44 Bible Verses About Circumcision

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Circumcision
  1. 5 Jina lako hutaitwa tena Abramu, bali jina lako litakuwa Abrahamu, kwa maana nimekufanya wewe baba wa mataifa mengi. 6 Nitakufanya uwe na uzao mwingi sana, kwako yatatoka mataifa nao wafalme watatoka kwako. 7 Nitalithibitisha Agano langu kama Agano la milele kati yangu na wewe na wazao wako baada yako na vizazi vijavyo niwe Mungu wako na Mungu wa wazao wako. 8 Nchi yote ya Kanaani, unakoishi sasa kama mgeni, nitakupa kuwa milki yako milele, na uzao wako, nami nitakuwa Mungu wao.”

    9 Ndipo Mungu akamwambia Abrahamu, “Kwa upande wako, lazima ushike Agano langu, wewe na wazao wako kwa ajili ya vizazi vijavyo. 10 Hili ni Agano langu na wewe pamoja na wazao wako baada yako, Agano mtakalolishika: Kila mwanaume miongoni mwenu atatahiriwa. 11 Mtafanyiwa tohara na hii itakuwa ni alama ya Agano kati yangu na ninyi. 12 Kwa vizazi vijavyo, kila mwanaume miongoni mwenu mwenye siku nane ni lazima atahiriwe, pamoja na watakaozaliwa nyumbani mwako au walionunuliwa kwa fedha kutoka kwa mgeni, wale ambao sio watoto wako. 13 Awe amezaliwa nyumbani mwako au amenunuliwa kwa fedha yako, ni lazima watahiriwe. Agano langu katika mwili wako litakuwa ni Agano la milele. 14 Kila mwanaume asiyetahiriwa, ambaye hajapata tohara ya mwilini, atatengwa na watu wake, amelivunja Agano langu.”

    15 Pia Bwana akamwambia Abrahamu, “Kwa upande wa Sarai mkeo, hutamwita tena Sarai bali jina lake litakuwa Sara. 16 Nitambariki na hakika nitakupatia mwana kwake. Nitambariki na kwamba atakuwa mama wa mataifa, wafalme wa mataifa watatoka kwake.”

  2. 25 Kutahiriwa kuna thamani ikiwa unatii sheria, lakini kama unavunja sheria, kutahiriwa kwako kumekuwa kutokutahiriwa. 26 Hivyo, ikiwa wale wasiotahiriwa wanatimiza mambo ambayo sheria inataka, je, kutokutahiriwa kwao hakutahesabiwa kuwa sawa na kutahiriwa? 27 Ndipo wale ambao hawakutahiriwa kimwili lakini wanaitii sheria watawahukumu ninyi, ambao ingawa mmetahiriwa na kuijua sana sheria ya Mungu iliyoandikwa, lakini mwaivunja.

    28 Kwa maana mtu si Myahudi kwa vile alivyo kwa nje, wala tohara ya kweli si kitu cha nje au cha kimwili. 29 Lakini mtu ni Myahudi alivyo ndani, nayo tohara ya kweli ni jambo la moyoni, ni la Roho, wala si la sheria iliyoandikwa. Mtu wa namna hiyo hapokei sifa kutoka kwa wanadamu bali kwa Mungu.

  3. 8 Angalieni mtu yeyote asiwafanye ninyi mateka kwa elimu batili na madanganyo matupu yanayotegemea mapokeo ya wanadamu na mafundisho ya ulimwengu badala ya Kristo.

    9 Maana ukamilifu wote wa Uungu umo ndani ya Kristo katika umbile la mwili wa kibinadamu, 10 nanyi mmepewa ukamilifu ndani ya Kristo, ambaye ndiye mkuu juu ya kila enzi na kila mamlaka. 11 Katika Kristo pia mlitahiriwa kwa kutengwa mbali na asili ya dhambi, si kwa tohara inayofanywa kwa mikono ya wanadamu, bali kwa ile tohara iliyofanywa na Kristo, 12 mkiwa mmezikwa pamoja naye katika ubatizo, na kufufuliwa pamoja naye kwa njia ya imani yenu katika uweza wa Mungu, aliyemfufua kutoka kwa wafu.

    13 Mlipokuwa wafu katika dhambi zenu na kutokutahiriwa katika asili yenu ya dhambi, Mungu aliwafanya mwe hai pamoja na Kristo. Alitusamehe dhambi zetu zote, 14 akiisha kuifuta ile hati yenye mashtaka yaliyokuwa yanatukabili, pamoja na maagizo yake. Aliiondoa isiwepo tena, akiigongomea kwenye msalaba wake.

  4. 9 Je, huku kubarikiwa ni kwa wale waliotahiriwa peke yao, au pia na kwa wale wasiotahiriwa? Tunasema, “Imani ya Abrahamu ilihesabiwa kwake kuwa haki.” 10 Je, ni lini basi ilipohesabiwa kwake kuwa haki? Je, ilikuwa kabla au baada ya kutahiriwa kwake? Haikuwa baada, ila kabla hajatahiriwa. 11 Alipewa ishara ya tohara kuwa muhuri wa haki aliyokuwa nayo kwa imani hata alipokuwa bado hajatahiriwa. Kusudi lilikuwa kumfanya baba wa wote wale waaminio pasipo kutahiriwa na ambao wamehesabiwa haki. 12 Vivyo hivyo awe baba wa wale waliotahiriwa ambao si kwamba wametahiriwa tu, bali pia wanafuata mfano wa imani ambayo Baba yetu Abrahamu alikuwa nayo kabla ya kutahiriwa.

    13 Kwa maana ile ahadi kwamba angeurithi ulimwengu haikuja kwa Abrahamu au kwa wazao wake kwa njia ya sheria bali kwa njia ya haki ipatikanayo kwa imani.

  5. 1 Kristo alitupa uhuru, akataka tubaki huru. Hivyo simameni imara wala msikubali tena kulemewa na kongwa la utumwa.

    2 Sikilizeni! Mimi, Paulo, nawaambieni kwamba kama mkikubali kutahiriwa, basi Kristo hatawafaidia chochote. 3 Namshuhudia tena kila mtu anayekubali kutahiriwa kwamba inampasa kushika sheria yote. 4 Ninyi mnaotafuta kuhesabiwa haki kwa njia ya sheria mmetengwa na Kristo, mko mbali na neema ya Mungu. 5 Kwa maana, kwa njia ya Roho kwa imani, tunangojea kwa shauku tumaini la haki. 6 Kwa maana ndani ya Kristo Yesu, kutahiriwa au kutokutahiriwa hakuleti tofauti, bali lililo muhimu ni imani itendayo kazi kwa njia ya upendo.

    7 Mlikuwa mkipiga mbio vizuri. Ni nani aliyewazuia msiitii kweli? 8 Ushawishi wa namna hiyo haukutokana na yule anayewaita. 9 “Chachu kidogo huchachua donge zima.” 10 Nina hakika katika Bwana kwamba hamtakuwa na msimamo mwingine. Mtu anayewachanganya anastahili adhabu, hata awe nani. 11 Lakini ndugu zangu, kama mimi bado ninahubiri kuhusu kutahiriwa, kwa nini bado ninateswa? Katika hiyo hali basi, kwazo la msalaba limeondolewa. 12 Laiti hao wanaowavuruga wangejihasi wao wenyewe!

  6. 12 Wale wanaotaka kuonekana wazuri kwa mambo ya mwili wanataka wawalazimishe kutahiriwa. Sababu pekee ya kufanya hivyo ni kuepuka kuteswa kwa ajili ya msalaba wa Kristo. 13 Hata wale waliotahiriwa wenyewe hawaitii sheria, lakini wanataka ninyi mtahiriwe ili wapate kujivuna kwa habari ya miili yenu. 14 Mungu apishie mbali nisije nikajivunia kitu chochote isipokuwa msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa yeye ulimwengu umesulubiwa kwangu, nami nimesulubiwa kwa ulimwengu. 15 Kwa maana katika Kristo Yesu, kutahiriwa au kutokutahiriwa si kitu, bali kule kuwa kiumbe kipya ni kila kitu! 16 Amani na rehema viwe na wote wanaofuata kanuni hii, na juu ya Israeli wa Mungu.

  7. 1 Hatimaye, ndugu zangu, furahini katika Bwana! Mimi kuwaandikia mambo yale yale hakuniudhi, kwa maana ni kinga kwa ajili yenu.

    2 Jihadharini na mbwa, wale watenda maovu, jihadharini na wale wajikatao miili yao, wasemao ili kuokoka ni lazima kutahiriwa. 3 Kwa maana sisi ndio tulio tohara, sisi tumwabuduo Mungu katika Roho, tunaona fahari katika Kristo Yesu, ambao hatuweki tumaini letu katika mwili, 4 ingawa mimi mwenyewe ninazo sababu za kuutumainia mwili.

    Kama mtu yeyote akidhani anazo sababu za kuutumainia mwili, mimi zaidi. 5 Nilitahiriwa siku ya nane, mimi ni Mwisraeli wa kabila la Benyamini, Mwebrania wa Waebrania. Kwa habari ya sheria, ni Farisayo, 6 kwa habari ya juhudi, nilikuwa nalitesa kanisa, kuhusu haki ipatikanayo kwa sheria, mimi nilikuwa sina hatia.

    7 Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, sasa nayahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo.

  8. 12 Na sasa, ee Israeli, Bwana Mungu wako anataka nini kwako ila kumcha Bwana Mungu wako, kwenda katika njia zake, kumpenda na kumtumikia Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote, 13 na kuyashika maagizo ya Bwana na amri zake ninazokupa leo kwa mafanikio yako mwenyewe?

    14 Mbingu, hata mbingu za juu sana, dunia na kila kitu kilichomo ndani yake, ni mali ya Bwana Mungu wako. 15 Hata hivyo Bwana alikuwa na shauku na baba zako, akawapenda na akawachagua ninyi, wazao wao, kuliko mataifa yote, kama ilivyo leo. 16 Kwa hiyo tahirini mioyo yenu, na msiwe na shingo ngumu tena. 17 Kwa kuwa Bwana Mungu wenu ni Mungu wa miungu na Bwana wa mabwana, Mungu mkuu, mwenye uweza na wa kutisha, ambaye hana upendeleo na hapokei rushwa.

  9. 1 Wakati baraka hizi zote pamoja na laana nilizoziweka mbele yako zitakapokujia, nawe ukazitafakari moyoni popote Bwana Mungu wako atakapokutawanya miongoni mwa mataifa, 2 hapo wewe na watoto wako mtakapomrudia Bwana Mungu wako, na kumtii kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote kulingana na kila kitu ninachokuamuru leo, 3 ndipo Bwana Mungu wako atakapokurudisha kutoka utumwani na kukuhurumia, naye atakukusanya tena kutoka mataifa yote kule alikutawanya. 4 Hata kama umefukuziwa katika nchi ya mbali kiasi gani chini ya mbingu, kutoka huko Bwana Mungu wako atakukusanya na kukurudisha. 5 Yeye Bwana atakurudisha katika nchi iliyokuwa mali ya baba zako, nawe utaimiliki. Naye atakufanya ufanikiwe sana na kukuzidisha kwa idadi kuliko baba zako. 6 Bwana Mungu wako ataitahiri mioyo yenu na mioyo ya wazao wenu ili mweze kumpenda kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote ukaishi. 7 Bwana Mungu wako ataweka laana hizi zote juu ya adui zako ambao wanakuchukia na kukutesa. 8 Utamtii tena Bwana na kuzishika amri zake zote ninazokupa leo.

  10. 17 Lakini kila mtu na aishi maisha aliyopangiwa na Bwana, yale Mungu aliyomwitia. Hii ni sheria ninayoiweka kwa makanisa yote. 18 Je, mtu alikuwa tayari ametahiriwa alipoitwa? Asijifanye asiyetahiriwa. Je, mtu alikuwa hajatahiriwa alipoitwa? Asitahiriwe. 19 Kutahiriwa si kitu, na kutokutahiriwa si kitu. Lakini kuzitii amri za Mungu ndilo jambo muhimu. 20 Basi kila mmoja wenu na abaki katika hali aliyoitwa nayo.

  11. 25 “Siku zinakuja, nitakapowaadhibu wale wote ambao wametahiriwa kimwili tu, asema Bwana, 26 yaani Misri, Yuda, Edomu, Amoni, Moabu na wote wanaoishi jangwani sehemu za mbali. Kwa maana mataifa haya yote hayakutahiriwa mioyo yao, nayo nyumba yote ya Israeli haikutahiriwa.”

  12. 2 “Waambie Waisraeli: ‘Mwanamke ambaye atapata mimba na kuzaa mtoto wa kiume atakuwa najisi kwa kawaida ya ibada kwa siku saba, kama anavyokuwa najisi wakati wa siku zake za hedhi. 3 Mvulana atatahiriwa siku ya nane.

  13. 21 Hata zilipotimia siku nane, ulikuwa ndio wakati wa kumtahiri mtoto, akaitwa Yesu, jina alilokuwa amepewa na malaika kabla hajatungwa mimba.

    22 Ulipotimia wakati wa utakaso wake Maria kwa mujibu wa Sheria ya Mose, basi Yosefu na Maria walimpeleka mtoto Yerusalemu, ili kumweka wakfu kwa Bwana 23 (kama ilivyoandikwa katika Sheria ya Bwana, kwamba, “Kila mtoto wa kiume kifungua mimba atawekwa wakfu kwa Bwana”), 24 na pia kutoa dhabihu kulingana na yale yaliyonenwa katika Sheria ya Bwana: “Hua wawili au makinda mawili ya njiwa.”

  14. 1 Baadhi ya watu wakashuka Antiokia kutoka Uyahudi, nao wakawa wanawafundisha wandugu: “Msipotahiriwa kufuatana na desturi aliyofundisha Mose, hamwezi kuokoka.” 2 Baada ya Paulo na Barnaba kutokubaliana nao kukawa na mabishano makali, Paulo na Barnaba na baadhi ya wengine miongoni mwao wakachaguliwa kwenda Yerusalemu ili kujadiliana jambo hili na mitume na wazee. 3 Hivyo wakasafirishwa na kanisa, wakiwa njiani wakapitia nchi ya Foinike na Samaria, wakawaeleza jinsi watu wa Mataifa walivyookoka. Habari hizi zikaleta furaha kubwa kwa ndugu wote. 4 Walipofika Yerusalemu, walipokelewa na kanisa na mitume pamoja na wazee, ndipo Paulo na Barnaba wakawaarifu kila kitu Mungu alichokuwa amefanya kupitia kwao.

    5 Ndipo baadhi ya walioamini wa madhehebu ya Mafarisayo wakasimama na kusema, “Hao watu wa Mataifa lazima watahiriwe na waagizwe kutii sheria ya Mose.”

    6 Mitume na wazee wakakutana pamoja ili kufikiri jambo hili. 7 Baada ya majadiliano mengi, Petro akasimama na kusema, “Ndugu zangu, mnajua kwamba siku za kwanza Mungu alinichagua ili kwa midomo yangu watu wa Mataifa wapate kusikia ujumbe wa Injili na kuamini. 8 Mungu, yeye ajuaye mioyo, alionyesha kwamba anawakubali kwa kuwapa Roho Mtakatifu kama vile alivyotupa sisi. 9 Mungu hakutofautisha kati yetu na wao, bali alitakasa mioyo yao kwa imani. 10 Sasa basi, mbona mnataka kumjaribu Mungu kwa kuweka kongwa shingoni mwa wanafunzi ambalo baba zetu wala sisi hatukuweza kulibeba? 11 Lakini sisi tunaamini ya kuwa tunaokolewa kwa neema ya Bwana Yesu Kristo, kama wao wanavyookolewa.”

    12 Kusanyiko lote likakaa kimya, wakawasikiliza Paulo na Barnaba wakieleza jinsi Mungu alivyowatumia kutenda ishara na maajabu kwa watu wa Mataifa. 13 Walipomaliza kunena, Yakobo akasema, “Ndugu zangu, nisikilizeni. 14 Simoni amekwisha kutueleza jinsi Mungu, kwa mara ya kwanza alivyoonyesha kuhusika kwa kujichagulia watu kutoka watu wa Mataifa kwa ajili ya Jina lake. 15 Maneno ya manabii yanakubaliana na jambo hili, kama ilivyoandikwa:

    16 “ ‘Baada ya mambo haya nitarudi,

    nami nitajenga upya

    nyumba ya Daudi iliyoanguka.

    Nitajenga tena magofu yake

    na kuisimamisha,

    17 ili wanadamu wengine wote

    wapate kumtafuta Bwana,

    hata wale watu wa Mataifa wote

    ambao wanaitwa kwa Jina langu,

    asema Bwana, afanyaye mambo haya’

    18 ambayo yamejulikana tangu zamani.

    19 “Kwa hivyo uamuzi wangu ni kwamba, tusiwataabishe watu wa Mataifa wanaomgeukia Mungu. 20 Badala yake, tuwaandikie kwamba wajiepushe na vyakula vilivyonajisiwa kwa kutolewa sanamu, wajiepushe na uasherati, au kula mnyama aliyenyongwa, na damu. 21 Kwa maana katika kila mji kwa vizazi vilivyopita, Mose amekuwa na wale wanaotangaza sheria yake kwa kuwa imekuwa ikisomwa kwa sauti kubwa katika masinagogi kila Sabato.”

  15. 24 Mose alipokuwa mahali pa kulala wageni akiwa njiani kurudi Misri, Bwana akakutana naye, akataka kumuua. 25 Lakini Sipora akachukua jiwe gumu, akakata govi la mwanawe na kugusa nalo miguu ya Mose. Sipora akasema, “Hakika wewe ni bwana arusi wa damu kwangu.” 26 Sipora alipomwita Mose, “Bwana arusi wa damu,” alikuwa anamaanisha ile tohara. Baada ya hayo Bwana akamwacha.

  16. 1 “Ikiwa utataka kurudi, ee Israeli,

    nirudie mimi,”

    asema Bwana.

    “Ikiwa utaondoa sanamu zako za kuchukiza mbele ya macho yangu

    na usiendelee kutangatanga,

    2 ikiwa kwa kweli, kwa haki na kwa unyofu utaapa,

    ‘Kwa hakika kama vile Bwana aishivyo,’

    ndipo mataifa yatakapobarikiwa naye

    na katika yeye watajitukuza.”

    3 Hili ndilo asemalo Bwana kwa watu wa Yuda na kwa Yerusalemu:

    “Vunjeni mabonge kwenye mashamba yenu,

    wala msipande katikati ya miiba.

    4 Jitahirini katika Bwana,

    tahirini mioyo yenu,

    enyi wanaume wa Yuda

    na watu wa Yerusalemu,

    la sivyo ghadhabu yangu itatoka kwa nguvu

    na kuwaka kama moto

    kwa sababu ya uovu mliotenda,

    ikiwaka pasipo wa kuizima.

  17. 11 Kwa hiyo kumbukeni kwamba ninyi ambao hapo awali mlikuwa watu wa Mataifa kwa kuzaliwa na kuitwa “wasiotahiriwa” na wale wanaojiita “waliotahiriwa” (yaani tohara ifanyikayo katika mwili kwa mikono ya wanadamu), 12 kumbukeni kwamba wakati ule mlikuwa mbali na Kristo, mkiwa mmetengwa kutoka jumuiya ya Israeli, na mkiwa wageni katika yale maagano ya ahadi, nanyi mkiwa hamna tumaini wala Mungu duniani. 13 Lakini sasa katika Kristo Yesu, ninyi ambao hapo kwanza mlikuwa mbali na Mungu, sasa mmeletwa karibu kwa njia ya damu ya Kristo.

    14 Kwa maana yeye mwenyewe ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi tuliokuwa wawili, yaani, Wayahudi na watu wa Mataifa, tuwe wamoja kwa kuvunja kizuizi na kubomoa ule ukuta wa uadui uliokuwa kati yetu, 15 kwa kuibatilisha ile sheria pamoja na amri zake na maagizo yake alipoutoa mwili wake, ili apate kufanya ndani yake mtu mmoja mpya badala ya hao wawili, hivyo akifanya amani, 16 naye katika mwili huu mmoja awapatanishe wote wawili na Mungu kupitia msalaba, ili kwa huo msalaba akaangamiza uadui wao. 17 Alikuja na kuhubiri amani kwenu ninyi mliokuwa mbali na pia akahubiri amani kwao waliokuwa karibu. 18 Kwa maana kwa kupitia kwake, sisi sote tunaweza kumkaribia Baba katika Roho mmoja.

    19 Hivyo basi, ninyi sasa si wageni tena wala wapitaji, bali mmekuwa wenyeji pamoja na watakatifu na pia jamaa wa nyumbani mwake Mungu. 20 Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ndiye jiwe kuu la pembeni. 21 Ndani yake jengo lote limeshikamanishwa pamoja na kusimamishwa ili kuwa Hekalu takatifu katika Bwana. 22 Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja ili mpate kuwa makao ambayo Mungu anaishi ndani yake kwa njia ya Roho wake.

  18. 1 Kisha, baada ya miaka kumi na minne, nilipanda tena kwenda Yerusalemu pamoja na Barnaba, nikamchukua na Tito ili awe pamoja nami. 2 Nilikwenda kwa sababu nilikuwa nimefunuliwa na Mungu, ili nikawaeleze kwa faragha wale walioonekana kuwa viongozi, ile Injili ninayoihubiri kwa watu wa Mataifa. Nilifanya hivyo kwa kuhofia kwamba nisije nikawa nilikuwa ninakimbia au nilikimbia bure. 3 Lakini hata Tito ambaye alikuwa Myunani, hakulazimika kutahiriwa. 4 Lakini kwa sababu ya ndugu wa uongo ambao walijiingiza kwa siri katikati yetu ili kupeleleza uhuru wetu tulio nao katika Kristo Yesu, wapate kututia utumwani, 5 hatukukubaliana nao hata dakika moja, ili kwamba ukweli wa Injili ubaki nanyi.

  19. 9 Msiambiane uongo, kwa maana mmevua kabisa utu wenu wa kale pamoja na matendo yake, 10 nanyi mmevaa utu mpya, unaofanywa upya katika ufahamu sawasawa na mfano wa Muumba wake. 11 Hapa hakuna Myunani wala Myahudi, aliyetahiriwa wala asiyetahiriwa, asiyestaarabika wala aliyestaarabika, mtumwa wala mtu huru, bali Kristo ni yote, na ndani ya wote.

  20. 10 Niseme na nani na kumpa onyo?

    Ni nani atakayenisikiliza mimi?

    Masikio yao yameziba,

    kwa hiyo hawawezi kusikia.

    Neno la Bwana ni chukizo kwao,

    hawalifurahii.

    11 Lakini nimejaa ghadhabu ya Bwana,

    nami siwezi kuizuia.

    “Wamwagie watoto walioko barabarani,

    na juu ya vijana waume waliokusanyika;

    mume na mke watakumbwa pamoja ndani yake,

    hata nao wazee waliolemewa na miaka.

  21. 14 Ilipokaribia katikati ya Sikukuu, Yesu alipanda kwenda Hekaluni na kuanza kufundisha. 15 Wayahudi wakastaajabia mafundisho yake wakasema, “Mtu huyu amepataje kujua mambo haya bila kufundishwa?”

    16 Ndipo Yesu akawajibu, “Mafundisho yangu si yangu mwenyewe, bali yanatoka kwake yeye aliyenituma. 17 Mtu yeyote akipenda kufanya mapenzi ya Mungu, atajua kama mafundisho yangu yanatoka kwa Mungu au ninasema kwa ajili yangu mwenyewe. 18 Wale wanenao kwa ajili yao wenyewe hufanya hivyo kwa kutaka utukufu wao wenyewe. Lakini yeye atafutaye utukufu wa yule aliyemtuma ni wa kweli, wala hakuna uongo ndani yake. 19 Je, Mose hakuwapa ninyi sheria? Lakini hakuna hata mmoja wenu anayeishika hiyo sheria. Kwa nini mnataka kuniua?”

    20 Ule umati wa watu ukamjibu, “Wewe una pepo mchafu! Ni nani anayetaka kukuua?”

    21 Yesu akawajibu, “Nimefanya muujiza mmoja na nyote mkastaajabu. 22 Lakini kwa kuwa Mose aliwaamuru tohara (ingawa kwa kweli haikutoka kwa Mose bali kwa baba zenu wakuu), mnamtahiri mtoto hata siku ya Sabato. 23 Ikiwa mtoto aweza kutahiriwa siku ya Sabato kusudi sheria ya Mose isivunjwe, kwa nini mnanikasirikia kwa kumponya mtu mwili wake wote siku ya Sabato? 24 Acheni kuhukumu mambo kwa jinsi mnavyoona tu, bali hukumuni kwa haki.”

  22. 57 Ulipowadia wakati wa Elizabeti kujifungua, alizaa mtoto mwanaume. 58 Majirani zake na jamii zake wakasikia jinsi Bwana alivyomfanyia rehema kuu, nao wakafurahi pamoja naye.

    59 Siku ya nane wakaja kumtahiri mtoto, wakataka yule mtoto aitwe Zekaria, ambalo ndilo jina la baba yake. 60 Lakini mama yake akakataa na kusema, “Hapana! Jina lake ataitwa Yohana.”

    61 Wakamwambia, “Hakuna mtu yeyote katika jamaa yako mwenye jina kama hilo.”

    62 Basi wakamfanyia Zekaria baba yake ishara ili kujua kwamba yeye angependa kumpa mtoto jina gani. 63 Akaomba wampe kibao cha kuandikia na kwa mshangao wa kila mtu akaandika: “Jina lake ni Yohana.” 64 Papo hapo kinywa chake kikafunguliwa na ulimi wake ukaachiwa, akawa anaongea akimsifu Mungu. 65 Majirani wote wakajawa na hofu ya Mungu, na katika nchi yote ya vilima vya Uyahudi watu walikuwa wakinena juu ya mambo haya yote. 66 Kila aliyesikia habari hizi alishangaa akauliza, “Je, mtoto huyu atakuwa mtu wa namna gani?” Maana mkono wa Bwana ulikuwa pamoja naye.

  23. 1 Paulo akafika Derbe na kisha Listra, ambako kulikuwa na mwanafunzi mmoja jina lake Timotheo, ambaye mama yake alikuwa Myahudi aliyeamini, lakini baba yake alikuwa Myunani. 2 Alikuwa amesifiwa sana na wale ndugu waliokuwa wameamini huko Listra na Ikonio 3 Paulo alitaka Timotheo afuatane naye, hivyo akamchukua na kumtahiri kwa sababu ya Wayahudi waliokuwa wanaishi eneo lile kwa maana wote walimjua baba yake ni Myunani. 4 Walipokuwa wakienda mji kwa mji, wakawa wanawapa maamuzi yaliyotolewa na mitume na wazee huko Yerusalemu ili wayafuate. 5 Hivyo makanisa yakawa imara katika imani na kuongezeka kiidadi kila siku.

  24. 10 Kwa maana wako wengi wasiotii, wenye maneno yasiyo na maana, hasa wale wa kikundi cha tohara. 11 Hao ni lazima wanyamazishwe, kwa sababu wanaharibu watu wa nyumba nzima wakifundisha mambo yasiyowapasa kufundisha. Wanafanya hivyo kwa ajili ya kujipatia mapato ya udanganyifu. 12 Hata mmojawapo wa manabii wao mwenyewe amesema, “Wakrete ni waongo siku zote, wanyama wabaya, walafi, wavivu.” 13 Ushuhuda huu ni kweli. Kwa hiyo, uwakemee kwa ukali wapate kuwa wazima katika imani, 14 ili wasiendelee kuangalia hadithi za Kiyahudi au maagizo ya wale watu wanaoikataa kweli.

  25. 44 Wakati Petro alikuwa akisema maneno haya, Roho Mtakatifu aliwashukia wote waliokuwa wakisikiliza ule ujumbe. 45 Wale wa tohara walioamini waliokuja na Petro walishangaa kwa kuona kuwa kipawa cha Roho Mtakatifu kimemwagwa juu ya watu wa Mataifa. 46 Kwa kuwa waliwasikia wakinena kwa lugha mpya na kumwadhimisha Mungu.

    Ndipo Petro akasema, 47 “Je, kuna mtu yeyote anayeweza kuzuia watu hawa wasibatizwe kwa maji? Wamempokea Roho Mtakatifu kama sisi tulivyompokea.” 48 Kwa hiyo akaamuru wabatizwe kwa jina la Yesu Kristo. Wakamsihi Petro akae nao kwa siku chache.

  26. 23 Siku ile ile, Abrahamu akamchukua Ishmaeli mwanawe na wote waliozaliwa nyumbani mwake pamoja na walionunuliwa kwa fedha zake, kila mwanaume wa nyumbani mwake, akawatahiri, kama Mungu alivyomwagiza. 24 Abrahamu alikuwa na umri wa miaka tisini na tisa alipotahiriwa, 25 naye Ishmaeli mwanawe alitahiriwa akiwa na umri wa miaka kumi na mitatu. 26 Abrahamu na Ishmaeli mwanawe walitahiriwa siku ile ile, 27 Kila mwanaume nyumbani mwa Abrahamu, pamoja na wote waliozaliwa nyumbani mwake au aliyenunuliwa kwa fedha kutoka kwa mgeni, alitahiriwa pamoja naye.

  27. 1 Mitume na ndugu walioamini waliokuwa huko Uyahudi wakasikia kuwa watu wa Mataifa nao wamepokea neno la Mungu. 2 Hivyo Petro alipopanda Yerusalemu, wale wa tohara waliokuwa wameamini wakamshutumu, 3 wakisema, “Ulikwenda kwa watu wasiotahiriwa na kula pamoja nao.”

    4 Ndipo Petro akaanza kuwaeleza kuhusu mambo yote yalivyotokea hatua kwa hatua akisema, 5 “Nilikuwa katika mji wa Yafa nikiomba, nami nikapitiwa na usingizi wa ghafula, nikaona maono. Kulikuwa na kitu kama nguo kubwa ikishuka kutoka mbinguni, ikishushwa kwa ncha zake nne, nayo ikanikaribia. 6 Nilipoangalia ndani yake kwa karibu niliona wanyama wenye miguu minne wa nchini, wanyama wa mwitu, watambaao na ndege wa angani. 7 Ndipo nikasikia sauti ikiniambia, ‘Petro, ondoka uchinje na ule.’

    8 “Nikajibu, ‘La hasha Bwana! Kitu chochote kilicho najisi hakijaingia kinywani mwangu.’

    9 “Sauti ikasema kutoka mbinguni mara ya pili, ‘Usikiite najisi kitu chochote Mungu alichokitakasa.’ 10 Jambo hili lilitokea mara tatu, ndipo kile kitu kikavutwa tena mbinguni.

    11 “Wakati ule ule watu watatu, waliokuwa wametumwa kutoka Kaisaria waliwasili katika nyumba niliyokuwa nikikaa. 12 Roho Mtakatifu akaniambia niende nao bila kuwa na ubaguzi kati yao na sisi. Hawa ndugu sita pia walifuatana nami, nasi tukaingia nyumbani mwa huyo Kornelio. 13 Akatuambia jinsi alivyoona malaika aliyekuwa amesimama katika nyumba yake na kusema, ‘Tuma watu waende Yafa wakamlete Simoni aitwaye Petro. 14 Yeye atakupa ujumbe ambao kwa huo wewe na wa nyumbani mwako wote mtaokoka.’

    15 “Nami nilipoanza kusema, Roho Mtakatifu akashuka juu yao kama vile alivyotushukia sisi hapo mwanzo. 16 Nami nikakumbuka neno la Bwana alivyosema, ‘Yohana alibatiza kwa maji, lakini ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu.’ 17 Basi ikiwa Mungu aliwapa hawa watu kipawa kile kile alichotupa sisi tuliomwamini Bwana Yesu Kristo, mimi ni nani hata nifikirie kuwa ningeweza kumpinga Mungu?”

    18 Waliposikia haya hawakuwa na la kupinga zaidi. Nao wakamwadhimisha Mungu wakisema, “Basi, Mungu amewapa hata watu wa Mataifa toba iletayo uzima wa milele.”

  28. 3 Abrahamu akamwita Isaki yule mwana ambaye Sara alimzalia. 4 Isaki alipokuwa na umri wa siku nane, Abrahamu akamtahiri, kama Mungu alivyomwamuru.

  29. 40 “ ‘Lakini kama watatubu dhambi zao na dhambi za baba zao, udanganyifu wao dhidi yangu na uadui wao kwangu, 41 ambao ulinifanya niwe na uadui nao hata nikawapeleka katika nchi ya adui zao, wakati mioyo yao isiyotahiriwa itanyenyekea na kutubu dhambi yao, 42 nami nitakumbuka agano langu na Yakobo, na agano langu na Isaki, na agano langu na Abrahamu, nami nitaikumbuka nchi.

  30. 1 Basi wafalme wote wa Waamori magharibi ya Yordani na wafalme wote wa Kanaani waliokuwa kwenye pwani waliposikia jinsi Bwana alivyoukausha Mto Yordani mbele ya Waisraeli hata tulipokwisha kuvuka, mioyo yao ikayeyuka kwa hofu, wala hawakuwa na ujasiri kuwakabili Waisraeli.

    2 Wakati huo Bwana akamwambia Yoshua, “Tengeneza visu vya mawe magumu sana na uwatahiri Waisraeli tena.” 3 Kwa hiyo Yoshua akatengeneza visu vya mawe magumu sana na kutahiri Waisraeli huko Gibeath-Haaralothi.

    4 Hii ndiyo sababu ya Yoshua kufanya hivyo: Wanaume wote waliotoka Misri, wote wenye umri wa kwenda vitani, walikufa jangwani wakiwa njiani baada ya kuondoka Misri. 5 Watu wote waliotoka Misri walikuwa wametahiriwa, lakini watu wote waliozaliwa jangwani wakiwa safarini toka Misri walikuwa hawajatahiriwa. 6 Waisraeli walitembea jangwani miaka arobaini mpaka wanaume wote wale waliokuwa na umri wa kwenda vitani wakati waliondoka Misri walipokwisha kufa, kwa kuwa hawakumtii Bwana. Kwa maana Bwana alikuwa amewaapia kuwa wasingeweza kuona nchi ambayo alikuwa amewaahidi baba zao katika kuapa kutupatia, nchi inayotiririka maziwa na asali. 7 Kwa hiyo akawainua wana wao baada yao na hawa ndio hao ambao Yoshua aliwatahiri. Walikuwa hawajatahiriwa bado kwa sababu walikuwa safarini. 8 Baada ya taifa lote kutahiriwa, waliendelea kukaa kambini mpaka walipokuwa wamepona.

  31. 8 Ndipo akampa Abrahamu Agano la tohara. Naye Abrahamu akamzaa Isaki na kumtahiri siku ya nane. Baadaye Isaki akamzaa Yakobo, naye Yakobo akawazaa wale wazee wetu kumi na wawili.

  32. 12 Lakini Mose akamwambia Bwana, “Ikiwa Waisraeli hawatanisikiliza, kwa nini yeye Farao anisikilize mimi, ambaye huzungumza kwa kigugumizi?”

  33. 4 Kisha yule mtu akanileta kwa njia ya lango la kaskazini mpaka mbele ya Hekalu. Nikatazama nami nikauona utukufu wa Bwana ukilijaza Hekalu la Bwana, nami nikaanguka kifudifudi.

    5 Bwana akaniambia, “Mwanadamu, angalia kwa uangalifu, usikilize kwa bidii na uzingatie kila kitu ninachokuambia kuhusu masharti yote yanayohusu Hekalu la Bwana. Uwe mwangalifu kuhusu wale wanaoruhusiwa hekaluni na wale wasioruhusiwa kuingia mahali patakatifu. 6 Iambie nyumba ya kuasi ya Israeli, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Matendo yenu ya machukizo yatosha, ee nyumba ya Israeli! 7 Zaidi ya matendo yenu yote ya machukizo, mmewaleta wageni wasiotahiriwa mioyo na miili katika patakatifu pangu, mkilinajisi Hekalu langu, huku mkinitolea chakula, mafuta ya wanyama na damu, nanyi mmevunja Agano langu. 8 Badala ya kutimiza wajibu wenu kuhusiana na vitu vyangu vitakatifu, mmeweka watu wengine kuwa viongozi katika patakatifu pangu. 9 Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Hakuna mgeni asiyetahiriwa moyo na mwilini anayeruhusiwa kuingia patakatifu pangu, wala hata wageni wanaoishi miongoni mwa Waisraeli.

  34. 27 Basi, kujivuna kuko wapi? Kumewekwa mbali. Kwa sheria gani? Je, ni kwa ile ya matendo? La hasha, bali kwa ile sheria ya imani. 28 Kwa maana twaona kwamba mwanadamu huhesabiwa haki kwa njia ya imani wala si kwa matendo ya sheria. 29 Je, Mungu ni Mungu wa Wayahudi peke yao? Je, yeye si Mungu wa watu wa Mataifa pia? Naam, yeye ni Mungu wa watu wa Mataifa pia. 30 Basi kwa kuwa tuna Mungu mmoja tu, atawahesabia haki wale waliotahiriwa kwa imani na wale wasiotahiriwa kwa imani iyo hiyo. 31 Je, basi ni kwamba tunaibatilisha sheria kwa imani hii? La, hasha! Badala yake tunaithibitisha sheria.

  35. 3 Baba yake na mama yake wakamjibu, “Je, hakuna mwanamke miongoni mwa jamaa yako au miongoni mwa ndugu zako, hata ulazimike kwenda kujitwalia mwanamke kutoka kwa hawa Wafilisti wasiotahiriwa?”

    Lakini Samsoni akamwambia baba yake, “Nipatieni huyo kwa maana ndiye alinipendeza.”

  36. 51 “Enyi watu wenye shingo ngumu, msiotahiriwa mioyo wala masikio, daima hamwachi kumpinga Roho Mtakatifu, kama walivyofanya baba zenu. 52 Je, kuna nabii gani ambaye baba zenu hawakumtesa? Waliwaua wale waliotabiri habari za kuja kwake yule Mwenye Haki. Nanyi sasa mmekuwa wasaliti wake na wauaji. 53 Ninyi ndio mlipokea sheria zilizoletwa kwenu na malaika, lakini hamkuzitii.”

  37. 11 Lakini Petro alipofika Antiokia, mimi nilimpinga ana kwa ana kwa sababu alikuwa amekosea kwa wazi. 12 Kabla baadhi ya watu waliotoka kwa Yakobo hawajafika, alikuwa akila pamoja na watu wa Mataifa. Lakini hao watu walipofika alianza kujiondoa na kujitenga na watu wa Mataifa kwa sababu aliwaogopa wale wa kundi la tohara. 13 Pia Wayahudi wengine waliungana naye katika unafiki huu, hata Barnaba naye akapotoshwa na unafiki wao.

    14 Nilipoona kwamba hawatendi sawasawa na kweli ya Injili, nilimwambia Petro mbele ya wote, “Wewe ni Myahudi, nawe unaishi kama mtu wa Mataifa na wala si kama Myahudi. Imekuwaje basi, mnawalazimisha watu wa Mataifa kufuata desturi za Kiyahudi?

    15 “Sisi wenyewe ni Wayahudi kwa kuzaliwa na si watu wenye dhambi kama watu wa Mataifa, 16 bado tunajua ya kwamba mtu hahesabiwi haki kwa matendo ya sheria bali kwa njia ya imani katika Yesu Kristo. Hivyo sisi pia, tumemwamini Kristo Yesu ili tupate kuhesabiwa haki kwa njia ya imani katika Kristo, wala si kwa matendo ya sheria, kwa sababu kwa kushika sheria hakuna hata mtu mmoja atakayehesabiwa haki.

    17 “Lakini tukitafuta kuhesabiwa haki katika Kristo, inakuwa dhahiri kwamba sisi ni wenye dhambi. Je, ina maana kwamba Kristo amekuwa mtumishi wa dhambi? La hasha! 18 Lakini ikiwa mimi ninajenga tena kile ambacho nimekwisha kukibomoa, basi ninaonyesha kwamba mimi ni mkosaji. 19 Kwa maana mimi kwa njia ya sheria, nimeifia sheria ili nipate kuishi kwa ajili ya Mungu. 20 Nimesulubiwa pamoja na Kristo, wala si mimi tena ninayeishi, bali Kristo ndiye aishiye ndani yangu. Uhai nilio nao sasa katika mwili, ninaishi kwa imani ya Mwana wa Mungu, aliyenipenda na kujitoa kwa ajili yangu. 21 Siibatilishi neema ya Mungu, kwa maana kama haki ingeweza kupatikana kwa njia ya sheria, basi Kristo alikufa bure!”

  38. 43 Bwana akamwambia Mose na Aroni, “Haya ndiyo masharti kwa ajili ya Pasaka:

    “Mgeni hataruhusiwa kula Pasaka. 44 Mtumwa yeyote ambaye mmemnunua aweza kuila kama mmemtahiri, 45 lakini kibarua yeyote au msafiri haruhusiwi kula.

    46 “Sharti iliwe ndani ya nyumba; msichukue nyama yoyote nje ya nyumba hiyo. Msiuvunje mfupa wowote. 47 Jumuiya yote ya Israeli ni lazima waiadhimishe Pasaka hiyo.

    48 “Mgeni aishiye miongoni mwenu ambaye anataka kuadhimisha Pasaka ya Bwana ni lazima wanaume wote waliomo nyumbani mwake wawe wametahiriwa, ndipo aweze kushiriki kama mzawa. Mwanaume yeyote asiyetahiriwa haruhusiwi kuila. 49 Sheria iyo hiyo itamuhusu mzawa na mgeni anayeishi miongoni mwenu.”

    50 Waisraeli wote walifanya kama vile Bwana alivyomwagiza Mose na Aroni. 51 Siku ile ile Bwana akawatoa Waisraeli katika nchi ya Misri kwa vikosi vyao.

  39. 1 Basi Dina, binti wa Yakobo aliyezaliwa na Lea, akatoka nje kuwatembelea wanawake wa nchi ile. 2 Ikawa Shekemu mwana wa Hamori Mhivi, mtawala wa eneo lile alipomwona, akamchukua na kumnajisi. 3 Moyo wake ukavutwa sana kwa Dina binti Yakobo, akampenda huyu msichana na akazungumza naye kwa kumbembeleza. 4 Shekemu akamwambia baba yake Hamori, “Nipatie msichana huyu awe mke wangu.”

    5 Yakobo aliposikia kwamba binti yake Dina amenajisiwa, wanawe walikuwa mashambani wakichunga mifugo yake, kwa hiyo akalinyamazia jambo hilo mpaka waliporudi nyumbani.

    6 Kisha Hamori baba yake Shekemu akaenda kuzungumza na Yakobo. 7 Basi wana wa Yakobo walikuwa wamerudi kutoka mashambani mara tu waliposikia kilichotokea. Walikuwa wamejawa na huzuni na ghadhabu, kwa sababu Shekemu alikuwa amefanya jambo la aibu katika Israeli kwa kukutana kimwili na binti wa Yakobo, kitu ambacho hakingepasa kufanyika.

    8 Lakini Hamori akawaambia, “Moyo wa mwanangu Shekemu umeelekea kwa binti yenu. Tafadhali mpeni awe mke wake. 9 Oaneni na sisi, tupeni binti zenu, nanyi mchukue binti zetu. 10 Mwaweza kuishi katikati yetu, nchi ni wazi kwenu. Ishini ndani yake, fanyeni biashara humu na mjipatie mali.”

    11 Kisha Shekemu akamwambia baba yake Dina pamoja na ndugu zake, “Na nipate kibali machoni penu, nami nitawapa chochote mtakachosema. 12 Niambieni kiasi cha mahari na zawadi nitakayoileta, hata iwe kubwa kiasi gani, nami nitawalipa chochote mtakachodai. Nipeni tu huyu msichana awe mke wangu.”

    13 Kwa sababu ndugu yao Dina alikuwa amenajisiwa, wana wa Yakobo wakajibu kwa udanganyifu walipozungumza na Shekemu pamoja na baba yake Hamori. 14 Wakawaambia, “Hatuwezi kufanya jambo kama hili, hatuwezi kumtoa dada yetu kwa mtu ambaye hakutahiriwa. Hiyo itakuwa aibu kwetu. 15 Tutakuruhusu kwa sharti moja tu, kwamba mtakuwa kama sisi kwa kuwatahiri wanaume wenu wote. 16 Kisha tutawapa binti zetu na sisi tutawachukua binti zenu. Tutaishi kwenu na tutakuwa watu wamoja nanyi. 17 Lakini mkikataa kutahiriwa, tutamchukua ndugu yetu na kuondoka.”

    18 Pendekezo lao likawa jema kwa Hamori na Shekemu mwanawe. 19 Kijana mdogo, ambaye alikuwa ameheshimiwa kati ya wote walioishi nyumbani mwa baba yake, hakupoteza muda kufanya waliyoyasema, kwa sababu alikuwa amependezwa sana na binti Yakobo. 20 Kwa hiyo Hamori na Shekemu mwanawe walikwenda kwenye lango la mji kuzungumza na wenzao wa mjini. 21 Wakasema, “Hawa watu ni marafiki kwetu, tuwaruhusu waishi katika nchi yetu na kufanya biashara ndani yake, nchi ina nafasi tele kwa ajili yao. Tunaweza kuoa binti zao. Nao wanaweza kuoa binti zetu. 22 Lakini watu hao watakuwa tayari kukubali kuishi nasi kama watu wamoja nao kwa sharti kwamba wanaume wetu watahiriwe, kama wao. 23 Je, si mifugo yao, mali zao na wanyama wao wengine wote watakuwa wetu? Basi na tuwape kibali, nao wataishi miongoni mwetu.”

    24 Wanaume wote waliotoka nje ya lango la mji walikubaliana na Hamori na Shekemu mwanawe na kila mwanaume katika mji ule akatahiriwa.

    25 Baada ya siku tatu, wakati wote wakiwa wangali katika maumivu, wana wawili wa Yakobo, yaani Simeoni na Lawi, ndugu zake Dina, wakachukua panga zao na kuvamia mji ambao haukutazamia vita, wakaua kila mwanaume. 26 Wakawaua Hamori na Shekemu mwanawe kwa upanga kisha wakamchukua Dina kutoka nyumba ya Shekemu na kuondoka. 27 Wana wa Yakobo walipita juu ya maiti katika kuteka nyara mji ule ambamo dada yao alikuwa amenajisiwa. 28 Wakachukua kondoo na mbuzi, ngʼombe, punda na kila kitu kilichokuwa chao ndani ya mji ule na mashambani. 29 Walichukua utajiri wao wote pamoja na wanawake na watoto wao, wakachukua nyara kila kitu ndani ya nyumba zao.

  40. 30 Lakini Mose akamwambia Bwana, “Kwa kuwa mimi huzungumza kwa kigugumizi, Farao atanisikiliza mimi?”

  41. 1 Amka, amka, ee Sayuni,

    jivike nguvu.

    Vaa mavazi yako ya fahari,

    ee Yerusalemu, mji mtakatifu.

    Asiyetahiriwa na aliye najisi

    hataingia kwako tena.

  42. 31 “Siku zinakuja,” asema Bwana,

    “nitakapofanya agano jipya

    na nyumba ya Israeli

    na nyumba ya Yuda.

    32 Halitafanana na agano

    nililofanya na baba zao

    wakati nilipowashika mkono

    kuwaongoza watoke Misri,

    kwa sababu walivunja agano langu,

    ijapokuwa nilikuwa mume kwao,”

    asema Bwana.

    33 “Hili ndilo agano nitakalofanya na nyumba ya Israeli

    baada ya siku zile,” asema Bwana.

    “Nitaweka sheria yangu katika nia zao,

    na kuiandika mioyoni mwao.

    Nitakuwa Mungu wao,

    nao watakuwa watu wangu.

    34 Mtu hatamfundisha tena jirani yake,

    wala mtu kumfundisha ndugu yake akisema, ‘Mjue Bwana Mungu,’

    kwa sababu wote watanijua mimi,

    tangu aliye mdogo kabisa kwao, hadi aliye mkuu sana,”

    asema Bwana.

    “Kwa sababu nitasamehe uovu wao,

    wala sitazikumbuka dhambi zao tena.”

  43. 18 “ ‘Ni miti ipi ya Edeni inayoweza kulinganishwa nawe kwa fahari na utukufu? Hata hivyo, wewe pia, utashushwa chini pamoja na miti ya Edeni mpaka kuzimu, utalala miongoni mwa wasiotahiriwa, pamoja na wale waliouawa kwa upanga.

    “ ‘Huyu ni Farao pamoja na makundi yake yote ya wajeuri, asema Bwana Mwenyezi.’ ”

  44. Kukamatwa Kwa Paulo, Na Safari Yake Kwenda Rumi

    17 Tulipofika Yerusalemu ndugu wakatukaribisha kwa furaha. 18 Kesho yake Paulo pamoja na wengine wetu tulikwenda kumwona Yakobo, na wazee wote walikuwepo. 19 Baada ya kuwasalimu, Paulo akatoa taarifa kamili ya mambo yote ambayo Mungu alikuwa amefanya miongoni mwa watu wa Mataifa kupitia huduma yake.

    20 Baada ya kusikia mambo haya wakamwadhimisha Mungu. Ndipo wakamwambia Paulo, “Ndugu, unaona kulivyo na maelfu ya Wayahudi walioamini, nao wote wana juhudi kwa ajili ya sheria. 21 Lakini wameambiwa habari zako kwamba unafundisha Wayahudi wote waishio miongoni mwa watu wa Mataifa kumkataa Mose, na kwamba unawaambia wasiwatahiri watoto wao wala kufuata desturi zetu. 22 Sasa tufanyeje? Bila shaka watasikia kwamba umekuja Yerusalemu. 23 Kwa hiyo fanya lile tunalokuambia. Tunao watu wanne hapa ambao wameweka nadhiri. 24 Jiunge na watu hawa, mfanye utaratibu wa ibada ya kujitakasa pamoja nao, na ulipe gharama ili wanyoe nywele zao. Kwa njia hii kila mtu atafahamu ya kuwa mambo waliyosikia si ya kweli na kwamba wewe unaishika sheria. 25 Lakini kuhusu wale watu wa Mataifa walioamini, tumewaandikia uamuzi wetu: kwamba wajitenge na vyakula vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, au kula nyama ya mnyama aliyenyongwa, na wajiepushe na uasherati.”

    26 Ndipo kesho yake Paulo akawachukua wale watu na akajitakasa pamoja nao. Akaingia ndani ya hekalu ili atoe taarifa ya tarehe ambayo siku zao za utakaso zingemalizika na sadaka ingetolewa kwa ajili ya kila mmoja wao.