40 Bible Verses About Hope in Hard Times

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Hope in Hard Times
  1. 1 Kwa hiyo, kwa kuwa tumekwisha kuhesabiwa haki kwa imani, tuna amani na Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, 2 ambaye kwa kupitia kwake tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo ndani yake sasa tunasimama, nasi twafurahia katika tumaini letu la kushiriki utukufu wa Mungu. 3 Si hivyo tu, bali twafurahi pia katika mateso, kwa sababu tunajua kuwa mateso huleta saburi, 4 nayo saburi huleta uthabiti wa moyo, na uthabiti wa moyo huleta tumaini, 5 wala tumaini halitukatishi tamaa, kwa sababu Mungu amekwisha kumimina pendo lake mioyoni mwetu kwa njia ya Roho Mtakatifu ambaye ametupatia.

  2. 18 Nayahesabu mateso yetu ya wakati huu kuwa si kitu kulinganisha na utukufu utakaodhihirishwa kwetu.

  3. 28 Je wewe, hufahamu?

    Je wewe, hujasikia?

    Bwana ni Mungu wa milele,

    Muumba wa miisho ya dunia.

    Hatachoka wala kulegea,

    wala hakuna hata mmoja

    awezaye kuupima ufahamu wake.

    29 Huwapa nguvu waliolegea

    na huongeza nguvu za wadhaifu.

    30 Hata vijana huchoka na kulegea,

    nao vijana wanaume hujikwaa na kuanguka,

    31 bali wale wamtumainio Bwana

    atafanya upya nguvu zao.

    Watapaa juu kwa mbawa kama tai;

    watapiga mbio wala hawatachoka,

    watatembea kwa miguu wala hawatazimia.

  4. 13 Mungu wa tumaini awajaze ninyi furaha yote na amani katika kumwamini, ili mpate kujawa na tumaini tele kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.

  5. 4 Furahini katika Bwana siku zote, tena nasema furahini! 5 Upole wenu na ujulikane na watu wote. Bwana yu karibu. 6 Msijisumbue kwa jambo lolote, bali katika kila jambo kwa kuomba na kusihi pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. 7 Nayo amani ya Mungu, inayopita fahamu zote, itailinda mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.

    8 Hatimaye, ndugu zangu, mambo yote yaliyo ya kweli, yoyote yaliyo na sifa njema, yoyote yaliyo ya haki, yoyote yaliyo safi, yoyote ya kupendeza, yoyote yenye staha, ukiwepo uzuri wowote, pakiwepo chochote kinachostahili kusifiwa, tafakarini mambo hayo. 9 Mambo yote mliyojifunza au kuyapokea au kuyasikia kutoka kwangu, au kuyaona kwangu, yatendeni hayo. Naye Mungu wa amani atakuwa pamoja nanyi.

  6. 11 Kwa maana ninajua mipango niliyo nayo kwa ajili yenu,” asema Bwana, “ni mipango ya kuwafanikisha na wala si ya kuwadhuru, ni mipango ya kuwapa tumaini katika siku zijazo. 12 Kisha mtaniita, na mtakuja na kuniomba, nami nitawasikiliza. 13 Mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote.

  7. 13 Mungu alipompa Abrahamu ahadi yake, kwa kuwa hakuwepo mwingine aliyekuwa mkuu kuliko yeye ambaye angeweza kuapa kwa jina lake, aliapa kwa nafsi yake, 14 akisema, “Hakika nitakubariki na kukupa wazao wengi.” 15 Abrahamu naye, baada ya kungoja kwa saburi, alipokea kile kilichoahidiwa.

    16 Wanadamu huapa kwa yeye aliye mkuu kuwaliko, nacho kiapo hicho huthibitisha kile kilichosemwa na hivyo humaliza mabishano yote. 17 Mungu alipotaka kuonyesha kwa udhahiri zaidi ile asili ya kutokubadilika kwa ahadi yake kwa warithi wa ahadi, aliithitibisha kwa kiapo. 18 Mungu alifanya hivyo ili kwa vitu viwili visivyobadilika, yaani ahadi yake na kiapo chake, ambavyo kwavyo Mungu hawezi kusema uongo, sisi ambao tumemkimbilia ili tulishike lile tumaini lililowekwa mbele yetu tuwe na faraja thabiti. 19 Tunalo tumaini hili kama nanga ya roho iliyo imara na thabiti. Tumaini hili huingia katika sehemu takatifu iliyopo nyuma ya pazia, 20 mahali ambapo Yesu mtangulizi wetu aliingia kwa niaba yetu. Yeye amekuwa Kuhani Mkuu milele, kwa mfano wa Melkizedeki.

  8. 10 Hivyo usiogope, kwa maana niko pamoja nawe;

    usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako.

    Nitakutia nguvu na kukusaidia;

    nitakutegemeza kwa mkono wa kuume wa haki yangu.

    11 “Wote walioona hasira dhidi yako

    hakika wataaibika na kutahayarika,

    wale wakupingao

    watakuwa kama vile si kitu, na kuangamia.

    12 Ingawa utawatafuta adui zako,

    hutawaona.

    Wale wanaopigana vita dhidi yako

    watakuwa kama vile si kitu kabisa.

    13 Kwa maana Mimi ndimi Bwana, Mungu wako,

    nikushikaye mkono wako wa kuume

    na kukuambia, Usiwe na hofu,

    nitakusaidia.

  9. 6 Basi, nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake. 7 Mtwikeni yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana na mambo yenu.

    8 Mwe na kiasi na kukesha, maana adui yenu ibilisi huzungukazunguka kama simba angurumaye akitafuta mtu ili apate kummeza. 9 Mpingeni, mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kwamba mateso kama hayo yanawapata ndugu zenu pote duniani.

    10 Nanyi mkiisha kuteswa kwa kitambo kidogo, Mungu wa neema yote, aliyewaita kuingia katika utukufu wake wa milele ndani ya Kristo, yeye mwenyewe atawarejesha na kuwatia nguvu, akiwaimarisha na kuwathibitisha. 11 Uweza una yeye milele na milele. Amen.

  10. 2 Ndugu zangu, hesabuni kuwa ni furaha tupu mnapopatwa na majaribu mbalimbali, 3 kwa sababu mnajua ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi. 4 Saburi na iwe na kazi timilifu, ili mpate kuwa wakamilifu, mmekamilishwa, bila kupungukiwa na kitu chochote.

  11. 3 Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo! Kwa rehema zake kuu ametuzaa sisi mara ya pili katika tumaini lenye uzima kupitia kwa kufufuka kwa Yesu Kristo kutoka kwa wafu, 4 ili tuupate urithi usioharibika, usio na uchafu, ule usionyauka: uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu, 5 ninyi ambao mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani, hadi uje ule wokovu ulio tayari kufunuliwa nyakati za mwisho. 6 Katika hili mnafurahi sana, ingawa sasa kwa kitambo kidogo mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna nyingi. 7 Haya yamewajia ili kwamba imani yenu, iliyo ya thamani kuliko dhahabu ipoteayo, ingawa hujaribiwa kwa moto, ionekane kuwa halisi na imalizie katika sifa, utukufu na heshima wakati Yesu Kristo atadhihirishwa. 8 Ingawa hamjamwona, mnampenda; tena ingawa sasa hammwoni, mnamwamini na kujawa na furaha isiyoneneka yenye utukufu usioelezeka.

  12. Kwa mwimbishaji. Zaburi ya wana wa Kora. Mtindo wa alamothi.

    1 Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu,

    msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso.

    2 Kwa hiyo hatutaogopa, hata kama dunia ikiondolewa

    nayo milima ikiangukia moyoni mwa bahari.

    3 Hata kama maji yake yatanguruma na kuumuka,

    milima nayo ikitetemeka kwa mawimbi yake.

  13. 15 Haya yote ni kwa faida yenu, ili kwamba neema ile inavyowafikia watu wengi zaidi na zaidi, ipate kusababisha shukrani nyingi kwa utukufu wa Mungu.

    16 Kwa hiyo, hatukati tamaa. Ingawa utu wetu wa nje unachakaa, utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku. 17 Kwa maana dhiki yetu nyepesi iliyo ya kitambo inatutayarisha kwa ajili ya utukufu wa milele unaozidi kuwa mwingi kupita kiasi, 18 kwa sababu hatuangalii yale yanayoweza kuonekana bali yale yasiyoweza kuonekana. Kwa maana yale yanayoweza kuonekana ni ya kitambo tu, bali yale yasiyoweza kuonekana ni ya milele.

  14. 1 Basi, ndugu, kwa habari ya nyakati na majira hatuna haja ya kuwaandikia, 2 kwa kuwa mnajua vyema kwamba siku ya Bwana itakuja kama mwizi ajapo usiku. 3 Wakati watu wanaposema, “Kuna amani na salama,” maangamizi huwajia ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwanamke mwenye mimba; nao hakika hawatatoroka.

    4 Bali ninyi, ndugu, hampo gizani hata siku ile iwakute ghafula kama mwizi. 5 Ninyi nyote ni wana wa nuru na wana wa mchana. Sisi si wana wa giza wala wa usiku. 6 Kwa hiyo basi, tusilale kama watu wengine walalavyo, bali tukeshe na kuwa na kiasi. 7 Kwa kuwa wote walalao hulala usiku na wale walewao hulewa usiku. 8 Lakini kwa kuwa sisi ni wana wa mchana, basi tuwe na kiasi, tukijivika imani na upendo kama dirii kifuani na tumaini letu la wokovu kama chapeo. 9 Kwa maana Mungu hakutuita ili tupate ghadhabu bali tupate wokovu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. 10 Yeye alikufa kwa ajili yetu ili hata kama tuko macho au tumelala, tupate kuishi pamoja naye. 11 Kwa hiyo farijianeni na kujengana, kama vile mnavyofanya sasa.

  15. 4 Ee Mungu wangu uniokoe kutoka kwenye mkono wa mwovu,

    kutoka kwenye makucha ya watu wabaya na wakatili.

    5 Kwa kuwa umekuwa tumaini langu, Ee Bwana Mwenyezi,

    tegemeo langu tangu ujana wangu.

    6 Tangu kuzaliwa nimekutegemea wewe,

    ulinitoa tumboni mwa mama yangu.

    Nitakusifu wewe daima.

    7 Nimekuwa kama kioja kwa wengi,

    lakini wewe ni kimbilio langu imara.

    8 Kinywa changu kimejazwa sifa zako,

    nikitangaza utukufu wako mchana kutwa.

  16. 5 Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote

    wala usizitegemee akili zako mwenyewe;

    6 katika njia zako zote mkiri yeye,

    naye atayanyoosha mapito yako.

  17. 26 Lakini huyo Msaidizi, yaani, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwenu kwa Jina langu, atawafundisha mambo yote na kuwakumbusha yote niliyowaambia. 27 Amani nawaachia, amani yangu nawapa, amani hii niwapayo si kama ile ulimwengu utoayo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiogope.

  18. 6 Kuweni imara na moyo wa ushujaa. Msiogope wala msifadhaike kwa sababu yao, kwa kuwa Bwana Mungu wenu anakwenda pamoja nanyi; kamwe hatawaacha wala hatawatupa ninyi.”

  19. Zaburi ya Daudi.

    1 Bwana ndiye mchungaji wangu,

    sitapungukiwa na kitu.

    2 Hunilaza katika malisho

    ya majani mabichi,

    kando ya maji matulivu huniongoza,

    3 hunihuisha nafsi yangu.

    Huniongoza katika njia za haki

    kwa ajili ya jina lake.

    4 Hata kama nikipita katikati

    ya bonde la uvuli wa mauti,

    sitaogopa mabaya,

    kwa maana wewe upo pamoja nami;

    fimbo yako na mkongojo wako

    vyanifariji.

    5 Waandaa meza mbele yangu

    machoni pa adui zangu.

    Umenipaka mafuta kichwani pangu,

    kikombe changu kinafurika.

    6 Hakika wema na upendo vitanifuata

    siku zote za maisha yangu,

    nami nitakaa nyumbani mwa Bwana

    milele.

  20. 18 Lakini macho ya Bwana yako kwa wale wamchao,

    kwa wale tumaini lao liko katika upendo wake usio na kikomo,

  21. 22 Kwa sababu ya upendo mkuu wa Bwana, hatuangamii,

    kwa kuwa huruma zake hazikomi kamwe.

    23 Ni mpya kila asubuhi,

    uaminifu wako ni mkuu.

    24 Nimeiambia nafsi yangu, “Bwana ni fungu langu,

    kwa hiyo nitamngojea.”

    25 Bwana ni mwema kwa wale ambao tumaini lao ni kwake,

    kwa yule ambaye humtafuta;

    26 ni vyema kungojea kwa utulivu

    kwa ajili ya wokovu wa Bwana.

    27 Ni vyema mtu kuchukua nira

    bado angali kijana.

  22. 20 Basi hii ndiyo sababu nimewatumania, ili niseme nanyi. Kwa kuwa ni kwa ajili ya tumaini la Israeli nimefungwa kwa minyororo.”

  23. 28 Nasi tunajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hutenda kazi pamoja na wote wampendao, katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.

  24. 3 Ahimidiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa huruma na Mungu wa faraja yote. 4 Yeye hutufariji katika taabu zetu, ili tuweze kuwafariji walio katika taabu yoyote kwa faraja ambayo sisi wenyewe tumepokea kutoka kwa Mungu. 5 Kama vile mateso ya Kristo yanavyozidi ndani ya maisha yetu, hivyo ndivyo faraja yetu inavyofurika kwa njia ya Kristo.

  25. 5 Kwa maana, kwa njia ya Roho kwa imani, tunangojea kwa shauku tumaini la haki.

  26. 13 Lakini ndugu, hatutaki mkose kujua kuhusu wale waliolala mauti, ili msihuzunike kama watu wengine wasiokuwa na tumaini. 14 Kwa kuwa tunaamini kwamba Yesu alikufa na kufufuka, na kwa hivyo, Mungu kwa njia ya Yesu atawafufua pamoja naye wale waliolala mautini ndani yake. 15 Kulingana na neno la Bwana mwenyewe, tunawaambia kwamba sisi ambao bado tuko hai, tuliobaki hadi kuja kwake Bwana, hakika hatutawatangulia waliolala mauti. 16 Kwa maana Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni, akitoa amri kwa sauti kuu, pamoja na sauti ya malaika mkuu, na sauti ya tarumbeta ya Mungu. Nao waliokufa wakiwa katika Kristo watafufuka kwanza. 17 Baada ya hilo sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu ili kumlaki Bwana hewani, hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele. 18 Kwa hiyo farijianeni kwa maneno haya.

  27. 9 Ingawa tunasema hivi, ndugu zangu wapendwa, kwa upande wenu tuna hakika ya mambo mema zaidi, mambo yale yahusuyo wokovu. 10 Mungu si mdhalimu: yeye hataisahau kazi yenu na upendo ule mlioonyesha kwa ajili yake katika kuwahudumia watakatifu na hata sasa mnaendelea kuwahudumia.

  28. 32 Kumbukeni siku zile za kwanza, ambazo mkiisha kutiwa nuru mlistahimili mashindano makali ya maumivu. 33 Wakati mwingine mlitukanwa na kuteswa hadharani; wakati mwingine mlikuwa radhi kuungana na wale waliofanyiwa hivyo. 34 Mliwahurumia wale waliokuwa kifungoni, mkikubali kwa furaha kunyangʼanywa mali zenu kwa maana mlijua kwamba mnayo mali iliyo bora zaidi idumuyo.

    35 Kwa hiyo msiutupe ujasiri wenu, kwa maana una thawabu kubwa mno. 36 Inawapasa kuvumilia ili mkiisha kufanya mapenzi ya Mungu mpate kile alichoahidi. 37 Kwa kuwa bado kitambo kidogo tu,

    “Yeye ajaye atakuja wala hatakawia.

    38 Lakini mwenye haki wangu

    ataishi kwa imani.

    Naye kama akisitasita,

    sina furaha naye.”

    39 Lakini sisi hatumo miongoni mwa hao wanaositasita na kuangamia, bali tuko miongoni mwa hao wenye imani na hivyo tunaokolewa.

  29. 8 Bwana mwenyewe atakutangulia naye atakuwa pamoja nawe; kamwe hatakuacha wala hatakutupa. Usiogope, wala usifadhaike.”

  30. 9 Bwana ni kimbilio la watu wanaoonewa,

    ni ngome imara wakati wa shida.

    10 Wote wanaolijua jina lako watakutumaini wewe,

    kwa maana wewe Bwana,

    hujawaacha kamwe wakutafutao.

  31. 17 Wenye haki hulia, naye Bwana huwasikia,

    huwaokoa katika taabu zao zote.

    18 Bwana yu karibu na waliovunjika moyo,

    na huwaokoa waliopondeka roho.

    19 Mwenye haki ana mateso mengi,

    lakini Bwana humwokoa nayo yote,

  32. 22 Mtwike Bwana fadhaa zako,

    naye atakutegemeza,

    hatamwacha kamwe mwenye haki wake aanguke.

  33. 7 Ili kunizuia nisijivune kwa sababu ya ufunuo huu mkuu, nilipewa mwiba katika mwili wangu, mjumbe wa Shetani, ili anitese. 8 Kwa habari ya jambo hili nilimsihi Bwana mara tatu aniondolee mwiba huu. 9 Lakini aliniambia, “Neema yangu inakutosha, kwa kuwa uweza wangu hukamilika katika udhaifu.” Kwa hiyo nitajisifu kwa furaha zaidi kuhusu udhaifu wangu, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. 10 Hii ndiyo sababu, kwa ajili ya Kristo, nafurahia udhaifu, katika kutukanwa, katika taabu, katika mateso na katika shida, kwa maana ninapokuwa dhaifu, ndipo nina nguvu.

  34. 10 (nasi kwa ajili ya hili tunajitaabisha na kujitahidi), kwamba tumeweka tumaini letu kwa Mungu aliye hai, ambaye ni Mwokozi wa watu wote, hasa wale waaminio.

  35. 13 Kwa hiyo, tayarisheni nia zenu kwa kazi; mwe na kiasi, mkitumainia kikamilifu ile neema mtakayopewa Yesu Kristo atakapodhihirishwa.

  36. 9 Je, si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na shujaa. Usihofu wala usivunjike moyo, kwa kuwa Bwana Mungu wako atakuwa pamoja nawe kokote uendako.”

  37. 6 Kwa hiyo kila mtu mcha Mungu akuombe

    wakati unapopatikana,

    hakika maji makuu yatakapofurika

    hayatamfikia yeye.

    7 Wewe ndiwe mahali pangu pa kujificha,

    utaniepusha na taabu

    na kunizunguka kwa nyimbo za wokovu.

    8 Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea;

    nitakushauri na kukuangalia.

  38. 28 “Njooni kwangu, ninyi nyote mnaotaabika na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. 29 Jifungeni nira yangu, mjifunze kutoka kwangu, kwa maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtapata raha nafsini mwenu. 30 Kwa maana nira yangu ni laini na mzigo wangu ni mwepesi.”

  39. 33 Nimewaambia mambo haya, ili mpate kuwa na amani mkiwa ndani yangu. Ulimwenguni mtapata dhiki. Lakini jipeni moyo, kwa maana mimi nimeushinda ulimwengu.”

  40. 1 Hata kama nitasema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa kengele inayolialia au toazi livumalo. 2 Ningekuwa na karama ya unabii na kujua siri zote na maarifa yote, hata kama nina imani kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, mimi si kitu. 3 Kama nikitoa mali yote niliyo nayo na kama nikijitolea mwili wangu uchomwe moto, kama sina upendo, hainifaidi kitu.

    4 Upendo huvumilia, upendo hufadhili, upendo hauoni wivu, hauna majivuno, hauna kiburi. 5 Haukosi kuwa na adabu, hautafuti mambo yake, haukasiriki upesi, hauweki kumbukumbu ya mabaya. 6 Upendo haufurahii mabaya bali hufurahi pamoja na kweli. 7 Upendo huvumilia yote, huamini yote, hutumaini yote, hustahimili yote.

    8 Upendo haushindwi kamwe. Lakini ukiwepo unabii, utakoma; zikiwepo lugha, zitakoma; yakiwepo maarifa, yatapita. 9 Kwa maana tunafahamu kwa sehemu na tunatoa unabii kwa sehemu. 10 Lakini ukamilifu ukija, yale yasiyo kamili hutoweka. 11 Nilipokuwa mtoto, nilisema kama mtoto, niliwaza kama mtoto, nilifikiri kama mtoto. Nilipokuwa mtu mzima niliacha mambo ya kitoto. 12 Kwa maana sasa tunaona taswira kama kwa kioo, lakini wakati huo tutaona wazi. Sasa nafahamu kwa sehemu, wakati huo nitafahamu kikamilifu, kama vile mimi ninavyofahamika kikamilifu.

    13 Basi sasa, yanadumu mambo haya matatu: Imani, tumaini na upendo. Lakini lililo kuu miongoni mwa haya matatu ni upendo.