63 Bible Verses About Being In Love
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
-
1 Wimbo ulio bora wa Solomoni.
Mpendwa
2 Unibusu kwa busu la kinywa chako,
kwa maana upendo wako unafurahisha kuliko divai.
3 Manukato yako yananukia vizuri,
jina lako ni kama manukato yaliyomiminwa.
Ndiyo sababu wanawali wanakupenda!
4 Nichukue twende nawe, na tufanye haraka!
Mfalme na anilete ndani ya vyumba vyake.
Marafiki
Tunakushangilia na kukufurahia,
tutasifu upendo wako zaidi kuliko divai.
Mpendwa
Tazama jinsi ilivyo bora wakupende!
5 Mimi ni mweusi, lakini napendeza,
enyi binti za Yerusalemu,
mweusi kama mahema ya Kedari,
kama mapazia ya hema la Solomoni.
6 Usinikazie macho kwa sababu mimi ni mweusi,
kwa sababu nimefanywa mweusi na jua.
Wana wa mama yangu walinikasirikia
na kunifanya niwe mtunza mashamba ya mizabibu.
Shamba langu mwenyewe la mizabibu nimeliacha.
7 Niambie, wewe ambaye ninakupenda,
unalisha wapi kundi lako la kondoo
na ni wapi unapowapumzisha kondoo wako adhuhuri.
Kwa nini niwe kama mwanamke aliyefunikwa shela
karibu na makundi ya rafiki zako?
Marafiki
8 Kama hujui, ewe mwanamke mzuri kuliko wote,
fuata nyayo za kondoo,
na kulisha wana-mbuzi wako
karibu na hema za wachungaji.
-
Marafiki
5 Ni nani huyu anayekuja kutoka nyikani
akimwegemea mpenzi wake?
Mpendwa
Nilikuamsha chini ya mtofaa,
huko mama yako alipotunga mimba yako,
huko yeye alipata utungu akakuzaa.
6 Nitie kama muhuri moyoni mwako,
kama muhuri kwenye mkono wako;
kwa maana upendo una nguvu kama mauti,
wivu wake ni mkatili kama kuzimu.
Unachoma kama mwali wa moto,
kama mwali mkubwa wa moto wa Bwana hasa.
7 Maji mengi hayawezi kuuzimisha upendo,
mito haiwezi kuugharikisha.
Kama mtu angelitoa mali yote ya nyumbani mwake
kwa ajili ya upendo,
angelidharauliwa kabisa.
Marafiki
8 Tunaye dada mdogo,
matiti yake hayajakua bado.
Tutafanya nini kwa ajili ya dada yetu
wakati atakapokuja kuposwa?
9 Kama yeye ni ukuta,
tutajenga minara ya fedha juu yake.
Na kama yeye ni mlango,
tutamzungushia mbao za mierezi.
Mpendwa
10 Mimi ni ukuta,
nayo matiti yangu ni kama minara.
Ndivyo ambavyo nimekuwa machoni pake
kama yule anayeleta utoshelevu.
11 Solomoni alikuwa na shamba la mizabibu huko Baal-Hamoni;
alikodisha shamba lake la mizabibu kwa wapangaji.
Kila mmoja angeleta kwa ajili ya matunda yake
shekeli 1,000 za fedha.
12 Lakini shamba langu la mizabibu
ambalo ni langu mwenyewe
ni langu kutoa;
hizo shekeli 1,000 ni kwa ajili yako, ee Solomoni,
na shekeli mia mbili ni kwa ajili
ya wale wanaotunza matunda yake.
-
1 Usiku kucha kwenye kitanda changu
nilimtafuta yule moyo wangu umpendaye;
nilimtafuta, lakini sikumpata.
2 Sasa nitaondoka na kuzunguka mjini,
katika barabara zake na viwanja;
nitamtafuta yule moyo wangu umpendaye.
Kwa hiyo nilimtafuta lakini sikumpata.
3 Walinzi walinikuta
walipokuwa wakizunguka mji.
Nikawauliza, “Je, mmemwona
yule moyo wangu umpendaye?”
4 Kitambo kidogo tu baada ya kuwapita
nilimpata yule moyo wangu umpendaye.
Nilimshika na sikumwachia aende
mpaka nilipomleta katika nyumba ya mama yangu,
katika chumba cha yule aliyenichukua mimba.
5 Binti za Yerusalemu, ninawaagiza
kwa paa na kwa ayala wa shambani:
Msichochee wala kuamsha mapenzi
hata yatakapotaka yenyewe.
-
Mpenzi
6 Ni nani huyu anayekuja kutoka jangwani
kama nguzo ya moshi,
anayenukia manemane na uvumba
iliyotengenezwa kwa vikolezo vyote
vya mfanyabiashara?
7 Tazama! Ni gari la Solomoni
lisindikizwalo na mashujaa sitini,
walio wakuu sana wa Israeli,
8 wote wamevaa panga,
wote wazoefu katika vita,
kila mmoja na upanga wake pajani,
wamejiandaa kwa ajili ya hofu za usiku.
9 Mfalme Solomoni alijitengenezea gari;
alilitengeneza kwa mbao kutoka Lebanoni.
10 Nguzo zake alizitengeneza kwa fedha,
kitako chake kwa dhahabu.
Kiti chake kilipambwa kwa zambarau,
gari lake likanakshiwa njumu kwa upendo
na binti za Yerusalemu.
11 Tokeni nje, ninyi binti za Sayuni,
mkamtazame Mfalme Solomoni akiwa amevaa taji,
taji ambalo mama yake alimvika
siku ya arusi yake,
siku ambayo moyo wake ulishangilia.
-
Mpenzi
4 Wewe ni mzuri, mpenzi wangu, kama Tirsa,
upendezaye kama Yerusalemu,
umetukuka kama jeshi lenye bendera.
5 Uyageuze macho yako mbali nami,
yananigharikisha.
Nywele zako ni kama kundi la mbuzi
wanaoteremka kutoka Gileadi.
6 Meno yako ni kama kundi la kondoo
watokao kuogeshwa.
Kila mmoja ana pacha lake,
hakuna hata mmoja aliye peke yake.
7 Mashavu yako nyuma ya shela yako
ni kama vipande viwili vya komamanga.
8 Panaweza kuwepo malkia sitini,
masuria themanini
na mabikira wasiohesabika;
9 lakini hua wangu, mkamilifu wangu,
ni wa namna ya pekee,
binti pekee kwa mama yake,
kipenzi cha yeye aliyemzaa.
Wanawali walimwona na kumwita aliyebarikiwa;
malkia na masuria walimsifu.
Marafiki
10 Ni nani huyu atokeaye kama mapambazuko,
mzuri kama mwezi, mwangavu kama jua,
ametukuka kama nyota zifuatanazo?
-
9 na kinywa chako kama divai
bora kuliko zote.
Mpendwa
Divai na iende moja kwa moja hadi kwa mpenzi wangu,
ikitiririka polepole juu ya midomo na meno.
10 Mimi ni mali ya mpenzi wangu,
nayo shauku yake ni juu yangu.
11 Njoo, mpenzi wangu, twende mashambani,
twende tukalale huko vijijini.
12 Hebu na twende mapema
katika mashamba ya mizabibu
tuone kama mizabibu imechipua,
kama maua yake yamefunguka,
na kama mikomamanga imetoa maua:
huko nitakupa penzi langu.
13 Mitunguja hutoa harufu zake nzuri,
kwenye milango yetu kuna matunda mazuri,
mapya na ya zamani,
ambayo nimekuhifadhia wewe,
mpenzi wangu.
-
10 Mpenzi wangu alizungumza na kuniambia,
“Inuka, mpenzi wangu,
mrembo wangu, tufuatane.
11 Tazama! Wakati wa masika umepita,
mvua imekwisha na ikapita.
12 Maua yanatokea juu ya nchi;
majira ya kuimba yamewadia,
sauti za njiwa zinasikika
katika nchi yetu.
13 Mtini unatunga matunda yake ya mwanzoni,
zabibu zinazochanua zaeneza harufu nzuri.
Inuka, njoo mpenzi wangu.
Mrembo wangu, tufuatane.”
Mpenzi
14 Hua wangu penye nyufa za majabali,
mafichoni pembezoni mwa mlima,
nionyeshe uso wako,
na niisikie sauti yako,
kwa maana sauti yako ni tamu,
na uso wako unapendeza.
15 Tukamatie mbweha,
mbweha wale wadogo
wanaoharibu mashamba ya mizabibu,
mashamba yetu ya mizabibu yaliyochanua.
-
12 Wewe ni bustani iliyofungwa, dada yangu,
bibi arusi wangu;
wewe ni chanzo cha maji kilichozungushiwa kabisa,
chemchemi yangu peke yangu.
13 Mimea yako ni bustani ya mikomamanga
yenye matunda mazuri sana,
yenye hina na nardo,
14 nardo na zafarani,
mchai na mdalasini,
pamoja na kila aina ya mti wa uvumba,
manemane na udi,
na aina zote za vikolezo bora kuliko vyote.
15 Wewe ni chemchemi ya bustani,
kisima cha maji yatiririkayo,
yakitiririka kutoka Lebanoni.
Mpendwa
16 Amka, upepo wa kaskazini,
na uje, upepo wa kusini!
Vuma juu ya bustani yangu,
ili harufu yake nzuri iweze kuenea mpaka ngʼambo.
Mpendwa wangu na aje bustanini mwake
na kuonja matunda mazuri sana.
-
4 Mpenzi wangu aliweka mkono wake kwenye tundu la komeo;
moyo wangu ulianza kugonga kwa ajili yake.
5 Niliinuka kumfungulia mpenzi wangu,
mikono yangu ikidondosha manemane,
vidole vyangu vikitiririka manemane,
penye vipini vya komeo.
6 Nilimfungulia mpenzi wangu,
lakini mpenzi wangu alishaondoka;
alikuwa amekwenda zake.
Moyo wangu ulishuka kwa kuondoka kwake.
Nilimtafuta lakini sikumpata.
Nilimwita lakini hakunijibu.
7 Walinzi walinikuta
walipokuwa wakifanya zamu za ulinzi mjini.
Walinipiga, wakanijeruhi,
wakaninyangʼanya joho langu,
hao walinzi wa kuta!
8 Enyi binti za Yerusalemu, ninawaagiza:
kama mkimpata mpenzi wangu,
mtamwambia nini?
Mwambieni ninazimia kwa mapenzi.
-
Marafiki
1 Mpenzi wako amekwenda wapi,
ewe mzuri kupita wanawake wote?
Mpenzi wako amegeukia njia ipi,
tupate kumtafuta pamoja nawe?
Mpendwa
2 Mpenzi wangu amekwenda bustanini mwake,
kwenye vitalu vya vikolezo,
kujilisha bustanini
na kukusanya yungiyungi.
3 Mimi ni wake mpenzi wangu,
na mpenzi wangu ni wangu;
yeye hujilisha katikati ya yungiyungi.
-
Mpenzi
11 Niliteremka kwenye bustani ya miti ya milozi
ili kutazama machipuko ya bondeni,
kuona kama mizabibu imechipua
au kama mikomamanga imechanua maua.
12 Kabla sijangʼamua,
shauku yangu iliniweka
katikati ya magari ya kifalme ya kukokotwa na farasi ya watu wangu.
Marafiki
13 Rudi, rudi, ee Mshulami;
rudi, rudi ili tupate kukutazama!
Mpenzi
Kwa nini kumtazama Mshulami,
kama kutazama ngoma ya Mahanaimu?
-
1 Laiti ungelikuwa kwangu kama ndugu wa kiume,
ambaye aliyanyonya matiti ya mama yangu!
Kisha, kama ningekukuta huko nje,
ningelikubusu,
wala hakuna mtu yeyote angelinidharau.
2 Ningelikuongoza na kukuleta
katika nyumba ya mama yangu,
yeye ambaye amenifundisha.
Ningelikupa divai iliyokolezwa unywe,
asali ya maua ya mikomamanga yangu.
3 Mkono wake wa kushoto uko chini ya kichwa changu,
na mkono wake wa kuume unanikumbatia.
4 Binti za Yerusalemu, ninawaagiza:
msichochee wala kuamsha mapenzi
hata yatakapotaka yenyewe.
-
29 Mungu akampa Solomoni hekima na akili kubwa, pia ufahamu mpana usiopimika kama mchanga ulioko pwani ya bahari. 30 Hekima ya Solomoni ilikuwa kubwa kuliko hekima ya watu wote wa Mashariki na kubwa kuliko hekima yote ya Misri. 31 Alikuwa na hekima kuliko kila mwandishi, akiwemo Ethani Mwezrahi: kuliko Hemani, Kalkoli na Darda, wana wa Maholi. Umaarufu wake ukaenea kwa mataifa yote yaliyomzunguka. 32 Akanena mithali 3,000 na nyimbo zake zilikuwa 1,005. 33 Akaelezea maisha ya mimea kuanzia mwerezi wa Lebanoni hadi hisopo iotayo ukutani. Pia akafundisha kuhusu wanyama na ndege, wanyama wenye damu baridi, wakiwemo samaki. 34 Watu wa mataifa yote wakaja kusikiliza hekima ya Solomoni, waliotumwa na wafalme wote wa ulimwengu, waliokuwa wamesikia juu ya hekima yake.
-
Mpenzi
9 Mpenzi wangu, ninakufananisha na farasi jike
aliyefungwa katika mojawapo ya magari ya vita ya Farao.
10 Mashavu yako yanapendeza yakiwa na vipuli,
shingo yako ikiwa na mikufu ya vito.
11 Tutakufanyia vipuli vya dhahabu,
vyenye kupambwa kwa fedha.
Mpendwa
12 Wakati mfalme alipokuwa mezani pake,
manukato yangu yalisambaza harufu yake nzuri.
13 Mpenzi wangu kwangu mimi ni kifuko cha manemane
kati ya matiti yangu.
14 Mpenzi wangu kwangu mimi ni kama kishada cha maua ya mhina
kutoka mashamba ya mizabibu ya En-Gedi.
-
4 Amenichukua mpaka kwenye ukumbi wa karamu,
na bendera ya huyu mwanaume
juu yangu ni upendo.
5 Nitie nguvu kwa zabibu kavu,
niburudishe kwa matofaa,
kwa maana ninazimia kwa mapenzi.
-
Mpendwa
16 Mpenzi wangu ni wangu, nami ni wake,
yeye hujilisha katikati ya yungiyungi.
17 Mpaka jua linapochomoza,
na vivuli vikimbie,
rudi, mpenzi wangu,
na uwe kama paa,
au kama ayala kijana
juu ya vilima vya Betheri.
-
Mpenzi
1 Tazama jinsi ulivyo mzuri, mpenzi wangu!
Ee, jinsi ulivyo mzuri!
Macho yako nyuma ya shela yako
ni kama ya hua.
Nywele zako ni kama kundi la mbuzi
zikishuka kutoka Mlima Gileadi.
2 Meno yako ni kama kundi la kondoo waliokatwa manyoya sasa hivi,
watokao kuogeshwa.
Kila mmoja ana pacha lake,
hakuna hata mmoja aliye peke yake.
3 Midomo yako ni kama uzi mwekundu,
kinywa chako kinapendeza.
Mashavu yako nyuma ya shela yako
ni kama vipande viwili vya komamanga.
4 Shingo yako ni kama mnara wa Daudi,
uliojengwa kwa madaha,
juu yake zimetundikwa ngao elfu,
zote ni ngao za mashujaa.
5 Matiti yako mawili ni kama wana-paa wawili,
kama wana-paa mapacha
wajilishao katikati ya yungiyungi.
-
1 Ee binti wa mwana wa mfalme,
tazama jinsi inavyopendeza miguu yako katika viatu!
Miguu yako yenye madaha ni kama vito vya thamani,
kazi ya mikono ya fundi stadi.
2 Kitovu chako ni kama bilauri ya mviringo
ambayo kamwe haikosi divai iliyochanganywa.
Kiuno chako ni kichuguu cha ngano
kilichozungukwa kwa yungiyungi.
3 Matiti yako ni kama wana-paa wawili,
mapacha wa paa.
4 Shingo yako ni kama mnara wa pembe ya ndovu.
Macho yako ni vidimbwi vya Heshboni
karibu na lango la Beth-Rabi.
Pua lako ni kama mnara wa Lebanoni
ukitazama kuelekea Dameski.
5 Kichwa chako kinakuvika taji kama mlima Karmeli.
Nywele zako ni kama zulia la urujuani;
mfalme ametekwa na mashungi yake.
6 Tazama jinsi ulivyo mzuri na unavyopendeza,
ee pendo, kwa uzuri wako!
7 Umbo lako ni kama la mtende,
nayo matiti yako kama vishada vya matunda.
8 Nilisema, “Nitakwea mtende,
nami nitayashika matunda yake.”
Matiti yako na yawe kama vishada vya mzabibu,
harufu nzuri ya pumzi yako kama matofaa,
-
10 Tazama jinsi pendo lako linavyofurahisha,
dada yangu, bibi arusi wangu!
Pendo lako linafurahisha aje zaidi ya divai,
na harufu ya manukato yako zaidi ya kikolezo chochote!
11 Midomo yako inadondosha utamu kama sega la asali,
bibi arusi wangu;
maziwa na asali viko chini ya ulimi wako.
Harufu nzuri ya mavazi yako ni kama ile ya Lebanoni.
-
Mpenzi
13 Wewe ukaaye bustanini
pamoja na marafiki mliohudhuria,
hebu nisikie sauti yako!
Mpendwa
14 Njoo, mpenzi wangu,
uwe kama swala
au kama ayala kijana
juu ya milima iliyojaa vikolezo.
-
16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. 17 Kwa maana Mungu hakumtuma Mwanawe kuuhukumu ulimwengu, bali kupitia kwake ulimwengu upate kuokolewa.
-
1 Hata hivyo, Mfalme Solomoni akawapenda wanawake wengi wa kigeni zaidi, mbali na binti Farao: wanawake wa Wamoabu, Waamoni, Waedomu, Wasidoni na Wahiti. 2 Walitoka katika mataifa ambayo Bwana aliwaambia Waisraeli, “Msije mkaoana nao, kwa kuwa hakika wataigeuza mioyo yenu mgeukie miungu yao.” Hata hivyo, Solomoni akakaza kuwapenda. 3 Alikuwa na wake 700 mabinti wa uzao wa kifalme, na masuria 300, nao wake zake wakampotosha. 4 Kadiri Solomoni alivyozidi kuzeeka, wake zake wakaugeuza moyo wake kuelekea miungu mingine, na moyo wake haukujitolea kikamilifu kwa Bwana Mungu wake, kama ulivyokuwa moyo wa Daudi baba yake.
-
Mpendwa
1 Mimi ni ua la Sharoni,
yungiyungi ya bondeni.
Mpenzi
2 Kama yungiyungi katikati ya miiba
ndivyo alivyo mpenzi wangu katikati ya wanawali.
-
7 Binti za Yerusalemu, ninawaagiza
kwa paa na kwa ayala wa shambani:
Msichochee wala kuamsha mapenzi
hata yatakapotaka yenyewe.
-
4 Upendo huvumilia, upendo hufadhili, upendo hauoni wivu, hauna majivuno, hauna kiburi. 5 Haukosi kuwa na adabu, hautafuti mambo yake, haukasiriki upesi, hauweki kumbukumbu ya mabaya. 6 Upendo haufurahii mabaya bali hufurahi pamoja na kweli. 7 Upendo huvumilia yote, huamini yote, hutumaini yote, hustahimili yote.
8 Upendo haushindwi kamwe. Lakini ukiwepo unabii, utakoma; zikiwepo lugha, zitakoma; yakiwepo maarifa, yatapita.
-
25 Ninyi waume, wapendeni wake zenu, kama vile Kristo alivyolipenda Kanisa akajitoa kwa ajili yake 26 kusudi alifanye takatifu, akilitakasa kwa kuliosha kwa maji katika Neno lake, 27 apate kujiletea Kanisa tukufu lisilo na doa wala kunyanzi au waa lolote, bali takatifu na lisilo na hatia. 28 Vivyo hivyo imewapasa waume kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe. 29 Hakuna mtu anayeuchukia mwili wake mwenyewe, bali huulisha na kuutunza vizuri, kama Kristo anavyolitunza Kanisa lake. 30 Sisi tu viungo vya mwili wake. 31 “Kwa sababu hii, mwanaume atamwacha baba yake na mama yake, naye ataambatana na mkewe, na hao wawili watakuwa mwili mmoja.” 32 Siri hii ni kubwa, bali mimi nanena kuhusu Kristo na Kanisa. 33 Hata hivyo, kila mmoja wenu ampende mkewe kama anavyoipenda nafsi yake mwenyewe, naye mke lazima amheshimu mumewe.
-
12 Kwa hiyo, kwa kuwa ninyi mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao sana, jivikeni moyo wa huruma, utu wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu. 13 Vumilianeni na kusameheana mtu akiwa na lalamiko lolote dhidi ya mwenzake. Sameheaneni kama vile Bwana alivyowasamehe ninyi. 14 Zaidi ya maadili haya yote jivikeni upendo, ambao ndio unaofunga kila kitu pamoja katika umoja mkamilifu.
15 Amani ya Kristo na itawale mioyoni mwenu, kwa kuwa ninyi kama viungo vya mwili mmoja mmeitiwa amani. Tena kuweni watu wa shukrani. 16 Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu, mkifundishana na kuonyana katika hekima yote, mkimwimbia Mungu zaburi, nyimbo na tenzi za rohoni, huku mkiwa na shukrani mioyoni mwenu. 17 Lolote mfanyalo, ikiwa ni kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba katika yeye.
-
8 Enda nami kutoka Lebanoni, bibi arusi wangu,
enda nami kutoka Lebanoni.
Shuka kutoka ncha ya Amana,
kutoka juu ya Seniri, kilele cha Hermoni,
kutoka mapango ya simba
na kutoka mlima wapendapo kukaa chui.
9 Umeiba moyo wangu, dada yangu, bibi arusi wangu;
umeiba moyo wangu
kwa mtazamo mmoja wa macho yako,
kwa kito kimoja cha mkufu wako.
-
Mpendwa
2 Nililala lakini moyo wangu ulikuwa macho.
Sikiliza! Mpenzi wangu anabisha:
“Nifungulie, dada yangu, mpenzi wangu,
hua wangu, asiye na hitilafu.
Kichwa changu kimeloa umande,
na nywele zangu manyunyu ya usiku.”
3 Nimevua joho langu:
je, ni lazima nivae tena?
Nimenawa miguu yangu:
je, ni lazima niichafue tena?
-
16 Hivyo nasi twajua na kulitumainia pendo la Mungu alilo nalo kwa ajili yetu.
Mungu ni Upendo. Kila akaaye katika upendo hukaa ndani ya Mungu na Mungu hukaa ndani yake. 17 Kwa njia hii, pendo hukamilishwa miongoni mwetu ili tupate kuwa na ujasiri katika siku ya hukumu, kwa sababu kama alivyo ndivyo tulivyo sisi katika ulimwengu huu. 18 Katika pendo hakuna hofu. Lakini pendo lililo kamili huitupa nje hofu, kwa sababu hofu inahusika na adhabu. Kila mwenye hofu hakukamilika katika pendo.
19 Twampenda yeye kwa sababu yeye alitupenda kwanza. 20 Ikiwa mtu atasema, “Nampenda Mungu,” lakini anamchukia ndugu yake, yeye ni mwongo. Kwa maana kila mtu asiyempenda ndugu yake ambaye anamwona, atampendaje Mungu asiyemuona? 21 Naye ametupa amri hii: Yeyote anayempenda Mungu lazima pia ampende ndugu yake.
-
Mpenzi
1 Nimekuja kwenye bustani yangu, dada yangu,
bibi arusi wangu;
nimekusanya manemane yangu pamoja
na kikolezo changu.
Nimekula sega langu la asali na asali yangu;
nimekunywa divai yangu na maziwa yangu.
Marafiki
Kuleni, enyi marafiki, mnywe;
kunyweni ya kutosha, ee wapenzi.
-
37 Yesu akamjibu, “ ‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote na kwa akili zako zote.’ 38 Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. 39 Nayo ya pili ni kama hiyo, nayo ni hii: ‘Mpende jirani yako kama nafsi yako.’ 40 Amri hizi mbili ndizo msingi wa Sheria na Manabii.”
-
16 Kwa namna hii twaweza kulijua pendo la Mungu: Kwa sababu Yesu Kristo aliutoa uhai wake kwa ajili yetu. Nasi imetupasa kuutoa uhai kwa ajili ya hao ndugu. 17 Ikiwa mtu anavyo vitu vya ulimwengu huu na akamwona ndugu yake ni mhitaji lakini asimhurumie, upendo wa Mungu wakaaje ndani ya mtu huyo? 18 Watoto wapendwa, tusipende kwa maneno au kwa ulimi bali kwa tendo na kweli. 19 Basi hivi ndivyo tutakavyoweza kujua ya kuwa sisi tu wa kweli na hivyo twaithibitisha mioyo yetu mbele za Mungu
-
7 Wapendwa, tupendane, kwa kuwa pendo latoka kwa Mungu. Kila apendaye amezaliwa na Mungu, naye anamjua Mungu. 8 Yeye asiyependa hamjui Mungu, kwa sababu Mungu ni pendo.
-
Mpenzi
15 Tazama jinsi ulivyo mzuri, mpenzi wangu!
Tazama jinsi ulivyo mzuri!
Macho yako ni kama ya hua.
Mpendwa
16 Tazama jinsi ulivyo mzuri, mpenzi wangu!
Ee, tazama jinsi unavyopendeza!
Na kitanda chetu ni cha majani mazuri.
Mpenzi
17 Nguzo za nyumba yetu ni mierezi,
na mapao yetu ni miberoshi.
-
6 Hata kupambazuke na vivuli vikimbie,
nitakwenda kwenye mlima wa manemane
na kwenye kilima cha uvumba.
7 Wewe ni mzuri kote, mpenzi wangu,
hakuna hitilafu ndani yako.
-
12 Amri yangu ndiyo hii: Mpendane kama mimi nilivyowapenda ninyi. 13 Hakuna mtu mwenye upendo mkuu kuliko huu, mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.
-
6 Kisha nikasikia sauti kama ya umati mkubwa, kama sauti ya maji mengi yaendayo kasi na kama ngurumo kubwa ya radi wakipiga kelele wakisema:
“Haleluya!
Kwa maana Bwana Mungu wetu Mwenyezi anatawala.
7 Tufurahi, tushangilie
na kumpa utukufu!
Kwa maana arusi ya Mwana-Kondoo imewadia
na bibi arusi wake amejiweka tayari.
8 Akapewa kitani safi, nyeupe
inayongʼaa, ili avae.”
(Hiyo kitani safi inawakilisha matendo ya haki ya watakatifu.)
9 Ndipo malaika akaniambia, “Andika: ‘Wamebarikiwa wale walioalikwa kwenye karamu ya arusi ya Mwana-Kondoo!’ ” Naye akaongeza kusema, “Haya ndiyo maneno ya kweli ya Mungu.”
-
23 Huyo mwanaume akasema,
“Huyu sasa ni mfupa wa mifupa yangu
na nyama ya nyama yangu,
ataitwa ‘mwanamke,’
kwa kuwa alitolewa katika mwanaume.”
24 Kwa sababu hii mwanaume atamwacha baba yake na mama yake na kuambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.
-
15 Haya ni maelezo kuhusu kazi za kulazimishwa ambazo Mfalme Solomoni, alivyowafanyiza watu ili kulijenga hekalu la Bwana, na jumba lake la kifalme, na Milo, ukuta wa Yerusalemu, Hazori, Megido na Gezeri. 16 (Farao mfalme wa Misri alikuwa ameushambulia na kuuteka mji wa Gezeri. Alikuwa ameuchoma moto. Akawaua Wakanaani waliokuwa wakikaa humo na kisha kuutoa kwa binti yake, yaani mkewe Solomoni, kama zawadi ya arusi. 17 Solomoni akaujenga tena Gezeri.) Akajenga Beth-Horoni ya Chini, 18 akajenga Baalathi na Tamari kwenye jangwa katika eneo la nchi yake, 19 vilevile miji ya ghala na miji kwa ajili ya magari yake na kwa ajili ya farasi wake: chochote alichotaka kujenga katika Yerusalemu, katika Lebanoni, na katika eneo yote aliyotawala.
-
Mpendwa
3 Kama mti wa mtofaa miongoni mwa miti ya msituni
ndivyo alivyo mpenzi wangu
miongoni mwa wanaume vijana.
Ninafurahia kuketi kivulini mwa mwanaume huyu,
na tunda lake ni tamu kwangu.
-
Mpendwa
8 Sikiliza! Mpenzi wangu!
Tazama! Huyu hapa anakuja,
akirukaruka juu milimani
akizunguka juu ya vilima.
9 Mpenzi wangu ni kama paa au ayala kijana.
Tazama! Anasimama nyuma ya ukuta wetu,
akitazama kupitia madirishani,
akichungulia kimiani.
-
16 Kinywa chake chenyewe ni utamu,
kwa ujumla yeye ni wa kupendeza.
Huyu ndiye mpenzi wangu, huyu ndiye rafiki yangu,
ee binti za Yerusalemu.
-
30 Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote.’ 31 Ya pili ndiyo hii: ‘Mpende jirani yako kama nafsi yako.’ Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi.”
32 Yule mwalimu wa sheria akamwambia Yesu, “Mwalimu, umejibu vyema kwamba Mungu ni mmoja, wala hakuna mwingine ila yeye. 33 Kumpenda Mungu kwa moyo wote na kwa akili zote na kwa nguvu zote, na kumpenda jirani kama mtu anavyojipenda mwenyewe ni bora zaidi kuliko kutoa sadaka za kuteketezwa na dhabihu zote.”
-
2 Kwa unyenyekevu wote na upole, mkiwa wavumilivu, mkichukuliana kwa upendo. 3 Jitahidini kudumisha umoja wa Roho katika kifungo cha amani.
-
8 Mungu ni shahidi wangu jinsi ninavyowaonea shauku ninyi nyote kwa huruma ya Kristo Yesu.
9 Haya ndiyo maombi yangu: kwamba upendo wenu uongezeke zaidi na zaidi katika maarifa na ufahamu wote,
-
1 Kadhalika enyi wake, watiini waume zenu, ili kama kunao wasioamini lile neno, wapate kuvutwa na mwenendo wa wake zao pasipo neno, 2 kwa kuuona utakatifu na uchaji wa Mungu katika maisha yenu. 3 Kujipamba kwenu kusiwe kwa nje tu, kama vile kusuka nywele, kuvalia vitu vilivyofanyizwa kwa dhahabu na kwa mavazi. 4 Badala yake, kujipamba kwenu kuwe katika utu wenu wa moyoni, yaani uzuri usioharibika wa roho ya upole na utulivu, ambayo ni ya thamani sana machoni pa Mungu. 5 Kwa kuwa hivi ndivyo walivyokuwa wakijipamba wanawake watakatifu wa zamani, waliomtumaini Mungu. Wao walikuwa ni watiifu kwa waume zao, 6 kama Sara alivyomtii mumewe Abrahamu, hata akamwita bwana. Ninyi ni watoto wa Sara kama mkitenda yaliyo mema, bila kuogopa jambo lolote.
-
20 Kwa hiyo Yakobo akatumika miaka saba ili kumpata Raheli, lakini ilionekana kwake kama siku chache tu kwa sababu ya upendo wake kwa Raheli.
-
18 “ ‘Usijilipizie kisasi wala kuwa na kinyongo dhidi ya mmoja wa jamaa yako, lakini mpende jirani yako kama unavyojipenda wewe mwenyewe. Mimi ndimi Bwana.
-
26 Mfalme Solomoni pia akatengeneza pia meli huko Esion-Geberi, ambayo iko karibu na Elathi katika Edomu, kwenye ukingo wa Bahari ya Shamu. 27 Naye Hiramu akawatuma watu wake; mabaharia walioijua bahari, kuhudumu katika hizo meli pamoja na watu wa Solomoni. 28 Wakasafiri kwa bahari mpaka Ofiri na kurudi na talanta 420 za dhahabu, ambazo walimkabidhi Mfalme Solomoni.
-
1 Benyamini akamzaa: Bela mzaliwa wake wa kwanza,
Ashbeli mwanawe wa pili, Ahara mwanawe wa tatu,
2 Noha mwanawe wa nne na Rafa mwanawe wa tano.
3 Wana wa Bela walikuwa:
Adari, Gera, Abihudi, 4 Abishua, Naamani, Ahoa, 5 Gera, Shefufani na Huramu.
6 Hawa ndio wazao wa Ehudi, waliokuwa viongozi wa jamaa za wale walioishi huko Geba na ambao walihamishiwa Manahathi:
-
15 Kunywa maji kutoka kwenye kisima chako mwenyewe,
maji yanayotiririka kutoka kwenye kisima chako mwenyewe.
16 Je, chemchemi zako zifurike katika barabara za mji
na vijito vyako vya maji viwanjani?
17 Na viwe vyako mwenyewe,
kamwe visishirikishwe wageni.
18 Chemchemi yako na ibarikiwe
na umfurahie mke wa ujana wako.
19 Kulungu jike apendaye, kulungu mzuri:
matiti yake na yakutosheleze siku zote,
nawe utekwe daima na upendo wake.
20 Kwa nini mwanangu, utekwe na mwanamke kahaba?
Kwa nini ukumbatie kifua cha mke wa mwanaume mwingine?
-
13 Mashavu yake ni kama matuta ya vikolezo
yakitoa manukato.
Midomo yake ni kama yungiyungi
inayodondosha manemane.
-
37 “Yeyote ampendaye baba yake au mama yake kuliko anavyonipenda mimi, hastahili kuwa wangu. Yeyote ampendaye mwanawe au binti yake kuliko anavyonipenda mimi, hastahili kuwa wangu. 38 Tena yeyote asiyeuchukua msalaba wake na kunifuata, hastahili kuwa wangu. 39 Kwa maana yeyote anayetaka kuyaokoa maisha yake atayapoteza, lakini yeyote atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu atayapata.
-
15 “Kama mnanipenda, mtazishika amri zangu.
-
6 Kwa maana hata tulipokuwa dhaifu, wakati ulipowadia, Kristo alikufa kwa ajili yetu sisi wenye dhambi. 7 Hakika, ni vigumu mtu yeyote kufa kwa ajili ya mwenye haki, ingawa inawezekana mtu akathubutu kufa kwa ajili ya mtu mwema. 8 Lakini Mungu anaudhihirisha upendo wake kwetu kwamba: Tulipokuwa tungali wenye dhambi, Kristo alikufa kwa ajili yetu.
9 Basi, kwa kuwa sasa tumehesabiwa haki kwa damu yake, si zaidi sana tutaokolewa kutoka ghadhabu ya Mungu kupitia kwake! 10 Kwa kuwa kama tulipokuwa adui wa Mungu tulipatanishwa naye kwa njia ya kifo cha Mwanawe, si zaidi sana tukiisha kupatanishwa, tutaokolewa kwa uzima wake. 11 Lakini zaidi ya hayo, pia tunafurahi katika Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kupitia kwake tumepata upatanisho.
-
9 Upendo lazima usiwe na unafiki. Chukieni lililo ovu, shikamaneni na lililo jema. 10 Pendaneni ninyi kwa ninyi kwa upendo wa ndugu. Waheshimuni na kuwatanguliza wengine.
-
9 Lakini kama hawawezi kujizuia, basi waoe na kuolewa, kwa maana ni afadhali kuoa au kuolewa kuliko kuwaka tamaa.
-
23 Ninavutwa kati ya mambo mawili: Ninatamani kuondoka nikakae pamoja na Kristo, jambo hilo ni bora zaidi. 24 Lakini kwa sababu yenu ni muhimu zaidi mimi nikiendelea kuishi katika mwili. 25 Kwa kuwa nina matumaini haya, ninajua kwamba nitaendelea kuwepo na kuwa pamoja nanyi nyote, ili mpate kukua na kuwa na furaha katika imani. 26 Ili kwamba furaha yenu iwe nyingi katika Kristo Yesu kwa ajili yangu kwa kule kuja kwangu kwenu tena.
-
12 Bwana na auongeze upendo wenu na kuuzidisha kati yenu na kwa wengine wote, kama vile tulivyo na upendo mwingi kwenu. 13 Tunamwomba Mungu aimarishe mioyo yenu ili msiwe na lawama katika utakatifu mbele za Mungu wetu aliye Baba yetu wakati wa kuja kwake Bwana Yesu pamoja na watakatifu wote.
-
8 Ingawa hamjamwona, mnampenda; tena ingawa sasa hammwoni, mnamwamini na kujawa na furaha isiyoneneka yenye utukufu usioelezeka.
-
8 Zaidi ya yote, dumuni katika upendo kwa maana upendo husitiri wingi wa dhambi.
-
4 “Lakini nina neno dhidi yako: Umeuacha upendo wako wa kwanza.
Shows Read in context, Share and Copy.