77 Bible Verses About Sin

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Sin
  1. 18 Ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni dhidi ya uasi wote na uovu wa wanadamu ambao huipinga kweli kwa uovu wao, 19 kwa maana yote yanayoweza kujulikana kumhusu Mungu ni dhahiri kwao, kwa sababu Mungu mwenyewe ameyadhihirisha kwao. 20 Kwa maana tangu kuumbwa kwa ulimwengu, asili ya Mungu asiyeonekana kwa macho, yaani, uweza wake wa milele na asili yake ya Uungu, imeonekana waziwazi, ikitambuliwa kutokana na yale aliyoyafanya ili wanadamu wasiwe na udhuru.

    21 Kwa maana ingawa walimjua Mungu, hawakumtukuza yeye kama ndiye Mungu wala hawakumshukuru, bali fikira zao zimekuwa batili na mioyo yao ya ujinga ikatiwa giza. 22 Ingawa walijidai kuwa wenye hekima, wakawa wajinga 23 na kubadili utukufu wa Mungu aishiye milele kwa sanamu zilizofanywa zifanane na mwanadamu ambaye hufa, na mfano wa ndege, wanyama na viumbe vitambaavyo.

  2. 28 Nao kwa kuwa hawakuona umuhimu wa kudumisha ufahamu wa Mungu, yeye akawaachilia wafuate akili za upotovu, watende mambo yale yasiyostahili kutendwa. 29 Wakiwa wamejawa na udhalimu wa kila namna, uasherati, uovu, tamaa mbaya na hila. Wamejawa na husuda, uuaji, ugomvi, udanganyifu, hadaa na nia mbaya. Wao pia ni wasengenyaji, 30 wasingiziaji, wanaomchukia Mungu, wajeuri, wenye kiburi na majivuno, wenye hila, wasiotii wazazi wao, 31 wajinga, wasioamini, wasio na huruma na wakatili. 32 Ingawa wanafahamu sheria ya haki ya Mungu kwamba watu wanaofanya mambo kama hayo wanastahili mauti, si kwamba wanaendelea kutenda hayo tu, bali pia wanakubaliana na wale wanaoyatenda.

  3. 19 Basi tunajua ya kwamba chochote sheria inachosema, inawaambia wale walio chini ya sheria ili kila kinywa kinyamazishwe na ulimwengu wote uwajibike kwa Mungu. 20 Kwa hiyo hakuna binadamu hata mmoja atakayehesabiwa haki mbele za Mungu kwa matendo ya sheria, kwa maana sheria hutufanya tuitambue dhambi.

    21 Lakini sasa, haki itokayo kwa Mungu imedhihirishwa pasipo sheria, ambayo Sheria na Manabii wanaishuhudia. 22 Haki hii itokayo kwa Mungu hupatikana kwa Yesu Kristo kwa wote wamwaminio. Kwa maana hapo hakuna tofauti, 23 kwa kuwa wote wametenda dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu, 24 wanahesabiwa haki bure kwa neema yake kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu. 25 Yeye ambaye Mungu alimtoa awe dhabihu ya upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake. Alifanya hivi ili kuonyesha haki yake, kwa sababu kwa ustahimili wake aliziachilia zile dhambi zilizotangulia kufanywa. 26 Alifanya hivyo ili kuonyesha haki yake wakati huu, ili yeye awe mwenye haki na mwenye kumhesabia haki yule anayemwamini Yesu.

  4. 10 Kifo alichokufa, aliifia dhambi mara moja tu, lakini uzima alio nao anamwishia Mungu.

    11 Vivyo hivyo, jihesabuni wafu katika dhambi lakini mlio hai kwa Mungu katika Kristo Yesu. 12 Kwa hiyo, msiruhusu dhambi itawale ndani ya miili yenu, ipatikanayo na kufa, ili kuwafanya mzitii tamaa mbaya. 13 Wala msivitoe viungo vya miili yenu vitumike kama vyombo vya uovu vya kutenda dhambi, bali jitoeni kwa Mungu, kama watu waliotolewa kutoka mautini kuingia uzimani. Nanyi vitoeni viungo vya miili yenu kwake kama vyombo vya haki. 14 Kwa maana dhambi haitakuwa na mamlaka juu yenu, kwa sababu hampo chini ya sheria, bali chini ya neema.

    15 Ni nini basi? Je, tutende dhambi kwa kuwa hatuko chini ya sheria bali chini ya neema? La, hasha! 16 Je, hamjui kwamba mnapojitoa kwa mtu yeyote kama watumwa watiifu, ninyi ni watumwa wa yule mnayemtii, aidha watumwa wa dhambi, ambayo matokeo yake ni mauti, au watumwa wa utii ambao matokeo yake ni haki? 17 Lakini Mungu ashukuriwe kwa kuwa ninyi ambao kwanza mlikuwa watumwa wa dhambi, mmekuwa watii kutoka moyoni kwa mafundisho mliyopewa. 18 Nanyi, mkiisha kuwekwa huru mbali na dhambi, mmekuwa watumwa wa haki.

    19 Ninasema kwa namna ya kibinadamu kwa sababu ya udhaifu wenu wa hali ya asili. Kama vile mlivyokuwa mkivitoa viungo vya miili yenu kama watumwa wa mambo machafu na uovu uliokuwa ukiongezeka zaidi, hivyo sasa vitoeni viungo vyenu kama watumwa wa haki inayowaelekeza mpate kutakaswa. 20 Mlipokuwa watumwa wa dhambi, mlikuwa hamtawaliwi na haki. 21 Lakini mlipata faida gani kwa mambo hayo ambayo sasa mnayaonea aibu? Mwisho wa mambo hayo ni mauti. 22 Lakini sasa kwa kuwa mmewekwa huru mbali na dhambi na mmekuwa watumwa wa Mungu, faida mnayopata ni utakatifu, ambao mwisho wake ni uzima wa milele. 23 Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti, bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.

  5. 5 Huu ndio ujumbe tuliosikia kutoka kwake na kuwatangazia ninyi: kwamba Mungu ni nuru na ndani yake hamna giza lolote. 6 Kama tukisema kwamba twashirikiana naye huku tukienenda gizani, twasema uongo, wala hatutendi lililo kweli. 7 Lakini tukienenda nuruni, kama yeye alivyo nuruni, twashirikiana sisi kwa sisi na damu yake Yesu, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote.

    8 Kama tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe wala kweli haimo ndani yetu. 9 Kama tukiziungama dhambi zetu, yeye ni mwaminifu na wa haki, atatusamehe dhambi zetu na kutusafisha kutoka kwenye udhalimu wote. 10 Kama tukisema hatukutenda dhambi, twamfanya yeye kuwa mwongo na neno lake halimo ndani yetu.

  6. 26 Kama tukiendelea kutenda dhambi kwa makusudi baada ya kupokea ufahamu wa ile kweli, haibaki tena dhabihu kwa ajili ya dhambi. 27 Lakini kinachobaki ni kungoja kwa hofu hukumu ya moto uwakao, utakaowaangamiza adui za Mungu. 28 Yeyote aliyeikataa sheria ya Mose alikufa pasipo huruma kwa ushahidi wa watu wawili au watatu. 29 Je, mnadhani ni adhabu kali kiasi gani anayostahili kupewa mtu aliyemkanyaga Mwana wa Mungu chini ya nyayo zake, yeye aliyeifanya damu ya Agano iliyomtakasa kuwa kitu najisi na kumtendea maovu Roho wa neema? 30 Kwa kuwa tunamjua yeye aliyesema, “Ni juu yangu kulipiza kisasi; nitalipiza.” Tena asema, “Bwana atawahukumu watu wake.” 31 Ni jambo la kutisha kuanguka mikononi mwa Mungu aliye hai.

  7. 6 Kwa maana hata tulipokuwa dhaifu, wakati ulipowadia, Kristo alikufa kwa ajili yetu sisi wenye dhambi. 7 Hakika, ni vigumu mtu yeyote kufa kwa ajili ya mwenye haki, ingawa inawezekana mtu akathubutu kufa kwa ajili ya mtu mwema. 8 Lakini Mungu anaudhihirisha upendo wake kwetu kwamba: Tulipokuwa tungali wenye dhambi, Kristo alikufa kwa ajili yetu.

    9 Basi, kwa kuwa sasa tumehesabiwa haki kwa damu yake, si zaidi sana tutaokolewa kutoka ghadhabu ya Mungu kupitia kwake! 10 Kwa kuwa kama tulipokuwa adui wa Mungu tulipatanishwa naye kwa njia ya kifo cha Mwanawe, si zaidi sana tukiisha kupatanishwa, tutaokolewa kwa uzima wake. 11 Lakini zaidi ya hayo, pia tunafurahi katika Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kupitia kwake tumepata upatanisho.

  8. 2 Wapendwa, sasa tu wana wa Mungu, lakini bado haijadhihirika tutakavyokuwa, lakini twajua ya kwamba yeye atakapodhihirishwa, tutafanana naye, kwa maana tutamwona kama alivyo. 3 Kila mmoja mwenye matumaini haya ndani yake hujitakasa, kama vile yeye alivyo mtakatifu.

    4 Kila mtu atendaye dhambi afanya uasi, kwa kuwa dhambi ni uasi. 5 Lakini mwajua ya kuwa yeye alidhihirishwa ili aziondoe dhambi, wala ndani yake hamna dhambi. 6 Kila mtu akaaye ndani yake hatendi dhambi. Kila mtu atendaye dhambi hakumwona yeye wala hakumtambua.

    7 Watoto wapendwa, mtu yeyote asiwadanganye. Kila mtu atendaye haki ana haki, kama yeye alivyo na haki. 8 Yeye atendaye dhambi ni wa ibilisi, kwa sababu ibilisi amekuwa akitenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili aziangamize kazi za ibilisi. 9 Yeyote aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wa Mungu wakaa ndani yake, wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa na Mungu. 10 Kwa jinsi hii tunaweza kujua dhahiri watoto wa Mungu na pia watoto wa ibilisi. Yeyote asiyetenda haki hatokani na Mungu, wala yeye asiyempenda ndugu yake.

  9. 1 Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa porini ambao Bwana Mungu aliwafanya. Nyoka akamwambia mwanamke, “Ati kweli Mungu alisema, ‘Kamwe msile matunda ya mti wowote wa bustanini’?”

    2 Mwanamke akamjibu nyoka, “Tunaweza kula matunda ya miti iliyoko bustanini, 3 lakini Mungu alisema, ‘Kamwe msile tunda la mti ulio katikati ya bustani, wala kuugusa, la sivyo mtakufa.’ ”

    4 Lakini nyoka akamwambia mwanamke, “Hakika hamtakufa. 5 Kwa maana Mungu anajua ya kuwa wakati mtakapoyala, macho yenu yatafumbuliwa, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.”

    6 Mwanamke alipoona ya kuwa tunda la mti huo lilikuwa zuri kwa chakula na la kupendeza macho, tena linatamanika kwa kujipatia hekima, basi akachuma katika matunda yake, akala, pia akampa mumewe, aliyekuwa pamoja naye, naye akala. 7 Ndipo macho yao wote wawili yakafumbuliwa, wakajiona kwamba walikuwa uchi; hivyo wakashona majani ya mtini, wakajifunika.

    8 Ndipo yule mwanaume na mkewe, waliposikia sauti ya Bwana Mungu alipokuwa akitembea bustanini jioni, wakajificha kutoka mbele za Bwana Mungu katikati ya miti ya bustani. 9 Lakini Bwana Mungu akamwita Adamu, “Uko wapi?”

    10 Naye akajibu, “Nilikusikia katika bustani nikaogopa kwa sababu nilikuwa uchi, hivyo nikajificha.”

    11 Mungu akamuuliza, “Ni nani aliyekuambia ya kuwa ulikuwa uchi? Je, umekula matunda ya mti niliokuamuru usile?”

    12 Adamu akasema, “Huyu mwanamke uliyenipa awe pamoja nami alinipa sehemu ya tunda kutoka kwenye huo mti, nami nikala.”

    13 Ndipo Bwana Mungu akamuuliza mwanamke, “Ni nini hili ambalo umelifanya?” Mwanamke akajibu, “Nyoka alinidanganya, nami nikala.”

  10. 16 Basi kama ninatenda lile nisilotaka kutenda, ni kwamba ninakubali kuwa sheria ni njema. 17 Lakini, kwa kweli si mimi tena nitendaye lile nisilotaka bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu. 18 Kwa maana ninafahamu kwamba hakuna jema lolote likaalo ndani yangu, yaani, katika asili yangu ya dhambi. Kwa kuwa nina shauku ya kutenda lililo jema, lakini siwezi kulitenda. 19 Sitendi lile jema nitakalo kutenda, bali lile baya nisilolitaka, ndilo nitendalo. 20 Basi kama ninatenda lile nisilotaka kutenda, si mimi tena nifanyaye hivyo, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu.

    21 Hivyo naiona sheria ikitenda kazi. Ninapotaka kutenda jema, jambo baya liko papo hapo. 22 Kwa maana katika utu wangu wa ndani naifurahia sheria ya Mungu. 23 Lakini ninaona kuna sheria nyingine inayotenda kazi katika viungo vya mwili wangu inayopigana vita dhidi ya ile sheria ya akili yangu. Sheria hii inanifanya mateka wa ile sheria ya dhambi inayofanya kazi katika viungo vya mwili wangu.

    24 Ole wangu mimi maskini! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti?

    25 Ashukuriwe Mungu kwa njia ya Yesu Kristo Bwana wetu! Hivyo basi, mimi mwenyewe kwa akili zangu ni mtumwa wa sheria ya Mungu, lakini katika asili ya dhambi ni mtumwa wa sheria ya dhambi.

  11. 2 Unioshe na uovu wangu wote

    na unitakase dhambi yangu.

    3 Kwa maana ninajua makosa yangu,

    na dhambi yangu iko mbele yangu daima.

    4 Dhidi yako, wewe peke yako, nimetenda dhambi

    na kufanya yaliyo mabaya machoni pako,

    ili uthibitike kuwa wa kweli unenapo,

    na kuwa na haki utoapo hukumu.

    5 Hakika mimi nilizaliwa mwenye dhambi,

    mwenye dhambi tangu nilipotungwa mimba kwa mama yangu.

    6 Hakika wewe wapendezwa na kweli itokayo moyoni,

    ndani sana ya moyo wangu wanifundisha hekima.

    7 Nioshe kwa hisopo, nami nitakuwa safi,

    unisafishe, nami nitakuwa mweupe kuliko theluji.

    8 Unipe kusikia furaha na shangwe,

    mifupa uliyoiponda na ifurahi.

    9 Ufiche uso wako usizitazame dhambi zangu,

    na uufute uovu wangu wote.

    10 Ee Mungu, uniumbie moyo safi,

    uifanye upya roho ya uthabiti ndani yangu.

    11 Usinitupe kutoka mbele zako

    wala kuniondolea Roho wako Mtakatifu.

    12 Unirudishie tena furaha ya wokovu wako,

    unipe roho ya utii, ili initegemeze.

  12. 17 Kwa hiyo kama mtu akiwa ndani ya Kristo, amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita, tazama, yamekuwa mapya. 18 Haya yote yanatokana na Mungu, ambaye ametupatanisha sisi na nafsi yake kwa njia ya Yesu Kristo na kutupata sisi huduma ya upatanisho: 19 Kwamba Mungu alikuwa ndani ya Kristo akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake mwenyewe, akiwa hawahesabii watu dhambi zao. Naye ametukabidhi sisi ujumbe huu wa upatanisho. 20 Kwa hiyo sisi ni mabalozi wa Kristo, kana kwamba Mungu anawasihi kupitia kwa vinywa vyetu. Nasi twawaomba sana ninyi kwa niaba ya Kristo, mpatanishwe na Mungu. 21 Kwa maana Mungu alimfanya yeye asiyekuwa na dhambi kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kufanywa haki ya Mungu kwake yeye.

  13. 1 Kwa hiyo, sasa hakuna hukumu ya adhabu kwa wale walio ndani ya Kristo Yesu, wale ambao hawaenendi kwa kuufuata mwili bali kwa kufuata Roho. 2 Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima katika Kristo Yesu imeniweka huru mbali na sheria ya dhambi na mauti. 3 Kwa maana kile ambacho sheria haikuwa na uwezo wa kufanya, kwa vile ilivyokuwa dhaifu katika mwili, Mungu kwa kumtuma Mwanawe mwenyewe kwa mfano wa mwanadamu mwenye mwili ulio wa dhambi na kwa ajili ya dhambi, yeye aliihukumu dhambi katika mwili, 4 ili kwamba haki ipatikanayo kwa sheria itimizwe ndani yetu sisi, ambao hatuenendi kwa kuufuata mwili bali kwa kufuata Roho.

    5 Kwa maana wale wanaoishi kwa kuufuata mwili huziweka nia zao katika vitu vya mwili, lakini wale wanaoishi kwa kufuata Roho, huziweka nia zao katika mambo ya Roho. 6 Kwa maana kuwa na nia ya mwili ni mauti, bali kuwa na nia inayoongozwa na Roho ni uzima na amani. 7 Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui na Mungu, kwa maana haiitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii. 8 Wale wanaotawaliwa na mwili, hawawezi kumpendeza Mungu.

  14. 12 Heri mtu anayevumilia wakati wa majaribu, kwa sababu akiisha kushinda hilo jaribio atapewa taji la uzima Mungu alilowaahidia wale wampendao.

    13 Mtu anapojaribiwa asiseme, “Ninajaribiwa na Mungu.” Kwa maana Mungu hawezi kujaribiwa na maovu wala yeye hamjaribu mtu yeyote. 14 Lakini kila mtu hujaribiwa wakati anapovutwa na kudanganywa na tamaa zake mwenyewe zilizo mbaya. 15 Basi ile tamaa mbaya ikishachukua mimba, huzaa dhambi, nayo ile dhambi ikikomaa, huzaa mauti.

  15. 17 Kwa maana mwili hutamani yale yaliyo kinyume na Roho, naye Roho hutamani yale yaliyo kinyume na mwili. Roho na mwili hupingana na kwa sababu hiyo hamwezi kufanya mnayotaka. 18 Lakini kama mkiongozwa na Roho, hamko chini ya sheria.

    19 Basi matendo ya mwili ni dhahiri nayo ni haya: Uasherati, uchafu, ufisadi, 20 kuabudu sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, 21 husuda, ulevi, ulafi na mambo mengine yanayofanana na hayo. Nawaonya, kama nilivyokwisha kuwaonya kabla, kwamba watu watendao mambo kama hayo, hawataurithi Ufalme wa Mungu.

  16. 16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. 17 Kwa maana Mungu hakumtuma Mwanawe kuuhukumu ulimwengu, bali kupitia kwake ulimwengu upate kuokolewa. 18 Yeyote amwaminiye hahukumiwi, lakini asiyeamini amekwisha kuhukumiwa, kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu. 19 Hii ndiyo hukumu kwamba: Nuru imekuja ulimwenguni, nao watu wakapenda giza kuliko nuru kwa sababu matendo yao ni maovu. 20 Kwa kuwa kila atendaye maovu huchukia nuru, wala haji kwenye nuru ili matendo yake maovu yasifichuliwe.

  17. 16 Kama mtu akimwona ndugu yake akitenda dhambi isiyo ya mauti, inampasa aombe, naye Mungu atampa uzima mtu huyo. Ninamaanisha wale ambao dhambi yao si ya mauti. Iko dhambi ya mauti, sisemi kwamba utaomba kwa ajili ya hiyo. 17 Jambo lolote lisilo la haki ni dhambi, lakini iko dhambi isiyo ya mauti.

  18. 31 Kwa hiyo nawaambia, kila dhambi na kufuru watu watasamehewa, lakini mtu atakayemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa. 32 Mtu yeyote atakayesema neno dhidi ya Mwana wa Adamu atasamehewa, lakini yeyote anenaye neno dhidi ya Roho Mtakatifu hatasamehewa, iwe katika ulimwengu huu au katika ulimwengu ujao.

  19. 17 Basi mtu yeyote anayejua jema limpasalo kutenda, lakini asilitende, mtu huyo anatenda dhambi.

  20. 16 Kwa mwanamke akasema,

    “Nitakuzidishia sana utungu wakati wa kuzaa kwako;

    kwa utungu utazaa watoto.

    Tamaa yako itakuwa kwa mumeo

    naye atakutawala.”

    17 Kwa Adamu akasema, “Kwa sababu umemsikiliza mke wako na ukala kutoka kwenye mti niliokuamuru, ‘Msile tunda lake,’

    “Ardhi imelaaniwa kwa sababu yako,

    kwa kazi ngumu utakula chakula kitokacho humo

    siku zote za maisha yako.

    18 Itazaa miiba na mibaruti kwa ajili yako,

    nawe utakula mimea ya shambani.

    19 Kwa jasho la uso wako

    utakula chakula chako

    hadi utakaporudi ardhini,

    kwa kuwa ulitwaliwa kutoka humo,

    kwa kuwa wewe u mavumbi

    na mavumbini wewe utarudi.”

  21. 13 Yeye afichaye dhambi zake hatafanikiwa,

    bali yeyote aziungamaye na kuziacha hupata rehema.

  22. 24 Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, ili tufe kwa mambo ya dhambi, bali tupate kuishi katika haki. Kwa kupigwa kwake, ninyi mmeponywa.

  23. 21 “Mmesikia walivyoambiwa watu wa zamani kwamba, ‘Usiue. Yeyote atakayeua atapaswa hukumu.’ 22 Lakini mimi nawaambia kwamba, yeyote atakayemkasirikia ndugu yake, atapaswa hukumu. Tena, yeyote atakayemwambia ndugu yake, ‘Raka,’ atapaswa kujibu kwa Baraza la Wayahudi. Lakini yeyote atakayesema ‘Wewe mpumbavu!’ atapaswa hukumu ya moto wa jehanamu.

    23 “Kwa hiyo, kama unatoa sadaka yako madhabahuni, ukakumbuka kuwa ndugu yako ana kitu dhidi yako, 24 iache sadaka yako hapo mbele ya madhabahu. Enda kwanza ukapatane na ndugu yako; kisha urudi na ukatoe sadaka yako.

  24. 34 Yesu akajibu, “Amin, amin nawaambia, kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi. 35 Mtumwa hakai nyumbani anakotumika siku zote, lakini mwana hukaa nyumbani daima.

  25. 9 Je, hamjui kwamba wasio haki hawataurithi Ufalme wa Mungu? Msidanganyike: Waasherati, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wahanithi, wala walawiti, 10 wala wezi, wala wenye tamaa mbaya, wala walevi, wala wanaodhihaki, wala wanyangʼanyi hawataurithi Ufalme wa Mungu. 11 Baadhi yenu mlikuwa kama hao. Lakini mlioshwa, mlitakaswa, mlihesabiwa haki kwa jina la Bwana Yesu Kristo na katika Roho wa Mungu wetu.

  26. 1 Watoto wangu wapendwa, nawaandikia haya ili msitende dhambi. Lakini kama mtu yeyote akitenda dhambi, tunaye Mwombezi kwa Baba: ndiye Yesu Kristo, Mwenye Haki. 2 Yeye ndiye dhabihu ya upatanisho kwa ajili ya dhambi zetu, wala si kwa ajili ya dhambi zetu tu, bali pia kwa ajili ya dhambi za ulimwengu wote.

    3 Basi katika hili twajua ya kuwa tumemjua, tukizishika amri zake. 4 Mtu yeyote asemaye kuwa, “Ninamjua,” lakini hazishiki amri zake, ni mwongo, wala ndani ya mtu huyo hamna kweli. 5 Lakini mtu yeyote anayelitii neno lake, upendo wa Mungu umekamilika ndani yake kweli kweli. Katika hili twajua kuwa tumo ndani yake. 6 Yeyote anayesema anakaa ndani yake hana budi kuenenda kama Yesu alivyoenenda.

  27. 5 Bwana akaona jinsi uovu wa mwanadamu ulivyokuwa mkubwa duniani, na ya kuwa kila mwelekeo wa mawazo ya moyo wake wakati wote ulikuwa mbaya tu. 6 Bwana akasikitika kwamba alimuumba mwanadamu duniani, moyo wa Mungu ukajaa masikitiko. 7 Kwa hiyo Bwana akasema, “Nitamfutilia mbali mwanadamu niliyemuumba kutoka kwenye uso wa dunia, wanadamu na wanyama, pamoja na viumbe vitambaavyo na ndege wa angani. Kwa maana nasikitika kuwaumba.”

  28. 5 Kwa hiyo, ueni kabisa chochote kilicho ndani yenu cha asili ya kidunia: yaani uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya na ulafi, ambayo ndiyo ibada ya sanamu. 6 Kwa sababu ya mambo haya, ghadhabu ya Mungu inakuja. 7 Ninyi pia zamani mlienenda katika mambo haya mlipoishi maisha hayo. 8 Lakini sasa yawekeni mbali nanyi mambo kama haya yote: yaani hasira, ghadhabu, uovu, masingizio na lugha chafu kutoka midomoni mwenu. 9 Msiambiane uongo, kwa maana mmevua kabisa utu wenu wa kale pamoja na matendo yake, 10 nanyi mmevaa utu mpya, unaofanywa upya katika ufahamu sawasawa na mfano wa Muumba wake. 11 Hapa hakuna Myunani wala Myahudi, aliyetahiriwa wala asiyetahiriwa, asiyestaarabika wala aliyestaarabika, mtumwa wala mtu huru, bali Kristo ni yote, na ndani ya wote.

  29. 27 Kama vile mwanadamu alivyowekewa kufa mara moja tu na baada ya kufa akabili hukumu, 28 vivyo hivyo Kristo alitolewa mara moja tu kuwa dhabihu ili azichukue dhambi za watu wengi. Naye atakuja mara ya pili, sio kuchukua dhambi, bali kuwaletea wokovu wale wanaomngoja kwa shauku.

  30. 1 Ni kitu gani kinachosababisha mapigano na ugomvi miongoni mwenu? Je, haya hayatokani na tamaa zenu zinazoshindana ndani yenu? 2 Mnatamani lakini hampati, kwa hiyo mwaua. Mwatamani kupata lakini hampati vile mnavyotaka, kwa hiyo mnajitia katika magomvi na mapigano. Mmepungukiwa kwa sababu hammwombi Mungu. 3 Mnapoomba hampati kwa sababu mnaomba kwa nia mbaya, ili mpate kuvitumia hivyo mtakavyopata kwa tamaa zenu.

    4 Ninyi wanaume na wanawake wazinzi, hamjui ya kwamba urafiki na dunia ni uadui na Mungu? Kwa hiyo mtu yeyote anayetaka kuwa rafiki wa dunia hufanyika adui wa Mungu. 5 Au mwadhani kwamba Andiko lasema bure kuwa huyo Roho ambaye Mungu amemweka ndani yetu hututamani kiasi cha kuona wivu? 6 Lakini yeye hutupatia neema zaidi. Hii ndiyo sababu Andiko husema:

    “Mungu huwapinga wenye kiburi,

    lakini huwapa wanyenyekevu neema.”

    7 Basi mtiini Mungu. Mpingeni ibilisi, naye atawakimbia. 8 Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu ninyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu ninyi wenye nia mbili.

  31. 2 Heri mtu yule ambaye Bwana

    hamhesabii dhambi,

    na ambaye rohoni mwake

    hamna udanganyifu.

    3 Niliponyamaza, mifupa yangu ilichakaa

    kwa kulia kwa maumivu makali mchana kutwa.

    4 Usiku na mchana

    mkono wako ulinilemea,

    nguvu zangu zilinyonywa

    kama vile katika joto la kiangazi.

    5 Kisha nilikujulisha dhambi yangu

    wala sikuficha uovu wangu.

    Nilisema, “Nitaungama

    makosa yangu kwa Bwana.”

    Ndipo uliponisamehe

    hatia ya dhambi yangu.

  32. 17 Je, hamwelewi kwamba chochote kiingiacho kinywani huenda tumboni, na hatimaye hutolewa nje kikiwa uchafu? 18 Lakini kitokacho kinywani hutoka moyoni, na hiki ndicho kimtiacho mtu unajisi. 19 Kwa maana ndani ya moyo hutoka mawazo mabaya, uuaji, uzinzi, uasherati, wizi, ushahidi wa uongo na masingizio. 20 Haya ndiyo yamtiayo mtu unajisi; lakini kula bila kunawa mikono hakumtii mtu unajisi.”

  33. 20 Akaendelea kusema, “Kile kimtokacho mtu ndicho kimtiacho unajisi. 21 Kwa maana kutoka ndani ya moyo wa mtu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wizi, uuaji, uzinzi, 22 tamaa mbaya, uovu, udanganyifu, ufisadi, wivu, matukano, kiburi na upumbavu. 23 Maovu haya yote hutoka ndani ya mtu, nayo ndiyo yamtiayo mtu unajisi.”

  34. 12 Kwa hiyo ndugu zangu, sisi tu wadeni, si wa mwili, ili tuishi kwa kuufuata mwili, 13 kwa maana mkiishi kwa kuufuata mwili, mtakufa, lakini kama mkiyaua matendo ya mwili kwa Roho, mtaishi. 14 Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio watoto wa Mungu. 15 Kwa maana hamkupokea roho ya utumwa iwaleteayo tena hofu, bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambaye kwa yeye twalia, “Abba, yaani, Baba,” 16 Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu ya kwamba sisi tu watoto wa Mungu. 17 Hivyo, ikiwa sisi ni watoto, basi tu warithi, warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo, naam, tukiteswa pamoja naye tupate pia kutukuzwa pamoja naye.

  35. 15 “Kama ndugu yako akikukosea, nenda ukamwonyeshe kosa lake, kati yenu ninyi wawili peke yenu. Kama akikusikiliza, utakuwa umempata tena ndugu yako. 16 Lakini kama hatakusikiliza, nenda na mtu mwingine mmoja au wawili ili kila neno lithibitishwe kwa ushahidi wa mashahidi wawili au watatu. 17 Kama akikataa kuwasikiliza hao, liambie kanisa. Naye kama akikataa hata kulisikiliza kanisa, basi awe kwenu kama mtu asiyeamini au mtoza ushuru.

    18 “Amin, nawaambia, lolote mtakalolifunga duniani litakuwa limefungwa mbinguni, na lolote mtakalolifungua duniani litakuwa limefunguliwa mbinguni.

    19 “Tena nawaambia, ikiwa wawili wenu watakubaliana duniani kuhusu jambo lolote watakaloomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni. 20 Kwa kuwa wanapokusanyika pamoja watu wawili au watatu kwa Jina langu, mimi niko papo hapo pamoja nao.”

    21 Ndipo Petro akamjia Yesu na kumuuliza, “Bwana, ndugu yangu anikosee mara ngapi nami nimsamehe? Je, hata mara saba?”

    22 Yesu akamjibu, “Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini.

  36. 1 Tuseme nini basi? Je, tuendelee kutenda dhambi ili neema ipate kuongezeka? 2 La hasha! Sisi tulioifia dhambi, tutawezaje kuendelea kuishi tena katika dhambi? 3 Au hamjui ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake? 4 Kwa hiyo tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti, ili kama vile Kristo alivyofufuliwa kutoka kwa wafu kwa utukufu wa Baba, vivyo hivyo sisi nasi pia tupate kuenenda katika upya wa uzima.

  37. 4 Lakini Abeli akaleta fungu nono kutoka baadhi ya wazaliwa wa kwanza wa mifugo yake. Bwana akamkubali Abeli pamoja na sadaka yake, 5 lakini Mungu hakumkubali Kaini pamoja na sadaka yake. Kwa hiyo Kaini akakasirika sana, uso wake ukawa na huzuni.

    6 Kisha Bwana akamwambia Kaini, “Kwa nini umekasirika? Kwa nini uso wako una huzuni? 7 Ukifanya lililo sawa, je, hutakubalika? Lakini usipofanya lililo sawa, dhambi inakuvizia mlangoni mwako, inakutamani wewe, lakini inakupasa uishinde.”

    8 Basi Kaini akamwambia ndugu yake Abeli, “Twende shambani.” Walipokuwa shambani, Kaini akamshambulia Abeli ndugu yake, akamuua.

    9 Kisha Bwana akamuuliza Kaini, “Ndugu yako Abeli yuko wapi?”

    Akamjibu, “Sijui, je, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?”

    10 Bwana akasema, “Umefanya nini? Sikiliza! Damu ya ndugu yako inanililia mimi kutoka ardhini. 11 Sasa umelaaniwa na umehamishwa kutoka ardhi, ambayo imefungua kinywa chake na kupokea damu ya ndugu yako kutoka mkononi mwako. 12 Utakapoilima ardhi, haitakupa tena mazao yake. Utakuwa mtu wa kutangatanga duniani asiye na utulivu.”

  38. 12 Ndugu zangu, angalieni, asiwepo miongoni mwenu mtu mwenye moyo mwovu usioamini, unaojitenga na Mungu aliye hai. 13 Lakini mtiane moyo mtu na mwenzake kila siku, maadamu iitwapo Leo, ili asiwepo hata mmoja wenu mwenye kufanywa mgumu kwa udanganyifu wa dhambi. 14 Kwa kuwa tumekuwa washiriki wa Kristo, kama tukishikamana tu kwa uthabiti na tumaini letu la kwanza hadi mwisho.

  39. 1 Kwa sababu hii, kwa kuwa tumezungukwa na wingu kubwa namna hii la mashahidi, basi na tuweke kando kila kitu kinachotuzuia na ile dhambi inayotuzinga kwa urahisi, nasi tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa kwa ajili yetu. 2 Basi na tumtazame sana Yesu mwanzilishi na mkamilishaji wa imani yetu, yeye ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake alistahimili msalaba, bila kujali aibu ya huo msalaba, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu. 3 Mtafakarini sana yeye aliyestahimili upinzani mkuu namna hii kutoka kwa watu wenye dhambi, ili kwamba msije mkachoka na kukata tamaa.

  40. 12 Yeyote kati yenu anayependa uzima

    na kutamani kuziona siku nyingi njema,

    13 basi auzuie ulimi wake na mabaya,

    na midomo yake kutokana na kusema uongo.

    14 Aache uovu, atende mema,

    aitafute amani na kuifuatilia.

    15 Macho ya Bwana huwaelekea wenye haki,

    na masikio yake yako makini kusikiliza kilio chao.

    16 Uso wa Bwana uko kinyume na watendao maovu,

    ili kufuta kumbukumbu lao duniani.

  41. 1 Ndugu zangu, ikiwa mtu ameghafilika akatenda dhambi, basi ninyi mlio wa rohoni, mrejesheni upya mtu huyo kwa roho ya upole. Lakini jihadharini, ili ninyi wenyewe msije mkajaribiwa. 2 Chukulianeni mizigo ninyi kwa ninyi, nanyi kwa njia hii mtatimiza sheria ya Kristo. 3 Kama mtu yeyote akijiona kuwa yeye ni bora na kumbe sivyo, basi mtu huyo anajidanganya mwenyewe. 4 Lakini kila mtu na aipime kazi yake mwenyewe, ndipo aweze kujisifu, bila kujilinganisha na mtu mwingine. 5 Kwa maana, kila mtu atauchukua mzigo wake mwenyewe.

  42. 24 Wote walio wa Kristo Yesu wameusulubisha mwili na shauku zake pamoja na tamaa zake.

  43. 15 Msemo huu ni wa kweli na unaostahili kukubalika, usemao kwamba: Kristo Yesu alikuja ulimwenguni kuokoa wenye dhambi, ambao mimi ndiye niliye mbaya kuliko wote. 16 Lakini kwa sababu hiyo nilipata rehema, ili katika mimi, niliyekuwa mwenye dhambi kuliko wote, Kristo Yesu apate kuonyesha uvumilivu wake usio na kikomo, ili niwe kielelezo kwa wale watakaomwamini na wapate uzima wa milele. 17 Basi Mfalme wa milele, asiye na mwisho, asiyeonekana, aliye Mungu pekee, apewe heshima na utukufu milele na milele. Amen.

  44. 10 Mwanangu, kama wenye dhambi wakikushawishi,

    usikubaliane nao.

    11 Kama wakisema, “Twende tufuatane;

    tukamvizie mtu na kumwaga damu,

    njoo tukavizie nafsi isiyo na hatia;

    12 tuwameze wakiwa hai kama kaburi,

    wakiwa wazima kama wale wanaotumbukia shimoni.

    13 Tutapata aina zote za vitu vya thamani

    na kujaza nyumba zetu kwa nyara.

    14 Njoo ushirikiane nasi,

    vitu vyote tutakavyopata tutagawana.”

    15 Mwanangu, usiandamane nao.

    Usiweke mguu wako katika njia zao,

  45. 18 “Njooni basi tuhojiane,”

    asema Bwana.

    “Ingawa dhambi zenu ni kama rangi nyekundu,

    zitakuwa nyeupe kama theluji;

    ingawa ni nyekundu sana kama damu,

    zitakuwa nyeupe kama sufu.

    19 Kama mkikubali na kutii,

    mtakula mema ya nchi,

    20 lakini kama mkikataa na kuasi,

    mtaangamizwa kwa upanga.”

    Kwa kuwa kinywa cha Bwana kimenena.

  46. 34 Haki huinua taifa,

    bali dhambi ni aibu kwa watu wote.

  47. 14 Kwa kuwa kama mkiwasamehe watu wengine wanapowakosea, Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi pia. 15 Lakini msipowasamehe watu wengine makosa yao, naye Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.

  48. 18 Ikimbieni zinaa. Dhambi zingine zote atendazo mtu ziko nje ya mwili wake, lakini yeye aziniye hutenda dhambi ndani ya mwili wake mwenyewe. 19 Je, hamjui ya kwamba miili yenu ni hekalu la Roho Mtakatifu akaaye ndani yenu, ambaye mmepewa na Mungu? Ninyi si mali yenu wenyewe, 20 kwa maana mmenunuliwa kwa gharama. Kwa hiyo mtukuzeni Mungu katika miili yenu.

  49. 5 Haya yote ni uthibitisho kwamba hukumu ya Mungu ni ya haki, na kwa sababu hiyo ninyi mtahesabiwa kwamba mnastahili kuwa wa Ufalme wa Mungu, mnaoteswa kwa ajili wake. 6 Mungu ni mwenye haki: yeye atawalipa mateso wale wawatesao ninyi 7 na kuwapa ninyi mnaoteseka raha pamoja na sisi, wakati Bwana Yesu atakapodhihirishwa kutoka mbinguni katika mwali wa moto pamoja na malaika wake wenye nguvu. 8 Atawaadhibu wale wasiomjua Mungu na ambao hawakuitii Injili ya Bwana wetu Yesu. 9 Wataadhibiwa kwa uangamivu wa milele na kutengwa na uso wa Bwana na utukufu wa uweza wake,

  50. 19 Ndugu zangu, yeyote miongoni mwenu akipotoka na kuicha kweli, naye akarejezwa na mtu mwingine, 20 hamna budi kujua kwamba yeyote amrejezaye mwenye dhambi kutoka upotovu wake, ataiokoa roho ya huyo mwenye dhambi kutoka mauti na kusitiri wingi wa dhambi.

  51. 6 Kumbuka, Ee Bwana, rehema zako kuu na upendo,

    kwa maana zimekuwepo tangu zamani.

    7 Usizikumbuke dhambi za ujana wangu

    wala njia zangu za uasi,

    sawasawa na upendo wako unikumbuke,

    kwa maana wewe ni mwema, Ee Bwana.

    8 Bwana ni mwema na mwenye adili,

    kwa hiyo huwafundisha wenye dhambi njia zake.

    9 Huwaongoza wanyenyekevu katika haki,

    naye huwafundisha njia yake.

    10 Njia zote za Bwana ni za upendo na uaminifu

    kwa wale wanaoshika shuhuda za agano lake.

  52. 16 Kuna vitu sita anavyovichukia Bwana,

    naam, viko saba vilivyo chukizo kwake:

    17 macho ya kiburi,

    ulimi udanganyao,

    mikono imwagayo damu isiyo na hatia,

    18 moyo uwazao mipango miovu,

    miguu iliyo myepesi kukimbilia uovu,

    19 shahidi wa uongo ambaye humwaga uongo,

    na mtu ambaye huchochea fitina kati ya ndugu.

  53. 13 Kumcha Bwana ni kuchukia uovu;

    ninachukia kiburi na majivuno,

    tabia mbaya na mazungumzo potovu.

  54. 28 Amin, nawaambia, dhambi zote na makufuru yote ya wanadamu watasamehewa. 29 Lakini yeyote anayemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa kamwe, atakuwa na hatia ya dhambi ya milele.”

    30 Yesu alisema hivi kwa sababu walikuwa wanasema, “Ana pepo mchafu.”

  55. 10 Yesu akainuka na kumwambia, “Wako wapi wale waliokuwa wanakuhukumu kuwa mwenye hatia?”

    11 Yule mwanamke akajibu, “Hakuna hata mmoja Bwana.”

    Yesu akamwambia, “Hata mimi sikuhukumu. Nenda zako, kuanzia sasa usitende dhambi tena.”]

  56. 44 Ninyi ni watoto wa baba yenu ibilisi, nanyi mnataka kutimiza matakwa ya baba yenu. Yeye alikuwa muuaji tangu mwanzo, wala hakushikana na kweli maana hamna kweli ndani yake. Asemapo uongo husema yaliyo yake mwenyewe kwa maana yeye ni mwongo na baba wa huo uongo.

  57. 8 Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani, wala si kwa matendo yenu mema. Hii ni zawadi kutoka kwa Mungu, 9 si kwa matendo, ili mtu yeyote asije akajisifu. 10 Kwa maana sisi ni kazi ya mikono ya Mungu, tulioumbwa katika Kristo Yesu, ili tupate kutenda matendo mema, ambayo Mungu alitangulia kuyaandaa tupate kuishi katika hayo.

  58. 16 Kwa hiyo ungamianeni dhambi zenu ninyi kwa ninyi na kuombeana ili mpate kuponywa. Maombi ya mwenye haki yana nguvu tena yanafaa sana.

  59. 13 Ndipo Daudi akamjibu Nathani, “Nimefanya dhambi dhidi ya Bwana.”

    Nathani akamjibu, “Bwana amekuondolea dhambi yako. Hutakufa. 14 Lakini kwa sababu kwa kufanya hili umefanya adui za Bwana kuonyesha dharau kabisa, mwana atakayezaliwa kwako atakufa.”

  60. 2 Enyi watu, mtabadilisha utukufu wangu

    kuwa aibu mpaka lini?

    Mtapenda udanganyifu

    na kufuata miungu ya uongo mpaka lini?

    3 Fahamuni hakika kwamba Bwana amewatenga

    wale wamchao kwa ajili yake;

    Bwana atanisikia nimwitapo.

    4 Katika hasira yako, usitende dhambi.

    Mkiwa vitandani mwenu, mtulie kimya

    mkiichunguza mioyo yenu.

    5 Toeni dhabihu zilizo haki;

    mtegemeeni Bwana.

    6 Wengi wanauliza, “Ni nani awezaye

    kutuonyesha jema lolote?”

    Ee Bwana, tuangazie nuru ya uso wako.

  61. 23 Ee Mungu, nichunguze, uujue moyo wangu,

    nijaribu na ujue mawazo yangu.

    24 Uone kama kuna njia iletayo machukizo ndani yangu,

    uniongoze katika njia ya milele.

  62. 1 Basi watoza ushuru na wenye dhambi wote walikuwa wanakusanyika ili wapate kumsikiliza Yesu. 2 Lakini Mafarisayo na walimu wa sheria wakanungʼunika wakisema, “Huyu mtu anawakaribisha wenye dhambi na kula nao.”

    3 Ndipo Yesu akawaambia mfano huu: 4 “Ikiwa mmoja wenu ana kondoo mia moja, naye akapoteza mmoja wao, je, hawaachi wale tisini na tisa nyikani na kwenda kumtafuta huyo aliyepotea mpaka ampate? 5 Naye akishampata, humbeba mabegani mwake kwa furaha 6 na kwenda nyumbani. Kisha huwaita rafiki zake na majirani, na kuwaambia, ‘Furahini pamoja nami; nimempata kondoo wangu aliyepotea.’ 7 Nawaambieni, vivyo hivyo kutakuwa na furaha zaidi mbinguni kwa sababu ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa wenye haki tisini na tisa ambao hawana haja ya kutubu.”

  63. 14 Baadaye Yesu akamkuta yule mtu aliyemponya ndani ya Hekalu na kumwambia, “Tazama umeponywa, usitende dhambi tena. La sivyo, lisije likakupata jambo baya zaidi.”

  64. 11 Msishiriki matendo ya giza yasiyofaa, bali yafichueni. 12 Kwa maana ni aibu hata kutaja mambo yale ambayo wasiotii wanayafanya sirini.

  65. 10 Kwa maana mtu yeyote anayeishika sheria yote lakini akajikwaa katika kipengele kimoja tu, ana hatia ya kuivunja sheria yote. 11 Kwa sababu yeye aliyesema, “Usizini,” alisema pia, “Usiue.” Basi kama huzini lakini unaua, umekuwa mvunjaji wa sheria.

  66. 11 Wapenzi, ninawasihi, mkiwa kama wageni na wapitaji hapa ulimwenguni, epukeni tamaa mbaya za mwili ambazo hupigana vita na roho zenu. 12 Kuweni na mwenendo mzuri mbele ya watu wasiomjua Mungu, ili kama wanawasingizia kuwa watenda mabaya, wayaone matendo yenu mema nao wamtukuze Mungu siku atakapokuja kwetu.

  67. 20 Mose akawaambia watu, “Msiogope! Mungu amekuja kuwajaribu, ili kwamba hofu ya Mungu iwakalie, msitende dhambi.”

  68. KITABU CHA KWANZA

    1 Heri mtu yule ambaye

    haendi katika shauri la watu waovu,

    wala hasimami katika njia ya wenye dhambi,

    au kuketi katika baraza la wenye mizaha.

    2 Bali huifurahia sheria ya Bwana,

    naye huitafakari hiyo sheria usiku na mchana.

  69. 6 Kwa upendo na uaminifu uovu huondolewa;

    kwa kumcha Bwana mtu hujiepusha na ubaya.

  70. 5 Ndipo nikalia, “Ole wangu! Nimeangamia! Kwa kuwa mimi ni mtu mwenye midomo michafu, nami ninaishi katikati ya watu wenye midomo michafu, nayo macho yangu yamemwona Mfalme, Bwana Mwenye Nguvu Zote.”

    6 Ndipo mmoja wa wale maserafi akaruka kunijia akiwa na kaa la moto linalowaka mkononi mwake, ambalo alikuwa amelichukua kwa koleo kutoka madhabahuni. 7 Akanigusa nalo kinywa changu na kusema, “Tazama, hili limegusa midomo yako, uovu wako umeondolewa, nayo dhambi yako imesamehewa.”

  71. 4 Kwa kuwa kila roho ni mali yangu, kama vile ilivyo roho ya baba, vivyo hivyo roho ya mtoto ni mali yangu. Roho itendayo dhambi ndiyo itakayokufa.

  72. 19 Tubuni basi mkamgeukie Mungu, dhambi zenu zifutwe, ili zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwepo kwake Bwana, 20 naye apate kumtuma Kristo, ambaye ameteuliwa kwa ajili yenu, yaani Yesu.

  73. 21 Kwa maana kama vile mauti ilivyokuja kwa njia ya mtu mmoja, vivyo hivyo, ufufuo wa wafu umekuja kwa njia ya mtu mmoja. 22 Kwa maana kama vile katika Adamu watu wote wanakufa, vivyo hivyo katika Kristo wote watafanywa hai.

  74. 17 Hivyo nawaambia hivi, nami nasisitiza katika Bwana kwamba, msiishi tena kama watu wa Mataifa waishivyo, katika ubatili wa mawazo yao. 18 Watu hao akili zao zimetiwa giza na wametengwa mbali na uzima wa Mungu kwa sababu ya ujinga wao kutokana na ugumu wa mioyo yao. 19 Wakiisha kufa ganzi, wamejitia katika mambo ya ufisadi na kupendelea kila aina ya uchafu, wakiendelea kutamani zaidi.

    20 Lakini ninyi, hivyo sivyo mlivyojifunza Kristo. 21 Kama hivyo ndivyo ilivyo, ninyi mmemsikia, tena mmefundishwa naye, vile kweli ilivyo katika Yesu. 22 Mlifundishwa kuuvua mwenendo wenu wa zamani, utu wenu wa kale, ulioharibiwa na tamaa zake za udanganyifu, 23 ili mfanywe upya roho na nia zenu, 24 mkajivike utu mpya, ulioumbwa sawasawa na mfano wa Mungu katika haki yote na utakatifu.

  75. 24 Dhambi za watu wengine ni dhahiri nazo zinawatangulia kwenda hukumuni; na dhambi za watu wengine zinawafuata nyuma yao.

  76. 1 Kwa hiyo, kwa kuwa Kristo aliteswa katika mwili wake, ninyi nanyi jivikeni nia iyo hiyo kwa maana mtu aliyekwisha kuteswa katika mwili ameachana na dhambi. 2 Kwa hivyo, haishi maisha yake yaliyobaki ya kuishi hapa duniani kwa tamaa mbaya za wanadamu, bali anaishi kwa mapenzi ya Mungu. 3 Maana wakati uliopita mmekwisha kutumia muda wa kutosha katika maisha yenu mkifanya yale ambayo wapagani hupenda kutenda: wakiishi katika uasherati, tamaa mbaya, ulevi, karamu za ulafi, vileo, ngoma mbaya, na ibada chukizo za sanamu.

  77. 13 Nawaandikia ninyi, akina baba,

    kwa sababu mmemjua

    yeye aliye tangu mwanzo.

    Nawaandikia ninyi vijana

    kwa sababu mmemshinda yule mwovu.

    Nawaandikia ninyi watoto wadogo,

    kwa sababu mmemjua Baba.

    14 Nawaandikia ninyi akina baba,

    kwa sababu mmemjua

    yeye aliye tangu mwanzo.

    Nawaandikia ninyi vijana,

    kwa sababu mna nguvu,

    na neno la Mungu linakaa ndani yenu,

    nanyi mmemshinda yule mwovu.

    15 Msiupende ulimwengu wala mambo yaliyo ulimwenguni. Kama mtu yeyote akiupenda ulimwengu, upendo wa Baba haumo ndani yake. 16 Kwa maana kila kitu kilichomo ulimwenguni, yaani tamaa ya mwili, tamaa ya macho na kiburi cha uzima, havitokani na Baba bali hutokana na ulimwengu.