45 Bible Verses About Tithing

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Tithing
  1. 6 Kumbukeni kwamba: Yeyote apandaye kwa uchache pia atavuna kwa uchache, naye apandaye kwa ukarimu pia atavuna kwa ukarimu. 7 Kila mtu atoe kama anavyokusudia moyoni mwake, si kwa uchoyo au kwa kulazimishwa, kwa maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo mkunjufu. 8 Naye Mungu aweza kuwapa kila baraka kwa wingi, ili katika mambo yote kila wakati, mwe na kila kitu mnachohitaji, ili mweze kushiriki kwa wingi katika kila kazi njema. 9 Kama ilivyoandikwa:

    “Ametawanya vipawa vyake kwa ukarimu

    akawapa maskini;

    haki yake hudumu milele.”

    10 Yeye ampaye mpanzi mbegu kwa ajili ya kupanda na mkate kuwa chakula, atawapa na kuzizidisha mbegu zenu za kupanda na kuongeza mavuno ya haki yenu. 11 Mtatajirishwa kwa kila namna ili mpate kuwa wakarimu kila wakati, na kupitia kwetu, ukarimu wenu utamletea Mungu shukrani.

  2. 5 “Basi nitakuja karibu nanyi ili kuhukumu. Nami nitakuwa mwepesi kushuhudia dhidi ya wachawi, wazinzi, waapao kwa uongo, wanaopunja vibarua malipo yao, wanaowaonea wajane na yatima, na wanaowanyima wageni haki, lakini hawaniogopi mimi,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.

    6 “Mimi Bwana sibadiliki. Kwa hiyo ninyi, enyi uzao wa Yakobo, hamjaangamizwa. 7 Tangu wakati wa baba zenu mmegeukia mbali na amri zangu nanyi hamkuzishika. Nirudieni mimi, nami nitawarudia ninyi,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.

    “Lakini mnauliza, ‘Tutarudi kwa namna gani?’

    8 “Je, mwanadamu atamwibia Mungu? Hata hivyo mnaniibia mimi.

    “Lakini mnauliza, ‘Tunakuibia kwa namna gani?’

    “Mnaniibia zaka na dhabihu. 9 Mko chini ya laana, ninyi taifa lote, kwa sababu mnaniibia mimi. 10 Leteni zaka kamili ghalani, ili kuwe na chakula katika nyumba yangu. Nijaribuni katika hili,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote, “nanyi mwone kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni na kuwamwagieni baraka nyingi mpaka mkose nafasi ya kutosha. 11 Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu, wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote. 12 “Ndipo mataifa yote yatawaita mliobarikiwa, kwa maana nchi yenu itakuwa ya kupendeza sana,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.

  3. 30 “ ‘Zaka ya kila kitu kutoka shambani, iwe ni nafaka kutoka kwa ardhi, au tunda kutoka kwa miti, ni mali ya Bwana; ni takatifu kwa Bwana. 31 Kama mtu akikomboa chochote cha zaka yake, lazima aongeze sehemu ya tano ya thamani yake. 32 Zaka yote ya kundi la ngʼombe au la kondoo na mbuzi, kila mnyama wa kumi apitaye chini ya fimbo ya yule awachungaye, atakuwa mtakatifu kwa Bwana. 33 Yule mnyama wa kumi hatachaguliwa kwa kigezo cha uzuri au ubaya, naye haruhusiwi kubadiliwa. Ikiwa atabadiliwa, basi mnyama yule wa kwanza na huyo aliyebadiliwa wote watahesabiwa kuwa watakatifu, na haiwezekani kuwakomboa.’ ”

    34 Haya ndiyo maagizo Bwana aliyompa Mose juu ya Mlima Sinai kwa ajili ya Waisraeli.

  4. 14 “Kila kitu katika Israeli ambacho kimetolewa kwa Bwana ni chenu. 15 Kila mzaliwa wa kwanza wa mwanadamu na wa mnyama, ambaye ametolewa kwa Bwana ni wenu. Lakini ni lazima mtamkomboa kila mwana mzaliwa wa kwanza na kila mzaliwa wa kwanza wa kiume wa wanyama wasio safi. 16 Watakapokuwa na umri wa mwezi mmoja, ni lazima mtawakomboa kwa bei ya ukombozi iliyowekwa, kwa shekeli tano za fedha, kulingana na shekeli ya mahali patakatifu, yenye uzito wa gera ishirini.

    17 “Lakini kamwe usimkomboe mzaliwa wa kwanza wa maksai, kondoo au mbuzi; hawa ni watakatifu. Nyunyizia damu yao juu ya madhabahu na uchome mafuta yao kama sadaka itolewayo kwa moto, harufu nzuri inayompendeza Bwana. 18 Nyama zao zitakuwa chakula chenu, kama ilivyokuwa kidari cha kuinuliwa na paja la mguu wa kulia. 19 Chochote kitakachotengwa kutoka sadaka takatifu ambazo Waisraeli wanamtolea Bwana, ninakupa wewe, wanao na binti zako kama fungu lenu la kawaida. Ni Agano la milele la chumvi mbele za Bwana kwako na watoto wako.”

    20 Bwana akamwambia Aroni, “Hutakuwa na urithi wowote katika nchi yao, wala hutakuwa na sehemu miongoni mwao; Mimi ni fungu lako na urithi wako miongoni mwa Waisraeli.

    21 “Ninawapa Walawi zaka yote katika Israeli kama urithi wao kuwa kama malipo kwa kazi wanayoifanya wakati wanapohudumu katika Hema la Kukutania. 22 Kuanzia sasa, kamwe Waisraeli wasisogelee karibu na Hema la Kukutania, la sivyo watabeba matokeo ya dhambi zao, nao watakufa. 23 Ni Walawi watakaofanya kazi katika Hema la Kukutania na kubeba wajibu wa makosa dhidi yake. Hili ni agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo. Hawatapokea urithi wowote miongoni mwa Waisraeli. 24 Badala yake, ninawapa Walawi zaka zote zinazotolewa na Waisraeli kama sadaka kwa Bwana kuwa urithi wao. Hiyo ndiyo sababu nimesema hivi kuhusu wao: ‘Hawatakuwa na urithi miongoni mwa Waisraeli.’ ”

    25 Bwana akamwambia Mose, 26 “Sema na Walawi na uwaambie: ‘Mtakapopokea zaka kutoka kwa Waisraeli ambayo ninawapa kama urithi wenu kutoka kwao, ni lazima mtoe sehemu ya kumi ya hiyo zaka kama sadaka kwa Bwana, iwe zaka ya hiyo zaka. 27 Sadaka yenu itahesabiwa kwenu kama nafaka kutoka sakafu ya kupuria, au divai kutoka kwenye shinikizo la kukamulia zabibu. 28 Kwa njia hii, ninyi pia mtatoa sadaka kwa Bwana kutoka zaka zote mtakazopokea kutoka kwa Waisraeli. Kutoka kwenye zaka hizi, ni lazima mtoe sehemu ya Bwana kwa Aroni, kuhani. 29 Ni lazima mtoe kama sehemu ya Bwana iliyo nzuri sana tena ile sehemu iliyo takatifu sana kuliko zote ya kile kitu mlichopewa.’

  5. 1 Kwa kuwa huyu Melkizedeki alikuwa mfalme wa Salemu na kuhani wa Mungu Aliye Juu Sana. Alipokutana na Abrahamu akirudi kutoka kuwashinda hao wafalme, Melkizedeki alimbariki, 2 naye Abrahamu alimpa sehemu ya kumi ya kila kitu. Kwanza, jina hilo Melkizedeki maana yake ni “mfalme wa haki.” Na pia “mfalme wa Salemu” maana yake ni “mfalme wa amani.” 3 Hana Baba wala mama, hana ukoo, hana mwanzo wala mwisho wa siku zake. Kama Mwana wa Mungu, yeye adumu akiwa kuhani milele.

    4 Tazama jinsi alivyokuwa mkuu: Hata Abrahamu, baba yetu mkuu, alimpa sehemu ya kumi ya nyara zake. 5 Basi sheria inawaagiza wana wa Lawi ambao hufanyika makuhani kupokea sehemu ya kumi kutoka kwa watu ambao ni ndugu zao, ingawa ndugu zao ni wazao wa Abrahamu. 6 Huyu Melkizedeki, ingawa hakufuatia ukoo wake kutoka kwa Lawi, lakini alipokea sehemu ya kumi kutoka kwa Abrahamu na kumbariki yeye aliyekuwa na zile ahadi. 7 Wala hakuna shaka kwamba mdogo hubarikiwa na aliye mkuu kumliko yeye. 8 Kwa upande mmoja, sehemu ya kumi hupokelewa na wale ambao hupatikana na kufa; lakini kwa upande mwingine hupokelewa na yeye ambaye hushuhudiwa kuwa yu hai. 9 Mtu anaweza hata kusema kwamba Lawi, ambaye hupokea sehemu ya kumi, alitoa hiyo sehemu ya kumi kupitia kwa Abrahamu, 10 kwa sababu Melkizedeki alipokutana na Abrahamu, Lawi alikuwa bado katika viuno vya baba yake wa zamani.

  6. 41 Kisha Yesu akaketi mkabala na sehemu ambapo sadaka zilikuwa zinawekwa na kuangalia umati wa watu wakiweka fedha zao kwenye sanduku la hazina ya Hekalu. Matajiri wengi wakaweka kiasi kikubwa cha fedha. 42 Lakini mjane mmoja maskini akaja na kuweka sarafu mbili ndogo za shaba zenye thamani ya senti mbili.

    43 Yesu akawaita wanafunzi wake, akawaambia, “Amin, nawaambia, huyu mjane maskini ameweka katika sanduku la hazina zaidi ya watu wengine wote. 44 Wengine wote wametoa kutokana na ziada ya mali zao. Lakini huyu mjane ametoa kutokana na umaskini wake, akaweka kila kitu alichokuwa nacho, hata kile alichohitaji ili kuishi.”

  7. 22 Hakikisheni mmetenga sehemu ya kumi ya mazao yote ya mashamba yenu kila mwaka.

  8. 16 Akarudisha mali zote, na akamrudisha Loti jamaa yake na mali zake, pamoja na wanawake na watu wengine.

    17 Abramu aliporudi baada ya kumshinda Mfalme Kedorlaoma na wale wafalme waliojiunga naye, mfalme wa Sodoma akatoka kwenda kumlaki katika Bonde la Shawe (yaani Bonde la Mfalme).

    18 Ndipo Melkizedeki mfalme wa Salemu alipoleta mkate na divai. Alikuwa kuhani wa Mungu Aliye Juu Sana. 19 Naye akambariki Abramu, akisema,

    “Abarikiwe Abramu na Mungu Aliye Juu Sana,

    Muumba wa mbingu na nchi.

    20 Abarikiwe Mungu Aliye Juu Sana,

    ambaye amewaweka adui zako mkononi mwako.”

    Ndipo Abramu akampa Melkizedeki sehemu ya kumi ya kila kitu.

  9. 23 “Ole wenu walimu wa sheria na Mafarisayo, ninyi wanafiki! Kwa maana mnatoa zaka ya mnanaa, bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu zaidi ya sheria, yaani haki, huruma na uaminifu. Iliwapasa kufanya haya makuu ya sheria bila kupuuza hayo matoleo. 24 Ninyi viongozi vipofu, mnachuja kiroboto lakini mnameza ngamia!

  10. 32 “Tunakubali wajibu wa kutimiza amri za kutoa theluthi ya shekeli kila mwaka kwa ajili ya utumishi wa nyumba ya Mungu: 33 Kwa ajili ya mikate ya Wonyesho, kwa ajili ya sadaka za kawaida za nafaka na sadaka za kuteketezwa, kwa ajili ya sadaka za siku za Sabato, Sikukuu za Mwandamo wa Mwezi na sikukuu nyingine zilizoamriwa, kwa ajili ya sadaka takatifu, kwa ajili ya sadaka za dhambi ili kufanya upatanisho kwa ajili ya Israeli, na kwa ajili ya kazi zote za nyumba ya Mungu wetu.

    34 “Sisi makuhani, Walawi na watu, tumepiga kura kuamua kuwa kila mmoja wa jamaa zetu lazima alete katika nyumba ya Mungu wetu kwa nyakati maalum kila mwaka mchango wa kuni za kukokea moto katika madhabahu ya Bwana Mungu wetu, kama ilivyoandikwa katika Sheria.

    35 “Pia tunachukua wajibu wa kuleta malimbuko ya mazao yetu na matunda ya kwanza ya kila mti wa matunda katika nyumba ya Bwana kila mwaka.

    36 “Kama pia ilivyoandikwa katika Sheria, tutawaleta wazaliwa wetu wa kwanza wa kiume, na wa mifugo yetu, yaani wa ngʼombe wetu na wa makundi yetu ya kondoo na mbuzi, katika nyumba ya Mungu wetu, kwa ajili ya makuhani wanaohudumu huko.

    37 “Zaidi ya hayo, tutaleta katika ghala za nyumba ya Mungu wetu, kwa makuhani, vyakula vya kwanza vya mashamba yetu, sadaka zetu za nafaka, matunda ya miti yetu yote, divai yetu mpya na mafuta. Nasi tutaleta zaka za mazao yetu kwa Walawi, kwa kuwa Walawi ndio ambao hukusanya zaka katika miji yote tunakofanya kazi. 38 Kuhani atokanaye na uzao wa Aroni atashirikiana na Walawi wakati wanapopokea zaka, nao Walawi itawapasa kuleta sehemu ya kumi ya zaka katika nyumba ya Mungu wetu katika ghala za hazina. 39 Watu wa Israeli pamoja na Walawi itawapasa kuleta michango yao ya nafaka, divai mpya na mafuta katika vyumba vya ghala, mahali vifaa vya mahali patakatifu vinapohifadhiwa, na wanapokaa makuhani wanaohudumu, na mabawabu na waimbaji.

    “Hatutaacha kuijali nyumba ya Mungu wetu.”

  11. 20 Kisha Yakobo akaweka nadhiri, akisema, “Kama Mungu akiwa pamoja nami na kunilinda katika safari niendayo, akinipa chakula nile na nguo nivae 21 na nirudi salama nyumbani kwa baba yangu, hapo ndipo Bwana atakuwa Mungu wangu, 22 nalo jiwe hili nililolisimamisha kama nguzo litakuwa nyumba ya Mungu na katika yote utakayonipa nitakutolea wewe sehemu ya kumi.”

  12. 9 Mheshimu Bwana kwa mali zako na

    kwa malimbuko ya mazao yako yote;

    10 ndipo ghala zako zitakapojaa hadi kufurika,

    viriba vyako vitafurika kwa mvinyo mpya.

  13. 4 Akawaagiza watu wanaoishi Yerusalemu watoe sehemu iliyo haki ya makuhani na Walawi ili waweze kujitoa kikamilifu kutimiza wajibu wao katika Sheria ya Bwana. 5 Mara tu baada ya kutolewa tangazo hilo, Waisraeli wakatoa kwa ukarimu malimbuko ya nafaka zao, divai mpya, mafuta na asali pamoja na vyote vilivyotoka mashambani. Wakaleta kiasi kikubwa cha fungu la kumi la kila kitu. 6 Watu wa Israeli na Yuda walioishi katika miji ya Yuda wakaleta pia fungu la kumi la makundi yao ya ngʼombe na makundi ya kondoo na mbuzi pia na fungu la kumi la vitu vitakatifu vilivyowekwa wakfu kwa ajili ya Bwana Mungu wao na kuvikusanya katika malundo. 7 Wakaanza kufanya haya katika mwezi wa tatu na kumaliza katika mwezi wa saba. 8 Wakati Hezekia na maafisa wake walipokuja na kuona yale malundo, wakamsifu Bwana na kuwabariki watu wake Israeli.

    9 Hezekia akawauliza makuhani na Walawi kuhusu yale malundo, 10 naye Azaria aliyekuwa kuhani mkuu, kutoka jamaa ya Sadoki, akajibu, “Tangu watu walipoanza kuleta sadaka zao katika Hekalu la Bwana tumekuwa na chakula cha kutosha na vingi vya kuweka akiba kwa sababu Bwana amewabariki watu wake, hivyo tumekuwa na kiasi kingi kilichobaki.”

    11 Hezekia akatoa agizo la kutengeneza vyumba vya ghala katika Hekalu la Bwana nalo hili likafanyika. 12 Kisha kwa uaminifu wakaleta sadaka zao, mafungu yao ya kumi na vitu vilivyowekwa wakfu. Konania Mlawi, ndiye alikuwa msimamizi wa vitu hivi na Shimei ndugu yake ndiye alikuwa msaidizi wake.

  14. 42 “Lakini ole wenu, Mafarisayo, kwa maana mnampa Mungu zaka za mnanaa, mchicha na kila aina ya mboga, lakini mnapuuza haki na upendo wa Mungu. Iliwapasa kufanya haya ya pili bila kupuuza hayo ya kwanza.

  15. 5 Je, hatuna haki ya kusafiri na mke anayeamini, kama wanavyofanya mitume wengine na ndugu zake Bwana na Kefa? 6 Au ni mimi na Barnaba tu inatubidi kufanya kazi ili tuweze kupata mahitaji yetu?

    7 Ni askari yupi aendaye vitani kwa gharama zake mwenyewe? Ni nani apandaye shamba la mizabibu na asile matunda yake? Ni nani achungaye kundi na asipate maziwa yake. 8 Je, nasema mambo haya katika mtazamo wa kibinadamu tu? Je, sheria haisemi vivyo hivyo? 9 Kwa maana imeandikwa katika Sheria ya Mose: “Usimfunge maksai kinywa apurapo nafaka.” Je, Mungu hapa anahusika na ngʼombe? 10 Je, Mungu hasemi haya hasa kwa ajili yetu? Hakika yameandikwa kwa ajili yetu, kwa sababu mtu anapolima na mpuraji akapura nafaka, wote wanapaswa kufanya hivyo wakiwa na tumaini la kushiriki mavuno. 11 Je, ikiwa sisi tulipanda mbegu ya kiroho miongoni mwenu, itakuwa ni jambo kubwa iwapo tutavuna vitu vya mwili kutoka kwenu? 12 Kama wengine wana haki ya kupata msaada kutoka kwenu, isingepasa tuwe na haki hiyo hata zaidi?

    Lakini sisi hatukutumia haki hii. Kinyume chake, tunavumilia kila kitu ili tusije tukazuia Injili ya Kristo. 13 Je, hamjui kwamba, watu wafanyao kazi hekaluni hupata chakula chao kutoka hekaluni, nao wale wahudumiao madhabahuni hushiriki kile kitolewacho madhabahuni? 14 Vivyo hivyo, Bwana ameamuru kwamba wale wanaohubiri Injili wapate riziki yao kutokana na Injili.

  16. 9 Yesu akatoa mfano huu kwa wale waliojiamini kuwa wao ni wenye haki na kuwadharau wengine: 10 “Watu wawili walikwenda Hekaluni kusali, mmoja wao alikuwa Farisayo na mwingine alikuwa mtoza ushuru. 11 Yule Farisayo, akasimama, akasali hivi na kuomba kwake mwenyewe: ‘Mungu, nakushukuru kwa sababu mimi si kama watu wengine ambao ni wanyangʼanyi, wadhalimu, na wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. 12 Mimi nafunga mara mbili kwa juma, na natoa sehemu ya kumi ya mapato yangu.’

    13 “Lakini yule mtoza ushuru akasimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua uso wake kutazama mbinguni, bali alijipigapiga kifuani na kusema: ‘Mungu, nihurumie, mimi mwenye dhambi.’

    14 “Nawaambia, huyu mtoza ushuru alirudi nyumbani akiwa amehesabiwa haki mbele za Mungu zaidi ya yule Farisayo. Kwa maana yeyote ajikwezaye atashushwa, na yeyote ajishushaye atakwezwa.”

  17. 19 “Msijiwekee hazina duniani, mahali ambapo nondo na kutu huharibu, nao wevi huvunja na kuiba. 20 Lakini jiwekeeni hazina mbinguni, mahali ambapo nondo na kutu haviharibu, wala wevi hawavunji na kuiba. 21 Kwa sababu mahali hazina yako ilipo, hapo ndipo pia moyo wako utakapokuwa.

    22 “Jicho ni taa ya mwili. Kama jicho lako ni nyofu, mwili wako wote utajaa nuru. 23 Lakini kama jicho lako ni ovu, mwili wako wote utajawa na giza. Kwa hiyo basi, kama nuru iliyomo ndani yako ni giza, hilo ni giza kuu namna gani!

    24 “Hakuna mtu awezaye kuwatumikia mabwana wawili. Kwa kuwa atamchukia huyu na kumpenda yule mwingine, au atashikamana sana na huyu na kumdharau yule mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu pamoja na Mali.

  18. 1 Basi kuhusu changizo kwa ajili ya watakatifu: Kama nilivyoyaagiza makanisa ya Galatia, fanyeni vivyo hivyo. 2 Siku ya kwanza ya kila juma, kila mmoja wenu atenge kiasi cha fedha, kulingana na mapato yake na fedha hizo aziweke akiba, ili nitakapokuja pasiwe na lazima ya kufanya mchango. 3 Kwa hiyo nitakapowasili, nitawapa wale mtakaowachagua barua za kuwatambulisha, ili kuwatuma wapeleke zawadi zenu huko Yerusalemu. 4 Kama ikionekana ni vyema na mimi niende, basi hao watu watafuatana nami.

  19. 38 Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa. Kipimo cha kujaa na kushindiliwa na kusukwasukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile mpimacho, ndicho mtakachopimiwa.”

  20. 6 “Mwana humheshimu baba yake, naye mtumishi humheshimu bwana wake. Kama mimi ni baba, iko wapi heshima ninayostahili? Kama mimi ni bwana, iko wapi heshima ninayostahili?” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote. “Ni ninyi, enyi makuhani, mnaolidharau Jina langu.

    “Lakini mnauliza, ‘Tumelidharau Jina lako kwa namna gani?’

    7 “Mnatoa sadaka chakula kilichotiwa unajisi juu ya madhabahu yangu.

    “Lakini ninyi mnauliza, ‘Tumekutia unajisi kwa namna gani?’

    “Kwa kusema kuwa meza ya Bwana ni ya kudharauliwa. 8 Wakati mletapo dhabihu za wanyama walio vipofu, je, hilo si kosa? Mnapoleta dhabihu zilizo vilema au wanyama wagonjwa, je, hilo si kosa? Jaribuni kuvitoa kwa mtawala wenu! Je, angefurahishwa nanyi? Je, atawakubalia?” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.

    9 “Basi mwombeni Mungu awe na neema kwetu. Je, kwa sadaka kama hizo kutoka mikononi mwenu, atawapokea?” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.

    10 “Laiti mmoja wenu angalifunga milango ya Hekalu, ili msije mkawasha moto usiokuwa na faida juu ya madhabahu yangu! Sina furaha nanyi,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote, “nami sitaikubali sadaka toka mikononi mwenu. 11 Jina langu litakuwa kuu miongoni mwa mataifa, kuanzia mawio ya jua hata machweo yake. Kila mahali uvumba na sadaka safi zitaletwa kwa Jina langu, kwa sababu Jina langu litakuwa kuu miongoni mwa mataifa,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.

    12 “Lakini mnalinajisi Jina langu kwa kusema kuhusu meza ya Bwana, ‘Imetiwa unajisi pamoja na chakula chake. Ni ya kudharauliwa.’ 13 Nanyi mnasema, ‘Mzigo gani huu!’ Nanyi mnaidharau kwa kiburi,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.

    “Wakati mnapowaleta wanyama mliopokonya kwa nguvu, walio vilema au walio wagonjwa na kuwatoa kama dhabihu, je, niwakubali kutoka mikononi mwenu?” asema Bwana. 14 “Amelaaniwa yeye adanganyaye, aliye na mnyama wa kiume anayekubalika katika kundi lake na kuweka nadhiri ya kumtoa, lakini akatoa dhabihu ya mnyama aliye na dosari kwa Bwana. Kwa kuwa mimi ni Mfalme Mkuu, nalo Jina langu linapaswa kuogopwa miongoni mwa mataifa,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.

  21. 6 Ndipo viongozi wa jamaa, maafisa wa kabila za Israeli, majemadari wa maelfu na majemadari wa mamia, pamoja na maafisa waliokuwa wasimamizi wa kazi za mfalme wakatoa kwa hiari yao.

    7 Wakatoa kwa ajili ya kazi ya Hekalu la Mungu talanta 5,000 na darkoni 10,000 za dhahabu, talanta 10,000 za fedha, talanta 18,000 za shaba na talanta 100,000 za chuma. 8 Kila mmoja aliyekuwa na vito vya thamani akavitoa katika hazina ya Hekalu la Bwana chini ya uangalizi wa Yehieli Mgershoni. 9 Watu wakafurahi kwa sababu ya itikio la hiari la viongozi wao, kwa kuwa walikuwa wametoa kwa hiari na kwa moyo wote kwa Bwana. Mfalme Daudi pia akafurahi sana.

    10 Daudi akamhimidi Bwana mbele ya kusanyiko lote, akisema:

    “Uhimidiwe wewe, Ee Bwana,

    Mungu wa Israeli baba yetu,

    tangu milele hata milele.

    11 Ukuu na uweza, ni vyako, Ee Bwana,

    na utukufu na enzi na uzuri,

    kwa kuwa kila kilichoko mbinguni na duniani

    ni chako wewe.

    Ee Bwana, ufalme ni wako;

    umetukuzwa kuwa mkuu juu ya yote.

    12 Utajiri na heshima vyatoka kwako;

    wewe ndiwe utawalaye vitu vyote.

    Mikononi mwako kuna nguvu na uweza

    ili kuinua na kuwapa wote nguvu,

    13 Sasa, Mungu wetu, tunakushukuru

    na kulisifu Jina lako tukufu.

  22. 10 nami sasa ninaleta malimbuko ya ardhi ambayo wewe, Ee Bwana, umenipa.” Weka kapu mbele za Bwana Mungu wako na usujudu mbele zake. 11 Kisha wewe pamoja na Walawi na wageni wote walioko miongoni mwenu mtafurahi katika vitu vyote vizuri ambavyo Bwana Mungu wenu amewapa pamoja na wa nyumbani mwenu.

    12 Wakati utakapokuwa umeshatoa zaka zote za mazao yako katika mwaka wa tatu, ambao ni mwaka wa zaka, utampa Mlawi, mgeni, yatima na mjane, ili waweze kula katika miji yenu na kushiba.

  23. 4 “Nendeni Betheli mkatende dhambi;

    nendeni Gilgali mkazidi kutenda dhambi.

    Leteni dhabihu zenu kila asubuhi,

    zaka zenu kila mwaka wa tatu.

    5 Mchome mkate uliotiwa chachu kama sadaka ya shukrani,

    jisifuni kuhusu sadaka zenu za hiari:

    jigambeni kwa ajili ya sadaka hizo, enyi Waisraeli,

    kwa kuwa hili ndilo mnalopenda kulitenda,”

    asema Bwana Mwenyezi.

  24. 24 Kuna mtu atoaye kwa ukarimu, hata hivyo hupata zaidi,

    mwingine huzuia, lakini huwa maskini.

    25 Mtu mkarimu atastawi;

    yeye awaburudishaye wengine

    ataburudishwa mwenyewe.

  25. 16 Wanaume wenu wote lazima wajitokeze mara tatu kwa mwaka mbele za Bwana Mungu wenu mahali atakapopachagua: kwa ajili ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, Sikukuu ya Majuma, na Sikukuu ya Vibanda. Hakuna mtu atakayejitokeza mbele za Bwana mikono mitupu: 17 Kila mmoja wenu ni lazima alete zawadi kulingana na jinsi ambavyo Bwana Mungu wenu alivyowabariki.

  26. 6 Lakini utauwa na kuridhika ni faida kubwa. 7 Kwa kuwa hatukuja humu duniani na kitu chochote, wala hatuwezi kutoka humu na kitu. 8 Lakini kama tuna chakula na mavazi, tutaridhika navyo. 9 Lakini wale watu wanaotamani kuwa na mali kwa haraka huanguka kwenye majaribu, na wamenaswa na tamaa nyingi za kipumbavu zenye kudhuru, zinazowazamisha watu katika uharibifu na maangamizi. 10 Kwa maana kupenda fedha ndiyo shina moja la maovu ya kila namna. Baadhi ya watu wakitamani fedha, wameiacha imani na kujichoma wenyewe kwa maumivu mengi.

    11 Lakini wewe, mtu wa Mungu, yakimbie mambo haya yote. Fuata haki, utauwa, imani, upendo, saburi na upole.

  27. 1 “Angalieni msitende wema wenu mbele ya watu ili wawaone. Kwa maana mkifanya hivyo, hamna thawabu kutoka kwa Baba yenu aliye mbinguni.

    2 “Hivyo mnapowapa wahitaji, msipige panda mbele yenu kama wafanyavyo wanafiki katika masinagogi na mitaani, ili wasifiwe na watu. Amin nawaambia wao wamekwisha kupokea thawabu yao. 3 Lakini ninyi mtoapo sadaka, fanyeni kwa siri, hata mkono wako wa kushoto usijue mkono wako wa kuume unachofanya, 4 ili sadaka yako iwe ni siri. Ndipo Baba yako wa mbinguni, yeye aonaye sirini atakupa thawabu kwa wazi.

  28. 35 Katika kila jambo nimewaonyesha kwamba kwa njia hii ya kufanya kazi kwa bidii imetupasa kuwasaidia wadhaifu, mkikumbuka maneno ya Bwana Yesu mwenyewe jinsi alivyosema, ‘Ni heri kutoa kuliko kupokea.’ ”

  29. 1 Basi sasa ndugu, nataka ninyi mjue kuhusu ile neema ambayo Mungu amewapa makanisa ya Makedonia. 2 Pamoja na majaribu makali na taabu walizopata, furaha waliyokuwa nayo ilikuwa kubwa, ingawa walikuwa maskini kupindukia, kwa upande wao walifurika kwa wingi wa ukarimu. 3 Kwa maana nashuhudia kwamba wao walitoa kwa kadiri wawezavyo, hata na zaidi ya uwezo wao, kwa hiari yao wenyewe, 4 wakitusihi kwa bidii wapewe fursa ya kushiriki katika huduma hii ya kuwasaidia watakatifu. 5 Wala hawakufanya tulivyotazamia, bali walijitoa wao wenyewe kwa Bwana kwanza na ndipo wakajitoa kwa ajili yetu, kufuatana na mapenzi ya Mungu.

  30. 6 Basi, yeye afundishwaye katika neno na amshirikishe mwalimu wake mema yote.

    7 Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi. Kwa kuwa kile apandacho mtu ndicho atakachovuna. 8 Apandaye kwa mwili, katika mwili wake atavuna uharibifu, lakini yeye apandaye katika Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele. 9 Hivyo, tusichoke katika kutenda mema, kwa kuwa tutavuna kwa wakati wake tusipokata tamaa. 10 Kwa hiyo, kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema, hasa wale wa jamaa ya waaminio.

  31. 10 Pia niligundua kuwa mafungu yaliyopangwa kupewa Walawi hawakuwa wamepewa, nao Walawi wote na waimbaji waliowajibika kwa huduma walikuwa wamerudi katika mashamba yao.

  32. 15 Ataichukua sehemu ya kumi ya nafaka yenu na ya zabibu zenu na kuwapa maafisa wake na watumishi wake.

  33. 2 Ndipo Mose akawaita Bezaleli na Oholiabu na kila mtu mwenye ustadi ambaye Bwana alikuwa amempa uwezo na mwenye kupenda kuja na kufanya kazi. 3 Wakapokea kutoka kwa Mose sadaka zote ambazo Waisraeli walikuwa wameleta ili kuifanya kazi ya ujenzi wa Mahali Patakatifu. Nao watu wakaendelea kuleta sadaka za hiari kila asubuhi. 4 Ikafika wakati mafundi wote wenye ujuzi waliokuwa wakiifanya kazi yote ya mahali patakatifu wakasimamisha kazi zao, 5 wakaja na kumwambia Mose, “Watu wanaleta vitu vingi kuliko tunavyohitaji kwa ajili ya kazi hii ambayo Bwana ameagiza ifanyike.”

    6 Ndipo Mose akatoa agizo, nao wakapeleka neno hili katika kambi yote: “Mtu yeyote mwanaume au mwanamke asilete tena kitu chochote kwa ajili ya sadaka ya mahali patakatifu.” Hivyo watu wakazuiliwa kuleta zaidi, 7 kwa sababu walivyokuwa navyo tayari vilitosha na kuzidi kuifanya kazi yote.

  34. 17 Waagize wale ambao ni matajiri wa ulimwengu huu waache kujivuna, wala wasiweke tumaini lao katika mali ambayo si ya hakika, bali waweke tumaini lao katika Mungu ambaye hutupatia vitu vyote kwa wingi ili tuvifurahie. 18 Waagize watende mema, wawe matajiri katika matendo mema, pia wawe wakarimu na walio tayari kushiriki mali zao na wengine. 19 Kwa njia hii watajiwekea hazina kama msingi kwa ajili ya wakati ujao na hivyo watajipatia uzima, yaani, ule uzima ambao ni wa kweli.

  35. 10 Kisha msherehekee Sikukuu ya Majuma kwa Bwana Mungu wenu kwa kutoa sadaka ya hiari kwa kadiri ya baraka ambayo Bwana Mungu wenu amewapa.

  36. 1 Makuhani ambao ni Walawi, yaani kabila lote la Lawi, hawatakuwa na mgawo wala urithi pamoja na Israeli. Wataishi kwa sadaka zitolewazo kwa ajili ya Bwana za kuteketezwa kwa moto, kwa maana huo ndio urithi wao. 2 Hawatakuwa na urithi miongoni mwa ndugu zao; Bwana ndiye urithi wao, kama alivyowaahidi.

    3 Hili ndilo fungu la makuhani kutoka kwa watu watakaotoa dhabihu ya fahali au kondoo: mguu wa mbele, mataya na matumbo. 4 Mtawapa malimbuko ya nafaka zenu, divai mpya, mafuta na sufu ya kwanza kutoka manyoya ya kondoo zenu, 5 kwa kuwa Bwana Mungu wenu amewachagua pamoja na wazao wao kutoka makabila yenu kusimama na kuhudumu katika jina la Bwana siku zote.

  37. 15 Zaidi ya hayo, ninyi Wafilipi mnajua kwamba siku za kwanza nilipoanza kuhubiri Injili, nilipoondoka Makedonia, hakuna kanisa jingine lililoshiriki nami katika masuala ya kutoa na kupokea isipokuwa ninyi. 16 Kwa maana hata nilipokuwa huko Thesalonike, mliniletea msaada kwa ajili ya mahitaji yangu zaidi ya mara moja. 17 Si kwamba natafuta sana yale matoleo, bali natafuta sana ile faida itakayozidi sana kwa upande wenu. 18 Nimelipwa kikamilifu hata na zaidi; nimetoshelezwa kabisa sasa, kwa kuwa nimepokea kutoka kwa Epafrodito vile vitu mlivyonitumia, sadaka yenye harufu nzuri, dhabihu inayokubalika na ya kumpendeza Mungu. 19 Naye Mungu wangu atawajaza ninyi na kila mnachohitaji kwa kadiri ya utajiri wake katika utukufu ndani ya Kristo Yesu.

    20 Mungu wetu aliye Baba yetu apewe utukufu milele na milele. Amen.

  38. 15 Basi kwa njia ya Yesu, tuzidi kumtolea Mungu dhabihu ya sifa, yaani matunda ya midomo inayolikiri Jina lake. 16 Na msiache kutenda mema na kushirikiana vile vitu mlivyo navyo, kwa kuwa dhabihu kama hizo ndizo zinazompendeza Mungu.

  39. 6 Kwa sababu hii mnalipa kodi, kwa maana watawala ni watumishi wa Mungu, ambao hutumia muda wao wote kutawala. 7 Mlipeni kila mtu kile mnachodaiwa. Kama mnadaiwa kodi lipeni kodi, kama ni ushuru, lipeni ushuru, astahiliye hofu, mhofu, astahiliye heshima, mheshimu.

  40. 16 Kwa namna hii twaweza kulijua pendo la Mungu: Kwa sababu Yesu Kristo aliutoa uhai wake kwa ajili yetu. Nasi imetupasa kuutoa uhai kwa ajili ya hao ndugu. 17 Ikiwa mtu anavyo vitu vya ulimwengu huu na akamwona ndugu yake ni mhitaji lakini asimhurumie, upendo wa Mungu wakaaje ndani ya mtu huyo? 18 Watoto wapendwa, tusipende kwa maneno au kwa ulimi bali kwa tendo na kweli. 19 Basi hivi ndivyo tutakavyoweza kujua ya kuwa sisi tu wa kweli na hivyo twaithibitisha mioyo yetu mbele za Mungu

  41. 31 “Mwana wa Adamu atakapokuja katika utukufu wake na malaika wote watakatifu pamoja naye, ndipo atakapoketi juu ya kiti cha enzi cha utukufu wake. 32 Mataifa yote watakusanyika mbele zake, naye atawatenga kama mchungaji anavyotenga kondoo na mbuzi. 33 Atawaweka kondoo upande wake wa kuume, na mbuzi upande wake wa kushoto.

    34 “Ndipo Mfalme atawaambia wale walioko upande wake wa kuume, ‘Njooni, ninyi mliobarikiwa na Baba yangu; urithini Ufalme ulioandaliwa kwa ajili yenu tangu kuumbwa kwa ulimwengu. 35 Kwa maana nilikuwa na njaa mkanipa chakula, nilikuwa na kiu mkaninywesha, nilikuwa mgeni mkanikaribisha, 36 nilikuwa uchi mkanivika, nilikuwa mgonjwa mkanitunza, nami nilikuwa kifungoni mkaja kunitembelea.’

    37 “Ndipo wale wenye haki watakapomjibu, ‘Bwana, ni lini tulikuona ukiwa na njaa tukakulisha, au ukiwa na kiu tukakunywesha? 38 Lini tulikuona ukiwa mgeni tukakukaribisha, au ukiwa uchi tukakuvika? 39 Tena ni lini tulikuona ukiwa mgonjwa tukakutunza, au ukiwa kifungoni tukakutembelea?’

    40 “Naye Mfalme atawajibu, ‘Amin nawaambia, kwa jinsi mlivyomtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.’

    41 “Kisha atawaambia wale walio upande wake wa kushoto, ‘Ondokeni kwangu, ninyi mliolaaniwa, nendeni kwenye moto wa milele ulioandaliwa kwa ajili ya ibilisi na malaika zake. 42 Kwa maana nilikuwa na njaa hamkunipa chakula, nilikuwa na kiu hamkuninywesha, 43 nilikuwa mgeni nanyi hamkunikaribisha, nilikuwa uchi hamkunivika, nilikuwa mgonjwa hamkunitunza, na nilikuwa gerezani nanyi hamkuja kunitembelea.’

    44 “Ndipo wao pia watajibu, ‘Bwana ni lini tulikuona ukiwa na njaa au kiu, au ukiwa mgeni au uchi, au ukiwa mgonjwa na kifungoni na hatukukuhudumia?’

    45 “Naye atawajibu, ‘Amin nawaambia, kwa jinsi ambavyo hamkumtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu walio wadogo, hamkunitendea mimi.’

    46 “Ndipo hawa watakapoingia kwenye adhabu ya milele, lakini wale wenye haki wataingia katika uzima wa milele.”

  42. 33 Uzeni mali zenu mkawape maskini. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, mkajiwekee hazina mbinguni isiyokwisha, mahali ambapo mwizi hakaribii wala nondo haharibu. 34 Kwa sababu mahali hazina yako ilipo, hapo ndipo moyo wako utakapokuwa pia.

  43. 42 Nao wakawa wanadumu katika mafundisho ya mitume, katika ushirika, katika kumega mkate na katika kusali. 43 Kila mtu akaingiwa na hofu ya Mungu, nayo miujiza mingi na ishara zikafanywa na mitume. 44 Walioamini wote walikuwa mahali pamoja, nao walikuwa na kila kitu shirika. 45 Waliuza mali zao na vitu walivyokuwa navyo, kila mtu akagawiwa kadiri ya mahitaji yake.

  44. 32 Wale walioamini wote walikuwa na moyo mmoja na nia moja. Wala hakuna hata mmoja aliyesema chochote alichokuwa nacho ni mali yake mwenyewe, lakini walishirikiana kila kitu walichokuwa nacho. 33 Mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwa Bwana Yesu kwa nguvu nyingi na neema ya Mungu ilikuwa juu yao wote. 34 Wala hapakuwepo mtu yeyote miongoni mwao aliyekuwa mhitaji, kwa sababu mara kwa mara wale waliokuwa na mashamba na nyumba waliviuza, wakaleta thamani ya vitu vilivyouzwa, 35 wakaiweka miguuni pa mitume, kila mtu akagawiwa kadiri ya mahitaji yake.

  45. 10 Mungu si mdhalimu: yeye hataisahau kazi yenu na upendo ule mlioonyesha kwa ajili yake katika kuwahudumia watakatifu na hata sasa mnaendelea kuwahudumia.