69 Bible Verses About Visions

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Visions
  1. 3 Basi akiwa katika safari yake, alipokaribia Dameski, ghafula nuru kutoka mbinguni ikamwangaza kotekote. 4 Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, “Sauli, Sauli, mbona unanitesa?”

    5 Sauli akajibu, “U nani wewe, Bwana?”

    Ile sauti ikajibu, “Mimi ni Yesu unayemtesa. 6 Sasa inuka uingie mjini, nawe utaambiwa yakupasayo kutenda.”

    7 Watu waliokuwa wakisafiri pamoja na Sauli wakasimama bila kuwa na la kusema, kwa sababu walisikia sauti lakini hawakumwona aliyekuwa akizungumza. 8 Sauli akainuka kutoka pale chini na alipojaribu kufungua macho yake hakuweza kuona kitu chochote. Basi wakamshika mkono wakamwongoza mpaka Dameski. 9 Naye kwa muda wa siku tatu alikuwa kipofu naye hakula wala kunywa chochote.

    10 Huko Dameski alikuwepo mwanafunzi mmoja jina lake Anania. Bwana alimwita katika maono, “Anania!”

    Akajibu, “Mimi hapa Bwana.”

    11 Bwana akamwambia, “Ondoka uende katika barabara iitwayo Nyofu ukaulize katika nyumba ya Yuda mtu kutoka Tarso, jina lake Sauli, kwa maana wakati huu anaomba, 12 katika maono amemwona mtu aitwaye Anania akija na kuweka mikono juu yake ili apate kuona tena.”

  2. 1 Nitasimama katika zamu yangu,

    na kujiweka mwenyewe juu ya maboma;

    nitatazama nione atakaloniambia,

    na ni jibu gani nitakalotoa kuhusu lalamiko hili.

    2 Kisha Bwana akajibu:

    “Andika ufunuo huu,

    na ukaufanye wazi juu ya vibao,

    ili mpiga mbiu akimbie nao.

    3 Kwa kuwa ufunuo huu unasubiri wakati uliokubalika;

    unazungumzia mambo ya mwisho,

    na kamwe hautakosea.

    Iwapo utakawia, wewe usubiri;

    kwa hakika utakuja na hautachelewa.

    4 “Tazama, amejaa majivuno;

    anavyovitamani si vya unyofu:

    lakini mwenye haki ataishi kwa imani yake:

  3. 18 Mahali pasipo na ufunuo, watu kujizuia,

    bali ana heri mtu yule aishikaye sheria.

  4. 6 Bwana akasema, “Sikilizeni maneno yangu:

    “Akiwapo nabii wa Bwana miongoni mwenu,

    nitajifunua kwake kwa maono,

    nitanena naye katika ndoto.

    7 Lakini sivyo kwa mtumishi wangu Mose;

    yeye ni mwaminifu katika nyumba yangu yote.

    8 Kwake nitanena naye uso kwa uso,

    waziwazi wala si kwa mafumbo;

    yeye ataona umbo la Bwana.

    Kwa nini basi ninyi hamkuogopa

    kuzungumza kinyume cha mtumishi wangu Mose?”

  5. 6 Paulo pamoja na wenzake wakasafiri sehemu za Frigia na Galatia, kwa kuwa Roho Mtakatifu hakuwaruhusu kulihubiri neno huko Asia. 7 Walipofika mpaka wa Misia, wakajaribu kuingia Bithinia lakini Roho wa Yesu hakuwaruhusu. 8 Kwa hiyo wakapita Misia, wakafika Troa. 9 Wakati wa usiku Paulo akaona maono, mtu wa Makedonia amesimama akimsihi, “Vuka uje huku Makedonia utusaidie.” 10 Baada ya Paulo kuona maono haya, tulijiandaa kwa haraka kuondoka kwenda Makedonia tukiwa tumesadiki kuwa Mungu alikuwa ametuita kuhubiri habari njema huko.

  6. 1 Kisha nikatazama na hapo mbele yangu alikuwepo Mwana-Kondoo, akiwa amesimama juu ya Mlima Sayuni. Pamoja naye walikuwa wale 144,000 wenye Jina la Mwana-Kondoo na Jina la Baba yake likiwa limeandikwa kwenye vipaji vya nyuso zao. 2 Nami nikasikia sauti kutoka mbinguni kama sauti ya maji mengi yaendayo kwa kasi na sauti kama ngurumo ya radi. Sauti hiyo niliyoisikia ilikuwa kama sauti ya wapiga vinubi wakipiga vinubi vyao. 3 Nao wakaimba wimbo mpya mbele ya hicho kiti cha enzi na mbele ya wale viumbe wanne wenye uhai na wale wazee. Hakuna mtu yeyote aliyeweza kujifunza wimbo huo isipokuwa hao 144,000 waliokuwa wamekombolewa kutoka duniani. 4 Hawa ndio wale ambao hawakujitia unajisi kwa wanawake, kwa kuwa wao ni bikira. Wao humfuata Mwana-Kondoo kila aendako. Hawa wamekombolewa kutoka miongoni mwa wanadamu wakawa malimbuko kwa Mungu na kwa Mwana-Kondoo. 5 Vinywani mwao hapakuonekana uongo, wala hawakuwa na hatia yoyote.

    6 Kisha nikamwona malaika mwingine akiruka juu angani, naye alikuwa na Injili ya milele ya kuwatangazia wale waishio duniani, yaani, kwa kila taifa, kabila, lugha na jamaa. 7 Akasema kwa sauti kubwa, “Mcheni Mungu na kumpa utukufu, kwa maana saa ya hukumu yake imewadia. Mwabuduni yeye aliyeziumba mbingu, dunia, bahari na chemchemi za maji.”

    8 Malaika wa pili akafuata akisema, “Umeanguka! Umeanguka Babeli Mkuu, ule uliyafanya mataifa yote kulewa kwa mvinyo wa ghadhabu ya uasherati wake.”

    9 Malaika wa tatu akawafuata hao wawili akisema kwa sauti kubwa, “Kama mtu yeyote anamwabudu huyo mnyama na sanamu yake na kutiwa chapa yake kwenye kipaji chake cha uso au kwenye mkono wake, 10 yeye pia atakunywa mvinyo wa hasira kali ya Mungu ambayo imemiminwa katika kikombe cha ghadhabu yake pasipo kuchanganywa na maji. Naye atateswa kwa moto uwakao na kiberiti mbele ya malaika watakatifu na mbele za Mwana-Kondoo. 11 Nao moshi wa mateso yao hupanda juu milele na milele. Hakuna mapumziko, mchana wala usiku, kwa wale wamwabuduo huyo mnyama na sanamu yake, au kwa yeyote anayepokea chapa ya jina lake.” 12 Hapa ndipo penye wito wa subira na uvumilivu wa watakatifu; wale wanaozishika amri za Mungu na kudumu katika uaminifu kwa Yesu.

    13 Kisha nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, “Andika: Wamebarikiwa wafu wafao katika Bwana tangu sasa.”

    “Naam,” asema Roho, “watapumzika kutoka taabu zao, kwa kuwa matendo yao yatawafuata.”

    14 Nikatazama, hapo mbele yangu palikuwa na wingu jeupe, na aliyekuwa ameketi juu ya hilo wingu alikuwa “kama Mwana wa Adamu” mwenye taji ya dhahabu kichwani mwake na mundu mkali mkononi mwake. 15 Kisha malaika mwingine akaja kutoka hekaluni naye akamwita kwa sauti kubwa yule aliyekuwa ameketi juu ya lile wingu akasema, “Chukua mundu wako ukavune kwa kuwa wakati wa mavuno umewadia, kwa maana mavuno ya dunia yamekomaa.” 16 Hivyo yule aliyekuwa ameketi juu ya lile wingu akauzungusha mundu wake duniani, nayo dunia ikavunwa.

    17 Malaika mwingine akatoka katika hekalu lililoko mbinguni, naye pia alikuwa na mundu mkali. 18 Kisha malaika mwingine, aliyekuwa na mamlaka juu ya moto, akatoka kwenye madhabahu, naye akamwita yule malaika mwenye mundu mkali kwa sauti kubwa, akisema, “Chukua mundu wako mkali ukakusanye vichala vya mizabibu ya dunia, maana zabibu zake zimeiva.” 19 Hivyo yule malaika akauzungusha mundu wake duniani na kukusanya zabibu za dunia na kuzitupa kwenye shinikizo kubwa la ghadhabu ya Mungu. 20 Lile shinikizo likakanyagwa nje ya mji, nayo damu ikatiririka kama mafuriko kutoka hilo shinikizo kufikia kimo cha hatamu za farasi, kwa umbali wa maili 200.

  7. 2 Mungu akanena na Israeli katika maono usiku na kusema, “Yakobo! Yakobo!”

    Akajibu, “Mimi hapa.”

    3 Mungu akamwambia, “Mimi ndimi Mungu wa baba yako, usiogope kushuka Misri, kwa maana huko nitakufanya taifa kubwa. 4 Nitashuka Misri pamoja nawe, nami hakika nitakurudisha tena Kanaani. Mikono ya Yosefu mwenyewe ndiyo itakayofunga macho yako.”

  8. 1 Baada ya jambo hili, neno la Bwana likamjia Abramu katika maono:

    “Usiogope, Abramu.

    Mimi ni ngao yako,

    na thawabu yako kubwa sana.”

    2 Lakini Abramu akasema, “Ee Bwana Mwenyezi, utanipa nini na mimi sina hata mtoto na atakayerithi nyumba yangu ni huyu Eliezeri Mdameski?” 3 Abramu akasema, “Hukunipa watoto, hivyo mtumishi katika nyumba yangu ndiye atakuwa mrithi wangu.”

    4 Ndipo neno la Bwana lilipomjia: “Mtu huyu hatakuwa mrithi wako, bali mwana atakayetoka katika viuno vyako mwenyewe ndiye atakayekuwa mrithi wako.” 5 Akamtoa nje na kusema, “Tazama juu kuelekea mbinguni na uhesabu nyota, kama hakika utaweza kuzihesabu.” Ndipo akamwambia, “Hivyo ndivyo uzao wako utakavyokuwa.”

    6 Abramu akamwamini Bwana, naye kwake hili likahesabiwa kuwa haki.

  9. 1 Kijana Samweli alihudumu mbele za Bwana chini ya Eli. Katika siku zile neno la Mungu lilikuwa adimu, hapakuwepo na maono mengi.

  10. 1 Katika mwaka ule Mfalme Uzia alikufa, nilimwona Bwana ameketi katika kiti cha enzi, kilicho juu na kilichotukuzwa sana, nalo pindo la joho lake likajaza Hekalu. 2 Juu yake walikuwepo maserafi, kila mmoja alikuwa na mabawa sita: Kwa mabawa mawili walifunika nyuso zao, kwa mengine mawili walifunika miguu yao, na kwa mawili walikuwa wakiruka. 3 Nao walikuwa wakiitana kila mmoja na mwenzake:

    “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu

    ni Bwana Mwenye Nguvu Zote;

    dunia yote imejaa utukufu wake.”

    4 Kwa sauti zao, miimo ya milango na vizingiti vilitikisika, nalo Hekalu likajaa moshi.

    5 Ndipo nikalia, “Ole wangu! Nimeangamia! Kwa kuwa mimi ni mtu mwenye midomo michafu, nami ninaishi katikati ya watu wenye midomo michafu, nayo macho yangu yamemwona Mfalme, Bwana Mwenye Nguvu Zote.”

    6 Ndipo mmoja wa wale maserafi akaruka kunijia akiwa na kaa la moto linalowaka mkononi mwake, ambalo alikuwa amelichukua kwa koleo kutoka madhabahuni. 7 Akanigusa nalo kinywa changu na kusema, “Tazama, hili limegusa midomo yako, uovu wako umeondolewa, nayo dhambi yako imesamehewa.”

    8 Kisha nikasikia sauti ya Bwana ikisema, “Nimtume nani? Ni nani atakayekwenda kwa ajili yetu?”

    Nami nikasema, “Mimi hapa. Nitume mimi!”

  11. 28 “Hata itakuwa, baada ya hayo,

    nitamimina Roho wangu juu ya wote wenye mwili.

    Wana wenu na binti zenu watatabiri,

    wazee wenu wataota ndoto,

    na vijana wenu wataona maono.

    29 Hata juu ya watumishi wangu, wanaume kwa wanawake,

    katika siku zile nitamimina Roho wangu.

    30 Nami nitaonyesha maajabu katika mbingu

    na duniani:

    damu, moto na mawimbi ya moshi.

    31 Jua litageuzwa kuwa giza

    na mwezi kuwa mwekundu kama damu,

    kabla ya kuja siku ya Bwana

    ile kuu na ya kutisha.

    32 Na kila mtu atakayeliitia

    jina la Bwana ataokolewa.

    Kwa maana juu ya Mlima Sayuni na katika Yerusalemu

    kutakuwepo wokovu,

    kama Bwana alivyosema,

    miongoni mwa walionusurika

    ambao Bwana awaita.

  12. 9 Usiku mmoja Bwana akamwambia Paulo katika maono, “Usiogope, lakini endelea kusema wala usinyamaze, 10 kwa maana mimi niko pamoja nawe, wala hakuna mtu atakayeweza kukushambulia ili kukudhuru, kwa kuwa ninao watu wengi katika mji huu ambao ni watu wangu.” 11 Hivyo Paulo akakaa huko kwa muda wa mwaka mmoja na nusu, akiwafundisha neno la Mungu.

  13. 1 Katika mwaka wa kwanza wa utawala wa Belshaza mfalme wa Babeli, Danieli aliota ndoto, nayo maono yakapita mawazoni yake alipokuwa amelala kitandani mwake. Akayaandika mambo aliyoyaona katika ndoto yake.

    2 Danieli akasema: “Katika maono yangu usiku nilitazama, na hapo mbele yangu kulikuwepo na upepo kutoka pande nne za mbingu, ukivuruga bahari kuu. 3 Wanyama wanne wakubwa, kila mmoja tofauti na mwenzake, wakajitokeza kutoka bahari.

    4 “Mnyama wa kwanza alifanana na simba, naye alikuwa na mabawa kama ya tai. Nikatazama mpaka mabawa yake yalipongʼolewa, naye akainuliwa katika nchi, akasimama kwa miguu miwili kama mwanadamu, naye akapewa moyo wa binadamu.

    5 “Hapo mbele yangu kulikuwa na mnyama wa pili, ambaye alionekana kama dubu. Upande wake mmoja ulikuwa umeinuka, na alikuwa na mbavu tatu katika kinywa chake kati ya meno yake. Akaambiwa, ‘Amka, ule nyama mpaka ushibe!’

    6 “Baada ya huyo, nilitazama, na mbele yangu kulikuwa na mnyama mwingine, aliyefanana na chui. Juu ya mgongo wake alikuwa na mabawa manne kama ya ndege. Mnyama huyu alikuwa na vichwa vinne, naye akapewa mamlaka ya kutawala.

    7 “Baada ya huyo, katika maono yangu usiku nilitazama, na mbele yangu kulikuwa na mnyama wa nne, mwenye kutisha na kuogofya, tena mwenye nguvu nyingi. Alikuwa na meno makubwa ya chuma; akapondaponda na kuangamiza wahanga wake, na kukanyaga chini ya nyayo zake chochote kilichosalia. Alikuwa tofauti na wanyama wote waliotangulia, naye alikuwa na pembe kumi.

    8 “Wakati nilipokuwa ninafikiri kuhusu pembe hizo, mbele yangu kulikuwa na pembe nyingine, ambayo ni ndogo, iliyojitokeza miongoni mwa zile kumi; pembe tatu za mwanzoni zilingʼolewa ili kuipa nafasi hiyo ndogo. Pembe hii ilikuwa na macho kama ya mwanadamu, na mdomo ulionena kwa majivuno.

    9 “Nilipoendelea kutazama,

    “viti vya enzi vikawekwa,

    naye Mzee wa Siku akaketi.

    Mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji;

    nywele za kichwa chake zilikuwa nyeupe kama sufu.

    Kiti chake cha enzi kilikuwa kinawaka kwa miali ya moto,

    nayo magurudumu yake yote yalikuwa yanawaka moto.

    10 Mto wa moto ulikuwa unatiririka,

    ukipita mbele yake.

    Maelfu elfu wakamhudumia;

    kumi elfu mara kumi elfu wakasimama mbele zake.

    Mahakama ikakaa kuhukumu,

    na vitabu vikafunguliwa.

    11 “Kisha nikaendelea kutazama kwa sababu ya yale maneno ya majivuno yaliyosemwa na ile pembe. Nikaendelea kuangalia mpaka yule mnyama alipouawa, na mwili wake ukaharibiwa na kutupwa katika ule moto uliowaka. 12 (Wanyama wengine walikuwa wamevuliwa mamlaka yao, lakini waliruhusiwa kuishi kwa muda fulani.)

  14. 17 “ ‘Katika siku za mwisho, asema Mungu,

    nitamimina Roho wangu

    juu ya wote wenye mwili.

    Wana wenu na binti zenu watatabiri,

    vijana wenu wataona maono,

    na wazee wenu wataota ndoto.

  15. 16 Hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote asemalo:

    “Msisikilize wanachowatabiria manabii,

    wanawajaza matumaini ya uongo.

    Wanasema maono kutoka akili zao wenyewe,

    hayatoki katika kinywa cha Bwana.

  16. 1 Katika mwaka wa thelathini, mwezi wa nne, siku ya tano ya mwezi, wakati nilipokuwa miongoni mwa hao waliokuwa uhamishoni kando ya Mto Kebari, mbingu zilifunguka nami nikaona maono ya Mungu.

  17. 10 Niliongea na manabii, nikawapa maono mengi

    na kusema mifano kupitia wao.”

  18. 1 Yanipasa nijisifu, ingawa haifaidi kitu. Nitaenda kwenye maono na ufunuo kutoka kwa Bwana. 2 Namjua mtu mmoja katika Kristo ambaye miaka kumi na minne iliyopita alichukuliwa juu hadi mbingu ya tatu. Kama ni katika mwili au nje ya mwili, sijui, Mungu ajua. 3 Nami najua ya kwamba mtu huyu, kwamba ni katika mwili au nje ya mwili mimi sijui, lakini Mungu ajua, 4 alinyakuliwa hadi Paradiso. Huko alisikia mambo yasiyoelezeka, mambo ambayo binadamu hana ruhusa ya kuyasimulia. 5 Nitajisifu kwa ajili ya mtu kama huyo, lakini sitajisifu kuhusu mimi mwenyewe ila mimi nitajisifia udhaifu wangu. 6 Hata kama ningependa kujisifu, sitakuwa mjinga, kwa maana nitakuwa nasema kweli. Lakini najizuia, ili mtu yeyote asije akaniona mimi kuwa bora zaidi kuliko ninavyoonekana katika yale ninayotenda na kusema.

  19. 9 Mimi, Yohana, ndugu yenu ninayeshiriki pamoja nanyi mateso katika Yesu na katika ufalme na uvumilivu katika saburi, nilikuwa katika kisiwa cha Patmo kwa ajili ya neno la Mungu na ushuhuda wa Yesu. 10 Katika siku ya Bwana, nilikuwa katika Roho na nikasikia sauti kubwa kama ya baragumu nyuma yangu 11 ikisema, “Andika kwenye kitabu haya yote unayoyaona, kisha uyapeleke kwa makanisa saba, yaani: Efeso, Smirna, Pergamo, Thiatira, Sardi, Filadelfia na Laodikia.”

    12 Ndipo nikageuka ili nione ni sauti ya nani iliyokuwa ikisema nami. Nami nilipogeuka, nikaona vinara saba vya taa vya dhahabu, 13 na katikati ya vile vinara vya taa, alikuwamo mtu kama Mwana wa Adamu, akiwa amevaa joho refu, na mkanda wa dhahabu ukiwa umefungwa kifuani mwake. 14 Kichwa chake na nywele zake zilikuwa nyeupe kama sufu, nyeupe kama theluji, nayo macho yake yalikuwa kama mwali wa moto. 15 Nyayo zake zilikuwa kama shaba inayongʼaa, katika tanuru ya moto, nayo sauti yake ilikuwa kama mugurumo ya maji mengi. 16 Katika mkono wake wa kuume alishika nyota saba, na kinywani mwake ulitoka upanga mkali wenye makali kuwili. Uso wake ulikuwa kama jua likingʼaa kwa nguvu zake zote.

    17 Nilipomwona, nilianguka miguuni pake kama aliyekufa. Ndipo akauweka mkono wake wa kuume juu yangu na kusema: “Usiogope, Mimi ndiye wa Kwanza na wa Mwisho. 18 Mimi ni Yeye Aliye Hai, niliyekuwa nimekufa, na tazama, ni hai milele na milele! Nami ninazo funguo za mauti na kuzimu.

    19 “Basi andika mambo uliyoyaona, yaliyopo na yale yatakayotukia baada ya haya. 20 Kuhusu siri ya zile nyota saba ulizoziona katika mkono wangu wa kuume na vile vinara saba vya taa vya dhahabu ni hii: Zile nyota saba ni malaika wa yale makanisa saba, navyo vile vinara saba ni hayo makanisa saba.

  20. 14 Ndipo Bwana akaniambia, “Manabii wanatabiri uongo kwa jina langu. Sikuwatuma, wala sikuwaweka, wala sikusema nao. Wanawatabiria maono ya uongo, maaguzi, maono ya sanamu zisizofaa kitu, na madanganyo ya mawazo yao wenyewe.

  21. 31 “Ee mfalme, ulitazama, na mbele yako ilisimama sanamu kubwa, kubwa mno kupita kiasi, sanamu iliyongʼaa na kutisha kwa kuonekana kwake. 32 Kichwa cha ile sanamu kilikuwa kimetengenezwa kwa dhahabu safi, kifua chake na mikono yake vilikuwa vya fedha, tumbo lake na mapaja yake vilikuwa vya shaba, 33 miguu yake ilikuwa ya chuma, na nyayo zake zilikuwa chuma nazo sehemu nyingine zilikuwa udongo wa mfinyanzi uliochomwa. 34 Ulipokuwa unaangalia, jiwe lilikatwa, lakini si kwa mikono ya mwanadamu. Lile jiwe liliipiga ile sanamu kwenye nyayo zake za chuma na udongo wa mfinyanzi, na kuivunja. 35 Ndipo ile chuma, ule udongo wa mfinyanzi, ile shaba, ile fedha na ile dhahabu vikavunjika vipande vipande kwa wakati mmoja, na vikawa kama makapi katika sakafu ya kupuria nafaka wakati wa kiangazi. Upepo ukavipeperusha bila kuacha hata alama. Lakini lile jiwe lililoipiga ile sanamu likawa mlima mkubwa mno na kuijaza dunia yote.

    36 “Hii ndiyo iliyokuwa ndoto, nasi sasa tutamfasiria mfalme. 37 Ee mfalme, wewe ni mfalme wa wafalme. Mungu wa mbinguni amekupa wewe utawala, uweza, nguvu na utukufu. 38 Mikononi mwako amewaweka wanadamu, wanyama wa kondeni, na ndege wa angani. Popote waishipo amekufanya wewe kuwa mtawala juu yao wote. Wewe ndiye kile kichwa cha dhahabu.

    39 “Baada yako, ufalme mwingine utainuka, ulio dhaifu kuliko wako. Baadaye utafuata ufalme wa tatu, ule wa shaba, nao utatawala juu ya dunia yote. 40 Hatimaye, kutakuwako na ufalme wa nne, wenye nguvu kama chuma, kwa maana chuma huvunja na kupondaponda kila kitu; kama vile chuma ivunjavyo vitu vipande vipande, ndivyo ufalme huo utakavyopondaponda na kuvunjavunja nyingine zote. 41 Kama vile ulivyoona kuwa kwa sehemu nyayo na vidole vilikuwa vya udongo wa mfinyanzi uliochomwa na kwa sehemu nyingine chuma, hivyo huu utakuwa ufalme uliogawanyika; hata hivyo utakuwa na sehemu zenye nguvu za chuma ndani yake, kama vile ulivyoona chuma imechanganywa na udongo wa mfinyanzi. 42 Kama vile vidole vyake vya miguu vilikuwa kwa sehemu chuma na sehemu udongo wa mfinyanzi, hivyo ufalme huo kwa sehemu utakuwa na nguvu na kwa sehemu udhaifu. 43 Kama vile ulivyoona chuma kikiwa kimechanganyikana na udongo wa mfinyanzi uliochomwa, ndivyo watu watakavyokuwa mchanganyiko, wala hawatabaki wameungana tena, kama vile chuma kisivyoweza kuchanganyikana na udongo wa mfinyanzi.

    44 “Katika siku za wafalme hao, Mungu wa mbinguni atauweka ufalme ambao kamwe hautaangamizwa, wala hautaachiwa taifa jingine. Utaziponda zile falme zote na kuzikomesha, bali wenyewe utadumu milele. 45 Hii ndiyo maana ya maono ya jiwe lililochongwa kutoka mlimani, lakini si kwa mikono ya mwanadamu, lile jiwe ambalo lilivunja chuma, shaba, udongo wa mfinyanzi, fedha na dhahabu vipande vipande.

    “Mungu Mkuu amemwonyesha mfalme kile kitakachotokea wakati ujao. Ndoto hii ni ya kweli na tafsiri yake ni ya kuaminika.”

  22. 9 Malango yake yamezama ardhini,

    makomeo yake ameyavunja na kuyaharibu.

    Mfalme wake na wakuu wake wamepelekwa uhamishoni

    miongoni mwa mataifa,

    sheria haipo tena,

    na manabii wake hawapati tena

    maono kutoka kwa Bwana.

  23. 17 Mungu akawapa hawa vijana wanne maarifa na ufahamu wa kila aina ya maandiko na elimu. Naye Danieli aliweza kufahamu maono na aina zote za ndoto.

  24. 15 Mimi Danieli nilipokuwa ninaangalia maono na kujaribu kuelewa, mbele yangu alisimama mmoja aliyefanana na mwanadamu. 16 Kisha nikasikia sauti ya mwanadamu kutoka Mto Ulai ikiita, “Gabrieli, mwambie mtu huyu maana ya maono haya.”

    17 Alipokuwa akikaribia pale nilipokuwa nimesimama, niliogopa, nikaanguka kifudifudi. Akaniambia, “Mwana wa mwanadamu, fahamu kuwa maono haya yanahusu siku za mwisho.”

    18 Alipokuwa akinena nami, nilikuwa katika usingizi mzito, huku nimelala kifudifudi. Ndipo aliponigusa na kunisimamisha wima.

    19 Akaniambia, “Nitakuambia yale yatakayotokea baadaye wakati wa ghadhabu, kwa sababu maono haya yanahusu wakati wa mwisho ulioamriwa. 20 Kondoo dume mwenye pembe mbili ambaye ulimwona anawakilisha wafalme wa Umedi na Uajemi. 21 Yule beberu mwenye nywele nyingi ni mfalme wa Uyunani, nayo ile pembe ndefu katikati ya macho yake ni mfalme wa kwanza. 22 Zile pembe nne zilizoota badala ya ile pembe iliyovunjika zinawakilisha falme nne ambazo zitatokea kutoka taifa lake, lakini hakuna hata mmoja utakaokuwa na nguvu kama ule uliovunjika.

    23 “Katika sehemu ya mwisho ya utawala wao, wakati waasi watakapokuwa waovu kabisa, atainuka mfalme mwenye uso mkali, aliye stadi wa hila. 24 Atakuwa na nguvu nyingi, lakini si kwa uwezo wake mwenyewe. Atasababisha uharibifu wa kutisha, na atafanikiwa kwa chochote anachofanya. Atawaangamiza watu maarufu na watu watakatifu. 25 Atasababisha udanganyifu ustawi, naye atajihesabu mwenyewe kuwa bora. Wakati wajisikiapo kuwa wako salama, atawaangamiza wengi, na kushindana na Mkuu wa wakuu. Lakini ataangamizwa, isipokuwa si kwa uwezo wa mwanadamu.

    26 “Maono kuhusu jioni na asubuhi ambayo umepewa ni kweli, lakini yatie muhuri maono haya, kwa maana yanahusu wakati mrefu ujao.”

    27 Mimi Danieli nilikuwa nimechoka sana, na nikalala nikiwa mgonjwa kwa siku kadhaa. Ndipo nikaamka, nikaenda kwenye shughuli za mfalme. Nilifadhaishwa na maono hayo, nami sikuweza kuyaelewa.

  25. 22 Isitoshe, baadhi ya wanawake katika kundi letu wametushtusha. Walikwenda kaburini leo alfajiri, 23 lakini hawakuukuta mwili wake. Walirudi wakasema wameona maono ya malaika ambao waliwaambia kwamba Yesu yu hai.

  26. 10 Yakobo akatoka Beer-Sheba kwenda Harani. 11 Alipofika mahali fulani, akalala hapo kwa sababu jua lilikuwa limetua. Akachukua jiwe moja la mahali pale, akaliweka chini ya kichwa chake akajinyoosha akalala usingizi. 12 Akaota ndoto ambayo aliona ngazi imesimamishwa juu ya ardhi, ncha yake ikiwa imefika mbinguni na malaika wa Mungu wakawa wakipanda na kushuka juu yake. 13 Juu yake alisimama Bwana, akasema, “Mimi ni Bwana, Mungu wa baba yako Abrahamu na Mungu wa Isaki. Nchi ambayo umelala juu yake, nitakupa wewe na uzao wako. 14 Uzao wako utakuwa kama mavumbi ya nchi, nawe utaenea upande wa magharibi na mashariki, kaskazini na kusini. Kupitia wewe na uzao wako mataifa yote ya duniani yatabarikiwa. 15 Niko pamoja nawe nami nitakulinda kila uendako na nitakurudisha katika nchi hii. Sitakuacha mpaka nitakapofanya hayo niliyokuahidi.”

    16 Yakobo alipoamka kutoka usingizini, akawaza, “Hakika Bwana yuko mahali hapa, wala mimi sikujua.” 17 Kwa hiyo akaogopa, akasema, “Mahali hapa panatisha kama nini! Bila shaka hapa ndipo nyumba ya Mungu ilipo, hili ni lango la mbinguni.”

  27. 7 Katika siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kumi na moja, yaani mwezi uitwao Shebati, katika mwaka wa pili wa utawala wa Mfalme Dario, neno la Bwana lilimjia nabii Zekaria mwana wa Berekia mwana wa Ido.

    8 Wakati wa usiku nilipata maono, mbele yangu alikuwepo mtu akiendesha farasi mwekundu! Alikuwa amesimama katikati ya miti ya mihadasi kwenye bonde. Nyuma yake walikuwepo farasi wekundu, wa kikahawia na weupe.

    9 Nikauliza, “Hivi ni vitu gani bwana wangu?”

    Malaika aliyekuwa akizungumza na mimi akanijibu, “Nitakuonyesha kuwa ni nini.”

    10 Kisha yule mtu aliyesimama katikati ya miti ya mihadasi akaeleza, “Ni wale ambao Bwana amewatuma waende duniani kote.”

    11 Nao wakatoa taarifa kwa yule malaika wa Bwana, aliyekuwa amesimama katikati ya miti ya mihadasi, “Tumepita duniani kote na kukuta ulimwengu wote umepumzika kwa amani.”

  28. 10 Bwana akaja akasimama hapo, akiita kama mara zile nyingine, “Samweli! Samweli!”

    Kisha Samweli akasema, “Nena Bwana, kwa kuwa mtumishi wako anasikiliza.”

    11 Naye Bwana akamwambia Samweli: “Tazama, nipo karibu kufanya kitu katika Israeli ambacho kitafanya masikio ya kila mmoja atakayesikia yawashe. 12 Wakati huo nitatimiza dhidi ya Eli kila kitu nilichonena dhidi ya jamaa yake, kuanzia mwanzo mpaka mwisho. 13 Kwa kuwa nilimwambia kwamba ningehukumu jamaa yake milele kwa sababu ya dhambi aliyoijua, wanawe kumkufuru Mungu, naye akashindwa kuwazuia. 14 Kwa hiyo, nikaapa kuhusu nyumba ya Eli, ‘Hatia ya nyumba ya Eli kamwe haitaweza kufidiwa kwa dhabihu au sadaka.’ ”

    15 Samweli akalala mpaka asubuhi, kisha akafungua milango ya nyumba ya Bwana. Aliogopa kumwambia Eli yale maono,

  29. 11 Neno la Bwana likanijia kusema, “Je, Yeremia unaona nini?”

    Nami nikajibu, “Naona tawi la mti wa mlozi.”

    12 Bwana akaniambia, “Umeona vyema kwa maana ninaliangalia neno langu ili kuona kwamba limetimizwa.”

    13 Neno la Bwana likanijia tena, “Unaona nini?”

    Nikajibu, “Naona chungu kinachochemka, kikiwa kimeinama kutoka kaskazini.”

    14 Bwana akaniambia, “Kutoka kaskazini maafa yatamwagwa kwa wote waishio katika nchi. 15 Nitawaita watu wote wa falme za kaskazini,” asema Bwana.

    “Wafalme wao watakuja na kuweka viti vyao vya enzi

    katika maingilio ya malango ya Yerusalemu,

    watakuja dhidi ya kuta zake zote zinazouzunguka,

    na dhidi ya miji yote ya Yuda.

    16 Nitatoa hukumu zangu kwa watu wangu

    kwa sababu ya uovu wao wa kuniacha mimi,

    kwa kufukiza uvumba kwa miungu mingine

    na kuabudu kile ambacho mikono yao imekitengeneza.

  30. 5 Wakati wa Herode mfalme wa Uyahudi, palikuwa na kuhani mmoja jina lake Zekaria, ambaye alikuwa wa ukoo wa kikuhani wa Abiya. Elizabeti mkewe alikuwa pia mzao wa Aroni. 6 Zekaria na Elizabeti mkewe wote walikuwa watu wanyofu mbele za Mungu, wakizishika amri zote za Bwana na maagizo yote bila lawama. 7 Lakini walikuwa hawana watoto, kwa sababu Elizabeti alikuwa tasa; nao wote wawili walikuwa wazee sana.

    8 Siku moja ilipokuwa zamu ya kikundi cha Zekaria, yeye akifanya kazi ya ukuhani Hekaluni mbele za Mungu, 9 alichaguliwa kwa kura kwa kufuata desturi za ukuhani, kuingia Hekaluni mwa Bwana ili kufukiza uvumba. 10 Nao wakati wa kufukiza uvumba ulipowadia, wale wote waliokuwa wamekusanyika ili kuabudu walikuwa nje wakiomba.

    11 Ndipo malaika wa Bwana, akiwa amesimama upande wa kuume wa madhabahu ya kufukizia uvumba, akamtokea Zekaria. 12 Zekaria alipomwona huyo malaika, akafadhaika sana, akajawa na hofu. 13 Lakini malaika akamwambia, “Usiogope, Zekaria, kwa maana Mungu amesikia maombi yako. Mkeo Elizabeti atakuzalia mtoto wa kiume, nawe utamwita jina lake Yohana. 14 Yeye atakuwa furaha na shangwe kwako, nao watu wengi watashangilia kwa sababu ya kuzaliwa kwake. 15 Kwa kuwa atakuwa mkuu mbele za Bwana, kamwe hataonja mvinyo wala kinywaji chochote cha kulevya, naye atajazwa Roho Mtakatifu hata kabla ya kuzaliwa kwake. 16 Naye atawageuza wengi wa wana wa Israeli warudi kwa Bwana Mungu wao. 17 Naye atatangulia mbele za Bwana katika roho na nguvu ya Eliya, ili kuigeuza mioyo ya baba kuwaelekea watoto wao, na wasiotii warejee katika hekima ya wenye haki, ili kuliweka tayari taifa lililoandaliwa kwa ajili ya Bwana.”

    18 Zekaria akamuuliza malaika, “Jambo hilo linawezekanaje? Mimi ni mzee na mke wangu pia ana umri mkubwa.”

    19 Malaika akamjibu, akamwambia, “Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele za Mungu, nami nimetumwa kwako ili nikuambie habari hizi njema. 20 Basi sasa kwa kuwa hujaamini maneno yangu ambayo yatatimizwa kwa wakati wake, utakuwa bubu hadi siku ile mambo haya yatakapotukia.”

    21 Wakati huo watu walikuwa wanamngojea Zekaria nje huku wakishangaa kukawia kwake mle Hekaluni. 22 Alipotoka akawa hawezi kusema nao, wao wakatambua kuwa ameona maono ndani ya Hekalu. Lakini kwa kuwa alikuwa bubu, akawa anawaashiria kwa mikono.

    23 Muda wake wa kuhudumu Hekaluni ulipomalizika, akarudi nyumbani kwake. 24 Baada ya muda usio mrefu, Elizabeti mkewe akapata mimba, naye akajitenga kwa miezi mitano.

    25 Akasema, “Hili ndilo Bwana alilonitendea aliponiangalia kwa upendeleo na kuniondolea aibu yangu mbele ya watu.”

  31. 14 Kwa kuwa Mungu husema, wakati huu kwa njia moja,

    au wakati mwingine kwa njia nyingine,

    ingawa mwanadamu anaweza asielewe.

    15 Mungu husema na mwanadamu katika ndoto,

    katika maono ya usiku,

    wakati usingizi mzito uwaangukiapo

    wanadamu wasinziapo vitandani mwao,

    16 anaweza akasemea masikioni mwao,

    na kuwatia hofu kwa maonyo,

    17 ili kumgeuza mtu kutoka kwenye kutenda mabaya

    na kumwepusha na kiburi,

    18 kuiokoa nafsi yake na shimo,

    uhai wake usiangamizwe kwa upanga.

  32. 12 Nao wakiisha kuonywa katika ndoto wasirudi kwa Herode, wakarudi kwenda katika nchi yao kwa njia nyingine.

    13 Walipokwisha kwenda zao, malaika wa Bwana akamtokea Yosefu katika ndoto akamwambia, “Ondoka, mchukue mtoto na mama yake mkimbilie Misri. Kaeni huko mpaka nitakapowaambia, kwa maana Herode anataka kumtafuta huyu mtoto ili amuue.”

  33. 1 Malaika wa tano akaipiga tarumbeta yake, nami nikaona nyota iliyokuwa imeanguka toka angani hadi ardhini. Nyota hiyo ilipewa ufunguo wa lile Shimo. 2 Alipolifungua hilo Shimo, moshi ukapanda kutoka humo kama moshi wa tanuru kubwa sana. Jua na anga vikatiwa giza na ule moshi uliotoka katika hilo Shimo. 3 Ndipo katika ule moshi wakatoka nzige wakaenda juu ya nchi, nao wakapewa nguvu kama zile za nge wa duniani. 4 Wakaambiwa wasidhuru nyasi ya nchi, wala mmea wala mti wowote, bali wawadhuru tu wale watu ambao hawana muhuri wa Mungu kwenye vipaji vya nyuso zao. 5 Wakaruhusiwa kuwatesa kwa muda wa miezi mitano, lakini wasiwaue. Uchungu wa kuuma kwao ulikuwa kama ule wa mtu aumwapo na nge. 6 Katika siku hizo watu watatafuta kifo lakini hawatakiona, watatamani kufa, lakini kifo kitawakimbia.

    7 Wale nzige walikuwa na umbo kama la farasi waliotayarishwa kwa ajili ya vita. Kwenye vichwa vyao kulikuwa na kitu kama taji za dhahabu na nyuso zao zilikuwa kama za binadamu. 8 Walikuwa na nywele kama za wanawake, na meno yao yalikuwa kama ya simba. 9 Walikuwa na dirii kama za chuma, na sauti za mabawa yao zilikuwa kama ngurumo za farasi wengi na magari mengi yakikimbilia vitani. 10 Walikuwa na mikia yenye miiba ya kuumia kama nge. Nguvu yao ya kutesa watu kwa huo muda wa miezi mitano ilikuwa katika hiyo mikia yao. 11 Walikuwa na mfalme wao, ambaye ni malaika wa lile Shimo, ambaye jina lake kwa Kiebrania ni Abadoni, na kwa Kiyunani ni Apolioni.

    12 Ole ya kwanza imepita, bado nyingine mbili zinakuja.

    13 Malaika wa sita akaipiga tarumbeta yake, nami nikasikia sauti ikitoka katika zile pembe za madhabahu ya dhahabu iliyoko mbele za Mungu. 14 Ile sauti ikamwambia yule malaika wa sita mwenye tarumbeta, “Wafungulie wale malaika wanne waliofungwa kwenye ule mto mkubwa Frati.” 15 Basi wale malaika wanne, waliokuwa wamewekwa tayari kwa ajili ya saa hiyo, na siku hiyo, na mwezi huo, na mwaka huo ili wawaue theluthi ya wanadamu wakafunguliwa. 16 Idadi ya majeshi wapanda farasi ilikuwa 200,000,000. Nilisikia idadi yao.

    17 Hivi ndivyo nilivyowaona hao farasi na wapanda farasi katika maono yangu: Wapanda farasi walivaa dirii vifuani zenye rangi nyekundu sana kama ya moto na yakuti samawi na kiberiti. Vichwa vya hao farasi vilikuwa kama vichwa vya simba, na moto, moshi na kiberiti vilitoka vinywani mwao. 18 Theluthi ya wanadamu wakauawa kwa mapigo hayo matatu, yaani, huo moto, moshi na kiberiti, vilivyotoka kwenye vinywa vya hao farasi. 19 Nguvu za hao farasi zilikuwa katika vinywa vyao na kwenye mikia yao, kwa sababu mikia yao ilikuwa kama nyoka, yenye vichwa ambayo waliitumia kudhuru.

    20 Wanadamu waliosalia, ambao hawakuuawa katika mapigo hayo, bado walikataa kutubia kazi za mikono yao na hawakuacha kuabudu mashetani na sanamu za dhahabu, za fedha, za shaba, za mawe na za miti, ambazo haziwezi kuona, kusikia wala kutembea. 21 Wala hawakutubu na kuacha matendo yao ya uuaji, uchawi, uasherati wala wizi wao.

  34. 11 Kisha nikaona mbingu imefunguka na hapo mbele yangu akiwepo farasi mweupe, ambaye yeye aliyempanda aliitwa Mwaminifu na Kweli. Yeye huhukumu kwa haki na kufanya vita. 12 Macho yake ni kama miali ya moto na juu ya kichwa chake kuna taji nyingi. Ana jina lililoandikwa ambalo hakuna mtu yeyote anayelijua isipokuwa yeye mwenyewe. 13 Amevaa joho lililochoviwa katika damu, na Jina lake ni “Neno la Mungu.” 14 Majeshi ya mbinguni walikuwa wakimfuata, wakiwa wamepanda farasi weupe, hali wamevaa mavazi ya kitani safi, nyeupe na nzuri. 15 Kinywani mwake hutoka upanga mkali ambao kwa huo atayaangusha mataifa. “Atayatawala kwa fimbo yake ya utawala ya chuma.” Hulikanyaga shinikizo la mvinyo wa ghadhabu ya Mungu Mwenyezi. 16 Kwenye joho lake na paja lake pameandikwa jina hili:

    Mfalme wa wafalme, na Bwana wa mabwana.

    17 Nami nikamwona malaika amesimama ndani kwenye jua, akaita ndege wote warukao angani kwa sauti kuu, “Njooni, kusanyikeni kwa ajili ya karamu kubwa ya Mungu, 18 ili mpate kula nyama ya wafalme na ya majemadari, ya mashujaa, ya farasi na ya wapanda farasi, nyama ya wanadamu, wote walio huru na watumwa, wadogo na wakubwa.”

    19 Kisha nikamwona yule mnyama na wafalme wa dunia pamoja na majeshi yao wakiwa wamekusanyika pamoja ili kufanya vita dhidi ya yule aliyempanda farasi pamoja na jeshi lake. 20 Lakini yule mnyama akakamatwa pamoja na huyo nabii wa uongo ambaye alikuwa amefanya ishara kwa niaba ya huyo mnyama, ambaye kwa ishara hizi aliwadanganya wale waliopokea chapa ya huyo mnyama na kuiabudu sanamu yake. Hawa wawili wakatupwa wakiwa hai ndani ya ziwa la moto liwakalo kwa kiberiti. 21 Wale waliosalia waliuawa kwa upanga uliotoka kinywani mwa yule aliyekuwa amempanda farasi nao ndege wote wakajishibisha kwa nyama yao.

  35. 13 “Katika maono yangu ya usiku nilitazama, na mbele yangu nikamwona anayefanana na mwanadamu, akija pamoja na mawingu ya mbinguni. Akamkaribia huyo Mzee wa Siku, na akaongozwa mbele zake. 14 Akapewa mamlaka, utukufu na ufalme wenye nguvu; nao watu wa kabila zote, mataifa, na watu wa kila lugha wakamwabudu. Utawala wake ni utawala wa milele ambao hautapita, nao ufalme wake ni ule ambao kamwe hautaangamizwa.

    15 “Mimi, Danieli, nilipata mahangaiko rohoni, nayo maono yale yaliyopita ndani ya mawazo yangu yalinisumbua. 16 Nikamkaribia mmoja wa wale waliosimama pale na kumuuliza maana halisi ya haya yote.

    “Basi akaniambia na kunipa tafsiri ya vitu hivi: 17 ‘Hao wanyama wanne wakubwa ni falme nne zitakazoinuka duniani. 18 Lakini watakatifu wa Yeye Aliye Juu Sana watapokea ufalme na kuumiliki milele: naam, milele na milele.’

    19 “Kisha nilitaka kufahamu maana ya kweli ya mnyama yule wa nne, ambaye alikuwa tofauti na wale wengine wote, tena wa kutisha sana, na meno yake ya chuma na makucha ya shaba: mnyama ambaye alipondaponda na kuangamiza wahanga wake, na kukanyaga chochote kilichosalia. 20 Pia mimi nilitaka kujua kuhusu zile pembe kumi juu ya kichwa chake, na pia kuhusu ile pembe nyingine iliyojitokeza, ambayo mbele yake zile tatu za mwanzoni zilianguka, ile pembe ambayo ilionekana kuvutia macho zaidi kuliko zile nyingine, na ambayo ilikuwa na macho na kinywa kilichonena kwa majivuno. 21 Nilipoendelea kutazama, pembe hii ilikuwa inapigana vita dhidi ya watakatifu na kuwashinda, 22 mpaka huyo Mzee wa Siku alipokuja na kutamka hukumu kwa kuwapa ushindi watakatifu wa Yeye Aliye Juu Sana, na wakati ukawadia walipoumiliki ufalme.

    23 “Alinipa maelezo haya: ‘Mnyama wa nne ni ufalme wa nne ambao utatokea duniani. Utakuwa tofauti na falme nyingine zote, nao utaharibu dunia nzima, ukiikanyaga chini na kuipondaponda. 24 Zile pembe kumi ni wafalme kumi watakaotokana na ufalme huu. Baada yao mfalme mwingine atainuka, ambaye atakuwa tofauti na wale waliotangulia, naye atawaangusha wafalme watatu. 25 Atanena maneno kinyume cha Yeye Aliye Juu Sana na kuwaonea watakatifu wake, huku akijaribu kubadili majira na sheria. Watakatifu watatiwa chini ya mamlaka yake kwa wakati, nyakati mbili, na nusu wakati.

    26 “ ‘Lakini mahakama itakaa kuhukumu, nayo mamlaka yake yataondolewa na kuangamizwa kabisa milele. 27 Ndipo ufalme, mamlaka na ukuu wa falme chini ya mbingu yote utakabidhiwa kwa watakatifu, watu wa Yeye Aliye Juu Sana. Ufalme wake utakuwa ufalme wa milele, nao watawala wote watamwabudu na kumtii yeye.’

    28 “Huu ndio mwisho wa jambo lile. Mimi Danieli nilitaabika sana katika mawazo yangu, nao uso wangu ukabadilika, lakini nililiweka jambo hilo moyoni mwangu.”

  36. 7 Hili ndilo alilonionyesha katika maono: Bwana alikuwa amesimama karibu na ukuta ambao ulikuwa umejengwa kwa timazi, akiwa na uzi wa timazi mkononi mwake. 8 Naye Bwana akaniuliza, “Je, Amosi unaona nini?”

    Nikamjibu, “Uzi wa timazi.”

    Kisha Bwana akasema, “Tazama, ninaweka uzi wa timazi miongoni mwa watu wangu Israeli; sitawahurumia tena.

    9 “Mahali pa Isaki pa juu pa kuabudia miungu pataangamizwa,

    na mahali patakatifu pa Israeli pa kuabudia pataharibiwa;

    kwa upanga wangu nitainuka

    dhidi ya nyumba ya Yeroboamu.”

  37. 1 Nilimwona Bwana akiwa amesimama kando ya madhabahu, naye akasema:

    “Piga vichwa vya nguzo

    ili vizingiti vitikisike.

    Viangushe juu ya vichwa vya watu wote;

    na wale watakaosalia nitawaua kwa upanga.

    Hakuna awaye yote atakayekimbia,

    hakuna atakayetoroka.

  38. 18 Basi Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi: Maria mama yake alikuwa ameposwa na Yosefu, lakini kabla hawajakutana kimwili, Maria alionekana kuwa na mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu. 19 Kwa kuwa Yosefu, mwanaume aliyekuwa amemposa alikuwa mtu mwadilifu, hakutaka kumwaibisha Maria hadharani, aliazimu kumwacha kwa siri.

    20 Lakini mara alipoazimu kufanya jambo hili, malaika wa Bwana akamtokea katika ndoto na kusema, “Yosefu mwana wa Daudi, usiogope kumchukua Maria awe mke wako, kwa maana mimba aliyo nayo ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu. 21 Naye atamzaa mwana, nawe utamwita Jina lake Yesu, kwa maana yeye ndiye atakayewaokoa watu wake kutoka dhambi zao.”

    22 Haya yote yalitukia ili litimie lile Bwana alilokuwa amenena kupitia nabii, akisema: 23 “Tazama, bikira atachukua mimba, naye atamzaa mwana, nao watamwita Jina lake Imanueli”: maana yake, “Mungu pamoja nasi.”

    24 Yosefu alipoamka kutoka usingizini, akafanya kama vile alivyoagizwa na malaika wa Bwana, akamchukua Maria kuwa mke wake. 25 Lakini hawakukutana kimwili mpaka Maria alipojifungua mwanawe kifungua mimba akamwita Jina lake Yesu.

  39. 5 Akamtafuta Mungu katika siku za Zekaria, aliyemwelekeza kumcha Mungu. Wakati wote alipomtafuta Bwana, Mungu alimfanikisha.

  40. 24 Roho akaniinua na kunileta mpaka kwa watu wa uhamisho huko Ukaldayo nikiwa katika yale maono niliyopewa na Roho wa Mungu.

    Ndipo maono niliyokuwa nimeyaona yakanitoka, 25 nami nikawaeleza wale watu wa uhamisho kila kitu Bwana alichokuwa amenionyesha.

  41. 5 Niliota ndoto iliyoniogopesha. Nilipokuwa nimelala kitandani mwangu, njozi na maono yaliyopita mawazoni mwangu vilinitisha.

  42. 1 Katika mwaka wa tatu wa utawala wa Mfalme Belshaza, mimi Danieli, nilipata maono, baada ya maono ambayo yalikuwa yamenitokea mbeleni. 2 Katika maono yangu, nilijiona nikiwa ndani ya ngome ya Shushani katika jimbo la Elamu. Katika maono nilikuwa kando ya Mto Ulai. 3 Nikatazama juu, na hapo mbele yangu kulikuwa na kondoo dume mwenye pembe mbili, akiwa amesimama kando ya mto, nazo pembe zake zilikuwa ndefu. Pembe moja ilikuwa ndefu kuliko hiyo nyingine, lakini iliendelea kukua baadaye. 4 Nikamtazama yule kondoo dume alivyokuwa akishambulia kuelekea magharibi, kaskazini na kusini. Hakuna mnyama yeyote aliyeweza kusimama dhidi yake, wala hakuna aliyeweza kuokoa kutoka nguvu zake. Alifanya kama atakavyo, naye akawa mkuu.

    5 Nilipokuwa ninatafakari hili, ghafula beberu mwenye pembe moja kubwa sana katikati ya macho yake alikuja kutoka magharibi, akiruka kasi juu ya dunia yote bila kugusa ardhi. 6 Alikuja akimwelekea yule kondoo dume mwenye pembe mbili niliyemwona akisimama kando ya mto, akamshambulia kwa hasira nyingi. 7 Nikamwona akimshambulia yule kondoo dume kwa hasira nyingi, akimpiga yule kondoo dume na kuvunja pembe zake mbili. Yule kondoo dume hakuwa na nguvu za kumzuia yule beberu, hivyo akamwangusha yule kondoo dume chini na kumkanyaga, wala hakuna aliyeweza kumwokoa yule kondoo dume kutoka nguvu za huyo beberu. 8 Yule beberu akawa mkubwa sana, lakini katika kilele cha nguvu zake ile pembe yake ndefu ilivunjika, na mahali pake pakaota pembe nne kubwa kuelekea pande nne za dunia.

    9 Kutoka mojawapo ya zile pembe nne palitokea pembe ndogo ukaongezeka nguvu kuelekea kusini, na kuelekea mashariki, na kuelekea Nchi ya Kupendeza. 10 Pembe hiyo ikaendelea kukua hadi kufikia jeshi la mbinguni, nayo ikalitupa baadhi ya jeshi la vitu vya angani hapa chini duniani, na kulikanyaga. 11 Pembe hiyo ikajikweza ili iwe kama Mkuu wa hilo jeshi; ikamwondolea dhabihu ya kila siku, napo mahali pake patakatifu pakashushwa chini. 12 Kwa sababu ya uasi, jeshi la watakatifu na dhabihu za kila siku vikatiwa mikononi mwake. Ikafanikiwa katika kila kitu ilichofanya, nayo kweli ikatupwa chini.

    13 Kisha nikamsikia mtakatifu mmoja akizungumza na mtakatifu mwingine, akamwambia, “Je, itachukua muda gani maono haya yatimie: maono kuhusu dhabihu ya kila siku, uasi unaosababisha ukiwa, kutwaliwa kwa mahali patakatifu, na jeshi litakalokanyagwa chini ya nyayo?”

    14 Akaniambia, “Itachukua siku 2,300. Ndipo mahali patakatifu patawekwa wakfu tena.”

  43. 1 Hili ndilo alilonionyesha Bwana Mwenyezi katika maono: kikapu cha matunda yaliyoiva. 2 Akaniuliza, “Amosi, unaona nini?”

    Nikajibu, “Kikapu chenye matunda yaliyoiva.”

    Ndipo Bwana akaniambia, “Wakati umewadia kwa watu wangu Israeli; sitawahurumia zaidi.”

    3 Bwana Mwenyezi asema, “Katika siku ile, nyimbo katika Hekalu zitageuka kuwa maombolezo. Miili mingi, mingi sana: itatupwa kila mahali! Kimya!”

    4 Lisikieni hili, ninyi ambao mnawagandamiza wahitaji,

    na kuwaonea maskini wa nchi,

    5 mkisema,

    “Ni lini Mwezi Mwandamo utakapopita

    ili tupate kuuza nafaka,

    na Sabato itakwisha lini

    ili tuweze kuuza ngano?”

    Mkipunguza vipimo,

    na kuongeza bei,

    na kudanganya kwa mizani zisizo sawa,

    6 mkiwanunua maskini kwa fedha,

    na wahitaji kwa jozi ya viatu,

    na mkiuza hata takataka za ngano

    pamoja na ngano.

  44. 1 Neno alilosema Mungu kuhusu Ninawi. Kitabu cha maono cha Nahumu, Mwelkoshi.

  45. 1 Kisha akanionyesha Yoshua, kuhani mkuu, akiwa amesimama mbele ya malaika wa Bwana, naye Shetani amesimama upande wake wa kuume ili amshtaki. 2 Bwana akamwambia Shetani, “Bwana akukemee Shetani! Bwana, ambaye ameichagua Yerusalemu, akukemee! Je, mtu huyu siyo kijinga kinachowaka kilichonyakuliwa kwenye moto?”

    3 Wakati huu, Yoshua alikuwa amevaa nguo chafu alipokuwa amesimama mbele ya malaika. 4 Malaika akawaambia wale waliokuwa wamesimama mbele yake, “Mvueni hizo nguo zake chafu.”

    Kisha akamwambia Yoshua, “Tazama, nimeiondoa dhambi yako, nami nitakuvika mavazi ya kitajiri.”

    5 Kisha nikasema, “Mvike kilemba kilicho safi kichwani mwake.” Kwa hiyo wakamvika kilemba safi kichwani na kumvika yale mavazi mengine, wakati malaika wa Bwana akiwa amesimama karibu.

  46. 5 “Nilikuwa katika mji wa Yafa nikiomba, nami nikapitiwa na usingizi wa ghafula, nikaona maono. Kulikuwa na kitu kama nguo kubwa ikishuka kutoka mbinguni, ikishushwa kwa ncha zake nne, nayo ikanikaribia. 6 Nilipoangalia ndani yake kwa karibu niliona wanyama wenye miguu minne wa nchini, wanyama wa mwitu, watambaao na ndege wa angani. 7 Ndipo nikasikia sauti ikiniambia, ‘Petro, ondoka uchinje na ule.’

    8 “Nikajibu, ‘La hasha Bwana! Kitu chochote kilicho najisi hakijaingia kinywani mwangu.’

    9 “Sauti ikasema kutoka mbinguni mara ya pili, ‘Usikiite najisi kitu chochote Mungu alichokitakasa.’ 10 Jambo hili lilitokea mara tatu, ndipo kile kitu kikavutwa tena mbinguni.

    11 “Wakati ule ule watu watatu, waliokuwa wametumwa kutoka Kaisaria waliwasili katika nyumba niliyokuwa nikikaa. 12 Roho Mtakatifu akaniambia niende nao bila kuwa na ubaguzi kati yao na sisi. Hawa ndugu sita pia walifuatana nami, nasi tukaingia nyumbani mwa huyo Kornelio. 13 Akatuambia jinsi alivyoona malaika aliyekuwa amesimama katika nyumba yake na kusema, ‘Tuma watu waende Yafa wakamlete Simoni aitwaye Petro. 14 Yeye atakupa ujumbe ambao kwa huo wewe na wa nyumbani mwako wote mtaokoka.’

    15 “Nami nilipoanza kusema, Roho Mtakatifu akashuka juu yao kama vile alivyotushukia sisi hapo mwanzo. 16 Nami nikakumbuka neno la Bwana alivyosema, ‘Yohana alibatiza kwa maji, lakini ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu.’ 17 Basi ikiwa Mungu aliwapa hawa watu kipawa kile kile alichotupa sisi tuliomwamini Bwana Yesu Kristo, mimi ni nani hata nifikirie kuwa ningeweza kumpinga Mungu?”

    18 Waliposikia haya hawakuwa na la kupinga zaidi. Nao wakamwadhimisha Mungu wakisema, “Basi, Mungu amewapa hata watu wa Mataifa toba iletayo uzima wa milele.”

  47. 17 “Baada ya kurudi Yerusalemu, nilipokuwa ninaomba Hekaluni, nilipitiwa na usingizi wa ghafula 18 nikamwona Bwana akiniambia, ‘Harakisha utoke Yerusalemu upesi, maana hawataukubali ushuhuda wako kunihusu mimi.’

    19 “Nami nikasema, ‘Bwana, wao wenyewe wanajua jinsi nilivyokwenda kwenye kila sinagogi ili kuwatupa gerezani na kuwapiga wale waliokuamini. 20 Wakati damu ya shahidi wako Stefano ilipomwagwa, mimi mwenyewe nilikuwa nimesimama kando, nikikubaliana na kitendo hicho na kutunza mavazi ya wale waliomuua.’

    21 “Ndipo Bwana akaniambia, ‘Nenda, kwa maana nitakutuma mbali, kwa watu wa Mataifa.’ ”

  48. 3 Lakini Mungu akamjia Abimeleki katika ndoto wakati wa usiku na kumwambia, “Wewe ni kama mfu kwa sababu ya huyu mwanamke uliyemchukua; yeye ni mke wa mtu.”

    4 Wakati huo Abimeleki alikuwa bado hajamsogelea, kwa hiyo akasema, “Je, Bwana utaliharibu taifa lisilo na hatia? 5 Hakusema kwangu, ‘Huyu ni dada yangu,’ naye Sara pia hakusema, ‘Huyu ni kaka yangu’? Nimefanya haya kwa dhamiri njema na mikono safi.”

    6 Kisha Mungu akamwambia katika ndoto, “Ndiyo, najua ya kwamba umefanya haya kwa dhamiri safi, kwa hiyo nimekuzuia usinitende dhambi. Ndiyo sababu sikukuacha umguse. 7 Sasa umrudishe huyo mke wa mtu, kwa maana ni nabii, naye atakuombea nawe utaishi. Lakini kama hutamrudisha, ujue kwa hakika kuwa wewe na watu wako wote mtakufa.”

    8 Kesho yake asubuhi na mapema Abimeleki akawaita maafisa wake wote, na baada ya kuwaambia yote yaliyotokea, waliogopa sana.

  49. 2 Huko malaika wa Bwana akamtokea Mose katika mwali wa moto kutoka kichakani. Mose akaona kwamba ingawa kile kichaka kilikuwa kinawaka moto, kilikuwa hakiteketei. 3 Ndipo Mose akawaza, “Nitageuka sasa nione kitu hiki cha ajabu, nami nione ni kwa nini kichaka hiki hakiteketei.”

  50. 9 Mose na Aroni, Nadabu na Abihu, pamoja na wazee sabini wa Israeli wakapanda mlimani, 10 nao wakamwona Mungu wa Israeli. Chini ya miguu yake kulikuwa na kitu kama sakafu ya mawe ya yakuti samawi, iliyo safi kama anga angavu. 11 Lakini Mungu hakuinua mkono wake dhidi ya hawa viongozi wa Waisraeli; walimwona Mungu, nao wakala na kunywa.

  51. 1 Kama nabii, au yule anayetabiri kwa njia ya ndoto, akijitokeza miongoni mwenu na akawatangazia ishara ya miujiza na ajabu, 2 ikiwa ishara au ajabu ya aliyozungumza ikatokea, naye akasema, “Na tufuate miungu mingine” (miungu ambayo hamjaifahamu) “na tuiabudu,” 3 kamwe msiyasikilize maneno ya nabii wala mwota ndoto huyo. Bwana Mungu wenu anawajaribu kuangalia kama mnampenda kwa moyo wenu wote na kwa roho yenu yote. 4 Ni Bwana Mungu wenu ambaye mnapaswa kumfuata tena ni yeye mnapaswa kumheshimu. Shikeni maagizo yake na kumtii, mtumikieni na kushikamana naye. 5 Huyo nabii au mwota ndoto lazima auawe, kwa sababu amehubiri uasi dhidi ya Bwana Mungu wenu, ambaye aliwatoa kutoka nchi ya Misri na kuwakomboa kutoka nchi ya utumwa; amejaribu kuwageuza kutoka njia ambayo Bwana Mungu wenu aliwaagiza mfuate. Ni lazima mwondoe uovu miongoni mwenu.

  52. 5 Bwana akamtokea Solomoni huko Gibeoni wakati wa usiku katika ndoto, naye Mungu akasema, “Omba lolote utakalo nikupe.”

    6 Solomoni akajibu, “Umemfanyia mtumishi wako, baba yangu Daudi, fadhili nyingi, kwa kuwa alikuwa mwaminifu kwako na mwenye haki, tena mnyofu wa moyo. Nawe umemzidishia fadhili hii kuu kwani umempa mwana wa kuketi kwenye kiti chake cha ufalme, kama ilivyo leo.

    7 “Sasa, Ee Bwana Mungu wangu, umemfanya mtumishi wako mfalme badala ya baba yangu Daudi. Lakini mimi ni mtoto mdogo tu, wala sijui jinsi ya kutekeleza wajibu wangu. 8 Mtumishi wako yuko hapa miongoni mwa watu uliowachagua: taifa kubwa, watu wengi wasioweza kuhesabika wala kutoa idadi yao. 9 Hivyo mpe mtumishi wako moyo wa ufahamu ili kutawala watu wako na kupambanua kati ya mema na mabaya. Kwa maana, ni nani awezaye kutawala watu wako hawa walio wengi hivi?”

    10 Bwana akapendezwa kwamba Solomoni ameliomba jambo hili. 11 Basi Mungu akamwambia, “Kwa kuwa umeomba neno hili na hukuomba maisha marefu au upate utajiri kwa nafsi yako, wala adui zako wafe, bali umeomba ufahamu katika kutoa haki, 12 nitafanya lile uliloomba. Nitakupa moyo wa hekima na wa ufahamu, kiasi kwamba hajakuwepo mtu mwingine kama wewe, wala kamwe hatakuwepo baada yako. 13 Zaidi ya hayo, nitakupa yale ambayo hukuomba, yaani utajiri na heshima, ili kwamba maisha yako yote hapatakuwa na mtu kama wewe miongoni mwa wafalme. 14 Nawe kama ukienenda katika njia zangu na kutii sheria na amri zangu kama baba yako Daudi alivyofanya, nitakupa maisha marefu.” 15 Ndipo Solomoni akaamka, akatambua kuwa ilikuwa ndoto.

    Akarudi Yerusalemu, akasimama mbele ya Sanduku la Agano la Bwana, naye akatoa dhabihu za kuteketezwa na sadaka za amani. Kisha akawafanyia watumishi wake wote karamu.

  53. 16 Nabii akajibu, “Usiogope. Wale walio pamoja nasi ni wengi zaidi kuliko wale walio pamoja nao.”

    17 Kisha Elisha akaomba, “Ee Bwana, mfumbue macho huyu mtumishi ili apate kuona.” Ndipo Bwana akayafumbua macho ya yule mtumishi, naye akatazama na kuona vilima vimejaa farasi na magari ya moto, yamemzunguka Elisha pande zote.

  54. 21 Neno la Bwana likanijia kusema: 22 “Mwanadamu, ni nini hii mithali mlio nayo katika nchi ya Israeli: ‘Siku zinapita na hakuna maono yoyote yanayotimia?’ 23 Waambie, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Nitaikomesha mithali hii, nao hawataitumia tena katika Israeli.’ Waambie, ‘Siku zimekaribia wakati kila maono yatakapotimizwa. 24 Kwa maana hapatakuwepo tena na maono ya uongo wala ubashiri wa udanganyifu miongoni mwa watu wa Israeli. 25 Lakini Mimi Bwana nitasema neno nitakalo, nalo litatimizwa bila kuchelewa. Kwa maana katika siku zako, wewe nyumba ya kuasi, nitatimiza kila nisemalo, asema Bwana Mwenyezi.’ ”

  55. 6 Maono yao ni ya uongo na ubashiri wao ni wa udanganyifu. Wao husema, “Bwana amesema,” wakati Bwana hakuwatuma, bado wakitarajia maneno yao kutimizwa. 7 Je, hamjaona maono ya uongo na kusema ubashiri wa udanganyifu hapo msemapo, “Bwana asema,” lakini Mimi sijasema?

    8 “ ‘Kwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Kwa sababu ya uongo wa maneno yenu na kwa madanganyo ya maono yenu, Mimi ni kinyume na ninyi, asema Bwana Mwenyezi. 9 Mkono wangu utakuwa dhidi ya manabii ambao huona maono ya uongo na kusema ubashiri wa udanganyifu. Hawatakuwa katika baraza la watu wangu au kuandikwa katika kumbukumbu ya nyumba ya Israeli wala hawataingia katika nchi ya Israeli. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Bwana Mwenyezi.

  56. 1 Nikatazama tena: na hapo mbele yangu kulikuwa na kitabu kilichoruka!

    2 Akaniuliza, “Unaona nini?”

    Nikamjibu, “Naona kitabu kinachoruka chenye, urefu wa dhiraa ishirini na upana wa dhiraa kumi.”

    3 Akaniambia, “Hii ni laana inayotoka kwenda juu ya nchi yote, kwa kuwa kufuatana na yale yaliyoandikwa katika upande mmoja, kila mwizi atafukuziwa mbali, pia kufuatana na yaliyo upande wa pili, kila aapaye kwa uongo atafukuziwa mbali. 4 Bwana Mwenye Nguvu Zote asema, ‘Nitaituma hiyo laana, nayo itaingia katika nyumba ya mwizi na nyumba ya huyo aapaye kwa uongo kwa Jina langu. Itabaki katika nyumba yake na kuiharibu, pamoja na mbao zake na mawe yake.’ ”

  57. 3 Yesu alipokuwa ameketi kwenye Mlima wa Mizeituni, wanafunzi wake wakamjia faraghani, wakamuuliza, “Tuambie, mambo haya yatatukia lini, nayo dalili ya kuja kwako na ya mwisho wa dunia ni gani?”

    4 Yesu akawajibu, “Jihadharini, mtu yeyote asiwadanganye. 5 Kwa maana wengi watakuja kwa Jina langu, wakidai, ‘Mimi ndiye Kristo,’ nao watawadanganya wengi. 6 Mtasikia habari za vita na matetesi ya vita. Angalieni msitishike, kwa maana haya hayana budi kutukia. Lakini ule mwisho bado. 7 Taifa litainuka dhidi ya taifa, na ufalme dhidi ya ufalme. Kutakuwa na njaa na mitetemeko ya ardhi sehemu mbalimbali. 8 Haya yote yatakuwa ndio mwanzo wa utungu.

    9 “Ndipo mtasalitiwa, ili mteswe na kuuawa, nanyi mtachukiwa na mataifa yote kwa ajili yangu. 10 Wakati huo, wengi wataacha imani yao, nao watasalitiana kila mmoja na mwenzake na kuchukiana. 11 Watatokea manabii wengi wa uongo, nao watawadanganya watu wengi. 12 Kwa sababu ya kuongezeka kwa uovu upendo wa watu wengi utapoa, 13 lakini yule atakayevumilia hadi mwisho ataokolewa. 14 Injili ya Ufalme itahubiriwa ulimwenguni kote kuwa ushuhuda kwa mataifa yote. Ndipo mwisho utakapokuja.

  58. 54 Waliposikia haya wakaghadhibika, wakamsagia meno. 55 Lakini yeye Stefano, akiwa amejaa Roho Mtakatifu, alikaza macho mbinguni, akaona utukufu wa Mungu, na Yesu akiwa amesimama mkono wa kuume wa Mungu. 56 Akasema, “Tazameni! Naona mbingu zimefunguka, na Mwana wa Adamu amesimama upande wa kuume wa Mungu.”

    57 Lakini wao wakapiga kelele kwa sauti kubwa, wakaziba masikio yao, wakamrukia kwa nia moja. 58 Wakamtupa nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi wakaweka mavazi yao miguuni mwa kijana mmoja ambaye jina lake aliitwa Sauli.

    59 Walipokuwa wakimpiga mawe, Stefano aliomba, “Bwana Yesu, pokea roho yangu.” 60 Kisha akapiga magoti, akalia kwa sauti kubwa akasema, “Bwana usiwahesabie dhambi hii.” Baada ya kusema hayo, akalala.

  59. 1 Katika mji wa Kaisaria palikuwa na mtu jina lake Kornelio, ambaye alikuwa jemadari wa kile kilichojulikana kama kikosi cha Kiitalia. 2 Yeye alikuwa mcha Mungu pamoja na wote wa nyumbani mwake. Aliwapa watu sadaka nyingi na kumwomba Mungu daima. 3 Siku moja alasiri, yapata saa tisa, aliona maono waziwazi, malaika wa Mungu akimjia na kumwambia, “Kornelio!”

    4 Kornelio akamkazia macho kwa hofu akasema, “Kuna nini, Bwana?”

    Malaika akamwambia, “Sala zako na sadaka zako kwa maskini zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu. 5 Sasa tuma watu waende Yafa wakamwite mtu mmoja jina lake Simoni aitwaye Petro. 6 Yeye anaishi na Simoni mtengenezaji ngozi ambaye nyumba yake iko kando ya bahari.”

    7 Yule malaika aliyekuwa akizungumza naye alipoondoka, Kornelio akawaita watumishi wake wawili pamoja na askari mmoja mcha Mungu aliyekuwa miongoni mwa wale waliomtumikia. 8 Akawaambia mambo yote yaliyotukia, kisha akawatuma waende Yafa.

    9 Siku ya pili yake, walipokuwa wameukaribia mji, wakati wa adhuhuri, Petro alipanda juu ya nyumba kuomba. 10 Alipokuwa akiomba akahisi njaa, akatamani kupata chakula. Lakini wakati walikuwa wakiandaa chakula, akalala usingizi mzito sana. 11 Akaona mbingu zimefunguka na kitu kama nguo kubwa kikishushwa duniani kwa ncha zake nne. 12 Ndani yake walikuwepo aina zote za wanyama wenye miguu minne, nao watambaao nchini, na ndege wa angani. 13 Ndipo sauti ikamwambia “Petro, ondoka, uchinje na ule.”

    14 Petro akajibu, “La hasha Bwana! Sijawahi kamwe kula kitu chochote kilicho najisi.”

    15 Ile sauti ikasema naye mara ya pili, “Usikiite najisi kitu chochote Mungu alichokitakasa.”

    16 Jambo hili lilitokea mara tatu na ghafula ile nguo ikarudishwa mbinguni.

    17 Wakati Petro akiwa bado anajiuliza kuhusu maana ya maono haya, wale watu waliokuwa wametumwa na Kornelio wakaipata nyumba ya Simoni mtengenezaji wa ngozi wakawa wamesimama mbele ya lango. 18 Wakabisha hodi na kuuliza kama Simoni aliyeitwa Petro alikuwa anaishi hapo.

    19 Wakati Petro akiwa anafikiria juu ya yale maono, Roho Mtakatifu akamwambia, “Simoni, wako watu watatu wanaokutafuta. 20 Inuka na ushuke, usisite kwenda nao kwa kuwa mimi nimewatuma.”

    21 Petro akashuka na kuwaambia wale watu waliokuwa wametumwa kutoka kwa Kornelio, “Mimi ndiye mnayenitafuta. Mmekuja kwa sababu gani?”

    22 Wale watu wakamjibu, “Tumetumwa na Kornelio yule jemadari. Yeye ni mtu mwema anayemcha Mungu, na anaheshimiwa na Wayahudi wote. Yeye ameagizwa na malaika mtakatifu akukaribishe nyumbani kwake, ili asikilize maneno utakayomwambia.” 23 Basi Petro akawakaribisha wakafuatana naye ndani, akawapa pa kulala. Kesho yake akaondoka pamoja nao, na baadhi ya ndugu kutoka Yafa wakafuatana naye.

    24 Siku iliyofuata wakawasili Kaisaria. Kornelio alikuwa akiwangoja pamoja na jamaa yake na marafiki zake wa karibu. 25 Petro alipokuwa akiingia ndani, Kornelio alikuja kumlaki, akaanguka miguuni pake kwa heshima. 26 Lakini Petro akamwinua akamwambia, “Simama, mimi ni mwanadamu tu.”

    27 Petro alipokuwa akizungumza naye akaingia ndani na kukuta watu wengi wamekusanyika. 28 Akawaambia, “Mnajua kabisa kwamba ni kinyume cha sheria yetu Myahudi kuchangamana na mtu wa Mataifa au kumtembelea. Lakini Mungu amenionyesha kwamba nisimwite mtu yeyote kuwa najisi au asiye safi. 29 Ndiyo sababu ulipotuma niitwe nilikuja bila kupinga lolote. Basi sasa naomba unieleze kwa nini umeniita?”

    30 Kornelio akajibu, “Siku nne zilizopita, nilikuwa nyumbani nikisali saa kama hii, saa tisa alasiri. Ghafula mtu aliyevaa nguo zilizongʼaa akasimama mbele yangu, 31 akasema, ‘Kornelio, maombi yako yamesikiwa na sadaka zako kwa maskini zimekumbukwa mbele za Mungu. 32 Basi tuma watu waende Yafa wakaulize mtu mmoja Simoni aitwaye Petro, yeye ni mgeni katika nyumba ya Simoni mtengenezaji ngozi, ambaye nyumba yake iko kando ya bahari.’ 33 Nilituma watu kwako mara moja, nawe umefanya vyema kuja. Basi sasa sisi sote tuko hapa mbele za Mungu kuyasikiliza yote ambayo Bwana amekuamuru kutuambia.”

    34 Ndipo Petro akafungua kinywa chake akasema, “Mungu hana upendeleo, 35 Lakini katika kila taifa, kila mtu amchaye na kutenda yaliyo haki hukubaliwa naye. 36 Ninyi mnajua ule ujumbe uliotumwa kwa Israeli, ukitangaza habari njema za amani kwa Yesu Kristo. Yeye ni Bwana wa wote. 37 Mnajua yale yaliyotukia katika Uyahudi wote kuanzia Galilaya baada ya mahubiri ya Yohana Mbatizaji: 38 Jinsi Mungu alivyomtia Yesu wa Nazareti mafuta katika Roho Mtakatifu na jinsi alivyokwenda huku na huko akitenda mema na kuponya wote waliokuwa wameonewa na nguvu za ibilisi, kwa sababu Mungu alikuwa pamoja naye.

    39 “Sisi ni mashahidi wa mambo yote aliyoyafanya katika Uyahudi na Yerusalemu. Wakamuua kwa kumtundika msalabani. 40 Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu siku ya tatu na akamwezesha kuonekana na watu. 41 Hakuonekana kwa watu wote, lakini kwetu sisi tuliochaguliwa na Mungu kuwa mashahidi, ambao tulikula na kunywa naye baada ya kufufuka kwake kutoka kwa wafu. 42 Naye alituamuru kuhubiri kwa watu wote na kushuhudia kwamba ndiye alitiwa mafuta na Mungu kuwa hakimu wa walio hai na wafu. 43 Manabii wote walishuhudia juu yake kwamba kila mtu amwaminiye hupokea msamaha wa dhambi katika Jina lake.”

    44 Wakati Petro alikuwa akisema maneno haya, Roho Mtakatifu aliwashukia wote waliokuwa wakisikiliza ule ujumbe. 45 Wale wa tohara walioamini waliokuja na Petro walishangaa kwa kuona kuwa kipawa cha Roho Mtakatifu kimemwagwa juu ya watu wa Mataifa. 46 Kwa kuwa waliwasikia wakinena kwa lugha mpya na kumwadhimisha Mungu.

    Ndipo Petro akasema, 47 “Je, kuna mtu yeyote anayeweza kuzuia watu hawa wasibatizwe kwa maji? Wamempokea Roho Mtakatifu kama sisi tulivyompokea.” 48 Kwa hiyo akaamuru wabatizwe kwa jina la Yesu Kristo. Wakamsihi Petro akae nao kwa siku chache.

  60. 9 Usiku ule ule Bwana akamwambia Gideoni, “Ondoka, ushuke kambini, kwa kuwa nimeitia mkononi mwako. 10 Lakini kama unaogopa kushambulia, shuka kambini pamoja na mtumishi wako Pura, 11 nawe sikiliza wanayosema. Hatimaye, utatiwa moyo kushambulia kambi.” Basi yeye na Pura mtumishi wake wakashuka na kufikia walinzi wa mbele wenye silaha waliokuwa mle kambini. 12 Wamidiani, Waamaleki na mataifa mengine yote ya mashariki walikaa bondeni, nao walikuwa mfano wa nzige kwa wingi wao. Ngamia zao hazikuhesabika, wingi wao ulikuwa kama mchanga wa ufuoni mwa bahari.

    13 Gideoni alifika wakati huo huo kukiwa na mtu mmoja aliyekuwa anamweleza mwenzake ndoto yake, akisema, “Niliota ndoto: Tazama mkate wa shayiri ulioviringana ulianguka katika kambi moja ya Wamidiani, ukaipiga na ikaanguka nao ukaipindua juu chini na hema ikaporomoka chini.”

    14 Rafiki yake akamjibu, “Habari hii si kitu kingine zaidi ya upanga wa Gideoni mwana wa Yoashi, Mwisraeli. Mungu amewatia Wamidiani na jeshi lote mkononi mwake.”

    15 Gideoni alipoisikia hiyo ndoto na tafsiri yake, akamwabudu Mungu. Akarudi kwenye kambi ya Israeli na kusema, “Inukeni! Bwana amelitia jeshi la Wamidiani mikononi mwenu.” 16 Akawagawa wale watu 300 katika makundi matatu, akawakabidhi tarumbeta mikononi mwao wote na mitungi isiyokuwa na maji yenye mienge ndani yake.

    17 Akawaambia, “Nitazameni, fanyeni kama nitakavyofanya, nitakapofika mwisho wa kambi mfanye kama nitakavyofanya. 18 Wakati mimi na wale walio pamoja nami wote, tutakapopiga tarumbeta zetu, ninyi nanyi pigeni tarumbeta pande zote za kambi na mpige kelele, mseme, ‘Upanga wa Bwana na wa Gideoni.’ ”

  61. 17 Nathani akamwarifu Daudi maneno yote ya maono haya.

  62. 28 Manabii wake wanapaka chokaa matendo haya kwa maono ya uongo na utabiri wa udanganyifu. Wanasema, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo,’ wakati Bwana hajasema.

  63. 7 Mimi Danieli, ni mimi peke yangu niliyeona hayo maono; watu waliokuwa pamoja nami hawakuyaona, lakini waligubikwa na hofu kuu, hata wakakimbia na kujificha.

  64. 1 Kisha malaika aliyezungumza nami akarudi na kuniamsha, kama mtu aamshwavyo kutoka usingizi wake. 2 Akaniuliza, “Unaona nini?”

    Nikajibu, “Ninaona kinara cha taa cha dhahabu tupu, nacho kina bakuli juu yake na taa zake saba juu yake, tena iko mirija saba ya kuleta mafuta, kwenye taa zote zilizo juu yake. 3 Pia kuna mizeituni miwili karibu yake, mmoja upande wa kuume wa bakuli na mwingine upande wa kushoto.”

    4 Nikamuuliza malaika aliyezungumza nami, “Hivi ni vitu gani, bwana wangu?”

    5 Akanijibu, “Hujui kuwa hivi ni vitu gani?”

    Nikajibu, “Hapana, bwana wangu.”

    6 Kisha akaniambia, “Hili ni neno la Bwana kwa Zerubabeli: ‘Si kwa uwezo, wala si kwa nguvu, bali ni kwa Roho yangu,’ asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.

    7 “Wewe ni kitu gani, ee mlima mkubwa sana? Mbele ya Zerubabeli wewe utakuwa ardhi tambarare. Kisha ataweka jiwe la juu kabisa la mwisho na watu wakipiga kelele wakisema, ‘Mungu libariki! Mungu libariki!’ ”

    8 Kisha neno la Bwana likanijia: 9 “Mikono ya Zerubabeli iliweka msingi wa Hekalu hili, mikono yake pia italimalizia. Kisha mtajua ya kuwa Bwana Mwenye Nguvu Zote amenituma mimi kwenu.

    10 “Ni nani anayeidharau siku ya mambo madogo? Watu watashangilia watakapoona timazi mkononi mwa Zerubabeli.

    “(Hizi saba ni macho ya Bwana ambayo huzunguka duniani kote.)”

    11 Kisha nikamuuliza yule malaika, “Hii mizeituni miwili iliyoko upande wa kuume na wa kushoto wa kinara cha taa ni nini?”

    12 Tena nikamuuliza, “Haya matawi mawili ya mizeituni karibu na hiyo mirija miwili ya dhahabu inayomimina mafuta ya dhahabu ni nini?”

    13 Akajibu, “Hujui kuwa haya ni nini?”

    Nikamjibu, “Hapana, bwana wangu.”

    14 Kwa hiyo akasema, “Hawa ni wawili ambao wamepakwa mafuta ili kumtumikia Bwana wa dunia yote.”

  65. 1 Nikatazama juu tena: nikaona mbele yangu magari manne ya vita yakija kutoka kati ya milima miwili, milima ya shaba! 2 Gari la kwanza lilivutwa na farasi wekundu, la pili lilivutwa na farasi weusi, 3 la tatu lilivutwa na farasi weupe na gari la nne lilivutwa na farasi wa madoadoa ya kijivu, wote wenye nguvu. 4 Nikamuuliza malaika aliyekuwa akizungumza nami, “Hawa ni nani bwana wangu?”

    5 Malaika akanijibu, “Hizi ni roho nne za mbinguni zisimamazo mbele ya uwepo wa Bwana wa dunia yote, zinatoka kwenda kufanya kazi yake. 6 Gari linalovutwa na farasi weusi linaelekea katika nchi ya kaskazini, la farasi weupe linaelekea magharibi na la farasi wa madoadoa ya kijivu linaelekea kusini.”

    7 Wakati hao farasi wenye nguvu walipokuwa wakitoka, walikuwa wakijitahidi kwenda duniani kote. Akasema, “Nenda duniani kote!” Kwa hiyo wakaenda duniani kote.

    8 Kisha akaniita, “Tazama, wale wanaokwenda kuelekea nchi ya kaskazini wamepumzisha Roho yangu katika nchi ya kaskazini.”

  66. 19 Pilato akiwa ameketi kwenye kiti cha hukumu, mkewe akampelekea ujumbe huu: “Usiwe na jambo lolote juu ya mtu huyu asiye na hatia, kwa kuwa leo nimeteseka sana katika ndoto kwa sababu yake.”

  67. 30 “Basi baada ya miaka arobaini kupita, malaika wa Mungu akamtokea Mose jangwani karibu na Mlima Sinai katika kichaka kilichokuwa kinawaka moto. 31 Alipoona mambo haya, alishangaa yale maono. Aliposogea ili aangalie kwa karibu, akaisikia sauti ya Bwana, ikisema: 32 ‘Mimi ndimi Mungu wa baba zako, Mungu wa Abrahamu, Isaki na Yakobo.’ Mose alitetemeka kwa hofu na hakuthubutu kutazama.

  68. 6 Usiku ule kabla ya siku ambayo Herode Agripa alikuwa amekusudia kumtoa na kumfanyia mashtaka, Petro alikuwa amelala kati ya askari wawili, akiwa amefungwa kwa minyororo miwili. Nao walinzi wa zamu walikuwa wakilinda penye lango la gereza. 7 Ghafula malaika wa Bwana akatokea na nuru ikamulika mle ndani ya gereza. Yule malaika akampiga Petro ubavuni na kumwamsha, akisema, “Ondoka upesi!” Mara ile minyororo ikaanguka kutoka mikononi mwa Petro.

    8 Yule malaika akamwambia, “Vaa nguo zako na viatu vyako.” Petro akafanya hivyo. Kisha akamwambia, “Jifunge vazi lako na unifuate.” 9 Petro akatoka mle gerezani akiwa amefuatana na yule malaika. Hakujua wakati huo kuwa yaliyokuwa yakitukia yalikuwa kweli. Alidhani kuwa anaona maono. 10 Wakapita lindo la kwanza na la pili, ndipo wakafika kwenye lango la chuma linaloelekea mjini. Lango likawafungukia lenyewe, nao wakapita hapo wakatoka nje. Baada ya kutembea umbali wa mtaa mmoja, ghafula yule malaika akamwacha Petro.

    11 Ndipo Petro akarudiwa na fahamu, akasema, “Sasa ninajua bila shaka yoyote kuwa Bwana amemtuma malaika wake na kuniokoa kutoka makucha ya Herode Agripa na kutoka matazamio yote ya Wayahudi.”

  69. 1 Mwana-Kondoo alipoivunja ile lakiri ya saba, pakawa kimya mbinguni kwa muda wa nusu saa.

    2 Nami nikawaona wale malaika saba wanaosimama mbele za Mungu, nao wakapewa tarumbeta saba.

    3 Malaika mwingine aliyekuwa na chetezo cha dhahabu, akaja na kusimama mbele ya madhabahu. Akapewa uvumba mwingi ili autoe pamoja na maombi ya watakatifu wote, juu ya yale madhabahu ya dhahabu yaliyo mbele ya kile kiti cha enzi. 4 Ule moshi wa uvumba pamoja na yale maombi ya watakatifu, vikapanda juu mbele za Mungu, kutoka mkononi mwa huyo malaika. 5 Kisha yule malaika akachukua kile chetezo, akakijaza moto kutoka kwa yale madhabahu, akautupa juu ya dunia. Pakatokea sauti za radi, ngurumo, umeme wa radi na tetemeko la ardhi.

    6 Basi wale malaika saba waliokuwa na zile tarumbeta saba wakajiandaa kuzipiga.

    7 Malaika wa kwanza akaipiga tarumbeta yake, pakatokea mvua ya mawe na moto uliochanganyika na damu, navyo vikatupwa kwa nguvu juu ya nchi. Na theluthi ya dunia ikateketea, theluthi ya miti ikateketea, na nyasi yote mbichi ikateketea.

    8 Malaika wa pili akaipiga tarumbeta yake na kitu kama mlima mkubwa unaowaka moto kikatupwa baharini. Theluthi ya bahari ikawa damu, 9 theluthi ya viumbe vyenye uhai viishivyo baharini vikafa na theluthi ya meli zikaharibiwa.

    10 Malaika wa tatu akaipiga tarumbeta yake, na nyota kubwa iliyokuwa ikiwaka kama taa ikaanguka toka angani, ikaangukia theluthi ya mito na chemchemi za maji. 11 Nyota hiyo inaitwa Uchungu. Theluthi ya maji yakawa machungu na watu wengi wakafa kutokana na maji hayo kwa maana yalikuwa machungu.

    12 Kisha malaika wa nne akaipiga tarumbeta yake, na theluthi ya jua, theluthi ya mwezi na theluthi ya nyota zikapigwa. Kwa hiyo theluthi moja ya mwanga ikawa giza. Theluthi ya mchana ikawa haina mwanga na pia theluthi ya usiku.

    13 Nilipokuwa tena nikitazama, nikamsikia tai mmoja akipiga kelele kwa sauti kuu wakati akiruka katikati ya mbingu, akisema, “Ole! Ole! Ole wa watu waishio duniani, kwa sababu ya tarumbeta ambazo malaika hao wengine watatu wanakaribia kuzipiga!”