86 Bible Verses About Boasting

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Boasting
  1. 26 Ndugu zangu, kumbukeni mlivyokuwa mlipoitwa. Kwa kipimo cha kibinadamu, si wengi wenu mliokuwa na hekima. Si wengi mliokuwa na ushawishi, si wengi mliozaliwa katika jamaa zenye vyeo. 27 Lakini Mungu alivichagua vitu vipumbavu vya ulimwengu ili awaaibishe wenye hekima, Mungu alivichagua vitu dhaifu vya ulimwengu ili awaaibishe wenye nguvu. 28 Alivichagua vitu vya chini na vinavyodharauliwa vya dunia hii, vitu ambavyo haviko, ili avibatilishe vile vilivyoko, 29 ili mtu yeyote asijisifu mbele zake. 30 Bali kwa yeye ninyi mmepata kuwa katika Kristo Yesu, aliyefanyika kwetu hekima itokayo kwa Mungu, yaani haki, na utakatifu na ukombozi. 31 Hivyo, kama ilivyoandikwa: “Yeye ajisifuye na ajisifu katika Bwana.”

  2. 23 Hili ndilo asemalo Bwana:

    “Mwenye hekima asijisifu katika hekima yake,

    au mwenye nguvu ajisifu katika nguvu zake,

    wala tajiri ajisifu katika utajiri wake,

    24 lakini yeye ajisifuye, na ajisifu kwa sababu hili:

    kwamba ananifahamu na kunijua mimi,

    kwamba mimi ndimi Bwana, nitendaye wema,

    hukumu na haki duniani,

    kwa kuwa napendezwa na haya,”

    asema Bwana.

    25 “Siku zinakuja, nitakapowaadhibu wale wote ambao wametahiriwa kimwili tu, asema Bwana, 26 yaani Misri, Yuda, Edomu, Amoni, Moabu na wote wanaoishi jangwani sehemu za mbali. Kwa maana mataifa haya yote hayakutahiriwa mioyo yao, nayo nyumba yote ya Israeli haikutahiriwa.”

  3. 13 Basi sikilizeni ninyi msemao, “Leo au kesho tutakwenda katika mji huu ama ule tukae humo mwaka mmoja, tufanye biashara na kupata faida.” 14 Lakini hamjui hata litakalotukia kesho. Maisha yenu ni nini? Ninyi ni ukungu ambao huonekana kwa kitambo kidogo kisha hutoweka. 15 Badala yake, inawapasa kusema, “Kama Bwana akipenda, tutaishi na kufanya hili ama lile.” 16 Kama ilivyo sasa, mnajisifu na kujigamba. Kujisifu kwa namna hiyo ni uovu. 17 Basi mtu yeyote anayejua jema limpasalo kutenda, lakini asilitende, mtu huyo anatenda dhambi.

  4. 8 Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani, wala si kwa matendo yenu mema. Hii ni zawadi kutoka kwa Mungu, 9 si kwa matendo, ili mtu yeyote asije akajisifu. 10 Kwa maana sisi ni kazi ya mikono ya Mungu, tulioumbwa katika Kristo Yesu, ili tupate kutenda matendo mema, ambayo Mungu alitangulia kuyaandaa tupate kuishi katika hayo.

  5. 13 Hata wale waliotahiriwa wenyewe hawaitii sheria, lakini wanataka ninyi mtahiriwe ili wapate kujivuna kwa habari ya miili yenu. 14 Mungu apishie mbali nisije nikajivunia kitu chochote isipokuwa msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa yeye ulimwengu umesulubiwa kwangu, nami nimesulubiwa kwa ulimwengu. 15 Kwa maana katika Kristo Yesu, kutahiriwa au kutokutahiriwa si kitu, bali kule kuwa kiumbe kipya ni kila kitu! 16 Amani na rehema viwe na wote wanaofuata kanuni hii, na juu ya Israeli wa Mungu.

    17 Hatimaye, tangu sasa mtu yeyote asinitaabishe, kwa maana nachukua katika mwili wangu chapa zake Yesu.

    18 Ndugu zangu, neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe pamoja na roho zenu. Amen.

  6. 1 Usijisifu kwa ajili ya kesho,

    kwa kuwa hujui ni nini kitakachozaliwa kwa siku moja.

    2 Mwache mwingine akusifu,

    wala si kinywa chako mwenyewe;

    mtu mwingine afanye hivyo

    na si midomo yako mwenyewe.

  7. 12 Hatuthubutu kujiweka kwenye kundi moja au kujilinganisha na hao wanaojitukuza wenyewe kuwa wao ni wa maana sana. Wanapojipima na kujilinganisha wenyewe kwa wenyewe, wanaonyesha ya kuwa hawana busara. 13 Lakini sisi hatujajivuna kupita kiasi, bali majivuno yetu yatakuwa katika mipaka ile Mungu aliyotuwekea, mipaka ambayo inawafikia hata ninyi. 14 Kwa maana hatukuwa tunavuka mipaka katika kujisifu kwetu, kama vile ambavyo ingekuwa kama hatukuwa tumekuja kwenu. Kwa maana sisi ndio tuliokuwa wa kwanza kuja kwenu na Injili ya Kristo. 15 Wala hatuvuki mipaka kwa kujisifu kwetu kwa ajili ya kazi iliyofanywa na watu wengine. Tumaini letu ni kwamba imani yenu inavyozidi kukua, eneo letu la utendaji miongoni mwenu litapanuka zaidi, 16 ili tuweze kuhubiri Injili sehemu zilizo mbali na maeneo yenu. Kwa maana hatutaki kujisifu kwa ajili ya kazi ambayo imekwisha kufanyika tayari katika eneo la mtu mwingine. 17 Lakini, “Yeye ajisifuye na ajisifu katika Bwana.” 18 Kwa maana si yeye ajisifuye mwenyewe akubaliwaye, bali yeye ambaye Bwana humsifu.

  8. 6 Basi ndugu zangu, mambo haya nimeyafanya kwangu binafsi na Apolo kwa faida yenu, ili mweze kujifunza kutoka kwetu maana ya ule usemi usemao, “Msivuke zaidi ya yale yaliyoandikwa.” Hivyo hamtajivunia mtu fulani na kumdharau mwingine. 7 Kwa maana ni nani aliyewafanya kuwa tofauti na wengine? Ni nini mlicho nacho ambacho hamkupokea? Nanyi kama mlipokea, kwa nini mnajivuna kama vile hamkupokea?

    8 Sasa tayari mnayo yale yote mnayohitaji! Tayari mmekwisha kuwa matajiri! Mmekuwa wafalme, tena bila sisi! Laiti mngekuwa wafalme kweli ili na sisi tupate kuwa wafalme pamoja nanyi!

  9. 2 Katika kiburi chake, mwovu humtesa maskini,

    waovu na wanaswe katika hila wanazozitunga.

    3 Hujivunia tamaa za moyo wake;

    humbariki mlafi na kumtukana Bwana.

    4 Katika kiburi chake, mwovu hamtafuti Mungu,

    katika mawazo yake yote

    hakuna nafasi ya Mungu.

    5 Njia zake daima hufanikiwa;

    hujivuna na amri zako ziko mbali naye,

    huwacheka kwa dharau adui zake wote.

    6 Anajisemea mwenyewe, “Hakuna kitakachonitikisa,

    daima nitakuwa na furaha,

    kamwe sitakuwa na shida.”

  10. 12 Bwana atakapokuwa amemaliza kazi yake yote dhidi ya Mlima Sayuni na Yerusalemu, atasema, “Nitamwadhibu mfalme wa Ashuru kwa ajili ya majivuno ya ukaidi wa moyo wake na kutazama kwa macho yenye dharau.” 13 Kwa kuwa anasema:

    “ ‘Kwa nguvu za mkono wangu nimefanya hili,

    kwa hekima yangu, kwa sababu nina ufahamu.

    Niliondoa mipaka ya mataifa,

    niliteka nyara hazina zao,

    kama yeye aliye shujaa

    niliwatiisha wafalme wao.

    14 Kama mtu atiavyo mkono kwenye kiota,

    ndivyo mkono wangu ulivyochukua utajiri wa mataifa;

    kama watu wakusanyavyo mayai yaliyoachwa,

    ndivyo nilivyokusanya nchi zote;

    wala hakuna hata mmoja aliyepiga bawa

    au kufungua kinywa chake kutoa mlio.’ ”

    15 Je, shoka laweza kujigamba kuwa na nguvu zaidi

    kuliko yule anayelitumia,

    au msumeno kujisifu

    dhidi ya yule anayeutumia?

    Ni kana kwamba fimbo ingeweza kumwinua yeye aichukuaye,

    au mkongojo ungemwinua mwenye kuutumia!

    16 Kwa hiyo Bwana, Bwana Mwenye Nguvu Zote,

    atatuma ugonjwa wa kudhoofisha kwa askari wake walio hodari,

    katika fahari yake moto utawaka

    kama mwali wa moto.

  11. 1 Hata kama nitasema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa kengele inayolialia au toazi livumalo. 2 Ningekuwa na karama ya unabii na kujua siri zote na maarifa yote, hata kama nina imani kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, mimi si kitu. 3 Kama nikitoa mali yote niliyo nayo na kama nikijitolea mwili wangu uchomwe moto, kama sina upendo, hainifaidi kitu.

    4 Upendo huvumilia, upendo hufadhili, upendo hauoni wivu, hauna majivuno, hauna kiburi. 5 Haukosi kuwa na adabu, hautafuti mambo yake, haukasiriki upesi, hauweki kumbukumbu ya mabaya. 6 Upendo haufurahii mabaya bali hufurahi pamoja na kweli. 7 Upendo huvumilia yote, huamini yote, hutumaini yote, hustahimili yote.

  12. 26 Alifanya hivyo ili kuonyesha haki yake wakati huu, ili yeye awe mwenye haki na mwenye kumhesabia haki yule anayemwamini Yesu.

    27 Basi, kujivuna kuko wapi? Kumewekwa mbali. Kwa sheria gani? Je, ni kwa ile ya matendo? La hasha, bali kwa ile sheria ya imani. 28 Kwa maana twaona kwamba mwanadamu huhesabiwa haki kwa njia ya imani wala si kwa matendo ya sheria.

  13. 18 Msijidanganye. Kama mtu yeyote miongoni mwenu akidhani kuwa ana hekima kwa viwango vya dunia hii, inampasa awe mjinga ili apate kuwa na hekima. 19 Kwa maana hekima ya ulimwengu huu ni upuzi mbele za Mungu. Kama ilivyoandikwa: “Mungu huwanasa wenye hekima katika hila yao,” 20 tena, “Bwana anajua kwamba mawazo ya wenye hekima ni ubatili.” 21 Hivyo basi, mtu asijivune kuhusu wanadamu! Vitu vyote ni vyenu, 22 ikiwa ni Paulo au Apolo au Kefa au dunia au uzima au mauti, au wakati uliopo au wakati ujao, haya yote ni yenu 23 na ninyi ni wa Kristo, naye Kristo ni wa Mungu.

  14. 15 Msiupende ulimwengu wala mambo yaliyo ulimwenguni. Kama mtu yeyote akiupenda ulimwengu, upendo wa Baba haumo ndani yake. 16 Kwa maana kila kitu kilichomo ulimwenguni, yaani tamaa ya mwili, tamaa ya macho na kiburi cha uzima, havitokani na Baba bali hutokana na ulimwengu. 17 Nao ulimwengu unapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu milele.

  15. 9 Yesu akatoa mfano huu kwa wale waliojiamini kuwa wao ni wenye haki na kuwadharau wengine: 10 “Watu wawili walikwenda Hekaluni kusali, mmoja wao alikuwa Farisayo na mwingine alikuwa mtoza ushuru. 11 Yule Farisayo, akasimama, akasali hivi na kuomba kwake mwenyewe: ‘Mungu, nakushukuru kwa sababu mimi si kama watu wengine ambao ni wanyangʼanyi, wadhalimu, na wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. 12 Mimi nafunga mara mbili kwa juma, na natoa sehemu ya kumi ya mapato yangu.’

    13 “Lakini yule mtoza ushuru akasimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua uso wake kutazama mbinguni, bali alijipigapiga kifuani na kusema: ‘Mungu, nihurumie, mimi mwenye dhambi.’

    14 “Nawaambia, huyu mtoza ushuru alirudi nyumbani akiwa amehesabiwa haki mbele za Mungu zaidi ya yule Farisayo. Kwa maana yeyote ajikwezaye atashushwa, na yeyote ajishushaye atakwezwa.”

  16. 16 Nasema tena, mtu yeyote asidhani kwamba mimi ni mjinga. Lakini hata kama mkinidhania hivyo, basi nipokeeni kama mjinga ili nipate kujisifu kidogo. 17 Ninayosema kuhusiana na huku kujisifu kwa kujiamini, sisemi kama vile ambavyo Bwana angesema, bali kama mjinga. 18 Kwa kuwa wengi wanajisifu kama vile ulimwengu ufanyavyo, mimi nami nitajisifu. 19 Ninyi mwachukuliana na wajinga kwa sababu mna hekima sana! 20 Kweli ni kwamba mnachukuliana na mtu akiwatia utumwani au akiwatumia kwa ajili ya kupata faida au akiwanyangʼanya au akijitukuza mwenyewe au akiwadanganya. 21 Kwa aibu inanipasa niseme kwamba sisi tulikuwa dhaifu sana kwa jambo hilo!

    Lakini chochote ambacho mtu mwingine yeyote angethubutu kujisifia, nanena kama mjinga, nami nathubutu kujisifu juu ya hilo.

  17. 1 Lakini yakupasa ufahamu jambo hili, kwamba siku za mwisho kutakuwa na nyakati za hatari. 2 Kwa maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kumkufuru Mungu, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio watakatifu, 3 wasio na upendo, wasiopenda kupatanishwa, wasingiziaji, wasiozuia tamaa zao, wakatili, wasiopenda mema, 4 wasaliti, wakaidi, waliojaa majivuno, wapendao anasa zaidi kuliko kumpenda Mungu: 5 wakiwa na mfano wa utauwa kwa nje, lakini wakizikana nguvu za Mungu. Jiepushe na watu wa namna hiyo.

  18. 14 Kama vile mawingu na upepo pasipo mvua

    ndivyo alivyo mtu ajisifuye kwa zawadi ambazo hatoi.

  19. 28 Haya yote yalimpata Mfalme Nebukadneza. 29 Miezi kumi na miwili baadaye, mfalme alipokuwa akitembea juu ya paa la jumba la kifalme la Babeli, 30 alisema, “Je, huu si Babeli mji mkuu nilioujenga kama makao ya kifalme, kwa uwezo wangu mkubwa, na kwa ajili ya utukufu wa enzi yangu?”

    31 Maneno hayo yalikuwa bado katika midomo yake wakati sauti ilipokuja kutoka mbinguni, ikisema, “Mfalme Nebukadneza, hiki ndicho kilichoamriwa kwa ajili yako: Mamlaka yako ya ufalme yameondolewa kutoka kwako. 32 Utafukuzwa mbali na wanadamu, ukaishi pamoja na wanyama pori, na utakula manyasi kama ngʼombe. Nyakati saba zitapita juu yako, mpaka utakapokubali kuwa Yeye Aliye Juu Sana ndiye anayetawala juu ya falme za wanadamu, naye humtawaza yeyote amtakaye.”

    33 Papo hapo yale yaliyokuwa yamesemwa kuhusu Nebukadneza yakatimia. Alifukuzwa mbali na wanadamu, akala majani kama ngʼombe. Mwili wake uliloweshwa kwa umande wa mbinguni mpaka nywele zake zikakua kama manyoya ya tai na kucha zake kama makucha ya ndege.

  20. 17 Lakini kama baadhi ya matawi yalikatwa, nawe chipukizi la mzeituni mwitu ukapandikizwa mahali pao ili kushiriki unono pamoja na matawi mengine kutoka shina la mzeituni, 18 basi usijivune juu ya hayo matawi. Kama ukijivuna, kumbuka jambo hili: si wewe unayelishikilia shina, bali ni shina linalokushikilia wewe. 19 Basi utasema, “Matawi yale yalikatwa ili nipate kupandikizwa katika hilo shina.” 20 Hii ni kweli. Matawi hayo yalikatwa kwa sababu ya kutokuamini kwake, lakini wewe umesimama tu kwa sababu ya imani. Kwa hiyo usijivune, bali simama kwa kuogopa. 21 Kwa maana kama Mungu hakuyahurumia matawi ya asili, wala hatakuhurumia wewe.

  21. 2 Nafsi yangu itajisifu katika Bwana,

    walioonewa watasikia na wafurahi.

  22. 18 Kiburi hutangulia maangamizi,

    roho ya majivuno hutangulia maanguko.

  23. 1 “Angalieni msitende wema wenu mbele ya watu ili wawaone. Kwa maana mkifanya hivyo, hamna thawabu kutoka kwa Baba yenu aliye mbinguni.

    2 “Hivyo mnapowapa wahitaji, msipige panda mbele yenu kama wafanyavyo wanafiki katika masinagogi na mitaani, ili wasifiwe na watu. Amin nawaambia wao wamekwisha kupokea thawabu yao. 3 Lakini ninyi mtoapo sadaka, fanyeni kwa siri, hata mkono wako wa kushoto usijue mkono wako wa kuume unachofanya, 4 ili sadaka yako iwe ni siri. Ndipo Baba yako wa mbinguni, yeye aonaye sirini atakupa thawabu kwa wazi.

    5 “Nanyi msalipo, msiwe kama wanafiki, maana wao hupenda kusali wakiwa wamesimama katika masinagogi na kando ya barabara ili waonekane na watu. Amin nawaambia, wao wamekwisha kupata thawabu yao. 6 Lakini wewe unaposali, ingia chumbani mwako, funga mlango na umwombe Baba yako aliye sirini. Naye Baba yako aonaye sirini atakupa thawabu yako.

  24. 28 Nao kwa kuwa hawakuona umuhimu wa kudumisha ufahamu wa Mungu, yeye akawaachilia wafuate akili za upotovu, watende mambo yale yasiyostahili kutendwa. 29 Wakiwa wamejawa na udhalimu wa kila namna, uasherati, uovu, tamaa mbaya na hila. Wamejawa na husuda, uuaji, ugomvi, udanganyifu, hadaa na nia mbaya. Wao pia ni wasengenyaji, 30 wasingiziaji, wanaomchukia Mungu, wajeuri, wenye kiburi na majivuno, wenye hila, wasiotii wazazi wao, 31 wajinga, wasioamini, wasio na huruma na wakatili. 32 Ingawa wanafahamu sheria ya haki ya Mungu kwamba watu wanaofanya mambo kama hayo wanastahili mauti, si kwamba wanaendelea kutenda hayo tu, bali pia wanakubaliana na wale wanaoyatenda.

  25. 1 Kisha Hana akaomba na kusema:

    “Moyo wangu wamshangilia Bwana,

    katika Bwana pembe yangu imeinuliwa juu.

    Kinywa changu chajisifu juu ya adui zangu,

    kwa kuwa naufurahia wokovu wako.

    2 “Hakuna yeyote aliye mtakatifu kama Bwana,

    hakuna mwingine zaidi yako;

    hakuna Mwamba kama Mungu wetu.

    3 “Msiendelee kusema kwa kiburi hivyo

    wala msiache vinywa vyenu kunena kwa kiburi,

    kwa kuwa Bwana ndiye Mungu ajuaye,

    na kwa yeye matendo hupimwa.

  26. 13 Kumcha Bwana ni kuchukia uovu;

    ninachukia kiburi na majivuno,

    tabia mbaya na mazungumzo potovu.

  27. 17 Tazama, wewe ukiwa unaitwa Myahudi na kuitegemea sheria na kujisifia uhusiano wako na Mungu, 18 kama unajua mapenzi ya Mungu na kukubali lililo bora kwa sababu umefundishwa na hiyo sheria, 19 kama unatambua kuwa wewe ni kiongozi wa vipofu, na mwanga kwa wale walio gizani, 20 mkufunzi wa wajinga na mwalimu wa watoto wachanga, kwa kuwa una maarifa ya kweli katika hiyo sheria, 21 basi wewe, uwafundishaye wengine, mbona hujifunzi mwenyewe? Wewe uhubiriye kwamba mtu asiibe, wewe mwenyewe waiba? 22 Wewe usemaye mtu asizini, wewe mwenyewe wazini? Wewe uchukiaye miungu ya sanamu, wafanya jambo la kumchukiza katika mahekalu? 23 Wewe ujivuniaye sheria, wamwaibisha Mungu kwa kuvunja sheria? 24 Kama ilivyoandikwa, “Kwa ajili yenu ninyi, Jina la Mungu linatukanwa miongoni mwa watu wa Mataifa.”

  28. 1 Ndugu zangu, ikiwa mtu ameghafilika akatenda dhambi, basi ninyi mlio wa rohoni, mrejesheni upya mtu huyo kwa roho ya upole. Lakini jihadharini, ili ninyi wenyewe msije mkajaribiwa. 2 Chukulianeni mizigo ninyi kwa ninyi, nanyi kwa njia hii mtatimiza sheria ya Kristo. 3 Kama mtu yeyote akijiona kuwa yeye ni bora na kumbe sivyo, basi mtu huyo anajidanganya mwenyewe. 4 Lakini kila mtu na aipime kazi yake mwenyewe, ndipo aweze kujisifu, bila kujilinganisha na mtu mwingine. 5 Kwa maana, kila mtu atauchukua mzigo wake mwenyewe. 6 Basi, yeye afundishwaye katika neno na amshirikishe mwalimu wake mema yote.

    7 Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi. Kwa kuwa kile apandacho mtu ndicho atakachovuna. 8 Apandaye kwa mwili, katika mwili wake atavuna uharibifu, lakini yeye apandaye katika Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele. 9 Hivyo, tusichoke katika kutenda mema, kwa kuwa tutavuna kwa wakati wake tusipokata tamaa. 10 Kwa hiyo, kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema, hasa wale wa jamaa ya waaminio.

  29. 6 Siutumaini upinde wangu,

    upanga wangu hauniletei ushindi;

    7 bali wewe unatupa ushindi juu ya adui zetu,

    unawaaibisha watesi wetu.

    8 Katika Mungu wetu tunajivuna mchana kutwa,

    nasi tutalisifu jina lako milele.

  30. 3 Mtu yeyote na asiwadanganye kwa namna yoyote kwa maana siku ile haitakuja mpaka uasi utokee kwanza, na yule mtu wa kuasi adhihirishwe, yule ambaye amehukumiwa kuangamizwa kabisa. 4 Yeye atapingana na kujitukuza juu ya kila kitu kiitwacho Mungu au kinachoabudiwa, ili kujiweka juu katika Hekalu la Mungu, akijitangaza mwenyewe kuwa ndiye Mungu.

  31. 3 Hata lini, waovu, Ee Bwana,

    hata lini waovu watashangilia?

    4 Wanamimina maneno ya kiburi,

    watenda mabaya wote wamejaa majivuno.

  32. 2 Kiburi kinapokuja, ndipo huja aibu,

    bali unyenyekevu huja na hekima.

  33. 15 Nimewaandikia kwa ujasiri vipengele kadha wa kadha katika waraka huu kama kuwakumbusha tena kwa habari ya ile neema Mungu aliyonipa, 16 ili kuwa mhudumu wa Kristo Yesu kwa watu wa Mataifa nikiwa na huduma ya kikuhani ya kutangaza Injili ya Mungu, ili watu wa Mataifa wapate kuwa dhabihu inayokubaliwa na Mungu, iliyotakaswa na Roho Mtakatifu.

    17 Kwa hiyo ninajisifu katika Kristo Yesu, kwenye utumishi wangu kwa Mungu. 18 Kwa maana sitathubutu kusema kitu chochote zaidi ya kile ambacho Kristo amefanya kwa kunitumia mimi katika kuwaongoza watu wa Mataifa wamtii Mungu kwa yale niliyosema na kufanya, 19 kwa nguvu za ishara na miujiza, kwa uweza wa Roho wa Mungu, hivyo kuanzia Yerusalemu hadi maeneo yote ya kandokando yake mpaka Iliriko, nimekwisha kuihubiri Injili ya Kristo kwa ukamilifu.

  34. 12 Basi haya ndiyo majivuno yetu: Dhamiri yetu inatushuhudia kwamba tumeenenda katika ulimwengu na hasa katika uhusiano wetu na ninyi, katika utakatifu na uaminifu utokao kwa Mungu. Hatukufanya hivyo kwa hekima ya kidunia bali kwa neema ya Mungu. 13 Kwa maana hatuwaandikii mambo ambayo hamwezi kusoma au kuyaelewa. Natumaini kwamba, 14 kama vile mlivyotuelewa kwa sehemu, mtakuja kuelewa kwa ukamilifu ili mweze kujivuna kwa ajili yetu, kama na sisi tutakavyojivuna kwa ajili yenu katika siku ya Bwana Yesu.

  35. 5 Bwana huwachukia sana wote wenye kiburi cha moyo.

    Uwe na hakika kwa hili: Hawataepuka kuadhibiwa.

  36. 12 Je, unamwona mtu ajionaye mwenye hekima

    machoni pake mwenyewe?

    Liko tumaini zaidi kwa mpumbavu kuliko kwake.

  37. 1 Tuseme nini basi, kuhusu Abrahamu baba yetu kwa jinsi ya mwili: yeye alipataje kujua jambo hili? 2 Kwa maana ikiwa Abrahamu alihesabiwa haki kwa matendo, basi, anacho kitu cha kujivunia, lakini si mbele za Mungu. 3 Kwa maana Maandiko yasemaje? “Abrahamu alimwamini Mungu na ikahesabiwa kwake kuwa haki.”

    4 Basi mtu afanyapo kazi, mshahara wake hauhesabiwi kwake kuwa ni zawadi, bali ni haki yake anayostahili. 5 Lakini kwa mtu ambaye hafanyi kazi na anamtumaini Mungu, yeye ambaye huwahesabia waovu haki, imani yake inahesabiwa kuwa haki.

  38. 5 Kila amsingiziaye jirani yake kwa siri,

    huyo nitamnyamazisha;

    mwenye macho ya dharau na moyo wa kiburi

    huyo sitamvumilia.

  39. 23 Kiburi cha mtu humshusha,

    bali mtu mwenye roho ya unyenyekevu

    hupata heshima.

  40. 1 Kwa hiyo, kwa kuwa tumekwisha kuhesabiwa haki kwa imani, tuna amani na Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, 2 ambaye kwa kupitia kwake tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo ndani yake sasa tunasimama, nasi twafurahia katika tumaini letu la kushiriki utukufu wa Mungu. 3 Si hivyo tu, bali twafurahi pia katika mateso, kwa sababu tunajua kuwa mateso huleta saburi, 4 nayo saburi huleta uthabiti wa moyo, na uthabiti wa moyo huleta tumaini, 5 wala tumaini halitukatishi tamaa, kwa sababu Mungu amekwisha kumimina pendo lake mioyoni mwetu kwa njia ya Roho Mtakatifu ambaye ametupatia.

  41. 3 Kwa ajili ya neema niliyopewa nawaambia kila mmoja miongoni mwenu, asijidhanie kuwa bora kuliko impasavyo, bali afikiri kwa busara kwa kulingana na kipimo cha imani Mungu aliyompa.

  42. 30 Kama ni lazima nijisifu, basi nitajisifia yale mambo yanayoonyesha udhaifu wangu.

  43. 34 Huwadhihaki wale wanaodhihaki,

    lakini huwapa neema wale wanyenyekevu.

  44. 4 Macho ya kudharau na moyo wa kiburi,

    ambavyo ni taa ya waovu, vyote ni dhambi!

  45. 11 Majivuno yako yote yameshushwa mpaka kuzimu,

    pamoja na kelele ya vinubi vyako,

    mafunza yametanda chini yako,

    na minyoo imekufunika.

    12 Tazama jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni,

    ewe nyota ya asubuhi, mwana wa mapambazuko!

    Umetupwa chini duniani,

    wewe uliyepata kuangusha mataifa!

    13 Ulisema moyoni mwako,

    “Nitapanda juu hadi mbinguni,

    nitakiinua kiti changu cha enzi

    juu ya nyota za Mungu,

    nitaketi nimetawazwa

    juu ya mlima wa kusanyiko,

    kwenye vimo vya juu sana vya Mlima Mtakatifu.

    14 Nitapaa juu kupita mawingu,

    nitajifanya kama Yeye Aliye Juu Sana.”

    15 Lakini umeshushwa chini hadi kuzimu,

    hadi kwenye vina vya shimo.

  46. 5 “Wao hutenda mambo yao yote ili waonekane na watu. Hupanua vikasha vyao vyenye maandiko ya sheria na kurefusha matamvua ya mavazi yao. 6 Wanapenda kukalia viti vya heshima katika karamu, na vile viti maalum sana katika masinagogi. 7 Hupenda kusalimiwa masokoni na kutaka watu wawaite ‘Rabi.’

  47. 9 Basi mtu mmoja jina lake Simoni alikuwa amefanya uchawi kwa muda mrefu katika mji huo akiwashangaza watu wote wa Samaria. Alijitapa kwamba yeye ni mtu mkuu, 10 nao watu wote wakubwa kwa wadogo wakamsikiliza na kumaka, wakisema “Mtu huyu ndiye uweza wa Mungu ujulikanao kama ‘Uweza Mkuu.’ ”

  48. 25 Lakini moyo wa Hezekia ukajaa majivuno na hakuonyesha itikio kwa wema aliotendewa, kwa hiyo ghadhabu ya Bwana ikawa juu yake na juu ya Yuda na Yerusalemu.

  49. 2 Kila mmoja humwambia jirani yake uongo;

    midomo yao ya hila huzungumza kwa udanganyifu.

    3 Bwana na akatilie mbali midomo yote ya hila

    na kila ulimi uliojaa majivuno,

    4 ule unaosema, “Kwa ndimi zetu tutashinda;

    midomo ni mali yetu, bwana wetu ni nani?”

  50. 10 Umeutegemea uovu wako,

    nawe umesema, ‘Hakuna yeyote anionaye.’

    Hekima yako na maarifa yako vinakupoteza

    unapojiambia mwenyewe,

    ‘Mimi ndiye, wala hakuna mwingine zaidi yangu.’

    11 Maafa yatakujia,

    nawe hutaweza kuyaondoa kwa uaguzi.

    Janga litakuangukia,

    wala hutaweza kulikinga kwa fidia;

    msiba mkuu usioweza kuutabiri

    utakujia ghafula.

  51. 49 “ ‘Sasa hii ilikuwa ndiyo dhambi ya dada yako Sodoma: yeye na binti zake walikuwa na majivuno, walafi na wazembe, hawakuwasaidia maskini na wahitaji. 50 Walijivuna na kufanya mambo ya machukizo sana mbele zangu. Kwa hiyo niliwakatilia mbali nami kama mlivyoona.

  52. 1 Neno la Bwana likanijia kusema: 2 “Mwanadamu, mwambie mfalme wa Tiro, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo:

    “ ‘Kwa sababu moyo wako umejivuna

    na umesema, “Mimi ni mungu;

    nami ninaketi katika kiti cha enzi cha mungu

    katika moyo wa bahari.”

    Lakini wewe ni mwanadamu, wala si mungu,

    ingawa unafikiri kuwa una hekima kama mungu.

    3 Je, wewe una hekima kuliko Danieli?

    Je, hakuna siri iliyofichika kwako?

    4 Kwa hekima yako na ufahamu wako,

    umejipatia utajiri,

    nawe umejikusanyia dhahabu

    na fedha katika hazina zako.

    5 Kwa werevu wako mwingi katika biashara,

    umeongeza utajiri wako

    na kwa sababu ya utajiri wako

    moyo wako umekuwa na kiburi.

    6 “ ‘Kwa hiyo, hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo:

    “ ‘Kwa sababu unafikiri una hekima,

    mwenye hekima kama mungu,

    7 mimi nitawaleta wageni dhidi yako,

    taifa katili kuliko yote;

    watafuta panga zao dhidi ya uzuri wa hekima yako,

    na kuchafua fahari yako inayongʼaa.

    8 Watakushusha chini shimoni,

    nawe utakufa kifo cha kikatili

    katika moyo wa bahari.

    9 Je, wakati huo utasema, “Mimi ni mungu,”

    mbele ya wale wanaokuua?

    Utakuwa mwanadamu tu, wala si mungu,

    mikononi mwa hao wanaokuua.

    10 Utakufa kifo cha wasiotahiriwa

    kwa mkono wa wageni.

    Kwa kuwa mimi nimenena, asema Bwana Mwenyezi.’ ”

  53. 3 Kiburi cha moyo wako kimekudanganya,

    wewe unayeishi katika majabali ya miamba

    na kufanya makao yako juu,

    wewe unayejiambia mwenyewe,

    ‘Ni nani awezaye kunishusha chini?’

  54. 5 Vivyo hivyo ulimi ni kiungo kidogo sana katika mwili, lakini hujivuna majivuno makuu. Fikirini jinsi moto mdogo unavyoweza kuteketeza msitu mkubwa!

  55. 13 Ni nani aliye na hekima na ufahamu miongoni mwenu? Basi na aionyeshe hiyo kwa maisha yake mema na kwa matendo yake yaliyotendwa kwa unyenyekevu utokanao na hekima. 14 Lakini ikiwa mna wivu na ni wenye chuki na ugomvi mioyoni mwenu, msijisifu kwa ajili ya hayo wala msiikatae kweli. 15 Hekima ya namna hiyo haishuki kutoka mbinguni, bali ni ya kidunia, isiyo ya kiroho, na ya kishetani. 16 Kwa maana panapokuwa na wivu na ubinafsi, ndipo penye machafuko na uovu wa kila namna.

    17 Lakini hekima itokayo mbinguni kwanza ni safi, kisha inapenda amani, tena ni ya upole, iliyo tayari kusikiliza wengine kwa unyenyekevu, iliyojaa huruma na matunda mema, isiyopendelea mtu, tena isiyokuwa na unafiki. 18 Mavuno ya haki hupandwa katika amani na wale wafanyao amani.

  56. 7 Mpatie mateso na huzuni nyingi sawa na

    utukufu na anasa alizojipatia.

    Kwa kuwa moyoni mwake hujivuna, akisema,

    ‘Mimi ninatawala kama malkia;

    mimi si mjane, wala sitaona huzuni kamwe.’

    8 Kwa hiyo mapigo yatampata kwa siku moja:

    mauti, maombolezo na njaa.

    Naye atateketezwa kwa moto,

    kwa maana Bwana Mungu amhukumuye ana nguvu.

  57. 14 Mafarisayo, waliokuwa wapenda fedha, waliyasikia hayo yote na wakamcheka kwa dharau. 15 Yesu akawaambia, “Ninyi mnajionyesha kuwa wenye haki mbele za wanadamu, lakini Mungu anaijua mioyo yenu. Kwa maana vile vitu ambavyo wanadamu wanavithamini sana, kwa Mungu ni machukizo.

  58. 30 Nasi kwa upande wetu kwa nini tunajihatarisha kila saa? 31 Kama majivuno yangu kwa ajili yenu katika Kristo Yesu Bwana wetu ni kweli, ndugu zangu, ninakufa kila siku.

  59. 13 Ndugu zangu, ninyi mliitwa ili mwe huru, hivyo msitumie uhuru wenu kama fursa ya kufuata tamaa za mwili, bali tumikianeni ninyi kwa ninyi kwa upendo. 14 Kwa maana sheria yote hukamilika katika amri moja: “Mpende jirani yako kama nafsi yako.” 15 Kama mkiumana na kutafunana, angalieni, msije mkaangamizana.

    16 Kwa hiyo nasema, enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili. 17 Kwa maana mwili hutamani yale yaliyo kinyume na Roho, naye Roho hutamani yale yaliyo kinyume na mwili. Roho na mwili hupingana na kwa sababu hiyo hamwezi kufanya mnayotaka. 18 Lakini kama mkiongozwa na Roho, hamko chini ya sheria.

    19 Basi matendo ya mwili ni dhahiri nayo ni haya: Uasherati, uchafu, ufisadi, 20 kuabudu sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, 21 husuda, ulevi, ulafi na mambo mengine yanayofanana na hayo. Nawaonya, kama nilivyokwisha kuwaonya kabla, kwamba watu watendao mambo kama hayo, hawataurithi Ufalme wa Mungu.

    22 Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, 23 upole na kiasi. Katika mambo kama haya hakuna sheria. 24 Wote walio wa Kristo Yesu wameusulubisha mwili na shauku zake pamoja na tamaa zake. 25 Kwa kuwa tunaishi kwa Roho, basi, tuenende kwa Roho. 26 Tusijisifu bure, tukichokozana na kuoneana wivu.

  60. 1 Kama kukiwa na jambo lolote la kutia moyo katika kuunganishwa na Kristo, kukiwa faraja yoyote katika upendo wake, kukiwa na ushirika wowote na Roho, kukiwa na wema wowote na huruma, 2 basi ikamilisheni furaha yangu kwa kuwa na nia moja, mkiwa na upendo huo moja, mkiwa wa roho na kusudi moja. 3 Msitende jambo lolote kwa nia ya kujitukuza wala kujivuna, bali kwa unyenyekevu kila mtu amhesabu mwingine bora kuliko nafsi yake. 4 Kila mmoja wenu asiangalie faida yake mwenyewe tu, bali pia ajishughulishe kwa faida ya wengine.

    5 Kuweni na nia ile ile aliyokuwa nayo Kristo Yesu:

    6 Yeye, ingawa alikuwa na asili ya Mungu hasa,

    hakuona kule kuwa sawa na Mungu

    kuwa kitu cha kushikilia,

    7 bali alijifanya si kitu,

    akachukua hali hasa na mtumwa,

    naye akazaliwa katika umbo la mwanadamu.

    8 Naye akiwa na umbo la mwanadamu,

    alijinyenyekeza, akatii hata mauti:

    naam, mauti ya msalaba!

  61. 6 Lakini yeye hutupatia neema zaidi. Hii ndiyo sababu Andiko husema:

    “Mungu huwapinga wenye kiburi,

    lakini huwapa wanyenyekevu neema.”

  62. 5 Vivyo hivyo, ninyi mlio vijana watiini wazee. Nanyi nyote imewapasa kujivika unyenyekevu kila mtu kwa mwenzake, kwa kuwa,

    “Mungu huwapinga wenye kiburi,

    lakini huwapa wanyenyekevu neema.”

  63. 11 Jihadharini msimsahau Bwana Mungu wenu, mkashindwa kushika maagizo yake, sheria na amri zake ambazo ninawapa leo. 12 Angalia wakati mtakapokuwa mmekula na kushiba, mkajenga nyumba nzuri na kukaa humo, 13 na wakati makundi yenu ya ngʼombe na mbuzi na kondoo yatakapoongezeka na fedha na dhahabu yenu itakapoongezeka na vyote mlivyo navyo vitakapozidishwa, 14 basi mioyo yenu isiwe na kiburi mkamsahau Bwana Mungu wenu aliyewatoa katika nchi ya Misri, kutoka nchi ya utumwa. 15 Aliwaongoza kupitia jangwa lile kubwa na la kutisha, nchi ile ya kiu isiyo na maji, yenye nyoka wa sumu na nge. Aliwatolea maji kutoka kwenye mwamba mgumu. 16 Aliwapa mana ya kula jangwani, kitu ambacho baba zenu hawakukijua, ili kuwanyenyekesha na kuwajaribu ninyi ili mwishoni apate kuwatendea mema. 17 Mnaweza kusema, “Uwezo wangu na nguvu za mikono yangu ndizo zilizonipatia utajiri huu.” 18 Lakini kumbukeni Bwana Mungu wenu, ndiye ambaye huwapa uwezo wa kupata utajiri, na hivyo kulithibitisha Agano lake, ambalo aliwaapia baba zenu, kama ilivyo leo.

    19 Ikiwa mtamsahau Bwana Mungu wenu, mkaifuata miungu mingine, mkaiabudu na kuisujudia, ninashuhudia dhidi yenu leo kwamba hakika mtaangamizwa. 20 Kama mataifa Bwana aliyoyaangamiza mbele yenu, ndivyo ninyi mtakavyoangamizwa kwa kutokumtii Bwana Mungu wenu.

  64. 4 Kwa wale wenye majivuno ninasema,

    ‘Msijisifu tena,’

    kwa wale waovu, ‘Msiinue pembe zenu.

    5 Msiinue pembe zenu dhidi ya mbingu;

    msiseme kwa shingo zilizonyooshwa.’ ”

    6 Hakuna yeyote atokaye mashariki wala magharibi

    au kutoka jangwani awezaye kumkweza mwanadamu.

  65. 6 Ingawa Bwana yuko juu,

    humwangalia mnyonge,

    bali mwenye kiburi

    yeye anamjua kutokea mbali.

  66. 16 Kuna vitu sita anavyovichukia Bwana,

    naam, viko saba vilivyo chukizo kwake:

    17 macho ya kiburi,

    ulimi udanganyao,

    mikono imwagayo damu isiyo na hatia,

    18 moyo uwazao mipango miovu,

    miguu iliyo myepesi kukimbilia uovu,

    19 shahidi wa uongo ambaye humwaga uongo,

    na mtu ambaye huchochea fitina kati ya ndugu.

  67. 25 Bwana hubomoa nyumba ya mtu mwenye kiburi,

    bali huilinda mipaka ya mjane isiguswe.

  68. 11 Macho ya mtu mwenye majivuno yatanyenyekezwa

    na kiburi cha wanadamu kitashushwa,

    Bwana peke yake ndiye atakayetukuzwa siku hiyo.

    12 Bwana Mwenye Nguvu Zote anayo siku aliyoiweka akiba

    kwa wote wenye kujivuna na wenye kiburi,

    kwa wote wanaojikweza

    (nao watanyenyekezwa),

  69. 20 Akaendelea kusema, “Kile kimtokacho mtu ndicho kimtiacho unajisi. 21 Kwa maana kutoka ndani ya moyo wa mtu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wizi, uuaji, uzinzi, 22 tamaa mbaya, uovu, udanganyifu, ufisadi, wivu, matukano, kiburi na upumbavu. 23 Maovu haya yote hutoka ndani ya mtu, nayo ndiyo yamtiayo mtu unajisi.”

  70. 22 Ingawa walijidai kuwa wenye hekima, wakawa wajinga 23 na kubadili utukufu wa Mungu aishiye milele kwa sanamu zilizofanywa zifanane na mwanadamu ambaye hufa, na mfano wa ndege, wanyama na viumbe vitambaavyo.

  71. 6 Majivuno yenu si mazuri. Je, hamjui ya kwamba chachu kidogo huchachusha donge zima la unga? 7 Ondoeni chachu ya kale ili mpate kuwa donge jipya lisilotiwa chachu, kama vile mlivyo. Kwa maana Kristo, Mwana-Kondoo wetu wa Pasaka amekwisha tolewa kuwa dhabihu. 8 Kwa hiyo, tusiiadhimishe sikukuu hii, kwa chachu ya zamani, chachu ya nia mbaya na uovu, bali kwa mkate usiotiwa chachu, ndio weupe wa moyo na kweli.

  72. 11 Basi, kwa kuwa tunajua kumcha Bwana, tunajitahidi kuwavuta wengine. Lakini Mungu anatufahamu dhahiri, nami natumaini kwamba tu dhahiri katika dhamiri zenu pia. 12 Sio kwamba tunajaribu kujistahilisha kwenu tena, lakini tunataka kuwapa nafasi ili mwone fahari juu yetu mweze kuwajibu hao wanaoona fahari juu ya mambo yanayoonekana badala ya mambo yaliyo moyoni.

  73. 19 Kwa maana tumaini letu ni nini, au furaha yetu au taji yetu ya kujisifia mbele za Bwana Yesu Kristo wakati wa kuja kwake? Je, si ni ninyi? 20 Naam, ninyi ndio fahari yetu na furaha yetu.

  74. 19 Nitakivunja kiburi chenu cha ukaidi na kuifanya anga iliyo juu yenu iwe kama chuma, na ardhi yenu kama shaba.

  75. 5 Wenye kiburi hawawezi kusimama mbele yako,

    unawachukia wote watendao mabaya.

  76. 10 Kiburi huzalisha magomvi tu,

    bali hekima hupatikana kwa wale wanaozingatia ushauri.

  77. 24 Mtu mwenye kiburi na majivuno, “Mdhihaki” ndilo jina lake;

    hutenda mambo kwa kiburi kilichozidi.

  78. 31 “Tazama, niko kinyume nawe, ewe mwenye majivuno,”

    asema Bwana, Bwana Mwenye Nguvu Zote,

    “kwa kuwa siku yako imewadia,

    yaani, wakati wako wa kuadhibiwa.

    32 Mwenye majivuno atajikwaa na kuanguka,

    wala hakuna yeyote atakayemuinua;

    nitawasha moto katika miji yake,

    utakaowateketeza wote wanaomzunguka.”

  79. 8 “Wakati nilipokuwa ninafikiri kuhusu pembe hizo, mbele yangu kulikuwa na pembe nyingine, ambayo ni ndogo, iliyojitokeza miongoni mwa zile kumi; pembe tatu za mwanzoni zilingʼolewa ili kuipa nafasi hiyo ndogo. Pembe hii ilikuwa na macho kama ya mwanadamu, na mdomo ulionena kwa majivuno.

  80. 21 Katika siku iliyochaguliwa Herode Agripa akavaa mavazi yake ya kifalme, akaketi kwenye kiti chake cha enzi na kuwahutubia watu. 22 Watu waliokuwa wamekusanyika wakapiga kelele, wakisema, “Hii si sauti ya mwanadamu, bali ni ya Mungu.” 23 Ghafula, kwa kuwa Herode hakumpa Mungu utukufu, malaika wa Bwana akampiga, naye akaliwa na chango, akafa.

  81. 16 Kaeni kwa amani ninyi kwa ninyi. Msijivune, bali mwe tayari kushirikiana na wanyonge. Wala msiwe watu wenye kujivuna kwamba mnajua kila kitu.

  82. 7 Je, nilitenda dhambi kwa kujishusha ili kuwainua ninyi kwa kuwahubiria Injili ya Mungu pasipo malipo? 8 Niliyanyangʼanya makanisa mengine kwa kupokea misaada kutoka kwao ili niweze kuwahudumia ninyi. 9 Nami nilipokuwa pamoja nanyi, nikipungukiwa na chochote, sikuwa mzigo kwa mtu yeyote, kwa maana ndugu waliotoka Makedonia walinipatia mahitaji yangu. Kwa hiyo nilijizuia kuwa mzigo kwenu kwa njia yoyote, nami nitaendelea kujizuia. 10 Kwa hakika kama vile kweli ya Kristo ilivyo ndani yangu, hakuna mtu yeyote katika Akaya nzima atakayenizuia kujivunia jambo hili. 11 Kwa nini? Je, ni kwa sababu siwapendi? Mungu anajua ya kuwa nawapenda! 12 Nami nitaendelea kufanya lile ninalofanya sasa ili nisiwape nafasi wale ambao wanatafuta nafasi ya kuhesabiwa kuwa sawa na sisi katika mambo wanayojisifia.

    13 Watu kama hao ni mitume wa uongo, ni wafanyakazi wadanganyifu, wanaojigeuza waonekane kama mitume wa Kristo.

  83. 1 Yanipasa nijisifu, ingawa haifaidi kitu. Nitaenda kwenye maono na ufunuo kutoka kwa Bwana.

  84. 17 Watu hawa ni chemchemi zisizo na maji, na ukungu upeperushwao na tufani. Giza nene limewekwa tayari kwa ajili yao. 18 Kwa maana wao hunena maneno makuu mno ya kiburi cha bure, na kwa kuvutia tamaa mbaya za asili ya mwili, huwashawishi watu ambao ndipo tu wamejiondoa miongoni mwa wale wanaoishi katika ufisadi. 19 Huwaahidi uhuru hao waliowanasa, wakati wao wenyewe ni watumwa wa ufisadi: kwa maana mtu ni mtumwa wa kitu chochote kinachomtawala.

  85. 14 Enoki, mtu wa saba kuanzia Adamu alitoa unabii kuhusu watu hawa, akisema: “Tazama, Bwana anakuja pamoja na maelfu kwa maelfu ya watakatifu wake, 15 ili kumhukumu kila mmoja na kuwapatiliza wote wasiomcha Mungu kwa matendo yao yote ya uasi waliyoyatenda, pamoja na maneno yote ya kuchukiza ambayo wenye dhambi wamesema dhidi yake.” 16 Watu hawa ni wenye kunungʼunika na wenye kutafuta makosa; wao hufuata tamaa zao mbaya, hujisifu kwa maneno makuu kuhusu wao wenyewe na kuwasifu mno watu wenye vyeo kwa ajili ya kujipatia faida.

  86. 14 “Kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika:

    “Haya ndiyo maneno yake yeye aliye Amen, shahidi mwaminifu na wa kweli, mtawala wa uumbaji wote wa Mungu. 15 Nayajua matendo yako, ya kwamba wewe si baridi wala si moto. Afadhali ungelikuwa moja au lingine. 16 Hivyo kwa kuwa u vuguvugu, si baridi wala moto, nitakutapika utoke kinywani mwangu. 17 Kwa maana unasema: ‘Mimi ni tajiri, nimejilimbikizia mali, wala sihitaji kitu chochote.’ Lakini hutambui ya kwamba wewe ni mnyonge, wa kuhurumiwa, maskini, kipofu, tena uliye uchi. 18 Nakushauri ununue kutoka kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, ili upate kuwa tajiri, na mavazi meupe ili uyavae upate kuficha aibu ya uchi wako, na mafuta ya kupaka macho yako ili upate kuona.

    19 “Wale niwapendao, ninawakemea na kuwaadibisha. Hivyo uwe na bidii ukatubu. 20 Tazama! Nasimama mlangoni nabisha. Kama mtu yeyote akisikia sauti yangu na kufungua mlango, nitaingia ndani na kula pamoja naye, naye pamoja nami.

    21 “Yeye ashindaye nitampa haki ya kuketi pamoja nami kwenye kiti changu cha enzi, kama vile mimi nilivyoshinda na nikaketi pamoja na Baba yangu kwenye kiti chake cha enzi. 22 Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho ayaambia makanisa.”