54 Bible Verses About Waiting on the Lord

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Waiting on the Lord
  1. 2 ni wewe ninayekutumainia,

    Ee Mungu wangu.

    Usiniache niaibike,

    wala usiache adui zangu wakanishinda.

    3 Kamwe hakuna hata mmoja anayekutegemea

    atakayeaibishwa,

    bali wataaibishwa

    wafanyao hila bila sababu.

    4 Nionyeshe njia zako, Ee Bwana,

    nifundishe mapito yako,

    5 niongoze katika kweli yako na kunifundisha,

    kwa maana wewe ni Mungu Mwokozi wangu,

    nalo tumaini langu liko kwako wakati wote.

    6 Kumbuka, Ee Bwana, rehema zako kuu na upendo,

    kwa maana zimekuwepo tangu zamani.

    7 Usizikumbuke dhambi za ujana wangu

    wala njia zangu za uasi,

    sawasawa na upendo wako unikumbuke,

    kwa maana wewe ni mwema, Ee Bwana.

    8 Bwana ni mwema na mwenye adili,

    kwa hiyo huwafundisha wenye dhambi njia zake.

    9 Huwaongoza wanyenyekevu katika haki,

    naye huwafundisha njia yake.

  2. Zaburi ya Daudi.

    1 Usisumbuke kwa ajili ya watendao maovu,

    wala usiwaonee wivu watendao mabaya,

    2 kwa maana kama majani watanyauka mara,

    kama mimea ya kijani watakufa mara.

    3 Mtumaini Bwana na utende yaliyo mema;

    Kaa katika nchi ukafurahie malisho salama.

    4 Jifurahishe katika Bwana

    naye atakupa haja za moyo wako.

    5 Mkabidhi Bwana njia yako,

    mtumaini yeye, naye atatenda hili:

    6 Yeye atafanya haki yako ingʼae kama mapambazuko,

    na hukumu ya shauri lako kama jua la adhuhuri.

    7 Tulia mbele za Bwana

    na umngojee kwa uvumilivu;

    usisumbuke watu wanapofanikiwa katika njia zao,

    wanapotekeleza mipango yao miovu.

    8 Epuka hasira na uache ghadhabu,

    usihangaike: itakuongoza tu kutenda uovu.

    9 Kwa maana waovu watakatiliwa mbali,

    bali wale wanaomtumaini Bwana watairithi nchi.

    10 Bado kitambo kidogo, nao waovu hawataonekana,

    ingawa utawatafuta, hawataonekana.

    11 Bali wanyenyekevu watairithi nchi

    na wafurahie amani tele.

  3. 27 Kwa nini unasema, ee Yakobo,

    nanyi ee Israeli, kulalamika,

    “Njia yangu imefichwa Bwana asiione,

    Mungu wangu hajali shauri langu?”

    28 Je wewe, hufahamu?

    Je wewe, hujasikia?

    Bwana ni Mungu wa milele,

    Muumba wa miisho ya dunia.

    Hatachoka wala kulegea,

    wala hakuna hata mmoja

    awezaye kuupima ufahamu wake.

    29 Huwapa nguvu waliolegea

    na huongeza nguvu za wadhaifu.

    30 Hata vijana huchoka na kulegea,

    nao vijana wanaume hujikwaa na kuanguka,

    31 bali wale wamtumainio Bwana

    atafanya upya nguvu zao.

    Watapaa juu kwa mbawa kama tai;

    watapiga mbio wala hawatachoka,

    watatembea kwa miguu wala hawatazimia.

  4. 11 Nifundishe njia yako, Ee Bwana,

    niongoze katika njia iliyonyooka

    kwa sababu ya watesi wangu.

    12 Usiniachilie kwa nia za adui zangu,

    kwa maana mashahidi wa uongo

    wameinuka dhidi yangu,

    wakipumua ujeuri.

    13 Nami bado nina tumaini hili:

    nitauona wema wa Bwana

    katika nchi ya walio hai.

    14 Mngojee Bwana,

    uwe hodari na mwenye moyo mkuu,

    nawe, umngojee Bwana.

  5. 21 Hata hivyo najikumbusha neno hili

    na kwa hiyo ninalo tumaini.

    22 Kwa sababu ya upendo mkuu wa Bwana, hatuangamii,

    kwa kuwa huruma zake hazikomi kamwe.

    23 Ni mpya kila asubuhi,

    uaminifu wako ni mkuu.

    24 Nimeiambia nafsi yangu, “Bwana ni fungu langu,

    kwa hiyo nitamngojea.”

    25 Bwana ni mwema kwa wale ambao tumaini lao ni kwake,

    kwa yule ambaye humtafuta;

    26 ni vyema kungojea kwa utulivu

    kwa ajili ya wokovu wa Bwana.

  6. 5 Namngojea Bwana, nafsi yangu inangojea,

    katika neno lake naweka tumaini langu.

    6 Nafsi yangu inamngojea Bwana

    kuliko walinzi waingojeavyo asubuhi,

    naam, kuliko walinzi

    waingojeavyo asubuhi.

    7 Ee Israeli, mtumaini Bwana,

    maana kwa Bwana kuna upendo usiokoma,

    na kwake kuna ukombozi kamili.

    8 Yeye mwenyewe ataikomboa Israeli

    kutoka dhambi zao zote.

  7. 18 Nayahesabu mateso yetu ya wakati huu kuwa si kitu kulinganisha na utukufu utakaodhihirishwa kwetu. 19 Kwa maana viumbe vyote vinangoja kwa shauku kudhihirishwa kwa watoto wa Mungu. 20 Kwa kuwa viumbe vyote viliwekwa chini ya ubatili, si kwa chaguo lao, bali kwa mapenzi yake yeye aliyevitiisha katika tumaini, 21 ili kwamba viumbe vyote vipate kuwekwa huru kutoka kwa utumwa wa kuharibika na kupewa uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu.

    22 Kwa maana twajua ya kuwa hata sasa viumbe vyote vimekuwa vikilia kwa maumivu kama utungu wa mwanamke wakati wa kuzaa. 23 Wala si hivyo viumbe peke yao, bali hata sisi ambao ndio matunda ya kwanza ya Roho, kwa ndani tunalia kwa uchungu tukisubiri kwa shauku kufanywa wana wa Mungu, yaani, ukombozi wa miili yetu. 24 Kwa kuwa tuliokolewa kwa tumaini hili. Lakini kama kinachotumainiwa kikionekana hakiwi tumaini tena. Je, kuna mtu anayetumaini kupata kitu alicho nacho tayari? 25 Lakini tunapotumaini kupata kitu ambacho hatuna, basi twakingojea kwa saburi.

  8. 5 Ee nafsi yangu, upumzike, kwa Mungu peke yake,

    tumaini langu latoka kwake.

    6 Yeye peke yake ndiye mwamba wangu na wokovu wangu;

    ndiye ngome yangu, sitatikisika.

    7 Wokovu wangu na heshima yangu viko kwa Mungu,

    ndiye mwamba wangu wenye nguvu

    na kimbilio langu.

    8 Enyi watu, mtumainini yeye wakati wote,

    miminieni mioyo yenu kwake,

    kwa kuwa Mungu ni kimbilio letu.

  9. 7 Lakini mimi, namtazama Bwana kwa matumaini,

    namngoja Mungu Mwokozi wangu;

    Mungu wangu atanisikia mimi.

  10. 17 Nitamngojea Bwana,

    ambaye ameificha nyumba ya Yakobo uso wake.

    Nitaliweka tumaini langu kwake.

  11. Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.

    1 Nilimngoja Bwana kwa saburi,

    naye akaniinamia, akasikia kilio changu.

    2 Akanipandisha kutoka shimo la uharibifu,

    kutoka matope na utelezi;

    akaiweka miguu yangu juu ya mwamba

    na kunipa mahali imara pa kusimama.

    3 Akaweka wimbo mpya kinywani mwangu,

    wimbo wa sifa kwa Mungu wetu.

    Wengi wataona na kuogopa

    na kuweka tumaini lao kwa Bwana.

    4 Heri mtu yule amfanyaye Bwana kuwa tumaini lake,

    asiyewategemea wenye kiburi,

    wale wenye kugeukia miungu ya uongo.

  12. 6 Lakini ni lazima urudi kwa Mungu wako;

    dumisha upendo na haki,

    nawe umngojee Mungu wako siku zote.

  13. 7 Kwa hiyo, ndugu zangu, vumilieni hadi kuja kwake Bwana. Angalieni jinsi mkulima angojavyo ardhi itoe mavuno yake yaliyo ya thamani na jinsi anavyovumilia kwa ajili ya kupata mvua za kwanza na za mwisho. 8 Ninyi nanyi vumilieni, tena simameni imara, kwa sababu kuja kwa Bwana kumekaribia. 9 Ndugu zangu, msinungʼunikiane msije mkahukumiwa. Hakimu amesimama mlangoni!

    10 Ndugu zangu, waangalieni manabii walionena kwa Jina la Bwana, ili kuwa mfano wa uvumilivu katika kukabiliana na mateso. 11 Kama mnavyojua, tunawahesabu kuwa wabarikiwa wale waliovumilia. Mmesikia habari za uvumilivu wake Ayubu na mmeona kile ambacho hatimaye Bwana alimtendea. Bwana ni mwingi wa huruma, na amejaa rehema.

  14. 18 Hata hivyo Bwana anatamani kutupatia neema,

    anainuka ili kuwaonyesha huruma.

    Kwa kuwa Bwana ni Mungu wa haki.

    Wamebarikiwa wote wanaomngojea yeye!

  15. 18 “Ee Bwana, nautafuta wokovu wako.

  16. 9 Mwana-kondoo alipoivunja ile lakiri ya tano, nikaona chini ya madhabahu, roho za wale waliochinjwa kwa ajili ya neno la Mungu na kwa ajili ya ushuhuda walioutunza. 10 Wakalia kwa sauti kuu, wakisema, “Hata lini, Ee Bwana Mwenyezi, uliye mtakatifu na mwaminifu, hutawahukumu na kulipiza kisasi juu ya watu waishio duniani kwa ajili ya damu yetu?” 11 Kisha kila mmoja wao akapewa joho jeupe na wakaambiwa wangoje kwa muda kidogo zaidi, mpaka idadi ya ndugu zao na watumishi wenzao watakaouawa kama wao walivyouawa, itakapotimia.

  17. 20 Sisi tunamngojea Bwana kwa matumaini,

    yeye ni msaada wetu na ngao yetu.

    21 Mioyo yetu humshangilia,

    kwa maana tunalitumainia jina lake takatifu.

    22 Upendo wako usio na mwisho ukae juu yetu, Ee Bwana,

    tunapoliweka tumaini letu kwako.

  18. 7 “Lakini sasa Bwana, nitafute nini?

    Tumaini langu ni kwako.

    8 Niokoe kutoka kwenye makosa yangu yote,

    usinifanye kuwa dhihaka ya wapumbavu.

  19. 6 Wenye haki wataona na kuogopa,

    watamcheka, wakisema,

    7 “Huyu ni yule mtu ambaye

    hakumfanya Mungu kuwa ngome yake,

    bali alitumainia wingi wa utajiri wake,

    na akawa hodari kwa kuwaangamiza wengine!”

    8 Lakini mimi ni kama mti wa mzeituni

    unaostawi katika nyumba ya Mungu,

    nautegemea upendo wa Mungu usiokoma

    milele na milele.

    9 Nitakusifu milele kwa yale uliyoyatenda,

    nitatumaini jina lako, kwa kuwa jina lako ni jema.

    Nitakusifu mbele ya watakatifu wako.

  20. Wimbo wa kwenda juu.

    1 Ninayainua macho yangu kwako,

    kwako wewe ambaye kiti chako cha enzi kiko mbinguni.

    2 Kama vile macho ya watumwa

    yatazamavyo mkono wa bwana wao,

    kama vile macho ya mtumishi wa kike

    yatazamavyo mkono wa bibi yake,

    ndivyo macho yetu yamtazamavyo Bwana Mungu wetu,

    mpaka atakapotuhurumia.

  21. 14 Bwana huwategemeza wote waangukao,

    na huwainua wote waliolemewa na mizigo yao.

    15 Macho yao wote yanakutazama wewe,

    nawe huwapa chakula chao wakati wake.

    16 Waufumbua mkono wako,

    watosheleza haja ya kila kitu kilicho hai.

  22. 35 “Kuweni tayari mkiwa mmevikwa kwa ajili ya huduma na taa zenu zikiwa zinawaka, 36 kama watumishi wanaomngojea bwana wao arudi kutoka kwenye karamu ya arusi, ili ajapo na kubisha mlango waweze kumfungulia mara. 37 Heri wale watumishi ambao bwana wao atakapokuja atawakuta wakiwa wanakesha. Amin, nawaambia, atajifunga mkanda wake na kuwaketisha ili wale, naye atakuja na kuwahudumia. 38 Itakuwa heri kwa watumwa hao ikiwa bwana wao atakapokuja atawakuta wamekesha hata kama atakuja mnamo usiku wa manane, au karibu na mapambazuko. 39 Lakini fahamuni jambo hili: Kama mwenye nyumba angalijua saa mwizi atakuja, asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa. 40 Ninyi nanyi hamna budi kuwa tayari, kwa sababu Mwana wa Adamu atakuja saa msiyotazamia.”

  23. Kwa mwimbishaji. Mtindo wa Yeduthuni. Zaburi ya Daudi.

    1 Kwa Mungu peke yake nafsi yangu inapata pumziko;

    wokovu wangu watoka kwake.

    2 Yeye peke yake ndiye mwamba wangu na wokovu wangu;

    yeye ni ngome yangu, sitatikisika kamwe.

  24. 22 Usiseme, “Nitakulipiza kwa ajili ya kosa hili!”

    Mngojee Bwana, naye atakuokoa.

  25. 5 Kwa maana, kwa njia ya Roho kwa imani, tunangojea kwa shauku tumaini la haki.

  26. 4 Wakati mmoja alipokuwa pamoja nao, aliwapa amri hii, “Msitoke Yerusalemu, bali ingojeni ahadi ya Baba, ambayo mmenisikia nikisema habari zake. 5 Yohana aliwabatiza kwa maji, lakini baada ya siku chache mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu.”

  27. 5 Kwa hiyo msihukumu jambo lolote kabla ya wakati wake. Ngojeni mpaka Bwana atakapokuja. Yeye atayaleta nuruni mambo yale yaliyofichwa gizani, na kuweka wazi nia za mioyo ya wanadamu. Wakati huo kila mmoja atapokea sifa anayostahili kutoka kwa Mungu.

  28. 11 Kwa maana neema ya Mungu ambayo inawaokoa wanadamu wote imefunuliwa. 12 Nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia, ili tupate kuishi maisha ya kiasi, ya haki na ya utaua katika ulimwengu huu wa sasa, 13 huku tukilitazamia tumaini lenye baraka na ufunuo wa utukufu wa Mungu wetu Mkuu, aliye Mwokozi wetu Yesu Kristo. 14 Ndiye alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, ili atukomboe kutoka uovu wote na kujisafishia watu kuwa mali yake Mwenyewe, yaani, wale walio na juhudi katika kutenda mema.

  29. 9 Ee nguvu yangu, ninakutazama wewe,

    wewe, Ee Mungu, ndiwe ngome yangu,

    10 Mungu wangu unipendaye.

    Mungu atanitangulia,

    naye atanifanya niwachekelee

    wale wanaonisingizia.

  30. 4 Tangu nyakati za zamani hakuna yeyote aliyesikia,

    hakuna sikio lililotambua,

    hakuna jicho lililomwona Mungu mwingine ila wewe,

    anayetenda mambo kwa ajili ya wale wamngojeao.

  31. 34 Mngojee Bwana,

    na uishike njia yake.

    Naye atakutukuza uirithi nchi,

    waovu watakapokatiliwa mbali,

    utaliona hilo.

  32. 7 Juu ya mlima huu ataharibu

    sitara ihifadhiyo mataifa yote,

    kile kifuniko kifunikacho mataifa yote,

    8 yeye atameza mauti milele.

    Bwana Mwenyezi atafuta machozi katika nyuso zote;

    ataondoa aibu ya watu wake duniani kote.

    Bwana amesema hili.

    9 Katika siku ile watasema,

    “Hakika huyu ndiye Mungu wetu;

    tulimtumaini, naye akatuokoa.

    Huyu ndiye Bwana, tuliyemtumaini;

    sisi tushangilie na kufurahia katika wokovu wake.”

  33. 1 Nitasimama katika zamu yangu,

    na kujiweka mwenyewe juu ya maboma;

    nitatazama nione atakaloniambia,

    na ni jibu gani nitakalotoa kuhusu lalamiko hili.

    2 Kisha Bwana akajibu:

    “Andika ufunuo huu,

    na ukaufanye wazi juu ya vibao,

    ili mpiga mbiu akimbie nao.

    3 Kwa kuwa ufunuo huu unasubiri wakati uliokubalika;

    unazungumzia mambo ya mwisho,

    na kamwe hautakosea.

    Iwapo utakawia, wewe usubiri;

    kwa hakika utakuja na hautachelewa.

  34. 3 Nimechoka kwa kuomba msaada,

    koo langu limekauka.

    Macho yangu yanafifia,

    nikimtafuta Mungu wangu.

  35. 21 Uadilifu na uaminifu vinilinde,

    kwa sababu tumaini langu ni kwako.

  36. 23 Wafalme watakuwa baba zenu wa kuwalea,

    na malkia wao watakuwa mama zenu wa kuwalea.

    Watasujudu mbele yako nyuso zao zikigusa ardhi;

    wataramba mavumbi yaliyo miguuni mwako.

    Ndipo utajua ya kuwa Mimi ndimi Bwana;

    wale wanaonitumaini mimi hawataaibika.”

  37. 27 Hawa wote wanakutazamia wewe,

    uwape chakula chao kwa wakati wake.

    28 Wakati unapowapa,

    wanakikusanya,

    unapofumbua mkono wako,

    wao wanashibishwa mema.

  38. 2 Ee Bwana, uturehemu,

    tunakutamani.

    Uwe nguvu yetu kila asubuhi

    na wokovu wetu wakati wa taabu.

  39. 5 Haki yangu inakaribia mbio,

    wokovu wangu unakuja,

    nao mkono wangu utaleta hukumu kwa mataifa.

    Visiwa vitanitegemea

    na kungojea mkono wangu kwa matumaini.

  40. 8 Bwana anasema,

    “Kwa hiyo ningojee mimi,

    siku nitakayosimama kuteka nyara.

    Nimeamua kukusanya mataifa,

    kukusanya falme

    na kumimina ghadhabu yangu juu yao,

    hasira yangu kali yote.

    Dunia yote itateketezwa

    kwa moto wa wivu wa hasira yangu.

  41. 28 vivyo hivyo Kristo alitolewa mara moja tu kuwa dhabihu ili azichukue dhambi za watu wengi. Naye atakuja mara ya pili, sio kuchukua dhambi, bali kuwaletea wokovu wale wanaomngoja kwa shauku.

  42. 8 Lakini wapenzi, msisahau neno hili: kwamba kwa Bwana, siku moja ni kama miaka elfu, na miaka elfu ni kama siku moja. 9 Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama watu wengine wanavyokudhani kukawia. Badala yake, yeye anawavumilia ninyi, maana hataki mtu yeyote aangamie, bali kila mtu afikilie toba.

  43. 3 Asubuhi, unasikia sauti yangu, Ee Bwana;

    asubuhi naleta haja zangu mbele zako,

    na kusubiri kwa matumaini.

  44. 13 Lakini mara walisahau aliyowatendea,

    wala hawakungojea shauri lake.

    14 Jangwani walitawaliwa na tamaa zao,

    walimjaribu Mungu nyikani.

    15 Kwa hiyo aliwapa kile walichoomba,

    lakini akatuma juu yao ugonjwa wa kudhoofisha.

  45. 7 Mapito ya wenye haki yamenyooka.

    Ewe uliye Mwenye Haki,

    waisawazisha njia ya mtu mnyofu.

    8 Naam, Bwana, tukienenda katika sheria zako,

    twakungojea wewe,

    jina lako na sifa zako

    ndizo shauku za mioyo yetu.

    9 Nafsi yangu yakutamani wakati wa usiku,

    wakati wa asubuhi roho yangu yakuonea shauku.

    Wakati hukumu zako zinapokuja juu ya dunia,

    watu wa ulimwengu hujifunza haki.

  46. 4 hatazimia roho wala kukata tamaa,

    mpaka atakaposimamisha haki juu ya dunia.

    Visiwa vitaweka tumaini lao katika sheria yake.”

  47. 20 Lakini uenyeji wetu uko mbinguni. Nasi tunamngoja kwa shauku Mwokozi kutoka huko, yaani, Bwana Yesu Kristo, 21 atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, ili upate kufanana na mwili wake wa utukufu, kwa uweza ule ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote chini yake.

  48. 12 Amebarikiwa mtu yule atakayevumilia hadi kufikia mwisho wa hizo siku 1,335.

  49. 28 Nasi tunajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hutenda kazi pamoja na wote wampendao, katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.

  50. 12 Heri mtu anayevumilia wakati wa majaribu, kwa sababu akiisha kushinda hilo jaribio atapewa taji la uzima Mungu alilowaahidia wale wampendao.

  51. 24 Kuweni hodari na mjipe moyo,

    ninyi nyote mnaomtumaini Bwana.

  52. 13 Lakini Ee Bwana, ninakuomba,

    kwa wakati ukupendezao;

    katika upendo wako mkuu, Ee Mungu,

    unijibu kwa wokovu wako wa hakika.

  53. 10 Hili ndilo asemalo Bwana: “Miaka sabini itakapotimia kwa ajili ya Babeli, nitakuja kwenu na kutimiza ahadi yangu ya rehema ya kuwarudisha mahali hapa. 11 Kwa maana ninajua mipango niliyo nayo kwa ajili yenu,” asema Bwana, “ni mipango ya kuwafanikisha na wala si ya kuwadhuru, ni mipango ya kuwapa tumaini katika siku zijazo. 12 Kisha mtaniita, na mtakuja na kuniomba, nami nitawasikiliza. 13 Mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote.

  54. 7 “Ombeni nanyi mtapewa; tafuteni nanyi mtapata; bisheni nanyi mtafunguliwa mlango. 8 Kwa kuwa kila aombaye hupewa; naye kila atafutaye hupata; na kila abishaye hufunguliwa mlango.

    9 “Au ni nani miongoni mwenu ambaye mwanawe akimwomba mkate atampa jiwe? 10 Au mwanawe akimwomba samaki atampa nyoka? 11 Ikiwa ninyi basi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri, si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa vitu vizuri wale wamwombao?