118 Bible Verses About Righteousness

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Righteousness
  1. 21 Lakini sasa, haki itokayo kwa Mungu imedhihirishwa pasipo sheria, ambayo Sheria na Manabii wanaishuhudia. 22 Haki hii itokayo kwa Mungu hupatikana kwa Yesu Kristo kwa wote wamwaminio. Kwa maana hapo hakuna tofauti, 23 kwa kuwa wote wametenda dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu, 24 wanahesabiwa haki bure kwa neema yake kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu. 25 Yeye ambaye Mungu alimtoa awe dhabihu ya upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake. Alifanya hivi ili kuonyesha haki yake, kwa sababu kwa ustahimili wake aliziachilia zile dhambi zilizotangulia kufanywa. 26 Alifanya hivyo ili kuonyesha haki yake wakati huu, ili yeye awe mwenye haki na mwenye kumhesabia haki yule anayemwamini Yesu.

    27 Basi, kujivuna kuko wapi? Kumewekwa mbali. Kwa sheria gani? Je, ni kwa ile ya matendo? La hasha, bali kwa ile sheria ya imani. 28 Kwa maana twaona kwamba mwanadamu huhesabiwa haki kwa njia ya imani wala si kwa matendo ya sheria.

  2. 20 Kwa hiyo sisi ni mabalozi wa Kristo, kana kwamba Mungu anawasihi kupitia kwa vinywa vyetu. Nasi twawaomba sana ninyi kwa niaba ya Kristo, mpatanishwe na Mungu. 21 Kwa maana Mungu alimfanya yeye asiyekuwa na dhambi kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kufanywa haki ya Mungu kwake yeye.

  3. 1 Ndugu zangu, shauku ya moyo wangu na maombi yangu kwa Mungu ni kwa ajili ya Waisraeli, kwamba waokolewe. 2 Kwa maana ninaweza nikashuhudia wazi kwamba wao wana juhudi kubwa kwa ajili ya Mungu, lakini juhudi yao haina maarifa. 3 Kwa kuwa hawakuijua haki itokayo kwa Mungu, wakatafuta kuweka haki yao wenyewe, hawakujitia chini ya haki ya Mungu. 4 Kwa maana Kristo ni ukomo wa sheria ili kuwe na haki kwa kila mtu aaminiye.

    5 Mose anaandika kuhusu haki ile itokanayo na sheria, kwamba, “Mtu atendaye matendo hayo ataishi kwa hayo.” 6 Lakini ile haki itokanayo na imani husema hivi: “Usiseme moyoni mwako, ‘Ni nani atakayepanda mbinguni?’ ” (yaani ili kumleta Kristo chini) 7 “au ‘Ni nani atashuka kwenda kuzimu?’ ” (yaani ili kumleta Kristo kutoka kwa wafu.) 8 Lakini andiko lasemaje? “Lile neno liko karibu nawe, liko kinywani mwako na moyoni mwako,” yaani, lile neno la imani tunalolihubiri. 9 Kwa sababu kama ukikiri kwa kinywa chako kwamba “Yesu ni Bwana,” na kuamini moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, utaokoka. 10 Kwa maana kwa moyo mtu huamini na hivyo kuhesabiwa haki, tena kwa kinywa mtu hukiri na hivyo kupata wokovu. 11 Kama yasemavyo Maandiko, “Yeyote amwaminiye hataaibika kamwe.” 12 Kwa maana hakuna tofauti kati ya Myahudi na Myunani, yeye ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao. 13 Kwa maana, “Kila mtu atakayeliitia Jina la Bwana, ataokolewa.”

  4. 2 Jihadharini na mbwa, wale watenda maovu, jihadharini na wale wajikatao miili yao, wasemao ili kuokoka ni lazima kutahiriwa. 3 Kwa maana sisi ndio tulio tohara, sisi tumwabuduo Mungu katika Roho, tunaona fahari katika Kristo Yesu, ambao hatuweki tumaini letu katika mwili, 4 ingawa mimi mwenyewe ninazo sababu za kuutumainia mwili.

    Kama mtu yeyote akidhani anazo sababu za kuutumainia mwili, mimi zaidi. 5 Nilitahiriwa siku ya nane, mimi ni Mwisraeli wa kabila la Benyamini, Mwebrania wa Waebrania. Kwa habari ya sheria, ni Farisayo, 6 kwa habari ya juhudi, nilikuwa nalitesa kanisa, kuhusu haki ipatikanayo kwa sheria, mimi nilikuwa sina hatia.

    7 Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, sasa nayahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo. 8 Zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara tupu nikiyalinganisha na faida kubwa ipitayo kiasi cha kumjua Kristo Yesu Bwana wangu, ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote, nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nimpate Kristo. 9 Nami nionekane mbele zake bila kuwa na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa imani katika Kristo, haki ile itokayo kwa Mungu kwa njia ya imani. 10 Nataka nimjue Kristo na uweza wa kufufuka kwake na ushirika wa mateso yake, ili nifanane naye katika mauti yake, 11 ili kwa njia yoyote niweze kufikia ufufuo wa wafu.

  5. 1 Tuseme nini basi, kuhusu Abrahamu baba yetu kwa jinsi ya mwili: yeye alipataje kujua jambo hili? 2 Kwa maana ikiwa Abrahamu alihesabiwa haki kwa matendo, basi, anacho kitu cha kujivunia, lakini si mbele za Mungu. 3 Kwa maana Maandiko yasemaje? “Abrahamu alimwamini Mungu na ikahesabiwa kwake kuwa haki.”

    4 Basi mtu afanyapo kazi, mshahara wake hauhesabiwi kwake kuwa ni zawadi, bali ni haki yake anayostahili. 5 Lakini kwa mtu ambaye hafanyi kazi na anamtumaini Mungu, yeye ambaye huwahesabia waovu haki, imani yake inahesabiwa kuwa haki. 6 Daudi pia alisema vivyo hivyo aliponena juu ya baraka za mtu ambaye Mungu humhesabia haki pasipo matendo:

    7 “Wamebarikiwa wale

    ambao wamesamehewa makosa yao,

    ambao dhambi zao zimefunikwa.

    8 Heri mtu yule

    Bwana hamhesabii dhambi zake.”

    9 Je, huku kubarikiwa ni kwa wale waliotahiriwa peke yao, au pia na kwa wale wasiotahiriwa? Tunasema, “Imani ya Abrahamu ilihesabiwa kwake kuwa haki.” 10 Je, ni lini basi ilipohesabiwa kwake kuwa haki? Je, ilikuwa kabla au baada ya kutahiriwa kwake? Haikuwa baada, ila kabla hajatahiriwa. 11 Alipewa ishara ya tohara kuwa muhuri wa haki aliyokuwa nayo kwa imani hata alipokuwa bado hajatahiriwa. Kusudi lilikuwa kumfanya baba wa wote wale waaminio pasipo kutahiriwa na ambao wamehesabiwa haki. 12 Vivyo hivyo awe baba wa wale waliotahiriwa ambao si kwamba wametahiriwa tu, bali pia wanafuata mfano wa imani ambayo Baba yetu Abrahamu alikuwa nayo kabla ya kutahiriwa.

  6. 30 Kwa hiyo tuseme nini basi? Kwamba watu wa Mataifa ambao hawakutafuta haki, wamepata haki ile iliyo kwa njia ya imani. 31 Lakini Israeli, ambao walijitahidi kupata haki kwa njia ya sheria, hawakuipata. 32 Kwa nini? Kwa sababu hawakuitafuta kwa njia ya imani bali kwa njia ya matendo. Wakajikwaa kwenye lile “jiwe la kukwaza.” 33 Kama ilivyoandikwa:

    “Tazama naweka katika Sayuni jiwe la kukwaza watu

    na mwamba wa kuwaangusha.

    Yeyote atakayemwamini

    hataaibika kamwe.”

  7. 13 Kwa maana ile ahadi kwamba angeurithi ulimwengu haikuja kwa Abrahamu au kwa wazao wake kwa njia ya sheria bali kwa njia ya haki ipatikanayo kwa imani. 14 Kwa maana ikiwa wale waishio kwa sheria ndio warithi, imani haina thamani na ahadi haifai kitu, 15 kwa sababu sheria huleta ghadhabu. Mahali ambapo hakuna sheria hakuna makosa.

    16 Kwa hiyo, ahadi huja kwa njia ya imani, ili iwe ni kwa neema, na itolewe kwa wazao wa Abrahamu, si kwa wale walio wa sheria peke yao, bali pia kwa wale walio wa imani ya Abrahamu. Yeye ndiye baba yetu sisi sote. 17 Kama ilivyoandikwa: “Nimekufanya wewe kuwa baba wa mataifa mengi.” Yeye ni baba yetu mbele za Mungu, ambaye yeye alimwamini, yule Mungu anaye fufua waliokufa, na kuvitaja vile vitu ambavyo haviko kana kwamba vimekwisha kuwako.

    18 Akitarajia yasiyoweza kutarajiwa, Abrahamu akaamini, akawa baba wa mataifa mengi, kama alivyoahidiwa kwamba, “Uzao wako utakuwa mwingi mno.” 19 Abrahamu hakuwa dhaifu katika imani hata alipofikiri juu ya mwili wake, ambao ulikuwa kama uliokufa, kwani umri wake ulikuwa unakaribia miaka mia moja, au alipofikiri juu ya ufu wa tumbo la Sara. 20 Lakini Abrahamu hakusitasita kwa kutokuamini ahadi ya Mungu, bali alitiwa nguvu katika imani yake na kumpa Mungu utukufu, 21 akiwa na hakika kabisa kwamba Mungu alikuwa na uwezo wa kutimiza lile aliloahidi. 22 Hii ndio sababu, “ilihesabiwa kwake kuwa haki.” 23 Maneno haya “ilihesabiwa kwake kuwa haki,” hayakuandikwa kwa ajili yake peke yake, 24 bali kwa ajili yetu sisi pia ambao Mungu atatupa haki, sisi tunaomwamini yeye aliyemfufua Yesu Bwana wetu kutoka kwa wafu. 25 Alitolewa afe kwa ajili ya dhambi zetu, naye alifufuliwa kutoka mauti ili tuhesabiwe haki.

  8. 16 Je, hamjui kwamba mnapojitoa kwa mtu yeyote kama watumwa watiifu, ninyi ni watumwa wa yule mnayemtii, aidha watumwa wa dhambi, ambayo matokeo yake ni mauti, au watumwa wa utii ambao matokeo yake ni haki? 17 Lakini Mungu ashukuriwe kwa kuwa ninyi ambao kwanza mlikuwa watumwa wa dhambi, mmekuwa watii kutoka moyoni kwa mafundisho mliyopewa. 18 Nanyi, mkiisha kuwekwa huru mbali na dhambi, mmekuwa watumwa wa haki.

    19 Ninasema kwa namna ya kibinadamu kwa sababu ya udhaifu wenu wa hali ya asili. Kama vile mlivyokuwa mkivitoa viungo vya miili yenu kama watumwa wa mambo machafu na uovu uliokuwa ukiongezeka zaidi, hivyo sasa vitoeni viungo vyenu kama watumwa wa haki inayowaelekeza mpate kutakaswa. 20 Mlipokuwa watumwa wa dhambi, mlikuwa hamtawaliwi na haki. 21 Lakini mlipata faida gani kwa mambo hayo ambayo sasa mnayaonea aibu? Mwisho wa mambo hayo ni mauti. 22 Lakini sasa kwa kuwa mmewekwa huru mbali na dhambi na mmekuwa watumwa wa Mungu, faida mnayopata ni utakatifu, ambao mwisho wake ni uzima wa milele.

  9. 14 Mimi ni mdeni kwa Wayunani na kwa wasio Wayunani, kwa wenye hekima na kwa wasio na hekima. 15 Ndiyo sababu ninatamani sana kuihubiri Injili kwenu pia ninyi mlioko Rumi.

    16 Mimi siionei haya Injili ya Kristo kwa maana ni uweza wa Mungu uletao wokovu kwa kila aaminiye, kwanza kwa Myahudi na kwa Myunani pia. 17 Kwa maana katika Injili haki itokayo kwa Mungu imedhihirishwa, haki ile iliyo kwa njia ya imani hadi imani. Kama ilivyoandikwa: “Mwenye haki ataishi kwa imani.”

  10. 29 Kama mkijua kuwa yeye ni mwenye haki, mwajua kwamba kila atendaye haki amezaliwa naye.

  11. 16 Tena, ile karama ya Mungu si kama matokeo ya ile dhambi. Hukumu ilikuja kwa njia ya mtu mmoja, ikaleta adhabu, bali karama ya neema ya Mungu ilikuja kwa njia ya makosa mengi, ikaleta kuhesabiwa haki. 17 Kwa maana ikiwa kutokana na kosa la mtu mmoja, mauti ilitawala kupitia huyo mtu mmoja, zaidi sana wale wanaopokea wingi wa neema ya Mungu na karama yake ya kuhesabiwa haki, watatawala katika uzima kwa njia ya huyo mtu mmoja, yaani, Yesu Kristo.

    18 Kwa hiyo, kama vile kosa la mtu mmoja lilivyoleta adhabu kwa watu wote, vivyo hivyo pia kwa tendo la haki la mtu mmoja lilileta kuhesabiwa haki ambako huleta uzima kwa wote. 19 Kwa maana kama vile kwa kutokutii kwa yule mtu mmoja wengi walifanywa wenye dhambi, vivyo hivyo kwa kutii kwa mtu mmoja wengi watafanywa wenye haki.

  12. 5 Bwana asema, “Siku zinakuja,

    nitakapomwinulia Daudi Tawi lenye haki,

    Mfalme atakayetawala kwa hekima,

    na kutenda lililo haki na sawa katika nchi.

    6 Katika siku zake, Yuda ataokolewa

    na Israeli ataishi salama.

    Hili ndilo jina atakaloitwa:

    Bwana Haki Yetu.

    7 “Hivyo basi, siku zinakuja, wakati ambapo watu hawatasema tena, ‘Hakika kama Bwana aishivyo, aliyewapandisha Waisraeli kutoka Misri,’

  13. 6 Heri wenye njaa na kiu ya haki,

    maana hao watatoshelezwa.

  14. 1 Kwa hiyo, kwa kuwa tumekwisha kuhesabiwa haki kwa imani, tuna amani na Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, 2 ambaye kwa kupitia kwake tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo ndani yake sasa tunasimama, nasi twafurahia katika tumaini letu la kushiriki utukufu wa Mungu. 3 Si hivyo tu, bali twafurahi pia katika mateso, kwa sababu tunajua kuwa mateso huleta saburi, 4 nayo saburi huleta uthabiti wa moyo, na uthabiti wa moyo huleta tumaini, 5 wala tumaini halitukatishi tamaa, kwa sababu Mungu amekwisha kumimina pendo lake mioyoni mwetu kwa njia ya Roho Mtakatifu ambaye ametupatia.

    6 Kwa maana hata tulipokuwa dhaifu, wakati ulipowadia, Kristo alikufa kwa ajili yetu sisi wenye dhambi. 7 Hakika, ni vigumu mtu yeyote kufa kwa ajili ya mwenye haki, ingawa inawezekana mtu akathubutu kufa kwa ajili ya mtu mwema. 8 Lakini Mungu anaudhihirisha upendo wake kwetu kwamba: Tulipokuwa tungali wenye dhambi, Kristo alikufa kwa ajili yetu.

    9 Basi, kwa kuwa sasa tumehesabiwa haki kwa damu yake, si zaidi sana tutaokolewa kutoka ghadhabu ya Mungu kupitia kwake! 10 Kwa kuwa kama tulipokuwa adui wa Mungu tulipatanishwa naye kwa njia ya kifo cha Mwanawe, si zaidi sana tukiisha kupatanishwa, tutaokolewa kwa uzima wake. 11 Lakini zaidi ya hayo, pia tunafurahi katika Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kupitia kwake tumepata upatanisho.

  15. 26 Ndugu zangu, kumbukeni mlivyokuwa mlipoitwa. Kwa kipimo cha kibinadamu, si wengi wenu mliokuwa na hekima. Si wengi mliokuwa na ushawishi, si wengi mliozaliwa katika jamaa zenye vyeo. 27 Lakini Mungu alivichagua vitu vipumbavu vya ulimwengu ili awaaibishe wenye hekima, Mungu alivichagua vitu dhaifu vya ulimwengu ili awaaibishe wenye nguvu. 28 Alivichagua vitu vya chini na vinavyodharauliwa vya dunia hii, vitu ambavyo haviko, ili avibatilishe vile vilivyoko, 29 ili mtu yeyote asijisifu mbele zake. 30 Bali kwa yeye ninyi mmepata kuwa katika Kristo Yesu, aliyefanyika kwetu hekima itokayo kwa Mungu, yaani haki, na utakatifu na ukombozi. 31 Hivyo, kama ilivyoandikwa: “Yeye ajisifuye na ajisifu katika Bwana.”

  16. 6 Sisi sote tumekuwa kama mtu aliye najisi,

    nayo matendo yetu yote ya uadilifu ni kama matambaa machafu;

    sisi sote tunasinyaa kama jani,

    na kama upepo maovu yetu hutupeperusha.

  17. 31 Kwa hiyo msiwe na wasiwasi, mkisema, ‘Tutakula nini?’ au ‘Tutakunywa nini?’ au ‘Tutavaa nini?’ 32 Watu wasiomjua Mungu ndio wanaoshindania hayo, lakini Baba yenu wa mbinguni anafahamu kuwa mnahitaji haya yote. 33 Lakini utafuteni kwanza Ufalme wa Mungu na haki yake, na haya yote atawapa pia.

  18. 24 Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, ili tufe kwa mambo ya dhambi, bali tupate kuishi katika haki. Kwa kupigwa kwake, ninyi mmeponywa.

  19. 9 Haya ndiyo maombi yangu: kwamba upendo wenu uongezeke zaidi na zaidi katika maarifa na ufahamu wote, 10 ili mpate kutambua yale yaliyo mema, mkawe safi, wasio na hatia hadi siku ya Kristo, 11 mkiwa mmejawa na matunda ya haki yapatikanayo kwa njia ya Yesu Kristo, kwa utukufu na sifa za Mungu.

  20. 4 “Nisikilizeni, watu wangu;

    nisikieni, taifa langu:

    Sheria itatoka kwangu;

    haki yangu itakuwa nuru kwa mataifa.

    5 Haki yangu inakaribia mbio,

    wokovu wangu unakuja,

    nao mkono wangu utaleta hukumu kwa mataifa.

    Visiwa vitanitegemea

    na kungojea mkono wangu kwa matumaini.

    6 Inueni macho yenu mbinguni,

    mkaitazame dunia chini;

    mbingu zitatoweka kama moshi,

    dunia itachakaa kama vazi,

    na wakazi wake kufa kama mainzi.

    Bali wokovu wangu utadumu milele,

    haki yangu haitakoma kamwe.

    7 “Nisikieni, ninyi mnaojua lililo sawa,

    ninyi watu ambao mna sheria yangu mioyoni mwenu:

    Msiogope mashutumu ya wanadamu

    wala msitiwe hofu na matukano yao.

    8 Kwa maana nondo atawala kama vazi,

    nao funza atawatafuna kama sufu.

    Lakini haki yangu itadumu milele,

    wokovu wangu kwa vizazi vyote.”

  21. 1 Baada ya jambo hili, neno la Bwana likamjia Abramu katika maono:

    “Usiogope, Abramu.

    Mimi ni ngao yako,

    na thawabu yako kubwa sana.”

    2 Lakini Abramu akasema, “Ee Bwana Mwenyezi, utanipa nini na mimi sina hata mtoto na atakayerithi nyumba yangu ni huyu Eliezeri Mdameski?” 3 Abramu akasema, “Hukunipa watoto, hivyo mtumishi katika nyumba yangu ndiye atakuwa mrithi wangu.”

    4 Ndipo neno la Bwana lilipomjia: “Mtu huyu hatakuwa mrithi wako, bali mwana atakayetoka katika viuno vyako mwenyewe ndiye atakayekuwa mrithi wako.” 5 Akamtoa nje na kusema, “Tazama juu kuelekea mbinguni na uhesabu nyota, kama hakika utaweza kuzihesabu.” Ndipo akamwambia, “Hivyo ndivyo uzao wako utakavyokuwa.”

    6 Abramu akamwamini Bwana, naye kwake hili likahesabiwa kuwa haki.

  22. 13 Kwa hiyo tusiendelee kuhukumiana: Badala yake mtu asiweke kamwe kikwazo au kizuizi katika njia ya ndugu mwingine. 14 Ninajua tena nimehakikishiwa sana katika Bwana Yesu kwamba hakuna kitu chochote ambacho ni najisi kwa asili yake. Lakini kama mtu anakiona kitu kuwa ni najisi, basi kwake huyo kitu hicho ni najisi. 15 Kama ndugu yako anahuzunishwa kwa sababu ya kile unachokula, basi huenendi tena katika upendo. Usiruhusu kile unachokula kiwe sababu ya kumwangamiza ndugu yako ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake. 16 Usiruhusu kile ambacho unakiona kuwa chema kisemwe kuwa ni kiovu. 17 Kwa maana Ufalme wa Mungu si kula na kunywa, bali ni haki, amani na furaha katika Roho Mtakatifu. 18 Kwa sababu mtu yeyote anayemtumikia Kristo kwa jinsi hii, anampendeza Mungu na kukubaliwa na wanadamu.

    19 Kwa hiyo na tufanye bidii kutafuta yale yaletayo amani na kujengana sisi kwa sisi.

  23. 2 Roho wa Bwana atakaa juu yake,

    Roho wa hekima na wa ufahamu,

    Roho wa shauri na wa uweza,

    Roho wa maarifa na wa kumcha Bwana

    3 naye atafurahia kumcha Bwana.

    Hatahukumu kwa yale ayaonayo kwa macho yake,

    wala kuamua kwa yale ayasikiayo kwa masikio yake,

    4 bali kwa uadilifu atahukumu wahitaji,

    kwa haki ataamua wanyenyekevu wa dunia.

    Ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake,

    kwa pumzi ya midomo yake atawaua waovu.

    5 Haki itakuwa mkanda wake

    na uaminifu utakuwa mshipi kiunoni mwake.

  24. 1 “Nisikilizeni, ninyi mnaofuatia haki

    na mnaomtafuta Bwana:

    Tazameni mwamba ambako mlichongwa,

    na mahali pa kuvunjia mawe ambako mlichimbwa;

    2 mwangalieni Abrahamu, baba yenu,

    na Sara, ambaye aliwazaa.

    Wakati nilipomwita alikuwa mmoja tu,

    nami nikambariki na kumfanya kuwa wengi.

  25. 1 Kwa hiyo, sasa hakuna hukumu ya adhabu kwa wale walio ndani ya Kristo Yesu, wale ambao hawaenendi kwa kuufuata mwili bali kwa kufuata Roho. 2 Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima katika Kristo Yesu imeniweka huru mbali na sheria ya dhambi na mauti. 3 Kwa maana kile ambacho sheria haikuwa na uwezo wa kufanya, kwa vile ilivyokuwa dhaifu katika mwili, Mungu kwa kumtuma Mwanawe mwenyewe kwa mfano wa mwanadamu mwenye mwili ulio wa dhambi na kwa ajili ya dhambi, yeye aliihukumu dhambi katika mwili, 4 ili kwamba haki ipatikanayo kwa sheria itimizwe ndani yetu sisi, ambao hatuenendi kwa kuufuata mwili bali kwa kufuata Roho.

    5 Kwa maana wale wanaoishi kwa kuufuata mwili huziweka nia zao katika vitu vya mwili, lakini wale wanaoishi kwa kufuata Roho, huziweka nia zao katika mambo ya Roho. 6 Kwa maana kuwa na nia ya mwili ni mauti, bali kuwa na nia inayoongozwa na Roho ni uzima na amani. 7 Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui na Mungu, kwa maana haiitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii. 8 Wale wanaotawaliwa na mwili, hawawezi kumpendeza Mungu.

    9 Lakini ninyi, hamtawaliwi na mwili, bali na Roho, ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu. Mtu yeyote ambaye hana Roho wa Kristo, yeye si wa Kristo. 10 Lakini kama Kristo anakaa ndani yenu, miili yenu imekufa kwa sababu ya dhambi, lakini roho zenu zi hai kwa sababu ya haki. 11 Nanyi ikiwa Roho wa Mungu aliyemfufua Yesu kutoka kwa wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu kutoka kwa wafu ataihuisha pia miili yenu ambayo hufa, kwa njia ya Roho wake akaaye ndani yenu.

  26. 14 Lakini mmebarikiwa hata kama ikiwalazimu kuteseka kwa ajili ya haki. “Msiogope vitisho vyao, wala msiwe na wasiwasi.”

  27. 4 Utajiri haufaidi kitu katika siku ya ghadhabu,

    bali haki huokoa kutoka mautini.

    5 Haki ya wasio na lawama, huwatengenezea njia iliyonyooka,

    bali waovu huangushwa kwa uovu wao wenyewe.

    6 Haki ya wanyofu huwaokoa,

    bali wasio waaminifu hunaswa na tamaa mbaya.

  28. 24 Watasema kuhusu mimi,

    ‘Katika Bwana peke yake

    ndiko kuna haki na nguvu.’ ”

    Wote ambao wamemkasirikia Mungu

    watamjia yeye, nao watatahayarika.

    25 Lakini katika Bwana wazao wote wa Israeli

    wataonekana wenye haki na watashangilia.

  29. 11 Lakini wewe, mtu wa Mungu, yakimbie mambo haya yote. Fuata haki, utauwa, imani, upendo, saburi na upole. 12 Pigana vile vita vizuri vya imani. Shika uzima wa milele ambao ndio ulioitiwa ulipokiri ule ukiri mzuri mbele ya mashahidi wengi. 13 Nakuagiza mbele za Mungu avipaye vitu vyote uhai, na mbele za Kristo Yesu ambaye alipokuwa anashuhudia mbele ya Pontio Pilato alikiri ukiri mzuri, 14 uishike amri hii bila dosari wala lawama mpaka kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo, 15 ambaye Mungu atamleta kwa wakati wake mwenyewe: yeye ahimidiwaye, aliye peke yake Mtawala, Mfalme wa wafalme, na Bwana wa mabwana, 16 yeye peke yake ambaye hapatikani na mauti, na anakaa katika nuru isiyoweza kukaribiwa, ambaye hakuna mwanadamu aliyemwona wala awezaye kumwona. Heshima na uweza una yeye milele. Amen.

  30. 6 Kwa maana mimi sasa ni tayari kumiminwa kama sadaka ya kinywaji, nayo saa yangu ya kuondoka imetimia. 7 Nimevipiga vita vizuri, mashindano nimeyamaliza, imani nimeilinda. 8 Sasa nimewekewa taji ya haki ambayo Bwana, mwamuzi wa haki, atanitunukia siku ile: wala si mimi tu, bali pia wote ambao wamengoja kwa shauku kudhihirishwa kwake.

  31. 16 Haki itakaa katika jangwa,

    na uadilifu utakaa katika shamba lenye rutuba.

    17 Matunda ya haki yatakuwa amani,

    matokeo ya haki yatakuwa utulivu

    na matumaini milele.

    18 Watu wangu wataishi katika makao ya mahali pa amani,

    katika nyumba zilizo salama,

    katika mahali pa kupumzika pasipo na usumbufu.

  32. 17 “Msidhani kwamba nimekuja kufuta Sheria au Manabii; sikuja kuondoa bali kutimiza. 18 Kwa maana, amin nawaambia, mpaka mbingu na dunia zitakapopita, hakuna hata herufi moja ndogo wala nukta itakayopotea kwa namna yoyote kutoka kwenye Sheria, mpaka kila kitu kiwe kimetimia. 19 Kwa hiyo, yeyote atakayevunja mojawapo ya amri ndogo kuliko zote ya amri hizi, naye akawafundisha wengine kufanya hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika Ufalme wa Mbinguni, lakini yeyote azitendaye na kuzifundisha hizi amri ataitwa mkuu katika Ufalme wa Mbinguni. 20 Kwa maana nawaambia, haki yenu isipozidi haki ya Mafarisayo na walimu wa sheria, kamwe hamtaingia katika Ufalme wa Mbinguni.

  33. 17 Hivyo nawaambia hivi, nami nasisitiza katika Bwana kwamba, msiishi tena kama watu wa Mataifa waishivyo, katika ubatili wa mawazo yao. 18 Watu hao akili zao zimetiwa giza na wametengwa mbali na uzima wa Mungu kwa sababu ya ujinga wao kutokana na ugumu wa mioyo yao. 19 Wakiisha kufa ganzi, wamejitia katika mambo ya ufisadi na kupendelea kila aina ya uchafu, wakiendelea kutamani zaidi.

    20 Lakini ninyi, hivyo sivyo mlivyojifunza Kristo. 21 Kama hivyo ndivyo ilivyo, ninyi mmemsikia, tena mmefundishwa naye, vile kweli ilivyo katika Yesu. 22 Mlifundishwa kuuvua mwenendo wenu wa zamani, utu wenu wa kale, ulioharibiwa na tamaa zake za udanganyifu, 23 ili mfanywe upya roho na nia zenu, 24 mkajivike utu mpya, ulioumbwa sawasawa na mfano wa Mungu katika haki yote na utakatifu.

  34. 8 Lakini kwa habari za Mwana asema,

    “Kiti chako cha enzi, Ee Mungu,

    kitadumu milele na milele,

    nayo haki itakuwa fimbo ya utawala

    ya ufalme wako.

    9 Umependa haki na kuchukia uovu;

    kwa hiyo Mungu, Mungu wako,

    amekuweka juu ya wenzako

    kwa kukupaka mafuta ya furaha.”

  35. 18 Mtu mwovu hupata ujira wa udanganyifu,

    bali yeye apandaye haki huvuna tuzo ya uhakika.

    19 Mtu mwenye haki kweli kweli hupata uzima,

    bali yeye afuatiliaye ubaya huendea kifo chake.

  36. 12 Jipandieni wenyewe haki,

    vuneni matunda ya upendo usio na kikomo,

    vunjeni ardhi yenu isiyolimwa;

    kwa kuwa ni wakati wa kumtafuta Bwana,

    mpaka atakapokuja

    na kuwanyeshea juu yenu haki.

  37. 9 Tusemeje basi? Je, sisi ni bora kuwaliko wao? La hasha! Kwa maana tumekwisha kuhakikisha kwa vyovyote kwamba Wayahudi na watu wa Mataifa wote wako chini ya nguvu ya dhambi. 10 Kama ilivyoandikwa:

    “Hakuna mwenye haki, hakuna hata mmoja.

    11 Hakuna hata mmoja mwenye ufahamu,

    hakuna hata mmoja amtafutaye Mungu.

    12 Wote wamepotoka,

    wote wameoza pamoja;

    hakuna atendaye mema,

    naam, hakuna hata mmoja.”

  38. 1 Ninyi Wagalatia wajinga! Ni nani aliyewaroga? Yesu Kristo aliwekwa wazi mbele yenu kwamba amesulubiwa. 2 Nataka nijifunze neno moja kutoka kwenu: Je, mlipokea Roho wa Mungu kwa kushika sheria, au kwa kuyaamini yale mliyosikia? 3 Je, ninyi ni wajinga kiasi hicho? Baada ya kuanza kwa Roho, je, sasa mwataka kumalizia katika mwili? 4 Je, mlipata mateso kiasi hicho bure? Ni kama kweli yalikuwa bure! 5 Je, Mungu huwapa Roho wake na kufanya miujiza katikati yenu kwa sababu mnatii sheria, au kwa sababu mnaamini kile mlichosikia?

    6 Kama vile “Abrahamu alimwamini Mungu na ikahesabiwa kwake kuwa haki.” 7 Fahamuni basi kwamba wale walio na imani, hao ndio watoto wa Abrahamu. 8 Maandiko yakitabiri kwamba Mungu angewahesabia haki watu wa Mataifa kwa imani, alitangulia kumtangazia Abrahamu Injili akisema kwamba, “Kwa kupitia kwako mataifa yote yatabarikiwa.” 9 Kwa sababu hii, wale wote wanaoamini wanabarikiwa pamoja na Abrahamu, mtu wa imani.

  39. 22 Zikimbie tamaa mbaya za ujana, ufuate haki, imani, upendo na amani pamoja na wale wamwitao Bwana kwa moyo safi.

  40. 7 Kwa kuwa Bwana ni mwenye haki,

    yeye hupenda haki.

    Wanyofu watauona uso wake.

  41. 2 Njia zote za mwanadamu huonekana sawa kwake,

    bali Bwana huupima moyo.

    3 Kufanya yaliyo sawa na haki inakubalika

    zaidi kwa Bwana kuliko dhabihu.

  42. 7 “Bwana, wewe ni mwenye haki, lakini siku hii ya leo tumefunikwa na aibu: tukiwa wanaume wa Yuda, na watu wa Yerusalemu, na Israeli yote, wote walio karibu na walio mbali, katika nchi zote ulikotutawanya kwa sababu ya kukosa uaminifu kwako. 8 Ee Bwana, sisi na wafalme wetu, wakuu wetu na baba zetu tumefunikwa na aibu kwa sababu tumefanya dhambi dhidi yako.

  43. 11 Vivyo hivyo, jihesabuni wafu katika dhambi lakini mlio hai kwa Mungu katika Kristo Yesu. 12 Kwa hiyo, msiruhusu dhambi itawale ndani ya miili yenu, ipatikanayo na kufa, ili kuwafanya mzitii tamaa mbaya. 13 Wala msivitoe viungo vya miili yenu vitumike kama vyombo vya uovu vya kutenda dhambi, bali jitoeni kwa Mungu, kama watu waliotolewa kutoka mautini kuingia uzimani. Nanyi vitoeni viungo vya miili yenu kwake kama vyombo vya haki. 14 Kwa maana dhambi haitakuwa na mamlaka juu yenu, kwa sababu hampo chini ya sheria, bali chini ya neema.

  44. 5 Kwa maana, kwa njia ya Roho kwa imani, tunangojea kwa shauku tumaini la haki.

  45. 14 Bali wewe, udumu katika yale uliyojifunza na kuyaamini kwa uthabiti, ukitambua ya kuwa ulijifunza hayo kutoka kwa nani, 15 na jinsi ambavyo tangu utoto umeyajua Maandiko matakatifu, ambayo yanaweza kukuhekimisha upate wokovu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. 16 Kila Andiko limevuviwa na Mungu na lafaa kwa mafundisho, kwa kuwaonya watu makosa yao, kwa kuwaongoza na kwa kuwafundisha katika haki, 17 ili mtu wa Mungu awe amekamilishwa, apate kutenda kila kazi njema.

  46. 15 Macho ya Bwana huwaelekea wenye haki,

    na masikio yake yako makini kusikiliza kilio chao.

  47. 3 Nyumbani mwake kuna mali na utajiri,

    haki yake hudumu milele.

  48. 15 Yeye aendaye kwa uadilifu

    na kusema lililo haki,

    yeye anayekataa faida ipatikanayo kwa dhuluma

    na kuizuia mikono yake isipokee rushwa,

    yeye azuiaye masikio yake dhidi ya mashauri ya mauaji,

    na yeye afumbaye macho yake yasitazame sana uovu:

    16 huyu ndiye mtu atakayeishi mahali pa juu,

    ambaye kimbilio lake litakuwa ngome ya mlimani.

    Atapewa mkate wake,

    na maji yake hayatakoma.

    17 Macho yenu yatamwona mfalme katika uzuri wake

    na kuiona nchi inayoenea mbali.

  49. 23 Hili ndilo asemalo Bwana:

    “Mwenye hekima asijisifu katika hekima yake,

    au mwenye nguvu ajisifu katika nguvu zake,

    wala tajiri ajisifu katika utajiri wake,

    24 lakini yeye ajisifuye, na ajisifu kwa sababu hili:

    kwamba ananifahamu na kunijua mimi,

    kwamba mimi ndimi Bwana, nitendaye wema,

    hukumu na haki duniani,

    kwa kuwa napendezwa na haya,”

    asema Bwana.

  50. 10 Heri wanaoteswa kwa sababu ya haki,

    maana Ufalme wa Mbinguni ni wao.

  51. 22 Basi wale watu wakageuka wakaenda kuelekea Sodoma, lakini Abrahamu akabaki amesimama mbele za Bwana. 23 Ndipo Abrahamu akamsogelea akasema: “Je, utawaangamiza wenye haki na waovu? 24 Je, ikiwa watakuwepo watu wenye haki hamsini katika mji huo, hivi kweli utauangamiza na wala hutauacha kwa ajili ya hao watu hamsini wenye haki waliomo ndani yake? 25 Hilo na liwe mbali nawe, kufanya jambo kama hilo, kuwaua wenye haki pamoja na waovu, kuwatendea wenye haki sawasawa na waovu. Iwe mbali nawe! Je, Mwamuzi wa dunia yote hatafanya lililo sawa?”

    26 Bwana akasema, “Kama nikipata watu hamsini wenye haki katika mji wa Sodoma, nitausamehe huo mji wote kwa ajili yao.”

    27 Kisha Abrahamu akasema tena: “Sasa kwa kuwa nimekuwa na ujasiri wa kuzungumza na Bwana, ingawa mimi si kitu bali ni mavumbi na majivu; 28 je, kama hesabu ya wenye haki imepungua watano katika hamsini, utauangamiza huo mji wote kwa ajili ya hao watano waliopungua?”

    Bwana akamwambia, “Kama nikiwakuta huko watu arobaini na watano, sitauangamiza.”

    29 Abrahamu akazungumza naye kwa mara nyingine, “Je, kama huko watapatikana watu arobaini tu?”

    Akamjibu, “Kwa ajili ya hao arobaini, sitauangamiza.”

    30 Ndipo akasema, “Bwana na asikasirike, lakini niruhusu nizungumze. Je, kama huko watakuwepo thelathini tu?”

    Akajibu, “Sitapaangamiza ikiwa nitawakuta huko watu thelathini.”

    31 Abrahamu akasema, “Sasa kwa kuwa nimekuwa na ujasiri sana kuzungumza na Bwana, je, kama wakipatikana huko watu ishirini tu?”

    Bwana akajibu, “Kwa ajili ya hao ishirini, sitauangamiza.”

    32 Abrahamu akasema, “Bwana na asikasirike, lakini niruhusu nizungumze tena mara moja tu. Itakuwaje kama watapatikana huko watu kumi tu?”

    Bwana akajibu, “Kwa ajili ya hao kumi, sitauangamiza.”

    33 Bwana alipomaliza kuzungumza na Abrahamu, akaondoka, naye Abrahamu akarudi nyumbani kwake.

  52. 25 Kama tukizitii kwa bidii amri hizi zote mbele za Bwana Mungu wetu, kama alivyotuamuru sisi, hiyo itakuwa haki yetu.”

  53. 7 Unaipenda haki na kuchukia uovu;

    kwa hiyo Mungu, Mungu wako,

    amekuweka juu ya wenzako,

    kwa kukupaka mafuta ya furaha.

  54. 2 Hazina zilizopatikana kwa njia mbaya hazifai,

    lakini uadilifu huokoa kutoka mautini.

    3 Bwana hawaachi waadilifu kukaa njaa,

    lakini hupinga tamaa ya mtu mwovu.

  55. 9 Bwana huchukia sana njia ya waovu,

    bali huwapenda wale wafuatao haki.

  56. 10 Ninafurahia sana katika Bwana,

    nafsi yangu inashangilia katika Mungu wangu.

    Kwa maana amenivika mavazi ya wokovu,

    na kunipamba kwa joho la haki,

    kama vile bwana arusi apambavyo

    kichwa chake kama kuhani,

    na kama bibi arusi ajipambavyo

    kwa vito vyake vya thamani.

  57. 14 Msifungiwe nira pamoja na watu wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa, kwa maana pana uhusiano gani kati ya haki na uovu? Au kuna ushirika gani kati ya nuru na giza?

  58. 9 (kwa kuwa tunda la nuru hupatikana katika wema wote, haki na kweli),

  59. 10 Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. 11 Vaeni silaha zote za Mungu ili kwamba mweze kuzipinga hila za ibilisi. 12 Kwa maana kushindana kwetu si juu ya nyama na damu, bali dhidi ya falme, mamlaka, dhidi ya wakuu wa giza na majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. 13 Kwa hiyo vaeni silaha zote za Mungu ili mweze kushindana siku ya uovu itakapokuja nanyi mkiisha kufanya yote, simameni imara. 14 Kwa hiyo simameni imara mkiwa mmejifunga kweli kiunoni na kuvaa dirii ya haki kifuani, 15 nayo miguu yenu ifungiwe utayari tuupatao kwa Injili ya amani. 16 Zaidi ya haya yote, twaeni ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu. 17 Vaeni chapeo ya wokovu na mchukue upanga wa Roho, ambao ni Neno la Mungu. 18 Mkiomba kwa Roho siku zote katika sala zote na maombi, mkikesha kila wakati mkiwaombea watakatifu wote.

    19 Niombeeni na mimi pia, ili kila nifunguapo kinywa changu, nipewe maneno ya kusema, niweze kutangaza siri ya Injili kwa ujasiri, 20 ambayo mimi ni balozi wake katika vifungo. Ombeni ili nipate kuhubiri kwa ujasiri kama inipasavyo.

  60. 7 Vumilieni taabu kwa ajili ya kufunzwa adabu. Mungu anawatendea ninyi kama watoto wake, kwa maana ni mtoto yupi asiyeadibishwa na mzazi wake? 8 Kama hakuna kuadibishwa (ambalo ni fungu la watoto wote), basi ninyi ni watoto wa haramu wala si watoto halali. 9 Tena, sisi sote tunao baba wa kimwili, waliotuadibisha nasi tukawaheshimu kwa ajili ya hilo. Je, si inatupasa kujinyenyekeza zaidi kwa Baba wa roho zetu ili tuishi? 10 Baba zetu walituadibisha kwa kitambo kidogo kama wao wenyewe walivyoona vyema, lakini Mungu hutuadibisha kwa faida yetu ili tupate kushiriki utakatifu wake. 11 Kuadibishwa wakati wowote hakuonekani kuwa kitu cha kufurahisha bali chenye maumivu kinapotekelezwa. Lakini baadaye huzaa matunda ya haki na amani kwa wale waliofunzwa nayo.

    12 Kwa hiyo, itieni nguvu mikono yenu iliyo dhaifu na magoti yenu yaliyolegea. 13 Sawazisheni mapito ya miguu yenu, ili kitu kilicho kiwete kisidhoofishwe bali kiponywe.

    14 Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote na huo utakatifu, ambao bila kuwa nao hakuna mtu atakayemwona Bwana. 15 Angalieni sana mtu yeyote asiikose neema ya Mungu na kwamba shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo. 16 Angalieni miongoni mwenu asiwepo mwasherati au mtu asiyemcha Mungu kama Esau, ambaye kwa ajili ya mlo mmoja aliuza haki ya uzaliwa wake wa kwanza. 17 Baadaye kama mnavyofahamu, alipotaka kurithi ile baraka, alikataliwa, maana hakupata nafasi ya kutubu, ingawa aliitafuta kwa machozi.

  61. 16 Kwa hiyo ungamianeni dhambi zenu ninyi kwa ninyi na kuombeana ili mpate kuponywa. Maombi ya mwenye haki yana nguvu tena yanafaa sana.

  62. 4 Hata gizani nuru humzukia mtu mwadilifu,

    yule mwenye rehema, huruma na haki.

    5 Mema yatamjia mtu yule aliye mkarimu na mwenye kukopesha bila riba,

    anayefanya mambo yake kwa haki.

    6 Hakika hatatikisika kamwe,

    mtu mwenye haki atakumbukwa milele.

    7 Hataogopa habari mbaya,

    moyo wake ni thabiti, ukimtegemea Bwana.

    8 Moyo wake ni salama, hatakuwa na hofu,

    mwishoni ataona ushindi dhidi ya adui zake.

  63. 142 Haki yako ni ya milele,

    na sheria yako ni kweli.

  64. 28 Katika njia ya haki kuna uzima;

    katika mapito hayo kuna maisha ya milele.

  65. 3 Mtafuteni Bwana, enyi nyote wanyenyekevu wa nchi,

    ninyi ambao hufanya lile analoamuru.

    Tafuteni haki, tafuteni unyenyekevu;

    labda mtahifadhiwa

    siku ya hasira ya Bwana.

  66. 29 “Kwa kuwa sisi ni watoto wa Mungu, haitupasi kudhani kuwa uungu ni kama sanamu ya dhahabu au ya fedha au ya jiwe, mfano uliotengenezwa kwa ubunifu na ustadi wa mwanadamu. 30 Zamani wakati wa ujinga, Mungu alijifanya kama haoni, lakini sasa anawaamuru watu wote kila mahali watubu. 31 Kwa kuwa ameweka siku ambayo atauhukumu ulimwengu kwa haki akimtumia mtu aliyemchagua. Amewahakikishia watu wote mambo haya kwa kumfufua Kristo kutoka kwa wafu.”

  67. 20 Kwa hiyo hakuna binadamu hata mmoja atakayehesabiwa haki mbele za Mungu kwa matendo ya sheria, kwa maana sheria hutufanya tuitambue dhambi.

  68. 12 Kwa maana macho ya Bwana

    huwaelekea wenye haki,

    na masikio yake yako makini

    kusikiliza maombi yao.

    Bali uso wa Bwana uko kinyume

    na watendao maovu.”

  69. 4 Kila mtu atendaye dhambi afanya uasi, kwa kuwa dhambi ni uasi. 5 Lakini mwajua ya kuwa yeye alidhihirishwa ili aziondoe dhambi, wala ndani yake hamna dhambi. 6 Kila mtu akaaye ndani yake hatendi dhambi. Kila mtu atendaye dhambi hakumwona yeye wala hakumtambua.

    7 Watoto wapendwa, mtu yeyote asiwadanganye. Kila mtu atendaye haki ana haki, kama yeye alivyo na haki. 8 Yeye atendaye dhambi ni wa ibilisi, kwa sababu ibilisi amekuwa akitenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili aziangamize kazi za ibilisi. 9 Yeyote aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wa Mungu wakaa ndani yake, wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa na Mungu. 10 Kwa jinsi hii tunaweza kujua dhahiri watoto wa Mungu na pia watoto wa ibilisi. Yeyote asiyetenda haki hatokani na Mungu, wala yeye asiyempenda ndugu yake.

  70. 4 Sivyo walivyo waovu!

    Wao ni kama makapi

    yapeperushwayo na upepo.

    5 Kwa hiyo waovu hawatastahimili hukumu,

    wala wenye dhambi katika kusanyiko la wenye haki.

    6 Kwa maana Bwana huziangalia njia za mwenye haki,

    bali njia ya waovu itaangamia.

  71. 12 Kwa hakika, Ee Bwana, unawabariki wenye haki,

    unawazunguka kwa wema wako kama ngao.

  72. 15 Kinywa changu kitasimulia haki yako,

    wokovu wako mchana kutwa,

    ingawa sifahamu kipimo chake.

  73. 3 Heri wale wanaodumisha haki,

    ambao daima wanafanya yaliyo mema.

  74. 24 “Majuma sabini yameamriwa kwa ajili ya watu wako na kwa ajili ya mji wako mtakatifu, ili kumaliza makosa, kukomesha dhambi, kufanya upatanisho kwa ajili ya uovu, kuleta haki ya milele, kutia muhuri maono na unabii, na pia kumtia mafuta yeye aliye mtakatifu sana.

  75. 14 Ndugu zangu, yafaa nini ikiwa mtu atadai kuwa anayo imani lakini hana matendo? Je, imani kama hiyo yaweza kumwokoa? 15 Ikiwa ndugu yako au dada hana mavazi wala chakula, 16 mmoja wenu akamwambia, “Enenda zako kwa amani, ukaote moto na kushiba,” pasipo kumpatia yale mahitaji ya mwili aliyopungukiwa, yafaa nini? 17 Vivyo hivyo, imani peke yake kama haikuambatana na matendo, imekufa.

    18 Lakini mtu mwingine atasema, “Wewe unayo imani; mimi ninayo matendo.”

    Nionyeshe imani yako pasipo matendo nami nitakuonyesha imani yangu kwa matendo. 19 Unaamini kwamba kuna Mungu mmoja. Vyema! Hata mashetani yanaamini hivyo na kutetemeka.

    20 Ewe mpumbavu! Je, wataka kujua kwamba imani bila matendo haifai kitu? 21 Je, Abrahamu baba yetu hakuhesabiwa haki kwa kile alichotenda, alipomtoa mwanawe Isaki madhabahuni? 22 Unaona jinsi ambavyo imani yake na matendo yake vilikuwa vinatenda kazi pamoja, nayo imani yake ikakamilishwa na kile alichotenda. 23 Kwa njia hiyo yakatimizwa yale Maandiko yasemayo, “Abrahamu alimwamini Mungu na ikahesabiwa kwake kuwa haki,” naye akaitwa rafiki wa Mungu. 24 Mnaona ya kwamba mtu huhesabiwa haki kwa yale anayotenda wala si kwa imani peke yake.

    25 Vivyo hivyo, hata Rahabu, yule kahaba, hakuhesabiwa haki kwa yale aliyotenda alipowapokea wale wapelelezi na kuwaambia waende njia nyingine? 26 Kama vile ambavyo mwili pasipo roho umekufa, kadhalika nayo imani pasipo matendo imekufa.

  76. 18 Mavuno ya haki hupandwa katika amani na wale wafanyao amani.

  77. 7 Yeye haondoi macho yake kwa wenye haki;

    huwaketisha penye viti vya enzi pamoja na wafalme

    na kuwatukuza milele.

  78. 137 Ee Bwana, wewe ni mwenye haki,

    sheria zako ni sahihi.

  79. 17 Bwana ni mwenye haki katika njia zake zote,

    na mwenye upendo kwa vyote alivyovifanya.

  80. 16 Ujira wa wenye haki huwaletea uzima,

    lakini mapato ya waovu huwaletea adhabu.

  81. 29 Njia ya Bwana ni kimbilio kwa wenye haki,

    lakini ni maangamizi ya wale watendao mabaya.

    30 Kamwe wenye haki hawataondolewa,

    bali waovu hawatasalia katika nchi.

    31 Kinywa cha mwenye haki hutoa hekima,

    bali ulimi wa upotovu utakatwa.

    32 Midomo ya wenye haki inajua kile kinachofaa,

    bali kinywa cha mwovu hujua kile kilichopotoka tu.

  82. 17 Hakuna silaha itakayofanyizwa dhidi yako

    itakayofanikiwa,

    nawe utauthibitisha kuwa mwongo

    kila ulimi utakaokushtaki.

    Huu ndio urithi wa watumishi wa Bwana

    na hii ndiyo haki yao itokayo kwangu,”

    asema Bwana.

  83. 1 Hili ndilo asemalo Bwana:

    “Dumisheni haki

    na mkatende lile lililo sawa,

    kwa maana wokovu wangu u karibu

    na haki yangu itafunuliwa upesi.

  84. 3 Wale wenye hekima watangʼaa kama mwanga wa mbingu, nao wale ambao huwaongoza wengi kutenda haki, watangʼaa kama nyota milele na milele.

  85. 13 Kisha Yesu akaja kutoka Galilaya mpaka Mto Yordani ili Yohana ambatize. 14 Lakini Yohana akajitahidi kumzuia, akimwambia, “Mimi ninahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu nikubatize?”

    15 Lakini Yesu akamjibu, “Kubali hivi sasa, kwa maana ndivyo itupasavyo kwa njia hii kuitimiza haki yote.” Hivyo Yohana akakubali.

    16 Naye Yesu alipokwisha kubatizwa, mara alipotoka ndani ya maji, ghafula mbingu zikafunguka, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua na kutulia juu yake. 17 Nayo sauti kutoka mbinguni ikasema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa, ambaye ninapendezwa sana naye.”

  86. 5 Wakati wa Herode mfalme wa Uyahudi, palikuwa na kuhani mmoja jina lake Zekaria, ambaye alikuwa wa ukoo wa kikuhani wa Abiya. Elizabeti mkewe alikuwa pia mzao wa Aroni. 6 Zekaria na Elizabeti mkewe wote walikuwa watu wanyofu mbele za Mungu, wakizishika amri zote za Bwana na maagizo yote bila lawama. 7 Lakini walikuwa hawana watoto, kwa sababu Elizabeti alikuwa tasa; nao wote wawili walikuwa wazee sana.

  87. 9 Yesu akatoa mfano huu kwa wale waliojiamini kuwa wao ni wenye haki na kuwadharau wengine: 10 “Watu wawili walikwenda Hekaluni kusali, mmoja wao alikuwa Farisayo na mwingine alikuwa mtoza ushuru. 11 Yule Farisayo, akasimama, akasali hivi na kuomba kwake mwenyewe: ‘Mungu, nakushukuru kwa sababu mimi si kama watu wengine ambao ni wanyangʼanyi, wadhalimu, na wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. 12 Mimi nafunga mara mbili kwa juma, na natoa sehemu ya kumi ya mapato yangu.’

    13 “Lakini yule mtoza ushuru akasimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua uso wake kutazama mbinguni, bali alijipigapiga kifuani na kusema: ‘Mungu, nihurumie, mimi mwenye dhambi.’

    14 “Nawaambia, huyu mtoza ushuru alirudi nyumbani akiwa amehesabiwa haki mbele za Mungu zaidi ya yule Farisayo. Kwa maana yeyote ajikwezaye atashushwa, na yeyote ajishushaye atakwezwa.”

  88. 25 “Baba Mwenye Haki, ingawa ulimwengu haukujui, mimi ninakujua, nao wanajua ya kuwa umenituma.

  89. 34 Ndipo Petro akafungua kinywa chake akasema, “Mungu hana upendeleo, 35 Lakini katika kila taifa, kila mtu amchaye na kutenda yaliyo haki hukubaliwa naye.

  90. 28 Nasi tunajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hutenda kazi pamoja na wote wampendao, katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. 29 Maana wale Mungu aliowajua tangu mwanzo, pia aliwachagua tangu mwanzo, wapate kufanana na mfano wa Mwanawe, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. 30 Nao wale Mungu aliotangulia kuwachagua, akawaita, wale aliowaita pia akawahesabia haki, nao wale aliowahesabia haki, pia akawatukuza.

  91. 34 Zindukeni mwe na akili kama iwapasavyo, wala msitende dhambi tena; kwa maana watu wengine hawamjui Mungu. Nasema mambo haya ili mwone aibu.

  92. 1 Watoto wangu wapendwa, nawaandikia haya ili msitende dhambi. Lakini kama mtu yeyote akitenda dhambi, tunaye Mwombezi kwa Baba: ndiye Yesu Kristo, Mwenye Haki.

  93. 11 Kisha nikaona mbingu imefunguka na hapo mbele yangu akiwepo farasi mweupe, ambaye yeye aliyempanda aliitwa Mwaminifu na Kweli. Yeye huhukumu kwa haki na kufanya vita.

  94. 6 Solomoni akajibu, “Umemfanyia mtumishi wako, baba yangu Daudi, fadhili nyingi, kwa kuwa alikuwa mwaminifu kwako na mwenye haki, tena mnyofu wa moyo. Nawe umemzidishia fadhili hii kuu kwani umempa mwana wa kuketi kwenye kiti chake cha ufalme, kama ilivyo leo.

  95. 15 Ee Bwana, Mungu wa Israeli, wewe ni mwenye haki! Leo hii tumeachwa kama mabaki. Tupo hapa mbele zako na hatia yetu, ingawa katika hali hii hakuna hata mmoja wetu anayeweza kusimama mbele zako.”

  96. 7 “Wewe ni Bwana Mungu uliyemchagua Abramu na kumtoa kutoka Uru ya Wakaldayo, nawe ukamwita Abrahamu. 8 Uliona kuwa moyo wake ni mwaminifu kwako, nawe ukafanya Agano naye kuwapa wazao wake nchi ya Wakanaani, Wahiti, Waamori, Waperizi, Wayebusi na Wagirgashi. Umetimiza ahadi yako kwa sababu wewe ni mwenye haki.

  97. 14 Niliivaa haki kama vazi langu;

    uadilifu ulikuwa joho langu na kilemba changu.

  98. 9 Ee Mungu mwenye haki,

    uchunguzaye mawazo na mioyo,

    komesha ghasia za waovu

    na ufanye wenye haki waishi kwa amani.

  99. 10 Ee Mungu, uniumbie moyo safi,

    uifanye upya roho ya uthabiti ndani yangu.

  100. 22 Mtwike Bwana fadhaa zako,

    naye atakutegemeza,

    hatamwacha kamwe mwenye haki wake aanguke.

  101. Zaburi ya Solomoni.

    1 Ee Mungu, mjalie mfalme aamue kwa haki yako,

    mwana wa mfalme kwa haki yako.

    2 Atawaamua watu wako kwa haki,

    watu wako walioonewa kwa haki.

    3 Milima italeta mafanikio kwa watu,

    vilima tunda la haki.

    4 Atawatetea walioonewa miongoni mwa watu

    na atawaokoa watoto wa wahitaji,

    ataponda mdhalimu.

  102. 11 Mbingu na zishangilie, nchi na ifurahi;

    bahari na ivume, na vyote vilivyomo ndani yake;

    12 mashamba na yashangilie,

    pamoja na vyote vilivyomo ndani yake.

    Kisha miti yote ya msituni itaimba kwa furaha;

    13 itaimba mbele za Bwana kwa maana anakuja,

    anakuja kuihukumu dunia.

    Ataihukumu dunia kwa haki,

    na mataifa katika kweli yake.

  103. 2 Mawingu na giza nene vinamzunguka,

    haki na hukumu ndio msingi wa kiti chake cha enzi.

    3 Moto hutangulia mbele zake

    na huteketeza adui zake pande zote.

  104. 4 Ndipo nikaliitia jina la Bwana:

    “Ee Bwana, niokoe!”

    5 Bwana ni mwenye neema na haki,

    Mungu wetu ni mwingi wa huruma.

    6 Bwana huwalinda wanyenyekevu,

    nilipokuwa katika shida kubwa, aliniokoa.

  105. 8 Bwana huwafumbua vipofu macho,

    Bwana huwainua waliolemewa na mizigo yao,

    Bwana huwapenda wenye haki.

  106. 34 Haki huinua taifa,

    bali dhambi ni aibu kwa watu wote.

  107. 21 Yeye afuatiaye haki na upendo

    hupata uzima, mafanikio na heshima.

    22 Mtu mwenye hekima huushambulia mji wa wenye nguvu,

    na kuangusha ngome wanazozitegemea.

  108. 10 Waambie wanyofu itakuwa heri kwao,

    kwa kuwa watafurahia tunda la matendo yao.

  109. 14 Ninyi mlimkataa huyo Mtakatifu na Mwenye Haki mkaomba mpewe yule muuaji. 15 Hivyo mkamuua aliye chanzo cha uzima, lakini Mungu akamfufua kutoka kwa wafu. Sisi tu mashahidi wa mambo haya. 16 Kwa imani katika jina la Yesu, huyu mtu mnayemwona na kumfahamu ametiwa nguvu. Ni kwa jina la Yesu na imani itokayo kwake ambayo imemponya kabisa huyu mtu, kama ninyi wote mnavyoona.

  110. 11 Kwa maana neema ya Mungu ambayo inawaokoa wanadamu wote imefunuliwa. 12 Nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia, ili tupate kuishi maisha ya kiasi, ya haki na ya utaua katika ulimwengu huu wa sasa, 13 huku tukilitazamia tumaini lenye baraka na ufunuo wa utukufu wa Mungu wetu Mkuu, aliye Mwokozi wetu Yesu Kristo. 14 Ndiye alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, ili atukomboe kutoka uovu wote na kujisafishia watu kuwa mali yake Mwenyewe, yaani, wale walio na juhudi katika kutenda mema.

  111. 5 alituokoa, si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyotenda, bali kwa sababu ya rehema zake. Alituokoa kwa kutuosha kwa kuzaliwa mara ya pili na kwa kufanywa wapya kwa njia ya Roho Mtakatifu, 6 ambaye Mungu alitumiminia kwa wingi kwa njia ya Yesu Kristo Mwokozi wetu, 7 ili kwamba, tukiisha kuhesabiwa haki kwa neema yake, tupate kuwa warithi tukiwa na tumaini la uzima wa milele.

  112. 4 Kwa imani Abeli alimtolea Mungu dhabihu bora zaidi kuliko Kaini. Kwa imani alishuhudiwa kuwa mwenye haki, Mungu mwenyewe akazishuhudia sadaka zake. Kwa imani bado ananena ingawa amekufa.

  113. 17 Ndipo Bwana akasema, “Je, nimfiche Abrahamu jambo ninalokusudia kufanya? 18 Hakika Abrahamu atakuwa taifa kubwa na lenye nguvu, kupitia kwake mataifa yote ya dunia yatabarikiwa. 19 Kwa maana nimemchagua yeye, ili awaongoze watoto wake na jamaa yake kufuata njia ya Bwana, kwa kuwa waadilifu na kutenda haki, ili Bwana atimize ahadi yake kwa Abrahamu.”

  114. 31 Watatangaza haki yake kwa watu

    ambao hawajazaliwa bado,

    kwa maana yeye ametenda hili.

  115. 10 Sikuficha haki yako moyoni mwangu;

    ninasema juu ya uaminifu wako na wokovu wako.

    Sikuficha upendo wako na kweli yako

    mbele ya kusanyiko kubwa.

  116. 10 Ee Mungu, kama jina lako lilivyo,

    sifa zako zinafika hadi miisho ya dunia,

    mkono wako wa kuume umejazwa na haki.

  117. 14 Ee Mungu, Mungu uniokoaye,

    niokoe na hatia ya kumwaga damu,

    nao ulimi wangu utaimba juu ya haki yako.

  118. 3 Ndugu, imetubidi kumshukuru Mungu kwa ajili yenu siku zote, kama ulivyo wajibu wetu, kwa sababu imani yenu inakua zaidi na zaidi na upendo wa kila mmoja wenu alio nao kwa mwenzake unazidi kuongezeka. 4 Ndiyo sababu miongoni mwa makanisa ya Mungu, tunajivuna kuhusu saburi yenu na imani mliyo nayo katika mateso yote na dhiki mnazostahimili.

    5 Haya yote ni uthibitisho kwamba hukumu ya Mungu ni ya haki, na kwa sababu hiyo ninyi mtahesabiwa kwamba mnastahili kuwa wa Ufalme wa Mungu, mnaoteswa kwa ajili wake. 6 Mungu ni mwenye haki: yeye atawalipa mateso wale wawatesao ninyi 7 na kuwapa ninyi mnaoteseka raha pamoja na sisi, wakati Bwana Yesu atakapodhihirishwa kutoka mbinguni katika mwali wa moto pamoja na malaika wake wenye nguvu. 8 Atawaadhibu wale wasiomjua Mungu na ambao hawakuitii Injili ya Bwana wetu Yesu. 9 Wataadhibiwa kwa uangamivu wa milele na kutengwa na uso wa Bwana na utukufu wa uweza wake, 10 siku hiyo atakapokuja kutukuzwa katika watakatifu wake na kustaajabiwa miongoni mwa wote walioamini. Ninyi pia mtakuwa miongoni mwa hawa kwa sababu mliamini ushuhuda wetu kwenu.

    11 Kwa sababu hii, tunawaombea ninyi bila kukoma, ili Mungu apate kuwahesabu kuwa mnastahili wito wake na kwamba kwa uwezo wake apate kutimiza kila kusudi lenu jema na kila tendo linaloongozwa na imani yenu. 12 Tunaomba hivi ili Jina la Bwana wetu Yesu lipate kutukuzwa ndani yenu, nanyi ndani yake, kulingana na neema ya Mungu wetu na Bwana Yesu Kristo.