36 Bible Verses About Generosity
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
-
6 Kumbukeni kwamba: Yeyote apandaye kwa uchache pia atavuna kwa uchache, naye apandaye kwa ukarimu pia atavuna kwa ukarimu. 7 Kila mtu atoe kama anavyokusudia moyoni mwake, si kwa uchoyo au kwa kulazimishwa, kwa maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo mkunjufu. 8 Naye Mungu aweza kuwapa kila baraka kwa wingi, ili katika mambo yote kila wakati, mwe na kila kitu mnachohitaji, ili mweze kushiriki kwa wingi katika kila kazi njema.
-
9 Kwa maana mnajua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba ingawa alikuwa tajiri, kwa ajili yenu alikubali kuwa maskini, ili kwa umaskini wake ninyi mpate kuwa matajiri.
10 Ushauri wangu kuhusu lile lililo bora kwenu juu ya jambo hili ni huu: Mwaka uliopita ninyi mlikuwa wa kwanza si tu kutoa lakini pia mlikuwa na shauku ya kufanya hivyo. 11 Sasa ikamilisheni kazi hii kwa shauku kama mlivyoanza, jitoleeni kulingana na uwezo wenu. 12 Kwa kuwa kama nia ya kutoa ipo, kitolewacho kinakubalika kulingana na kile mtu alicho nacho, wala si kwa kile ambacho hana.
13 Nia yetu si kwamba wengine wasaidike wakati ninyi mnateseka, bali pawe na uwiano. 14 Kwa wakati huu, wingi wa vitu mlivyo navyo usaidie kutosheleza mahitaji yao, ili wakati wao watakapokuwa na wingi wa vitu, nao wapate kutosheleza mahitaji yenu. 15 Ndipo patakuwa na usawa, kama ilivyoandikwa: “Aliyekusanya zaidi hakuwa na ziada, wala aliyekusanya kidogo hakupungukiwa.”
-
24 Kuna mtu atoaye kwa ukarimu, hata hivyo hupata zaidi,
mwingine huzuia, lakini huwa maskini.
25 Mtu mkarimu atastawi;
yeye awaburudishaye wengine
ataburudishwa mwenyewe.
26 Watu humlaani mtu awanyimae watu nafaka,
bali baraka itamkalia kichwani kama taji
yeye aliye radhi kuiuza.
27 Yeye atafutaye mema hupata ukarimu,
bali ubaya huja kwake yeye autafutaye.
28 Yeyote ategemeaye utajiri wake ataanguka,
bali mwenye haki atastawi kama jani bichi.
-
34 Tena mnapowakopesha wale tu mnaotegemea wawalipe, mwapata sifa gani? Hata ‘wenye dhambi’ huwakopesha ‘wenye dhambi’ wenzao wakitarajia kulipwa mali yao yote. 35 Lakini wapendeni adui zenu, watendeeni mema, wakopesheni bila kutegemea kurudishiwa mlichokopesha. Ndipo thawabu yenu itakapokuwa kubwa, nanyi mtakuwa wana wa Aliye Juu Sana, kwa sababu yeye ni mwema kwa watu wasio na shukrani na kwa wale waovu. 36 Kuweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma.
37 “Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa. Msilaumu, nanyi hamtalaumiwa. Sameheni, nanyi mtasamehewa. 38 Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa. Kipimo cha kujaa na kushindiliwa na kusukwasukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile mpimacho, ndicho mtakachopimiwa.”
-
8 “Je, mwanadamu atamwibia Mungu? Hata hivyo mnaniibia mimi.
“Lakini mnauliza, ‘Tunakuibia kwa namna gani?’
“Mnaniibia zaka na dhabihu. 9 Mko chini ya laana, ninyi taifa lote, kwa sababu mnaniibia mimi. 10 Leteni zaka kamili ghalani, ili kuwe na chakula katika nyumba yangu. Nijaribuni katika hili,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote, “nanyi mwone kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni na kuwamwagieni baraka nyingi mpaka mkose nafasi ya kutosha.
-
1 “Angalieni msitende wema wenu mbele ya watu ili wawaone. Kwa maana mkifanya hivyo, hamna thawabu kutoka kwa Baba yenu aliye mbinguni.
2 “Hivyo mnapowapa wahitaji, msipige panda mbele yenu kama wafanyavyo wanafiki katika masinagogi na mitaani, ili wasifiwe na watu. Amin nawaambia wao wamekwisha kupokea thawabu yao. 3 Lakini ninyi mtoapo sadaka, fanyeni kwa siri, hata mkono wako wa kushoto usijue mkono wako wa kuume unachofanya, 4 ili sadaka yako iwe ni siri. Ndipo Baba yako wa mbinguni, yeye aonaye sirini atakupa thawabu kwa wazi.
-
41 Kisha Yesu akaketi mkabala na sehemu ambapo sadaka zilikuwa zinawekwa na kuangalia umati wa watu wakiweka fedha zao kwenye sanduku la hazina ya Hekalu. Matajiri wengi wakaweka kiasi kikubwa cha fedha. 42 Lakini mjane mmoja maskini akaja na kuweka sarafu mbili ndogo za shaba zenye thamani ya senti mbili.
43 Yesu akawaita wanafunzi wake, akawaambia, “Amin, nawaambia, huyu mjane maskini ameweka katika sanduku la hazina zaidi ya watu wengine wote. 44 Wengine wote wametoa kutokana na ziada ya mali zao. Lakini huyu mjane ametoa kutokana na umaskini wake, akaweka kila kitu alichokuwa nacho, hata kile alichohitaji ili kuishi.”
-
16 Kwa namna hii twaweza kulijua pendo la Mungu: Kwa sababu Yesu Kristo aliutoa uhai wake kwa ajili yetu. Nasi imetupasa kuutoa uhai kwa ajili ya hao ndugu. 17 Ikiwa mtu anavyo vitu vya ulimwengu huu na akamwona ndugu yake ni mhitaji lakini asimhurumie, upendo wa Mungu wakaaje ndani ya mtu huyo? 18 Watoto wapendwa, tusipende kwa maneno au kwa ulimi bali kwa tendo na kweli.
-
17 Waagize wale ambao ni matajiri wa ulimwengu huu waache kujivuna, wala wasiweke tumaini lao katika mali ambayo si ya hakika, bali waweke tumaini lao katika Mungu ambaye hutupatia vitu vyote kwa wingi ili tuvifurahie. 18 Waagize watende mema, wawe matajiri katika matendo mema, pia wawe wakarimu na walio tayari kushiriki mali zao na wengine. 19 Kwa njia hii watajiwekea hazina kama msingi kwa ajili ya wakati ujao na hivyo watajipatia uzima, yaani, ule uzima ambao ni wa kweli.
-
12 Huduma hii mnayofanya si tu kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya watakatifu, bali huzidi sana kwa shukrani nyingi apewazo Mungu. 13 Kwa sababu ya huduma ambayo mmejithibitisha wenyewe, watu watamtukuza Mungu kwa ajili ya utiifu ufuatanao na ukiri wenu wa Injili ya Kristo, na kwa ukarimu wenu wa kushiriki pamoja nao na pia wengine wote.
-
32 Wale walioamini wote walikuwa na moyo mmoja na nia moja. Wala hakuna hata mmoja aliyesema chochote alichokuwa nacho ni mali yake mwenyewe, lakini walishirikiana kila kitu walichokuwa nacho. 33 Mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwa Bwana Yesu kwa nguvu nyingi na neema ya Mungu ilikuwa juu yao wote. 34 Wala hapakuwepo mtu yeyote miongoni mwao aliyekuwa mhitaji, kwa sababu mara kwa mara wale waliokuwa na mashamba na nyumba waliviuza, wakaleta thamani ya vitu vilivyouzwa, 35 wakaiweka miguuni pa mitume, kila mtu akagawiwa kadiri ya mahitaji yake.
-
16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. 17 Kwa maana Mungu hakumtuma Mwanawe kuuhukumu ulimwengu, bali kupitia kwake ulimwengu upate kuokolewa.
-
9 Mtu mkarimu yeye mwenyewe atabarikiwa
kwa kuwa hushiriki chakula chake na maskini.
-
5 Mema yatamjia mtu yule aliye mkarimu na mwenye kukopesha bila riba,
anayefanya mambo yake kwa haki.
-
32 “Msiogope enyi kundi dogo, kwa maana Baba yenu ameona vyema kuwapa ninyi Ufalme. 33 Uzeni mali zenu mkawape maskini. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, mkajiwekee hazina mbinguni isiyokwisha, mahali ambapo mwizi hakaribii wala nondo haharibu. 34 Kwa sababu mahali hazina yako ilipo, hapo ndipo moyo wako utakapokuwa pia.
-
16 Na msiache kutenda mema na kushirikiana vile vitu mlivyo navyo, kwa kuwa dhabihu kama hizo ndizo zinazompendeza Mungu.
-
22 Wote waliokuwa na utayari, wanaume kwa wanawake, wakaja wakaleta vito vya dhahabu vya kila aina: vipini, vipuli, pete na mapambo. Wote wakatoa dhahabu zao kama sadaka ya kuinuliwa kwa Bwana.
-
35 “ ‘Ikiwa mmoja wa wazawa wa nchi yako amekuwa maskini, naye akashindwa kujitegemeza mwenyewe katikati yako, msaidie kama vile ambavyo ungelimsaidia mgeni au kama mkazi wa muda, ili aweze kuendelea kuishi katikati yako. 36 Usichukue riba wala faida yoyote kutoka kwake, bali utamwogopa Mungu wako, ili mzawa wa nchi yako aweze kuendelea kuishi katikati yako. 37 Usimkopeshe fedha ili alipe na riba, wala usimuuzie chakula kwa faida.
-
7 Wakati mnapokwenda, hubirini mkisema, ‘Ufalme wa Mbinguni umekaribia.’ 8 Ponyeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo wachafu. Mmepata bure, toeni bure.
-
42 Nao wakawa wanadumu katika mafundisho ya mitume, katika ushirika, katika kumega mkate na katika kusali. 43 Kila mtu akaingiwa na hofu ya Mungu, nayo miujiza mingi na ishara zikafanywa na mitume. 44 Walioamini wote walikuwa mahali pamoja, nao walikuwa na kila kitu shirika. 45 Waliuza mali zao na vitu walivyokuwa navyo, kila mtu akagawiwa kadiri ya mahitaji yake. 46 Siku zote kwa moyo mmoja walikutana ndani ya ukumbi wa Hekalu, wakimega mkate nyumba kwa nyumba, wakila chakula chao kwa furaha na moyo mweupe, 47 wakimsifu Mungu na kuwapendeza watu wote. Kila siku Bwana akaliongeza kanisa wale waliokuwa wakiokolewa.
-
7 Ikiwa kuna mtu maskini miongoni mwa ndugu zenu, katika mji wowote wa hiyo nchi ambayo Bwana Mungu wenu anawapa, msiwe na moyo mgumu wala usimfumbie mkono ndugu yako aliye maskini. 8 Afadhali fungua mikono yako na umkopeshe kwa hiari chochote anachohitaji.
-
17 Yeye amhurumiaye maskini humkopesha Bwana,
naye atamtuza kwa aliyotenda.
-
33 Lakini Msamaria mmoja aliyekuwa akisafiri alipomwona, alimhurumia. 34 Akaenda alipokuwa na akasafisha majeraha yake kwa divai na mafuta, kisha akayafunga. Ndipo akampandisha kwenye punda wake, akampeleka mpaka kwenye nyumba ya wageni na kumtunza. 35 Kesho yake, yule Msamaria akachukua dinari mbili akampa yule mwenye nyumba ya wageni na kusema, ‘Mtunze, nami nirudipo nitakulipa gharama yoyote ya ziada uliyotumia kwa ajili yake.’
36 “Ni yupi basi miongoni mwa hawa watatu wewe unadhani ni jirani yake yule mtu aliyeangukia mikononi mwa wanyangʼanyi?”
37 Yule mtaalamu wa sheria akajibu, “Ni yule aliyemhurumia.”
Ndipo Yesu akamwambia, “Nenda, ukafanye vivyo hivyo.”
-
1 Kwa hiyo, ndugu zangu, nawasihi kwa rehema zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu na inayompendeza Mungu, hii ndiyo ibada yenu yenye maana. 2 Msifuatishe tena mfano wa ulimwengu huu, bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu. Ndipo mtaweza kuonja na kuhakikisha ni nini mapenzi ya Mungu yaliyo mema, yanayopendeza machoni pake na ukamilifu.
-
9 Hivyo, tusichoke katika kutenda mema, kwa kuwa tutavuna kwa wakati wake tusipokata tamaa. 10 Kwa hiyo, kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema, hasa wale wa jamaa ya waaminio.
-
2 Ndipo Mose akawaita Bezaleli na Oholiabu na kila mtu mwenye ustadi ambaye Bwana alikuwa amempa uwezo na mwenye kupenda kuja na kufanya kazi. 3 Wakapokea kutoka kwa Mose sadaka zote ambazo Waisraeli walikuwa wameleta ili kuifanya kazi ya ujenzi wa Mahali Patakatifu. Nao watu wakaendelea kuleta sadaka za hiari kila asubuhi. 4 Ikafika wakati mafundi wote wenye ujuzi waliokuwa wakiifanya kazi yote ya mahali patakatifu wakasimamisha kazi zao, 5 wakaja na kumwambia Mose, “Watu wanaleta vitu vingi kuliko tunavyohitaji kwa ajili ya kazi hii ambayo Bwana ameagiza ifanyike.”
6 Ndipo Mose akatoa agizo, nao wakapeleka neno hili katika kambi yote: “Mtu yeyote mwanaume au mwanamke asilete tena kitu chochote kwa ajili ya sadaka ya mahali patakatifu.” Hivyo watu wakazuiliwa kuleta zaidi, 7 kwa sababu walivyokuwa navyo tayari vilitosha na kuzidi kuifanya kazi yote.
-
9 Mheshimu Bwana kwa mali zako na
kwa malimbuko ya mazao yako yote;
10 ndipo ghala zako zitakapojaa hadi kufurika,
viriba vyako vitafurika kwa mvinyo mpya.
-
42 Kama yeyote akimpa hata kikombe cha maji baridi mmoja wa hawa wadogo kwa kuwa ni mwanafunzi wangu, amin, nawaambia, hataikosa thawabu yake.”
-
30 Mpe kila akuombaye, na kama mtu akichukua mali yako usitake akurudishie. 31 Watendeeni wengine kama ambavyo mngetaka wawatendee ninyi.
32 “Kama mkiwapenda tu wale wanaowapenda, mwapata sifa gani? Hata ‘wenye dhambi’ huwapenda wale wawapendao.
-
13 Basi ikiwa ninyi mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri, si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa Roho Mtakatifu wale wamwombao!”
-
15 Ndipo Yesu akawaambia, “Jihadharini! Jilindeni na aina zote za choyo. Kwa maana maisha ya mtu hayatokani na wingi wa mali alizo nazo.”
-
8 Lakini Zakayo akasimama na kumwambia Bwana, “Tazama, Bwana! Sasa hivi nusu ya mali yangu ninawapa maskini, nami kama nimemdhulumu mtu yeyote kitu chochote, nitamrudishia mara nne ya hicho kiwango.”
-
3 Kama nikitoa mali yote niliyo nayo na kama nikijitolea mwili wangu uchomwe moto, kama sina upendo, hainifaidi kitu.
-
1 Basi kuhusu changizo kwa ajili ya watakatifu: Kama nilivyoyaagiza makanisa ya Galatia, fanyeni vivyo hivyo. 2 Siku ya kwanza ya kila juma, kila mmoja wenu atenge kiasi cha fedha, kulingana na mapato yake na fedha hizo aziweke akiba, ili nitakapokuja pasiwe na lazima ya kufanya mchango. 3 Kwa hiyo nitakapowasili, nitawapa wale mtakaowachagua barua za kuwatambulisha, ili kuwatuma wapeleke zawadi zenu huko Yerusalemu. 4 Kama ikionekana ni vyema na mimi niende, basi hao watu watafuatana nami.
-
6 Basi, yeye afundishwaye katika neno na amshirikishe mwalimu wake mema yote.
-
5 Kama mtu yeyote miongoni mwenu amepungukiwa na hekima na amwombe Mungu, yeye awapaye watu wote kwa ukarimu wala hana kinyongo, naye atapewa.
Shows Read in context, Share and Copy.