24 Bible Verses About Teamwork

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Teamwork
  1. 11 Ndiye aliweka wengine kuwa mitume, wengine kuwa manabii, wengine kuwa wainjilisti, wengine kuwa wachungaji na walimu, 12 kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu kwa ajili ya kazi za huduma, ili kwamba mwili wa Kristo upate kujengwa 13 mpaka sote tutakapoufikia umoja katika imani na katika kumjua sana Mwana wa Mungu na kuwa watu wazima kwa kufikia kimo cha ukamilifu wa Kristo.

    14 Ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwatupwa huku na huku na kuchukuliwa na kila upepo wa mafundisho kwa hila za watu, kwa ujanja, kwa kufuata njia zao za udanganyifu. 15 Badala yake, tukiambiana kweli kwa upendo, katika mambo yote tukue, hata tumfikie yeye aliye kichwa, yaani, Kristo. 16 Kutoka kwake, mwili wote ukiwa umeungamanishwa na kushikamanishwa pamoja kwa msaada wa kila kiungo, hukua na kujijenga wenyewe katika upendo, wakati kila kiungo kinafanya kazi yake.

  2. 12 Kama vile mwili ulivyo mmoja nao una viungo vingi, navyo viungo vyote vya mwili ingawa ni vingi, ni mwili mmoja, vivyo hivyo na Kristo. 13 Kwa maana katika Roho mmoja wote tulibatizwa katika mwili mmoja, kama ni Wayahudi au Wayunani, kama ni watumwa au watu huru, nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja.

    14 Basi mwili si kiungo kimoja, bali ni viungo vingi. 15 Kama mguu ungesema, “Kwa kuwa mimi si mkono basi mimi si wa mwili,” hiyo isingefanya huo mguu usiwe sehemu ya mwili. 16 Na kama sikio lingesema, “Kwa kuwa mimi si jicho, basi mimi si wa mwili,” hiyo isingefanya hilo sikio lisiwe sehemu ya mwili. 17 Kama mwili wote ungelikuwa jicho, kusikia kungekuwa wapi? Au kama mwili wote ungelikuwa sikio, kunusa kungekuwa wapi? 18 Lakini kama ilivyo, Mungu ameweka viungo katika mwili, kila kimoja kama alivyopenda.

  3. 9 Wawili ni afadhali kuliko mmoja,

    kwa sababu wana malipo mazuri kwa kazi yao:

    10 Kama mmoja akianguka,

    mwenzake atamwinua.

    Lakini ni jambo la kuhuzunisha

    kwa mtu yule aangukaye

    naye hana wa kumwinua!

    11 Pia, kama wawili wakilala pamoja

    watapashana joto.

    Lakini ni vipi mtu aweza

    kujipasha joto mwenyewe?

    12 Ingawa mtu mmoja aweza kushindwa,

    watu wawili wanaweza

    kumkabili adui na kumshinda.

    Kamba ya nyuzi tatu

    haikatiki kwa urahisi.

  4. 5 Mungu atoaye saburi na faraja, awajalie ninyi roho ya umoja miongoni mwenu mnapomfuata Kristo Yesu, 6 ili kwa moyo mmoja mpate kumtukuza Mungu aliye Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo.

  5. 24 Tuangaliane na kuhimizana sisi kwa sisi katika upendo na katika kutenda mema. 25 Wala tusiache kukutana pamoja, kama wengine walivyo na desturi, bali tuhimizane sisi kwa sisi kadiri tuonavyo Siku ile inakaribia.

  6. 8 Zaidi ya yote, dumuni katika upendo kwa maana upendo husitiri wingi wa dhambi. 9 Kuweni wakarimu kila mtu na mwenzake pasipo manungʼuniko. 10 Kila mmoja na atumie kipawa chochote alichopewa kuwahudumia wengine, kama mawakili waaminifu wa neema mbalimbali za Mungu. 11 Yeyote asemaye hana budi kusema kama mtu asemaye maneno ya Mungu mwenyewe. Yeyote ahudumuye hana budi kuhudumu kwa nguvu zile anazopewa na Mungu, ili Mungu apate kutukuzwa katika mambo yote kwa njia ya Yesu Kristo. Utukufu na uweza una yeye milele na milele. Amen.

  7. 1 Kwa hiyo, ndugu zangu, nawasihi kwa rehema zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu na inayompendeza Mungu, hii ndiyo ibada yenu yenye maana. 2 Msifuatishe tena mfano wa ulimwengu huu, bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu. Ndipo mtaweza kuonja na kuhakikisha ni nini mapenzi ya Mungu yaliyo mema, yanayopendeza machoni pake na ukamilifu.

    3 Kwa ajili ya neema niliyopewa nawaambia kila mmoja miongoni mwenu, asijidhanie kuwa bora kuliko impasavyo, bali afikiri kwa busara kwa kulingana na kipimo cha imani Mungu aliyompa. 4 Kama vile katika mwili mmoja tulivyo na viungo vingi, navyo viungo vyote havina kazi moja, 5 vivyo hivyo na sisi tulio wengi, tu mwili mmoja katika Kristo, nasi kila mmoja ni kiungo cha mwenzake. 6 Tuna karama zilizotofautiana kila mmoja kutokana na neema tuliyopewa. Kama ni unabii na tutoe unabii kwa kadiri ya imani. 7 Kama ni kuhudumu na tuhudumu, mwenye kufundisha na afundishe, 8 kama ni kutia moyo na atie moyo, kama ni kuchangia kwa ajili ya mahitaji ya wengine na atoe kwa ukarimu, kama ni uongozi na aongoze kwa bidii, kama ni kuhurumia wengine na afanye hivyo kwa furaha.

  8. 18 Bwana Mungu akasema, “Si vyema huyu mtu awe peke yake. Nitamfanyia msaidizi wa kumfaa.”

  9. 17 Kama vile chuma kinoavyo chuma,

    ndivyo mtu amnoavyo mwenzake.

  10. 10 Nawasihi ndugu zangu, katika Jina la Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba mpatane nia zenu ninyi kwa ninyi, ili pasiwepo na matengano katikati yenu na kwamba mwe na umoja kikamilifu katika nia na katika kusudi.

  11. 1 Kama kukiwa na jambo lolote la kutia moyo katika kuunganishwa na Kristo, kukiwa faraja yoyote katika upendo wake, kukiwa na ushirika wowote na Roho, kukiwa na wema wowote na huruma, 2 basi ikamilisheni furaha yangu kwa kuwa na nia moja, mkiwa na upendo huo moja, mkiwa wa roho na kusudi moja. 3 Msitende jambo lolote kwa nia ya kujitukuza wala kujivuna, bali kwa unyenyekevu kila mtu amhesabu mwingine bora kuliko nafsi yake. 4 Kila mmoja wenu asiangalie faida yake mwenyewe tu, bali pia ajishughulishe kwa faida ya wengine.

  12. Wimbo wa kwenda juu. Wa Daudi.

    1 Tazama jinsi ilivyo vyema na kupendeza

    wakati ndugu wanapoishi pamoja katika umoja!

  13. 1 Kwa hiyo, ndugu zangu, ninaowapenda na ambao ninawaonea shauku, ninyi mlio furaha yangu na taji yangu, hivi ndivyo iwapasavyo kusimama imara katika Bwana, ninyi wapenzi wangu.

    2 Nawasihi Euodia na Sintike wawe na nia moja katika Bwana. 3 Naam, nakusihi wewe pia, mwenzangu mwaminifu, uwasaidie hawa wanawake, kwa sababu walijitaabisha katika kazi ya Injili pamoja nami bega kwa bega, wakiwa pamoja na Klementi na watendakazi wenzangu ambao majina yao yameandikwa katika kitabu cha uzima.

  14. 5 Rafiki mpendwa, wewe ni mwaminifu kwa yale unayowatendea ndugu, ingawa wao ni wageni kwako. 6 Wameshuhudia kuhusu upendo wako mbele ya kanisa. Utafanya vyema ukiwasafirisha kama inavyostahili kwa Mungu. 7 Ilikuwa ni kwa ajili ya hilo Jina waliondoka, bila kukubali kupokea msaada wowote kutoka kwa watu wasioamini. 8 Kwa hiyo imetupasa sisi kuonyesha ukarimu kwa watu kama hao ili tuweze kutenda kazi pamoja kwa ajili ya kweli.

  15. 7 Akawaita wale kumi na wawili, akawatuma wawili wawili, na kuwapa mamlaka kutoa pepo wachafu.

  16. 20 “Siwaombei hawa peke yao, bali nawaombea na wale wote watakaoniamini kupitia neno lao 21 ili wawe na umoja kama vile wewe Baba ulivyo ndani yangu na mimi nilivyo ndani yako, wao nao wawe ndani yetu, ili ulimwengu upate kuamini ya kuwa wewe ndiye uliyenituma mimi. 22 Utukufu ule ulionipa nimewapa wao, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo wamoja. 23 Mimi ndani yako na wewe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja na ulimwengu upate kujua ya kuwa umenituma, nami nimewapenda wao kama unavyonipenda mimi.

  17. 9 Kwa kuwa sisi tu watendakazi pamoja na Mungu. Ninyi ni shamba la Mungu, jengo la Mungu.

  18. 5 Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote

    wala usizitegemee akili zako mwenyewe;

    6 katika njia zako zote mkiri yeye,

    naye atayanyoosha mapito yako.

  19. 14 Pasipo ushauri wa hekima taifa huanguka,

    bali washauri wengi hufanya ushindi uwe wa hakika.

  20. 13 Yesu akapanda mlimani na kuwaita wale aliowataka, nao wakamjia. 14 Akawachagua kumi na wawili, ambao aliwaita mitume, ili wapate kuwa pamoja naye, na awatume kwenda kuhubiri 15 na kuwa na mamlaka ya kutoa pepo wachafu. 16 Hawa ndio wale kumi na wawili aliowachagua: Simoni (ambaye alimwita Petro); 17 Yakobo mwana wa Zebedayo, na Yohana nduguye (ambao aliwaita Boanerge, maana yake Wana wa Ngurumo); 18 Andrea, Filipo, Bartholomayo, Mathayo, Tomaso, Yakobo mwana wa Alfayo, Thadayo, Simoni Mkananayo, 19 na Yuda Iskariote aliyemsaliti Yesu.

  21. 1 Sisi tulio na nguvu, hatuna budi kuchukuliana na kushindwa kwa wale walio dhaifu wala si kujipendeza nafsi zetu wenyewe.

  22. 32 Kuweni wafadhili na wenye kuhurumiana ninyi kwa ninyi, mkisameheana, kama vile naye Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.

  23. 18 Yeye ndiye kichwa cha mwili, yaani kanisa, naye ndiye mwanzo na mzaliwa wa kwanza kutoka kwa wafu, ili yeye awe mkuu katika vitu vyote. 19 Kwa kuwa ilimpendeza Mungu kwamba utimilifu wake wote ukae ndani yake, 20 na kwa njia yake aweze kuvipatanisha vitu vyote na yeye mwenyewe, viwe ni vitu vilivyo duniani au vilivyo mbinguni, kwa kufanya amani kwa damu yake, iliyomwagika msalabani.

  24. 7 Lakini tukienenda nuruni, kama yeye alivyo nuruni, twashirikiana sisi kwa sisi na damu yake Yesu, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote.