67 Bible Verses About Compassion
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
-
35 Yesu akazunguka katika miji yote na vijiji vyote, akifundisha katika masinagogi yao, akihubiri habari njema za Ufalme, na akiponya kila ugonjwa na kila aina ya maradhi. 36 Alipoona makutano, aliwahurumia kwa sababu walikuwa wanasumbuka bila msaada, kama kondoo wasiokuwa na mchungaji. 37 Ndipo akawaambia wanafunzi wake, “Mavuno ni mengi lakini watendakazi ni wachache. 38 Kwa hiyo mwombeni Bwana wa mavuno, ili apeleke watendakazi katika shamba lake la mavuno.”
-
12 Kwa hiyo, kwa kuwa ninyi mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao sana, jivikeni moyo wa huruma, utu wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu. 13 Vumilianeni na kusameheana mtu akiwa na lalamiko lolote dhidi ya mwenzake. Sameheaneni kama vile Bwana alivyowasamehe ninyi. 14 Zaidi ya maadili haya yote jivikeni upendo, ambao ndio unaofunga kila kitu pamoja katika umoja mkamilifu.
15 Amani ya Kristo na itawale mioyoni mwenu, kwa kuwa ninyi kama viungo vya mwili mmoja mmeitiwa amani. Tena kuweni watu wa shukrani. 16 Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu, mkifundishana na kuonyana katika hekima yote, mkimwimbia Mungu zaburi, nyimbo na tenzi za rohoni, huku mkiwa na shukrani mioyoni mwenu. 17 Lolote mfanyalo, ikiwa ni kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba katika yeye.
-
8 Hatimaye, ninyi nyote kuweni na nia moja, wenye kuhurumiana, mkipendana kama ndugu, na mwe wasikitivu na wanyenyekevu. 9 Msilipe ovu kwa ovu, au jeuri kwa jeuri, bali barikini, kwa maana hili ndilo mliloitiwa ili mpate kurithi baraka.
-
30 Yesu akamjibu akasema, “Mtu mmoja alikuwa akiteremka kutoka Yerusalemu kwenda Yeriko, naye akaangukia mikononi mwa wanyangʼanyi. Wakampiga, wakaondoka, wakamwacha akiwa karibu kufa. 31 Kuhani mmoja alikuwa akipitia njia ile, alipomwona huyo mtu, akapita upande mwingine, akamwacha hapo barabarani. 32 Vivyo hivyo, Mlawi mmoja naye alipofika mahali pale, alimwona, akapita upande mwingine, akamwacha hapo barabarani 33 Lakini Msamaria mmoja aliyekuwa akisafiri alipomwona, alimhurumia. 34 Akaenda alipokuwa na akasafisha majeraha yake kwa divai na mafuta, kisha akayafunga. Ndipo akampandisha kwenye punda wake, akampeleka mpaka kwenye nyumba ya wageni na kumtunza. 35 Kesho yake, yule Msamaria akachukua dinari mbili akampa yule mwenye nyumba ya wageni na kusema, ‘Mtunze, nami nirudipo nitakulipa gharama yoyote ya ziada uliyotumia kwa ajili yake.’
36 “Ni yupi basi miongoni mwa hawa watatu wewe unadhani ni jirani yake yule mtu aliyeangukia mikononi mwa wanyangʼanyi?”
37 Yule mtaalamu wa sheria akajibu, “Ni yule aliyemhurumia.”
Ndipo Yesu akamwambia, “Nenda, ukafanye vivyo hivyo.”
-
32 Kuweni wafadhili na wenye kuhurumiana ninyi kwa ninyi, mkisameheana, kama vile naye Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.
-
13 Yesu aliposikia yaliyokuwa yametukia, aliondoka kwa chombo akaenda mahali pasipo na watu ili awe peke yake. Lakini watu walipopata habari, wakamfuata kwa miguu kupitia nchi kavu kutoka miji. 14 Yesu alipofika kando ya bahari, aliona makutano makubwa ya watu, akawahurumia na akawaponya wagonjwa wao.
-
29 Yesu na wanafunzi wake walipokuwa wakiondoka Yeriko, umati mkubwa wa watu ulimfuata. 30 Vipofu wawili walikuwa wameketi kando ya barabara. Waliposikia kwamba Yesu alikuwa anapita, wakapiga kelele wakisema, “Bwana, Mwana wa Daudi, tuhurumie!”
31 Ule umati wa watu ukawakemea na kuwaambia wanyamaze, lakini wao wakazidi kupaza sauti, wakisema, “Bwana, Mwana wa Daudi, tuhurumie.”
32 Yesu akasimama na kuwaita, akawauliza, “Mnataka niwafanyie nini?”
33 Wakamjibu, “Bwana, tunataka kuona.”
34 Yesu akawahurumia na kuwagusa macho yao. Mara macho yao yakapata kuona, nao wakamfuata.
-
30 Wale mitume wakakusanyika kwa Yesu na kumpa taarifa ya mambo yote waliyokuwa wamefanya na kufundisha. 31 Basi kwa kuwa watu wengi mno walikuwa wakija na kutoka, hata wakawa hawana nafasi ya kula, Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Twendeni peke yetu mahali pa faragha, mpate kupumzika.”
32 Hivyo wakaondoka kwa mashua peke yao, wakaenda mahali pasipo na watu. 33 Lakini watu wengi waliowaona wakiondoka, wakawatambua, nao wakaenda haraka kwa miguu kutoka miji yote, nao wakatangulia kufika. 34 Yesu alipofika kando ya bahari, aliona makutano makubwa ya watu, akawahurumia kwa maana walikuwa kama kondoo wasiokuwa na mchungaji. Kwa hiyo akaanza kuwafundisha mambo mengi.
-
11 Baadaye kidogo, Yesu alikwenda katika mji mmoja ulioitwa Naini. Nao wanafunzi wake na umati mkubwa wa watu walikwenda pamoja naye. 12 Alipokaribia lango la mji, alikutana na watu waliokuwa wamebeba maiti wakitoka nje ya mji. Huyu aliyekufa alikuwa mwana pekee wa mwanamke mjane. Umati mkubwa wa watu wa mji ule ulikuwa pamoja na huyo mwanamke. 13 Bwana Yesu alipomwona yule mjane, moyo wake ulimhurumia, akamwambia, “Usilie.”
14 Kisha akasogea mbele akaligusa lile jeneza na wale waliokuwa wamelibeba wakasimama kimya. Akasema, “Kijana, nakuambia inuka.” 15 Yule aliyekuwa amekufa akaketi akaanza kuongea, naye Yesu akamkabidhi kwa mama yake.
-
17 Ikiwa mtu anavyo vitu vya ulimwengu huu na akamwona ndugu yake ni mhitaji lakini asimhurumie, upendo wa Mungu wakaaje ndani ya mtu huyo? 18 Watoto wapendwa, tusipende kwa maneno au kwa ulimi bali kwa tendo na kweli.
-
8 Neno la Bwana likamjia tena Zekaria: 9 “Hivi ndivyo asemavyo Bwana Mwenye Nguvu Zote: ‘Fanyeni hukumu za haki, onyesheni rehema na huruma ninyi kwa ninyi. 10 Msimwonee mjane wala yatima, mgeni wala maskini. Msiwaziane mabaya mioyoni mwenu ninyi kwa ninyi.’
-
3 Ahimidiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa huruma na Mungu wa faraja yote. 4 Yeye hutufariji katika taabu zetu, ili tuweze kuwafariji walio katika taabu yoyote kwa faraja ambayo sisi wenyewe tumepokea kutoka kwa Mungu. 5 Kama vile mateso ya Kristo yanavyozidi ndani ya maisha yetu, hivyo ndivyo faraja yetu inavyofurika kwa njia ya Kristo.
-
40 Mtu mmoja mwenye ukoma alimjia Yesu, akamwomba akipiga magoti, akamwambia, “Ukitaka, waweza kunitakasa.”
41 Yesu, akiwa amejawa na huruma, akanyoosha mkono wake akamgusa, akamwambia, “Nataka. Takasika!” 42 Mara ukoma ukamtoka, naye akatakasika. 43 Baada ya Yesu kumwonya vikali, akamruhusu aende zake 44 akimwambia, “Hakikisha humwambii mtu yeyote habari hizi, bali nenda ukajionyeshe kwa kuhani, na ukatoe sadaka alizoagiza Mose kwa utakaso wako, ili kuwa ushuhuda kwao.” 45 Lakini yule mtu akaenda akaanza kutangaza habari za kuponywa kwake waziwazi. Kwa hiyo, Yesu hakuweza tena kuingia katika miji waziwazi lakini alikaa sehemu zisizo na watu. Hata hivyo watu wakamfuata huko kutoka kila upande.
-
2 Chukulianeni mizigo ninyi kwa ninyi, nanyi kwa njia hii mtatimiza sheria ya Kristo. 3 Kama mtu yeyote akijiona kuwa yeye ni bora na kumbe sivyo, basi mtu huyo anajidanganya mwenyewe. 4 Lakini kila mtu na aipime kazi yake mwenyewe, ndipo aweze kujisifu, bila kujilinganisha na mtu mwingine. 5 Kwa maana, kila mtu atauchukua mzigo wake mwenyewe. 6 Basi, yeye afundishwaye katika neno na amshirikishe mwalimu wake mema yote.
7 Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi. Kwa kuwa kile apandacho mtu ndicho atakachovuna. 8 Apandaye kwa mwili, katika mwili wake atavuna uharibifu, lakini yeye apandaye katika Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele. 9 Hivyo, tusichoke katika kutenda mema, kwa kuwa tutavuna kwa wakati wake tusipokata tamaa. 10 Kwa hiyo, kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema, hasa wale wa jamaa ya waaminio.
-
15 Lakini wewe, Ee Bwana, ni Mungu wa huruma na neema,
si mwepesi wa hasira, bali ni mwingi wa upendo na uaminifu.
-
13 Kama baba alivyo na huruma kwa watoto wake,
ndivyo Bwana anavyowahurumia wale wanaomcha;
14 kwa kuwa anajua tulivyoumbwa,
anakumbuka kwamba sisi tu mavumbi.
15 Kuhusu mwanadamu, siku zake ni kama majani,
anachanua kama ua la shambani;
16 upepo huvuma juu yake nalo hutoweka,
mahali pake hapalikumbuki tena.
17 Lakini kutoka milele hata milele
upendo wa Bwana uko kwa wale wamchao,
nayo haki yake kwa watoto wa watoto wao:
18 kwa wale walishikao agano lake
na kukumbuka kuyatii mausia yake.
-
15 “Je, mama aweza kumsahau mtoto
aliyeko matitini mwake akinyonya,
wala asiwe na huruma
juu ya mtoto aliyemzaa?
Ingawa anaweza kusahau,
mimi sitakusahau wewe!
16 Tazama, nimekuchora kama muhuri
katika vitanga vya mikono yangu,
kuta zako zi mbele yangu daima.
-
14 Kwa kuwa tunaye Kuhani Mkuu kuliko wote ambaye ameingia mbinguni, Yesu Mwana wa Mungu, basi na tushikamane sana kwa uthabiti na ule ukiri wa imani yetu. 15 Kwa kuwa hatuna Kuhani Mkuu asiyeweza kuchukuliana na sisi katika udhaifu wetu, lakini tunaye mmoja ambaye alijaribiwa kwa kila namna, kama vile sisi tujaribiwavyo: lakini yeye hakutenda dhambi. 16 Basi na tukikaribie kiti cha rehema kwa ujasiri, ili tupewe rehema na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.
-
17 Yeye amhurumiaye maskini humkopesha Bwana,
naye atamtuza kwa aliyotenda.
-
20 Basi akaondoka, akaenda kwa baba yake.
“Lakini alipokuwa bado yuko mbali, baba yake akamwona, moyo wake ukajawa na huruma. Akamkimbilia mwanawe, akamkumbatia na kumbusu.
-
8 Bwana ni mwenye neema na mwingi wa huruma,
si mwepesi wa hasira, bali ni mwingi wa upendo.
9 Bwana ni mwema kwa wote,
ana huruma kwa vyote alivyovifanya.
-
32 Kisha Yesu akawaita wanafunzi wake, akawaambia, “Ninauhurumia huu umati wa watu, kwa sababu sasa wamekuwa pamoja nami kwa muda wa siku tatu, na hawana chakula chochote. Nami sipendi kuwaaga wakiwa na njaa, wasije wakazimia njiani.”
33 Wanafunzi wake wakasema, “Tutapata wapi mikate ya kutosha kuwalisha umati huu wa watu mkubwa namna hii, nasi tuko nyikani?”
34 Yesu akawauliza, “Mnayo mikate mingapi?”
Wakamjibu, “Tunayo mikate saba na visamaki vichache.”
35 Yesu akawaambia ule umati wa watu waketi chini. 36 Kisha akachukua ile mikate saba na wale samaki, naye akiisha kumshukuru Mungu, akavimega na kuwapa wanafunzi wake, nao wakawapa ule umati wa watu. 37 Wote wakala na kushiba. Baadaye wanafunzi wakakusanya vipande vilivyosalia, wakajaza vikapu saba.
-
5 Ndipo binti Farao akateremka mtoni Naili kuoga, nao wahudumu wake wakawa wanatembea ukingoni mwa mto. Binti mfalme akaona kisafina katikati ya manyasi, akamtuma mmoja wa watumwa wake wa kike kukichukua. 6 Alifungua kisafina akaona mtoto ndani yake. Mtoto alikuwa akilia, akamhurumia. Akasema, “Huyu ni mmoja wa watoto wa Kiebrania.”
-
8 Bwana ni mwingi wa huruma na mwenye neema;
si mwepesi wa hasira, bali amejaa upendo.
-
15 Furahini pamoja na wenye kufurahi, lieni pamoja na wale waliao.
-
3 Nyumbani mwake kuna mali na utajiri,
haki yake hudumu milele.
4 Hata gizani nuru humzukia mtu mwadilifu,
yule mwenye rehema, huruma na haki.
5 Mema yatamjia mtu yule aliye mkarimu na mwenye kukopesha bila riba,
anayefanya mambo yake kwa haki.
-
22 Kwa sababu ya upendo mkuu wa Bwana, hatuangamii,
kwa kuwa huruma zake hazikomi kamwe.
23 Ni mpya kila asubuhi,
uaminifu wako ni mkuu.
-
33 Yesu alipomwona Maria akilia na wale Wayahudi waliokuja pamoja naye pia wakilia, Yesu alisikia uchungu moyoni, akafadhaika sana. 34 Akauliza, “Mmemweka wapi?”
Wakamwambia, “Bwana, njoo upaone.”
35 Yesu akalia machozi.
36 Ndipo Wayahudi wakasema, “Tazama jinsi alivyompenda Lazaro!”
37 Lakini wengine wakasema, “Je, yule aliyefungua macho ya kipofu, hakuweza kumfanya na huyu asife?”
38 Yesu kwa mara nyingine akiwa amefadhaika sana, akafika penye kaburi. Hilo kaburi lilikuwa pango ambalo jiwe lilikuwa limewekwa kwenye ingilio lake. 39 Yesu akasema, “Liondoeni hilo jiwe.”
Martha ndugu yake yule aliyekuwa amekufa akasema, “Lakini Bwana, wakati huu atakuwa ananuka kwani amekwisha kuwa kaburini siku nne.”
40 Yesu akamwambia, “Sikukuambia kwamba kama ukiamini utauona utukufu wa Mungu?”
41 Kwa hiyo wakaliondoa lile jiwe kutoka kaburini. Yesu akainua macho yake juu akasema, “Baba, ninakushukuru kwa kuwa wanisikia. 42 Ninajua ya kuwa wewe hunisikia siku zote, lakini nimesema haya kwa ajili ya umati huu uliosimama hapa, ili wapate kuamini ya kuwa wewe umenituma.”
43 Baada ya kusema haya, Yesu akapaza sauti yake akaita, “Lazaro, njoo huku!” 44 Yule aliyekuwa amekufa akatoka nje, mikono yake na miguu yake ikiwa imeviringishiwa vitambaa vya kitani na leso usoni pake.
Yesu akawaambia, “Mfungueni, mwacheni aende zake.”
-
1 Wakati baraka hizi zote pamoja na laana nilizoziweka mbele yako zitakapokujia, nawe ukazitafakari moyoni popote Bwana Mungu wako atakapokutawanya miongoni mwa mataifa, 2 hapo wewe na watoto wako mtakapomrudia Bwana Mungu wako, na kumtii kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote kulingana na kila kitu ninachokuamuru leo, 3 ndipo Bwana Mungu wako atakapokurudisha kutoka utumwani na kukuhurumia, naye atakukusanya tena kutoka mataifa yote kule alikutawanya. 4 Hata kama umefukuziwa katika nchi ya mbali kiasi gani chini ya mbingu, kutoka huko Bwana Mungu wako atakukusanya na kukurudisha.
-
18 Hata hivyo Bwana anatamani kutupatia neema,
anainuka ili kuwaonyesha huruma.
Kwa kuwa Bwana ni Mungu wa haki.
Wamebarikiwa wote wanaomngojea yeye!
-
41 Alipokaribia Yerusalemu na kuuona mji, aliulilia, 42 akisema, “Laiti ungalijua hata wewe leo yale ambayo yangeleta amani, lakini sasa yamefichika machoni pako. 43 Hakika siku zinakujia, ambazo adui zako watakuzingira, nao watakuzunguka pande zote na kukuzuilia ndani. 44 Watakuponda chini, wewe na watoto walioko ndani ya kuta zako. Nao hawataacha hata jiwe moja juu ya jingine, kwa sababu hukutambua wakati wa kujiliwa kwako.”
-
38 Hata hivyo alikuwa na huruma,
alisamehe maovu yao
na hakuwaangamiza.
Mara kwa mara alizuia hasira yake,
wala hakuchochea ghadhabu yake yote.
-
31 Kwa kuwa watu hawakatiliwi mbali
na Bwana milele.
32 Ingawa huleta huzuni, ataonyesha huruma,
kwa kuwa upendo wake usiokoma ni mkuu.
33 Kwa maana hapendi kuwaletea mateso
au huzuni watoto wa wanadamu.
34 Kuwaponda chini ya nyayo
wafungwa wote katika nchi,
35 Kumnyima mtu haki zake
mbele za Aliye Juu Sana,
36 kumnyima mtu haki:
Je, Bwana asione mambo kama haya?
-
11 Mashahidi wakatili wanainuka,
wananiuliza mambo nisiyoyajua.
12 Wananilipa baya kwa jema
na kuiacha nafsi yangu ukiwa.
13 Lakini walipokuwa wagonjwa, nilivaa nguo ya gunia
na nikajinyenyekesha kwa kufunga.
Maombi yangu yaliponirudia bila kujibiwa,
14 niliendelea kuomboleza
kama vile wao ni rafiki au ndugu.
Niliinamisha kichwa chini kwa huzuni
kama ninayemwombolezea mama yangu.
-
13 Pigeni kelele kwa furaha, enyi mbingu;
furahi, ee dunia;
pazeni sauti kwa kuimba, enyi milima!
Kwa maana Bwana anawafariji watu wake,
naye atakuwa na huruma kwa watu wake walioumizwa.
-
28 “Njooni kwangu, ninyi nyote mnaotaabika na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. 29 Jifungeni nira yangu, mjifunze kutoka kwangu, kwa maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtapata raha nafsini mwenu. 30 Kwa maana nira yangu ni laini na mzigo wangu ni mwepesi.”
-
3 Wakumbukeni wale waliofungwa gerezani kana kwamba ninyi mmefungwa pamoja nao. Pia wakumbukeni wale wanaotendewa vibaya, kana kwamba ni ninyi wenyewe mnateswa.
-
11 Kama mnavyojua, tunawahesabu kuwa wabarikiwa wale waliovumilia. Mmesikia habari za uvumilivu wake Ayubu na mmeona kile ambacho hatimaye Bwana alimtendea. Bwana ni mwingi wa huruma, na amejaa rehema.
-
20 Lakini ninyi wapendwa, jijengeni katika imani yenu iliyo takatifu sana tena ombeni katika Roho Mtakatifu. 21 Jilindeni katika upendo wa Mungu mkitazamia kwa furaha rehema ya Bwana wetu Yesu Kristo ili awalete katika uzima wa milele.
22 Wahurumieni walio na mashaka; 23 wengine waokoeni kwa kuwanyakua kutoka kwenye moto; nao wengine wahurumieni mkiwa na hofu, mkichukia hata vazi lenye mawaa na kutiwa unajisi na mwili.
-
1 Yesu aliposhuka kutoka mlimani, makutano makubwa ya watu yakamfuata. 2 Mtu mmoja mwenye ukoma akaja na kupiga magoti mbele yake, akasema, “Bwana, kama ukitaka, unaweza kunitakasa.”
3 Yesu akanyoosha mkono wake akamgusa yule mtu, akamwambia, “Nataka. Takasika!” Mara yule mtu akatakasika ukoma wake. 4 Kisha Yesu akamwambia, “Hakikisha humwambii mtu yeyote. Lakini nenda ukajionyeshe kwa kuhani, na utoe sadaka aliyoamuru Mose, ili kuwa ushuhuda kwao.”
-
14 Tuseme nini basi? Je, Mungu ni dhalimu? La, hasha! 15 Kwa maana Mungu alimwambia Mose,
“Nitamrehemu yeye nimrehemuye,
na pia nitamhurumia yeye nimhurumiaye.”
16 Kwa hiyo haitegemei kutaka kwa mwanadamu au jitihada, bali hutegemea huruma ya Mungu.
-
17 Hakuna kimoja kati ya vitu vilivyolaaniwa kitakachokutwa mikononi mwenu, ili Bwana ageuze hasira yake kali. Atawahurumia na kuwa na rehema kwenu pia kuongeza idadi yenu, kama alivyowaahidi baba zenu, 18 kwa sababu mnamtii Bwana Mungu wenu, mkizishika amri zake zote zile ninazowapa leo na kufanya lile lililo jema machoni pake.
-
9 Kama mkimrudia Bwana ndipo wale ndugu zenu waliotekwa pamoja na watoto wenu watakapoonewa huruma na wale waliowateka na kuwaachia warudi katika nchi hii, kwa kuwa Bwana Mungu wenu ni mwenye neema na huruma, hatageuzia uso wake mbali nanyi kama ninyi mkimrudia yeye.”
-
15 Tazama chini kutoka mbinguni ukaone
kutoka kiti chako cha enzi
kilichoinuliwa juu, kitakatifu na kitukufu.
Uko wapi wivu wako na uweza wako?
Umetuzuilia wema wako na huruma zako.
16 Lakini wewe ni Baba yetu,
ingawa Abrahamu hatufahamu sisi
wala Israeli hatutambui;
wewe, Ee Bwana, ndiwe Baba yetu,
Mkombozi wetu tangu zamani za kale ndilo jina lako.
-
18 Ni nani Mungu kama wewe,
ambaye anaachilia dhambi
na kusamehe makosa
ya mabaki ya urithi wake?
Wewe huwi na hasira milele,
bali unafurahia kuonyesha rehema.
19 Utatuhurumia tena,
utazikanyaga dhambi zetu
chini ya nyayo zako,
na kutupa maovu yetu yote
katika vilindi vya bahari.
20 Utakuwa wa kweli kwa Yakobo,
nawe utamwonyesha Abrahamu rehema,
kama ulivyowaahidi kwa kiapo baba zetu
siku za kale.
-
42 Kama yeyote akimpa hata kikombe cha maji baridi mmoja wa hawa wadogo kwa kuwa ni mwanafunzi wangu, amin, nawaambia, hataikosa thawabu yake.”
-
11 Basi marafiki watatu wa Ayubu, ndio Elifazi Mtemani, na Bildadi Mshuhi na Sofari Mnaamathi, waliposikia juu ya taabu yote iliyompata Ayubu, wakajipanga toka manyumbani mwao, nao wakakutana pamoja kwa makubaliano kwenda kumtuliza katika taabu hiyo na kumfariji. 12 Walipomwona kwa mbali, ilikuwa vigumu kumtambua. Wakaanza kulia kwa sauti kubwa, wakayararua majoho yao na kujirushia mavumbi juu ya vichwa vyao. 13 Kisha wakaketi chini kwenye udongo pamoja na Ayubu kwa siku saba usiku na mchana. Hakuna yeyote aliyesema naye neno, kwa sababu waliona jinsi mateso yake yalivyokuwa makubwa.
-
25 Je, sikulia kwa ajili ya wale waliokuwa katika taabu?
Je, nafsi yangu haikusononeka kwa ajili ya maskini?
-
1 Hata kama nitasema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa kengele inayolialia au toazi livumalo. 2 Ningekuwa na karama ya unabii na kujua siri zote na maarifa yote, hata kama nina imani kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, mimi si kitu. 3 Kama nikitoa mali yote niliyo nayo na kama nikijitolea mwili wangu uchomwe moto, kama sina upendo, hainifaidi kitu.
4 Upendo huvumilia, upendo hufadhili, upendo hauoni wivu, hauna majivuno, hauna kiburi. 5 Haukosi kuwa na adabu, hautafuti mambo yake, haukasiriki upesi, hauweki kumbukumbu ya mabaya. 6 Upendo haufurahii mabaya bali hufurahi pamoja na kweli. 7 Upendo huvumilia yote, huamini yote, hutumaini yote, hustahimili yote.
-
2 Kwa kuwa yeye mwenyewe ni dhaifu, aweza kuwachukulia kwa upole wale wasiojua na kupotoka.
-
15 Kisha watu waliotajwa kwa majina wakawachukua wale mateka na kutoka zile nyara, wakachukua mavazi wakawavika wale wafungwa wote waliokuwa uchi. Wakawapatia nguo na viatu, chakula na cha kunywa, wakawapa matibabu, wote waliokuwa dhaifu miongoni mwao wakawapandisha juu ya punda, wakawaleta ndugu zao mpaka Yeriko, ndio Mji wa Mitende, kisha wakarudi Samaria.
-
156 Ee Bwana, huruma zako ni kuu,
uyahifadhi maisha yangu sawasawa na sheria zako.
-
21 Yeye anayemdharau jirani yake hutenda dhambi,
bali amebarikiwa yeye aliye na huruma kwa mhitaji.
-
16 jiosheni na mkajitakase.
Yaondoeni matendo yenu maovu
mbele zangu!
Acheni kutenda mabaya,
17 jifunzeni kutenda mema!
Tafuteni haki,
watieni moyo walioonewa.
Teteeni shauri la yatima,
wateteeni wajane.
-
14 Hili ndilo asemalo Bwana: “Kwa habari ya majirani zangu wote wabaya wanaonyangʼanya urithi ambao ninawapa watu wangu Israeli, nitawangʼoa kutoka nchi zao, nami nitaingʼoa nyumba ya Yuda kutoka katikati yao. 15 Lakini baada ya kuwangʼoa, nitawahurumia tena na kumrudisha kila mmoja wao kwenye urithi wake mwenyewe na kwenye nchi yake mwenyewe.
-
1 Neno la Bwana likanijia kusema: 2 “Mwanadamu, ijulishe Yerusalemu kuhusu mwenendo wake wa machukizo 3 na useme, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi, analomwambia Yerusalemu: Wewe asili yako na kuzaliwa kwako ni katika nchi ya Kanaani, baba yako alikuwa Mwamori, naye mama yako alikuwa Mhiti. 4 Siku uliyozaliwa kitovu chako hakikukatwa, wala hukuogeshwa kwa maji ili kukufanya safi, wala hukusuguliwa kwa chumvi wala kufunikwa kwa nguo. 5 Hakuna yeyote aliyekuonea huruma au kukusikitikia kiasi cha kukutendea mojawapo ya mambo haya. Badala yake, ulipozaliwa ulitupwa nje penye uwanja, kwa kuwa katika siku uliyozaliwa ulidharauliwa.
6 “ ‘Ndipo nilipopita karibu nawe nikakuona ukigaagaa kwenye damu yako, nawe ulipokuwa umelala hapo penye hiyo damu nikakuambia, “Ishi!” 7 Nilikufanya uote kama mmea wa shambani. Ukakua na kuongezeka sana, ukawa kito cha thamani kuliko vyote. Matiti yako yakatokeza na nywele zako zikaota, wewe uliyekuwa uchi na bila kitu chochote.
8 “ ‘Baadaye nikapita karibu nawe, nilipokutazama na kukuona kuwa umefikia umri wa kupendwa, nililitandaza vazi langu juu yako na kuufunika uchi wako. Nikakuapia na kuingia kwenye Agano na wewe, asema Bwana Mwenyezi, nawe ukawa wangu.
9 “ ‘Nilikuogesha kwa maji, nikakuosha ile damu na kukupaka mafuta. 10 Nikakuvika vazi lililotariziwa na kukuvalisha viatu vya kamba vya ngozi. Nikakuvika nguo za kitani safi na kukufunika kwa mavazi ya thamani kubwa. 11 Nikakupamba kwa vito: nikakuvika bangili mikononi mwako na mkufu shingoni mwako, 12 nikaweka hazama puani mwako, vipuli masikioni mwako na taji nzuri sana kichwani mwako. 13 Kwa hiyo ulipambwa kwa dhahabu na fedha, nguo zako zilikuwa za kitani safi, hariri na nguo iliyokuwa imetariziwa. Chakula chako kilikuwa unga laini, asali na mafuta ya zeituni. Ukawa mzuri sana ukainuka kuwa malkia. 14 Umaarufu wako ulifahamika miongoni mwa mataifa kwa ajili ya uzuri wako, kwani ulikuwa mkamilifu kwa ajili ya utukufu wangu niliokuwa nimeuweka juu yako, asema Bwana Mwenyezi.
-
8 Amekuonyesha yaliyo mema, ee mwanadamu.
Bwana anataka nini kwako?
Ila kutenda kwa haki na kupenda rehema,
na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako.
-
23 “Kwa hiyo Ufalme wa Mbinguni unaweza kufananishwa na mfalme aliyetaka kufanya hesabu zake za fedha na watumishi wake. 24 Alipoanza kufanya hesabu zake, mtu mmoja aliyekuwa anadaiwa talanta 10,000, aliletwa kwake. 25 Kwa kuwa alikuwa hawezi kulipa deni hilo, bwana wake akaamuru kwamba auzwe, yeye, mkewe, watoto wake na vyote alivyokuwa navyo, ili lile deni lipate kulipwa.
26 “Yule mtumishi akampigia magoti, akamsihi yule bwana akisema, ‘Naomba univumilie, nami nitakulipa deni lako lote.’ 27 Yule bwana wa huyo mtumishi akamwonea huruma, akafuta deni lake lote, akamwacha aende zake.
28 “Lakini yule mtumishi alipokuwa anatoka nje, akakutana na mtumishi mwenzake aliyekuwa amemkopesha dinari mia moja. Akamkamata, akamkaba koo akimwambia, ‘Nilipe kile ninachokudai!’
29 “Yule mtumishi mwenzake akapiga magoti akamsihi akisema, ‘Naomba univumilie, nami nitakulipa deni lako lote.’
30 “Lakini akakataa. Badala yake, alienda akamtupa gerezani hata atakapolipa hilo deni. 31 Watumishi wenzake walipoona haya yaliyotukia wakaudhika sana, nao wakaenda na kumwambia bwana wao kila kitu kilichokuwa kimetukia.
32 “Yule bwana akamwita yule mtumishi akamwambia, ‘Wewe mtumishi mwovu! Mimi nilikusamehe deni lako lote uliponisihi. 33 Je, haikukupasa kumhurumia mtumishi mwenzako kama mimi nilivyokuhurumia wewe?’ 34 Kwa hasira, yule bwana wake akamtia yule mtumishi mikononi mwa askari wa gereza ili ateswe mpaka atakapolipa yote aliyokuwa anadaiwa.
35 “Hivi ndivyo Baba yangu wa mbinguni atakavyomfanyia kila mmoja wenu ikiwa hatamsamehe ndugu yake kutoka moyoni mwake.”
-
36 Kuweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma.
-
6 Bwana akapita mbele ya Mose, akitangaza, “Bwana, Bwana, Mungu mwenye huruma na neema, asiye mwepesi wa hasira, mwingi wa upendo na uaminifu, 7 akidumisha upendo kwa maelfu, pia akisamehe uovu, uasi na dhambi. Lakini haachi kuadhibu mwenye hatia; huwaadhibu watoto na watoto wao kwa ajili ya dhambi ya baba zao hata katika kizazi cha tatu na cha nne.”
-
7 “Kwa kitambo kidogo nilikuacha,
lakini kwa huruma nyingi nitakurudisha.
8 Katika ukali wa hasira
nilikuficha uso wangu kwa kitambo,
lakini kwa fadhili za milele
nitakuwa na huruma juu yako,”
asema Bwana Mkombozi wako.
-
14 “Mtu anayekata tamaa angetazamia moyo wa kujitoa wa rafiki zake,
hata kama akiacha uchaji wa Mwenyezi.
-
13 Rarueni mioyo yenu
na siyo mavazi yenu.
Mrudieni Bwana, Mungu wenu,
kwa maana yeye ndiye mwenye neema
na mwingi wa huruma,
si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa upendo,
huona huruma, hujizuia kuleta maafa.
-
12 Kwa hiyo chochote mnachotaka mtendewe na watu, ninyi nanyi watendeeni vivyo hivyo. Kwa kuwa hii ndiyo Sheria na Manabii.
-
41 Amin, nawaambia, yeyote awapaye ninyi kikombe cha maji kwa Jina langu kwa sababu ninyi ni mali ya Kristo, hakika hataikosa thawabu yake.”
-
11 Yesu alipokuwa njiani akienda Yerusalemu, alipitia mpakani mwa Samaria na Galilaya. 12 Alipokuwa akiingia kwenye kijiji kimoja, watu kumi waliokuwa na ukoma wakakutana naye. Wakasimama mbali, 13 wakapaza sauti, wakasema, “Yesu, Bwana, tuhurumie!”
14 Alipowaona akawaambia, “Nendeni mkajionyeshe kwa makuhani.” Nao walipokuwa njiani wakienda, wakatakasika.
15 Mmoja wao alipoona kwamba amepona, akarudi kwa Yesu, akimsifu Mungu kwa sauti kuu. 16 Akajitupa miguuni mwa Yesu akamshukuru. Yeye alikuwa Msamaria.
17 Yesu akauliza, “Je, hawakutakaswa wote kumi? Wako wapi wale wengine tisa? 18 Hakuna hata mmoja aliyeonekana kurudi ili kumshukuru Mungu isipokuwa huyu mgeni?” 19 Yesu akamwambia, “Inuka na uende zako, imani yako imekuponya.”
-
20 Badala yake:
“Kama adui yako ana njaa, mlishe;
kama ana kiu, mpe kinywaji.
Kwa kufanya hivyo,
unaweka makaa ya moto yanayowaka kichwani pake.”
Shows Read in context, Share and Copy.