake

  29. 6 Basi, nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake. 7 Mtwikeni yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana na mambo yenu.

  30. 11 Hekima ya mtu humpa uvumilivu,

    ni kwa utukufu wake kusamehe makosa.

  31. 20 Nasi pia twajua ya kwamba Mwana wa Mungu amekuja, naye ametupa sisi ufahamu ili tupate kumjua yeye aliye Kweli. Nasi tumo ndani yake yeye aliye Kweli, yaani, ndani ya Yesu Kristo Mwanawe. Yeye ndiye Mungu wa kweli na uzima wa milele.

  32. 40 “ ‘Lakini kama watatubu dhambi zao na dhambi za baba zao, udanganyifu wao dhidi yangu na uadui wao kwangu, 41 ambao ulinifanya niwe na uadui nao hata nikawapeleka katika nchi ya adui zao, wakati mioyo yao isiyotahiriwa itanyenyekea na kutubu dhambi yao, 42 nami nitakumbuka agano langu na Yakobo, na agano langu na Isaki, na agano langu na Abrahamu, nami nitaikumbuka nchi.

  33. 16 “Lakini wao, baba zetu, wakawa na kiburi na shingo ngumu, nao hawakutii maagizo yako. 17 Wakakataa kusikiliza na kushindwa kukumbuka miujiza uliyoifanya miongoni mwao. Wakawa na shingo ngumu, na katika uasi wao wakamchagua kiongozi ili warudi kwenye utumwa wao. Lakini wewe ni Mungu mwenye kusamehe, mwenye neema na mwingi wa huruma, si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa upendo. Kwa hiyo hukuwaacha,

  34. 22 Kwa sababu ya upendo mkuu wa Bwana, hatuangamii,

    kwa kuwa huruma zake hazikomi kamwe.

    23 Ni mpya kila asubuhi,

    uaminifu wako ni mkuu.

    24 Nimeiambia nafsi yangu, “Bwana ni fungu langu,

    kwa hiyo nitamngojea.”

  35. 9 Bwana Mungu wetu ni mwenye rehema na anayesamehe, hata ingawa tumefanya uasi dhidi yake.

  36. 38 “Kwa hiyo ndugu zangu, nataka ninyi mjue kwamba kwa kupitia huyu Yesu msamaha wa dhambi unatangazwa kwenu. 39 Kwa kupitia yeye, kila mtu amwaminiye anahesabiwa haki kwa kila kitu ambacho asingeweza kuhesabiwa haki kwa sheria ya Mose.