99 Bible Verses About Church
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
-
36 “Kwa hiyo Israeli wote na wajue jambo hili kwa uhakika kwamba: Mungu amemfanya huyu Yesu, ambaye ninyi mlimsulubisha, kuwa Bwana na Kristo.”
37 Watu waliposikia maneno haya yakawachoma mioyo yao, wakawauliza Petro na wale mitume wengine, “Ndugu zetu tufanye nini?”
38 Petro akawajibu, “Tubuni, mkabatizwe kila mmoja wenu kwa jina la Yesu Kristo, ili mpate kusamehewa dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu. 39 Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu na watoto wenu, na kwa wote walio mbali, na kila mtu ambaye Bwana Mungu wetu atamwita amjie.”
40 Petro akawaonya kwa maneno mengine mengi na kuwasihi akisema, “Jiepusheni na kizazi hiki kilichopotoka.” 41 Wale wote waliopokea ujumbe wa Petro kwa furaha wakabatizwa na siku ile waliongezeka watu wapatao 3,000.
42 Nao wakawa wanadumu katika mafundisho ya mitume, katika ushirika, katika kumega mkate na katika kusali. 43 Kila mtu akaingiwa na hofu ya Mungu, nayo miujiza mingi na ishara zikafanywa na mitume. 44 Walioamini wote walikuwa mahali pamoja, nao walikuwa na kila kitu shirika. 45 Waliuza mali zao na vitu walivyokuwa navyo, kila mtu akagawiwa kadiri ya mahitaji yake. 46 Siku zote kwa moyo mmoja walikutana ndani ya ukumbi wa Hekalu, wakimega mkate nyumba kwa nyumba, wakila chakula chao kwa furaha na moyo mweupe, 47 wakimsifu Mungu na kuwapendeza watu wote. Kila siku Bwana akaliongeza kanisa wale waliokuwa wakiokolewa.
-
11 Ndiye aliweka wengine kuwa mitume, wengine kuwa manabii, wengine kuwa wainjilisti, wengine kuwa wachungaji na walimu, 12 kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu kwa ajili ya kazi za huduma, ili kwamba mwili wa Kristo upate kujengwa 13 mpaka sote tutakapoufikia umoja katika imani na katika kumjua sana Mwana wa Mungu na kuwa watu wazima kwa kufikia kimo cha ukamilifu wa Kristo.
14 Ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwatupwa huku na huku na kuchukuliwa na kila upepo wa mafundisho kwa hila za watu, kwa ujanja, kwa kufuata njia zao za udanganyifu. 15 Badala yake, tukiambiana kweli kwa upendo, katika mambo yote tukue, hata tumfikie yeye aliye kichwa, yaani, Kristo. 16 Kutoka kwake, mwili wote ukiwa umeungamanishwa na kushikamanishwa pamoja kwa msaada wa kila kiungo, hukua na kujijenga wenyewe katika upendo, wakati kila kiungo kinafanya kazi yake.
-
15 Akawauliza, “Je, ninyi mnasema mimi ni nani?”
16 Simoni Petro akamjibu, “Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.”
17 Naye Yesu akamwambia, “Heri wewe, Simoni Bar-Yona, kwa maana hili halikufunuliwa kwako na mwanadamu, bali na Baba yangu aliye mbinguni. 18 Nami nakuambia, wewe ndiwe Petro na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu, hata malango ya Kuzimu hayataweza kulishinda. 19 Nitakupa funguo za Ufalme wa mbinguni, na lolote utakalolifunga duniani litakuwa limefungwa Mbinguni, nalo lolote utakalofungua duniani litakuwa limefunguliwa mbinguni.”
-
22 Ninyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana. 23 Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe kama vile Kristo alivyo kichwa cha Kanisa, ambalo ni mwili wake, naye Kristo ni Mwokozi wake. 24 Basi, kama vile Kanisa linavyomtii Kristo, vivyo hivyo na wake nao imewapasa kuwatii waume zao kwa kila jambo.
25 Ninyi waume, wapendeni wake zenu, kama vile Kristo alivyolipenda Kanisa akajitoa kwa ajili yake 26 kusudi alifanye takatifu, akilitakasa kwa kuliosha kwa maji katika Neno lake, 27 apate kujiletea Kanisa tukufu lisilo na doa wala kunyanzi au waa lolote, bali takatifu na lisilo na hatia. 28 Vivyo hivyo imewapasa waume kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe. 29 Hakuna mtu anayeuchukia mwili wake mwenyewe, bali huulisha na kuutunza vizuri, kama Kristo anavyolitunza Kanisa lake. 30 Sisi tu viungo vya mwili wake. 31 “Kwa sababu hii, mwanaume atamwacha baba yake na mama yake, naye ataambatana na mkewe, na hao wawili watakuwa mwili mmoja.” 32 Siri hii ni kubwa, bali mimi nanena kuhusu Kristo na Kanisa. 33 Hata hivyo, kila mmoja wenu ampende mkewe kama anavyoipenda nafsi yake mwenyewe, naye mke lazima amheshimu mumewe.
-
9 Msiambiane uongo, kwa maana mmevua kabisa utu wenu wa kale pamoja na matendo yake, 10 nanyi mmevaa utu mpya, unaofanywa upya katika ufahamu sawasawa na mfano wa Muumba wake. 11 Hapa hakuna Myunani wala Myahudi, aliyetahiriwa wala asiyetahiriwa, asiyestaarabika wala aliyestaarabika, mtumwa wala mtu huru, bali Kristo ni yote, na ndani ya wote.
12 Kwa hiyo, kwa kuwa ninyi mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao sana, jivikeni moyo wa huruma, utu wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu. 13 Vumilianeni na kusameheana mtu akiwa na lalamiko lolote dhidi ya mwenzake. Sameheaneni kama vile Bwana alivyowasamehe ninyi. 14 Zaidi ya maadili haya yote jivikeni upendo, ambao ndio unaofunga kila kitu pamoja katika umoja mkamilifu.
15 Amani ya Kristo na itawale mioyoni mwenu, kwa kuwa ninyi kama viungo vya mwili mmoja mmeitiwa amani. Tena kuweni watu wa shukrani. 16 Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu, mkifundishana na kuonyana katika hekima yote, mkimwimbia Mungu zaburi, nyimbo na tenzi za rohoni, huku mkiwa na shukrani mioyoni mwenu. 17 Lolote mfanyalo, ikiwa ni kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba katika yeye.
-
4 Kama vile katika mwili mmoja tulivyo na viungo vingi, navyo viungo vyote havina kazi moja, 5 vivyo hivyo na sisi tulio wengi, tu mwili mmoja katika Kristo, nasi kila mmoja ni kiungo cha mwenzake. 6 Tuna karama zilizotofautiana kila mmoja kutokana na neema tuliyopewa. Kama ni unabii na tutoe unabii kwa kadiri ya imani. 7 Kama ni kuhudumu na tuhudumu, mwenye kufundisha na afundishe, 8 kama ni kutia moyo na atie moyo, kama ni kuchangia kwa ajili ya mahitaji ya wengine na atoe kwa ukarimu, kama ni uongozi na aongoze kwa bidii, kama ni kuhurumia wengine na afanye hivyo kwa furaha.
-
26 Basi tuseme nini ndugu zangu? Mnapokutana pamoja, kila mmoja ana wimbo, au neno la mafundisho, au ufunuo, lugha mpya au atatafsiri. Mambo yote yatendeke kwa ajili ya kulijenga kanisa. 27 Kama mtu yeyote akinena kwa lugha, basi waseme watu wawili au watatu si zaidi, mmoja baada ya mwingine na lazima awepo mtu wa kutafsiri. 28 Lakini kama hakuna mtu wa kutafsiri, hao watu na wanyamaze kimya kanisani na wanene na nafsi zao wenyewe na Mungu.
29 Manabii wawili au watatu wanene na wengine wapime yale yasemwayo. 30 Kama mtu yeyote aliyeketi karibu, akipata ufunuo, basi yule wa kwanza na anyamaze. 31 Kwa maana wote mnaweza kutoa unabii, mmoja baada ya mwingine, ili kila mtu apate kufundishwa na kutiwa moyo. 32 Roho za manabii huwatii manabii. 33 Kwa maana Mungu si Mungu wa machafuko bali ni Mungu wa amani.
Kama ilivyo katika makusanyiko yote ya watakatifu, 34 wanawake wanapaswa kuwa kimya kanisani. Hawaruhusiwi kusema, bali wanyenyekee kama sheria isemavyo. 35 Kama wakitaka kuuliza kuhusu jambo lolote, wawaulize waume zao nyumbani. Kwa maana ni aibu kwa mwanamke kuzungumza kanisani.
36 Je, neno la Mungu lilianzia kwenu? Au ni ninyi tu ambao neno la Mungu limewafikia? 37 Kama mtu yeyote akidhani kwamba yeye ni nabii, au ana karama za rohoni, basi na akubali kwamba haya ninayoandika ni maagizo kutoka kwa Bwana. 38 Kama mtu akipuuza jambo hili yeye mwenyewe atapuuzwa.
39 Kwa hiyo ndugu zangu, takeni sana kutoa unabii na msikataze watu kusema kwa lugha. 40 Lakini kila kitu kitendeke kwa heshima na kwa utaratibu.
-
15 Yeye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. 16 Kwake yeye vitu vyote vilivyoko mbinguni na juu ya nchi viliumbwa: vitu vinavyoonekana na visivyoonekana, viwe ni viti vya enzi au falme, au wenye mamlaka au watawala; vitu vyote viliumbwa na yeye na kwa ajili yake. 17 Yeye alikuwepo kabla ya vitu vyote, na katika yeye vitu vyote vinashikamana pamoja. 18 Yeye ndiye kichwa cha mwili, yaani kanisa, naye ndiye mwanzo na mzaliwa wa kwanza kutoka kwa wafu, ili yeye awe mkuu katika vitu vyote. 19 Kwa kuwa ilimpendeza Mungu kwamba utimilifu wake wote ukae ndani yake, 20 na kwa njia yake aweze kuvipatanisha vitu vyote na yeye mwenyewe, viwe ni vitu vilivyo duniani au vilivyo mbinguni, kwa kufanya amani kwa damu yake, iliyomwagika msalabani.
-
1 Kwa wazee waliomo miongoni mwenu, nawasihi mimi nikiwa mzee mwenzenu, shahidi wa mateso ya Kristo, na mshiriki katika utukufu utakaofunuliwa: 2 lichungeni kundi la Mungu mlilokabidhiwa, mkitumika kama waangalizi, si kwa kulazimishwa bali kwa hiari, kama Mungu anavyowataka mwe; si kwa tamaa ya fedha, bali mlio na bidii katika kutumika. 3 Msijifanye mabwana juu ya wale walio chini ya uangalizi wenu, bali kuweni vielelezo kwa hilo kundi. 4 Naye Mchungaji Mkuu atakapodhihirishwa, mtapokea taji ya utukufu isiyoharibika.
5 Vivyo hivyo, ninyi mlio vijana watiini wazee. Nanyi nyote imewapasa kujivika unyenyekevu kila mtu kwa mwenzake, kwa kuwa,
“Mungu huwapinga wenye kiburi,
lakini huwapa wanyenyekevu neema.”
6 Basi, nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake. 7 Mtwikeni yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana na mambo yenu.
8 Mwe na kiasi na kukesha, maana adui yenu ibilisi huzungukazunguka kama simba angurumaye akitafuta mtu ili apate kummeza. 9 Mpingeni, mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kwamba mateso kama hayo yanawapata ndugu zenu pote duniani.
-
Mateso Na Kuenea Kwa Injili
1 Basi ikawa katika siku hizo, wakati idadi ya wanafunzi ilipokuwa ikiongezeka sana, palitokea manungʼuniko kati ya Wayahudi wa Kiyunani, dhidi ya Waebrania kwa sababu wajane wao walisahaulika katika mgawanyo wa chakula wa kila siku. 2 Wale mitume kumi na wawili wakakusanya wanafunzi wote pamoja wakasema, “Haitakuwa vyema sisi kuacha huduma ya neno la Mungu ili kuhudumu mezani. 3 Kwa hiyo ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, watu wenye sifa njema, waliojawa na Roho Mtakatifu na hekima, ambao tunaweza kuwakabidhi kazi hii, 4 nasi tutatumia muda wetu kuomba na huduma ya neno.”
5 Yale waliyosema yakawapendeza watu wote, nao wakamchagua Stefano (mtu aliyejawa na imani na Roho Mtakatifu) pamoja na Filipo, Prokoro, Nikanori, Timoni, Parmena na Nikolao, mwongofu kutoka Antiokia. 6 Wakawaleta watu hawa mbele ya mitume, nao wakawaombea na kuwawekea mikono juu yao.
-
8 Maana mtu mmoja kwa Roho hupewa neno la hekima na mwingine neno la maarifa kwa Roho huyo huyo. 9 Mtu mwingine imani kwa huyo Roho na mwingine karama za kuponya kwa huyo Roho mmoja. 10 Kwa mwingine matendo ya miujiza, kwa mwingine unabii kwa mwingine kupambanua roho, kwa mwingine aina mbalimbali za lugha, na kwa mwingine bado, tafsiri za lugha. 11 Haya yote hufanywa na huyo huyo Roho mmoja, Roho naye humgawia kila mtu, kama apendavyo.
-
1 Basi, mimi niliye mfungwa wa Bwana, nawasihi mwenende kama inavyostahili wito wenu mlioitiwa. 2 Kwa unyenyekevu wote na upole, mkiwa wavumilivu, mkichukuliana kwa upendo. 3 Jitahidini kudumisha umoja wa Roho katika kifungo cha amani. 4 Kuna mwili mmoja na Roho mmoja, kama vile mlivyoitwa katika tumaini moja. 5 Tena kuna Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja, 6 Mungu mmoja ambaye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote, katika yote na ndani ya yote.
-
24 Tuangaliane na kuhimizana sisi kwa sisi katika upendo na katika kutenda mema. 25 Wala tusiache kukutana pamoja, kama wengine walivyo na desturi, bali tuhimizane sisi kwa sisi kadiri tuonavyo Siku ile inakaribia.
-
26 Kwa maana ninyi nyote mmekuwa watoto wa Mungu katika Kristo Yesu kwa njia ya imani. 27 Kwa maana wote mliobatizwa ndani ya Kristo, mmemvaa Kristo. 28 Wala hakuna tena Myahudi au Myunani, mtumwa au mtu huru, mwanaume wala mwanamke, maana nyote mmekuwa wamoja ndani ya Kristo Yesu. 29 Nanyi mkiwa ni mali ya Kristo, basi ninyi ni wa uzao wa Abrahamu na warithi sawasawa na ile ahadi.
-
28 Jilindeni nafsi zenu na mlilinde lile kundi lote ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi wake. Lichungeni kanisa lake Mungu alilolinunua kwa damu yake mwenyewe. 29 Najua kwamba baada yangu kuondoka, mbwa mwitu wakali watakuja katikati yenu ambao hawatalihurumia kundi. 30 Hata kutoka miongoni mwenu watainuka watu na kuupotosha ukweli ili wawavute wanafunzi wawafuate. 31 Hivyo jilindeni! Kumbukeni kwamba kwa miaka mitatu sikuacha kamwe kuwaonya kila mmoja kwa machozi usiku na mchana.
-
14 Kwa maana yeye mwenyewe ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi tuliokuwa wawili, yaani, Wayahudi na watu wa Mataifa, tuwe wamoja kwa kuvunja kizuizi na kubomoa ule ukuta wa uadui uliokuwa kati yetu, 15 kwa kuibatilisha ile sheria pamoja na amri zake na maagizo yake alipoutoa mwili wake, ili apate kufanya ndani yake mtu mmoja mpya badala ya hao wawili, hivyo akifanya amani, 16 naye katika mwili huu mmoja awapatanishe wote wawili na Mungu kupitia msalaba, ili kwa huo msalaba akaangamiza uadui wao. 17 Alikuja na kuhubiri amani kwenu ninyi mliokuwa mbali na pia akahubiri amani kwao waliokuwa karibu. 18 Kwa maana kwa kupitia kwake, sisi sote tunaweza kumkaribia Baba katika Roho mmoja.
19 Hivyo basi, ninyi sasa si wageni tena wala wapitaji, bali mmekuwa wenyeji pamoja na watakatifu na pia jamaa wa nyumbani mwake Mungu. 20 Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ndiye jiwe kuu la pembeni. 21 Ndani yake jengo lote limeshikamanishwa pamoja na kusimamishwa ili kuwa Hekalu takatifu katika Bwana. 22 Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja ili mpate kuwa makao ambayo Mungu anaishi ndani yake kwa njia ya Roho wake.
-
16 Basi wale wanafunzi kumi na mmoja wakaenda hadi Galilaya kwenye ule mlima ambao Yesu alikuwa amewaagiza. 17 Walipomwona, wakamwabudu; lakini baadhi yao wakaona shaka. 18 Yesu akawajia na kusema, “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. 19 Kwa sababu hii, enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, 20 nanyi wafundisheni kuyashika mambo yote niliyowaamuru ninyi. Hakika mimi niko pamoja nanyi siku zote, hadi mwisho wa nyakati.”
-
15 “Kama ndugu yako akikukosea, nenda ukamwonyeshe kosa lake, kati yenu ninyi wawili peke yenu. Kama akikusikiliza, utakuwa umempata tena ndugu yako. 16 Lakini kama hatakusikiliza, nenda na mtu mwingine mmoja au wawili ili kila neno lithibitishwe kwa ushahidi wa mashahidi wawili au watatu. 17 Kama akikataa kuwasikiliza hao, liambie kanisa. Naye kama akikataa hata kulisikiliza kanisa, basi awe kwenu kama mtu asiyeamini au mtoza ushuru.
18 “Amin, nawaambia, lolote mtakalolifunga duniani litakuwa limefungwa mbinguni, na lolote mtakalolifungua duniani litakuwa limefunguliwa mbinguni.
19 “Tena nawaambia, ikiwa wawili wenu watakubaliana duniani kuhusu jambo lolote watakaloomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni. 20 Kwa kuwa wanapokusanyika pamoja watu wawili au watatu kwa Jina langu, mimi niko papo hapo pamoja nao.”
21 Ndipo Petro akamjia Yesu na kumuuliza, “Bwana, ndugu yangu anikosee mara ngapi nami nimsamehe? Je, hata mara saba?”
22 Yesu akamjibu, “Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini.
-
9 Lakini ninyi ni taifa teule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu walio milki ya Mungu, mlioitwa ili kutangaza sifa zake yeye aliyewaita kutoka gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu. 10 Mwanzo ninyi mlikuwa si taifa, lakini sasa ninyi ni taifa la Mungu. Mwanzo mlikuwa hamjapata rehema, lakini sasa mmepata rehema.
-
9 Mungu ambaye mmeitwa naye ili mwe na ushirika na Mwanawe Yesu Kristo, Bwana wetu ni mwaminifu.
10 Nawasihi ndugu zangu, katika Jina la Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba mpatane nia zenu ninyi kwa ninyi, ili pasiwepo na matengano katikati yenu na kwamba mwe na umoja kikamilifu katika nia na katika kusudi. 11 Ndugu zangu, nimepata habari kutoka kwa baadhi ya watu wa nyumbani mwa Kloe kwamba kuna magomvi katikati yenu. 12 Maana yangu ni kwamba: Mmoja wenu husema, “Mimi ni wa Paulo”; mwingine, “Mimi ni wa Apolo”; mwingine, “Mimi ni wa Kefa,” na mwingine, “Mimi ni wa Kristo.”
13 Je, Kristo amegawanyika? Je, Paulo ndiye alisulubishwa kwa ajili yenu? Je, mlibatizwa kwa jina la Paulo?
-
11 Kwa maana hakuna mtu yeyote awezaye kuweka msingi mwingine wowote isipokuwa ule uliokwisha kuwekwa, ambao ni Yesu Kristo. 12 Kama mtu yeyote akijenga juu ya msingi huu kwa kutumia dhahabu, fedha, vito vya thamani, miti, majani au nyasi, 13 kazi yake itaonekana ilivyo, kwa kuwa Siku ile itaidhihirisha. Itadhihirishwa kwa moto, nao moto utapima ubora wa kazi ya kila mtu. 14 Kama kile alichojenga kitabaki, atapokea thawabu yake. 15 Kama kazi kitateketea, atapata hasara, ila yeye mwenyewe ataokolewa, lakini tu kama mtu aliyenusurika kwenye moto.
16 Je, hamjui ya kwamba ninyi wenyewe ni hekalu la Mungu na kwamba Roho wa Mungu anakaa ndani yenu? 17 Kama mtu yeyote akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamwangamiza; kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, na ninyi ndiyo hilo hekalu.
-
5 Sababu ya mimi kukuacha huko Krete ni ili uweke utaratibu mambo yale yaliyosalia na kuwaweka wazee wa kanisa katika kila mji, kama nilivyokuagiza. 6 Mzee wa kanisa asiwe na lawama, awe mume wa mke mmoja, mtu ambaye watoto wake ni waaminio na wala hawashtakiwi kwa ufisadi. 7 Kwa kuwa mwangalizi, kama wakili wa Mungu, imempasa kuwa mtu asiye na lawama, asiwe mwenye majivuno au mwepesi wa hasira, wala mlevi, wala asiwe mtu mwenye tamaa ya mapato yasiyo ya halali. 8 Bali awe mkarimu, anayependa mema, mwenye kiasi, mwenye haki, mwadilifu, mnyofu, mtakatifu na mwenye kuitawala nafsi yake. 9 Inampasa alishike kwa uthabiti lile neno la imani kama lilivyofundishwa, kusudi aweze kuwaonya wengine kwa mafundisho manyofu na kuwakanusha wale wanaopingana nayo.
-
13 Naweza kuyafanya mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.
14 Lakini, mlifanya vyema kushiriki nami katika taabu zangu. 15 Zaidi ya hayo, ninyi Wafilipi mnajua kwamba siku za kwanza nilipoanza kuhubiri Injili, nilipoondoka Makedonia, hakuna kanisa jingine lililoshiriki nami katika masuala ya kutoa na kupokea isipokuwa ninyi. 16 Kwa maana hata nilipokuwa huko Thesalonike, mliniletea msaada kwa ajili ya mahitaji yangu zaidi ya mara moja. 17 Si kwamba natafuta sana yale matoleo, bali natafuta sana ile faida itakayozidi sana kwa upande wenu. 18 Nimelipwa kikamilifu hata na zaidi; nimetoshelezwa kabisa sasa, kwa kuwa nimepokea kutoka kwa Epafrodito vile vitu mlivyonitumia, sadaka yenye harufu nzuri, dhabihu inayokubalika na ya kumpendeza Mungu. 19 Naye Mungu wangu atawajaza ninyi na kila mnachohitaji kwa kadiri ya utajiri wake katika utukufu ndani ya Kristo Yesu.
-
Safari Ya Kwanza Ya Paulo Kueneza Injili
1 Katika kanisa huko Antiokia ya Shamu walikuwako manabii na walimu, yaani: Barnaba, Simeoni aitwaye Nigeri, Lukio Mkirene, Manaeni aliyekuwa amelelewa pamoja na Mfalme Herode Agripa, na Sauli. 2 Walipokuwa wakimwabudu Bwana na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, “Nitengeeni Sauli na Barnaba kwa kazi ile maalum niliyowaitia.” 3 Ndipo baada ya kufunga na kuomba, wakawawekea mikono yao na wakawatuma waende zao.
-
8 Vivyo hivyo, mashemasi nao wawe watu wanaostahili heshima, wasiwe wenye kauli mbili au wenye kujifurahisha kwa mvinyo, wala wanaotamani faida isiyo halali. 9 Inawapasa kushikamana sana na ile siri ya imani kwa dhamiri safi. 10 Ni lazima wapimwe kwanza; kisha kama hakuna neno dhidi yao, basi na waruhusiwe kuhudumu kama mashemasi.
11 Vivyo hivyo, wake zao wawe wanawake wanaostahili heshima, wasio wasingiziaji, bali wawe na kiasi na waaminifu katika kila jambo.
12 Shemasi awe mume wa mke mmoja na inampasa aweze kusimamia watoto wake na watu wa nyumbani mwake vyema. 13 Wale ambao wamehudumu vyema katika huduma ya ushemasi hujipatia msimamo bora na ujasiri mkubwa katika imani yao ndani ya Kristo Yesu.
14 Ingawa ninatarajia kuja kwako hivi karibuni, ninakuandikia maagizo haya sasa ili kwamba, 15 kama nikikawia, utajua jinsi iwapasavyo watu kuenenda katika nyumba ya Mungu, ambayo ndiyo kanisa la Mungu aliye hai, lililo nguzo na msingi wa kweli.
-
12 Kama vile mwili ulivyo mmoja nao una viungo vingi, navyo viungo vyote vya mwili ingawa ni vingi, ni mwili mmoja, vivyo hivyo na Kristo. 13 Kwa maana katika Roho mmoja wote tulibatizwa katika mwili mmoja, kama ni Wayahudi au Wayunani, kama ni watumwa au watu huru, nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja.
14 Basi mwili si kiungo kimoja, bali ni viungo vingi. 15 Kama mguu ungesema, “Kwa kuwa mimi si mkono basi mimi si wa mwili,” hiyo isingefanya huo mguu usiwe sehemu ya mwili. 16 Na kama sikio lingesema, “Kwa kuwa mimi si jicho, basi mimi si wa mwili,” hiyo isingefanya hilo sikio lisiwe sehemu ya mwili. 17 Kama mwili wote ungelikuwa jicho, kusikia kungekuwa wapi? Au kama mwili wote ungelikuwa sikio, kunusa kungekuwa wapi? 18 Lakini kama ilivyo, Mungu ameweka viungo katika mwili, kila kimoja kama alivyopenda. 19 Kama vyote vingekuwa kiungo kimoja, mwili ungekuwa wapi? 20 Kama ulivyo, una viungo vingi, lakini mwili ni mmoja.
21 Jicho haliwezi kuuambia mkono, “Sina haja nawe!” Wala kichwa hakiwezi kuiambia miguu, “Sina haja na ninyi!” 22 Lakini badala yake, vile viungo vya mwili vinavyoonekana kuwa dhaifu, ndivyo ambavyo ni vya muhimu sana. 23 Navyo vile viungo tunavyoviona havina heshima, ndivyo tunavipa heshima maalum. Vile viungo vya mwili ambavyo havina uzuri, tunavipa heshima ya pekee; 24 wakati vile viungo vyenye uzuri havihitaji utunzaji wa pekee. Lakini Mungu ameviweka pamoja viungo vya mwili na akavipa heshima zaidi vile vilivyopungukiwa, 25 ili pasiwe na mafarakano katika mwili, bali viungo vyote vihudumiane kwa usawa kila kimoja na mwenzake. 26 Kama kiungo kimoja kikiumia, viungo vyote huumia pamoja nacho, kama kiungo kimoja kikipewa heshima, viungo vyote hufurahi pamoja nacho.
27 Sasa ninyi ni mwili wa Kristo na kila mmoja wenu ni sehemu ya huo mwili. 28 Mungu ameweka katika kanisa, kwanza mitume, pili manabii, tatu walimu, kisha watenda miujiza, pia karama za kuponya, karama za kusaidiana, karama za uongozi, aina mbalimbali za lugha. 29 Je, wote ni mitume? Je, wote ni manabii? Je, wote ni walimu? Je, wote wanatenda miujiza? 30 Je, wote wana karama ya kuponya? Je, wote hunena kwa lugha mpya? Je, wote wanatafsiri? 31 Basi tamanini sana karama zilizo kuu.
Nami nitawaonyesha njia iliyo bora zaidi.
-
14 “Mimi ndimi mchungaji mwema. Ninawajua kondoo wangu nao kondoo wangu wananijua. 15 Kama vile Baba anavyonijua mimi, nami ninavyomjua Baba, nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo. 16 Ninao kondoo wengine ambao si wa zizi hili, inanipasa kuwaleta, nao wataisikia sauti yangu, hivyo patakuwa na kundi moja na mchungaji mmoja.
-
18 Hamjaufikia mlima ule uwezao kuguswa na ambao unawaka moto; wala kwenye giza, utusitusi na dhoruba; 19 kwenye mlio wa tarumbeta, au kwenye sauti isemayo maneno ya kutisha kiasi ambacho wale walioisikia waliomba wasiambiwe neno jingine zaidi, 20 kwa sababu hawangeweza kustahimili neno lile lililoamriwa: “Hata kama mnyama atagusa mlima huu, atapigwa mawe.” 21 Waliyoyaona yalikuwa ya kutisha kiasi kwamba Mose alisema, “Ninatetemeka kwa hofu.”
22 Lakini ninyi mmekuja Mlima Sayuni, Yerusalemu ya mbinguni, mji wa Mungu aliye hai. Mmekuja penye kusanyiko kubwa la malaika maelfu kwa maelfu wasiohesabika wanaoshangilia, 23 kwenye kanisa la wazaliwa wa kwanza wa Mungu, ambao majina yao yameandikwa mbinguni. Mmekuja kwa Mungu, mhukumu wa watu wote, kwenye roho za wenye haki waliokamilishwa, 24 kwa Yesu mpatanishi wa agano jipya, na kwa damu iliyonyunyizwa, ile inenayo mambo mema kuliko damu ya Abeli.
-
1 Kisha nikaona mbingu mpya na nchi mpya, kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza vimekwisha kupita, wala hapakuwepo na bahari tena. 2 Nikaona Mji Mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, ukiwa umeandaliwa kama bibi arusi aliyepambwa kwa ajili ya mumewe. 3 Nami nikasikia sauti kubwa kutoka kile kiti cha enzi ikisema, “Sasa makao ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atakaa pamoja nao. Yeye atakuwa Mungu wao nao watakuwa watu wake, naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao. 4 Atafuta kila chozi kutoka macho yao. Mauti haitakuwepo tena, wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu, kwa maana mambo ya kwanza yamekwisha kupita.”
5 Naye yule aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi akasema, “Tazama, nayafanya mambo yote kuwa mapya!” Kisha akasema, “Andika haya, maana maneno haya ni ya kuaminika tena ni kweli.”
-
20 “Siwaombei hawa peke yao, bali nawaombea na wale wote watakaoniamini kupitia neno lao 21 ili wawe na umoja kama vile wewe Baba ulivyo ndani yangu na mimi nilivyo ndani yako, wao nao wawe ndani yetu, ili ulimwengu upate kuamini ya kuwa wewe ndiye uliyenituma mimi. 22 Utukufu ule ulionipa nimewapa wao, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo wamoja. 23 Mimi ndani yako na wewe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja na ulimwengu upate kujua ya kuwa umenituma, nami nimewapenda wao kama unavyonipenda mimi.
-
10 Kwa hiyo, kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema, hasa wale wa jamaa ya waaminio.
-
14 Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio watoto wa Mungu. 15 Kwa maana hamkupokea roho ya utumwa iwaleteayo tena hofu, bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambaye kwa yeye twalia, “Abba, yaani, Baba,” 16 Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu ya kwamba sisi tu watoto wa Mungu. 17 Hivyo, ikiwa sisi ni watoto, basi tu warithi, warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo, naam, tukiteswa pamoja naye tupate pia kutukuzwa pamoja naye.
-
1 Paulo, niliyeitwa kwa mapenzi ya Mungu kuwa mtume wa Kristo Yesu, na Sosthene ndugu yetu.
2 Kwa kanisa la Mungu lililoko Korintho, kwa wale waliotakaswa katika Kristo Yesu na walioitwa kuwa watakatifu, pamoja na wale wote ambao kila mahali wanaliitia Jina la Kristo Yesu Bwana wetu, aliye Bwana wao na wetu pia:
3 Neema na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo iwe nanyi.
-
14 Msifungiwe nira pamoja na watu wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa, kwa maana pana uhusiano gani kati ya haki na uovu? Au kuna ushirika gani kati ya nuru na giza? 15 Kuna mapatano gani kati ya Kristo na Beliari? Yeye aaminiye ana sehemu gani na yeye asiyeamini? 16 Kuna mapatano gani kati ya Hekalu la Mungu na sanamu? Kwa kuwa sisi tu Hekalu la Mungu aliye hai. Kama Mungu alivyosema: “Nitakaa pamoja nao na kutembea katikati yao, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.”
17 “Kwa hiyo tokeni miongoni mwao,
mkatengwe nao,
asema Bwana.
Msiguse kitu chochote kilicho najisi,
nami nitawakaribisha.”
18 “Mimi nitakuwa Baba kwenu,
nanyi mtakuwa wanangu na binti zangu,
asema Bwana Mwenyezi.”
-
22 Naye Mungu ameweka vitu vyote viwe chini ya miguu yake na amemfanya yeye awe kichwa cha vitu vyote kwa ajili ya Kanisa, 23 ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake yeye aliye yote katika yote.
-
1 Kwa habari zenu, mlikuwa wafu katika makosa na dhambi zenu, 2 ambazo mlizitenda mlipofuatisha namna ya ulimwengu huu na za yule mtawala wa ufalme wa anga, yule roho atendaye kazi sasa ndani ya wale wasiotii. 3 Sisi sote pia tuliishi katikati yao hapo zamani, tukitimiza tamaa za asili yetu ya dhambi na kufuata tamaa zake na mawazo yake. Nasi kwa asili tulikuwa wana wa ghadhabu, kama mtu mwingine yeyote. 4 Lakini Mungu kwa upendo wake mwingi kwetu sisi, ambaye ni mwingi wa rehema, 5 hata tulipokuwa wafu kwa ajili ya makosa yetu, alitufanya tuwe hai pamoja na Kristo Yesu, yaani, mmeokolewa kwa neema. 6 Mungu alitufufua pamoja na Kristo na kutuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho katika Kristo Yesu, 7 ili katika ule ulimwengu ujao apate kuonyesha wingi wa neema yake isiyopimika, iliyodhihirishwa kwetu kwa wema wake ndani ya Kristo Yesu. 8 Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani, wala si kwa matendo yenu mema. Hii ni zawadi kutoka kwa Mungu, 9 si kwa matendo, ili mtu yeyote asije akajisifu. 10 Kwa maana sisi ni kazi ya mikono ya Mungu, tulioumbwa katika Kristo Yesu, ili tupate kutenda matendo mema, ambayo Mungu alitangulia kuyaandaa tupate kuishi katika hayo.
-
17 Wazee wa kanisa wanaoongoza shughuli za kanisa vizuri wanastahili heshima mara mbili, hasa wale ambao kazi yao ni kuhubiri na kufundisha. 18 Kwa maana Maandiko husema, “Usimfunge maksai kinywa apurapo nafaka,” tena, “Mfanyakazi anastahili mshahara wake.”
-
1 Kwa hiyo, wekeni mbali nanyi uovu wote na udanganyifu wote, unafiki, wivu na masingizio ya kila namna. 2 Kama watoto wachanga, waliozaliwa sasa, yatamanini maziwa ya kiroho yasiyochanganywa na kitu kingine chochote, ili kwa hayo mpate kukua katika wokovu, 3 ikiwa kweli mmeonja ya kwamba Bwana ni mwema.
4 Mnapokuja kwake, yeye aliye Jiwe lililo hai, lililokataliwa na wanadamu bali kwa Mungu ni teule na la thamani kwake, 5 ninyi nanyi, kama mawe yaliyo hai, mnajengwa kuwa nyumba ya kiroho, ili mpate kuwa ukuhani mtakatifu, mkitoa dhabihu za kiroho zinazokubaliwa na Mungu kwa njia ya Yesu Kristo.
-
25 Kisha Barnaba akaenda Tarso kumtafuta Sauli, 26 naye alipompata akamleta Antiokia. Hivyo kwa mwaka mzima Barnaba na Sauli wakakutana na kanisa na kufundisha idadi kubwa ya watu. Ilikuwa ni katika kanisa la Antiokia kwa mara ya kwanza wanafunzi waliitwa Wakristo.
27 Wakati huo manabii walishuka toka Yerusalemu hadi Antiokia. 28 Mmoja wao, jina lake Agabo, akasimama akatabiri kwa uweza wa Roho Mtakatifu kwamba njaa kubwa itaenea ulimwengu mzima. Njaa hiyo ilitokea wakati wa utawala wa Klaudio. 29 Mitume wakaamua kwamba kila mtu, kulingana na uwezo alio nao, atoe msaada kwa ajili ya ndugu wanaoishi Uyahudi. 30 Wakafanya hivyo, misaada yao ikapelekwa kwa wazee kwa mikono ya Barnaba na Sauli.
-
10 Heri wanaoteswa kwa sababu ya haki,
maana Ufalme wa Mbinguni ni wao.
11 “Heri ninyi watu watakapowashutumu, na kuwatesa na kunena dhidi yenu mabaya ya aina zote kwa uongo kwa ajili yangu. 12 Furahini na kushangilia kwa maana thawabu yenu ni kubwa mbinguni, kwa kuwa hivyo ndivyo walivyowatesa manabii waliokuwa kabla yenu.
13 “Ninyi ni chumvi ya ulimwengu. Lakini chumvi ikipoteza ladha yake, yawezaje kurudishiwa ladha yake tena? Haifai tena kwa kitu chochote, ila kutupwa nje ikanyagwe na watu.
14 “Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji uliojengwa kilimani hauwezi kufichika. 15 Wala watu hawawashi taa na kuifunika kwa bakuli. Badala yake, huiweka kwenye kinara chake, nayo hutoa mwanga kwa kila mtu aliyemo ndani ya ile nyumba. 16 Vivyo hivyo, nuru yenu iangaze mbele ya watu, ili wapate kuona matendo yenu mema wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.
-
12 Mtu yeyote asikudharau kwa kuwa wewe ni kijana, bali uwe kielelezo kizuri kwa waumini katika usemi, mwenendo, upendo, imani na usafi. 13 Fanya bidii kusoma Maandiko hadharani, kuhubiri na kufundisha, mpaka nitakapokuja. 14 Usiache kutumia kipawa kilicho ndani yako, ambacho ulipewa kwa neno la unabii wakati wazee walikuwekea mikono.
15 Uwe na bidii katika mambo haya; ujitolee kwa ajili ya mambo haya kikamilifu, ili kila mtu aone kuendelea kwako.
-
31 Ndipo kanisa katika Uyahudi wote, Galilaya na Samaria likafurahia wakati wa amani. Likatiwa nguvu, na kwa faraja ya Roho Mtakatifu, idadi yake ikazidi kuongezeka, na likaendelea kudumu katika kumcha Bwana.
Matendo Ya Petro
32 Petro alipokuwa akisafiri sehemu mbalimbali, alikwenda kuwatembelea watakatifu walioishi huko Lida.
-
22 Mitume na wazee pamoja na kanisa lote, wakaamua kuwachagua baadhi ya watu wao na kuwatuma Antiokia pamoja na Paulo na Barnaba. Wakamchagua Yuda aitwaye Barsaba pamoja na Sila, watu wawili waliokuwa viongozi miongoni mwa ndugu. 23 Wakatumwa na barua ifuatayo:
Sisi mitume na wazee, ndugu zenu,
Kwa ndugu Mataifa mlioamini mlioko Antiokia, Shamu na Kilikia:
Salamu.
-
13 Je, mtu yeyote miongoni mwenu amepatwa na taabu? Basi inampasa aombe. Je, kuna yeyote mwenye furaha? Basi na aimbe nyimbo za kusifu. 14 Je, kuna yeyote miongoni mwenu aliye mgonjwa? Basi inampasa awaite wazee wa kanisa wamwombee na kumpaka mafuta kwa Jina la Bwana. 15 Kule kuomba kwa imani kutamwokoa huyo mgonjwa, naye Bwana atamwinua na kama ametenda dhambi, atasamehewa. 16 Kwa hiyo ungamianeni dhambi zenu ninyi kwa ninyi na kuombeana ili mpate kuponywa. Maombi ya mwenye haki yana nguvu tena yanafaa sana.
-
1 Petro, mtume wa Yesu Kristo:
Kwa wateule wa Mungu, wageni katika ulimwengu, waliotawanyika kote katika Ponto, Galatia, Kapadokia, Asia na Bithinia. 2 Ni ninyi ambao mlichaguliwa tangu mwanzo na Mungu Baba kulingana na alivyotangulia kuwajua, kupitia kwa kazi ya utakaso wa Roho, katika utiifu kwa Yesu Kristo na kunyunyiziwa damu yake:
Neema na amani ziwe kwenu kwa wingi.
-
8 Zaidi ya yote, dumuni katika upendo kwa maana upendo husitiri wingi wa dhambi. 9 Kuweni wakarimu kila mtu na mwenzake pasipo manungʼuniko. 10 Kila mmoja na atumie kipawa chochote alichopewa kuwahudumia wengine, kama mawakili waaminifu wa neema mbalimbali za Mungu. 11 Yeyote asemaye hana budi kusema kama mtu asemaye maneno ya Mungu mwenyewe. Yeyote ahudumuye hana budi kuhudumu kwa nguvu zile anazopewa na Mungu, ili Mungu apate kutukuzwa katika mambo yote kwa njia ya Yesu Kristo. Utukufu na uweza una yeye milele na milele. Amen.
-
32 Wale walioamini wote walikuwa na moyo mmoja na nia moja. Wala hakuna hata mmoja aliyesema chochote alichokuwa nacho ni mali yake mwenyewe, lakini walishirikiana kila kitu walichokuwa nacho. 33 Mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwa Bwana Yesu kwa nguvu nyingi na neema ya Mungu ilikuwa juu yao wote. 34 Wala hapakuwepo mtu yeyote miongoni mwao aliyekuwa mhitaji, kwa sababu mara kwa mara wale waliokuwa na mashamba na nyumba waliviuza, wakaleta thamani ya vitu vilivyouzwa, 35 wakaiweka miguuni pa mitume, kila mtu akagawiwa kadiri ya mahitaji yake.
36 Yosefu, Mlawi kutoka Kipro, ambaye mitume walimwita Barnaba (maana yake Mwana wa Faraja), 37 aliuza shamba alilokuwa nalo, akaleta hizo fedha alizopata na kuziweka miguuni pa mitume.
-
1 Kama kukiwa na jambo lolote la kutia moyo katika kuunganishwa na Kristo, kukiwa faraja yoyote katika upendo wake, kukiwa na ushirika wowote na Roho, kukiwa na wema wowote na huruma, 2 basi ikamilisheni furaha yangu kwa kuwa na nia moja, mkiwa na upendo huo moja, mkiwa wa roho na kusudi moja. 3 Msitende jambo lolote kwa nia ya kujitukuza wala kujivuna, bali kwa unyenyekevu kila mtu amhesabu mwingine bora kuliko nafsi yake. 4 Kila mmoja wenu asiangalie faida yake mwenyewe tu, bali pia ajishughulishe kwa faida ya wengine.
5 Kuweni na nia ile ile aliyokuwa nayo Kristo Yesu:
6 Yeye, ingawa alikuwa na asili ya Mungu hasa,
hakuona kule kuwa sawa na Mungu
kuwa kitu cha kushikilia,
7 bali alijifanya si kitu,
akachukua hali hasa na mtumwa,
naye akazaliwa katika umbo la mwanadamu.
8 Naye akiwa na umbo la mwanadamu,
alijinyenyekeza, akatii hata mauti:
naam, mauti ya msalaba!
-
3 Yesu ameonekana anastahili heshima kubwa kuliko Mose, kama vile mjenzi wa nyumba alivyo wa heshima kubwa kuliko nyumba yenyewe. 4 Kwa kuwa kila nyumba hujengwa na mtu fulani, lakini Mungu ni mjenzi wa kila kitu. 5 Basi Mose kama mtumishi alikuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Mungu, akishuhudia kwa yale ambayo yangetamkwa baadaye. 6 Lakini Kristo ni mwaminifu kama Mwana katika nyumba ya Mungu. Sisi ndio nyumba yake, kama tutashikilia sana ujasiri wetu na tumaini tunalojivunia.
-
23 Nao baada ya kuwateua wazee katika kila kanisa, kwa kufunga na kuomba wakawakabidhi kwa Bwana waliyemwamini.
-
11 Basi Mungu wetu na Baba yetu mwenyewe na Bwana wetu Yesu atengeneze njia ya sisi kuja kwenu. 12 Bwana na auongeze upendo wenu na kuuzidisha kati yenu na kwa wengine wote, kama vile tulivyo na upendo mwingi kwenu. 13 Tunamwomba Mungu aimarishe mioyo yenu ili msiwe na lawama katika utakatifu mbele za Mungu wetu aliye Baba yetu wakati wa kuja kwake Bwana Yesu pamoja na watakatifu wote.
-
1 “Kwa malaika wa kanisa lililoko Sardi andika:
“Haya ndiyo maneno ya aliye na zile Roho saba za Mungu na zile nyota saba. Nayajua matendo yako, kwamba una sifa ya kuwa hai, lakini umekufa. 2 Amka! Nawe uyaimarishe yale yaliyosalia na yaliyo karibu kufa, kwa maana sikuona kwamba kazi zako zimekamilika machoni pa Mungu wangu. 3 Kumbuka basi yale uliyoyapokea na kuyasikia, yatii na ukatubu. Lakini usipoamka, nitakuja kama mwizi wala hutajua saa nitakayokuja kwako.
4 “Lakini bado una watu wachache katika Sardi ambao hawajayachafua mavazi yao. Wao wataenda pamoja nami, wakiwa wamevaa mavazi meupe, kwa maana wanastahili. 5 Yeye ashindaye atavikwa vazi jeupe kama wao. Sitafuta jina lake kutoka kitabu cha uzima, bali nitalikiri jina lake mbele za Baba yangu na mbele za malaika wake.
-
1 Haya ndiyo maagizo, amri na sheria ambazo Bwana Mungu wenu aliniagiza niwafundishe ninyi ili mpate kuyashika katika nchi ambayo ninyi mnavuka Yordani kuimiliki, 2 ili kwamba ninyi, watoto wenu na watoto wao baada yao wamche Bwana Mungu wenu siku zote kwa kushika amri na maagizo yake yote ninayowapa, ili mweze kuyafurahia maisha marefu. 3 Sikia, ee Israeli, nawe uwe mwangalifu kutii ili upate kufanikiwa na kuongezeka sana katika nchi itiririkayo maziwa na asali, kama Bwana, Mungu wa baba zenu, alivyowaahidi ninyi.
4 Sikia, ee Israeli: Bwana Mungu wako, Bwana ni mmoja. 5 Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote. 6 Amri hizi ninazokupa leo zitakuwa katika moyo wako. 7 Wafundishe watoto wako kwa bidii. Nena kuhusu amri hizi uketipo nyumbani na wakati utembeapo njiani, ulalapo na uamkapo. 8 Zifunge kama alama juu ya mkono wako, na uzifunge juu ya paji la uso wako. 9 Ziandike kwenye miimo ya milango ya nyumba yako na juu ya malango yako.
-
28 Nasi tunajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hutenda kazi pamoja na wote wampendao, katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. 29 Maana wale Mungu aliowajua tangu mwanzo, pia aliwachagua tangu mwanzo, wapate kufanana na mfano wa Mwanawe, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. 30 Nao wale Mungu aliotangulia kuwachagua, akawaita, wale aliowaita pia akawahesabia haki, nao wale aliowahesabia haki, pia akawatukuza.
31 Tuseme nini basi kuhusu haya? Ikiwa Mungu yuko upande wetu, ni nani awezaye kuwa kinyume chetu? 32 Ikiwa Mungu hakumhurumia Mwanawe, bali alimtoa kwa ajili yetu sote, atakosaje basi kutupatia vitu vyote kwa ukarimu pamoja naye? 33 Ni nani atakayewashtaki wale ambao Mungu amewateua? Ni Mungu mwenyewe ndiye mwenye kuwahesabia haki. 34 Ni nani basi atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu aliyekufa, naam, zaidi ya hayo, aliyefufuliwa kutoka kwa wafu, yuko mkono wa kuume wa Mungu, naye pia anatuombea.
-
16 Je, kikombe cha baraka ambacho tunakibariki, si ushirika katika damu ya Kristo? Mkate tuumegao, si ushirika wa mwili wa Kristo? 17 Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja, kwa kuwa wote twashiriki mkate mmoja.
18 Waangalieni watu wa Israeli: Je, wale wote walao dhabihu si ni wale watendao kazi madhabahuni? 19 Je, nina maana kwamba kafara iliyotolewa kwa sanamu ni kitu chenye maana yoyote? Au kwamba sanamu ni kitu chenye maana yoyote? 20 La hasha! Lakini kafara za watu wasiomjua Mungu hutolewa kwa mashetani, wala si kwa Mungu. Nami sitaki ninyi mwe na ushirika na mashetani. 21 Hamwezi kunywa katika kikombe cha Bwana na cha mashetani pia. Hamwezi kuwa na sehemu katika meza ya Bwana na katika meza ya mashetani pia. 22 Je, tunataka kuamsha wivu wa Bwana? Je, sisi tuna nguvu kuliko yeye?
-
2 Katika siku za mwisho
mlima wa Hekalu la Bwana utaimarishwa
kama mlima mkuu miongoni mwa milima yote,
utainuliwa juu ya vilima,
na mataifa yote yatamiminika huko.
3 Mataifa mengi yatakuja na kusema,
“Njooni, twendeni mlimani mwa Bwana,
kwenye nyumba ya Mungu wa Yakobo.
Atatufundisha njia zake,
ili tuweze kuenenda katika mapito yake.”
Sheria itatoka Sayuni,
neno la Bwana litatoka Yerusalemu.
4 Atahukumu kati ya mataifa
na ataamua migogoro ya mataifa mengi.
Watafua panga zao ziwe majembe,
na mikuki yao kuwa miundu ya kukata matawi.
Taifa halitainua upanga dhidi ya taifa jingine,
wala hawatajifunza vita tena.
-
20 Kisha mama yao wana wa Zebedayo akamjia Yesu pamoja na wanawe, naye akapiga magoti mbele yake, akamwomba Yesu amfanyie jambo fulani.
21 Yesu akamuuliza, “Unataka nini?” Akajibu, “Tafadhali, wajalie wanangu hawa ili mmoja aketi upande wako wa kuume, na mwingine upande wako wa kushoto katika Ufalme wako.”
22 Yesu akawaambia, “Ninyi hamjui mnaloliomba. Je, mnaweza kukinywea kikombe nitakachonywea mimi?”
Wakajibu, “Tunaweza.”
23 Yesu akawaambia, “Kwa kweli kikombe changu mtakinywea, lakini kuketi upande wangu wa kuume au wa kushoto si langu mimi kuwapa. Nafasi hizo ni za wale ambao wameandaliwa na Baba yangu.”
24 Wale wanafunzi wengine kumi waliposikia haya, waliwakasirikia hao ndugu wawili. 25 Lakini Yesu akawaita wote pamoja na kuwaambia, “Mnafahamu kuwa watawala wa watu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, nao wenye vyeo huonyesha mamlaka yao. 26 Isiwe hivyo kwenu. Badala yake, yeyote anayetaka kuwa mkuu miongoni mwenu hana budi kuwa mtumishi wenu, 27 naye anayetaka kuwa wa kwanza miongoni mwenu hana budi kuwa mtumwa wenu: 28 kama vile ambavyo Mwana wa Adamu hakuja ili kutumikiwa, bali kutumika na kuutoa uhai wake uwe fidia kwa ajili ya wengi.”
-
17 Ndugu zangu, nawasihi mjihadhari na kujiepusha na wale watu waletao matengano na kuweka vikwazo mbele yenu dhidi ya mafundisho mliyojifunza.
-
19 Makanisa ya Asia yanawasalimu. Akila na Prisila, pamoja na kanisa lililoko nyumbani kwao wanawasalimu sana katika Bwana. 20 Ndugu wote walioko hapa wanawasalimu. Salimianeni kwa busu takatifu.
-
1 Kwa hiyo, mfuateni Mungu kama watoto wapendwao, 2 mkiishi maisha ya upendo, kama vile Kristo alivyotupenda sisi akajitoa kwa ajili yetu kuwa sadaka yenye harufu nzuri na dhabihu kwa Mungu.
3 Lakini uasherati, usitajwe miongoni mwenu, wala uchafu wa aina yoyote, wala tamaa, kwa sababu mambo haya hayastahili miongoni mwa watakatifu. 4 Wala pasiwepo mazungumzo machafu ya aibu, au maneno ya upuzi au mzaha, ambayo hayafai, badala yake mshukuruni Mungu. 5 Kwa habari ya mambo haya mjue hakika kwamba: Msherati, wala mtu mwovu, wala mwenye tamaa mbaya, mtu kama huyo ni mwabudu sanamu, kamwe hataurithi Ufalme wa Kristo na wa Mungu. 6 Mtu yeyote na asiwadanganye kwa maneno matupu, kwa kuwa hasira ya Mungu huwaka kwa sababu ya mambo kama haya juu ya wale wasiomtii. 7 Kwa hiyo, msishirikiane nao.
8 Kwa maana zamani ninyi mlikuwa giza, lakini sasa ninyi ni nuru katika Bwana. Enendeni kama watoto wa nuru 9 (kwa kuwa tunda la nuru hupatikana katika wema wote, haki na kweli), 10 nanyi tafuteni yale yanayompendeza Bwana. 11 Msishiriki matendo ya giza yasiyofaa, bali yafichueni. 12 Kwa maana ni aibu hata kutaja mambo yale ambayo wasiotii wanayafanya sirini.
-
16 Kwa hiyo mtu asiwahukumu ninyi kuhusu vyakula au vinywaji, au kuhusu kuadhimisha sikukuu za dini, au Sikukuu za Mwezi Mwandamo au siku ya Sabato. 17 Hizi zilikuwa kivuli cha mambo ambayo yangekuja, lakini ile iliyo halisi imo ndani ya Kristo. 18 Mtu yeyote asiwaondolee thawabu yenu kwa kusisitiza kunyenyekea kwake na kuabudu malaika. Mtu kama huyo hudumu katika maono yake, akijivuna bila sababu katika mawazo ya kibinadamu. 19 Yeye amepoteza ushirikiano na Kichwa, ambaye kutoka kwake mwili wote unalishwa na kushikamanishwa pamoja kwa viungo na mishipa, nao hukua kwa ukuaji utokao kwa Mungu.
-
2 Baada ya Paulo na Barnaba kutokubaliana nao kukawa na mabishano makali, Paulo na Barnaba na baadhi ya wengine miongoni mwao wakachaguliwa kwenda Yerusalemu ili kujadiliana jambo hili na mitume na wazee.
-
16 Kwa hiyo nasema, enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili. 17 Kwa maana mwili hutamani yale yaliyo kinyume na Roho, naye Roho hutamani yale yaliyo kinyume na mwili. Roho na mwili hupingana na kwa sababu hiyo hamwezi kufanya mnayotaka. 18 Lakini kama mkiongozwa na Roho, hamko chini ya sheria.
19 Basi matendo ya mwili ni dhahiri nayo ni haya: Uasherati, uchafu, ufisadi, 20 kuabudu sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, 21 husuda, ulevi, ulafi na mambo mengine yanayofanana na hayo. Nawaonya, kama nilivyokwisha kuwaonya kabla, kwamba watu watendao mambo kama hayo, hawataurithi Ufalme wa Mungu.
22 Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, 23 upole na kiasi. Katika mambo kama haya hakuna sheria. 24 Wote walio wa Kristo Yesu wameusulubisha mwili na shauku zake pamoja na tamaa zake. 25 Kwa kuwa tunaishi kwa Roho, basi, tuenende kwa Roho. 26 Tusijisifu bure, tukichokozana na kuoneana wivu.
-
7 Nimekuwa mtumishi wa Injili hii kwa kipawa cha neema ya Mungu niliyopewa kwa nguvu yake itendayo kazi. 8 Ingawa mimi ni mdogo kuliko aliye mdogo kabisa miongoni mwa watakatifu wote, nilipewa neema hii: ili niwahubirie watu wa Mataifa kuhusu utajiri usiopimika ulio ndani ya Kristo, 9 na kuweka wazi kwa kila mtu siri hii iliyokuwa imefichwa tangu zamani katika Mungu, aliyeumba vitu vyote. 10 Ili sasa kwa njia ya Kanisa, hekima yote ya Mungu ipate kujulikana kwa watawala na wenye mamlaka katika ulimwengu wa roho, 11 sawasawa na kusudi lake la milele katika Kristo Yesu Bwana wetu. 12 Ndani yake na kwa njia ya imani katika yeye twaweza kumkaribia Mungu kwa uhuru na kwa ujasiri.
-
13 Kwa ajili ya Bwana, tiini kila mamlaka iliyowekwa na wanadamu: Kwa mfalme kwani ndiye aliye na mamlaka ya juu zaidi, 14 au kwa maafisa aliowaweka, kwa kuwa mfalme amewatuma ili kuwaadhibu wale wanaokosa, na kuwapongeza wale watendao mema. 15 Kwa maana ni mapenzi ya Mungu kwamba kwa kutenda mema mnyamazishe maneno ya kijinga ya watu wapumbavu. 16 Ishini kama watu huru, lakini msitumie uhuru wenu kama kisingizio cha kutenda uovu, bali ishini kama watumishi wa Mungu. 17 Mheshimuni kila mtu ipasavyo: Wapendeni jamaa ya ndugu waumini, mcheni Mungu, mpeni heshima mfalme.
-
1 “Mimi ndimi mzabibu wa kweli na Baba yangu ndiye mkulima. 2 Kila tawi ndani yangu lisilozaa matunda, Baba yangu hulikata, nalo kila tawi lizaalo, hulisafisha ili lipate kuzaa matunda zaidi. 3 Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililonena nanyi. 4 Kaeni ndani yangu, nami nikae ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa matunda lisipokaa ndani ya mzabibu, vivyo hivyo ninyi msipokaa ndani yangu hamwezi kuzaa matunda.
5 “Mimi ni mzabibu, ninyi ni matawi. Akaaye ndani yangu, nami ndani yake, huyo huzaa sana, maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya jambo lolote. 6 Mtu yeyote asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka. Matawi kama hayo hukusanywa na kutupwa motoni, yakateketea. 7 Ninyi mkikaa ndani yangu na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni lolote mtakalo, nanyi mtatendewa. 8 Kwa hiyo Baba yangu hutukuzwa, kwa vile mzaavyo matunda mengi, nanyi mtakuwa wanafunzi wangu.
9 “Kama vile Baba alivyonipenda mimi, hivyo ndivyo mimi nilivyowapenda ninyi. Basi kaeni katika pendo langu. 10 Mkizishika amri zangu mtakaa katika pendo langu, kama mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake. 11 Nimewaambia mambo haya ili furaha yangu iwe ndani yenu na furaha yenu iwe kamili. 12 Amri yangu ndiyo hii: Mpendane kama mimi nilivyowapenda ninyi. 13 Hakuna mtu mwenye upendo mkuu kuliko huu, mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. 14 Ninyi ni rafiki zangu mkifanya ninayowaamuru. 15 Siwaiti ninyi watumishi tena, kwa sababu watumishi hawajui bwana wao analofanya, bali nimewaita ninyi rafiki, kwa maana nimewajulisha mambo yote niliyoyasikia kutoka kwa Baba yangu. 16 Si ninyi mlionichagua, bali mimi ndiye niliyewachagua ninyi na kuwaweka mwende mkazae matunda, na matunda yenu yapate kudumu. Ili nalo lolote mtakalomwomba Baba katika Jina langu, awape ninyi. 17 Amri yangu ndiyo hii: Mpendane.
-
5 Lisalimuni pia kanisa linalokutana nyumbani mwao.
Msalimuni rafiki yangu mpendwa Epaineto, aliyekuwa mtu wa kwanza kumwamini Kristo huko Asia.
-
9 Kwa kuwa sisi tu watendakazi pamoja na Mungu. Ninyi ni shamba la Mungu, jengo la Mungu.
-
1 Basi kuhusu changizo kwa ajili ya watakatifu: Kama nilivyoyaagiza makanisa ya Galatia, fanyeni vivyo hivyo. 2 Siku ya kwanza ya kila juma, kila mmoja wenu atenge kiasi cha fedha, kulingana na mapato yake na fedha hizo aziweke akiba, ili nitakapokuja pasiwe na lazima ya kufanya mchango. 3 Kwa hiyo nitakapowasili, nitawapa wale mtakaowachagua barua za kuwatambulisha, ili kuwatuma wapeleke zawadi zenu huko Yerusalemu.
-
6 Kumbukeni kwamba: Yeyote apandaye kwa uchache pia atavuna kwa uchache, naye apandaye kwa ukarimu pia atavuna kwa ukarimu. 7 Kila mtu atoe kama anavyokusudia moyoni mwake, si kwa uchoyo au kwa kulazimishwa, kwa maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo mkunjufu. 8 Naye Mungu aweza kuwapa kila baraka kwa wingi, ili katika mambo yote kila wakati, mwe na kila kitu mnachohitaji, ili mweze kushiriki kwa wingi katika kila kazi njema. 9 Kama ilivyoandikwa:
“Ametawanya vipawa vyake kwa ukarimu
akawapa maskini;
haki yake hudumu milele.”
10 Yeye ampaye mpanzi mbegu kwa ajili ya kupanda na mkate kuwa chakula, atawapa na kuzizidisha mbegu zenu za kupanda na kuongeza mavuno ya haki yenu. 11 Mtatajirishwa kwa kila namna ili mpate kuwa wakarimu kila wakati, na kupitia kwetu, ukarimu wenu utamletea Mungu shukrani.
-
1 Roho asema waziwazi kwamba katika siku za mwisho baadhi ya watu wataiacha imani na kufuata roho zidanganyazo na mafundisho ya mashetani. 2 Mafundisho kama hayo huja kupitia kwa waongo ambao ni wanafiki, hali dhamiri zao zikiungua kwa kuchomwa moto. 3 Wao huwakataza watu wasioe na kuwaagiza wajiepushe na vyakula fulani, ambavyo Mungu aliviumba ili vipokewe kwa shukrani na wale wanaoamini na kuijua kweli.
-
15 Basi kwa njia ya Yesu, tuzidi kumtolea Mungu dhabihu ya sifa, yaani matunda ya midomo inayolikiri Jina lake. 16 Na msiache kutenda mema na kushirikiana vile vitu mlivyo navyo, kwa kuwa dhabihu kama hizo ndizo zinazompendeza Mungu.
-
5 Huu ndio ujumbe tuliosikia kutoka kwake na kuwatangazia ninyi: kwamba Mungu ni nuru na ndani yake hamna giza lolote. 6 Kama tukisema kwamba twashirikiana naye huku tukienenda gizani, twasema uongo, wala hatutendi lililo kweli. 7 Lakini tukienenda nuruni, kama yeye alivyo nuruni, twashirikiana sisi kwa sisi na damu yake Yesu, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote.
8 Kama tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe wala kweli haimo ndani yetu. 9 Kama tukiziungama dhambi zetu, yeye ni mwaminifu na wa haki, atatusamehe dhambi zetu na kutusafisha kutoka kwenye udhalimu wote. 10 Kama tukisema hatukutenda dhambi, twamfanya yeye kuwa mwongo na neno lake halimo ndani yetu.
-
1 “Kwa malaika wa kanisa lililoko Efeso andika:
“Haya ndiyo maneno ya yule aliyezishika zile nyota saba katika mkono wake wa kuume na ambaye hutembea kati ya vile vinara saba vya taa vya dhahabu. 2 Nayajua matendo yako, bidii yako na saburi yako. Najua kuwa huwezi kuvumiliana na watu waovu na ya kwamba umewajaribu wale wanaojifanya kuwa mitume na kumbe sio, nawe umewatambua kuwa ni waongo. 3 Umevumilia na kustahimili taabu kwa ajili ya Jina langu, wala hukuchoka.
4 “Lakini nina neno dhidi yako: Umeuacha upendo wako wa kwanza. 5 Kumbuka basi ni wapi ulikoangukia! Tubu na ukafanye matendo yale ya kwanza. Kama usipotubu, nitakuja kwako na kukiondoa kinara chako cha taa kutoka mahali pake. 6 Lakini una jambo hili kwa upande wako: Unayachukia matendo ya Wanikolai, ambayo nami pia nayachukia.
7 “Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye, nitampa haki ya kula matunda toka kwa mti wa uzima, ambao uko katika paradiso ya Mungu.
-
7 Tufurahi, tushangilie
na kumpa utukufu!
Kwa maana arusi ya Mwana-Kondoo imewadia
na bibi arusi wake amejiweka tayari.
8 Akapewa kitani safi, nyeupe
inayongʼaa, ili avae.”
(Hiyo kitani safi inawakilisha matendo ya haki ya watakatifu.)
9 Ndipo malaika akaniambia, “Andika: ‘Wamebarikiwa wale walioalikwa kwenye karamu ya arusi ya Mwana-Kondoo!’ ” Naye akaongeza kusema, “Haya ndiyo maneno ya kweli ya Mungu.”
-
15 Akawaambia, “Enendeni ulimwenguni kote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. 16 Yeyote aaminiye na kubatizwa ataokoka. Lakini yeyote asiyeamini atahukumiwa.
-
4 Walipokuwa wakienda mji kwa mji, wakawa wanawapa maamuzi yaliyotolewa na mitume na wazee huko Yerusalemu ili wayafuate.
-
1 Mkaribisheni yeye ambaye imani yake ni dhaifu, lakini si kwa kugombana na kubishana juu ya mawazo yake. 2 Mtu mmoja imani yake inamruhusu kula kila kitu, lakini mwingine ambaye imani yake ni dhaifu, hula mboga tu. 3 Yeye alaye kila kitu asimdharau yeye asiyekula. Wala yeye asiyekula kila kitu asimhukumu yule alaye kila kitu, kwa maana Mungu amemkubali. 4 Wewe ni nani hata umhukumu mtumishi wa mtu mwingine? Kwa bwana wake tu anasimama au kuanguka. Naye atasimama kwa sababu Bwana anaweza kumsimamisha.
5 Mtu mmoja anaitukuza siku fulani kuwa ni bora kuliko nyingine, na mwingine anaona kuwa siku zote ni sawa. Basi kila mmoja awe na hakika na yale anayoamini. 6 Yeye anayehesabu siku moja kuwa takatifu kuliko nyingine, hufanya hivyo kwa kumheshimu Bwana. Naye alaye nyama hula kwa Bwana, kwa maana humshukuru Mungu, naye akataaye kula nyama hufanya hivyo kwa Bwana na humshukuru Mungu. 7 Kwa kuwa hakuna hata mmoja wetu anayeishi kwa ajili yake mwenyewe, wala hakuna hata mmoja wetu afaye kwa ajili yake mwenyewe. 8 Kama tunaishi, tunaishi kwa Bwana, nasi pia tukifa tunakufa kwa Bwana. Kwa hiyo basi, kama tukiishi au kama tukifa, sisi ni mali ya Bwana.
9 Kwani kwa sababu hii hasa, Kristo alikufa na akawa hai tena kusudi apate kuwa Bwana wa wote, yaani, waliokufa na walio hai. 10 Basi kwa nini wewe wamhukumu ndugu yako? Au kwa nini wewe unamdharau ndugu yako? Kwa kuwa sote tutasimama mbele ya kiti cha Mungu cha hukumu. 11 Kwa kuwa imeandikwa:
“ ‘Kama vile niishivyo,’ asema Bwana,
‘kila goti litapigwa mbele zangu,
na kila ulimi utakiri kwa Mungu.’ ”
12 Hivyo basi kila mmoja wetu atatoa habari zake mwenyewe kwa Mungu.
-
5 Lakini ikiwa mtu yeyote amesababisha huzuni, kwa kiasi fulani hakunihuzunisha mimi kama vile alivyowahuzunisha ninyi nyote, ili nisiwe mkali kupita kiasi. 6 Adhabu hii aliyopewa na wengi inamtosha. 7 Basi sasa badala yake, inawapasa kumsamehe na kumfariji, ili asigubikwe na huzuni kupita kiasi. 8 Kwa hiyo, nawasihi, mpate kuuthibitisha tena upendo wenu kwa ajili yake. 9 Sababu ya kuwaandikia ni kuona kama mngeweza kushinda hilo jaribio na kutii katika kila jambo. 10 Kama ninyi mkimsamehe mtu yeyote, mimi pia nimemsamehe. Kile nilichosamehe, kama kulikuwa na kitu chochote cha kusamehe, nimekwisha kusamehe mbele ya Kristo kwa ajili yenu, 11 ili Shetani asitushinde. Kwa maana hatuachi kuzijua hila zake.
-
26 Lakini Yerusalemu wa juu ni huru, nayo ndiye mama yetu.
-
24 Sasa nafurahia kule kuteseka kwangu kwa ajili yenu, na katika mwili wangu ninatimiliza yale yaliyopungua katika mateso ya Kristo kwa ajili ya mwili wake, ambao ni kanisa.
-
15 Wasalimuni ndugu wote wa Laodikia, na pia Nimfa, pamoja na kanisa linalokutana katika nyumba yake.
-
2 Basi, imempasa mwangalizi awe mtu asiye na lawama, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi, anayejitawala, anayeheshimika, mkarimu, ajuaye kufundisha, 3 asiwe mlevi, wala mkali bali awe mpole, asiwe mgomvi wala mpenda fedha. 4 Lazima aweze kuisimamia nyumba yake mwenyewe vizuri na kuhakikisha kwamba watoto wake wanamtii na kuwa na heshima kwa kila njia. 5 (Kwa maana kama mtu hajui jinsi ya kusimamia nyumba yake mwenyewe, atawezaje kuliangalia kanisa la Mungu?)
-
9 Mtu yeyote asiyedumu katika mafundisho ya Kristo, bali akayaacha, yeye hana Mungu. Yeyote anayedumu katika mafundisho ana Baba na Mwana pia. 10 Msimpokee mtu yeyote anayewajia ambaye hawaletei mafundisho haya, wala msimkaribishe nyumbani mwenu. 11 Yeyote amkaribishaye mtu wa namna hiyo anashiriki katika matendo maovu ya mtu huyo.
-
18 Kwa kuwa waliwaambia, “Siku za mwisho kutakuwa na watu wenye kudhihaki, watakaofuata tamaa zao wenyewe za upotovu.” 19 Hawa ndio watu wanaowagawa ninyi, wafuatao tamaa zao za asili, wala hawana Roho.
20 Lakini ninyi wapendwa, jijengeni katika imani yenu iliyo takatifu sana tena ombeni katika Roho Mtakatifu. 21 Jilindeni katika upendo wa Mungu mkitazamia kwa furaha rehema ya Bwana wetu Yesu Kristo ili awalete katika uzima wa milele.
-
6 “Uwe hodari na shujaa, kwa sababu wewe ndiwe utakayewaongoza watu hawa kuirithi nchi niliyowaapia baba zao kuwapa. 7 Uwe hodari na uwe na ushujaa mwingi. Uwe na bidii kutii sheria yote aliyokupa Mose mtumishi wangu, usiiache kwa kugeuka kuelekea kuume au kushoto, ili upate kufanikiwa popote uendako. 8 Usiache Kitabu hiki cha Sheria kiondoke kinywani mwako; yatafakari maneno yake usiku na mchana, ili upate kuwa mwangalifu kufanya kila kitu sawasawa na yote yaliyoandikwa ndani yake. Ndipo utakapofanikiwa na kisha utastawi. 9 Je, si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na shujaa. Usihofu wala usivunjike moyo, kwa kuwa Bwana Mungu wako atakuwa pamoja nawe kokote uendako.”
-
44 Wakati Petro alikuwa akisema maneno haya, Roho Mtakatifu aliwashukia wote waliokuwa wakisikiliza ule ujumbe. 45 Wale wa tohara walioamini waliokuja na Petro walishangaa kwa kuona kuwa kipawa cha Roho Mtakatifu kimemwagwa juu ya watu wa Mataifa. 46 Kwa kuwa waliwasikia wakinena kwa lugha mpya na kumwadhimisha Mungu.
Ndipo Petro akasema, 47 “Je, kuna mtu yeyote anayeweza kuzuia watu hawa wasibatizwe kwa maji? Wamempokea Roho Mtakatifu kama sisi tulivyompokea.” 48 Kwa hiyo akaamuru wabatizwe kwa jina la Yesu Kristo. Wakamsihi Petro akae nao kwa siku chache.
-
1 Kwa hiyo, kwa kuwa tumekwisha kuhesabiwa haki kwa imani, tuna amani na Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, 2 ambaye kwa kupitia kwake tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo ndani yake sasa tunasimama, nasi twafurahia katika tumaini letu la kushiriki utukufu wa Mungu. 3 Si hivyo tu, bali twafurahi pia katika mateso, kwa sababu tunajua kuwa mateso huleta saburi, 4 nayo saburi huleta uthabiti wa moyo, na uthabiti wa moyo huleta tumaini, 5 wala tumaini halitukatishi tamaa, kwa sababu Mungu amekwisha kumimina pendo lake mioyoni mwetu kwa njia ya Roho Mtakatifu ambaye ametupatia.
-
9 Niliwaandikia katika waraka wangu kuwa msishirikiane na wazinzi. 10 Sina maana kwamba msishirikiane na wazinzi wa ulimwengu huu, au wenye tamaa mbaya, wanyangʼanyi au waabudu sanamu. Kwa kufanya hivyo ingewalazimu mtoke ulimwenguni humu. 11 Lakini sasa nawaandikia kwamba msishirikiane na mtu yeyote anayejiita ndugu, hali akiwa ni mzinzi, au mwenye tamaa mbaya, mwabudu sanamu au msingiziaji, mlevi au mdhalimu. Mtu kama huyo hata msile naye.
12 Yanihusu nini kuwahukumu wale watu walio nje ya kanisa? Je, si mnapaswa kuwahukumu hao walio ndani? 13 Mungu atawahukumu hao walio nje. “Ninyi mwondoeni huyo mtu mwovu miongoni mwenu.”
-
1 Kama mtu yeyote wa kwenu ana ugomvi na mwenzake, anathubutuje kuupeleka kwa wasiomcha Mungu ili kuamuliwa badala ya kuupeleka kwa watakatifu? 2 Je, hamjui kwamba watakatifu watauhukumu ulimwengu? Nanyi kama mtauhukumu ulimwengu, je, hamwezi kuamua mambo madogo madogo? 3 Hamjui kwamba tutawahukumu malaika? Je, si zaidi mambo ya maisha haya? 4 Kwa hiyo kama kuna ugomvi miongoni mwenu kuhusu mambo kama haya, chagueni kuwa waamuzi, watu ambao wanaonekana hata sio wa heshima katika kanisa. 5 Nasema hivi ili mwone aibu. Je, inawezekana kuwa miongoni mwenu hakuna mtu mwenye hekima ya kutosha kuamua ugomvi kati ya waaminio? 6 Badala yake ndugu mmoja anampeleka mwenzake mahakamani, tena mbele ya watu wasioamini!
7 Huko kuwa na mashtaka miongoni mwenu ina maana kwamba tayari ni kushindwa kabisa. Kwa nini msikubali kutendewa mabaya? Kwa nini msikubali kunyangʼanywa? 8 Badala yake, ninyi wenyewe mwadanganya na kutenda mabaya, tena mwawatendea ndugu zenu.
9 Je, hamjui kwamba wasio haki hawataurithi Ufalme wa Mungu? Msidanganyike: Waasherati, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wahanithi, wala walawiti, 10 wala wezi, wala wenye tamaa mbaya, wala walevi, wala wanaodhihaki, wala wanyangʼanyi hawataurithi Ufalme wa Mungu. 11 Baadhi yenu mlikuwa kama hao. Lakini mlioshwa, mlitakaswa, mlihesabiwa haki kwa jina la Bwana Yesu Kristo na katika Roho wa Mungu wetu.
-
1 Je, mimi si huru? Je, mimi si mtume? Je, mimi sikumwona Yesu, Bwana wetu? Je, ninyi si matunda ya kazi yangu katika Bwana? 2 Hata kama mimi si mtume kwa wengine, hakika mimi ni mtume kwenu, kwa maana ninyi ni mhuri wa utume wangu katika Bwana.
-
8 Twataabika kila upande lakini hatuangamizwi; twaona wasiwasi lakini hatukati tamaa; 9 twateswa lakini hatuachwi; twatupwa chini lakini hatupondwi. 10 Siku zote twachukua katika mwili kufa kwake Yesu ili kwamba uzima wa Yesu uweze kudhihirika katika miili yetu. 11 Kwa maana sisi tulio hai siku zote tumetolewa tufe kwa ajili ya Yesu, ili kwamba uzima wake upate kudhihirishwa katika mwili wetu upatikanao na mauti.
-
11 Vaeni silaha zote za Mungu ili kwamba mweze kuzipinga hila za ibilisi. 12 Kwa maana kushindana kwetu si juu ya nyama na damu, bali dhidi ya falme, mamlaka, dhidi ya wakuu wa giza na majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.
-
9 Haya ndiyo maombi yangu: kwamba upendo wenu uongezeke zaidi na zaidi katika maarifa na ufahamu wote, 10 ili mpate kutambua yale yaliyo mema, mkawe safi, wasio na hatia hadi siku ya Kristo, 11 mkiwa mmejawa na matunda ya haki yapatikanayo kwa njia ya Yesu Kristo, kwa utukufu na sifa za Mungu.
12 Basi, ndugu zangu, nataka mjue kwamba mambo yale yaliyonipata kwa kweli yamesaidia sana kueneza Injili. 13 Matokeo yake ni kwamba imejulikana wazi kwa walinzi wote wa jumba la kifalme na kwa wengine wote kuwa nimefungwa kwa ajili ya Kristo. 14 Kwa sababu ya vifungo vyangu, ndugu wengi katika Bwana wametiwa moyo kuhubiri neno la Mungu kwa ujasiri zaidi na bila woga.
-
1 Basi, kwa kuwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu, Kristo alikoketi mkono wa kuume wa Mungu. 2 Yafikirini mambo yaliyo juu, wala si ya duniani. 3 Kwa maana ninyi mlikufa, nao uhai wenu sasa umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu. 4 Wakati Kristo, aliye uzima wenu, atakapotokea, ndipo nanyi mtakapotokea pamoja naye katika utukufu.
-
12 Sasa tunawaomba, ndugu, waheshimuni wale wanaofanya kazi kwa bidii miongoni mwenu, wale ambao wana mamlaka juu yenu katika Bwana na ambao wanawaonya. 13 Waheshimuni sana katika upendo kwa ajili ya kazi zao. Ishini kwa amani ninyi kwa ninyi.
-
16 Furahini siku zote; 17 ombeni bila kukoma; 18 shukuruni kwa kila jambo, kwa maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu kwa ajili yenu katika Kristo Yesu.
-
17 Waagize wale ambao ni matajiri wa ulimwengu huu waache kujivuna, wala wasiweke tumaini lao katika mali ambayo si ya hakika, bali waweke tumaini lao katika Mungu ambaye hutupatia vitu vyote kwa wingi ili tuvifurahie. 18 Waagize watende mema, wawe matajiri katika matendo mema, pia wawe wakarimu na walio tayari kushiriki mali zao na wengine. 19 Kwa njia hii watajiwekea hazina kama msingi kwa ajili ya wakati ujao na hivyo watajipatia uzima, yaani, ule uzima ambao ni wa kweli.
20 Timotheo, linda kile kilichowekwa amana kwako. Epuka majadiliano yasiyo ya utauwa na mabishano ambayo kwa uongo huitwa elimu, 21 ambayo wengine kwa kujidai kuwa nayo wameiacha imani.
Neema iwe nanyi. Amen.
-
10 Mtu anayesababisha mafarakano, mwonye mara ya kwanza, kisha mwonye mara ya pili. Baada ya hapo, usihusike naye tena. 11 Kwa kuwa unajua kwamba mtu kama huyo amepotoka na tena ni mwenye dhambi. Yeye amejihukumu mwenyewe.
Shows Read in context, Share and Copy.