33 Bible Verses About Family

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Family
  1. 18 Ninyi wake, watiini waume zenu, kama inavyostahili katika Bwana.

    19 Ninyi waume, wapendeni wake zenu, wala msiwe na uchungu dhidi yao.

    20 Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika mambo yote, kwa maana hivi ndivyo inavyompendeza Bwana.

    21 Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, wasije wakakata tamaa.

    22 Ninyi watumwa, watiini mabwana zenu wa hapa duniani katika mambo yote. Fanyeni hivyo si wakiwepo tu, wala si kwa kutafuta upendeleo wao, bali kwa moyo mnyofu na kumcha Bwana. 23 Lolote mfanyalo, fanyeni kwa moyo kama watu wanaomtumikia Bwana, na si wanadamu, 24 kwa kuwa mnajua kwamba mtapokea urithi wenu kutoka kwa Bwana ukiwa thawabu yenu. Ni Bwana Yesu Kristo mnayemtumikia. 25 Yeyote atendaye mabaya atalipwa kwa ajili ya mabaya yake, wala hakuna upendeleo.

  2. 1 Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, kwa kuwa hili ni jema. 2 “Waheshimu baba yako na mama yako,” hii ndio amri ya kwanza yenye ahadi, 3 “upate baraka na uishi siku nyingi duniani.”

    4 Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, bali waleeni kwa nidhamu na mafundisho ya Bwana.

  3. 21 Hivyo Bwana Mungu akamfanya Adamu kulala usingizi mzito, naye alipokuwa amelala akachukua moja ya mbavu zake, akapafunika mahali pale kwa nyama. 22 Kisha Bwana Mungu akamfanya mwanamke kutoka kwenye ule ubavu aliouchukua kutoka kwa huyo mwanaume, akamleta huyo mwanamke kwa huyo mwanaume.

    23 Huyo mwanaume akasema,

    “Huyu sasa ni mfupa wa mifupa yangu

    na nyama ya nyama yangu,

    ataitwa ‘mwanamke,’

    kwa kuwa alitolewa katika mwanaume.”

    24 Kwa sababu hii mwanaume atamwacha baba yake na mama yake na kuambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.

  4. 12 Waheshimu baba yako na mama yako, ili upate kuishi siku nyingi katika nchi anayokupa Bwana Mungu wako.

  5. 15 Lakini msipoona vyema kumtumikia Bwana, chagueni hivi leo mtakayemtumikia, kama ni miungu ile ambayo baba zenu waliitumikia ngʼambo Frati, au miungu ya Waamori, ambao mnakaa katika nchi yao. Lakini mimi na nyumba yangu, tutamtumikia Bwana.”

  6. 6 Mfundishe mtoto njia impasayo kuiendea,

    naye hataiacha hata akiwa mzee.

  7. 3 Wana ni urithi utokao kwa Bwana,

    watoto ni zawadi kutoka kwake.

    4 Kama mishale mikononi mwa shujaa

    ndivyo walivyo wana awazaao mtu katika ujana wake.

    5 Heri mtu ambaye podo lake

    limejazwa nao.

    Hawataaibishwa wanaposhindana

    na adui zao langoni.

  8. 22 Ninyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana. 23 Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe kama vile Kristo alivyo kichwa cha Kanisa, ambalo ni mwili wake, naye Kristo ni Mwokozi wake. 24 Basi, kama vile Kanisa linavyomtii Kristo, vivyo hivyo na wake nao imewapasa kuwatii waume zao kwa kila jambo.

    25 Ninyi waume, wapendeni wake zenu, kama vile Kristo alivyolipenda Kanisa akajitoa kwa ajili yake 26 kusudi alifanye takatifu, akilitakasa kwa kuliosha kwa maji katika Neno lake, 27 apate kujiletea Kanisa tukufu lisilo na doa wala kunyanzi au waa lolote, bali takatifu na lisilo na hatia. 28 Vivyo hivyo imewapasa waume kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe.

  9. 26 Ndipo Mungu akasema, “Tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu, wakatawale juu ya samaki wa baharini na ndege wa angani, juu ya mifugo, juu ya dunia yote, na juu ya viumbe wote watambaao juu ya nchi.”

    27 Kwa hiyo Mungu akamuumba mtu kwa mfano wake mwenyewe,

    kwa mfano wa Mungu alimuumba;

    mwanaume na mwanamke aliwaumba.

    28 Mungu akawabariki na akawaambia, “Zaeni na mkaongezeke, mkaijaze tena dunia na kuitiisha. Mkatawale samaki wa baharini, ndege wa angani, na kila kiumbe hai kiendacho juu ya ardhi.”

  10. 4 Sikia, ee Israeli: Bwana Mungu wako, Bwana ni mmoja. 5 Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote. 6 Amri hizi ninazokupa leo zitakuwa katika moyo wako. 7 Wafundishe watoto wako kwa bidii. Nena kuhusu amri hizi uketipo nyumbani na wakati utembeapo njiani, ulalapo na uamkapo. 8 Zifunge kama alama juu ya mkono wako, na uzifunge juu ya paji la uso wako. 9 Ziandike kwenye miimo ya milango ya nyumba yako na juu ya malango yako.

  11. 2 Baadhi ya Mafarisayo wakaja ili kumjaribu kwa kumuuliza, “Je, ni halali mtu kumwacha mke wake?”

    3 Yesu akawajibu, “Je, Mose aliwaamuru nini?”

    4 Wakajibu, “Mose aliruhusu kwamba mume anaweza kumwandikia mkewe hati ya talaka na kumwacha.”

    5 Yesu akawaambia, “Mose aliwaandikia sheria hiyo kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu. 6 Lakini tangu mwanzo wa uumbaji, ‘Mungu aliwaumba mwanaume na mwanamke. 7 Kwa sababu hii mwanaume atamwacha baba yake na mama yake na kuambatana na mkewe, na hao wawili watakuwa mwili mmoja.’ 8 Kwa hiyo hawatakuwa wawili tena, bali mwili mmoja. 9 Basi, alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe.”

  12. 2 Basi, imempasa mwangalizi awe mtu asiye na lawama, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi, anayejitawala, anayeheshimika, mkarimu, ajuaye kufundisha, 3 asiwe mlevi, wala mkali bali awe mpole, asiwe mgomvi wala mpenda fedha. 4 Lazima aweze kuisimamia nyumba yake mwenyewe vizuri na kuhakikisha kwamba watoto wake wanamtii na kuwa na heshima kwa kila njia. 5 (Kwa maana kama mtu hajui jinsi ya kusimamia nyumba yake mwenyewe, atawezaje kuliangalia kanisa la Mungu?)

  13. 8 Kama mtu hawatunzi wale wa jamaa yake, hasa wale wa nyumbani mwake mwenyewe, ameikana imani, tena ni mbaya kuliko yeye asiyeamini.

  14. 4 Upendo huvumilia, upendo hufadhili, upendo hauoni wivu, hauna majivuno, hauna kiburi. 5 Haukosi kuwa na adabu, hautafuti mambo yake, haukasiriki upesi, hauweki kumbukumbu ya mabaya. 6 Upendo haufurahii mabaya bali hufurahi pamoja na kweli. 7 Upendo huvumilia yote, huamini yote, hutumaini yote, hustahimili yote.

    8 Upendo haushindwi kamwe. Lakini ukiwepo unabii, utakoma; zikiwepo lugha, zitakoma; yakiwepo maarifa, yatapita.

  15. 26 Kwa maana ninyi nyote mmekuwa watoto wa Mungu katika Kristo Yesu kwa njia ya imani. 27 Kwa maana wote mliobatizwa ndani ya Kristo, mmemvaa Kristo. 28 Wala hakuna tena Myahudi au Myunani, mtumwa au mtu huru, mwanaume wala mwanamke, maana nyote mmekuwa wamoja ndani ya Kristo Yesu. 29 Nanyi mkiwa ni mali ya Kristo, basi ninyi ni wa uzao wa Abrahamu na warithi sawasawa na ile ahadi.

  16. Wimbo wa kwenda juu. Wa Daudi.

    1 Tazama jinsi ilivyo vyema na kupendeza

    wakati ndugu wanapoishi pamoja katika umoja!

  17. 10 Kwa hiyo, kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema, hasa wale wa jamaa ya waaminio.

  18. 1 Kadhalika enyi wake, watiini waume zenu, ili kama kunao wasioamini lile neno, wapate kuvutwa na mwenendo wa wake zao pasipo neno, 2 kwa kuuona utakatifu na uchaji wa Mungu katika maisha yenu. 3 Kujipamba kwenu kusiwe kwa nje tu, kama vile kusuka nywele, kuvalia vitu vilivyofanyizwa kwa dhahabu na kwa mavazi. 4 Badala yake, kujipamba kwenu kuwe katika utu wenu wa moyoni, yaani uzuri usioharibika wa roho ya upole na utulivu, ambayo ni ya thamani sana machoni pa Mungu. 5 Kwa kuwa hivi ndivyo walivyokuwa wakijipamba wanawake watakatifu wa zamani, waliomtumaini Mungu. Wao walikuwa ni watiifu kwa waume zao, 6 kama Sara alivyomtii mumewe Abrahamu, hata akamwita bwana. Ninyi ni watoto wa Sara kama mkitenda yaliyo mema, bila kuogopa jambo lolote.

    7 Vivyo hivyo ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili, nanyi wapeni heshima mkitambua ya kuwa wao ni wenzi walio dhaifu, na kama warithi pamoja nanyi wa kipawa cha neema cha uzima, ili kusiwepo na chochote cha kuzuia maombi yenu.

  19. 3 Mke wako atakuwa kama mzabibu uzaao

    ndani ya nyumba yako;

    wana wako watakuwa kama machipukizi ya mizeituni

    kuizunguka meza yako.

    4 Hivyo ndivyo atakavyobarikiwa

    mtu amchaye Bwana.

    5 Bwana na akubariki kutoka Sayuni

    siku zote za maisha yako,

    na uone mafanikio ya Yerusalemu,

    6 nawe ujaliwe kuishi uone watoto wa watoto wako.

    Amani iwe juu ya Israeli.

  20. 29 Yeye aletaye taabu kwa jamaa yake atarithi tu upepo,

    naye mpumbavu atakuwa mtumishi wa wenye hekima.

  21. 20 Mwana mwenye hekima huleta furaha kwa baba yake,

    bali mtu mpumbavu humdharau mama yake.

  22. 33 Hata hivyo, kila mmoja wenu ampende mkewe kama anavyoipenda nafsi yake mwenyewe, naye mke lazima amheshimu mumewe.

  23. 11 Hili ndilo neno mlilolisikia tangu mwanzo: Kwamba imetupasa tupendane sisi kwa sisi. 12 Msiwe kama Kaini aliyekuwa wa yule mwovu akamuua ndugu yake. Basi kwa nini alimuua? Ni kwa sababu matendo yake Kaini yalikuwa mabaya na ya ndugu yake yalikuwa ya haki. 13 Ndugu zangu, ninyi msistaajabu kama ulimwengu ukiwachukia. 14 Sisi tunajua ya kwamba tumepita mautini kuingia uzimani, kwa sababu tunawapenda ndugu. Kila asiyempenda ndugu yake akaa mautini. 15 Yeyote amchukiaye ndugu yake ni muuaji, nanyi mwajua ya kwamba muuaji hana uzima wa milele ndani yake.

    16 Kwa namna hii twaweza kulijua pendo la Mungu: Kwa sababu Yesu Kristo aliutoa uhai wake kwa ajili yetu. Nasi imetupasa kuutoa uhai kwa ajili ya hao ndugu. 17 Ikiwa mtu anavyo vitu vya ulimwengu huu na akamwona ndugu yake ni mhitaji lakini asimhurumie, upendo wa Mungu wakaaje ndani ya mtu huyo? 18 Watoto wapendwa, tusipende kwa maneno au kwa ulimi bali kwa tendo na kweli.

  24. 5 Baba wa yatima, mtetezi wa wajane,

    ni Mungu katika makao yake matakatifu.

    6 Mungu huwaweka wapweke katika jamaa,

    huwaongoza wafungwa wakiimba,

    bali waasi huishi katika nchi kame.

  25. 13 Basi sasa, yanadumu mambo haya matatu: Imani, tumaini na upendo. Lakini lililo kuu miongoni mwa haya matatu ni upendo.

  26. 19 Twampenda yeye kwa sababu yeye alitupenda kwanza.

  27. 6 Wana wa wana ni taji la wazee,

    nao wazazi ni fahari ya watoto wao.

  28. 15 Yeye huamka kungali bado giza

    huwapa jamaa yake chakula

    na mafungu kwa watumishi wake wa kike.

    16 Huangalia shamba na kulinunua,

    kutokana na mapato yake hupanda shamba la mizabibu.

    17 Hufanya kazi zake kwa nguvu,

    mikono yake ina nguvu kwa ajili ya kazi zake.

  29. 46 Wakati alikuwa angali anazungumza na makutano, mama yake na ndugu zake wakasimama nje wakitaka kuongea naye. 47 Ndipo mtu mmoja akamwambia, “Tazama, mama yako na ndugu zako wamesimama nje, wanataka kuongea na wewe.”

    48 Lakini yeye akamjibu na kumwambia yule mtu, “Mama yangu ni nani, nao ndugu zangu ni nani?” 49 Akawanyooshea mkono wanafunzi wake, akasema, “Hawa hapa ndio mama yangu na ndugu zangu! 50 Kwa maana yeyote afanyaye mapenzi ya Baba yangu wa mbinguni, huyo ndiye ndugu yangu, na dada yangu na mama yangu.”

  30. 7 Kumcha Bwana ndicho chanzo cha maarifa,

    lakini wapumbavu hudharau hekima na adabu.

    8 Mwanangu, sikiliza mwongozo wa baba yako,

    wala usiyaache mafundisho ya mama yako.

    9 Hayo yatakuwa taji la maua la neema kichwani pako,

    na mkufu wa kuipamba shingo yako.

  31. 20 Mwanangu, zishike amri za baba yako,

    wala usiyaache mafundisho ya mama yako.

  32. 3 Napenda mfahamu kwamba kichwa cha kila mwanaume ni Kristo, na kichwa cha mwanamke ni mwanaume, nacho kichwa cha Kristo ni Mungu.

  33. 20 Ikiwa mtu atasema, “Nampenda Mungu,” lakini anamchukia ndugu yake, yeye ni mwongo. Kwa maana kila mtu asiyempenda ndugu yake ambaye anamwona, atampendaje Mungu asiyemuona?